Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rukia Ahmed Kassim (14 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kuweza kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza na ukurasa wa 12; Serikali kuhamia Dodoma. Hili ni jambo jema sana Mheshimiwa Rais kuamua kama sasa kweli Serikali ihamie Dodoma, lakini nahisi bado Manispaa ya Dodoma haijajielewa kama Rais katoa amri hii kuwa Serikali ihamie Dodoma. Hivi ninavyosimama hapa hakuna stand ya magari, mabasi yanahangaikahangaika tu, wameondolewa hapo wamepelekwa Kilimo Kwanza, huko Kilimo Kwanza ni eneo la Jeshi ambalo wameliazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kama kweli Serikali imeamua kuhamia Dodoma wao bado hawajaliona hili na wakaanza kutayarisha kuwa hili ni eneo la ku-park na basi na eneo lingine waweke kwa ajili ya magari madogo madogo? Hiace zinarandaranda tu hapo barabarani, lakini hawana parking za kukaa wala za kuweza kuchukua abiria. Hili ni tatizo, kwa hiyo naiomba Serikali waieleze Manispaa na wajielewe kwamba Serikali sasa imehamia Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuna viukuta hivi vya road reserve, hivi vimekuja mpaka kufikia nadhani Kilimo Kwanza, hapa katika mji havipo, lakini kuna viwanja ambavyo bado ni vitupu na wenyewe watajenga, kwa hiyo kama hawakuviweka mapema watu wakijenga wataingia katika eneo la road reserve baadae itabidi kuvunjwe. Kwa hiyo, mimi nawashauri wajipange na wajielewe na waweze kuweka vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mitaro ya majitaka; bado haijarekebishwa vizuri. Tunayaona maji yanasambaasambaa hovyo tu. Tatizo hili limejitokeza Dar es Salaam, Dar es Salaam wakati mji ule ulikuwa na watu wachache mitaro ya majitaka ilikuwa inakidhi haja kwa idadi ya watu waliokuwepo kwa wakati ule, lakini hivi sasa kama hawakuwaza kuliweka mapema na wakajua kwamba huu utakuwa ni mji wakaanza kutayarisha mitaro hiyo ili ikidhi haja ya watu watakapokuwa wengi, italeta shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo hili la mji hapo ambapo kuna vichochoro vile, kuna barabara za mitaa, zile barabara ni nyembamba mno utafikiria ulimi wa paka, hawajarekebisha, watu wanavunja majumba ya zamani wanajenga, lakini bado hawajaweka ile mitaa iongezeke, yaani walau gari ziweze kipishana. Kwa hiyo, mimi naishauri Serikali, mtu yeyote ambaye atajenga sasa katika eneo la mji kwanza ianze sheria kuwa ajenge ghorofa na waache nafasi ambayo itasaidia magari yaweze kupishana katika ile mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege, uwanja uliopo hapa ni aibu, ule si uwanja, sijui hata ni kitu gani, useme ni uwanja wa volleyball au sijui useme kitu gani. Serikali imepanga kujenga uwanja Msalato, kwa hiyo, mimi naishauri Serikali waanze kujenga ule uwanja Msalato ili aibu hii iondoke. Wakianza kujenga uwanja kwa sababu sasa hivi mji umeanza kukua kuna Mabalozi wamehamia hapa, kuna maafisa chungu nzima wa Serikali wako hapa, sisi Wabunge tuko hapa, lakini uwanja uliopo ni mdogo, ndege kubwa haziwezi kutua, kwa hiyo hii ni aibu. Mimi naishauri Serikali waanze kujenga uwanja wa Msalato ili tatizo hili liondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa manispaa tunawaomba, sisi watu tunaokaa Area D, Area D sasa hivi imekuwa ni kisiwa. Ukitaka kwenda Area D mpaka uzunguke Mji wote wa Dodoma ndiyo uweze kufika. Kwa hiyo, mimi nawasauri angalau mle kandokando ya ule uwanja watutengenezee japo kijinjia kidogo magari yaweze kupita, wanaokwenda Area D isiwe kama ni watu wanaokwenda katika mji mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo najielekeza sasa katika vyama vya siasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria akimshauri Msajili wa Vyama vya Siasa vyama ambavyo vinakiuka maadili na Sheria ya Vyama vya Siasa vifutwe. Jambo hili si jema na ninaomba lisije likatokea katika nchi yetu, kwa sababu unapokifutia chama usajili ni kuwafanya wale walio na chama sasa,kwa sababu chama kile sio cha viongozi, chama ni cha wananchi wote; unapounda chama hata mkiwa ni wachache mmeunda kile chama lakini ni sawa na kujenga msikiti au kanisa, utalijenga baadae likikamilika muumini yeyote anayekwenda kusali pale tayari ana haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hivi vyama vya siasa sio vya viongozi, ni vyama vya wananchi, vitakapofutwa itabidi wale wanaofanya siasa sasa watakapokosa pa kufanyia watakwenda kufanya katika misikiti, kwenye nyumba za ibada, makanisa, hii itakuwa ni shida kubwa na italeta tatizo kubwa katika nchi. Mimi namshauri Msajili kama ni mlezi wa vyama chama kinapotokea matatizo awaite na awashauri na si kuwafutia usajili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimemsikia Mheshimiwa Mchengerwa akisema katika hotuba ya Kamati yake kumshauri Msajili wa Vyama vya Siasa aendelee kutatua matatizo kusaidia kusuluhisha tatizo lililopo katika Chama cha Wananchi (CUF). Mimi ni Mbunge kupitia CUF, nakiri kweli kuna matatizo katika Chama cha Wananchi (CUF) ambayo yamesababisha hata sisi wenyewe humu ndani hatuelewani, ni bora mtu wa chama kingine unamuona ni mwema zaidi kwako kuliko yule wa chama chako, hili ni tatizo. Na tunamuomba Msajili aendelee kutushauri na kutupatanisha kwa sababu mwisho wa yote haya ni matatizo kwetu. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi hayo maneno yake ya kisimani siyataki, nataka aongee maneno ya Kibunge. Msajili ana haki, Msajili ndiye mlezi wa vyama kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Sheria Na. 5 ya mwaka 1992, Sheria ya Vyama vya Siasa, inampa mamlaka Msajili kuvishauri na pia kushughulikia vyama vya siasa. Kwa hiyo yeye ikiwa anasema Msajili kashtakiwa, kashtakiwa na nani na kwa sheria gani? Mimi nadhani hayo maneno ya kisimani akayasemee Kilwa, si humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Atakapoweza kutatua tatizo hili litatusaidia lakini inaonekana kuna baadhi ya watu hawataki, lakini mimi naona tu hawajajijua kwa sababu kama wanajijua, Profesa ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na ndiye mwenye mamlaka ya kuweza kuteua na ku… (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nasema huyo ni comedy katika siasa. Na ninamuomba u-comedy wake akaufanyie kule Konde, si katika Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa ni Mwenyekiti kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Wananchi (CUF). Kama wao wanasema kwamba Profesa alijiuzulu anapojiuzulu Mwenyekiti au Katibu Mkuu au Makamu Mwenyekiti kwa mujibu wa Katiba ya CUF mpaka mamlaka iliyomchagua ikubali, iridhie kujiuzulu kwake, kikao hicho hakikufanyika na Profesa alirudia nafasi yake kama Mwenyekiti.

Mheshimiwa Mwneyekiti, kwa hiyo, namuomba kama ni Mbunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF) amheshimu na ajue kwamba ni Mwenyekiti wake, na akiendelea na huo utumbo kuna Kamati imeundwa ambayo ni ya maadili ambayo mimi ni mjumbe wake, tutamshughulikia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi jioni hii ya leo nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na Jeshi la Polisi. Wakati mwingine Jeshi la Polisi wanakwenda tofauti na dhana ambayo tumeizoea. Jeshi la Polisi tunasema kama ni wanaolinda usalama wa raia na mali zao, lakini inakuwa ni tofauti kabisa na mambo wanayoyafanya, kwa sababu kuna baadhi ya Vituo vya Polisi unapokwenda, kauli wanazozitumia mtu anapokwenda pale ana tatizo, siyo nzuri. Kwa hiyo, tunaomba wajirekebishe. Hili nalisema nikiwa na ushahidi kamili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kituo kimoja cha Polisi Zanzibar, Kituo cha Mazizini. Mheshimiwa Waziri ananisikia na namwomba hili jambo alifanyie kazi. Hili lilinitokea hata mimi mwenyewe binafsi nilikwenda pale. Ilikuwa ni kesi ndogo tu ya traffic, lakini nilipokwenda, huyo niliyemkuta, aliniuliza: “Mama wewe unahoji neno hili;” kwanza kauli aliyoitumia mimi kama mtu mzima siwezi kuitaja hapa. Kwa sababu mtu
mzima unapotukanwa, unapovuliwa nguo unatakiwa uchuchumae siyo unyanyuke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno aliyoyatumia kwa kweli ni kumkashifu mtu au kuwakashifu baadhi ya watu na pia ingeleta uchochezi ndani ya nchi. Kwa sababu mimi ni mtu mzima, sikutaka maneno yale niyarudie wala niyaseme hapa. Finally, aliniambia “wewe mama unataka nikuheshimu au nikuvunjie heshima?” nikamwambia nitafurahi sana kama ukinivunjia heshima, lakini bahati nzuri sana nafikiri baada ya kujiamini kumwambia vile aliogopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema sitaki niwataje wala sitaki niongeze la ziada hapo, ila hiki Kituo cha Polisi kimekaa kama ni kijiwe labda cha wacheza Keram au wavutaji wa bangi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akifutalie sana kituo hiki. Hata baadhi ya majina ya hao Polisi waliopo pale, ni ya ajabu ajabu na yanaashiria shari kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasema kama Jeshi la Polisi ni usalama wa raia na mali zao, lakini wakati inapotokea operation, kwa nini Jeshi la Polisi linatumia nguvu kubwa? Ni sawa na kumuua labda inzi kwa kutumia bunduki jambo ambalo siyo sahihi. Inapotokea operation watumie nguvu za kiasi ili wananchi wetu wajenge imani na Jeshi letu la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya vituo anakamatwa mtu pengine kwa shinikizo tu la mtu fulani, anawekwa lockup zaidi ya siku saba, wakati Sheria inaeleza wazi kwamba mtu anaweza kukaa lockup kwa muda wa masaa 48. Kwa hiyo, naiomba Serikali waliangalie hili ili haki itendeke katika vituo vyetu vya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo, nataka nijielekeze kwenye Jeshi la Zimamoto. Katika Wilaya zetu, hakuna Ofisi wala vituo vya Zimamoto, viko katika Mikoa. Unapotokea moto katika Wilaya zetu inakuwa ni shida na kwa kweli inakuwa ni janga kubwa sana. Hata hapo inapopatikana hiyo gari, pengine itafika katika eneo la tukio lakini hawana maji. Kwa hiyo, naishauri Serikali katika Wilaya zetu waweke vituo na Ofisi za Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo, nitajielekeza sasa kwenye vitambulisho vya NIDA. Bunge limepitisha pesa nyingi sana kupeleka katika zoezi hili, lakini utendaji kazi wa NIDA unasuasua. Inachukua muda mrefu kupatikana kwa vitambulisho. Kwa hiyo, naishauri Serikali iangalie sana jambo hili ili ituambie hasa, Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, baada ya muda gani watu watakuwa wamepata vitambulisho? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo, nataka nijielekeze katika Jeshi la Polisi vilevile. Askari wetu wanaishi katika mazingira magumu sana. Ni ushahidi, hata hapa Dodoma tunawaona wanaishi katika nyumba za mabati, nyumba zimeezekwa kwa mabati na pia hazikukandikwa, zina mabati, joto tupu. Jamani hawa ni binadamu kama sisi, wanastahili na wao wakae sehemu nzuri. Wanapopata utulivu wa mwili na akili ndiyo wataweza kufanya kazi vizuri. Leo wanaishi mle kama wanyama, ni kuwadhalilisha na kulidhalilisha jeshi letu. Kwa hiyo, naishauri Serikali tuanze na hapa Dodoma kwanza kuwarekebishia makazi yao Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Vituo tunawapa mizigo mikubwa. Hakuna mgao wa fedha kwa ajili ya umeme wala maji. Unapomalizika pengine umeme katika kituo, Mkuu wa kitengo kile cha mahabusu, kunakuwa pengine ndani kuna mahabusu chungu nzima, hawawezi kuwacha wale na giza, wanaweza wakadhuriana, kunaweza kukatokea neno lolote. Mkuu wa Kituo anajilazimisha kutoa hela yake mfukoni, mshahara wenyewe tunaujua haukidhi haja, ana watoto, ana familia; jamani wenzetu tuwaoneeni huruma na Serikali ihakikishe kila Kituo cha Polisi kinaweka fungu la fedha kwa ajili ya maji na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nakushukuru kwa kunipa heshima iliyo kubwa, nakuhaidi kwamba nitaienzi. Baada ya kusema hayo, naipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio chetu Waheshimiwa Wabunge Wanawake (PWPG) pamoja na akinababa ambao walituunga mkono kwa kuondoa VAT kwenye taulo za kike. Sasa watoto wetu watasoma vizuri na utoro shuleni utapungua. Tunaishukuru sana Serikali katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo, naanza na kuchangia kwa kusema kwenye pato la Taifa. Katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri amesema kama pato la Taifa limeongezeka kwa asilimia 7.2 kwa mwaka 2018 kutoka asilimia 7.1 mwaka 2017. Pia katika kitabu hicho hicho kasema kama mapato ya ndani yamekua, yamefikia asilimia 15.8 katika mwaka 2018/2019 kutoka asilimia 15.3 kutoka mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa pato la Taifa, pia ni kuongezeka kwa fedha kwa wananchi wetu na wao wakawa nazo mfukoni. Hali ya wananchi wetu ni ngumu sana, maisha yamekuwa magumu kupita maelezo. Sasa tukisema kama pato linaongezeka, lakini maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu, bado naona pato halijaongezeka na hali bado ni ngumu. Kwa hiyo, Serikali ifikirie namna gani ya kuwatoa watu wetu katika umaskini huu uliokithiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake, sijui kama ni kwa mwono wangu mdogo lakini kachangia zaidi, yaani kaelezea zaidi namna ya kuongeza mapato kwa kodi, lakini hakuna mahali nilipopaona ambapo kaonesha namna gani tutafanya biashara ili watu wetu waweze kupata ajira na kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali ya nchi, maisha ni magumu. Ushahidi wa haya, tuliangalieni Jiji la Dar es Salam lilivyo. Watu wengi wameanza kuhama, kuna baadhi ya matajiri wamefunga milango ya maduka, hawauzi; kodi na tozo zimekuwa ni nyingi. Zamani ilikuwa ukitaka mlango Kariakoo
mpaka umwondoe mtu kwa kumpa pesa, yaani kilemba zaidi ya shilingi milioni 10 au 20, anaondoka anakuachia wewe mlango ufanye biashara. Leo ukienda Kariakoo milango ni bure zaidi ya ile kodi utakayolipa, unachukua wala hakuna mtu wa kumwondoa. Hii yote ni kutokana na ugumu wa maisha na biashara haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani wafanyabiashara walikuwa wanakwenda Zanzibar kuchukua biashara kuleta Bara. Leo hakuna anayekwenda, kodi zimekuwa kubwa, gubu na kero la TRA imekuwa kubwa, wafanyabiashara wanashindwa, wamefunga mikono, wengine wanarudi vijijini, wengine wanahama.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya matajiri sasa hivi wanauza majumba yao, wanafunga biashara Tanzania wanakwenda nchi za Arabuni wanapewa resident permit na wanapewa na nyumba wanaishi huko. Sasa hali ikiendelea hivi, maisha yatazidi kuwa magumu kwa sababu hawa wananchi wadogo wa kipato cha chini wanashindwa kupata ajira. Kwa hiyo, naishauri Serikali tutafute namna gani ya kuwasaidia watu wetu waondokane na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mpango, kasema katika ukurasa wake wa 32, kuwa kuna mikakati ya Serikali ya kuongeza mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na urasimishaji wa majengo na kupima viwanja. Sasa napenda niitanabaishe Serikali, katika kupima viwanja huku ikiwa wataona tutaongeza mapato, tunawaumiza wananchi wetu wa hali ya chini. Kwa sababu kuna watu wameishi katika Vijiji miaka pengine 20 au 30 wamezaliwa hapo, wameishi wamejenga nyumba zao za tope, Serikali inakwenda kupima inawaondoa halafu bila ya kuwalipa.

Mheshimiwa Spika, haya nasema kwa ushahidi hapa Dodoma, Swaswa Ng’ambo kuna watu ambao wamekwenda kupimiwa pale wameambiwa wakahamie Mkalama. Matokeo yake hawalipwi na hivyo viwanja wanavyopewa Mkalama wanaambiwa walipe Sh.200,000.

Hivi jamani tujiulize Mama Lishe anapika chakula ile hela hata ya ugali wake na watoto wake hapati au anajitwika beseni la ndizi anapita akiuza, ikifika jioni hata hela ya kula hana. Serikali inamlazimisha atoe Sh.200,000/=, atazipatia wapi?

Mheshimiwa Spika, sasa napenda niiulize Serikali, wale wananchi tunaowahamisha sasa Ng’ambo tunawalazimisha wakanunue viwanja Mkalama, kama mtu kashindwa ina maana nyumba yake itavunjwa na yeye hatalipwa na atakosa pa kukaa? Tunawatia watu wetu umaskini. Serikali lazima iangalie, tusiwafanye watu kuichukia Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli kutokana na mambo tunayoyafanya sisi viongozi. Naishauri Serikali watu hawa walipwe na huko wanakopewa viwanja wapewe bure, siyo waambiwe wanunue. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, nataka kuzungumzia kuhusu BoT. BoT wanasajili Benki ambazo hazina sifa. Kuna Benki zimefunguliwa kwa mfano, FBNE. Benki hii ilifilisiwa tokea mwezi Agosti, 2017. Sasa najiuliza, hivi BoT mlivyoisajili hii Benki hamkujua kama haina viwango? Haikidhi haja? Benki hii imefilisiwa, kuna watu wamefanya kazi miaka 40, kachukua pesa zake za gratuity kaziweka katika benki ile, matokeo yake Benki imekuja kufilisiwa anaambiwa mtu huyu atalipwa; maana yake imewekwa ufilisi chini ya Benki ya Amana. Wamelipwa shilingi milioni 1.5, wameanza kulipwa Novemba, 2017. Wameambiwa kama watalipwa tena ni baada ya kuuzwa mali za ile Benki. Hapo mwanzo walipoisajili Benki hawakujua kama haina vigezo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, BoT waache kusajili Benki ambazo hazina viwango. Benki zilizoshindwa kufanya kazi zifungwe. Tusiwatie umaskini wananchi wetu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja hapa atuambie watu walioweka pesa zao FBNE, watu wale hawana makosa, ni maskini wa Mungu, sisi ndio tuliwahamasisha waweke fedha zao benki. Kwa hiyo, tuambiwe lini watalipwa pesa zao? Kama hatukuambiwa, tunashawishi watu, tunazuia shilingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mpango, hiyo mipango yake yote aipange, atuambie lini watu hawa watalipwa fedha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nataka nijielekeze kwenye Zimamoto. inavyoonekana Serikali imeshindwa kusimamia vifaa vya umeme nchini; havina viwango, ni vibovu. Kila siku yanatokea maafa ya moto, ukiuliza unaambiwa ni fault ya umeme. Inakuaje hata nchini viingizwe vifaa ambavyo havina sifa? Vibovu! Tunawatia watu hasara, tunawatia umaskini. Maafa ya moto yamekuwa makubwa. Juzi Kariakoo imeungua nyumba siku tatu imeshindikana kuzimwa. Kwanza hatuna vifaa. Serikali iagize vifaa vya Zimamoto, halafu tuongeze magari ya Zimamoto. Katika Wilaya zetu hakuna Ofisi za Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kwanza ihakikishe vifaa vya umeme vinavyoingia nchini viangaliwe, viwe vina viwango na pia tuhakikishe tunaagiza magari ya Zimamoto ambayo yatasaidia kuzima moto, tena tuagize na vifaa vya kisasa. Maafa ya moto yamezidi, kuna mashule yameungua, juzi Buguruni zimeungua nyumba zaidi ya nne, sijui tano; Kariakoo moto umeshindikana kuzimwa siku tatu; Zanzibar kila siku moto unatokea. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuhakikishie jambo hili analifanyia kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nataka nijielekeze sasa kwenye huduma za afya. Mheshimiwa Waziri Mpango wanawake tunakufa bila ya kiasi. Tunakufa kutokana na Vituo vya Afya kutokuwa na Wodi ya Mama na Mtoto, hatuna Wodi ya Wazazi. Naomba Serikali ihakikishe kila Wilaya kuwe na hospitali ambayo itakuwa na Wodi ya Wazazi, chumba cha upasuaji pamoja na chumba cha mama na mtoto.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami kuwezakupata nafasi hii ya kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu. Naanza katika kitabu hiki cha Waziri Mkuu, ukurasa wa 11 unaozungumzia mfumko wa bei. Taarifa za kitabu hiki zinasema kwamba mfumko wa bei umepungua kwa wastan wa asilimia nne kwa mwaka 2018 hadi asilimia tatu kwa mwaka 2019. Jambo ambalo naliona liko tofauti kabisa, hali ya maisha ya mtanzania wa kawaida bado ni ngumu sana na kadri tunavyokwenda mbele maisha yanazidi kuwa magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa kutoa na mifano, mwaka 2018 Juni, Mtanzania wa kawaida alikuwa ananunua sukari kilo moja kwa Sh.2,100/=, leo Mtanzania huyu huyu ananunua sukari kwa Sh.2,400/=. Mwaka huo huo 2018, Mtanzania alikuwa ananunua maharage kilo moja Sh.1,700/=, mwaka huu 2019 ananunua kwa Sh.2,400/=. Mtanzania huyo huyo alikuwa ananunua tambi kilo moja Sh.1,700/=, lakini hivi sasa ananunua tambi Sh.2,500/= kwa kilo moja. Mafuta ya kula Mtanzania alikuwa ananunua lita moja ya mafuta Sh.1,100/=, lakini Mtanzania huyo huyo mwaka huu 2019 ananunua mafuta ya kula Sh.2,000/= kwa lita moja. Tulikuwa tunanunua mafuta ya petrol, kwa bei lita moja Sh.1,600/=, lakini hivi sasa ni Sh.2,206/=. Hapa napata ukakasi, naomba nipatiwe ufafanuzi. Je, mfumuko wa bei umepungua au umezidi? Mheshimiwa Waziri naomba awafafanulie Watanzania wajue, je, maisha yamezidi kuwa magumu au yamekuwa mazuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo, nataka niende katika kitabu hikihiki cha Waziri Mkuu, ukurasa namba 44, unaozungumzia kupunguza kwa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Ni kweli msongamano wa magari umepungua, tokea kujengwe lile daraja la juu la Mfugale. Pia tunategemea hali itazidi kuwa nzuri likimalizika kujengwa daraja la juu lile la makutano ya Ubungo, pamoja na daraja la Salender Bridge.Pia naishauri Serikali, Halmashauri ya Jiji sasa, ili na wao wajitahidi katika hili, waweze kutengeneza barabara zile za ndani, za mitaa, zilizoko Kariakoo wazitie lami, barabara za Kariakoo zile za mitaani, barabara za Ilala, za Magomeni ili sasa magari yaweze kupita kiurahisi katika zile barabara za mitaa kuliko kusubiri kupitia katika barabara zile kubwa tu,hapo nahisi kidogo foleni itaweza kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, naomba kutoa ushauri kwa Serikali. Wenzetu wa Senegal nchi yao ni ndogo tu, wana beaches nzuri, kama hizi zetu zilizopo Tanzania, Tanzania tumebahatika kuwa na beaches nzuri, tuna ufukwe wa bahari ambao ni wa kupendeza, una upepo wa kuvutia, lakini jiji hawajajitayarisha kuutengeneza huu mji wetu wakati huu mji wetu ni kioo cha Tanzania. Wageni wengi wanakuja hapa, hata sisi wenyewe, mji wetu ukijengwa, ukiwa katika mazingira mazuri na sisi pia tutafurahia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, Halmashari ya Jiji ya Dar es Salaam watengeneze fukwe zile za Oysterbay, badala ya kuziacha katika mazingira yale. Sasa hivi watengeneze public gym, ambayo watu wetu wataweza kwenda kufanya mazoezi, wataweza kupata afya bora, tutajenga vijana walio na afya bora na tutatengeneza Taifa ambalo lina vijana walio na afya bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, watengeneze sehemu za kupumzikia, kama vile Zanzibar tulivyofanya Forodhani ili watoto wetu waweze kupata sehemu za kwenda kucheza, kupumzika, watu wazima waende pale kupumzika na kupunga upepo wa bahari na pia mji wetu utapendeza na utavutia hata kwa wageni watakaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitakwenda sasa kwenye barabara, kwanza naipongeza Serikali kwa kutekeleza Sera yake ya kuunganisha barabara za mikoa hizi kwa lami, wakiendelea na sera hii tutaweza kukuza uchumi, kitakuwa ni kichocheo cha kuleta maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawaomba watu wa barabara, yaani watu wa TANROADS, wajitahidi kutekeleza ile Sera na Sheria Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2019, waweze kuweka vigingi katika barabara, waweze kuangalia alama za barabarani, watoe taaluma kwa wananchi wetu, wasiharibu barabara. Kwa sababu watu wengi wanatoa alama za barabarani na hawajui adhabu yake ni nini. Wakiweza kutoa taaluma katika vyombo vya habari na watu wakajua kama unapotoa alama za barabarani kosa lake ni hili, watu wetu wataweza kuogopa na wataheshimu zile alama za barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri watu wa TANROADS waweke watu maalumu ambao wataangalia alama zote za barabarani zitakazotolewa pamoja na rangi ambazo zinaweza kuwa zimefutika. Alama za barabarani zinasadia sana kuepusha ajali za mara kwa mara. Nasema hili kwa mfano, unapotoka Dar es Salam jioni ukafika huku Dodoma alfajiri, ukifika maeneo ya Gairo unakumbana na ukungu. Ukungu ule unakuwa huoni mbele yako kama kunakuja gari au haiji, huoni hata zile alama tena na barabara huioni, lakini zile alama za barabarani nyeupe zilizochorwa katikati ya barabara ndiyo alama pekee ambazo zinamwelekeza dereva wapi apite na wapi aelekee, bila alama zile nadhani magari mengi yangelianguka. Kwa hiyo, nashauri watu wa TANROAD wajitahidi, kila ambapo alama zile zimefutika wazirudishe na kila ambapo kuna alama za barabarani nyingine zilizotolewa wazirudishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo, sasa nataka nijielekeze kwenye Jeshi la Zimamoto, mara kwa mara tunakumbana na maafa ya moto katika maeneo yetu, lakini Jeshi la Zimamoto halijajipanga kutoa taaluma kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, naomba wawe na kitengo maalumu cha kutoa mafunzo, aidha kwenye Luninga, kwenye vyombo vya habari na watoe hata vingine kwa vitendo katika maeneo yetu. Kwa sababu ajali za moto, kuna mioto ya aina nne, kuna moto unaosababishwa na makaratasi au mbao. Moto huu unakuwa unazima kwa kupitia maji, watu wetu wakishajua pindi inapotokea moto wa namna hii…..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rukia ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami kuweza kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Naanza na Mitaala ya Elimu. Mitaala yetu ya elimu bado ni tegemezi, haioneshi ni namna gani mwanafunzi anapomaliza shule anaweza kujitegemea mwenyewe kimaisha. Mwanafunzi pengine anamaliza anakuwa na degree ya engineering lakini akitoka pale hana uwezo wa kutengeneza hata baiskeli. Wanafunzi wanakuwa si wabunifu, elimu wanayopata inakuwa ni ya theory zaidi kuliko elimu ya vitendo. Kwa hiyo, nashauri Serikali ihakikishe kuwa, wanafunzi katika vyuo wanapata zaidi elimu ya vitendo kuliko theory ili wanapotoka pale wanafunzi wetu waweze kujitegemea wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea, ilikuwa ikifika time kuna vipindi wanafunzi wanatolewa darasani wanakwenda kufundishwa namna gani ya kulima. Wanafundishwa kutengeneza mbolea, kutengeneza pengine shamba linakuwa kutoka pengine mche wa mgomba mpaka kufikia mwingine pana urefu wa mita ngapi, wanatengeneza mashimo yanakuwa na ukubwa gani, wanaweka mbolea mpaka kima gani, mwanafunzi anapomaliza shule anakuwa ni mkulima mzuri sana na anaweza kujitegemea. Kwa hiyo nashauri tuige mambo ya namna hii ili wanafunzi wetu wanapotoka vyuo waweze kujitegemea wenyewe siyo tena wawe bado ni tegemezi kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka kuchangia kuhusu shule za private. Shule hizi za private tunazipenda sana na zinatusaidia sana lakini kwa kweli baadhi ya shule watoto wengi wanaharibika hasa watoto wadogo. Kunakuwa na ulawiti mkubwa katika shule hizi za private, hasa shule ambazo zinachukua watoto wadogo, watoto wanaharibiana wao wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri awaite hawa walio na shule za private, wamiliki wa shule za private, wawape elimu wajue kama wanafunzi wanaowachukua ni wadogo kwa hiyo watoto wanapokuja pale wengi wao wanakuwa na tabia tofauti katika majumba yao. Baadhi ya wazazi wanakuwa wale watoto wameshawashinda kule nyumbani, kwa hiyo mtu anaamua bora nimpeleke boarding. Anapokwenda kule anakutana na watoto wengine wana tabia nzuri, lakini kwa sababu wale wana tabia mbaya wanaanza kuwaharibu na wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawashauri walio na mashule haya ya private wahakikishe kila bweni, kuwe kuna mtu ambaye analala nao watoto anawaangalia. Watoto wanaharibiwa usiku wanapokwenda chooni, watoto wakubwa wanawasubiri, wanawaharibu wadogo. Tutakuja kuzalisha watoto sisi tunaona watoto wetu wanakwenda kujifunza, kumbe wanajifunza mambo mengine ya ajabu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Elimu awaite watu walio na shule za private wahakikishe watoto wanawawekea ulinzi wa hali ya juu watoto wasiharibiane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitakwenda kwenye mishahara ya Walimu. Mheshimiwa Waziri asishangae kutuona kila anayenyanyuka anazungumzia suala la mishahara ya Walimu. Kama kuna watu ambao wanaishi katika maisha ya umaskini basi ni Walimu, Mwalimu anafikia kustaafu hana pa kukaa. Mwalimu siku zote anakaa katika nyumba ya kupanga, ikikaribia Januari Mwalimu kichwa chake hakifanyi kazi anafikiria ni namna gani atapata hela ya kwenda kulipia kodi ya nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Walimu wetu tukiwaongezea mishahara na stahiki zao tukiwapa, kidogo akili zao zitaweza kutulia kwa sababu atakuwa hana wasiwasi wa mambo mengine, ataweza kusomesha vizuri na tutapata mafanikio mazuri. Walimu wengi ambao wanafanya kazi katika shule za private, wanalipwa vizuri na ndiyo maana tukaona wanafunzi wanaofaulu wengi wanatoka katika shule za binafsi. Kwa hiyo ingawa hawa walio na shule za private isije ikiwa ni ile tunayosema Mgema akisifiwa tembo atalitia maji, wakaja wakaona kama kweli wao wanawalipa vizuri wakawashusha, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali stahiki za Walimu ziongezwe, tuwaongezee mishahara ili anapokuwa darasani asifikirie watoto wake watakula nini, wala asifikirie mke wake atapata wapi nguo ya kuvaa au atapata wapi fedha ya kwenda kulipia nyumba ili akiwa pale atulie kabisa aweze kutoa elimu nzuri kwa watoto wetu na tupate ufaulu mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa nitajielekeza kuhusu ajira ya Walimu. Katika vyuo vyetu wanamaliza pengine wanafunzi kama elfu thelathini ambao wote wale wanakuwa tayari ni Walimu, lakini kwenye ajira wanaajiriwa pengine elfu kumi, wengine wanabakia mitaani, utamkuta mtu ameshasoma vizuri, ana uwezo wa kufundisha lakini anakwenda kufanya kazi ya majumbani, kwa sababu hana kazi ya kufanya. Kwa hiyo nashauri Serikali iongeze ajira kwa Walimu ili katika madarasa iwe hakuna vipindi ambavyo hakuna Mwalimu wa kusomesha pengine topic fulani, hapana. Kwa hiyo nashauri tuongeze ajira kwa Walimu, watoto waliomaliza vyuo ambao wamesomea elimu waajiriwe ili tupate Walimu wengi katika vyuo na watoto wetu waweze kufanikiwa vizuri katika elimu zao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umekwisha au bado. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako. Nilikuona karibu na eneo la Maganzo juzi, unaimarisha Muungano eeh! Mheshimiwa Rukia. Mmh! Nilikuona eneo la Maganzo.

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam!

MWENYEKITI: Maganzo, ulikwenda kufanya nini? Ni kwenu huko, Muungano ule! Haya tunaendelea Mheshimiwa.

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Maganzo nilienda kutembea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa juhudi zake za kupeleka Madaktari Bingwa katika mikoa ya pembezoni kwa huduma za kibingwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi walikuwa wakishinda kufuatilia huduma hizi Muhimbili jambo ambalo limeleta faraja kubwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ongezeko kubwa la maradhi ya kisukari mpaka kwa watoto wadogo jambo ambalo limeleta hofu sana kwa wananchi wetu. Hivyo naishauri Serikali ifanye utafiti tuweze kujua sababu au chanzo cha maradhi hayo. Inawezekana pengine kuna vitu ambavyo vinasababisha ongezeko la kasi lililojitokeza la maradhi haya ya kisukari.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Afya akisema katika hotuba yake kwamba kuna kitengo cha matibabu ya kupandikiza figo kwa wagonjwa walio na matatizo ya figo. Hivyo basi naipongeza Serikali pamoja na Waziri wa Afya kwa mafanikio haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua mgonjwa anapopata tatizo hili anapata wapi figo hizi kwa ajili ya kupandikiza? Anakuja na mtu wake ambaye atatoa figo au ananunua? Naomba Serikali watupatie majibu ili tuelewe kwa sababu hili jambo limetufanya tupate faraja kubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano pamoja na Naibu Mawaziri wake wawili, Mheshimiwa Makame Mnyaa Mbarawa na Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye na Mheshimiwa Elias Kwandikwa kwa juhudi zao za kuijenga nchi yetu katika sekta hii ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na bandari; bandari ndiyo chanzo kikubwa cha mapato katika nchi yetu lakini bado ujenzi wa Gati Namba 13 hadi 14 katika Bandari ya Dar es Salaam unazorota. Toka mwaka 2010 tumeanza na wimbo wa ujenzi wa Gati hii Namba 13 hadi 14 mpaka leo haujaanza, jambo hili linazorotesha uchumi wa nchi. Naishauri Serikali itenge pesa kwa ajili ya ujenzi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi za dhati kwa ununuzi wa ndege, tulikuwa hatuna ndege na ilikuwa ni aibu kubwa lakini leo nashukuru Serikali kwa ununuzi wa ndege. Naishauri Serikali kuwa na tahadhari ya kutosha katika kuhakikisha kuwa ATCL inajipanga kufanya kazi kwa faida. Kuna hujuma kubwa sana zinazofanywa na mawakala ambao wanatumiwa na mashirika binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lilikuwa likifanywa na wakaua shirika hili. Ninaomba Serikali ifungue ofisi za kuuzia tiketi na siyo kutegemea mawakala. Unapokwenda kukata tiketi unaambiwa ndege imejaa lakini ukienda kuangalia airport ndege ni tupu haijajaa, mawakala wanakuambia ukate tiketi ya ndege nyingine kumbe siyo kweli wanataka ukate tiketi mashirika mengine.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza Profesa Ndalichako kwa kufanya juhudi ya kuwafanya watoto wetu waweze kuwa na ufaulu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kusema kwamba watoto wetu wengi wanakwenda masafa marefu kufuata shule. Shule nyingi ziko mbali sana na makazi ya watoto, hivyo basi, naishauri Serikali iweke sehemu ambazo wazee watalipia ili watoto waweze kukaa pamoja na kuweza kubadilishana mawazo na kusoma kwa pamoja kwa wale ambao watakuwa na uwezo wa kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwa wale wanafunzi ambao wanaonekana wana uwezo mzuri wawekwe pamoja kuanzia shule za msingi. Ikiwa wataanza kuwekwa pamoja kukawa na madarasa maalum na baadae wawe na madarasa maalum sekondari basi tutapata wanafunzi wazuri wa sayansi na masomo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia tatizo sugu la maslahi ya walimu. Walimu wanaishi katika mazingira magumu sana nashauri waboreshewe maslahi yao. Bila ya mwalimu kupata utulivu basi hawezi kuwa na moyo wa kufundisha vizuri, anakuwa na mawazo mengi sana hajui atalala wapi, atakula nini na huku ana familia inamtegemea. Naiomba Serikali ijitahidi sana kuboresha maslahi haya ya walimu ili watoto wetu waweze kufundishwa kwa utulivu na waweze kupata ufaulu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu vyoo katika shule zetu. Watoto wa kike wanapata shida sana wanapokuwa kwenye hedhi wanashindwa kuhudhuria masomo. Hivyo basi, naishauri Serikali ihakikishe katika shule zetu kuna matundu ya vyoo pamoja na maji.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Spika, tumekuwa na matatizo mengi hasa baina ya wakulima na wafugaji. Tatizo hili limekuwa sugu sana hasa kwa wafugaji kuwa na mifugo ndani ya nchi hii imekuwa ni shida sana. Wafugaji wanahangaika sana na mifugo, kila wanapoelekea wanafukuzwa na wakati mwingine mifugo yao inakamatwa na kupigwa mnada, wanalipishwa fedha nyingi sana ambazo hata uwezo wa kuikomboa mifugo yao hawa wanabakia na umaskini mkubwa, wengine wanapata mshituko wa moyo wanakufa. Serikali ilione tatizo hili kuwa ni kubwa na ipo haja ya kuingilia kati ili tuweze kuishi kwa amani na hawa wenzetu ambao ni wafugaji wajisikie kuwa na wao wanathaminiwa ndani ya nchi yao.

Mheshimiwa Spika, pia najielekeza kwa wakulima wetu wanapata shida sana wanapolima wakati mwingine wanabanwa wamelima kwenye hifadhi ya akiba. Hivyo basi Serikali yetu iwatengee eneo wananchi wetu waweze kulima isiwe kila eneo ambalo ni zuri kwa kilimo linawekwa kuwa ni kwa ajili ya hifadhi tu. Tuwasaidie wakulima wetu na wao wahisi kuwa wanathaminiwa na kupewa nafasi ya kuweza kujiendeshea maisha yao. Serikali itenge maeneo maalum kwa ajili ya kilimo.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kusema kuwa Wizara hii ni moyo wa Wizara zote, bila ya Wizara hii Wizara zote haziwezi kufanya kazi. Tunapitisha fedha za maendeleo haziendi kwenye Wizara husika, hakuna Wizara hata moja ambayo fedha za maendeleo zinapelekwa kikamilifu. Kazi na miradi ya maendeleo inashindwa kufanywa, hili ni tatizo kubwa sana. Nashauri Serikali tunapopitisha fedha za maendeleo basi zipelekwe katika Wizara husika.

Mheshimiwa Spika, kushuka kwa thamani ya shilingi yetu kila siku. Shilingi yetu inashuka sana na maisha yanakuwa magumu sana. Biashara hazifanyiki, maduka yanafungwa na hali ya maisha inazidi kuwa ngumu sana. Hivyo basi, naishauri Serikali iangalie nini tatizo lililosababisha mpaka shilingi yetu ikashuka kiasi hiki ili tuweze kurekebisha hii hali isiendelee.

Mheshimiwa Spika, kwenye kitabu ukurasa wa 47 unazungumzia huduma za kibenki na pameandikwa kuwa Watanzania wanaotumia huduma za kibenki wameongezeka na kufikia asilimia 65 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 57 ya mwaka 2013. Hata hivyo kuongezeka huku kunasababisha baadhi ya wananchi wetu kufilisika, kuna watu wamewekwa chini ya ufilisi. Hili jambo limewatia watu wetu umaskini mkubwa. Serikali iangalie sana hizi benki za kigeni zinazokuja kuwekeza hapa nchini, zinatuletea usumbufu mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa kila siku linaongezeka, hili jambo ni kubwa sana, hivyo basi, naishauri Serikali tusiendelee kukopa ni vyema kwanza hili deni likapunguzwa ndiyo baadae tukaendelea kukopa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuipongeza Serikali kwa jinsi wanavyojitahidi kuhakikisha kila wilaya inapata huduma stahiki kama vile elimu na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu ni mtu ambaye inapaswa Serikali imuangalie kwa jicho la huruma sana. Mwalimu hana muda wa kufanya kazi nyingine ya kujitafutia riziki. Anafundisha darasani, wakati mwingine lina wanafunzi karibu 70 na anaporudi nyumbani hapumziki ana kazi ya kusahihisha madaftari mpaka anapomaliza keshachoka hawezi tena kufanya kazi nyingine. Hivyo basi, Mwalimu wa nchi yetu anabakia na umaskini mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora ni pamoja na kuheshimu kila mmoja anafanya kazi ambayo inamhusu. Nakusudia kuwa kama wewe sio kiongozi katika nafasi fulani basi huwezi kufanya kazi ile ambayo sifa yako kwa mujibu wa sheria na kanuni ya vyama vya siasa. Kuna Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992, Kifungu cha 8B(2) ni marufuku kujitambulisha kwa vyeo ambavyo sio vyako.

Mheshimiwa Spika, utawala bora ni pamoja na kuheshimina na kuhakikisha kila mmoja anafanya kazi ambayo inayomhusu. Nakusudia kuwa kama wewe sio kiongozi katika nafasi fulani, basi huwezi kufanya kazi ile ambayo siyo yako kwa mujibu wa sheria na kanuni ya vyama vya siasa. Kuna Sheria ya Vyama vya Siasa ni ya mwaka 1992 kifungu 8B(2) ni marufuku kujitambulisha kwa vyeo ambavyo siyo vyako.

Mheshimiwa Spika, tunaowaona baadhi ya watu wanasema vyama kwa nafasi ambazo siyo zao na Serikali haiwachukulii hatua stahiki. Hapa utawala bora ndiyo unakosekana. Tunaishauri Serikali, watu hawa wapo na wanajulikana wachukuliwe hatua za kisheria ili utawala bora upatikane.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na uzima nami nikaweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Madini. Pili, napenda kuwapongeza Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri wake, kwa utendaji wao mzuri wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ndicho chanzo kikubwa cha mapato katika nchi yetu. Tuna madini mengi sana katika nchi yetu lakini bado nchi yetu haijaongeza pato la Taifa kwa kiasi kikubwa kwa sababu Serikali haijajipanga kudhibiti madini haya. Bado tuna watu wasioitakia mema nchi yetu, wanayatorosha madini yetu na kuyapeleka nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali ijenge viwanda vya kuchakata madini ili watu wetu waweze kupata ajira. Tuna vijana wengi ambao hawana ajira, wamekaa vijiweni hawana shughuli ya kufanya. Hivyo, naishauri Serikali iwape mafunzo hawa wachimbaji wadogo wadogo ili na wenzao wakiona hawa vijana wamefanikiwa nao wataacha kukaa vijiweni watajishughulisha na huu uchimbaji na watajikwamua kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho namalizia kwa kusema kwamba mikataba ya madini iangaliwe upya imepitwa na wakati haileti maslahi kwa Watanzania.
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nikaweza kuchangia katika Muswada huu uliopo mbele yetu. Kabla ya hapo kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia nikiwa na uhai na uzima nikaweza kusimama katika Bunge hili Tukufu na nikaweza kuchangia kama hivi nitakavyoweza kusema katika Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kuiondoa ile ibara ya 2(2) katika Muswada huu ambao kidogo ungeleta sintofahamu kati yetu sisi Wazanzibari na wenzetu wa huku Mainland kwa kuona kuwa suala hili sio la Muungano.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nataka niende kwenye Muswada. Muswada huu NASAC unatokana na neno NASACO. Kwa mujibu wa uelewa na kumbukumbu za huko nyuma tunasikia maana yake mimi nilikuwa ni mdogo, NASACO ilikuwa inafanya kazi vizuri sana. Kwa hiyo, Serikali ilipoleta Muswada huu ikaita jina la NASAC ni kuwa tunategemea nayo itafanya vizuri kama vile ilivyofanya NASACO. NASACO ilifanya vizuri lakini baadaye labda Serikali ituambie kulitokea nini mpaka NASACO mwisho ilishindwa na ikafa kabisa.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, NASAC sasa tunaambiwa kama itakuwa yeye ni mdhibiti (regulator) na wakati huo huo atakuwa ni operator. Kwa hiyo, naishauri Serikali vitu hivi vitofautishwe kabisa; kuwe kuna mdhibiti ambaye atadhibiti na pia kuwe na operator ambaye atafanya kazi kama mawakala wengine wa kibiashara, aingie katika mashindano ya kibiashara pamoja na makampuni mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikiwa Serikali itafanya hivyo, itatofautisha mambo mawili haya, basi nadhani sheria hii itakwenda vizuri na NASAC kama ambavyo tunategemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bandari zetu kuna upotevu mkubwa wa fedha na pia kuna wizi mkubwa ambao unafanyika. Wizi huu unatokana na kweli lazima tusifiche ni TRA. Sasa pale palikuwa pana SUMATRA na TPA; nadhani SUMATRA haina kosa na wala haijafanya vibaya, TPA haina tatizo lolote, lakini wizi na upotevu mkubwa ni kwa wenzetu TRA ambao ndio wanaosababisha wizi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watuambie Serikali je, NASAC itaziba vipi mwanya huu wa upotevu wa pesa ambao unasababishwa na baadhi ya wafanyakazi wa TRA ambao sio waaminifu. Wakishatuambia hilo ndio tutajenga imani kubwa kama kweli NASAC itafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi na-declare interest kama ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu; wakati tulipokuwa tukiwasikiliza wadau, aliyekuwa Mkurugenzi wa SUMATRA alituambia kama yeye aliwahi kusafirisha kontena sita
akiambiwa ni majani ya chai na kumbe ni bangi. Kwa sababu sheria ilikuwa inawabana SUMATRA hawezi kujua kilichomo ndani ya lile kontena wala TPA hawajui, anayejua ni TRA peke yake. Kwa hiyo, TRA ndio ali-take advantage kusafirisha kitu kile huku akijua kuwa ni bangi lakini ikawa SUMATRA yeye hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watuambie je, NASAC itaziba vipi mwanya huu wa upotevu wa fedha hizi, kwa sababu sisi tunajua bandarini kuna wizi mkubwa na fedha nyingi sana za Serikali zinapotea bandarini. Ndio maana Serikali inaumia na hili na imetuletea chombo hiki kuja kudhibiti wizi huu. Sasa lakini watufafanulie je, watafanyaje wakati TRA pale ipo na wao ndio source ya matatizo yote tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TRA imesababisha wafanyabiashara wadogo wafe kabisa kibiashara, anapokuja tajiri na mali nyingi pale wanaficha, wanadanganya, hawasemi kilichomo katika yale makontena na badala yake wanawatoza ushuru mdogo tu na wafanyabiashara wakubwa wale wanapitisha mali huku ukiwa ni wizi Serikali inapoteza mapato. Mfanyabiashara mdogo pengine wame-share na mwenzie wameleta kontena moja tu la biashara, watawapiga bakora ya ushuru kiasi cha kuwaambia kuwa nyie nendeni mkafie kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawawezi tena kufanya kazi mara ya pili kwa sababu ya ushuru wanaotozwa pale. Sasa NASAC ituambie itawasaidiaje wafanyabiashara wadogo waweze kufanya kazi na wale wakubwa watoe ushuru ambao unastahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi sitaki niende mbele sana katika hili isipokuwa nai-support Serikali kwa kuleta Muswada huu na naipongeza iweze kudhibiti mapato ya Serikali kikamilifu.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia furasa nami nichangie katika hoja hii tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la kuutangaza Mji wa Dodoma kuwa ni Makao Makuu ya nchi ni jambo jema sana na kwa kweli naipongeza Serikali kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mambo ni lazima Serikali sasa ijipange kuyatekeleza ili ile hadhi na azma ya Dodoma kuwa Jiji na Makao Makuu ya nchi ipatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba master plan ya Mji huu wa Dodoma ilitengenezwa zamani sana tokea uhai wa Mwalimu Nyerere. Baadhi ya nchi walizoiga master plan yetu kwa mfano kama wenzangu walivyosema Abuja na Accra Ghana miji yao imekuwa ni mizuri kupita mfano, lakini sisi tuliotengeneza master plan hii bado hatujaanza kuitekeleza. Kwa hiyo, naiomba Serikali, sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza azma hii. Katika kuitekeleza kwetu, basi tusiwaumize wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Wagogo wa Dodoma pamoja na makabila mengine ambayo yako Dodoma ambao ni wazawa, kuna baadhi yao wameumia sana. Kuna baadhi ya wazawa wa Dodoma, Manispaa pamoja na Watendaji wa Kata wamechukua maeneo yao bila ya kuwafikiria watu hawa watakaa wapi? Nasema jambo hili kwa uchungu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mama mmoja ambaye ana asili ya Kinyamwezi. Mama huyu kafyatuka anapita akilia peke yake njiani. Huyu mama anaitwa mama Kashinde. Alikuwa na nyumba yake pale karibu na Meriwa Secondary School. Nyumba yake ilipigwa grader ikapita barabara. Matokeo yake hata kiwanja hakupewa na eneo lile ni kubwa na ni eneo ambalo alirithi kutoka kwa wazee wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mama huyu ana watoto yatima, hajui aende nao wapi? Kapewa kiwanja mtumba. Hivi kweli mtu mwenye miaka 75 anaweza tena kujenga nyumba akaweza kwenda kukaa mtumba? Huu ni uonevu. Kwa hiyo, hawa wenzetu waliolipokea jambo hii, naomba Serikali iwafikirie ili ile furaha yao izidi na sisi tuliokuja hapa kuhamia kama wenyeji wetu ili nao waweze kutuunga mkono katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mama huyu ana eneo kubwa sana alilorithi, Mtendaji pamoja na Manispaa wamelichukua, wamesema eti wanawapa watu ambao wana Taasisi. Hivi Taasisi gani itakayochukua eneo la mtu wakapewa bila mwenyewe kupewa hata sehemu ya kukaa? Ana watoto wake wengine wamejenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilimfuata mpaka huko kwake nikaona, kwa sababu mimi sipendi jambo la kuhadithiwa, napenda nione. Nilipokwenda, nikaona ana mtoto wake mmoja kajenga nyumba, CDA walimpa kiwanja akanitajia mpaka namba ni 50. Kuna mtu kajenga chumba kimoja tu mbele na mwingine kajenga chumba vile vile, wamemwambia hapa hatuwezi kukupa, tunammilikisha mtu mwingine kwa sababu kiwanja hiki wamepewa watu saba. Hii ni dhuluma. Namwomba Waziri wa Ardhi na watu wa Manispaa, dhuluma hii wasiendelee nayo. Wazawa wa Dodoma ambao walikuwa kwenye ardhi yao wapewe priority ya kupewa kwanza maeneo ya kujenga wao baada ya kupimwa ndiyo baadaye wapewe wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, nitajielekeza kwenye watumishi wa Serikali. Kuhamia kwa Mji wa Dodoma ni jambo jema na wafanyakazi wa Serikali walipokuja wamekuja kwa furaha kubwa lakini matokeo yake hawana sehemu za kukaa. Wengi wao wanakaa kwenye guest, wengine wamepanga kwa watu, wameacha familia zao Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ijenge kwa haraka sana nyumba za kukaa watumishi wa Serikali ili wasiendelee kuchoshwa na jambo hili na kuwa na maisha magumu kwa sababu mtu familia yake inapokuwa mbali naye maisha yanamwendea vigumu. Naiomba Serikali ijenge nyumba kwa haraka ili watumishi wa Serikali wasiendelee kupata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nitazungumzia kuhusu miundombinu. Wenzangu wengi wamesema, lakini tatizo lililojitokeza katika Mji wa Dar es Salaam ni miundombinu kutokupangwa mapema kabla mji ule kuongezeka. Kwa hiyo, kabla mji huu haujaanza kuongezeka watu wengi, Serikali ijipange kutanua hizi barabara. Kwa mfano, barabara inayotoka CBE – Mpwapwa ni nyembamba sana. Kwa hiyo, kabla watu hawajaanza kujenga mle barabarani, naomba Serikali ianze kutanua ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko tulilonalo halikidhi haja ya idadi ya watu iliyoongezeka. Naomba Serikali iharakishe sana kujenga soko hapa Dodoma. Stendi ya mabasi iko mbali. Ingawa iko mbali, eneo tulilonalo ni la kuazima. Naomba Serikali ijenge haraka ili hadhi ya Dodoma kuwa ni Jiji ipatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono jambo hili mia kwa mia.