Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Nuru Awadh Bafadhili (22 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuwa hapa kwa muda huu na kuweza kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Vilevile napenda kukishukuru chama changu, Chama cha Wananchi (CUF) kinachoongozwa na Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuweza kuniteua kuweza kuwakilisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, nitajikita kwanza kwenye masuala ya elimu. Kwa kweli elimu yetu ni nzuri, lakini kuna matatizo katika elimu. Matatizo yaliyopo ni kwamba mtoto mwenye njaa hafundishiki. Watoto wetu hawafanyi vizuri katika masomo kwa sababu ya njaa kutokana na hali duni ya uchumi. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali, ihakikishe inafanya utaratibu angalau wanafunzi wetu wa shule zetu waweze kupata angalau mlo mmoja kwa siku ili waweze kuhudhuria vizuri masomo. Kuna baadhi ya wanafunzi wanashindwa kwenda shuleni, wanakuwa watoro kutokana na ukosefu wa vyakula majumbani kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Serikali italitilia mkazo hilo, itawezekana na wanafunzi wetu wakaweza kufanya vizuri katika masomo yao. Kwani sisi tuliposoma pia, tulikuwa tunakwenda shule lakini tunapata milo miwili. Saa 4.00 tunapata uji wa bulga na mchana tunapata chakula ambacho kilikuwa ni mlo uliokamilika. Basi hata kama Serikali itakuwa haina uwezo wa kufanya milo miwili, basi angalau huo mlo mmoja ili mwanafunzi aweze kukaa darasani na kumsikila Mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu suala zima la afya. Kwa kweli katika Wizara hii ya Afya kuna matatizo mengi sana. Kwa mfano katika hospitali yangu ya Rufaa ya Tanga, kuna matatizo ya Daktari Bingwa wa Wanawake, yaani Daktari Bingwa wa Akinamama, Daktari Bingwa wa Koo na Masikio. Kwa hiyo, wenye matatizo hayo ya koo, sikio wanashindwa kupata huduma nzuri kutokana na ukosefu wa daktari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna tatizo la watumishi katika kada zote. Kwa hiyo, Wizara iangalie katika mgawanyo huo wa Watumishi wa kada zote na Hospitali yetu ya Rufaa ya Tanga iangaliwe ili waweze kupata huduma nzuri na zilizo bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia vilevile kuhusu UKIMWI. Hili ni janga la kitaifa kwa kweli na vijana wetu ndio wanaoathirika zaidi na UKIMWI. Vijana wa umri kuanzia miaka 15 mpaka 24 ndio wanaoathirika zaidi na UKIMWI. Kuna vishawishi vingi kwa vijana hawa na wakati mwingine kuna wazee wengine wanawafuata wasichana wadogo wadogo eti wanadai kuwa wake zao majumbani wamechuja. Kwa hiyo, wanawafuata watoto wadogo na wengine tayari wanaume wale wazee au vijana wakubwa wameathirika, kwa hiyo, wanawaambukiza watoto wetu au vijana wetu wadogo maradhi ambayo hayana tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mila potofu ambazo zinachangia pia kuambukiza au kuenea gonjwa hili la UKIMWI, mfano kuna mila nyingine mwanamke anapokuwa na mimba, mchumba anachumbiwa akiwa ndani ya tumbo, haijulikani kama kutazaliwa mwanamke au mwanaume. Kwa hiyo, atakapozaliwa mwanaume siyo wake, lakini akizaliwa mwanamke ndiyo atakuwa ni wa kwake. Kwa hiyo, pia hizi ndoa za utotoni zinachangia katika kueneza gonjwa hili la UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna mila za kurithi wajane. Utakuta mke akifiwa na mume wake anarithiwa au wakati mwingine na vile vile mume anarithiwa na mke mwingine. Kwa hiyo, hii inaleta matatizo kwa sababu hajulikani mmojawapo kati ya hao waliokufa amekufa kwa ugonjwa gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaiomba Serikali hili lipigiwe kelele zaidi, lakini vilevile sisi kama wazazi, tuwafundishe watoto wetu maadili mazuri. Kwa kweli kuna wazazi ambao wanajifanya wao kila wakati wako busy, wako kazini tu, hawawaangalii watoto wao nyumbani. Kwa hiyo, maadili yanaporomoka na baada ya maadili kuporomoka, utakuta watoto wanaharibikiwa. (Makofi)

Kwa hiyo, sisi kama wazazi, tuhakikishe tunafuatilia nyendo zote za watoto wetu kwa sababu sisi kama Wabunge nadhani wazazi wetu walitufuatilia tukaenda shuleni tukasoma mpaka leo tumefikia kupata nafasi hii ya kuwawakilisha wananchi wetu. Kwa hiyo, sisi kama wazazi aidha wanaume au wanawake, tuhakikishe tunakwenda vizuri katika kutengeneza maadili katika nyumba zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo hilo kuhusu UKIMWI. Kuna mila nyingine wanatumia vifaa ambavyo havichemshwi. Kwa mfano, watu wanapotahiriwa, wanapokeketwa, wanaotogwa masikio sijui na pua na nini, unaona vitu vile havichemshwi wala haviko katika usalama, kwa hiyo, hivi pia vilevile vinachangia katika kueneza gonjwa hili la UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaiomba Serikali ihakikishe inaongeza bajeti kwa ajili ya kununua dawa za waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzunguzaji)

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa nikiwa katika afya nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na bajeti hii nitazungumzia kuhusu elimu na afya. Nikianzia na suala zima la elimu, hivi karibuni tulimsikia Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamini William Mkapa, akilalamikia ufaulu mdogo wa wanafunzi wetu katika shule zetu za Serikali. Ni kweli wanafunzi wetu katika shule za Serikali wanapata elimu lakini haifanani na wanafunzi wa shule za binafsi. Kwa sababu shule za sekondari za Serikali utakuta darasa moja lina wanafunzi 45, 50 mpaka 60; ni sekondari nayo hiyo. Shule za binafsi utakuta labda form one wako 20, form two wako 25, lakini hawazidi 40 na Walimu wapo wa kutosha ambao wanawafundisha wale wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitaaluma mimi ni mwalimu. Mwalimu unatakiwa katika muda wa dakika 40 unazopewa, uzungukie wanafunzi wote wa darasani kwako ili ujue kosa lake; amefanya nini katika kazi uliyompa au anahitaji msaada gani? Sasa utakuta darasa lina wanafunzi 70 au 80, utawazungukiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iangalie pia uwiano wa wanafunzi katika madarasa yetu. Walimu wanafanya kazi, wanajitahidi, lakini madarasa yanajaa wanafunzi kiasi ambacho msaada unakuwa ni mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali iwaangalie sana wanafunzi wetu. Kila siku mimi natamka, nasema, “mwanafunzi mwenye njaa, hafundishiki.” Kuna wanafunzi wengine, pengine amekula saa 11.00; asubuhi hajala chochote anaambiwa aende shule. Kwa kweli mwanafunzi yule kwake itakuwa ni vigumu sana kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu kule shule za watu binafsi, au wenzetu Wazungu wanasema za private, utakuta wanafika kule saa 4.00 kuna kantini, mzazi kampa mtoto wake pesa, anajinunulia chakula. Mchana vilevile anajinunulia chakula. Sisi watoto wetu, anaondoka nyumbani pengine hata uji hakunywa asubuhi na hata senti 20 au Sh.50/= za kwenda kumuwezesha kununua chochote cha kutafuna, hakupewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa akili itakuwa kwenye kusoma au atawaza njaa? Mara nyingi wanafunzi wa namna ile, utakuta hawashiki lolote katika akili zao, kwa sababu anawaza nikitoka hapa nitakwenda kula nini? Kwa hiyo, Serikali ifanye utaratibu wa kuwawezesha angalau wapate uji. Saa 4.00 mwanafunzi akipata uji, atajua kuwa nikifika shuleni nitapata uji, nitakunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia kuhusu Walimu. Walimu kweli wanafanya kazi, lakini kuna maneno. Sisi tulipoanza kazi ya Ualimu tuliambiwa Ualimu ni wito kama Shehe, Padri, Sister au Askofu. Imani ile sisi ilituingia. Sasa hivi tuna Walimu wenye matatizo. Mwalimu amekwenda shule, asubuhi tayari ameshalewa. Hivi mwanafunzi atakwenda kusoma nini kwa Mwalimu yule ambaye amelewa? Au Mwalimu usiku anakwenda kwenye mabaa mwingine anajiuza. Mpaka wanafunzi wanafikia kumdharau Mwalimu darasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali ihakikishe kuwe na utaratibu maalum au kuwe na circular maalum inayowafanya Walimu wawe wanaiheshimu ile kazi ya Ualimu, kama sisi tulivyoambiwa kuwa Ualimu ni wito. Ndiyo maana viongozi wengi hapa ni Walimu kwa sababu walikuwa na nidhamu nzuri sana. Kwa hiyo, tuwaangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie stahiki za Walimu. Kuna Mwalimu anapandishwa daraja lakini anaweza kukaa miaka miwili hajapewa pesa zake. Kwa hiyo, Walimu nao wanachoka, ndio wanafanya kazi vilevile wanavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kuhusu suala la afya. Nitazungumzia kuhusu hospitali yangu ya Mkoa ya Rufaa ya Tanga, Bombo. Kwa kweli ile hospitali inapokea wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali, lakini ile hospitali ina tatizo moja; Hospitali ya Bombo haina lifti ya kuwapandisha wagonjwa katika jengo la Galanos.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wagonjwa inabidi wapandishwe kwa kutumia mabaunsa. Kuna watu maalum wenye miili mikubwa wamekaa pale, unawalipa ndio wanakupandishia mgonjwa wako juu ili aende wodini akalazwe. Kwa hiyo, Serikali iangalie jinsi gani itaitengeneza ile lifti ya Hospitali ya Bombo ukizingatia hospitali ile ndiyo Hospitali yetu ya Rufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia kuhusu Hospitali ya Wilaya. Sisi kama Wilaya ya Tanga nasema hatuna Hospitali ya Wilaya. Hospitali ya Wilaya huwezi kuifananisha na Kituo cha Afya kimoja kinaitwa Makorora, kingine kinaitwa Ngamiani, kingine kinaitwa Pongwe katika Kata ya Pongwe. Vile vituo huwezi kuvilinganisha na hospitali yetu ya Wilaya. Nimeitembelea ile Hospitali ya Wilaya, nimekuta vile vyumba ni kama mabweni ya wanafunzi wa sekondari, yaani kabisa haikujengwa kihospitali ya Wilaya. Ni ili mradi tuambiwe Tanga tuna Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hiyo ya Wilaya haikuzingatia miundombinu ya walemavu. Kuna ghorofa ya kupanda huko juu. Sasa mlemavu akiambiwa apande juu, atapanda vipi? Hospitali hiyo ya Wilaya pia hatuna ambulance ya Wilaya. Kwa hiyo, watu wa Tanga Hospitali ya Wilaya pia tunategemea pia hivyo Vituo vya Afya na vilevile tunategemea Hospitali ya Rufaa ya Bombo. Kwa hiyo, naiomba Serikali ihakikishe Tanga na sisi tunapata hospitali yetu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya iliyojengwa, inaelekea kama ilijengwa kwa mshtuko sijui; imejengwa labda kisiasa au vipi, kwa sababu tulikuwa na kiwanja chetu cha hospitali kiko sehemu za Mwakibila Kata ya Tangasisi. Miaka kati ya 2007 mpaka 2010, kiwanja kile kiliuziwa mwekezaji. Mwekezaji yeye hakujenga chochote, badala yake kikahamishwa kiwanja kilichokuwa kijengwe hospitali kikapelekwa hiyo sehemu ambayo inaitwa Masiwanishamba, lakini miundombinu ya kwenda huko Masiwanishamba pia hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hiyo hiyo tunayoambiwa ni Hospitali ya Wilaya, ikifika saa 9.30 hospitali inafungwa. Ina maana wagonjwa wanaambiwa wasiugue tena hapo mpaka kesho tena saa moja na nusu, kunakuwa hakuna tena huduma ya hospitali. Kwa hiyo, naiomba Serikali itusaidie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie suala zima la kuhusu madawa ya kulevya. Kama tulivyoona kwenye vitabu vyetu tulivyopewa kuhusu masuala mazima ya dawa za kulevya, ni dhahiri kwamba vijana wengi wanaotumia dawa za kulevya wakipelekwa kwenye Sober House wanatulia vizuri wanakuwa wazuri, lakini wanaporudi tu kwenye maeneo yao na akikutana na wale wengine, wanarudia tena kazi yao. Kwa hiyo, inakuwa ni kama kumpigia mbuzi gitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali kama itawezekana ihakikishe tujengewe Sober Houses kwa ajili ya vijana wetu wale ambao wameathirika na dawa za kulevya. Pia katika hizo Sober Houses tuhakikishe wakifika kule at least wanapata mafunzo mbalimbali ya kazi za mikono. Kuna mwingine atafundishwa labda useremala, mwingine atafundishwa kushona cherehani, kwa hiyo, akirudi huku uraiani anaweza akaajirika pengine akipewa nyezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika hii Serikali ni sikivu. Kwa hiyo, tuhakikishe wale tunaowapeleka katika Sober Houses, tuhakikishe tunawapatia mafunzo maalum. Siyo tu yale mafunzo ya kuwazuia wasile unga, lakini wapate mafunzo ya kuhakikisha kwamba wanapata mafunzo ya kazi za mikono ili akirudi aende akajitegemee mwenyewe katika maisha yake anayoishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nizungumzie kuhusu rushwa sasa. Hii rushwa yaani imekuwa kama ni donda ndugu, kwa sababu mtu anaambiwa kabisa hapa hatupokei rushwa, lakini ukimaliza anakwambia unaniondoaje...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NURU AWADHI BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uwezo wa kuzungumza. Vile vile nimpe pole Mheshimiwa Spika, Mungu azidi kuimarisha afya yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu barabara zilizo chini ya TARURA. TARURA kwa kweli hadi hivi sasa hawajaeleweka kwa wananchi. TARURA japo inashughulikia barabara lakini bora ingewashirikisha Madiwani. Madiwani ndio wanaozijua barabara zetu zilivyo. Ikiwa TARURA haitawashirikisha Madiwani barabara zetu zitazidi kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kauli ya Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli ya Tanzania ya viwanda. Tanzania ya kuelekea uchumi wa viwanda hiyo ni kaulimbiu nzuri lakini tujiulize, je, umeme wa kuendesha viwanda hivyo upo wa kutosha? Lazima Serikali ihakikishe tunatumia mito tuliyonayo, mfano Mto Rufiji, Kilombero na Mito mingine ambayo ina maji ya kutosha ili izalishe umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme tulionao hauwezi kukidhi kuendesha viwanda vinavyohamasishwa vianzishwe.

Kila mkoa umepewa agizo la kujenga viwada 100, je, viwanda hivyo vilijengewa umeme wa kutosha na utapatikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atueleze, Je na umeme wa kuendesha viwanda utapatikana bila tatizo?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Waziri, Naibu Mawaziri na watendaji wote kwa juhudi wanayoifanya katika kuitendea mema nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijikite katika ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani - Saadani - Bagamoyo. Najua katika bajeti hii ya 2018/2019 barabara hii imo kwenye mipango ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Naiomba Serikali ihakikishe barabara hii inajengwa kama ilivyopangwa katika bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo inapitia Pangani - Saadani -Bagamoyo ina umuhimu sana. Kuna mbuga ya wanyama ya Saadani ambapo simba na tembo wanacheza pamoja katika ufukwe wa bahari wa maeneo ya Saadani yaliyopo karibu na Pangani. Barabara hii itasaidia kuleta watalii na kuweza kuliingizia Taifa fedha. Mbuga hii ni nzuri kwa hiyo ujenzi wa barabara utasaidia kukuza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa kununua ndege ambazo ni hatua kubwa ya maendeleo. Katika Kata ya Bweni, Wilaya ya Pangani kuna hoteli inaitwa Mashadu. Hoteli hii ina kiwanja kizuri cha ndege ambapo ndege ndogo hutua kushusha na kupandisha abiria. Naiomba Serikali ifanye utafiti ili kama kuna uwezekano ndege ndogo za kwetu zitue katika kiwanja hicho kilichopo Mashadu, Wilaya ya Pangani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Wizara kwa taarifa yake ya bajeti. Nitaongea machache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu walimu wastaafu. Kuna walimu waliostaafu toka mwaka 2016 lakini mpaka leo bado hawajalipwa posho ya nauli ya kuwarudisha makwao. Serikali inatuambia nini kuhusu wastaafu hawa ambao hawajui hatma ya posho yao ya nauli ya kuwarudisha makwao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni UMISHUMTA. Shule za msingi zinashiriki michezo hiyo. Je, Serikali inatuambia nini kuhusu shule kuwezeshwa fedha kwa ajili ya kuwahudumia wanafunzi wakati wanashiriki michezo? Kuna baadhi ya wanafunzi wanatoka mbali kwenda kushiriki michezo na wakati huo wengine wanatoka majumbani kwao ikiwa hawajakula chochote? Je, Serikali haioni ushiriki wa wanafunzi hao wao katika michezo mbalimbali utadhoofika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu madai ya walimu. Kuna baadhi ya Halmashauri zinadaiwa fedha na walimu zikiwemo za likizo na kusimamia mitihani ya darasa la nne na la saba. Tunaomba Serikali ifuatilie Halmashauri huenda kuna baadhi ya Halmashauri zinafanyia ubadhirifu maslahi ya walimu. Hii pia inachangia kushuka kwa morali ya walimu kufundisha madarasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu jengo la Kitega Uchumi la CWT lililopo Ilala Boma, Dar es Salaam. Chama cha Walimu kilichangisha walimu sehemu mbalimbali kwa ujenzi wa jengo hilo. Kuna walimu waliostaafu au kufa ambao walichangia fedha zao. Je, Serikali itueleze, walimu wananufaika vipi na kitega uchumi hicho? Je, wale waliostaafu au kufa watanufaikaje?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ile kaulimbiu ya kumtua mwanamke ndoo bado haijatekelezwa kutokana na jitihada za Serikali zinazoonesha kwenda kidogo kidogo katika kuwapatia wananchi wengi maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga kuna baadhi ya vijiji bado havina maji, kuna mabomba lakini hayatoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Madanga Wilaya ya Pangani kuna vitongoji ambavyo havina maji. Vitongoji hivyo ni Zimbiri, Jaira, Barabarani, Nunda na vinginevyo wananchi wanasaidiwa na maji ambayo taasisi za dini wamechimba visima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ije na majibu ya lini Kata ya Madanga, Wilaya ya Pangani watapata maji safi na salama?

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika Kata ya Mwalijembe Wilaya ya Mkinga wananchi wana tatizo la maji, wanashirikiana maji yao na wanyama. Maji ya kwenye mabwawa siyo safi na salama. Serikali iwahurumie wananchi hawa ili kuwaepusha na magojwa ya mlipuko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi napenda niende haraka haraka, nianze na suala zima la walimu waliostaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna walimu ambao wamestaafu hadi leo hawajapewa posho zao za usafiri kurudi makwao. Mpaka leo wamebaki katika vituo vya kazi. Sasa tunaomba Serikali ituambie lini itawalipa mafao yao hayo?
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuzungumzia kuhusu walimu. Kuna walimu ambao wanadai baadhi ya malimbikizo yao, lakini baya zaidi kuna baadhi ya walimu walisimamia mitihani ya darasa la nne na darasa la saba toka mwaka 2015 hadi leo hawajalipwa pesa zao hizo za kusimamia mitihani. Nadhani kosa sio la Wizara lakini naiomba Wizara ihakikishe, iulizie hizi Halmashauri. Nadhani kuna ubadhirifu fulani katika hizi Halmashauri, kwa sabbau pesa zinatolewa, lakini walimu husika hawapewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu suala la UMITASHUMTA. Wanafunzi wa shule za msingi kuanzia sasa hivi nadhani wako katika michezo hii ya UMITASHUMTA, nadhani Serikali inatoa pesa, lakini bila shaka zile pesa ni kidogo. Kwa sababu kuna baadhi ya shule wako mbali na vituo vinavyofanyika hiyo michezo, hivyo inabidi wapate usafiri wa kwenda kule, kwa hiyo, inawagharimu walimu wao wenyewe wajitolee pesa zao kutokana na uhaba wa ile pesa inayopelekwa katika shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu hao hao maskini ya Mungu hawana fedha za kutosha kujikimu wao wenyewe lakini pia wanaona kheri wawasaidie wale wanafunzi, kwa sababu utakuta mwanafunzi wakati mwingine anatoka nyumbani kwao hajala inabidi mwalimu ajitolee awaununulie angalau hata karanga watafune, pesa ile inatoka mfukoni kwa mwalimu. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali inapoandaa hii michezo ya UMITASHUMTA ihakikishe kuwa wanaweka fungu kubwa ambalo litawasaidia walimu kuwawezesha watoto waweze kwenda kucheza ile michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna hiki kitega uchumi cha CWT. Enzi hizo tuliambiwa kuwa ni kitega uchumi ambacho kitawasaidia walimu na jengo hili limejengwa Dar es Salaam, Ilala Boma pale Mwalimu Nyerere House. Lakini cha kushangaza sijui kitega uchumi hiki kinawasaidiaje walimu kwa sababu kuna walimu wengine kama sisi tumestaafu, kuna walimu wengine wamekufa na kitega uchumi bado kiko pale pale. Je, hawa waliostaafu na hawa waliokufa watasaidiwaje na kitega uchumi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mimba za utotoni. Kweli watoto wetu wa kike wanapata mimba, miaka tuliyosoma sisi ilikuwa mtu akipata mimba ilikuwa ni mambo ya ajabu sana, lakini sishangai sana kwa sasa hivi kutokana na utandawazi uliopo. Mambo ni mengi, watoto wanaangalia luninga na wanakuta mambo mengi ambayo na wao wanafanya majaribio.

Ombi langu kwa Serikali, naomba ikiwezekana wafanye mobile clinics wawapitie kila wakati watoto wetu wa kike. Kwa sababu mwanafunzi atakapoona, eeh, nitakuwa kila wakati nafuatiliwa fuatiliwa afya yangu, kwa hiyo ataliogopa lile tendo kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwennyekiti, vile vile wanafunzi wetu wanapokuwa shuleni wanakuwa ni wengi mno madarasani kiasi ambacho mwalimu anashindwa kusahihisha, anashindwa kuwapa kazi za kutosha na hiyo haitoshi, utakuta mwalimu kutokana na wingi wa wanafunzi, darasa moja ni wanafunzi 80 anachagua baadhi ya wanafunzi wa madarasa ya juu wamsaidie kusahihisha. (Makofi)

Hata mitihani inasahihishwa na baadhi ya wanafunzi wa madarasa ya juu. Utakuta mwanafunzi karudi shuleni swali amelipata lakini amewekewa kosa na marks zake nimekatwa na akienda kwa mwalimu akimwambia, mwalimu, hili swali nimelikosa, anamwambia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi kwa kuniwezesha kuchangia machache. Ni kweli awamu hii ni ya uchumi wa viwanda lakini tujiulize viwanda hivyo vinavyoongelewa vitajengwa na kumalizika kwa wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo nia thabiti ya ujenzi wa viwanda lakini tatizo lipo kwa watendaji. Wapo baadhi ya watendaji ambao hawana nia nzuri na Taifa hili, wanadumaza maendeleo ya Taifa. Hawa watendaji wanakuwa wepesi wa kuomba rushwa kiasi kwamba hata wawekezaji wanahofia kuwekeza nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga kulikuwa na Kiwanda cha Mbolea ambacho kimeng’olewa mitambo na habari nilizonazo eti kimehamishiwa Minjingu. Namuomba Waziri aeleze ni sababu zipi zilizosababisha kuhamisha kiwanda hicho ukizingatia kilikuwa karibu na bahari, jambo lililosababisha kupata unafuu wa upokeaji wa malighafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Chuma, kiwanda hiki kimekuwa ni chaka la uhalifu. Kuna watu wanaishi humo kama vivuli vyao vya kujificha. Hata mashine zake zilianza kung’olewa. Mheshimiwa Waziri anatuambia nini kuhusu utendaji kazi wa hiki Kiwanda cha Chuma cha Tanga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga kuna viwanda vya wamiliki wa sekta binafsi, viwanda ambavyo vinatoa ajira kwa wananchi wa Tanga hususani vijana. Tunalalamika kuwa vijana wengi wamejiingiza katika dawa za kulevya hii huenda inasababishwa na ukosefu wa kazi za kufanya matokeo yake wanaamua kutumia dawa za kulevya. Serikali iangalie umuhimu wa kuanzisha viwanda ili viweze kutoa ajira hususani kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema kuwa wanafunzi wanaomaliza masomo wanaweza wakajiajiri wao wenyewe, siyo kweli kwa vile mtu hawezi kumaliza masomo kisha akawa ana mtaji wa kufanya biashara yoyote, biashara ni mtaji. Je, anayetoka chuoni atapata wapi mtaji wa kumuwezesha kufanya biashara?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo tunacholima Watanzania siyo chenye tija. Wakulima wengi wanalima kwa mazoea, siyo kama biashara ya kuwapatia kipato.

Mheshiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga kuna Kituo cha Utafiti cha Kilimo kilichopo Mlingano Wilaya ya Muheza. Kutokana na kituo hiki, wakulima hawapati msaada wowote kutokana utafiti wa udongo wa mazao yanayostahili kulimwa katika eneo hilo. Ombi, kwa nini Mheshimiwa Waziri asihamasishe umuhimu wa kupima udongo na kuelewa aina ya mazao yanayoweza kustawi katika maeneo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Pwani ni maarufu kwa kilimo cha minazi. Minazi ikivunwa ina manufaa sana. Mafuta ya nazi ni mazuri sana, hayana lehemu. Mheshimiwa Waziri atueleze, ni lini Tanga kutaanzishwa kiwanda cha kutengeneza mafuta kutokana na nazi zinazovunwa Tanga, Pangani, Mkinga na Muheza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 1960 sekta binafsi waliweza kutengeneza kiwanda cha kukamua mafuta ya nazi. Kiwanda hiki kilikuwa katika Jiji la Tanga. Mafuta yaliyozalishwa hapo yaliitwa Nicolin. Wananchi walitumia mafuta hayo kupikia vyakula mbalimbali na wala hayakuleta madhara kwa walaji. Tunaomba Serikali itujengee kiwanda cha kusindika mafuta ya nazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kabla sijachangia chochote nimshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama hapa kwa siku ya leo. Kwanza napenda kutoa pongezi kwa Serikali kudhibiti uvuvi haramu. Kwa sababu uvuvi haramu sina maana ya nyavu tu, uvuvi haramu ni wale pia wanaotumia mabomu. Vijana wetu wanaathirika kwa kutumia mabomu, kuna wengine wamekuwa ni vipofu, kuna wengine wamekuwa ni viwete hawana miguu, wengine hawana mikono na wengine wanapoteza maisha kutokana na mabomu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mabomu haya yanaharibu matumbawe ambayo ndiyo nyumba za kuzalia samaki. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali kudhibiti hali hiyo na tunaiomba Serikali iendelee na hili zoezi kwa sababu tunao vijana na ushahidi upo wapo tayari wamepoteza hali yao ya kuona kutokana na mabomu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia kuhusu hizi nyavu; kwa kweli wavuvi siyo wanaotengeneza nyavu, wavuvi wananunua. Sasa ilitakiwa wale wanaouza nyavu wazuiliwe kuuza zile nyavu ambazo hazistahili kwa ajili ya kuvulia samaki, badala ya kumwadhibu mvuvi ambaye yeye anakwenda kununua kwa ajili ya kufanya kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili wana maneno wanasema unapofagia unaanzia kufagia pale miguuni kwako kwenda mbele. Sasa ninachosema sisi Mwenyezi Mungu ametupa bahari, Mungu ametupa maziwa na Mwenyezi Mungu ameweza kutupa mito. Kwa hiyo, tuna samaki wengi sana, sasa kabla hatujanunua samaki kutoka nje kwenye makopo, kwenye super markets ni lazima sisi tutumie samaki wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, samaki wetu ni wazuri sana, kwanza unapokula samaki unakuwa una akili, mtu yoyote anayetumia samaki anakuwa na akili nzuri sana. Vilevile samaki ni chakula kizuri hata kama huna chakula chochote cha kula lakini unaweza ku-survive kwa kula samaki. Kwa hiyo, tujitahidi kula tuweze kula samaki wetu ambao wanavuliwa hapahapa, tuone fahari kutumia samaki wetu kuliko kununua samaki ambao wanatoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wenzangu nadhani walikwishasema kuhusu leseni hizi ambapo mvuvi anakata leseni, mwenye chombo anakata leseni, msaidizi anakata leseni. Sasa hizo leseni zimekuwa nyingi kabisa kiasi ambacho wanalalamika hawapati faida. Matokeo yake wanapokwenda kwenye bahari kuu kule samaki wanauzwa hukohuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kama Tanga sisi tumepakana na Kenya. Kwa hiyo, samaki wanapopatikana pale wanauzwa mvuvi anarudi hivihivi anakwambia sikupata chochote. Kwa hiyo, tunapoteza mapato kwa ajili ya nchi yetu, hivyo, tuhakikishe hizi leseni zinapungua ili kuwapungizia wavuvi adha ya kupata kiasi kidogo katika hela zao wanazozipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna viwanda vya samaki kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa lakini sisi watu wa Pwani hatuna viwanda vya kuchakata samaki. Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini Serikali itafanya mpango wa kutujengea viwanda ambavyo tunaweza tukachakata samaki, kwa sababu tuna samaki wengi sana, tuna jodari, changu, kolekole, ngisi, pweza na wengineo. Pia tunajua pweza anawasaidia sana akinamama wazazi wakati wanapokuwa wamejifungua wanapata maziwa na akinababa pia wanasaidiwa na hao pweza, wenyewe wanajua jinsi gani wanavyowasaidia hao pweza. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee kuhusu ufugaji. Nadhani hapa ufugaji una matatizo kwa watu wanaoishi katika maeneo ya Miji. Kwa mfano, katika Jiji la Tanga watu wanajitahidi wanafuga ng’ombe katika nyumba zao, lakini inakuja amri kutoka Halmashauri ya Jiji kwamba atakayeonekana anafuga ng’ombe ndani ya nyumba yake atachukuliwa hatua. Sasa hiyo inamvunja moyo mtu ambaye anataka kufanya ujasiriamali wa ufugaji. Kwa hiyo, Serikali ihakikishe inaandaa utaratibu vilevile wale wafugaji wafuge kwa amani badala kwa kunyanyasika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna mifugo inayotembea tembea barabani sasa mifugo hii hatujui ina wenyewe au haina wenyewe ile ndiyo mifugo ambayo inayotakiwa idhibitiwe ili isiweze kuzunguka barabarani wakati mwingine inagongwa na gari, wakati mwingine inasababisha ajali kwa watu, kwa hiyo mifugo ile inatakiwa iangaliwe.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kupata muda wa kutoa mawazo yangu kwa faida ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa kwanza nitajikita katika suala zima la utalii. Utalii ni sekta ambayo inalipatia faida Taifa letu. Mbuga nyingi zinazotangazwa ni Mikumi, Serengeti, Ngorongoro, Manyara na Selous. Mbuga hizi ndizo ambazo kila leo utasikia zikitangazwa katika vyombo vyetu mbalimbali vya habari. Kuna mbuga ya Saadani katika Wilaya ya Pangani, mbuga hii imepakana na ufukwe wa bahari. Katika maajabu ya mbuga hii utakuta simba na tembo na wanyama wengine wanacheza pamoja katika ufukwe wa bahari hivyo nayo ni maajabu.

Mheshimiwa Spika, ukiacha huo utalii wa wanyama pia kuna eneo katika Wilaya ya Tanga ambapo kuna maji moto yenye sulphur ambayo wenye matatizo ya ugonjwa wa upele huenda kuogelea hapo. Sehemu hiyo huitwa Amboni, Kata ya Mzizima Wilaya ya Tanga, eneo hilo ni maarufu kwa jina la Amboni Sulphur Baths.

Mheshimiwa Spika, katika vivutio vya utalii pia kuna sehemu katika Bandari ya Jiji la Tanga kuna eneo linaitwa Jambe, eneo hili kuna magofu ya mahandaki ambayo zamani watu walioishi hapo walitumia kujificha na pia kuna visima vilivyochimbwa na wenyeji walioishi wakati huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wachangiaji waliotangulia kuwapongeza Waziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. Nianze na kuchangia kuhusu Walimu. Walimu wanafanya kazi nzuri na ni walezi wa pili katika familia baada ya wazazi/walezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda mwingi Walimu wanashinda na watoto wanaotoka katika malezi mbalimbali lakini wanapofika shuleni wao huwa ndiyo walezi, Madaktari, Manesi, Mahakimu, Polisi na kadhalika. Kazi zote hizi Walimu wanakuwa kama ndiyo mbadala wa watajwa hapo juu kutokana na majukumu wanayoyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu ndiyo chimbuko la wafanyakazi wa fani zote katika nchi hii. Kama Mwalimu angeacha kumpatia mwanafunzi msaada wa kumudu kusoma vizuri darasani akafaulu vizuri na hatimaye kufika hadi chuo kikuu na kuweza kupata kazi nzuri ya kumwendeshea maisha yake au hata kuweza kujiajiri mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu huyu yuko katika mazingira magumu sana lakini bado wanaendelea na mikakati ya kufundisha ili kujenga Taifa la wasomi. Naiomba Serikali angalau iwarudishie Walimu ile posho waliyokuwa wakipewa miaka ya 80 yaani teaching allowance. Hii teaching allowance, ilikuwa ni asilimia 25 ya mshahara wa Mwalimu. Hii ingewasaidia Walimu katika kupunguza makali ya maisha na kumudu kufanya vizuri kazi yao ya kuwafundisha watoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uzima asubuhi hii. Vilevile napenda kuwapa pole wananchi wa Buyungu kwa kuondokewa na Mbunge wao. Mwenyezi Mungu atawapa subra katika kipindi hiki kigumu walichokipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sina budi kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri na Naibu wake, pamoja na Watendaji wake wote kwa bidii wanayoionyesha katika sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania siyo nchi maskini lakini kuna baadhi ya wananchi na hata wawekezaji wanatuongezea umaskini. Madini tuliyonayo ni ya aina mbalimbali ambazo kama zitafuatiliwa vizuri, Taifa letu lingeneemeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya wachimbaji hawauzi bidhaa zao katika masoko husika ila wanauza katika njia za panya. Naomba Serikali iwe madhubuti, wachimbaji wakubwa na wadogo wauze bidhaa zao katika masoko yanayotambuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ajali za mara kwa mara zinatokea katika migodi ikiwamo wananchi kuangukiwa na kifusi au migodi kujaa maji. Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hali hii ya hatari haitokei mara kwa mara?

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya pekee ambayo hayapo nchi yoyote duniani ni tanzanite. Madini haya Wakenya huyanunua sana na kuyapeleka nje na kujifanya kuwa wao ndiyo wachimbaji wa madini haya. Naiomba Serikali itangaze madini yetu na pia iieleweshe dunia kuwa tanzanite ni madini yanayopatikana Tanzania tu, siyo nchi yoyote katika dunia hii.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa na kuweza kuchangia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Kamati yangu ya miundombinu kwa taarifa nzuri iliyotolewa. Mimi ntazungumzia suala zima la Barabara yetu hii ya Dodoma – Dar es Salaam; kwa kweli Wizara imejitahidi sana kutengeneza barabara nzuri hii ya Dodoma – Dar es Salaam, lakini kuna tatizo linalojitokeza; Dodoma kama Jiji tukifika pale Ihumwa karibu kilometa sijui 10 mpaka kufika hapa katikati ya jiji kunakuwa na giza mno, kwa hiyo naiomba Serikali ijitahidi angalau kutuwekea taa za barabarani ili unapoingia katika sehemu zile za kukaribia jiji ujihisi kweli naingia katika jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sio tu Barabara ya Dodoma – Dar es Salaam, ile barabara ya Iringa, ile barabara ya kwenda Kondoa na barabara ya kwenda Singida, barabara zote hizi unapokaribia karibu na jiji ziwe zimewekwa taa kwa usalama wa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna tatizo linalojitokeza katika hizo barabara. Katika barabara zile kuna zile zebra crossing, naiomba Serikali iwape wananchi elimu ya kuzitumia zile zebra, kwa sababu mwananchi anajua kuwa ukifika kwenye zebra pale gari inasimama anapishwa yeye, basi unakuta mtu anachezea simu, eti anavuka kwenye barabara anachezea simu. Sasa kuna madereva wengine wanakuwa na uvumilivu lakini dereva mwingine anapita tu. Hiyo inaweza ikasababisha vifo vya watu kutokana na uzembe wao ambao wameona kuwa Serikali imetengeneza sheria kuwa zile zebra crossing gari inasimama na wao wanavuka, sasa badala ya kuvuka straight yeye anachezea simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia sasa barabara yetu ya kutoka Dar es Salaam – Tanga, Dar es Salaam – Tanga tunaunganishwa na Daraja ambalo liko katika Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Tanga, Daraja la Wami. Kwa kweli daraja lile tunaambiwa na Serikali kuwa litatengenezwa na lipo katika mkakati wa kutengenezwa, lakini ninachoomba, Serikali ilipe kipaumbele lile daraja kwa sababu mwaka jana mwezi Desemba tu kwa siku mfululizo magari yalitumbukia mara mbili kwenye lile daraja. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali itakapojenga lile daraja ihakikishe inajenga daraja pana ambalo litaruhusu magari kupishana kwa sababu pale magari wakati mwingine inabidi gari moja lisimame lipishe lingine na wakati mwingine gari inafeli breki, kwa hiyo yanaweza yakaingiliana na kuweza kusababisha ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu viwanja vyetu vya ndege; Uwanja wa Ndege wa Tanga una mgogoro na wakazi wa maeneo ya karibu ya ule uwanja. Kwa hiyo tunaiomba Serikali ihakikishe ule mgogoro unamalizika ili uwanja uweze kupanuliwa. Uwanja wetu ni mkubwa, hatuna sababu yoyote ya kuhamishwa uwanja mwingine, lakini tatizo linakuja kuna mgogoro uliopo kati ya wananchi pamoja na shirika la ndege, kwa hiyo tunaomba hilo Serikali ilifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuomba Serikali ihakikishe kama inavyosema kuwa itahakikisha kuwa inaunganisha barabara kati ya wilaya na wilaya. Katika barabara ya Tanga kuelekea Jimbo la Mkinga lakini kwenye Tarafa ya Maramba, kwa kweli mpaka leo barabara ile haina lami na wakati wa mvua kunakuwa na matatizo magari yanateleza na wakati mwingine wananchi pia wanashindwa kupitia. Kwa hiyo tunaiomba Serikali ihakikishe barabara ile ya Tanga – Maramba iwekwe lami ambayo itafika mpaka Daluni itaunganisha mpaka Korogwe, kwa sababu biashara nyingi zinafanyika kule lakini unakuta barabara haina lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini sio kwa umuhimu, kuna mabango yale yanayowekwa ya alama mbalimbali za barabarani na watu wetu ambao sio waangalifu wala hawana uchungu na pesa za Serikali wanang’oa yale mabango kwa ajili ya kwenda kuuza vyuma chakavu. Naiomba Serikali ihakikishe katika zile alama za barabarani badala ya kuweka mabango yanayotumia mabati ihakikishe inaweka mabango yanayowekwa kwa kutumia zege kwa sababu mtu mpaka akaja akavunja zege itakuwa ni kazi kubwa, lakini yale mabati wanayang’oa na kwenda kuuza vyuma chakavu. Vilevile wito kwa wananchi, Watanzania wenzangu; tulinde miundombinu yetu ili tuweze kupata maendeleo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Serikali kutuletea ndege; ni kweli watu wanabeza lakini vitu vingine jamani, Waswahili wana methali wanasema: “Mengine ehee, mengine mmh”. Kwa hiyo, tunasema kuletewa ndege pia kumetusaidia tumerahisisha kazi ya kusafiri kwa muda mrefu. Mwezi uliopita nilitoka hapa Dodoma asubuhi nikaenda Dar es Salaam, tulikwenda kwenye kikao cha Kamati na tukaweza kuwahi na tumefika Dar es Salaam kutokana na kurekebishwa miundombinu ya Daraja la Mfugale tuliweza kutoka Airport mpaka tukafika jengo la bandari kule mjini haikuzidi nusu saa, tumefika pale na tukaweza kuwahi kikao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vitu vingine sio tubeze, tunashukuru tumerahisishiwa kuliko tungepanda Noah, ingebidi tuondoke siku moja kabla kuelekea Dar es Salaam na kwenda kuhudhuria hivyo vikao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu na kuweza kuchangia. Vilevile nikushukuru wewe kwa kuweza kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kuzungumzia afya na hali ya kisiasa. Kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa kujali afya za wananchi wake. Serikali imejitahidi imeweza kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali katika kila mkoa. Cha kusikitisha katika Jiji la Tanga, Kata ya Mianjani, wao wamejengewa zahanati na imemalizika toka mwaka jana lakini mpaka leo haijafunguliwa. Matokeo yake vibaka wanaingia kwenye zahanati ile wanaiba madirisha, milango na taa. Bahati nzuri Mwenyekiti wa Mtaa ametafuta walinzi na anawalipa ili kulinda ile zahanati. Kwa hiyo, naiomba Serikali ihakikishe kuwa zahanati hii inafunguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku nikisimama hapa nazungumzia kuhusu hospitali yangu ya Bombo. Hospitali ya Bombo ipo katika Jiji la Tanga, ndiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga. Cha kusikitisha hospitali ile haina lift, wanatumia mabaunsa, sasa mabaunsa wakati mwingine wanawadondosha wagonjwa. Hebu Serikali ifikirie kwa moyo mkunjufu kuipelekea hospitali ile lift na kuweza kuwasaidia wale wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujali afya zetu Serikali yetu inatilia mkazo sana kuhusu vijana wanaojihusisha na madawa ya kulevya. Kwa kweli Serikali imejitahidi sana kupunguza hili wimbi la wanaotumia madawa ya kulevya lakini binadamu si sawa na mnyama, binadamu ana kila mbinu ya kuweza kufanya kumshinda mnyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi vijana wetu wanapokosa hizi dawa za kulevya wamekuwa wezi wa zile taa zinazowashwa nyumbani zina unga mweupe unaotoka, wanachanganya na maji ya kuchanganyia sindano wanajichoma au wengine wanachukua valium wanasaga wanaweka kwenye sigara wanavuta. Kwa hiyo, Serikali bado ina kazi kubwa kwa hawa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa letu kwa sababu mimi nasema vijana ni taifa la leo. Sasa tukiwatupa hawa vijana, tukiwaacha wawe wamejihusisha kwenye madawa ya kulevya hatimaye tutajajikuta taifa ambalo linakosa nguvu kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumza kuhusu hali ya siasa. Tunajua mwaka huu 2019 tutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwakani tutakuwa na Uchaguzi Mkuu. Katika chaguzi unapotaka kupiga kura unatakiwa uwe na kitambulisho cha uraia na cha kupigia kura. Kuna baadhi ya vijana ambao wakati vitambulisho vya uraia vinatoka walikuwa hawajatimiza miaka 18, sasa hivi tayari wameshatimiza miaka 18 lakini wakati mwingine wanapovifuatilia vitambulisho vile vya uraia inakuwa ni tabu sana kuvipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, masikitiko yangu, mimi nashangaa sisi tunaambiwa tuwe na vitambulisho vya uraia au kitambulisho cha kupiga kura ili kiweze kutusaidia wakati wa kupiga kura. Nilikuja kushangaa wakati wa marudio ya Chaguzi za Madiwani katika Kata, Mkurugenzi wangu wa Jiji la Tanga alitoa Waraka kuwa ambaye atakuwa hana kitambulisho cha kupigia kura au cha uraia anaweza kutumia aidha passport au leseni ya udereva. Sasa kumbe kuna leseni za udereva, passport na kadhalika kuna haja gani ya kuwa na vitambulisho hivyo? Hii inasababisha kuleta faulo katika uchaguzi kwa sababu watu wanachukuliwa kutoka mitaa mingine na kuja kupiga kura pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, tunajua katika kituo cha kupigia kura kuna orodha ya wapiga kura, anayekuja pale anaenda kuangalia jina lake lakini cha kushangaza kituo kile kile cha kupigia kura Msimamizi wa Uchaguzi tena ana karatasi yake nyingine. Kwa hiyo, wale wanaokuja aidha na passport, leseni au birth certificate yake wanapiga kura na unajua hivi hivi kuwa hawa watu si wakazi wa eneo husika, wanachukuliwa kwa magari, wanaletwa wanapiga kura, hii inahatarisha pia amani ya nchi. Kwa hiyo, Serikali ihakikishe kuwa anayepiga kura ni yule anayefuata masharti ya kupiga kura. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka kuzungumzia kuhusu zao la michikichi. Tunashukuru Serikali imeipa kipaumbele zao la michikichi. Kweli michikichi ni zao ambalo litaleta faida sana kwa nchi yetu. Wenzetu Malaysia wameendelea kwa sababu ya zao la michikichi. Katika historia michikichi hiyo ya Malaysia nasikia ilitolewa huku huku Tanzania ikapelekwa kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali isielekeze kilimo cha michikichi katika Mkoa wa Kigoma peke yake ipeleke pia zao hili katika mikoa ambayo michikichi inaweza ikastawi ili watu waweze kuvuna mafuta ambapo tutakuwa tunatumia mafuta yetu sisi wenyewe kwa afya yetu kuliko kutumia mafuta ambayo yanatuathiri. Kuna mafuta tunayoletewa ambayo siyo mazuri, yana cholesterol ambayo inaweza ikatuletea matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba kama itawezekana Serikali iangalie sana wazee. Kuna wazee ambao wanaishi katika nyumba za wazee wasiojiweza. Nina hakika Serikali inatenga fungu kwa ajili ya kuwahudumia wazee wale lakini utakuta hali zao ni duni halafu wanarandaranda mitaani kuomba, ile ni aibu kwa taifa letu, kumbe wana vituo vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika vituo vyao wangekuwa wanaangaliwa kwa malazi, chakula na kwa afya zao kwa sababu utakuta kwenye vituo vingine vya kulelea wazee wale afya zao sio nzuri, sehemu wanazo lala sio nzuri, utakuta wengine godoro analolalia lina mikojo mpaka wanatoka funza kiasi cha kumkosesha raha yule mzee. Kwa hiyo, Serikali iangalie umuhimu na pia iwasisitize wale wanaohusika kuangalia wale wazee wawe wanapata chakula cha kutosha na tiba na pia wawazuie wasirande mitaani kwa sababu anapokuja mgeni akiona watu wanarandaranda mitaani kwa kweli ni aibu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nasema ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda napenda kuongelea kuhusu taratibu za kisheria. Moja, wananchi wapewe elimu kuhusu sheria mbalimbali, mfano, anakamatwa mwizi aidha anapigwa au anachomwa moto hadi kufa kabisa. Wananchi wanajichukulia sheria mikononi mwao, wananchi waeleweshwe umuhimu wa kulitumia Jeshi la Polisi kwa tatizo lolote linalotokea ikiwa mitaani, maofisini au kwenye mikusanyiko yoyote ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Jeshi la Polisi litoe mafunzo kwa Askari wake ambao wanamhukumu mtuhumiwa kabla hata kosa lililomtuhumu halijajulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama nyingi ni chakavu sana kiasi kwamba nyingine zinavuja au wakati mwingine mafaili yanakosa mahali pa kuhifadhiwa. Tunaiomba Serikali ikarabati mahakama ambazo zimechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazee wa Baraza wengine ni wala rushwa sana wala hawashughulikii kuleta haki katika kesi zinazopelekwa kwao, Serikali iangalie kuwaweka wazee wenye weledi katika mahakama ili haki itendeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa ya jinai, kuna wanaoshtakiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai, lakini baadhi walipelekwa mahakamani kesi imezungushwa kiasi mwisho wake mtuhumiwa anaachiwa huru. Serikali ione umuhimu wa kudhibiti wenye makosa ya jinai, wachukuliwe hatua zinazostahiki na kuwaachia huru wale wenye tuhuma ambazo ni za kubambikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuchangia hotuba iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu walimu. Zamani unapoingia chuoni unaambiwa ualimu ni wito kama Padre, Askofu au Shekhe. Hii iliwafanya wote wanaochukua mafunzo ya ualimu kuwa na nidhamu katika kazi yao. Sasa hivi tuna walimu ambao wengine hawastahili kuitwa au kuwa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu anatoka shuleni badala ya kurudi kule anakoishi moja kwa moja anakwenda kwenye vilabu vya pombe. Kule analewa kiasi kwamba anakuwa hajitambui hususan walimu wa kiume. Anapita mitaani anayumba watoto ambao wengine ni wanafunzi wake wanamsindikiza kwa kumzomea. Hii inashusha hadhi ya mwalimu na ualimu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee kuhusu walimu kupata mafunzo ya mara kwa mara (refresher courses) wakati wanapokuwa likizo. Hii itawasaidia walimu kwenda na wakati uliopo kwa maana pengine kuna mabadiliko ya mitaala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu utoro wa watoto kwa baadhi ya shule. Kuna sababu mbalimbali zinazosababisha utoro kwenye shule zetu. Moja, ni ukosefu wa walimu. Kuna baadhi ya shule hususan shule za vijijini utakuta kuna madarasa saba lakini walimu wanne tu, pale lazima kuwepo na utoro. Pili, watoto kwenda shuleni wakiwa na njaa kwani mtoto mwenye njaa hafundishiki. Tatu, ukosefu wa uzio katika shule kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Nashauri shule ziwe na walimu wa kutosha katika madarasa. Pia shule ziwe na utaratibu wa kuwapikia wanafunzi angalau uji ili waweze kukaa madarasani na kusikiliza mafundisho wanayopewa. Shule nyingi hazina wigo ni rahisi wanafunzi kutoroka na kupotea mitaani kwenda kuungana na wale ambao wana tabia mbaya. Kwa hiyo, Serikali ione umuhimu wa kujenga uzio katika shule zetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nashauri shule za msingi zifundishe masomo ya ufundi kama useremala, uashi, ushonaji, upakaji nyumba rangi na kadhalika. Serikali ianzishe karakana za kufundishia ufundi huo ili kuwaandaa wanafunzi wale wanaokosa nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari waweze kujiajiri au kujiendeleza katika vyuo vya VETA na kupata ujuzi mzuri na kujiajiri ili kupunguza wimbi la wazururaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbeye yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wengi wanalalamikia suala zima la ushuru. Wafanyabiashara wanapofikia mpakani kibali cha kuingiza bidhaa nchini imekuwa ni kero. Kuna kulipia ushuru wa TFDA, VAT na tozo nyingine nyingi. Mfano unaingiza pipi, biskuti, tende na kadhalika unatakiwa ulipie Sh.800,000 kwa kila bidhaa, mfano hizo bidhaa tatu itabidi ulipie Sh.2,400,000 kwa miaka mitano. Je, mfanyabiashara ambaye mtaji wake ni mdogo Serikali haioni kuwa inamkandamiza mfanyabiashara huyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta magari ya mizigo, mfano Kenya kuja Tanzania ni mengi kuliko Tanzania kwenda Kenya kwa vile kuingiza bidhaa Kenya kuna unafuu wa ushuru. Nashauri kama itawezekana masharti yalegezwe TFDA angalau mzigo utozwe kodi 1% kila mzigo unapoingizwa. Pia Soko la Afrika Mashariki wawe na kituo kimoja cha Bureau of Standards ambapo bidhaa zao zinalipwa ushuru baada ya kupimwa badala ya kazi hii kufanywa na TFDA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna magari maalum ya kubeba kemikali lakini magari haya yanawaumiza wafanyabiashara wadogo kutokana na tozo ilivyo kubwa. Mfano, kuna wafanyabiashara wadogowadogo ambao wanaingiza nchini office glue, inabidi mfanyabiashara awe na gari maalum lililosajiliwa hata kama ana carton 50 za office glue inahesabika kuwa ni kemikali, huwezi kubeba carton 50 katika gari la tani 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri uwepo utaratibu wa kusajili magari hata kuanzia tani moja. Hii ya kusajili tani 10 imelenga kwa wafanyabiashara wakubwa na kuwaacha wafanyabiashara wadogo kuendelea kubaki maskini. Naiomba Serikali iangalie suala hili la magari ya kubeba kemikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi kuzungumza machache kuhusu Wizara hii ya Habari, Utamaduni na Michezo. Kwanza, nitazungumzia kuhusu utamaduni. Watanzania tuna tamaduni zetu za asili, tamaduni ambazo zilikuwa zinatuonesha kama kweli sisi Watanzania, lakini sasa hivi hizi tamaduni zinapotoshwa sana kwa kuiga mambo ya kimagharibi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, pale Tanga kuna makabila katika Mkoa wa Tanga; kuna Wabondei, Wasambaa, Wazigua, Wadigo, tuseme ndio wenyeji wa Mkoa wa Tanga na wana ngoma zao nzuri tu; wanacheza ngoma zao vizuri, lakini utakuta ngoma hizi sasa hivi zinapotoshwa katika ile michezo yake ya kiasili.

Kwa mfano, katika Jiji la Tanga kuna ngoma inaitwa Baikoko. Yaani ukitaja ngoma ya asili ya Tanga ni Baikoko. Nataka kuwaambia ngoma ya Tanga ya asili siyo Baikoko, ile Baikoko ni ngoma ambayo inapotosha sana watoto na kizazi hiki tulichonacho kwa sababu ile ngoma ni matusi matupu mwanzo mwisho. Matusi na watu kukatika katika, yaani mtu kukatakata mauno ambayo hayana maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi mtu ukimwambia utamaduni anaona labda kusimama na kukatikakatika inakuwa ndiyo utamaduni. Kumbe akiimba ule wimbo ukiwa una ujumbe fulani utawafikia watu, watu wakauelewa ule ujumbe, ndio utamaduni wetu.

Mheshimiwa Spika, pia mfano mwingine kuna ngoma ile ya Hiyari ya Moyo, nilipokuwa mdogo, tulikuwa tunakwenda Tanga kuangalia ile ngoma. Mimi nilikuwa naona ngoma ya Hiyari ya Moyo wanacheza tu wanatingisha mabega, lakini sasa hivi mpaka mtu anakatika kabisa mpaka…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, kama mtu anaangalia yaani ile ngoma…

SPIKA: Mheshimiwa Nuru pokea taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa mzungumzaji, huu ni utamaduni wa kukatika viuno, sasa nashangaa anasema wanakatika viuno. Hivi tuulizane humu ndani ya Bunge, kuna watu wasiokatika viuno?

SPIKA: Mheshimiwa Nuru vipi, mimi sijamwelewa lakini labda umemwelewa.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Aaa.

SPIKA: Haya endelea Mheshimiwa Nuru labda mwenzangu umemwelewa, pokea taarifa.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, taarifa siipokei kwa sababu Mheshimiwa Keissy naye anapenda kujipitisha pitisha, samahani kama panya, panya akitaka kutajwa ajipitisha kwa watu.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee na mchango wangu. Kwa hiyo, mimi ninachosema, hebu tujaribu turudi kwenye tamaduni zetu…

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Turudi kwenye tamaduni zetu za kizamani, tufanye…

SPIKA: Samahani Mheshimiwa Nuru, taarifa nyingine unapata. Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla tafadhali.

T A A R I F A

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge anayesema hapa Bungeni kwamba utamaduni sio kitu static, utamaduni ni dynamic unabadilika kutokana na nyakati. Kwa hivyo, utamaduni wa watu wa Tanga hata mimi bibi yangu anatokea Tanga, Machui, umeendelea kubadilika zama na zama ndio maana leo hii hata muziki upo unaoitwa muziki wa kizazi kipya ambao wanaimba akina Sugu na Profesa Jay.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, utamaduni unabadilika, hata lugha ya Kiswahili ukitaka kutafuta lugha ya Kiswahili ni nini imetoka wapi, ni lugha imeibuka zama hizi za miaka hii ya 1900, lakini haikuwepo, sio lugha ya asili. Kulikuwa na makabila zaidi ya 128, lakini yanaunganishwa na utamaduni mmoja wa lugha ya Kiswahili. Kwa hivyo, napenda afahamu kwamba utamaduni sio static ni kitu dynamic.

SPIKA: Endelea Mheshimiwa, anakwambia tu mambo yanabadilika, hayo unayoyaona leo ndio yenyewe.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, asante na ndio kanipeleka mbele ngoja niende mbele halafu nitarudi nyuma, ndio hayo nilikuwa mengine nataka kuchangia. Sasa hivi Watanzania tunachanganya lugha ya Kiingereza na Kiswahili, tunatakiwa tukinyooka kwenye Kiswahili twende kwenye Kiswahili tu tusichanganye lugha Kiswahili na Kiingereza hapana, tunapoteza uzalendo wetu na Utanzania wetu. Tuzungumze lugha moja tu, sisi tunasema tunazungumza Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa, tusichanganye maneno.

SPIKA: Anasema tusichanganye changanye maneno Waheshimiwa, unazungumza, mara mother tongue sasa inakuwa tabu. (Kicheko)

Mheshimiwa Nuru endelea.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Vile vile nikizungumzia kuhusu muziki wa kizazi kipya, kweli tunaupenda muziki wa kizazi kipya, lakini na huo muziki wa kizazi kipya tuuangalie je, ukoje? Je, Wizara kama Wizara au BASATA je, inazihakiki zile nyimbo? Mfano tukiimba sijui nyege nyege Nyegezi kwetu Mwanza Nyegenzi, wimbo kama huu…

SPIKA: Mheshimiwa Nuru unavunja Kanuni. (Kicheko)

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, samahani.

SPIKA: Endelea Mheshimiwa.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Kwa hiyo, tunatakiwa tulete nyimbo ambazo zina mantiki, zinapendeza mpaka anayezisikia pia pale alipo hata kama alikuwa anaandika atachezesha hata mkono kuona kuwa ule wimbo umemwingia. Kwa hiyo, nyimbo tunazoziimba tunataka nyimbo za kizazi kipya lakini nyimbo ziwe nyimbo zenye mafundisho mazuri sio nyimbo ambazo zinaleta maana mbaya mpaka watoto wanaozisikiliza haziwasaidii chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani kulikuwa na nyimbo zenye mafunzo, tulikuwa na akina Mwinamila walikuwa wakiimba mpango wa pili wa maendeleo, unasema, kuleni kuku, mayai, mboga, samaki, maziwa; kuleni chakula bora cha kujenga mwili na kulala kwenye nyumba bora, si ndio? Tulikuwa tunafundishwa kuwa tunatakiwa tule chakula na wakati huo huo tulale kwenye nyumba ambazo ni bora, lakini leo nani kamwaga pombe yangu, nauliza. Sasa hiyo jamani kweli tutakuwa, kwa hiyo tutakuwa hapo hatufanyi… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Sugu uende ukawaeleze wenzako, huu ndio ujumbe, ukaeleze kundi lako huko. (Kicheko)

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, Ninachoomba twendeni turudi kwenye tamaduni zetu za asili japokuwa kuna nyimbo za kizazi kipya, lakini zile nyimbo za kizazi kipya ziwe na nyimbo ambazo maudhui yake yanalenga kuwajenga wale wanaozisikiliza.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuzungumzia kuhusu Serikali kuona umuhimu tuwe na shule zetu maalum za wanafunzi wenye vipaji maalum yaani tuwe na shule ambazo tutawapeleka kweli wanasoma masomo mengine lakini wakati huo huo anaendelezwa kimichezo kama ni bondia, mchezaji mpira, labda ni muigizaji, vyovyote inavyokuwa vile.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawajengea ile shule na wanakwenda pale, kwa hiyo wakimaliza pale, tunapata wanafunzi ambao ni cream kwa kuwapeleka mahali na kuwa wanashiriki katika kuliinua Taifa letu kwa sababu michezo ni afya na vilevile michezo ni ajira.

Kwa hiyo, tukipata watu namna ile tunaweza tukaendelea, kama wenzetu Nigeria walivyowekeza, akina Kanu wale walikuwa wapo kwenye shule za vipaji maalum mpaka leo tumeweza kupata wachezaji wazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umuhimu wake, Mheshimiwa Naibu Waziri alikwenda Tanga kuweka jiwe la msingi katika eneo ambalo litajengwa kiwanja kikubwa sana cha michezo. Ninachoomba sasa hivi Serikali angalau ijaribu kujenga uzio kwa sababu wananchi wanajaribu kusogea na mwisho ule uwanja utamezwa, utakuja kukuta wengine watakwambia wanadai fidia walipwe ili waweze kupisha ujenzi wa kiwanja. Kiwanja kile kama kitajengwa kitakuwa kizuri na kitapendeza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Nuru.

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na napenda kuzungumzia kuhusu ujenzi wa barabara kama Serikali ilivyosema kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam nimejaribu kujenga barabara, lakini sasa barabara hizo ambazo zinatokea Ardhi - Makongo - Goba, mpaka kufika Kimara na Mbezi kwa kweli kwenye kitabu imeeleza kwamba barabara ya kutoka Ardhi mpaka Makongo tayari imeshakamilika kwa kiwango cha lami. Napenda kuiarifu Serikali kwamba barabara hii bado haijakamilika kwa kiwango cha lami, bado barabara hii ni changarawe kutoka Ardhi hadi Makongo, kwa hiyo naiomba Serikali ihakikishe hizi kilometa nne zinazotoka Ardhi mpaka Makongo zijengwe katika kiwango cha lami ili kupunguza msongamano kwa sababu eneo la kutoka Ardhi mpaka Makongo kuna kuwa na msongamano na magari kutokana na mashimo mashimo.

Mheshimiwa Spika, nikizungumzia kuhusu barabara ya Tanga - Pangani, Tanga - Pangani siku zote tunaambiwa itajengwa kwa kiwango cha lami, lakini hapa sioni, sasa hivi ninaona kwenye kitabu imeandikwa kwamba tutajengwa kiwango cha changarawe kuanzia Mabanda ya Papa hadi Boza Buyuni, sasa Mabanda ya Papa pale ni katikati ya jiji pale, kuna lami mpaka sehemu ya Mwang’ombe ambayo ni kilometa nne kutoka Mabanda ya Papa, kwa hiyo, pale pana lami, changarawe inaanzia pale Mabanda ya Papa mpaka inafika huko Boza Buyuni. Sasa Serikali iangalie uwezekano wa kuifanya barabara ile iwe katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenykiti, na kwa taarifa yenu ni kwamba sasa hivi mvua zinazonyesha barabara kutoka Pangani mpaka Tanga haipitiki tena, inabidi sasa hivi wapitie eneo jingine linaloitwa Tongoni, wapiti Tongoni waende Lumbwa waingie Kisima Tui - Pongwe ndiyo warudi tena Tanga kwa sababu kuna daraja linaitwa Neema limearibika, gari haziwezi kupita. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa hizi barabara ikamilike kwa kiwango cha lami badala ya kutengeneza tena changarawe maana yake hapa inaonesha kuwa barabara itawekwa changarawe kuanzia Mabanda Papa hadi Buyuni Boza.

Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kuzungumzia kuhusu mabasi haya ya mwendokasi. Mabasi ya mwendokasi yametusaidia sana lakini yard ya mwendokasi kwa kweli inasikitisha. Imejengwa mahali ambapo mvua zikinyesha panajaa maji kiasi cha kuharibu miundombinu yote. Kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano wa kujenga tena upya na kufanya drainage system ili maji yaweze kupita chini na ile yard ikaweza kutumika au vinginevyo ile yard ya mwendokasi ihamishwe pale iwekwe mahali pengine, kwa sababu maji pale jangwani yanajaa kiasi cha kuyafanya mabasi tena hayafanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikizungumzia kuhusu reli ya Tanga hadi Arusha, kwa kweli reli hiyo imeshaanzwa kutengenezwa Tanga hadi Same. Cha kusikitisha ile reli pia inatakiwa ifanyiwe usafi. Kwa sababu kuna nyasi zimeota. Sasa mtu mwingine anaweza kung’oa reli, bila mtu kujua reli pale imeng’olewa. Kwa hiyo, Serikali ihakikishe kwamba maeneo yale ambayo tayari yameshatengenezwa na ile reli vile vile inakuwa safi, inalimiwa vizuri ili kama kutakuwa na uharibifu wowote utakaotokea inaweza ikajua.

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kuzungumzia kuhusu viwanja vya ndege. Kwa kweli Serikali inajitahidi kujenga viwanja mbalimbali vya ndege lakini tatizo linakuja, kuna baadhi ya viwanja vya ndege vinakosa taa na kusababisha usiku ndege haziwezi kutua. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika viwanja vyote vile ambavyo havina taa za ndege ihakikishe taa zinawekwa ili kuwezesha ndege kutua wakati wa usiku.

Mheshimiwa Spika, mwisho...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Mchango wangu nitajikita juu ya utendaji kazi wa wanajeshi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanajeshi wameonesha uadilifu katika utendaji kazi zao katika maeneo mbalimbali. Tukichukulia uadilifu na uharaka walioonesha katika ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na ofisi za Mji Mpya wa Serikali, Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa tender za ujenzi wa nyumba na ofisi za Serikali kutokana na ubora wa majengo yao wanayoyajenga na pia uharaka wa kuyakamilisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana ambao wapo katika Kambi za JKT vikosi mbalimbali ambao wako tayari kutekeleza litakaloamrishwa. Je, kwa nini badala ya kuweka walinzi katika aidha Ofisi za Serikali, majumbani na nyumba za watu binafsi kuajiri walinzi ambao siyo waaminifu na wengine hawajulikani makazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini tusitumie vijana wetu wa JKT kufanya kazi hizo ili kuinua vipato vyao na pia Serikali kupata fedha? Mfano hawa Security Groups wanapolinda aidha nyumbani wanadai shilingi 300,000 kwa mwezi, yule mlinzi analipwa shilingi 60,000, sasa hii inapelekea mlinzi kutokuwa mwadilifu katika kazi yake. JKT wakipewa hii tender watalinda kwa uadilifu na vilevile mfano hizo shilingi 300,000 anaweza akapewa mlinzi shilingi 150,000 na 150,000 ikaingia katika mfuko wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu wanajeshi wetu, wanajeshi hawa wanaendelea kuonesha uaminifu wao kwa nchi na Serikali kwa ujumla. Basi Serikali ione umuhimu wa kuwapa stahili zao vilevile na upandishwaji wa vyeo. Hawa ni watu muhimu katika ulinzi wa amani ya nchi yetu, lazima tuwathamini na kuonesha umuhimu wa Serikali kwao, tusiwakatishe tamaa. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nchi ya amani na utulivu wakati kuna nchi nyingine tuko jirani nazo hawalali wala kufanya kazi kwa amani kutokana na vurugu za mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaenzi wanajeshi wetu na tuwathamini kwa kazi zao nzito wanazofanya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na afya aliyonipa. Napenda kuipongeza Wizara kwa kufungua maduka mbalimbali ya kuuza madini.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha ufunguzi wa maduka haya kitasaidia kupatikana madini yetu kwa wingi badala ya madini yetu kusafirishwa kwa njia za panya kwenda nje. Vilevile ufunguzi wa maduka haya utawasaidia wachimbaji wadogo kuweza kuuza madini yao na kupata fedha katika njia za usalama badala ya hapo awali baadhi walikuwa wanadhulumiwa haki zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wachimbaji wadogo wadogo, wahamasishwe kuwa na vifaa vya uchimbaji siyo wachimbe kiholela. Wachimbaji hawa wadogo wahamasishwe kuuza madini yao katika masoko yaliyoanzishwa ili kuepuka kudhulumiwa haki zao. Serikali ihakikishe wenye maduka ya kuuza vitu vya dhahabu (sonara) wasichanganye madini wakati wanapotengeneza vitu hivyo mfano pete, vipuli (hereni), mikufu, vikuku na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.