Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Shamsia Aziz Mtamba (9 total)

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:-
Katika Mkoa wa Mtwara kuna tatizo kubwa la kukatika kwa umeme mara kwa mara jambo ambalo linaathiri wananchi ikiwemo wafanyabiashara ambao wanategemea sana umeme na hivyo kusababisha wakati mwingine biashara hizo kuharibika na kuwasababishia hasara wananchi hao.
Je, ni lini Serikali itawahakikishia wananchi wa Mtwara kupata umeme wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Aziz Mtamba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wanapata umeme wa uhakika ili kuboresha maisha yao. Serikali kupitia TANESCO imeweka jitihada kubwa kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha katika Mikoa ya Mtwara na Lindi unapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kufanya ukarabati mkubwa wa mitambo yote tisa iliyopo Mtwara yenye uwezo wa kuzalisha megawati 18. Ukarabati huu ulianza mwishoni mwa mwezo Oktoba, 2017 na utakamilika mapema mwezi Desemba, 2017. Gharama ya matengenezo kwa mitambo yote ni shilingi 4,800,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ukarabati huo, Serikali imeagiza mitambo miwili mipya kutoka Kampuni ya Caterpillar yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati nne kwa gharama ya shilingi 8,300,000,000. Ufungaji wa mitambo hiyo unatarajiwa kuanza mwezi Januari, 2018 na kukamilika mwezi Aprili, 2018. Mitambo hiyo itaongeza uwezo wa mashine zilizopo kufikia megawati 21.75.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO imeanza utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 300 kwa kutumia gesi asilia Mkoani Mtwara. Kazi inayoendelea kwa sasa ni kukamilisha upembuzi yakinifu kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japani (JICA). Mradi huo unategemewa kuanza mwezi Aprili, 2018 na kukamilika mwezi Desemba, 2019. Mradi huu utakapokamilika utatoa suluhisho la kudumu la upatikanaji wa umeme wa kutosha katika Mikoa ya kusini ikiwa ni pamoja na Lindi na Mtwara.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:-

Gesi ambayo imegunduliwa katika Mkoa wa Mtwara itanufaisha wananchi wote nchini na Taifa kwa ujumla:-

Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kujenga Chuo kitakachotoa mafunzo ya gesi na mafuta katika Kanda ya Kusini ili vijana wa Lindi na Mtwara na maeneo mengine waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta hii?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Aziz Mtamba, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuvitumia vyuo vilivyopo nchini kuwajengea uwezo wa kitaaluma wananchi katika masuala ya utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia. Kwa mfano, kwa mwaka 2010 Kampuni ya Petrobras ilitumia Dola za Marekani 350,000 sawa na shilingi milioni 780 kufundisha na kukipatia Chuo cha VETA Mtwara vifaa vya mafunzo. Aidha, kupitia mpango huo wanafunzi 50 na wakufunzi wawili walifundishwa kwenye fani ya umeme na makanika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Statoil imekuwa ikifadhili mafunzo mbalimbali kwa ngazi za vyuo kwa mfano mwaka 2013 ilifadhili wananchi tisa kusoma shule ya biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, masuala ya fedha na uchumi wamafuta na gesi asilia. Aidha, Kampuni ya BG waliendesha mafunzo na VETA Mtwara kwenye fani za English Language, Food preparation, Plumbing, Welding, Carpentry, Motor Vehicle Maintenance, Electrical Installation and Maintenance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2013 ilitoa ufadhili kwa wanafunzi 50 kusoma Chuo cha VETA Mtwara. Aidha, Serikali kupitia TPDC imefungua klabu 32 za mafuta na gesi katika shule za sekondari za mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kutoa elimu inayohusu tasnia ya mafuta na gesi asilia pamoja namna inavyoweza kuwanufaisha kupitia fursa zinazotengenezwa na tasnia hii katika maeneo yao.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji ya Mto Ruvuma kwa Wananchi wa Mtwara ili kuondoa shida ya maji iliyodumu kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ambapo Serikali inatarajia kuanza utekelezaji wake katika mwaka wa fedha 2021/2022 kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika kuhakikisha wananchi wa Mtwara wanaendelea kupata huduma ya majisafi na salama, wakati ukisubiriwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kutoa maji Mto Ruvuma, Serikali imeendelea kutekeleza kazi mbalimbali za kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Mtwara Mjini ikiwemo uchimbaji wa visima vinne, ufungaji wa pampu tatu, ujenzi wa matanki matatu, ulazaji wa bomba kuu kilomita saba na bomba la usambazaji maji kilometa 27.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vijijini, Serikali kupitia RUWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji 81. Miradi hii itakapokamilika itahudumia vijiji 285 ambapo jumla ya vituo vya kuchotea maji 1,562 vitajengwa/ kuboreshwa na inakadiriwa kunufaisha wananchi zaidi ya 454,375, hivyo, kuboresha utoaji wa huduma ya maji na kufikia wastani wa asilimia 79.91 kutoka asilimia 64 za sasa.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Mtwara Mjini kwenda Msimbati ambako kuna mitambo ya visima vya gesi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mtwara Mjini kuanzia Mangamba – Madimba – Msimbati inayokwenda kwenye visima vya gesi vya Mnazi Bay yenye urefu wa kilometa 35.63 na barabara ya Madimba – Kilambo inayokwenda kwenye Kivuko cha Kilambo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji yenye urefu wa kilometa 16.87 ni barabara za mkoa zinazosimamiwa na Wizara yangu. Barabara hizi zinafanyiwa matengenezo kila mwaka na Wakala wa Barabara nchini Tanzania (TANROADS) na zinapitika wakati wote. Katika mwaka wa fedha ujao wa 2021/2022 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 231 kwa ajili ya matengenezo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hizi pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kuzijenga kwa kiwango cha lami. Ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hizi utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia wazee hasa wa vijijini bima ya afya ikiwemo ya CHF inayotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, huduma za tiba ni haki ya msingi ya wazee wote. Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa matibabu hususan kwa wazee wasiojiweza nchini kwa kuanzisha madirisha kwa ajili ya matibabu kwa wazee. Serikali imeendelea na zoezi la utambuzi wa wazee na kuwapatia vitambulisho vya matibabu. Hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya wazee 2,344,747 wametambuliwa sawa na asilimia 87 ya makadirio ya wazee wote nchini. Kati yao wanaume ni 1,092,310 na wanawake ni 1,252,437. Aidha, wazee wasio na uwezo 1,087,008 na wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na wazee 856,052 wamepatiwa kadi za matibabu za Afya ya Jamii yaani CHF.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na kukamilisha rasimu ya Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha wananchi wote wakiwemo wazee kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha kwa mfumo rasmi na ulio mzuri zaidi. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Serikali ilikuwa na mpango mzuri juu ya uwepo wa nishati ya gesi asilia nchini, lakini mpaka sasa kumekuwa na sintofahamu juu ya mwendelezo wa uwekezaji wa miradi hiyo ikiwemo gesi ya Mkoa wa Mtwara.

Je, nini kauli ya Serikali juu ya mwendelezo wa miradi hii nchini?
NAIBU WAZIRI NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) inaendelea na uwekezaji katika sekta ya rasilimali ya gesi nchini kuanzia shughuli za utafutaji, uchorongaji na uendelezaji wa shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa takribani mikataba 11 ya utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia inaendelea kufanyiwa kazi kati ya makampuni mbalimbali ya uwekezaji kwa ushirikiano na Serikali kupitia TPDC. Hadi sasa gesi iliyogunduliwa imefikia futi za ujazo trilioni 57.54. Sehemu ya gesi hii hutumika katika kuzalisha umeme kwa asilimia zaidi ya 50 ya umeme wote nchini, lakini pia viwandani, katika majumba na katika magari.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa gesi hiyo inaendelea kunufaisha Taifa, Serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa kuchakata gesi kuwa katika kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) unaotarajiwa kuanza ujenzi ifikapo mwaka 2023. Serikali kupitia tayari imelipa fidia ya shilingi bilioni 5.71. Gharama ya mradi ni dola za Marekani bilioni 30.5. Mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2028.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza vipimo vya maabara hasa vya malaria katika zahanati za Mtwara Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Septemba, 2022, kipimo cha Malaria (mRDT), kuna vitepe vya kutosheleza matumizi ya miezi mitano na kabla ya kufika tarehe 30 Desemba, 2022 Bohari Kuu ya Dawa inategemea kupokea shehena nyingine ya vitendanishi hivyo vya malaria. Aidha, hali ya upatikanaji wa vitendanishi vya vipimo vya malaria katika Kanda ya Mtwara kufikia Oktoba, 2022 ni vitepe 631,825 ukilinganisha na matumizi ya vitepe hivyo ambavyo ni 84,150 kwa mwezi katika Kanda ya Mtwara, hivyo kuna shehena ya kutosheleza miezi saba ijayo.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kuwakumbusha watumishi wanaohusika kuandaa taarifa na kuomba vitendanishi kwa ajili ya vipimo hivyo, kufanya maoteo kwa usahihi na kuomba kwa wakati maana vitendanishi hivyo vipo vya kutosha MSD Makao Makuu na kwenye Kanda husika.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Iyari hadi Mkunwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania imepanga kujenga kilometa 2.2 katika barabara ya Iyari – Mkunwa (kilometa 79) kwa kiwango cha lami na mkandarasi yupo anaendelea na ujenzi ambapo kazi zinatarajiwa kukamilika Juni, 2023. Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha hadi kuikamilisha yote, ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara inayotoka Mtwara Mjini mpaka Msimbati ni barabara ya Mangamba – Madimba hadi Msimbati yenye urefu wa kilometa 35.63 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii imekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.