Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rehema Juma Migilla (22 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru Kamati yangu ya Guantanamo ambayo imeshiriki kwa namna moja katika kuleta taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwanakamati nitajikita zaidi katika suala la elimu. Ni wazi kuwa Serikali yetu ipo katika hatua za kuelekea katika Tanzania ya viwanda, lakini hatuwezi kufikia Tanzania ya viwanda bila kuwa na wataalam ambao wataenda kuvihudumia hivi viwanda. Wataalam hao ni wanafunzi na hawa wanafunzi hawawezi kupata yale yanayohitajiwa kama hawatakuwa na walimu wazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi walimu wamekuwa na changamoto nyingi sana zinazosababisha mpaka morale ya kufanya kazi ipotee. Sababu mojawapo kwanza ni kudhalilishwa kwa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi walimu wanadhalilishwa sana kana kwamba hawana taaluma, leo hii na siku za nyuma baadhi ya ma-DC, ma-RC hata Wakurugenzi wamekuwa ni watu wa kuwadhalilisha walimu, wanawatandika fimbo, kuna walimu wameshadekishwa vyumba vya madarasa, kwa kweli hali hii inasababisha mpaka morale ya kazi ipungue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la kushusha vyeo walimu. Hili suala limekuwa sasa hivi ni too much. Mwalimu mwenye professional yake, leo kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo wake, anashushwa cheo na Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, eti tu kwa sababu shule imefelisha, je, anayefanya mtihani ni Mwalimu au mwanafunzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu ya Serikali, kazi au majukumu ya kushusha vyeo au kutoa nidhamu na maadili kwa walimu yako chini ya Tume ya Utumishi wa Walimu, sasa nataka nijue, hili jukumu la kushusha vyeo walimu linachukuliwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, je, mmeinyang’anya madaraka Tume ya Utumishi wa Walimu na kuwapa hawa viongozi wa Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine linalochangia hadi kuzorota kwa elimu yetu ni kuchanganywa kwa kauli mbalimbali zinazotolewa na viongozi wetu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa juzi kulikuwa kuna kauli mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa Serikali, mfano Mheshimiwa Rais alisema kwamba walimu wasihamishwe kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine mpaka pale atakapopewa mafao yake ya uhamisho. Ghafla kuna kauli imetolewa tena na Wizara ikisema kwamba kuna Walimu wanahamishwa kutoka sekondari kwenda primary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, hata kama ukimhamisha kutoka kituo ‘A’ kwenda ‘B’….

T A A R I F A . . .

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ni Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ila hiyo ni a.k.a. (alias known as). (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalochanganya pia ni huku huku kuendelea kupotoshwa au kauli tatanishi. Leo hii Serikali ilisema kwamba hakuna kurudisha watoto shule za msingi mpaka sekondari, lakini leo hii hii Serikali inasema hakuna kukaririsha. Hivi tuelewe lipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukirudi tena kwenye suala lingine la hizi hizi kauli, Waraka wa Elimu Namba Tatu wa mwaka 2006 umetamka wazi majukumu ya kila mdau wa elimu kuanzia wazazi, Wakuu wa Mikoa hadi na walimu, lakini leo hii Mheshimiwa Rais anasema mzazi asihusishwe kwa mchango wa aina yoyote. Sasa je, hii michango ambayo inapaswa itolewe na wazazi au Serikali inaposema elimu bure, hii ni elimu bure au elimu bila ada? Tunaomba majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia point nyingine kwamba sababu nyingine zinazochangia kuwepo kwa udororaji wa elimu ni kutolipwa kwa madai ya walimu kutokana na vigezo mbalimbali mara uhakiki wa watumishi hewa, mara uhakiki wa wenye vyeti fake, sasa tunataka tujue huu uhakiki wa wenye vyeti fake na watumishi hewa utaisha lini ili hawa walimu waweze kulipwa madeni yao mbalimbali kama madeni ya uhamisho, madeni ya kupanda madaraja nauli na vitu mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee kuhusu uendeshaji wa shule za private. Shule hizi hazipo kwa kuwa tu eti zimejiamulia zenyewe. Shule hizi za private zimeanzishwa kwa kufuata kanuni na taratibu mbalimbali mojawapo ikiwa ni kupata usajili toka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imeanza kuziingilia hizi shule. Shule hizi zimewekeza, zinalipa ada na mzazi mwenyewe ameguswa, hakuangalia gharama, hakuangalia masharti mbalimbali akaamua kupeleka mtoto kwa matakwa yake yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii shule za private wanaambiwa wasikaririshe watoto. Wakati mwanzo walipewa masharti na wakakubali na Serikali ikawapa usajili, lakini leo hii haieleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue, hii Serikali ina mpango wa kuturudisha kule kwenye idadi ya kuongeza division four na tukose division one au two...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu jioni ya leo, kuwa nami ni miongoni mwa wanaochangia hotuba zilizopo mbele yetu kuhusu hizi Kamati zetu tatu. Tena nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa zawadi ya uhai mpaka leo nipo humu ndani ya hili bunge.

Mheshimiwa Spika, nikiwa mjumbe wa Kamati ya LAAC, ambapo umenitua hivi karibuni, ninakushukuru sana wewe kunipeleka kwenye hiyo Kamati, kiukweli ninashuruku sana.

Mheshimiwa Spika, nikiwa mjumbe wa Kamati ya LAAC ambao umenitua hivi karibuni, ninakushukuru sana wewe kunipeleka kwenye hiyo Kamati, kiukweli ninashuruku sana kwa sababu ninaenda kuifanyia kazi nchi yangu ambayo wananchi wamenituma.

Mheshimiwa Spika, kwenye kamati yetu kuna mambo mengi sana ambayo tumeyapitia, hasa hizi hoja za CAG. Ni mambo mengi sana yanasikitisha, very very sad stories hasa yanayofanyika kwenye hizi halmashauri zetu. Tumeangalia hoja nyingi ambazo kiukweli kama tutazifumbia macho, halmashauri zetu nyingi zinakwenda ku-collapse. Mbaya zaidi, wanaofanya yote haya yatokee mpaka sasa hivi wako ofisini wanakula kiyoyozi lakini bado wanatembelea V8 zetu na mafuta yetu wanatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwenye 10% ya mapato ya ndani. Hili ni eneo ambalo halmashauri nyingi wanatumia kama mwanya wa kupiga hela za wananchi wetu. Serikali ilitunga hii sheria ili kuweza kuyasaidia haya makundi matatu ambayo hayana uwezo wa kukopesheka katika benki zetu. Kuna kundi la wanawake ambalo ni kubwa sana, haliwezi kukopesheka na wala hawana dhamana, kuna kundi kubwa la vijana, na kundi la walemavu. Hata hivyo, halmashauri zetu zilizo nyingi, kwa masikitiko makubwa zinatumia kama mwanya wa kuweza kuyaminya haya makundi yasiweze kupata hizi fedha kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, ukipiga hesabu, hizi fedha kama zitasimamiwa vizuri, Shilingi bilioni 75, ni nyingi sana ambapo zingeenda kuwasaidia akina mama na vijana wakaondokana na umasikini. Katika hali ya kusikitisha, mfano hapa tukiangalia kuna halmashauri 17. Hizi halmashauri 17 zilitoa mikopo ya Shilingi 3,260,000,000/= bila kuzingatia uwiano. Tunajua kabisa sheria inasema ni 4:4:2 lakini wao kuna kundi moja wanalipendela zaidi. Tuangalie kabisa hili kundi ambalo linapendelewa lina athari kiasi gani na ambalo halipewi lina athari kiasi gani katika maendeleo ya nchi yetu?

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kundi la vijana; vijana sasa hivi ni wengi sana, graduates ni wengi sana, wako huko mitaani, hawana mikopo wanahangaika na bahasha kila kukicha. Bado hili kundi halipewi fungu lake kama inavyotakiwa. Kwenye ripoti ya CAG inaonesha kwamba vijana ndio hawapewi fedha kwa kiasi kikubwa kwa kigezo cha kwamba wana-misuse hizi fedha. Cha kushangaza, kwani ni lazima hawa vijana tuwape fedha? Ni ukweli kabisa kwamba ukiwapa vijana fedha, wanaweza wakazitumia ndivyo sivyo, lakini kwanini tu- stick katika aina moja tu ya mikopo?

Mheshimiwa Spika, kwenye halmashauri nyingi ukitembelea kule, hii mikopo kwa ajili ya vijana, unakuta ni boda boda tu; hivi hakuna creativity nyingine ya kuwasaidia hawa vijana zaidi ya kuendesha tu bodaboda? Tumeona kuna halmashauri moja vijana ambao wamesoma mambo ya medicine wameweza kuji-organize wakapewa mkopo wakaweza kufungua hadi kituo cha afya ambacho kimeenda kuajiri na watu wengine, lakini hawa watu wetu wa Maendeleo ya Jamii wanakosa ubunifu, wanashindwa kutoa elimu kwa watu wetu, matokeo yake vijana wetu wote wanakomalia mradi mmoja tu wa bodaboda. Kila siku ni bodaboda, mwisho wa siku zinakosa thamani huko kama vijijini, hata abiria hawapati na wanashindwa kupeleka marejesho. Matokeo yake kipengele cha kupeleka marejesho hakipo. Tunakuwa tunatoa hizi fedha, lakini mwisho wa siku hazirejeshwi.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia pia nature ya utoaji wa hii mikopo, tunawapa for free, wanafikiria hizi fedha ni kama za TASAF. Kwa hiyo, hata kusema kama kuna mechanism ya kusaidia hizi fedha zirudi, na hizi fedha ni revolving, hakuna. Kwa hiyo, ifikie mahali sasa Wizara iweke mkazo kuhakikisha kabisa hizi fedha zinakwenda kuwa ni zenye manufaa kwa vijana, akina mama na watu wenye ulemavu. Isifikie kwamba hizi fedha ni kama za TASAF, wanapewa for free, hakuna cha kurejesha. Ni lazima uwepo mkakati wa kuhakikisha hizi fedha zinarudi ili watu wengine waweze kukopesheka. Pia hizi fedha ziende zikawafikie hadi watu wa chini kabisa huko.

Mheshimiwa Spika, taarifa inaonesha wanaopewa hasa ni vijana na akina mama wa mijini. Kwani huko vijijini kwetu akina mama hawahitaji mikopo? Wanahitaji. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kupitia TAMISEMI, wahakikishe wanawasimamia na kutoa amri kwa hawa watu wa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha hii mikopo inakuwa ni yenye tija kwa vijana wetu, akina mama na watu wenye ulemavu, na isiwe tu inaingia kwenye mifuko ya watu.

Mheshimiwa Spika, kuna halmashauri nyingine hata kutenga, hawatengi, na pia hawasimamii urejeshaji. Hicho ndiyo kinatumika kama kichaka. Unakuta watu hawarudishi, hawatengi au wanachukua zile zilizorudi kidogo ndiyo wanaenda kutoa kwenye awamu inayofuata. Hapana, hilo halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu uwekezaji wa mitaji ya Umma katika miradi ya halmashauri. Ni kweli kabisa ili halmashauri zetu ziweze kuendelea ku-exist ni lazima basi ziweke miradi ya aina mbalimbali ambayo itazifanya halmashauri zetu ziweze kupata mapato mengi na ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaona na ripoti inaonesha halmashauri nyingi sana zinafanya uwekezaji ambao hauna maana, unakwenda kuzitia halmashauri zetu hasara, na yote haya yanasababisha hazifanyi upembuzi yakinifu vya kutosha, hata maandiko ya miradi hawafanyi. Unakuta kila halmashauri sasa kama ilivyosema ripoti, wanafaya uwekezaji kwa kuiga. Leo hii kila halmashauri ukienda ni soko na stendi. Sasa kama kila halmashauri kutakuwa kuna soko na stendi, leo hii hata bei za nauli zimepanda kwa sababu kunakuwa kila mahali kuna stendi.

Mheshimiwa Spika, leo dereva kila akiingia stendi lazima aache tax. Sasa huyu anayeendesha biashara ya mabasi, yeye atapata nini? Kwa maana hiyo lazima wampandishie nauli huyu mtumiaji wa mwisho, ambaye ni abiria, lakini yote haya ni kwa sababu tu tuna miradi ya kuigana. Kwa nini tusiwe na miradi ambayo itakuwa ni tofauti na ambayo inakwenda kuzalisha?

Mheshimiwa Spika, leo hii tunaona kuna masoko hayazalishi chochote. Mfano Soko la Ndugai pale, ni white elephant. Tuna soko pale la Machinga Complex, ni white elephant. Sasa hivi eti imefikia, Soko la Ndugai limelazimishwa sasa daladala zote ziende zikashushe watu kule Ndugai. Hivi tuliandaa lile soko kwa ajili ya kupeleka abiria kule au wanunuzi? Yaani tunafanya fanya ilimradi ionekane kule kuna ka-movement ka watu. Are we serious? Hebu tu-plan vitu ambavyo vinakwenda kuliletea hili Taifa faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la NHIF. Huku ndiyo kwenye majanga makubwa. NHIF ndiyo tunaiamini kama tool ya kutusaidia sisi wananchi tuweze kutibiwa pindi ambapo hatuna fedha. Jana tumeangalia tunakwenda kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo NHIF ndiyo atakuwa kingi wa kuweza kutuhakikishia afya zetu zinakuwa bora, lakini NHIF imegundulika ina madudu mengi sana. Kwanza, inashindwa kurejesha fedha kwenye halmashauri zetu. Halmashauri zinatoa huduma kwenye vituo vyetu vya afya lakini yenyewe inashindwa kurejesha. Cha kusikitisha zaidi, ujazaji mbovu wa fomu unaofanywa kwenye hosipitali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, sasa hawa watu wanafanya kazi purposely kurudisha nchi yetu nyuma au vipi? Kwa nini hawachukuliwi hatua? Wapo tu wamekaa ofisini, na mbaya zaidi tunaambiwa hapa; ukiangalia ukurasa wa nane pale unasema, yanafanyika hayo kwa sababu Serikali imeshindwa kuchukua haraka hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaobainika kuhusika na ubadhirifu. Serikali ndiyo chanzo cha haya. Tumeona watumishi wengi wanaofanya huu ubadhirifu Serikali ndiyo inawalinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumehoji halmashauri nyingi. Watu wengi tunaowahoji; Maafisa Masuuli na Wahasibu, ukimwuliza anakwambia yuko pale kwa miezi miwili, mwaka mmoja au miaka miwili. Kwa maana hiyo, ni kwamba kuna kamchezo kanaendelea huko kwenye Serikali hasa TAMISEMI. Wanamhamisha mtu, wanampeleka sehemu nyingine. Huyo mtu ameshaharibu. Leo nemesema huyu mtu ni mwizi, ukimhamisha kutoka Halmashauri A, kumpeleka Halmashauri B, huo wizi atakuwa ameuacha? Kwa nini umhamishe? Kwamba mnakwenda sasa kumtoa kafara yule anayekwenda kwenye hiyo post au vipi? Kwa nini tuwalinde hao watu? Kwa nini Serikali isiwachukulie hatua?

Mheshimiwa Spika, eti hatua tunazowachukulia; tunamhamisha kutoka kituo A kumpeleka B. Tayari huyu mtu ni mwizi, ni mbadhirifu, ataendeleza kufanya yale aliyokuwa anafanya Halmashauri A. Ifikie mahali tuonee uchungu hizi fedha. Wanapiga sana hizi fedha, lakini tunawalinda. Halafu mbaya zaidi juzi tunaambiwa kwamba, timu ya TAMISEMI imekwenda halmashauri fulani kuweka kambi. Siku zote mlikuwa wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mpaka madudu yafanyike ndiyo mnakwenda kuweka kambi. Kambi for what? Tunaweka kambi for what? Watu wameshapiga hela halafu tunawaangalia, tunawahamisha hamisha tu! Ifike mahali hawa watu walioiba fedha za Watanzania, fedha zinapotea, washughulikiwe. Siyo tu kuwahamisha kituo kimoja, watu wamepiga dili za mchongo sasa hivi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Rehema Migilla, kengele ilikuwa imeshagonga, lakini naona kuna taarifa hapa. Mheshimiwa Charles Kajege.

T A A R I F A

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa msemaji, kwamba mkakati wa TAMISEMI kuhamishana siyo kwamba ni wajinga, hapana. Ni namna ya protection. maana yake ni kwamba anayeiba kwa sababu mkimbana kule wanaona dah, sasa tufanyeje? Wanamhamishia katika halmashauri nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mifano mingi katika jimbo langu. Watu ambao ni wezi wamehamishiwa katika maeneo mengine. Nami nasema kesho, wale wote lazima wakamatwe. Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Rehema Migilla, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa asilimia 100. Hawa watu tusiwachekee. Masuala ya kulindana tunamrudisha mama. Mama anahangaika kila kukicha, anatafuta fedha kwa ajili ya Watanzania halafu kuna watu wachache, tena Serikali eti inawalinda, wamrudishe mama nyuma, hatukubali kabisa. Tunaongea hapa, kesho tutashika shilingi! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani jioni hii. Awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na upendeleo aliotupatia sisi wanadamu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru sana Viongozi wa Kamati yetu lakini pia Mawaziri ambao wanaiongoza Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora. Mimi nikiri kwanza ni Mjumbe wa kamati ya USEMI. Mawaziri hawa Dada yangu Mheshimiwa Jenista, Kaka yangu Mheshimiwa Deo Ndejembi na Watumishi wote walio chini ya Wizara hii, wanafanya kazi vizuri na wanatupa ushirikiano wa kutosha. Kwa sababu ya muda naomba niende haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kuishukuru Serikali kwa mambo yote inayoyafanya juu ya watumishi wetu wa umma. Tumeona jitihada nyingi sana zimefanyika ili kuhakikisha hawa Watumishi wa Umma wanafanya kazi katika mazingira very conducive.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wafanyakazi sasa hivi baadhi wamebadilishiwa madaraja, wamelipwa madeni yao ya arrears, madeni ya likizo, matibabu na vitu vingi pia wamefanyiwa re-categorization. Hivyo ningependa sana kuishukuru Serikali kwa kuwa sikivu juu ya hawa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, panapokuwa na mazuri pia mabaya yanaweza yakawepo, nitajikita zaidi kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina raia ambao walikuwa wananchi wa Burundi. Wananchi hawa baadhi yao wamezaliwa Tanzania, wamesomea Tanzania na wanafanya kazi Tanzania. Raia hawa tuliwapa uraia, baada ya kuwapa uraia bado wanaendelea kufanya kazi kwa kibali. Tangu waanze kufanya kazi wengine wameanza mwaka 2003 mpaka leo hii hawa raia wanafanya kazi kwa mkataba. Walisainishwa barua ya mkataba mara moja tu lakini tangu hapo hawajapewa tena barua ya mkataba. Sasa sijajua wanafanya kazi kwa utaratibu upi?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa, ama watumishi hawa wanateseka sana. Hivi ninavyokwambia haki yao kama watumishi ni ile Check Number tu inayowapa mshahara. Hawana haki ya likizo, hawana haki ya pensheni na wakati huo huo kila mwezi wanakatwa pesa za PSSSF. Hawa wananchi hawana haki ya kushiriki kwenye Vyama vya Wafanyakazi lakini hawana haki ya kupata likizo ya uzazi, likizo maalum, lakini hawana haki hata ya kuweza kushiriki kwenye baadhi ya shughuli mbalimbali za Kitaifa kama sensa, sijui uchaguzi, hawana hiyo haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba hawa watu tayari wameshakuwa ni raia wetu, hivyo nikuombe sana Dada yangu, najua Wizara hii ni sikivu na ninyi ni wasikivu, kilio cha hawa wananchi, hawa watumishi wetu kwa sababu tumewakuza wenyewe, wamesoma kwenye vyuo vyetu, wanayo mahitaji yao ya msingi sana, ninaomba Wizara na Serikali iyasikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo wanaomba hawa watumishi. Kwanza wapatiwe ajira ya kudumu, hii ajira waliyonayo haina sustainability. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuna watu ambao walistaafu lakini mpaka leo kwa sababu walikuwa wanafanya kazi kwa mkataba hawajui hata pensheni zao watapa lini, ilihali kila mwezi walikuwa wanakatwa PSSSF inapofika wamestaafu hawana wanachoondoka nacho kama Mtumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo wanahitaji hawa watu ni kupata stahiki kwa wale ambao wameshafariki, wale warithi wao, wajane, wagane, watoto basi waweze kupata stahiki zao ambazo alikuwa anazifanyia kazi huyo Mtumishi wa Umma. Ninakuomba sana najua Serikali yetu ni sikivu sana, kilio cha hawa watu naomba tukisikie kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua hili suala nimeshaliongelea sana, najua Mheshimiwa Waziri na tangu akiwa Mheshimiwa Mchengerwa nilishalifikisha sana na Mheshimiwa Jenista nimeshakufikishia na hata Katibu Mkuu Dkt. Ndumbaro nimeshamfikishia. Kwa sababu leo mpo cabinet yote najua kilio cha hawa wananchi kimefika tamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine ni suala la uhaba wa watumishi hasa wa Kada ya Afya. Ni ukweli uliowazi kabisa watumishi wa Kada ya Afya hususani kwenye Majimbo ya Vijijini unasikitisha mno. Kituo cha Afya au Zahanati unakuta ina Mtumishi mmoja tu. Mimi Kata ninayotoka Kata ya Ichemba kuna Zahanati pale Mtumishi mmoja tu ndiyo anafanya kazi pale. Sasa anapokuwa Mtumishi mmoja au wawili kiukweli utendaji wa kazi unakuwa ni mgumu. Mtu huyo huyo ahudumie familia yake lakini mtu huyo huyo anatakiwa ahudumie hawa wananchi. Sasa anapokuwa peke yake kuna mambo yanajitokeza mengi sana ambayo yanaweza kwa namna moja au nyingine yakamsababishia hata akafukuzwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokuambia Mheshimiwa Waziri huko kijijini kwetu kuna utaratibu watumishi wa zahanati wanafanya kazi kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa tena kuanzia saa mbili mpaka saa kumi, kwa hiyo mgonjwa anapopatikana baada muda huo hana msaada.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia bado kuna unyanyasaji mkubwa sana unaofanywa na hawa watumishi kwa sababu ya uchache wao. Unakuta Mama Mjamzito anapofika pale anaambiwa kwamba hii ni mimba ya ngapi, akisema ya kwanza anaambiwa aende Hospitali nyingine. Lakini anaambiwa hayo ni kwa sababu Mtaalam wa kuzalisha pale hiyo mimba ya kwanza anakuwa pale hayupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hawa wataalam mnaowapeleka huko, utaalam ni ukoje? Haiwezekani huyo mtaalam aliyosomea eti atuwekee masharti kwamba mimba ya kwanza kituo cha Afya, mimba ya pili mpaka ya tatu ndiyo zahanati pale. Hivi haya mafunzo ndiyo wanafanya hivyo kweli? Tunaomba sana hawa watumishi kwenye Kada ya Afya tuwapeleke huko vijijini. Kwenye ajira hizi niombe sana watu wa vijijni tuongezewe watumishi wa Kada ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine ni kuhusu Mishahara na mabadiliko ya mishahara kwa watumishi. Kiukweli watumishi, hata mimi nilikuwa Mtumishi wana manung’uniko makubwa sana. Watumishi wa Serikali takribani miaka mitano iliyopita hawajawahi kupata nyongeza ya mshahara, maisha yao yamekuwa ni magumu sana, gharama za maisha zimepanda, lakini mshahara wao haupandi. Imefikia sasa hivi hata tamaa ya kufanya kazi imekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nimeshuhudia huko kwangu Mfanyakazi ana-bet, ukiuliza wanakuambia hali ngumu ya maisha. Wafanyakazi wanakopa mpaka songesha, wanakopa vikoba hebu ifikie mahali hawa wafanyakazi tuwaonee huruma jamani wana maisha magumu, mfumuko wa bei unawahusu, kodi, nyumba kila kitu matibabu jamani tuwaonee huruma hawa wafanyakazi, this time tuwaongezee mshahara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni matumizi mabaya hasa ya ubadhirifu wa fedha. Sifa mojawapo ya mtumishi wa umma ni kuwa muadilifu katika kazi anayoifanya lakini wafanyakazi walio wengi tunaona wana ubadhirifu mkubwa sana wa madaraka yao. Hapa juzi kuna crip ime- trend sana hapa ya temporary offices, hivi kweli mtu anatumia milioni 100 kwa kujenga temporary office kiasi kwamba mpaka Waziri Mbarawa anawaambia TAKUKURU fanyeni kazi. Ina maana huyu mtu mpaka Mbarawa anasema TAKUKURU wafanye kazi hakuna means nyingine zilizomwangalia mpaka amefikia kufanya ubadhirifu wa kiasi hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu ninachoshangaa hawa wanaofanya ubadhirifu hivyo, hatuoni hatua za makusudi zikichukuliwa dhidi yao. Tunaona wengi akishagundulika na tatizo anaweza akahamishwa kituo, anatolewa kituo A anakwenda kituo B. Hivi huyu ameshakuwa ni mwizi kwanza ukimtoa kituo A ukimpeleka kituo B ndiyo ataacha wizi? Huo wizi ataendeleza. Kwa hiyo, kuwahamisha sioni kama ni solution ya hawa wanaofanya ubadhirifu wa mali za wananchi. Wananchi wanalipa kodi kwa shida, maisha ni magumu halafu wao tu wanapiga, hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri kwa hao wanaofanya hivi, nafikiri hatua kali zichukuliwe dhidi yao. Isiishie tu kumsimamisha kazi au kumfukuza kazi; iendelee aidha, wafungwe jela au hata wafilisiwe mali zao. Hivi mimi Rehema hapa nimekaa najua kabisa nina mchongo wa maana ambao najua mwisho wa siku nitasimamishwa tu kazi au nitafukuzwa kazi, si nitaiba? Nitaiba, halafu najua kabisa mwisho wa siku nitafukuzwa kazi lakini tayari nimeshatengeneza mchongo wa maana fedha ya maana. Kwa hiyo, akifikiria fedha yake ya kustaafu ni ndogo kuliko huo mchongo, nafikiria tuongeze adhabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi jioni hii nichangie kuhusu Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mawaziri wote Wizara hizi mbili, Mheshimiwa Jafo na timu yake Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege, lakini vile vile Mheshimiwa Mkuchika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naanza kuchangia kama ifuatavyo na nianze na suala la elimu. Ni ukweli usiopingika kuwa elimu yetu kwa sasa imedolora na inashuka kiwango siku hadi siku. Hii inatokana na ukweli kwamba nchi yetu imeifanya elimu kama huduma na kuwaandaa watu kuwa ni wa kufaulu mitihani tu na si kwenye uwekezaji. Kama nchi haina kipaumbele kwenye elimu na inaifanya elimu kama huduma obviously hatuwezi kufika mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yetu, kama kweli tunataka elimu yetu ikue naomba sana ijikite kwanza kuifanya elimu ni uwekezaji na badala ya huduma. Vilevile ili elimu hii iweze kuwa na tija kwa hawa vijana ni lazima basi hii mitaala ya elimu ifanyiwe reformation, kwa sababu sasa hivi ukiangalia inawaandaa tu wanafunzi kufaulu mitihani, lakini hakuna ujuzi wowote inayowapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kijana anamaliza darasa la saba, anamaliza form four, anamaliza form six mpaka Chuo Kikuu hana ujuzi wa aina yoyote, matokeo yake kila siku wanatembea na bahasha mitaani mpaka zinapauka. Naiomba Serikali yetu kama kweli tunataka tujikite katika elimu basi haya ninayoyasema, mitaala ifanyiwe reformation na ijikite zaidi katika kuwapa wananfunzi skills ili wahitimu hawa wanapomaliza, kama ni kidato cha nne basi ajue anatoka na ujuzi gani badala ya kuwa anazurura mitaani. Leo hii vijana hata wa chuo kikuu badala ya kuwa ni job creators wamekuwa ni job seekers, naomba hili suala tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya ualimu na walimu. Kazi hii ya ualimu inaonekana kama ni kazi ya watu waliofeli, mimi ni mwalimu by profession, inaniuma sana jamii inaiona hii kazi ya ualimu kama ni kazi ya waliofeli. Hii inajidhihirisha unapoangalia kwenye matokeo hata ya form four, division one, division two wanaenda high school, halafu divison three hadi four ndio wanaopelekwa ualimu. Kama tanataka kweli tuwekeze kwa nini hii division one na division two ndio wasipelekwe ualimu? Mpaka jamii inamuona mwalimu ni mtu mjinga mpaka inafikia anaulizwa yaani umekosa hata nafasi ya kwenda kwenye ualimu! Jamani ualimu ni kazi kama zilivyo kazi zingine wote tuliomo humu tumepita kwa mwalimu kwa nini huyu mwalimu leo hathaminiki? Naomba Serikali impe hadhi mwalimu kama inavyompa mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu wa Tanzania ana changamoto nyingi sana ambazo zinamkumba. Leo hii walimu wamekosa morali wa kufanya kazi na takwimu zinaonesha wanafanya kazi chini ya kiwango, yote hii inasababishwa na Serikali kwa kutowajali walimu. Walimu wana stahiki nyingi sana ambazo wanazidai lakini Serikali haitekelezi. Wana madeni ya arrears, wana madeni ya nauli, ya nini Serikali haitekelezi. Nataka nijue leo hii Serikali inatumia vigezo gani pindi inapowalipa hawa wafanyakazi au walimu stahiki zao mbalimbali. Kwa mfano katika Jimbo la Tabora mjini kuna hizi shilingi bilioni mia mbili zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwalipa walimu, lakini ni walimu 18 tu ndio wamelipwa wakati kuna idadi kubwa ya walimu hawajalipwa. Sasa nataka TAMISEMI mtuambie ni vigezo gani ambavyo mnavitumia kuwalipa hawa walimu stahiki ili hali wana madeni mengi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuanzisha elimu bure, elimu bure inaende sambasamba na kutoa posho kwa walimu wakuu wakuu wa shule na waratibu wa elimu kata. Hata hivyo ndugu walimu wana mishahara midogo sana. Tunaomba basi katika hii posho mnayowapa walimu sijui wakuu wa shule ma-headmaster na waratibu wa elimu kata basi na walimu na wenyewe wapewe hata kidogo, kwa sababu hawa wakuu wa shule mnaowapa pesa hawafanyi kazi peke yao wanafanya kazi na walimu wengine, nao tunaomba muwape hata kidogo kama motisha ya kuweza kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie mchakato wa kuhamisha walimu wa sekondari wa arts na kuwapeleka primary. Mheshimiwa Haonga amesema ni ukweli usiopingika ni wazo zuri, lakini approach inayotumika sio nzuri. Walimu hawa walivyokuwa wanasoma kwenye vyuo vyao walisomea masomo mawili, leo hii unawaambia wakafundishe kule watafundisha kitu gani? Mbaya zaidi hakuna hata induction course ambayo mmewaandalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali basi angalau iwape induction course hawa walimu ili waweze kwenda kufundisha kwenye mazingira yale. Tukumbuke kwamba walimu hawa wamekuwa trained kufundisha wanafunzi wenye kimo kikubwa, leo wakafundishe watoto wadogo wataweza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado njia za ufundishaji watoto wa sekondari ni tofauti na watoto wa primary. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali yetu kama kweli tunadhamiria kuinua kiwango hiki cha elimu, japokuwa ni approach, nzuri basi hawa walimu wapatiwe induction course angalau ya mwezi hata mmoja kwenye methodologies. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie hii Tume Utumishi wa Walimu. Tume hii inafanya kazi kubwa sana na naiomba Serikali iiongezee pesa ili iweze kufanya kazi yake kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kazi nyingine ambayo inafanywa na Wizara ya TAMISEMI. Kazi moja wapo ni kuhakikisha inatatua migogoro inayotokana na ardhi. Mkoa wa Tabora hususani Manispaa ya Tabora walikumbwa na bomoa bomoa, watu hawa walijenga katika maeneo ambayo walipewa kisheria na bado Serikali yetu ikaweka hadi miundombinu kule na bado walikuwa wanachukua hadi kodi lakini leo hii hawa watu wanaambiwa wahame lile eneo ilhali walipimiwa na Serikali na wako pale kisheria lakini hatuoni dalili zozote za kupewa fidia au kutafutiwa eneo jingine. Naiomba sana Serikali iwanusuru watu hawa, tunaomba basi watu hawa wapatiwe eneo jingine au wapewe fidia waweze kuanza maisha mengine mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni katika uwezeshaji wa vikundi vya wanawake na vijana, ile asilimia 10 ya mapato ya ndani. Hizi asilimia zipo kisheria lakini halmashauri zimekuwa hazitengi pesa kwa ajili ya kuwapatia vijana, hali inayopelekea vijana sasa hivi wafanye kazi ambazo ni tofauti na ndoto zao. Tunajua kabisa kila mmoja ana kazi ya ndoto yake, lakini vijana wengi sasa hivi wanafanya kazi ya kuendesha boda boda, wanawake wengi wamekuwa bar maid ni kazi ambazo ziko nje ya ndoto zao. Kama Serikali itahimiza halmashauri kutenga asilimia 10 vijana hawa watanufaika na wataacha kuhangaika huko mitaani. Tunaiomba Serikali hizi halmashauri zisizipe mzigo mkubwa yaani mapato yarudi kule kwenye Serikali za mitaa badala ya kwenda Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni kuhusu utumishi. Tulipiga kelele sana kuhusu watumishi wa darasa la saba. Ni kweli kabisa watumishi hawa waliajiriwa na Serikali na Serikali hii ndio tena ikawatoa kazini, lakini Serikali hii tena imewarudisha kazini, ni jambo zuri na wazo zuri, lakini suala langu ni hili, je, Wizara ina mpango gani au itawalipa kwa fungu lipi watu ambao hawajafanya kazi kwa muda mrefu sana? Pia kuna watu ambao tayari walishaajiriwa ku-cover hizi nafasi za watu walioko darasa la saba, je, hawa watu ambao sasa wameshaajiriwa kuziba zile nafasi za watu wa darasa la saba watatolewa kazini au vipi? Naomba majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni ya leo na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunipa uhai na afya mpaka leo muda nipo humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri anayofanya na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini ina mapungufu katika baadhi ya sekta zake, nianze na NECTA. Kwa kipindi kirefu Baraza la Mitihani limekuwa likitunga mtihani wa darasa la saba kwa kutumia aina moja tu ya maswali yaani multiple choice. Sasa unapotunga mtihani kwa kutumia multiple choice peke ina maana hau- provide room kwa huyu mwanafunzi kuweza kujieleza kwa zaidi. Vilevile mtihani wa hivyo haupimi hizi skills zingine za language kama vile kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili hawa watoto wetu waweze kufanya vizuri na kwenye mitihani ijayo ni lazima basi mitihani itungwe kwa ku-mix other types of questions ili mwanafunzi aweze kuwa na nafasi ya kujieleza zaidi. Kwa sababu sasa hivi mwanafunzi anafanya mtihani kwa kutumia aina moja tu ya maswali, swali la kwanza mpaka la 50 na anafanya tu betting kwa sababu anahisi tu kwamba hili litakuwa jibu na kuna wengine wana bahati anaweza akajibu lile jibu na likawa jibu sahihi kweli. Kwa hiyo, naomba wizara iangalie utungaji wa maswali haya ili kuweza kupima other skills of language kwa hawa wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuangalie namna gani wanavyojibu hii mitihani ya darasa la saba. Wanafunzi wetu wanajibu hii mitihani kwa kutumia karatasi za OMR. Serikali imetumia hizo karatasi kwa ajili ya kujirahisishia wao usahihishaji, lakini hawampimi huyu mwanafunzi namna gani anaweza kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi karatasi hazimpi mwanafunzi uwezo wa kuandika zaidi ya kuweka shading pale kwenye lile jibu. Unakuta mtoto anafaulu kwenda form one ilhali hajui kuandika chochote lakini amefaulu, this is shame, naomba Serikali iliangalie suala hili kwa undani ili watoto wetu waweze kufanya mitihani yao vizuri na waweze kufaulu kwa kiwango kinachotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi inakuwaje hadi mtihani wa hisabati unakuwa na multiple choice, mtihani kuwa na multiple choice ina maana unamsaidia huyu mwanafunzi kuelekea jibu. Mwanafunzi akokotoe mwenyewe, naomba sana wizara tuache mtihani wa hisabati uwe wa kawaida na usiwe na multiple choice.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu Loans Board. Loans Board wanafanya kazi nzuri sana, watoto wengi wa kimaskini wameweza kwenda vyuo vikuu na kutimiza ndoto zao. Hata hivyo, hii Loans Board imekuwa ni mwiba sana kwa hawa wafanyakazi hususan Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wazi kabisa mwaka 2016 mlifanya mabadiliko ya sheria kutoka kulipa asilimia nane mpaka 15. Jamani, huyu mtumishi wa Tanzania ana makato mengi sana yanayomkabili, ana income tax, ana PSPF, ana makato ya NSSF, ana makato ya CWT, makato mengi kiasi kwamba mshahara unabakia mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo sheria imekiuka ile thamani ya kubakia mshahara 1/3 imekiuka, kwa hiyo, inampa mtihani mkubwa sana huyu mtumishi kufanya kazi kwa mashaka na stress nyingi. Kwa hiyo naomba basi kama hii sheria ipo na sheria sio maandishi ya Qur-an au Msahafu kwamba hayawezi kufanyiwa marekebisho. Naomba basi sheria kama ipo iletwe kwa sababu ni sheria kandamizi, inawakandamiza watu wengi sana hata sisi inatukandamiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba hii sheria iletwe humu au Serikali sasa itoe tamko wale watu waliokumbwa na hii sheria ina maana loans beneficiaries before 2016 basi walipe ile ile asilimia nane na hawa ambao wako baada ya 2016 walipe kwa hiyo asilimia 15, itakuwa inawasaidia hawa wafanyakazi. Kwa kweli wanafanya kazi kwa stress nyingi maisha yamekuwa ni magumu vitu vimekuwa bei juu wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. REHEMA J. MIGILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni katika Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu katika uchumi na maendeleo ya wananchi wake. Tunajua kabisa asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania wamejikita katika kilimo. Hata hivyo, kilimo leo hakipewi kipaumbele hali inayopelekea wananchi waone kilimo si jambo lenye tija kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze zaidi katia zao la tumbaku. Zao la tumbaku ni muhimu sana kwa wakazi wa Tabora na Tanzania kwa ujumla kwani linapelekea nchi yetu na Serikali kwa ujumla lipate pato kubwa hasa katika fedha za kigeni. Hata hivyo, zao hili leo hii limekuwa halina tija kwa mkulima wa Tabora kutokana na changamoto mbalimbali mfano suala la masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi soko la tumbaku si la uhakika, wananchi wanalima mazao kwa shida sana, wanatumia muda mrefu na gharama kubwa lakini hawajui zao lao la tumbaku wataliuza wapi na hata wakija kuliuza bado wanapangiwa bei ndogo sana tofauti na gharama za uzalishaji. Hivyo, naiomba Serikali yetu basi iwahakikishie hawa wakulima wa Tabora soko la uhakika ili kilimo hiki kiwe chenye tija. Serikali ituambie, hivi zao hili ina mpango wa kulifuta kabisa au vipi? Kama ndivyo, kuna zao gani mbadala ambalo Serikali imewaandalia wakulima wa Tabora ili shughuli zao za kiuchumi ziendelee? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia napenda niongelee matumizi ya Tanzania shilling badala ya dola. Kulitolewa tamko la matumizi ya Tanzania shilling badala ya dola kwenye shughuli mbalimbali za ununuaji wa tumbaku na uagizaji wa pembejeo kutoa nje ya nchi. Naomba nijue, je, Serikali ilifanya utafiti kujua ni gharama kiasi gani ambayo inawa-face wakulima wanapotumia shilingi badala ya dola? Nasema hivi nikiwa na sababu kwamba, mkulima anapoingia mkataba na wanunuzi huwa anaingia kwa gharama ya dola lakini inapokuja kwenye suala la manunuzi anaambiwa auze kwa Tanzania shilling.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa kwamba shilingi yetu ya Tanzania inashuka thamani siku baada ya siku, lakini inapokuja kwenye suala la uuzaji anauza kwa dola ambayo kwa wakati huo inaweza kuwa imepanda. Tunaomba Serikali ituambie, je, walifanya tafiti za kutosha kubadilisha matumizi ya dola kwenda kwenye shilingi kwa sababu shilingi inamuumiza mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu pembejeo hususani mbolea. Mbolea imekuwa ni janga kubwa sana kwa wakulima wetu pamoja na kwamba Serikali imekuja na mfumo mzuri wa ununuzi wa pamoja lakini ununuzi huo au mfumo huu kwa sasa inaonekana kama vile umefeli kutokana na ukweli kwamba mbolea haiji kwa wakati. Wakati mkulima anahitaji kupanda mbolea haipo akishapanda ndiyo mbolea inakuja, wakati anapotaka kukuza mazao yake mbolea haipo, anapotaka kuvuna ndiyo mbolea inakuja, sasa tunamsaidia huyu mkulima au tunamchezea makidamakida? Naomba Serikali ije na majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imewekwa bei elekezi lakini haifuatwi. Kwa hiyo, tunataka tujue kwa nini Serikali inatoa maagizo ambayo hayatekelezeki? Kama hayatekelezeki ni hatua gani mnachukua kwa watu hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni utitiri wa kodi. Kumekuwa na tatizo la kodi na tozo nyingi sana kwenye suala la tumbaku na anatozwa mununuzi. Kutokana na kwamba mnunuzi huyu anatozwa kodi na tozo nyingi na yeye sasa anaamua kwenda kumbana huyu mkulima wa chini hali ambayo inamuathiri katika bei ya tumbaku. Tunaomba hizi tozo zipunguzwe au zifutwe kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni hivi vyama vya msingi (AMCOS) vimekuwa ni shida. Kwanza, havipewi bajeti ya kutosha kwa ajili ya kujiendeleza lakini pia vimekuwa vinawadhulumu sana hawa wakulima wetu. Tunaomba hili suala liangaliwe hawa wakulima wasiteseke sana, wanalima kwa kuteseka bado waje kudhulumiwa, hapana hili jambo haliwezekani na halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watendaji wa hivi vyama vya ushirika na hata Bodi za Tumbaku wanateuliwa tofauti na watu wanaojua tumbaku. Mtu hana taaluma ya tumbaku lakini anakwenda kuchaguliwa kufanya kazi kwenye AMCOS na kwenye Bodi la Tumbaku. Kama mtu hana utaalam wa tumbaku unafikiria ataifanya kazi hii effectively? Tunaomba kabisa Serikali iwaaangalie hawa watendaji wa kwenye hivi vyama vya ushirika pia hawa watu wanaoteuliwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. REHEMA JUMA MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia kidogo katika hotuba ya bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia vitabu hivi na kuvisoma kwa umakini sana, kimaandishi vitabu hivi vina maelezo mazuri sana, lakini kwenye utekelezaji napata ukakasi. Kiukweli bajeti ya mwaka huu haiakisi maisha halisi ya Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kutokana na sababu kwamba leo hii ukiangalia maisha ya kila Mtanzania ni magumu sana. Bado kuna Watanzania wanakula mlo mmoja kwa siku, lakini sokoni mfumuko wa bei ni mkubwa sana, vitu vinauzwa kwa bei kubwa sana. Sambamba na hilo, hata mzunguko wa pesa huko mitaani haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wafanyakazi wanalia, hawana pesa; wakulima wanalia, hawana pesa; wafanyabiashara wanalia hawana pesa, halafu tunasema ni bajeti nzuri, huu ni uwongo. Bado katika vitabu hivi tunasema kwamba, eti bajeti hii ina lengo la kuondoa umaskini na kupeleka nchi kwenye nchi ya viwanda ilhali hatuyapi kipaumbele maeneo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na matatizo hayo ambayo yanaikumba hii bajeti yetu, naomba Serikali sasa ifanye yafuatayo ili kuhakikisha maisha ya Mtanzania ambayo tunalenga yamwondolee umasikini yanafanyiwa kazi. Kwanza Serikali idhibiti mfumuko wa bei, bei ni kubwa sana, lakini pia kupunguza riba kwenye mikopo. Suala lingine kuwepo basi na nidhamu kwenye matumizi ya mapato yetu. Leo hii tunachokipanga siyo ambacho tunakitekeleza. Bajeti ya mwaka 2017 haijatekelezeka kwa asilimia zinazotakiwa, halafu leo tunaleta bajeti nyingine ambayo ni kubwa zaidi kuliko ya mwaka 2017. Naomba haya masuala yafuatiliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuongelea leo ni kutoongezwa kwa mishahara kwa wafanyakazi na kulipa madeni ya wafanyakazi. Suala la kuongezewa mishahara kwa hawa wafanyakazi siyo suala la mtu kupenda, ni la kisheria. Annual increment iko kisheria, lakini leo hii uongezaji wa mishahara kwa wafanyakazi imekuwa mpaka mtu apende. Jamani kwa nini tunakwenda kinyume na utaratibu wa sheria inavyotaka? Tunataka sasa pindi anapo-wind up atuambie hii sheria ambayo iliruhusu annual increment iwepo na mliitunga humu Bungeni inafanyiwa kazi kwa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ulipaji wa madeni. Wafanyakazi wa Tanzania especially walimu, wana madeni mengi sana. Wana madeni ya arreas, likizo, tofauti na mshahara, lakini madeni haya hayalipiki kwa kigezo cha uhakiki. Hivi ni uhakiki gani ambao hauna kikomo? Serikali inatumia upenyo wa uhakiki kutowalipa watu stahiki zao. Tunaomba huu uhakiki uwe na kikomo, watu walipwe stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni ajira kwa vijana. Naipongeza Serikali kwa kutoa riba kwenye hii 10% ya maendeleo ya vijana na wanawake. Hata hivyo, kutoa riba haimaanishi kwamba ndiyo hawa vijana watakuwa wamekomboka kwenye suala la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo, nikiwa na sababu kwamba Halmashauri zetu tumezinyang’anya vyanzo vikubwa vya mapato kiasi kwamba mapato yanayobakia yanakuwa ni madogo hali inayosababisha ile 10% iwe ndogo. Wanapoenda kwenye vile vikundi vyao wanapatiwa hela ndogo sana kiasi kwamba watu wanaamua kuacha pesa ile. Kwa hiyo, naomba sasa Halmashauri zirejeshewe vile vyanzo vyao vya mapato ili watu waweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine tujikite katika maeneo ya kipaumbele. Malengo ya bajeti hii yanalenga kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda, lakini tunaufikishaje uchumi wa viwanda ilhali maeneo ya kipaumbele kama kwenye kilimo, afya, elimu, tunayapelekea bajeti ndogo mno ambayo haitekelezeki? Naomba kilimo lipewe kipaumbele kwa sababu kwanza kinaajiri Watanzania walio wengi lakini pia kipelekewe pesa kwa wakati ili wakulima waweze kuwa na tija na kilimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni TRA. TRA na wenyewe ni another disaster. TRA tunaamini ndiyo chombo chetu cha kutukusanyia mapato lakini wamekuwa ni mwiba kwa wafanyabiashara na kwa kila kitu. Leo TRA anakwenda kukagua na wanatembea na makufuli muda wote. Sasa kama wanatembea na makufuli muda wote, wafanyabiashara wataogopa kufanya biashara na wakiogopa, watafunga biashara zao. Wakifunga biashara hatuwezi kupata mapato ambayo tunayatarajia. TRA wanatembea mpaka kwenye ma-guest usiku, kweli! Mtawatisha hadi wawekezaji, tuiangalie TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye kuboresha viwanda vyetu. Tuko kwenye nchi ya viwanda na tunaelekea kwenye Serikali ya viwanda. Viwanda tunavyo vingi sana lakini mpaka dakika hii havifanyi kazi, vimekufa. Tunaiomba Serikali yetu, kabla ya kuanzisha viwanda vingine iviboreshe vile vilivyopo na kama kuna wawekezaji ambao wanashindwa kuviendesha basi wapewe wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kodi ndogo ndogo ambazo ni kero kwa wawekezaji zipunguzwe. Mfano Mkoa wa Tabora kuna Kiwanda cha Nyuzi, kipo siku nyingi sana, kilikuwa kinatoa ajira kwa wakazi wengi sana wa Tabora. Kiwanda kile kimekufa na walipewa Wahindi na bado kuna wananchi wa Tabora wanadai pesa ambazo zilizotokana na kiwanda hiki. Kama kweli, tunataka tuboreshe ajira na tufikie uchumi wa viwanda, basi hivi vilivyopo kwanza vihakikishwe vinaboreshwa na hao wawekezaji wanapunguziwa adha ndogo ndogo ili waweze kuwekeza kwa umakini sana. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei. Naomba niendelee, nilindie muda wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mheshimiwa Waziri hawezi kutuambia kwamba eti tuanzishe viwanda vingine ilhali kuna vingine ambavyo vimekufa. Kwa nini tusifufue hivi kwanza? Leo uanze mradi mwingine wakati wa kwanza haujaukamilisha, ndiyo maana tuna-fail katika mambo yetu mengi kwa sababu ya kuanzisha miradi ambayo haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Suala lingine ni elimu bure. Elimu bure ina faida nyingi sana lakini hatukujiandaa. Tumeanzisha elimu bure ilhali hatujaandaa miundombinu ya kuhakikisha tunaenda sambamba na hii elimu bure.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi jioni hii nichangie kuhusu mawasilisho ya hizi Kamati tatu. Jambo la kwanza, napenda nimshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kutuwezesha jioni hii kuwepo mahali hapa kwani bila yeye sisi hatuwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jioni ya leo, napenda kuchangia mada zifuatazo. Suala la kwanza ni kuhusu uhaba wa vyumba vya madarasa. Hivi karibuni yalitoka matokeo ya darasa la saba hali iliyopekelea kuonekana ufaulu umekuwa mkubwa ambao hauendani na sambamba na vyumba vya madarasa. Hali hii ilipelekea watoto wengi kukosa vyumba madarasa na hatimaye wengine wakaanza kusoma wengine wamechelewa kuanza kusoma. Hali hii inakatisha tamaa wazazi hata na watoto wenyewe kwa sababu wanaona wenzao wameanza kusoma wengine hawajaanza kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali ili kuweza kumaliza hili tatizo ni vyema basi wafikie mahali pa kutumia takwimu kutoka kwenye Halmashauri zetu hususani takwimu ambazo ni maoteo ya watu wanaomaliza shuleni. Wakiweza kutumia hizi takwimu za maoteo watajua upungufu upo kiasi gani na mahitaji kiasi, watakapojua hivyo wataweza kuwasadia kama ni wadau wa elimu, wazazi, walezi ili kujumuika ku-cover ule upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine nataka niongelee kuhusu utitiri wa kodi uliokithiri katika Halmshauri zetu. Ni ukweli usiopingika kwamba uhai wa Halmashauri yoyote unategemea makusanyo ya kodi lakini kodi hizi kwa sasa baada ya Serikali Kuu kuchukua vyanzo vingi vya mapato kutoka kwenye Halmashauri zetu, Halmashauri zimebakia hazina kitu hivyo zimebuni njia mbalimbali za kupata kodi. Matokeo yake kumekuwa kuna msururu wa kodi mkubwa sana ambapo wananchi maskini hawezi kulipa. Matokeo yake wanatengeza njia za kusababisha kukwepa kodi au kutokulipa kodi bila shuruti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali iweze kutengeneza mazingira rafiki au elimu itolewe kwa hao wananchi ili waweze kulipa kodi bila shuruti kwa sababu tumeshuhudia, tumesikiliza kwenye taarifa ya habari tumeona Singida kule mauaji yametokeo, raia ameuwawa kwa risasi lakini raia huyu chanzo chake tumeambiwa alikwepa kodi. Kwa hiyo, niiombe Serikali ihakikishe kunakuwa na mazingira rafiki ya ulipaji wa kodi lakini pia na hawa watu wanaokusanya kodi wawe ni marafiki kwa walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine napenda kuzungumzia ukatili wa kijinsia. Ukatili wa kijinsia sasa hivi umekuwa mkubwa kupita kiasi ambapo wanafunzi wetu wanabakwa, wanalawitiwa na wanafanyiwa vitendo hivi na watu tu wenye akili zao timamu lakini hata huko shuleni wanafunzi kwa wanafunzi wanalawitiana. Kwa hiyo, niiombe sasa Wizara ya Elimu na TAMISEMI tuangalie tunamalizaje suala hili, kujenga mabweni mfano ya Ihungo Sekondari, yale majengo yakijengwa vizuri wanafunzi wataepuka kufanya vitendo vya ubakaji na kulawitiana. Nishauri tena wazazi tusipeleke shule watoto wenye umri mdogo kwa sababu ndio wanaoathirika kwa kuharibiwa na kaka zao. (Makofi)

Suala lingine ni upandaji madaraja kwa walimu. Walimu kwa sasa wamekosa morale ya kufanya kazi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipata nafasi nami jioni hii nichangie hotuba iliyopo mbele yetu. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa nanyi jioni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwashukuru wanachama wa Chama cha Wananchi CUF, kwani kwa kupitia wao kwenye Mkutano wetu wa Saba tumeweza kumchagua Mheshimiwa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti wetu mpya. Hakika wana-CUF tunaweza na Mheshimiwa Prof. Lipumba ndiyo Mwenyekiti wetu halali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja, naomba nijielekeze kwenye mada na nitajikita kwenye suala la upandishwaji wa mishahara ya watumishi wa umma. Ni ukweli ulio wazi kwamba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani watumishi hawa wa umma hawajaweza kuongezwa mshahara wao. Itambulike kwamba annual increment ni takwa la Kikatiba kwa mujibu wa Standing Order lakini watumishi hawa wa Tanzania kwa miaka mitatu mfululizo hawajaongezwa mshahara kama Katiba inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue ni lini sasa Serikali yetu itawaongeza mishahara hawa watu ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanafanya kazi pasipo motisha wa aina yoyote? Nataka niiulize Serikali, kwa sababu kupandishwa mishahara ni takwa la kisheria, je, iko tayari sasa kuwapa mishahara yao kwa mkupuo ambayo wame-delay kuwapa kwa miaka mitatu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nijikite kwenye vitambulisho vya wajasiriamali. Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa vitambulisho 670,000, lengo ikiwa ni kuwatambua hawa wajasiriamali wadogo lakini pia ni kuwatafutia mahali ambapo watafanyia biashara zao pasipo kubughudhiwa kwa aina yoyote. Mimi sikudhani kama hili lilikuwa ndiyo hitaji lao haswa la kuwatambua hawa wafanyabiashara ns wajasiriamali wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya nikiwa na sababu kwamba wafanyabiashara hawa kwanza wanatakiwa walipe Sh.20,000 ambayo baadhi yao ni kubwa mno. Unamkuta mama anauza mbogamboga, mtaji wake ni Sh.3,000 lakini unamtaka mjasiriamali huyu mdogo alipe Sh.20,000 anaitoa wapi? Hata kama tunataka tuongeze mapato siyo kwa namna hii. Nashauri Serikali ifanya tathmini itambue, je, hawa wajasiriamali wadogo wanahitaji kutambuliwa au wanahitaji mitaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba lengo ni kuwatambua na kuwatafutia mahali pa kufanyia biashara wafanyabiashara wadogo lakini bado maeneo ya kufanyia biashara hawana, wanatembea hovyo na bado huko mitaani wakitembea wanasumbuliwa na Mgambo, bado watendaji wetu huko wanawasumbua. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa iweze kutumiza lengo lake la kuwatambua, lakini pia waweze kuwatafutia mahali pa kufanyia biashara ili waweze kufanya biashara kama wafanyabiashara wengine. Kama itawezekana, hii Sh.20,000 ni kubwa sana, tunaiomba Serikali hawa wafanyabiashara wapunguziwe iweze kuendana na mitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upandishwaji wa vyeo na madaraja kwa wafanyakazi especially walimu. Suala la kupandishwa madaraja kwa walimu sasa hivi limewekewa masharti magumu sana. Leo hii walimu wanaambiwa watapandishwa madaraja kwa kuangalia bajeti ya Serikali, lakini pia wataangalia Performance Appraisal ya huyu mwalimu na uwezo wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wazi kabisa vyanzo vingi vya mapato vimechukuliwa na Serikali Kuu, baadhi ya Halmashauri hazina vyanzo vya mapato vya kueleweka. Kwa hiyo, kama hizi Halmashauri hazina vyanzo, leo tunawaambia hawa wafanyakazi watapandishwa kwa kuangalia bajeti ya Halmashauri, ni lini hawa walimu sasa au Halmashauri zitaweza kujikidhi mpaka ziweze kuwapandisha hawa walimu madaraja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema Performance Appraisal, kazi ya mwalimu ni kufundisha lakini suala la kusema kumpima kwa kuangalia wanafunzi wamefaulu kwa kiasi gani, hilo suala halimhusu mwalimu. Hivi vigezo vilivyowekwa kwa ajili ya kumpandisha huyu mtumishi naomba viangaliwe kwa jicho lingine tena kwa sababu ni kumbana mwalimu na kumpotezea haki zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuangalia posho za Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji. Kama walivyosema wenzangu, hawa Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji ndiyo viongozi wa kwanza katika maeneo yetu. Hawa watu wanasumbuliwa usiku kucha, watu wakipigana huko na wake zao kwa Mwenyekiti wa Mtaa, mtu amekosea njia, amepotea anakwenda kwa Mwenyekiti wa Mtaa, amlishe na amfanyie kila kitu lakini mtu huyu hana posho wala kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilimsikia Mheshimiwa Waitara pale anasema ni kazi za kujitolea na wawe na shughuli nyingine. Kama Serikali imepanga hadi bajeti ya kuweza kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ina maana tunawatambua hawa watu lakini leo hii tunasema ni kazi ya kujitolea. Kama ni kazi ya kujitolea basi kulikuwa hakuna haja ya kutenga hata bajeti kwa ajili ya uchaguzi wa kuwachagua viongozi hao. Naiomba Serikali iwatambue watu hawa, wao ndiyo wanafanya kazi kubwa na ndiyo hata sisi tunapopatia kura zetu huko. Naomba tuwaangalie hawa watu kwa jicho la tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni elimu bure. Suala hili ni zuri sana, kwanza limeweza kusaidia watoto wa kimaskini waweze kwenda shule kwa wingi lakini pia wazazi wamepunguza baadhi ya gharama kwa elimu bure. Hata hivyo, hili suala la elimu bure haliendi sambamba na uongezekaji wa miundombinu. Sasa hivi asilimia ya wanafunzi itakuwa ni kubwa sana lakini miundombinu ni ile ile, madarasa yale yale na matundu ya vyoo yale yale. Kama tutakuwa tunajisifu tu tuna elimu bure ilhali tunachofanya pale ni kuongeza idadi ya wanafunzi lakini quality education haipo. Ili tuweze kupata quality education ni lazima basi hii elimu bure iende sambamba na ongezeko la wanafunzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kumekuwa na matatizo sana sasa hivi wanafunzi wengi wamechelewa kuanza kidato cha kwanza kwa sababu madarasa hayakuwepo na ndiyo maana wadau wengi wa elimu wamejishirikisha kwa njia moja au nyingine kuhakikisha madarasa yanapatikana. Niiombe Serikali kama kweli tunataka kuboresha elimu yetu, tutumie takwimu za maoteo, takwimu zipo zinafanya kazi gani? Kama kweli takwimu zinafanya kazi leo Serikali ingekuwa haina mzigo wa kujua wilaya fulani kuna upungufu wa madarasa ama nini, ni kwa sababu tu hizi takwimu za maoteo hazitumiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni TASAF. Tunaelewa kabisa kwamba TASAF ni mpango wa kunusuru kaya zilizo maskini na mradi huu ni mradi unaofadhiliwa na mashirika ya nje ya nchi lakini nachokiona kwenye TASAF bado hatuna nia ya dhati kabisa ya kuwasaidia hawa watu wa kaya maskini. Unakuta pesa anayopata mtu wa Dar es Salaam ni sawasawa na anayopata mtu Ulindwanoni huko Kaliua. Tuelewe kabisa kwamba tuna lengo la kuzisaidia hizi kaya maskini lakini hizi kaya maskini ziko maeneo tofauti na zina mahitaji tofauti. Kama tunawapa pesa ambayo inatolewa kwa kiwango kile kile, kwa maeneo tofauti, tunakuwa hatufanyi sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Dar es Salaam …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya na uzima mpaka leo nipo humu ndani.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpe pongezi sana Mheshimiwa Kangi na Naibu wake, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Mkoani kwangu Tabora yalitokea matatizo ya watoto kukamatwa, nilishirikiana na Mheshimiwa Kangi kuhakikisha hali hiyo inakuwa shwari.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, napenda nimwambie Mheshimiwa Kangi wanafanya kazi nzuri lakini bado wanahitaji maboresho katika maeneo yafuatayo. Nitaanza na usalama barabarani, hawa watu wanafanya kazi nzuri sana, tumeona ajali za barabarani zimepungua na watu wanaendesha magari yao vizuri sana lakini eneo hili kuna shida mpaka baadhi ya Askari wa Usalama wa Barabarani wamebadilishwa majina badala ya kuitwa traffic wanaitwa MaxMalipo au TRA ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhana nzima ya kulinda usalama wa barabarani wa watembea kwa miguu na wa magari haipo tena badala yake wamefanya kama kile ni kitengo cha kukusanya kodi. Mtu anakamatwa badala ya kuambiwa kosa lake kwanza anaulizwa leseni. Baada ya hapo wanamwambia njoo nyuma huku. Sasa unampeleka kule nyuma kufanya nini?

MBUNGE FULANI: Nyuma wapi?

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Namaanisha nyuma ya gari. Akirudi tayari lile kosa limekwisha anaendelea na safari.

SPIKA: Mheshimiwa Rehema, nakukumbusha lugha za Kibunge. (Kicheko)

Endelea kuchangia Mheshimiwa Rehema.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi napenda niishauri Serikali, tunaomba dhana nzima ya hawa Askari wa Usalama Barabarani iwe ni kuelimisha hawa watumiaji wa magari na watembea kwa miguu na isiwe ni kitengo cha kukusanya kodi. Leo hawatoi elimu wanakaa kufanya kazi ya kukusanya kodi. Mheshimiwa Kangi, tunataka utuambie hivi Kitengo cha Usalama Barabani na chenyewe ni source ya mapato ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikisalia hapo hapo kuna hawa watu wanaitwa PT, kiukweli hawa mfano kwa kule kwetu Tabora imekuwa ni shida. Badala ya kutembea mipakani mwa mji sasa wanasumbua bodaboda kila kukicha yaani bodaboda hawafanyi kazi kwa amani. Tukumbuke kwamba hawa watu wamejiajiri wenyewe na wengine pikipiki sio zao, aweze kupata hela ya tajiri na ya kuhudumia familia yake lakini hawa PT kila bodaboda akijipindua wako naye na wanataka chao na hiyo haina risiti wala nini, wanaweka mifukoni mwao. Mheshimiwa Kangi tunaomba hawa watu wa PT uwaangalie kwa jicho lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la upoteaji wa vithibitisho pindi vinapofika Polisi. Nasema hili nikiwa na uhakika, mimi namiliki bodaboda. Kuna siku bodaboda yangu imekamatwa ilivyofika Polisi, kesho yake nakwenda kuchukua pikipiki yangu haina mafuta wala betri. Sasa tunaamini kabisa kwenye Kituo cha Polisi ni mahali salama na wana kazi ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, nataka utuambie Mheshimiwa Kangi…

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, ajenda hiyo naomba uiache kwanza ni conflict of interest lakini pili biashara nyingine tuwaachie wananchi jamani, Mbunge unafanya biashara ya bodaboda inakuwaje? (Kicheko)

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ndiyo ni katika kuongeza uchumi.

SPIKA: Endelea na ajenda nyingine Mheshimiwa Rehema.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. Suala lingine nataka tuambiwe maana ya VTS (Vehicle Tracking System). Tunajua Jeshi la Polisi linafanya kazi na Idara nyingine kama SUMATRA na tumeona magari ya mizigo na mabasi yamefungiwa hivi ving’amuzi lakini mimi sijajua lengo halisi la kufunga hivi vidubwasha ni lipi? Kwa sababu nimepanda kwenye basi yaani dereva akiongeza spidi kinachofanyika pale ni ule mlio tu unasikia chwi, chwi, chwi lakini hakuna kusema kama ni kile kifaa kinapunguza ule mwendo wa gari. Kama lengo ni kusikiliza tu ule mlio haina haja ya kuwawekea hao wenye magari hivi vitu.

Mheshimiwa Spika, tunataka tujue, hii sauti inavyolia mule kwenye basi hatua gani zinachukuliwa dhidi yake kama hatapunguza mwendo? Atakapoamua kuongeza mwendo kwa sababu kuna magari siku hizi yana TV na music dereva akaamua tu kuchapa mwendo kwa sababu abiria hawatasikia ile sauti matokeo yake atasababisha ajali na huyu mtu bado akienda kule mbele kwa sababu ameenda spidi kubwa atakutana na tochi, je, atakuwa charged mara mbili au vipi? Maana tunaambiwa ikilia ile sauti kwa bosi na SUMATRA inasoma, je, huyu mtu atakuwa anachajiwa mara mbili?

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ucheleweshwaji wa upelelezi wa makosa mbalimbali. Haki ya mtuhumiwa ni kupelekwa Mahakamani. Tunajua kabisa muda wa kumpeleka Mahakamani mtuhumiwa ni saa 48 au 24 lakini kuna watu leo wako mahabusu takriban miaka sita hawapelekwi Mahakamani na hata wakipelekwa Mahakamani wanaambiwa hii Mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi yao. Kwa nini waendelee kukaa mahabusu ilhali Mahakama ambayo itashughulia kesi zao haipo? Wanaongeza msongamano na gharama kubwa ya kuhudumia mahabusu wengine. Tunaomba tuambiwe, je, hawa watu wanaokaa mahabusu muda mrefu mfano hawa Mashekhe wa Uamsho, kuna watu walikamatwa kule Arusha mpaka leo takriban miaka sita hawajasomewa hukumu yao, ni lini upelelezi wao utakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni utumikaji wa Polisi kama sehemu ya wasimamizi wa uchaguzi. Inahuzunisha sana Polisi kutumika kama wasimamizi wa uchaguzi ilhali wao kazi yao ni kusimamia usalama wa raia na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya chaguzi za marudio sehemu mbalimbali lakini unakuta Polisi anakwenda mpaka chumba cha kuhesabia kura, Polisi huyu naye anakuwa ni msimamizi. Kweli leo Polisi wanaacha kutekeleza majukumu yao wanayopaswa kufanya wamekuwa wasimamizi wa uchaguzi. Tunaomba hawa Polisi wasitumike, wafanye kazi wanazopaswa kufanya na kama wanafanya hivyo, basi wafanye kwa pande zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu maslahi ya Polisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami nichangie kidogo kwenye hii Wizara. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala, kwani bila yeye sisi hatuwezi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba moja kwa moja nijikite kwenye mada. Ni ukweli uliowazi kwamba sekta ya kilimo inachangia kwa asilimia kubwa sana katika kutoa ajira kwa watu wenye elimu na hata wasiokuwa na elimu. Hata hivyo, sekta hii imekumbwa na changamoto kubwa sana hususan kwenye changamoto ya masoko especially mazao ya biashara.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye zao la tumbaku. Mkoa wa Tabora kama ilivyo mikoa mingine inayolima tumbaku umekumbwa na tatizo kubwa kabisa la zao la tumbaku kuwa linadorora siku baada ya siku. Yote hii inasababishwa na kauli mbalimbali kwamba zao hili linasababisha kansa na kauli nyingine mbalimbali ambazo hazina tija kwa mkulima. Mimi naona tatizo kubwa sio hizi kauli, tatizo kubwa lipo kwenye Serikali na nini kinasababisha, kinachosababisha mpaka hili zao kuzorota ni kupotea kwa hawa wanunuzi wa zao la tumbaku baada ya kuwa kuna milolongo mingi ya kodi na tozo zisizokuwa na faida kwa hawa wanunuzi.

Mheshimiwa Spika, mfano, ni hii export levy; sasa hivi export levy imepanda kutoka 0.25% mpaka 1% kwenye export value sasa kama hii tozo inapanda kwa kiasi hicho inamkandamiza sana na kumuumiza huyu mnunuzi hali inayopelekea mpaka aamue asinunue mazao yetu. Hii impact yake ni nini? Tumeona kuna kampuni moja ya kununua tumbaku sasa hivi imefunga oparesheni kutokana na kwamba imeshindwa ku-afford hizi gharama.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Serikali kushindwa kurudisha hii VAT returns, suala la VAT returns ni suala ambalo lipo kisheria na kikatiba na inapaswa kila mwaka lirejeshwe kwenye haya makampuni ya net exporters, lakini sasa hivi kwa miaka kama mitatu mfululizo huko nyuma hii VAT returns hairudishwi. Sasa tunajiuliza kama huko nyuma VAT returns ilikuwa inarudishwa nini kimesababisha mpaka dakika hii VAT returns ambayo ndiyo ilikuwa inawa-bust hawa wanunuzi waweze kununua tumbaku kwa wingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa tunaomba Wizara ituambie je, hii export levy ambayo imepanda kwa kiasi hicho itairudisha lini lakini vile vile hii export value na yenyewe itarudishwa lini na VAT kwa sababu tunaona wakulima wetu hawajui hatima yao ni nini, leo makampuni ambayo yanafunga operesheni zao tunaona kuna redundancy kubwa ya wafanyakazi, lakini tunaona pia halmashauri nyingi mfano Tabora Mjini, Urambo wapi zinakosa cess, lakini pia wakulima sasa hivi mpaka wanapewa limitation, badala ya kulima kama walivyokuwa wanalima zamani sasa hivi anaambiwa lima tani kadhaa au kilo kadhaa kitu ambacho kinaikosesha hata Serikali yetu mapato ya forex.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kwenye korosho; korosho ndiyo limekuwa zao mbadala kwa Mkoa wa Tabora baada ya kuonekana zao la tumbaku linasuasua kwa kiasi kikubwa sana. Hata hivyo, zao hili linapelekwa kisiasa siasa zaidi hali ambayo inawakatisha tamaa wakulima kuingia kwenye hicho kilimo cha korosho. Naomba sasa hii Wizara ili zao hili liweze kulimwa na wengi na liwe lenye tija basi kwanza tunaomba elimu itolewe juu ya zao la korosho. Pia suala lingine hii miche kule kwetu inauzwa sasa kama inauzwa watu wanashindwa kununua badala ya kupewa bure, leo wanauziwa mche mmoja ni shilingi 1,000. Kwa hiyo tunaomba hii kama inawezekana wapewe bure ili waweze kupata moral.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni vitambulisho vya wakulima na hii bima ya wakulima. Hili suala ni zuri sana kwani litawawezesha wakulima wetu kuwa na wenyewe wanatambulika juu ya kilimo chao, lakini tunaona tu kuna story story tu kwenye hiki kitabu cha Waziri kwamba mpaka dakika hii hakuna kanzidata inayoonesha ni wakulima wangapi wa tumbaku ambao wamesajiliwa kwenye hiyo kanzidata yake.

Mheshimiwa Spika, pia suala lingine ni kwenye hii bima ya wakulima. Tunaelewa kabisa kwamba sasa hivi kuna mabadiliko makubwa sana ya hali ya hewa, mafuriko yamekuwa ni mengi, ukame umekuwa wa kutosha, sasa hivi wakulima wetu wanalima kilimo cha mashaka mashaka sana. Kama kweli hii bima itatolewa kwa hawa watu wetu basi nina uhakika kabisa hili suala ni zuri na namwomba Waziri waliendeleze ili wakulima wetu sasa pindi wanapolima wawe wana uhakika kwamba hata ikitokea janga Fulani, basi wawe na uwezo wa kufidiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine ni kwenye suala la pembejeo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni ya leo kuchangia hotuba ya Rais. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuiona siku leo. Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwepo hapa leo katika Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kunikubali na kunipokea na kuwa mwanacha wa Chama cha Mapinduzi kwani awali nilikuwa upande ule wa pili. Hivyo, nikishukuru sana Chama cha Mapinduzi kwa mapenzi yake mema kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Ulyankulu ambao walikuwa na imani na mimi wakiamini kabisa ni mwakilishi wao mzuri. Naamini nina deni kubwa kwao na nitahakikisha nawatendea kulingana na uwezo wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais kama ifuatavyo. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amesisitiza jambo kubwa sana kuhusu amani lakini hii amani kwa baadhi ya wananchi wa Jimbo langu hususan kata zile tatu ambazo zilikuwa zikikaliwa na wakimbizi amani inaweza ikatoweka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa dhidi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa mwaka 2015 wakiwa wakimbizi walipewa uraia wa Tanzania lakini bado wanakuwa treated kama wakimbizi. Hakuna jambo lolote la maana linalofanyika kule, shughuli za kimaendeleo hazifanyika lakini bado wanachangia shughuli kubwa za ulipaji wa kodi, wanateseka kwa kiasi kikubwa. Niiombe sasa Serikali kupitia Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Mambo ya Ndani na Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria waweze kuiangalia hii Sheria Na.9 ya Wakimbizi ambayo inawabana sana hawa watu ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani na waishi kama wananchi wengine wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa jimbo hili hawawezi kufanya shughuli zozote, hivi sasa hata kujenga nyumba pale hawajengi, hata choo kikidondoka pale ni lazima wapate kibali kutoka kwa mkuu wa makazi ndiyo waweze kujenga. Tunaiona Serikali inafanya jitahada sana kuhakikisha inapeleka maendeleo pale lakini bado sheria ile inazidi kukwamisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetupelekea shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga nyumba kwenye Chuo cha Ufundi VETA, lakini sheria ile imebana zimekataliwa kujengwa. Pia shughuli za maendeleo kama kujenga madarasa na miundombinu mingine zimekataliwa. Hivyo nawaomba Mawaziri wanaohusika na suala hili mtupe mwongozo leo ili hao wananchi wetu wapate nafuu na wajue hatima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye nishati ya umeme. REA huko vijijini kwetu imekuwa ni mkombozi mkubwa, sasa hivi vijiji vingi umeme unawaka lakini kuwaka kwa umeme huko bado kuna changamoto. Umeme huu umepita kwenye vijiji tu haujaenda kwenye vitongoji. Hivi navyoongea baadhi ya kata zangu kama mbili Silambo na Kata ya Uyowa hazijapata umeme kabisa, hivyo naomba zipate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikibakia hapo hapo kwenye umeme wa REA suala la nguzo imekuwa ni tatizo, tunauziwa nguzo kwa kiasi cha shilingi laki tatu na zaidi. Mimi mwenyewe ni muhanga wa kuuziwa nguzo kwenye eneo langu. Tunaambiwa kwamba umeme wa REA ni Sh.27,000 lakini tunapohitaji kuingiziwa umeme, nyumba ikiwa umbali kuanzia mita mia moja na kuendelea mwananchi unahitajika ulipie nguzo ya umeme. Hii hali haikubaliki na wananchi walio wengi ni maskini hawawezi ku-afford kununua nguzo hizi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aweze kuliingilia kati suala hili na ikiwezekana kama ni suala la kununua nguzo basi itolewe bei elekezi ambayo ni rafiki kwa hao wananchi ili waweze kumudu gharama hizi na kuingiza umeme kwenye nyumba zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni afya. Jimbo langu la Ulyankulu lina kata 15 lakini vituo vya afya vilivyoko na vinavyofanya kazi ni kituo kimoja tu cha Barabara ya 10, hivyo msongamano ni mkubwa sana kutoka sehemu mbalimbali ambapo watumishi wa ile hospitali wanazidiwa. Niombe sasa bajeti ipangwe ili vituo vingine vya afya kama Kituo cha Mwongozo, Uyowa na Kashishi na vyenyewe viwekwe kwenye mpango ili vipatiwe pesa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami nichangie Mpango ulioko mbele yetu. Kwanza, niungane na waliotangulia kuchangia Mpango huu wa maendeleo ambao dhima yake kubwa ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wowote hauwezi kufanikiwa endapo maeneo fulani hayatapewa kipaumbele. Nitaanza na eneo la kilimo. Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanashiriki kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kilimo lakini kilimo hiki sasa hivi badala ya kuwa uti wa mgongo kinakuwa ni kiua mgongo cha wananchi walio wengi, hasa wa maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu, kilimo sasa hivi hakina tija kwa wakulima wetu badala yake kimekuwa kinaleta dhiki kwa hawa wakulima wetu na hatimaye kuwasababishia kukata tamaa. Hivyo, niiombe na kuishauri Serikali, kama kweli tuna nia ya dhati ya kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mpango huu, basi Sekta hii ya Kilimo ipewe kipaumbele hasa kwa kuiongezea bajeti. Pia masoko kwa ajili ya bidhaa za wakulima wetu yapatikane na yawe na bei elekezi ili hawa wananchi wetu waweze kuwa na uhakika wa kuuza mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bima ya kilimo; suala hili kama halitapewa kipaumbele wananchi wetu watakuwa na uhakika hata kama yatatokea mabadiliko ya hali ya hewa, basi watakuwa na uhakika wa kufidiwa endapo matatizo ya kijiografia yanaweza yakatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye kilimo ni suala la kuanzisha hizi block farming ambazo kwa kiasi kikubwa zitakuwa zina tija kwa hawa wananchi wetu kwani asilimia kubwa ya maeneo yaliyopo Tanzania hayalimwi kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, kama tutaanzisha hizi block farming, nina uhakika kabisa wananchi watalima kwa eneo kubwa na pia watakuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uhakika wa pembejeo kufika kwa wakati na kuwezesha mazao ambayo yako kwenye ushindani katika Soko la Dunia. Mfano kwenye maeneo yetu, mazao kama tumbaku, chikichi na korosho, ni mazao ambayo yanaweza yakahimili udongo kwenye maeneo yetu. Hivyo, naomba mazao haya sasa yawekewe umuhimu mkubwa na wananchi waweze kuelimishwa juu ya kulima mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la TARURA. Hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda endapo tu uhakika wa kusafirisha mazao yetu hautakuwepo kutokana na barabara nyingi kuwa mbovu. Barabara nyingi sana ambazo ndiyo zinalisha barabara kubwa ni mbovu na hazipitiki. Hivi mfano ninavyoongea mimi barabara yangu ya kutoka Mnange - Uliyanhulu, Urambo - Uliyanhulu, Uliyanhulu – Tabora ambazo zinapitisha bidhaa nyingi sana, ni mbovu na hazipitiki. Naomba TARURA iongezewe bajeti kwani bajeti inayowekwa ni ndogo sana ukilinganisha na mtandao wa barabara unaohudumiwa na TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naziomba Halmashauri na ikiwezekana zilazimishwe, ziweze kuwa na vitendea kazi; mitambo ya kutendea kazi kama excavator, magreda na kadhalika. Vifaa hivi vikiwepo Halmashauri zetu zitakuwa na uwezo wa kufanya matengenezo ya barabara zetu pindi inapotokea uharibifu wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nafikiria kuna haja sasa ya kufanya mabadiliko kwenye bajeti ya TARURA ya TANROADS. Haiwezekani kila mwaka tutegemee bajeti hiyo hiyo ya TARURA ya asilimia 30 na TANROADS asilimia 70. Naomba kama kutakuwa na demand na kwa wakati huo, basi pawepo na mabadiliko. Kama demand itakuwa ni kubwa kwa wakati huo, TARURA iweze kuongezewa bajeti kuliko mtindo uliopo sasa hivi wa kutegemea bajeti hiyo hiyo tu kila mwaka bila kuangalia kwamba mahitaji yanabadilika kulingana na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la ukusanyaji wa mapato. Katika Mpango huu kilicholeta mtafaruku mpaka changamoto hizi zitokee na Mpango usifanikiwe inavyotakiwa ni kukosekana kwa mapato kwa wakati na yanayotosheleza. Hivyo, naomba sasa Halmashauri na Serikali ziweze kubuni vyanzo vingine vya mapato ambavyo ni vikubwa kuliko kutegemea vyanzo vidogo vidogo. Leo Serikali inategemea vyanzo vidogo vya mapato hali ambavyo inasababisha mapato yasipatikane. Pia ni kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia watu wenye utaalam kuliko task force, kazi yao ni ku-force tu watu na kusababisha utoroshaji wa mapato kwa njia ambazo siyo stahiki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni ya leo niweze kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. Awali ya yote, napenda kuwapongeza dada yangu Ummy na timu yake wanafanya kazi nzuri na tuna imani nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja, nitaanza kujikita kwenye suala la afya. Afya ndiyo mtaji wa mwanadamu wa aina yoyote lakini suala hili kwa baadhi ya maeneo linaonekana kama halipewi kipaumbele cha hali ya juu. Mfano nikiangalia katika Jimbo langu huwa naliita Burundi kwa sababu linahudumia asilimia kubwa ya wananchi waliotoka Burundi lakini lina jumla ya Kata 15 lakini ndani ya hizo kituo cha afya ni kimoja tu. Hali hii inasababisha msongamano mkubwa sana wa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali kwenda kutibiwa kwenye kituo hicho hali inayowafanya mpaka wahudumu kuzingirwa na wagonjwa. Pia wagonjwa wanaweza wakafa pale pale kwa sababu wanasubiri huduma kwa muda mrefu na wengine kujifungulia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali kwa maeneo ya pembezoni hebu tuyape kipaumbele na kuona na yenyewe yanafaa kupatiwa huduma za afya kama zahanati na vituo vya afya. Jimboni kwangu kuna kituo kimoja tu lakini kuna vituo viwili vya afya mfano Kituo cha Uyoo na Mwongozo tayari vimeshaanza kujengwa na vimefikia hatua za mwisho. Niiombe Serikali iweze kupeleka fedha kwenye vituo hivyo viweze kumalizika na vianze kufanya kazi kuwahudumia hawa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine kwenye afya hapo hapo ni bima iliyoboreshwa. Suala la bima iliyoboreshwa naona kama haiwasaidii wananchi wetu kwa sababu walivyokuwa wanakata waliona kwamba itakuwa ni suluhisho na mbadala pindi wanapokuwa hawana pesa lakini wanapokwenda kwenye hivi vituo vyetu vya afya wakifika pale, mfano kama vituo vya afya na zahanati nyingi hazina hata maabara, kwa hiyo akifika pale inamlazimu aende kwenye zahanati zingine au mahali pengine kwenda kupima ambapo inamuongezea gharama, kwa hiyo, hii bima inakuwa kama vile haina faida. Vilevile ana bima anakwenda kwenye zahanati hakuna dawa anatakiwa anunue. Tunakwenda kuanzisha bima ya afya kwa wote hivyo kabla hatujaanzisha niombe Serikali ifanye tathmini, je, hii bima ya afya iliyoboreshwa imesaidia kwa kiasi gani kabla ya kuingia kwenye hii bima ya afya mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye sekta ya elimu. Kiukweli elimu bado kwenye maeneo yetu ni changamoto kubwa sana. Miundombinu ya elimu kama madawati, madarasa, matundu ya vyoo bado hayatoshelezi. Cha ajabu tunapongeza Serikali imeanzisha mifumo mingi sana ya kupata taarifa lakini hazitumiki. Leo ikifika mwisho wa mwaka Waziri Mkuu anaanza kupiga kelele madarasa; hivi haya maoteo na hizi takwimu ambazo mnazikusanya kila mahali mnazitumia kwa shughuli gani kiasi kwamba tunafanya haya mambo ni kama vile dharura. Niiombe Serikali mifumo iliyoianzisha basi itumike kusaidia mambo yasifanyike kwa ghafla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni masharti ya uhamisho. Mtumishi kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni suala la kawaida na lipo kisheria na anapokwenda kuhamia sehemu nyingine ana sababu ambazo yeye zinamfanya mpaka ahamie kule lakini masharti ya uhamisho sasa hivi yamekuwa magumu mno. Leo mtu anaambiwa kuhama kituo kimoja kwenda kituo kingine mpaka apate mtu wa kubadilishana naye, anamtoa wapi? Unakuta watu wengine mfano wa vijijini; shule nyingi za vijijini kule watumishi wengi ni wanaume wanataka wafuate wake zao au wanawake wafuate waume zao, inafikia wakati kama walimu wanaamua kutumia watoto wetu kujipoza. Hali hii kweli ni mbaya, inawaingiza watu kwenye majaribu makubwa, wanaume wanajiingiza kwenye mambo ambayo hayafai, ndoa zinavunjika na wanafunzi wetu tunawaingiza katika mtego mkubwa wa kufanya mapenzi na walimu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni TARURA. Kiukweli TARURA bado ni changamoto, barabara zetu huko vijijini hazipitiki. Niombe TARURA basi iongezewe bajeti lakini tofauti na hapo TARURA izilazimishe Halmashauri kama nilivyoongea Bunge lililopita ziweze kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuongeza bajeti ya TARURA ili iweze kuhudumia barabara kwa kiwango kinachotakiwa. Unakuta sasa hivi TARURA kwanza hawashirikishi hata Madiwani au Wabunge, unaambiwa barabara yako hii itatengenezwa bila hata wewe Mbunge au Diwani kushirikishwa wakati wewe Diwani au Mbunge ndiyo unajua barabara zipi zina changamoto na barabara zipi zina manufaa kwa ajili wananchi wetu. Nimuombe Waziri awaambie TARURA waweze kushirikisha Madiwani na Wabunge kwenye upangaji wa ujenzi wa hizi barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kwenye mgawanyo hizi asilimia 10 za vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Hizi pesa kwa kiasi kikubwa sana zinakwenda kwa vikundi ambavyo vinakuwa vinarejesha lakini vile ambavyo vinaonekana vinasuasua bado havipewi kipaumbele. Nina maana kwamba tunakwenda kwa kuangalia vile vinavyorejesha lakini hatujui ni changamoto gani zinasababisha hao wengine wasirejeshe ili watu wengine wapate. Hivyo niombe sasa kwenye vikundi ambavyo vinakuwa labda havirejeshi ile pesa ambayo inapangwa kwa ajili ya kwenda kufanya ufuatiliaji ifanye kazi ikiwa ni pamoja na kujua changamoto ambazo wanapitia hivi vikundi ambavyo vinashindwa kurejesha ili waweze kuwasaidia kwa sababu lengo ni kuwafanya hawa wananchi waweze kujikwamua kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni nyongeza ya mishahara. Watumishi wetu ndani ya miaka mitano hawajapata nyongeza yoyote ya mishahara. Ndugu zangu hata sisi humu ni watumishi wa Serikali lakini ndani ya miaka mitano kweli hata kanyongeza kidogo! Jamani maisha sasa hivi yamekuwa magumu na vitu vimepanda bei. Nyongeza ya mshahara inamfanya huyu mtumishi apate morale ya kufanya kazi lakini kama hawa watu wananung’unika wanakwenda kutafuta vyanzo vingine mpaka walimu wanakuwa bodaboda, hebu mwaka huu tuwaongeze za mshahara. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kunipatia nafasi hii awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai mpaka leo nipo hapa Bungeni. Lakini sambamba na hilo nianze kwa kuwapongeza viongozi wa wizara hii Kaka yangu Mheshimiwa Profesa Mkenda na kaka yangu Mheshimiwa Bashe pale mnafanyakazi vizuri Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na mchango wangu kwenye hii wizara nikiwa kama mkulima wa zao la tumbaku namwakilishi wananchi waliowengi wanaolima zao la tumbaku naiona kabisa Serikali haina nia ya dhati kabisa ya kuhakikisha hili zao linaendelea kuwa ni kitega uchumi cha wananchi wetu, lakini pia ni mbadala wa kuweza kuhakikisha hawa watu badala ya mazao mengine yanayowafanya waweze kudidimia liweze kupanda mbele.

Mheshimiwa Spika, zao hili limekuwa na changamoto sana pamoja na kuwa Serikali ilituahidi mambo mazuri sana kuanzia mwaka juzi na mwaka jana, lakini bado naona kama ahadi zake hazitekelezeki na zaidi ya yote tunawadanganya wakulima wetu. Ni miongoni mwa wakulima watumbaku, nimefaidika sana na tumbaku, lakini kwa miaka mitano iliyopita bado hili zao limekuwa lina misukosuko mingi na bado mbadala wake hatujapata.

Mheshimiwa Spika, mfano leo hii tuliahidiwa wakulima tumbaku kwamba tutakuwa na uhakika wa soko la tumbaku yetu. Ninachokuambia kwenye jimbo langu wanunuzi watumbaku badala ya kununua bei elekezi iliyopangwa na Serikali ambayo ilikuwa ni dola 1.61, leo hii wakulima wameuza tumbaku yao chini ya bei elekezi dola 1.2. Wakati gharama za uzalishaji wazao hili kwa kilo moja ni dola 1.4, leo hii, gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa halafu unakwenda kununua tumbaku ya huyu mkulima kwa bei ndogo, tunania ya dhati kuhakikisha kweli huyu mkulima anasonga mbele au tunamrudisha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kama tunania ya dhati kabisa kuhakikisha ili zao na wakulima wetu wanasonga mbele hebu tuweze kuhakikisha haya masoko ya tumbaku yanakuwa yanafuata bei elekezi, lakini pia yawe na uhakika wa kununua hizi tumbaku. Tunaona kuna makampuni mengi yatumbaku halafu tunaita ya wazawa hayana uwezo wa kununua tumbaku matokeo yake wananchi wetu wanakuwa na madeni siku baada ya siku hawalipwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Wizara na Kaka yangu Bashe pale nakumbuka tumeongea sana hili suala la hawa wakulima wa tumbaku, kuna kampuni kama ya GRAND, kuna kampuni ya MAGEFA hizi kampuni zina waletea mzigo sana wananchi wetu. Tunaona kabisa, kwanza kuna riba ya asilimia nane ya mkopo, anayesababisha hii riba iongezeke ni hawa hawa wanunuzi wanashindwa kupeleka pesa kwenye vyama vya msingi matokeo yake anayekuwa responsible kwa ajili ya kulipia hiyo riba ya asilimia nane ni mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa Serikali msione kuna haja ya huyu anayesababisha hii riba iongezeke ndiyo awajibishwe. Nataka Kaka yangu Mheshimiwa Bashe na Kaka yangu Mheshimiwa Prof. Mkenda pale mkija ku-windup mtuambie hawa wanaouza kwanza tumbaku yetu chini ya bei elekezi mnawachukulia hatua gani? Lakini pia hawa wanaosababisha riba ya asilimia nane iongezeke ili hali Serikali imekaa kimya tunataka mtupe majibu la sivyo nitashika shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini, nakumbuka mwaka jana tukiwa kwenye kampeni Mheshimiwa Bashe tulikuwa naye kule na Mama Samia Suluhu wananchi wa Urambo, Kaliua, Ulyankulu wa Tabora kwa ujumla walipewa matumaini kwamba mwaka huu tumbaku yao itauzwa kwa bei nzuri na hata yale makinikia yale ma-reject yatauzwa kwa shilingi 500, nataka niwaulize hivi mlishawahi kufanya research kwamba hivi haya makinikia haya ma-reject mnaenda kuyanunua kwa shilingi 500 mnakwenda kuyafanyia kazi gani? Hatujawahi kuambiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunaona mwaka jana kuna mnunuzi kutoka Kenya na Sudan walikuwa wayanunue haya ma-reject kwa bei ya shilingi 100 je, mliweza kujifunza kwamba huko wanakoyapeleka wanayafanyia shughuli gani? Kuliko kuwaacha wakulima wetu huku mnanunua kwa shilingi 500 kumbe yanaweza kuwa yanabei kubwa huko nje ya nchi kuliko kuwakandamiza wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niombe tena suala jingine, suala jingine niombe sasa kulikuwa kuna mnunuzi mkubwa TLTC ambaye alikuwa anauhakika wa kununua tumbaku yetu…

(Hapa kengele ililia na kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu, lakini nikushukuru pia wewe kwa kunipatia nafasi ya kuchangia jioni hii. Nianze kwanza kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati hizi mbili kwa mawasilisho mazuri. Nianze moja kwa moja kwa kwenda kwenye point.

Mheshimiwa mwenyekiti, leo nitajikita hasa hasa kwenye mambo mawili. Jambo langu la kwanza ni kwenye utengaji wa asilimia 10 kwa ajili vijana, wanawake na wenye ulemavu. Ni ukweli usiopingika kabisa hili suala la utengaji wa hizi fedha asilimia 10 liko kisheria. Hata hivyo, tunaona katika baadhi ya halmashauri nyingi utengwaji wa hizi fedha hauendi na unakwenda kwa kusuasua mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inajitokeza pale ambapo tunaona kuna baadhi ya vikundi vingi sana vya akinamama, vikundi vya vijana lakini vya wenye ulemavu kila siku wanakwenda kule halmashauri kufuatilia hawapati, kina mama wanasumbuka mno na isitoshe kuna baadhi wanatoka mbali mno. Imagine kama mimi halmashauri yangu ipo mbali na jimbo langu, kwa hiyo kila siku wanagharamika kwenda halmashauri kufuatilia lakini hawapati majibu. Hii inatokana na ukweli kwamba hivi vikundi vingi vinavyopewa hizi fedha ni vikundi vya watu binafsi. Watu wengi wanaopewa hivi vikundi either ni viongozi wa vyama, lakini vikundi vingi ukivichunguza hivi wamiliki wa hivi vikundi ni watumishi wa halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sasa, nataka nitoe ushauri ili takwa la hizi fedha ziwalenge walengwa kabisa. Moja ya ombi tunaiomba Serikali kwanza iwe na database, kila halmashauri ituambie ni vikundi vingapi vimeomba, lakini ni vikundi vingapi vimepatiwa fedha na ni vikundi vingapi vimerejesha hizo fedha, tunataka tuzione.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uwepo na ufuatiliaji; hawa Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo hawafiki kule kwenye vile vikundi matokeo yake kuna vikundi hewa vingi mno. Kwa hiyo, kuwepo na model ya ufuatilia ili tuvijue vikundi halisi ni vipi? Kwa sababu kama hawa wananchi ambao tunaishi nao vijana na akinamama hawapati, hivi vikundi vinavyopata ni vya wapi? Ina maana kuna vikundi hewa vingi ambavyo vinamilikiwa na watu. Kwa hiyo, uwepo huo wa ufuatiliaji na data zijulikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uendeshaji wa masoko yetu na kuungua kwa masoko. Masoko yetu kwa sasa tunapata taarifa kila siku yameungua, yameungua, yameungua, lakini hatuambiwi nini chanzo cha kuungua masoko haya. Hata huvyo, tunajua kabisa haya masoko yamegharimu fedha nyingi sana katika ujenzi wake. Tukiangalia tu mfano wa Soko la Ndungai, lile soko ni miongoni mwa masoko yaliyogharimu fedha nyingi sana, lakini haya masoko hata uzalishaji wake kiukweli hauleweki na pamoja na kwamba yanatumia gharama kubwa lakini bado yanaungua kila siku. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwanza ije na mpango, pamoja na kwamba inayajenga lakini yawe na mpango wa kuya-rescue haya masoko yetu kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba Serikali pamoja na kwamba inayajenga haya majengo, tunaambiwa tuweke fire extinguishers kila sehemu zinasaidia nini zile fire extinguisher wakati kila siku yale masoko yanaungua. Ningeshauri kila masoko basi ziwekwe zile fire detectors ili angalau hata kama kuna viashiria vya moto viweze kutoa ashirio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapo hapo kwenye masoko, ningeweza kushauri Serikali kama inaweza inapofanya usajili wa hawa wafanyabiashara basi iweze kuweka na takwa la lazima la kila mfanyabiashara aweze kuwa na bima ya biashara. Hii bima ya biashara itawasaidia pale inapotokea majanga ya aina mbalimbali mfano pale inatokea moto. Tunaona wafanyabiashara wanawekeza mitaji yao mingi sana, wanakopa kwenye mabenki na sehemu mbalimbali ili kuendesha biashara zao. Linapotokea suala la moto soko limeungua, wanaambiwa tu mabenki wawaongezee muda wa kulipa so what? Wakati watu wameshaweka mitaji yao na imepotea, kwa hiyo nafikiria suala la bima litakuwa ni mkombozi kwa hawa wananchi ili waweze kufanya biashara vizuri, lakini wawe na uhakika wa kulinda mitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ameweza sasa kutuletea miundombinu ya elimu, maji na afya. Tumeona kwenye suala la UVIKO tumeletewa madarasa mengi sana, vituo vya afya lakini na kwenye miradi ya maji. Hata hivyo, huwezi kuwa unaongeza tu kitu bila ya kuangalia population, tumeongeza madarasa ya kutosha well and good lakini je, hawa watumishi ambao watakwenda kufanya kazi kule wapo wapi? Niiombe sasa Serikali pamoja na juhudi hizi nzuri inazozifanya lakini iende sambamba na kuongeza watumishi katika hii miradi ambayo imeianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai lakini pia niwapongeze Wizara na Mawaziri kwa presentation nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze hotuba yangu kwa kujielekeza hasa hasa kwenye uandaaji wa wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ni dhana pana sana na ni ndoto ya kila mtoto anapozaliwa na ni hitaji lakini pia elimu ni huduma. Tunapozungumzia suala la elimu linaanzia hasa hasa kumuandaa mwanafunzi akiwa ngazi ya awali. Lakini mfumo wetu wa elimu wa Tanzania hauanzi kumuandaa huyu kijana akiwa kwenye ngazi ya awali. Tunajua mtoto yoyote anapozaliwa huwa ana carrier yake, na hizi carrier zinatakiwa ziwe developed, lakini sisi hatufanyi hayo. Na kwa sababu dunia ya sasa hivi na Tanzania tupo kwenye mchakato wa kubadili mitaala; ninaomba sana na nisisitize, tuanze kuandaa hii Mitaala yetu kwa kuangalia hizi carriers za hawa watoto wetu ili kuwaendeleza kulingana na kile ambacho wanatamani wao kukifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mtoto anatamani asome hivi lakini Mtaala wa Elimu una-force asome hivi. Matokeo yake tunamrundikia masomo mengi, vitu vingi ambavyo hatimaye siku haviendi kuwa msaada kwa huyu mtoto. Leo mtoto anasoma yale yale aliyosoma Mheshimiwa Gulamali, anasoma historia, kwamba nyani alikuwa anabadilika na kuwa binaadamu. Sasa hayo mabadiliko ya kuwa binaadamu kwa nini mpaka leo yasiwepo. Kumbe kuna vitu ambavyo vimepitwa na wakati kwa sasa hatutakiwi tuviendeleze.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe sana, ili elimu iwe bora ni lazima huyu mtoto aandaliwe kwa kuangalia carrier yake iko vipi. Nchi za wenzetu zinaendelea kielimu ni kwa sababu tu watoto wao wanawaandaa kwa kuangalia carrier zao.

Leo mimi Rehema ni Mwalimu nilikuwa nina element za ualimu tangu nikiwa mdogo, hatimaye nikawa naendelezwa. Lakini leo hii elimu yetu inayotolewa inamlazimisha tu huyu mtoto asome kile kitu ambacho Serikali na Wizara inataka, kwa hiyo niombe nifanye huo mpango. Lakini tuhakikishe tunaandaa walimu wakuweza ku-impart hizi studies.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kwenye utunzi wa mitihani ya mwisho na usahishaji. Nchi yetu ya Tanzania tumeona a big success kwa elimu yetu ni kufanya mtihani au kumpima huyu mtu eti kwa kufanya mtihani ndipo tunapima achievement yake. Lakini hii achievement au hii mitihani ni lazima nayo sasa tuifanyie reformation tuone namna gani mitihani inatungwa lakini namna gani hii Mitihani inasahishwa. Tumeona sasa hivi mitihani the way inavyotungwa haitamsaidia huyu mwanafunzi kuweza kuyatumia yale maarifa aliyoyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliongea Bunge lililopita, leo mtihani wa shule ya msingi wa darasa la saba, mtoto unamtungia wa multiple choices, swali la kwanza mpaka la 50 multiple choices; hauoni kama unamsaidia huyu mtoto ku-guess majibu? Na unakuta kuna watoto wengine wana bahati sana anafanya ana ana ana doo; pale anapogusa tu jibu na kweli inakuwa jibu sahihi. Matokeo yake tunakuja kupata wanafunzi waliofaulu ambao hawajui kitu na wanakwenda sekondari. Tunawapa shida sana walimu wa sekondari. Mwanafunzi hajui kusoma wala kuandika vizuri. Halafu bado hata mitihani yenyewe anafanya tu shading.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufanya shading ni jambo la kawaida, lakini kwa sababu tunataka tuwapunguzie Wizara suala la usahishaji tunalenga kuwapima hawa watoto maarifa waliyoyapata na siyo kuwapunguzia mzigo wasahishaji au Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimeona kwenye taarifa ya Waziri, inasema wanakwenda kusahihisha mitihani kidijitali, ina maana huyu mtu awe amejibu majibu kulingana na ninyi mlivyotunga mtihani. Sasa hapo nataka nifahamu; na hata huu mtihani nao utakuwa multiple choice mwanzo mwisho, kwa sababu kama atakuwa na maelezo yake binafsi yakienda tofauti na ninyi hamuoni kama mtaenda kutuletea shida kwenye matokeo?

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, huu utungaji wa mitihani na usahihishaji tuuangalie upya, uende kupima zile study zote ambazo tunatarajia tuzipate au mwanafunzi azipate na si tu kufaulu mtihani.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uendeshaji wa shule binafsi. Shule binafsi ni wadau wazuri sana wa elimu, wanatoa elimu sana wanaisaidia Serikali katika kutoa elimu kwa watoto wetu. Tunajua kwamba wanachukua wanafunzi wakiwa cream, wazuri sana, lakini hatimaye kuna baadhi ya manyanyaso wanayapata sana wazazi na wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanafunzi leo wanamchukua akiwa mzuri lakini anapokaribia kwenye mwaka wa mtihani, kwa sababu alikuwa na matokeo mabaya wanamwambia ahame. Sasa, tangu mwanzo huyu mtoto mlimpokea akiwa mzuri lakini kwa sababu hamtaki kuharibu soko la biashara zenu mnaamua mumtoe; na bado tena huyo mtoto akitaka kurudi Serikalini anawekewa mizengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana huko kwenye shule za private, kwamba pamoja na udau wao mzuri wa elimu nao waangaliwe upya, na wasilete manyanyaso. Lakini bado Serikalini mtoto anapokwama labda mzazi kakwamba mtoto arudi akasome kwenye shule hiyo hiyo ya kwetu ya Kayumba kwa nini tena anakataliwa? Ile ni haki yake ya kupata elimu bila kuangalia uwezo wa mzazi au nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kwenye maslahi ya walimu. Hatuwezi kuwa tunaboresha elimu bila kumboresha na huyu mwalimu ambaye anaitoa hiyo elimu. Walimu wana mahitaji makubwa sana na wanafanya kazi katika mazingira magumu. Mwalimu leo anafundisha na anakuwa na madaftari anayosahihsha mpaka yanamzidi; ilhali mazingira yake ya kufundishia ni magumu mno. Niiombe sasa Serikali kumpunguzia… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kukushukuru kwa nafasi ili niweze nami kuchangia Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na afya. Pia niwashukuru Mawaziri wote wawili, Kaka yangu mzee wa ukinizingua nakuzingua, na dada yangu pale Mheshimiwa Maryprisca, mnafanya kazi nzuri, bila kuwasahau viongozi wetu, hasa wa RUWASA, Engineer wangu makini sana Kapufi, Engineer wangu wa Wilaya, Engineer Mapambano na kwa ushirikiano mkubwa kabisa wa Mkuu wetu wa Wilaya, Kaka yangu Rashid Chuachua.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo nataka nianze kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri yetu ya Kaliua yenye Kata 28, vijiji 99 na idadi ya watu 700,000 mpaka leo upatikanaji wa maji ni asilimia 45, very shameful. Miaka 62 ya uhuru sasa, karne ya 21 bado tuna asilimia 45 tu ya usambaaji wa maji, hii hali haikubaliki! Mheshimiwa Aweso, nikuulize, hivi ninyi Wizara yenu haina ile sera ya Wizara ya Afya kwamba mgonjwa aliye mahututi ndiye anapewa huduma haraka? Kama Kaliua tuna asilimia 45 hamtuongezei miradi mnapeleka maeneo mengine, Kaka yangu safari hii ukinizingua tunakuzingua Wanakaliua. Tunaomba miradi ya maji iende Kaliua na maji yapatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ninapenda nichangie leo ni kuhusu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria. Kwanza tuanze kushukuru kwamba katika mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria wa miji 28 na Kaliua tumo, ambao utakwenda ku-save Kaliua na Jimbo la Ulyankulu.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwekwa kwenye huu mradi, tukiwa Tabora pale kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kulikuwa kuna nyomi ya hatari, Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliongea kwamba wakati anazindua mradi wa maji wa Tabora, Igunga na Nzega kuna fedha ilibaki shilingi bilioni 25, na akasema zile fedha zitakwenda kusambaza maji Kaliua, Urambo na Sikonge, lakini mpaka leo zile hela hatujui zimeyeyukia wapi. Kaka yangu, Mheshimiwa Aweso, leo nimesema nakuzingua kwa kushika shilingi yako, nataka nipate majibu, hizi shilingi bilioni 25 ambazo tulitengewa zimekwenda wapi, hatuoni mradi umeanza, hatuoni ma-caterpillar huko au wakandarasi. Kaka yangu tunaomba utupe maelezo ya kutoka hizi fedha zimekwenda wapi, kwa sababu watu bado wanapata shida ya maji, tunaendelea ku-share maji na wanyama, karne ya 21 hii ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndoa nyingi zinakufa huko vijijini kwetu kwa sababu ya watu kwenda kutafuta maji, bado wananchi wangu hasa akina mama kule watu wanasema siyo pisi kali kwa sababu hata kusuka nywele hawasuki vizuri. Atasuka nywele aende kufuata maji mbali? Naomba Kaka yangu Mheshimiwa Aweso, leo kitaumana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kutoa shukrani, nimeona Bwawa langu la Ichemba tumelitengea shilingi milioni 750 kwa ajili ya kuanza utekelezaji. Sasa hivi hatutaki mbambamba, yale masuala ya ukinizingua nakuzingua au ubwabwa unaonekana kwenye sahani hatutaki, tunataka kwamba tumetenga hizi fedha tuone wakandarasi wamekwenda site kule na hawa wakandarasi wawe ni wakandarasi wasio makanjanja, tumeteseka kwa kutosha Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni katika gharama za uunganishaji wa maji na bei ya maji. Mheshimiwa Waziri, maji tunayotumia ni ya RUWASA, hatuna chanzo kingine. Kama inavyofahamika utafiti umeonesha Wilaya za Kaliua na Urambo vyanzo vya maji haviko karibu. Kwa hiyo, chanzo kikubwa cha maji ni kutumia sources nyingine. Urambo na Kaliua maji yaliyo karibu ni kutoka kwenye Mto Ugalla au Mto Malagarasi, lakini mpaka leo hatuoni mchakato wowote wa kuchukua maji kutoka Mto Ugalla au Mto Malagarasi.

Mheshimiwa Spika, sasa tunauliza hivi kuna agenda gani juu ya maji ya Ziwa Victoria? Why maji kutoka Ziwa Victoria? Why hatuoni mpango wa kutoa maji Ziwa Tanganyika au Mto Ugalla ambapo ndiyo karibu na kwetu Kaliua na Ulyankulu? Why hatuoni kuna mpango wa kuyatoa maji kutoka Malagarasi kuyaleta Kaliua lakini tunataka tuyatoe Ziwa Victoria? Kuna utafiti gani ambao mmefanya mkaona maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu ni ya Ziwa Victoria na siyo ya Ugalla wala siyo majiya mto Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii kwa sababu mnayatoa mbali mnasababisha hata gharama za uunganishaji kuwa kubwa lakini bado hata hakuna bei elekezi, leo mtu anatamani aunganishe maji lakini kwa sababu hakuna bei elekezi maji yanachacha. Tunashukuru kuna miradi ya maji pale lakini yale maji yanachacha, watu wanaunganishiwa kwa bei kubwa lakini bado hata ndoo shilingi 50. Shilingi 50 kwa mwanakijiji jamani ni kubwa sana. Leo hana uwezo wa shilingi 50 kwenda kununua maji, matokeo yake wanasafiri umbali mrefu kwenda kuchukua maji kwenye vile visima walivyovizoea. Hebu tu-regulate hii bei ya maji ili wananchi wengi waweze kuunganishwa na kuendana na kasi ya Mama Samia ya kutua ndoo kichwani.

Mheshimiwa Spika, tumekalia tu kusema RUWASA, maji bombani, maji bombani hayatoki. Hatujawahi kufungua maji. Niombe sana huu mpango wa kuunganisha itoke bei elekezi ili hawa wananchi wetu waweze kupata maji, waweze kuingiza majumbani kwao kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hilohilo la maji, tunaona kwamba bado kuna migogoro mingi sana na ushirikishwaji kwenye miradi ya maji watu wetu hawashirikishwi. Hali hii inasababisha miradi iweze kukwama au isifanyike kwa wakati. Unakuta hata Wabunge tupo huku mambo kule yanaendelea. Matokeo yake wale wananchi wanazua migogoro, hawalipwi fidia zao, tunaomba sasa tunapopeleka hii miradi tuhakikishe kuna suala la ushirikishwaji wa wananchi kwenye hii miradi, waione kwamba ni ya kwao sasa ili hata uvunjifu wa mikataba au uharibifu mwngine usiweze kutokea. Kwa hiyo, ninaomba sana wananchi washirikishwe, kama ni fidia walipwe kwa wakati wasiwe na kinyongo. Mwananchi akiwa na kinyongo ukipeleka mradi usiku kwa usiku atauhujumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kaka yangu Mheshimiwa Aweso, naamini wewe ni kijana na ninaamini utendaji wako wa kazi na Watendaji wako mnafanya kazi vizuri sana na nina- appreciate, lakini leo suala la kusema ubwabwa wa kushiba unaonekana kwenye sahani Kaka yangu leo nitakamata shilingi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, siungi mkono hoja mpaka maelezo yangu na mahitaji yetu ya Wanaulyankulu na Kaliua yatakapokamilika. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara yetu ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Utukufu wake. Pia ninapenda kumshukuru Rais wetu kipenzi, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake ya dhati kabisa kuhakikisha elimu ya Tanzania inakuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumshukuru pia Kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Kaka yangu, Mheshimiwa Omari Kipanga na dada yangu makini sana, Profesa Carolyne Nombo, kwa kazi nzuri sana ambayo mnaifanya katika Wizara ya Elimu. Tunaona Wizara ya Elimu sasa hivi ina mafanikio makubwa sana ambayo yanakwenda kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta yetu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kuna kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya elimu, tunaona walimu wetu wamepewa vishkwambi, tumeona wanafunzi zaidi ya 1,967 walikuwa wamekwama wameweza kurudishwa shuleni, tumeona pia kuna wanafunzi 593 wote hawa wameweza kupata Samia Scholarship. Mwenyezi Mungu awabariki sana muendelee kuwatumikia Watanzania kwenye suala la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya mafanikio makubwa tuliyoyapata kwenye sekta yetu ya elimu, ninaona bado kuna changamoto mahali fulani. Suala la kwanza ni uboreshwaji wa maslahi ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwalimu kabisa. Tunapokwenda kwenye suala la uboreshaji wa mitaala na sera, suala hili haliwezi kukamilika vizuri bila kuhakikisha maslahi ya walimu yanakamilishwa na kutekelzwa. Sasa hivi walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, hawana nyumba za kukaa, mishahara midogo, madeni mengi, huku wanafundisha wamerundikana darasani watoto kibao, kiasi kwamba ukiwapima sasa hivi afya za akili walimu wetu haziko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitaka Serikali kuhakikisha kwamba tunapokwenda kutimiza hii sera na mitaala ya elimu tuhakikishe walimu wanaboreshewa maslahi yao, bila hivi tutakuwa tunapiga mark time. Suala lingine ni kuhakikisha kabisa hao walimu wanapewa mafunzo. Sasa hivi walimu wanapewa mafunzo pale tu Serikali inapotaka, tena kuna wengine yaani kuisikia semina mpaka afanye lobbying, wakati ni hitaji. Kuna walimu ambao wanataka kujiendeleza wenyewe, lakini hao walimu wanaojiendeleza wenyewe Serikali mnakwepa majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Halmashauri zetu mwalimu akitaka kwenda kujiendeleza inamwambia kabisa mpaka uingie kwenye mpango. Anasubiri kuingia kwenye mpango lakini huo mpango anakuja kupewa barua kwenda mafunzoni anaambiwa atajigharamia gharama za masomo tena iko bolded kabisa. Bado huyu mwalimu anapotoka kwenye masomo hathaminiwi, habadilishiwi muundo wake wa mshahara kwa wakati, na bado hata unapofika wakati wa kupanda daraja wakati yuko masomoni wenzake wakipanda daraja yeye hapandi daraja, eti kisa yuko masomoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamkatisha tamaa huyu mwalimu kujiendeleza, lakini bado ataona amepoteza muda wake bure, na ametumia gharama zake. Niombe Serikali tusikwepe hizi gharama. Naomba sana hizi Halmashauri zinaposema uko kwenye mpango, mpango huo ni pamoja na kumpa rushusa na kumsomesha kwa sababu ndiyo jukumu la mwajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu wadau wa elimu kuwekewa vikwazo vingi sana. Mheshimiwa Waziri Serikali ndiyo ina jukumu la kusimamia shughuli za elimu a hundred percent, lakini Serikali peke yake haitoshi, inabidi hao wadau wa elimu, hasa private sectors waweze kushirikishwa na wamekubali kujitoa lakini wanawekewa vikwazo vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaona shule za private zinafutiwa matokeo eti kisa tu wamefanya udanganyifu kwenye mitihani, labda niulize swali moja, anayetunga mtihani huu wa Taifa si ni NECTA? Ni Serikali huyo huyo, Msimamizi wa hii mitihani ni NECTA, anapeleka walimu wakasimamie mitihani. Siyo walimu peke yao, kuna TAKUKURU, mgambo, polisi, Usalama wa Taifa, wote hao wanasimamia huu mtihani. Bado anayekwenda kusahihisha ni huyuhyu NECTA. Halafu leo matokeo yanapotoka mnatangaza shule mmezifungia. Kabla ya kuzifungia jitafakarini huko ndani, nani anasababisha haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wazazi tunachangia pesa nyingi sana, tunawekeza hela nyingi sana kwa watoto wetu mnatuumiza wazazi, lakini pia mnawaumiza watoto. Mbaya zaidi baadaye mnawapa mtihani wale watoto kwenye mazingira mengine wamekuja ku-perform tofauti na ile mwanzo, this is shame jamani. Tunawakatisha tamaa hawa wawekezaji, hebu tuache hii tabia, tuweke mazingira ambayo private sector watafanya kazi yao ya kuisaidia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimeoa eti tumeacha kutangaza matokeo, kuya-rank kwa sababu mazingira yako tofauti. Hivi wewe ukipeleka kwenye shule zako walimu wa kutosha, miundombinu ya kutosha na madarasa ya kutosha, wanafunzi watashindwa ku-perform? Wanafunzi wata-perform vizuri tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba hili suala la kutozi-rank hizi shule kwa kigezo hicho hapo hatufanyi sawa. Kwa sababu hii pamoja na kwamba ni huduma lakini kwenye sekta binafsi ni biashara. Tunaposema tunazi-promote hizi shule, kwani hakuna shule za Serikali ambazo zinachukua wanafunzi cream? hazipo? Zipo, zinachukua wanafunzi cream kabisa, mnaziita shule maalum, zinachukua wanafunzi cream.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado sasa hivi, kama alivyochangia Mheshimiwa Taska pale, kuna shule sasa hivi Halmashauri na zenyewe zinafanya biashara. Maana yake walimu wa Halmashauri wanalipwa mshahara na Serikali, wengine wanafundisha private schools, Serikali haifanyi biashara. Kama inafanya biashara basi hawa wanafunzi wetu na wenyewe tuwafanyie ranking.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niulize swali, hivi ingetokea shule kumi bora zikawa za Serikali, msingetangaza? Tuwe wakweli. Tunawakatisha moyo hawa wawekezaji wetu, wanaisaidia sana Serikali, lakini tunakuja na sababu ambazo wakati mwingine tusikwepe majukumu yetu, tutangaze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ni ushindani, shindaneni ili ajulikane bora ni yupi. Hauwezi kufanya biashara bila promotion, huu ndiyo ukweli. Wekezeni huko miundombinu iwe mizuri, walimu wawe wa kutosha, mtaona matokeo, hata hizi shule za private zitaji-phase out zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni vyuo vya VETA. Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana, tumeona kuna ujenzi wa vyuo vipya vya VETA 29 na vyuo vingine 63 vinakwenda kujengwa, hongereni sana kwa huu ubunifu. Ndiyo tunataka sasa haya mageuzi tunayosema tunakwenda kuyafanya yafanyike huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila tunachoomba sasa, VETA zilizopo, mfano VETA yangu mimi ya Ulyankulu ambayo inawakilisha Halmashauri ya Kaliua, kiukweli imechoka mno, imechakaa mno, haifai. Bado hata karakana hazitoshi. Kozi zinazotolewa kule zilishapitwa na wakati. Hebu tunaomba sasa kwenye hili, haya mageuzi ambayo tunakwenda kuyafanya tuweke kozi ambazo zinakwenda na soko la ajira. Leo kuna kozi ya udereva vijana wengi sana watashawishika kwenda huko, kuna kozi ya saluni, kozi ziko nyingi sana. Tumekazania kozi nyingine ambazo hazitoi ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana walimu wapelekwe huko, kama chuo changu kikarabatiwe, na kilishawahi kutengewa pesa, milioni 638, zirudishwe huko vifanyiwe ukarabati, walimu mahiri waweze kupatikana ili waweze kuendana na soko la ajira. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mikopo ya vyuo vya kati.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Migilla, kengele ya pili imegonga.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nianze kukushukuru kwa kunipatia nafasi nami ya kuweza kuchangia kwenye Wizara yetu nyeti ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini pia nimshukuru Rais wetu, mama yetu kipenzi, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwapigiania Watanzania, anakesha kila kukicha kuhakikisha wananchi wake wanaboreshewa miundombinu.

Mheshimiwa Spika, nipende tena kumshukuru kaka yangu, Mheshimiwa January; mdogo wangu, Mheshimiwa Byabato pale, kazi mnayofanya siyo ya kitoto, tunaona mambo mengi sasa hivi yamekuwa mazuri. Lakini bila kuwasahau viongozi wangu wa mkoa Eng. wangu Khadija pale Engineer wangu wa Kanda na Engineer wangu wa wilaya, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Wanatupa ushirikiano wa kutosha kiukweli hata tukiwapigia simu wana-respond kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, baada ya hizi salamu nianze mchango wangu kwa kuanza na REA. Ni kweli REA wanafanya kazi vizuri sana, sasa hivi hata ukipita huko kwenye maeneo yetu unaona kabisa taa zinawaka waka na mji unabadilika. Kwa kweli tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu na Wilaya yetu ya Kaliua tuna vijiji vipatavyo 100 lakini katika vijiji hivi 100, vijiji 82 tu ndivyo vina umeme lakini vijiji 18 bado. Kati ya hivyo vijiji 18 nina vijiji vyangu mimi kumi ambavyo havijapata umeme kabisa. Nina Kijiji cha Unsungwa, Silambo, Kabanga, Mwamashimba, Tupendane, Imagi, Busubi, Uhindi, Mpagasha na Lusanda. Mheshimiwa Waziri hivi vijiji kiukweli ndivyo vijiji ambavyo vina nibeba mimi kama Rehema na vinawapiga kura wengi sana. Hivyo niombe sasa harakati za kupeleka umeme kule na wakandarasi waharakishe ili wananchi wangu wasione tu umeme unatokea kwenye maeneo mengine. Taa wanaziona maeneo mengine, tunataka nao wawashe taa.

Mheshimiwa Spika, lakini tatizo kubwa la REA ni tatizo la uhaba wa nguzo. Hizi nguzo ni chache sana. Unaambiwa kilometa moja moja wanatoa nguzo 22 hazitoshi. Matokeo yake wanatwambia nguzo ni bure. Mheshimiwa Waziri mimi nikuombe tu brother, yaani tunaomba mtuambie ukweli hivi hizi nguzo ni bure au vipi. Nikiwa kama mimi ni Mbunge nilishanunua nguzo 350,000. Mimi kama mimi Mbunge nimenunua 350,000, hivi kwa nini sasa msiweke wazi kabisa wananchi wakajua kwamba hizi nguzo badala ya kuwaambia bure mkaweka bei elekezi. Kwamba labda kuanzia mita ngapi kutoka kwenye chanzo labda iwe laki moja au elfu hamsini. Watu wanatamani umeme wanatamani kuweka, mkiweka bei elekezi ya hizi nguzo na mkawa wazi. Mimi ninaimani wenye uhitaji watajichanga na kuweka umeme kwenye nyumba zao.

Mheshimiwa Spika, lakini leo tunawaambia 27,000, hizi ni ela ndogo sana, wananchi wetu wana uwezo, akiuza kuku wake wawili tu ameshapata fedha ya kuweka umeme; lakini shida ni nguzo. Mheshimiwa Waziri nikuombe nakujua wewe kijana sana mchapa kazi, hili suala naomba ulichukue, hebu wekeni wazi sasa bei ya nguzo. Mkae mfikirie mfanyie bei tu elekezi ili hawa wananchi wetu wenye uhitaji waweze kujichangachanga waweze kufikisha nguzo kwenye maeneo yao wapate umeme, na si tu kila siku kuona umeme kwenye maeneo ya jirani.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu umeme kukatika katika; suala la umeme kukatikakatika bado lipo kubwa sana. Mbaya zaidi umeme unakatika kwenye maeneo ya wananchi wetu na hawapewi taarifa. Zamani kulikuwa na siku maalum ya kufanya matengenezo ndipo wananchi wanapewa taarifa kwamba umeme utakatika lini; lakini sasa hivi umeme unakatika mno na mgao upo wa kutosha. Kaka yangu kwa hiyo nikuombe, huku kukatika kwa umeme wananchi wetu wanaharibiwa vitu vingi sana, hawapewi taarifa. Tuombe sasa wananchi wawe wanapewa taarifa lakini hata ikitokea kuna tatizo basi wananchi waambiwe na lisichukue muda mrefu hili kushughulikiwa. Nimeona kuna kata yangu ya Uyowe kule vijiji vya Mnange, Kashishi wapi kule takribani mwezi mzima wananchi wangu wamekaa gizani lakini tunashukuru process zinaendelea. Tunaomba hizi harakati ziendelee, maintenance yafanyike kwa haraka ili wananchi watoke gizani.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu kumtua mama kuni kichwani. Nikupongeze kaka yangu Mheshimiwa Januari, tumeona hizi hatua za mwanzo. Tunaenda kupeleka majiko ya gesi kule vijijini kwetu. Hii ni approach nzuri sana. Lakini napenda nishauri jambo kidogo hapa. Mwananchi tunampelekea gesi lakini akishamaliza ile gesi hakuna filling station kule. Vijijini kwetu kule hata maduka ya kubadilisha gesi hayapo. Nadhani sasa kuna haja ya Wizara mkae chini mfikirie namna gani ya kuweza kuwaboreshea hao watu wa majiko bainifu lakini na hii mikaa jadidifu.

Mheshimiwa Spika, kuna tafiti mimi nimefanya kidogo, inaonesha kwamba mtu anayekata mkaa anatumia miti tani kumi mpaka kumi na mbili ambapo akichoma mkaa anapata mkaa wa kawaida tani moja tu. Tunaona namna gani wanavyoharibu mazingira na miti inakwisha. Kwa hiyo nikuombe sasa either twende kuanzisha mashamba darasa ya kupanda miti inayokua haraka, kama walivyofanya watu kwenye BBT. Tuanzishe mashamba kuna miti inaota haraka sana. Kuna miti inaitwa mianzi, mabingobingo yale ndani ya miezi sita mpaka mwaka unatosha kabisa kutaka kutengeneza mikaa hii bainifu na mikaa ambayo ni sahihi kabisa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ningeweza kupendekeza hapa. Hii gesi ishuke bei badala ya kuwapandishia naamini kabisa mwananchi hata akiuza mayai mangapi ataweza kwenda kunua gesi kuliko tukiacha gesi ilipo halafu tumewapa majiko, itakuwa useless; kesho tutakuta wameweka chuma chakavu. Nikuombe kaka yangu tupunguze hii bei ya gesi na hao wananchi wetu waweze kununua.

Mheshimiwa Spika, kwenye hiyo gesi ninafikiria sasa tuanzishe yale majiko ya kama mtu anavyokwenda kutumia luku. Tulifanyiwa semina kule tuliona; yaani mtu atumie gesi kulingana na uwezo wake na si mtu mtungi wa kilo kumi na tano ambao hawezi kununua kwa wakati. Tukiweka kama vile matumizi ya luku mtu ana buku anapika maharagwe na maisha yanaenda. Lakini kuachia mtungi wa 60,000 ishirini na ngapi wananchi wetu hawawezi kutumia hizi.

Mheshimiwa Spika, tumeona Serikali bado haijatenga bajeti. Tumeona asilimia 90 ya Watanzania wanatumia mkaa. Kwa hiyo kama wanatumia mkaa tuweke bajeti kuhakikisha kwamba hao wadau wetu wabunifu wadogo wadogo wanaweza kuingizwa kwenye mpango wa kutengeneza mkaa ambao unatumiwa na watu wengi. Kuna majiko mbadala, tumetoka kununua kule. Kwa hiyo kama tutawawezesha hawa wadau wetu wazawa wa ndani, na kule kwenye mabango yako kule kwenye mabanda tumewaona, hebu tuwatengee bajeti hawa, nina uhakika kabisa ile azma kaka yangu Mheshimiwa Januari uliyonayo ya kuwafanya wakina mama wawe wasafi wakipika yani wasichafue masufuria mazingira yawe safi nafikiri itatimia. Hilo nikuombe kaka yangu panga bajeti vizuri mambo yako yatakuwa safi. Leo sitarajii kushika shilingi mambo yako yamekaa vizuri. Lakini, kama umeme hautafika kwangu kule nitashika shilingi, lakini leo sijadhamiria kwa sababu mambo yako makubwa nimeyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru umenitengenezea sub-station pale kutoka Tabora mpaka Ulyankulu, tunatumia peke yetu. Pale mwanzo tulikuwa tunatumia Tabora, Kaliua na Ulambo. Kwa hiyo kaka yangu nikushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema kwa siku ya leo. Alhamdulillah.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kuchangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwashukuru Mawaziri wote wa Wizara hii Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako na Naibu wake Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi nzuri wanazofanya kuhakikisha elimu yetu inasonga mbele. Naomba nichangie Wizara hii kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Mitihani; nitoe pongezi nyingi kwa kazi nzuri zinazofanywa na Baraza hili hususani ya kuandaa mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya walimu. Pamoja na kazi nzuri lakini napenda nitoe ushauri hasa kwenye utungaji wa mitihani wa kumaliza elimu ya msingi (standard vii). Kwa muda mrefu mtihani huu umekuwa ukitungwa kwa kutumia aina moja ya maswali (multiple choice questions) kutoa swali la kwanza hadi 50 pasipo kutunga aina nyingine ya maswali hasa yale yenye kupima stadi nyingine kama kuandika. Hivyo nashauri Baraza litunge mtihani kwa kuchanganya aina nyingine ya maswali ili tuwapime wanafunzi wetu hasa kwenye kuandika na kushirikisha ubongo wao. Pia nashauri mtihani wa hisabati usitungwe kwa multiple choice ili kuwafanya wanafunzi wakokotoe wenyewe pasipokupewa msaada wa majibu ya kuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu lugha ya kufundishia, wanafunzi wetu wengi wanafeli mitihani kwa kushindwa kujua lugha ya kufundishia hususani kiingereza pale wanapokwenda sekondari, hivyo naiomba Serikali kusisitiza lugha ya kiingereza ianze kufundishwa vizuri na walimu mahiri tangu elimu ya awali kwani ndiyo lugha atakayoitumia sekondari hadi chuo kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bodi ya Taaluma ya Ualimu, ni ukweli usiopingika kuwa walimu wetu wengi waliingia kwenye kazi ya ualimu kama kazi mbadala baada ya kazi za career zao kukwama hivyo kufundisha pasipo weledi na kwa ubora unaotakiwa hali inayopelekea kuzalisha wanafunzi wabovu. Hivyo naiomba Serikali kuanzisha Bodi ya Taaluma ya Walimu ili kuweza kuhakikisha elimu yetu inatolewa kwa ubora unaotakiwa na pia inatolewa na walimu bora na siyo bora walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), niipongeze Wizara kupitia Bodi ya Mikopo kwa kuwawezesha wanafunzi maskini kupata mikopo ya kuwawezesha kutimiza ndoto zao za kusoma elimu ya chuo kikuu. Lakini bodi hii imekuwa ni mwiba kwa wale wanufaika pale wanapoanza kurejesha mikopo hiyo kwani baada ya mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2016 ambapo makato yalibadilika toka asilimia nane hadi asilimia 15 pasipokumuangalia mwalimu anakabiliwa na makato mengi kama kodi, NHIF, PSPF na CWT hali inayopelekea mshahara kuwa chini ya 1/3. Niishauri Serikali kuwapunguzia mzigo wa makato walimu hawa kwa kuacha asilimia nane kwa wale walionufaika kabla ya mwaka 2016 na wale wanufaika baada ya sheria ya mwaka 2016 ndiyo waendelee na asilimia 15 kwani sheria siyo maandika ya Biblia au Qurani hivyo inaweza kuletwa Bungeni na kujadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule binafsi, hawa ni wadau muhimu sana katika kuisaidia Serikali kutoa elimu kwa wananchi. Lakini shule hizi zinapambana na changamoto nyingi sana katika uendeshaji hasa changamoto ya kodi na tozo mbalimbali, lakini pia gharama za ukaguzi za kudhibiti ubora. Hivyo, naomba Serikali yetu Tukufu izipunguzie kodi hizo ili zijiendeshe vema. Pia ningeomba Serikali iwe na utaratibu wa kuongea na wamiliki wa shule hizi juu ya changamoto mbalimbali na namna pia ya kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukaririsha wanafunzi. Napenda niishauri Wizara kwenye suala la kukaririsha wanafunzi hasa pale inapobainika wamefeli mitihani au hawajui kusoma wala kuandika warudie tu. Pia kwenye shule binafsi ambazo imeonekana suala la kukaririsha ni mwiba kwao wapewe masharti kuwa kama wanafunzi ameshindwa kufikisha alama zinazotakiwa basi aruhusiwe kukariri ila kwa sharti la kutolipa ada upya kama kweli wanataka ku-improve quality na siyo academic business.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa uhai wa afya mpaka leo nipo humu Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sitakuwa na uchoyo wa fadhili pasipo kuwapongeza watendaji wa Wizara ya Maji wakiongozwa na Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Naibu Waziri Juma Aweso, Katibu wa Wizara - Kitila Mkumbo na wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichukue fursa hii ya kuchangia kwa maandishi katika hotuba ya Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kuwa maji ni muhimu kwa binadamu, wanyama na mimea, lakini pia maji ni chanzo cha uchumi kwa nchi yetu kwani bila maji umeme haupatikani, bila maji barabara hazitengenezwi, bila maji mitambo haifanyi kazi, bila maji vyakula havipikwi, bila maji operation hazifanyiki katika hospitali. Hivyo naomba maji yapewe kipaumbele cha hali ya juu na kupelekewa fedha zinazotosheleza na zifike kwa wakati kwani ripoti ya Wizara na ya Kamati zinaonesha ni asilimia 22 tu ya fedha zinazoidhinishwa ndiyo zinakwenda kwenye maji. Naomba sana pesa zinazoidhinishwa ziwe zinakwenda kama zilivyoombwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa miradi ya maji; Mkoa wa Tabora umebahatika kuwemo kwenye mikoa itakayopata maji toka Ziwa Victoria, lakini mradi huu utachukua muda mrefu mpaka kukamilika, hivyo tunaiomba Serikali ituwezeshe wananchi wa Tabora tupate vyanzo mbadala vya maji hususani Manispaa ya Tabora ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikipata vyanzo vya maji toka Bwawa la Igombe na Kazima ambapo mabwawa hayo kwa mujibu wa taarifa ya engineer wa maji ni kwamba yame- expire hivyo inapofika wakati wa kiangazi hukauka na kufikia kutoa tope badala ya maji na kuwasababishia adha kubwa wakazi wa Tabora Manispaa kukosa maji kwa muda mrefu na pia kulipuka kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na watumiaji wengi kutumia maji yasiyo safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Manispaa ya Tabora wamekuwa wakikumbwa na adha kubwa ya bili ya maji ambapo inawapasa walipe bili kubwa kinyume na matumizi ya maji wanayotumia. Hivyo tunaiomba Serikali kuwa na mita nzuri na wasoma mita wenye weledi kwani wamekuwa wakiwabambikia bili kubwa tofauti na maji wanayotumia. Lakini pia tunaiomba Serikali iwatolee wateja wa maji service charge kwani wanalipa bili kama kawaida, kufanya hivyo kutawasaidia wananchi hususani kina mama kuingiza maji kwenye majumba yao na hivyo kuiongezea Serikali mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, kumekuwa na tabia ya wakazi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji kufanya shughuli mbalimbali za uchumi kama vile kilimo cha bustani hali inayosababisha vyanzo hivyo kuwa katika hatari ya kukauka. Hivyo niombe Serikali iweke sheria kali na kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wale wote watakobainika kuharibu vyanzo vya maji ili viweze kutumika kwa muda mrefu. Pia naomba vyanzo hivyo vitunzwe kwani pasipofanyika hivyo, kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani haitafainikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upoteaji hovyo wa maji, maji yamekuwa yakipotea hovyo hivyo kwenye vyanzo vya maji au kwenye mabomba baada ya kukatika na hivyo maji kupotea au kusambaa njiani kabla ya kuwafikia watumiaji wa mwisho na hivyo kuwafanya wakose maji mara kwa mara.

Hivyo naomba Serikali iweke mikakati ya kuzuia upoteaji wa maji na pia kuwawajibisha wale wote wanaokata mabomba makusudi ili wajinufaishe au wapate maji bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha.