Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juma Ali Juma (2 total)

MHE. JUMA ALI JUMA aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi na wananchi wa Kisakasaka hali inayoleta wasiwasi kwa wananchi.
(a) Je, ni lini Serikali itaupatia ufumbuzi mgogoro huo?
(b) Je, kwa nini Serikali isiwaruhusu wananchi hao kuendelea na shughuli za kilimo na mifugo wakati wakisubiri ufumbuzi wa tatizo hilo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Ali Juma, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, inatambua uwepo wa mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi na Wananchi katika eneo la Kisakasaka. Katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huu, Makao Makuu ya Jeshi iliridhia kurekebisha mpaka wa Kambi ya Kisakasaka ili kuwaachia wananchi eneo lenye mgogoro na hivyo kuleta suluhisho la kudumu kwenye mgogoro huo. Zoezi hilo halijafanyika kutokana na ufinyu wa bajeti, hata hivyo katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 tunategemea kutekeleza zoezi hili.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa napenda kuwasihi wananchi wawe wastahimilivu wakati Serikali inachukua hatua stahiki ili kuzuia madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wananchi endapo wataendelea na shughuli za kilimo na mifugo katika eneo hilo.
MHE. JUMA ALI JUMA aliuliza:-

Serikali imezuia kutoa leseni kwa sababu ya ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na taasisi za utoaji leseni, hivyo kusababisha kupoteza mapato mengi ya Serikali na kuifanya Taasisi ya Uvuvi wa Bahari Kuu kushindwa kufanya kazi zake inavyotakiwa:-

(a) Je, ni lini Serikali itamaliza mchakato wa kujipanga na kuanza kutoa leseni?

(b) Je, Taasisi ya Uvuvi wa Bahari Kuu imesaidiwa kwa kiasi gani ili iweze kujiendesha kwa kipindi hicho ambacho haikupata mgao utokanao na leseni?
NAIBU WAZIRI WA M IFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Ali Juma, Mbunge wa Dimani, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilisimamisha utoaji wa leseni za uvuvi wa Bahari Kuu kuanzia tarehe 8 Agosti, 2016 mpaka Desemba, 2016 ili kuruhusu marekebisho ya Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu za mwaka 2009 yakiwemo maboresho ya masharti ya leseni yaliyopo katika kifungu cha 10 ya kanuni za mwaka 2009 na kanuni za kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali. Kufuatia marekebisho hayo, wamiliki wa meli zinazovua katika Bahari Kuu wamesita kukata leseni kutokana na kutokukubaliana na masharti mapya yaliyoongezwa katika Kanuni mpya za mwaka 2016.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 1998 na Marekebisho yake ya mwaka 2007, mamlaka hupatiwa asilimia 50 ya mapato yote yanayokusanywa kwa mwaka. Ni kutokana na bakaa (akiba) ya mgao huo mamlaka imeendelea kujiendesha na kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zipo kwenye hatua za mwisho kutatua changamoto ya meli za uvuvi kutokukata leseni na kuiwezesha mamlaka hii kujiendesha.