Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Sonia Jumaa Magogo (7 total)

MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani dhidi ya waajiri ambao hawawaandikishi Watumishi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuwasababishia kukosa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali katika kuhakikisha waajiri wote wanaandikisha wafanyakazi wao kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya Mwaka 2008, Kifungu cha 30 ambacho kimeweka utaratibu unaomtaka mwajiri kuwaandikisha watumishi wake katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Aidha, mwajiri anayekiuka matakwa ya kifungu hiki anastahili adhabu ya kulipa faini ya kiasi kisichozidi shilingi milioni ishirini kwa mujibu wa kifungu cha 55 cha Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha usimamizi wa Sheria za Kazi, Serikali kupitia Bunge ilifanyia marekebisho ya Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 ili kuimarisha mfumo wa kaguzi za kazi mahali pa kazi kwa kuruhusu kutoa adhabu za papo kwa papo kwa waajiri wanaokiuka matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kutosajili au kuandikisha wafanyakazi katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. SONIA J. MAGOGO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama ambao wanajifungua kabla ya kipindi cha kuruhusiwa kupata tena miezi mitatu ya mapumziko ili waweze kuwahudumia (kuwanyonyesha) vichanga hao huku wakiendelea na majukumu yao ya kiofisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni namba H12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, mtumishi wa umma anapojifungua hupewa likizo ya malipo ya siku 84. Hata hivyo, iwapo atajifungua zaidi ya mtoto mmoja (mapacha au zaidi), ataongezewa siku 14 na hivyo kuwa na likizo ya siku 98.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mtumishi wa umma atajifungua mtoto/watoto kabla ya kutimiza miaka mitatu atapewa likizo maalum ya wiki sita ili kuhudumia mtoto wake kwa mujibu wa Kanuni H12(6) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009. Baada ya hapo Serikali inaweza kumuongezea siku za kupumzika kulingana na ushauri wa daktari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, likizo ya uzazi hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu kwa kuzingatia Sera ya Afya ya Mama na Mtoto inayosisitiza kulinda afya ya mama na mtoto na pia kuhimiza uzazi wa mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sera hii, msingi wa Serikali kuhimiza likizo ya uzazi kwa utaratibu huu ni kutoa fursa kwa watumishi wa umma kupata muda wa kutosha kutekeleza majukumu ya ajira yao na kuzingatia pia uzazi wa mpango.
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-
Je, Serikali inasaidiaje watoto wa Shule za Msingi Wilayani Handeni ambao wamekuwa wakisongamana sana kwenye darasa moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba uniruhusu nimkaribishe Mheshimiwa Sonia kwenye kazi za Bunge baada ya kuwa ameugua kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ongezeko la wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ni moja ya changamoto iliyotokana na utekelezaji wa Sera ya Elimu Bila Malipo. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilikamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa sita kwa kiasi cha shilingi milioni 40.96 katika shule za msingi Kwazala, Ugweno na Gumba na Mbunge wa Handeni Mheshimiwa Mboni Mhita, kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo alikamilisha ujenzi wa madarasa saba kwa gharama ya shilingi milioni 37.63 katika shule za Kabuku Mjini, Gole, Mnyuzi na Msilwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imejenga vyumba sita vya madarasa kwa gharama ya shilingi milioni 120 katika Shule za Mhalango, Kitumbi na Komkonga na kukamilisha ujenzi wa vyumba sita vya madarasa kwa gharama ya shilingi milioni 23.5 katika Shule za Kwachaga na Kibundu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 137.2 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika Shule za Msingi Kiselya na Mhalango.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Handeni na inawaomba wananchi na wadau kushiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa, maana Serikali peke yake haitoweza kuwa na bajeti ya kutosheleza mahitaji yote ya Ujenzi wa miundombinu ya shule kwa kipindi kifupi.
MHE. NURU A. BAFADHILI (K. n. y. MHE. SONIA J. MAGOGO) aliuliza:-
Tatizo la maji limekuwa sugu sana Wilayani Handeni:-
Je, Serikali imefikia wapi katika kutatua tatizo hili la kunusuru maisha ya wananchi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, ambapo kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018, ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 921 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya maji nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatekeleza ujenzi wa Mabwawa ya Kwandugwa, Mkata na Manga ambayo hadi sasa wakandarasi wapo katika maeneo ya kazi. Serikali inaendelea na usanifu wa miundombinu ya miradi ya maji katika Kijiji cha Pozo na kufanya utafiti wa kuchimba visima katika Vijiji vya Msirwa na Mkata Komnara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inatekeleza mradi wa kitaifa wa Handeni ambao utahudumia vijiji 70 vya Wilaya ya handeni. Serikali imepata fedha za mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi wa kitaifa wa Handeni. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha mitambo ya kusafisha maji, ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji na ulazaji wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji. Ujenzi wa mradi huo utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la maji kwenye Halmashauri ya Handeni na utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2018/2019. (Makofi)
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Handeni ambao wanakosa ardhi ya kuendesha shughuli zao za kilimo kwa sababu ya kumilikiwa na wachache?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa mashamba uliofanyika katika kipindi cha 2018/2019 Wilayani Handeni ulibaini kuwepo kwa mashamba manne makubwa yenye hekta 7,279.26 ambayo hayajaendelezwa ipasavyo na hivyo kupelekea baadhi ya mashamba hayo kuvamiwa na wananchi. Serikali inaendelea na utaratibu wa ufutaji wa miliki za mashamba hayo yaliyokiuka masharti ya uendelezaji ambapo wamiliki wanne wameshatumiwa ilani zao ubatilisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miliki hizo kubatilishwa, ardhi husika itaandaliwa mipango ya matumizi ikiwemo ya kilimo na ufugaji na kugawia kwa wananchi wenye uhaba wa ardhi. Aidha, mipango hiyo itazingatia utengaji wa ardhi ya akiba (land bank) kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa wananchi kutumia ardhi yao kwa tija kwani ardhi haiongezeki wakati idadi ya watu, mifugo na shughuli za uzalishaji zinahitaji ardhi zinaongezeka. Vilevile, viongozi wa Vijiji na Kata waache tabia ya kuwagawia ardhi kwa mtindo wa kuwakodisha wananchi kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na sheria za nchi yetu.
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza Madaktari Bingwa nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jin sia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa katika ngazi mbalimbali za huduma nchini ikiwa ni pamoja na hospitali yetu ya Taifa Muhimbili. Katika Mwaka 2017/2018, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilitenga kiasi cha shilingi bilioni Mbili zilizotumika kwa ajili ya kusomesha Madaktari Bingwa 125 wa fani za kipaumbele katika Chuo cha Muhimbili (MUHAS) ambao wanatarajia kukamilisha masomo yao mwaka 2020/ 2021. Aidha, katika mwaka 2018/2019, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ili kuendelea kugharamia mafunzo ya ngazi ya kibingwa katika kada mbalimbali za afya 127 katika Chuo cha MUHAS. Aidha katika mwaka 2018/2019 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ili kuendelea kugharamia mafunzo ya ngazi za bingwa kwa kada mbalimbali za afya 127 katika Chuo cha MUHAS.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni, 2019 jumla ya watumishi wa sekta ya afya 458 walikuwa wanaendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za taaluma kwa idadi hiyo, 435 wanaendelea na masomo yao ndani ya nchi na 23 nje ya nchi kwa ufadhili wa Serikali; katika idadi hiyo, jumla ya madaktari bingwa 365 wanatarajiwa kuhitimu mafunzo kuanzia mwaka 2019/2020, 2020/2021, 2021/2122. Wataalam wote hawa watasambazwa katika hospitali mbalimbali nchini kulingana na uwiano wa wataalam waliopo na kwa kuzingatia maeneo yenye uhaba mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/2020 Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya watalaam bingwa katika fani za kipaumbele. Kutokana na uhaba uliopo katika hospitali za rufaa za mkoa Wizara itahakikisha fedha hizi zinatumika vyema katika kusomesha wataalam wanaotoka katika maeneo yenye uhaba mkubwa. Aidha Wizara kupitia hospitali za rufaa za Taifa na taasisi za nje inaendelea kuendesha kambi za udaktari bingwa hapa nchini kwa lengo la kusogeza huduma za kibingwa na kuwajengea uwezo wataalam wetu.
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kubadilisha au kurekebisha sheria ambazo zinaonekana kupitwa na wakati au kuchochea ukandamizaji kwa mama na mtoto?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya tathmini na kuwasilisha baadhi ya sheria zenye upungufu ili Bunge lako tukufu likiona inafaa kuzibadili au kufanya marekebisho ya sheria hizo. Serikali imefanya marekebisho ya baadhi ya sheria na kupitia Bunge hili marekebisho mbalimbali yamefanyika naomba kutoa mifano michache. Sheria ya makosa ya Jinai Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kifungu cha 130(1)(2)(e) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela au kifungo cha maisha kwa kosa la kujiamiana na mtoto wa chini ya umri wa miaka 18.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 Sura ya 353 kifungu cha 60A(1)(2) na (3), inayotoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu yeyote atakayempa mwanafunzi mimba. Marekebisho haya yanalenga kulinda haki ya mtoto wa kike kupata elimu, vilevile Serikali ilitunga Sheria ya Msaada wa Kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 ambayo inasaidia upatikanaji wa msaada wa kisheria bure kwa wanawake na watoto wasio na uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na marekebisho ya sheria hizo zinazolenga kulinda haki na ustawi wa wanawake na watoto, Serikali imeandaa mpango kazi jumuishi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa 2017/2018 - 2021/2022. Mpango huu wa kisekta unatekelezwa na wizara 11 chini ya uratibu ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wengine wa wanawake na watoto.

Mpango huu una eneo mahususi linaloshughulika na utekelezaji wa sheria zinazohusu wanawake na watoto.