Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. William Vangimembe Lukuvi (40 total)

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza nikupongeze kwa kuzaliwa juzi Muhimbili na Mama Ulega, Mungu akubariki sana.
Swali langu ni kwamba, kwa kuwa baraza la ardhi la Wilaya ya Korogwe linafanya kazi katika mazingira magumu. Kuna kesi nyingi za kutoka mwaka 2009 mpaka leo hazijamalizika.
Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi pale ili kesi zile ambazo zimekaa kwa muda mrefu katika Baraza la Ardhi la Korogwe ziwe zimepata ufumbuzi wa haraka ili wananchi waone umuhimu wa Serikali yao?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo sababu tumetenganisha yale Mabaraza na kuunda Baraza jingine la Lushoto, kwa sababu kesi nyingi zilizokuwa zinakuja Korogwe ni za Lushoto na Wilaya nyingine. Kwa hiyo tumeunda Baraza la Lushoto, tutakwenda kuunda Baraza jingine la Kilindi. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza mzigo wa Korogwe na hivyo Baraza lile litakuwa limepunguziwa mzigo wa kuhudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tukichukua hatua hizo Baraza lile litahudumia watu wachache zaidi na hasa wananchi wa Korogwe.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri akiwa Mbulu aliwaahidi wananchi wa Mbulu kwamba Halmashauri ya Mbulu itafute jengo kwa ajili ya Mahakama. Namuomba Mheshimiwa Waziri katika mwaka huu wa fedha Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu itafanikiwa kwa kuwa ina kesi nyingi za ardhi ili Baraza hilo liweze kuzinduliwa na tayari Hamshauri imepata jingo.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, rafiki yangu anajua majibu lakini anataka nirudie ili watu wake wasikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishakwenda, nimetangaza kwamba tutazindua Baraza la Mbulu mwaka huu, bahati mbaya sana majengo waliyotupa yalikuwa na „mushkeli‟ kidogo, Katibu Mkuu wangu ameandika barua kuomba majengo mengine, nafikiri yakirekebishwa hayo majengo, nimeshamuahidi na nimeshawaahidi watu wa Mbulu kwa sababu nimekwenda mwenyewe na Serikali hii haifanyi longo longo inafanya mambo ya uhakika, kwa hiyo tutazindua hilo Baraza mwaka huu la Mbulu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba limekuwa likiwapa notice wafanyabiashara eneo la Keko Furniture ambao wanafanya biashara chini ya majengo ya National Housing kwamba wahame wakatafute sehemu nyingine ya kufanyia biashara ili shirika izikarabati nyumba zile na iweze kuwapangisha wapangaji wengine. Wafanya biashara hawa ni zaidi ya 300 na shirika linataka liwafukuze ili lipangishe watu wasiozidi 50. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari sasa kulishauri Shirika la Nyumba wawe flexible badala ya kuwafukuza hawa watu 300, wavunje zile nyumba wajenge mabanda ambayo yatawa-accommodate hawa wafanyabiashara ili wawe wapangaji wao? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na mchezo mchafu, watu ambao hawakai kwenye nyumba zile lakini ndiyo wanaonekana wapangaji wa nyumba za National Housing, kisha wao wanawapangisha watu wengine kwa gharama kubwa. Je, shirika litakuwa tayari sasa kufanya uhakiki wa kuhakikisha kwamba anayekaa kwenye nyumba ndiye ana mkataba na National Housing ili kuzifanya nyumba hizo zisiwe za gharama kubwa na zitumike na watu wenye mahitaji nazo? Ahsante.
Naibu Spika, ni kweli hayo anayoyasema ya wafanyabiashara wa Keko Furniture na hata juzi alikuja mmoja kuonesha vifaa vya hospitali hapa, nawajua, lakini kwa ufupi ningemshauri, mimi na yeye na baadhi yao tukipata fursa tukutane maana majibu yanaweza kuwa marefu hapa, tuone namna ya kutekeleza kwa pamoja ili kuwawezesha hawa vijana wafanyabiashara 500 waendelee kujiajiri katika eneo hilo. Sasa tutoke nje tuzungumze zaidi badala ya kukujibu hapa maana nitajibu majibu marefu sana, tutafute muafaka wa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ni kweli shirika linafanya uhakiki. Hivi sasa ukiomba nyumba ya Shirika la Nyumba hupati, yule aliyepo anampa funguo mwenzake na hata wafanyabiashara wa maduka makubwa kama Samora na kadhalika wengine wanakula kodi za mtu wa tatu. Hilo nalijua na nimeshatoa maelekezo, kama unavyosema Mheshimiwa Mtolea, kwa National Housing wafanye uhakiki ili wachukue kodi kwa mpangaji na isitokee mtu mwingine kuchukua kilemba cha mpangaji. Kwa hiyo, hilo tunalifanyia kazi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Mimi nilifuata utaratibu nimeuliza swali fupi sana, lakini ukiona majibu marefu ujue hapa kuna udanganyifu. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza hili swali tangu nikiwa Mbunge wa Viti Maalum na Ofisi ya Wanyamapori wakati huo alikuwa Ndugu Sarakikya alinijibu kwamba walienda kupima na nikaenda Ofisi ya Ardhi Kilombero wakasema wananchi hawajashirikishwa. Baada ya kuwabana sana mkasema kwamba mnasubiri hela kutoka Ubelgiji na mmeshapata shilingi milioni 100 na sasa mnaaenda kushirikisha na mpaka kwenye Halmashauri yetu tunazo hizi taarifa, mnaenda mkashirikishe vijiji mkapime upya leo unaniletea majibu marefu. Nakuambia mradi wa ardhi hauendi kutatua migogoro unaenda kupima vipande vya ardhi ambavyo havina migogoro, Mheshimiwa Lukuvi huyu hapa. Sasa haya majibu yako mimi siyakubali, hiyo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kuna barua ninayo hapa, Meneja wa Ramsar ametoa barua iko Kilombero anasema wataenda kutatua hiyo migogoro…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Susan nenda kwenye swali.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Sasa ni lini mtaenda kutatua ile migogoro na mmeruhusu wafugaji waende kule kwa wakulima, magomvi karibu yatatokea, ardhi mmeitwaa, mmeenda kufanya nini? Lini mtaenda kurekebisha ile mipaka? Ninachotaka ni safari ya kwenda Kilombero. Mimi nasemea Kilombero lakini kuna Wilaya tatu, Ulanga na Malinyi, kuna vijiji 126 mmechukua bila idhini yao. Nendeni mkafanye kazi, hilo ndilo swali langu, ndiyo, lini mtaenda Kilombero na barua mnayo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaomjua Mheshimiwa Susan ndiyo lugha yake, hatumshangai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo marefu ya Mheshimiwa Susan ni kweli kwamba tunayo migogoro mingi sana na Serikali tunajua kwamba tunayo migogoro mingi. Iko migogoro inayoweza kutatuliwa na Wizara moja moja, lakini iko migogoro ambayo haiwezi kutatuliwa na Wizara moja moja. Juzi nimetoka Kilombero yale yanayonihusu mimi nimejaribu kuyatatua, lakini hayo mengine anayoyasema sisi Serikali tumeunda timu. Hivi sasa tumekutana mimi na mwenzangu Waziri wa Mifugo, Waziri wa Maliasili na TAMISEMI tumeunda timu ziko mtaani huko mikoani na huko Kilombero watafika na nimewaambia hata juzi kwamba haya anayoyasema hayo siyo yangu, kuna Madiwani wameniambia kama alivyoniambia Mheshimiwa Susan.
Kwa hiyo, nimewaambia hili si letu kwa sababu haiwezekani Lukuvi anayekwenda siku moja akatatua mgogoro. Kwa hiyo, tumeunda timu ya wataalam wa Wizara nne wanapitia kuangalia namna bora ya kutushauri sisi Mawaziri tuamue juu ya migogoro hiyo mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wanakumbuka wakati uliopita tuliwapa fomu fulani mkatupa ile migogoro iko, Mheshimiwa Susan ameandika kwenye kile kitabu. Kwa hiyo, kutokana na kile kitabu sasa tumeunda timu, nataka kukuhakikishia hata sisi kama Serikali tumejiwekea lengo katika miaka hii mitano lazima tuwe tumemaliza migogoro yote. Kwa hiyo, nataka tu kumueleza Mheshimiwa Susan kwamba migogoro ilikuwepo na itaendelea kuwepo lakini tumeamua kuikabili kisayansi.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa Serikali wa kuhamisha nyumba zilizokuwa chini ya Halmashauri kwenda Serikali Kuu umeacha watumishi katika Halmashauri ya Karagwe bila makazi, takribani kaya za Watumishi 60 hivi sasa hazina makazi kwa sababu Serikali Kuu imechukua nyumba ambazo zilikuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Je, Wizara haioni kwamba inabidi iwasaidie watumishi hawa kwa kuiomba NHC ishirikiane na
Halmashauri, Halmashauri tunaweza tukawapa eneo la kujenga nyumba nafuu kwa ajili ya watumishi hawa? Nashukuru
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nyumba zilizokuwa awali za Wizara ya TAMISEMI baadae zikaenda NHC sasa zimerudishwa Serikali Kuu. Hivi sasa wataalam wangu na Wataalam wa Wizara ya Ujenzi wanapima maeneo hayo ili yamilikishwe kwa Serikali Kuu. Lengo la Serikali ni kujenga nyumba mpya ili ziweze kuboresha mandhari ya Miji, kwa sababu nyumba hizi tangu zimemilikiwa na Serikali za Mitaa na NHC ingawa maeneo yale ni mijini lakini nyumba zimekuwa chakavu na hivyo
zinaleta mandhari mbaya katika miji. Hivyo, lengo la Serikali ni kuzijenga upya.
Pili, kuchukua zile nyumba kuziweka Serikali Kuu hakumaanishi kwamba wale wanaokaa katika nyumba zile sasa wafukuzwe. Mheshimiwa Rais ameagiza kwamba zoezi hili linakoendelea kupima mpaka itakapofikia zamu ya kujenga nyumba mpya katika maeneo hayo, waliomo wanaopanga sasa wabaki katika nyumba hizo wasibughudhiwe na wasifukuzwe. Whether ni watumishi wa leo au watumishi wa zamani wenye mikataba ya kukaa kwenye nyumba hizo wabaki wale wale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale wa Karagwe hao hawapaswi kutoka, wakae humo humo whether ni watumishi au wananchi wa kawaida. Nyumba hizi ingawa si lazima wakae watumishi tu lakini kuna sehemu nyingine watumishi wa Serikali wanakaa na wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, waliomo kwenye nyumba hizo wasifukuzwe. Huko Karagwe kama wananisikia wanafikiri kwamba hao wafanyakazi wanatakiwa kufukuzwa hapana. Tunahaulisha tu utaratibu wa umiliki wa Serikali lakini hatuwaondoi wapangaji.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; sambamba na wenzangu ni lini Serikali itakwenda vijijini kukutana na akina mama ambao wanahodhi maeneo mengi na maeneo hayo wanaweza wakaanzisha viwanda vidogo vidogo lakini unakuta wanakwama kwa kuwa hawana hati za kimila au zile za kiserikali ambazo zinaweza zikawasaidia kuwapa mikopo na wao kuingia katika uchumi wa viwanda? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumalizia kazi la Mheshimiwa Mdee, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri kwamba ni kweli sheria hazibagui, lakini pia hata kama akipata mwanaume hati ya kimila au hati ya muda mrefu, wakati wowote ule mwanamke ajue ile hati ni salama. Hii ni kwa sababu kwa utaratibu wa sasa mwanaume akitaka kuuza au kubadilisha ile hati hatumkubalii mpaka tumuulize mkewe na vilevile mwanamke akitaka kuuza lazima tumuulize mumewe ili kuonyesha kwamba mali haipotei whether imeandikwa mwanaume au mwanamke wakati wa kupoteza lazima yoyote aulizwe. Kwa hiyo, mwanamke amelindwa sana katika sheria za sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Vulu nataka kukushauri tu kwamba hayo mashamba na maeneo ambayo wanawake wanamiliki au yapo kwenye mtaa au vijiji, washauri hao wanawake wajihusishe na mamlaka zinazohusika ndani ya Halmashauri ili wawapimie waweze kupata. Kama wapo mijini hawapati hati za kimila wanapata Title Deed za muda mrefu, lakini kama wapo vijijini wapete hati za kimila. Ardhi inapimwa na inamilikishwa na Halmashauri za Wilaya. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, majibu ya Serikali yameonesha kwamba eneo pekee lililopimwa katika Jimbo la Ubungo ni eneo la Kimara ambalo kumepimwa viwanja 3,196 au nyumba 3,196; je, Serikali inasemaje katika maeneo yaliyobaki ya Makuburi, Manzese, Ubungo na maeneo mengine ya Jimbo la Ubungo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri amejibu vizuri. Maswali haya yanapaswa kuwa ndani ya mipango ya Halmashauri husika, kama tunavyopanga mipango juu ya shughuli nyingine za maendeleo ndani ya Wilaya basi tujipangie mipango ya namna ya kupima na kupanga miji yetu ndani ya Wilaya zetu, haiwezi kuanzia hapa. Nataka niwaambie wote wawili hata huo mnaosema Mheshimiwa yangu Kubenea tulikuwa wote hapa Kimara, hatupimi pale tunarasimisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam ni moja ya miji ambayo imejengwa siku nyingi, imejengwa vibaya ni makazi holela. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kurasimisha angalau wananchi waweze kupata barabara za kupitisha huduma zao, waweze kupata hati kidogo ili angalau nyumba zao thamani zile zisipotee, angalau thamani ya mali waliyowekeza pale na zile hati ziwasaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imekuja na mpango mbadala wa kuwawezesha hawa maskini kurasimisha mali zao ili angalau ziwasaidie katika kujitegemea. Kwa hiyo, tunafanya zoezi la urasimishaji, hapa unaposema ndugu yangu Kubenea tulienda wote Kimara tunafanya zoezi la urasimishaji na haya anayosema ndugu yangu tunafanya zoezi la urasimishaji, upimaji mpya utafanywa Dar es Salaam baada ya kumaliza master plan, tuliyonayo ni ya mwaka 1979, sasa hivi tunaandaa master plan tume-engage wataalam, tukishamaliza master plan ambayo itashirikisha viongozi wote wa Dar es Salaam na wananchi wa Dar es Salaam, Dar es Salaam itapangwa upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ni zoezi la urasimishaji kuwawezesha wananchi kutoka kwenye hadhi ile ya makazi holela angalau waitwe nao wanaishi kwenye makazi rasmi. Hilo ni zoezi ambalo linaendelea sasa na zoezi hili ni shirikishi, wananchi kwenye mitaa wanashiriki wenyewe, wanachangia gharama wenyewe, kupanga maeneo yao katika mitaa yao. Kwa hiyo naomba zoezi hili tushirikiane na ninyi tuanzie kwenye mitaa kujadili halafu Wizara hizi mbili tushirikiane na mipango yenu. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la Mnazi Estate kule Lushoto - Mlalo limevamiwa kwa sababu Mmiliki ambae alikuwa anendelea kulimiliki ameshindwa kuliendesha. Je, pamoja na mchakato ambao tulikuwa tumeuanza wa kufuta, Serikali imefika hatua gani ya kumuondoa mmiliki katika ardhi hiyo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye kijiji cha Mnazi kuna Kampuni inatiwa Lemash Enterprise ambayo ilikuwa inamiliki shamba la Mkonge lenye hekta 1,275 lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kutokana na jitihada zake za kuondoa kero ya wananchi na katika kutekeleza spirit ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli walitimiza wajibu wao na nataka kumhakikishia kwamba na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli naye ametimiza wajibu wake. Tarehe 4 Septemba, 2017 shamba hilo limefutwa rasmi na mmiliki ameshaambiwa, nimeshachukua hatua ya kulitangaza kwenye Gazeti la Serikali kwa order ya Rais na hivi sasa nimeshamwandikia Mkuu wa Mkoa wa Tanga ili atupe mapendekezo mazuri zaidi ya namna ya kulitumia shamba hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nakuomba Mheshimiwa Shangazi kwa kuwa umelianza, basi naomba ushirikiane na Mkuu wa Mkoa wa Tanga kulimalizia mlete mapendekezo mazuri yatakayowezesha kutumika shamba hilo kuinua uchumi wa wananchi wa Mnazi. Tungependa shamba hili liendele kuwa shamba la Mkonge lakini ninyi watu wa Tanga muamue nani aendesha kilimo hicho kwa ajili ya kuongeza tija ya ajira na uchumi wa Taifa. (Makofi)
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Moshi vijijini kuna mashamba ambayo toka mwaka 1968 yalitaifishwa na kimsingi ni mashamba ya umma, lakini baada ya kutaifishwa na kupewa Vyama vya Ushirika yamekuwa yakigawanywa kwa taasisi mbalimbali kwa ajili ya shughuli za wananchi. Sasa hizo taasisi zikitaka kupima hayo mashamba sasa kulingana na shughuli ambazo zinafanyika inakuwa vigumu kwa sababu tayari kuna hati ambazo zilikuwepo toka wakati huo, ikiwa ni pamoja na eneo kama la Uru Seminari ambalo nilishalifikisha kwa Mheshimiwa Waziri.
Naomba kujua kutoka kwenye Serikalini ni lini Serikali itakwenda kufanya upimaji upya ili kutoa hati kulingana na matumizi ambayo yapo sasa hivi katika yale mashamba katika Kata zote hizo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mkoa wa Kilimanjaro na mashamba ya ushirika ni tatizo kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamna mashamba haya yalikuwa ni ya settlers, uamuzi wa Baba wa Taifa yalichukuliwa yakapewa Vyama vya Ushirika na mashamba haya ni mengi sana Mkoa wa Kilimanjaro ambayo yalimilikishwa Vyama vya Ushirika. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo nimeshamwandikia lakini tunazungumza nia njema zaidi ya kuhakiki upya mashamba yanayomilikiwa na Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro hivi sasa. Ni kweli Vyama vya Ushirika zamani vilipewa, lakini leo matumizi yake ya vyama vya ushirika na ushirika wenyewe ni tofauti na madhumuni ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Kilimanjaro maana hoja hii siyo ya Mheshimiwa Mbunge peke yake, Wabunge wote wa Kilimanjaro mashamba haya yanawahusu. Watuachie bado tuko kwenye mazungumzo na Wizara ya Kilimo ambaye ndiyo Msajili wa Vyama vya Ushirika ili tuone namna gani njema ya kuyahuisha mashamba yote ya ushirika ya Mkoa wa Kilimanjaro ili yawe na tija kwa wananchi wote kulingana na mazingira ya sasa. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jiji letu la Tanga kuna upimaji unaoendelea katika eneo la Amboni kwa ajili ya kuongeza Kiwanda cha Saruji cha Sinoma cha Wachina. Katika maeneo yale kuna tatizo kubwa la kwamba, wananchi wenye mashamba yao wanaambiwa watalipwa fidia ya mazao ya muda mrefu tu na mazao ya muda mfupi kama mahindi, mihogo na mengineyo hayatalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inalifahamu hilo na utaratibu huu ni utaratibu wa sheria gani inayotumika kulipa mazao ya muda mrefu, na pia pana maji koto au sulphur water pale katika eneo la Amboni ambayo ni kama tunu kwa mambo ya utalii.
Je, Serikali inafanya juhudi gani kuhakikisha ile sulphur bath itaendelea kuwepo ambayo iliendelezwa na Galanos lakini pia na wananchi wenye mzao mafupi nao watalipwa fidia yao?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni la Tanga. Walioamua kufanya haya ni Halmashauri ya Jiji la Tanga kwenye shamba hili. ningemuomba Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kazi hii hata tathmini ya pale imesimamiwa na kufanywa na Wathamini waliopo kwenye Jiji la Tanga na upitishaji wa viwango huu ulikuwa shirikishi na maelekezo haya yametolewa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba, unajua ni rahisi kufikiri kwamba Waziri akiwa hapa Dodoma anaweza akajua na akalitolea ufafanuzi kila jambo lakini jambo hili ni shirikishi limefanywa na Watendaji wenye Mamlaka ya Kisheria ya kutenda wa Jiji la Tanga kwahiyo kama halikufanyika vizuri, wale wananchi wanajua Bungeni hapa mwaka huu mmetunga Sheria ya Bodi ya Mfuko wa Fidia. Ninawaomba waisome, Waheshimiwa Wabunge muwasidie wananchi hawa wakate rufaa kwenye Bodi ya Mfuko wa Fidia ili iweze kufikiaria vinginevyo, lakini mimi kama aziri hapa siwezi kusimama nikatengua uamuzi halali uliofanywa na Halmashauri ya Jiji la Tanga. Hivyo, naomba wafuate hiyo sheria. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niulize maswali mawili madogo ya nyongeza; kama ambavyo Serikali imekiri katika majibu yake juu ya umuhimu wa zoezi hili la kupanga, kupima na hatimaye kumilikisha ardhi kisheria, lakini nakumbuka katika hotuba ya Waziri ya mwaka 2016/2017 aliliambia Bunge hili kwamba ni 15% tu ya ardhi ya nchi hii ndiyo imefanyiwa upangaji, upimaji na umilikishaji na nyingi ya hizo utazikuta ziko maeneo ya mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuliachia zoezi hili muhimu sana kama ambavyo Serikali imekiri kwa halmashauri zetu za wilaya na vijiji ni zoezi ambalo lina gharama kubwa na halmashauri nyingi hazitaweza kabisa. Je, kama Serikali inatambua umuhimu wa zoezi hili, kwa nini Serikali Kuu sasa isiingilie kati ikazisaidia mamlaka hizo za wilaya na vijiji kuhakikisha ardhi yote ya nchi hii inapimwa, inapangwa na pia kumilikishwa kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999 kifungu cha saba (7) kinamtaka Kamishna wa Ardhi kutoa cheti cha ardhi ya kijiji kwa vile vijiji ambavyo mipaka yake imetambulika na imekubalika lakini viko vijiji ambavyo vina sifa hiyo na havijapata hati hiyo. Nini kauli ya Serikali kwa Makamishna na Maafisa wa Ardhi wa Wilaya ili vijiji vipate hati hiyo muhimu sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu imekuwa inasaidia zoezi la upangaji, upimaji na hata kuandaa matumizi bora ya ardhi katika vijiji na master plan. Hata hivyo, kimsingi kwa mujibu wa sheria, zoezi hili lazima lisimamiwe na ni jukumu la halmashauri husika na vijiji. Ni kweli, kazi ya vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi unaweza ukasema ni gharama, lakini viko vijiji ambavyo vimesimamia na vimepanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyao na maisha yanaendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za upangaji wa matumizi bora katika kijiji kimoja haizidi shilingi milioni 22. Sasa kama wananchi wote wataona ni busara kutoa shilingi milioni 22 ili kila mmoja mwananchi wa kijiji kile awe na uhakika wa ardhi yake, wafanye hivyo, kwa sababu si gharama kwa sababu unapanga na kupima mara moja katika maisha yenu yote. Kwa hiyo, bado nahamasisha kwamba pamoja na Serikali Kuu kuendelea kusaidia, lakini jukumu hili lazima liwe ni jukumu la msingi, kwa mujibu wa sheria, la mamlaka za vijiji na wilaya husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, kama nilivyosema, Serikali inaandaa mpango wa jumla wa kupanga na kupima nchi nzima. Mpango huu tutaueleza vizuri kwenye budget speech nitakayosoma mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ni kweli kwamba ni jukumu la Kamishna kutoa cheti cha vijiji. Sasa kama ana taarifa juu ya vijiji ambavyo anahitaji na ambavyo havina vyeti vya vijiji, tuwasiliane ili tujue kwa nini imetokea hivyo tuweze kurekebisha tuwapatie hivyo vyeti.
Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea, Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima sasa aulize swali lake.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kulingana na uchache Halmashauri ya Wilaya ya Itilima haukuweza kupata shilingi milioni 400 kwa wakati. Tuliweza kujenga nyumba nne kwa kutumia utaratibu kwa kutumia mikataba ya halmashauri na Naibu Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Kandege alikuja kufungua hizo nyumba. Je Waziri atakubaliana nami kuangalia utaratibu mpya na wa masharti ya ujenzi wa nyumba za watumishi hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miji mingi nchini imekuwa ikikua kwa kasi bila mpangilio. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na halmashauri hapa nchini ili kuweka upimaji ikiwemo Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Njalu tukutane huko nje tufahamishane namna gani mahitaji yake namna gani anaweza tukajenga hizo nyumba, lakini ajue Shirika la Nyumba limewekwa kwa mujibu wa sheria lazima lifanye biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tulivyokubaliana kwamba wangekuwa wanatenga pesa halafu tunawajengea nyumba. Shirika la Nyumba ujenzi wake wa gharama za ujenzi ni nafuu kuliko contractor yoyote, Shirika la Nyumba ni contractor wa daraja la kwanza. Hata hivyo, kwa kujua ni Shirika la Nyumba la Serikali gharama za ujenzi ni nafuu na ubora wa nyumba zake ni mzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, labda tujadiliane huko nje kitu gani wamekwama badala ya kujenga nyumba 13 wanataka wajenge ngapi halafu tujue namna ya kushirikiana. Kwa kweli hatuwezi kujenga nyumba bila kupewa pesa Shirika la Nyumba haliwezi kwa sababu itabidi likope fedha benki liende kujenga nyumba zao. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Njalu kwa hili la nyumba tuwasiliane baadaye ili tuone jambo gani wamekwama, tuweze kushirikiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili upimaji kabla ya kupima Mji wa Itilima lazima ifanywe master plan na bahati nzuri Bariadi wameshafanya master plan. Kama tatizo ni utaalam, sisi tuko tayari kuwaazima Wataalam wa Mipango Miji wawasaidie Itilima namna ya kuandaa master plan, halafu baada ya master plan then sasa lije zoezi lingine la upimaji na upangaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kama halmashauri yoyote haina Wataalam wa Serikali wa upangaji na upimaji wasipate tatizo. Serikali imeshasajili makampuni ya upangaji na ya upimaji ya Wataalam wabobezi ambao tumewasajili na tumewapa ruksa ya kufanya kazi hizi kama wenzao wa ujenzi wanavyofanya kazi nyingine za ujenzi wa barabara na majengo.
Mheshimiwa Naibu Spka, kwa hiyo, halmashauri kama haina Wataalam isikae ikisubiri Wataalam wa Serikali tunayo makampuni ambayo yanaweza kuwasaida wananchi wa Itilima kupanga mji wao, kupima hadi umilikishaji. Kwa hiyo, tunaweza tukawasaidia Wataalam, lakini pia halmashauri inaweza ku-engage Wataalam binafsi kampuni binafsi wakafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, yote mawili yanawezakana kufanywa kwa Itilima.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali kupitia Waziri wa Ardhi kwa kazi kubwa inayofanya Wizara hii. Pili niulize maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa tatizo kubwa linalowakabili akina mama wajane, watoto, ambao wamepoteza wapendwa wazazi wao ni katika tatizo hili la kesi na mashtaka ya ardhi; na kwa kuwa familia nyingi zinazopata matatizo hayo hazina uwezo wa kifedha kuweka wanasheria. Je, ni kwa namna gani sasa Serikali itatafuta msaada wa kisheria kwa akina mama wajane na watoto warithi wa ardhi katika familia mbalimbali zinazopoteza wazazi wao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Wizara yameniridhisha kwa kiasi kikubwa, je, ni kwa namna gani Wilaya ya Mbulu ambayo hivi sasa kesi nyingi zinazoendeshwa katika Baraza la Ardhi la Babati zinapata nafasi ya fursa ya kupimiwa ardhi kwa msaada wa Serikali, wananchi na wadau wengine ili tatizo hili la mashtaka mengi ya ardhi katika Baraza la Babati yapungue na hata kwa Mbulu kwa sababu hata tukipata Baraza bado tatizo litakuwa kubwa kwa mashtaka yatakayoendelea kutokana na hali hii ya kunyang’anyana ardhi kwa wale wenye uwezo na wasio na uwezo? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali inao mkakati wa kutoa msaada wa kisheria kwa makundi kadhaa yenye shida kama hizi, lakini kwanza kwa Mbulu tulifikiri kitu cha muhimu tusogeze huduma na kuanzisha Baraza la Ardhi kwa sababu tusingeweza kufikiria huduma za kisheria wakati huduma yenyewe haitolewi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba kwanza atuvumilie, mwaka huu Mungu akipenda lazima lile Baraza ambalo amelipigania kwa muda mrefu Mbulu Mjini litaanzishwa.
Mheshimiwa Spika, pia lile Baraza la Babati linaendelea kufanya kazi. Tutahakikisha kesi zote za Mbulu ambazo ni nyingi sana, tukishamuweka pale Mwenyekiti pale Mbulu kesi zote za Mbulu zitarudi Mbulu kutoka Babati ili angalau iwarahisishie hawa akina mama na watu wasio na uwezo waweze kupata hii huduma karibu na mahali wanakoishi. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Mabaraza haya ya Ardhi hasa yale ya ngazi ya Kata yanafanya kazi kubwa sana kwa sababu yako karibu na wananchi lakini mabaraza haya yamekuwa na changamoto kubwa hususani eneo la maslahi yao kwa maana ya posho za usafiri na posho za vikao pamoja na vitendea kazi. Nini kauli ya Serikali juu ya kuhakikisha Mabaraza yale ya Kata yanawezeshwa ili yafanye kazi zao kwa ufanisi mkubwa? Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika muundo huu wa Mabaraza tunaanza na Mabaraza hayo ya Kata na kwa muundo wake Wajumbe wengi wa Baraza lile ni wenyeji wa maeneo yale. Kazi hii kwa kweli ni ya kujitolea kwa sababu inarahisisha na inaondoa kero ya watu wao, hatuna mtumishi wa kudumu kwenye Baraza la Kata.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatarajia wananchi wajue hilo na ikiwezekana Halmashauri za Vijiji vinavyozunguka Kata ile wafanye utaratibu wa kuchangia uendeshaji wa lile Baraza la Kata, kwa sababu Baraza lile la Kata linatakiwa kusimamia na kusuluhisha migogoro kadhaa inayokuwepo katika maeneo yanayozunguka pale kwenye Kata. Baada ya hapo rufaa huwa zinaenda kwenye Baraza la Wilaya, kutoka kwenye Baraza la Wilaya rufaa zinakwenda Mahakama Kuu.
Mheshimiwa Spika, nataka nimuarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatuna posho kwenye Mabaraza ya Kata. Tunataraji kwamba viongozi wanaopendekezwa na wenzao kufanya kazi ile ni wale ambao wana uwezo na wana uwezo wa kujitolea.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nilitegemea Waziri angeniambia kwa sababu kutaifisha ni suala lingine na kuendeleza ni suala jingine, kwamba hizi ekari zaidi ya elfu 67 ambazo zimetaifishwa Serikali hii imeziendeleza vipi? Sasa maswali yangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kumekuwa na matumizi mabaya ya hii sheria ya kutaifisha mashamba. Wapo watu ambao walikuwa wakimiliki mashamba kihalali na wana hati, lakini wamenyang’anywa mashamba hayo. Wapo watu ambao walishinda hata kesi Mahakamani, lakini mashamba yao wamenyang’anywa. Ni lini Serikali hii itaacha uonevu kwa wananchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Kata ya Tungi, eneo la Kiyegeya katika Manispaa ya Morogoro tangu mwaka 1984 walikuwa wakimiliki mashamba ya Tungi Estate, lakini mwaka 2014 wananchi wamenyang’anywa mashamba yale kwa maana ya kuachia ujenzi wa Star City.
Kwa kuwa, Serikali mpaka sasa haina lengo la kuanzisha mji ule wa Star City, lakini vilevile mpaka sasa Serikali haijalipa fidia. Naomba kufahamu ni kwa nini Serikali isiwaache wananchi hawa wakaendelea na shughuli zao za kilimo?

Mheshimiwa Spika, yapo malalamiko na tumekuwa tukifuatilia hata kwenye vyombo vya habari. Baadhi ya mashamba ambayo yanafutwa na wamiliki ambao wamekuwa wakilalamikia kwamba, walikuwa na mashamba hayo kwa muda mrefu, lakini wamenyang’anywa. Kwa hivyo, naomba Waziri anayafahamu vizuri, yakiwemo ya Mvomero, yakiwemo ya Hananasifu…
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali hatujataifisha mashamba. Nilimsahihisha kidogo kwenye swali lake nikasema, yaani kwa Kingereza ni revocation, revocation siyo kutaifisha. Rais anaweza akayachukua mashamba kwa manufaa ya umma, lakini hajafanya hivyo. Haya mashamba yote tuliyochukua niliyoyataja ni yale mashamba ambayo waendelezaji wamekiuka sheria.
Mheshimiwa Spika, kila mwananchi anapopewa shamba au kiwanja lazima azingatie sheria na masharti aliyopewa kwenye hati yake yameandikwa. Kama amepewa shamba kwa ajili ya mifugo, lazima alitumie kwa mifugo na alipe kodi stahili na aliendeleze. Kamishna ana uwezo wa kulipima uendelezaji wake kila mwaka ameendeleza kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, nataka kukuhakikishia mashamba haya niliyoyataja hayakutaifishwa kama anavyosema Mheshimiwa Devotha, isipokuwa wenye mashamba haya na wana hati. Ukisikia Mheshimiwa Devotha shamba limefutwa maana yake lina hati, kumbe afutiwe nani?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hawa watu wenye hati wamefutiwa kwa sababu, wamekiuka masharti ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 99, Sura 113, wakiwemo hao unaowasema, mimi siwajui, lakini hao ambao anafikiri tumewaonea, hakuna hata mwananchi mmoja ameonewa katika utekelezaji wa jambo hili.
Mheshimiwa Spika, nataka kuwahimiza wamiliki wote wa mashamba nchini, mtu yeyote ambaye ana shamba amepewa, lazima afuate masharti. Kama haliendelezi, kama halipi kodi stahili, shambapori, sheria itafuata mkondo wake. Sheria inaanzia kwenye Halmashauri husika, Afisa Ardhi husika anatoa notice kwa mhusika ya siku 90 ajieleze kwa nini hatua zisichukuliwe. Wengine hawa wote hawajibu hata notice, baada ya hapo Halmashauri inapandisha zoezi hilo mpaka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na mimi nampelekea Mheshimiwa Rais anatimiza wajibu wake.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Devotha Minja jambo hili wakikusikia wenye Halmashauri zao watakushangaa kweli kwa sababu wao ndiyo wamefanya, Halmashauri hizi ndiyo zimeleta maombi ya kufuta mashambapori. Nasi tutaendelea kutekeleza hili jambo na ninawahimiza Waheshimiwa Wabunge mahali popote mtakapokuta mashamba yasiyoendelezwa, bila kujali ya nani, bila kujali siasa, bila kujali mashamba haya alikuwa anamiliki mkubwa gani au mtu gani, yaleteni kwa mujibu wa sheria na sisi tutachukua hatua.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Shamba la Tungi. Shamba hili la Tungi ni la watu, linamilikiwa kwa mujibu wa sheria, lina mmiliki halali. Nataka nimwombe tu kwa sababu, maelezo haya ni mengi, nimwombe Mheshimiwa Devotha Minja aende pale kwa Mkuu wa Mkoa atampa maelezo mengi kwa sababu, mimi mwenyewe nimeshakaa na timu ya Mkoa, hawa wananchi walipelekwa tu pale kulima wakati wa siasa ya Kilimo cha Kufa na Kupona, lakini walikuwa wanalima kwenye shamba lisilo lao.
Mheshimiwa Spika, pale pana hati ya mtu na Mkuu wa Mkoa amefanya jitihada sana, Mheshimiwa Dkt. Kebwe ya kuwatetea wale wananchi na wenye shamba wamewapa ardhi wale wananchi wa pale ili waweze kuendeleza shughuli zao kwa hiyo, jambo hili Serikali imeshalishughulikia.
Mheshimiwa Spika, lile la mwisho ulilotaka kuuliza ushahidi la Mvomero, anajua Mvomero kuna shamba limefutwa na naamini bado limefutwa na Mheshimiwa Rais ametimiza wajibu wake. Mashamba yote yaliyofutwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya tunawaomba watupe mapendekezo namna bora ya kuyatumia katika Wilaya zao.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuamrishi tunataka mashamba yaliyofutwa wayapange viongozi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ili wananchi wale ambao wameyachungulia kwa muda mrefu na hawana nyenzo za mashamba ya kulima waweze kugawiwa yale mashamba. Kwa hiyo, kama kuna shamba Mvomero limefutwa, namwomba Mheshimiwa Murad na Viongozi wote wa Mvomero wapange utaratibu wa kutumia lile Shamba la Mvomero lililofutwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pia niruhusu nimshukuru na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilimpelekea shida ya mpaka wa Kenya na Tanzania kule Tarakea, alikwenda kule amesaidia sana kuleta utulivu kule mpakani. Mheshimiwa Waziri namshukuru sana.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa sana eneo la Holili, viwanja vimegawanywa hovyohovyo, vimechukuliwa kiholela kabisa na ni tatizo la miaka zaidi ya 10. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, akipata tena nafasi, kama timu yako inaweza kwenda pale kuangalia uhalali wa namna ambavyo vile viwanja vimegawanywa kwa sababu, ni tatizo ambalo limeshindikana, Wakuu wote wa Mikoa wamejaribu wameshindwa. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikwenda Rombo, lakini tulikuwa na zoezi la kuangalia mpaka. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua kuweka mpaka wenye alama zinazoonekana kwa wananchi kati ya nchi ya Tanzania na Kenya, Wilaya ya Rombo ni Wilaya ya mpakani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli nilikwenda huko na nimekwenda mpaka Mkoa wa Mara na zoezi hili litazinduliwa na viongozi wa nchi hizi mbili hivi karibuni. Tumeweka mipaka ya alama mia mia, ili wananchi waweze kuona alama zile waweze kujua nchi yao ya Tanzania inaishia wapi. Kama tunavyojua kwamba, alama hizi zilikuwa zimewekwa kwa umbali wa kilometa elfu moja, mpaka elfu mbili, nyingine mpaka kilometa mia mbili mpaka mia tatu. Kwa hiyo, zilikuwa hazionekani na watu walikuwa wanaingiliana, wananchi wa upande mmoja walikuwa wanaingia upande mwingine bila kujua na wananchi wa upande mwingine walikuwa wanaingia.
Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa pongezi zake na tutaangalia hayo maeneo mengine, sina taarifa kamili hizo alizoniambia nitafurahi zaidi kama Mheshimiwa Selasini akiniandikia vizuri ili nipate message vizuri. Amezungumza kwa haraka sana lakini kwa kadri tutakavyolielewa,
tutalishughulikia. (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nisema kwa masikitiko makubwa sana Wilaya ya Kilosa ni moja kati ya Wilaya zinazoongoza kwa migogoro mikubwa sana ya mashamba na migogoro mikubwa sana kati ya wakulima na wafugaji kutokana na upungufu wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika Kata ya Tindiga kumekuwa na mgogoro mkubwa sana kati ya Kijiji cha Tindiga na NARCO ambao wamemega eneo la Tindiga na kuwapa wafugaji lakini kulikuwa na kesi tangu mwaka 2013 mpaka 2019 wananchi wa Kijiji cha Tindiga wameshinda lakini mpaka leo wanazuiwa kulima na ndiyo tunaowategemea kwa kilimo cha mpunga.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumetokea maafa makubwa sana akina mama wamebakwa na wakulima wamepigwa vibaya sana na kulazwa hospitali kwa sababu ya kuzuiwa kwenda kulima. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wa Tindiga ambao wameshinda kwenye Mahakama ya Ardhi ili warudishiwe ardhi yao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilitoa mashamba kwa wawekezaji katika Kata ya Kisanga, Kata ya Masanze pia Sumargo pale Kilangale. Hata hivyo, hawa wawekezaji wameshindwa kutumia mashamba haya ipasavyo na kupoteza ajira kwa wananchi na Serikali inakosa mapato mengi kwa sababu yale mashamba ni pori na hayatumiki. Imeleta migogoro mikubwa sana pale Masanze mtu alipgwa risasi akafariki, pale Kisanga mwananchi alipigwa risasi akafariki, pale Sumargo, Kilangali migogoro ni mikubwa watu wanaumia sana. Wizara ya Ardhi mnatoa kauli gani kwa Wilaya ya Kilosa ili wananchi waweze kurudishiwa mamshamba haya na kuyaendeleza kwa kilimo ili kusaidia Taifa letu la Tanzania? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Haule, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza juu ya wananchi wa Tindiga, wiki iliyopita niliongea na wananchi hawa waliletwa na Mheshimiwa Mbunge, nimekubaliana naye aniletee mimi barua na vielelezo hivyo vya kesi, maana mimi siwezi kujua yanayoendelea na kesi na mimi nina wanasheria, walete hizo hukumu za kesi kama kweli wameshinda mimi nitawasaidia ili wapate haki yao. Tulishaelewana na nafikiri alitaka hapa sasa wananchi wengi zaidi wasikie. Serikali lazima itekeleze uamuzi wa Mahakama na Serikali haiwezi kumwonea mtu. Kwa hiyo, fanyeni yale niliyowaelekeza leteni barua na vielelezo vile ili tuweze kuchukua hatua.

Mheshimiwa Spika, la pili, swali hili ni swali la msingi ambalo umeuliza. Katika mashamba ambayo yameshafutwa Mkoa wa Morogoro 15 yanatoka Wilaya ya Kilosa. Niliunda timu ya wizara, ilipokwenda kukagua mashamba yote ya Kilosa tukagundua kuna mashamba mengine mapya 23 ambayo yana sifa ya kufutwa pamoja na haya uliyoyataja.

Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu wa kufuta hauanzii Wizarani unaanzia Wilaya ya Kilosa. Tulikuwa na timu ya hovyo pale wilayani Maafisa Ardhi waliokuwa wanafanya kazi ile pale wao sio Maafisa Ardhi walikuwa wamejivisha tu Uafisa Ardhi lakini hatukuwa na Afisa Ardhi. Kwa hiyo, tumefanya utaratibu tumeleta Maafisa Ardhi, kuna Afisa Ardhi mzuri sana tumemtoa kutoka Mkoa wa Mbeya tumempeleka pale sasa ndio wanaanza kazi ya utaratibu wa awali wa kisheria wa kusababisha haya mashamba yafutwe.

Mheshimiwa Spika, lazima notice ya wale wenye mashamba itolewe na Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kilosa hamkuwa naye. Kwa hiyo, nimeelekeza huyo Afisa Ardhi aanze na mashamba haya. Hivi sasa ameshatoa notice ya siku 90 kwa wenye mashamba wajieleze kwanza hatua itapanda itafika kwangu tukiridhika na maelezo yao kwamba wanazo sifa za kufutiwa tutampalekea Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa sheria.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa moja ya chimbuko la migogoro ya mipaka katika vijiji vyetu ni kutokuwepo kwa alama imara na zinazoonekana kati ya mipaka iliyobainishwa kati ya Kijiji na Kijiji, Kata na Kata, Tarafa na Tarafa mpaka hata Wilaya na Wilaya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakiki kuweka alama madhubuti na kutengeneza ramani zitakazowezesha jamii zenye migogoro ya mipaka kujitambua na kuheshimu mipaka hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa katika Jimbo langu la Longido tuna migogoro michache sugu ambayo imekuwepo tangu Wilaya ya Longido ianzishwe zaidi ya miaka 20 iliyopita, ambayo ni mpaka wa Kijiji cha Wosiwosi Kata ya Gilailumbwa na Kata ya Matali Kijiji cha Matali ‘B’ na mpaka huo huo ulio Kaskazini mwa ziwa Natron una mgogoro na eneo la Ngorongoro ambapo Kitongoji cha Ilbilin kimevamiwa na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na kuanzisha vituo vyao vya kudumu pamoja na eneo la Engaruka na sehemu ya Kitumbeine vijiji vya Sokon na Nadare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili kuja katika Jimbo langu atusaidie kutatua migogoro hiyo sugu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishamkubalia hata kwenye Kamati, huyu ni Mjumbe wa Kamati yangu na ni Mjumbe makini sana na ni mchambuzi mzuri sana wa masuala ya ardhi. Tulishakubaliana kwamba tutatafuta nafasi ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwaka huu tufike huko kwenye site ili tuzungumze pamoja na viongozi wenzangu wa Wilaya namna bora ya kukabiliana na hiyo migogoro. Kwa hiyo, Dkt. Kiruswa nitakuja huko kushirikiana ili kuhakikisha hiyo mipaka inatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili juu ya alama zinavyoonekana, katika uwekaji wa mipaka ya vijiji na vijiji huwa kunakuwepo na alama. Labda nimjulishe kwamba Seriakli kupitia Wizara ya TAMISEMI ndiyo huwa inatangaza, Mheshimiwa Rais ndiyo huwa anatangaza uanzishwaji wa mamlaka wa WIlaya, Mikoa na Vijiji vinatangazwa kwenye Ofisi ya Rais, kwa hiyo kuna mipaka ambayo huwa inawekwa pamoja na coordinates zinawekwa kwenye GN, zinatangazwa kwenye GN kwamba Wilaya fulani na Wilaya fulani itapakana na alama za msingi huwa zinawekwa kwenye GN na kwenye vijiji tunapopima huwa kunakuwa na alama zinatangazwa na zinawekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kama kuna matatizo ya kutokukubaliana kati ya kijiji na kijiji huko kwenye Wilaya yake nitakwenda lakini alama hizi za vijiji huwa zinawekwa na wanakijiji wanakubaliana ni alama gani na kila tunapopima huwa tunaweka mawe ambayo yanakuwa na alama na namba ambazo zile coordinates ndiyo zinaingizwa kwenye GN inayotangazwa maeneo ya mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mawe yale huwa tunaweka, sema labda pengine mawe yale yanafukiwa chini labda yeye angependa yawekwe juu, kwa hiyo kama kuna maeneo ambayo yana mwingiliano mkubwa, tuko tayari kuweka alama zinazoonekana badala ya zile ambazo tunaweka chini. Lakini sehemu kubwa huwa tunaweka alama na zile alama zina namba ambazo huwa zinatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi katika kushughulikia makazi, tunayo changamoto ya waajiriwa wapya, watumishi wapya na hasa wale wa kipato cha chini kumudu makazi bora hasa katika mazingira ambayo wamiliki wengi wa nyumba za kupangisha wanataka kodi ya miezi sita mpaka mwaka mzima jambo ambalo watumishi hawa hawawezi kumudu na hivyo kusababisha mazingira ya wao sasa kujihusisha na rushwa ili wapate fedha za kulipia kodi. Sasa Serikali haioni umefika wakati wa kuleta sheria itakayoharamisha kitendo cha wamiliki wa nyumba kudai kodi ya zaidi ya mwezi mmoja? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli jambo hili linaleta kero sana na kama Wizara tumeshalitolea maelekezo mara kadhaa kwa mujibu wa sera, Waziri wa Ardhi na Makazi ana uwezo wa kutoa maelekezo fulani fulani au kuweka kanuni zitakazoweza kutawala masuala haya yote yanayohusiana na makazi. Mimi nimeshawahi kutangaza na kupiga marufuku utaratibu huu kwa sababu sio wa kiungwana wala sio wa kisheria. Ni kweli kwamba watu wanalazimisha wapangaji kulipa miezi 12, si vijana wanaoanza kazi tu, hata wanafunzi wanaokaa kwenye hostel wanalazimishwa kulipa miezi 12, hili jambo halikubaliki hata kidogo. Serikali haitaingilia gharama ya upangishaji, upangishaji ni makubaliano ingawa iko katika utaratibu wa kuweka regulatory authority ambayo itaangalia na viwango vyenyewe vya upangishaji ili kulinda haki za wenye nyumba na haki za wapangaji vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili la kulazimisha mpangaji alipe miezi 12 au sita halikubaliki! Ila ni kweli kwamba ushauri wa ndugu Nnauye tunauchukulia maanani wakati tunasubiri Real Estate Regulatory Authority na sheria kuja Bungeni, tutaweka Kanuni kidogo itakayowabana hawa wasiosikia. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza sijui kama wewe kwako kule Kongwa umesalimika. Miji mingi inageuka kuwa Miji holela, kuwa squarter kwa sababu haipimwi, haipangwi na halmashauri nyingi hazina fedha ya kufanyakazi hiyo, ndiyo ulikuwa msingi wangu wa swali sasa nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hii interim plan ya Kasulu ya 2008 mpaka 2018 mwenyewe kwenye jibu lake Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba iliishia njiani haikukamilika na taarifa nilizonazo ni kwamba mpango huu haukukamilika, sasa swali la kwanza; Je, sasa Mheshimiwa Waziri madam wewe mwenyewe uko hapo Je, ni lini sasa mtakuja kukamilisha hiyo Land use planning ya Kasulu ili ikamilike? Maana iliisha tu 2018 haikukamilika 2018.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Miji 18 ambayo Waziri umeitaja Je, katika Miji hiyo ambayo itakuwa katika hiyo program ya kuendeleza na kupanga Miji Je, Mji wa Kasulu umo? Na kama Mji wa Kasulu haumo ni lini utakuwemo kwenye program hiyo? Suala la miji ni suala kubwa sana, kubwa sana vinginevyo Miji itakuwa squarter yote katika nchi yetu. Ahsante sana.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Nsanzugwanko aongee na Halmashauri ya Kasulu ili waonesha mahitaji ya master plan maana yake ukihitaji unaanza kwenye Kamati ya Mipango Miji na halmashauri yenyewe ya Wilaya inaonesha uhitaji wa kuwa na master plan ya Wilaya yake. Wakishaazimia hivyo, basi waweke bajeti kwenye halmashauri yao ya kufanya master plan ya Mji wao wa Kasulu na Miji yote.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara, wenye Miji yao maana mamlaka ya upangaji kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji ni wenye Wilaya (halmashauri) ambao ni Madiwani. Sisi kama Wizara hatuwezi ku-dectate, hata matumzi ya ardhi wanaosimamia zaidi ni halmashauri yenyewe kwahiyo wakishaazimia kwamba sasa wanafikiri ni wakati muafaka watengeneze master plan basi waazimie vilevile na kuweka bajeti.

Mheshimiwa Spika, tunajua liko tatizo la wataalam wa halmashauri, hatuna wataalam wa kutosha wa Mipango Miji lakini serikali imechukua jitihada ya kutambua weledi na utaalam uliko Nchi hii kwa hiyo tumeanzisha Makapuni chini ya Bodi ya Mipango Miji Makampuni ambayo ya Watanzania wenye weledi na utaalam mkubwa wa kufanya hizi master plan ambayo Halmashauri zinaweza zikawatumia.

Mheshimiwa Spika, lakini halmashauri ambayo haina uwezo huo, Wizara inaweza kusaidia wataalam wa Wizara tulionao wachache kuja kushirikiana na halmashauri ile katika kutoa usimamizi wa utayarishaji wa master plan. Kwa hiyo, nakushauri Mheshimiwa Nsanzugwanko utakapokuwa tayari Manispaa ya Kasulu basi tushirikishe na sisi lakini kama hujui mahali pakuanzia tuzungumze mimi na wewe naweza nikamtuma mtaalam mmoja kule Kasulu akawaeleze wale Madiwani namna master plan inavyoweza kuandaliwa.

Mheshimiwa Spika, lakini katika mipango hii ya hizi master plan 18 zinazoandaliwa naomba Mheshimiwa Nsanzugwanko nimuombe nitamtajia Wilaya zote ambazo ziko kwenye huu mpango wa master plan kwenye bajeti yangu ijumaa na Waheshimiwa Wabunge wote watasoma lakini ijumaa nitawapeni pia nafasi ya kujua pamoja na Miji hii ya Wilaya mnayoijua, lakini viko vijiji vyenu wengine hamvijui vimeshaiva sasa ili kuzuia hizo squatter, vijiji vingine Wilaya imeshaamua kuvitangaza vimeletwa kwangu na nimeshavitangaza na vyenyewe vipangwe kimji ili watu wanaoishi katika vijiji hivyo wapangwe, wapimiwe na wapewe hati kama za Mjini navyo nitawapa jedwali ili Waheshimiwa Wabunge wote mjue vijiji vyenu ambavyo vina hadhi ya kimji ambavyo tumeshavitangaza Tanzania nitawapeni ijumaa nakushukuru. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri na kwa sababu swali langu litafanana kidogo na swali la Kasulu linahusu Mji mdogo sio Mji mdogo, Mji wa Hai ambao zamani ukiitwa Bomang’ombe Makao Makuu ya Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa Spika, mji huu ni Mji ambao unakuwa na kwa kasi kuliko pengine Miji yote katika Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa ni mkoa ni Mji ambao unaunganisha Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na Manyara kwa upande wa Simanjiro. Mji huu sasa hivi unakaribiwa kuwa na takribani na wakazi zaidi ya 100,000 na unahudumia eneo lenye viunga vya karibu watu 200,000 kuanzia Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na ni get way to the Kilimanjaro international Airport ambapo ni karibu sana na uwanja wa ndege wa Kimataifa na of course ndio njia na lango la kuingilia katika Mlima Kilimanjaro ambao ni chanzo kikubwa sana cha mapato kwa Taifa letu.

Mheshimiwa spika, sasa Mji huu ukiacha barabara Kuu ya Lami inayotoka Arusha kwenda Moshi na inayotoka kwenye ene la Hai kwenda Sanyajuu katika Jimbo la Siha Mji huu hauna barabara hata moja ya lami. Sasa katika kupanga Miji ni pamoja na ujenzi wa barabara za lami ili ujenzi na upangaji miti uwe kamili ni lazima uendane vilevile na mitaro ya maji pamoja na ujenzi wa barabara za lami.

Mheshimiwa Spika, halmashauri zetu sasa hivi hazina uwezo wowote wa kuweza kufanya miradi mikubwa ya kiwango hiki. Na natambua hapo nyuma kidogo kulikuwa kuna program kuna project ya sustainable cities ambalo nafikiri limekuwa funded na World Bank ambayo ilichagua baadhi ya Miji ambayo kwa umuhimu wake wa kiuchumi iliweza kuwekewa miundombinu ya barabara za lami. Na hata Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alitoa ahadi ya kujenga barabara kilomita 5 za lami ambazo kwa bahati mbaya bado tunazisubiri kwa hamu sana.

Mheshimiwa spika, sasa Mheshimiwa Waziri katika utaratibu huo wa kupanga Miji nini kifanyike ili Miji muhimu kama hii ambayo inahudumia watu wengi na ni sura ya Taifa inaweza kufanyika ili ipate lami? Nini kifanyike katika hiyo mipango Miji kuikamilisha kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara za lami? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa spika, master plan haijengi miundombinu master plan ni dira ya kuonesha mahitaji ya mpango au mahitaji ya huduma ndani ya Wilaya. Master plan wenye Wilaya yenu mtapanga kutaka kujua barabara zipite wapi, maeneo ya mazishi ni wapi, maeneo ya makazi ni wapi, maeneo ya biashara na huduma mbalimbali. Kwa sababu hata mkiwa na fedha ya barabara kama hamna maeneo mliyopanga kujenga barabara hazitafanya kazi na ndio maana mnakuwa na hela halafu mnaamua kufanya vyovyote au mnavunja nyumba za watu hovyo. Kwa hiyo, la kwanza nakushauri Mheshimiwa Mbowe pangeni master plan ili muone uhitaji wa leo mnahitaji kuwa na barabara kiasi gani, za saizi gani, za lami na kila kitu na mahitaji mengine.

Mheshimiwa Spika, then mkishapanga master plan kuainisha maeneo hayo mtakuja kuyapima lakini baadaye sasa ndio mtawaomba sasa huduma mbalimbali na kuziwekea bajeti ili ziwemo kulingana na master plan iliyopo.

Kwa hiyo, nimelichukua ombi lako hilo, lakini nashauri kama nilivyosema kwa Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Kasulu naomba halmashauri yako mkae kama council katika miradi kingi mnayobuni pale Hai basi mbuni utengenezaji wa master plan kama hamna mtu wa kuwaelekeza pale Moshi kuna Kanda na nimepeleka pale mtalaam mbobezi Afisa Mipango Miji Mkurugenzi Msaidizi wa Kanda mnaweza mkamualika yule bure akaja kuwapa maelekezo na utalaam wa awali wa namna ya kutayarisha master plan ya Hai ili iweze kuwaoneshea huduma zenu zipangwe namna gani katika Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa spika, lakini hilo jingine ulilosema nakushauri kwa sababu Wizara ya TAMISEMI iko hapa Dodoma pengine ukipata fursa ungepita pale kwenye Ofisi za TAMISEMI ili angalau hayo majibu mengine ya lini zitajengwa hizo barabara uweze kujibiwa pale ofisini.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Mheshimiwa Ruth Mollel, bado ana maswali amwili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ni moja na Serikali Kuu alikasimu baadhi ya madaraka yake katika Serikali za Mitaa, basi Serikali Kuu haina budi kusimamia na kuratibu shughuli mbalimbali za Serikali za Mitaa. Serikali haioni ni vyema sasa kusimamia na kutoa maelekezo mahususi katika Serikali za Mitaa katika kujikita kupanga ili tujue kwamba matumizi ya ardhi ni nani anatumia nini kwa ajili ya shughuli za kiuchumi?

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kuwa Serikali Kuu imechukua vyanzo vikuu vya mapato katika Serikali za Mitaa, Serikali Kuu haioni sasa ni muhimu ku-ring fence fedha fulani kwa ajili ya shughuli mahususi za kuratibu shughuli za upangaji wa matumizi ya ardhi? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Wizara ya Ardhi ina wajibu ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ardhi Na. 5 na utekelezaji wa Sheria ya Mipango Miji zote zinahusiana na mambo ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunafanya hivyo, tunatoa mwongozo wa kusimamia na kupitia wataalam wetu waliopo kila Halmashauri wanashiriki, kwa sababu kazi hii inasimamiwa na wataalam wa Sekta ya Ardhi ambao wako katika kila wilaya. Ndiyo maana imewezesha leo hii Wilaya hiyo ya Mkuranga anayoiulizia swali, Mheshimiwa Ulega, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, ni shahidi, vijiji 21 tayari vimeshafanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mafunzo ambayo Wizara tumeyatoa na uwezeshaji tulioufanya katika Wilaya ya Mkuranga, wale viongozi, Madiwani pamoja na watendahi wa Sekta ya Ardhi wa Mkuranga wameweza kujiongeza wenyewe kutekeleza wajibu wao na kwenda kufanya sasa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 21. Kwa hiyo, kazi hiyo ndiyo tunayofanya.

Mheshimiwa Spika, la pili ni fedha. Sisi kama Wizara, hata kwenye bajeti yangu kesho mtaona, tumekuwa tunapanga fedha kusaidia kazi hii tunayofanya. Leo kwa mfano tunapanga matumizi bora ya ardhi na kupanga na kupima kila kipande cha ardhi. Tumeanza Mkoa wa Morogoro katika wilaya tatu. Namwalika mwuliza swali siku moja katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ifakara ili aje uone kazi inayofanywa.

Mheshimiwa Spika, tumeanza mpango mwingine ambao tunakamilisha sasa wa kutaka kupanga na kupima kila kipande cha ardhi nchi nzima. Sasa huo ndiyo mpango wa Serikali Kuu kwa uwezo wa Serikali Kuu. Kwa hiyo, yote mawili tunafanya; hatuwezi kuwaacha wenye jukumu lao wasifanye, lakini Serikali Kuu nayo imekuwa ikishiriki katika kufanya kazi hii tukijua kwamba tuna wajibu wa kufanya hivyo.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa tatizo la migogoro ya ardhi Mkoa wa Pwani inasababishwa na makundi makubwa ya mifugo inayotoka sehemu mbalimbali: Je, Serikali ina mpango gani kukaa Wizara ya Mifugo na Wizara ya Ardhi kupanga na kuzuia makundi hayo ya mifugo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, anasema ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, dawa siyo kuzuia. Tunashirikiana kama Serikali moja na Wizara zote zinazohusika na matumizi ya ardhi ambao ni wadau kupanga matumizi bora ya ardhi, kupanga maeneo ya malisho na kuweka miundombinu. Hiyo ndiyo dawa ya kuwawezesha wafugaji watulie, wafanye shughuli zao za ufugaji kwa tija zaidi. Dawa siyo kuwaondoa wala kuwafukuza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali kwa ujumla kwa pamoja tunafanya hiyo mikakati na katika kazi ambayo alitutuma Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, katika ile timu ya Mawaziri wanane tumeandaa utaratibu ambao tunapendekeza utakuwa ndiyo mwarobaini ambao utawezesha kuainisha maeneo, kuyatambua, kuyapanga na kupanga miundombinu katika maeneo hayo ili wafugaji na wakulima waweze kukaa mahali salama ili waweze kuzalisha na kuongeza tija katika nchi hii.

Kwa hiyo Serikali kwa ujumla kwa pamoja tunafanya hiyo mikakati na katika kazi ambayo alitutuma Dkt. John Pombe Magufuli, katika ile timu ya Mawaziri nane tumeandaa utaratibu ambao tunapendekeza utakuwa ndiyo muarobaini ambao utawawezesha kuainisha maeneo kuyatambua, kuyapanga na kupanga miundombinu katika maeneo hayo ili wafugaji nao na wakulima waweze kukaa mahali salama ili waweze kuzalisha na kuongeza tija katika nchi hii.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina maswali madogo ya nyongeza; kuna baadhi ya watu wanajenga katika mabonde na wengine wanajenga katika hifadhi za barabara na pia karibu kabisa na njia za reli lakini Serikali yetu kupitia halmashauri zetu kila mwaka hukusanya kodi za majengo na kodi za ardhi katika maeneo hayo. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu kadhia hii?

Mheshimiwa Spika, Swali langu la pili ili mwananchi aweze kujenga katika eneo husika ni lazima apate kibali kutoka katika mamlaka na sasa nauliza swali langu. Je, ni nini adhabu ambazo wanapewa watendaji ambao wanatoa vibali katika maeneo ambayo ni hatarishi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli wako watu ambao wamejenga katika hifadhi za barabara, hifadhi za miundombinu mbalimbali na mabondeni lakini wamefanya hivyo kinyume cha sheria na Serikali hairuhusu na hata zoezi la urasimishaji na utoaji wa leseni za makazi hautafanyika wala hatutarasimisha makazi kwa watu ambao wamejenga katika maeneo hatarishi na maeneo ambayo yamepangwa na wapangamiji kama maeneo ya hifadhi ya barabara au maeneo ya miundombinu. Kwa hilo nakiri ni kosa wako watu wamefanya namna hiyo na sheria lazima ichukue mkondo wake kwa sababu ya kuwasaidia wao lakini kusaidia maendeleo ya miji yetu.

Mheshimiwa Spika, pia ni kweli kwamba kodi inakusanywa kwa sababu hawa watu lazima walipe kodi, kuishi kwao kule wanatumia rasilimali za Halmashauri husika, kwa hiyo halmashauri zile zinapaswa kuwatoza kodi katika maeneo yale kwa sababu na wenyewe wanatumia rasilimali na infrastructure zilizoko kule lazima wachangie, Hilo linafanyika na ni kweli lazima watoe kodi, lakini ujenzi katika maeneo hayo hairuhusiwi. Kwa hiyo huwezi kujenga tu eti kwa sababu unataka kukaa mabondeni halafu usitozwe kodi kama wanavyotozwa Watanzania wengine. Ni kweli kodi za majengo zitatozwa na kodi mbalimbali za halmashauri wanazotoza raia wengine zitazozwa, lakini hiyo haihalalishi kwamba wewe hapo umekaa kihalali. Lolote likitokea linaweza likatokea kama wapangaji na halmashauri husika wakiamua kuchukua hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, la pili vibali vya ujenzi zamani vilikuwa vinatolewa zamani vilikuwa vinatolewa na Kamati ya Mipangomiji ya Madiwani lakini sasa utaratibu Serikali ya Awamu ya Tano imebadilisha kwa sababu ilikuwa inachelewesha sana na ilikuwa inachukua gharama kubwa sana, inamaliza hela nyingi kwa ajili ya posho ya vikao na kila kitu. Sasa hivi iko timu ya wataalam tu wa Serikali ambao ndiyo wanatoa vibali vya ujenzi na tumesema vibali visichukue zaidi ya siku tatu viwe vimeshatoka, kwa sababu watu wako pale wana uwezo wa kwenda kufanya ukaguzi na ni wataalam waliobobea katika kazi hiyo na vibali vya ujenzi lazima zitolewe. Kwa hiyo vibali sasa vinatolewa kwa kasi na hii imesababisha kupunguza hata gharama kwa wananchi za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ni kweli kwamba siku za nyuma ilionekana kwamba watu waliweza kutoa vibali hata kwa watu ambao wametakiwa kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa. Serikali kwa wakati tofauti imechukua hatua kali na wengine wameachishwa kazi kwa wale ambao wametoa vibali katika maeneo ambayo hayastahili. Kwa hiyo Serikali imekuwa inachukua hatua za kinidhamu mara kwa mara, lakini nataka kumhakikishia katika Awamu hii ya Tano hilo halifanyiki. Awamu ya Tano imejenga nidhamu tofauti, watu ni wale wale lakini nidhamu yao imekuwa tofauti, hawatoi vibali tena hovyo hovyo na hawatatoa tena vibali katika maeneo ambayo ni hatarishi.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la makazi holela sehemu nyingi linasababishwa na kukosa wataalam wa kupanga, kupima na hatimaye kutoa hati. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe hatuna Afisa Ardhi wala hatuna Afisa Mpima, tuliyenaye pale ni afisa tu ni kama technician. Je ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Njombe itapata Afisa Ardhi ili aweze kutusaidia katika kupanga na kupima na baadaye kutoa hati? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu Mbunge wa Njombe la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maswali haya bila shaka yananipunguzia muda wa kujadili kesho pengine utapungua utakuwa siku moja, maana ni haya haya ambayo nitasema kesho.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama ulivyosema mwenye tunao upungufu wa Maafisa Ardhi na katika speech yangu nimetoa uwiano ikama inasema nini lakini tulionao ni wangapi. Nataka kukuhakikishia zoezi hili litapunguza makali kidogo mwezi wa Saba ambapo Wizara yangu sasa itaanza kupanga upya hawa maafisa, wanahamishwa na kupangwa na Wizara yangu, kwa sababu tumegundua siyo kwamba ikama ilikuwa inasababisha lakini upangaji ulikuwa hauzingatii mahitaji. Ukienda Mkoa wa Mwanza kwa mfano Wilaya za Nyamagana na Ilemela unakuta kuna Maafisa Ardhi themanini lakini Njombe hakuna hata mtu mmoja. Kwa sababu tatizo ni kwamba wale wapangaji pengine pale walipokuwa wanasimamiwa hawakuwa na fani zinazofanana nao, kwa hiyo walikuwa hawajui fani gani ipangwe namna gani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka niwahakikishie Wabunge wote mwezi wa Saba tutawapanga hawa hawa wachache, lakini tutajitahidi angalau kila wilaya iwe na afisa angalau wa taaluma moja ya ardhi aweze kuwepo. Nazijua baadhi ya wilaya ambazo hazina hata mtu mmoja wa sekta nzima ya ardhi ambayo ina vitengo vitano, hawawezi kufanya shughuli.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi lako tutalitekeleza mwezi wa Saba na la Waheshimiwa Wabunge, tutawapanga upya na Njombe, tatizo la Njombe Afisa Ardhi alikuwa mtendaji mzuri sana nimempandisha cheo amekuwa Kamishna Msaidizi. Kwa hiyo nitampelekea mtu mwingine baada ya hapo na Waheshimiwa Wabunge wote wenye swali kama hili watusubiri mwezi wa Saba Mungu akipenda tumeamua kuwapanga upya, nitawaita hapa kwanza niwaelekeze lakini tutawapanga upya ili angalau kila wilaya tuwe na afisa anayeweza kufanya kazi fulani.
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi tunajua moja ya Serikali kuwa na mikakati ya mipango bora ya ardhi ni pamoja na kuzuia watu kujenga mabondeni na pamoja kwenye mikondo ya mito na Serikali ilianzisha operesheni ya kubomoa nyumba za watu ambao wamejenga kwenye mikondo ya mito na hili ni tangu Bunge lililopita Mheshimiwa Lukuvi nadhani analijua na amebomoa nyumba nyingi tu kule Kawe lakini kuna nyumba ya kigogo mmoja tu ameiacha na wamekuwa wakitoa ahadi humu ndani hiyo nyumba itabomolewa. Nataka kujua ni lini ile nyumba itabomolewa?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inachukua hatua za mara kwa mara na nikisema Serikali maana yake kwa umoja wetu na wasimamizi wa sheria zote za mipangomiji ni mamlaka ya upangaji ambayo ni halmashauri yenyewe. Ukisikia operesheni ya vunja vunja au kuondoa watu waliojenga kinyume cha sheria katika halmashauri fulani, ujue inaendeshwa na halmashauri ambayo ndiyo yenye mamlaka na hata ile enviction order ya kwenda kuwavunjia haitolewi na Wizara yangu, hapana inatolewa na Afisa Ujenzi wa Wilaya. Kwa hiyo mazoezi haya yamekuwa yanafanyika katika wilaya mbalimbali ili kuwaondoa watu ambao wamevunja sheria naamini ni kweli katika wilaya mbalimbali ikiwepo Dar es Salaam Kinondoni operesheni kama hizo zimeendeshwa kwenye bonde la Msimbazi kwa watu ambao wamevunja sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachoomba tu ni kwamba wananchi wazingatie sheria. Wasijenge bila vibali, wahakikishe kwamba kila wanapojenga wanajenga maeneo ambayo siyo hatarishi, wanafuata sheria ili angalau hatua kama hizi zinazozungumzwa na Mheshimiwa Mbunge zisiwapate. Hilo ndilo ombi langu.
MHE. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa nilipofika ofisini kwa Mheshimiwa Waziri akaniambia kwamba Meko tayari amepima viwanja 840 na akanijulisha kwamba amepima viwanja 4,000 Basihaya. Sasa kwa kuwa Chasimba, Chachui Chatembo na Kasangwe Burumawe, Kissanga na maeneo mengine ni maeneo ya Jimbo la Kawe na yaligubikwa na migogoro ya ardhi, sasa ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakwenda pamoja nami, Mbunge wa Kawe ili tukamalize migogoro iliyodumu kwa muda mrefu? (Kicheko)
WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo amempa Mheshimiwa Njau. Pili nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima, mimi Askofu Gwajima nilikuwa simjui lakini amenitafuta kwa shughuli hizi za kero za wananchi wa Kawe hata kabla hajawa Mbunge, ilinilazimu kutoka kwenye kampeni, kuacha kampeni zangu Isimani kwenda kumsikiliza Dar es Salaam kwa sababu ya hiki. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Gwajima….

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mimi najua angeuliza Mheshimiwa Halima ningemjibu, ninyi siwajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Gwajima tukimaliza Bunge hili, nimepanga ratiba ya kwenda kukamilisha kero za migogoro ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatatua tatizo la Chasimba, Chatembo, Chachui kwa sababu mimi nilifanya kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwaonea huruma wale wananchi waliokuwa wafukuzwe. Kwa hiyo tutakwenda pamoja tutakwenda Basihaya, tutakwenda Chasimba na wananchi wanaoishi huko wajue kwamba nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge Askofu Gwajima kuhakikisha kwamba jambo hili la kero za wananchi kule sasa linaisha. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza, nitakuwa tu na swali moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa za Benki ya Dunia za Easy Way of Doing Business moja wapo ya kikwazo kwa wawekezaji ni uchelewaji wa kupatikana hati kwa wakati na utaratibu uliopo ni kwamba ile Kamati ya Kugawa Ardhi ya Kitaifa inakaa mara nne tu kwa mwaka. Je, Serikali ipo tayari kurahisisha walau hiyo Kamati ikakaa hata kila mwezi ili wawekezaji wapate hati kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa niaba ya Wizara hiyo, ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kanuni zilikuwa zinataka Kamati hii ikutane mara nne kwa mwaka na ndivyo walivyokuwa wanafanya lakini kutokana na ripoti hiyo na outcry ya wawekezaji na umuhimu wa kuharakisha uwekezaji, kwa sababu Kamati hii inaundwa na mimi, nimeelekeza sasa Kamati hii ikutane kila mwezi badala ya miezi minne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuanzia Awamu hii ya Sita wameshaanza kukutana mara moja kila mwezi na mwezi uliopita wamekutana kila wiki na ndio maana imewezesha katika maombi 174 yaliyowasilishwa katika Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Samia, tayari maombi 173 yameshapata vibali na yameshaandikiwa hati za uwekezaji na tayari zimeshakabidhiwa kwa EPZA na TIC kwa ajili ya utekelezaji. (Makofi)
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, tatizo la Pori la Hifadhi la Akiba la Mkungunero ni tatizo kubwa ambalo limegharimu maisha wa wananchi wetu limegharimu maisha hata ya wanyama pori wenyewe.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kondoa wangependa kujua ni lini ripoti ya Mawaziri ambayo ilikuwa ni taarifa ni timu iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ikaenda timu ya Mawaziri nane kwenda kufanya kazi na kuzunguka kwenye mapori yote likiwepo Pori la Hifadhi ya Mkungunero. Sasa ni lini ripoti ile itatolewa kwa wananchi na mipaka ikajulikana ili matatizo ambayo wananchi wameyaishi kwa miaka 50 na zaidi yaweze kufika mwisho sasa? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili nilisaidia kuchangia na nikasema kwamba tumekubaliana tutapita kwenye maeneo haya yote ya migogoro ili kuhakiki kwa pamoja kwa kutumia idara inayohusika na upimaji wa ramani ambayo ipo chini ya Wizara yangu, kwenda kuhakiki maeneo yote haya yenye migogoro ili tuweze kuchukua hatua. (Makofi)

Lakini nataka kumpa taarifa katika eneo hilo la Mkungunero timu ya Wizara yangu ipo huko wiki hii, kwa maombi ya Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, lengo ni kwenda kuhakiki mipaka ya Mkungunero kulinganisha na GN iliyoanzisha pori na ndicho kilichoombwa na Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, kwamba yeye hapingi pori, lakini anataka kujua ana mashaka pori lina mipaka tofauti na ile ya GN kwa hiyo timu ya wataalam wa Wizara yangu na Wizara ya Maliasili wako Mkungunero hivi sasa kwenye pori hilo hilo wanafanya hiyo kazi ya uhakiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini juu ya matokeo ya ile timu ambayo iliagizwa na Serikali tulikuwa tumeshasema hapa kwamba tuliomba fedha mwaka huu na tumepewa kwenye bajeti hii, tunakwenda sasa kuwajulisha na Wakuu wa Mikoa wanajua.

Mheshimiwa Spika, lakini tunakwenda kutelekeza sasa uamuzi wa Baraza la Mawaziri yale maeneo ambayo wananchi wameachiwa tutakwenda kuwaonesha na yale maeneo ambayo yanaondoshwa ndani ya hifadhi tutakwenda kuwaonesha na yale maeneo ambayo yanakaa ndani ya hifadhi tutawaonesha na tutaweka mipaka inayoonekana.

Kwa hiyo shughuli hiyo hatujaifanya katika maeneo yale lakini mwaka huu Wizara ya Maliasili na ya kwangu tumepewa fedha tunakwenda kufanya kazi hiyo rasmi baada ya bajeti hii. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ndiyo Mamlaka za Upangaji: ni lini Wizara ya Ardhi itakabidhi viwanja vya mradi wa viwanja 20,000 kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ili kuyapangia matumizi mengine maeneo yote ya Taasisi ambayo hayakuendelezwa katika Kata ya Tuangoma na Kibada hasa katika Kiwanja kilichopo Goroka Block D, Block 10 Kiwanja Na. 219, Changanyikeni Block 9 Kiwanja Na. 215, mashamba pori ya NSSF ya Mtaa wa Masuliza, Mwapemba, Vikunai na Changanyikeni? (Makofi)

Swali la pili: Je, ni lini Wizara ya Ardhi itaweka miundombinu ya barabara katika mradi wa viwanja 20,000 katika maeneo yote ya Kata ya Tuangoma. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula, nataka tu niwaeleze Waheshimiwa Wabunge, alichosema Mheshimiwa Chaurembo ni kweli kwamba kwa mujibu wa Sheria Mamlaka za Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri. Kwa hiyo, sisi kama Madiwani ni sehemu ya Mamlaka ya Upangaji wa Ardhi. Kila Halmashauri inapanga yenyewe matumizi ya ardhi yake. Ingawa tunashirikiana katika kuthibitisha ule upangaji, lazima uthibitishwe na Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam kuna mradi ulianzishwa miaka ya nyuma ya viwanja 20,000. Sasa leo nataka niseme hapa mbele ya Mheshimiwa Mbunge, viwanja 20,000 vilivyopimwa katika Wilaya ya Temeke, kwa mfano hivi vya Tuangoma iliyokuwa miradi 20,000 na Kibada, nimeshaagiza na ninarudia tena kuagiza, Wizara ya Ardhi ikabidhi michoro ya viwanja hivi 20,000 kwa Manispaa ya Temeke na wiki hii lazima makabidhiano yafanyike ili wananchi na Wilaya ya Kigamboni waweze kusimamia ipasavyo miradi hii ya viwanja 20,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ulikuwa ni mradi ndani ya Wilaya ya Temeke, sasa michoro yote na taarifa zote za umiliki ziwe ni open space, maeneo ambayo hayajaendelezwa, Temeke liwe ni jukumu lao kufuatilia. Kama kuna watu hawajaendeleza Temeke ni Mamlaka halisi. Pekuweni tutoe notice kwa watu ambao hawajaendeleza tuchukue hatua mchukue ardhi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naagiza Kamishina wa Ardhi akabidhi michoro na taarifa zote. Kuanzia leo, eneo lote la Viwanja 20,000 la Kibada na Tuangoma lazima liwe chini ya Mamlaka ya Manispaa ya Temeke. Hayo mengine mtafanya wenyewe. (Makofi)
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Naomba niulize swali moja tu la nyongeza nalo ni hili lifuatalo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utekelezaji wa maamuzi wa maelekezo na kazi nzuri iliyofanywa na mawaziri hawa nane bado hayajafanyika, na kwa kuwa bado maelekezo yaliyotolewa wakati timu hiyo inaundwa kwamba wananchi waachwe maeneo yao wakiendelea na shughuli za maendeleo bado halijavunjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa je, ni kwa nini wananchi wa vijiji 11 wanavyozunguka pori la Akiba Mkungunero bado mifugo yao inakamatwa? Na wananchi bado wanapigwa na maaskari hawa wakiwa kwenye maeneo yao hayo. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ashantu na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Kaimu Naibu Waziri wa Maliasili nilitaka nimpe maelezo Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepata maelekezo maalum ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu, kwamba sasa tuunde timu kwenda kufanya uhakiki wa maeneo hayo kama Mkungunero ambalo anahangaika nalo na mimi nalijua sana. Na ilikuwa lazima Mheshimiwa Rais mwenyewe atoe idhini na maelekezo hayo na ametoa maelekezo ya huruma kabisa kwamba pamoja na maelekezo yale ya awali, lakini nendeni mkafanye uhakiki kabisa ili tuone namna ya kumaliza jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kumhakikishia timu ya watalaam itakuja Mkungunero mwezi wa kumi na maeneo mengine yenye migogoro kama hii kwa sababu inajulikana. Tumeagizwa tufanye kazi hiyo ya uhakiki ili kukomesha kabisa migogoro hii kwa kadri itakavyowezekana. Uamuzi umetolewa na Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutakuja kushirikiana pamoja na wewe na viongozi wengine na viongozi wa mkoa katika kuhakikisha mambo haya yanakwisha.

Mheshimiwa Spika, tunajua yapo mengi huyu ameuliza katika mengi mengine na wewe hata leo uliunda kamati fulani niende kule nimewaambia kidogo, lakini nataka kukuhakikishia kwamba haya maneno Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo maalumu.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa maelezo haya mazuri, lakini sasa wakati wananchi wanaendelea kusubiri hii kauli ya njema sana ya Mheshimiwa Rais. Nini kauli ya Serikali kwa maafisa hawa wanyamapori ambao wanaendelea kunyanyasa wananchi na kukamata mifugo yao kwa kipindi hiki?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, narudia tena kwamba Mheshimiwa Rais amesema kazi iendelee. Anatambua uamuzi uliotolewa na Awamu ya Tano na yeye amesisitiza kwamba wananchi wote waliopo kwenye maeneo yao wasiondolewe katika vile vijiji 920, uamuzi huo upo vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ametupa kazi ya ziada kwenda kufanya uhakiki wa hali halisi iliopo. Kwa hiyo, ningeomba na wananchi nao wasitumie vibaya uamuzi huu wa Serikali wakafiri kwamba basi wasiondolewe maana yake ni kujipanua wanavyotaka. Tafadhali wakae kama walivyokuwa ili kazi hii ya uhakiki ije iwatendee haki kwa sababu hii pande mbili kuna upande huo wa wananchi, lakini upande wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuna wananchi wengine tulivyotoka na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kule Katavi, baada ya kutoa tamko lile pale watu waliingia kwenye Msitu wa Mbuga ya Katavi. Kwa hiyo, na wananchi nao wasubiri nia njema ya Rais wa Awamu ya Sita ni kutenda haki. Tufanye uhakiki kama alivyoagiza halafu uamuzi utatolewa.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, jambo hilo litatekelezwa, lakini wakati huo huo kazi iendelee maana yake uamuzi ule, ule uliotolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita amerudia maagizo yale yale kwamba nataka wananchi wote waliopo kwenye vile vijiji 920 wasiondolewe. Kwa hiyo, nadhani hakuna mtu wa Serikali anayewaondoa watu katika maeneo yale. (Makofi)

SPIKA: Kwa muda mrefu Wabunge walikuwa wakisubiri taarifa ile ya mawaziri nane, tunajua ni taarifa ya Serikali sijui kama imefikia kiwango cha Wabunge kuweza kujua angalau kilichomo au bado ni...Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana leo asubuhi uliunda kamati mbili twende tukawasilishe ile taarifa, lakini nimewaomba rasmi kwamba jambo hilo ndilo ambalo Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo mwezi huu uliopita. Kwa hiyo, nikawaomba radhi kwamba kwa sasa hatuna jipya watusubiri kidogo kazi hii ya kwenda kufanya uhakiki wa kina wa leo kwa sababu maamuzi haya yametolewa miaka mitatu, lakini hali ya leo ni tofauti na yeye ni Rais wa Awamu wa Sita amemetutuma mwezi uliopita.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimewaomba radhi kwamba kwa leo hatutatoa hiyo taarifa, lakini itakapokamilika huu uhakiki wa uandani ambao kwa vyovyote vile tukipita mikoani tutawakuta na Waheshimiwa Wabunge huko baada ya kukamilika hiyo kazi na Mheshimiwa Rais akitolea maamuzi tutakuja kuileta taarifa hiyo.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nataka kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa miaka mitatu, minne iliyopita mawaziri nane hawa walipewa kazi ya kupita huko wilayani na vijijini kwa ajili ya kuhakiki mipaka na matatizo mengine kama hayo. Lakini baadhi ya wilaya kama Wilaya ya Songwe ilikuwa bado wakati huo ni wilaya mpya hatukufikiwa na timu ile na wale watalaamu na sasa hivi ukimuambia Mheshimiwa Waziri anasema kwamba tena wameambiwa waende wakahakiki, lakini najua tunaweza tukasahaulika tena na anasema watapita huko na wataona na Wabunge, lakini Wabunge wanaweza wasiwepo wakati huo.

Mheshimiwa Spika, kwa nini siku nne ambazo zimebaki hapa tusipewe kazi Wabunge tuorodheshe vile vijiji ambavyo vina matatizo ya mipaka na mambo mengine ili angalau tumpe Waziri atakapokuwa anakwenda huko awe tayari na feedback ya Wabunge? Ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mulugo.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka tulipoanza Bunge hili, nilileta maombi kwa Katibu wa Bunge kuuliza swali hili kwa Mheshimiwa Mbunge yeyote ambaye anakero yake atuandikie, walioandika, wameandika. Nakupa ruksa Mheshimiwa Mulugo kama unayo nikabidhi tu, sisi tunapenda kuwa na hiyo directory ya migogoro hii ili itusaidie.

Mheshimiwa Spika, lakini hata utaratibu utakaokwenda tukienda mikoani tutakutana na viongozi wote kwa ujumla ili watuambie haya kwa sababu siyo kweli kwamba kamati hii ya watu nane ilipita kila mahali hapana. Tulienda maeneo machache, lakini tuli-take stop taarifa mbalimbali ya kamati mbalimbali ikiwemo Kamati ya Bunge mbalimbali zilizoundwa humu. Zilikuwa na taarifa nyingi sana ndiyo tumetumia zile taarifa kuchambua juu ya migogoro mbalimbali iliyopo, siyo kwamba sisi ndiyo tumegundua migogoro ilikuwepo katika nyaraka na tume mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanafikiri wanazo taarifa za ziada, ambazo wanafikiri tungependa kuzijua, ruksa tupo hapa tupatieni tu sisi tutaweka kwenye rekodi yetu siyo lazima iwe sisi kuna taarifa nyingine kama hizo za mipaka ya vijiji na vijiji siyo lazima sisi. Mamlaka zipo kule tutawaelekeza watafanya tu. Kwa hiyo, ni fursa kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wowote kutupa hiyo kazi. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la mwisho.

Mheshimiwa Spika, miaka mitatu iliyopita ni kweli iliundwa timu ya mawaziri wanane na walizunguka kwenye wilaya baadhi ya wilaya na wilaya nyingi. Lakini, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ziara ile ya mawaziri imekuwa kama ni ya kificho ficho, yaani tunawasikia tu, walipita, walipita, yaani sehemu hata ambazo hazina umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa na sisi ndiyo tunaolalamikiwa kila siku tunakuja kuuliza haya maswali. Kwa nini Serikali au Waziri asiweke mpango mzuri, timu inapoenda kwa mfano Wilaya ya Geita tujulishwe Wabunge na sisi tushiriki kwenye kuonyesha ile mipaka ili kuondoa ile sintofahamu. Ni hayo tu. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Musukuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, timu yetu ilikuwa na hadidu za rejea, haikuwa kutembea tu, na kuchunguza kila kitu, tulikuwa tumepewa hadidu za rejea na mambo fulani za kushughulikia, ilikuwa ni migogoro maalumu yenye mwiingiliano kati ya hifadhi na wananchi na vijiji, kulikuwa na migogoro hiyo maalumu.

Mheshimiwa Spika, lakini katika kufanya kazi hii nimesema hatukupita kila mahali kwa sababu tulikuwa tayari tuna taarifa, moja ya taarifa kubwa tuliyokuwa nayo ilikuwa migogoro ya wafugaji na wakulima ambayo ilikuwa ni Tume ya Bunge iliundwa hapa na Bunge lako Tukufu nayo tulitumia na tume nyingi nyingi na taarifa mbalimbali. Lakini tukawa tunataka kujiridhisha juu ya yale yaliyoandikwa kwa hiyo tulienda sehemu chache sana.

Mheshimiwa Spika, tunajua nchi hii kuna migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji ambayo si ngumu sana kusuluhisha. Tumeagiza sana viongozi wa mikoa na wilaya kwa sababu mwenye mamlaka ya kuunda maeneo ya utawala ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna kijiji kilichoanzishwa wala wilaya wala mkoa ambayo mipaka yake haikuandikwa kwenye GN ni suala la kwenda kusoma GN kwenye uwanda na kuamua mpaka upo wapi kwa sababu hawatakiwi kuunda mipaka ya utawala, mipaka ya utawala imeshaandikwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ipo migogoro mingi inayoendelea vijiji na vijiji kata kwa kata, sijui tarafa kwa tarafa ni uzembe tu. Tukishirikiana migogoro hii itaisha kwa sababu ina maandishi yake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Musukuma nataka kukuomba kama kuna mgogoro wa mpaka wa wilaya usisubiri ile tume, tuambie hizo ndiyo kazi zetu za kila siku.

Mheshimiwa Spika. kwa hiyo, tutenganishe kati ya ile kazi ya Tume na shughuli zetu za migogoro kila siku, shughuli kama kuna migogoro mingine mliyonayo Waheshimiwa Wabunge tupeni hizo ndiyo kazi zetu, wizara yangu inatatua migogoro kila siku, kama kuna mtu unamgogoro usisubiri Kamati ya Mawaziri msife na hiyo migogoro tupeni tuifanyie kazi hata sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutatuma wataalamu, tunavyo vifaa vya kutosha na wizara yangu hivi sasa imeanzisha Ofisi za Ardhi kila mkoa, kuna ma-surveyor kuna kila mtu, tutakuja kuainisha mipaka. Na katika kuahinisha mipaka Mheshimiwa Musukuma ndiyo tunavyofanya tunachukua viongozi wa pande mbili zote wanaobishania mipaka tunaamua kwa pamoja hatuendi sisi peke yetu, na ndiyo maana hata hii ya uhakiki wa Maliasili ipo mipaka iliyowekwa kwenye Hifadhi na Maliasili.

Mheshimiwa Spika, lakini tunataka tuunde timu maalumu ambayo wananchi na majirani pale na viongozi watahusika katika kuhakiki mipaka ya hifadhi ili waridhike kwamba mipaka hiyo inafanana kabisa na ile mipaka iliyoandikwa kwenye GN za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi hiyo tupeni tuifanye msisubiri kamati ya watu wa nane ni kazi yetu ya kila siku.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Shamba la Balali lenye ekari 2,000? Kwa sasa shamba lile yapata takribani miaka 20 Balali hajaliendeleza na wananchi wamekuwa wakilima humo. Ni lini sasa Serikali itafuta hati ya Balali na umiliki ule kupewa wananchi wa Jimbo la Mlimba, Kata ya Chita, pale Melela?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Shamba la Kambenga? Ahsante.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba marehemu Balali alikuwa anamiliki, sasa hivi msimamizi wa mirathi ambaye ni mke wake anamiliki shamba hilo alilolisema na nafahamu kwamba halijaendelezwa. Hata hivyo, Serikali ilifanya jitihada za kumtafuta yule mwekezaji na kumpa notisi, akajieleza, lakini bado tulichukua hatua ya kutaka kuchukua sehemu ya shamba hilo ili wananchi waweze kunufaika na yeye kumpa mpango wa muda mfupi aweze kuliendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya wakati wa kupima hilo shamba wananchi hawakuelezwa vizuri, walifikiri wale wapimaji wanakwenda kumsaidia yule mwenye shamba wakachoma vifaa na magari yaliyokuwa yanatumika kwa kazi ile ya Wilaya ya Kilombero, ni bahati mbaya sana. Kwa hiyo tunachukua hatua nyingine, nimeelekeza kule kwamba sasa tutapeleka notisi ya kumwomba huyu mwenye shamba ajieleze, lakini pia tunafikiria namna ya mwenye shamba kuweza kulipa fidia ya vifaa na mali zilizopotea katika kutekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili jambo nalifahamu vizuri na nikiwa nje nitamweleza mengine ambayo yalisababisha hili, lakini kwa hapa itoshe tu kwamba Serikali inalitambua na tunachukua hatua juu ya shamba hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; Shamba la Kambenga lilikuwa na mgogoro na vijiji na bahati mbaya sana mkuu wa mkoa aliyepita aliunda timu. Wizara yangu ilitaka kuingilia lakini Mkuu aa Mkoa mpya aliyekuja ameniomba muda kidogo atafsiri ile taarifa ya Kamati aliyoiunda mwenzake. Baada ya taarifa hiyo tutaamua, nilishaamua kumpeleka Kamishna kule, lakini nilisitisha kidogo baada ya maombi ya Mkuu wa Mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yote haya mawili nayajua, yako ndani ya uwezo wa Wizara. Naomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kukumbushana tutayashughulikia haya yote mawili.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali ikiwemo afya pamoja na shule, yamekuwa yakivamiwa na watu ambao hawana nia njema: -

Serikali ina mpango gani maeneo haya yote ili yaweze kupimwa kuondoa hii adha ambayo imekuwa ikijitokeza? (Makofi)

Swali la pili; tunayo miji midogo kama Nkwenda, Nsingiro, Mrongo na Mabira. Maeneo haya yanakua kwa kasi: Serikali ina mpango gani wa kupima haya maeneo ili baadaye wasije wakaanza kuwavunjia wananchi nyumba zao? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Naomba nijibu mawali mawili ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli uvamizi ni mkubwa sana katika maeneo mbalimbali, lakini nilitaka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji, Mamlaka ya Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri za Wilaya. Maana yake ni kwamba ukipanga unapaswa kusimamia, wanaopanga master plan. Wanaopanga mipango flani flani ya utekeleaji wa master plan ndani ya sheria za nchi hii ni Halmashauri ndiyo wanaohitaji na ndiyo wanaojua kwamba ardhi yao itumike namna gani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwa Halmashauri zote, zisimamie na zilinde maeneo kama yalivyopangwa na mamlaka zao. Maeneo yote ya wazi hayapaswi kutumika kwa shughuli nyingine na nimeelekeza wenzangu kwamba maeneo yote ya Umma kama yanaangukia kwenye sekta fulani, basi sekta hiyo iyalinde, ichukue hati na iweke mipaka inayoonekana/alama zinazoonekana, kama ni maeneo ya shule wayalinde wachukue hati, nasi tulisema hatutawadai kodi ya ardhi ya kila mwaka. Kama ni maeneo ya afya, basi yalindwe, yapimwe yachukuliwe hati na yawekewe alama zinazonekana ili wananchi waweze kujua. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuyalinda.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kweli kutokana na ustaarabu na utekelezaji ulio mzuri wa sera za CCM na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, leo tuna umeme kila kijiji. Umeme unaleta ustaarabu na unabadilisha maisha. Kwa hiyo, imetokea kwamba baadhi ya vijiji vingi sasa vimeanza tabia ya kimji. Sheria inaelekeza kwamba maeneo hayo, Halmashauri myawahi mapema. Maeneo ambayo mnajua yameanza kuchipukia na maisha yanakuwa ya kimji, pelekeni na mjadili kwanza muainishe maeneo hayo hata kama ni ya vijiji, mpelekeeni Waziri wa Ardhi ayatangaze kama town planning areas ili maeneo hayo ya vijiji yanayochipukia kuwa na maisha ya kimji, Waziri ayatangaze ili yapangwe kimji na Halmashauri zipime na watu wapewe viwanja na hati kama za mjini. Kwa namna hiyo tunaweza tukalinda, baadaye kukawa hakuna squatter katika mji yetu. Kwa hiyo, ni jukumu letu Mheshimiwa Mbunge Halmashauri na sisi kama Wajumbe tusimamie katika kupanga na kusimamia ardhi yetu.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, mimi naomba nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza siyo peke yake mgogoro huu umekuwepo nyakati za kiangazi mgogoro huu umekuwepo nyakati zote masika na kiangazi na sasa hivi tunapozungumza habari za shughuli za kilimo maana yake zinapoenda kutekelezwa na wananchi wa maeneo haya kipindi hiki pia mgogoro huu unaweza ukaibuka. Kwa hiyo siyo sahihi kwamba ni nyakati za kiangazi peke yake na hata masika kwa sababu shughuli za kibinadamu zinafanyika nyakati zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgogoro huu umekuwa ukichangia sehemu kubwa sana uvunjifu wa amani wa wananchi wetu nataka nipate commitment ya kutosha ya Serikali kwamba ni lini sasa watakwenda kutatua mgogoro huu ikiwa ni pamoja na kuijumlisha Wizara ya Ardhi kuhakikisha wanaenda kuainisha na kuweka beacon ili mipaka ya maeneo ya kiutawala yaweze kuainishwa sawasawa. (Makofi)

Swali la pili Wizara ya Ardhi mwaka 2019 walifika katika eneo hili la mgogoro na kwa bahati mbaya kwa sababu walifika nyakati za masika maji yalikuwa yametapakaa katika maeneo hayo ya mipaka na kwa hali hiyo walishindwa kufanya suala zima la kuainisha lakini pia na kuweka beacon na waliahidi wangeweza kutekeleza na kuumaliza mgogoro huu uliokuwepo katika maeneo haya ya Iramba na Kishapu.

Je, ni lini Wizara ya Ardhi watafika na kuhakikisha wanaweka beacon kuainisha maeneo ya kiutawala lakini na kuweka beacon ili mgogoro huu sasa usiendelee na wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI naomba nichangie kidogo nyongeza ya swali hili, nafikiri nilikutana na huyu Mheshimiwa Mbunge nalijua hili tatizo lakini mimi sijawahi kushiriki vizuri, lakini niliwaahidi kwamba tungeweza tukakutana na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI tukazungumza kwanza kiutawala kati ya Wakuu wa Mikoa hawa wawili lakini mimi Wizara yangu kazi ya kutafsiri mipaka ndiyo kazi yake kwa GN zilizoandikwa.

Mheshimiwa Spika, hivyo nataka kumuahidi Mheshimiwa Mbunge nitalisimamia mwenyewe hilo la kuweka mipaka ili wananchi wa Wilaya hizi waweze kujua mipaka yao iliyoainishwa na mwenye mamlaka kwa sababu mamlaka ya kugawa mipaka ya utawala ni ya Mheshimiwa Rais, sasa wakati mwingine huwa inatokea wananchi wanasema nilikuwa hapa nilikuwa hapa nawakumbusha tu mwenye mamlaka ya kugawa mipaka ya utawala ni Mheshimiwa Rais na mipaka hii huwa inaandikwa kwenye Kanuni zinaitwa GN na GN tunazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mbunge wananchi waambie Wizara yangu itakuja kutafsiri ardhini mipaka iliyoainishwa kama nia ya Mheshimiwa Rais ya kupanga na kuunda hizo Wilaya mipaka ya ardhini itakuja kuainishwa na kutafsiriwa na Wizara yangu na jambo hili litafanyika mara moja. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na majibu mazuri sana kutoka kwa Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Jambo la kwanza jambo hili limekuwa ni la muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri atakuwa shahidi wa jambo hilo pamoja na ahadi hii nzuri ulioitoa Mheshimiwa Waziri ningependa kujua uko tayari baada ya Bunge hili uongozane na mimi kwenda kuzungumza na wananchi wa Hale uwape matumaini ya kuharakisha jambo hili ili wapate ardhi kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kilimo?

Mheshimiwa Spika, Swali la pili Wilaya ya Korogwe sehemu kubwa ya ardhi yake ni mashamba makubwa ya wawekezaji wa chai na wawekezaji wa mkonge na maendelezo yake hayaridhishi sana na jambo hili limefanya wananchi wetu kukosa maeneo ya kufanya shughuli za kilimo hasa vijana wamekosa maeneo ya kujiajiri. Je, Serikali iko tayari kukaa pamoja na wawekezaji hawa pamoja na umuhimu wa uwekezaji wao kwenye maeneo haya lakini tufanye mazungumzo ya kuona namna gani ya kumega maeneo kwa ajili ya kuwapa vijiji ili wananchi wapate sehemu ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo suala la kilimo? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mnzava Mbunge kijana machachari wa Korogwe kama ifuatavyo: -

Kuhusu swali la kwanza, kwenda anauzoefu anajua akiniita naenda tulishaenda na nitakuja na huko na nitafanya yale ambayo tulifanya sehemu nyingine ambazo ulinipeleka. Kwa hiyo, wananchi wasiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mnzava akinihitaji kwangu mimi ni agizo nakwenda tu na Waheshimiwa Wabunge wote kama kuna matatizo kama haya mkiniambia ndiyo inanisaidia kupata kazi maana mkinituma ndiyo napata uhalali wa kuja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mnzava nakuja. (Makofi)

Swali lake la pili; ni kweli una mashamba mengi na ni kweli kwamba kwenye mashamba mengi najua wakati ule wenye mashamba wanapomiliki hasa Kanda hii ya Kaskazini wananchi walikuwa wachache sasa wananchi wameongezeka sana. Kwa hiyo nataka ukitoka hapa muulize Mheshimiwa Mbunge wa Same hapa Mama Kilango akufundishe namna alivyofanya na mpaka na mimi nikaenda kule na moja ya shamba wananchi wakarudishiwa ekari 300. Kwa hiyo uwezekano huo upo kwa sababu mifano tunayo tutakaa na wenye mashamba wanajua kabisa wanataka kuishi vizuri na majirani wao, hawakatai.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge aniorodheshee hao wenye mashamba ni watu gani halafu tupange ratiba tuzungumze nao wanajua hali halisi na wenyewe wanataka kuishi vizuri na wananchi wanaowazunguka kwa hiyo hilo tutafanya, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilipenda kujua tu kwamba Waziri anayezungumza hapa ndiyo mwenye mamlaka ya kugawa mipaka ilivyo kati ya wananchi na wanyamapori. Sasa nimuombe Mheshimiwa Lukuvi mpaka wa vijiji kama 11 hivi vya Jimbo la Bunda ukianzia mipaka ile ya Honyali, Maliwanda ukienda Mgeta mpaka Tingirima mpaka wao ni Mto Rubana ndiyo mto asili unaotumiwa na wananchi wa maeneo yale lakini mpaka uko katikati ya Mto Rubana. Ni lini Waziri ataenda pale kutenganisha mita 500 za wanyamapori na mita 500 za wananchi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Getere kwanza nitamuona hapa hapa anipe ufafanuzi vizuri zaidi lakini pia ninao uwezo wa kwenda Mkoa wa Mara kwenda kuzungumza nae na viongozi wengine ili tujue hilo kwa sababu hata vijiji huwa vinaanzishwa kwa mfumo ule ule unaofanywa na Wilaya na Mikoa.

Mapendekezo ya kuanzisha vijiji huwa yanaanzia Wilayani yanakuja mkoani mwishoni Ofisi ya Rais, TAMISEMI ndiyo inaidhinisha ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais na kutoa GN maandishi yanayoainisha kila Kijiji na mipaka yake iko namna gani. Jukumu langu mimi siyo kuanzisha mipaka ya vijiji vipya Wizara ya Ardhi hatuanzishi mipaka, tunasuluhisha lakini kwa kutafsiri ardhini GN za mipaka zilizoainishwa na mamlaka inayohusika.

Kwa sababu hiyo, nitakwenda huko kwenda kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo kuainisha mipaka iliyopendekezwa au iliyoamuliwa kuaanzisha vijiji hivyo kwa mujibu wa mapendekezo ya mamlaka. Lakini pia hiyo migogoro kati ya buffer zone na ardhi za vijiji nitapenda kumsikia lakini tutakwenda huko hivi karibuni tulikwenda Serengeti nako kulikuwa na migogoro ya buffer zone vijiji vilivyoanzishwa hifadhi ya Serikali ilichukua mita 500 za ardhi ya vijiji ikafanya buffer zone.

Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza ili kuondoa taharuki, ardhi ile ambayo Serengeti walichukua kuanzia Mkoa wa Mara kule Tarime mpaka Serengeti mita 500 kwenye ardhi za vijiji zirudishwe kwenye vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetekeleza maelekezo hayo mita 500, 500 zilizokuwa kwenye buffer zone ya Hifadhi ya Serengeti zimerudishwa kwenye vijiji na hivyo Serengeti sasa kama wanahitaji buffer zone watarudi ndani ya hifadhi yao. Lakini zile za vijiji zimerudishwa tayari, kwa hiyo hili nalo tutakwenda kujifunza nature ya mgogoro huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza, ili kuondoa taharuki, ardhi ile ambayo Serengeti walichukua kuanzia Mkoa wa Mara kule Tarime mpaka Serengeti, mita 500, kwenye ardhi za vijiji zirudishwe kwenye vijiji.

Mheshimiwa Spika, tumetekeleza maelekezo hayo, mita mia tano mia tano zilizokuwa kwenye buffer zone ya Hifadhi ya Serengeti zimerudishwa kwenye vijiji na hivyo, Serengeti sasa kama wanahitaji buffer zone watarudi ndani ya hifadhi yao, lakini zile za vijiji zimerudishwa tayari. Kwa hiyo, hili nalo tutakwenda kujifunza nature ya mgogoro huu.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi. Kwa sababu sehemu hizi mbili; Bendera na Mkomazi jambo kubwa wanalogombea ni mpaka kati ya Bendera na Mkomazi, ndiyo linapokuja suala la madini: Je, Serikali hamuoni ni muhimu sana Mkuu wa Mkoa akafika pale akaweka vizuri mpaka ule ili hili tatizo lililozungumzwa hapa ndani sasa hivi lisiendelee kutokea? Ahsante.

SPIKA: Haya tulikuwa na migogoro ya mipaka ya Wilaya kwa Wilaya, sasa huu mpaka wa Kata kwa Kata ambapo maana yake kuna vijiji na vijiji.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, ni mpaka wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mkoa wa Tanga, uko kati ya Bendera na Mkomazi.

SPIKA: Okay! Ni mipaka ya mikoa!

MHE. ANNE K. MALECELA: Ndiyo.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela. Kule kote ambako kuna migogoro ya tafsiri za mipaka sisi tunahusika. Kwa hiyo, hatutasita kwenda kutafsiri ardhini tafsiri ya mipaka iliyoainishwa na mwenye mamlaka. Tunazo GN, tutaifanya kazi hiyo. Nitaomba tu Mheshimiwa Kilango anipe maelezo ya ziada ili tuunde timu yetu ya pamoja ikafanye kazi hiyo. Hiyo ndiyo kazi yetu ya kutafsiri GN zilizoainisha mipaka na mwenye mamlaka. (Makofi)