Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Alfredina Apolinary Kahigi (7 total)

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-
Wananchi wa Mkoa wa Kagera wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa usafiri wa meli, jambo ambalo linawasababishia usumbufu mkubwa na usafiri wa mabasi umekuwa na gharama na hatari zaidi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia usafiri wa meli wananchi hao ili kuwapunguzia gharama pamoja na ajali za mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, vilevile nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu. Nimshukuru na Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuweza kumsaidia. Lakini vilevile nikushukuru kwa ushirikiano pamoja na Wabunge wote, ambao mmeendelea kunipa katika kipindi ambacho nilitumika kama Mwenyekiti wa Kamati na Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, huduma za usafiri katika Ziwa Victoria kati ya Mwanza na Bukoba zilisimama mwezi Machi, 2017 baada ya meli ya MV Serengeti kupata hitilafu katika engine na mfumo wa shafti. Serikali imeipatia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa meli nne za Ziwa Victoria ikiwemo meli ya MV Serengeti. Matengenezo ya meli hii yamekwishaaza baada ya vifaa vyake kupatikana na yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari, 2018.
Mheshimiwa Spika, mbali na ukarabati wa MV Serengeti, Serikali kupitia MSCL inatekeleza mradi wa ukarabati mkubwa wa Meli ya MV Victoria. Mzabuni kwa ajili ya kutekeleza kazi hii amekwishapatikana ambaye ni KTMI Company Limited kutoka nchini Korea Kusini. Taratibu za uhakiki (due diligence) wa kampuni hii zinaendelea na mkataba unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Novemba, 2017. Matengenezo haya yanatarajiwa kutumia muda wa miezi kumi tangu kusainiwa kwa mkataba.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imekamilisha utaratibu wa kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo. Mkandarasi aliyepatikana ni Kampuni ya STX Shipbuilding and Chipyard Company Limited kutoka nchini Korea Kusini. Utaratibu wa uhakiki wa kampuni hii unaendelea na mkataba wa utekelezaji wa kazi unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Novemba, 2017. Utekelezaji wa ujenzi huu utachukua takribani miezi 24 tangu kusainiwa kwa mkataba.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Serikali kuwa kukamilika kwa miradi hii mitatu itasaidia kuwaondolea adha ya usafiri wananchi wote watakaokuwa wanasafiri kwa njia ya maji katika Kanda ya Ziwa Victoria wakiwemo wakazi wa Mkoa wa Kagera. Ahsante.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-
Madarasa na Ofisi za Walimu katika shule mbalimbali katika Mkoa wa Kagera ni mabovu.
Je, Serikali inawasaidiaje wanafunzi wa Kagera kupata mahali pazuri pa kusomea kadhalika na walimu wao wapate ofisi nzuri ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera kuna mahitaji ya vyumba vya madarasa 14,275 kwa shule za msingi, vilivyopo ni 5,934 hivyo upungufu ni 8,341 sawa na asilimia 58. Aidha, mahitaji ya ofisi za walimu ni 1,780, zilizopo ni 925 na upungufu ni 855 sawa na asilimia 48. Kwa upande wa shule za sekondari kuna mahitaji ya vyumba vya madarasa 2,379, vilivyopo ni 1,582 upungufu ni 797 sawa na asilimia 34. Majengo ya Utawala mahitaji ni 212, yaliyopo ni 67 upungufu ni 145 sawa na asilimia 67.
Mheshimiwa Spika, upungufu pia umejitokeza katika miundombinu mingine mfano nyumba za walimu, vyoo na maabara. Hali hii ya upungufu wa miundombinu inatokana na mwamko mkubwa wa wazazi wa kuwaandikisha watoto shule kufuatia Mpango wa Serikali wa Elimu ya Msingi Bila Malipo ambapo idadi ya wanafunzi imeongezeka katika shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Spika, Serikali itachukua hatua na mikakati mbalimbali za kuhakikisha kuwa wanafunzi na walimu katika Mkoa wa Kagera wanapata mahali pazuri pa kusomea na kufundishia ili kuinua taaluma katika Mkoa wa Kagera. Serikali inaendelea kutoa fedha za ujenzi na ukarabati kupitia mpango wa EP4R ambapo jumla ya shilingi 1,243,600,000 zimetolewa katika Mkoa wa Kagera katika kipindi cha mwaka 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa, mabweni, maabara, matundu ya vyoo katika shule za Kagemu na Rugambwa zilizoko kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Nyailigamba na Profesa Joyce Lazaro Ndalichako katika Halmashauri ya Muleba, Murusagamba katika Halmashauri ya Ngara na Omurwelwe iliyoko Halmashauri ya Karagwe.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-
Wananchi wa Kagera wana tatizo la umeme na umeme wa REA II umeingia katika center za vijiji tu.
Je, ni lini wananchi hao watapatiwa umeme ili waondokane na adha ya kutumia vibatari?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Aporinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini ililenga pamoja na mambo mengine kufikisha umeme katika maeneo ya njia kuu, baadhi ya maeneo muhimu katika vijiji na katika taasisi za umma. Utekelezaji wa miradi ya REA Awamu ya Pili ulikamilika mwezi Desemba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ilianza kutekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza tangu mwezi Julai, 2017. Katika Mkoa wa Kagera vijiji vipatavyo 141 vinatarajia kupatiwa umeme kupitia mradi huu. Mradi huu utakamilika mwezi Juni, 2019. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi inahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 299, njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 574, ufungaji wa transfoma 287 za KVA 50 na 100 pamoja na kuunganishia umeme wateja wa awali 9,136. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 38.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Aprili, 2018 mkandarasi Kampuni ya Nakuroi Investment Ltd. aliyepewa kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera alikuwa ameshakamilisha kazi ya upimaji wa maeneo yatakayopelekewa umeme. Kazi zinazofanyika sasa ni kusambaza nguzo katika maeneo ya mradi na kujenga miundombinu, pamoja na kusambaza umeme.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-
Wananchi wa Bukoba Vijijini wanakabiliwa na tatizo kubwa la wanyama waharibifu kama vile ngedere na kadhalika na wanyama hao sasa wanavamia vijiji na kusababisha madhara kwa wananchi:-
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuwanusuru wananchi wa Bukoba Vijijini na balaa la wanyama hao waharibifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua uwepo wa tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu linalojitokeza katika wilaya zaidi ya 80 hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Bukoba Vijijini. Wanyamapori wanaoleta usumbufu kwa wananchi katika wilaya hiyo ni tembo, mamba na ngedere. Tembo kutoka kwenye Ranchi za Kagoma na Mabale wamekuwa wakivamia maeneo ya mashamba na makazi ya wananchi jirani na ranchi hizo. Aidha, mamba wamekuwa wakijeruhi wananchi pembezoni mwa Ziwa Viktoria hususan maeneo ya Kemondo. Vilevile ngedere wanasumbua wananchi kutoka kwenye misitu ya asili ya Kizi, Bugando, Katangarara, Kereuyangereko, Kemondo na Rasina. Misitu hiyo ipo kwenye Kata za Katoma, Karabagaine, Bujogo na Kishongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imechukua hatua za kudhibiti tatizo hilo kwa kufanya doria ambapo Askari wa Wanyamapori kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili - Mwanza na Pori la Akiba Biharamulo - Burigi - Kimisi (BBK) wakishirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo waliua jumla ya ngedere 103 na kufukuza makundi kadhaa. Doria hizo zilifanyika katika Kata za kemondo, Katerero, Kanyengereko, Maruku, Katoma, Bujugo, Karabagaine, Nyakato, Kikomela, Ibwela, Nyakibimbili, Kaibanjara, Buterankunzi, Mikoni, Kyamlaile, Lubafu, Kagya, Lukoma, Ruhunga, Buhendangobo na Kishanje. Sambamba na doria hizo, elimu kuhusu mbinu za kujiepusha na kujihami na wanyamapori wakali na waharibifu imetolewa katika kata 21 ka kushirikiana na Maafisa Ugani. Wananchi wameelekezwa mbinu rafiki za kuwafukuza na kuwadhibiti wanyamapori hao wakiwemo ngedere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua uhaba wa Askari wa Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini hivyo itaendelea kushirikiana na halmashauri husika katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ili wasilete madhara kwa maisha na mali za wananchi. Hata hivyo, naomba nitoe rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini kuajiri Askari wa Wanyamapori kwa ajili ya kuharakisha udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-

Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa hupata posho shilingi elfu ishirini kwa mwezi kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na kazi kubwa wanayoifanya:-

Je, ni lini Serikali itaongeza posho kwa Wenyeviti hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS – TAMISEMI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji katika shughuli za maendeleo. Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Mitaa, vitongoji na Wajumbe wa Serikali za Vijiji pamoja na Wajumbe wa Mitaa za mwaka 2014 zilizotolewa kupitia Tangazo la Serikali Na. 322 na Na. 323, sifa zinazomwezesha mkazi wa
Mtaa, Kijiji na Kitongoji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti au mjumbe wa Serikali za Mitaa ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa posho ya Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa kwa kutumia asilimia 20 ya mapato ya ndani inayorejeshwa na Halmashauri kwenye ngazi za Serikali za Mitaa. Hata hivyo, kiasi hicho kinategemea hali ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri yanayokusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Mkakati uliopo ni kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha makusanyo katika vyanzo vya mapato vilivyopo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ili kujenga uwezo wa kulipa posho kwa viongozi hao. Aidha, viwango vya posho inayolipwa vinatofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine kulingana na uwezo wa kifedha uliopo.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-

Wapo akina mama wanaojifungua wakiwa gerezani na kuendelea kutumikia adhabu zao huku wakiwa na watoto wachanga:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapumzisha kama miezi sita bila kufanya kazi ili wapate nguvu kwanza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wapo wafungwa wanawake wanaoingia na ujauzito gerezani na kujifungua wakiwa bado wanatumikia adhabu zao. Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Magereza inatambua umuhimu wa kumpatia huduma stahiki pamoja na kutofanya kazi ngumu kwa mama mjamzito na aliyejifungua akiwa gerezani, ili aweze kumnyonyesha na kumhudumia mwanae inavyostahili mfano, kupelekwa kliniki, kupewa maziwa kwa ajili ya mwanae, chakula cha ziada na kutengwa na wenzie kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu ili aweze kujihudumia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za wafungwa hawa zimeainishwa vizuri katika Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Jeshi la Magereza kifungu Na. 728 - 729 Toleo Na. 4 la mwaka 2003.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-

Katika Mkoa wa Kagera kuna Ranchi za Taifa zipatazo nne ambazo ni Kagoma, Mabare, Kitengula na Missenyi:-

Je, ni lini Serikali itajenga Kiwanda cha kuchakata ngozi katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) K.n.y. WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Kahigi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba uwepo wa Ranchi za Taifa Kagoma, Mabare, Kitengula na Missenyi pamoja na uwepo wa mifugo mingi katika Mkoa wa Kagera kunatoa fursa kubwa ya uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo. Aidha, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO)imeandaa mpango mkakati wa kibiashara wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017 mpaka mwaka 2022 kwa lengo la kuendeleza na kueneza ufugaji bora hususan ufugaji wa ng’ombe bora wa nyama aina ya boran kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi kwa kutumia mbinu za kisasa. Mpango huu pia unalenga kusaidia NARCO kuingia ubia na kampuni ambazo zinaweza kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo ikiwemo ngozi.

Mheshimiwa Mwenyeki, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Chuo cha DIT, campus ya Mwanza, umeandaliwa mpango kazi kwa kutoa mafunzo kwa vikundi vya vijana na akina mama hususan namna ya kusindika ngozi na uzalishaji wa bidhaa za ngozi, ambayo yakitumika ipasavyo yatasaidia kuongeza wigo wa kimasoko wa zao la ngozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya Mifugo, katika Mkoa wa Kagera, Wizara inashirikiana na Wizara ya Viwanda pamoja na Kituo cha Uwekezaji (TIC), kuendelea kutangaza fursa hizo na kutafuta wawekezaji makini wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata nyama, ngozi na mazao mengine ya mifugo ili kusaidia kutoa ajira kwa wananchi wa Kagera, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kuongeza kipato cha wafugaji.