Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Catherine Nyakao Ruge (6 total)

MHE. CATHERINE N. RUGE aliuliza:-
Kuna taarifa ya uwekezaji katika Bonde la Mto Mara na Kilimo cha Umwagiliaji cha Miwa na kwamba wawekezaji hao ni Waisrael:-
Je, ni kwa namna gani wananchi watanufaika na ulimaji wa miwa katika bonde hilo ambalo wananchi wamekuwa wakilitumia katika kilimo cha mazao ya chakula, biashara na pia kwa malisho ya ng’ombe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa sukari, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iliingia makubaliano na Kampuni ya Uwekezaji ya Nile Agro Industries ya Uganda, kuanzisha mradi mkubwa wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari. Utekelezaji wa mradi huu unategemewa kuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa wananchi katika Wilaya ya Tarime na Taifa kwa ujumla kutokana na mapato yanayotokana na shughuli za mashambani sambamba na ajira za kiwandani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unatarajiwa kuhusisha Wakandarasi wadogo wa hapa nchini na hivyo kuongeza fursa za ajira mpya zipatazo 5,000 kwa wakazi wa Wilaya hiyo, ambapo zaidi ya wakulima 2,000 watanufaika moja kwa moja kwa kujihusisha na kilimo cha miwa. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime itanufaika kupitia tozo (service levy) zitakazotokana na uzalishaji wa sukari katika mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia kuwa wananchi wamekuwa wakilitumia bonde hilo kwa shughuli zao za maendeleo, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inachukua hatua stahiki ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza. Hadi sasa tayari Serikali imekamilisha mipango ya matumizi bora ya ardhi katika Vijiji Vinne vinavyotegemea bonde hilo, hatua ambavyo imefanikisha kutenga eneo la kiasi cha hekta 6,000 kwa ajili ya mradi huo.
MHE. CATHERINE N. RUGE aliuliza:-
Upatikanaji wa vifaa vya walemavu ni mdogo sana lakini gharama zake ni kubwa sana hali inayofanywa walemavu kushindwa kumudu, kwa mfano mguu bandia mmoja unauzwa shilingi milioni mbili.
Je, ni lini Serikali itatoa agizo la kufutwa kodi za vifaa hivyo kama ilivyo katika nchi nyingine na kwa kuzingatia kauli mbiu ya Serikali ya kumkomboa mnyonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA I. ALEX): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa watu wenye ulemavu ni kundi kubwa miongoni mwa Watanzania ambalo linakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kujimudu vikiwemo miguu bandia ambayo huuzwa kwa gharama kubwa kiasi cha kuwafanya Watanzania wenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kuwepo kwa vifaa hivyo vya kujimudu kwa watu wenye ulemavu, Serikali ilitunga Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 inayotoa tamko juu ya upatikanaji wa nyenzo mbalimbali za kujimudu kwa watu wenye ulemavu ili kuwarahisishia utendaji wao wa kazi na katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo pamoja na kuwarahishia mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo bado kumekuwepo na changamoto ya upatikaji wa vifaa hivyo kwa bei kubwa ambayo inakuwa vigumu kwa wananchi wengi kuweza kumudu na pia vifaa hivyo kuagizwa nchi za nje kwa kuwa hapa nchini vinapatikana vichache. Hivyo, Serikali kwa kutambua changamoto hiyo na kwa lengo la kumkomboa mnyonge, ilifuta kodi kwa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kama alivyoeleza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mbunge) kupitia hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2017.
MHE. KHADIJA N. ALI (K.n.y. MHE. CATHERINE N. RUGE) aliuliza:-
Pamekuwa na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira kwa sasa huenda kuliko wakati mwingine wowote tangu nchi yetu ipate uhuru, wahitimu wa tangu mwaka 2015 hawajaajiriwa na Serikali mpaka sasa, sekta binafsi nazo kila kukicha zinapunguza wafanyakazi na kutoajiri wapya:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuhakikisha ajira zinapatikana kwa vijana hawa ambao hawajapatiwa elimu ya kutosha ya kujiajiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha tunakabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira nchini Tanzania Serikali ina mikakati ifuatayo:-
(a) Kuongeza fursa za wigo mpana wa nafasi za ajira kupita sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwekezaji katika uchumi wa viwanda na utekelezaji wa miradi mikubwa kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo nchini;
(b) Kutekeleza Programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayowezesha Nguvu Kazi ya Taifa kuwa na ujuzi stahiki na kutoa fursa kwa vijana kuwa na sifa ya kuajirika na kujiajiri;
(c) Kuendelea kusimamia vijana kujiunga katika makampuni, ushirika na vikundi vya uzalishaji mali ili kupatiwa fursa ya mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa lengo la kuwaongezea mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi.
MHE. CATHERINE N. RUGE aliuliza:-
Bado kuna kata ambazo hazina shule za sekondari hivyo kufanya baadhi ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, kutokana na hali hiyo baadhi ya wazazi wameamua kuwapangishia vyumba watoto wao mitaani kwenye mazingira ambayo si salama.
Je, kwa nini Serikali isije na mpango mahususi wa ujenzi wa mabweni kama inavyofanya kwenye madawati ili kuwapunguzia wanafunzi hasa wa kike adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi nyumbani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE.JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inamiliki na kuendesha shule za sekondari 3,634 Tanzania Bara. Kati ya hizo shule 3,519 ni za kutwa na shule 155 ni za bweni. Idadi hiyo ukiilinganisha na kata 4,420 inabainisha kuwepo na kata ambazo hazina shule za sekondari hivyo zipo changamoto za baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule kwenye kata za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pendekezo la Mheshimiwa Mbunge la kujenga mabweni katika shule zote sekondari kuwa zuri, Serikali imeweka kipaumbele kujenga mabweni kwanza kwenye shule za kidato cha tano na sita pamoja na zinazoandaliwa kupandishwa hadhi kuwa za kidato cha tano na sita ambazo husajili wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Tangu mwaka 2014 Serikali imetumia shilingi bilioni 29.4 kujenga mabweni 298 kwenye shule za sekondari na mabweni 25 kwenye shule za msingi.
Aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 15.7 kujenga mabweni 206 katika shule za sekondari na mabweni manne katika shule za msingi. Halmashauri zinahimizwa kuendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine kujenga shule za sekondari kwenye kata ambazo hazina shule na kujenga dahania (hostel) kwenye shule za sekondari zenye wanafunzi wanaotembea umbali mrefu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. CATHERINE N. RUGE) aliuza:-

Kumekuwa na idadi ndogo ya wasichana wanaodahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu katika fani ya sayansi ikizingatiwa kuwa sasa tunaelekea katika uchumi wa viwanda:-

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha inaongeza idadi ya wasichana katika masomo ya sayansi kuanzia ngazi ya chini mpaka vyuo vikuu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina dhamira ya kuhakiksha kuwa usawa wa kujinsia katika elimu na mafunzo unazingatiwa. Aidha, Serikali inatambua changamoto zinazosababisha wanafunzi wa kike kushindwa kumaliza mzunguko wa elimu na kupelekea kuwa na idadi ndogo ya wasichana wanaojiunga na ngazi nyingine za elimu hasa katika masomo ya sayansi na hisabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hali hii, Serikali inatoa fursa zaidi kwa wasichana kwa kuongeza nafasi za udahili kwa kidato cha V-VI katika tahasusi za sayansi ambapo katika shule 141 zinazochukua wasichana wanaosoma tahasusi za sayansi, shule 85 ni za wasichana tu na 56 za mchanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hizo, Serikali imeendelea na ujenzi wa mbweni na hosteli katika shule na vyuo hasa katika mazingira yenye changamoto ambapo wanafunzi wa kike hupewa kipaumbele kwenye mabweni na hosteli hizo. Vilevile ununuzi na usambazaji wa vifaa vya maabara pamoja na vitabu vya masomo ya sayansi umefanyika ambapo shule za sekondari 1,696 zimepata vifaa vya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi wote ili wafikie malengo yao katika elimu. Aidha, nitumie fursa hii kuwataka wazazi na jamii kuachana na mila, desturi na mitazamo hasi dhidi ya watoto wa kike kwani ni kikwazo katika maendeleo yao na jamii kwa ujumla.
MHE. CATHERINE N. RUGE aliuliza:-

Mji wa Shirati Wilayani Rorya unakabiliwa na changamoto kubwa ya maji safi na salama licha ya kuwa na umbali wa kilometa 3 tu kutoka Ziwa Victoria. Mji huu ni moja ya Miji Mikongwe ambapo miundombinu yote ya maji ipo tangu enzi za Awamu ya kwanza, lakini hadi leo hakuna maji licha ya kuwepo na Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi zinazohitaji sana huduma ya maji?

Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Shirati juu ya upatikanaji wa maji safi na salama ili kupunguza ukali wa maisha ambapo kwa sasa dumu moja la lita 20 linauzwa mpaka shilingi 100?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya India kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika Miji 28 kwa upande wa Tanzania Bara na mradi mmoja kwa upande wa Zanzibar ambapo Mji wa Shirati umejumuishwa. Utekelezaji wa miradi hiyo umegawanyika katika awamu mbili, awamu ya kwanza ni usanifu na awamu ya pili ni ujenzi wa miradi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Serikali ipo katika hatua ya kuwapata Wataalamu washauri watakaofanya usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni kwa miradi hiyo ya maji ukiwemo Mji wa Shirati. Ujenzi wa miradi hiyo utaanza katika mwaka wa fedha 2019/2020. Kukamilika kwa miradi hiyo kutamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa Mji wa Shirati.