Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Godfrey William Mgimwa (13 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo.
Awali ya yote, napenda sana kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Kalenga kwa nafasi ambayo wamenipa kuweza kuliwakilisha Jimbo langu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara nyingine tena, mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu wa Miaka mitano tunaenda kuchangia kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao, ningependa kuchangia mambo kadhaa yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kujikita kwenye masuala mazima ya ujenzi wa reli. Suala la Reli ya Kati ni suala la muhimu na kwa namna yeyote ile, uchumi wetu wa viwanda ambao tunaenda kuufanya katika kipindi hiki, lazima utegemee mawasiliano ya reli na biashara zake kwa ujumla.
Kwa hiyo, ni lazima tuangalie ni namna gani reli hii tunaweza tukaijenga na Serikali iseme kinagaubaga kwamba ni maeneo gani ambapo reli hii itaenda kujengwa ili tutakapokuja katika Mpango unaofuata tuweze kujua kiuhalisia kwamba Serikali ilifanya nini na imefanya wapi. Tunajua reli ya kati inapita katika mikoa gani, lakini tunaomba katika yale maeneo ya michepuko, basi tujue wazi Serikali inaongea maeneo gani katika uwakilishaji wa reli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa sana kuzungumza ni kwamba katika masuala haya, hasa katika viwanda tunavyovizungumzia, masuala ya viwanda yanaendana moja kwa moja na masuala ya umeme na upatikanaji wa elimu bora. Hatuwezi tukazungumzia masuala ya upatikanaji wa viwanda kama elimu yetu ni duni.
Vile vile hatuwezi tukazungumzia masuala ya viwanda kama masuala mazima ya nishati ya umeme bado haijapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda sana kuanza kuwashukuru na kuishukuru Serikali na Mheshimiwa Mhongo kwa kazi nzuri wanayoifanya, wametuonesha njia, hata kule vijijini umeme sasa hivi unawaka. Mheshimiwa Mhongo nakushukuru sana, katika vijiji vyangu 84, leo hii tunazungumza vijiji kama 50 hivi ambavyo vimeshapata umeme. (Makofi)
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Kwa hiyo, nakushukuru na naomba Mheshimiwa Muhongo na Wizara yako tuweze kufanya namna, tuweze kufika katika Jimbo langu, wananchi bado wanahitaji umeme. Ninaamini Mheshimiwa Muhongo na Serikali kwa ujumla na Wizara tutafanya kila namna tuweze kuhakikisha kwamba vijiji vilivyobaki vinapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa upatikanaji wa umeme katika vijiji hivi ndiyo itatoa dira nzuri ya namna gani tunavyoweza kusonga mbele katika masuala haya ya ukuaji wa viwanda. Tunavyoongelea masuala ya viwanda, ni muhimu sana kujua kwamba ikiwa kama gesi ambayo tayari tumeshaivumbua huko Mtwara tutaitumia vizuri na itakwenda kuwakilishwa au kwenda kutumika ipasavyo katika maeneo yetu, ina maana kwamba upatikanaji wa viwanda utakuwa ni mwepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika kupatikanaji wa viwanda, ni lazima tujue Serikali ina malengo gani au inalenga viwanda vya namna gani? Ni viwanda vya namna gani ambavyo Serikali inakwenda kuvijenga? Siyo tuamke asubuhi na kusema tunaenda kujenga kila aina ya Kiwanda, hatutaweza. Nchi yetu bado ni changa, tunahitaji tuweze kupata mchanganuo ni namna gani au Serikali imejipanga vipi katika ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashauri kwamba katika upande wa kilimo, kuna maeneo mbalimbali hasa ukiangalia maeneo ya nyanda za juu Kusini, tunalima sana mahindi na maharage, lakini bado hatuna viwanda ambavyo vinaweza kusaidia kuchakata haya mambo na kuhakikisha kwamba tunapata mazao na masoko bora katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, tukitaka kuangalia, Mkoa wa Iringa kipindi cha nyuma kulikuwa na Shirika la NMC; Shirika hili limekufa na hatujui litafufuka lini. Nina imani kubwa sana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi; na naamini kabisa Serikali ya Mheshimiwa Magufuli itakwenda kufufua viwanda hivi na kile kiwanda cha NMC ambacho kipo pale Iringa kitaenda kufufuliwa tuweze kupata nafaka kwa sababu kilikuwa kinainua uchumi katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuangalia katika maeneo mengine ya namna gani tunaweza tukakuza uchumi wa nchi yetu; nchi yetu bado ina matatizo makubwa sana katika upatikanaji wa mapato, nami lazima niongelee suala hili kwa sababu Bunge la Kumi lililopita, nilikuwa Mjumbe katika Kamati ya Bajeti. Tulijaribu kugusa maeneo mbalimbali kuona kama tunaweza tukafanikiwa vipi katika maeneo ambayo tunaweza tukapata vyanzo mbalimbali vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo Serikali bado inasuasua. Kuna maeneo ya uvuvi wa Bahari Kuu. Uvuvi wa bahari kuu ni uvuvi ambao Tanzania bado tupo nyuma na nchi za kigeni, wageni wanaendelea kuhakikisha kwamba wanaifilisi nchi yetu katika uvuvi wa bahari kuu. Lazima tuamke tuweze kuona kwamba uvuvi wa bahari kuu tunaufanyia kazi na Serikali inaingiza nguvu zake za kutosha ili kuhakikisha kwamba mapato yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania leo hii tuna loss ya zaidi ya Shilingi trioni moja kwa kutojiingiza kwenye uvuvi wa bahari kuu. Kuna wageni (foreigners) wengi ambao wanaenda kule kuhakikisha kwamba wanapata samaki, lakini vilevile tukiangalia soko la samaki katika bei ya dunia, liko juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uvuvi wa samaki wanaoitwa Tuna, ambao leo hii samaki hao kwa kilo moja inaanza Dola 10 mpaka Dola 50, lakini bado nchi yetu ya Tanzania hatujajikita huko kuhakikisha kwamba tunapata mapato ya kutosha. Leo hii bado tunaendelea kuwadidimiza wafanyabiashara ndogo ndogo ambao bado mitaji yao ni midogo. Ni lazima tuangalie maeneo makubwa kama haya ili kuhakikisha kwamba tunapata uchumi ambao ni endelevu na uchumi wetu binafsi, tukaachana na uchumi ule wa kuendelea kukopa nje wakati tunavyo vyanzo vyetu wenyewe katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningalie pia suala la utalii; nyanda za juu kusini tumeachwa sana. Najua kabisa kuna mambo mengi yanaendelea Kaskazini, nchi yetu ni moja lakini lazima Serikali iweze kuangalia maeneo ambayo tunaweza kupata vyanzo vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa tuna Mbunga ya Ruaha. Mkoa wa Iringa bado tunaendelea katika utaratibu wa kukuza viwanja vyetu vya ndege. Mheshimiwa Rais allivyokuja alituambia watu wa Iringa kwamba atahakikisha Airport yetu ya Mkoa wa Iringa inafufuliwa na inaendelea kuleta watalii katika Mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbuga yetu ya Ruaha ambayo inapita kwa Mheshimiwa Lukuvi, inapita kwenye Jimbo langu, bado mapato hatupati, jambo ambalo ni la ajabu na kusikitisha. (Makofi)
Vile vile upande wa kusini niliongea juzi, nikasema kuna Mbuga la Selous ambayo bado nayo tukiamua kuitumia vizuri kwa miundombinu yetu tuliyonayo tunaweza kupata fedha nyingi za kigeni na kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuisihi Serikali, kuhakikisha kwamba tunafanya kila njia kuweza kuangalia nyanda za juu kusini na maliasili zake kuhakikisha kwamba tunasonga mbele na tunapata hizi fedha ambazo Tanzania bado haijazipata ili kuhakikisha uchumi wetu unasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo kama sitazungumzia masuala ya maji. Jimbo langu la Kalenga lina matatizo makubwa sana ya maji.
Nimeongea na Mheshimiwa Waziri, tukakubaliana kwamba tuongee kuhusu masuala ya maji na naendelea kukuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji. Naomba miradi mitano ya maji ambayo haijakamilika katika Jimbo langu, ikamilike, tuokoe akina mama! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji bado ni kubwa! Wakandarasi hawajalipwa! Naomba fedha ambazo wanadai watu hawa ziweze kulipwa mapema ili bajeti inayokuja tusiweze tena kufika hapa, tukaanza kubishana na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana fedha zifike Halmashauri, Wakandarasi walipwe, waendelee kufanya kazi, miradi ikamilike, wananchi wapate faida na waendelee kuwa na matumaini na Chama chetu na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuendelea lakini, napenda sana kurudia kwamba suala hili la maji ni la muhimu. Tuhakikishe kwamba Wizara ya Maji inawezeshwa, inapata fedha na inafika vijijini kuhakikisha kwamba maji yanaweza kuwafikia wananchi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgimwa, ahsante sana, muda wako umekwisha.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo hotuba nzuri sana ambayo imewasilishwa na Waziri wa Afya, dada yangu Mheshimiwa Ummy. Vile vile nakushukuru sana kwa sababu nafasi hii niliyopewa ni nyeti lakini vile vile ni nafasi ambayo inaenda kuonesha kwamba Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imejipanga vipi kwa ajili ya masuala mazima ya afya katika kipindi kinachofuata cha mwaka mmoja. Kwa hiyo, napenda kuchukua nafasi hii kuweza kumshukuru sana Waziri wa Afya na msaidizi wake, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla. Nawashukuru sana kwa kazi nzuri mnazozifanya na sisi tuko nyuma yenu tukifanya kazi kwa ajili ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu, napenda kugusia masuala muhimu ambayo wenzangu wengi wameshayaongelea, masuala ya Mfuko wa Jamii. Tukitaka kuangalia kiundani suala la Mfuko huu wa Jamii (CHF), bado una changamoto, tena kubwa sana, lakini naamini kabisa kwamba bajeti hii itakwenda kutibu maeneo mengi ambayo Mfuko huu una matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CHF kwa ujumla wake ukiangalia katika ile Act ya mwaka 2001 ya Community Health Fund utaona kwamba tatizo kubwa la CHF ni mpangilio na namna gani huduma hii muhimu inatolewa kwa wananchi. Katika kuangalia hilo, utagundua kwamba katika Act ya mwaka 2001, suala la walemavu bado halijawekewa mkazo katika CHF. Namaanisha kwamba katika utaratibu huu wa CHF kuhakikisha kwamba wananchi wanachangia pesa kwa ajili ya kupata huduma za afya, watu wenye ulemavu hawajapa nafasi katika kupatiwa exemption.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko huu haujaeleza ni namna gani ambavyo watu wenye ulemavu wanaweza wakapata huduma hii bure moja kwa moja kulinganisha na watu wenye uwezo au wale ambao wana uwezo wa kufanya kazi moja kwa moja ambao sio disabled. Kwa hiyo, Mfuko huu bado una changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoa hilo suala la walemavu, CHF bado utaona kwamba ina uhaba wa madawa. Watu wanachangia katika jamii, lakini madawa bado hayapatikani. Hii bado ni changamoto. Vile vile ukiangalia CHF pamoja na NHIF, statistic inaonesha kwamba mwaka 2012 ni asilimia 27 tu ya Watanzania wote ambao walikuwa wamejiunga na CHF pamoja na NHIF. Kwa hiyo, bado kuna idadi kubwa ya watu ambao aidha hawana elimu ya kutosha au imeonekana kwamba Mifuko hii bado haijawanufaisha wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kalenga tatizo hili bado ni kubwa, nami nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuongea na wananchi, lakini bado wananchi wanasuasua na bado hawana uhakika juu ya suala hili. Kwa hiyo, napenda sana kuona Serikali inakuja na mkakati maalum wa kuweza kuleta mabadiliko ili wananchi waweze kuwa na imani na Mfuko huu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kuchangia, ni tatizo kubwa katika Hospitali ya Ipamba pale Jimboni Kalenga. Jimbo la Kalenga lina watu zaidi ya 200,000 lakini vile vile hospitali ya Ipamba inahudumia Wilaya nzima, nikimaanisha Jimbo la Kalenga na Jimbo la Isimani ambalo ni la Mheshimiwa Lukuvi, lakini bado hatuna gari la wagonjwa. Hili ni tatizo kubwa. Napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha, aweze kutoa majibu mahsusi ambayo yatakwenda kuwagusa wananchi wa Jimbo la Kalenga na Iringa Vijijini kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Iringa Vijijini kama Wilaya yenye watu zaidi ya 300,000, hakuna gari la wagonjwa katika hospitali kubwa kama Ipamba. Hospitali hii inahudumia wananchi mpaka wa Manispaa ya Iringa Mjini, lakini vile vile inahudumia wananchi wanaosogea mpaka maeneo ya Mafinga kwa ndugu yangu Chumi. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kuangalia kwamba, akinamama ambao wanatoka maeneo ya milimani, maeneo ya mbali wanapata shida kubwa sana kuhakikisha kwamba wanafika katika hospitali kubwa kama Ipamba kupata huduma kwa sababu tu ya kutokuwa na gari la wagonjwa. Kwa hiyo, napenda sana Serikali iweze kuja na majibu muhimu kuweza kuhakikisha kwamba hospitali hii inapatiwa gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja kubwa ambalo nchi yetu ya Tanzania inalipata sasa hivi. Tuna tatizo moja katika masuala ya afya ya akili ya binadamu. Nchi yetu ya Tanzania kwa takwimu za haraka haraka inaonesha kwamba kuna watu zaidi ya 450,000 ambao wana matatizo ya afya ya akili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tatizo hili ni kubwa na statistic inaonesha kwamba miaka inavyozidi kuendelea kutakuwa kuna changamoto kubwa na watu wataendelea kupata matatizo haya kwa sababu mbalimbali hususan matumizi ya sigara, vile vile bangi, bila kusahau matatizo makubwa ya vileo. Kwa hiyo, napenda sana Serikali iweke umakini zaidi katika eneo hili kwa sababu idadi kubwa ya vijana au idadi kubwa ya watu wanaangamia kwa sababu ya kukosa elimu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajaribu kugusia maeneo kadhaa. Hospitali yetu ya Milembe ambayo ndiyo hospitali kubwa ya Taifa ina changamoto kubwa. Leo hii hospitali ile inahudumia wagonjwa 250 mpaka 300 kwa siku, watu wenye matatizo ya afya ya akili. Tatizo hili bado ni kubwa katika nchi yetu ya Tanzania, ukienda pale utaona kwamba miundombinu haijakaa vizuri, utaona kwamba hakuna wahudumu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile utaona kwamba, uwezo wenyewe wa hospitali katika kujiendesha nikiwa naamanisha masuala mazima ya kuletewa bajeti kwa muda hayafikiwi kwa muda. Kwa hiyo, unakuta hospitali inapata changamoto kubwa na inakosa namna ya kujiendesha yenyewe na hivyo basi, kuendelea kusuasua kuhakikisha kwamba ndugu zetu hawa wenye matatizo ya akili wanaweza kupata tiba kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuona Serikali inakuja na majibu. Sehemu mojawapo ya kuweza kupata majibu haya ni kuhakikisha kwamba referrals zinatengenezwa, tunajenga vituo mbalimbali katika mikoa ili ndugu zetu hawa wasiweze moja kwa moja kutoka mikoani kuja Dodoma; kwa sababu kuna ndugu wanatoka Zanzibar, wanatoka Mwanza na Arusha wanakuja Dodoma kwa ajili ya huduma hii. Kwa hiyo, napenda referrals ziweze kutengenezwa, ziimarishwe katika mikoa yetu ili ndugu zetu wasiwe wanasafiri umbali mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukiangalia utaona kuna wale ambao wanakaa majumbani. Wanapokaa majumbani wanahudumiwa na familia zingine zenye uwezo mdogo sana kifedha. Akinamama wanahangaika kuwahudumia watoto wao wenye matatizo ya akili, wanashindwa kupata nafasi ya kuweza kusafiri umbali mrefu kuwaleta Dodoma. Kwa hiyo, napenda sana hospitali hizi ziweze kuimarishwa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinapatikana katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuangalia masuala ya UKIMWI. Nyanda za Juu Kusini tunaongoza katika tatizo hili kubwa la HIV. Naomba Serikali iweze kuja na mikakati maalum, kuweza kuangalia Mkoa kama Njombe wenye zaidi ya 14%; Mkoa wa Iringa wenye zaidi ya 9% ya maambukizi, Mkoa wa Ruvuma, yote ni Nyanda za Juu Kusini, napenda mikakati maalum iweze kuwekwa ili tuweze kupata majibu, namna gani tunaweza kuzuia tatizo hili la maambukizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuendelea zaidi, lakini napenda tu kuwasihi ndugu zangu wa upande wa pili kwamba tunavyochangia bajeti ya Serikali tuangalie kwa makini sana, kwa sababu Serikali inafanya kazi pande zote mbili. Ikiangalia masuala ya afya hakuna ambaye atasimama hapa na kusema kwamba hajatengenezewa mikakati maalum na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda kumalizia kwa kusema kwamba, kama nitapata ruhusa yako nisome Mathayo 7:9 – 10 unasema hivi: “Au kuna mtu yupi kwenu ambaye mwanaye akimwomba mkate atampa jiwe; au samaki akampa mkate?”
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nalisema kwa sababu kuna watu wako upande wa pili wanadhani Serikali haifanyi chochote. Serikali inawahudumia na nawaomba, kama wameshindwa kukaa upande wa pili, waje upande wetu, tutawaletea raha na hatutawaletea matatizo. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Muhongo na Naibu wake kwa kazi nzuri sana ambayo wamekuwa wakiifanya katika kuhakikisha kwamba umeme unasogea na nishati ya umeme na madini zinaweza kusogea katika majimbo yetu na katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu napenda kugusia maeneo machache sana. Hotuba hii wengi wameshachangia na wameeleza kwa undani zaidi namna gani umeme ulivyokuwa na umuhimu katika majimbo yetu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kujikita katika maeneo ya research na development. Nchi yetu ya Tanzania dakika hii kama tutafanya research ya kutosha, tutajikuta kwamba maeneo mengi ya nchi yetu yana madini, maeneo mengi ya nchi yetu yana kila aina ya utajiri ambao ungeweza kutusogeza mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu maeneo mengi ambayo tume-concentrate kama maeneo ya utafiti tumejikita katika eneo moja; eneo la madini tu. Madini hayo tumeangallya katika upande wa madini machache sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo katika nchi yetu ambayo yana madini ya kutosha na kuna watu ambao wameshaingia katika maeneo hayo na kuanza kupata faida na kuhakikisha kwamba wanachukua rasilimali zetu zote bila kujali nini wanakiacha katika nchi yetu ya Tanzania. Sababu moja, ni kukosa kufanya utafiti wa kutosha na kuhakikisha kwamba tunapata faida katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kalenga kuna eneo ambalo tayari watafiti wamefika, wageni wamefika na wameanza kuchimba, lakini bado kama nchi hatujapeleka wataalam kule kuhakikisha kwamba maeneo haya kama Watanzania tunafaidika vipi? Hii inatugharimu sana kwa sababu tumekosa kufanya utafiti wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo la utafiti, najikita hasa katika maeneo muhimu sana. Tanzanite kama nchi ya Tanzania tumeshindwa kuitumia na tumeshindwa kufaidika kupitia Tanzanite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1967 Tanzanite ilipogunduliwa katika nchi yetu ya Tanzania mpaka leo hii tunaweza tukasema yote lakini bado hatujapata faida. Kama watu ambao tunaichimba na tunaitoa Tanzanite katika nchi yetu, bado tunasimama katika nafasi ya nne katika uuzaji, haya ni maajabu ya dunia. Nchi ya Kenya inatutangulia, Afrika Kusini inatutangulia, India inatutangulia, sisi ndio wenye Tanzanite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utafiti umefanywa na Waingereza, pesa ambayo tunaikosa katika nchi yetu kupitia Tanzanite ni kubwa. Kama tutaamua kwa hali na mali kujikita katika eneo hili na kama wachangiaji waliopita walivyoelezea, inasimamisha au inasimama kwa nembo ya nchi yetu, inasimama kwa jina la nchi yetu, tufanye nini zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kusisitiza eneo hili ambalo lingetupa sisi pesa nyingi za kigeni, lingetusaidia sisi kuhakikisha kwamba miradi mbalimbali nayo inaendelea. Jambo moja ambalo naliona kama tatizo kubwa, ni namna gani tunaipeleka Tanzanite katika nchi za kigeni ili tuweze kwenda kuiuza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni kwamba bado tuna miundombinu mibovu, usafirishaji wetu bado haujakaa vizuri. Kama tutapata ndege ambazo zitakuwa zinaweza kusafirisha Tanzanite hii kupeleka nchi za nje kwenda kuuza tuka-compete na nchi kama Kenya ambao wana ndege zaidi ya 45, South Africa wenye ndege zaidi ya 76 wanachukua Tanzanite hapa wanakwenda kuuza nchi za nje, wanatangaza nchi zao kwamba zinapatikana katika nchi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la muhimu sana kuhakikisha kwamba tunaamka na tunafanya jambo moja la muhimu kuhakikisha kwamba pesa zote ambazo tumekuwa tukizikosa tunazirudisha katika nchi yetu kupitia Tanzanite. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujikita katika miradi ya REA. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake yote kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Kalenga, bado tunahitaji nishati ya umeme, lakini tunaipataje nishati ya meme? Leo hii bado ninafahamu kwamba tuko kwenye Phase Two ambapo miradi hii na nguzo zinapita kwenye barabara kuu. Ifike wakati sasa wananchi wetu tunajua kwamba wameshaanza kusogea ndani na vijiji vyetu vimeendelea kutanuka, mashamba yameendelea kulimwa na hivyo basi inawafanya wananchi waweze kusogea mbali kidogo na barabara.
Kwa hiyo, tunaomba sasa tutakapoingia kwenye Phase Three basi miradi hii ianze kuingia kule kwa wananchi, ifike kwenye vitongoji, ifike kule kwa mwananchi wa mwisho ili tuweze kuhakikisha kwamba watu wa vijijini wanapata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu hatuwezi tukasema tunakwenda kwenye industrialization kama hatujawafikia wananchi wa ndani. Wananchi wa ndani ambao nao wanafanya kilimo, ambao wanatakiwa wafikishe mjini, kuna viwanda ambavyo vinaanzishwa kule vijijini ndani. Ni jambo la msingi sana kuhakikisha kwamba tunapata umeme kwa wananchi wetu ambao wako ndani. Mimi nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Muhongo na msaidizi wake kwa kazi nzuri ambazo wameendelea kuzifanya kwa kipindi kirefu, na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais aliona ni bora aweze kumrudisha Mheshimiwa Muhongo aweze kuchukua nafasi ile ile ambayo alikuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikigusia masuala mengine, ninaangalia katika masuala ya bajeti kwamba asilimia 94 ya bajeti hii imeelekezwa kwenye maeneo ya maendeleo. Hili ni jambo la ajabu, kwa maana ya nzuri. Bado sijaona kwamba asilimia 94 katika nchi za Afrika kupeleka pesa za maendeleo kwenye nishati ya umeme na madini. Naomba tumpongeze sana Mheshimiwa Muhongo, tuipongeze Serikali yetu kwamba wamefanya jambo moja la maana sana. Na mimi naamini kwamba kwa utaratibu huu, miaka mitano ijayo tutafika mbali na nchi yetu itaendelea kusonga mbele kwa sababu tutapata viwanda vya kutosha kama tutaamua kuisimamia sera hii na tutaamua kuisimamia bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaelewa kwamba REA kuna pesa ambazo zinafungwa, lakini utaratibu kutoka Wizara ya Fedha kupeleka pesa kwenye mfuko huu au kupeleka pesa kwenye miradi ya umeme inachelewa. Hatuwezi tukasema tutafika asilimia 94 kama pesa hizi hazifiki kwa wakati. Hili ni tatizo kubwa, pesa ambazo zimefungwa zikae pale zisitumike vinginevyo ili tuweze kuhakikisha kwamba miradi hii inasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Waheshimiwa Wabunge wote bila kujali itikadi zetu tunahitaji umeme katika majimbo yetu. Tumuunge mkono Mheshimiwa Waziri na Serikali yetu tuweze kupata umeme na ninaamini ndoto yetu ya kuwa na viwanda, tutaweza kuwa na viwanda na tutasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ningependa kuvitaja baadhi ya vijiji na kata ambazo napenda Mheshimiwa Waziri aweze kuviangalia. Nina kijiji kimoja kinaitwa Kipera, kipo katika Kata ya Nzii. Katika kata hii nina vijiji sita. Kijiji hiki ni kijiji pekee ambacho hakijapata umeme. Napenda sana Mheshimiwa Muhongo ajitahidi kwa kadri ya uwezo wake tuweze kupata umeme katika kijiji hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kata nyingine za Ulanda, Luhota, Lyamgungwe, Maboga, Wasa, Kihwele na Kata ya Mgama, bado tunahitaji umeme. Ninaamini kwa kupitia jembe letu, Mheshimiwa Muhongo tutapata umeme katika kata hizi na katika vijiji hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda sana kuwashukuru wote ambao wamechangia, na ninaamini tutaisimamia Serikali vizuri kama tulivyotumwa na wananchi wetu tuweze kuisimamia Serikali yetu. Bila kujali itikadi, naomba tuunge mkono kwa asilimia mia moja bajeti yetu ya Wizara hii ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia mchana wa leo katika hotuba hii nzuri ambayo imewasilishwa na Waziri wa Maji. Kwanza kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi ambazo wameendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uwazi kabisa nachukua nafasi hii kuwashukuru na kwamba Mheshimiwa Waziri amekuwa bega kwa bega na mimi katika kuhakikisha kwamba Jimbo la Kalenga linapata maji ya kutosha. Vile vile Naibu wake ambaye tayari ameshatembelea Jimbo langu, napenda sana kuchukua nafasi hii kumshuru kwa kuwa ameonesha nia njema kwamba anawajua na ana nia nzuri na wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu, napenda sana kuipongeza hotuba nzuri ambayo imewasilishwa, hotuba ambayo imeleta matumaini mazuri kwa wananchi wote wa Tanzania, bila kusahau wananchi wangu wa Jimbo la Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni Kalenga tuna miradi mingi, lakini baadhi ya miradi ambayo wananchi wamekuwa wakiipigia makelele kwa muda mrefu, ni miradi ya umwagiliaji. Kwa uhalisia wa hali ya juu, napenda kutoa shukrani zangu kwa Serikali kwamba nimeona sasa scheme za umwagiliaji wa Mlambalasi na Cherehani zimeingizwa kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kilio kikubwa sana ambacho kilikuwa kimewakumba wananchi wa Jimbo la Kalenga lakini leo hii nawashukuru sana kwa sababu Jimbo litaenda sasa kunufaika; na wananchi ambao wanategemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 95, wataona kwamba Serikali yao imewaangalia, vilevile kuona ni namna gani wanaweza wakasonga mbele katika masuala mazima ya kilimo na upatikanaji wa maji bora na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea tu, nimeangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nimeona kwa undani kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wanapata maji kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. Nami nachukua nafasi kwa sababu naona jukumu kubwa la Serikali na naona namna gani ambavyo Serikali inahangaika kupata pesa kwa ajili ya miradi ya maji katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kwa sababu katika Jimbo langu la Kalenga bado tunasuasua kwenye miradi mbalimbali, lakini jitihada hizi ambazo zimeonyeshwa na Serikali naamini kabisa tutaweza kupata majibu katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kugusia tu, nina miradi mitatu ambayo inanisumbua Jimboni Kalenga. Nina mradi wa kwanza ambao ni Mradi wa Maji wa Mfyome, nina mradi wa pili ambao ni Mradi wa Weru, lakini mradi wa tatu unakusanya Vijiji vitatu; Kijiji cha Magunga, Itengulinyi na Isupilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kalenga lina zaidi ya watu 200,000, lakini upatikanaji wa maji katika Jimbo letu bado umekuwa ni mgumu. Nina imani kubwa kwamba kupitia Serikali ya Chama cha Mapinduzi, maji tutakwenda kuyapata lakini vilevile tutaenda kuwapa imani kubwa wananchi ili kufikia mwaka 2020 tuweze kupata kura nyingi na kukirudisha Chama cha Mapinduzi madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja katika upatikanaji wa fedha za miradi. Katika miradi hii mitatu niliyoitaja, kuna mradi mmoja unahitaji zaidi ya shilingi 1,100,000,000/=. Najua ni fedha nyingi lakini tuangalie ni vijiji vingapi vinavyokwenda kunufaika na mradi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ambao nimeutaja wa Magunga, Isupilo na Itengulinyi ni mradi mkubwa kwa sababu unawagusa wananchi wengi. Tatizo ni kwamba Wakandarasi wanapelekwa site, pesa hazilipwi; na Wakandarasi wanachukua nafasi ya kuwapeleka au kuipeleka Serikali Mahakamani ili pesa za miradi ziweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali na Wizara kwa ujumla tutakapokuwa tunapanga mikakati kwa ajili ya miradi, tuangalie miradi ambayo ina tija, miradi ambayo inawagusa wananchi wengi, inayowagusa akinamama ambao kwa namna moja au nyingine wanatumia muda wao mwingi kwenda kutafuta maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo moja ambalo linaingia kwenye jamii ni kwamba, akinamama wanavyoenda kuchota maji umbali mrefu na wanavyoamka asubuhi sana muda wa saa 10.00 au saa 11.00, wanahatarisha hata ndoa zao. Watakavyoenda kwa masaa matatu, manne huku nyumbani mwanaume anakuwa anapiga makelele kwamba mke wangu yuko wapi? Tuwaangalie wanawake ambao wanahangaika kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naunga mkono kwa hali na mali hotuba hii, lakini vilevile naunga mkono Wabunge wenzangu ambao wamechangia wakiomba kwamba Serikali iangalie kwa umakini namna gani tunavyoweza kupata maji. Kwa ujumla tu, nilikuwa nikiangalia bajeti nyingi zilizopita, nimeangalia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, bajeti ya Wizara ya Maji na Wizara ya Elimu. Elimu imeenda zaidi ya shilingi trilioni moja; Ujenzi imeenda zaidi ya shilingi trilioni nne na Maji inagusa kwenye shilingi bilioni 900. (Makofi)
Ndugu zangu, naomba tuangalie kwa umakini, tatizo la maji linapigiwa kelele nchi nzima. Bajeti hii kama kutakuwa kuna uwezekano, basi tuiunge mkono na fedha zote ambazo zinaombwa ziweze kufika kwa wananchi na Serikali iweze kuwafikishia wananchi maji, kwa sababu maji ni uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mapendekezo kadhaa; wenzangu wameongea kuhusu Rural Water Agency; naunga mkono suala hili kwamba katika ile tozo ya sh. 50/= hebu tuongeze tufike sh. 100/= ili tuweze kupata maji ya uhakika. Tukifanya hivi tutapata maji hata kama tatizo bado ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi bado haijakamilika, naamini kuna miradi mingi bado haijakamilika, lakini kama tutaridhia na tutaweka utaratibu kwamba tuweze kuchangia sh. 100/= tofauti na kiwango cha sasa hivi cha sh. 50/=, basi tutakuwa tumejaribu kupata pesa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimekuwa nikiangalia kwamba kuna tatizo lingine kwenye upambanuzi wa namna gani tunaweza tukainua mapato ya ndani ya nchi. Nilikuwa naangalia utaratibu wa watumiaji simu. Leo hii orodha ya watumiaji simu inaelekea kwenye milioni 39. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mahesabu madogo tu. Hivi kwa mfano, tukisema kila mtumiaji wa simu akachangia sh. 100/= kwa mwezi kwa watumiaji milioni 39 tulionao leo na hizo pesa zikaingia kwenye Mfuko wa Maji; tutapata zaidi ya shilingi bilioni 46 kwa mwaka. Kwa hiyo, hiyo itakuwa sehemu mojawapo ya kutatua tatizo hili na hizi pesa zote zikaenda kwenye miradi ya maji ambayo bado inasuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya namna hii, tukawatumia watalaam wa Wizara ya Fedha, tukawatumia wachumi ambao wapo, tukaona namna gani tutaweza kuweka mechanism ambayo tutaweza ku-charge at least sh. 100/= kwa kila mtumiaji wa simu pesa ikaenda kwenye maji, tutaweza kutatua tatizo kubwa la maji katika maeneo mengi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa nia nzuri ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, tatizo la maji ambalo mpaka leo hii ni kubwa, tunakwenda kulitatua. Leo hii zaidi ya nusu ya wananchi Watanzania bado hawana maji safi na salama ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala zuri na jema sana kuangalia na kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwa kazi ambazo anaendelea kuzifanya. Tumuunge mkono bajeti yake ipite, wananchi waweze kupata maji lakini vilevile tuunge mkono jitihada zote zinazofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tukiungana kwa pamoja tutapata maji, lakini vilevile miradi mbalimbali ambayo bado haijakamilika, itakwenda kukamilika bila kuwategemea wahisani wa nje, kwa sababu tunaenda na masharti ambayo wakati mwingine yanatuumiza sisi wenyewe kama Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Waziri, kukushukuru wewe na Serikali.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. DKT. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yameshazungumzwa kuhusu suala hili, lakini lazima tuwe wazi tunavyozungumza Halmashauri na tunavyozizungumzia Halmashauri ninaomba tuweze kujiuliza maswali kadhaa. Tatizo tunalolipata katika Halmashauri zetu ni tatizo la kutopelekwa kwa fedha kwa wakati au kutopelekwa fedha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukawasema Wakurugenzi, tunaweza tukasema Halmashauri hazifanyi kazi, lakini tatizo tunalolipata ni kwamba Wizara haipeleki pesa katika Halmashauri kwa muda. Sasa tatizo kama hili linapotokea kule kwenye Halmashauri kunakuwa hakuna namna nyingine ya kuweza kufanya kazi katika utaratibu ambao Serikali ilikuwa inataka na ndiyo maana tunakuta kwamba miradi mbalimbali haikamiliki. Kwa mfano, miradi ya maji inashindwa kukamilika, miradi ya barabara inashindwa kukamilika, lawama zinaenda kwa Wakurugenzi, lakini tatizo hili lazima tujiulize je, Wizara ya Fedha inasema nini kuhusu suala hili? Halmashauri ngapi ambazo tayari zimepata zaidi ya asilimia 70 ya bajeti? Ni nani ambaye anaweza akasimama na kusema Halmashauri yake imepata pesa za kutisha za miradi katika mwaka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tatizo hili kubwa tunalolipata lazima Wizara ya Fedha iweze kusimama na kusema pesa zinakwenda wapi au pesa zinapelekwa namna gani katika Halmashauri mbalimbali. Tunavyosema makusanyo yanaongezeka lazima tuangalie upande wa pili, unavyokusanya basi tujue tunavyopeleka katika Halmashauri twende kwa uwiano, hatuwezi kusema tunakusanya kiasi hiki, lakini kwenye Halmashauri hatupeleki pesa zozote. Kuna Halmashauri zimepata asilimia 30 ya bajeti, kuna Halmashauri zimepata asilimia 20, asilimia 30, asilimia 40; lakini kuna miradi mbalimbali na Halmashauri nyingi zina madeni makubwa. Wengine wameshazungumza hapa na wamesema kwa undani zaidi, kuna Halmashauri zinadaiwa mabilioni ya fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi lazima niwe wazi na niseme kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, nimeona mambo mengi na tumejadili na tumeziita Halmashauri mbalimbali kwenye Kamati. Tatizo tunalolipata si tatizo la Wakurugenzi peke yake. Ndiyo kuna Wakurugenzi wapya, ndiyo kuna watumishi wapya, lakini tunachokisema tunaomba sasa Wizara husika iweze kuchukua nafasi ya kuweza kuwaelimisha hawa Wakurugenzi wapya na watumishi wapya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchangiaji aliyepita alizungumza akasema tuna chuo pale Hombolo, sasa kwa nini tunashinwa kukitumia chuo hiki ili watu hawa waweze kufanya kazi katika hali ambayo tunadhani itaweza kuleta tija katika Halmashauri zetu? Kuna mambo mengi ambayo wanashindwa kuyafahamu, wanakuja kwenye Kamati wanashindwa kujieleza. Ile competitiveness haipo! Unashindwa kujua kwamba huyu mtu ame-qualify katika sekta gani, katika eneo gani? Unapomuuliza kwa nini uli-realocate fedha hizi anashindwa kueleza. Kwa hiyo, lazima tuweze kujua Wizara inayohusika imefanya kazi gani kuhakikisha kwamba watu hawa wanaweza wakatumika inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo kadhaa ambayo tumeweza kuyatizama, lakini jambo la msingi kuna asilimia 10 na kuna asilimia 20; asilimia 10 za vijana na akinamama na asilimia 20 zinazotakiwa kupelekwa kwenye vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko makubwa kuona Halmashauri zote tulizozihoji katika Kamati yetu hakuna Halmashauri ambayo ilifanikiwa kupeleka asilimia 10 kwa uzito wake au kwa ujumla wake. Sasa tunafanye ili kuhakikisha kwamba Halmashauri hizi zinawaangalia vijana? Halmashauri hizi zinawaangalia akinamama? Halmashauri hizi zinaangalia wananchi kule vijijini?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunavyoshindwa kupeleka hizi asilimia tano kwa vijana, na mimi kama kijana lazima niwe na masikitiko makubwa. Vijana wenzangu kule wanataka kuendesha miradi yao, lazima waone hizi hela zinakwenda. Sasa ni maajabu ambapo utaweza kusimama hapa na kutetea kwamba Halmashauri zinapeleka asilimia 20 jambo ambalo sio sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba kwamba Wizara iweze kuangalia kwa undani zaidi halmashauri zinafanyaje kazi, hizi asilimia 10 za vijana na akinamama ni fedha ambazo zinatoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri, lakini kwa bahati mbaya ukiangalia hata hizi Halmashauri zetu ukusanyaji wa mapato ya ndani bado unasuasua. Hatuna makusanyo ya kutosha, vyanzo vya mapato hatuna vya kutosha kwenye Halmashauri kuweza kuhakikisha kwamba, hizi asilimia 10 zinakwenda kwa wahusika na walengwa. Sasa tutakaa na tutajiuliza muda wote namna gani tunavyoweza kusonga mbele, lakini tatizo linabaki palepale kwamba kama Wizara haipeleki fedha kwenye Halmashauri na tunazituma Halmashauri ziweze kufanya makusanyo ya ndani kupitia miradi yake mbalimbali, tutaweza kupata matatizo makubwa huko mbele kwa sababu tunashindwa kuzihudumia hizi Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine baya zaidi, afadhali useme kijana, lakini unavyomnyanyasa mwanamke kwa kumnyima ile asilimia yake tano ni kitu kibaya kuliko vyote. Unakuta Mkurugenzi yuko pale kwenye Kamati anashindwa kujieleza kwa nini kashindwa kupeleka zile asilimia tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa nikiangalia katika chombo kimoja cha habari watu wanalalamika sehemu fulani wanasema akinamama na ndoa zao zinaenda kuvunjika kwa sababu ya kwenda mbali kutafuta maji, wanatumia masaa matatu, manne, matano. Sasa fedha hizi ambazo tunazisema ndizo ambazo tunataka watu wa kutoka halmashauri waweze kuhakikisha kwamba zinaenda kwa akinamama. Na akirudi nyumbani anapata kichapo vilevile kutoka kwa mume wake. Sasa hili sio jambo la kuweza kulifumbia macho, ni jambo la msingi sana kwa sababu, misingi ya jamii yetu nayo itaenda kuporomoka kwa sababu ya kukosa mambo ya namna hii ambayo tunayazungumza, na ni mambo ambayo yanajirudia mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyozungumza kuhusu upelekwaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yetu na tukiangalia hasa sisi tunaotoka katika maeneo ya vijijini kule tunajua changamoto ya maji, kwamba unavyoshindwa kuwa na maji hilo ni tatizo kubwa. Lakini vilevile tunavyoshindwa kuwaeleza wananchi wetu kwamba kuna asilimia tano, kwa sababu haya ni mambo ambayo aidha Wakurugenzi au wanasiasa tunashindwa kuwaeleza wananchi wetu kwamba kuna asilimia tano na mambo yanakuwa kimya kimya watu wanapiga ile pesa na ndiyo maana watu wanatumia maneno wanasema wanapiga-deal kwa sababu wamekula fedha ambazo zilitakiwa ziende kwa wahusika, sasa sijajua tunaweza kuwachukulia hatua gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ukiangalia katika miaka mitatu, mine, mitano ambayo tumekuwa tukikagua hizi Halmashauri, hakuna Halmashauri ambayo imetekeleza hilo, lakini bado tunakuta hakuna namna ambavyo hawa watu wa Halmashauri wanachukuliwa hatua za kisheria. Kwa hiyo, mimi ningependa kushauri kwamba, sheria iweze kuchukua mkondo wake wakati mwingine kwamba, tunavyoshindwa kuwapelekea hawa vijana, akinamama na hizi fedha za asilimia 20 kule vijijini basi tuweze kujua namna gani tunaweza kuwaadabisha hawa, nitumie hilo neno.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ningependa kuzungumza kwamba kuna matatizo ya watumishi ambao wamekaimishwa kwa muda mrefu, hili kwa sasa ni tatizo kubwa. Mtu amekaimishwa miaka mitatu, mtu amekaimishwa miezi zaidi ya sita, lakini unashindwa kujua kwa nini Serikali au TAMISEMI inashindwa kufanya huyu mtu sasa apewe nafasi yake kwa sababu kama anaweza kufanya kazi basi mpeni nafasi, lakini kama anashindwa basi mmuondoe. Unamkaimisha mtu kwa zaidi ya miezi sita, zaidi ya mwaka mmoja, zaidi ya miaka miwili, halafu unategemea kutakuwa kuna utendaji pale katika Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo ambayo yapo, si mambo ambayo tunayatoa kwenye hadithi ni mambo ambayo yapo kwenye Halmashauri zetu, na ndiyo maana hata utekelezaji wa baadhi ya majukumu katika Halmashauri yetu watu wanakuwa wanshindwa kuwa na uhakika, je, kesho watakuwepo au hawatakuwepo. Kwa hiyo, mimi nilikuwa napenda kushauri kwamba sasa umefika wakati kwa wale wanaokaimishwa waweze kupata nafasi zao au waweze kuondolewa katika nafasi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mbalimbali tumeyaona. Kuna mikataba mibovu imeingiwa katika maeneo mbalimbali, mikataba ambayo huwezi hata ukaamini kwamba hivi kwa nini mwanasheria aliweza kusaini mkataba kama huu?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni masuala hayo hayo kwamba watu wamekaimishwa kwa muda mrefu, wanashindwa kupata majibu ya ajira zao, wanaona tu wasaini mikataba wapate vijisentisenti wakimbie. Na kuna maeneo ambayo tumeyaangalia kwa undani tukajua kabisa hapa kuna tatizo la kimkataba. Kwa hiyo, mimi ningependa kuangalia hili kwa undani na kuiomba Serikali iweze kutizama kwa umakini masuala ya watumishi ili kwamba TAMISEMI sasa ichukue jukumu hili kuweza kuwapa nafasi hawa watu ambao wanakaimishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la CAG. Ni kweli kwamba wengine wengi wamezungumza wamesema CAG anashindwa kuwezeshwa. Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ilikuja kwenye Kamati ikarudishwa kwa sababu kulikuwa hakuna tathmini iliyofanywa na CAG. Sasa hii ni aibu kubwa kwamba unavyoirudisha Halmashauri je, hizi fedha ambazo wamekujanazo kwenye Kamati, kama ilikuwa Dar es Salaam au Dodoma? Lakini kumbe tatizo linakuwa ni CAG ameshindwa kuwezeshwa. Kwa hiyo, mimi ningependa kuishauri Serikali kwamba sasa kama tunasema CAG ndio jicho letu basi tumuwezeshe CAG, tatizo liko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa tunalalamika kila siku kwamba, hatuna fedha huku hatuna fedha kule, lakini ninachokisema ni kwamba lazima tuwe tuna mikakati. Tuweke mikakati yetu sawa ili kwamba kama CAG tutamtumia na tunaendelea kumtumia basi tumuwezeshe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu sisi tunashindwa kwenda kukagua miradi mbalimbali katika maeneo mbalimbali, tunakaa tunawaita Wakurugenzi waje na mavitabu makubwa namna hii. Mtu ukiliangalia lile likitabu unashindwa hata kuanza useme nianzie wapi. Lakini kumbe ile miradi ambayo ipo kule majimboni, iko kule vijijini, tunashindwa sisi kwenda kuiangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanakuja wana-manipulate tu zile figures wanasema hivi sawa sawa na vile, hivi sawa sawa na vile, mradi hujauona, na tupokuja huku kutoa ripoti na tunavyosema kwamba kitu hiki hakijakaa vizuri, ile value for money, lakini ni mambo ya kusikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningependa kuishauri Serikali, najua Bunge lilikuwa lina mfuko sasa sijui ule mfuko uko wapi? Kwamba watuwezeshe basi twendeni tukafanye kazi, tuko tayari kufanya kazi. Lakini sasa tunavyoshindwa kwenda kufanya kazi kule na tunakaa tu kama ni Dodoma au kama ni Dar es Salaam haisaidii. Twende kule tukafanye kazi tukaangalie miradi, fedha ambazo Serikali ilipeleka tukaangalie kwamba huu mradi upo au haupo. Sasa utaambaiwa kuna mradi umepelekwa kule umekamilika una milioni 300; milioni 500, lakini ukienda kule ule mradi haupo, mnazungushwa tu kwenye magari kule mpaka unachoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba niishie hapo, lakini ninaunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, nakushukru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri lakini vilevile niweze kumshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama na msaidizi wake Mheshimiwa Anthony Mavunde kwa kazi nzuri ambazo wameendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jioni ya leo napenda kuzungumza machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tunazungumza kuhusu masuala mazima ya kuhamia Dodoma. Suala la kuhamia Dodoma kama lilivyoelezwa kwenye hotuba ni suala jema na lazima tuipongeze Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa maamuzi haya ambayo yamefikiwa. Ingawa Serikali zilizopita zilijitahidi kufanya hivi lazima tupongeze hatua zilizofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nigusie kidogo kuhusu suala la wanawake na vijana. Mheshimiwa Mavunde amejitahidi sana kufanya kazi na vijana. Katika utaratibu ambao ameuanzisha wa kuhakikisha kwamba vijana Tanzania nzima wanawezeshwa, napenda sana utaratibu huu Mheshimiwa
Mavunde uendelee nao na mimi kama kijana nakuunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazungumza uwezeshwaji wa vijana na akinamama lakini tunapofanya uwezeshaji huu tuhakikishe kwamba ajira inakwenda sambamba na uwezeshwaji wa mambo haya yaliyozungumzwa katika hotuba. Tunavyozungumza kuhusu uwiano wa ajira na namna ambavyo Wizara husika inafanya kazi kuinua uchumi wa akinamama na vijana tuangalie Kanda ya Afrika Mashariki namna gani ambavyo wenzetu wamefanikiwa au wameshindwa.
Mheshimiwa Spika, katika uwiano wa ajira Tanzania tuko kwenye asilimia 10.3 lakini vijana wako kwenye uwiano wa asilimia 13 tuko vizuri ukilinganisha na nchi ya Kenya ambao wao uwiano wa ajira kwa upande wa vijana ni mkubwa zaidi hata mara tatu ya Tanzania. Kwa sababu hiyo niipongeze sana Serikali na Mawaziri husika kwa kazi ambazo wanaendelea kuzifanya. Namwalika Mheshimiwa Mavunde kuja pale Kalenga kuwahakikishia vijana wenzangu kwamba nao wananufaika na utaratibu huu ulioanzisha.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite sasa kwenye suala maji. Maji ni tatizo kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania na hususan katika Jimbo langu la Kalenga. Nina miradi mbalimbali ambayo bado haijakamilika ambayo nimezungumza sasa zaidi ya miaka miwili na kwa sababu ipo
kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lazima niizungumze.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kalenga lina wananchi wengi ambao wanaiona miradi yao lakini haijakamilika. Nina mradi wa maji ambao unatoka Isupilo, Magunga na Itengulinyi ambapo jumla ya shilingi bilioni mbili ziliwekwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huu wa maji unatekelezeka na wananchi katika vijiji hivi wananufaika. Leo ni miaka miwili mkandarasi aliyekuwa pale site ameondoka ingawa amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 1.2, hakuna malipo yoyote yanayofanyika na hivyo basi kufanya wananchi waweze kuleta mkanganyiko na kutokuwa na
makubaliano kati ya Mbunge, wananchi, viongozi na Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, napenda sana kuona kwamba Serikali inakuja na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba mkandarasi huyu analipwa ili maji yaweze kutoka katika vijiji hivi vitatu. Tutakapofanikiwa kupata maji katika vijiji hivi vitatu nina uhakika tunaweza kusaidia vijiji vingine kwa sababu mtandao utakuwa umeshasogea katika vijiji vya jirani. Sasa kupoteza shilingi bilioni 1.2 na kumuacha mkandarasi aende ni hasara kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, mkandarasi huyu ameishtaki Halmashauri ya Wilaya yangu, anadai riba ya zaidi ya shilingi milioni 250 kwa sababu ya mradi ambao haujakamilika. Nashangaa wakati mwingine kwa nini Serikali inaweza ikaruhusu vitu vya namna hii kutokea katika Majimbo yetu
na mwisho wa siku fedha zinapotea, wananchi wanaendelea kulalamika maji na vilevile hata baada ya kuongea sana bado maji yanakuwa hayatoki. Huo ni mradi wa kwanza.
Mheshimiwa Spika, mradi wa pili ni wa maji wa Nyamulenge ambao nilizungumza hata katika bajeti iliyopita nikasema mradi huu unaweza ukahudumia zaidi ya vijiji 18 katika Jimbo la Kalenga na hata vijiji vingine katika upande wa pili wa Mheshimiwa Mwamoto katika Jimbo la Kilolo. Mradi huu unahitaji shilingi milioni 49 na nilipeleka dokezo kwa Mheshimiwa Naibu Waziri akanieleza kwamba tatizo hili tutalitatua. Leo hii bado hatujaweza kupata majibu, wananchi wanaendelea kupiga makelele na tuliwaahidi katika kampeni zetu tutawaletea maji lakini mpaka leo hii hakuna dalili za maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisisitize zaidi na zaidi kwamba tunavyozungumzia maji tunazungumza uhai wa wananchi wetu waliotupa kura zetu. Tutakuja kudaiwa baadaye kipindi tutakapokuja kuomba kura. Ni kumbukumbu ambazo napenda kuzitoa kwa sababu tulipita tukiwaomba kura kwa vigezo hivi. Leo hii unazungumza na mkandarasi anakwambia sijalipwa, unazungumza na Mhandisi wa Halmashauri anasema nimepeleka certificate kwenye Wizara. Ukiongea na Wizara wanasema hapana hatujapokea certificate, sasa sijui nani tumtafute hapa?
Mheshimiwa Spika, ni jambo ambalo linasikitisha sana, lakini napenda kuona kwamba maeneo mbalimbali siyo Jimbo la Kalenga tu, Wabunge wengi wamepiga kelele kuhusu maji, uwekwe mkakati maalum ambapo tutaweza kuona kwamba maji yanawafikia wananchi wetu kwa ukaribu na katika namna ambayo ni ya kipekee. Tumefanikiwa katika umeme kwa nini tushindwe kwenye maji? Naomba hayo yaweze kuwekwa kwenye kumbukumbu.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Jimbo la Kalenga lina Hospitali ya Ipamba nimeomba gari la wagonjwa sasa miaka miwili na nusu. Jimbo la Kalenga ambalo ndilo linabeba hospitali ile ambayo inahudumia Majimbo mawili ya Wilaya nzima leo hii hakuna gari la wagonjwa. Narudia
tena, Wilaya ya Iringa Vijijini ina Hospitali ya Ipamba ambayo haina gari la wagonjwa yaani nimeongea mpaka sasa naona kichwa kinaniuma.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iweze kuiangalia hospitali hii inayohudumia zaidi ya wananchi ya 300,000 wa Jimbo la Isimani na Jimbo la Kalenga na hata Iringa Mjini kama Manispaa lakini bado tunaendela kuomba. Kuna mambo ambayo tunatakiwa tuyaangalie tu kwa haraka
haraka tukaona hawa ni wananchi wetu, hawa ni akinamama wanaokwenda kuhudumiwa katika huduma hizi ambazo ni za msingi. Kwa hiyo, napenda sana Serikali iweze kuliangalia suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine niipongeze sana Serikali na Wizara kwa ujumla kwa namna ambavyo wameweza kuliangalia suala la UKIMWI. Nimesoma katika kitabu nimeona kwamba kuna shilingi milioni 347 ambazo tumechangia kama harambee, niipongeze sana Serikali kwa hilo lakini vilevile kuna shilingi bilioni 5.6 ambazo zimetengwa. Tatizo hili ni kubwa, tunaomba zile fedha ziweze kutengwa kwa watu hawa ambao kwa namna moja au nyingine wamenyanyasika kwa muda mrefu. Mheshimiwa Spika, katika kitabu hiki jambo moja ambalo limenisikitisha kuna neno moja limetumiwa linaitwa WAVIU, WAVIU ni watu gani hawa? Watu wenye virusi vya UKIMWI ni watu gani? Watu hawa tukiwatafutia maneno ya stereotype tukasema kuna hawa wenye UKIMWI, hawa wenye hivi tutashindwa kufikia majibu yetu. Haya ni maneno ambayo tunayaweka wenyewe na tunakuja kufika wakati ambapo tunashindwa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Godfrey.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya, vilevile kushukuru sana Serikali na Wizara kwa ujumla kuanzia Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kuzifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo machache sana, jambo la kwanza ningependa kuanza na suala la mkanganyiko ambao upo kati ya TBS na TFDA. Tatizo tunaloliona hapa ni mkanganyiko au muingiliano wa kazi kati ya taasisi hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwamba katika maeneo mengi taasisi hizi mbili zinaingiliana katika utendaji wake wa kazi, na katika kutenda kazi unakuta kuna mambo ambayo yanaendelea katika taasisi hizi ambazo zipo kwa mujibu wa sharia, kwamba unakuta wakati kwa mfano, misaada inatolewa kutoka kwa wahisani mbalimbali nje ya nchi, misaada ile inapokuja nchini kunakuwa kuna mkanganyiko hapa, TFDA wataingia, TBS wataingia vilevile, TFDA kuna charge nyingine ambazo wanaziweka kwa ajili ya misaada hii ambayo tunapewa kutoka kwa wahisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi yetu tuinajua, bajeti iliyoelezwa ni bajeti kubwa lakini ni lazima tuwe wazi kwamba bajeti iliyopita ilikuwa finyu sana vilevile haikutekelezeka kwa asilimia nyingi, sasa tunapopata fedha hizi au tunapopata misaada hii kutoka kwa wahisani halafu inavyofika bandarini inatozwa kodi kubwa, kwa mfano, magari ya wagonjwa, vifaa tiba na kadhalika, inapofika wakati Serikali inatoza kodi za namna hii, inarudisha nyuma maendeleo katika sekta hii ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kabisa kwamba hata wananchi wetu kule vijijini wanakosa huduma hizi kwa sababu ya urasimu ambao upo katika taasisi mbalimbali za Serikali hasa pale TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye hata hivyo kipindi cha nyuma aliliongelea hili suala akatoa majibu kuhusu tatizo hili, ningependa sana kumsihi tena kwa mara nyingine Waziri wa Fedha aweze kuliangalia suala hili ili tunapopata misaada kutoka kwa wahisani iweze kupita bure katika bandari zetu na huduma hizo ziweze kuwafikia wananchi moja kwa moja, kwa sababu tatizo la afya bado ni kubwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nigusie sasa suala kubwa ambalo lipo Jimboni kwangu Kalenga. Nimeongea sana na ninaomba nirudie tena kwamba Jimbo la Kalenga na Jimbo la Isimani katika Wilaya ya Iringa Vijijini tuna tatizo la gari la wagonjwa. Narudia tena kwa sababu tatizo hili ni kubwa. Wilaya ya Iringa Vijijini ina zaidi ya watu 300,000, tuna gari la wagonjwa ambalo ni hiace, kwa kweli kwa miundombinu tuliyonayo halikidhi mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mwezi, akina mama ambao wanajifungua ni zaidi ya 200 ambao wanatoka maeneo mbalimbali lakini inahudumia majimbo mengine hata Jimbo la Mheshimiwa Mwamoto pia lipo katika huduma hii, hivyo ningependa sana Serikali iweze kuona uzito wa kutupatia ambulance katika Hospitali ya Ipamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea hili suala kwa muda mrefu na ninachokiomba zawadi pekee ambayo nitaiomba kutoka kwenye Wizara, Mheshimiwa Dada Ummy, Mheshimiwa Kigwangalla zawadi ambayo mtanipa mimi katika miaka hii mitano naombeni mnipe ambulance katika Hospitali ya Ipamba ili tuweze kuokoa maisha ya wananchi katika Jimbo letu, tuweze kuokoa maisha ya Watanzania katika Jimbo la Kalenga, tuweze kuokoa maisha ya Watanzania ambao wapo katika Wilaya ya Iringa vijijini. Ni muda mrefu kwa kweli inasikitisha sana kama Serikali ambayo tumeona kwa namna moja au nyingine maeneo mbalimbali ambulance zimepelekwa, ninaamini kabisa Serikali itafanya namna tunaweza tukapa ambulance katika Jimbo la Kalenga, katika hospitali hii ya Ipamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuongea sana, nimshkuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Kigwangalla kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Kigwangalla ulikuja Jimboni, umefanya kazi nzuri na wananchi bado wanakukumbuka na wamenipa salamu kwamba wanaomba yale uliyowaahidi waweze kutekelezewa. Na mimi nitaendelea kuongea haya na kuendelea kuwapongeza Serikali kwa sababu ninaamini Serikali hii ya Awamu ya Tano imejizatiti vizuri kabisa katika kuhakikisha sekta hii ya afya inakua na inaenda kuwafikia wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana niweze kukushukuru na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema lakini vile vile nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru sana Rais wangu Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana ambayo ameendelea kuifanya kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijaribu tu kugusia mambo machache katika hotuba ya Bajeti ya Serikali. Kabla sijaanza, niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais amejitahidi sana kufanya mabadiliko makubwa sana katika nchi yetu na baadhi ya mambo ambayo ameyafanya ambayo lazima tumshukuru na tuendelee kumuunga mkono ni mambo yafuatayo:-

Kwanza, suala la kuhamia Dodoma halikuwa jambo dogo kwa hiyo kwa nia hiyo njema ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya kuhakikisha kwamba Makao Makuu ya Serikali yanahamia Dodoma na kufanikisha zoezi hilo baada ya miaka zaidi ya 40 ni jambo la kumshukuru sana na kumpongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo ni masuala ya usafirishaji. Zoezi hili la kuunda reli kwa kiwango cha standard gauge ni jambo ambalo lazima tuishukuru Serikali na tuendelee kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi ambazo wanaendelea kufanya kwa sababu ninaamini kabisa kama reli hii itakamilika ina maana uchumi wa nchi yetu utaboreshwa zaidi na hatimaye tunaweza tukapata mafanikio makubwa katika siku chache zijazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile amejitahidi sana kuhakikisha kwamba masuala ya watumishi hewa, wanafunzi hewa, manunuzi ya ndege, meli mbili lakini vile vile amerudisha nidhamu katika masuala mazima ya kazi. Haya ni mambo ambayo tulikuwa tukiyatamani na tumempata sasa kiongozi au Rais ambaye ameweza kweli kufanya mabadiliko makubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo moja ambalo limetokea kipindi kifupi kilichopita nalo ni kuhusu masuala la madini, masuala ambayo ni muhimu sana katika ujenzi wa Taifa letu. Suala la makinikia ni suala ambalo kweli ni la muhimu sana katika ujenzi wa Taifa letu. Tukiangalia kwa namna ambavyo Mheshimiwa Rais amejitahidi kulifuatilia na kulifanyia kazi suala hili na hatimae leo hii tunaenda kuunda sasa utaratibu mpya wa kuleta ule Muswada katika Bunge hili ili tuweze kuweka sheria ambayo itaweza kuhakikisha kwamba tatizo la madini katika nchi yetu linakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili sio jambo dogo, ni kweli kwamba katika nchi/mataifa mbalimbali mbalimbali wamejitahidi sana kufanya utaratibu wa kuja katika nchi maskini, kunyonya nchi maskini, kuchukua rasilimali zetu, kuondoka nazo na kutuachia na umaskini katika nchi yetu. Lakini tumempata Rais ambaye ameenda kufanya mabadiliko, amelichukua hili kama jambo lake, amelichukua hili kama jambo la Serikali na hatimae sasa kuwafanya Watanzania waanze kuanza maisha mapya kwa kuwa na imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba jambo kama hili ni jambo ambalo linahitaji kwa ujumla wetu bila kujali upinzani, bila kujali Chama Tawala kuhakikisha kwamba tunamuunga mkono Rais katika kuhakikisha kwamba tunaleta maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niseme tu kwamba kwenye Bajeti ya Serikali, bajeti ya mwaka jana ilieleza kwa undani zaidi ikasema kwamba kuna zile dola milioni 500 ambazo zilikuwa zinatakiwa kutoka katika Serikali ya India ambazo zilikuwa zinalenga uboreshaji wa miundombinu ya maji katika nchi yetu. Lakini mpaka leo fedha hizo hazijatoka.

Ningependa kuishauri Serikali na kuendelea kuwashauri wadau ambao wako nje katika nchi ya India, wafanye kazi ya ziada, Serikali iendelee kusukuma, kutoa msukumo wa hali ya juu ili tuweze kupata fedha hizi ziweze kusambaa katika maeneo mbalimbali ya Taifa letu ili tatizo la maji sasa liweze kupungua. Tukiweza kufanya hivi tutapunguza adha ya maji katika Taifa letu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna akina mama ambao wako vijijini, kuna watoto ambao wako vijijini, kuna shule na taasisi mbalimbali ambazo hazijafikiwa na huduma hii ya maji. Tukipata fedha hizi inakuwa inaleta sababu moja au maana moja kwamba tutapunguza adha ya maji katika maeneo mbalimbali hasa katika yale maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba Taifa letu linapita katika wakati mgumu sana, wakati ambapo katika vijiji vyetu kila kona utakayoenda tatizo la maji litakuwa ndilo tatizo la kwanza kuzungumzwa. Lakini lazima tuendelee kuiwekea mkazo hii ya kwamba fedha ambazo zimewekwa katika Wizara au zimeombwa na Wizara husika Serikali iweze kupeleka fedha zile ili maji yaweze kutatuliwa kama changamoto kubwa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ongezeko la Deni la Taifa limekua. Lakini ni lazima tuangalie, je, ongezeko hili tunaweza tukalihimili au hatuwezi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokisema ni kitu kimoja, nchi mbalimbali katika dunia hii bado wanaendelea kukopa, wala isiwe shida kwamba Tanzania deni la nchi au Deni la Taifa limeendelea kuongezeka. Tuangalie nchi kama Marekani, tuangalie nchi zingine kama Kenya, tuangalie nchi zingine za Bara la Afrika, je, zinaendelea kukopa au haziendelea kukopa na je, katika suala la ukopaji tunakopa kwa ajili gani, hauwezi ukakopa bila kuwa na sababu maalum, na sisi tunavyoendelea kukopa isimaanishe kwamba Watanzania labda ni maskini, isimaanishe kwamba Watanzania hatuna mikakati ya namna gani tunaweza kukamilisha changamoto zetu za kimaendeleo, tunakopa kwa sababu tunataka tukamilishe miradi mbalimbali ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata fedha hizi ina maana ni moja kwa moja tunaenda kuhudumia miradi mbalimbali katika vijiji vyetu katika miji yetu na kuhakikisha kwamba miundombinu ambayo tunaiona kwa mfano fly over tunazoziona Dar es Salaam, hii ni sababu mojawapo kwamba tunavyoendelea kukopa ina maana tunaboresha miundombinu yetu, kama tunatengeneza reli, barabara na miundombinu mingine yoyote ambayo tunaweza kuitamka, kama tutatumia fedha hizi kwa uangalifu na tukakopa kwa uangalifu basi wala isiwe shida kwa sababu deni hili ni sustainable.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi ya kuongea nijaribu kugusia tatizo moja la benki ya FBME ambayo miezi kama miwili iliyopita ilisimamishiwa leseni yake, niseme tu kwamba benki hii ni muhimu kwa wananchi, na kuna wateja ambao waliweka fedha zao katika benki ile. Imefika sasa wakati kwamba Serikali iweze kutoa tamko la moja kwa moja kwamba ni lini sasa fedha hizi ambazo wananchi au wateja ambao wapo katika benki hii wataenda sasa kuzipata, kwa sababu mpaka sasa hivi imekuwa kama ni dilemma, haieleweki kama Je, Serikali itatoa lini tamko kwamba leseni hii baada ya kufungiwa sasa wateja waende wapi kuchukua fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa nchi yoyote na hasa uchumi katika mataifa madogo kama Tanzania ambayo yanategemea ukuaji wa mabenki, ambayo yanategemea ukuajia wa fedha ambazo zinakuwa deposited katika mabenki mbalimbali...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana naomba nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja, nakushukuru sana Mungu akubariki. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii, lakini vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kushukuru Wizara, Waziri husika, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na wasaidizi wake wote. Kazi tunaiona na tunaendelea kuwa-support, tupo nyuma yenu, endeleeni kufanya kazi na tunaamini Tanzania itaendelea kubadilika kwa muda tunaotarajia kuweza kufika huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema kwamba Wizara ya Ujenzi ni muhimu sana katika Taifa letu lakini hatuwezi tukasonga mbele kama tutakuwa hatuangalii au tuka-review bajeti zetu ambazo tunazipitisha mwaka baada ya mwaka. Kuna mambo mengi ambayo yameelezwa bajeti iliyopita mwaka 2017/2018 na 2018/2019 kuna baadhi ya mambo ambayo nimeangalia kwenye hotuba na nimeona yanakwenda vizuri lakini bila kuangalia tulichokifanya mwaka jana na mwaka juzi tunaweza tusiweze kufika tunakoenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala kubwa ambalo tunaliangalia la TARURA na TANROARDS ambako tunakuta asilimia 30 kwa asilimia 70 ya maendeleo. Sasa tuangalie uwezekano kwa sababu TARURA tuna barabara nyingi, zaidi ya 100,000 ambazo tunatarajia kuzitengeneza lakini asilimia ambayo imetengwa ni ndogo sana. TARURA inaangalia vijijini ambako ndiko kwenye watu wengi na ndiko kwenye tija. Napenda kuishauri Serikali namna gani ambavyo tunaweza tuka-balance sasa at least tupeleke kwenye 40% kwa 60%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba viwanja vya ndege vimeendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali lakini niseme mahsusi kwa Kiwanja cha Nduli ambacho kipo Iringa. Kiwanja hiki cha ndege ni cha muhimu sana. Upande wa Nyanda za Juu Kusini ndiyo tuna Kiwanja cha Songwe ambacho Serikali imeshatenga fedha lakini naamini kabisa Kiwanja cha Nduli ambacho kipo Iringa kitakuwa ni sehemu ya ukuaji wa uchumi katika Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Nimshukuru sana Makamu wa Rais alikuja Jimboni na alikuja Mkoani Iringa na akaangalia maendeleo ya mkoa.

Kupitia Benki ya Dunia tumepata ufadhili wa kujenga ile barabara ya kutoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park kwa kiwango cha lami. Hiyo peke yake ni maendeleo ya makubwa sana kwa Taifa letu na watu wa Iringa tunajivunia sana kwa sababu tunaamini sasa tutaenda kupata uchumi ambao tunautarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba maendeleo bila barabara au bila kuhakikisha kwamba masuala mazima ya usafiri wa anga yanakaa vizuri bado tunaweza tukawa nyuma tukijilinganisha na nchi zingine za Afrika Mashariki. Niseme tu kwamba Tanzania tumejipanga vizuri na naamini kabisa kwa Awamu hii ya Tano tunaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali katika eneo moja, kuna mikataba mbalimbali ya usafiri wa anga ambayo Serikali inaingia inaitwa Bilateral Air Service Agreement, Tanzania bado tuko nyuma kidogo, tuingie mikataba mingi na mashirika mbalimbali ya kimataifa ili ndege mbalimbali ziendelee kufika Tanzania na sisi tuweze kurusha ndege zetu katika viwanja mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya wenzetu wameshasogea sana, Uganda nao wanakwenda sisi Tanzania mpaka mwaka 2017 tulikuwa tumeingia mikataba mingine mipya 10, hiyo haitoshi. Napenda kushauri Serikali kwamba bila kuingia mikataba mikubwa ya namna hii tunaweza tukabaki nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa ni la PPP. Naamini kabisa maendeleo yetu Watanzania bila PPP tunaweza tukawa nyuma, tunaweza tusifanikiwe. Ni lazima tufanye utaratibu wa kuji-engage sisi wenyewe katika miradi ya PPP. Wenzetu wa Rwanda wamejenga uwanja wa Busegera ambao ni asilimia 25 kwa asilimia 75, utakuwa ni uwanja mmoja mzuri sana katika ukanda wa Afrika Mashariki. Naamini kwa sababu wameamua kufanya hivyo sio lazima watumie fedha zao zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi bado tuko nyuma kimaendeleo. Afrika tunahitaji tuweze kujilinganisha na nchi zingine lakini tutafikaje huko tunakotaka kwenda kama tutakuwa tunatumia nguvu zetu nyingi bila kushiriki katika uchumi unaostahili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, vilevile nichukue fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Makatibu wote Wakuu.

Wizara hii ya Maji ni Wizara muhimu kama ilivyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, binafsi ninapongeza shughuli ambazo zinaendelea kwenye Taifa letu na kwenye Jimbo langu la Kalenga. Binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuweza kufika Jimboni kwangu. Siyo tu Waziri Kiongozi lakini Naibu Waziri pia amefanya kazi kubwa sana kuweza kuhakikisha kwamba Jimbo la Kalenga linakaa vizuri. Pongezi zangu zifike kwako kwa sababu hata ile fedha uliyonipa shilingi 500,000 kuwapelekea wananchi wangu ninakushukuru sana, Mheshimiwa Waziri naamini ni mwanzo mzuri. Ilikuwa ni fedha binafsi kutoka kwenye mfuko wake na mimi nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba kuna miradi mbalimbali ambayo inaendelea, lakini nizungumzie mradi mahsusi ambao sasa hivi una takribani miaka sita tokea uanze. Mradi wa Itengulinyi, Isupilo kuelekea Magunga. Huu ni mradi mkubwa sana ambao Serikali iliingia mkataba na Mkandarasi RJR kwa zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 2.4. Leo hii tunavyozungumza, nimeshaongea mara kwa mara Bungeni kukumbusha umuhimu wa mradi huu wa maji. Mpaka leo fedha ambazo zimetolewa ni zaidi ya shilingi bilioni 1.2 na mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yangu ya Iringa Vijijini leo hii tunavyoongea imepelekwa mahakamani kwa ajili ya mradi huu, mradi haujakamilika na mkandarasi ameipeleka Halmashauri mahakamani na tunaendelea kusubiri nini kitatokea kwa sababu mkandarasi huyu anadai Serikali fedha ya riba ziadi ya shilingi milioni 250, nashindwa kufahamu tumeshapeleka fedha za mradi zaidi ya shilingi bilioni 1.2 lakini utaratibu unavyokwenda mpaka leo ni muda mrefu sasa Serikali imeshindwa kuingia makubaliano na Mkandarasi huyu ili mradi huu ukamilike na wananchi wangu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mradi ambao ungeweza kutatua tatizo la maji kwa zaidi ya vijiji vinne na ni mradi ambao binafsi ungekamilika ningeshukuru sana na wananchi wangu ambao katika bajeti hii iliyoelezwa kwa kweli hatujatengewa fedha za kutosha kwenye suala la maji, na kama tunavyofahamu maji ni uhai na wananchi wa Jimbo la Kalenga wanahitaji maji kama majimbo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona utaratibu ambao umeoneshwa kwenye Wizara kuhusu suala la maji, lakini kwanza fedha ambazo tumekopa kutoka India jumla ya dola za Kimarekani milioni 500 ningependa kujua, je, ni utaratibu gani umetumika kwa Serikali kupeleka hizi fedha katika yale maeneo ambayo tumeyatenga 17, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima tufahamu kwamba kuna maeneo mengine mengi ambayo yameshaelezwa na yameoneshwa kwenye kitabu cha hotuba, mengine yamepata miradi ya maendeleo, mengine fedha kutoka Serikali, mengine miradi ya umwagiliaji, lakini kuna maeneo kama Jimbo langu la Kalenga hatujapata hata senti moja kutokana na maeneo haya ambayo yametengwa. Kwa sababu inaonesha kabisa kwamba fedha zimetolewa na kuna fedha zingine kutoka Serikali Kuu, fedha kutoka miradi mbalimbali kwa ajili ya mwaka huu wa fedha na mambo mengine chungu nzima, lakini Jimbo langu la Kalenga bado halijapata au halijatengewa fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kwamba tumetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya bajeti hii ya 2018/2019 lakini Serikali lazima itambue kwamba kuna maeneo au kuna Wilaya ambazo zina majimbo mawili, fedha hizi bilioni 1.3 zikitenganishwa katika majimbo mawili bado zinakuwa hazitoshi. Jimbo langu la Kalenga peke yake bajeti yake ni jumla ya shilingi za Kitanzania milioni 735, sasa sina uhakika kama fedha hizi zitafika kwa wakati au hazitafika kwa wakati lakini ninachoomba Wizara ni kwamba hebu tujitahidi kupeleka fedha katika maeneo ambayo matatizo ya maji ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo ambayo tulipitisha mwaka jana ya shilingi 50, sasa hivi ningependa tu kuishauri Serikali kwamba kama tukakubaliana zikawa shilingi 100 zikaenda katika kwenye maji basi nina uhakika kabisa tatizo la maji linaweza likawa limepungua. Shilingi 50 ambayo tumeitenga mwaka jana imeweza kukusanywa na tukapata jumla ya shilingi bilioni 158, ina maana kama tungefanya kwa shilingi 100 tungepata zaidi ya shilingi bilioni 300 ambazo tungegawanya katika Wilaya au katika Majimbo tungepata fedha nyingi sana. Hili ningependa Wizara iweze kuliangalia sana na kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo dogo kuhusu miradi ya umwagiliaji, pale Jimboni kwangu tuna mradi wa maji wa umwagiliaji wa Mlambalasi, ambao kwenye kitabu hiki cha hotuba inaonesha kwamba mradi umekamilika, lakini ukweli ni kwamba mradi haujakamilika na zaidi ya shilingi milioni 800 bado zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ulifika Jimboni na umezunguka mara kwa mara umeona, ninaamini hata hili ninalolizungumza unalifahamu, tunachohitaji ni shilingi milioni 800 ili mradi huu uweze kukamilika, naona kwamba umuhimu wa umwagiliaji ni mkubwa lakini tunasahau eneo hili la umwagiliaji kwa sababu tumejikita sana kwenye miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie suala la miradi mbalimbali ya maji ambayo haikamiliki katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ningeomba kuishauri Serikali kwamba sasa ifike wakati Serikali ipeleke special audit kwenye miradi yote ya maji katika nchi hii. Nilikuwa kwenye Kamati ya LAAC kwenye kipindi kilichopita nimeshuhudia miradi mbalimbali ya maji ambayo imetelekezwa na wakandarasi, imetekelezwa na Halmashauri, aidha fedha hazijakwenda au kama fedha hazikwenda basi kuna utapeli wa hali ya juu ambao umefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni suala la msingi kwa sababu tutakapoongeza hizi fedha hizi za tozo nina uhakika kabisa kwamba tunaweza kufanya special audit na tukapata miradi mbalimbali ya maji ambayo ilikuwa haijakamilika na hatimaye ikakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kuna Wasimamizi Elekezi (Consultants), katika maeneo mbalimbali ukiangalia watu hawa, ndiyo wamefanya kazi nzuri na wanaendelea kufanya kazi nzuri, lakini kuna maeneo ambayo wamekuwa kama kichaka cha kujipatia fedha bila kuangalia ufanisi wa kazi. Consultant anapewa kazi, anafanya kazi lakini baada ya muda fulani anatokomea na zile fedha ambazo alitakiwa alipwe, analipwa lakini mradi unakuwa haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaotokea vijijini tunaona mengi na tunajua kuwa miradi ya maji ni mikubwa lakini kama fedha zinakuwa haziendi au zinatumiwa vibaya nina uhakika kabisa kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo lazima sasa kama Wizara iweze kuweka jicho lake na kuangalia na kwa umakini zaidi na kuona je ni wapi ambapo tumekosea? Eneo hili ni mojawapo na ninaamini kama tutaweka macho ya uhakika na tukaangalia vizuri tunaweza tukawa na uhakika wa kupata maji katika maeneo mbalimbali ya vijiji vyetu na miji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia mradi mmoja wa Nyamlenge katika Jimbo langu. Design inahitaji shilingi milioni 49, ningeomba Serikali iweze kuangalia mradi huu kwa sababu unakidhi viwango vilevile utapeleka maji katika vijiji zaidi ya 15. Mheshimiwa Waziri naamini unanisikia, uko hapo pamoja na Naibu Waziri ninaomba mradi huu wa maji muweze kuangalia. Nilishapeleka proposal sijajua mpaka leo imefikia wapi na nimejaribu sana kufuatilia bado sijajua hizi milioni 49 ambazo zingeweza kukidhi mahitaji ya mradi huu kama zingepatikana zingeweza kuleta tija sana katika suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema mengi naamini kwa haya machache ambayo nimeyaeleza Serikali itayachukua itaenda kuyafanyia kazi na hatimaye Jimbo la Kalenga na Mkoa wa Iringa uweze kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nikushukuru sana na ninawatakia kila la kheri Wizara ya Maji. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nitajikita zaidi kwenye Kamati yangu…

SPIKA: Dakika tano eeh.

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nitajikita zaidi kwenye masuala ya UKIMWI kwa sababu na mimi pia ni Mjumbe wa Kamati hii ya UKIMWI. Nipongeze juhudi za Kamati ambazo zimefanyika, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kufanya kwa ajili ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, kwenye masuala ya UKIMWI lazima tufahamu kwamba, tatizo la UKIMWI ni kubwa katika nchi yetu, asilimia tano katika asilimia 100 ya Watanzania ndio wenye maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI, lakini tatizo tunalolipata ni bajeti ambayo tunakumbana nayo,
changamoto ya bajeti. Tumeshauri hapa kwenye Kamati kwamba, ufinyu wa bajeti sehemu kubwa au ni chanzo kikubwa sana cha kutoweza kuwafikia ndugu zetu ambao wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo, ingekuwa vizuri zaidi kwamba, Serikali tungeweza kujikita na kuzipeleka fedha, hasa fedha ambazo zinatoka Hazina kuelekea kwenye mifuko mbalimbali, hasa huu Mfuko wa TACAIDS ili tunapopeleka ujumbe wetu kwa ajili ya Watanzania na kuhakikisha kwamba, tatizo hili au ugonjwa huu wa UKIMWI unapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, kuna mikanganyiko au mgongano kati ya Sheria ya UKIMWI na Sheria ya Ndoa, ambapo unakuta Sheria ya UKIMWI inamtaka mtoto mwenye miaka 15 aweze kuambatana na mzazi kwenda kupima, lakini Sheria ya Ndoa inasema mtoto mwenye miaka 14 kwa ridhaa ya mzazi anaweza akaolewa. Sasa ina maana mtoto huyu mwenye miaka 14 ameshaolewa, lakini vilevile arudi tena kwenda kupima akiwa na mzazi wake. Hilo jambo linaleta mkanganyiko kidogo, kwa hiyo, Sheria ya UKIMWI tuiangalie inavyokinzana na Sheria ya Ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna tatizo la takwimu. Kuna takwimu ambazo zinatolewa na NBS, kuna takwimu ambazo zinatolewa na TACAIDS, takwimu nyingine zinatolewa na wadau mbalimbali wa huko nje ya nchi, Ulaya na kadhalika ambao wanatoa fedha kwa ajili ya kuendelea kusaidia changamoto ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, ni vyema sasa ifike wakati hizi changamoto ziweze kupungua, ili kwamba, tunapopeleka takwimu tuweze kupeleka takwimu zinazoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna sehemu nyingine unakuta wanasema Nyanda za Juu Kusini, Mkoa wa Iringa tunaongoza kwa asilimia 13, takwimu nyingine zinasema 11, takwimu nyingine zinasema 10 kwa hiyo, kuna mkanganyiko namna hiyo. Kwa hiyo, lazima tupate takwimu ambazo zinaeleweka ili tuweze kuwaambia Watanzania ukubwa wa tatizo.

Mheshimiwa Spika, lingine nieleze, tatizo la UKIMWI ukubwa wake labda kwa takwimu tu, maambukizi kwa mwaka kwa Tanzania ni maambukizi 81,000. Ina maana kwa mwezi maambukizi ni 6,750 kwa wiki ni 1,687 kwa siku ni 241 na kwa saa ina maana ni watu 10 wanapata virusi vya ugonjwa wa UKIMWI kwa saa. Kwa hiyo, ukiangalia kwa upana wake na ufinyu wa bajeti ambao tunao bado tuko nyuma sana na tunahitaji tuweze kuweka mkazo ili changamoto hii iweze kupungua.

Mheshimiwa Spika, vilevile niseme tu kwamba, kwenye ule mkakati wa 90 90 90 ambao tunaenda nao mpaka mwaka 2020, ni kwamba, kwenye 90 ya kwanza Tanzania bado hatujafanya vizuri, tuko kwenye asilimia 52 ya malengo ya asilimia 90 ambapo hapa ndio kwenye changamoto kubwa ambapo watu wanashindwa kwenda kupima, hasa sisi wanaume tunakuwa wagumu sana kwenda kupima. Vilevile akinamama kwa sababu wanapata nafasi ya kwenda kupima wakiwa wajawazito, inaonesha kwamba, idadi ya akinamama ndio kubwa zaidi kwenye maambukizi, jambo ambalo inaweza ikawa lisiwe sahihi kwa sababu, wanaume tumekuwa ni wazito kidogo kwenda kupima. Kwa hiyo, changamoto hii lazima tui- address kwa wanaume pia kwamba, twende sasa tukapime kwa wingi. Nami Mbunge wa Kalenga nitakuwa miongoni mwa Wabunge wa kwanza kwenda kupima kuwaongoza Wabunge wengine wanaume katika majimbo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye 90 ya pili ni kwamba, kwenye masuala ya upatikanaji wa dawa; ni kweli kwamba, tuna tatizo, lakini kwa sasa hivi tatizo limeshapungua kwa kiasi kikubwa. Niishukuru Serikali kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba niunge mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, kwanza niishukuru sana Wizara ya Maji nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, nimshukuru sana Naibu Waziri, nimshukuru sana, Katibu Mkuu kwa nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji katika Majimbo yetu na katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda sana kuanza na mambo matatu ya muhimu sana, jambo la kwanza nitaenda kwenye mapendekezo ya Kamati, mapendekezo ya Kamati yako mengi, lakini nitazungumza mapendekezo matatu ambayo ningependa sana Wizara iweze kuyasisitiza na kuyaangalia kwa jicho la kipekee, ili tuweze kutatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza katika ukurasa wa 18, katika ripoti ya Kamati, imeelezea na imeshangazwa na kushuka kwa kiwango cha bajeti cha asilimia 9 katika kipindi cha bajeti cha mwaka 2019/2020 ukilinganisha na 2018/2019. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ikiwa kama tuna malengo mazuri ya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya maji, naungana na Kamati kuuliza swali hili, hivi kwa nini kama tuna malengo ya kutatua tatizo la maji katika nchi yetu ya Tanzania bajeti ipungue kwa asilimia 9? Lakini jambo la pili ninaenda tena kwenye ukurasa wa 19 ambapo unasema inazungumzia masuala mazima ya mfuko wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba mwaka uliopita tulizungumza na miaka mitatu sasa mfululizo tumekuwa tukiendelea kuishauri Serikali kuongeza tozo kutoka shilingi 50 mpaka shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kipindi cha miaka mitatu yote, bado hakuna lolote ambalo limefanyika, na kwa kweli kwa sisi Wabunge ambao hasa tunatoka kule vijijini. Tunajua adha ya maji, changamoto kubwa ambayo ipo vijijini ni suala zima la maji, ukienda kule hawaongelei kitu kingine zaidi ya maji, na hata sisi ambao tuko mjini huku wakati tukiwa Dodoma, kitu kikubwa ni maji. Sio kitu kingine, ni maji, utaenda mjini maji, utaenda vijijini maji, sehemu yoyote utakayoenda Tanzania hapa, tatizo ni maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachouliza hivi ni kwa nini Serikali inashindwa kusikiliza na kuamua tu sasa tufanye utaratibu wa kuwa na shilingi 100 badala ya shilingi 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nadhani peke yake itaweza kutatua changamoto hii kubwa sana, kwa sababu kwa asilimia kubwa mfuko wa maji, umechangia kwa asilimia 67 ambao unalipa pamoja na mengineyo unalipa wakandarasi, na unasaidia kuendelea kuwa na vyanzo mbalimbali vya maji. Kwa hiyo, ikiwa kama tutaongeza shilingi 50 kwenda 100 basi nadhani changamoto ya maji tunaweza tukaipunguza kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia ukilinganisha kati ya vyanzo vya mapato ya ndani na hii tozo, utaona kwamba asilimia kubwa ya vyanzo vya ndani havikidhi mahitaji na ndipo hapo utakapoona kwamba asilimia saba ya vyanzo vya ndani vya mapato ndivyo vilivyokidhi mahitaji, lakini kwa asilimia kubwa, asilimia 67 imetokana na changamoto ambayo tumejaribu kuweka tozo ya shilingi 50. Nilikuwa nadhani ni wakati sasa umefika 2019 tuweze kuweka mguu chini, tuweze kuishauri Serikali na Serikali isikilize maoni yetu kama Wabunge kwa sababu tunatoka vijijini tunajua changamoto na tatizo kubwa kule vijijini ni maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine au kitu kingine cha tatu ambacho ningependa kushauri kupitia ripoti ya bajeti ni kwamba kuna maeneo ambayo yameonekana fedha ambazo zinatolewa na Wizara ya Fedha kwenda kwenye maji zinaenda kwa kusuasua. Ningependa kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba fedha zinaenda kwa wakati. Vilevile maeneo mengine madogo madogo kwa mfano kuna misamaha ya kodi kwenye vifaa vya maji, vifaa pia kuchelewa pale bandarini ambapo vyote vimeelezwa kwenye ripoti ya Kamati. Ningependa sana kuendelea kuishauri Serikali kuangalia mambo haya matatu. Pia tunaweza tukaangalia katika yale mapendekezo mengine ya Kamati, lakini kwangu nadhani kwamba haya matatu ni ya msingi sana kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kitu kimoja kwamba Naibu Waziri amefika pale Jimboni kwangu, kuna mradi mkubwa sana ambao unaendelea kwa zaidi ya miaka mitano ambao umekwama, Mradi wa Isupilo, Itengulinyi, Magunga ambao kwa kadri ya nafasi ambayo nimeipata nimekuwa nikiongea na Waziri, amejitahidi kufanya kazi yake, amekuja jimboni kuangalia changamoto hii, amejaribu kutatua, lakini bado changamoto iko pale pale. Wananchi wangu sasa hivi wameshachoka, toka mwaka 2014 wameongea kitu hicho hicho na wamenituma niendelee kuongea kuhusu mradi huu, mradi ambao umegharimu jumla ya shilingi bilioni 2.2, umelipwa bilioni 1.2 lakini mradi umekufa. Sasa hebu tuangalie tunapoteza au hatupotezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea tu kuwasihi viongozi wa Wizara, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwamba tuangalie namna ambayo tunaweza tukalisaidia Jimbo la Kalenga, tukasaidia Mkoa wa Iringa, tukasaidia namna ambavyo tunaweza tukapata maji katika Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia Wizara kwa kutusaidia zile milioni 49 katika Mradi wa Nyamlenge ambao Mheshimiwa Naibu Waziri alitusaidia na Mheshimiwa Waziri analifahamu hili, nilikwenda kwake nimeongea, ametusaidia kuweza kuziweka zile milioni 49 kwa ajili ya ku-design Mradi wa Nyamlenge ambao kwa namna moja au nyingine utasaidia kutatua changamoto katika vijiji 16 katika Jimbo la Kalenga. Naendelea kuishukuru Serikali na kuendelea kuipongeza Serikali kwa sababu nina imani na Mheshimiwa Mbarawa, nina imani na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini vilevile Katibu Mkuu na Wizara yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme tu shukrani kwa baadhi ya taasisi ambazo zimeendelea kulisaidia Jimbo la Kalenga kupata maji. Niseme WARIDI wametusaidia sana ambao ni wa Marekani, USAID wametusaidia pia kwa kiasi kikubwa lakini pia Makanisa ya Anglikana na baadhi ya Makanisa mengine wameendelea kutusaidia katika kuhakikisha kwamba tunapata maji katika Jimbo la Kalenga. Zaidi ya yote niendelee kusisitiza zaidi na zaidi Mheshimiwa Mbarawa alikuja jimboni wiki tatu zilizopita, tukaongea kuhusu Mradi wa Kalenga- Tanangozi na akanisaidia na akasema kwamba niandike andiko ili tuweze kupata fedha kwa ajili ya mradi huu. Maandiko nimeshaandika nitamsaidia kuyafikisha katika meza yake aweze kututatulia tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa yote, pale Kanisani kwetu sisi tuna wimbo huwa tunasema usinipite Mwokozi, usinipite Mwokozi, kwa hiyo nami leo nasema Mheshimiwa Mbarawa asinipite katika bajeti hii, aje Kalenga atusaidie kupata maji. Mungu ambariki, Wizara yake ibarikiwe na namshukuru sana, naamini kabisa kwamba 2019/2020 atatatua tatizo la maji katika Jimbo la Kalenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitambue kazi nzuri ambayo anafanya Engineer Mfugale, kazi nzuri anayofanya Engineer Kindole wa pale Iringa na Ma-engineer wote wa TANROADS Tanzania nzima ninawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya yote namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Manaibu wake wawili wote kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kufanya. Juu ya yote, namshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa ajili ya mabadiliko ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kwa kuzungumzia suala la Uwanja wa Ndege wa Nduli. Uwanja huu upo Mkoani Iringa. Naipongeza sana Serikali kwamba kipindi hiki cha bajeti ya 2019/2020, tumetengewa jumla ya zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa uwanja huu wa ndege. Uwanja huu wa ndege, kwa kweli ukifika sasa hivi pale Iringa ni burudani tupu. Tunajiandaa kwa ajili ya upanuzi na kuelekea sasa kwenye utalii katika upande wa Nyanda za Juu Kusini. Kwa hiyo, tumejipanga na tunaishukuru Serikali kwamba kazi inaonekana na tunaendelea kuipongeza Serikali kwa ajili ya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza pia juu ya takwimu ambazo zimetolewa na Kamati ambayo inahusu masuala ya SUMATRA na ajali kwa ujumla. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba unaona ajali kwa kipindi hiki cha mwaka 2018/2019 bajeti iliyopita, unakuta inasema makosa ya kibinadamu kwenye ajali ilikuwa asilimia 76. Ubovu wa magari asilimia 16, miundombinu na mazingira ni 8%. Sasa mimi nataka nijikite kwa 8%. Tuna barabara mbalimbali ambazo zinajengwa na zimeendelea kuboreshwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza barabara inayotoka Dodoma kuelekea Iringa ambayo imekamilika miaka minne iliyopita. Barabara hii ukiiangalia katika kipindi kifupi imeharibika na haitamaniki tena. Sasa unajiuliza, ni kwa nini tunawatafuta Wakandarasi ambao sio waaminifu? Barabara ile ukipita sasa hivi ina makorongo, ina mashimo na ndiyo inayosababisha ajali kubwa katika maeneo mbalimbali hasa katika njia hii kutoka Dodoma kuelekea Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda pia kuishauri Serikali kwamba tunapotafuta Wakandarasi, basi tutafute Wakandarasi wenye viwango na tuwaadabishe Wakandarasi wote ambao wanafanya kazi bila kujali maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisemi kwamba kuwe na Wakandarasi wa nje au wa ndani, lakini ninachokisema ni kwamba Wakandarasi waweze kutazamwa kwa namna ya tofauti, kwa sababu fedha nyingi zinatumika lakini matokeo yanakuwa ni mabovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza pia suala moja kubwa sana ambalo lipo katika Mkoa wangu wa Iringa kwa barabara ambayo inatoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park, ambayo hata juzi niliongea. Barabara hii ni ya muhimu sana; na umuhimu wake ni kule kwenye mbuga za wanyama za Ruaha National Park. Mbuga hii ya Ruaha National Park, ndiyo mbuga kubwa katika nchi yetu ya Tanzania. Vilevile katika ukanda wa Afrika Mashariki ni mbuga yenye maslahi makubwa sana, ni mbuga ambayo ingetuingizia fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitakwimu Ngorongoro kwa mwaka inaingiza watalii 400,000, Serengeti 150,000, Mikumi 70,000, Ruaha National Park ambayo ndiyo mbuga kubwa ina watalii 35,000. Sasa sioni kama kuna sababu ya kuendelea kutoijenga barabara hii ya Ruaha National Park, kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park ambayo ni kilometa 104. Tumetengewa shilingi milioni 650 tu. Hili jambo lina umuhimu, litatuingizia kipato kikubwa nchi yetu ya Tanzania kama tutakuwa makini kuiangalia kwa namna nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikumbushe kwamba kuna maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Kalenga ambayo hayana mawasiliano ya kutosha. Kijiji cha Lyamgungwe, Kijiji cha Kihanga, Kijiji cha Magunga, Sadani, Kikombwe, Makota, Ulata, Mwambao, Ikungwe, Kidilo, Kaning’ombe, Makombe, Malagosi, Kihanzi na Lyasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Wizara iweze kutazama kwa jicho la kipekee tuweze kupata mawasiliano ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niseme yafuatayo. Naomba ninukuu Biblia Takatifu, Luka 11:9 inasema hivi, “Nami nawaambieni ombeni nanyi mtapewa.”

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba. Inasema, “tafuteni nanyi mtaona,” nimetafuta; sasa naamini nitapata. “Bisheni nanyi mtafunguliwa,” nimebisha naamini Mheshimiwa Waziri utafungua milango.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho mstari wa 10 inasema: “kwa kuwa kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa,” jamani naombeni mnifungulie. Mstari wa 11 unasema: “maana ni yupi kwenu aliye baba ambaye mwanaye akimwomba mkate atampa jiwe au samaki? Badala ya samaki atampa nyoka? Au akiomba yai, atampa ng’e.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba barabara inayotoka Iringa Mjini kuelekea Ruaha National Park. Haya yote naomba yaweze kunukuliwa na Mheshimiwa Waziri muweze kuyafanyia kazi, Iringa tuweze kupata barabara ya Ruaha National Park.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, Mungu awabariki, tuko pamoja sana. Ahsanteni sana. (Kicheko/ Makofi)