Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sonia Jumaa Magogo (19 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa na afya njema mpaka wakati huu na kuweza kusimama mbele yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kukishukuru Chama changu cha Wananchi CUF chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wetu, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, akisaidiana na Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Magdalena Sakaya. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa sijafanya busara kama sitalishukuru Bunge lote kwa kutupokea vizuri na kutupa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeupitia Mpango wa Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Mpango uko vizuri. Pamoja na uzuri wa Mpango huo, nami ninayo machache ambayo natamani yaingie au yatiliwe mkazo katika Mpango ambao upo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa ni suala la lishe. Katika Mpango huo sikuona kama suala la lishe limetiliwa umuhimu sana kama lilivyo katika jamii yetu. Kila mtu anafahamu umuhimu wa lishe na hata sisi tusingekuwa hapa kama tusingekuwa na afya njema na kupata lishe iliyo bora. Hivyo, naishauri Serikali iliangalie sana suala la lishe. Iziwezeshe taasisi ambazo zinahusika na suala la lishe ili wananchi wapate elimu na kuelewa umuhimu wa lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna utajiri wa vyakula na kama wananchi wangepata elimu ya kutosha, tusingekuwa na watoto wanaozaliwa wakiwa wamedumaa akili. Hivyo, naishauri Serikali itilie mkazo kwenye suala la lishe kwa sababu kuna usemi unasema prevention is better than cure. Kwa hiyo, naishauri Serikali i-stick katika kuepusha maradhi kwa kizazi kilichopo na kijacho kuliko kusubiri tumeshapata matatizo tunanunua dawa kwa pesa ambazo zingesaidia kwenye vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa viwanda, kitu cha kwanza napenda tujiulize ni kwa nini vile viwanda vilivyokuwepo vilikufa. Je, zile sababu zilizosababisha vile viwanda vikafa leo hazipo tena? Kama zipo tunafanyaje ili kuhakikisha kwamba viwanda hivyo ambavyo vinakwenda kuanzishwa tena havitakufa na vitakuwa endelevu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano suala la malighafi. Naishauri Serikali ijiandae vizuri kwenye suala la malighafi kabla ya kuanzisha viwanda vingi. Tulikuwa na mazao ambayo sasa hivi tunaona yameshuka ama mengine hayapo kabisa, kama mazao ya mkonge, pamba na michikichi. Kwa hiyo, naishauri Serikali, kabla hatujaenda kufungua viwanda vingine zaidi tuangalie uwepo wa malighafi ili viwanda hivyo visije vikaenda na vyenyewe vikafa kama vile ambavyo vilikufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie workforce, je, workforce iliyopo inatosha kwa hivyo viwanda ambavyo tunahitaji kuvianzisha? Elimu ikoje kwa wale watu ambao wanakuja kufanya kazi kwenye viwanda hivyo, ujuzi wao ni kiasi gani katika kuendesha viwanda hivyo? Kwa sababu kama tukiwa hatuna workforce ya kutosha hivyo viwanda na vyenyewe vitakwenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mitaji, nauliza Serikali imejipangaje kwa suala la mitaji ya kuendesha viwanda hivyo. Je, tumeiandaa vipi Benki yetu ya TIB katika suala hilo la kuendesha viwanda? Kama tunategemea watu binafsi, je, Serikali imejiandaaje katika kukusanya kodi kuhakikisha kwamba kodi zetu hazipotei na zinapatikana kwa wakati muafaka na kuendeleza Taifa letu kama tulivyopanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kugusia suala la elimu, natamani kuona Serikali ikiwa imetilia sana mkazo kwenye suala la elimu hasa elimu ya msingi. Watoto wanajazana kwenye madarasa na pale hatutegemei ma- engineer, ma-doctor wala Wabunge na Mawaziri ambao watakuwa na akili tulivu kama tulivyo sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wetu tumesoma kwenye shule za kulipia lakini population kubwa iko kwenye shule zile ambazo tunaita za kata, lakini ukiangalia wale watoto mazingira wanayosomea ni magumu sana, hata wale Walimu wanaowafundisha hawapati ile motisha ya kutosha kuweza kuwahudumia wale watoto. Hivyo, naishauri Serikali iangalie kwa sababu msingi wa elimu unaanzia chini, hata sisi tusingekuwa na msingi mzuri mimi na wewe leo tusingekuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie elimu zinazotolewa kwenye vyuo vyetu. Wasomi wengi wanatoka vyuoni lakini wanakuwa kama wame-cram, ukimpeleka kwenye kufanya kazi ile aliyoisomea, hawezi. Kwa hiyo, tuangalie ile quality ya elimu inayotolewa katika vyuo vyetu na inatolewa kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutoe elimu ya ujasiriamali hasa kwa vijana. Vijana wengi wanamaliza vyuo wakiwa na mentality ya kwamba nakwenda kuajiriwa Serikalini. Tunaweza kuwajengea uwezo kuanzia chini ya kwamba sio lazima kila mtu aajiriwe, unaweza kujiajiri na ukawa na maendeleo zaidi hata ya yule mtu aliyeajiriwa. Hivyo, naiomba Serikali iangalie sana juu ya elimu ya ujasiriamali kwa vijana na vilevile kuwawezesha mitaji pale wanapopata hiyo elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila aliyesimama hapa aligusia suala la maji. Mimi pia naomba nichangie kuhusu maji. Maji imekuwa ni tatizo kubwa katika nchi yetu, kuendesha viwanda kunahitaji maji, shughuli zote maofisini zinahitaji maji, hospitali zinahitaji maji na shule zinahitaji maji. Hivyo, tunaomba sana Mpango huu utilie mkazo suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi vijijini wanateseka sana na suala la maji. Kama mwananchi ananunua ndoo moja ya maji kwa Sh.1,000/= kijijini, je, ana uwezo kweli wa kuhimili maisha yake? Kwa sababu tunajua kipato cha wananchi wa chini, wale wa vijijini, lakini kama anatakiwa
kununua ndoo moja ya maji ya Sh.1,000/= kwa siku maisha yake yanakuaje? Naomba sana na hilo litiliwe mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi kukazia kwenye bomba la mafuta linalopita Tanga. Huu ni mradi mkubwa sana unaopita mkoani kwetu. Naiomba Serikali iwasaidie wananchi wa Tanga kupitia mradi huu waweze kunufaika zaidi kwa kuwapa elimu na vitendea kazi na kuwapa kipaumbele hata katika zile ajira ambazo zinatokea ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kabisa nianze kwa kuzipongeza Kamati zote kwa uwasilishaji mzuri. Pili, ningependa pia kuipongeza Kamati ya Maliasili ambayo imeona umuhimu wa mapango ya Amboni na kuishauri Serikali kuyafanyia ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Tanga una vivutio vingi sana ambavyo vilikuwa vinausaidia mkoa wetu kuinuka zaidi kiuchumi, lakini kwa sasa vivutio hivyo vimekuwa kama vimetelekezwa. Hivyo, ninaishauri Serikali kupitia upya vivutio hivi na kuona inafanya nini ili kurudisha ile hadhi ya Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda kuchangia kuhusu migogoro ya ardhi. Hapa katika migogoro ya ardhi, ukiangalia sana chimbuko linakuwa ni Serikali ambazo ziko kule vijijini hasa viongozi wa Serikali za Vijiji. Viongozi hawa wamekuwa wakiuza ardhi za wananchi bila kuwashirikisha na kusababisha migogoro mikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekuwa wakikosa ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, hivyo kupeleka wenyewe kwa wenyewe kugombana na kusababisha uhasama mkubwa baina ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie na kudhibiti hivi vyanzo vya migogoro ya ardhi hasa kwa hawa Wenyeviti wa Serikali kwa kuwachukulia hatua ambazo zitasababisha waache hii tabia ya kuuza ardhi na kusababisha wananchi kushindwa kuendeleza kilimo chao ambacho ndiyo sehemu kubwa ya utegemezi ya kukuza uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine na mimi naomba kuchangia kuhusu maji. Wewe mwenyewe umekuwa shahidi hapa, kila Mbunge anayesimama analia kuhusu maji katika eneo lake. Maji ni kama uti wa mgongo, hakuna shughuli yoyote inayoweza kuendelea bila uwepo wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia viwanda, lazima kuwe na maji, tukizungumzia afya, lazima kuwe na maji na hata kilimo hakiwezi kuendelea bila uwepo wa maji. Mathalani mkoa wetu wa Tanga una vyanzo vya maji kama Ruvu na Pangani, lakini bado tatizo la maji limekuwa ni kubwa sana. Naishauri Serikali ingalie sehemu zile ambazo zina vyanzo vya maji iweze kuvitumia ili kupunguza haya matatizo ya maji kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna miradi mikubwa ambayo bado Serikali inaitekeleza, nilikuwa naishauri Serikali, wakati inatekeleza miradi hiyo, iangalie njia mbadala za kuwasaidia wananchi kama kuchimba mabwawa na visima ili waweze kujikimu wakati wanasubiri utatuzi wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niongelee kuhusu kilimo. Kipindi cha nyuma tulikuwa tunaona watu ambao wanajikita kwenye kilimo zaidi ni wazee, lakini kwa sasa tunaona asilimia kubwa ya vijana nao wameamua kuingia kwenye kilimo. Kwa hiyo, naishauri Serikali iwape motisha hawa vijana ili wasirudi nyuma kwa kuwapatia mitaji, kuwasaidia kupata masoko, kuangalia miundombinu, kuwapatia elimu ya nini walime na kwa wakati gani na kutokana na ardhi iliyoko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda ni muhimu sana. Kwa mfano, Mkoa wetu wa Tanga, vijana wanalima matunda kwa wingi, lakini yale matunda yamekuwa yakiozea mashambani kwa sababu hakuna viwanda vya kuweza kusindika yale matunda. Iwapo watakuwa na miundombinu mizuri, watapatiwa viwanda vya kuwasaidia kusindika mazao yao, nina imani wale vijana hawatarudi nyuma na tutaondoa Taifa la wazembe na tutakuwa na Taifa la wachapakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Serikali iangalie kuhusu suala la pembejeo. Wakulima wawezeshwe kuhusu pembejeo, pia zipatikane kwa wakati ili waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zinapotokea ahadi, kwa mfano, kama kipindi walichoambiwa walime mbaazi na kwamba zitakwenda kuuzwa India na ikashindikana, Serikali ni lazima ije na mpango mbadala kuliko kuwaachia wananchi ule mzigo wa mazao kuwaaharibikia mikononi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na leo tena nimeweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya PAC na ningependa kuchukuwa fursa hii kumpongeza Mwenyekiti wangu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa kuwasilisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza, nilikuwa na ushauri kidogo kwenye haya Mashirikia na Taasisi ambazo Serikali inawekeza fedha zake. Ninachoona hapa kwanza haya Mashirika yenyewe kwa yenyewe wanatakiwa yawe na mahusiano mazuri. Ikiwa haya mashirikia yatajitangaza vizuri na ikajulikana yanafanya nini na wenyewe kwa wenyewe wakawa wanapeana huduma, kwa mfano SUMA JKT, wanatengeneza furniture nzuri sana, wanatengeneza product ya maji ambayo walileta kwenye Kamati yetu na tuliyaona ni mazuri na bei yake ni nzuri. Hivyo kama Serikali itaunga mkono na wenyewe kwa wenyewe wakasaidiana, kwa mfano, kukawa kuna maelekezo kwamba furniture zote zinunuliwe kutoka SUMA JKT, ama sehemu kubwa furniture za Serikali ziwe zinatoka SUMA JKT, itawasaidia kutengeneza faida zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bandari, tukiangalia bandari yetu ya Dar es Salaam, ina mlundikano wa mizigo mingi sana; lakini kuna bandari ya Tanga na bandari ya Mtwara. Kama kutakuwa na categorization ya mizigo mingine inakwenda Tanga, mingine inakwenda Mtwara, itasaidia na zile bandari nyingine kuweza kujiendesha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunaona Serikali yetu inavyotumia fedha nyingi katika kutengeneza miundombinu ya barabara. Bandari wanaweza wakawatumia zaidi TRC kusafirisha mizigo kuliko kutumia malori ambayo yanapita na mizigo mikubwa kwenye barabara na kuharibu miundombinu ya barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni bajeti ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Kama tulivyoona, hii Ofisi ina mashirika mengi sana ya kusimamia. Kama watapewa bajeti nzuri ya kutosha na ikaenda kwa wakati na wakawa wanafanya performance contract na zile Taasisi, pia wakawa na ufuatiliaji wa expenditure kwenye zile taasisi mara kwa mara, itasaidia kufanya zile taasisi ziwe na uwoga na kutengeneza faida kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo tunaona kuna madeni mengi sana hizi taasisi zinadai. Serikali ingeweza kuwasaidia ili waweze kukusanya yale madeni yao pale ambapo wao wamefikia ukomo. Kwa mfano, tunaona wengine ni waajiriwa Serikali na wengine wanajulikana wako wapi, wanaweza kutaifishiwa mali zao. Serikali iwasaidie kama vile ilivyowezekana kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na wenyewe wasaidiwe ili hizi fedha zirudi ziwadaidie kuendesha shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni suala la kukaimu. Mtu anapokuwa anakaimu, anakuwa na hali ya uwoga. Yaani anakuwa hana ile full mandate, anakuwa na wasi wasi kwenye kile kitu anachokifanya, hasa kwenye zile level za Management. Kwa hiyo, kama watasaidiwa kuondoa hili tatizo la kukaimu na wakawa wanawapa wale watu wanaokaimu madaraka au kuziba zile nafasi kwa wakati, itasaidia sana kuchochea maendeleo katika zile taasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote ningependa kuupongeza uongozi mzima wa Chama changu cha Wananchi (CUF) ukiongozwa na Mwenyekiti wetu mahiri kabisa, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuaminiwa na Wanachama wote na kupewa tena ridhaa ya kukiongoza chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende moja kwa moja kuchangia kwenye hoja na nitaanza na suala la uwekezaji. Katika kuwekeza, Serikali pia inawekeza kwenye Mashirika ya Umma ambayo yapo nchini kwetu na inaweka mtaji wake kwa lengo la kupata gawiwo ambalo litakuja kuisaidia Serikali katika shughuli zake mbalimbali za kuinua uchumi pamoja na huduma mbalimbali za jamii na tumeona mwaka jana baadhi ya Mashirika haya yametoa gawio zuri kwa Serikali. Ndhani kama Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo ndio msimamizi mkuu wa mashirika haya, ikiwezeshwa vizuri na kupewa bajeti ya kutosha na kwa wakati ikayasimamia zaidi haya mashirika gawio hili litaongezeka maradufu ya lile ambalo tulipata mwaka jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kuongelea kuhusu wazee waliokuwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wazee hawa waliitumikia nchi yetu kwa uaminifu, walisaidia kuleta mahusiano mazuri baina ya nchi yetu na waliokuwa Washirika wetu wa Afrika Mashariki, lakini bado wazee hawa wanahangaika kila kukicha na madai ambayo bado hayajapata suluhu mpaka leo. Kumekuwa kuna kesi mbalimbali wanaendesha, kwa hiyo, inabidi wakati mwingine watoe michango kwa ajili ya zile kesi, wakati mwingine inabidi wasafiri kutoka sehemu mbalimbali kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mikutano yao ya kukutana kufuatilia madai na ukizingatia wazee hawa hali yao ya kiuchumi siyo nzuri. Kwa hiyo napenda kuishauri Serikali katika suala hili watoe tamko rasmi kwa hawa Wazee. Kama kuna chochote ambacho wanadai basi Serikali iwalipe ili waweze kupumzika na kama hakuna madai vilevile lingetoka tamko ili wakajua ni nini ukweli wa haya madai ambayo wanafuatilia kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine bado nipo kwa Wazee na nazungumzia suala la pensheni wanayopata kila mwezi. Kwa kweli pension wanayopata kila mwezi baadhi ya Wazee ni ndogo. Kumlipa Mzee pension ya chini ya kiwango cha laki moja kwa mwezi ni kama unamwonea. Tukilinganisha hali ya maisha tuliyonayo kwa sasa na kile kiwango wanachopata, wazee wale wana familia, wazee wale wanatunza wajukuu lakini kile kiwango wanacholipwa kwa ajili ya kuendesha maisha yao ni kidogo sana. Hivyo naiomba Serikali iangalie inawasaidiaje ili kuongeza hiki kiwango cha pensheni ya kila mwezi hawa wazee waweze kujikwamua na umasikini ambao wanao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi nikizingatia wazee hawa pia hawana mfuko maalum kama walivyo vijana, walemavu, wanawake ambao wanapata asilimia 10 kwenye Halmashauri zao, lakini kwa upande wa Wazee wao hawamo katika hii asilimia 10. Kwa mujibu wetu ni kwamba vijana wanaishia miaka 45. Kwa hiyo, kuanzia miaka 46 tunasema tunawachukulia kwamba wapo kwenye kundi la Wazee, lakini bado ni watu ambao wana nguvu, wanaweza kuitumikia nchi yetu, wanaweza kujenga uchumi. Kwa hiyo, wakiwezeshwa na Serikali kama wanavyowezeshwa vijana, akinamama na walemavu nao wataweza kuchangia kwenye uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni vijana; mara nyingi tumekuwa tukiwalaumu vijana kwamba wana akili mgando ya kutaka kuajiriwa hawataki kujiajiri. Hata hivyo, hili mimi nalitazama kwa mtazamo mwingine kwamba, je, hawa vijana tunawaandaa vipi ili waje kujiajiri? System yetu ikoje kuanzia shule ya msingi, sekondari hata vyuoni, wanaandaliwa vipi ili baadaye wanapomaliza elimu yao waje kujiajiri na kuondokana na lile wimbi la kuwaza kwamba nitaajiriwa, nitaajiriwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kuna wale ambao wana mawazo yale ya kujiajiri lakini mazingira yenyewe ya kujiajiri yanakuwa ni magumu. Mlolongo wa kuanzisha mathalan biashara au sehemu yake ya kazi unakuwa ni mrefu sana au unakuwa na gharama ambazo yule kijana anashindwa kuzikidhi na kuweza kufungua biashara yake na kujiajiri. Pia wakati huo huo tuna mapori mengi sana katika Tanzania yetu. Ingewezekana Serikali kuwakusanya wale vijana kwenye makundi, kuwapatia zana za kilimo ama kwa kuwakopesha au kuwasaidia wakaweza kuanzisha kilimo na kuweza kuendeleza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye ndugu zetu walemavu; kumekuwa na kesi mbalimbali za walemavu na wengine wanasababishiwa ulemavu huo na watu ambao ni wageni katika nchi yetu, labda wawekezaji ama watu mbalimbali. Hata hivyo, zinapokwenda zile kesi za hawa ndugu zetu walemavu na ukiangalia na mazingira ambayo wanakuwa tayari wanayo zile kesi zinachukua milolongo mingi sana, zinakuwa na ucheleweshwaji ndani yake hivyo kuwasababishia kuwa na maisha magumu zaidi. Hivyo, ningependa pia Serikali iwasaidie hawa ndugu zetu kwa kuwasimamia kwenye kesi zao na kuwahakikisha ufumbuzi unapatikana haraka kwenye hizo kesi ili waweze kuendelea na harakati za maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri kugusia baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga kuwemo katika miradi ambayo inaendelea kutekelezwa lakini ningeiomba Wizara iiangale miradi hii kwa jicho la tofauti. Nasema hivi kwa sababu miradi mingi ya maji Mkoani Tanga imechukua muda mrefu sana kukamilika na imezua sintofahamu kwa wananchi, hawajui ni kwa nini miradi hii imekuwa ni ya muda mrefu lakini haikamiliki na kuendelea kuacha changamoto ya maji ikiwakabili Wananchi hawa wa Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano wa mradi wa maji wa HTM; huu mradi umechukua muda mrefu sana na umesababisha tatizo kubwa sana la maji kwa wananchi wa Wilaya ya Handeni. Wilaya ya Handeni tatizo la maji limekuwa kama ni historia sasa na kila siku wanapewa ahadi juu ya huu mradi kwamba kuna mradi wa maji, kuna mradi wa maji lakini huu mradi umekuwa haukamiliki na wananchi wanaendelea kuteseka sana na maji. Hivyo, niiombe Serikali iangalie kwa jicho la tofauti ni nini kinazuia huu mradi usikamilike na wananchi wale waweze kupata maji kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga tuna vyanzo vingi vya maji na sioni ni kwa nini tunakuwa na tatizo kubwa sana la maji kiasi hiki. Hivyo Serikali iangalie vile vyanzo ambavyo tunavyo kuweza kuwasaidia wananchi hawa wa Mkoa wa Tanga kuondokana na hili tatizo la maji. Sisi sote tunafahamu umuhimu wa maji katika maisha ya mwanadamu na Mkoa wetu wa Tanga shughuli zetu nyingi sana zimetawaliwa na viwanda na kilimo, lakini tunapokuwa na uhaba wa maji tayari kwetu hili linakuwa ni tatizo kubwa sana. Huwezi kuendesha viwanda kwa ufanisi kama huna maji ya kutosha, huwezi kuendesha shughuli za kilimo kwa ufanisi kama huna maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Sera ya Elimu bure ambayo inatolewa na Serikali. Hii sera ya elimu bure itakuwa haimfikii hasa mtoto wa kike vile ipasavyo kwa maana watoto hawa muda mwingi ndiyo wanatumika kwenda kusaka maji. Ule muda ambao wangeweza kuutumia kwenye masomo unakuta wanautumia kwenda kutafuta maji na katika harakati hizo za kutafuta maji ndiyo unakuta watoto wengi wanapata mimba za utotoni na maradhi mengine ambayo hayatibiki. Wakati huo huo kuna kipindi ambacho mtoto wa kike anakuwa kwenye hedhi na shule nyingi hazina maji. Unakuta mtoto ile hali inampelekea asiende shule kwa kuogopa kwamba nikienda shule nitajisitiri vipi nitakapokuwa katika hali hii. Hivyo Serikali iwasaidie watoto hawa kama tumeamua kuwapa elimu bure basi ikamilike pia, tuangalie na vichocheo ambavyo nivapelekea hii elimu iweze kuwafikia kwa ufanisi ikiwemo suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye miundombinu ya maji; miundombinu yetu ya maji haijakaa vizuri na hii inapelekea wananchi wengi kulalamikia suala la bili ambazo haziko realistic kutokana na kile ambacho wanakitumia. Mabomba mengi yanavuja na unaweza ukamwita fundi labda ukapiga simu ili upate msaada, lakini hupati ule msaada kwa wakati, hivyo kupelekea kupata bili ambayo pengine ilikuwa siyo tatizo lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hii system ambayo inanipa utata ya kwamba maji yanapovuja mbele ya mita inakuwa ni juu ya ofisi lakini inapovuja nyuma ya mita inakuwa ni juu ya mteja. Hili ni tatizo kwa sababu kama miundombinu yenu haiko sahihi ni lazima maji yatavuja. Pia tungeweza kuzuia pale mwanzo wakati yule mteja anaweka ile system yake ya maji kukawa na watu ambao wanakuaja kukagua kabla hamjamwekea maji ili kuona kama ameweka vitu vyake kwa usahihi ambapo itapelekea mwananchi huyu asipate bili zinazosababishwa na uvujaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine naomba pia Serikali iangalie umuhimu wa kutoa elimu juu ya matumizi ya vyanzo vya maji kwa wananchi. Wananchi wengi hawana uelewa juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kupelekea vyanzo vingi kukauka na uharibifu wa vyanzo hivi vya maji. Hivyo, niiombe Serikali kuliko kuangalia zaidi kwenye kuwapa adhabu hawa wananchi waangalie zaidi kuwaelimisha kuwasababisha wawe mabalozi wazuri kwa utunzaji wa vile vyanzo vya maji ambavyo vinawazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nizungumzie mfumo wa prepaid. Mfumo huu kama ungeweza kusisitizwa nchi nzima na ukatolewa elimu kila mtu akaufahamu vizuri ungeweza kusaidia kupunguza haya malalamiko ya bili za wateja. Hivyo, niiombe pia Serikali iangalie umuhimu wa kuhakikisha hii huduma ya prepaid inaenea nchi nzima na kila mwananchi anaelewa matumizi yake ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza watendaji wote wa Wizara hii kutokana na ugumu wa kazi yao, lakini pamoja na vile wanavyojitahidi kuendana na hizo changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuja na mpango mzuri sana wa huduma ya afya kwa wannachi na hii imekuwa ikiwasaidia sana wananchi wengi, hasa pale wanapopata matatizo mbalimbali ya afya. Hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia mrundikano wa watu wengi kwenye madirisha zinapotolewa huduma hizi kwenye hospitali zetu, hivyo kusababisha wagonjwa kuchukua muda mrefu sana mpaka kuja kuhudumiwa. Naiomba Serikali iangalie utatuzi wa changamoto hii kwa kuongeza waajiriwa, hasa katika madirisha haya yanayotoa huduma hizi za afya kwenye hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea kuhusu watoto; tumekuwa tukizungumza sana kuhusu tatizo la lishe kwa watoto wetu na tumeona changamoto zinazojitokeza, hasa maeneo ya vijijini. Kwa upande wangu sioni kama changamoto hapa ni ukosefu wa chakula, kwa mfano, kama tunavyoongelea huko vijijini ambako ndiyo kuna vyakula vingi vinapatikana na vingi ni natural kabisa, lakini bado watoto wengi wa maeneo hayo wanapata utapiamlo na udumavu. Hivyo hapa naona tatizo ni elimu kwa hii jamii na hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuwapa elimu hawa wananchi hasa wa vijijini ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wao wakapata lishe bora na kuondokana na haya matatizo ya udumavu na utapiamlo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile jamii ingefundishwa kuhusu sheria mbalimbali ambazo zinasaidia kumlinda na kumtetea mtoto anapokutana na changamoto mbalimbali huko katika jamii. Changamoto nyingi zimekuwa zikijitokeza, lakini unakuta mzazi hajui aanzie wapi, inasababisha mtoto anakosa haki yake na kuishia kuishi kwenye janga la umaskini ama kuishia kwenye matatizo ambayo baadaye yanakuwa ni changamoto kubwa sana kwake. Hivyo niiombe Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii kuwasaidia hawa watoto na kuwalinda ili tuweze kujenga kizazi bora cha kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine nililoliona ni katika tafiti na elimu mbalimbali. Kwenye jamii yetu sasa hivi kuna matatizo mbalimbali ya kiafya, mathalani, tunaona watu wengi hata kushika mimba limekuwa ni tatizo; pia kuna tatizo lingine la kutoka mimba kabla ya wakati; kuna tatizo la mimba kutunga nje ya kizazi; kuna vifo vya watoto wachanga; na kuna tatizo la nguvu za kiume. Haya matatizo yamekuwa ni mengi sana katika jamii na hivyo napenda kuishauri Serikali ifanye tafiti mbalimbali na kuja na majibu ambayo yataisaidia jamii yetu kuondokana na haya matatizo ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe pia Wizara iangalie hospitali zetu. Hospitali nyingi zinakuwa hazina vifaa vya kutosha, mathalani ni Kituo cha Afya cha Mombo. Kile kituo cha afya kipo katika njiapanda na kinahudumia watu wengi sana, lakini kituo kile hakina x ray, hakina ultra sound, hakina hata jenereta. Hivyo niwaombe watusaidie kwa sababu ni sehemu kubwa sana ya wananchi wanaohudumiwa na kituo kile, lakini kutokana na changamoto hizi wanashindwa kutekeleza kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kabla sijaanza kuchangia nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wetu wa Kamati kwa wasilisho zuri. Nijielekeze sasa moja kwa moja kwenye kuchangia kwenye Kamati ya Uwekezaji ambayo ndiyo Kamati niliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua dhamira kuuu ya Serikali kuwekeza katika mashirika ya umma ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi, kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali na kutengeneza ajira kwa wananchi. Pamoja na haya yote, tumekuwa tukushuhudia Serikali ikiwekeza fedha zake kwenye baadhi ya mashirika, lakini mashirika haya miaka yote yamekuwa yakizalisha hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sioni sababu ya kwa nini Serikali iendelee kuchoma pesa zake kwenye mashirika haya ambayo hayana tija. Kwa sababu Serikali imekuwa ikitoa mitaji yake kulingana na mahitaji ya mashirika yale, lakini unakuta mashirika mengine yanafanya vizuri sana na mashirikia mengine yanashindwa hata kutoa gawio kwa Serikali. Kwa hiyo badala kuendelea kuyaangalia haya mashirika ambayo yamekuwa yakizalisha hasara kila mwaka ningeishauri Serikali iangalie kwa upande wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano wa Mkoa wangu wa Tanga, Mkoa wa Tanga tumejaliwa kuwa na viwanda vingi sana, lakini vile viwanda sasa hivi vimegeuka kuwa magofu, mfano tulikuwa na Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Mbolea, Kiwanda cha Mkonge, Matunda na Chai. Hivi viwanda vyote sasa hivi havifanyi kazi. Iwapo serikali itaviangalia hivi viwanda na kuviwezesha nina imani vinaweza kuleta tija katika mapato na vilevile kuongeza ajira kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine nigusie mashirika yenyewe ambayo Serikali inaweka mitaji yake. Hizi taasisi unakuta zenyewe kwa zenyewe zinasababishana kurudurishana nyuma na kuweka ugumu katika utendaji. Hii ni kwa sababu utakuta taasisi moja inaihudumia taasisi nyingine kwa mkopo, lakini imekuwa ni ngumu sana zile taasisi kurejesha ile mikopo kwa wakati, hivyo kufanya ugumu katika utendaji wa hizi taasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie mfano mashirika ya hifadhi ya jamii, haya mashirika sehemu yake kubwa ya uendeshaji yanategemea michango ya wanachama ya kila mwezi. Unakuta michango ile ya wanachama inakatwa vizuri kwenye mishahara wa mwanachama, lakini haipelekwi kwa wakati ama haipelekwi kabisa sehemu husika. Hii hupelekea Mifuko yetu hii ya Hifadhi ya Jamii kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Hivyo, niiombe Serikali ingalie ni namna gani inaweza kusaidia haya mashirika ambayo yamekuwa yakitoa huduma na mwisho wa siku hayapati mrejesho wa fedha ili yaweze na yenyewe kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo ningezumzia suala la ubunifu; unakuta mashirika yetu haya yana fursa nyingi sana ambazo wanaweza kuzitumia na kupata kipato ambacho kingewasaidia kujiendesha wakati wanasubiri ruzuku za Serikali. Kwa kushindwa kutumia ubunifu wao wanakaa muda mrefu bila kutekeleza majukumu yao, kwa sababu ya kukosa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu hata kwenye kujitangaza, sisi wenyewe kama Wajumbe wa Kamati tulikuwa tunakwenda maeneo mengine tunashangaa. Tunakuta bidhaa ambazo ni nzuri sana lakini sisi wenyewe hatufahamu kama zile bidhaa zinategenezwa mahali pale ama zinapatikana pale. Kwa hiyo kwa kujitangaza haya mashirika itasaidia kukuza kipato chao na kuweza kutoa gawio kwa Serikali.

Pia niipongeze Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa jitihada zao walizofanya na wanazoendelea kufanya na kupelekea kupata gawio zuri kwa mwaka 2018/2019. Pia niiombe Serikali iangalie yale yaliyoainishwa kama changamoto na Msajili wa Hazina ikiwemo mfumo hafifu wa TEHAMA, Sheria ya Msajili wa Hazina, ongezeko la mahitaji ya watumishi wenye utaalam na kukosekana kwa mfumo wa fedha za uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo pia ningekazia kwamba hii Ofisi ya Msajili wa Hazina iongezewe bajeti, kutokana na ukubwa wa kazi yake ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na tupate kile tunachokihitaji. Kwa upande kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ningependa kushauri wafanye Audit Management za mara kwa mara kwa haya mashirika na taasisi ambazo Serikali inawekeza fedha zake. Kwa sababu tumeshuhudia hapa kuna mashirika yalikuwa yanasema kwamba hawawezi kutoa gawio, lakini baada ya kupewa siku 60 wameweza kupata, wengine wameanza kuleta gawio, kwa hiyo hii inaonesha kwamba wakati mwingine taarifa wanazotoa zinakuwa sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kuona umuhimu wa mazingira na afya kwa wananchi kwa kutoa tamko la kusitisha matumizi ya mifuko ya plasitikic kuanzia tarehe 1 Juni, 2019. Kama tujuwavyo, mazingira bora na usafi ni kiunganishi kikubwa cha kuondoa umasikini na kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii ni lazima ihamasishwe kuwa rafiki wa mazingira na waelimishwe kuwa uharibifu wa mazingira ndiyo unaopelekea kuharibika kwa miundombinu, upungufu wa maji, matatizo ya kiafya, upungufu wa mazao kutokana na uharibifu wa rutuba katika udongo. Vile vile kukosekana kwa mvua na ongezeko la joto vyote hivyo vinachangiwa na uharibifu wa mazingira hayo. Elimu ya kutosha kwa wananchi ni lazima iendelee kutolewa kwa kasi ili wajue umuhimu wa kutunza mazingira. Maana ukiangalia vijijini suala hili la elimu ya mazingira bado sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingine ya wazoa taka mitaani. Unapomwambia Mtanzania wa kawaida, yaani mwenye maisha duni atoe shilingi 5,000/= ili taka zake zibebwe kila wiki, hapa suala la utunzaji wa mazingira tunaweza kulifanya kuwa gumu. Serikali iangalie inafanya nini katika hili ili kila mtu aweze kumudu kutoa taka kila wiki (gharama za wazoaji taka).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la mitaro katika mitaa yetu; watu wamekuwa wakikamatwa kwa kumwaga maji nje ya nyumba zao na wakati mwingine kutozwa faini hadi shilingi 50,000/= ili mradi tu pakiwa pabichi hata kama ni maji safi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutunza mazingira na kuweka urahisi na amani kwa wananchi ili wawe rafiki na mazingira yao, Serikali iwatengezee mazingira mazuri ya kuyatunza. Kama hilo la kuwa na mitaro mitaani, tozo ya shilingi 5,000/= kwa wanaomwaga maji ovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusikiliza hotuba hii, pia nimeona upungufu kwa sehemu kubwa ya hotuba kugusa mazingira kuliko Muungano na hiyo kupelekea kuziacha changamoto nyingi za Muungano bila majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka elimu ya Muungano kwenye vyombo vya habari ili watu wengi wajifunze na kupata majibu ya maswali waliyonayo, ikibidi elimu hii ianzie Shule za Msingi, watoto wakue na uelewa wa Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto zinazokua addressed zipatiwe ufumbuzi ili tuudumishe Muungano wetu na kuondoa malalamiko yanayokuwa yanajirudia rudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa wasilisho zuri pia jitihada za dhati kabisa za kusimamia tasnia hizi za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nianze kwa kuchangia upande wa vipaji ambavyo vinahitaji kuendelezwa. Watoto wengi hasa mikoani (vijijini) wana vipaji lakini wanakosa mtu wa kuwashika mkono, mfano, ni Kituo cha Michezo cha Manga, Wilayani Handeni, Tanga ambao wamefikia kutoa mtoto mmoja anayeshiriki timu ya under 17, lakini hawana uangalizi ambao laiti ungekuwepo tungepata wachezaji bora kabisa wa mpira wa miguu. Pia vipaji mashuleni viufuatiliwe na kuendelezwa.

Mheshimiwa Spika, pia tunaona kumekua na wimbi la vijana wengi wakijiunga na ajira ya online TV. Hili limesaidia katika kupunguza tatizo la ajira. Ila vijana hawa wanakwamba kwenye ada za kujisajili, Serikali ingeangalia uwezekano wa kuwasaidia angalau waruhusiwe kufanya kazi zao ili mradi wanafuata taratibu na sheria za nchi na hizo ada za usajili zikatwe katika mapato yao ya kila mwezi au wapewe muda walipe taratibu hadi wakamilishe huku wakiendelea na shughuli zao na kujiingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mitandao kusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kila siku za jamii kujiingizia kipato, burudani na hata kupashana habari mbalimbali bado kuna wimbi la wanaotumia mitandao vibaya kama vile kutuma ujumbe mfupi unaolenga kutapeli, kufanya biashara za ngono, kutukana katika mitandao, vitu ambavyo nashauri Serikali iweke adhabu kali na zitangazwe hadharani ili wengine waogope wasione kama ni maneno tu bila vitendo.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali iboreshe viwanja vya mpira hasa mikoani. Viwanja vingi vipo katika hali mbaya na vinahitaji maboresho hasa uwanja wa Mkwawani, Tanga ambao ni uwanja wa siku nyingi na moja ya viwanja vikubwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, bado mikataba ya wasanii wetu haiko vizuri na wanachopata hakilingani na kazi wanazofanya. Serikali ingeangalia uwezekano wa kuwa na mkataba maalum unaotoa maelekezo ya ujumla kwa wasanii wote, mfano, kama msanii atatumika katika tangazo au kazi ya aina fulani malipo yake yaweje ili kuondoa ukandamizaji unaotokea kwa wasanii wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa wasilisho zuri, lakini pamoja na hilo, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinahitajika zaidi kuangaliwa na kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, nianze na vitambulisho vya uraia. Ni haki ya kila Mtanzania kupata kitambulisho hiki ambacho kimekua ni mojawapo ya sifa za kupata baadhi ya huduma za muhimu kabisa. Upatikanaji wake umekuwa ni changamoto sana. Ili kufanya zoezi hili kuwa rahisi, kwa nini vitambulisho hivi visiwe zoezi endelevu mfano mashuleni, vyuoni, sehemu za kazi hata Ofisi za Kata kiasi kwamba mtu anapotaka kupata kitambulisho hiki ni zoezi jepesi kuliko ilivyo sasa. Pia mianya ya rushwa iangaliwe sana ili kuondoa uzoroteshaji wa zoezi hili. Elimu itolewe kwa wananchi jinsi ambavyo anaweza kupata kitambulisho na umuhimu wake.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni wageni wanaokuja katika nchi yetu kufanya kazi za mikataba. Watu hawa mara nyingi wanajenga mahusiano na Watanzania wanawazalisha, mwisho wa siku wanaacha watoto bila malezi ya kueleweka na kuongeza watoto wa mitaani katika Taifa letu. Serikali iangalie inawasaidiaje hawa watoto wasio na hatia ili wapate malezi wanayostahili toka kwa wazazi wao.

Mheshimiwa Spika, pia wengine wamekuwa wakifunga miradi yao ghafla na kuacha wale waliowaajiri katika wakati mgumu na kukosa stahiki zao ikiwemo michango yao ya kila mwezi kwa Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Mara nyingi kesi za namna hii zimekuwa zikichukua muda mrefu sana na hivyo kuwafanya waishi maisha magumu sana. Serikali iangalie ni namna gani inawabana katika mikataba yao ikiwemo aidha kuwa na bima ambazo zita-take off linapotokea tatizo kama hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine ni suala la bima hasa za magari. Unapokwenda kukata bima, kunakuwa hakuna milolongo wala kucheleweshwa kwa namna yoyote ile. Ila unapopata ajali sasa ndiyo balaa juu ya balaa. Inachukua muda mrefu sana na wakati mwingine hadi watu wanaghairi kufuatilia, jinsi usumbufu unavyokuwa mkubwa. Mimi tayari nimepata ajali, sina usafiri na inachukua mwaka hadi miaka miwili mtu unafuatilia tu malipo. Sasa hamwoni kama badala ya kumsaidia huyu mtu mwenye matatizo, tayari ndiyo kwanza unamwongezea gharama ambazo hata baada ya malipo anakua amepata hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, suala la ulinzi shirikishi ni muhimu sana kwa jamii zetu. Serikali isisitize zaidi juu ya suala hili ikiwezekana kuwe na utaratibu rasmi wa kuhakikisha ulinzi shirikishi unafanyika ipasavyo. Tumeona kumekua na matukio ya wizi majumbani hasa vifaa vya magari na magari yenyewe pamoja na matukio ya ujambazi na mauaji ambayo yanaweza kupungua zaidi au kutoweka kama suala la ulinzi shirikishi litawekewa mkazo.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuiomba Serikali izidishe elimu hasa Zimamoto majumbani, maofisini na mashuleni ili kupunguza au kuondoa kabisa majanga haya ya moto, wakati huo huo pia mazingira ya kazi ya maofisa wetu wa ulinzi yaboreshwe maana hawa watu ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi yetu ili akili zao zitulie katika kazi ya ulinzi wa nchi yetu na wafanye kazi zao wakiwa na furaha.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza Wizara kwa wasilisho zuri na jithada zinazofanywa kuboresha elimu. Pamoja na pongezi hizi, nina mchango kidogo kwa baadhi ya maeneo. Elimu yetu ilenge kuibua na kukuza vipaji hasa mashuleni. Kuna watoto tangu shule ya msingi wanaonyesha vipaji vikubwa sana. Laiti watoto hawa wangetiliwa maanani wakaendelezwa kwa namna ya tofauti wangekuja kusaidia sana Taifa letu. Utakuta mtoto ana akili sana ana kipaji fulani lakini wazazi kwa kukosa uwezo mtoto yule anaishia njiani. Hivyo, tunajikuta tunapoteza rasilimali kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni mazingira mazuri ya kusomea. Kuna tatizo ambalo kwa sasa tunaweza tusilione ila baadaye likawa janga la Taifa. Watoto wamekuwa wakibeba mabegi yenye mzigo mzito sana kutokana na kutokuwa na ratiba maalum. Serikali ingeangalia uwezekano wa kujenga angalau makabati au kuhakikisha kunakuwa na ratiba maaum na zinafuatiliwa ili kuepusha matatizo ya uti wa mgongo yanayoweza kuwapata watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waalimu wawe motivated hasa katika mishahara, mathalan wanapofanya kazi kijijini, mshahara uwe juu zaidi ya aliye mjini ili kuondoa tatizo la walimu wengi kukwepa kwenda vijijini. Shule za boarding watoto wanahitaji sana uangalizi. Watoto wengi wanaanzisha mahusiano yasiyofaa. Hili lifanyiwe utafiti na awepo mtu wa kuwaangalia watoto hawa hasa kipindi cha usiku. La sivyo, watoto wataendelea kuharibika mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la taulo za kike hasa vijijini ni muhimu kwani watoto hawapati nafasi ya kusoma vizuri. Mfano shule unakuta haina vyoo vya kutosha, haina maji kiasi kwamba mtoto katikati ya masomo anaweza kwenda kujisitiri kwa wale wanaotumia njia nyingine zaidi ya pad, hivyo kuamua kukaa nyumbani mpaka pale atakapomaliza siku zake. Hivyo, kukosa masomo kwa kipindi chote hicho na wengine wanaenda hadi siku saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi kwa kukosa uwezo wa kifedha kwa wazazi au walezi wao wamejikuta hawana uwezo wa kufika kidato cha nne na kuendelea kwa kujibana na kuhangaika sana. Unakuta wanapata nafasi ya kujifunza ufundi stadi, udereva na ni katika vyuo vyetu vinavyotambulika kama VETA, NIT lakini linapokuja suala la ajira rasmi wanakosa sifa. Serikali iwaangalie sana hawa vijana na wengi wao wana vipaji vikubwa na ufanisi mkubwa. Iangaliwe ni jinsi gani wanaweza kuajiriwa au kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure bado ina changamoto nyingi sana. Kuna wazazi, walezi wengine hawana hata uwezo wa kununua sare za shule, madaftari, vitabu na nauli ili watoto hawa waweze kufikia hiyo elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa nia ya kifufua reli yetu ya Tanga Moshi ambayo ni mwokozi mkubwa sana kwa wananchi wa kanda nzima ya Kaskazini, kwani kwenye suala la usafirishaji mizigo na imeepusha barabara yetu kuharibika mara kwa mara kutokana na mizigo mingi kupita kwa njia ya barabara. Tunaomba mradi huu uwekewe mkazo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, naiomba Wizara ione umuhimu wa kupanua barabara ya Dodoma inayoenda Dar es Salaam, maana kwa sasa hasa wakazi wa njia hiyo wameshaanza kukumbana na tatizo la foleni hasa kipindi cha jioni na asubuhi.

Mheshimiwa Spika, pia bado matumizi mabaya ya mitandao yanaendelea. Watu wamekuwa wakitapeliwa na hata kutuma vitu visivyofaa kwa jamii yetu na hivyo kupelekea mmomonyoko wa maadili kwa vitendo vya ukatili. Naiomba Wizara itoe adhabu kali na ziwe hadharani ili watu waogope kutenda mambo yasiyofaa. Anayeadhibiwa itangazwe na wengine wasikie waogope na wao.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri tunaomba ukarabati ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani kwa kiwango cha lami. Barabara hii imekuwa ni kero ya muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, pia barabara ya Bagamoyo – Msata, matuta yamezidi, yapunguzwe kama zilivyo barabara za highway nyingine.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Tanga vitendea kazi vyake ni chakavu sana na ni bandari muhimu sana kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia kuliko mizigo kulundikana bandari ya Dar es Salaam, Bandari za Tanga na Mtwara ziimarishwe na mizigo igawanywe kikanda ili kuzijengea uwezo Bandari za Tanga na Mtwara na kupunguza mlundikano sehemu moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuwapongeza watendaji wote wa Wizara kwa jitihada kubwa wanazozifanya kuendeleza sekta hii ya viwanda na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niiombe sana Wizara iiangalie Tanga kwa jicho la huruma kabisa. Mkoa wetu unazalisha matunda kwa kiwango kikubwa sana tena mengine ambayo huwezi kuyapata mahali pengine popote tatizo hatuna kiwanda. Matunda yanaoza sana na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi, hivyo Serikali iwasaidie wananchi hawa kuondokana na tatizo hili na kukuza wigo wa biashara na uchumi kwa Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunaomba tupatiwe kiwanda kwa ajili ya nafaka kama mahindi, mihogo, ambayo inalimwa kwa kiasi kikubwa sana katika Mkoa wa Tanga. Kuna viwanda vinasuasua sana kama cha chuma, kamba hakiko vizuri kabisa kwa sasa. Pia tungeomba turejeshewe viwanda vya mbolea na plastic ambavyo vilihamishwa hivyo kudororesha kwa kiasi kikubwa uchumi wa Mkoa wa Tanga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya ulinzi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Wizara ni kwamba watengeneze products nzuri sana na kutoa services ambayo kama itafanyiwa marketing ya kutosha itaongeza kipato kwa Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na vijana wengi wanaomaliza shule na kubaki wakizagaa mtaani. Jeshi lingewachukua na kuwapatia ujuzi ili wanaporudi mitaani kwanza wawe wakakamavu, nidhamu na ujuzi wa kuweza kujiajiri. Lakini wakati huo huo Jeshi linakuwa na akiba ya kutosha yanapotokea matukio kama vita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine maslahi ya wanajeshi yazingatiwe sana ili kujenga uaminifu na kujiepusha na matukio yasiyofaa. Lakini pia wapewe motisha ya kuwafanya wafanye kazi kwa furaha maana kazi yao ya risk sana kwa maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanajeshi wangekuwa wanakatiwa bima ya maisha maana tayari wameyatoa maisha yao kwa ajili ya Taifa. Wakati wowote wapo katika risk ya kupoteza maisha na wengi wanategemewa na siyo kupoteza maisha tu, hata ulemavu wa kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kitendo cha kuwazuia wanajeshi wapya wasioe mpaka baada ya muda fulani sioni kama ni busara, na pia kunachochea maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na msongo wa mawazo kwa wanajeshi wetu, kitu ambacho ni hatari sana kwa watu wanaohusika na ulinzi wa nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kukuza kilimo nchini.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa changamoto ya ahadi wanazopewa wakulima lakini zinageuka kuwa vilio. Mfano ni Mkoa wa Tanga; mwaka 2018 walipewa ahadi wakalima mihogo kwa kiwango kikubwa sana mwisho wake ikageuka hasara kubwa kwao. Hamasa hii ilitoka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na mashirika yasiyokua ya kiserikali. Tatizo hili liliwapata pa wananchi wa Tunduma kwenye kilimo cha mbaazi. Niiombe Serikali iliangalie hili tatizo na kuona inazuiaje lisijirudie, na pia kuwasaidia wale wanaokumbwa na hasara hii kwa kuwafidia walau kwa kiwango fulani ili wasikate tama maana kilimo ndio uti wa mgongo kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia niiombe Serikali ione umuhimu wa kuwaelimisha na kuwapa hamasa hasa vijana ambao ndio wana nguvu kujiunga sana na kilimo kwa kuwasaidia pembejeo, elimu na maeneo ili kuwavutia wasizagae tu mitaani kwa kukosa ajira rasmi hatimaye kujiajiri katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, vilevile wakulima wa mbogamboga wengi wao wanalima katika mabonde ya maji machafu, labda ni kwa kukosa elimu ya afya au kukosa maeneo hivyo kupelekea matatizo ya kiafya kwa watumiaji wa mboga hizo ikiwemo kuumwa matumbo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wengi wanalima tu kimazoea bila kuwa na elimu ya kilimo bora. Serikali ione umuhimu wakuwaelimisha wakulima kwa ngazi za vijiji maana si wote wana uwezo wa kusikiliza kupitia redio au televisheni.

Mheshimiwa Spika, lakini kabla ya kumalizia niiombe Serikali iwasaidie sana wakulima pembejeo za kilimo kwa wakati. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia upande wa uvuvi. Wavuvi wa Mkoa wa Tanga wana malalamiko makubwa sana juu ya nyavu zao ambazo tamko lililotoka warudishiwe lakini mpaka leo hawajarudishiwa ukizingatia wanategemea shughuli za uvuvi kusomesha watoto na kuendesha shughuli zao za familia kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, tozo na faini zimekuwa nyingi, lakini kwa nini Serikali isijikite kutoa zaidi elimu kwa watu hawa ili kupunguza matatizo yanayosababisha tozo hizo?

Mheshimiwa Spika, tunaomba tupatiwe kiwanda cha kusindika samaki, Tanga samaki ni wengi ila masoko na sehemu ya kutunzia ni tatizo. Hivyo, tusaidiwe kiwanda Mkoa wa Tanga kitakachosaidia hata kwa upande wa ajira. Pia mitaji hasa kwa vijana ambao wanajua uvuvi lakini wanazagaa tu kwa kukosa vitendeakazi. Vile vile iwasaidie hata kuboresha mazingira yao ya kuvulia, ikibidi hata wakopeshwe.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mifugo tuna migogoro mingi sana kati ya wafugaji na wakulima, hasa Wilaya ya Handeni Kata za Misima, Sindeni, Kwamatuku, Mkata na Ndolwa. Tatizo la ni malisho ya mifugo, kesi ni nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote niiombe Wizara ione umuhimu wa kutoa zaidi elimu kwa wafugaji na hata wavuvi ili kuboresha shughuli zao. Mfano mdogo ni Tanzania kuwa termed chini ya kiwango cha kutumia maziwa kilichowekwa na FAO huku tukiwa na mifugo ya kutosha. Hapa tatizo ni elimu, wapewe elimu na mazingira bora ili wapate matokeo yaliyo bora zaidi. Pia wahamasishwe kujiunga katika vikundi ambavyo vitawasaidia sana katika kupata matokeo yaliyo bora na kulinda pamoja na kutunza mazingira ya kazi zao wakati huohuo kufuata sheria na taratibu za nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri na jitihada kubwa tunazoziona katika kuiendeleza hii tasnia. Pamoja na pongezi hizi niombe Wizara izingatie sana changamoto zinazowakabili hasa wachimbaji wadogo. Mojawapo ikiwa ni ufahamu mdogo wa Sera ya Madini inayopelekea kushindwa kukuza shughuli zao na wengi kuishia kupata hasara.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la mitaji; wachimbaji hawa wadogo hasa wanawake wapewe mitaji hata mikopo toka katika mabenki kwa kutumia leseni zao na hata madini ambayo wanayo.

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingine ya masoko ya uhakika kwa madini yanyopatikana wengi hawajui exactly masoko watapata wapi na hata bei zinazoendana na ile wanachokipata hivyo kupelekea kuuza bidhaa zao chini ya bei. Wachimbaji hawa wangepewa elimu juu ya madini mbalimbali na hata dalili za kuwa sehemu fulani kuna madini ya aina fulani ili kupunguza tatizo la kuhama hama linalochangia kuleta hasara.

Mheshimiwa Spika, pia manyanyaso dhidi ya wachimbaji hasa wadogo wadogo yadhibitiwe ili kuwajengea mazingira mazuri ya kazi zao.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kwa jitihada kubwa wanazofanya pamoja na kwamba bado kuna baadhi ya changamoto zinazotakiwa kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya vijiji katika Mkoa wa Tanga bado havijafikiwa na mradi wa REA. Pamoja na kwamba jitihada za Wizara tunaziona lakini tunaomba kasi zaidi ili vijiji vilivyobaki vipate umeme.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bomba la Gesi la Hoima ulenge zaidi kuwanufaisha wananchi wazawa wa maeneo husika kwa kuwapa elimu ya kutosha juu ya opportunities zilizopo na ni jinsi gani wanaweza kuzifikia. Pia, ikibidi wasaidiwe mitaji au mikopo maana kwa kufanya hivi wananchi hawa ndio watakuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, niiombe Wizara itoe elimu ya kutosha juu ya matumizi ya gesi asilia majumbani na viwandani na kuongeza kasi ili ienee kwa watu wengi zaidi, maana manufaa yake ni mengi na ni makubwa kwa ustawi wa nchi yetu kiuchumi na hata katika utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niiombe Wizara iangalie maeneo ambayo miradi hii inatekelezwa; kwa mfano Kinyerezi. Jamii inayozunguka miradi hii ipate faida na kufikiriwa kwa mfumo wa give back to the society. Unakuta miundombinu; mfano ni eneo lililopo mradi wa Kinyerezi, barabara ya kuendea katika mradi huu ni mbovu sana na magari yenye mizigo mizito yanaenda katika mradi yakichangia, hivyo kuwapa hali ngumu sana wananchi wa eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, napenda kuipongeza Serikali kwa
kuleta muswada huu wa kuunganisha mifuko. Ninaona ni wakati muafaka kabisa kwa kuwa hiki kilikuwa ni kilio cha muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali, nilikuwa napenda kutoa angalizo, kwa vile tunakwenda kuunganisha mifuko na kunakuwa kuna monopolization, kwa hiyo hakuna ushindani kati ya mfuko mmoja na mfuko mwingine kama ilivyokuwa mwanzo, napenda kuishauri Serikali iwe makini sana katika huduma zinazokwenda kutolewa na mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo kulikuwa na mafao ambayo yanatolewa ambayo yalikuwa yanatumika kama kichocheo cha kuvutia wanachama kutoka mfuko mmoja kwenda mfuko mwingine. Vilevile mifuko ilikuwa inajitahidi kila mfuko utoe huduma bora zaidi ya mwingine ili kuweza kuvutia wanachama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kuweka hili suala la kuwa na mifuko miwili ambapo mwanachama hatakuwa na nafasi ya kuchagua aende mfuko gani, nilikuwa naishauri Serikali iwe makini sana kuhakikisha kwamba wanachama hawa hawapati usumbufu katika huduma wanazokwenda kuzipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuongelea kuhusu suala la fao la unemployment ambalo limekuwa introduced kwenye muswada. Hili fao kwa kweli nami naliunga mkono. Mimi ni mmoja wapo wa watu ambao walikuwa wanatoa huduma kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Kwa hiyo, wakati mwingine nilikuwa nakutana na wanachama ambao walitamani kuwepo na fao kama hili ili liweze kuwasaidia kulinda credit zao pindi watakapostaafu. Kwa kuwa kulikuwa hakuna hili fao, ilibidi kipindi kingine wa- withdraw hata bila kupenda pamoja na kwamba walikuwa bado wana credit chache ili waweze ku-qualify kuwa pensioners.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunakwenda kulitoa hili fao la unemployment, naishauri Serikali iangalie hili fao linakwenda kutolewaje na litawasaidiaje wale waathirika wa hii unemployment kwa kipindi kile ambacho watakuwa hawana kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo naishauri Serikali iangalie, kuna makundi kadhaa ambayo sidhani kama hii unemployment benefit ambayo ni sehemu tu ya mafao itaweza kuwasaidia. Mathalani wale wanaofanya kazi kwa mikataba mifupi na hawana tena room ya kwenda kupata kazi sehemu nyingine na vilevile kuna wengine ambao wanapata ugonjwa ambao kwa ripoti ya Daktari unaona kabisa huyu mtu hawezi kuja kuendelea na kazi au labda ile pesa angeweza kusaidiwa kupata, ingeweza kumsaidia katika matibabu au shida anayoipitia.

Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na kuondoa fao la withdrawal, lakini naomba waangalie makundi. Kuna kesi ambazo ukiliweka hili fao la unemployment na wakashindwa kupata ile pesa yao, bado tutakuwa hatujawatendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ningependa kuishauri Serikali, kwa kuwa sasa hivi tunakwenda kuwa na mifuko miwili, sioni tena sababu ya mfuko mmoja unakata asilimia 15 kwa asilimia tano na mfuko mwingine unaendelea kukata asilimia 10 kwa asilimia 10. Naiomba Serikali, kwa kuwa sasa hivi tunakwenda kuwa na mifuko miwili, mifuko yote iwe uniform; wote wawe wanakata asilimia 15 kwa mwajiri na asilimia tano inakatwa kutoka kwa mfanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa mafao, nilikuwa naishauri Serikali iyapite upya mafao ambayo wameyapendekeza. Ukiangalia vitu vikubwa ambavyo vinamuumiza mwanachama, ni elimu na afya na mimi napendekeza kama wenzangu waliotangulia kwamba tuangalie fao la elimu. Fao la elimu ni muhimu sana kwa wanachama na tutakwa tumewasaidia kutua mzigo na vilevile tutakuwa tunatengeneza kizazi ambacho baadaye
kitakuja kuwa wanachama wetu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali kwa sababu tayari wafanyakazi watakuwa ni wanachama wa NSSF, sioni sababu tena ya yule mwanachama kukatwa pesa kwa ajili ya matibabu ya NHIF. Kwa hiyo, ni vyema mwanachama ambaye atakuwa tayari yuko kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii akaunganisha moja kwa moja kupitia ile michango yake kikawa ndiyo kigezo cha yeye kumfanya atibiwe kupitia NHIF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho naomba kuishauri Serikali ni hili suala la kusema kwamba Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Umma utachanganywa na yale makampuni ya private. Kwangu mimi hili naona kama litakuja kuleta mkanganyiko, kwa sababu terms za public service ukiangalia na private ziko tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hawa wafanyakazi wa Private Sector watakwenda kwenye Public Sector baadaye itakuja kuleta shida hata kwenye suala la unemployment, kwa sababu terms zao hawa, anaacha kazi hapa leo, anahamia hapa. Kwa hiyo, itakuwa badala ya ku-concentrate kuendeleza hii mifuko, kila siku itakuwa ni ku-deal na hilo fao la unemployment.