Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Anne Kilango Malecela (14 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza leo kwa sababu ni mara ya kwanza kuongea katika Bunge hili la Kumi na Moja, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtoa haki. Pili, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona, kwa kutambua mchango wangu na kunirejesha Bungeni. Namshukuru sana, namshukuru sana, namshukuru sana! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu nitachangia kitu kimoja tu. Nitachangia ukurasa wa 21 Kifungu cha 31 kuhusu kilimo. Hotuba yangu itakuwa ni ndefu, kwa hiyo, nusu nitaongea kwenye hotuba ya Waziri Mkuu sitamaliza, nusu nitaongea kwenye Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara ya Kilimo na nitaongea kitu kimoja kuhusu tangawizi. Leo naiongea tangawizi kwa mapana yake. Watu wanaweza wakajiuliza, hii tangawizi ni nini? Wengine hawaelewi tangawizi ni nini. Tangawizi ni zao la viungo (Spices), lakini tangawizi ni
malighafi ya kutengeneza dawa za binadamu, kutengeneza cosmetics, nikiwa na maana ya vipodozi, vinywaji na vitu vingine vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niigawe hii tangawizi katika mafungu matatu; kwanza nitaiongea tangawizi kiulimwengu, kwa Afrika na mwisho nitaiongea kwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, duniani hapa, ulimwenguni, nchi bora tano zinazoongoza kwa kulima tangawizi ya kwanza ni India, lakini India inaongoza kwa kulima tangawizi duniani na inayoongoza kwa kutumia tangawizi duniani. Nchi ya pili ni China; ya tatu ni Nepal; na ya nne ni Nigeria. Ni nchi ya Kiafrika hii na inalima tangawizi kweli na ina-export tangawizi kwa wingi mno.
Waheshimiwa Wabunge, kama mnasoma vitabu vya kilimo, utakuta kwamba Nigeria imekuwa inategemea zao la tangawizi kwa export mpaka ilipofika mwaka 1960 ndipo ilipogundua mafuta, ikawa mafuta yako juu kwa tangawizi. Sisi huku, nikisema tangawizi, watu wanasema, “huyu naye na tangawizi!” Tangawizi ni zao zuri sana na lina export nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya nne ni Nigeria kwa hiyo ni ya kwanza kwa Afrika. Nchi ya tano ni Thailand. Nisiishie hapo kwa upande wa ulimwengu, twendeni tuangalie nchi zinazo- export tangawizi kwa wingi. Sasa kwa sababu India inalima tangawizi kwa wingi, lakini anaiconsume yeye mwenyewe sana. Ameshindwa kuwa wa kwanza kwenye ku-export. Nchi ya kwanza inayo-export tangawizi kwa wingi ni China; ya pili inakuja kuwa India; ya tatu, watu hawataamini, Nigeria ni giant number three kwa ku-export tangawizi; ya nne inakuwa ni German na Netherland.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nirudi Afrika. Nilitaka kutoa picha ya tangawizi na ulimwengu kidogo tu. Twende Afrika sasa. Nigeria inaongoza kwa kulima tangawizi Afrika. Nigeria inajipambanua kwamba kwa nini inaongoza kulima tangawizi na ku-export? Inasema kwa nini inafanya hivyo? Kwa nini imeweza? Inasema ina ardhi kubwa sana yenye rutuba; inasema, ina mvua za kutosha na mito isiyokauka, lakini inasema ina hali ya hewa nzuri, ndiyo maana imeweza kuwa na comperative advantage upande wa tangawizi kuliko nchi zote za Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Nigeria imefika hapo, kwamba ina-export tangawizi inapeleka USA, Europe, Morocco na nchi nyingi tu. Kitu cha ajabu, yenyewe kama Taifa inakubali kwamba wakulima wakubwa wa tangawizi kwa Nigeria asilimia 40 ni wanawake. Wanawake wa Nigeria ndio walioshika mashamba makubwa ya tangawizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hali ya hewa ya Nigeria, nakubali ni nzuri; ardhi ya Nigeria, nakubali ni nzuri. Ile hali ya hewa ya Nigeria ambayo imeruhusu kulima tangawizi, ipo Tanzania! Ukisema mvua, Tanzania tuna mvua; ukizungumza mito isiyokauka; tunayo, twende tuone mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Mkoa wa Ruvuma kuna mvua ya kutosha; Mkoa wa Njombe una mvua ya kutosha; Mbeya ina mvua ya kutosha, Rukwa na kigoma; Tanzania haina maana kwamba hatuna sehemu zenye hali ya hewa nzuri, haina maana kwamba hatuna mito ya
kutosha, haina maana kwamba hatuna ardhi ya kutosha. Kwa nini wenzetu wamefanikiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Nigeria imethamini zao la tangawizi, imekwenda imesimama imara kwenye zao la Tangawizi, lakini kwetu sisi, Kipare tuna methali inasema, “Ng’ombe kuramoshe ukuhundue.” Ina maana Ng’ombe anajipeleka mwenyewe machungani, anajirudisha
mwenyewe. Wakulima wa Tanzania wanaolima tangawizi wako wenyewe. Serikali haijasimama imara ikalishika hili zao, ikatayarisha project maalum ya ku-study hili zao la tangawizi na ikasimama imara ikatafuta hili zao wapi tutalilima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwa na Tanzania ya viwanda kama hatutakuwa na kilimo bora, hatuwezi. Itakuwa tunasema, Tanzania ya viwanda, Tanzania ya viwanda! Ni lazima tukaboreshe kwanza kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nitaliongea miaka mitatu na nusu. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Jimbo langu sasa ni Tangawizi. Nitazunguka nchi nzima kuhakikisha naboresha kilimo cha Tanzania na nina uhakika Serikali mtaniunga mkono kila siku. Ofisi nitakayokwenda
kuiona mimi ni Ofisi ya Wizara ya Kilimo. Nitakwenda, nitashauri, nitapita, nitakwenda, nitarudi. Serikali naomba zao la tangawizi hebu tuliangalie, tukae, tuandike project, tutafute wenzetu wa Nigeria, twende tukai-visit Nigeria; siyo lazima mtulipie nauli, tutalipa wenyewe. Mimi nitakwenda Kaduna nikajue kwa nini Kaduna wanalima tangawizi kwa wingi? Nitafanya hiyo kazi. Hatuwezi kuzungumza suala la viwanda kwa nguvu, tutafika, lazima tujenge viwanda; kilimo kiko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze ukweli; zao la tangawizi ndugu zangu, ukiona Muhindi, ni very aggressive huku duniani; Mchina ni very aggressive; MNigeria ni very aggressive; kwa nini haya Mataifa matatu yanasimama kulima tangawizi? Wanajua faida yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo, naomba niishie nusu ya hotuba yangu. Wizara ya Kilimo, naendelea na zao la tangawizi na nitachangia kwa maandishi, nitamletea Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kabla sijamaliza, nirudi niseme naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Nilikuwa nje kwa mwaka mmoja na miezi kadhaa. Nilikuwa nawaangalia mnavyochacharika, Serikali mnafanya kazi sana, lakini naomba mwongeze nguvu kwenye kilimo cha Tanzania. Ni lazima tuondoke hapa tulipo. Tutaondoka tu kama tutakuwa na viwanda vya uhakika. Hilo linawezekana iwapo tutashirikiana wote tena tukitaka kujenga nchi vizuri, tushirikiane bila kujali itikadi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE.ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, hizi Wizara mbili ni muhimu sana hebu kila mtu atumie dakika kumi vizuri zaidi kuliko kuzipoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niseme mimi nimekuwepo Bungeni hapa tangu mwaka 2000. Suala nitakaloliongea leo nimeliongea tangu mwaka 2001, naongelea upande wa TAMISEMI. Wilaya ya Same ni kubwa sana katika Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro una
Wilaya saba lakini Wilaya ya Same ina ukubwa wa kilomita za mraba 5,152 ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Mkoa mzima wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Same hiyo ina majimbo mawili, Same Magharibi na Same Mashariki. Makao Makuu ya Wilaya yako Same Magharibi yako katika Kata ya Same ambayo ndiyo ya mwisho unakwenda Wilaya ya Mwanga. Jimbo la Same Mashariki liko mwishoni na Mkoa wa Tanga. Kata ya kwanza inaanza Bendera, Kiurio, Ndungu, Kalemawe, Maore hapa ni tambarare.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo linapojitokeza ni hapa. Tunapata tatizo kwamba Hospitali ya Wilaya ya Same iko, Kata ya Same ambako ni mbali sana na Jimbo la Same Mashariki. Kwa hiyo, athari kubwa inawakuta kina mama wajawazito, hili suala nimeliongelea kwa miaka 15. Kina mama wengi sana kutoka Jimbo la Same Mashariki wanapohitaji huduma ya upasuaji dakika za mwisho anataka kujifungua anagunduliwa kwamba upasuaji unahitajika ni lazima apelekwe Same, wengi sana wanapoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia 2010-2015 tumepoteza akina mama 18 na watoto wao. Hao ni wale waliofika Same. Waliopotezea maisha majumbani au kwenye zahanati sina takwimu za kusema.Watoto wachanga 28 wamepoteza maisha. Namshukuru sana Mheshimiwa Jafo alikuja Wilaya ya Same. Wabunge hatukuwa na habari tungekuja tukulalamikie kule kule, lakini mimi kwa sababu nimesema kwa miaka 15 naiomba sasa TAMISEMI ione umuhimu wa hapa Ndungu ndani ya Jimbo la Same Mashariki kwenye Makao Makuu ya Jimbo la Same Mashariki, kile kituo cha afya kipate huduma ya upasuaji. Inapokuja kuzungumzia akina mama nitapaza sauti mpaka dakika ya mwisho. Jimbo la Same Mashariki akina mama wanapoteza maisha sana kwa sababu ya kukosa huduma ya upasuaji. Kipare tunasema; “wekienda kutana na nashindaki taganyamaa.” Naomba nitafsiri, wewe kama umebeba nyama kichwani nzi watakufuata. Sasa kama unataka wale nzi wasikufuate hiyo nyama itupe. Hili suala ili nisilipigie makelele Serikali malizeni hili jambo, hamtanisikia tena nikisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapo nimetoka TAMISEMI nije Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Mimi nazungumzia Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Huu Mfuko wa Rais wa Kujitegemea umeanza takribani miaka 33 iliyopita.
Mimi nimeungalia vizuri Waheshimiwa Wabunge, huu mfuko unawasaidia akina mama na vijana wanapata mahali pa kukopea kwa ajali ya miradi midogo dogo ya kujiendeleza ili waweze kujitengemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku duniani, nizungumzie Tanzania na Afrika akina mama pamoja na vijana ni wazalishaji wakubwa sana na mjue akina mama ndiyo wanaoangalia vijana, sijui mmenielewa? Kwa hiyo, mama anacheza kotekote anazalisha na anaangalia vijana. Huu
Mfuko wa Rais wa Kujitegemea takribani miaka 33 sasa hivi lakini umeonyesha kufanya vizuri sana. Kwa sababu gani nasema hivyo Mwenyekiti? Inapokuja kwenye marejesho hawa wanarejesha asilimia mia moja hakuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nizungumze kwa unyenyekevu. Kwanza tuwapongeze wanaoratibu mfuko huu kwa sababu mahali popote ambapo kuna kukopa kurejesha kuna matatizo, lakini hawa wanarejesha asilimia 100 ina maana wanaoratibu mfuko huu
wanafanya kazi vizuri sana. Hata hivyo, kuna changamoto kwamba Serikali haiwapi pesa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo huu Mfuko wa Rais wa Kujitegemea inapokuja kwenye repayment ni 100% jamani kwa nini wasipewe fedha za kutosha? Kazi wanayoifanya inawasaidia akina mama na vijana kwa hiyo moja kwa moja inachangia kwenye uchumi. Naiomba Serikali
mfuko huu uangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hapo tu, tangu 33 iliyopita mfuko huu uko kwenye Mikoa mitano tu ya Dar es Salaam, Lindi, Njombe na mwingine wa tano mniwie radhi nimeusahau.
Ombi langu kwa unyenyekevu mkubwa, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi naomba unisikilize, kwa sababu marejesho ni 100% hebu sasa ongezeni mikoa mingine mitano. Katika hiyo mikoa mitano itakayoongezwa naomba Mkoa wa Kilimanjaro uwepo. Ukienda Same Magharibi akina mama wa Ruvu wanalima vitunguu wakipata mikopo watafanya kazi vizuri. Ukija Same Mashariki kuna akina mama wanaolima tangawizi na mpunga wakipata mikopo hiyo watafanya kazi vizuri zaidi. Naomba iongezwe mikoa mingine mitano na huu mfuko upewe pesa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kupata nafasi, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yangu nilianzia kwnye bajeti ya Waziri Mkuu nikatoa 50 percent, nikazungumzia suala la tangawizi ka ulimwengu, nikazungumzia suala la tangawizi kwa Afrika na nikasema nusu nitazungumzia suala la tangawizi kwa Tanzania na ninaanza hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakapozungumzia tangawizi Tanzania moja kwa moja utaigusa Wilaya ya Same, upande wa Mashariki mwa Wilaya ya Same ambao wao wenyewe katika nchi hii wanalima takribani asilimia 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna asilimia 40 iliyobaki, asilimia 40 sasa hivi inalimwa na Songea Vijijini ukienda Jimbo la Madaba wanalima tangawizi sana, ukienda Mkoa wa Kigoma wameanza kulima tangawizi sana kwa hiyo, ukiangalia vizuri Tanzania sasa hivi zao la tangawizi linakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuzungumzie safari ya maendeleo. Maendeleo ni safari ambayo ina misuko suko sana, hasa niongelee maendeleo yanayotupeleka kwenye viwanda na uchumi wa kati. Tusitegemee tufike kwenye viwanda, tufike kwenye uchumi wa kati kwa lele mama ni lazima tukutane na misukosuko mingi. Sasa mimi naomba niizungumzie hii hii tangawizi ya Same Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilianza kuwa Mbunge mwaka 2005 Same Mashariki, niliwakuta wananchi wanalima tangawizi. Mwaka 2007 mimi ndiyo nikaasisi wazo la kujenga Kiwanda cha Kusindika Tangawizi pale Same Masharuki. Tulianza kwa misukosuko mingi, lakini nakumbuka mwaka 2008 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alikuja akaweka jiwe la msingi, tukajenga, tukahangaika mimi na Halmashauri na wananchi wakati huo tulikuwa na wana ushirika 613, wao walichangia shilingi 6,000, mimi kama Mbunge pamoja na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne tulifanya fund raising tukapata shilingi milioni 301; Halmashauri ikachangia shilingi milioni 45, lakini na Serikali ikatujengea godown lenye thamani ya milioni 287 na safari ikafikia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nizungumze kitu ambacho kinanipa nguvu sana leo na ninaomba Waheshimiwa Wabunge mfurahi pamoja na mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais amekuja na kauli ya Tanzania ya viwanda, lakini Mheshimiwa Rais kazi anayofanya ni kuchochea na kuwavuta watu, kuivuta mifuko ya jamii iwekeze kwenye viwanda kwa sababu by principle Serikali haijengi viwanda, lakini ina-facilitate. Sasa nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na nashukuru kwamba yupo hapa. Leo nazungumza jambo ambalo limenifariji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani zangu za pili, tena hizi ni shukrani za unyenyekevu na moyo uliopondeka sana nipeleke kwa Bodi ya Wadhamini wa LAPF, nipeleke shukurani zangu za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu wa LAPF Ndugu Eliud Sanga kwa sababu LAPF imekubali kuingia ubia na kile kiwanda nilichokijenga miaka ile. Leo tunazungumza LAPF inakwenda Same Mashariki, inakwenda Miamba, inakwenda kuingiza zaidi ya shilingi bilioni moja kwenye kile kiwanda, sasa hapo unazungumzia ile ndoto niliyokuwa naiona kila siku. Nilikuwa natamani tupate kiwanda kama cha Kaduna, Nigeria kwasababu gani sasa mimi nimepata furaha? LAPF inadhania imefanya kitu kidogo, hapana, imefanya mambo matatu makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, LAPF kwa kuingia ubia na Kiwanda kile cha Same Mashariki cha Tangawizi cha Miamba inepanua kilimo cha tangawizi Tanzania kwa sababu wakulima wa tangawizi wa nchi nzima watakuwa na uhakika wa kupata soko. Kiwanda kile kinajengwa na watu wenye uwezo wa kifedha, kinapanuliwa lakini walima tangawizi wote wa nchi hii, walima tangawizi wa Madaba, Wilaya ya Same, Kigoma wote watakuwa wana mahali pa kuuza tangawizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, inatuweka kwenye nafasi nzuri ya sisi kuingia kwenye export. Nigeria wenyewe kupitia kiwanda chao cha Kaduna kinachoitwa Kachia wana-export asilimia tisa yaani katika soko la dunia ile tangawizi iliyoko kwenye soko la dunia kuna asilimia tisa kutoka Kaduna. Hii ni kwa sababu wana Kiwanda kikubwa cha Tangawizi cha Kachia ambacho kiko kwenye state ya Kaduna ambapo wananchi wa Nigeria wanaolima tangawizi wote wanauzia pale na kile kiwanda kina-export 92 percent ya tangawizi ambayo inasindikwa pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi ninakiona Kiwanda cha Miamba, hiki ambacho LAPF sasa inaingia ubia pale kama ni pacha wa hiki Kiwanda cha Kaduna cha Nigeria. Hivyo hapo lazima tukubali kwamba LAPF imemuunga mkono Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais anazungumzia viwanda kwenye nchi hii, anachochea viwanda kwenye nchi hii, LAPF ilipokwenda kuingia ubia na kile kiwanda cha tangawizi imemuunga mkono Mheshimiwa Rais, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu ambalo si dogo; hakuna kitu kinachomuumiza mkulima kama alime halafu hana soko. Mimi ninalima tangawizi si kwamba ninaihubiri tu, mimi ni muanzilishi wa kile kiwanda, nalima tangawizi. Kule Same nimekosa nafasi kwa sababu ardhi ya Same yote imejaa tangawizi kwa hiyo imebidi nitafute makazi, mimi nina makazi yangu Madaba kwa Mheshimiwa Mhagama, nalima tangawizi, nimeanza na hekari 20, kuanzia Julai navuna. Hata hivyo siri ya tangawizi si lazima nivune Julai, naweza nikaiacha kwa mwaka mzima, itategemea kama nina soko. Tangawizi unaweza ukaiacha chini ya ardhi kwa mwaka mzima na ikakusubiri upate soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niseme ukweli kuwa wakulima wa tangawizi ambao tuko Madaba na tuko wengi tunalima tangawizi kwa wingi na sisi hiki kiwanda ni faida kwetu kwa sababu kile kiwanda kitachukua tangawizi ya nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine lazima tujifunze, hiki kiwanda kikubwa kilichoko Nigeria ni mali ya Serikali. Ni Serikali ya Kaduna imekijenga sasa lazima sisi tujipe big up, tumeanza wananchi, mimi kama Mbunge nimetoa lile wazo, wananchi 613 wakachangia shilingi 6,000, Rais Kikwete akaniunga mkono kwenye fund raising tukapata shilingi milioni 301, Halmashauri ikaniunga mkono na sasa LAPF inakuja inatuunga mkono hapo ni lazima tuone kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya vizuri. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia, sitaki kuogongewa kengele. Kwa moyo uliopondeka na kwa unyenyekevu mkubwa niishukuru LAPF, nawashukuru sana na huko walipo wajue wameitendea nchi, hawakumfanyia mtu, wameifanyia nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa nakushukuru kwa dakika ulizonipa, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amesaidia hili kuwezekana namshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kushukuru kupata nafasi hii ya kuongea. Naomba niseme neno dogo kidogo, hata unapoamua kumnyonga mnyonge lakini mpe haki yake. Serikali ya Chama cha Mapinduzi Awamu ya Tano inafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuzungumze kwa takwimu, tuwe tunazungumza kwa takwimu. Kwanza nazungumzia Kamati ya Nishati na Madini, nazungumzia upande wa madini sasa. Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Rais Magufuli imefanya mambo makubwa mawili na mambo haya yamewavutia Madiwani wengine wanakuja wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kudhibiti madini yasipotee na jambo la pili ni upande wa ukusanyaji wa pesa za madini. Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano kwa kipindi hiki cha mwaka 2017/2018 nusu tu tuhatujafika mwaka 2018, Serikali imekusanya asilimia 80.4 ya makusanyo ya mwaka mzima. Lengo ilikuwa mwaka 2017/2018, Serikali ikusanye bilioni 194.397 hadi Mwaka 2018 Desemba lakini Serikali hii imekusanya bilioni 156.311 sawa na asilimia 80, sasa utasema hiyo Serikali inacheza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, msiwasikilize hawa, tumewazoea, sisi tunaangalia kazi inayofanywa na wananchi angalieni vizuri Serikali ya Awamu ya Tano inachapa kazi. Ningeshangaa sana Serikali inavyochapa kazi iungwe mkono na hawa, ningeshangaa, lazima hawa wakasirike. Kwa hiyo, msipate tabu Waheshimiwa Wabunge, twendeni kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende kwenye suala la REA, nipongeze Bunge la Kumi ndilo lilikuja na hii tozo ambayo imeleta manufaa kwa nchi yetu. Naomba nikubali kwamba jambo lolote linapoanza lina changamoto, huwezi kuanza jambo mara ya kwanza ukalifanya kwa asilimia 100, mara ya pili ukalifanya asilimia 100, kidogo kidogo REA itasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe takwimu, mwaka 2008 umeme vijijini ulikuwepo kwa asilimia 2.2 tu kabla ya kuwa na REA. Ilipofika 2015 umeme vijijini ukafikia asilimia 21.02, hayo ni madogo jamani? Serikali inachapa kazi, sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 mpaka Desemba, 2017 angalieni Serikali ya Awamu ya Tano inavyochapa kazi, umeme vijijini umefikia asilimia 49.5. Sasa najiuliza hivi hamuyaoni hayo, wenzetu mna macho gani, tafuteni miwani. Serikali inachapa kazi jamani Wabunge wa CCM tujivune. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Subira Mgalu, anajitahidi sana. Wiki iliyopita alikwenda Kilimanjaro, nampongeza sana, kuangalia matatizo yaliyotokana na REA I na REA II. Kwa hiyo, Serikali inafahamu kwamba kuna changamoto, alikwenda Mwanga, Rombo na akaja Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemshangaa, Kata ya Vulha, Kata ambayo Mawaziri wachache sana wanafika, amefika Subira. Kule kuna mradi wa REA II, nilipambana nayo sana ile, Serikali ikapeleka umeme kule lakini haikumaliza. Mheshimiwa Waziri amekwenda kuangalia na amekwenda kuwahakikishia wananchi kwamba REA III inakwenda kumalizia, Serikali inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Waheshimiwa Mawaziri, Waziri wa Nishati pamoja na Naibu Waziri mlikwenda Kilimanjaro lakini kuna Wilaya ina matatizo sana naomba nisimame hapa niiombee umeme kule ambapo haujafika, Wilaya ya Siha. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Siha kuna Kata moja ambayo ina vijiji vinne, hiyo Kata inaitwa Donyomurwakna. Kuna vijiji vinne kwenye kata hii, vijiji viwili vina umeme na vijiji viwili bado umeme haujafika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kitu kimoja, waacheni hawa, hakuna Serikali ambayo inaweza ikafanya mambo yote kwa wakati mmoja, haipo duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiombea Wilaya yangu ya Siha kwamba vile vijiji ambavyo Mheshimiwa Waziri nimekuletea kimaandishi uhakikishe vinapata umeme na Alhamisi ya wiki hii nahamia Siha. Naomba Watanzania wawe na uhakika kwamba Siha litakuwa Jimbo la Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishe Watanzania kwamba CCM inashinda Siha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu uvuvi haramu. Tunapata matatizo makubwa kama nchi kuhusu nyavu za kuvulia ambazo si rafiki kwa samaki zinazopelekea kuzaliwa uvuvi haramu. Niende mbele zaidi kwa kusema nyavu hizi ambazo si rafiki kwa samaki ni mara nyingi zinakamatwa na kuteketezwa lakini tatizo hili la nyavu haramu halijapata kamwe kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwa kuwa wananchi wetu wanazipenda sana hizi nyavu na kupelekea wao kuingia hasara za mamilioni ya fedha kwani pindi wanapokamatwa zinateketezwa na kwa kuwa hawakomi wanaendelea kuzitumia kinyume na maelekezo ya Serikali. Basi sasa ni vyema Serikali yenyewe ichukue jukumu la kuingiza nchini nyavu za kuvulia na pia Serikali ichukue jukumu la kumiliki viwanda vya kutengeneza nyavu ili tuondokane na kuteketeza nyavu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyavu zinazoteketezwa ambazo ni haramu tunateketeza mabilioni ya fedha za wavuvi ambao ni Watanzania tunavuruga uchumi wa nchi.

Namalizia kwa kusema nyavu za kuvulia ziwe chini ya Serikali yenyewe, Serikali ihusike na utengenezaji na uagizwaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ya pili kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake. Nitachangia maeneo matatu tu. Nitaanza na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, nitakuja Wizara ya Afya na mwisho nitamalizia Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nitakalolizungumza, nafikiri ni jambo ambalo linamgusa kila Mbunge hapa ndani na nina uhakika linamkera kila Mbunge hapa ndani; suala la kuchoma nyavu za kuvulia samaki. Kwanza naomba niipongeze Serikali sana. Serikali inafanya kazi nyingi, inafayanya kazi nzuri sana na Watanzania wanaridhika na mwenendo wa ufanyaji kazi, kwa jinsi ambavyo Serikali inafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la uvuvi haramu, linanipa taabu kidogo. Wavuvi ni wafanyabiashara. Wanapokwenda kuvua na nyavu zao, mtaji wao ni nyavu zao. Suala linalonisumbua kwenye Serikali, jamani Serikali naomba mnisaidie, wavuvi hawa wananunua nyavu madukani. Wao ndio watumiaji wa mwisho. Wanapotumia kuvua wanakamatwa na zile nyavu ambazo zinazaa uvuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu najiuliza kila wakati, kwani hizi nyavu wamezipata wapi? Suala linalonisumbua, hizi nyavu wamezipata wapi? Kikatiba Serikali Kuu ndiye anayetakiwa asimamie maendeleo ya wananchi. Aangalie wananchi wanavyopambana katika kujitafutia maendeleo. Serikali Kuu inatakiwa ihakikishe wakulima wanapata pembejeo, wanapata mbolea lakini mbolea sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashindwaje kutafuta chanzo cha nyavu hizi ambazo ndizo zinazozaa uvuvi haramu? Swali liko hapo, kwa sababu mvuvi yule kwa ufahamu wangu mdogo, maana yake kule kwetu Same sisi hatuko kama watu wa kwenye Ziwa Victoria. Nina imani kwamba mvuvi anakwenda kununua nyavu, lakini nina uhakika Serikali inapaswa kuangalia zile nyavu kama ambavyo inaangalia pembejeo na mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inanisumbua. Inakuwaje Waziri wa Mifugo anakwenda Ziwa Victoria, anakuta nyavu zilizotumika Ziwa Victoria asilimia 90 ya nyavu zile eti ni haramu? Zinatoka wapi hizi nyavu? Hawa wavuvi wanatengeneza wenyewe? Ndiyo kitu kinanisumbua. Naiomba Serikali sasa kwa sababu hili la kuchoma nyavu za wavuvi, kwanza tunachoma mtaji wa mvuvi yule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mfanyabiashara, ukinichomea mtaji wangu unaniua mimi. Naiomba Serikali ifanye kila njia idhibiti nyavu hizi ambazo ndiyo zinazaa uvuvi haramu. Iangalie hizi nyavu kule zinakotengenezwa; ina maana Serikali haijui nyavu zimetoka wapi? Kama zinaingia kwenye nchi kutoka nje, kwa nini inaruhusu nyavu ambazo zitazaa uvuvi haramu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona tusikimbilie kuchoma hizi nyavu zikiwa kwa mtumiaji wa mwisho.

Tuziwahi hizi nyavu zinapoingia nchini. Nafikiri Serikali imenielewa. Tutamwonea mvuvi, unless kama hawa wavuvi wana viwanda vyao wenyewe vya kutengeneza hizi nyavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itakapokuja kutujibu, itoe jibu ambalo litatatua hili tatizo. Mwisho kabisa, tusisikie nyavu zinachomwa. Tusikie huko kwenye viwanda vya hizo nyavu au huko bandarini, nyavu zinarudishiwa huko huko. Nimeeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili linahusu Wizara ya Afya. Mimi ni mwanamke ambaye nimepata watoto mara nne. Nashukuru kwa Sheria ya Nchi yangu kila nilipopata mtoto nilipata Maternity Leave ya siku 84. Namshukuru Mungu kwamba nilizaa watoto wangu salama. Sasa sheria ya nchi hii kwenye Maternity Leave iko sahihi, unajifungua mtoto, unapata siku 84 za kumwangalia mtoto mpaka anapata nguvu na wewe unarudi kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sheria iangaliwe upya, kwa sababu kuna mwanamke anazaa watoto wawili, kuna mwingine anazaa pacha watatu, kuna mwingine anazaa pacha wanne, kuna mwingine bahati mbaya anazaa mtoto mwenye kichwa kikubwa, kuna mwingine anazaa mgongo wazi, watoto hawa wanahitaji uangalizi wa zaidi ya siku 84. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu aliyepata mtoto mmoja, tena mwenye afya ni tofauti sana na mtu aliyezaa kitoto njiti. Ni tofauti na mwanamke aliyezaa mtoto ambaye mgongo uko wazi. Ni tofauti na mwanamke aliyezaa mtoto mwenye kichwa kikubwa, anahitaji uangalizi wa zaidi ya siku 84. Naiomba Serikali ikaingalie hii sheria upya kuliko inavyo- generalize kwamba kila mwanamke akijifungua, 84 days anapumzika. Je, wale waliozaa njiti? Je, ambaye Mungu amempa watoto wanne? Je, ambaye amepewa watoto wawili, wameungana na wana matatizo kichwani? Siku 84 hazitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, turudi tuangalie hii sheria upya tena kwa uharaka, maana yake juzi nimemwona yule mwanamke aliyetoka pale Aga Khan, amejifungua watoto watatu na ameajiriwa na Serikali hii iliyopo madarakani, hii Serikali yetu. Hivi huyu siku 84 na watoto watatu hawa zinamtosha? Hapo nitaomba Serikali iangalie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye Wizara ya Ardhi. Hapa nazungumzia Kata ya Ndungu. Hii kata iko Wilaya ya Same. Mimi naishi next door na Kata ya Ndungu. Kata ya Ndungu ni kata yenye population, tukienda kwenye sensa ya mwaka 2012, population yake ni wananchi 16,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kata, nakwenda kwenye ardhi kwa sababu kwa vipindi viwili nimekaa hapa Bungeni nikitetea wananchi wa Jimbo la Same Mashariki. Hili suala nilikuwa naliongea, kwamba nusu ya ardhi ya Kata ya Ndungu, ardhi yake ina mwekezaji sijui wa mkonge lakini ule mkonge hauendelezwi. Nililalamika hapa Bungeni, Waziri wa Uwekezaji wa kipindi kile Mheshimiwa Mama Maria Nagu, akaja akaona ile shida, akaona kwamba kwa kweli pale kuna tabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 60 ya wananchi 16,000 ni vijana, hawana ardhi, hawana mashamba, hawana makazi, ardhi yote iko kwa mwekezaji ambaye ule mkonge hauendelezi, upo tu. Namsihi Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, yupo Mheshimiwa Mama Angelina, aje Ndungu akaione ile ardhi ambavyo iko pale, hakuna kinachotokea, vijana wa Kata ya Ndungu hawana nyumba, wanaishi na wazazi wao. Anaoa mke, anakaa na mama yake na baba yake. Ndoa itavunjika ile; gubu la mama mkwe! Anataka ajenge nyumba yake, hana mahali pa kujenga. Mkonge umekufa, nusu ya ardhi ya Kata ya Ndungu. Nafikiri Serikali imenisikiliza. Sikuwa mtata sana, nimeeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukweli, nimekuwa hapa Bungeni tangu mwaka 2000. Tumekuwa tuna migogoro mingi sana ya ardhi kuanzia mwaka 2000 mpaka sasa hivi ni mwaka 2018. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Lukuvi, amepunguza migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme ukweli Mheshimiwa Waziri William Lukuvi, anachapa kazi sana. Anafanya kazi kubwa sana, lakini sio kwamba achukue sifa zote peke yake, ana mke wake ambaye anamwangalia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Mkoa wa Kilimanjaro. Mkoa wa Kilimanjaro una wilaya saba. Ndani ya wilaya saba, Wilaya ya Same iko hapo ambayo katika ardhi inachukua takriban asilimia 40 ya ardhi ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wilaya ya Same asilimia 68 iko milimani, asilimia 32 iko tambarare. Tuna matatizo makubwa mawili ambayo ndiyo yamenifanya nisimame hapa, Nianze kwa kusema kwa Mheshimiwa Waziri; Same tunamwita aje aone matatizo yetu. Haya matatizo ni matatizo yako sehemu kubwa katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata mbili, Kata ya Makanya ambayo iko Same Magharibi, kata hii tangu mwaka moja elfu mia tisa, kwanza population ya Kata ya Makanya ni takriban wananchi 15,000 kwa sensa ya mwaka 2012. Kwa hiyo, ni Kata yenye watu wengi sana. Kuna tatizo kubwa sana la ardhi pale kwenye Kata ya Makanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haya mashamba ya mikonge ambayo watu wengi tunayalalamikia kwamba yame-end up kutokuwa na tija kwa wananchi kwenye kata zetu. Kata ya Makanya ni kata yenye matatizo ya mafuriko ya mara kwa mara. Lile eneo zuri kwenye Kata hii ya Makanya ndilo eneo ambalo lina mkonge, la mwekezaji ambaye simjui ni nani lakini ni mwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1994, wakati huo Waziri wa Ardhi akiwa ni Mheshimiwa Edward Lowassa, kama sikosei, wananchi wa Kata ya Makanya, Kijiji cha Makanya walileta maombi kwamba wapatiwe ardhi takriban hekta 30, kwa sababu ile ardhi wanayoishi wao ndiyo ardhi ambayo ina mafuriko mara kwa mara. Kwa hiyo, hili tatizo ni kubwa sana kwa Kata ya Makanya. Mheshimiwa Waziri, namnyenyekea, aje aione kata ile, aone wananchi wanavyoteseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, hawana eneo la makazi, pili, ukiangalia kama unatokea Hedaru kwenda Same ardhi kbwa ya Makanya huku kando ya barabara ni kilimo cha mkonge. Vijana wa Kata ya Makanya nao wangependa kufanya biashara kandokando ya barabara ya lami, lakini kandokando ya ile barabara ya lami kuanzia Makanya mpaka Same ni mashamba ya mkonge ambayo nina uhakika hayana tija kwa wananchi wa Kata ya Makanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetumwa na wananchi wa Same nimwite Mheshimiwa Waziri aje Same na mimi nitakuwepo Same. Tuzunguke Kata ya Makanya aone ni kiasi gani wananchi wa Kata ya Makanya, Same ya Magharibi wanapata adha kwa ajili ya yale mashamba ya mkonge. Mheshimiwa Waziri nafikiri message ameipata vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Makanya ni kata ambayo mara kwa mara Watanzania mnasikia mafuriko, ni kwa sababu ardhi ile ambayo ni nzuri ndiyo yenye mkonge na ardhi ambayo ina mafuriko ndiko wanakoishi wananchi. Mheshimiwa Waziri nimalizie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Kata ya Ndungu. Tangu Bunge zima la Kumi nimekuwa nalalamikia Kata ya Ndungu. Kata ya Ndungu asilimia kubwa ni mashamba ya mkonge pia; vijana wa Kata ya Ndungu hawana sehemu ya makazi, hawana sehemu ya biashara, ni mashamba ya mkonge. Mheshimiwa Waziri, nimemwona anazunguka Tanzania, anafanya mikutano mpaka saa sita usiku; namsihi aje kwetu Same, tunamsubiri, tunamsubiri atapata zawadi ya mpunga, atapata tangawizi, aje aone matatizo ya ardhi, mashamba ya mkonge yametuzidi, lakini hayana tija kwa Kata ya Makanya na Kata ya Ndungu. Karibu Same tunakusubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba ku-decalre interest kwamba mimi ni mwananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Same lakini mimi pia ni mwananchi wa Mkoa wa Dodoma, Jimbo la Mtera. Kwa niaba ya walima zabibu, ndugu zangu Wagogo, nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ametugusa wakulima wa Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiri kabisa tulikuwa tunapata shida sana. Niseme ukweli, mume wangu ni mkulima mkubwa wa zabibu, ana ekari 11 pale Chinangali. Nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa unyenyekevu mkubwa, Bunge lijalo la Bajeti uje Chinangali uone ni kiasi gani wakulima wa zabibu pale tuna shida. Serikali kwa hili mlilolifanya la kupunguza huu ushuru wa mchuzi wa zabibu mmewapa usingizi wakulima wa zabibu hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ulivyozungumza, mwaka 2018 zabibu zilioza, zabibu ni zao tofauti na nazi na mazao mengine. Siku ya kuvuna ikifika usipovuna ndani ya wiki moja unapoteza kabisa. Wakulima wa zabibu kwa Mkoa wa Dodoma, including mume wangu, Mzee Malecela, mwaka 2018 tulipoteza moja kwa moja. Kwa hiyo, kwa unyenyekevu mkubwa nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ametufikiria sisi wakulima wa zabibu.

Mheshimiwa Spika, sina mengi ya kusema, nashukuru sana, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukumshukuru Mungu kwamba nimeweza kusimama katika Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ipo mbele yetu. Naomba nikushukuru na wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini nimshukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, ametoa hotuba nzuri iliyosheheni miradi mingi ya maendeleo, iliyofanywa na Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ukianza kusema kazi zilizofanywa na Awamu ya Tano utamaliza siku tatu unazungumza tu. Kwa hiyo, niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano, nampongeza Rais na Mawaziri wote na Wakuu wa Mikoa, nchi inasonga mbele. Naona kila mtu ana mtazamo wake katika mambo. Baada ya Rais kufanya mambo mengi sana, kuna jambo sasa hivi ameamua kama mnaangalia mambo vizuri, ameamua kuweka misisitizo kwenye uwekezaji. Kwa nini nasema hivyo? Mheshimiwa Rais ameangalia vizuri akaona uwekezaji ndani ya nchi haujakaa vizuri, akaamua kuteua Waziri wa Uwekezaji, Mheshimiwa Angella Kairuki ambaye mimi namwamini sana, amempa Wizara hii na ameiweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa nini ameweka msisitizo kwenye Wizara hii ya uwezekezaji? Dira ya nchi yetu ni kwamba ifikapo 2025 tuwe tumefikia kuwa kwenye Taifa ambalo ni la uchumi wa kati, lakini tuliangalie Taifa la uchumi wa kati na tulipo. Ili tufikie kwenye uchumi wa kati, tunahitaji tuboreshe viwanda kwenye nchi yetu, lakini viwanda tutaviboreshaje, lazima tusimame imara kwenye uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, ili Rais asisitize zaidi katika uwekezaji amewaita Mabalozi wote Ikulu akafanya dhifa, akala nao chakula, lakini akatoa tamko kwa wale ambao mnasomasoma magazeti, kwamba ni mwaka 2019 ni mwaka wa uwekezaji. Mheshimiwa Rais alizungumza kwa wale Mabalozi, lengo lake ni kwamba Mabalozi wote wachukue tamko lile kwenye nchi zao kwamba Tanzania imeamua mwaka 2019 ni wa uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, naomba dakika zangu zote nichangie kwenye uwekezaji. Mimi ni Mwalimu ndugu zangu na Walimu tunaamini unafanya vizuri ukisimamia specialization. Nisingependa kuzungumza mambo mengi sana nitazungumzia uwekezaji na nitachangia kwa maandishi pia nikizungumzia uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, naifahamu nchi yangu vizuri na nimekuwa Bungeni hapa kwa muda wa kutosha. Tumezungumza sana kuhusu pamba na naomba Waheshimiwa Wabunge wanaolima pamba mnisikilize kidogo. Tumezungumza sana kuhusu zao letu la pamba, lakini nikiri bado hatajatumia pamba vizuri kwenye nchi hii. Kuna mikoa minne mikubwa inayolima pamba, Mkoa wa kwanza Simiyu, Mkoa wa pili Shinyanga, Mkoa wa Tatu ni Mwanza pamoja na Geita na wengine wanajaribu jaribu, lakini hii ndio mikoa minne inayolima pamba vizuri. Ukiangalia Mkoa wa Simiyu ukisoma vizuri utaona, Simiyu pekee inalima zaidi ya 40% ya pamba inayolimwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, hapa nimezungumzia pamba ndani ya nchi, twende kwenye zao la pamba Tanzania katika Afrika na pia twende kimataifa. Tanzania katika kilimo cha pamba ni namba nane, inachukua nafasi ya nane katika nchi 30 za Afrika zinazolima pamba. Hiyo ni upande wa Afika, lakini Tanzania katika kulima pamba Tanzania inashika nafasi ya 22 duniani katika nchi 77 zinazolima pamba. Kwa hiyo, tunaweza Watanzania tukajipambanua kwamba tunalima pamba. Kama dunia nzima nchi zinazolima pamba zipo 77, Tanzania tunashikika nafasi ya 22; kama Afrika zipo nchi 30, Tanzania tunashika nafasi ya nane Waheshimiwa hatulimi pamba? Tunalima pamba.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kama Mbunge mzoefu kusema bado hatujatumia zao za pamba vizuri. Nilipomsikia Mheshimiwa Rais ametangaza 2019 ni mwaka wa uwekezaji, naomba Serikali waende wakajitikite kwenye kuwekeza kwa kutumia zao la pamba, kwa nini nasema hivi? Kwa sababu kuna nchi ndogo hapa Asia inatiwa Bangladesh, mnaifahamu, Bangladeshi hana umaarufu katika kulima pamba hata kidogo, soma vitabu vyote hana, lakini Bangladesh anaongoza kwa kuwa na textile Industry, anaongoza kutuvisha watu wote duniani. Mmarekani anauza nguo sana duniani, lakini viwanda vyote vipo huko Vietnam. Bangladesh ni namba one, anatumia pamba ya ku-export, sasa sisi tuko namba 22 duniani, tuko namba nane Afrika, tuna uwezo wa kufanya vizuri kama Bangladesh na kumzidi. Hivyo, ni lazima Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji aende akamsaidie Mheshimiwa Rais, hakumchagua kwa sababu nyingine, amemwamini. Uwekezaji ndio utakaotupeleka kufika kwenye Taifa uchumi kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu katika uwekezaji iwapo Serikali wata-invite mataifa mengi kuja kuwekeza katika textile Industry, tutafika mbali, tutakuwa kileleni, tutafika mbali, nina imani kabisa. Naona vibaya kweli kale kanchi ka Bangladesh hakana umaarufu lakini kila nguo unayonunua Marekani made in Bangladesh, Bangladesh, Bangladesh, hawana umaarufu ni kanchi kadogo kenye takribani square mita laki moja hamsini elfu, kitu kama hicho, lakini kanaongoza duniani kwa kutuvisha mavazi ni number one akifuatiwa na China.

Mheshimiwa Spika, niinyenyekee Serikali, sasa ni wakati wa kusimamia uwekezaji, Mheshimiwa Rais amefanya vizuri sana tangu ameanza, jamani kuna ambaye hawatakubali? Rais anafanya kazi nyingi sana, sasa namwomba Mheshimiwa Rais kwa unyenyekevu mkubwa, nampigia na magoti, aipeleke nguvu yake kwenye uwekezaji na uwekezaji huo aende akaitumie pamba ya nchi hii, tutumie pamba ya nchi hii, tutafika mbali sana.

Mheshimiwa Spika, nisingependa kusema sana kwa sababu nataka kusimama kwenye pamba na Mheshimiwa Waziri naomba niseme nachangia nitampelekea faili lenye data akamsaidie Mheshimiwa Rais kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono haja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 21, miradi ya kuzalisha umeme; mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya Mto Rufiji, megawatt 2,115. Kwanza nianze kusema kwamba naunga mkono hoja ya ujenzi wa mradi huu kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kumshukuru Mungu kutupatia maporomoko ya Mto Rufiji kwa sababu siyo kila nchi imepata maporomoko kama yale. Huku duniani kuna mabwawa makubwa 70 tu na ili bwawa liitwe kubwa linatakiwa liwe na sifa ya kuweza kufua umeme wenye zaidi ya megawatt 2,000. Bwawa letu hili ambalo linajengwa litakuwa na uwezo wa kufua umeme megawatt 2,115 na hivyo kuingia kuwa kwenye sifa ya kuwa mabwawa makubwa 70 duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende katika dunia, katika dunia kama nilivyosema mabwawa makubwa yapo 70, lakini ukienda duniani bwawa la kwanza kubwa liko China; la pili kubwa lipo Brazil na Uruguay na la tatu lipo Brazil. Twende Afrika, mabwawa ni mengi makubwa lakini tuanze bwawa kubwa mpaka sasa hivi linaloonekana ni kubwa ni bwawa lililopo Msumbiji bwawa la Cahora Bassa Dam ambalo linafua umeme kwa megawatt 2,075. Ina maana la kwetu linalojengwa litakuwa kubwa kuliko hili ambalo linaongoza sasa hivi. Bwawa lingine ni Aswan High Dam ambalo lipo Egypt ambalo linafua umeme megawatt 2,100, hili la kwetu ambalo linajengwa Rufiji litakuwa kubwa kuliko hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Ethiopia walianza kujenga bwawa ambalo litakuwa kubwa kuliko yote Afrika, Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance. Bwawa hili litakuwa na uwezo wa kufua umeme kwa megawatt 6,000 na lilianza tangu mwaka 2011 likikamilika litatumia dola bilioni 6.4, bado halijakamilika mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili bwawa linalojengwa hapo katika maporomoko ya Mto Rufiji; ni kweli kelele ni nyingi sana, upinzani ni mkubwa sana katika ujenzi wa bwawa hili lakini naiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ielewe kwamba hakuna mtu yeyote duniani, hata haya mabwawa yote yaliyojengwa China, Brazil, Uruguay na wapi, si kwamba walijenga bila ya kuwa na changamoto, wote walipata changamoto kubwa sana na wote walipata upinzani, lakini naomba tuelewe kwamba huwezi kufanya jambo kubwa lenye manufaa katika nchi kama manufaa tutakayopata kutoka kwenye bwawa hili tunalojenga usiwe na changamoto, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yangu kwa unyenyekevu naisihi twendeni bila kusikiliza kelele zozote. Kwanza, ni lazima mwelewe kwamba moja ya tano ya umeme wote unaotumika duniani unatoka kwenye mabwawa haya 70. Sasa sisi tumepata nafasi ya kuwa na bwawa kubwa na sisi tuingie katika kuwa kwenye moja ya tano ya umeme unaozalishwa duniani, tunasikiliza kelele, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasihi sana, changamoto zilizopo tusisikilize kelele kushoto wala kulia, Serikali wasonge mbele kwa sababu kwanza ukiangalia umeme huu wa hydro ni rahisi. Pili huu umeme wa hydro utatusaidia kwa mambo makubwa mawili; kwanza; ajira kwa vijana wetu; pili. tayari tutakuwa na uwezo wa kuwa na uwekezaji mkubwa kwenye nchi hii. Sasa iwapo hatutakuwa watu tunaothubutu Serikali ya CCM, tunaogopa kelele za watu, tutakuwa wapumbavu. Naomba uthubutu huu uliooneshwa na Awamu ya Tano tusikatishwe tamaa na kelele zozote zile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anne muda umeisha, ni dakika tano.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, nafikiri Watanzania wamenielewa. (Makofi/Vigelegele)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai nikaweza kuwepo Bungeni leo. Naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Same Mashariki kwa unyenyekevu mkubwa kwa jinsi ambavyo walifanya uchaguzi mzuri sana na kuhakikisha wananirejeshea Jimbo langu la Same Mashariki. Nilishinda kwa kishindo tena kwa haki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza amesimama imara akahakikisha nchi yetu inafanya uchaguzi kwa pesa zake za ndani. Nafikiri wote tunaoelewa uchaguzi tumekaa kwenye uchaguzi muda mrefu, siku zote tumekuwa tunabebwa na mataifa makubwa, lakini Mheshimiwa Rais kipindi hiki alisimama imara sana akaiheshimisha nchi yetu tukafanya uchaguzi kwa pesa zetu wenyewe. Waheshimiwa Wabunge naomba hili tulichukue kwa uzito sana na tuone kwamba, Rais ametukomboa kwa kitu kikubwa sana. Vile vile nimpongeze pia Rais alifanya kampeni za kutosha. Alizunguka nchi na aliomba kura na akashinda kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nirudi sasa kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Rais ametoa hotuba siku ya kwanza hapa Bungeni, ilikuwa ni hotuba nzito sana. Namuunga mkono katika area tatu ambazo nimeona nizichague; kwanza katika viwanda, pili katika barabara na tatu nitakuja kwenye afya.

Mheshimiwa Spika, nchi yoyote inakua vizuri zaidi inapokuwa na viwanda vya nguvu. Mimi naomba nirudi kwenye Jimbo la Same Mashariki, Jimbo la Same Mashariki sisi tunalima tangawizi kwa muda mrefu. Kwa muda mrefu sana tunalima tangawizi na tumejenga kiwanda cha tangawizi, mnaokumbuka tangu nimeanza kuingia bungeni hapa nazungumzia tangawizi nikasimama na wale wananchi imara tukajenga kiwanda cha tangawizi.

Mheshimiwa Spika, nikiri kile kiwanda kilikuwa ni dhaifu, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Mhagama amekuja ziara kwenye jimbo langu akaja mlimani Mamba Miamba kukiona kiwanda kile. Amekuja nikajua ni Serikali imekuja kuona kile kiwanda. Kiwanda kile yeye mwenyewe amesimama imara pamoja na taasisi yake ya PSSSF, ambao wameingia ubia na sisi wananchi tunaolima tangawizi sasa pale Mamba Miamba, sasa pale Mamba Miamba tunakuwa na kiwanda kikubwa cha tangawizi katika Tanzania kwa sababu PSSSF wameamua kuingiza fedha nyingi sana kuwaunga wananchi wangu wa Jimbo la Same Mashariki.

Mheshimiwa Spika, wao wamechukua asilimia 60 sisi tumechukua asilimia 40, lakini ndugu zangu Wabunge hicho ni kitu kikubwa sana. Ina maana kiwanda kile ambacho kitakuwa kikubwa wananchi wangu wataondoka katika umaskini. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, namshukuru mama Jenista Mhagama mno mno, alikuja jimboni kwangu, nilipata furaha sana ambavyo aliwafanya wananchi wangu wakafurahi. Naipongeza sana Serikali kujali viwanda kwa wananchi. Nimeanza tu kusema kidogo, nitakavyokuwa niko hapa ndani nitaongea sana kuhusu hiki kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono suala la ujenzi wa barabara kwenye nchi yetu. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuangalieni tulitoka wapi tuko wapi sasa hivi. Tulikuwa kwenye barabara kwenye miji mikuu, ukiangalia Dar es Salaam, ukienda Arusha, ukija Moshi, ukija Dodoma, barabara zilikuwa za kawaida mno, lakini mimi nikienda Dar es Salaam na dereva wangu kwa sababu, mimi niseme ukweli mimi naishi Dodoma, kama sipo Dodoma niko Same Mashariki, Dar es Salaam mimi ni mgeni; tukienda na dereva wangu Dar es Salaam sasa hivi inabidi tupate dereva wa kuingia na sisi mjini. Dar es Salaam Rais amesimama imara mno, ameisimamia nchi yetu imara sana. Sasa hivi Tanzania katika Afrika Mashariki, sio kwamba tujisifu tuseme ukweli, tunaongoza upande wa barabara.

Mheshimiwa Spika, tunaongoza upande wa barabara, lakini naomba nizungumze kama mama. Mama sisi tunapokuwa na watoto unawaangalia Watoto wako sana, unamwangalia mtoto wako wa kwanza, unaangalia wa pili, unaangalia wa tatu, sisi tuliozaa zaidi unaangalia wa nne. Kila mtu anapozaliwa, anapoumbwa na Mwenyezi Mungu akija duniani ana kitu amepewa, ana kitu Mungu amempa cha kwake kwamba, huyu nampa kitu fulani. Tumshukuru Mungu amempa Rais wetu silika ya kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais Magufuli pamoja na usomi wake, amesoma mathematics na kadhalika lakini nadni ya damu yake ni mjenzi, anajenga barabara. Mimi tangu nimekuwa bungeni hapa nimekuwa nae, hiki ni kipindi changu cha tano, yeye ni Waziri wa ujenzi, Waziri wa Ujenzi, sasa ni Rais anaijenga nchi mpaka mimi na Mheshimiwa Mama Sitta tumekaa tukafikiria hivi akiondoka tutafanya nini, lakini Mungu atatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi imejengwa barabara. Mimi najivuna sasa hivi nikiona hata Dodoma yangu inavyofanana. Dodoma inajengwa na Rais Magufuli mno na nampongeza kwa sababu, mume wangu siku moja alisema aah, hivi kumbe kweli hata nikifa kesho Dodoma imekuwa Makao Makuu, alimshukuru Mungu, lakini Malecela anasifu sana, anamsifu Rais mno, naomba umfikishie message, jinsi anavyojenga barabara za Dodoma.

Mheshimiwa Spika, sasa narudi nikwambie hivi TARURA. Sisi Wabunge wengi wa majimbo tunaitegemea TARURA na mimi niko Kamati ya Miundombinu, kuna mgawo wa fedha za kujenga barabara upo 70 kwa 30. TANROADS anapewa 70; TARURA anapewa 30, mimi naona TARURA aongezewe pesa. Waheshimiwa Wabunge wa majimbo simameni imara sana TARURA aongezewe pesa ili wananchi wetu nao wapate barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshukuru Serikalini. Serikali imeona majiji makubwa, sasa tunaomba Serikali mrudi mtuangalie na sisi ambao tuko vijijini. Vijijini barabara zina hali mbaya sana. Sisi ambao majimbo yetu yako kwenye milima tuna shida kubwa ya barabara, tuna tabu sana ya barabara. Nasema ukweli lazima Wabunge bajeti inayokuja tusimame imara TARURA apewe pesa. Ule mgawo tunaoambiwa ni mgawo wa kisayansi wa 70 kwa 30 TARURA anapata pesa kidogo, Serikali itafute chanzo kingine cha kumpa TARURA pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudi kwenye afya sasa; namuunga Mheshimiwa Rais sana mkono kwa jinsi alivyosimama imara kujenga vituo vya afya. Amesimama imara kujenga vituo vya afya. Sasa ahakikishe vituo vya afya vinatoa huduma kikamilifu, Madaktari watoshe na vyombo.

Mheshimiwa Spika, sasa hapo lazima nirudi kwenye Jimbo langu, mimi nina tarafa tatu. Tarafa ya Ndungu ina kituo cha afya kimoja, nimetoka kuongea na Waziri wa Afya pale. Tarafa zangu mbili za milimani zote hazina vituo vya afya. Rais alipokuja Same nilimlilia nikamwambia wananchi wanakufa. Tarafa ya Gonja kuna kituo cha afya lakini ni cha KKKT ni biashara, wananchi hawana uwezo wa kulipia zile gharama pale. Tarafa ya Mamba Vunta kuna kituo cha afya cha Katoliki ni biashara. Nimekwenda kumlilia Mheshimiwa Waziri sasa hivi pale, nimempigia magoti aje aone jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kuunga mkono hoja hii ya hotuba za Mheshimiwa Rais, naipongeza sana Serikali inafanya kazi nzuri lakini naomba mtuangalie na sisi tunaotoka vijijini. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi. Kwanza naomba nizungumze kwamba, naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Tangu Awamu ya Tano imeanza wote tunashuhudia kazi zinazofanywa na Serikali. Nina uhakika wote ambao tuko sobber tunaona kwamba, Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi inafanya kazi kubwa sana. Naomba nichukue nafasi hii niipongeze na sio mimi na wananchi wangu wote wa Jimbo la Same Mashariki wanapongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia sehemu mbili ambazo zimeongelewa vizuri kwenye mpango, viwanda, lakini pamoja na kilimo. Naomba mimi niviunganishe hivi vitu viwili, viwanda na kilimo. Niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kusisitiza sana na kutuwezesha kufungua viwanda; viwanda vidogo, viwanda vya kati, viwanda vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vyote vinavyofunguliwa Tanzania vinasaidia sana kilimo kwa sababu, vinachukua malighafi kutoka kwenye kilimo chetu, nafikiri hapo nimeeleweka, lakini kuna tatizo kubwa ambalo tusipoangalia vizuri tutakwenda tunajenga viwanda kwa nguvu sana baadaye vitakosa malighafi. Naomba nizungumzie kule ninakokuona, tumejenga kiwanda cha tangawizi, kile ni kiwanda kimejengwa na wananchi na Mbunge aliyekuwepo madarakani wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi tumefika tumeungana na PSSSF ni mbia wa kiwanda cha tangawizi sio kwamba, ameleta mitambo, ni mbia wa Kiwanda cha Tangawizi cha Mambamiamba, naomba mnielewe vizuri ninalozungumza. Sasa hili jambo tuliangalie kwa nchi nzima, kiwanda kile kilipofika pale Same Mashariki nakiri kinakwenda kupanua kilimo cha tangawizi kwa sana. Wananchi watakuwa wana mahali pakuuzia tangawizi tena sio Same Mashariki tu na Same Magharibi watalima mpaka tukija Mlalo watalima, Lushoto watalima, Tanga watalima, kiwanda kiko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo nililoliona maana kwa sisi viongozi tuwe tunaangalia huku na huku, tutafute kila njia Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu namnyenyekea, watafute kila njia ya kwenda kuhakikisha miundombinu ya kilimo cha tangawizi inakuwa inayofanya wananchi waweze kulima kile kilimo. Sasa hivi wanaolima tangawizi kule kwangu ni wengi mno, nilianza na kata mbili, nikaja kata nne, sasa ni tarafa tatu zote za jimbo langu, wote wanalima tangawizi; miundombinu ya kilimo imekuwa haiwatoshelezi. Mifereji imekuwa ni midogo, mito imekuwa haina uwezo tena, lakini bado kuna uwezekano wa kuboresha miundombinu ya kilimo kama Serikali ikija kule na kuangalia hali halisi. Kuna sehemu ambazo zinawezekana kuchimbwa mabwawa makubwa wakati wa mvua maji yakajaa, mvua zinapokuwa hazipo mito ikapata maji kutoka kwenye mabwawa yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namnyenyekea Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo ni mwepesi sana, namkaribisha. Baada ya Bunge hili twende naye kule kwangu akaone hali halisi ya kuboresha miundombinu ya kilimo kwa ajili ya tangawizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye mpunga ni hilohilo, nina tarafa inayolima mpunga. Tarafa ya Ndungu kuanzia Bendera, Kihurio, Ndungu, Maore ni mpunga, lakini miundombinu ya kilimo imechoka. Sijui kwa majimbo ya wenzangu, lakini miundombinu ya kilimo Same Mashariki, Same Magharibi ni jirani yangu hata yeye ana hilo tatizo. Naomba Serikali itusaidie kuja kutuangalia kwa sababu, bila ya kilimo hata hivi viwanda tunavyovizungumza itakuwa havina malighafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kuzungumza hilo tu. Nashukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Kilimo. Kilimo kwangu mimi ni Wizara mama kwani wazazi wangu walionipa maisha haya wamenilea na kunisomesha kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wote wa Tanzania kuanzia vitongoji hadi Taifa na Watanzania wote kwa ujumla tunapaswa kujiuliza swali hili, ni Tanzania ipi tunayoitamani? Jibu sahihi ni Tanzania yenye nguvu ya kiuchumi. Ili Tanzania ifikie kuwa Taifa la uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda ni lazima na muhimu kupanua wigo katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yangu ya leo ya Wizara ya Kilimo, nitaongelea suala moja tu nalo ni zao la tangawizi. Nianze kwa kuuliza swali ambalo nitalijibu sawia. Tangawizi ni zao gani? Ni zao ambalo ni jamii ya viungo (spices). Pili, tangawizi ni malighafi ya kutengeneza madawa ya binadamu, vipodozi, vinywaji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea tangawizi kiulimwengu, Afrika na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiulimwengu; ukisoma vitabu vya zao la tangawizi ulimwenguni utaona kwamba mataifa tano bora yanayoongoza ulimwenguni kwa kulima zao la tangawizi ni India, China, Nepal, Nigeria, Thailand. Nchi hizi tano bora kwa kilimo cha tangawizi zimeweza kujiboresha kiuchumi kupitia zao hili la kilimo. India inalima asilimia 34.6 ya tangawizi yote inayolimwa duniani, inaongoza kwa kulima tangawizi na pia inaongoza kwa kuitumia. China inalima asilimia 19.1, Nepal inalima asilimia 10.1, Nigeria inalima asilimia 7.8, Thailand inalima asilimia 7.8. Nchi nyingine zinazojitahidi ni Indonesia, Bangladesh, Japan, Cameroon na Taiwan hizi zinaingia kwenye kumi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiishie hapo nchi tano ulimwenguni zinazoongoza kwa ku-export tangawizi aidha ikiwa mbichi (raw ginger) au ikiwa imesindikwa, kwa takwimu hizi za mwaka 2015 China inaongoza kwa ku-export asilimia
39.9 ya tangawizi yote iliyouzwa duniani, India inashika nafasi ya pili kwa ku-export asilimia 14.5 japo inaongoza kwa kulima tangawizi duniani lakini inaongoza kwa kutumia tangawizi pia. Nigeria inashika nafasi ya tatu kwa ku-export tangawizi duniani na ina-export asilimia tisa ya tangawizi inayofika kwenye soko la duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa unyenyekevu mkubwa, kwa moyo uliopondeka nitoe shukrani zangu za dhati kwa wafuatao:-

Bodi ya Wadhamini wa LAPF na Mkurugenzi wa LAPF kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli katika jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, LAPF wameingia ubia na kiwanda cha kusindika tangawizi cha Miamba Same Mashariki kupitia kampuni yake ya Mamba Ginger Company Limited. LAPF kuingia ubia na kiwanda cha kusindika tangawizi kuna yatokanayo yafuatayo:-

(i) Walima tangawizi wa Wilaya ya Same na Tanzania nzima watapata soko la uhakika la kuuza tangawizi yao.

(ii) Ni dhahiri kwamba kilimo cha tangawizi Tanzania kitapanuka na haswa kama Serikali itajali kujenga miundombinu endelevu kwa wakulima tangawizi.

(iii) Ni dhahiri kwamba tangawizi sasa tutaingia kwenye biashara ya uhakika ya kuuza tangawizi nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika na haya ninayoyasema kwamba walima tangawizi wa Tanzania wanapata taabu sana inapofikia kwenye kupata soko la zao kwa walanguzi ambao wanawapangia bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangawizi inastawi sana Same Mashariki na mpaka sasa hivi ninapoandika hotuba hii ardhi ya Same Mashariki ililimika tangawizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunayo mikoa yenye ardhi nzuri sana yenye rutuba kama ile ya Nigeria. Mvua ya kutosha, climate condition nzuri; mito isiyokauka. Mikoa hiyo kwa uchache wake niitaje ni pamoja na Ruvuma, Mbeya, Iringa, Rukwa, Kigoma, Arusha na Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangawizi sasa hivi imeonesha mwamko wa Watanzania kuanza kulima zao la tangawizi. Napata simu nyingi sana kutoka Kigoma wananchi wakinipa simu kuhusu wapi wanauza zao lao la tangawizi. Songea vijijini Jimbo la Madaba wananchi wameanza kilimo cha tangawizi tangu mwaka 2012. Mimi nahamasisha sana kilimo cha tangawizi nami nikiri kwamba nimewekeza katika kilimo cha tangawizi na nimeanza na ekari 20 nalima tangawizi Madaba, Songea Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naisihi sana Serikali ifanye kila jitihada kuliangalia zao hili la tangawizi kwani iwapo Serikali itajihusisha kikamilifu tutakuwa tunatengeneza zao litakaloweza kutuingizia fedha za kigeni. Leo hii nchi ya Nigeria inachangia asilimia tisa ya tangawizi yote inayouzwa kwenye soko la dunia na matumizi ya tangawizi kiulimwengu yamepanda kwa asilimia takriban asilimia 7.5
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze hotuba yangu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia na kunipa afya nikaweza kuchangia hotuba hii muhimu sasa ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa utendaji wake mzuri sana uliotukuka na uliojaa uzalendo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yangu hii ninayoitoa Bungeni hapa na pia nitachangia kwa maandishi nitachangia kuhusu hoja moja tu ya uwekezaji ndani ya nchi yangu ya Tanzania. Nimpongeze Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya miradi ya maendeleo ya nchi yetu, anamalizia viporo vya tangu Awamu ya Kwanza mpaka sasa Awamu ya Tano. Mungu ambariki sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi kwa Rais, nirudie kumpongeza kwa kuona umuhimu wa uwekezaji Tanzania. Nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais ameamua kuiunda Wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lengo lake likiwa ni kuimarisha uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dira yetu ya Maendeleo inataka ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe imeshafika kuwa nchi ya uchumi wa kati (middle income country). Nchi haitaweza kufikia nchi ya uchumi wa kati bila ya kuwa na viwanda vya kutosha. Rais wetu amechukua hatua nzuri sana
kumteua Waziri anayesimamia Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambako vilevile tuna Kituo cha Uwekezaji (Tanzania investment Centre) ili kuratibu vizuri juhudi zote za uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili alilolifanya katika mikakati yake ya kuboresha uwekezaji ni pale alipomtaka kwamba mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa uwekezaji Tanzania. Alitoa tamko hili mbele ya Mabalozi wote wa nchi za nje wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania. Tamko hili la Rais ni la Kitaifa na ni la Kimataifa. Mheshimiwa Rais kutoa tamko hili la kuutambua mwaka 2019 kuwa mwaka wa uwekezaji amewatuma Mabalozi wa nchi za nje kualika nchi zao kuja kuwekeza nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia uwekezaji nchini nikisema yafuatayo. Tanzania tunalima pamba kwenye Mikoa mikuu minne ambayo ni Simiyu; Shinyanga; Mwanza na Geita. Simiyu peke yake inaongoza kwa kulima pamba zaidi ya 40% ya pamba yote inayolimwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiangalie Tanzania kwenye kilimo cha pamba ndani ya Afrika na ulimwenguni. Tanzania kwa kulima pamba inashika nafasi ya 8 kati ya nchi 30 za Afrika zinazolima pamba. Tanzania inashika nafasi ya 22 duniani kati ya nchi 77 zinazolima pamba. Katika hali kama hiyo, Tanzania Afrika na duniani tunalima pamba. Pamoja na Tanzania kuwa nafasi nzuri sana katika kilimo cha pamba lakini kuna tunachokosea na hivyo hatupati faida kubwa kiuchumi kutokana na zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia muda wote nilio nao kuishauri Serikali kwamba tutumie zao hili la pamba kupata wawekezaji wa textile industry (viwanda vya nguo). Mheshimiwa Rais alipoteua Waziri wa Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lengo lake ni kwamba anataka kuboresha uwekezaji nchini. Mimi ni Mbunge mkongwe, namfahamu Mheshimiwa Waziri aliye na dhamana ya Uwekezaji, Mheshimiwa Angellah Kairuki, nimshauri afanye kila jitihada kuhakikisha zao la pamba linapata wawekezaji wa textile industry.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo niongelee nchi ya Bangladesh. Nchi ya Bangladesh ipo katika Bara la Asia. Ni nchi ndogo, ina eneo la kilomita za mraba takribani 148,000. Pamoja na udogo huo, Bangladesh ina population ya watu wapatao milioni 165. Nalinganisha Bangladesh na nchi yangu Tanzania. Tanzania ukiilinganisha kieneo na Bangladesh ni kubwa ina eneo za kilomita za mraba 945,087 na kulingana na sensa ya mwaka 2017, population yake ni milioni 57.31. Nimependa kuilinganisha Bangaladesh na Tanzania kutokana na jinsi ambavyo nchi hii ndogo ya Bangaladesh….