Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Wanu Hafidh Ameir (1 total)

MHE. WANU HAFIDH AMEIR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyotambua kwamba, kuna kazi nzuri ambayo inafanywa na wasaidizi wa kisheria nami natambua kazi nzuri hiyo na ya kizalendo ambayo wamekuwa wakiifanya wasaidizi wa kisheria katika kusaidia wanawake na wananchi kwa ujumla katika level ya chini kabisa katika nchi yetu. Swali, Je, Serikali haioni sasa ipo haja ya kuweka utaratibu maalum wa kuwasaidia hawa wasaidizi wa kisheria, ili kuwafikia wananchi wengi zaidi Tanzania, lakini hasa kuwafikia wanawake ambao hasa ndio wanaingia katika matatizo ya kisheria katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anachokieleza, lakini Wizara imekuwa na utaratibu mzuri sana wa kutoa mafunzo mbalimbali katika maeneo mbalimbali kwenye haya makundi ya watoa msaada wa kisheria. Tumekuwa tukipita katika kila mkoa kujaribu kutoa hii elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ombi lake kwamba, wanawake wengi washirikishwe kwenye suala hili ni ombi muhimu, lakini nipende tu kuwaarifuni kwamba, kumekuwa na shida moja ya akinamama kushiriki kwenye hili zoezi. Tulitembelea Mwanza akinamama walikuwa wanalalamika kwamba, hawaruhusiwi na waume zao kwenda kushiriki kwenye shughuli hii kwasababu, sehemu kubwa sana ya shughuli hii ni kujitolea. Kwa hiyo, kama mtatusaidia Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha akinamama, hii ni kazi huru ambayo mtu yeyote anaweza akaifanya kulingana na kuguswa kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipende tu kusema Wizara haina kizuizi kwa akinamama kushiriki kwenye hili zoezi la utoaji wa huduma za kisheria, lakini sisi wenyewe tuna chuo chetu cha sheria pale Dar-Es-Salaam (Law School) inafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, wataalamu wengi ambao wanatoa huduma hizi katika maeneo mbalimbali nchini wanapita kwenye hicho chuo, lakini tuna watu wa Legal Service Facility; ni taasisi binafsi ambayo nayo imeendelea kutusaidia kuwapa elimu wananchi ambao wamejitolea kutoa msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wizara tumefanya ziara katika maeneo ya Simiyu, Tanga na sasa hivi maafisa wetu wapo Shinyanga na wengine wako Kasulu. Nia ya msingi ni kuwakusanya hawa watoa msaada wa kisheria na kuwapa mbinu mbalimbali za jinsi ya kuwasaidia wananchi wetu, ahsante.