Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rehema Juma Migilla (7 total)

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mzuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna tatizo limejitokeza, kuna Waraka unasema walimu wa arts ambao wamezidi katika shule za sekondari wanahamishiwa shule za msingi. Huu uhamisho unakuwaje ilhali Rais wetu alisema walimu wasihamishwe mpaka pale fungu lao litakapopatikana.
Je, hao walimu wameshaandaliwa mafao yao ya uhamisho ili waende kwenye vituo vyao vipya huku tayari Wizara imeshasema mpaka itakapofikia tarehe 15 Februari walimu hawa wawe wamefika vituoni kwao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kujua, huu uhamisho wa kuwatoa walimu wa arts kutoka sekondari kuwapeleka primary unaweza kuathiri ufundishaji wa wanafunzi wa huko primary. Je, Serikali imeandaa induction course kwa ajili ya walimu hawa ili waweze ku-coup na ufundishaji wa walimu wa primary? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): MheshimiwaMwenyekiti, swali la kwanza kwa wale wanaohusika ambao wamepata Waraka Rasmi wakiusoma vizuri watagundua kwamba maelekezo yaliyomo katika Waraka ule ni kwamba uhamisho unafanyika kutoka kwenye shule ya sekondari kwenda kwenye shule ya msingi ambayo iko karibu na eneo hilo, siyo kumtoa kwenye Wilaya moja kumpeleka Wilaya nyingine. Uhamisho ule ni wa ndani ya kata kwa hiyo hauna gharama za uhamisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ule uhamisho kutoka shule za sekondari kwenda primary umezingatia kwanza kipaumbele kwa wale walimu ambao walijiendeleza, zamani walikuwa walimu wa shule ya msingi wakajiendeleza wakapata diploma na degree hatimaye wakahamishiwa katika shule za sekondari.
Kwa hiyo, kuwarejesha kwenye shule za msingi ambazo wana uzoefu nazo hakuhitaji induction course ya aina yoyote. Kwa hiyo, hicho ndiyo kipaumbele ambacho kimewekwa na kimezingatia walimu wa diploma na walimu wa degree ya kwanza. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa inayoongoza katika uzalishaji wa maembe. Mpaka jina la Unyanyembe likapatikana ni kutokana na uzalishaji wa hizo embe, lakini cha ajabu mkoa huo wa Tabora mpaka leo hauna kiwanda cha usindikaji wa maembe, hali inayopelekea maembe yanazagaa kila mahali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niiulize Serikali ni kwanini haitaki kujenga Kiwanda cha Usindikaji wa Maembe Tabora?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nirejee tena nazidi kuhamasisha Watanzania pamoja na Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwahamasisha wawekezaji katika maeneo hayo. Kwa mfano hapa Dodoma kuna Kiwanda kizuri cha Matobolo wanasindika maembe wanakausha na maembe hayo yanaweza kutumika kwa muda mrefu. Kwa hiyo, sisi tusisubiri kiwanda kije chenyewe ni lazima tuwahamasishe wadau mbalimbali hata sisi wenyewe tuweze kuwekeza ili kuhakikisha kuwa maembe hayo yanakaa muda mrefu.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali sikivu sana kwa wananchi wake hali iliyopelekea mpaka imewarudisha kazini watumishi wa darasa la saba. Swali langu, je, ni lini sasa Serikali itatoa tamko la kuwarudisha masomoni wasichana wote waliopata ujauzito na kuthibitishwa na Mahakama kuwa walibakwa kwani kwa kutowarudisha ni kuwanyima haki yao ya kupata elimu lakini vilevile ni kuwapotezea ndoto zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hata sisi Serikali kwa kweli hatupendi na hatutaki kusikia vitendo vya uonevu dhidi watoto wa kike, kwa sasa mfumo wetu wa elimu umepangwa katika namna ya kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao wanapata ujauzito wanapata fursa ya kusoma lakini nje ya mfumo rasmi.
Kwa hiyo, kuna fursa nyingine nyingi za kusoma kama nilivyosema katika swali langu la msingi kwa kupitia Elimu ya Watu Wazima na Vyuo vya Ufundi. Serikali haitarajii na naomba niweke wazi kuwarudisha wanafunzi ambao wamepata ujauzito kwa njia yoyote ile. Ni kwa sababu tukifanya hivyo maana yake tunahalalisha na kuhamasisha ngono shuleni wakati mila na sheria zetu haziruhusu ngono katika ngazi hizo maana yake shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kubakwa, tunaposema kwamba hawaruhusiwi kuendelea na elimu katika mfumo rasmi siyo kwamba ni adhabu kwa kujifungua, tunachochukulia ni kwamba tayari ana mtoto na hivyo tukifanya hivyo tunakuwa tumefungulia milango ya vitendo kama hivyo kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kuna fursa zingine ambazo watoto wale wanaweza kutumia kupata elimu, zipo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba suala la uzazi wa mpango ni makubaliano ya wanandoa kuhusu idadi ya watoto wanaowataka, lini wawazae na kwa wakati gani. Sasa, je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kuibadilisha hii sheria ili kuwawezesha wanandoa kupata watoto wanaowataka kutoka miaka mitatu hadi miwili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa kuna tabia kwa sekta binafsi kuwa hawawapi nafasi ya likizo wafanyakazi wao kutokana na masharti mbalimbali. Sasa, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba hawa wafanyakazi wa Sekta Binafsi nao wenyewe wanapata likizo badala ya kunyimwa mshahara ili akapumzike au aamue apumzike akose mshahara; Serikali ina mpango gani kwa wafanyakazi hawa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uzazi wa mpango sisi Watanzania tunaishi katika jamii, sisi ni wamoja. Sasa tumetafuta utaratibu gani unaweza kutuweka sisi pamoja; mwingine anataka azae kila mwaka, mwingine anataka azae kila baada ya mwaka mmoja na nusu, mwingine anataka baada ya miaka minne, baada ya mjadala mrefu Bunge hili likaweka utaratibu kwamba miaka mitatu inatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusisitiza; sheria hii kwanza inalinda afya ya mtoto mwenyewe kwamba unamwacha akue, lakini mhurumie na huyu unayemzalisha kila mwaka na yeye naye anahitaji kupumzika. Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba, hii sera Serikali imeweka kwa nia moja; kulinda afya ya mtoto apate kukomaa vizuri kabla hujamtafuta mwingine, lakini pia huyo mama naye anahitaji kupumzika, kumzalisha kila mwaka ukasema ni muafaka kati yetu sisi; hao wanandoa wanaishi katika jamii ambayo ina sheria, taratibu na kanuni na hiyo jamii inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sekta binafsi kwamba hawawapi nafasi; hizi labour laws, sheria za masuala ya kazi ni za nchi nzima. Kwa hiyo zinatakiwa ziheshimiwe na watu wote; binafsi na wale waliopo Serikalini na Mashirika ya Umma. Pale inapotokea kwamba mtu kanyimwa likizo ya uzazi ati kwa sababu anafanya kwenye shirika binafsi, Waziri wa Utumishi ajulishwe na ntachukua hatua stahiki.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuongeza swali dogo la nyongeza. Kwanza napenda nimpongeze Naibu Waziri wa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku kwa Mkoa wa Tabora na mikoa mingine inayolima tumbaku, tumbaku ni maisha, tumbaku ni uchumi, lakini tumbaku ni maisha yetu. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kwa kuwa kasi ya upandaji wa miti haiendani sambamba na upandaji na tunaona kabisa zoezi hili limefeli, nataka niulize Serikali, ina mpango gani kwa sasa kuzihakikishia hizi AMCOS ambazo zina jukumu la upandaji wa miti ili ziweze kutimiza Sheria ya Namba 24 ya mwaka 2001, ambayo inaitaka kila AMCOS kabla ya kusajiliwa iwe na shamba la miti ambayo itawatosha idadi ya wakulima wake kwa mwaka mzima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, napenda kufahamu; kwa kuwa Bodi ya Tumbaku ndiyo yenye jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote za tumbaku ikiwa ni sambamba na uhifadhi wa mazingira inashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na changamoto mbalimbali, je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha hii Bodi ya Tumbaku kuondokana na changamoto za magari, nyumba na ofisi za wafanyakazi ili iweze kufanya kazi kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini kabisa na yeye ni mkulima wa zao la tumbaku kule Tabora na amekuwa akilima hiyo tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika maswali yake mawili ya nyongeza, kuhusu suala AMCOS na wakulima ni kwamba sisi kwenye ile Tobacco Industrial Act. No. 24 ya Mwaka 2001 wakulima wetu wote pamoja na hizo AMCOS na mambo mengine ambayo yanaelezea katika Sheria hiyo Namba 24 ya Mwaka 2001, ni kuhakikisha kwamba, wakulima wote pamoja na hizo AMCOS wanaposajiliwa kuhakikisha kwamba mashamba yao yanaendana na miti isiyopungua 250. Vile vile kuhakikisha kabisa kwamba wanatumia yale mabani ya kisasa na si yale mabani ya zamani ambayo yalikuwa yanatumia magogo kama ilivyokuwa kule mwanzo. Hii yote ni katika kuhakikisha kwamba, tunatunza na kulinda hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili la nyongeza, kuhusu Bodi yetu ya Tumbaku; ni kweli sisi kama Serikali tunahakikisha kabisa kwamba tunaimarisha na tunaboresha hizi bodi zetu zote. Naomba niziase bodi zetu zote kwamba zifanye kazi kwa umahiri na kwa ubunifu zaidi, na vile vile waweze kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatumia zile fursa mbalimbali za kilimo zilizopo katika kuboresha mazao yao, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri, lakini napenda niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata athari kubwa sana ya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti ambayo inatumika zaidi kwa ajili ya mkaa na kuni. Hali hiyo
imepelekea Mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kupata mvua ya kusuasua ambayo ndio inatumika zaidi kwa kilimo. Sasa swali langu, je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba pamoja na athari zote hizo zilizopatikana wananchi wataendelea na shughuli za kilimo kama kawaida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na Serikali kuyaingiza maeneo ya Imalamihayo, Inala, Bonde la Kakulungu na Magoweko katika mpango wa umwagiliaji, lakini mpaka leo maeneo haya bado hayajaanza kufanya kazi. Sasa tunataka tupate majibu ya Serikali ni lini maeneo haya na skimu hizi zitaanza kufanya kazi kwani mpango huu unaonesha umeanza kazi tangu mwaka 2018?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekit, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rehema Juma Migilla kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua mikakati ya Serikali kwa ajili ya kuendeleza kilimokwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hapo Tabora. Sisi kama Serikali cha kwanza tulichokifanya, mkakati mkubwa tuliokuwa nao ambao badala ya kutegemea fedha za kibajeti, lakini pia badala ya kusubiri fedha za washirika wa maendeleo kutoka nje ya nchi tumeielekeza Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo kuja kwenye halmashauri mbalimbali nchini kukaa nao na kubainisha yale maeneo yanayofaa kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kubainisha kujua mahitaji yenu wataenda kuingia mikopo kwa dhamana ya halmashauri na sisi Serikali tutawadhamini zaidi ya asilimia 80 ili kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo huu Mkoa wa Tabora ili wakulima waendelee kulima cha kisasa cha uhakika na chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anasema, ni lini kwamba miradi hi tuliyiotaja kwenye jibu letu la msingi kwamba itaanza kufanya kazi. Hii miradi itaanza kufanya kazi muda mfupi ujao baada ya upatikanaji wa fedha za kibajeti na kama nilivyosema kwenye jibu la awali chanzo kingine cha pesa ni kupitia mikopo kupitia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naona majibu haya yamejibiwa kisiasa kuliko uhalisia wenyewe ulioko huko kwa waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio hai kabisa bodaboda hawa wamejiajiri wenyewe na wanafanya kazi katika mazingira magumu na wamekuwa wakisumbuliwa sana na polisi especially hawa PT. Wanawakamata na wakishawakamata hata uchunguzi wa kina haufanyiki na sometimes wanawabambikizia makosa. Wanapowabambikizia makosa wanawaaambia watoe hela, wasipotoa zile hela pikipiki zao zinapelekwa polisi. Zikifika polisi, pindi wanapotaka kuzichukua wanakuta baadhi ya vitu kama betri, mafuta na hata wakati mwingine wanakuta hadi gamba zimebadilishwa na tunaelewa kabisa polisi ni mahali ambapo pana usalama wa kutosha na hakuna mtu ambae anaweza akaenda kubadilisha kitu chochote pasipo kukamatwa.

Mheshimiwa Spika, sasa je, Mheshimiwa Waziri, unataka kutuambia wanaohusika na hili zoezi la kuchomoa vitu au vielelezo ni Polisi au akina nani na tunajua kabisa pale ni mahali salama?

Mheshimiwa Spika, swali la pili nataka kufahamu pia pamekuwa na mrundikano mkubwa sana wa pikipiki katika vituo vya polisi na ukizingatia chanzo cha kukamatwa kwa hizi pikipiki na mrundikano huo ni hawa hawa polisi wanazikamata na kuwataka hao watu walipe…

SPIKA: Sasa swali.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: … swali langu; Je, Serikali ina mpango gani kuwarudishia hawa watu pikipiki zao ambapo kwa kuendelea kukaa pale zinaidi kuharibika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Rehema, Mheshimiwa Mbunge ambaye kwa muda mfupi tangu alipoingia Bungeni ni Mbunge machachari na nimekuwa nikimpa ushirikiano kwa masuala ya Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Spika, mwanzoni nilikuwa najiuliza kwanini watu wanaoagiza magari bandarini vitu vinachomolewa au watu kwenye viwanda vya ndege kunakuwa na pilferage lakini baadaye nikaja kushangaa hata kwenye vituo vya polisi vitu vichomolewe nikaona ni jambo ambalo linashangaza sana.

Mheshimiwa Spika, nilichofanya, kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwenye ilani hii ya CCM Ibara ya Nne, CCM imeamua kwamba katika changamoto zile nne za Ibara ya 4 za kupunguza umaskini, za kutatua tatizo la ajira tena tukataja bayana vijana, nataka nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba bodaboda ambazo nimetoa maelekezo ili wapambane na umaskini na tatizo la ajira ni bodaboda za makundi manne tu zitakazochukuliwa kupelekwa kituo cha polisi na hata kwenye bajeti hapa nilisema.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kundi la kwanza, ni bodaboda ambayo imehusika kwenye uhalifu, kwa sababu bodaboda zinatumika kufanyia uhalifu. Hiyo ikikamatwa itapelekwa kituoni. Kundi la pili ni bodaboda ambayo inahusika na kesi na kesi yenyewe, moja ni kama bodaboda hiyo imehusika kwenye ajali ya barabarani ama bodaboda iliyoibiwa sasa katika recovery ikawa imekamatwa, ni kielelezo. Kundi la tatu na la mwisho ni bodaboda ambayo haina mwenyewe sisi (found and unclaimed property) sasa polisi kwa sababu wanalinda mali za raia wataichukua ikae kituo cha polisi, ikipata mwenyewe ichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, boda boda zingine zozote ambazo hazipo kwenye kundi hilo, sijui huyu hana helmet, huyu hana side mirror, huyu amepakia mshkaki, hakuna bodaboda itakayokamatwa kupelekwa kwenye kituo cha polisi. Nimewapata utaratibu wa kuwapa siku saba kama ni faini watalipa na nimeelekeza bodaboda ambazo ziko kwenye makundi matatu ztakazopelekwa kituo cha polisi na zenyewe wataandikiwa hati inayoonesha vitu ambavyo viko kwenye bodaboda ile ili atakapokuja huyu mtu a-cross check na hati aliyopewa ili yule aliyechukua kama kuna upotevu aweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi bodaboda nchi nzima wanakula raha mstarehe, wanajinafasi. Kama Tabora suala hilo bado linaendelea, Mheshimiwa Rehema nikuhakikishie itakapofika jioni kama Tabora pale kuna pikipiki ambayo haiko kwenye makundi hayo, ama zao ama zangu. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)