Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Wanu Hafidh Ameir (1 total)

MHE. WANU HAFIDH AMEIR aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha elimu ya Sheria zinazowapa kinga na haki Wanawake inatolewa kwa Wanawake wote Mijini na Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir, Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mipango iliyopo ya kutoa elimu ya sheria si tu kwa wanawake, bali ni pamoja na makundi mengine maalum katika jamii, wakiwemo watoto, watu wenye ulemavu na wazee. Na kuendelea kutoa mafunzo na kusajili watoa huduma ya msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria. Kuanzisha madawati ya huduma ya msaada wa kisheria katika Mahakama, kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili zidi ya Wanawake na Watoto. Mkakati huu unalenga kuimarisha na kulinda haki za wanawake na watoto, kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria katika Vituo vya Polisi na Magereza, kutafsiri sheria zote kwa lugha ya Kiswahili na kuendelea kutoa mafunzo ya sheria kwa wananchi kupitia mikutano na mihadhara mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Msaada wa Kisheria, Na. 1 ya Mwaka 2017. Madhumuni ya Sheria hii pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha msaada wa kisheria, ambao una maana ya utoaji wa elimu na ushauri wa kisheria, uandishi wa nyaraka za kisheria/kimahakama na/ au uwakilishi mahakamani kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili. Tangu kutungwa kwa sheria hii hadi Machi, 2021, takribani wanawake 3,162,421 kutoka mijini na vijijini wamepatiwa elimu na msaada wa kisheria kupitia madhimisho ya wiki ya sheria, wiki ya msaada wa kisheria ambayo inaadhimishwa kila mwaka katika mikoa yote hapa nchini, vipindi vya redio na luninga, ziara za viongozi na wataalamu wa Wizara katika magereza na mahabusu za polisi na majukwaa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kutimiza azma ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki kwa gharama nafuu na kwa wakati. Aidha nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi kuwatumia watoa huduma wa msaada wa kisheria, wakiwemo wasaidizi wa kisheria, walio katika maeneo yao nchi nzima wanapokabiliana na changamoto mbalimbali za kisheria ili kuifikia haki iliyokusudiwa, ahsante.