Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Machano Othman Said (11 total)

MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba kutokana na kwamba hii Sheria ya Fedha ipo kwa muda mrefu tangu mwaka 1991, na kutokana na mabadiliko ya kidunia ya uchumi na baadhi ya nchi jirani kubadilisha sheria hizi katika nchi zao; je, haaoni kwamba umefika wakati kwa Serikali kubadilisha sheria hii?
Na la pili, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba riba katika mwezi wa Juni, 2016 ilikua kwa kiwango cha 13.46 lakini ukweli halisi ilikuwa ni kati ya 16 mpaka 18. Katika swali langu niliuliza je, haoni kwamba Serikali inahitaji ichukue juhudi maalum kwa wafanyakazi wa Serikali kwa sababu fedha zao kulipwa ni rahisi na zina dhamana zaidi, anaonaje Mheshimiwa Waziri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza anauliza utayari wa Serikali kubadilisha sheria, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu, tuko katika soko huria na tunafuata soko huria hivyo haiwezekani kurudi katika kuelekeza mabenki yetu. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Benki Kuu ikifanya hivyo itakosa mamlaka sasa ya kuyasimamia mabenki hayo pindi yatakapopata hasara kutokana na riba elekezi iliyoyatoa. Hivyo nashauri tu tuendelee na mfumo uliopo kwa sababu tupo katika mfumo wa soko huria na hii pia ni global practice hivyo siamini kwamba ni njia njema kwa nchi yetu kuweza kurejea katika maelekezo kwa ajili ya riba zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, naomba niseme kwamba kuhusu kutoa riba elekezi kwa wafanyakazi pia haiwezekani kwa sababu riba tunazoziona zinakuwa ni wastani wa riba ambazo zimetolewa kutoka katika sekta na makundi mbalimbali, hivyo tukisema wafanyakazi tuwape riba nafuu itapelekea makundi mengine ambayo hasara yake au vihatarishi ni vya juu kupata riba kubwa sana na hivyo tutakuwa tumewaumiza.
Kwa hiyo, niliombe Bunge lako Tukufu na Wabunge kwamba tukubaliane na wastani huo ambao hutolewa na Benki Kuu baada ya kupata sasa riba zote kutoka katika mabenki yetu yote.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali moja la nyongeza lenye (a) na (b).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Benki ya FBME haikufilisika na Serikali ilitambua kwa muda mrefu kwamba inatakiwa kufungwa. Na kwa kuwa wateja wake wengi walikuwa hawajapata habari ya mwanzo. Serikali haioni kwamba ilifanya uzembe ili kuwatahadharisha wateja wao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wafanyakazi wa FBME ambao mpaka leo hawajajua hatima zao. Je, Serikali inataka kutuambia nini kuhusu suala hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja tu la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitoa tahadhari kipindi kirefu sana na jinsi mchakato mzima ulivyoendeshwa ulikuwa wa huru na haki na wateja wote walikuwa wakifahamu nini kinaendelea ndani ya benki hii. Kama Serikali nimesema tunaendelea kusimamia sheria zetu zinazosimamia uendeshaji wa mabenki pamoja na taasisi zote za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia BOT tumeendelea kutoa tahadhari kwa wateja wetu pale ambapo inaonekana mwenendo wa benki yoyote au taasisi yoyote ya kifedha haifanyi vizuri. (Makofi)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali dogo moja lenye (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa MIVARF ulikuwa na nia nzuri sana kuwasaidia wananchi wa Tanzania. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, kwa upande wa Zanzibar tumepata fedha na miradi, lakini katika utekelezaji wake inaonekana miradi hii haikuzingatia sana value for money na barabara ambazo zimejengwa kupitia mradi huu sasa hivi zimeharibika na hazipitiki ndani ya mwaka mmoja. Pia Wizara ya Kilimo ambayo imesimamia bado hawajazikabidhi kwa Wizara ya Ujenzi Zanzibar. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda kuzitembelea barabara hizi na kuzifanyia ukarabati?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa upande wa soko la Kinyasini nalo pia limejengwa chini ya viwango. Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwanza ameniomba kama nina uwezo wa kwenda kuzitembelea. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi binafsi pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria tulikwishafika katika eneo hilo. Tulitembelea na tulitoa maoni ya Kamati ambayo tuliwaagiza Watendaji pale Zanzibar waweze kuyafanyia kazi na hasa katika hili eneo ambalo amelisema la miundombinu, kwa sababu katika baadhi ya zile barabara ambazo tulizitembelea tayari MIVARF kwa maana ya programu na Halmashauri ya Wilaya pale waliingia makubaliano kwamba Manispaa inazichukua kwa ajili ya kuzi-upgrade na kuendelea kuzikarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tayari tulishafika katika eneo hilo, tumeziona na kuna hayo makubaliano ambayo yanaendelea. Pia nami nikipata fursa zaidi nitakwenda kuzitembea na kuhakikisha kwamba yale ambayo tumekubaliana yamefanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la soko la Kinyasini, nilisema katika majibu yangu ya msingi ya kwamba mradi huu pia unatarajia kuchangia kiasi cha shilingi bilioni nne na milioni mia sita, ambazo ukiacha shughuli nyingine zitasaidia katika ujenzi wa ghorofa yenye vyumba vya baridi katika eneo la Kinyasini – Unguja, Tibirizi na Konde pia Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia katika mradi huu, kazi kubwa sana imefanyika Zanzibar na ukiangalia kuanzia katika sehemu ya Kaskazini Unguja, maeneo ya Donge, Vijibweni, Pwani, Donge Mnyimbi, kote huko shughuli zimefanyika kupitia mradi huu. Vilevile katika maeneo ya Mjini Magharibi kule Mwakaje, Mwera, Fuoni, Kibondeni nako pia kazi hizi zimefanyika. Kwa hiyo, nimwondoe hofu kwamba hata hayo mengine yote aliyoyasema tutakuja kuyapitia na kuona namna gani mradi huu unaendelea kutekeleza. Huu ni mradi ambao una manufaa makubwa sana Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kumekuwa na Makaimu kwa sababu bado kuna muundo mpya unatengenezwa, lakini Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar inakaimu karibu miaka miwili na ukiacha kukaimu, pia wana uhaba wa staff na samani za Ofisi katika Ofisi ya Zanzibar.
Je, ni lini Wizara hii itashughulikia Ofisi ya Zanzibar ili iwe sawa na sehemu nyingine za Muungano?
La pili, miongoni mwa Kurugenzi zisizopungua 12 za Makao Makuu ya Wizara hii zote haziongozwi na Mzanzibar hata mmoja na kwa sababu Wizara hii ni kioo cha Muungano, Mheshimiwa Waziri anatuahidi nini katika muundo mpya kwamba Kurugenzi nyingine zitapata wafanyakazi kutoka upande wa pili wa Muungano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Machano kwa namna anavyowakilisha maslahi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Siyo mara ya kwanza kumsikia akifanya kazi hii kwa weledi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niseme tu kwamba ni kweli kuna changamoto alizozitaja kwenye Ofisi ya Zanzibar nimwahidi tu kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Wakurugenzi waliopo idadi yao Wazanzibar kuwa ni wachache, nimhakikishie tu kwamba Wizara ina Idara 14; siyo 12 kama yeye alivyosema. Nimhakikishie tu kwamba katika uteuzi utakaofanyika, bado Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba kigezo kukubwa inakuwa ni weledi, lakini kuangalia kwamba pande zote za Muungano zinawakilishwa vilivyo katika Wizara. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jibu lake. Lakini pamoja na jibu hilo naomba kuuliza maswala mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii ya dawa za kulevya ina mtandao mrefu, na katika mtandao huo wapo baadhi ya raia ya wa kigeni ambao wanaishi Tanzania wanajishirikisha na dawa hizi. Miaka miwili, mitatu, minne nyuma kuna mwanamke mmoja kutoka nchi jirani alikamatwa maeneo ya Mbezi beach na alikuwa akitumia passport nyingi na majina tofauti.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na wageni ambao wanaitumia Tanzania kwa uuzaji wa madawa ya kulevya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, miongoni mwa waathirika wakubwa watumiaji wa dawa za kulevya ni wasanii wetu. Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wasanii hawa kuondokana na tatizo hili la utumiaji wa dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwanza, sheria yetu haibagui wenyeji na ugeni. Inapotokea mtu yeyote anajihusisha na dawa za kulevya sheria yetu imekuwa ikitumika kwa kuhakikisha kwamba hatua stahiki zinachukuliwa na kufanya kitu ambacho kinaitwa deterrence ili kuwazuia watu wengine wasifanye biashara hii ya dawa za kulevya. Adhabu kali kali hutolewa na hatua stahiki huchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kuhusu kuwasaidia wasanii; katika mpango tulionao wa kuhakikisha kwamba tunatatua changamo hii ya dawa za kulevya ambayo inawaathiri vijana wengi ikiwemo nguvu kazi ya taifa hili, moja kati ya kazi kubwa tunayofanya ni kuendelea kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Vilevile katika mpango mmoja wapo ni kuhakikisha kwamba tunafanya kitu kinaitwa supply reduction kuhakikisha kwamba madawa hawa hayapatikani na hivyo kutokuwalazimu vijana wengi zaidi kuweza kuyatumia. Tume imefanya kazi kubwa mpaka hivi sasa na wameendelea kukamata na kuteketeza dawa nyingi na hivi sasa kuna upungufu mkubwa sana wa dawa za kulevya katika viunga vya miji yetu mingi ya Tanzania kutokana na kazi kubwa ambayo inafanywa na tume.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri majibu yake mazuri na ya ukweli, pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri aliahidi kulimaliza tatizo la Kambi ya Kisakasaka ambayo iko katika Wilaya ya Magharibi B. Je, ni hatua gani zimefikiwa hadi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kambi ya Mtoni ambayo iko katika Wilaya ya Magharibi A ni ya muda mrefu na watu waliikuta kambi kabla ya kuhamia wao na kuna viashiria vya kuvamiwa na wananchi; Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini kuhusu suala hili na kama kuna upimaji au tayari imeshapimwa kambi ile ya Mtoni ili kuepuka uvamizi wa wananchi katika eneo lile?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Kisakasaka ambalo tuliahidi kwamba tutamaliza tukiweza kupata bajeti, nieleze tu kwamba mpaka sasa fedha za ulipaji wa fidia na upimaji bado hazijapatikana, ni mategemeo yetu kwamba tunaweza tukapata kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha ili tuweze kulimaliza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kambi ya Mtoni ni dhahiri kwamba kambi karibu zote zimepimwa lakini kuna kuhuisha mipaka, kwa hivyo tutakachofanya kama nilivyoeleza awali ni kwamba tunatengeneza utaratibu maalum sasa wa kupitia maeneo yote ili tuweze kuhakikisha kwamba mipaka yetu inahuishwa na kuwataka wananchi wale ambao hawana stahili, basi waweze kutoka katika maeneo hayo, lakini wale ambao wataonekana na stahili aidha turekebishe mipaka au wapatiwe fidia zao ili tuondokane na migogoro ambayo imeonekana kwamba haiishi kati ya Wananchi na Wanajeshi. (Makofi)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uzinduzi wa Ukuta wa Mererani ambao Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuzindua, Mheshimiwa Rais aliridhika sana na kazi ambayo imefanywa na Jeshi na kuahidi kwamba vijana 2,500 wa JKT ambao walishiriki katika ujenzi huo waajiriwe na vyombo vya ulinzi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Je, ni hatua gani ambazo zimefikiwa kuhusu ajira za vijana wale hadi hivi sasa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Machano Othman Said, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuwaajiri vijana walioshughulika katika ujenzi wa Ukuta pale Mererani. Zoezi hilo kwa kweli limeshaanza, polisi wamepokea vibali vya ajira, usaili umeanza na ni mategemeo yetu kwamba vyombo vingine vya ulinzi na usalama watakapokuwa wamepata vibali wataendelea kuwachukua vijana hawa.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini pamoja na majibu hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa Wizara mbili zinahusika sana na makusanyo ya Viza katika nchi za nje kupitia Balozi zetu. Je, Wizara ya Mambo ya Ndani inakuwa inafanya nini katika kuhakikisha fedha hizo na zinawekwa katika vitabu vya Wizara gani?

Pili, katika mwaka wa fedha 2018/2019 wa bajeti, Viza kwa upande wa Zanzibar zimekusanywa kiasi gani kwa sababu tuna watalii zaidi ya 500,000 kwa mwaka. Je, ni kiasi gani cha fedha ambacho kimekusanywa kwa kupitia Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu hoja ya kwamba kuna Wizara mbili zinashughulikia nataka nimthibitishie tu kwamba baada ya Mheshimiwa Rais kuzindua utaratibu wa kuwa na mfumo wa e-visa ambayo inahusisha, tunapuzungumzia immigration inahusisha e-visa e-passport n.k. na sasa hivi nitoe taarifa hii hapo Bungeni kwamba mfumo huu umeshafungwa katika Balozi zetu nchi za nje. Kwa hiyo, sasa ile changamoto ambayo ilikuwepo mwanzo, haipo. Sasa hivi fedha yote tena inaingia katika mfumo na hivyo basi hiyo hoja ambayo Mheshimiwa ameuliza imeshapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na takwimu naomba nimhakikishie Mheshimiwa Machano kwamba nitampatia hizo takwimu baadaye.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa matatizo makubwa ya Askari Polisi wakati wa uchaguzi ni uchache wao, je, Wizara iko tayari kushirikiana na vikosi vya SMZ kuongeza idadi ya Askari wakati wa uchaguzi huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa imedhihirika kwamba kufanya uchaguzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar kwa siku moja unaleta matatizo zaidi. Je, Serikali iko tayari kutenganisha chaguzi hizi na kufanywa siku mbili tofauti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Machano Othman Said, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza kama tuko tayari na ndivyo ambavyo inatokea kwamba vyombo hivi vinafanya kazi kwa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mabadiliko ya uchaguzi, nadhani hili suala linazungumzika na ni hoja ya msingi. Kwa hiyo, tunaichukua tuone kipi kinaweza kufanyika kwa kutilia maanani maoni yake.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake lakini pamoja na majibu hayo nataka kumuuliza swali lifuatalo, kwa kuwa mwaka wa fedha 2018/ 2019 umebakisha kama mwezi mmoja kumalizika, na kwa kuwa ajira hizi bado hazijafanyika, na kwa kuwa upungufu huu wa wafanyakazi unasababisha wafanyakazi zaidi ya wale wa malindo kuingia kazini usiku na asubuhi kurejea tena kazini, Je, Mheshimiwa Waziri anatuhakikishia vipi kwamba ajira hizi 505 zitafanyika kwa wakati.

(b) lakini, Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi inafanya shughuli zake, wananchi wengi wa Zanzibar badala ya kwenda kwenye Mkoa wanakwenda Makao Makuu, Ofisi Kuu kwa sababu kule Mkoa hakuna nyenzo za kufanyia shughuli zao hasa passport. Ni hatua gani Serikali itachukua ili kupunguza mzigo Ofisi Kuu na wananchi kwenda katika Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ajira, kama ambavyo nimezungumza kwamba tunatarajia kuajiri na hivyo, basi pale ambapo kibali kitakuwa kimepatikana kutoka Utumishi vijana hao wataajiriwa, lakini swali lake la pili kuhusiana na kuboresha mazingira ya Ofisi ya Mjini Magharibi, ili kupunguza msongamano Makao Makuu nataka nimuhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha tumetenga takribani shilingi milioni mia tatu kwa ajili ya kukamilisha matengenezo ili tuweze sasa kutumia vizuri zaidi, mara kazi hizo zitakapokamilika kwa mwaka huu, basi ni dhahiri kwamba sasa mazingira ya kazi katika Ofisi ya Mjini Magharibi yataboreka na msongamano utapungua.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Pamoja na majibu yake, naomba kuuliza swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wengi wa Zanzibar shughuli zao ni uvuvi; na kwa kuwa biashara ya dagaa ni kubwa sana kwa Zanzibar na soko lake kubwa ni Congo (DRC) na Rwanda. Ni sababu gani inasababisha kila tani moja ya dagaa kutozwa dola 400 katika mpaka wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Machano, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nimemsikia vyema amezungumzia na kutaka kujua juu ya mgogoro wa usafirishaji wa mazao ya uvuvi (dagaa) kutoka Tanzania aidha Visiwani na Bara kwenda nje ya nchi na inaonekana tozo ni kubwa na wafanyabiashara kuishindwa kulipa tozo hiyo.

Mheshimiwa Spika, hapa karibuni Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi tulifanya mabadiliko ya tozo mbalimbali za mazao yetu ya mifugo na uvuvi. Tozo zile tulizoziweka zimepelekea wafanyabiashara hasa wa Ukanda wa Pwani kuwa juu ya uwezo wao. Baada ya malalamiko makubwa, Wizara imeyapokea malalamiko yao, imeyafanyia kazi na tumefanya marekebisho ya tozo zile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya bajeti ya Wizara ya Fedha na tozo mpya kupitishwa na Serikali na kutangazwa katika Gazeti la Serikali, kuanzia tarehe 1 Julai, tunayo matumaini kwamba tozo zile zitashuka sana na wafanyabiashara wataendelea kutoa mazao yale ya mifugo kupeleka katika nchi zingine zinazohitaji. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge na wafanyabiashara wote wawe na subra muda si mrefu majibu ya jambo hili yatakuwa yamepatikana.