Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Shamsia Aziz Mtamba (3 total)

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, pamoja na kupita bomba la gesi katika maeneo mengi ya Mtwara na Lindi, bado vijiji na mitaa mingi haina mtandao wa umeme. Je, ni lini REA III itamaliza tatizo hili kwa mikoa ya kusini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mkandarasi aliyepewa kusambaza mtandao wa umeme Mtwara yupo slow sana. Je, Serikali inachukua uamuzi gani kwa mkandarasi huyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza; ni lini REA III itamaliza tatizo la kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara. Nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kuwa Mkandarasi wa Mkoa wa Mtwara ni JV Radi Service Limited na ameshalipwa asilimia kumi na yupo Mkoani Mtwara akiendelea na kazi ya upimaji wa njia ya umeme, na kwa kuwa Wizara tumetoa maelekezo kwamba vifaa vyote vya mradi huu REA III vipatikane ndani ya nchi, wakandarasi wanachoendelea nacho sasa ni namna ya kutafuta vifaa vyote na kuagiza ndani ya nchi, na nimhakikishie kazi hii itafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia hatua gani zitachukuliwa dhidi ya mkandarasi huyu. Naomba nimwambie ratiba ya REA iko awamu mbili, awamu ya kwanza ni 2017 hii Julai mpaka 2019, kwa hiyo mkandarasi huyu yupo ndani ya muda. Na kwa kuwa amelipwa asilimia 10 na ameanza kazi, nimthibitishie tu zoezi la upelekaji umeme katika Mtwara kwa mkandarasi huyu JV Radi Service itakamilika kwa wakati.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipatia nafasi, ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Tatizo lililopo Lupembe linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara Mjini, viwanda vingi vimekufa ikiwemo Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Oram ambacho kilikuwa kinatoa ajira kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda hivyo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, kupitia Sera yetu ya Uendelezaji wa Viwanda endelevu, sisi wenyewe kama nchi tuliona kwamba, masuala yote yanayohusiana na uzalishaji yaondoke sasa kwenye mikono ya Serikali iende katika mikono ya sekta binafsi. Jambo ambalo tunafanya sisi ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira wezeshi kwa kuhakikisha kuwa ile miundombinu inayohitajika pamoja na uunganishaji wa taarifa na vikwazo vyote ambavyo vinawakabili hao wawekezaji viweze kutatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa korosho, kwanza tunashukuru kwamba kwa sasa hali ya korosho/bei ya korosho imekuwa ni nzuri, lakini sisi kama Taifa tusingependa tu kuuza korosho zikiwa ghafi. Kwa misingi hiyo, tunaendelea kufanya jitihada ya kuhakikisha kuwa viwanda mbalimbali vya korosho vinaimarishwa ili kuhakikisha kuwa tunapata tija katika zao hili.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa nini Serikali haitaki kuwapa gesi wawekezaji wa kiwanda cha mbolea ambao wako tayari kujenga Msangamkuu, Mkoani Mtwara vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, miongoni mwa manufaa ya gesi kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni pamoja na kupelekewa umeme lakini mpaka sasa baadhi ya maeneo hakuna umeme Mkoani Mtwara. Naomba kujua kwa nini Serikali haipeleki umeme maeneo mengi ya Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Shamsia, wifi yangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuna mwekezaji, ni kweli wapo wawekezaji kampuni ya WD capital ya Egypt pamoja na Oman Petra Chemical ya Oman na LMG ya Ujerumani ambayo iliingia makubalino na Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwekeza kiwanda cha mbolea katika Mji wa Msangamkuu ambayo itatumia malighafi ya gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme sio sahihi sana kwamba walikataliwa kupewa gesi, lakini kikwazo kilikuwa bei ya gesi ambao wawekezaji wetu walikuwa wanaitaka. Kwa mfano, sambamba na huyo pia kuna mradi wa Kampuni ya Ferrestal ambayo waliingia ubia na Kampuni yetu TPDC lakini wote hao walikuwa bei yao ya awali ambayo walikuwa wanaitaka ni iwe USD 2.26 ambako gharama za uzalishaji wa gesi hizi kwa mujibu wa EWURA ni USD 5.6. Kwa hiyo utaona gape yake lakini Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayovutia wawekezaji ili kupitia maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliridhia tuanze mchakato wa mazungumzo. Kupitia mchakato wa mazungumzo ambao ulihusisha TIC ambayo yalifanyika mwezi Machi mwaka huu 2019, tumefikia bei ambayo wenzetu wawekezaji hawa wamerejea ili kuitafakari na baada ya wiki mbili walisema watarejea tena na bei hiyo ni kama USD 3.36 ambayo tunaamini pengine hiyo inaweza sasa ikafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niwathibitishie wakazi wa maeneo ya Kilwa ambako Ferrestal na TPDC watajenga kiwanda hicho na wakazi wa maeneo ya Msangamkuu Mkoani Mtwara kwamba, fursa ya ujenzi wa viwanda vya mbolea ambao faida kubwa itatoa ajira na mapato bado ipo na Serikali hii ya Awamu ya Tano kupitia hata Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na hata Taasisi ya TIC na taasisi zingine tutahakikisha kwamba fursa hii itafanyika kwa ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ameulizia kwa nini Mkoa wa Mtwara kwa kuwa unatoa gesi haujapelekewa umeme kwa kiwango ambacho Mheshimiwa Mbunge ameulizia. Nataka niseme ni kweli Mkoa wetu wa Mtwara tunautegemea sana kwa gesi megawati 1,600, zinazozalishwa sasa asilimia 52 inatokana na gesi. Pia Mkoa wa Mtwara kwa REA awamu ya tatu inaendelea ina vijiji 167, lakini Manispaa ya Mtwara Mikindani baadhi ya maeneo hata mimi niliyatembelea Mkangaula, Mkanalebi na pale maeneo ya mjini na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo tulikuwa naye pamoja na amekuwa wakiliulizia mara kadhaa hapa ndani ya Bunge kwa kazi nzuri ya kufuatilia miradi hii nimhakikishie tu ujazilizi awamu ya pili unaendelea na utaugusa Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo mengine na hata Mkoa wa Lindi kwa sababu bado tunatarajia gesi kutoa mchango mkubwa katika kuzalisha umeme ahsante sana.