Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdallah Majurah Bulembo (21 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniingiza katika jengo hili, lakini pili, nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.
Tatu, nimpongeze Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia, anawawakilisha wanawake wote hapa, mambo anayoyafanya mnayaona. Nne, nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Mwalimu Majaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika nichukue nafasi hii kuwapongeza TAMISEMI kupitia Waziri wake wa TAMISEMI kwa kazi wanayoifanya. Nimpongeze Naibu Waziri wake kamanda Mheshimiwa Jafo kwa ziara anazopiga. Katibu Mkuu Injinia Iyombe, mzee maarufu yuko pale TAMISEMI
inasonga mbele. Nirudi kwenye Utawala Bora, nimpongeze Mheshimiwa Angellah kwa kazi anazozifanya na Dkt. Ndumbaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina ajenda kubwa sana, ninayo mambo kama mawili au matatu. La kwanza kwa nini TAMISEMI inapongezwa. TAMISEMI ndiyo inashughulika na kila Mtanzania TAMISEMI kwa sababu ukienda kule kwenye Serikali ya Mtaa, Mtendaji wa Mtaa, Mtendaji wa Kata, Diwani na Mbunge ni wa TAMISEMI. Tunawapongezeni sana TAMISEMI na tuna haki ya kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa sababu TAMISEMI ndiyo imebeba mzigo wa Watanzania waliokuwa wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini namba mbili nihamie Utumishi. Utumishi kwenye kitabu chao wametuonyesha wameweza kugundua watumishi hewa zaidi ya 13,000. Si kazi ndogo, ni kazi ya Chama cha Mapinduzi kuelekeza lazima tuwaondoe mafisadi ndani ya Serikali yetu, tunakupongezeni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze Utawala Bora kwenye eneo la TAKUKURU. Kwenye taarifa ya juzi ambayo TAKUKURU waliwasilisha kwa Mheshimiwa Rais imeonyesha wameokoa shilingi bilioni 53. Siyo kazi ndogo, ni kazi ya kusifia. Vilevile tayari tumeanzisha Mahakama ya Mafisadi tuwaombe TAKUKURU basi wale mnaookoa zile fedha waende kwenye Mahakama, msikae na mafaili pale
mezani ili impact ya kuokoa na watu wameenda kufanywa nini ionekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu sitasema sana, lakini mdogo wangu pale amesema, jana hapa kuna watu wanabeza elimu bure. Tumeenda pale kwenye semina ya TWAWEZA watu wanabeza elimu bure, sielewi, inawezekana hoja ya mpinzani ni kupinga. Kama ilikuwa shule watoto
wanaenda 200 leo darasa linaenda watoto 400 kwa sababu elimu ni bure kuna haja gani ya kutoipongeza Serikali hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliyoiuza kwa wananchi waliokuwa wengi na tukasema elimu itakuwa bure. Leo mwezi mmoja shilingi bilioni 18 zinaenda si kazi ndogo, ni kazi kubwa sana.
Taarifa....
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni taarifa ambayo imeletwa na wale wanaojifunza Chama cha Mapinduzi kinafanya nini. Kwa hiyo, ngoja tuwaunge mkono kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisema na nashukuru imetoka kule, wao walikuwa na ajenda wanasema ufisadi, ufisadi lakini kwenye kutafuta kura wao wakakumbatia mafisadi. Nafikiri hiyo kumbukumbu wanayo vizuri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye kitabu cha msemaji wa jana wa Kambi ya Upinzani. Wakati anailaumu TAMISEMI kwa kupeleka maombi ya kutaka kujenga stand Moshi, sijui Halmashauri gani imetaka nini lakini mwisho akasema, TAMISEMI inakataa kuwaruhusu wasijenge stand kwa sababu wao ni wapinzani na akasema inaruhusiwa Morogoro na Tanga. Naomba nimjulishe vizuri ni Diwani mwenzangu huyo, ni mzoefu wa muda mrefu anaelewa taratibu za Local Government lakini ukisema Morogoro ni ya CCM, Tanga je? Umesahau una mtu wa hapa wa CUF ni Mbunge wa Tanga Mjini? Umesahau Halmashauri ya Tanga ni ya upinzani?
Taarifa...
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulikuwa Madiwani zamani hawa nao wakaja vijana, kwa hiyo, Diwani ukimsema lazima itafikia hatua hiyo.
Mimi nimesoma kilichoandikwa kwenye kitabu maelezo ya ziada ameyatoa kwenye mdomo wake saa hizi, kwa maana leo Tanga iko chini ya Upinzani na mradi unafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyongeza unavyoandika mradi kama Diwani katika Halmashauri yenu kwa nini TAMISEMI anapatikana? TAMISEMI ndiyo guarantor wa hiyo hela mnayotaka kukopa. Ni sawasawa na unapoandika mradi unaupeleka benki ni lazima Meneja
akubali huwezi kumlazimisha. Kwa hiyo, nashauri yale majiji yanayoandika miradi kuomba Serikali iwadhamini, andikeni miradi kwa kujifunza kwa wenzenu ambao wameshapata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahamia kwenye kitabu cha mama mmoja namheshimu sana. Huyu mama ni Mheshimiwa Mbunge, eeh ni mama kwa sababu hata nikimsema utajua ni mama.
Mheshimiwa mama, mama haifutiki. Huyu Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye Utawala Bora, Mheshimiwa Ruth Mollel, jana amesema hapa kauli nzito kidogo. Akasema Mheshimiwa Rais kwenye uteuzi wake wale wote waliogombea ndani ya CCM wakashindwa ndiyo wamekuwa Wakurugenzi, ma-DC na kadhalika. Swali langu dogo, Mama Mollel tangu amestaafu ni juzi, anataka kutushawishi kwamba aliingiaje CHADEMA, wale aliokuwa anaajiri alikuwa anaajiri Wakurugenzi kwa ajili ya maandalizi ya CHADEMA? Kwa sababu ni mtumishi ambaye amekuwa Serikalini mpaka amestaafu, anaheshima yake, anakula pensheni aliwezaje kutengeneza ajira ya wapinzani wengi
na leo siku tano anakuwa Mbunge anatokea ndani ya Chama cha Upinzani? Sasa nasema hivi Rais anayo mamlaka ya kuona nani anamfaa, nani amteue, nani amwakilishe katika Serikali yake anayoiongoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyongeza, heshima anayopewa huyu mama hebu aendelee kuiheshimu pamoja na kuwa yuko upinzani, ana siri nyingi za nchi yetu huyu. Ikiwa ataonekana huko alikotoka alikuwa anaandaa mazingira ya CHADEMA basi tutaangalia sheria zinasema nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba hoja zilizopo mbele yetu Tanzania ni moja.
Kuna mwenzangu jana wa Kigoma alikuwa anasema barabara yangu, eneo langu la wapinzani, sijui Mheshimiwa nini mwalimu lakini, nataka kuuliza mnaposema maeneo ya wapinzani hayahudumiwi elimu bora kuna mwanafunzi wa CCM na mwanafunzi wa CHADEMA? Mbona wote mnasoma elimu bure, mbona kule hamsemi hayo mazuri.
Ndugu zangu sisi ni Watanzania tukitoka hapo nje tunakunywa chai pamoja, tunapanda magari pamoja tusiitenganishe nchi yetu kwa itikadi zetu. Tutajenga mzizi ambao siku tukija kusema usifanyike gharama yake itakuwa kubwa sana. Tupingane kwa hoja, tushauriane kwa hoja na
siku ya mwisho tuwe wamoja kama Watanzania wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi niweze kuchangia kwenye hoja ya Wizara hii muhimu sana kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hiyo, Naibu Waziri wake Dkt. Kigwangalla, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nianzie kwenye hili la madaktari. Mwezi uliopita tulikuwa na sherehe zetu za wazazi pale Kagera, mojawapo ya kazi yetu ni kwenda kutoa huduma katika hospitali. Hospitali ya Mkoa wa Kagera inahitaji Madaktari Bingwa 21, madaktari waliopo ni wawili. Sasa naiomba Wizara hii, nina imani hawa wakubwa niliyowapongeza ni wasikivu sana. Ukitafuta ratio ya 21 na mbili pale watu wanapata shida sana. Nawaamini, lakini nichukue nafasi hii kuomba kwamba kazi mnayofanya ni kubwa lakini hao wenzetu hospitali inalemewa na hawana mahali pa kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili tulikuta tatizo lingine pale, kama alivyosema aliyemaliza kuongea sasa hivi. Tuipongeze Serikali kwa mara ya kwanza pesa ya dawa ipo katika Halmashauri. MSD inafanya kazi kubwa lakini inawezekana imelemewa sasa. Isaidiwe, iongezewe nguvu ili dawa zipatikane ziweze kwenda kwenye vituo vya afya na hospitali zetu. Kila unayemuuliza hapa kwenye Halmashauri yake, pesa zipi, dawa hatujapata kutoka MSD.

Kwa hiyo, nina uhakika Mheshimiwa Ummy na Naibu kwa kazi mnayoifanya hebu elekezeni macho yenu kule kwenye MSD, kwa sababu MSD ndiye anafikisha dawa kwa Watanzania waliokuwa wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru hicho wanachokipata lakini kila mtu anakwambia nimeshapeleka hela sijapata dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niende kwenye hiyo hiyo MSD. Tunaomba MSD ule utaratibu mliotengeneza kidogo wa kuweka alama kwenye madawa ya Serikali, kila dawa ya Serikali iwe na alama yake ya nembo inayojulikana ili tuweze kuendelea kutunza dawa hizi zisiende kwenye maduka ya watu binafsi. Katika hilo naipongeza sana Serikali, lakini sasa yale maeneo ambako hamjaanza kuweka zile nembo ni vizuri zile alama ziwepo ili mtu akienda kuuziwa dukani anasema ile ni ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu kwa sababu bajeti iliyopita kwenye eneo la dawa ilikuwa kama shilingi bilioni 50 au 65, lakini mwaka huu wameenda zaidi ya shilingi bilioni 200 na mpaka leo Serikali yangu imeshaweza kutoa zaidi ya shilingi bilioni 120, ni kitu cha kupongeza sana kwa maana kwamba Serikali hii inajali afya ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kwenye maendeleo ya jamii, ndugu zangu haya maendeleo ya jamii mbona wanyonge hivi? Kila Halmashauri utakayokwenda ukamkuta mtu wa maendeleo ya jamii hana hamu na kazi yake. Hapewi gari, hapewi huduma, haonekani kama ni mtumishi, kwa nini ndugu zangu? Hawa ni watumishi na wana haki kama idara zingine! Lakini wao wanakuwa ni watumwa fulani katika ofisi, hakuna mtu utamkuta amechangamka kwenye kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe, Wizara hii ni kubwa dawa zipo, mazuri yapo. Mheshimiwa Ummy hebu hamia hapo kwenye watu wa maendeleo ya jamii. Hawa ni watu muhimu sana katika taasisi yetu, shughuli zao ni nyeti sana. Lakini unakuta Mkurugenzi akisema lazima “ah wewe subiri” akifanya hivi “wewe ngoja bado kasma haipo.” Kwa nini hawa watu wawe wanyonge? Hebu tuwaongezee nguvu basi kama idara zingine zinavyofanya kazi ili na wao wawe na afya katika meza zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niongelee madaktari. Tunaipongeza Serikali, imesema inaajiri madaktari hao 258; mimi nafikiri tumpongeze Rais kwa uamuzi wa haraka. Hotuba ya wenzangu huku wamesema kwa nini watu wanasikia hamu kwenda kufanya kazi nje. Unajua ajira ni nafasi, zamani tulikuwa kila mtu anaweza kuajiriwa kwa nafasi zilikuwa chache, lakini leo lazima ikama iwepo, mshahara uwepo, na taratibu ziwepo ndiyo mtu aajiriwe. Sasa watu wameambiwa wanaenda Kenya na wanajua wanaenda kulipwa dola, kuna mtu atabaki? Habaki mtu ukishatamka dola.

Sasa Rais wetu tumpongeze kwa maamuzi ya haraka kwamba hawa waliokwishajitolea wanataka kwenda nchini nyingine kufanya kazi hebu tuwape ajira moja kwa moja watufanyie uzalengo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri badala ya kulaumu hebu tumpongeze Rais kwenye uamuzi huo. Rais hata kama mtu unatakiwa kupinga akifanya jema basi tumpongeze, na siamini kama kuna Mbunge yeyote wa upinzani atasema madaktari wanaoajiriwa kesho kutwa kwenye Jimbo langu wasije, yupo? Mtawapokea, sasa kwenye kuwapongeza tumpongeze Rais anataka kutuondelea ile kero.

Kwa hiyo mimi nimeona niseme lakini watani wangu wa upande wa pili kwamba hoja Rais akiajiri kote Watanzania tutapata faida ya wale wanaoajiriwa. Sasa msingi wa kubeza unapunguza nguvu ya wale watendaji wetu. Mimi niwaombe sana, mema anayofanya Rais wetu tumpigie makofi, yakiwa mapungufu mna haki ya kusema kwa sababu kazi yenu ni kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naendelea kusema kwamba akifanya mema Rais tumpongeze wala haina tatizo. Hata hivyo ninyi kukosoa ni jukumu lenu ndiyo maana mmekuja humu mkosoe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo mimi hoja zangu zilikuwa zinaishia hapo. Naunga mkono hoja, naendelea kuipongeza Wizara chapeni kazi, mko vizuri, fanyeni muungano, tuko nyuma yenu, Chama cha Mapinduzi kitawaunga mkono. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya, kazi ni kubwa, Wizara ni kubwa na ina mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu umenipa dakika tano nitaongelea maeneo mawili. Suala la kwanza nitaongelea eneo la wawindaji na kwenye eneo la uwindaji kwenye vitalu miaka minne iliyopita tulikuwa tunaweza kukusanya kama dola milioni 20, jana wakati tunaangalia tuko kwenye dola 4,000,000 hapa kuna tatizo. Suala langu naliomba Wizara ya Mheshimiwa Profesa Maghembe hebu kaa na watendaji wako wakuambie ukweli, maana yake wewe ni Waziri, wao ndiyo wanatenda, bahati mbaya hawa watendaji siku zote huwa wapo tu, mambo yakichachamaa ninyi wakubwa ndiyo mnaangaliwa, hebu ingia mwenyewe ndani huku ujue tatizo liko wapi ili uweze kupata ufumbuzi angalau vitalu hivi visiwe tena kama mapambo. Vitalu vipo vinatakiwa vilipiwe viingize hela kwenye nchi, watu wakiingia leo, kesho wanarudisha wanaondoka lazima kuna tatizo hapa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi tatizo ni ninyi Mawaziri au Katibu Mkuu, lakini kuna watendaji wa chini wanaoshughulika na eneo hili wakae na ninyi chini wawape maelezo ya kutosha ili Bunge lijalo angalau tuweze kuwa na kitu kizuri cha kuongelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu yangu ya pili ni utalii. Utalii katika nchi yetu ni shida, tunapata watalii milioni 1.2 nchi kama Tanzania yenye vivutio kila eneo, kwa nini Wizara hii haiwezi kuwekeza moja kwa moja kwenye Balozi zetu zilizoko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nje ukaangalia Balozi za Kenya utakuta kuna dawati la utalii na kwa sababu hawa wana ndege wanatafuta watalii unalipia risiti hata miezi sita, watu wanajaa kwenda kule. Kwa nini sisi kwenye eneo la utalii tunaweka pesa kidogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu cha Waziri bajeti kwenye utalii tumeweka bilioni mbili, wenzetu wa Kenya wameweka bilioni nane kwa nini? Ukienda pale TANAPA, Ngorongoro yale maeneo ni kwa ajili ya watalii. Kama tunaweza kukusanya bilioni 200, tunashindwaje kutoa hata asilimia kumi ya makusanyo yetu kwa ajili ya utalii? Kwa ajili ya matangazo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Balozi nyingi, kwa nini Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje isione suala la utalii ni eneo lake? Kila Balozi ikapewa amri na masharti kwamba utaitangaza Serengeti, utatangaza Ruaha, utatangaza Ngorongoro, tukienda kwenye Balozi zetu watu hawana habari. Mwingine amepelekwa kwenye Ubalozi kama mchumi, lakini hawezi kuongelea utalii anaona siyo eneo lake, lakini ni Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini Wizara hii, Mheshimiwa Waziri, usiombe kwa wenzenu kwenye Cabinet, kama makusanyo ya TANAPA ni shilingi bilioni 200 chukua asilimia 10, kama Ngorongoro 150 chukua asilimia 10, yale maeneo yote. Tukipata 50 billion shillings kwa ajili ya kwenda kutangaza watu watajaa, maana mtaji wetu ni watalii. Utakuta kwenye utalii tunaweka gharama nyingi, mambo mengi. Je, huyu ng’ombe anakamuliwaje kama hawezi kupewa chakula? Chakula nenda China kuna watu wangapi? Nani anatangaza utalii? Nenda Urusi, nenda Amerika, lakini Balozi zetu ajenda hii siyo yao! Wizarani watu wa utalii au TANAPA au Ngorongoro ukiwauliza nini wanafanya, hata matangazo, tukipita njiani pale tunaona Tigo, tunaona Vodacom, tunaona nani, ninyi mnatangaza wapi, utalii wa ndani? Vipindi mnatoa wapi? Watu hawajui! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Serikali iwape hela mkafanye matangazo. Kuna CNN, kuna BBC, kuna maeneo mengi hujawahi kuiona Serengeti. Mheshimiwa Hasunga amesema pale, mnaitangaza timu ya Serengeti, hata kuwapa jezi ambazo zimechorwa maana ya Serengeti ni nini, hamuwezi! Sasa huko mnakotangaza ni wapi au Mawaziri muingine ndani muangalie hizi hela zinazotangazwa zinatangaza kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ya Taifa ya Wanawake imekwenda Uganda pale, hata ku-brand tu kuiweka Serengeti ile gari peke yake moja, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuwezi kuwekeza kwenye utalii tutalaumiana kila siku kwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya bosi wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia kwenye Wizara hii nyeti.

Awali ya yote, kwanza nawapongeza Serikali kwa kuondoa tozo zile ambazo zilikuwa ni usumbufu sana kwa wananchi wetu hasa wakulima. Nawapongeza sana kuwa Serikali sikivu na kuweza kutuondolea hiyo kero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianzie kwenye mifugo. Kuna sehemu moja inaitwa Nkenge, Misenyi kule kuna blocks. Zile blocks kuna watu wamezikodisha lakini hawana mifugo. Ajenda hii ni ya muda mrefu, tangu alipokuwa Mheshimiwa Mbunge Mshama, amekuja Kamala na mimi leo naichangia ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Serikali ni nini? Serikali inajua, kwamba wafugaji wa eneo lile sio wale ambao wana asili ya maeneo yale. Watu wamechukua ma-block wanakaa Dar es Salaam na popote wanapokaa, watu kutoka nje wanaingiza mle mifugo wanakodisha. Wananchi wa eneo la Misenyi hawana mahali pa kufugia, wanatangatanga na mifugo yao. Wasukuma walioko huko wanafukuzwa, wanafanya nini, sasa Serikali ituambie, suala hili limekuwa la muda mrefu. Mheshimiwa Waziri wakati anakuja hapa hebu, aje na majibu mazuri ili usituamishie kwenye taratibu zile nyingine za kutaka kujua kwa nini mpaka leo Serikali inakuwa na kigugumizi katika eneo hili la Misenyi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wana haki yao katika nchi yao, lakini unafanyaje kumpa block mtu mfanyabiashara? Je, vigezo vyenu ni vipi vya kugawa hizi blocks wakati mnawapa watu? Kila mwenye hela ndio anapewa, lakini hana mifugo. Watu wanateseka, wanaangaika, watu wa maliasili wanakamata ng’ombe za Watanzania, zinakwenda kwenye shida, lakini wale watu maeneo yapo. Serikali haifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tunaomba majibu sahihi ili angalau tuwaambie wananchi wetu kule kwamba haki yao ya kufuga inafananaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye eneo la uvuvi. Wavuvi hasa nchi nzima sasa, wamekuwa wakichomewa nyavu zao, wakinyang’anywa, wakikamatwa wakisumbuliwa, sisi wavuvi tunafuata maji yalipo, lakini nyavu zinauzwa madukani na viwandani. Sasa Serikali pamoja na kwamba inakusanya kodi kutoka kwenye nyavu, ni lini italeta sheria humu Bungeni kwamba labda hizo nyavu zisitengenezwe? Kwa sababu mimi ni mvuvi, nimeshanunua nyavu, nimepeleka majini, kesho nakamatwa mimi na mali yangu. Anayepata hasara ni mtu huyu mlalahoi. Sasa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inawajali wanyonge. Wanyonge hawa wa kuvua, lini haki yao itapatikana? Kule anayewauzia, anawapa risiti. Kwa nini, hamnyang’anyi mkafuata mwenye duka aliyemwuzia akarudisha gharama yake basi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi kwa kweli ni shida. Mheshimiwa Waziri atuambie, ni lini wanaleta sheria ya hao wanaosabisha kuuza halafu wananchi wanaonunua ndio wanakuwa na hatima ya kunyanganywa mali zao, kufilisika, kupata taabu na kuchomewa mitumbwi? Ni shida sana. Kwa hiyo, naomba viongozi wa Wizara ya Kilimo na Serikali yangu tuleteeni majibu mazuri ambayo yatawapa imani wavuvi kule walipo baharini na ziwani ili wawe na amani na kazi yao kwa sababu ndiyo maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la ajira, ambalo pia ni eneo la Kilimo. Katika utaratibu, tunapenda viwanda, tunapenda uwekezaji, na kadhalika. Nataka kuuliza swali moja, nina mtu anaomba nimtaje kabisa, nita-declare interest. Kuna mtu anaitwa Vedic yuko kwenye Kampuni inaitwa Alpha Group. Mtu huyu mwaka 1997 sisi wavuvi wa Kanda ya Ziwa tutakumbuka, alikuja kama mhasibu kwenye kiwanda kinaitwa TFP (Tanzania Fish Process) pale Mwanza kama mhasibu. Kibali chake cha kuishi alikuwa na kibali Class
B. Leo ni miaka 20 anaitwa Manager Group. Hivi akija mtu kama mhasibu mpaka akafikia umeneja, Watanzania wangapi wanakosa kazi kwenye eneo hilo? Huyu mtu analindwa kwa style gani? Kibaya zaidi mtu huyu amezidi kuongeza wafanyakazi wa nje akiwaleta kama watalaam wa samaki, lakini watu hao leo tukienda pale Kipawa wanauza samaki. Yaani yupo pale anapokea hela ameingia kama mhasibu. Ukienda pale Kilwa wanavua mpaka pweza. Mtu amekuja kama mhasibu ni mtu wa nje, anazuia Watanzania kufanya kazi ambazo ana uwezo nazo, anavua samaki pale, anavua mpaka pweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka pale, shuka kule Tunduru anauza, Kilwa Kivinje anauza, Mtwara Supermarket wanauza, Lindi, Songea, sasa hivi ajira mnazilindaje jamani? Ninyi watu wa Kilimo na Mifugo, inawezekanaje akaja mtu miaka 20 anapewa kibali huyo huyo? Kile alichokuja kufanya, haijawahi kupatikana Watanzania wenye sifa hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema mimi ni mfanyabiashara wa samaki, namjua, wala sisemi kwa bahati mbaya. Anayetaka kunijibu aje nimpe majibu, ninayo. Mtu huyu ameondoa Watanzania wote kwenye ajira, analeta ndugu zake, wanawaingiza mle kama wataalam samaki, kazi wanayofanya sasa, wako mtaani. Lini Mhindi akaenda kuchukua pweza baharini? Amepita wapi? Vibali (permit) hivi nani anatoa? Tunawalindaje Watanzania wetu waliosoma ambao wazawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme, Serikali yangu naomba inisamehe katika hili, lazima niseme. Huyu mtu anaitwa Vedic katika nchi hii, yeye ni nani? Mpaka anaingia kwenye siasa, naye anachagua watu wanaotakiwa kuwa viongozi katika nchi hii. Kwa kibali kipi? Naomba Mheshimiwa Waziri aje na maelezo hapa, huyu Vedic ana kibali cha aina gani katika nchi hii? Kwa nini vibali watu wanavyokuja navyo hawavifanyii kazi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu kama RK ana miaka 20 nchini. Tangu alivyokuja Vedic, RK akaja, wakienda ukaguzi, wanafungiwa kabatini. Nchi ipo, kwa nini? Hawa Watanzania mnawasaidiaje? Raslimali ni zetu lakini mnasema wawekezaji waje, hamwendi kuwakagua na ninyi ndio maliasili pale. Ndiyo wazee wa uvuvi mko hapa. Kwa nini hamwasaidii Watanzania wenzenu? Viwanda hivi si viko chini yenu? Kwani hamna haki ya kuuliza? Sisi tunawapa data, wataalam wenu kule kama wame-associate na wale, nao mwende mwambie. Haiwezekani, haiwezekani mtu miaka 20 amekuja mhasibu, leo ni Group Manager, haiwekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda pale Mafia, nimekaa Mafia Kilindoni. Pale Vedic, miaka hiyo, mpaka leo, hapana! haki ya Watanzania lazima ipatikane. Haki ya Watanzania kama Wizara ya Mifugo, ninyi ndio mmekalia; tutaleta na maswali mengine humu ndani. Mheshimiwa Waziri bila kunipa maelezo ya kina, sijawahi kushika shilingi, lakini leo niko na wewe. Lazima unipe majibu ya kina. Inakuwaje mtu mmoja anakuja kama mvuvi, leo anataka na kwenye siasa atupangie nani achaguliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, nina swali na ninaomba kutoa maelezo kidogo. Hivi suala hili vipi? Hawa watu wetu wanaouana kila siku, wakulima na wafugaji, Serikali mmejipangaje? Leo tunaliongelea kwenye kilimo, lakini kwa mawazo yangu kidogo naomba nitoe ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili linaihusu ardhi, kwa sababu lazima ardhi apange maeneo ili watu wasiuane. Eneo hili linahusu maliasili, leo ng’ombe wako kule, wanafukuzwa, wanachinjwa, wanauzwa shilingi 5,000. Suala hili linahusu sheria, linahusu maji, lazima kuwe na visima na malambo ya watu ambako watu watawapeleka ng’ombe, linahusu TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri atuambie, lini mnakuja na ajenda ya kuwanusuru wananchi wetu kufa. Watu kuuana kwa kugombania maeneo ya malisho ya uchungaji. Lini mnakuja natafasiri kamili hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua suala hili ni mtambuka hamwezi kulifanya ninyi, lakini ninyi kama Serikali lini mtakaa kuleta majibu kuwaokoa Watanzania hawa.

Hawa watu wanaouana ni Watanzania, tuna haki ya kuwalinda, tuna haki ya kuwahudumia, lakini tukisema leo, wewe Bwana Mifugo utasema mimi sina ardhi, utasema sina maji. Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri atuambie, Serikali mtuambie lini mnaenda kukaa pamoja mkakutana mkaleta majibu ya yanayofanana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kwa kuniona. Kabla ya yote nimponze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya. Hongereni sana, endeleeni kuchapa kazi. Tunajua mna kazi kubwa lakini kazi mnayoifanya nayo ni kubwa, Watendaji wenu wa Wizara tunawapongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kuweza kumteua Katibu Mkuu Profesa Kitila ambaye anatokea ACT. Nataka kuwaambia Wapinzani, ukionekana unafaa kwenye CCM kazi utafanya. Usikate tamAa, Bwana Kitila fanya kazi na nina imani wale watakupa ushirikiano mzuri ili utekeleze Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, kwanza kuna ndugu yangu mmoja, Mheshimiwa Kangi Lugola, simwoni hapa, jana alisema watakaopitisha hii bajeti ataenda kupiga miluzi nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Mheshimiwa Kangi Lugola ana shibe. Pale Jimboni kwake Mwibara maji yako hatua tano. Anaweza kuamua kuvua samaki wa saa nne, wa saa nane, wa saa tisa; ni kama kata mbili hazina maji. Yeye maji yamemzunguka. Ila namshauri, akitaka kupiga miluzi, apige kule Mwibara, akivuka geti sisi kwenye Chama tutamdhibiti. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku-declare interest, mimi kabla ya kuwa Mbunge nilikuwa Mjumbe wa Bodi ya DAWASA. Waheshimiwa Wabunge, mliochangia naomba nikwambieni wazi, tunaweza tukachangia lakini hujaingia ndani ya nyumba kujua kuna nini? DAWASA imeundwa kwa mujibu wa Sheria; DAWASCO anakasimiwa Mamlaka na DAWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, historia inaonesha, huko nyuma tulikuwa na kitu kinaitwa NUWA. Tukaiondoa NUWA kupunguza mzigo, ikaja City Water na DAWASA. City Water akafeli, alivyoondoka DAWASCO akapewa nafasi hiyo ili aichukue kwa mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yanasemwa hapa, kwamba nani mzuri? Haiwezekani mwenye nyumba akawa sio mzuri, mpangaji akawa mzuri. Sisi wote tunaishi Dar es Salaam, kazi kubwa aliyonayo DAWASCO ni kukusanya kutengeneza matengenezo madogo, akishapata zile bili kutoka kwa watu, anapata pesa; lakini anayetengeneza miundombinu ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, anaitwa DAWASA. Kwa hiyo, haiwezekani mtu akatengeneza miundombinu, wewe ukakusanya pesa, ukaonekana uko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara na Serikali yangu, hebu tuwe makini. Msemaji wa saa hivi amesema, anaipongeza REA na TANESCO. Kwa nini imetoka TANESCO tukaenda REA? Kwa nini? Unaipunguzia mzigo TANESCO; REA imepatikana, inafanya kazi zake vizuri. Leo mna mpango wa kuiunganisha, naomba Wizara muwe makini sana, tusije tukarudi tulikotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo TANROAD ipo kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi. Kwa nini hatusemi Wizara ya Ujenzi iende ijenge? Leo tunataka kuanzisha Mfuko wa Maji Vijijini, kwa nini tunauanzisha mfuko? Suala hili ni kumwondolea mtu mzigo mkubwa ili angalau wafanye wengi, ufanisi uweze kupatikana. Leo kwa Dar es Salaam ufanisi upo. Maji yanatosha, DAWASCO wapo, DAWASA wapo, hili neno linatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, wazo lenu labda ni zuri sana, lakini mrudi kwenye historia, kwa nini tulitoka huko na tukafika hapa? Kama hatukwenda vizuri, tunataka kuanzisha mgogoro mpya katika Jiji la Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam leo limepanuka, lilikuwa na Wilaya tatu, leo lina Wilaya tano; watu wameongezeka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tena niseme, kwa sababu ukienda kwa DAWASA leo, ndani ya Ilani yangu ya Chama cha Mpinduzi tumesema katika ukurasa wa 106 kwamba tutajenga bwawa la Kidunda. Ni DAWASA hiyo!

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kuna tatizo la TANESCO kukata umeme kwenye Mamlaka za Maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini wananchi hawadaiwi, anakuwa anadaiwa Mamlaka za Maji; sasa mkikata maji kule TANESCO mnawaumiza wananchi kwenye miji!
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nijielekeze, kama wengine wote walivyosema, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Wana haki ya kupewa hongera kwa sababu kazi wanafanya na nchi inajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi sana lakini nina hoja kama tatu. Hoja yangu ya kwanza ni juu ya National Housing; National Housing kwa sheria iliyoiunda kwa miaka hiyo mingi iliyopita iliundwa kwa sababu kubwa, watu wa hali ya chini waweze kupata makazi ambayo bei yake ni nafuu. Hata hivyo inawezekana kwa sababu limekuwepo la muda mrefu tunawapongeza leo wanajenga nyumba nyingi zenye nafasi nyingi lakini zenye uwezo wa watu wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana anayetoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akaajiriwa kazi mahali fulani hana uwezo wa kupanga nyumba ya National Housing, ingawaje pamoja na kwamba msingi wake ulikuwa ni kutoa unafuu kwa wale wanaoanza maisha, wenye kipato cha chini. Ombi langu Mheshimiwa Waziri chini ya National Housing, hebu wafanye mara mbili basi, wajenge nyumba zenye uwezo wa watu wa vipato vya juu lakini wajenge nyumba zenye uwezo wa watu wa vipato vya chini. Kwa sababu Watanzania hawa wa vipato vya chini bado wanaishi mijini. Mfano mdogo Dodoma hapa, TBA ni Idara ya Serikali, National Housing ni idara ya Serikali, ukienda TBA nyumba yake, kwa Dodoma, Sh.150,000/= mpaka Sh.250,000/=. Ukienda National Housing pale Medeli, Sh.500,000/= mpaka Sh.600,000/=, ni walewale tu, na wote ni Mji huo huo wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ombi langu kwa National Housing, sitaki kuharibu kazi yao kubwa na nzuri wanayoifanya, lakini sisi wanyonge tunakwenda wapi mjini, tutapanga wapi, tunawekwa wapi? Mheshimiwa Waziri hilo anaweza kulifanya, wala halitaki maelezo marefu. Akiamua kufanya… (Makofi)

TA A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa. Ngoja nimpe faida tu. TBA ni shirika ambalo lipo chini ya hao na National Housing. Hebu nenda pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uone yale majengo ya kulala wanafunzi, amejenga TBA, kwani yeye hakununua saruji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kwamba National Housing, basi taarifa yake kama inalenga kule, Mheshimiwa Waziri, pale Dar es Salaam tuna nyumba Upanga, Tabora zipo, Bukoba zipo, tulizorithi mwaka 1967, hazina ukarabati zinaongezekaje bei? Kwa nini? Kwa sababu iko wazi kabisa, zipo nyumba za asili zilizoanzishwa National Housing hata ukarabati haufanyiki ingawaje wanazikopea kujenga nyumba nyingine. Kwenye ile mikopo wanayokopa si warudishe na huku ndani basi nyumba angalau ziwe nzuri na wote tunaoishi mjini tunazijua. Kwa hiyo, bado natetea hoja yangu; tunavyosihi mjini bado kuna watu uwezo wa kupanga ni wa shida lakini wana haki ya kukaa kwenye nyumba za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; huyu amenitoa kwenye mood; suala la kibenki. Mheshimiwa Waziri, mtu yeyote anapokwenda kukopa benki kwa kawaida lazima apeleke hati benki na anapokwenda kukopa benki, kama ni mke na mume watasaini wanakubali mkopo. Wakishamaliza kukopa, Wizara ya Ardhi inasajili ile hati kwamba hii hati iko benki kwa sababu ya mkopo; tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anashindwa kulipa mkopo wa benki, nyumba inaenda mnadani, watu wanakimbilia mahakamani. Tatizo langu linaponipata, wanatoka tena mahakamani wanakwenda kuweka caveat kwenye nyumba ambayo walienda kukopa, benki imeuza, inakuwaje sasa? Kwani ile hati huwa inakwenda pale Ardhi mnahalalisha kwamba ana haki ya kukopa kwa nini? Nyumba ina mkopo, inawezaje tena kwenda kuwekewa caveat?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linasumbua benki zisikopeshe watu wanaofanya biashara kwa sababu sasa wanakuwa hawaaminiki. Maana unakopa, kurudisha umeshindwa, mali yako inauzwa unakwenda kuzuia isiuzwe mahakamani, unakwenda kuzuia ardhi na ardhi mnapokea, lakini picha zipo, kila kitu kipo. Kwa nini sasa ardhi hii badala ya kuwalinda benki kama wafanyabiashara inawaingiza kwenye matatizo kwa kutoa hati ya kwanza ya akope na hati ya pili mtu akaweke caveat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, Mheshimiwa Lukuvi, tunaposema kupima, halmashauri zinapima lakini asilimia 30 hairudi kwenye halmashauri hizi. Wakishakusanya ile kodi wawarudishie, kwa sababu wakiwarudishia ile kodi watawapa msingi wa kuendelea kupima ili viwanja viwe vingi. Halmashauri inapima, pesa inalipwa ila asilimia 30 hairudi, sasa hii halmashauri wanaisaidiaje na tunasema tupime maeneo mengi? Wakati mwingine sehemu nyingine hela ya miradi inapatikana, lakini tunazo halmashauri za vijijini ambazo uwezekano wa ku- expand kuendelea kupima, hela ile isiporudi hawawezi kupima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo hoja yangu na ushauri wangu katika Wizara hii, kazi kubwa wanafanya, wala haitakiwi kutiwa doa, lakini wawaarudishie hizi halmashauri ili ile asilimia 30 iweze kuwapa nguvu ya kuendelea kupima katika maeneo yao. Nina uhakika suala hili nina imani ataamua, siyo akiamua, anaweza tu, hata akisema kwenye majibu yake kesho watatekeleza tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niligusie hilo walilosema wengi. Ni kweli tusipokuwa na sababu za kuwa na maeneo maalum ya kilimo na yakalindwa na yakatunzwa yasibadilishwe matumizi, kizazi kinachokuja kulima itakuwa shida sana. Itakuwa shida kwa nini, kama kuna mtu anataka kujenga nyumba si aende maeneo kavu kule ajenge? Hata hivyo, sehemu hii ina maji inaweza kumwagiliwa. Mheshimiwa Waziri, kama walivyosema wengi, hebu aangalie eneo la kisheria fulani. Otherwise, kwa sababu hali ya tabianchi inabadilika, mambo yanabadilika, tutakuja kujikuta sehemu ya kulima sasa kwenye mito na nini haipo, watu wamejenga kwa sababu wana hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie hapo kwa kuunga mkono hoja, nawapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ABADALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa kwa sababu dakika tano ni chache, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri Mbarawa na wasaidizi wake, Katibu Mkuu, wasaidizi wake wengi wa taasisi mbalimbali, kazi mnayofanya inapendeza, tunawaona kila siku mnavyochapakazi, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwanza kwenye eneo la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Kiwanja cha Ndege cha Musoma nimeona mmeweka pesa fulani hapa, lakini shughuli yake haitakuwa nzuri, lipeni wale watu fidia basi; kwa sababu tusipate hela halafu fidia ikawa shida. Muanze fidia twende kwenye uwanja, lakini tukianza uwanja watu watakwenda Mahakamani itaonekana kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, Kiwanja cha Ndege cha Bukoba; mmefuta ile Mkajunguti ambayo ilikuwepo kuanzia karibu miaka 43, tumesema tunakwenda pale Bukoba, basi tulipeni fidia tupanue uwanja ule, kwa sababu ndege chache zinatatua pale kama uwanja huo hautaweza kupanuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja mwingine ni Sumbawanga pale, mimi naongea Kitaifa kidogo. Pale Sumbawanga nao walipeni fidia uwanja uwepo. Sasa kwa sabbau eneo hili sehemu fulani imekwenda TANROADS ni vizuri sana mkasimamia zaidi angalau viwanja na ndege Bombadier zinakuja nyingi tunawapongeza ili ndege zifike kila mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze standard gauge, kwa maana ya TRC. Hawa watu wanafanyakazi kubwa sana ambayo ilikuwa haijafanyika siku zote, na ni kitu cha historia. Lakini naomba wale wanaokwamisha kuzuia kubomoa Serikali ifanye kazi yake kwa sababu Serikali inatakiwa kutenda. Huwezi kubomoa kuanzia Dar es Salaam ukifika pale katikati ya Tabora mtu anakataa, standard gauge itafikaje? Tuwape ushirikiano na Wizara yako Mheshimiwa Mbarawa endeleeni kufanya ukali, haki ipatikane sisi tunataka maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kuhusiana na minara ya simu. Sisi tunatoka kwenye mikoa ya mbali kule. Ukianda pale Musoma, Sirari ukisogea kidogo inainga Safaricom, ukienda maeneo ya pale Bukoba karibu na Mutukura inakuja tena inaonekana unaanza kutumia roaming, wale wananchi mnawatesa, ni Watanzania, lakini nguvu ya upande wa pili inakuwa kubwa zaidi katika kutumia mawasiliano, kule tatizo lake naomba mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye TTCL, naomba niwapongeze Mwenyekiti Nundu na kijana Kindamba, kazi yenu ni kubwa mnayoifanya. Leo nilishawishi Bunge hili, kwa nini Wabunge mnakwenda Vodacom, Tigo hamtaki TTCL? Ndiyo yetu hii, ndiyo mali yetu. Mimi naomba tutumie hoja yangu kwamba kila mmoja akitoka nje ajiunge na TTCL, ni muda mfupi ujao miaka miwili TTCL itakuwa imepanda kuliko kampuni nyingine. Lakini unaweza kukuta hata ninyi Mawaziri TTCL hampo. Ninyi ni Mawaziri mnatumia pesa ya Serikali, TTCL hamjajiunga. Kwa kupitia hoja hii Waziri Mkuu, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu uwaulize Mawaziri wako wangapi wako ndani ya TTCL, ndiyo kwa sababu wanatumia hela yetu ya kodi lakini hawajiungi na TTCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu Bandari ya Dar es Salaam; nichukue fursa hii kuupongeza utawala ulioko Dar es Salaam, mambo yanatoka pale, mizigo inaondoka haraka. Tunaomba nguvu hiyo isirudi nyuma kwa sababu wako wachache wanaokwamisha kwamisha juhudi zile. Wachukulieni hatua sisi tuendelee kupiga maendeleo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu TANROADS. Hivi TANROADS Mheshimiwa Mbarawa, TARURA mmewapa asilimia 30 si mkae mapema muongezee hata wapate 40, barabara ni nyingi za vijijini kuliko hizi barabara kuu? Kwa nini mnajipendelea? Maendeleo ni yetu wote, kwa sababu TARURA wana safari ndefu zaidi na ndiyo wanaanza.

Nasikia kwenye bajeti ya juzi nao viwango vya mishahara hamtaki kuwapa, hapana, tuwe fair, TANROADS wanaopata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABADALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami nafasi hii ya kuchangia eneo muhimu sana hili la michezo. Pongezi zangu nizipeleke kwa kaka yangu Mheshimiwa Harrison Mwakyembe na Mheshimiwa Naibu wake, Katibu Mkuu, Watendaji wote na Ma-CEO wote waliokuwa katika taasisi zake. Pongezi zaidi nisisahau kuzipeleka kwenye timu yangu ya Simba ambayo inakaribia kuwa bingwa wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, pongezi zaidi zipelekwe kwa timu yangu ya Simba ambayo inakaribia kuwa bingwa wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mataifa yaliyoendelea, katika eneo la michezo wamekuwa wakiwapa nafasi wachezaji wao. Ni eneo muhimu sana kwa maendeleo ya nchi zao. Mfano, kwenye bajeti zetu hapa tunatafuta hela nyingi za barabara, maji na afya. Mataifa yaliyoendelea yanawekeza kama tunavyowekeza kwenye barabara, afya na elimu. Nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtoto aweze kuandaliwa, lazima uanze naye chini. Huyu anaweza kuikimbia, huyu anaweza kucheza mpira, anaweza ngumi, anaweza kutupa tufe; lakini wanaowekeza hivyo kila mwaka wanapofika kwenye mashindano ya Kimataifa utaona wanapokelewa na medani nyingi, wanaongeza uchumi wa nchi yao, wanaongeza pato la nchi yao. Kwa hiyo, katika michezo hii ni ajira, ni mapato, nchi inapata. lakini kwetu hapa sijui sana tunakwendaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye michezo ya Madola, ukienda kwenye michezo ya Olimpiki nchi nyingi, angalia jirani zetu Kenya wanakuja na medali. Hakuna medali inakwenda bure. Kila ukiona medali ni pesa zimeingia kwenye nchi yao. Sasa sisi ukiangalia historia ilivyo, tumeweza kupata medali kama sikosei, ilikuwa mwaka 1980, tulipoenda kushiriki Olimpiki Urusi na medali mbili ndiyo tulipata hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye sports ni 1992 kama sikosei kushiriki mashindano ya Afrika. Kuanzia hapo, shughuli hii ni kama haipo. Ni kwa nini? ni kwa sababu hatujakubali kuwekeza kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachezaji waliokuwa wengi ni sawasawa na waimbaji walivyo. Anajitokeza mchezaji mmoja kwa hiari yake, wanajitumikisha, anafanya nini, anapatikana, anafikia viwango tunaiambia Wizara anaondoka kesho njoo umkabidhi bendera. Huyu mchezaji katengenezwa na nani? Nani anajua alipo? Nani kamfanyia maandalizi? Thamani yake ni ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu katika eneo hili la mchezaji mmoja mmoja ndiyo tunashiriki naye, nchi yetu itaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, tuelekee kwenye vyuo. Katika nchi yetu Chuo cha Michezo ni Malya na Kaole kinachoitwa Chuo cha Sanaa. Ukiangalia kwenye bajeti ya maendeleo Malya ni shilingi milioni 150. Tuko serious? Tuna nia njema? Chuo hiki kinakufa. Mheshimiwa Mama Ndalichako nataka baadaye anijibu, Chuo hiki ni lini kitaweza kutoa degree katika nchi hii? Kwa nini kinachechemea? Kwa nini hawakithamini? Tunapendaje michezo ambako hatuwezi kuwekeza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende TAMISEMI. Kila mwaka wana UMISETA na UMITASHUMTA. Wanaokwenda kuratibu mashindano haya na kuwapata wachezaji, mnawatoa wapi? Au unamchukua Mwalimu kwenye darasa, anajua kufunga goli, unamwambia wewe ni Mwalimu wa Michezo? Haiwezekani. Chama changu na Serikali yangu tumetamka ndani ya Ilani kuendeleza michezo. Tunaendeleza michezo kwa kusababisha Malya kupata shilingi milioni 150? Chuo pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michezo hii, ukitoka hapo Mzee Mkuchika simwoni humu ndani, lakini naomba wanijibu wakati wanajibu; katika ajira 52,000 nataka aniambie Maafisa Utamaduni ni wangapi? Maafisa Michezo ni wangapi katika ajira hiyo? Katika Halmashauri, Maafisa Utamaduni hawa wapo? Wanafanya kazi hii? Au tunapenda michezo watu wamejishindia wenyewe tunawaita Bungeni kuwapigia makofi hapa! Tumewaandaaje? Tunawaandaa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Serikali yangu, haiwezekani. Kama tunataka kusimamia michezo, tuweke msingi kwenye michezo. Michezo hii ni ajira sana. Naomba niwapongeze TFF, bora kidogo wanachokipata tunakiona, wanaandaa timu za vijana under 17, under 20 wanashiriki, bora wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu aniambie TOC hela zao ziko wapi? Mashirikisho yoyote yaliyosajiliwa hapa nchini yanapata pesa kutoka nje. Pamoja na kwamba zile pesa zinatoka nje, wanaziratibu vipi? Wanamsaidia nani? Au ni meza tu watu wemekaa, ukishajili NGO yako, noti zinaingia, mambo yanaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumempata kwa Mheshimiwa Waziri pale mtu mmoja, nilisikia anamteua Mwenyekiti, Mheshimiwa Leodegar Tenga, mimi namkumbuka kama Mwalimu wangu. Wakati nagombea FAT alikuwa ananihoji, nashinda. Baadaye naye ameenda FAT, TFF, leo amekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo yangu kwa Mheshimiwa Waziri, naomba Baraza la Michezo atakalolizindua alipe kazi ya kwenda kupitia sera hii. Sera ya Michezo ni butu. Mpira na riadha katika Tanzania siyo mchezo peke yake. Kuna ngumi, karate, boxing na vitu vingi sana vipo, vinapatikanaje? Vinapatikana wapi? Wanaviandaa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri wakati mwingine akatae kwenda kutoa bendera, kwa sababu haiwezekani Serikali inatoa bendera, haimwandai anayeenda kushiriki michezo hiyo. Anamwandalia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kunijibu, aje na maelezo mazuri ya kuniambaia kama yuko tayari, wanaposema Sera ya Michezo ipo, imekuja lini hapa tukaipitisha ili wakatayarishe kanuni watu wakajua? Kwa sababu ipo ndani ya makomputa, iletwe hapa kwenye Bunge lijalo tuambiwe tunataka kufanya hiki na hiki kwenye michezo ili tuendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tupate mabadiliko ya kweli kwenye michezo. Lazima tukubali kuwekeza kwenye michezo, lakini hatuwezi kuipata michezo bila kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri; haiwezekani bajeti ya maendeleo ikawa shilingi bilioni nane. Kamati inasema tumeongeza. Wameongeza nini? Wameongeza asilimia 20. Nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC, nataka nitoe mfano. Nilibahatika kutembea kwenye nchi hii nikiomba kura na Mheshimiwa Rais wa nchi hii. Tulikuwa na chombo kimoja kinaitwa Star TV. Tukisema mkutano saa 4.00 anaweka chombo, tunarusha nchi nzima; tukisema saa 7.00, anaweka tunarusha nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC leo, Mheshimiwa Rais leo yuko Kondoa, Mheshimiwa Waziri Mkuu leo aende Nyasa, Makamu wa Rais aende Zanzibar, TBC haiwezi. Haina vyombo kwamba unaweza kumwona Mheshimiwa Rais ukamwona Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Kwa nini? Chombo hiki ndiyo cha nchi. Hizi hela amepewa hapa shilingi bilioni tano hazitoshi kabisa, yaani hawezi kuiweka TBC ika-compete na watu wengine kwa shilingi bilioni tano. Ni hela ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tutailamu TBC, tutawafukuza kila wanaokwenda kila siku, lakini kama hatukuwawezesha, tunategemea lini wafanye kazi vizuri? Nilitaka kusahau pale kwa Mheshimiwa Waziri Jafo, naye anijibu hapa ndani. UMITASHUMTA na UMISETA, wale Walimu wanaoenda kuchuja, wanawapata wapi? Wanawapataje? Au wazazi wanatoa hela, watoto wanaenda kule, majibu hayapatikani? Kwa sababu Wizara hizi ni mtambuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akifika hapa anijibu, lini Wizara inayohusiana na michezo walikutana kikao? Walikutana wapi? Waliamua nini? Wanaendeleza nini? Kwa sababu hapa kuna elimu, hapa kuna utumishi, hapa kuna TAMISEMI na Wizara yake. Lini wanakutana au kila mtu anafanya lake? Haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie hapa Bungeni, kwenye michezo niliuliza swali, kiti hicho alikuwa amekalia Mheshimiwa Mtemi Chenge...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi pia nimpongeze Profesa Waziri wetu, Naibu wake, Katibu Mkuu, watendaji wote na Wakurugenzi walioko Wizarani pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na sehemu moja Serikali yangu wakati inakuja inipe majibu. Nianze kwenye muundo huu ambao ni sera ya shule za msingi na sekondari ambapo wanafunzi wanatakiwa hawa walioanzia mwaka 2015 tangu sera imetungwa wataenda mpaka darasa la sita. Lakini hapo nyuma mwaka 2014 kuna wanafunzi nao ambao wanamaliza mwaka mmoja huo huo. Kwa hiyo, tuna watu wawili mara mbili, wengine wa darasa la sita wengine wa darasa la saba kutokana na muundo mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ninalolipata Serikali yangu imeshajiandaa kuwapokea hawa wanafunzi watakaomaliza la saba na la sita wote kwenda sekondari kwa mara moja? Kwa sababu hawa wanafunzi watakuwa wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mtindo huu kwa hawa walioanza kwa maana ya mwaka 2015 wanaoishia la sita na hawa wa mwaka 2014 wanaoishia la saba, sijui mtafanyaje? Tunawapokeaje? Shule tunazo, maandalizi mmenza rasilimali watu na walimu wa kufundisha? Kwa sababu ni double, kwa sababu wamemaliza hawa na hawa wamemaliza, mtihani ni huo huo mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo napata tabu kidogo kwa maana sijui, maana mwaka 2020 tuna mambo mengi, kuna uchaguzi, tuna mambo gani, kuna wanafunzi wengi wanamaliza wenye mitihani miwili la sita na la saba kwa wakati mmoja. Naomba Serikali ijipange kidogo na ikija hapa inipe majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni kuhusu suala la elimu. Ndugu zangu Awamu ya Tano kwenye elimu bure ni suala linaloenda kumuangalia mtoto wa maskini, si la bahati mbaya na elimu hii sio wale ambao mmezaliwa ninyi kwenu mnasoma tu, wale watoto wa wavuvi, watoto wa wakulima wasisome, hapana. Awamu ya Tano inaposema elimu bure ina maana huyu mama mpika kitumbua hawezi kulipa mtoto wake asome. Ndiyo dhamira ya Serikali iliyopo, kwamba kila mtoto anayetakiwa kwenda shule na aende na iko wazi, walivyosema elimu bure wametoka milioni moja wameenda milioni mbili, hiyo ni picha halisi inayoonesha kwamba tunao wengi waliokuwa wanabaki nyumbani bila kwenda shule kwa sababu ya mambo ya kulipa, naipongeza Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna watu wanasema elimu imeshuka, elimu sijui kufanya nini, mimi nakataa. Nakataa kwa sababu zifuatazo, nitakataa wewe una miaka 20 mimi nina 57, lazima nikatae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakataa kwa sababu, zifuatazo; sisi miaka yetu ilikuwa unafanya darasani mtihani vipindi vitano, kila kipindi marks 50. Ukipata marks 244 huendi sekondari, kwa sababu shule hazipo, lakini wale wazazi ambao walikuwa na uwezo akikupeleka private na huyu aliyeshinda kwenye kijiji mtu mmoja mkienda form four wote mnakutana kwenda high school; miaka hiyo ambayo watu hawataki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kila mwaka ukienda watoto wanaendelea kuzaliwa na changamoto ya elimu inaendelea, idadi inaongezeka, haiwezi kufanana. Unalinganisha na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kila kitu ni historia, historia inakataa kwamba mwalimu fulani aliposoma kwa sababu madarasa yalikuwepo na shule zilikuwa chache wanaenda wachache. Leo hii ukienda elimu ya juu watoto ni kama 150,000 wanaoenda kwenye vyuo wanadahiliwa na wanalipiwa na Serikali, lakini miaka ile walikuwa labda 20,000, sasa tutalinganishaje? Ndio maana nawapa Serikali yangu tahadhari kwamba kuna kitu kinaongezeka hapa. Mnapodahili watoto wa la saba wakawa wengi, je, miundombinu tumeongeza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naipongeza Wizara ya Elimu kwamba mnachokifanya ni sahihi na elimu iko vizuri. Marekebisho lazima yawepo, hatuwezi kutoka mbinguni, lakini kuna rafiki yangu mmoja amesema pale kwamba lakini watoto wa Wabunge wanasoma nje, okay, wako watu wanasomesha watoto nje, lakini mtoto wa dada yake je? Wa mjomba wake je? Kwa hiyo, tunapoongelea elimu tunaongelea kwamba elimu ya watu wote sio ya watu baadhi ambao wamechaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na watu ambao wamelisemea suala la lugha. Mimi nafikiri tufikie mahali Serikali ifanye maamuzi na maamuzi yenyewe yawe magumu tu. Kama tunaanza chekechea mpaka form five mpaka form six ni kiswahili, iwe kiswahili basi. Kwa sababu mtoto ili aweze kujifunza ni lugha gani anatokanayo nyumbani kwao. Hakuna mzazi ambaye ana mtoto akishajifungua ameanza kutambaa akaanza kizungu, ninyi wa mjini ndio mnafanya hivyo, lakini wa vijijini wote ni kiswahili, sasa tunakikwepaje kiswahili kwenda kujifunza lugha za watu wengine? Ndiyo lugha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na leo kiswahili kina nafasi kubwa ulimwenguni, watu wanaotaka kujua kiswahili ni wengi, wanaokuja kujifunza kwetu ni wengi, tunakiogopa kwa nini? Serikali mimi nasema biashara ya kizungu mtakutananayo huko Ulaya, hebu tuamue kwamba tunataka Kiswahili kutoka chekechea mpaka chuo kikuu, dhambi ni ipi? Kwa nini tunakwepa chetu? Fanyeni maamuzi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna watu wanasema kweli kiswahili ni kigumu, lakini ni kwa sababu hatufundishwi tunakiongea tu. Wakija wenzetu wanakuja kujifunza kiswahili wanajua fasihi, wanajua fasaha, wanajua nini. Kwa hiyo, Serikali yangu iamue kwamba lugha iwe ni fulani kufundisha kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu, sio aibu. Mbona tukienda mikutano ya kimataifa kila mtu anawekewa lugha yake mnaelewana? Kwa nini sisi tunaogopa kiswahili kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende Mkoa wa Kagera; Mheshimiwa Waziri Kagera pale tumeona mnadalili za kujenga Chuo cha VETA, pesa mnazo, watu kila siku wanazunguka. Naomba wakati kwa majibu yenu, mnaanza lini na mabilioni mmeshapewa yako benki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wamesema pale watoto wanamaliza la saba hawana mahali pakwenda. VETA ingekuwepo, Mkoa mkubwa kama Kagera ingesaidia sana hawa wazazi. Tunawaomba sana, suala hili la elimu jamani tuhurumieni wengine, Mkoa kama Kagera kwenye karne hii VETA haipo, pesa mnazo mmekaa nazo Wizarani. Pamoja na tunawapongeza, lakini mnatuumiza, haiwezekani. Kama pesa zipo si watu waanze, tatizo ni nini? Naomba wakati Waziri unarudi hapa kuja kuleta majibu uje vizuri maana sisi wengine! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, michango..., Dakika tano au kumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango shuleni. Kuna shule nataka kushauri tu; kuna shule ambako kule michango tumeiondoa, lakini watoto wengine walishazoea kunywa uji, wengine kula mchana, kule kumeporomoka sana, watoto hawarudi shuleni. Hamuwezi kuja na mawazo mapya kwamba pamoja na kwamba michango bure kwenda shule na na nini, lakini ile ambayo wazazi wanafanya kwa hiyari mkaipa nafasi ili angalao watoto wao wasishinde njaa wakapata hata uji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu shule za kwetu kule vijijini kuna hamasa nyingi ambazo watoto wanaenda shule. Akishika kikombe asubuhi anawahi shuleni anaenda, lakini akishajua na uji haupo na mchana hamna chochote hali inakuwa mbaya. Tumeamua tusichangishane, lakini je, ile michango ya hiyari nayo ni migumu? Mtufafanulie kidogo tujue maana tukienda huko nje tunaulizwa maswai mengi na maelezo mengi yanakuwa hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, juzi hapa niliuliza maswali hapa kuhusu Vyuo vya Michezo, nikajibiwa haraka haraka na wapenzi wenzangu wale wa michezo. Hebu Wizara ya Elimu mtuambie, zilikuwepo shule kama Butimba ambazo ni special kwa sababu ya elimu ya michezo tu. Ziko nyingi, zilikuwepo shule kama Korogwe, vilikuwepo vyuo kama flani, kwa nini mmezuwia michezo isiendelee shuleni? Kwa nini? Kwa nini hili suala mnaliondoa? Hawa watu watafundishwa wapi? Naomba mnipe majibu mazuri kwenye suala la michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vyuo vilienda Wizara ya Habari ambavyo navyo vinachechemea, lakini ninyi kwa sababu ni fani yenu, turudishieni vyuo vyetu. Kama mlikuwa na crush programme imeisha, lakini suala la wanamichezo kupata mahali pa kusoma ni la muhimu sana.

Sasa msije mkatuambia kuna UMITASHUMTA, kuna UMISETA, lakini vyuo havipo, mmevifunga havifundishi, masomo haya darasani hayafundishwi michezo mmeondoa, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nawaombeni sana suala la michezo msilifanyie mchezo. Suala la michezo ni ajira.

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siipokei sana kwa sababu inawezekana mwenzangu hata tangu mwaka umeanza hajagonga passport, kwa hiyo, sio tatizo sana. Lugha ziko nyingi, watu hana anayesafiri na lugha moja ya kizungu kuna nchi zinaongea kiarabu peke yake, kuna nchi zinaongea kireno, kiitaliano, hawajui kiingereza chenu hiki, kiingereza kiko kwenu huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa namalizia kwa kusema kwamba mimi kwenye michezo, bado naendeleo huko huko, Wizara ya Elimu mrudi mjipange, muangalie vyuo vyetu vilivyokuwa vinafundisha michezo mturudishie ili taaluma hii isipotee, lakini tukiwa na walimu ambao wanajua kucheza, akipiga mpira ndio mtaalam, haitusaidii katika nchi. Tutaacha kizazi ambacho hakiwezi kucheza na utamaduni ule ukipotea Taifa linapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishia hapo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ingawaje dakika tano ni kidogo, ngoja nijaribu tuone.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya na Naibu wake. Ziara zenu zinaleta tija Mwenyezi Mungu awape afya, muendelee kufanya kazi kama mlivyoagizwa. Nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu kwa kazi wanazozifanya. Vumilieni tu kwa sababu lazima tuwaseme kidogo kwa sababu kwenye Idara hiyo, lakini kazi mnachapa na Mungu anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie hapa, ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye eneo la maji tumesema kutakuwa na wakala wa maji, ndani ya ilani, leo tunaelekea mwaka wa tatu. Mheshimiwa Waziri kitu hiki ni muhimu sana kwa sababu kila ukiangalia Wabunge wanaosema wengi siyo wa mijini waliokuwa wengi ni wa vijijini, ni wa vijijini kwa sababu pesa zile ziko kule chini ndani ya Halmashauri ndiyo wanafanya nao kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hali ilivyo Wizara yako ni inaingiliana na TAMISEMI, Engineer aliyeko kwenye Halmashauri ukienda kesho kwenye ziara akiwa ameiba wewe huna file lake, file lake liko TAMISEMI. Chochote kitakachofanyika kule chini utaenda utafanya ziara, wanaoamua ni watu wengine. Wakala huu unakuja kukusaidia ninyi, kwa sababu leo ukija mijini tunazo zile taasisi kwa maana kuna bodi, kuna ile taasisi iliyoanzishwa, mjini hakuna shida, lakini wakala huu ukipatikana utakusaidieni sana ninyi Wizara. Kwa sababu unavyoenda kwenye Halmashauri Mhandisi yule unaweza kumuwajibisha, kama siyo hivyo utaenda kwa Katibu Mkuu Profesa, Profesa amwambie Mzee Iyombe, hapa kama hakuna mahusiano ya karibu nayo ni shida. Kwa hiyo, neno wakala hii ni muhimu sana. Muende kwenye meza mjipange, mliandae lije huku wabariki ili mpate wepesi wa kazi zenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwa utaratibu wa Madiwani tulivyokuwa tunaishi huko Mkuu wa Idara kumshughulikia, siyo rahisi ukatoka maji ukamshughulikia aliyepo TAMISEMI ni kazi ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali yangu suala hili kwa sababu, liko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi muende mezani mkae nao tuanzishe wakala huo ili uwape wepesi katika kazi zenu mnazofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niseme dogo hapa, katika Bunge lililopita hapa katikati kabla ya bajeti ndani ya Bunge hili tulikubaliana tuunganishe DAWASCO na DAWASA, ndani ya Bunge humu, ilipita hapa kwamba, DAWASA mpya azaliwe, lakini wachangiaji wengi humu wanasema mara DAWASCO mara DAWASA, hapana. Tulishakubali New DAWASA ipatikane, tuwape nguvu suala hili litekelezwe kwa sababu lilishapita ndani ya Bunge. Kwa hiyo, nakuombeni sana Wizara wala msirudi nyuma, yale mliyokwishayafikia undeni taasisi ili watu wa Dar es Salaam wapate maji kwa urahisi na watu wa Mkoa wa Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Dar es Salaam pale kuna shida moja, wakati wanaleta maji kutoka Ruvu Juu, Waziri ulishanijibu siku moja hapa ndani kuna watu wamekataa kutoka kwenye miundombinu ya maji pale, wameenda Mahakamani wameshindwa, lakini mpaka leo tunavyoongea hawataki kubomolewa, kunaingia siasa, ninyi ni Wizara, isaidieni DAWASA, wale watu wavunjiwe ili watu wa Chuo Kikuu wapate maji, kwa sasabu mtu ameshashindwa Mahakamani anatakiwa kutoka, mpaka leo hajatoka analindwa na nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nani anamlinda tusaidieni tu? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unakuja kwenye majibu yako, hebu njoo na majibu tunafanyaje kuwasaidia hawa watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii inatengenezwa na watu kutoka nje, wameshalipwa akifika pale anasimama anaanza kutudai Serikali alipwe fidia kwa sababu mmemchelewesha kumaliza kazi. Naomba Wizara mkija hapa mtuambie, kama mnaruhusu kwa sababu alishashindwa Mahakamani kwa mujibu wa sheria abomolewe mtamke wazi, ikishatamkwa sasa kule waulizwe kwa nini wale watu hawajaondolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme hili la jumla, ajenda ya maji kuna watu wanasema Tume na kadhalika, hebu mpeni Mheshimiwa Waziri huyu nafasi, amekuwa Waziri mwaka mmoja mnamuundiaje Tume? Alikuwa Naibu Waziri, ukiwa Naibu Waziri kama Mheshimiwa Aweso siyo mwenye Wizara. Huyu anao mwaka mmoja ndani ya Wizara leo unamuundia Tume, unaenda kufukua kaburi au unaenda kufanyaje. Tumpe nafasi, afanye kama anavyofanya na umri wake anajitahidi ili tumuunge mkono. Mpitishieni bajeti ili kipindi kijacho sasa kama liko jambo muweze kumuuliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika tano sina uwezo wa kuzipanga, acha niseme hayo machache, naomba kuunga mkono hoja tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi nashukuru kupata nafasi hii lakini awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa kaka yangu Mwijage na Naibu wake Engineer Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayoifanya, hongereni sana. Mungu awape nguvu ili mfikishe jahazi lenu hili, lakini nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu wake wawili, watendaji wakubwa wa taasisi zenu, kule Sabasaba, TBS, na kadhalika shughuli tunaziona. Endeleeni kuwa na nguvu mtumikie Taifa lenu. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianzie kwenye kupanda bei kwa vifaa vya ujenzi. Kwenye miezi mitano iliyopita, nondo zimepanda kuanzia mwezi wa tisa mwaka jana nondo ya milimita12 ilikuwa inanunuliwa shilingi 15,000 sasa hivi unanunuliwa kwa shilingi 22,000 na nondo ya milimita 10 ilikuwa shilingi 12,000 sasa hivi ni shilingi 16,000, mabati, bundle lilikuwa shilingi 250,000 sasa hivi shilingi 300,000; saruji, ilikuwa shilingi 12,000 sasa hivi ni shilingi 17,500 kuna nini kimetokea? Wanaojenga wanauliza, kuna nini kimetokea? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hebu tupe majibu tuwaambie Watanzania, kuna tatizo gani kubwa limetokea ndani kwenye eneo la ujenzi kwa sababu vifaa hivi ni vya watu wa kawaida ndiyo maisha yao ya kila siku wanaojenga nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kubwa kuliko vyote, viwanda. Viwanda vingi vilibinafsishwa lakini watu waliobinafsishwa viwanda hivi wameshindwa kuviendesha.

Serikali kupitia kwa Rais Magufuli nimeshasikia mara mbili Mheshimiwa Mwijage anakwambia wanyang’anye, anakuambia na ndiyo Rais wa nchi lakini kwanini huwanyang’anyi? Hao watendaji wako kwanini hawakusaidii? Mifano hai, kuna watu wamepewa viwanda vina mashine, sasa hivi havina kitu, hivi huyu naye kumnyang’anya ni shida? Tunafanyaje kwa sababu viwanda hivi hawa watu wakinyang’anywa kuna wawekezaji watakaokuja watakuta viwanda vipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam kuna kiwanda kimoja kinaitwa Uzi Bora Ubungo Spinning. Kile kiwanda yule mtu ameng’oa kila kitu, watu wanakodisha mle kuweka mizigo. Ukiweka mizigo, unalipa hela yake, inaendelea. Hivi jamani, tunafanyaje? Mheshimiwa Mwijage na Mheshimiwa Stella Manyanya mnafanya makubwa, hebu waambieni watendaji walioko chini wanaowahujumu hivi navyo vinataka sense gani ili kuwanyang’anya? Mpaka iweje? Yaani ni nini kifanyike? Ukienda Masasi kule kuna viwanda pale vilikuwa vya korosho, watu wameng’oa kila kitu wanafanya maghala, wakulima wa korosho wanaenda kukodisha kwenye kiwanda chao kulipwa wakati wa msimu wa kuvuna korosho. Tufanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaheshimu sana hawa ninaowasema lakini naomba mje na majibu, haiwezekani, Rais amesema wanyang’anye viwanda, hamwanyang’anyi kwanini? Kwanini? Kwanini hawanyang’anyi? Kwa nini waende Mahakamani? Ukipanga nyumba ya mtu, ameweka dirisha la nondo, kesho ukiweka mbao si anakufukuza? Sasa hawa wamekuta mashine, wameondoa, wameuza, wakulima wa korosho wanaenda kupanga kwenye viwanda vyao, wanalipishwa hela! Ubungo Spinning, MSD mkienda kuangalia kwenye mahesabu alikuwa anapanga kama store, MSD ni ya Serikali, anamlipa mtu ambaye ameua kiwanda. Sasa ni muagize Wakuu wa Mikoa wapo? Wawaletee orodha ya viwanda ambavyo havifanyi kazi na watu walishavunja mikataba, kuna watu wengine wana viwanda wanachechemea kidogo kidogo lakini hawa hawachechemei, wameng’oa kila kitu wanafanya biashara yao na sisi tunawaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi mliokaa hapa mnafaa na mnatosha, hebu isaidieni nchi yenu. Tuwanyang’anye vile viwanda, yabaki maghala ya nchi yetu, watakaokuja wana uwezo mpate nafasi ya kuwapa nafasi wafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie Mchuchuma na Liganga. Historia tunayopewa kwamba tunaweza kuchimba yale madini miaka 100 lakini tangu nimesikia utafiti tunajenga, na kadhalika ni kama miaka 12. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilisikia kama kuna mtu aliuliza, kwa nini kama tunaweza, tusiite watu wakaanza kuchimba tukawawekea bei wakapeleka hela Benki Kuu sisi wakati tunaendelea na utaratibu wetu? Si mmetuambia ni miaka 100, kwa nini tuendelee wakati kitu tunacho, kinatakiwa, hatuuzi, hatujengi, faida yake ni nini? Mwisho tutaondoka huku ulimwenguni hatujaona hata senti tano ya Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenu, hebu waruhusuni wananchi wa nje, wekeni utaratibu pale, waje wachimbe wasafirishe watulipe hela, wakati ninyi mnaandaa utaratibu wenu wa kupata kiwanda. Kigugumizi cha nini? Mheshimiwa Mwijage unaweza, mimi naamini unaweza, kigugumizi kinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wana urasimu mara mia kwa sababu sisi wanasiasa ni miaka mitano ikiisha, alikuwa Mheshimiwa Mwijage amepita, alikuwa Mheshimiwa Manyanya, amepita. Shukeni huko chini muwaambie, kama hataki kufanya si ufukuze! Si mamlaka mengine mnayo? Wimbo ni ule ule. Alikuwa Mheshimiwa Mzindakaya, ameondoka, sijui wamemweka tena nani Mwenyekiti mwingine. Wenyeviti wanabadilishana tu. Nini kinafanyika NDC kwenye hii Mchuchuma na Liganga? Mnatuficha nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungepata umeme, tungepata pesa, lakini maamuzi hamjafanya. Nawaombeni sana mwende mfanye maamuzi ili tuone nchi hii inakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mara kulikuwa na viwanda vya ginnery. Viwanda vile vilikuwa vinafanya kazi, lakini ushirika ulipokufa wakaviweka chini ya mfilisi. Ukienda pale Mgango kidogo kinachechemea, lakini mfilisi, kiwanda kinafilisika kikiwa kwenye mikono ya Serikali. Ukienda Bunda Ginnery, kinafilisika kiko pale. Ukienda kule Ushashi Ginnery, kiwanda kinafilisika kiko pale pale. Hawa wafilisi nao kwenye Hazina Mheshimiwa Mpango muungane, hawa ni akina nani? Kwa nini mfilisi anapewa mali lakini zinakuwa makopo naye yuko pale pale na ni Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana, Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi haiko hivyo, watendaji mnaowalea watawapa madhara kwenye kuomba kura, kwa sababu wao wameajiriwa wapo. Vitu vinafia mikononi mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa hiyo, maana yangu ni nini? Leo tunaenda kwenye zao la pamba, watu wanalia hapa. Ginnery zipo zilikuwa za Serikali, zinasaidia, lakini watu zimekuwa zao. Yule mfilisi ndio anakodisha kuweka pamba, anakodisha kila kitu, kesho anakwambia imeharibika. Hizi hela huwa zinaenda wapi? Kwa nini tunapata shida namna hii jamani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima pale Bukoba nilikuwa namwuliza Bukoba Town, kuna Kiwanda cha BUKOP, kile ndiyo kilikuwa kiwanda sisi tunasoma zamani kwenye KBCU. Leo kiwanda kile anacho mtu mmoja, KNCU hawana mahali pa kukoboa kahawa. Nini kilifanyika, ni shida! Ndugu zangu viwanda hivi tunavitaka sana. Tunawapongeza, mmefanya sana kazi ya kuleta viwanda, lakini vilivyokuwa vya zamani, cha zamani ni bora zaidi kuliko kipya ambacho hukioni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, turudisheni kwenye ushirika mzuri, viwanda viko chini yako Mheshimiwa Mwijage. Kama teknolojia ya zamani, waambie wang’oe walete ya kisasa, lakini viwanda viwe vyetu. Sasa tunakuwa watumwa kwenye viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze suala la Zanzibar, nataka kulisema kidogo, mnisamehe. Suala la Zanzibar hili, sipingani na Serikali yangu, lakini Mheshimiwa Turky hayupo hapa, ningemsema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini maji ya Mheshimiwa Turky yanatoka Zanzibar yanakuja Dar es Salaam yananyweka? Kwa nini sukari ile inayotoka kwenye Kiwanda cha Zanzibar haiji Bara? Kwa nini? Kwa nini haitugusi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmefanya jukumu kubwa sana kwenye sukari, mnaweka viwanda mnaleta utaratibu, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wizara hii ya viwanda imefanya kazi kubwa sana kwenye sukari, nawapongeza sana. Kwenye sukari kwa sababu kila mwezi wa nne viwanda vinafungwa, mnatoa nafasi kidogo, watu wanaleta sukari hali inakuwa stable, lakini kwa nini kwenye sukari hapa kwenye hivi viwanda ikifika mwezi wa kuelekea Ramadhani inakuwa shida? Kwa nini? Mafuta hayapo, sukari haipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa Mkulazi inakuja, tunawapongeza, lakini kwa nini tusiwe na bulk procurement ya sukari, Serikali ifanye kama inavyofanya kwenye NRFA? Wale watu wa vyakula, chukueni miezi ikifika tuwekeeni sukari tonnage inatosha, mafuta yanatosha, unapokaribia miezi ya Waislamu kuingia, Serikali itoe i-control. Leo hii sukari Mheshimiwa Mwijage nakuomba ukimaliza bajeti yako hamia bandarini, ili sukari iweze kushuka kule chini. Tutaingia mwezi wa Ramadhani sukari itafika shilingi 5,000 tutakuwa tunakusema wewe. Nendeni mfanye operation kama mlivyofanya ya mbolea, watu wana sukari wanafungia kwenye ma-godown sukari inazidi kupanda, kwa nini tunanyanyasika katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa 90% samahani kwa kauli hii, ni watu wanaogonga passport ndio wanatutesa. Ndio!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ALHAJ ABBDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Awali ya yote nami nianze kwa kulipongeza Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania. Pamoja na hayo nimpongeze Mheshimiwa Waziri, hongera sana kwa kazi anayoifanya, yuko peke yake na inaonesha nawe ni jemadari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Katibu Mkuu, ndugu yangu Turuka; Naibu Katibu Mkuu, Mama Immaculate Ngwale; Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo; Mnadhimu Mkuu Bwana Yacoub H. Mohamed; Mkuu wa JKT na wakubwa wengine wote ambao sikuwataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napongeza sana, mwaka 2017 nilikuwemo kwenye bajeti hii, hiki walichofanya Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Jenerali Mabeyo cha kuweza kuwaalika Majenerali wetu wote wastaafu, nawapongeza sana. Inatia moyo na inaonesha wapo na busara yao wanaitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa Maaskari wetu. Askari wetu wengi wako uraiani. Zamani sisi wakati tunakua, tulikuwa tunajua wanajeshi wanakaa kambini, lakini sasa Askari wetu wa Jeshi la Wananchi wako Mtaani. Naiomba Serikali yangu na Wizara, ni vizuri tukaendelea kuwaweka maaskari wetu kukaa kwenye vikosi; wakikaa huku uraiani ndio zile tabia ambazo fulani wamesema kwamba wanajiingiza kwenye mambo ambayo siyo sawa. Askari wa Jeshi la Wananchi eneo lake ni kikosini, ni kwenye detach, anapohitajika wakati wowote aweze kupatikana. Huo ni ushauri katika Serikali yangu, waliangalie tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, ukiendelea hapo, ukiangalia, vikosi vingi leo vimeanza kusogelewa na wananchi. Vikisogelewa na wananchi, Jeshi hili linavyo vitu vingi sana vya siri na visivyotakiwa kuonekana uraiani. Mfano hai, kama mnakumbuka pale Mbagala tukio lililotokea ni kwa sababu wananchi wamesogelea Jeshi. Sasa hata Jeshi kufanya mambo yake inakuwa ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, naiomba Serikali yangu, kama walivyosema, eneo la Jeshi siyo la kusogelea sogelea maana wale ni walinzi wa nchi hii na wana vitu vingi sana vinavyotakiwa kukaa kwenye siri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemaji amesema neno hapa. Jeshi letu nafikiri ndiyo chombo muhimu kuliko sehemu yoyote ndani ya Wizara hizi; lakini Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Mpango wako hapa, inakuwaje Jeshi linapewa asilimia 60? Jeshi la Wananchi linapewa mapato kwa mwaka asilimia 60. Jeshi! Hapana! Hela ya Jeshi isicheleweshwe, isiwekewe kitu chochote. Hawa ndio watu muhimu zaidi kuliko sisi hapa wote tuliokuwepo huku, lakini wanawapelekea asilimia 60! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanajitolea kufa. Ndiyo kama tunaosema wale 19. Sisi tunawapokea, tunawapa pole, kwa heri. Naishauri Serikali yangu, bajeti ya Jeshi isiguswe, isipunguzwe ni eneo muhimu. Mahitaji yao ni makubwa. Jeshi letu ni zuri, lina morali, lina majemadari wengi, makamanda wengi, ni la wananchi kweli, lakini haki ni stahili zao. Dunia inabadilika. Inaonekana Kenya kukiwa na kifaa, Jeshi la Tanzania halina; Rwanda ina kifaa, Jeshi la Tanzania halina, tunaongelea bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemaji mmoja amesema, bajeti yao ilikuwa kama trilioni tatu, tumewapa kidogo mno hii. Sasa hata hicho kidogo wanakimega! Hapana. Nafikiri Serikali ifanye operation kama inavyofanya kwenye madawa, inawapelekea bajeti kamili. Suala la hela ya Jeshi iende, wapate pesa zao, wafanye hayo wanayomudu kuyafanya bila kuweka suala lolote. Bahati nzuri niko Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Mpango huko nitakuwa nakumbusha kwamba jeshi haki yao imeenda? Tuwape. Hawa wako kwa ajili yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende JKT. JKT nawapongeza sana kwa kazi mnazofanya, nawapongeza kwa ukuta wa Mererani na Jeshi zima. Kazi waliyofanya ni kubwa, watu walisema haiwezekani, sasa imewezekana, lakini siku ile Rais alisema, wale vijana 3,000 wataendelea kuajiriwa. Naomba waajiriwe na wala wasicheleweshwe kwa sababu, kazi waliyoifanya ni ya mfano, imeonesha jeshi lipo, likitumwa linafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa nao wana tatizo. Ukiangalia SUMAJKT mambo yao wanayafanya kama Jeshi. Vifaa vyao bado ni duni. Hawawezi kufanya competition na wenzao, teknolojia yao bado ni ya chini. Sasa kama tunawasifia SUMAJKT wote humu ndani, tuwawezeshe basi tuwape vifaa liwe eneo la kujitegemea na kusaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wale vijana wanaokwenda kwa mujibu, bajeti yao ni ndogo. Nimeangalia kwenye kitabu cha Waziri hapa. Sasa tumesema watoto warudi kule, wapitie JKT, wajenge Utanzania, bajeti haipo. Tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, hapo ni muhimu sana. Wapeni nguvu JKT waimarishe vijana wetu na nina imani kuna vijana wetu wengi humu, Waheshimiwa Wabunge wameenda kule JKT akiwepo akina Mheshimiwa Ester Bulaya, baada ya kuja, mambo yamebadilika, maana wamepiga kwata. Sasa kwa sababu ni eneo la kujenga Utanzania tuiunge mkono JKT, haki yake anaomba apewe ili kuweza kutuendeleza. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siko Kamati ya Ulinzi, lakini walinzi mnisamehe, hili la mipaka naomba kusema kidogo. Zamani kulikuwa na detach za wanajeshi katika mipaka yetu; Kigoma, Rukwa, Kagera, kwa nini wameziondoa? Aah, kuna nini kimetokea? Kwa sababu, nikisema haya ya akina Jenerali Mboma au nani wanajua huko juu kwamba kulikuwa kule kuna detach za Wanajeshi. Watu wakitaka kusogelea wanaogopa, lakini leo wamewaondoa wanajeshi kule. Kwa nini wamewaondoa? Wamebaki Askari. Askari sawa, ni Jeshi, lakini akishasimama mwanajeshi hata wale wenzetu wa nje wanajua mpaka ule hauingiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka kutoa mfano, mtu anaweza kutoka Burundi akaja mpaka Tabora asionane na mtu yeyote kwa sababu, mpaka ule uko wazi. Kwa nini? Naomba sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Mabeyo hebu waturudishie detach zile, zilikuwa zina faida yake. Zilikuwa zinasababisha hata wanaoingia hawa wahamiaji haramu wanapungua, lakini leo, mpaka ni mkubwa, ulinzi ni kidogo, watu wanaingia wanavyotaka. Wananchi wetu wanauawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile Kigoma walikuwa wanauawa kila siku kwa sababu mipaka iko wazi, wale watu wa nje wanatoka na bunduki zao, wanateka magari yetu, wanasomba vitu wanarudi kwao. Naomba detach hizi za Jeshi zirudishwe kama hakuna sababu nyingine. Mheshimiwa Waziri anaweza akanijibu akija au atajua atakavyoniambia, lakini ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie maduka ya Jeshi. Maduka ya Jeshi yamefungwa, lakini yalikuwa yanawasaidia wanajeshi kupata afueni, wana exemption. Baada ya kuyafunga maduka yale, hawajawaongeza chochote kwenye mishahara yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maduka haya wameyafunga kwa nini? Kwa sababu, mwanajeshi alikuwa anaweza kwenda kule kununua mabati, cement na kadhalika. Kwa nini tunawapa exemption watu wengine, lakini hawa ndugu zetu wanaolala hoi kila siku wanatulinda, wanakesha maporini, wanaenda nje wanakufa, tunaona kama hili neno kuwawekea hii exemption ni kosa? Kwa nini jamani? Bati leo imefika Sh.300,000/= badala ya Sh.250,000/=, mwanajeshi atajenga huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanajeshi ana nini zaidi ya kusimama barabarani na kuweka gari pembeni? Mwanajeshi kazi yake, akiamka asubuhi ni kazi, usiku ni kazi, lakini tumemwondolea yale maduka. Mimi sijui sana kwenye Serikali yangu huko ndani waliangalia nini? Nasema hawa Wanajeshi kama tumeondoa mduka ya bei rahisi, wawaongezee kitu kwenye mshahara wao. Saa za kazi kule kwao wakishakuwa wanawapa kitu zinaweza zikaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyoambiwa, saa za kazi sasa zimeongezeka kwenye Jeshi; sasa mtu anaingia saa 12.00 anaondoka saa 8.00 za usiku, hana chochote. Naomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja anijibu kuhusu maduka haya, aniambie kwa nini wameyafunga maduka haya? Hata kama walikuwepo watu wanaenda kupata faida kwa ajili ya maduka, si wawazuie kule ni jeshini? Eeh, kama mtu anatoka kule kwenda kununua friji ya bei rahisi, wamzuie. Jeshini unaingiaje kirahisi rahisi? Eeh! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba maduka haya kwa kweli wasiyaache kwa sababu, ndugu zetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia la mwisho, Kagera Sugar. Pale kwenye Mto Kagera, kuna Kanisa lile lilipigana vita, Waheshimiwa Wanajeshi lile walifanyie utaratibu basi, ile hali iliyoko haifai, kwa sababu ni eneo la Vita vya Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nichangie Wizara hii ambayo kwa kweli tuna majonzi sana. Nashukuru sana leo umekaa hapo mbele, ni bahati. Kwa nini, nianzie na msemaji wa sasa hivi ambaye amepita.

Mheshimiwa Spika, kuunda Tume ya Bunge kwenda kuangalia matatizo na madhara yaliyowakuta wafugaji na wavuvi haiepukiki. Kwa nini? Wavuvi wa Tanzania leo wako kwenye utumwa, kwa sababu ni watu ambao wanaishi. Nataka kutoa mfano kidogo. Ukienda Ukerewe ni kisiwa, lakini kuna Kisiwa kidogo Kulazu, kuna Kisiwa kingine Kweru, kuna Irugwa, Liegoba, kuna Burara, ukienda Bukoba kuna Bumbile, kuna Gozba na Msira. Hawa watu wanaishi visiwani, maisha yao ni kuvua samaki tu. Wamelea watoto, wamesomesha watoto, wana ma-degree, ni samaki peke yake, hawana kitu wanachojua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu leo ni kilio siyo kidogo, ni kikubwa. Watu wamejinyonga na kupigwa risasi kwenye operation. Hii hatari ni kubwa. Wana-CCM wenzangu niwaambie, tutaenda kuomba kura sisi, tunaombaje kura hawa watu wanaoteswa hivi kwa operation ya ajabu hii? Operation zimeshafanyika nyingi, katika Bunge hili tunaona haiwezekani utu wa mtu ukaharibika kwa sababu Mheshimiwa Mpina ni Waziri. Huo Uwaziri hauwezi kuwa mtu mmoja halafu CCM ikashindwa kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili Tume haiepukiki. Nina imani Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi haijamwagiza Mheshimiwa Waziri afanye hivyo na haiwezi kumwagiza hivyo. Chama cha Mapinduzi ni chama cha watu, Rais wetu anajinafsisha, anaongelea wanyonge, wanyonge wa Kanda ya Ziwa, wa Pangani, Mtwara, Mafia wanaenda kuhudumiwa na nani kama sio sisi Wabunge tuliomo humu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, bado miezi tisa mnaenda kuomba kura kwenye Serikali za Mitaa, mnaenda kusema nini kwa hali hii? Mnaendaji kuongea na watu hawa? Mtanzania anakuwaje mtumwa kwenye nchi yake? Wafanyakazi wanalia, wafanyabiashara wanalia, watu wote wanalia, inawezekanaje? Hapana, Mheshimiwa Mpina huwatendei haki Watanzania! Huwatendei haki! Hii kuna siku Mungu atahukumu. Haiwezekani watu wamekuwa watumwa katika nchi yao kwa sababu ya kuvua. Ziwa lipo, tumelikuta, maeneo haya tumeyakuta, watu wanaishi hivyo, leo ni mateso. Haikubaliki hata siku moja, haikubaliki! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, neno hili ni gumu sana kulisema. Wafugaji wana dhambi gani? Kufuga ni dhambi? Mtu kuwa na ng’ombe ni dhambi? Mheshimiwa Waziri anafuatwa mpaka kwenye viwanja vya Bunge hataki kuwasikiliza watu, wewe ni Waziri wa nani? Waziri wa Wizara ya kufanya nini? Kama huhudumii watu, Uwaziri wako ni wa nini? Kama huwezi kusikiliza sekta, ni nini hiki? Wako hapo nje, kila mtu anagawa karatasi, nimeumizwa, ng’ombe wangu wameuzwa wamefanya nini, kwa nini? Hii haiko ndani Ilani ya CCM, kwamba utakuwa Waziri, badala kumsaidia Mheshimiwa Rais, unamsababishia matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya semina ya uvuvi, ilikuwa nzuri kiasi chake, lakini yule mseminishaji anasema Mheshimiwa Rais amempongeza Waziri kwa jukumu analofanya. Nilisema pale pale na ninasema hapa, niliwaambia msimchanganye Mheshimiwa Rais na hilo, Rais hawezi kushangilia wananchi wanateswa, hawezi kushangilia wananchi wake wanaumizwa.Rais amepigiwa kura, anatakiwa kurudi kuomba kura kule. Kwa nini mnamchanganya Mheshimiwa Rais na matatizo ya mtu mmoja ambaye ni Waziri? Kwani Mheshimiwa Waziri kwenye sekta hii ana muda gani? Si miezi tisa! Miezi tisa tu nchi inavurugika, amani inakosa, watu hawalali, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tupe Tume, ije na majibu. Simamisha operation zako. Mheshimiwa Waziri juzi ameenda Mwanza, amesema shughuli hii itaendelea, yale mambo ni ya wanasiasa. Wewe umetoka mbinguni? Wewe hujapigiwa kura? Hatujaja kwako kuomba kura wewe? Wewe umetoka mbinguni? Wanasiasa ni wapi? Haiwezekani, lazima tuwalinde wananchi wetu, lazima wananchi wetu wapate haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya huko nyuma nilikuwa kwenye CCM naongoza kitu fulani, nilitembea nchi nzima hii. Pili, nilipata bahati ya Mheshimiwa Rais kutembea naye. Watanzania ni wanyonge, watu wanaishi kwa mlo wa siku moja, watu wanajishughulisha na mambo yao, mtu anapewa Uwaziri anaona kazi ni hiyo. Haipo hivyo! CCM haitakubali, Serikali haitakubali, kila mtu abebe mzigo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ulega nakuhurumia, ukiwa Naibu Waziri huna mamlaka, mwenye mamlaka ni Waziri wako. Kwa nini mnataabisha watu? Kwa nini tunatesa Watanzania? Au niseme, inawezekana Mheshimiwa Mpina unataka Wapinzani watushinde? Ni nini hii? Inawezekana ni style hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba Tume kutoka ndani ya Bunge hili na operation zisimame. Hakuna operation haina muda. Kila operation ina muda wake. Bunge hili lituambie operation moja ni miezi mingapi? Operation mbili ni miezi mingapi? Leo unaambiwa inaenda operation three. Unamchukua Hakimu wa Mahakama ya Kutembea, unachukua watu wa operation, anakamatwa mvuvi, watu wanasema faini isiyokwenda benki, tunataka pesa cash. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa wanalala guest house, haki ya mvuvi iko wapi? Atapewaje haki yake wakati hawa watu wanakaa kwenye hoteli? Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana Mbunge wangu wa Musoma Mjini pale anasema vizuri samaki wanaongezeka. Wanaongezekaje samaki? Nyavu hazipo. Walikuwa wanavua watu 1000, leo wanavua watu 200, utaona samaki kama zipo, hazipo. Wasafirisha samaki wanaambiwa lazima muwe na mambo ya cold room sijui nini, watayatoa wapi? Lazima samaki wote waende viwanda ili viwanda vipate faida, ndiyo mtu asafirishe. Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili ni gumu kuliko kuwa kwenye ugumu. Tunasema suala hili ni gumu kwa sababu Wabunge wa CCM mtaenda kuomba kura. Maswali haya mtakutana nayo, lazima muwe na majibu. Haiwezekani watu wakawa wananyanyasika katika nchi yao na sisi tunaangalia, tunakubali. Wana-CCM iteteeni CCM, kesho kutwa kuna kura hapa, tutashindaje? Tutashinda kwa style gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kura zinapigwa na watu, hakuna Mbunge anayeingia humu kwa kupewa, ni sisi wachache, tumekuja kwa bahati mbaya huku labda au nzuri, muda wetu umeshaisha, mimi ni mstaafu wala siwazi chochote, sigombei popote, lakini kuisemea CCM, nitasema wakati wowote na mahali popote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpina umeingiaje kwenye mtego huu? Kuna mtego mmoja umeingia, nakusikitikia sana na ninakuhurumia sana. Nimesema mara mbili ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nilishasema mtu anaitwa Vediga, jana umemkaribisha hapa Bungeni mfanyakazi mzuri, ana viwanda na nini, lakini huyu ndio analeta Wahindi peke yake wanafungua butchery kuanzia Mtwara mpaka Singida, hakuna hata Mswahili anayefanya kazi hiyo. Wewe nawe umeingia kwenye mtego huo? Umeingia mtego huo tayari? Nakupongeza. Kwa sababu kama mtego mzuri umekunasa, acha ukunase. Haiwezekani mtu anayetesa Watanzania, anayenyanyasa Watanzania wetu, leo wewe ndio umemleta kwenye gallery kwamba ni mfanyakazi mzuri. Viwanda viko vingapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hili najua kuna wadogo zangu wengi inawagusa kwa sababu huyu ni mwenzenu. Nasema yuko kwa Mheshimiwa Mama Jenista, yuko kwa Mambo ya Ndani, kuna jibu siku litarudi hapa ndani. Haki ya Watanzania itapatikana na haki ya weupe mnaowatanguliza mbele itapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina zaidi, naomba kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri na Serikali mniambie mnaunda Tume, mniambie operation inasimama na kama operesheni haiwezi kusisimama, shilingi mimi sina. Leo nasema siungi mkono hoja katika hoja iliyopo mbele yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawakilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Dakika tano sijui kama nitazitumia vizuri, ngoja nianze. Nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu na Makatibu Wakuu na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianzie kwenye suala la pesa/dola. Naipongeza Wizara ya Fedha tuliongelea suala la dola huko nyuma, wamefanya marekebisho kwamba ukienda ku-change dola sasa utaombwa passport utapewa risiti. Naomba kushauri, hamjafanya kazi vizuri kwa sababu ukienda ku-change dola bila kuomba EFD machine, hawakupi. Sasa hiyo control mnaifanyaje? Lengo ni zuri lakini bado yako maduka yanauza dola bila kutaka kitambulisho, Hawa wakoje na mnawaonaje na mnawaangalia vipi?

Mheshimiwa Spika, la pili kwa haraka, niongelee madeni ya ndani. Nawapongeza juzi kwenye Kamati mmeniambia mmeshalipa madeni ya ndani shilingi 1.1 trillion.

Tatizo langu ninalolipata, kule mikoani kuna ndugu zetu ambao wanafanya biashara na Serikali, wanadai shilingi milioni tano, shilingi milioni 10 au 20 na inaonekana Wizara ya Fedha mnapeleka madeni yale kwa kutaja jina alipwe Bulembo. Sasa kuna watu wanaendelea kulipwa, kuna watu wana hela ndogo hawajawahi kulipwa. Naomba mliangalie upya. Kwenye madeni ya mwaka huu mnayoyalipa, uhakiki ni mzuri, lakini hela inapotoka asiwe ana-appear mtu mmoja katika mkoa fulani ndiyo analipwa na wale wengine nao wapewe haki ya kulipwa madeni hayo.

Mheshimiwa Spika, lingine ni ukusanyaji wa kodi kwa njia ya elektroniki. Nataka kuuliza swali, kila Wizara ina mtandao, je, mmeshaunda chombo cha kwenda kuhakiki ile electronic kwenye maeneo mengine? Maana sehemu moja iki-collapse, kama juzi ilivyotokea kwenye EFD katika nchi hii, watu wote walipata shida.

Je, mmeshaweka chombo kingine pembeni, kikishindikana hiki mbadala ni huu? Ni vizuri kwa sababu watu wameshaamua kulipa kodi, lakini system inapoharibika tunapata hasara kubwa na haiwezi kurekebika.

Mheshimiwa Spika, suala la tatu, ni bahati nasibu ya Taifa. Napingana na watu waliokuwa wanasema sijui Biko sijui nani, hapana. Mwisho tutafika mahali tutasema viwanda visitengeneze bia. Nchi zilizoendelea, Bahati Nasibu ni eneo linalokusanya pesa nyingi katika nchi. Ni chanzo kizuri, lakini huko nyuma Bahati Nasibu ya Taifa tulikuwa tunapata asilimia 10 kwenye michezo. Sisi wanamichezo kwenye timu za Taifa, timu gani ilikuwa inapata kule.

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara ya Fedha muimarishe suala hili eneo hilo, kwamba Bahati Nasibu ya Taifa iende mpaka vijijini, tukusanye hela. Ni hela za hiari kama kunywa pombe, kama kunywa chai, kama kunywa soda. Wale waliokuwa wanapinga watoto wanaumiza hela, haya. Mnawapa hela vibaya, matumizi ndiyo haya mabaya, lakini hatuwezi kuondoa Bahati Nasibu ya Taifa kwa sababu ni chanzo cha mapato katika Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, lingine ni elimu kwenye utakatishaji wa pesa. Hivi lini mnaenda kutoa elimu kwa hawa watu wanaotakatisha? Kuna jambo linafanyika sasa ambalo najua hamjalifanya. Mimi kusema ndiyo kazi yangu. Suala la kwamba kuna watu wanaenda kupata pesa Ulaya, wanalipwa huko, wanakusanya dhahabu hapa nchini, kwa sababu hamdhibiti dhahabu, wanaenda kupeleka kule hela na hela zile zinakuja kwa njia nyingine. Kwa nini ninyi mnaangalia mabenki tu? Huku pembeni mbona hamuangalii na bado mchezo huu wa hela chafu upo? Nilikuwa naomba Wizara ijielekeze huko zaidi.

Mhesimiwa Spika, la tano, kodi ya mabango; mwaka 2017 tuliwaambia kwenye kodi mlizotoa Halmashauri kwenda kwenye mabango. Mwaka huu imekusanywa kama asilimia 52, hamtaki ushauri. Njooni tuwape elimu wenye uzoefu wa shughuli hii, kwanini mnakuwa wachoyo? Style ya kukusanya kodi hii ipo, inaonekana kwenye Halmashauri walikuwa wanakusanya vizuri kuliko ninyi. Ninyi mmempelekea TRA, anafanya kama kazi ya ziada. Kwa hiyo, Halmashauri inaonekana ilikuwa inakusanya vizuri, ninyi Wizara hamkusanyi vizuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni Bodi za Mashirika; Bodi za Mashirika hizi, watu wanateuliwa, wanaambiwa walipwe hela miezi mitatu. Wakishapata ile hela, siku wakiitisha kikao, walikuwa watu kumi wanaenda wanne, kwa sababu siku anaenda halipwi, anaenda kula korosho na maji, itakuwaje? Kwa nini msiangalie? Ufanisi unapungua. Kwa nini tuone kama hizi bodi zinafaidika zaidi? Zilikuwa zinasimamia mambo mengi, lakini nini kinamshawishi mtu kwenda kwenye kikao kile hata kama umemteua?

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili naona mwende upya mwangalie zaidi. Siyo kuwaondolea watu hicho kidogo mlichokuwa mnawapa, si ni haki yao? Si wanasimamia zile taasisi za mabilioni? Mtu unamlipa shilingi 500,000 unasema inaishia hapo. Eneo hili naomba mwangalie zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nawapongeza tena Wizara, chapeni kazi, changamoto mnazozipata, ndiyo maana mlipata nafasi hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Dakika tano sijui kama nitazitumia vizuri, ngoja nianze. Nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu na Makatibu Wakuu na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianzie kwenye suala la pesa/dola. Naipongeza Wizara ya Fedha tuliongelea suala la dola huko nyuma, wamefanya marekebisho kwamba ukienda ku-change dola sasa utaombwa passport utapewa risiti. Naomba kushauri, hamjafanya kazi vizuri kwa sababu ukienda ku-change dola bila kuomba EFD machine, hawakupi. Sasa hiyo control mnaifanyaje? Lengo ni zuri lakini bado yako maduka yanauza dola bila kutaka kitambulisho, Hawa wakoje na mnawaonaje na mnawaangalia vipi?

Mheshimiwa Spika, la pili kwa haraka, niongelee madeni ya ndani. Nawapongeza juzi kwenye Kamati mmeniambia mmeshalipa madeni ya ndani shilingi 1.1 trillion.

Tatizo langu ninalolipata, kule mikoani kuna ndugu zetu ambao wanafanya biashara na Serikali, wanadai shilingi milioni tano, shilingi milioni 10 au 20 na inaonekana Wizara ya Fedha mnapeleka madeni yale kwa kutaja jina alipwe Bulembo. Sasa kuna watu wanaendelea kulipwa, kuna watu wana hela ndogo hawajawahi kulipwa. Naomba mliangalie upya. Kwenye madeni ya mwaka huu mnayoyalipa, uhakiki ni mzuri, lakini hela inapotoka asiwe ana-appear mtu mmoja katika mkoa fulani ndiyo analipwa na wale wengine nao wapewe haki ya kulipwa madeni hayo.

Mheshimiwa Spika, lingine ni ukusanyaji wa kodi kwa njia ya elektroniki. Nataka kuuliza swali, kila Wizara ina mtandao, je, mmeshaunda chombo cha kwenda kuhakiki ile electronic kwenye maeneo mengine? Maana sehemu moja iki-collapse, kama juzi ilivyotokea kwenye EFD katika nchi hii, watu wote walipata shida.

Je, mmeshaweka chombo kingine pembeni, kikishindikana hiki mbadala ni huu? Ni vizuri kwa sababu watu wameshaamua kulipa kodi, lakini system inapoharibika tunapata hasara kubwa na haiwezi kurekebika.

Mheshimiwa Spika, suala la tatu, ni bahati nasibu ya Taifa. Napingana na watu waliokuwa wanasema sijui Biko sijui nani, hapana. Mwisho tutafika mahali tutasema viwanda visitengeneze bia. Nchi zilizoendelea, Bahati Nasibu ni eneo linalokusanya pesa nyingi katika nchi. Ni chanzo kizuri, lakini huko nyuma Bahati Nasibu ya Taifa tulikuwa tunapata asilimia 10 kwenye michezo. Sisi wanamichezo kwenye timu za Taifa, timu gani ilikuwa inapata kule.

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara ya Fedha muimarishe suala hili eneo hilo, kwamba Bahati Nasibu ya Taifa iende mpaka vijijini, tukusanye hela. Ni hela za hiari kama kunywa pombe, kama kunywa chai, kama kunywa soda. Wale waliokuwa wanapinga watoto wanaumiza hela, haya. Mnawapa hela vibaya, matumizi ndiyo haya mabaya, lakini hatuwezi kuondoa Bahati Nasibu ya Taifa kwa sababu ni chanzo cha mapato katika Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, lingine ni elimu kwenye utakatishaji wa pesa. Hivi lini mnaenda kutoa elimu kwa hawa watu wanaotakatisha? Kuna jambo linafanyika sasa ambalo najua hamjalifanya. Mimi kusema ndiyo kazi yangu. Suala la kwamba kuna watu wanaenda kupata pesa Ulaya, wanalipwa huko, wanakusanya dhahabu hapa nchini, kwa sababu hamdhibiti dhahabu, wanaenda kupeleka kule hela na hela zile zinakuja kwa njia nyingine. Kwa nini ninyi mnaangalia mabenki tu? Huku pembeni mbona hamuangalii na bado mchezo huu wa hela chafu upo? Nilikuwa naomba Wizara ijielekeze huko zaidi.

Mhesimiwa Spika, la tano, kodi ya mabango; mwaka 2017 tuliwaambia kwenye kodi mlizotoa Halmashauri kwenda kwenye mabango. Mwaka huu imekusanywa kama asilimia 52, hamtaki ushauri. Njooni tuwape elimu wenye uzoefu wa shughuli hii, kwanini mnakuwa wachoyo? Style ya kukusanya kodi hii ipo, inaonekana kwenye Halmashauri walikuwa wanakusanya vizuri kuliko ninyi. Ninyi mmempelekea TRA, anafanya kama kazi ya ziada. Kwa hiyo, Halmashauri inaonekana ilikuwa inakusanya vizuri, ninyi Wizara hamkusanyi vizuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni Bodi za Mashirika; Bodi za Mashirika hizi, watu wanateuliwa, wanaambiwa walipwe hela miezi mitatu. Wakishapata ile hela, siku wakiitisha kikao, walikuwa watu kumi wanaenda wanne, kwa sababu siku anaenda halipwi, anaenda kula korosho na maji, itakuwaje? Kwa nini msiangalie? Ufanisi unapungua. Kwa nini tuone kama hizi bodi zinafaidika zaidi? Zilikuwa zinasimamia mambo mengi, lakini nini kinamshawishi mtu kwenda kwenye kikao kile hata kama umemteua?

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili naona mwende upya mwangalie zaidi. Siyo kuwaondolea watu hicho kidogo mlichokuwa mnawapa, si ni haki yao? Si wanasimamia zile taasisi za mabilioni? Mtu unamlipa shilingi 500,000 unasema inaishia hapo. Eneo hili naomba mwangalie zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nawapongeza tena Wizara, chapeni kazi, changamoto mnazozipata, ndiyo maana mlipata nafasi hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niungane na wenzangu lakini awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mpango, hongera sana, unajua mishale hii inavyopigwa ndiyo maana amekalia kiti hicho. Kwa hiyo, awe mvumilivu maana asingekikalia asingepigwa. Nimpongeze shemeji yangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Ndugu Dotto, Manaibu wake wote, Makamishna wa TRA na wengine wote, hongereni kwa kufanya kazi katika eneo ambalo kila mtu anaangalia maana ni maeneo ya pesa hayo, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza ni katika eneo la bima. Mwaka jana tulipitisha sheria hapa kwa ajili ya NIC lakini ndani ya bima hii kuna watu watatu. Kuna huyu mkubwa NIC, broker na agent. Mheshimiwa Mpango mbona broker hawa mnawaua? Kwa nini mnatoa maelekezo watu waende direct kwa insurer, hawa broker waende wapi? Leseni mnachukua, sheria iliyowaunda ipo, hamuwasaidii, kwa nini tunaiua hii industry? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatakiwa ifanye kazi na mashirika mbalimbali lakini broker mmemuweka ninyi. Kama hafai basi naomba tulete sheria ya kumfuta na tukimfuta mniambie kama NIC ana rasilimali watu wa kuweza kuhudumia maeneo yote haya, hawezi. Nakuombeni sana, kama kuna waraka mmeutoa ule kwenye bima, huyu bwana mgeni wa bima huyu mwambieni aanze kusoma upya kidogo kwamba hawa broker bila kuwepo yeye hawezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina miradi mingi mikubwa. Tuna ndege, standard gauge, tuna madude makubwa sana, kwa nini hamuweki kwenye clause za procurement zenu kwamba mwekezaji yeyote atakayekuja insurer atakuwa NIC? NIC kama hawezi ata-syndicate na watu wa nje lakini atapata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wakati anakuja kwenye ushauri wangu hebu walindeni brokers na agents. Kwa nini agent wanakuwepo, huwezi kukata insurance mahala popote, lakini mnaposema mtu aende direct hawa watu mnawaua.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni ushuru wa stamp, dakika 10 ni kidogo. Sipingani na ushuru wa stamp nakubaliana nao lakini nina maswali. Kwanza miaka mitano ni mingi kwa mujibu wa hesabu, Waziri akija hapa atuambie kama ni mwaka mmoja au miwili tutamuelewa. Pili, tatizo ninalolipata huyu mtu akitengeneza lita moja na nusu analipa Sh.13,500, lakini chupa moja na nusu ile ina mia tano mara tatu, ukipiga hesabu yake Sh.13,500 ni Sh.40,500 na hawa wanywa maji ndio wengi zaidi kuliko hii lita moja na nusu, hesabu mbona haikubali? Tunapiga hesabu gani? Unaenda kwa mtu wa soft drinks unataka alipe Sh.13,500 kama anauza 150 haiwezi tena kuendelea kuwa Sh.13,500 itakuwa Sh.13,200. Kwa nini huyu mtu wa chini ndiyo tunamuumiza zaidi? Kwa nini tusielekee kwenye bia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hakuna soda ulishasikia ni forgery, hakuna soda ya kutengeneza mtaani, lakini hizi pombe kali hizi ndiyo zinatengenezwa magarasha mengi huku mtaani, kwa nini bei kubwa hii tusingeipeleka kwenye pombe kali? Kwenye mapendekezo yenu pombe kali mnaiweka mbali kidogo. Naomba tuelekee hapa ili tumsaidie mtu wa kawaida anayekunywa maji na soda aendelee ku-relax. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukatai, kwenye Kamati ya Bajeti tumeangalia mtu huyu atapata hii hela kwa mwaka mmoja tu, hata tufanyeje capital anayoitumia na faida yake mwaka mmoja inamtosha, tunampa miaka mingi ya nini? Waheshimiwa Wabunge nawaombeni tuweke mguu chini, apewe mwaka mmoja au miwili, stamp hatuikatai baada ya hapo hii iwe shughuli ya TRA kiwe chanzo chao. Kwa nini tumtajirishe mtu mpaka mwisho na hizi hela anapeleka nje, hazikai nchini. Mheshimiwa Waziri tusaidie hapo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahamia kwa wakwe zangu kule Mtwara na Lindi kuhusu korosho. Hivi hii hela ya korosho ni yetu kwani? Serikali hii hela ni yetu? Tunaitaka ya nini? Kwa nini tutunge sheria kwa sababu tumeona kuna mapato? Hiki ni chanzo chao wapeni. Mkienda kwenye pamba chanzo chao wapeni, mkienda kwenye kahawa wapeni. Kwa nini Serikali tunaingia kwenye ugomvi ambao hauna msingi, msingi wa hizi hela ni nini? Kwa nini tuliue zao hili? Kwa nini tuue kahawa na pamba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hii siyo chanzo cha Mheshimiwa Dkt. Mpango, pesa hii inatoka kwa mkulima mwenyewe, sasa unaipangiaje bajeti, unaiwekaje kwenye Mfuko wa Pamoja? Jamani sisi tunakaa jukwaani kuomba kura, msitupe tabu kabisa. Yaliyotokea Mtwara tunayajua, tusijifanye kuna pamba masikioni. Tumefanyaje Mtwara kupata amani mnajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kasema Mheshimiwa Bwege hapa mkaona kawaida, siyo maneno madogo hayo kwenye siasa, ni maneno makubwa sana. Lazima muende mbele mrudi nyuma, hela hizi kwa nini zitupe kero zinatusaidia nini? Nawaombeni Serikali sikivu mpo mnasikia, wote mpo hapa, nendeni mjadiliane, achaneni na hela ya korosho msituletee balaa, wapeni hela zao tuendelee na vyanzo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeletewa Sheria ya Serikali za Mita, nataka kuunganisha mambo yote lakini sasa nataka kuongelea asilimia 10. Tumeondoa vyanzo vingi kwenye Local Government, kuna Halmashauri haziwezi kuwalipa Madiwani posho zao na kuweka mafuta lakini hapa tunasema asilimia 10 wakipata tunaiundia sheria, nakuja na wazo jipya nini tufanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye Municipality za Dar es Salaam, Ilala, Arusha, Mbeya na Ilemela Mwanza hawa walipe asilimia 10 lakini zile Halmashauri ambazo zinashindwa kununua mafuta, Serikali kwa sababu mmechukua vyanzo m-top up pale asilimia 10 muipeleke kama ruzuku kule chini ili akina mama na vijana wakope. Haiwezekani Halmashauri inakusanya shilingi milioni 100 posho za Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa haziwezekani halafu tunawaruhusu kwamba kweli kila Halmashauri itoe asilimia 10 kwenye chanzo gani? Kuna vyanzo gani mmebakiza huko? TARURA, mabango na property tax mmeondoa, hakuna kitu kule. Kwenye Municipality na Majiji kwa sababu kuna watu wengi inawezekana lakini huku chini siyo, naomba mrudi nyuma muangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea hapa nikiamini mwaka kesho ni mwaka wa uchaguzi, tusipate tabu za lazima hapa kwa sababu ya bajeti. Halmashauri hazijiwezi, hazijiendeshi wapelekeeni ruzuku ya 10% ili mikoa, wananchi na halmashauri zote wawe na uwezo wa kukopa asilimia
10. Tusitoe mfano wa Kinondoni au Ilala ukafananisha na Katavi na Tunduru, havifanani! Nchi hii iko tofauti na mapato yapo tofauti. Kwa hiyo, hiyo asilimia 10 huko juu muiangalie tuwapelekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye michezo ya kubahatisha kuna Bahati Nasibu ya Taifa haipo katika nchi yetu, ipo hatujui inafanya kazi wapi. Kwa nini Bahati Nasibu ya Taifa tunaitoa 6 kuipeleka 10, tunataka nini? Bahati Nasibu ya Taifa sehemu nyingi zilizoendelea ukienda Ghana, Nigeria na sehemu nyingine chanzo hiki ni cha Serikali Kuu kwa maana ya Wizara ya Fedha. Ninyi mnatakiwa mtafute anayeweza mkae naye lakini huyu akipatikana atatengeneza nchi nzima kwa sababu ata-invest mtaji wake. Kwa nini mnamzuia kabla hajaja, tunaweka hiki chanzo cha nini, kwa nini tunaongeza hela hapa? Tutakosa watu wa kuja kufanya kazi hii na hii hela ni ya Serikali. Chanzo hiki kingekuwa kinafanya kazi vizuri mngepata hela nyingi za bure pale zipo, lakini mkiongeza kodi wawekezaji watajikata, itakuwa shida. Kwa nini msikubaliane katika hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema ninyi watu wa Mifugo muende pale Masaka Uganda ukifika Lukaya wanafuga bycatch, mjifunze wenzenu wanafanyaje muache kutembea na rula.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nichukue fursa hii kuwapongeza ndugu zangu walioko Wizara ya Mambo ya Ndani Mheshimiwa Mwigulu, Naibu wake Mheshimiwa Masauni, Katibu Mkuu Wasaidizi wao wote, Makamishna Jenerali walioko hapo juu, Ma-RPC, Maafisa Uhamiaji katika Mikoa. Wizara nzima nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya kutulinda katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la ulinzi hasa polisi, wachangiaji wengi wamesema nani halindwi, nani kafanyiwa hivi, nani kafanyiwa hivi, mimi nataka niende Kibiti tu kidogo. Polisi walifanya kazi kubwa sana Kibiti inatakiwa tuwapongeze wote tuliomo humu ndani. Kazi yao waliofanya ni kubwa, ilifika mahali mtu ukitaka kwenda Kibiti inabidi utafute polisi wa kukusindikiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani wengine walimaliza kusema kwamba sisi Serikali haitutaki, haiwi hivi nataka kuuliza swali moja hasa kwa Wabunge, askari polisi mmoja anapokufa ni kwamba alikuwa vitani, Kibiti wamekufa askari kama sikosei kati ya 20 mpaka 25 haikutugusa, haionekani kama walikuwa vitani, wakapata shida na wala hata humu ndani hatukuitana kuchangiana hata elfu kumi kumi ya kusaidia familia zao. Ni watoto wetu wale! Ni wapiganaji wa nchi hii ndiyo kiapo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakaa hapa kuna watu wanabeza polisi. Hata ukiwa na Mmasai anakulinda huwezi kubeza polisi. Wasemaji wamesema polisi ni professional, haiwezekani kila mtu anaweza kwenda nyumbani akavaa akaitwa polisi. Kwa nini tunawafanya watu wa kawaida polisi? Naomba Waheshimiwa Wabunge polisi pamoja wanalipwa kwa kodi zetu hata nyie Wabunge humu mnalipwa kwa kodi ambapo hata polisi anakatwa makato yake, si ndiyo? Maana yake leo mtu anasema kodi yetu, nani halipwi kwa kodi? hata sisi mshahara tunaopata ni kodi ya polisi ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili ni letu sisi wote, lakini wachangiaji wanasema polisi kwa kodi zetu, kodi ni yetu sisi wote kama polisi anavyolipwa mshahara, kama wewe unavyolipwa posho, tuna haki ya kuthamini polisi. Naendelea kusema tukitoka nje hapa tunalindwa na polisi, popote unalindwa na polisi, lakini polisi hawa hatuwathamini wala hatuwapi value. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwamba, napenda niwapongeze matrafiki wote Tanzania wanaofanya kazi ya usalama barabarani. Sisi Wabunge tukienda na magari yetu traffic akikusimamisha, unasema naitwa Mbunge, kwani ukiitwa Mbunge ndio uvunje sheria? Nani amekwambia kuna mahali imeandikwa Mbunge avunje sheria? Tunawadharau wale watu hatuwapi haki, hata kama wewe ni Mbunge una haki nayo, basi simamisha gari msikilise jieleze mpe thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa Mheshimiwa IGP Sirro, hawa Wabunge wanaofanya makosa barabarani wakienda wawapeleke mahakamani. Ndiyo, kwa kuwa hakuna mahali mtu ameambiwa avunje sheria, sheria hii inatuhusu sisi wote. Unaona watu wanafanya vitu vya ajabu eti kwa sababu wanatumia nembo ya Ubunge, Ubunge siyo certificate ya kwenda kufanya makosa kwa kuwadhalilisha wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sehemu ya pili upande wa polisi, polisi kuna ile kitu wanaita Police General Order kwa maaskari wetu, wanakaa miaka 12 ndio wanaingia kwenye ajira, hii nyingine ni mkataba mkataba. Nafikiri wangefanya utarabu tulete sheria huku au tufanye marekebisho tuwape nafasi yao. Kwa sababu kama tunafanya hivyo hapa katikati wakiondoka kuna mambo mengi wanayapoteza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa polisi niende suala lingine ambalo ni gumu. Kwenye kitabu cha bajeti cha Waziri hapa nilipoangalia kwenye eneo la maendeleo kwenye ukurasa wa 51, polisi wamewapa hela kidogo. Pale Makao Makuu ya Polisi kuna jengo fulani pale linajengwa miaka mingi forensic bureau haliishi, kwa nini Mheshimiwa Mwigulu jengo hili haliishi? Kwa nini kwenye bajeti hii hatulioni? Jengo hili ni muhimu sana kwa nchi za wenzetu kwa sababu gani, mtu akipata ajali, mtu akiuawa usiku kuna mahali anapelekwa ajue, mitandao ipo, tutakwenda kuangalia wapi, kwa nini jengo hatulipi bajeti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo mengi katika nchi hii watu wanauawa, watu wanaonewa, watu wananyang’anywa mali zao, lakini hawana mahali pa kwenda. Naomba Mheshimiwa Mwigulu wakati akija hapa anijibu forensic bureau ya Makao Makuu pale inakwisha lini? Huo mradi ni mkubwa sana katika nchi za wenzetu, huwezi kutambua jambo mpaka uende kuazima kwa rafiki yako itakuaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, inawezekana hatuoni umuhimu, lakini nina uhakika eneo hili ni muhimu. Hawa watu wenu wa Kibiti wangekuwa wanapatikana, mitandao ya simu ingekuwa inapatikana polisi wajitegemee wenyewe, kwa nini wawe na mawazo ya kupiga hodi kwa watu wengine? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akija nafikiri majibu yake yatakuwa mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Uhamiaji. Kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Kamishina wa Uhamiaji, hongera sana mama, ameonesha mabadiliko, anafanya kazi. Pia katika pongezi hizo nimpongeze tena Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani niliuliza hoja hapa Bungeni kuna vijana wetu walifukuzwa pale polisi kwa kufoji viza, yule aliyesababisha wafoji viza akapigwa PI Uhamiaji wakawa bado wanamshikilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Naibu Waziri na Jenerali wa Uhamiaji, yule mtu baadaye walikamilisha utaratibu akarudi kwao, basi watoto wetu wamefukuzwa na yeye ameenda kwao. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa usikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uhamiaji kuna tatizo, tena si dogo kubwa sana. Namwomba Kamishna atoke Ofisini, atembelee Mikoa ya Tanzania yote ajue pamekaaje. Kwenye border kuna shida, kuna shida sana ukienda Namanga, ukienda Mtukula, ukienda Songwe pale kuna shida kubwa. Pamoja na hayo kila siku tunawakamata Waethiopia, tunawakamata Wasomali, lakini humu ndani kuna watu wanaishi bila utaratibu na wako wanalindwa na Uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali hapa nikasema kuna mtu amekuja hapa nchini anaitwa Mhasibu, leo ni group Meneja miaka 20, anaitwa Vedagiri yuko kwenye kampuni ya Alpha Group. Mtu yule anaishi kwa utarabu gani lakini niliposema neno lile kuna Wabunge humu niliwagusa wenye matakwa na watu kwa sababu ni wafanyabiashara wakubwa nafikiri wana mambo yao pale wanayoyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoongelea ni Utanzania kwenye uhamiaji. Baada ya kumtaja huyo nimeletewa wengine zaidi ya 20, wanaishi humu wanaonekana kama Watanzania, lakini hatuwafuatilii! Ukienda kwenye Idara ya Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu nimewaambia waanzie Mtwara mpaka waje Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli Watanzania hawana uwezo wa kuuza bucha za samaki? Hawa Wahindi wanaouza bucha za samaki wanawapa vibali gani? Uhamiaji wanawaona? Ni Wizara ya kazi ndiyo wanashirikiana na Wizara hizi ni mtambuka, lakini kazi haiwezi kuwapa kibali mpaka uhamiaji waseme anatakiwa kuwepo nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa eneo la Uhamiaji kwa nini wanashughulikiwa Waethiopia, Wasomali, ndiyo wanaguswa huku, lakini hawa wengine tunaoishi nao nchini kwa sababu wana mapesa, wamekaa zaidi ya miaka 20 mpaka wanaingia kwenye siasa zetu nani awe CCM, nani awe CHADEMA, wanawaangalia tu hawasemi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sasa namkabidhi Mheshimiwa Waziri, Kamishna Jenerali hajashindwa inawezekana alikuwa hajui wakae mezani wanipe majibu. Bahati mbaya nikilisema nitaenda nalo mpaka mwisho kwa sababu sitaliacha kama sitapa majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawalinda Wahindi humu, hawana vibali, hawana nini, wanakamata Wasomali akina Bashe waliozaliwa nchini, ndiyo wanahangaika nao. Akiguswa mtu wewe njoo, wewe njoo, lakini hawa wanaotoka nje hawafanyi nao kazi kwa nini? Uhamiaji ni pazuri, siwezi kumsema Jenerali huyu mpya ana siku chache, lakini pale kuna mizizi mibaya, ukienda sehemu ambako kuna wakimbizi, ukienda sehemu ambazo zina mipaka watu wa Uhamiaji wale ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize kati ya Uhamiaji na Polisi; nimeona IGP Sirro mwili wake mzuri, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji mzuri, Magereza mzuri, hawa wenye vitambi vikubwa vinakaa kwenye meza kuliko vyetu ni mapolisi kweli au…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, nianze kuwapongeza shemeji yangu, Waziri wangu Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kazi anazozifanya, Naibu Waziri Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri Mheshimiwa Doto Biteko, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Msanjila na Watendaji wote waliopo ndani ya Wizara hii mpya, nawapongeza sana kwa kazi mnazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona na kuweza kutenganisha Wizara ya Nishati na Madini. Wizara ya Madini ni Wizara nyeti sana katika nchi nyingi, hapa kwetu sasa imeonesha kwamba tunayataka madini yetu yaweze kuleta faida katika nchi yetu. Pia nizipongeze Tume zote zilizoundwa, Profesa Abdulkarim Mruma, siwezi kumsahau kwa kazi kubwa aliyoifanya, Profesa Nehemia Osoro simjui sana lakini Profesa Mruma tunatakiwa tukupongeze na tukupe hati ya shukrani kwa jinsi ulivyojitolea Utanzania wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madini katika nchi yetu tulivyoambiwa mara ya kwanza kwamba pato linalopatikana na madini ilikuwa haifikii hata shilingi bilioni moja lakini ukienda kwenye sekta ya madini watu hawa ndiyo wanaosamehewa kodi sana, watu hawa yaani wao ndiyo wao, wale wanaochenjua kidogo ni matajiri, lakini Serikali haipati pesa. Nalipongeza na Bunge kwa kupitisha sheria nzuri sana ambazo zitaongeza mapato kwenye Serikali angalau sekta hii iweze kuchangia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu rasilimali za nchi yetu zimepotea sana lakini leo mwarobaini umepatikana. Nichukue fursa hii zaidi kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais Mheshimiwa Magufuli kwa jinsi alivyoweza kuwajali wachimbaji wadogo wadogo. Wachimbaji wadogo wamekuwa wakinyanyasika sana katika nchi yao, wakifukuzwa huku na huku, wakipata taabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu katika nchi hii kwa sababu natoka Kanda ya Ziwa kule, hawajui kazi zaidi ya madini. Wakimwambia yako Singida anaenda, Chunya anaenda, wapi anaenda lakini anafukuzwa kila siku. Ombi langu kwa Serikali yangu, hebu hawa wachimbaji wadogo, wapate haki ya kuwa na leseni kwamba kuna mahali wanachimba, wako 500 wako 1,000 wapewe uhalali wa kumiliki eneo lile, liwe la kwao. Hawa wachimbaji wadogo, wanachimba kwenye sehemu unaweza kukuta leseni ya Bulembo mchimbaji mdogo yupo, inaleta tabu kidogo. Kwa sababu ni wenzetu, ni vijana wetu, ni watoto wetu, hebu basi tuwawekee utaratibu mzuri angalau wawe na amani, wakijua tunachimba hapa, magaragaja yako hapa, kila kitu kipo hapa, maisha yao yanajulikana yanavyopatikana lakini sasa wamekuwa ni watu wa kubahatisha. Mmewaruhusu wachimbe lakini kila wanapochimba mishale iko pembeni, bunduki ziko pembeni, hebu wapeni nafasi nzuri ili tuonekane thamani tunayowapa na kuna maeneo wanaenda kufanya hiyo kazi yao ili maisha yao waweze kubadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni mpya lakini kuna changamoto naomba niwape. Siku za nyuma kuna watu watendaji walikuwa wanakata leseni kama kule kwa Mama Mheshimiwa Wambura au Mheshimiwa Lukuvi, mtu anaweza kutoa hati kwa Bulembo, kesho akatoa kwa Musa kiwanja hicho hicho, ndani ya madini pia neno hilo lipo. Unakuta mtu ana ‘pele’ namba fulani na amemwekea ‘pele’ pale pale mgongoni na hawa watumishi mmewarithi, tunawaomba sana, hatuna mengi ya kusema kwenu zaidi ya kuwashauri, hebu watafuteni hawa watendaji waliofanya makosa yale wawajibike kwa sababu walikuwa na dhamana ya Serikali. Unawezaje ukagawa kitalu mara tatu kwa watu watatu tofauti kitalu kimoja? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha atuambie na watendaji wale atawafanyaje kwa sababu wataipa Tume hii shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naipongeza Tume iliyoundwa chini ya Profesa na wanakamati wake. Nampongeza Rais na Waziri, Tume ile ni muhimu sana kwa sababu sasa mwarobaini umepatikana lakini Tume ile nina uhakika itapata changamoto nyingi sana kwa sababu ni kitu kipya kimekuja kuna eneo lenye matajiri wengi, wachimbaji wa dhahabu ni matajiri. Tungekuwa kule Congo, kuanzia Waziri wa Madini na wenzake wote wangekuwa wamevaa cheni za dhahabu tu, mikono imejaa dhahabu si ndiyo? Eneo hili lina mambo makubwa sana. Sasa mnapoenda ku-deal na wale watu ambao ni matajiri, lazima Tume hii tuiombee wawe serious sana kwa sababu hawa watu kwenye sekta hii ni matajiri sana ingawa Serikali siyo tajiri. Kwa hiyo, walioteuliwa tunawaamini sana, wanaweze kufanya kazi vizuri sana lakini wawape ushirikiano kuwaonesha kwamba suala hili kwa kazi waliyopewa waitendee haki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye Tume, nawapongeza juzi kuna hati kama 9/10 mmefuta, kwa sababu watu walihodhi ardhi, wakaenda kwenye masoko ya ulimwengu, wakatajirika lakini sisi hatupati kitu. Hata hivyo, kuwanyang’anya isitoshe, waambieni kesho wachimbaji wadogo wadogo waanze kuchimba mpate chochote kama hamjapata watu wa kuwaweka katika maeneo yale. Kwa sababu kunyang’anya ni kitu kingine na kutekeleza ni kitu kingine. Bajeti ijayo kama mtakuwa hamjafanya chochote pale, nikiwa hai siwezi kuongea hivi nitakuwa naongea kwa sura tofauti, lakini leo sina uwezo wa kusema sana kwa sababu ni kitu kipya, mmekifanya kwa nia njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yale kwa sababu yanayo rasilimali, kama hamjajipanga wachimbaji wadogo waingie. Unajua hawa wachimbaji wadogo wako wengi katika nchi hii katika sekta hii, ukiwaambia leo kesho watakuwepo 10,000 hata 100,000 wanachimba mnapata pato kidogo, mmeshaweka sheria, kuliko tunawanyang’anya watu halafu tunakaa nayo tunaanza kutengeneza akili ya kufikirika, unajua bado, aah, tumeondoa kwa sababu hapatumiki, ni vizuri mkaandaa mazingira ya kuweza kupatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipongeze Jeshi la JKT kwa kutengeneza ule ukuta, watu walisema haiwezekani imewezekana. Wizara ya Madini nawapongeza sana kwa ushirikiano wenu, watu kitu walichokuwa wanafikiri kiko mbinguni sasa kiko tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Jenerali Venance Mabeyo na Meja Jenerali wa JKT, vijana wamefanya kazi nzuri sana na ya kupongezwa kwa sababu wametia moyo wanalinda nchi yao. Ombi langu kwenu Wizara na Jeshi, pale Mererani hamjafunga security. Mmemaliza kujenga ukuta, watu wako kwenye ukuta, haionyeshi faida ya ukuta ule, kama hatujazichunga rasilimali tulizotakiwa kujengea ukuta ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu, zile security mnatakiwa kujenga, inawezekana mmechelewa mnajipanga vizuri, jipangeni vizuri sana, wachimbaji wa madini mimi sijui tanzanite, lakini sehemu zingine nina uzoefu, wanaweza kutembea kilometa saba chini, wakatokea mle ndani ya tanzanite wakafanya kazi. Ni vizuri ile security mnayotaka kuiweka i-sense kwenda chini kama ni kilometa 10, 12 ili chochote kinachotokea kiweze kujulikana mapema lakini tukiutengeneza ule ukuta, halafu mkauacha muda mrefu, aah, si vizuri kusema sana. Nachoshauri, nguvu tuliyotumia, pesa, muda ni vizuri mkauweka ule ukuta security ili watu waone faida ya tanzania ya Tanzania sasa inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini, sitaki kutoa ushuhuda tangu mmejenga ule ukuta bado ule mchezo wa Nairobi unaendelea tu, hamna jinsi ya kuuzuia, kwa sababu hamna scanner ya kumwangalia mtu, tukiingia pale Airport unaangaliwa mpaka sindano. Pale kwenye tanzanite inatakiwa mtu anatoka nayo kwenye gari, chombo kinalia, anaambiwa simamisha hilo gari, mtu anakuja nayo kwenye viatu, anaambiwa simama pale, ndiyo tutaweza kuona faida ya hilo ambalo Mheshimiwa Rais na Wizara wamedhamiria kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, mimi ni mjasiriamali kidogo wa madini ya copper…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hutuba ya Waziri Mkuu kwanza ni kupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyotusomea kitabu chake chenye mafungu kama tisa hivi. La pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa ziara anazifanya kusimamia Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi, Makamu wa Rais mama Samia anavyozunguka kuweka mambo sawa huko na Mheshimiwa Majaliwa na Mawaziri na wengine wote nawapongeza sana kwa mambo wanayoyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika sijui ni tano au ni kumi?

NAIBU SPIKA: dakika ni kumi.

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. La kwanza nitaanzia kwenye eneo la madini na naomba ku-declare interest kuwa mimi ni mchimbaji mdogo. Kwanza tumpongeze Mheshimiwa Rais na Makamu wake, Waziri wa Madini na Waziri aliyehamia kwenye uwekezaji kwa mkutano tuliofanya pale Dar es Salaam siku mbili, tunaipongeza sana Serikali kwa kuweza kuwasikiliza wadau wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la madini tuliahidi mambo mengi. Serikali yetu cha Chama cha Mapinduzi ni sikivu ilitoa kodi kwenye 27 tukaenda royalty sita kuongeza moja. Si jambo dogo ni jambo kubwa sana. Hapa sasa nataka kuiomba Wizara ya Madini na wachimbaji wadogo wadogo, tulikubali mbele ya Rais kwamba tutalipa kodi, tulikubali mbele ya Rais kwamba hatutatorosha madini, tulikubali mbele ya Rais kwamba lazima tukusanye kodi ili nchi iweze kuendeshwa. Niiombe Wizara ya Madini na Tume waache kuchekacheka na watu wanaoharibu dhamira nzuri ya wachimbaji wadogo. Tumekubaliana mtu akikamatwa na madini mahakamani tena uhujumu uchumi basi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo ndani ya Wizara hao wachimbaji wadogo wanasimamiwa na wafanyakazi wa Wizara ya Madini, hawa wafanyakazi wa madini ambao sio waadilifu waanze kuwachuja wasituletee matatizo. Sisi tumeshakubali kuchimba, tumeshakubali kulipa kodi, lakini unajikuta watu wanaunga, wanafanya jambo baya sana hili. Nimpongeze Waziri wa Madini juzi nilimuona Chunya, wale watu wameondoshwa, waondoshwe wengi, wapo watu wengi sana wanaoharibu kwenye sekta hii. Sekta hii ni nzuri, mwaka kesho wakati tunasomewa hotuba, sekta ya madini itakuwa imepanda mara dufu. Kwa hiyo msingi sisi tunachimba tunalipa kodi, lakini Wizara na Tume wasimamie watu wao. Kwa sababu kule ndani ndio watopandisha leseni anampa huyu na huyu, anageuza huku na huku, lakini kama hatuwezi kuipa umuhimu kama Rais alivyoipa umuhimu kodi hii ukusanyaji wake utakuwa shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale pale kwenye madini walikamatwa watu kwenye makinikia wakazuia michanga yao, sheria imekuja, kuna wenzetu ambao hawana matatizo ya kulipa kodi na kusafirisha michanga yao, kwa nini hawawapi ruhusa Serikali ikapata fedha yake? Wanakosa gani hawa? Mtu yupo tayari kulipa kodi, mtu hana tatizo ni mchimbaji, kuna watu wamewekeza katika nchi hii, kwa nini hawawaruhusu wakafuata taratibu kodi ile ikakusanywa? Nawaomba sana watu wa madini, hili eneo ni nyeti, lakini kuna watu wanafilisika, watu hawahudumiwi. Kwa hiyo, naomba kosa la mtoto mmoja lisimzuie mtoto mwingine kupata haki yake ya maisha. Kwa hiyo nawaomba sana watu madini, waende waangalie eneo hilo, wale watu ambao hawana shida wawaruhusu wasafirishe, walipe kodi, kwa nini wanarundika, wameweka mitaji, hali si nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza niende katika suala la ardhi hapo hapo kwenye madini. Kwenye eneo la ardhi kumepimwa kuna madini lakini pale juu kuna mtu analima mahindi, siku ukienda kuchimba anakwambia sitaki, khaaa wewe unalima mahindi mimi nachimba dhahabu tofauti iko wapi? Niwaombe watu wa ardhi waende kule wawaelimishe hawa watu ambao wapo kwenye maeneo ya madini, nikishapewa ardhini kwa maana nimepewa leseni, mimi nitakuwa chini wewe utakuwa juu, msingi tujadiliane ili watu wote wawe wa moja. Hata hivyo, ukienda eneo la ardhini unakuta nao wameweka masharti yao, imeenda imerudi, wanachelewesha kuchangamsha uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maliasili na Utalii, mtu kapewa leseni ya madini pale vijimiti, kipori anasema ni hifadhi, hifadhi ipi? Wakati mali kubwa ya kuleta ushuru ipo wanaikatalia na hawaifanyii chochote? Hapo tusaidie Watanzania, wachimbaji wadogo wakusanye kodi hii msiweke vikwazo wakati sehemu hii haitumiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili naenda Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mwaka jana nilipambana na wao lakini mwaka huu nawapongeza sana, hongera sana kwa kazi wanayoifanya hasa hasa kwenye eneo la mifugo. Kwenye eneo la mifugo kulikuwa na shida sana sana tu, wafugaji wanatangatanga, wanaenda huku na huku wanafanya hivi, lakini naipongeza Wizara, juzi nimeona wamesaini mkataba wa kujenga viwanda vya nyama vingi na juzi nimeona wametangaza kule kwenye ranch, yale maeneo ya watu kupewa ranch, suala hili ni la muhimu na la
kupongeza, wapo Watanzania walikuwa wanakaa na vitalu hivi bila kulipa chachote Serikali haipati kodi. Sasa leo kwa sababu wamekuja na nia njema waisimamie, vitalu vipatikane, watu wachangie pato la Taifa, maziwa yapatikane, viwanda wanavyovijenga zaidi ya vitano, vipate malighafi. Katika hilo nampongeza Mheshimiwa Mpina, leo nampongeza na Mheshimiwa Ulega, nawapongeza sana wameenda vizuri, waweke utaratibu ili angalau makusanyo ya nchi yapatikane kila eneo yanapotakiwa kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lile la ranch kuna mwenzangu jana alisema Mheshimiwa Kamala sijui kama yupo, kwamba kuna wananchi walikuwepo, tunapotaka kuweka utaratibu watu wamekaa na ranchi miaka zaidi ya 15 Serikali haipati hata senti tano, acheni vitalu vigawiwe, Serikali ikusanye kodi, watu wafuge kwa uzuri ili maendeleo ya nchi yapatikane, sio cha mjomba, cha shangazi, mimi nasema wakaze kamba, tunataka kufuga, tunataka kufua, tunataka Tanzania uchumi uchangamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoka mifugo niende hapa kwenye Mambo ya Ndani, neno hili nalisema kwa mara ya nne, si zuri sana, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Mambo ya Ndani wafanyakazi wa nje waliopo humu nchini, vibali hivi kuna watu wana haki ya kupewa, kuna watu hawana haki ya kupewa. Wapo watu humu nikisema tunanuniana, lakini mimi ni mzee, sina shida, ukininunia mimi naenda kulala, kwa hiyo haisaidii kitu chochote. Yaani mtu ana miaka 20, leo hii wanafanya mpango kumpa uraia, Wizara ya Kazi na Mambo ya Ndani nasema suala hili tutaliweka hadharani hapa, mimi nakusanya vielelezo tu, mtu muda wake umekwisha, anatakiwa kutoka nchini, amekaa zaidi ya miaka 20, anafanya siasa, si Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kwa Mheshimiwa Jenista na Wizara ya Mambo ya Ndani nasema neno hili kwa mara ya mwisho, waende kwa huyu mtu, wampe vibali vya uraia, tutakutana hapa, sisi wote ni Watanzania. Kuna Mzee Raza jana kasema kuna kiwanda, kina watu zaidi ya 300, wanawaombea Engineers wawili wanakataa, watu 300 wote, hawatapata kazi? Huyu mtu anaitwa Vedigree anawalipa shilingi ngapi? Niko tayari kuweka vielelezo mezani nasema kwa mara ya tano leo ndani ya Bunge hili. Sasa wamwandalie uraia halafu tuone uraia huo ataupataje katika nchi hii, sababu si lazima watangaze. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa kengele ya pili.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulembo naomba ukae. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

T A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliweke vizuri jambo hili kwa sababu nisipoliweka vizuri sidhani kama maneno yaliyotumiwa na Mheshimiwa Mbunge kama yapo sawasawa sana kwamba tunapewa shilingi ngapi kwa ajili ya suala hili. Hapana, si sawa, sidhani kama ana hakika kama kuna fedha yoyote imeingia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba tu nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge Ofisi yangu jambo hili imeshalishughulikia na yeye anajua. Kwa hiyo masuala mengine ya mtu kuendelea kuomba kitu chochote, atafuata utaratibu na majibu ya kiutaratibu yatatolewa wakati utakapofika. Tukifika mahali Ofisi imeshachukua hatua na imeendelea kulishughulikia jambo lenyewe, halafu Mheshimiwa Mbunge anajenga hisia kwamba labda Ofisi ya Waziri Mkuu ina jambo fulani, nadhani si sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge na vinginevyo nitumie ile kanuni ya kumwomba aondoe hili jambo katika taarifa yake aliyoisema leo, ama tutumie kanuni nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimimu sana Mheshimiwa Bulembo na naomba nimpe hiyo taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulembo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa watu wenye busara suala la hela nalifuta lakini mazingira ya rushwa siwezi kufuta.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kabla ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri, Katibu Mkuu na Majaji wote wanaotoa haki katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianzie hapa, Mheshimiwa Balozi kabla hujateuliwa kuwa Waziri katika eneo hilo alikuwepo Waziri mmoja anaitwa Mheshimiwa Kabudi. Mheshimiwa Kabudi nilimuuliza kuhusu Mahakama ya Wilaya ya Misenyi. Wilaya ya Misenyi ina miaka zaidi ya 25, ipo boarder na ina kesi nyingi, nikaambiwa bajeti inayokuja Misenyi itakuwepo, kitabu chako hakina Misenyi. Mahakama ya Wilaya haionekani ndani ya kitabu hiki. Sitaki kusema sana Mwanasheria na Waziri tukitoka tuongee kidogo ili mjue utaratibu mtaufanyaje wa Mahakama ya Wilaya ya Misenyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Mahakimu wetu wa Mahakama za Mwanzo. Ni kweli tunajenga Mahakama za Mwanzo, tunarekebisha na kadhalika lakini haki inaanzia chini, hawa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo maisha yao mnayajua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Mahakimu wetu wa Mahakama za Mwanzo. Ni kweli tunajenga Mahakama za Mwanzo, tunarekebisha, tunafanya nini, lakini haki inaanzia chini. Hawa Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo maisha yao mnayajua; ambao wanaanza na kesi ili mtu akate rufaa mpaka Mahakama Kuu, mazingira waliyonayo mnayaona?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, hebu nafasi, wapeni haki ili haki itendeke na watu waweze kuona kwamba haki inaonekana. Maisha yao jamani yanatisha. Sitaki kuingia sana kwa undani lakini naomba Mheshimiwa Waziri pale alipo, hebu akakae na Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo aone wanaishije na wanafananaje ili haki ipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni wasaidizi wa Majaji. Hawa nao wana haki sawa na Mahakimu. Hivi hawa stahili zao ni zipi jamani? Ndio wanamsaidia Jaji kuandaa, kuandika na kadhalika. Hali zao ni dhofulhali, samahani nitumie kauli hiyo. Hebu wapeni value na wao, maana wakitoka pale mnawateua kuwapa nafasi za juu, lakini kazi zao ni ngumu na maisha yao ni magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu cha bajeti humu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika bajeti ya maendeleo haina hata shilingi, lakini ofisi hii ndiyo inafanya kesi zote za nje, ndiyo inasafiri, tunaenda kushindwa. Kuna nini hapa? Kesi za Kimataifa ziko kwenye ofisi yake, hamkumpa hela ya maendeleo hata shilingi moja, atafanyaje kazi? Au tumemaliza kesi za Kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuna Mahakama kama za rafiki zangu akina Mheshimiwa Bashe hawa. Wamejenga wenyewe, wamejenga maboma, wanatakiwa kumaliziwa, kwa nini msingekuwa mnaenda kwa hawa watu ambao wameshaturahisishia kazi ili wakapata huduma hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nampongeza Mheshimiwa Waziri, najua ameingia hivi karibuni bado ana siku chache, lakini hayo machache yanamtosha. Mwakani tutakuwa na mengi sana ya kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. ALHAJI ABDALLLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Awali ya yote kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri na viongozi wote kwa kukubali hii agenda ya wachimbaji wadogo, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili ni kubwa sana na Serikali imeonesha wazi ina nia njema katika suala la wachimbaji wadogo. Tumekaa kwenye Kamati ya Bajeti mpaka karibu saa sita za usiku, nampongeza Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Fedha, Waziri wa Madini ni kama tulitaka kukesha, lakini hatimaye tumekubalina na ajenda imekuja hapa, nawapongeza sana kwa yale tuliyokubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi, shida yangu ni ndogo sana hata dakika tatu sifiki. Mheshimiwa Waziri Mkuu alikaa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, ombi langu kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wasiingilie zoezi hili kwa sababu Rais ameshasema wafanyabiashara wachimbaji wadogo wapewe haki zao na waruhusiwe, wasiingilie. Hii ni kwa sababu atachimba mtu pale Nyamongo au Majimoto lakini bei nzuri iko Shinyanga, huyu mtu ana leseni ni broker/dealer asizuiwe kwenda kuuza Shinyanga kwa sababu Shinyanga ndio kuna mapato. Kwa hiyo, hapa kuna hatari Wakuu wa Mikoa hapa wakataka kila mtu kuonesha amekusanya kiasi gani katika Mkoa/Wilaya yake kuanza kuwasumbua wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, agenda yangu kubwa iko pale wachimbaji wadogo nia ya Rais imeonekana, tunampongeza sana tumekaa naye siku mbili, sheria ni nzuri, kodi zimeondolewa, mchimbaji yeyote Tanzania hii ana raha. Kwa kweli tunampongeza Rais, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu Wakuu wake wa Wilaya na Mikoa awaambie wakae mbali na zoezi hili kwa sababu tutakuwa tunapiga simu nyingi, wasituweke kikwazo njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kwa sababu ni mchimbaji na nawakilisha wachimbaji wenzangu mtuache raia Rais aliyofanya tulipe kodi, tusipeleke madini nje na Serikali ipate mapato yake.

Mheshimiwa Spika, ya kwangu ni hayo tu, nakushukuru sana. (Makofi)