Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zainab Mndolwa Amir (3 total)

MHE. ZAINAB M. AMIR aliuliza:-
Mboga za majani ni lishe bora kwa afya ya binadamu na wakulima wengi wa mbogamboga katika Jiji la Dar es Salaam wanatumia maji yasiyo salama kwa ajili ya kumwagilia na huenda maji hayo yana kemikali zinazoweza kusababisha mbogamboga hizo kudhuru afya za wananchi badala ya kuziimarisha:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji safi na salama wakulima hao wa mbogamboga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kuzingatia umuhimu wa afya za wananchi inaendelea kutoa miongozo na ushauri kuhusu maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu na kwa shughuli za uchumi. Katika kuhakikisha wananchi wanalima mbogamboga katika maeneo sahihi, Serikali iliunda Kikosikazi kwa kushirikisha Maafisa wa Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC).
Mheshimiwa Spika, kikosi hicho kilitembelea baadhi ya mito iliyopo Dar es Salaam na kugunda uchafuzi mkubwa wa mazingira unaosababishwa na utiririshaji wa maji taka kutoka majumbani na kwenye viwanda na hivyo maji hayo kuwa na kemikali zisizofaa kwa matumizi ya kilimo cha mbogamboga, kwa mfano maji ya Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inawakataza wananchi kulima mbogamboga katika maeneo hayo yenye uchafuzi kwa kuwa maji hayo yana athari kwenye afya. Aidha, kwa kuwa suala hili ni mtambuka na linahusu uchafuzi wa mazingira, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, inaendelea kupima maji ya mito hiyo na kutoa taarifa za hali ya maji. Pia halmashauri za manispaa katika Jiji la Dar es Salaam zinashauriwa kutunga na kusimamia sheria ndogo kwa ajii ya kudhibiti uchafuzi wa maji ya mito hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kufanya shughuli zao za kilimo cha umwagiliaji, ikiwemo umwagiliaji wa mbogamboga katika maeneo sahihi.
MHE. ZAINABU M. AMIRI aliuliza:-
Je ni lini Serikali itapunguza bei ya gesi kwa matumizi ya majumbani ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi yao ya nyumbani na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Mndolwa Amiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, gesi iliyogunduliwa nchini ni gesi asilia (natural gas) ambayo husafirishwa kutoka kwenye visima vya gesi hadi kwa watumiaji kupitia mabomba. Mpaka sasa watumiaji wakubwa wa gesi hapa nchini ni viwanda na mitambo ya kufua umeme. Mradi wa majaribio wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ulianza kupitia mradi wa mfano (pilot project) ambapo nyumba 70 zilizopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam zimeunganishwa na gesi kwa matumizi ya nyumbani.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa gesi inayotumiwa na wananchi kupikia majumbani ni Liquefied Petroleum Gas (LPG) ambayo huagizwa na wafanyabiashara kutoka nje kama ilivyo katika mafuta ya petrol, diesel na mafuta ya taa au ndege. Gesi hii hujazwa katika mitungi kwa ujazo tofauti tofauti na gharama ya gesi hii inategemeana na soko la dunia.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha wawekezaji katika sekta ya gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani ili kuleta ushindani katika sekta hii. Mpaka sasa makampuni mengi yameanza kujenga miundombinu ya gesi katika sehemu mbalimbali za nchi na kuonesha nia ya kushirikiana na Serikali katika kusambaza gesi asilia nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TPDC imeanza matayarisho ya kutekeleza mradi wa kuunganisha gesi majumbani ambapo awamu ya kwanza ya mradi huo utapita katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Mtwara na baadaye katika mikoa mingine ya nchi yetu. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ZAINAB M. AMIRI aliuliza:-
Daraja la Kigamboni ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na mawasiliano.
(a) Je, tangu daraja lianze kutumika Serikali imekusanya kiasi gani cha fedha kinachotokana na malipo kwa wanaovuka na vyombo vya moto?
(b) Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kutumia kadi maalum (smart card) kulipia kwa mwezi malipo kwa wanaovuka darajani hapo kwa vyombo vya moto?
wanaovuka darajani hapo kwa vyombo vya moto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao ndiyo wanasimamia uendeshaji wa daraja hilo hadi kufikia mwezi Machi, 2018 limeshakusanya kiasi cha Sh.19,734,655,482.70 tangu daraja hilo lilipoanza kutumika rasmi mwezi Mei, 2016. Aidha, katika mapato hayo, shilingi bilioni 15.2 ni makusanyo ya waliovuka na vyombo vya moto na shilingi bilioni 4.7 ni faida na pato la ziada la mtaji lililotokana na upatikanaji wa fedha hizo katika dhamana ya Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii lipo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi wa kuweka mfumo utakaotumia kadi maalum (smart card) kwa malipo ya wanaovuka darajani hapo. Mvukaji atakuwa na hiari yake ya kulipia kwa siku, wiki au mwezi kulingana na uwezo wake.