Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rehema Juma Migilla (5 total)

MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaondoa vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kwa hiari yao kutokana na sababu mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kufuata wenza wao au ugonjwa. Hata hivyo, katika kuhamisha mwalimu, Serikali inazingatia ikama ili kutoathiri taaluma kwa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kufundishwa masomo yote kwa mujibu wa mitaala ya elimu iliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hitaji hilo ndiyo husababisha katika baadhi ya maeneo walimu kusubiri apatikane mwalimu mbadala kwanza kabla ya kutolewa kibali cha uhamisho ili wanafunzi wasikose haki yao ya kusoma masomo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba uhamisho wa mtumishi wa umma ni haki yake endapo atazingatia utaratibu uliowekwa. Ndiyo maana kuanzia Julai, 2017 hadi sasa Serikali imetoa vibali vya uhamisho kwa walimu 2,755 nchi nzima. Aidha, taratibu za kutoa vibali vya uhamisho kwa walimu wengine walioomba uhamisho zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwaelekeza walimu nchi nzima na watumishi wengine wote kuzingatia utaratibu na waache kutumia viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kuwaombea uhamisho. (Kicheko)
MHE. NURU A. BAFADHILI (K.n.y. MHE. REHEMA J. MIGILLA) aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haitaki kujenga Hospitali ya Wilaya ya Tabora Mjini baada ya Hospitali ya Wilaya kupewa hadhi ya Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mhemishimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali Na. 96 la tarehe 18/4/2018 lilioulizwa na Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, Serikali imeanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Tabora Mjini tangu tarehe 19 Oktoba, 2015 kwa kuanza na jengo la OPD kwa gharama ya shilingi milioni 150 chini ya Mkandarasi HERU Construction Company Limited ambapo hadi sasa sehemu ya msingi, nguzo, ngazi na slabu vimekamilika kwa asilimia 100. Mkandarasi ameshalipwa jumla ya shilingi milioni 145.7 kutokana na fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Manispaa ya Tabora imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa jengo la OPD katika hospitali hiyo. Mkakati wa Serikali ni kuimarisha Vituo vya Afya 513 nchi nzima ili viweze kutoa huduma za dharura pamoja na kujenga Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kuweka kipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, ndiyo maana Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni 2.6 Mkoa wa Tabora, kwa ajili ya ukarabati wa vituo sita vya Afya katika Wilaya za Nzega, Tabora-Uyui, Igunga, Kaliua na Urambo kupitia awamu ya kwanza na ya pili ya miradi ya afya iliyoanza kutekelezwa Septemba, 2017. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga shilingi bilioni 101 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya 67 nchi nzima ambapo mbili kati ya hizo zipo katika Wilaya ya Uyui na Sikonge, Mkoani Tabora.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Tumbaku inayolimwa Mkoani Tabora inachangia pato kubwa la Taifa:-
Je, Serikali ipo tayari kuboresha mazingira ya kilimo hicho ili kisiathiri mazingira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la tumbaku hulimwa katika Mikoa 11 ambayo ni Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Mara, Songwe na Morogoro. Uzalishaji wa zao hili husimamiwa na Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania na kwa kufuata taratibu na kanuni za kilimo kinachojali hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora unazalisha tumbaku nyingi zaidi kuliko mikoa mingine inayozalisha tumbaku hapa nchini, na hivyo kuchangia sehemu kubwa ya Pato la Taifa. Aidha, katika msimu wa 2015/2016 Mkoa wa Tabora pekee ulizalisha asilimia 47 ya tumbaku yote iliyozalishwa nchini na asilimia 48 kwa ule msimu wa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania inasimamia taratibu na kanuni zote ambazo zinahamasisha kilimo bora cha tumbaku na kinachozingatia hifadhi ya mazingira. Pamoja na mambo mengine, Kanuni zinaelekeza kila mkulima wa tumbaku asajiliwe na awe na eneo la kupanda miti isiyopungua 250 au zaidi kwa kila hekta moja ya tumbaku anayolima.
Miti inayopandwa pamoja na kuwa chanzo cha nishati ya kukausha tumbaku pia husaidia kuhifadhi mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Tumbaku Tanzania imeendelea kuhamasisha na kusimamia ubadilishaji wa mabani ya kukaushia tumbaku kutoka ya awali yanayotumia magogo ya miti na kutumia mabani ya kisasa ambayo yameongezeka kutoka mabani 101,982 mwaka 2014/2015 na kufikia mabani 172,405 mwaka 2016/2017. Aidha, mabani ya zamani yamepungua kutoka mabani 192,975 mwaka 2014/2015 hadi mabani 135,410 mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kuhamasisha wakulima wote wa tumbaku nchini kutumia mabani ya kisasa kuanzia msimu wa mwaka 2018/2019 ikiwa ni pamoja na kuendeleza juhudi za kutafuta nishati mbadala. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-

Manispaa ya Tabora ipo kwenye mradi mkubwa wa maji toka Ziwa Victoria na Bwawa kubwa la Igombe linalotumika kuhudumia Wakazi wa Tabora Manispaa litakuwa halina matumizi tena.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuliweka Bwawa la Igombe kwenye scheme za umwagiliaji ili wakazi wa Tabora waendeshe Kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kupanga matumizi ya maji kutoka katika chanzo, utunzaji wa mazingira na matumizi ya kijamii hupewa umuhimu zaidi kabla ya matumizi mengine. Ujenzi wa miundombinu ya kutoa maji kutoka Ziwa Victoria umelenga zaidi katika kupunguza upungufu wa maji uliopo kwenye Manispaa ya Tabora ambayo kwa sasa inahudumiwa na Bwawa la Igombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji hayo ni kwa ajili ya matumizi ya kijamii tu kwani hayatatosha kwa Kilimo cha umwagiliaji. Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa tija na kukabiliana na mabadiliko tabianchi, Wizara yetu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ina mpango kabambe wa Taifa wa umwagiliaji unaotekelezwa kuanzia 2018/2019 hadi mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo katika Manispaa ya Tabora, mpango huu umejumuisha uboreshaji na ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Imalamihayo, Inala, Magoweko na Bonde la Kakulungu.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-

Pamoja na jitihada za vijana wengi kujiajiri wenyewe kwa kuendesha bodaboda wamekuwa wakisumbuliwa na polisi kwa pikipiki zao kukamatwa mara kwa mara:-

Je, kwa nini pikipiki zao zinapokamatwa na wanapoenda kuzichukua hukuta baadhi ya vifaa kama betri hazipo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002 inampa mamlaka Askari Polisi kusimamisha chombo chochote barabarani na kukikagua kubaini kama kina makosa na hatimaye kukizuia na kukamata. Chombo cha moto kinapokamatwa hutunzwa kituoni kwa mujibu wa mwongozo wa Jeshi la Polisi Namba 229.

Mheshimiwa Spika, inapotokea kielelezo kimeharibiwa uchunguzi hufanyika na hatua kuchukuliwa kwa waliohusika na upotevu huo.