Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rev. Peter Simon Msigwa (28 total)

MHE. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo hili la Rorya linafanana na tatizo la Iringa Mjini, baada ya kujua tatizo la hospitali ya Rufaa ya Iringa Mjini, Manispaa tumejenga hospitali ambayo inafanya kazi. Hata hivyo, tuna tatizo la vifaa tiba kwa mfano, akinamama wanavyofanyiwa operation wanahitaji wapange foleni kusubiri yale mashuka yakaoshwe kwenye hospitali ya Rufaa, ni lini sasa Serikali itatatua tatizo hili ambalo akinimama kwa kweli wanapata matatizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Peter Msigwa, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa swali lake na majibu ya Serikali ni kwamba yeye ni Mjumbe kwenye Halmashauri ya Mji wa Iringa Mjini. Kwa maana hiyo, anashiriki kikamilifu katika uendeshaji kuanzia kwenye kupanga na hata kusimamia utekelezaji wa sera ya afya na sera ya maendeleo ya jamii kwenye eneo lake.
Namshauri ashirikiane vizuri na Halmashauri yake waweze kupanga bajeti kwa ajili ya kununua mashine za kufulia nguo hizo, ambapo zinakosekana kwenye hospitali moja ili aweze kutoa hiyo huduma kwa ukaribu na kwa urahisi zaidi kwa wananchi wanaohitaji.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo naomba niseme tu kwamba. Uendeshaji wa hizi hospitali una changamoto kubwa ya kifedha, kama nilivyosema awali, na kwa maana hiyo, Waheshimiwa Wabunge wote wakitaka kutatua matatizo yanayozikabili hospitali zao ni lazima wawe makini kwenye kuelekeza mapato yanayotokana na own source collection za pale kwenye Halmashauri, kwenye eneo hili la huduma za afya.
Maana kila Mbunge sasa amekuwa anatuletea maswali sisi watu wa Wizara ya Afya wakati sisi kazi yetu ni kutoa technical support, kazi yetu ni kusimamia ubora na vitu vingine lakini wao wenyewe Wabunge, wakishirikiana na Madiwani na Halmashauri zao wana jukumu la kutoa huduma bora zaidi kwa Wananchi wanaowaongoza. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Pamoja na majibu ma… yasiyoridhisha sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwa na malalamiko mengi sana ya hawa wastaafu. Mmetutangazia kwamba hapa kazi tu, unaweza ukatuambia ni lini hawa wastaafu watapewa hizo hela kwa sababu sasa ni muda mrefu umepita? Tunataka tupate muda kwa sababu kwa kweli wanakuja kwenye maofisi yetu na wanatusumbua. Naibu Waziri ametangaza kwamba wamelipwa lakini hawajalipwa wakati waliahidiwa? Ni lini sasa Serikali hii ambayo inasema hapa kazi itatoa hizo pesa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Peter Msigwa kwa swali zuri lakini kwa kukiri japo ameishia njiani kwamba kwa majibu yangu mazuri, nakushukuru sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimesema kwamba bodi hizi zinaendelea na mchakato ili waweze kutangaza baada ya SSRA kumalizia actuarial valuation. Leo hii mchana nitakuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa SSRA kuhusu suala hili. Naomba niwaahidi wastaafu hawa kwamba pale tu tutakapomaliza, Serikali imeshaji-commit kwamba tutalipa malipo yao yote kuanzia Julai 2015.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa pesa ambazo MCC walikuwa waipatie Tanzania zingeshiriki kutatua tatizo kubwa na kero kubwa ya umeme na sasa wamesitisha kutoa pesa hizo. Je, Serikali inaweza kutuambia ni athari gani zinaweza kupatikana kwa wananchi kwa kukosa msaada huo wa MCC?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote wasikilize kwa makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna hata dola moja, hata senti moja ya MCC ilikuwa iko kwenye Miradi ya Umeme Vijijini. Hiyo hawezi kunibishia Mheshimiwa Msigwa kwa sababu mimi mwenyewe ndiyo nimeenda kukaa na watu wa MCC, nimekaa na Waziri wa Nishati na wa Fedha wa Marekani, hizo fedha zilikuwa haziji Bungeni hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la MCC halafu fedha zote za MCC hazikuwa za umeme vijijini. Hilo nalo ni kosa lingine ambalo lazima watu waelewe, kuna fedha za barabara halafu kuna fedha za maji na vitu vingi sana, katika zile fedha za MCC zilizokuwa za umeme hazivuki theluthi moja. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania ni kwamba mimi tunaongea kwa takwimu, siyo ubishi, ni takwimu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote naomba hili jambo tulielewe hivi, mimi hapa ninataka kulima heka nane za mahindi, ndugu yangu, rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango anasema Mheshimiwa Muhongo kwa nini ulime heka nane? Mimi naomba nikuongezee heka mbili, ili zitimie ziwe kumi na mimi nasema ahsante ndugu yangu nipatie. Kwa hiyo, asiponipatia hizo heka mbili mimi bado za kwangu nane nitalima.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru; Mheshimiwa Waziri dhana nzima ya diplomasia ya kiuchumi ni pana sana na hivi karibuni tumeona Tanzania inasita kusaini Mkataba wa EPA pamoja na Jumuiya ya Ulaya. Ni sababu zipi za kimsingi ambazo zinasabisha Tanzania iwe inasuasua, na muda mrefu Wabunge tumekuwa tukiuliza Serikali kwamba haijiandai ku-capitalize kwa fursa zinazotokea? Sasa Mheshimiwa Waziri unasema Serikali imejipanga, ni kwa nini hasa Serikali imekuwa ikisuasua pamoja na kwamba inaweza ikawa na sababu nzuri kusaini huu mkataba pamoja na Jumuiya za Ulaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu kwamba kama tunavyosema kwamba chochote sisi tunachokipigania kama Wizara na kama Serikali ni kwa manufaa ya nchi hii, ni kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, tumesema kwamba hatusaini kwa sababu mkataba ule kwa namna fulani jinsi ulivyokaa uta-affect maslahi ya Tanzania na hasa katika suala zima la kuhakikisha kwamba viwanda vinaweza kuendelea na wewe unajua kuhusu hilo. Kwa hiyo, hatusaini kwa sababu hizo. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, toka mpango huu umeanza baadhi yetu
tuli-challenge sana kwamba haukuanza kubadilisha fikra za watu kabla ya kuwapa hela. Nataka nimuulize Waziri ni kwa kiwango gani anaweza akaliambia Bunge hili huu mpango
wa kugawa hizi fedha umeleta impact katika jamii, kwa sababu bado hali ya umaskini imeendelea kuwa kubwa katika Taifa letu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, naamini, bahati nzuri wiki iliyopita tu tulikuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, tulikuwa
Iringa Mjini, tumetembelea walengwa wale na kaya zake. Sasa kama leo anasema kaya zile kweli hazijanufaika na hazijaondoka kwenye umaskini, kwa kweli inabidi hata wapiga kura wamwangalie kwa macho mawili, mawili.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ukiangalia
tumefanya tathmini kuangalia ni kwa namna gani fedha hizi zimeweza kuchochea mabadiliko. Vilevile ukiangalia katika TASAF Awamu ya I na II, kulikuwa hakuna ruzuku ya uhawilishaji lakini ilikuja kuonekana katika Watanzania asilimia 28.3 wenye pengo la umaskini walikuwa hawawezi
kumudu gharama za kupeleka familia zao katika matibabu, wengine watoto wao walikuwa wamedumaa, wengine walikuwa hawapati lishe ya kutosha, wengine walikuwa hata
shuleni mahudhurio hawahudhurii vizuri. Ukiangalia sasa hata Iringa peke yake zaidi ya asilimia 70 mpaka 90 mahudhurio yameimarika, wengine sasa zaidi ya asilimia 10 mpaka 15 wanaanza kukaribia kuondoka katika pengo la umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nipende tu kusema
wengi wameboresha mavazi, wengi ameboresha makazi yao, wengi sasa ukiangalia hata kwa zile kaya zilizokuwa zinajiweza ambazo zilikuwa haziwezi kuwavalisha watoto wao shuleni, wanaangalia kama mtoto maskini anaweza kuvaa nadhifu basi na yeye kidogo anajiongeza. Kwa hiyo, kwa kweli ni Mfuko ambao umekuwa na manufaa sana na nimwombe Mheshimiwa Msigwa aendelee kufuatilia kaya zake na aendelee kuziunga mkono. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Manispaa ya Iringa na kiwanja cha ndege cha Nduli kimekaa kimkakati, ukizingatia kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii inaboresha Southen Sackett kwa ajili ya kuimarisha utalii Kusini mwa Tanzania. Ni lini sasa Serikali ilikuwa imeahidi kwamba kiwanja hiki kitaboreshwa kama ambavyo Waziri amesema kwamba ni miongoni mwa viwanja 11 ili Manispaa ya Iringa iweze kukua kiuchumi na kimkakati kwa ajili ya ku-boost uchumi wa Taifa ambao kimsingi uchumi unaenda chini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilijibu swali la Mheshimiwa Sokombi, kwamba katika viwanja ambavyo tunatarajia kupata mkopo hivi karibuni ni kiwanja cha Musoma, Nduli na Mtwara. Kwa hiyo, naomba
nimhakikishie Mheshimiwa Msigwa kwamba kiwanja cha Nduli nacho kipo katika mtazamo wa mbele sana ili kuhakikisha kwamba utalii unaongezeka katika mbuga yetu ile ya Ruaha na kuleta mapato makubwa kwa Serikali.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nakubaliana naye kwamba kwa mujibu wa Sheria na Katiba yetu, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho na ndiye Mwajiri Mkuu.
Swali la msingi limeulizwa kwamba kumekuwa na practice ya kuanzia Rais mwenyewe na ma-DC na RCs kutumbua au kuwasimamisha watu kwa njia ya mnada, kupigia kura atumbuliwe au asitumbuliwe, kwa hiyo, swali la msingi linaulizwa hapa, ni kwa nini Serikali isifuate utaratibu na kanuni na sheria ambazo sisi wenyewe tumeziweka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa ma-RC na ma-DC ni kada ya kisiasa kama sisi Wabunge tulivyo, hawana weledi na ndiyo maana Baba wa Taifa alisema tuliweka sheria ngumu sana ili mtu asizuke tu na kufukuza watu ovyo ovyo. Kwa kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alithamini sana kada ya watendaji wa umma; je, Serikali itatoa tamko sasa kwamba ma-RC na ma-DC wasikurupuke tu kuwafukuzisha watu bila kufuata taratibu na kanuni za nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na kwa nini Serikali isifuate utaratibu, napenda kuendelea kusisitiza kwamba Serikali inafuata uratatibu na kwamba kwa wateule ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais, hatua zao za kinidhamu huchukuliwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa mujibu wa kifungu cha 4(3)(d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema katika Ibara ya 36(4), Mheshimiwa Rais pamoja na kukasimu bado anayo mamlaka ya mwisho na hakatazwi kutumia mamlaka yake. Kwa watumishi wengine wa umma, kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Mamlaka za Nidhamu zimepewa mamlaka yao ya mwisho kabisa ya kuweza kuchukua hatua kwa watumishi wengine ambao sio wateule wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuendelea kusisitiza kwamba jambo la msingi katika mamlaka za kinidhamu zinapochukua hatua, wanatakiwa wazingatie hatua tatu zifuatazo:-
Kwanza kabisa waweze kutoa hati ya nashtaka; pili, watoe fursa ya kujitetea kwa yule mtuhumiwa au mtumishi; na mwisho, tatu, uchunguzi wa kina uweze kufanyika ili kuthibitisha tuhuma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kusema, utaratibu mzima wa kina na mwongozo umefafanuliwa katika kanuni ya 46 na 47 za Kanuni za Utumishi wa Umma. Endapo kuna mtumishi wa umma anaona hajaridhika na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa, anayo fursa kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Utumishi wa Umma kuweza kukata rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili kwamba Serikali inatoa tamko gani katika hatua ambazo zimechukuliwa na ma-RC na ma-DC? Naendelea kusisitiza kwamba kifungu cha 6(1)(b) na kifungu cha 4(3)(d) kimeelekeza Mamlaka za Nidhamu ni zipi? Ndicho ambacho
Serikali imekuwa ikifuata.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi ambalo niliuliza kuhusu vivutio, Mji wetu wa Iringa ni Mji mkongwe ambao una historia kubwa ya Mtemi wetu Mkwawa jinsi alivyopambana na Mjerumani. Ni juhudi zipi za makusudi ambazo zinafanywa na maliasili kuhakikisha kwamba mji huu wa Iringa na historia kubwa ya Mtemi Mkwawa inaendelea kujulikana katika dunia nzima na Tanzania kwa ujumla?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua nyingi zinafanywa kuboresha utalii katika eneo zima la Kusini mwa Tanzania, lakini hususan Mji wa Iringa na viunga vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumefungua makumbusho ya historia ya Iringa na utemi wake kule. Pili, Serikali inapanua Uwanja wa Nduli kama ulivyoona kwenye bajeti. Vile vile Serikali imepanga kujenga barabara kutoka kwenye geti la Ruaha kuja Ruaha Mjini. Shughuli hii tumeishughulikia sana na Mheshimiwa Lukuvi katika kuitekeleza pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tumeanza kwa mara ya kwanza kuwa na Maonesho ya Utalii Kusini mwa Tanzania na yalikuwa Iringa na mwaka huu maonesho hayo ni makubwa zaidi. Waheshimiwa Wabunge, nawakaribisha mje kushiriki katika maonesho hayo. Ahsante.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kama ambavyo Wabunge wengi wanaliona tatizo hili, limekuwa tatizo kubwa sana. Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba ni suala la kumiliki, gari halimilikiwa kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalipa kwa ajili ya matumizi ya barabara, lakini watu wengi wamepata tabu katika hili, kwa nini Serikali isitoe tamko kwamba hili suala italifuta ili wananchi tulipe hiyo road license kutokana na matumizi ya barabara.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwa niaba ya Serikali kwa ujumla.
Swali hili limeonyesha kuwa na interest kubwa kwa Waheshimiwa Wabunge na simaanishi kwamba ni kwa ajili yao wenyewe ni kwa ajili ya nchi nzima na watu wanaowawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri sana, utaratibu tunaoutumia ndani ya Serikali Waheshimiwa Wabunge mnafahamu. Kwanza sheria iliyopo ndio inayotumika mpaka sasa, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza hapa kwa niaba ya Serikali tumesikia na kama tumesikia ina maana ni process ambayo inayotakiwa ya kurudi na kwenda kulitazama suala hili kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri hawezi sasa hapa ndani akatoa commitment ya kubadilisha sheria akiwa hapa ndani ya Bunge bila kuzingatia utaratibu wa kisheria wa kubadilisha sheria.
Mheshimiwa Spika, tunakuomba sana kwa heshima ya Bunge lako, haya yote yaliyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge Serikali imesikia lakini kwa pamoja tutajadiliana tujue namna nzuri ya kuweza kulishguhulikia jambo hili. Tunakuomba sana uielewe nia njema ya Serikali. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa niipongeze Wizara imekuwa mara nyingi ikihamasisha tutunze mazingira na sisi kama wawakilishi wa wananchi tumekuwa tukifanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi tumsikilize Rais au tumsikilize Waziri? Mara nyingi tumeambiwa Rais akisema ni sheria. Rais jana amewatangazia wananchi kwamba walime, waingie kwenye mabonde mpaka mvua itakapowatoa na hii sheria ya Rais anayoisema Mheshimiwa Waziri inahusu tu Kanda ya Ziwa na ni sheria namba ngapi kwa sababu anazungumza kila siku kwenye Kanda ya Ziwa, analeta upendeleo wa wazi. Je, tumsikilize Rais au tumsikilize Waziri? Kwa nini kila wakati Rais akienda Kanda ya Ziwa…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msigwa ambaye alikuwa commissioner mwenzangu sasa nime-retire, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu haiongozwi kwa kupendelea wananchi wa eneo moja. Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na Katiba. Nimhakikishie na nirudie tena, alichokisema Rais wetu kule Kagera hajavunja sheria nimekwambia kifungu cha 57 kasome ambacho kinatoa mamlaka ya kuruhusu na hata wewe Mheshimiwa Msigwa kama una shughuli zako unataka kuzifanya kando kando ya ziwa au mto lete Ofisini kwetu utapata kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Mheshimiwa Msigwa mimi nimeenda Kihansi nimekuta wananchi kule Kihansi pamoja Mufindi na Ifakara wanalima kwenye bonde la Mto Kihansi na tumewasaidia kabisa wananchi wale kwenye mradi wetu ili waendeleze lile bonde kwa kilimo. Hii inaonyesha dhahiri kwamba hatubagui, wananchi wote wako sawasawa.
heshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, wananchi ambao wamezoea kuchezea sheria, Serikali ya Awamu ya Tano haitamfumbia macho yeyote ama kwa kuchochea wananchi wavunje sheria ama yeye mwenyewe kuvunja sheria watapambana na mkono wa sheria na sheria hii inatoa adhabu kwa wanaochochea. Ahsante sana. (Makofi/ Vigelegele)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yamedhihirisha kwamba katika kipindi kifupi ambacho ameshika nafasi hii kwa kweli amejua mambo kwa haraka na kwa uzuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee mambo mawili, kwanza, Serikali kupitia Ofisi yetu iliziagiza lakini napenda nirudie kutoa agizo tena upya kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Halmashauri zetu kuorodhesha vyanzo vyote vya maji katika maeneo yao na kuvileta kwetu na kuelezea hatua ambazo zinachukuliwa katika kuvilinda, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kifungu cha 57 cha Sheria ya Mazingira, Na.20 ya mwaka 2004, kipengele cha (1) kinaweka zuio la kufanya shughuli mita 60 kwenye kingo za mito, fukwe na maziwa lakini kifungu kinachofuatia cha (2) kinasema, Waziri anaweza kuweka miongozo ya kuendesha shughuli za binadamu ndani ya maeneo yaliyoelezwa kwa mujibu wa kifungu hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya maelekezo mahsusi ya eneo mahsusi alilokuwepo Mheshimiwa Rais, kazi yetu sisi sasa ni kutengeneza mwongozo wa namna ya kufanya shughuli ile katika eneo lile lakini hapo hapo kwa kuzingatia hifadhi ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niliweke sawa kwa namna hiyo kwamba kutokana na maelekezo yaliyotolewa, sisi sasa sheria inatuelekeza kuweka mwongozo wa pale mahali ambapo wale watu waliomba kufanya ile shughuli namna ya kufanya ile shughuli bila kuathiri mazingira. Kwa hiyo, hakuna blanket permission ya kuvamia vyanzo vya maji na kingo za mito kote nchini. Tutaendelea kufuata sheria kwa sababu sheria bado ipo. Ahsante.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuweka kumbukumbu sawa kwenye jambo moja huku nikipongeza majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri pamoja na Waziri mwenye dhamana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili lililosemwa kwamba Rais anapendelea Kanda ya Ziwa, nataka niweke kumbukumbu sawa kwamba Mheshimiwa Rais siyo kwamba anapendelea Kanda ya Ziwa, isipokuwa Rais amekuwa akisikiliza vilio vya wananchi pale anapokuwa katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jambo ambalo nataka nitumie kumbukumbu, Mheshimiwa Rais alipokuwa Bagamoyo, wananchi walipolilia eneo la Magereza alilitoa hapo hapo huku sheria ikiwa inataka eneo lile litumike kwa ajili ya Magereza, lakini kwa kuwa kilio cha wananchi kilikuwa kikubwa na huko siyo Kanda ya Ziwa ni Pwani, hapo hapo wala hata hakusubiri maelekezo ya Wizara kukaa kama alivyosema Kanda ya Ziwa, pale aliamua hapo hapo akasema wananchi hawa wapewe eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ndivyo ambavyo nasemea ni kwamba anakuwa anatolea utatuzi changamoto za wananchi na hicho ndicho kilichomfanya achaguliwe na yuko kwa ajili hiyo. Siku atakapokuwa Ruvuma atatoa majibu hayo hayo kwenye kilio cha wananchi, siku akiwa Arusha atatoa majibu hivyo hivyo na maeneo mengine mengi ameshafanya shughuli za aina hiyo, hivyo tusije tukapotosha utekelezaji wa kazi za Mheshimiwa Rais. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini katika ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi yetu katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano umeongezeka sana.
Je, ni lini Tume hii itatoa ripoti kwa sababu polisi wamekuwa wakikaa na watu mahabusu zaidi ya saa 24 kinyume cha sheria kitu ambacho kinakiuka haki za binadamu. Mimi binafsi nasema haya kwa uzoefu nilionao, mara nyingi nimekuwa nakwenda kwenye custody nayaona haya na naongea kama Mbunge kwamba kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, kuna watu wanakaa zaidi ya miezi miwili katika vituo vya poilisi wanakuwa tortured, wanapigwa na wanaumizwa.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na tatizo hili ambapo kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu katika vituo vya polisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi la Mhehimiwa Msigwa hapa imebeba hoja, ni lini Tume italeta taarifa kuhusiana na vitendo ambavyo vinavyanywa na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwneyekiti, kazi ya Tume hii inajikita katika maeneo tofauti tofauti, ukiacha masuala ambayo yanahusisha polisi, lakini Tume hii ina kazi nyingi za kufanya kwa maana ya kutoa elimu lakini vilevile kwenda kutembelea katika shule za maadilisho, mahabusu za watoto na kila Tume inapokwenda kufanya kazi hiyo imekuwa ikiandaa taarifa na kuziwasilisha katika taasisi husika na mojawapo ikiwa ni kutoa maangalizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa tu ya Mheshimiwa Mbunge, Tume imekuwa ikifanya kazi hii. Kwa mfano, kipindi cha mwaka jana ilitolewa kauli moja kutoka kule Zanzibar na Jeshi la Polisi la kuzuia baadhi ya wafuasi wasiwakilishwe mahakamani na Tume ilitoa maelekezo na kulionya Jeshi la Polisi kwamba hizo ni haki za kimsingi kwa sababu ukisoma kwenye Sheria ya Mwenedo wa Makosa ya Jinai, kifungu cha 40 kinaelekeza kabisa kwamba kila mtu ana haki ya kuwasilishwa katika kesi za jinai.
Kwa hiyo, Tume imefanya kazi yake kuhakikisha kwamba likitokea jambo lolote lile kuhusu taasisi mbalimbali za Serikali au binafsi ambazo zinaonekana kama zinakiuka haki basi wamekuwa kwakitoa taarifa zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kumalizia ni kwamba pamoja na ukaguzi unaofanyika taarifa hizi zimekuwa zikiandaliwa na wahusika wamekuwa wakiwasilishiwa na hapa Bungeni taarifa itakuja rasmi kwa sababu ya ile taarifa ambayo tunaitegemea ya Tume ambayo itawasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na athari kubwa ambazo zimetokana na mabadiliko ya tabianchi, wakazi wa Mkoa wa Iringa wamekuwa wakihamasishwa sana namna ya kupanda miti na wamejitahidi sana kupanda miti ili kuokoa hii hali ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, kuna wakati wakazi hawa walikuwa wameambiwa kwamba jinsi wanavyoendelea kupanda miti watapata fidia kutokana na jinsi wanavyopata miti kutoka kwenye mashirika mbalimbali duniani. Je, hili limeishia wapi? Ningeomba nipate majibu kutoka Serikalini.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba nchi yetu imeanza kuwa na dalili za kuwa na jangwa, nchi yetu inakuwa na ukame na hatuna option, lazima Watanzania kote nchini tuweze kuwa na tabia ya kupanda miti. Na kama nilivyosema juzi, ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika Ilani hii ya CCM, ukurasa wa 212 mpaka 213 unazitaka Halmashauri zote nchini wapande miti kila mwaka isiyopungua 1,500,000.
Kwa hiyo, kwa kuwa, Wananchi wa Iringa wameanza juhudi hii sisi tuko tayari kuhakikisha kwamba, hewa ya ukaa ambayo inaharibu ozone layer yaani tabaka la ozone na kusababisha miale mikubwa ya jua ule mnururisho uweze kuleta joto jingi duniani, ni kweli mashirika ya kimataifa yananunua kitu tunaita karadha, kwa jinsi ambavyo miti ile ndio inayosaidia kufyonza hewa ya ukaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa wananchi wa Iringa wameanza na wananchi wengine wameanza, Ofisi ya Makamu wa Rais itaanzisha utaratibu wa kuona ni kiwango gani wananchi wameweza kupanda miti ili watalaam sasa waweze kuona kiwango cha karadha ya ufyonzaji wa hewa ya ukaa, ili waweze kupata fidia kwenye mashirika ya kimataifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri kuhusu demokrasia, hivi tunavyozungumza wanafunzi wa CHASO wanaohusiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo wanazuiwa kufanya mahafali yao wakati wanafunzi wa Chama cha Mapinduzi wanaruhusiwa na kuna barua za polisi zinazuia mikutano hiyo. Unawezaje kusema tunafanya demokrasia kwa kiwango kikubwa wakati kuna upendeleo wa wazi kabisa? Ni sawa na kwenye ndondi, mmoja amefungwa mikono halafu unasema upigane.
Je, Waziri atakuwa tayari kuliagiza Jeshi la Polisi liache kufanya upendeleo katika kutekeleza majukumu ya ku- practise demokrasia? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, niseme tu mambo mawili, moja, alilosema Mheshimiwa Masoud la mikutano ya hadhara, mikutano hii haijazuiwa ila imewekewa utaratibu na duniani kote standard ya mikutano ya hadhara ni kama hivi tunavyofanya sisi hapa sasa. Tusifanye vitu kimazoea, duniani kote standard ya mikutano ya hadhara ni hivi tunavyofanya sisi, nendeni hata kule tulikojifunza demokrasia ya siasa ya vyama vingi huu ndiyo utaratibu wanaoutumia. Mwaka jana Marekani imefanya uchaguzi, mmemuona Hillary akishukuru? Aliyeshinda ndiye anaendesha Serikali kwa utaratibu wa Kiserikali wa kuendesha taratibu, hili liko wazi duniani kote wala si la kuuliza, ndiyo utaratibu unaotumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu mikutano aliyoisemea Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, niseme tu taratibu ziko wazi. Kama CCM wamefuata taratibu wakapewa mikutano, chama kingine chochote wanachotakiwa ni kufuata taratibu zilezile waweze kupewa mikutano…

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, hili na lenyewe liko wazi. Kama wengine hawajafuata utaratibu hawatapewa tu kwa sababu CCM walipewa, watapewa kwa kufuata utaratibu. Mheshimiwa Mchungaji Msigwa tumekuwa tukifanya hivyo kote na si sehemu yako tu, mbona kuna sehemu nyingine CHASO haohao wamepewa mikutano? Kwa hiyo kinachotakiwa ni kufuata taratibu za kupewa mikutano hiyo. (Makofi)
Sasa Mheshimiwa Esther, Waziri wa Mambo ya Ndani akiongea unatakiwa unyamaze, nimeshajua kwa nini babu zangu kule Mara wanapiga wake zao. Mtu anapoongea, hasa Waziri ambaye ana Jeshi la Polisi unatakiwa unyamaze kimya umsikilize. (Makofi/Kicheko)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi ambalo niliuliza kuhusu vivutio, Mji wetu wa Iringa ni Mji mkongwe ambao una historia kubwa ya Mtemi wetu Mkwawa jinsi alivyopambana na Mjerumani. Ni juhudi zipi za makusudi ambazo zinafanywa na maliasili kuhakikisha kwamba mji huu wa Iringa na historia kubwa ya Mtemi Mkwawa inaendelea kujulikana katika dunia nzima na Tanzania kwa ujumla?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua nyingi zinafanywa kuboresha utalii katika eneo zima la Kusini mwa Tanzania, lakini hususan Mji wa Iringa na viunga vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumefungua makumbusho ya historia ya Iringa na utemi wake kule. Pili, Serikali inapanua Uwanja wa Nduli kama ulivyoona kwenye bajeti. Vile vile Serikali imepanga kujenga barabara kutoka kwenye geti la Ruaha kuja Ruaha Mjini. Shughuli hii tumeishughulikia sana na Mheshimiwa Lukuvi katika kuitekeleza pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tumeanza kwa mara ya kwanza kuwa na Maonesho ya Utalii Kusini mwa Tanzania na yalikuwa Iringa na mwaka huu maonesho hayo ni makubwa zaidi. Waheshimiwa Wabunge, nawakaribisha mje kushiriki katika maonesho hayo. Ahsante.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Na mimi nikupongeze kwa kurudi salama, tuliku- miss pia.
Mheshimiwa Spika, elimu ya kisasa ya sheria sasa hivi ina-encourage kupunguza misongamano kwenye Magereza, wanapokwenda kwenye Mahakama wahakikishe wanapunguza misongamano na kuwapeleka watu Magerezani bila sababu.
Mheshimiwa Spika, kama swali la msingi ambavyo limeulizwa ukienda kwenye Magereza yetu, kuna msongamano mkubwa sana. Kwa mfano, Gereza la Segerea ambalo nili-happen kulitembelea juzi, capacity yake ni mahabusu 700, lakini sasa hivi lina mahabusu na wafungwa 2,400. Wanalazimika watu kulala upande mmoja mmoja kwa zamu baada ya muda tena inapigwa alarm, halafu wageukie upande mwingine. Huu ni ukiukwaji kabisa wa haki za binadamu. Kuna watoto wengi ambao wako under age wamekaa pale, wengine wanatakiwa waende shuleni. Hii tuna-cripple Taifa la baadae, wala hatuwasaidii wale watoto ambao wako Magerezani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu; kwa kuwa hii modern law inafundisha kupunguza mahabusu kwa kadri iwezekanavyo wasiende Magerezani; ni kwa nini Serikali imekuwa ikipeleka wanasheria kutetea kesi za Serikali ambao wamekuwa wakilazimisha wale ambao wanaweza wakapata bail waende kukaa mahabusu, kama ambavyo kesi zetu sisi zilikuwa zina bail, lakini Mawakili wa Serikali wakawa wanalazimisha twende kule tukaongeze msongamano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, mahabusu kuwekwa ndani kwa muda mrefu siyo suala tu la kwamba Serikali haitaki kesi ziishe mapema, lakini kuna sababu nyingi za msingi za baadhi ya watuhumiwa kutoachiwa.
Mheshimiwa Spika, moja, mara nyingine ni kwa sababu ya usalama wao. Kwa mfano, kama ni watu ambao wametenda makosa ambao unahisi kwamba wakienda nje wanaweza wakapata matatizo, mara nyingi Serikali inajaribu kuwalinda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ya pili, kuna watuhumiwa ambao wakitoka nje wanaweza vilevile kwenda kuharibu ushahidi. Kwa hiyo, Serikali inaangalia hivyo vitu vyote. Siyo suala la kwamba hutaki kesi iishe, lakini yawezekana unapowaachia kurudi, wanaenda kusababisha kesi ichelewe kwa sababu wataharibu ushahidi. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri na kwamba kweli ujenzi wa matenki unaendelea, lakini kuna maeneo mengine ambayo ni korofi kama Mabwepande, Kijiji cha Mbopo na maeneo mbalimbali ya Kata ya Mbezi ikiwemo Mtaa wa Ndumbwanji. Ni lini sasa Serikali itatia mkazo kuhakikisha maeneo hayo yanapatiwa maji kwa haraka sana kwa sababu kumekuwa na shida?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Manispaa ya Iringa na Iringa kwa ujumla inategemewa kuwa ni kitovu kikubwa cha utalii wa Kusini na Manispaa ya Iringa imebakiza asilimia nne za upatikanaji wa maji. Je, ni lini sasa hizo asilimia nne zitaisha ili watalii watakapofika kule wasipate matatizo wanapokwenda katika maeneo yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa sana kuondoa tatizo la maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na mpaka sasa hali ya upatikanaji ipo katika asilimia 75 lakini yapo maeneo ambayo hayana maji. Serikali kwa kuona hilo sasa kuna mradi ambao unatekelezwa kutoka Mpiji – Tegeta
(a) Bagamoyo lakini Mbezi mpaka kwa kaka yangu Mheshimiwa Mnyika katika kuhakikisha inatatua tatizo la maji.
Kwa hiyo, mpaka mkataba huu utakapokuwa umesainiwa na kupata kibali kutoka Benki ya Dunia tutatekeleza kwa wakati ili wananchi wa Dar es Salaam waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kulishukuru Bunge lako Tukufu, katika bajeti yetu ya Wizara ya Maji tumepitishiwa kiasi cha shilingi 727,345,000,000. Katika fedha hizo tutauangalia Mji wa Iringa katika kuhakikisha tunaondoa tatizo la maji. Ahsante sana.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Manispaa ya Iringa ni moja ya Manispaa ambazo zinatekeleza kwa ukamilifu na kwa uaminifu suala hili la asilimia 10 kwa vijana na akina mama. Na kwa kuwa Serikali imekuwa ikichelewa wakati fulani kuleta pesa zinazotoka Serikali Kuu kwa ajili ya maendeleo, Wizara haioni ni muhimu sasa kuziona halmashauri kama Manispaa ya Iringa ambazo zinafanya vizuri ili ziwape kipaumbele kupeleka hela za kimaendeleo kwa sababu zinatekeleza wajibu wake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la rafiki yangu, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba nikiri wazi kuna manispaa nyingi sana zafanya vizuri hapa nchini kwetu katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Miongoni mwa manispaa inayofanya vizuri vilevile ni Manispaa ya Kinondoni ukiachana na Iringa na juzi juzi waliweza kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa ajili ya mikopo ya akina mama na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la upelekaji wa fedha za maendeleo tumejipanga na ndiyo maana hapa katikati unaona jinsi tunavyojitahidi kwa kadri iwezekanavyo na tuna matarajio kwamba kabla mwaka huu wa fedha haujafika, si Halmashauri ya Iringa peke yake isipokuwa manispaa zote na halmashauri zote kuhakikisha zinapata fedha na especially kwa ajili ya kwenda kukamilisha yale majengo yetu ya hospitali na madarasa. Tunawasiliana na wenzetu wa Hazina ikibidi tutatumia force account kuhakikisha kiwango kikubwa cha fedha kinapatikana katika halmashauri zetu ili miradi hii ya maendeleo iweze kutekelezeka katika eneo yetu.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Tatizo la wahamiaji haramu ni kubwa sana katika magereza nyingi za nchi hii na wengine wako under age. Tatizo kubwa ni pale ambapo hawa wahamiaji haramu kwa mfano Waethiopia wanakuwa wamemaliza vifungo vyao mfano mzuri ni Gereza la Lwanda, Mbeya Waethiopia 41 wamemaliza vifungo vyao zaidi ya miezi mitano, Serikali haina pesa za ku-process kuwarudisha nyumbani kwao wanaendelea kula chakula chetu. Ni lini Serikali itafanya mchakato wa makusudi wa kuwarudisha? Shahidi mzuri ni Mheshimiwa Sugu ambaye alikuwa katika gereza hilo.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kwamba wahamiaji hawa wanarudi majumbani kwao baada ya kukamilisha kifungo chao. Si tu kwa kutumia rasilimali zetu chache tulizokuwa nazo, lakini pia kwa kutumia ushirikiano na uhusiano tuliyokuwanayo na Taasisi ya Uhamiaji ya Dunia (IOM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mchungaji Msigwa atambue kwamba jitihada hizo tuendelee nazo kwa kasi. Hatupendelei wafungwa hawa waendelee kuishi magerezani kwani kufanya hivyo ni kuitia hasara Serikali. Sisi tutaendelea jitihada hizo kadri uwezo unavyoruhusu. Nadhani matukio kama haya ni machache sana nchini wengi tumekuwa tukiwarudisha.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na majibu yake ya swali la msingi, tukumbuke kwamba viwanja hivi vilitengwa wakati mfumo wa chama kimoja na maeneo mengi yalitengwa na wakoloni, kwa maana ya kwamba wananchi wote wafaidike na maeneo hayo. Chama cha Mapinduzi kime-take advantage na kwa kweli kimekuwa hakiendelezi hivyo viwanja.
Mheshimiwa Spika, hamuoni kwamba mnapingana na sera yenu ya kutenda haki na usawa katika nchi kwa kuendelea kupora na kunyang’anya hivo viwanja, kuwadhulumu Watanzania wote ambao walishiriki kutengeneza na kuviandaa viwanja hivyo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, viwanja hivi havikuporwa kwa mtu yeyote, hii dhana ya kuporwa inaondoka kabisa kwenye swali la msingi alilouliza Mheshimiwa Devotha Minja.
Mheshimiwa Spika, naomba tu kukuhakikishia tu kwamba kama kuna hoja ya msingi kwamba kuna kuporwa, maana kuporwa is a criminal act, basi naomba hili suala lifikishwe Mahakamani ili liweze kuamuliwa inavyostahili. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, amezungumza kwamba sababu nyingine inayochangia ni pamoja na imani za kidini na hali ngumu ya maisha. Ni kwa nini sasa Serikali isichukue jukumu la makusudi, kwa sababu tatizo la ombaomba kwa watu wengi ni mindset, la kuelimisha jamii kwa vipindi mbalimbali vya redio na television kuhakikisha tunabadilisha mtazamo kusudi hawa watu kama ni imani za kidini waende kwenye imani wanazoziamini wakapate misaada huko badala ya kuwa barabarani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wake ni mzuri na yeye ni kiongozi wa dini. Nadhani sababu mojawapo ya kuwepo kwa ombaomba wengi kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kwamba watu wengine wanatoa misaada kama sehemu ya ibada. Ndiyo maana unakuta ombaomba wengi siku kama za Ijumaa na Jumapili wanakuwa wengi zaidi katika maeneo hayo ambayo ni ya ibada ni kwa sababu watu wengine wanatoa fedha kama misaada. Kwa hiyo, kwa kweli kama ushauri wake ulivyotolewa tunauchukua kwa ajili ya kuupangia bajeti ya kutoa elimu kwa umma ili kusudi kupunguza hili tatizo la ombaomba.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabia hii ya polisi kutumia vibaya madaraka na kubambika kesi imekithiri sana katika nchi yetu. Mimi mwenyewe ni muathirika wa kubambikiwa kesi. Mfano mzuri ni RCO (Afisa Upelelezi) wa Mkoa wa Iringa ambaye amekuwa akibambikiza kesi na kuwalazimisha hasa wanachama wa CHADEMA wahame chama cha CHADEMA waingie Chama cha Mapinduzi ili wasifunguliwe mashtaka.
Je, Serikali itakuwa tayari kufanya uchunguzi kwa RCO huyu ambaye anatumitumia madaraka yake vibaya mfano mzuri ni mimi mwenyewe nimebambikiziwa kesi nimekuwa muathirika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msigwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai hayo Mheshimiwa Msigwa amekuwa akiyatoa mara kwa mara Bungeni na binafsi nimeshamuomba mara kadhaa kama ana vithibitisho wa tukio lolote la aina hii alilete lakini mpaka leo hajaleta.
Kwa hiyo, narudia tena maelezo ambayo Mheshimiwa Msigwa nimekuwa nikikupa mara nyingi wakati mwingine nje hata ya Bunge kwamba kama una uthibitisho wa jambo kama hilo lilete tulifanyie kazi.
Kwa taarifa zilizopo mpaka sasa hivi hakuna askari polisi ambaye amemzungumza ambaye amefanya matukio kama hayo kinyume na utaratibu wa sheria.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwamba mtalaa wa shule binafsi na Serikali ni mmoja, lakini kwa zaidi ya miaka kumi shule za binafsi zimekuwa zikiongoza katika ufaulu.
Je, Serikali pamoja na kwamba inasema ina wajibu wa kusimamia kiwango cha ubora elimu nchini, haioni sasa ni wakati muafaka kujifunza kwa watu binafsi ni kwa namna gani wanafundisha watoto wao wanafaulu katika shule zao; badala ya kwamba Serikali inayosimamia ubora lakini shule zake zimekuwa zikifanya vibaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, siyo kweli kwamba shule za binafsi zinafanya vizuri zaidi ya kuliko shule za Serikali. Ninachotaka kumhakikishia ni kwamba…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia idadi ya wanafunzi wanaokwenda kwenye shule za private ni wachache kuliko wanaokwenda kwenye shule za Serikali. Kwa hiyo, kwa vyovyote unapofanya rating ya wanafunzi, lazima pia uzingatie na wingi wa wanafunzi. Kwa hiyo, asilimia kumi ya wanafunzi 20 huwezi kulinganisha na asilimia kumi ya wanafunzi 1,000 kwa maana ya kwamba idadi inakuwa tofauti. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amezungumzia faida tunazozipata kwa kutunza haya maeneo ya urithi wa dunia. Selous ni moja ya world heritage; nilitaka kumuuliza Waziri kwamba serikali imeamua kujenga bwawa la umeme katika eneo hilo na nina amini Serikali ilifanya upembuzi yakinifu na kuangalia hasara na faida. Anaweza akaliambia Bunge hili ni kwa kiasi gani tutaathirika na UNESCO baada ya sisi kuamua kujenga bwawa hilo na kwamba tunapunguza ile dhana nzima ya urithi wa dunia katika Selous.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ina mradi wa umeme katika Mbuga ya Selous na kwamba mradi mzima wa umeme katika Mbuga ya Selous unachukua 1.8 ya eneo zima ambalo ni la Selous, na kwa hali hiyo utafiti ulifanyika kwanza hauna madhara yoyote ya uwepo wa Selous na pili hakuna pingamizi lolote ambalo Serikali mpaka leo imepata kutoka UNESCO. Kinachofanyika tu ni kuwaelimisha na kuwafanya waelewe zaidi kwamba uwepo wa bwawa hilo na mradi huo utaiongezea nguvu Serikali namna ya kuifanya Selous iwe mbuga bora zaidi.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Sugu alivyosema mnasema hatupongezi lakini katika hili nimpongeze Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu atleast wamefika maeneo mengi kufanya kazi yao vizuri. Kwa hiyo, kwa mazuri yanayofanyika sisi tunapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ni mawili. La kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kwa sasa hakuna changamoto, nakubaliana kwa sehemu zimeondoka lakini malalamiko makubwa ya kampuni binafsi ni kwamba hawapati ushirikiano kwa watendaji wa Serikali kwa sababu wanaona kwamba wanachukua kazi zao. Kwa hiyo, wanapotoa taarifa kuomba vibali wale watendaji wakati mwingine wanawazunguka wanakwenda kuchukua kazi zao kwa sababu wanakuwa kama intruders kwenye kazi zao, Serikali itatatuaje tatizo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, Mheshimiwa Lukuvi mwaka juzi alizindua masterplan katika Manispaa ya Iringa na tulikuwa Manispaa ya kwanza kuzindua masterplan jambo ambalo ni jema, nimesema nalipongeza na tumeendelea kufanya kazi vizuri. Hata hivyo, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa ametangaza katika Manispaa ya Iringa watu wajenge wanavyotaka hata kuingilia maeneo ya CBD. Je, Serikali inasemaje? Tumsikilize nani kati ya Waziri au Mkuu wa Mkoa? Bado niseme nawapongeza ningeomba nipate majibu ya Serikali kuhusiana na jambo kama hili.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amezungumzia habari ya wapimaji binafsi ambao hawapati ushirikiano. Tatizo hilo hatujalipata kama Wizara na lengo la kuwaweka wao ni kuhakikisha kwamba upimaji unaongezeka. Sasa kama suala ni kuongeza kasi halafu wanapata vikwazo, tunahitaji tupate uthibitisho wa hayo ili tuweze kuyafanyia kazi lakini kwa sasa hatujapata malalamiko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la masterplan na Mheshimiwa RC kuingilia kazi hiyo, naomba kusema kwamba hilo pia nalo hatujalipata lakini masterplan ndiyo kiongozi wa kupanga miji kama ilivyo na Iringa kweli mmekuwa wa kwanza. Kwa hiyo, tunachosema masterplan ikishapitishwa inahitaji kutekelezwa kama ilivyo na siyo vinginevyo.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri, asilimia 20 ambayo inatengwa ili irudi kwa ajili ya Wenyeviti wa Mitaa, kuna Halmashauri nyingine hiyo asilimia 20 ni ndogo sana. Ni kwa nini Serikali isitoe commitment ili hawa Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Vitongoji wapate mshahara kwa sababu wao ndio wanafanya kazi kubwa sana katika shughuli zote za maendeleo huko tunakotoka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nia njema ya Serikali tungeweza kuwalipa Wenyeviti wa Mitaa mishahara. Hapa tunazungumzia hali ya uwezo wa Serikali kufanya kazi. Wenyeviti wa Mitaa ni wengi sana, pamoja na kazi kubwa wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoelekeza, pamoja na kwamba hayo mapato ni madogo, kwa kinachopatikana, kuna Wenyeviti wa Mitaa hawalipwi kabisa fedha hizi na tuna malalamiko mengi wameleta. Tumeelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wahakikishe hawa watu wanalipwa stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kuweza kuwalipa kwa sasa, tumelichukua, tutalifanyia kazi. Uwezo wa Serikali ukiruhusu, hawa viongozi wenzetu watalipwa stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili linafanana sana na Hospitali ya Frelimo Mjini Iringa. Hospitali yetu ya Frelimo inatoa huduma kubwa kwa maeneo mengi ukizingatia kwamba Iringa Mjini ndiyo kitovu na maeneo mbalimbali wanakuja kutibiwa pale. Katika mpango wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mmekuwa mkitoa pesa za vifaa kwenye hospitali mbalimbali lakini cha kushangaza mwaka jana kwenye Hospitali yetu ya Frelimo hamkutoa mkiona kwamba ni Kituo cha Afya wakati ni hospitali. Nilitaka nipate majibu ni kwa nini hamkutoa vile vifaa kama hospitali zingine kwenye Hospitali yetu ya Frelimo ambayo kwa kweli inasaidia wagonjwa wengi sana katika Manispaa yetu ya Iringa Mjini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Msigwa na Mheshimiwa Msigwa anafahamu nimefika pale Flerimo mara kadhaa na nakumbuka tulikuwa na Mbunge pacha wako Mheshimiwa mama Kabati. Hospitali ile inachukua watu wengi sana na mimi nimefika pale nimeona. Naomba niwapongeze Madaktari wa pale wanafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni commitment yetu sisi Serikali, naomba nikuhakikishie kwamba eneo lile tutaenda kuliboresha zaidi. Nilivyofika pale nimeona kuna kila sababu ya kufanya maboresha na rasilimali ni chache lakini lazima tutazigawanya. Kwa hiyo, ni mpango wa Serikali tutafanya kila liwezekanalo ili wananchi wa Iringa waweze kupata huduma vizuri katika Hospitali ya Frelimo.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali moja dogo. Kwa mujibu wa United Nation World Tourism Organization mwaka 2018 dunia nzima imekuwa na watalii bilioni 1.4 ni kwanini Tanzania imeendelea kusuasua imeshindwa ku- capitalize kuwavutia watalii hawa kuja nchini ikizingatiwa kuwa watalii kutoka Israel na kutoka Ulaya hususan Ujerumani wamekuwa ni wale wale wanaokuja kutoka enzi za utawala uliopita?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza Mchungaji Msigwa ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa hiyo ninaamini kwamba kama ana mchango wowote utakaosababisha watalii waje nchini anaweza kuutoa kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tumetoka kwenye watalii 1,100,000 mpaka 1,500,000 watalii ni tofauti kabisa na mzigo wa mahindi kwamba unaweza ukaamka asubuhi ukawa na tani 10 kesho ukaleta tani 100. Wanahitaji maandalizi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikitokea leo Tanzania ikapata watalii 3,000,000 kwanza nafikiri takwimu wanazo, Tanzania kwa ujumla wake na hoteli zake zote hatujazidi vitanda 30,000. Sasa ikatokea leo tukapata watalii 2,000,000 kwa mpigo, Tanzania nzima itajaa watalii na inawezekana hata sehemu ya kuwapeleka hakuna. Lakini tunahitaji miundombinu. Katika nchi nyingi ambazo unaona zinapata watalii wengi, hakuna seasonal za utalii. Watalii wanafanya utalii mwaka mzima. Sisi katika kipindi kifupi cha mwaka tuna high season ambacho ndicho tunachopokea watalii 1,500,000 tunachofanya sasa hivi ni kuimarisha miundombinu, tunafungua barabara zipitike mwaka mzima, tunaimarisha usafiri tuwe na shirika ambalo linaweza likasafirisha watalii ndani na tunaendelea kuyafikia masoko na kuhamasiaha uwekezaji ili tuweze ku-accommodate idadi kubwa ya watalii ambao wanakuja nchini.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Msigwa kwamba idadi ya watalii wanaokuja sasa anaweza akawa ni yule yule kutokana na experience aliyoipata Tanzania nafikiri unafahamu kauli yetu ya Tanzania unforgettable kwa hiyo mtu anaweza kutamani kurudi mara kumi lakini tunaendelea kuyafikia masoko mengine nje na hivi sasa tunaendelea kufika Urusi, China, India masoko ambayo hatukuweza kuyazoea awali. Kwa hiyo naamini kwa muda mfupi ujao tutafikia watalii ambao anawataka Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kwa muda mfupi ujao tutafikia watalii wengi ambao anawataka Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya kisiasa ya Mheshimiwa Waziri, sasa hivi watu wanaomaliza elimu ya shule ya msingi, sekondari, diploma na digrii ni takribani 900,000. Wengi wao wanaingia kutafuta soko la ajira wakati huo huo Serikali imekuwa ikitoa elimu ambayo inapishana na soko lililoko. Sasa mipango unayosema, ukilinganisha na idadi ya vijana wengi ambao hawana kazi na idadi ya vijana ambao Serikali inasema inawa-train na kuwapa hizo fursa ni chache sana ukilinganisha na uhitaji wa watu. Sasa kuna mkakati gani wa makusudi au mpango maalum wa Serikali wa kutoa elimu ambayo itakwenda kukutana na soko wanapokwenda kukutana huko mtaani ukiachilia mbali hayo waliyoyasema?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningemwomba Mheshimiwa Mbunge aende ku-revisit tena takwimu zake alizonazo kumekuwa na upotoshaji juu ya watu wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka, anasema wahitimu lakini kwa mujibu wa takwimu kutoka NBS ya Juni, 2019 inasema watu wenye uwezo wa kufanya kazi kuanzia miaka 15 na kuendelea, the working age population. Kwa hiyo, siyo hicho ambacho amekisema Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo, namshauri aende ku-revist takwimu zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kulijibu swali lake, ni kweli hauwezi ukawa una suluhisho moja kwa matatizo mbalimbali ya vijana. Tulichokifanya kama Serikali, katika vijana ambao wengi ni wahitimu wa darasa la saba, kidato cha nne ambao kwa kiasi kikubwa sana tunaamini kwamba wakipata ujuzi wanaweza kujiajiri na kuajiri vijana wengine, Serikali inatekeleza Programu Maalum ya Mafunzo ya Ufundi Stadi ambako tumeanza mwaka juzi kushirikiana na Don Bosco. Mheshimiwa Msigwa katika Jimbo lako la Iringa Mjini wako vijana ambao wamenufaika na program hii kupitia ukuzaji wa ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya ni kwamba Serikali sasa inaingia kuwafadhili vijana kupata mafunzo ya ufundi stadi kama sehemu ya kuwafanya kuweza kujiajiri. Tunafanya program hiyo Don Bosco Oyster, Don Bosco Mafinga, Don Bosco Iringa, Don Bosco Shinyanga na Don Bosco Dodoma na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vijana ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu, Serikali ilichokifanya ni kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu amezindua program maalum ya mafunzo ya internship na uanagenzi ambako hivi sasa kwenye kuondoa changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kigezo cha uzoefu, hivi sasa Serikali inawachukua vijana wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu, tunakwenda kuwa- place katika makampuni na viwanda mbalimbali wanajifunza kwa miezi sita mpaka miezi kumi na mbili. Akitoka hapo anapewa certificate of recognition ambapo akienda kuomba kazi hiyo itakuwa ni kigezo kwamba kijana huyu tayari ameshapata uzoefu na imesaidia kwa kiwango kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko program nyingi sana na nitapata nafasi kuwaelezea Wabunge vizuri zaidi ili waweze kuzielewa program za Ofisi ya Waziri.