Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shamsia Aziz Mtamba (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya nzuri na leo hii kuweza kusimama katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Mwenyekiti wangu wa Chama-Taifa, full bright, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya ujenzi wa Chama changu. Pia napenda kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Magdalena Sakaya kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya ujenzi wa Chama changu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niingie katika mada. Wakati Tanzania tunaelekea katika uchumi wa viwanda, ni lazima tuwe na umeme wa uhakika na hakuna mwekezaji atakayekubali kujenga kiwanda ili apate hasara kwa sababu umeme unapokosekana kwa saa nne tu ni hasara kubwa kwa mwekezaji. Kwa mfano, itabidi apunguze wafanyakazi lakini pia wafanyakazi wataliobaki wanahitaji mishahara. Pia uzalishaji utakuwa chini ya kiwango, kwa mfano, kiwanda kilichopo kule kwetu Mtwara, Kiwanda cha Saruji cha Dangote kama kilikuwa kinazalisha kwa siku tani 100, umeme unapokatika uzalishaji utapungua, kiwanda kitazalisha tani 60 badala ya tani 100. Hii ni hasara kubwa kwa Taifa na mwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije katika masuala ya ajira. Umeme unapokuwa wa mgao au unapokatika mwekezaji itabidi apunguze wafanyakazi. Akifanya hivyo atakuwa amepunguza ajira na familia nyingi zitaishi maisha ya dhiki kwa kuwa kipato cha familia kitakuwa kimepungua.

Mheshimiwa Spika, vijana wengi sasa wameamua kujiajiri kwenye viwanda vidogo vidogo kama viwanda vya kuchomelea (welding), viwanda vya kuwekea samaki, viwanda vya kutengeneza barafu, viwanda vya salon za kike na za kiume, vyote vitakuwa hazifanyikazi kwa kukosa umeme wa uhakika. Hii ni hasara kubwa kwa Taifa.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije upande wa kodi za Serikali. Uzalishaji wa viwandani ukipungua hata kodi za Serikali nazo zitapungua. Serikali itashindwa kutimiza majukumu yake ya kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi wake. Ushauri wangu kwa Serikali iwekeze nguvu kubwa katika uzalishaji wa gesi iliyoko kule Msimbati, gesi ya Mnazi Bay ili iweze kutimiza majukumu yake ya kusambaza umeme wa majumbani na viwandani.

Mheshimiwa Spika, niongelee masuala ya kibiashara. Akina mama wengi tumepata mwamko wa kufanya biashara lakini kikwazo kikubwa tunachokumbana nacho ni kodi kubwa tunazotozwa na Maafisa wa TRA, tunafanyiwa makadirio makubwa mno. Naiomba Serikali yetu Tukufu ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli itupunguzie kodi hizi kwa sisi wajasiriamali, kama maduka ya nguo, vifaa vya ujenzi, mahoteli, biashara ya magari ya abiria yaendayo mikoani na daladala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Wiwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya mzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili. Pia nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Fulbright Prof. Ibrahimu Haruna Lipumba kwa kuchaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF. Nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Muftaha Abdalla Nachuma kwa kuchaguliwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF. Vilevile nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa kwa kumchagua Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya kuwa Naibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kuelekea Tanzania ya viwanda. Katika kuelekea Tanzania ya viwanda hatua ya kwanza ni kuondoa urasimu pale wanapokuja wawekezaji kwa kuwapatia maeneo ya ujenzi haraka na mapema iwezekanavyo. Hata hivyo, Wizara ya Viwanda kumekuwa na urasimu na kodi kubwa hali inayopelekea baadhi ya wawekezaji kuhamia nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ni Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Olam ambacho kilikuwa katika Mkoa wa Mtwara. Kiwanda kile kilifanya kazi vizuri sana na kuliweza kutoa ajira kwa wanachi wa Mkoa ule vijana na akina mama waliweza kuendesha maisha yao kupitia kiwanda hicho lakini mpaka sasa napozungumza kiwanda hicho hakipo kimehamia nchini Msumbiji. Je, Serikali haioni kuwa inakosa mapato na ajira kwa Watanzania? Nataka commitment ya Serikali hali hii ya kuhamahama wawekezaji katika nchi yetu itaisha lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoimarisha viwanda nchini tunahitaji malighafi (materials) zinazozalishwa na wakulima wetu. Wakulima wakiwa na masoko ya uhakika wataweza kuongeza juhudi za uzalishaji wa mazao ambayo ndiyo malighafi viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO). Tanzania tunalo Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO) lakini hatulitumii ipasavyo kwa sababu SIDO wanabuni na kutengeza mashine na mitambo mbalimbali inayoweza kutumika katika kilimo, ujenzi, nishati, uchimbaji wa visima, lakini havitangazwi. Tumekuwa tukiona karakana nyingi za SIDO mitambo yake ni chakavu na haifanyi kazi kabisa matokeo yake wananchi na Serikali wanatumia fedha nyingi kununua mashine na mitambo mbalimbali kutoka China. Natoa wito kwa Serikali itumie teknolojia yetu mzuri ya SIDO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la wafanyabiashara wadogo wadogo. Ni ukweli kuwa akina mama wengi ndiyo wafanyabiashara ndogondogo na za kati, lakini nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuliona suala la vitambulisho kwa wajasiliamali wadogo wadogo. Pia niishauri Serikali akina mama lishe, wauza matunda, maandazi, samaki, wasamehewe au walipe kidogo kidogo kutokana na kipato chao kuwa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili, lakini pia nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Mtwara Vijijini kwa heshima kubwa ambayo wamenipa na leo hii nikaweza kurudi tena katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi inayotumika kuzalisha umeme Kinyerezi inatoka Mtwara katika Kijiji cha Msimbati, inapitia Madimba ndipo inaposafirishwa kuelekea Kinyerezi. Kwa mshangao mkubwa sana sehemu ambako inatoka gesi asilia, Msimbati, miundombinu ya barabara ni mibovu mno. Barabara ni mbovu haipitiki kabisa hasa kipindi hiki cha masika. Hivyo, niiombe Serikali katika Mpango huu wa Maendeleo irekebishe barabara hii muhimu ambayo inaleta uchumi wa Taifa, ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaoishi katika eneo ambalo inatoka gesi wana mazingira duni sana. Hivyo, niiombe Serikali iwaangalie wananchi hawa kwa kuwawekea mazingira ya kuwaboreshea afya bora, elimu pamoja na uchumi kiujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla Mwenyezi Mungu ametujalia tuna korosho nzuri na bora kabisa, lakini pia tuna gesi asilia, lakini pia tuna bandari kubwa ambayo ina kina krefu. Kwa masikitiko makubwa sana Bandari hii ya Mtwara haifanyi kazi ipasavyo ukilinganisha na Serikali ilivyotumia pesa nyingi kuwekeza katika Bandari hii ya Mtwara; haifanyi kazi, hii inanyima maendeleo kwa Taifa na maendeleo kwa watu wa Kusini kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe ni shahidi. Nikiwa natoka Mtwara naelekea Dar-es-Salaam natumia barabara, lakini napishana na malori njiani ambayo yamebeba simenti pamoja na korosho. Mizigo hii ingeweza kupitia katika bandari yetu ya Mtwara, lakini inatumia barabara. Hii inaleta uharibifu mkubwa wa barabara na inaipa Serikali jukumu kubwa la kuikarabati barabara hii mara kwa mara. Sasa niishauri Serikali katika Mpango huu ione umuhimu mkubwa sana wa kuitumia Bandari ya Mtwara ambayo italeta maendeleo kwa watu wa Kusini, lakini pia kwa Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma tulikuwa tunaziona meli nyingi zikifika katika bandari yetu ya Mtwara na vijana wengi wa Mtwara waliweza kupata ajira…

(Hapa kengele ililia)

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuni… eeh, si nimesikia kengele?

MWENYEKITI: Ni kengele ya kwanza Mheshimiwa, bado ya pili.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali na niishauri kwa ajili ya Taifa kwa ujumla, ione umuhimu wa kuwekeza katika Bandari hii ya Mtwara ili iweze kufanya kazi ipasavyo. Bandari hii ingeweza kupata mizigo mingi kutoka Songea, Makambako, lakini pia na sehemu nyinginezo, wangeweza kuitumia bandari hii, leo hii hali ya maisha ya watu wa Mtwara yamekuwa magumu kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi walikuwa wanajipatia ajira katika bandari hii, lakini cha kushangaza bandari hii imetupwa kabisa, imesahaulika kabisa wakati bandari hii ina kina kirefu cha kupokea meli zaidi hata ya 15 au 20. Kwa hiyo, niiombe Serikali ione umuhimu wa kuitumia bandari hii. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kujenga hospitali ya kisasa ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma, lakini napenda kuishauri Serikali kwamba hospitali ile ina upungufu mkubwa wa madaktari pamoja na wauguzi. Hivyo basi Serikali iangalie hospitali ile kwa ukaribu mkubwa kwani inahudumia wananchi wa maeneo mengi sana kama vile UDOM ambapo wanafunzi takribani wote wanatibiwa pale, Wabunge na wananchi wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ongezeko kubwa la udhalilishaji wa wanawake na watoto. Naishauri Serikali iweze kutoa mafunzo pale akina mama wanapokuja kliniki ni namna gani inapotokea kubakwa kwa mtoto wake. Katika hatua ya awali kitu gani afanye ili ushahidi wa awali uweze kupatikana. Mara nyingi ushahidi huu hukosekana kwa vile huwasafisha kwa kuwakosha wakiona wanaweka vizuri kumbe wanapoteza ushahidi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nimeweza kusimama katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wa Jimbo langu la Mtwara Vijijini ni maji. Ifike wakati Serikali itoe fedha kwa ajili ya kusambaza maji kutoka Mto Ruvuma hadi kwa wananchi wangu. Sijui kwa nini suala hili limekuwa gumu wakati Serikali ilitenga fedha na wananchi walifanyiwa uthamini mwaka 2015 ili mradi huu uanze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Mtwara Vijijini lina kata 21, lakini ndani ya kata hizi 21, zote zimekuwa na changamoto kubwa sana ya maji ikiwemo Kata ya Mango pacha nne. Kata hii tokea tumepata uhuru haijawai kabisa kufurahia huduma hii ya majisafi na salama. Nikija Kata ya Libwidi, nayo imekuwa na changamoto kubwa sana ya maji; halikadhalika na Kata za Naguruwe, Kata ya Mkutimango, Kata ya Mbalawa na Makome, Kata ya Naumbu na Pemba Pwani nazo zimekuwa na changamoto kubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Mtwara kiujumla tuna changamoto kubwa sana ya maji, ndiyo maana tunataka mradi huu wa Mto Ruvuma ufanye kazi. Mradi huu wa Mto Ruvuma utaleta manufaa kwa maeneo mengi. Sitafaidika mimi katika jimbo langu tu, wanaweza kunufaika kwa kaka yangu Mheshimiwa Chikota; kwa kaka yangu Mheshimiwa Katani; utakwenda Nanyumbu; watakwenda Songea na Namtumbo. Kwa hiyo, mradi huu wa Mto Ruvuma una faida sana na utanufaisha maeneo mengi wataweza kupungukiwa na kero hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mtwara uchumi wetu mkubwa ni Korosho. Naomba katika Bajeti hii, zao hili la Korosho lisiyumbishwe yumbishwe, mwachie bodi ifanye kazi yake. Naiomba Serikali irudishe Mfuko wa Pembejeo. Mfuko huu ulikuwa ni mkombozi kwa mkulima wa Korosho. Kwa hiyo, wananchi na wakulima wa Korosho wa Mtwara wamenituma, ni lini Mfuko huu wa pembejeo utarudishwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi nikisimama ndani ya Bunge nimekuwa nikizungumzia sana masuala ya matibabu kwa wananchi hasa kwa wananchi wangu wa Mtwara Vijijini. Kusema kweli wamekuwa wakipata taabu sana wanapokwenda katika hospitali zetu hasa wale wenye magonjwa makubwa kama moyo pamoja na figo. Wapokwenda katika hospitali zetu wanakuta Madaktari Bingwa hakuna, wanaambiwa waende Muhimbili. Kutokana na uchumi wa watu wetu wanashindwa kwenda Muhimbili. Hivyo, naishauri Serikali iweke utaratibu angalau kwa miezi miwili au mmoja wawe wanatuletea Madaktari Bingwa katika mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi iboreshwe hasa katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini. Sekta hii napenda iboreshwe katika maeneo yafuatayo: wavuvi wapewe elimu ya kisasa, wapatiwe mikopo na vyombo vya kisasa vya uvuvi kama mashine za boti, nyavu, ndoana, pamoja na vifaa vingine. Pia wavuvi wapewe semina mbalimbali za kuwajengea uwezo ili kuhifadhi hifadhi ya bahari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na doria mbalimbali katika bahari zetu. Jeshi la Polisi wamekuwa wakifanya doria mbalimbali, lakini wavuvi wamekuwa wakilalamika kupigwa pamoja na kuchomewa nyavu zao. Kwa hiyo, naomba wasitumie nguvu kubwa, watoe elimu ya kutosha kwa wavuvi. Wakikamilisha haya, Serikali na Halmashauri wataweza kupata mapato ya kutosha kutokana na uvuvi. Pia zitengwe bandari maalum kwa ajili ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuwarudisha kazini wale wote ambao waliachishwa kazi kwa sababu ya kuwa na elimu ya darasa la saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali iangalie kwa jicho la huruma hospitali ya Rufaa ya Mtwara. Katika hospitali hii kuna upungufu mkubwa wa Madaktari pamoja na Wauguzi. Hospitali hii inahudumia wagonjwa wengi sana kutoka maeneo mengi sana ya Mkoa wa Mtwara. Katika hospitali pia kuna upungufu mkubwa wa dawa.

Naomba hospitali hii iongezewe bajeti ili wananchi wa Mkoa huu wa Mtwara waweze kupata dawa na huduma za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za vijana/ akinamama. Kwa mujibu wa sheria, kila halmashauri ina majukumu ya kutenga asilimia 10 kwa ajili ya vijana asilimia tano na akina mama asilimia tano. Hata hivyo, kwa kuwa vyanzo vya mapato ya kodi za majengo (property tax) na ushuru wa mabango vimechukuliwa na TRA, Halmashauri haziwezi kutoa fedha za mikopo kwa akinamama na vijana. Hii inasababisha vijana na akinamama kuchukua mikopo BRAC, FINCA na kadhalika. Taasisi hizi zina riba kubwa na akinamama wanachukuliwa vyombo vyao vitanda, makochi, TV, radio na kadhalika pale wanaposhindwa kulipa riba hizo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na uzima. Naomba Askari wetu waongezewe mishahara katika bajeti hii kwani wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, usiku na mchana, jua lao mvua yao. Kwa hiyo, naishauri Serikali iwaangalie Askari wetu hawa waongezewe posho kwani hali ya maisha ni ngumu sana. Posho ya shilingi 300,000/= kwa mwezi ni ndogo sana, haitoshi. Ina maana Askari huyu pamoja na familia yake inabidi atumie shilingi 10,000/= kwa siku kuanzia asubuhi mpaka jioni. Je, itamtosha Askari huyu? Hali hii inasababisha Askari wetu wajihusishe na masuala ya rushwa ili wakidhi mahitaji yao.

Mheshimiwa Spika, nyumba wanazoishi Askari wa Magereza ni aibu, nyumba za Polisi Mtwara ni za tangu enzi za mkoloni na hazijaboreshwa. Jengo la Kituo cha Polisi cha Mtwara ni chakavu, kuta zina nyufa, hali inayosababisha kuwa na hatari kwa Askari wetu na wanaweza kuangukiwa na jengo hilo.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, tunaomba Jeshi la Polisi lisitumike vibaya kwenye masuala ya kisiasa. Jeshi hili lifanye kazi yao kwa weledi bila kuegemea upande wowote.