Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Machano Othman Said (7 total)

MHE. SALUM MWINYI REHANI (K.n.y. MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:-
Serikali yetu kwa muda imekuwa na uhusiano wa karibu na watu wa China, Serikali ya Watu wa China ina Ubalozi Dar es salaam na Ubalozi Mdogo huko Zanzibar:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa sasa umefika wakati wa kufungua Ubalozi Mdogo wa Tanzania katika Mji wa Guangzhou ili kutoa huduma nzuri kwa Watanzania wengi katika mji huo?
(b) Je, ni utaratibu gani unatumika katika kuwapatia visa Watanzania ambao wameamua kuishi China zaidi ya mwaka mmoja.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mpango wa kufungua Ubalozi Mdogo katika Mji wa Guangzhou uliopo katika Jimbo la Guangdong, China. Hatua hii imefikiwa baada ya Serikali ya China kuchagua majimbo matatu yatakayokuwa na uhusiano maalum na nchi tatu za Afrika ikiwemo Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Majimbo haya ni pamoja na Jiangsu, Zhejiang na Guangdong ambayo yamepewa maelekezo mahususi na Serikali ya China kuhamasisha makampuni kutoka kwenye Majimbo yao kuhamisha viwanda vyao katika nchi hizo na kupeleka katika nchi za Afrika, Tanzania ikiwa mojawapo. Tunaamini kwa kuanzia katika mji huo, si tu tutakuwa na fursa ya kuyashawishi makampuni ya mji huo kuja kuwekeza nchini, bali tutaweza kutoa huduma mbalimbali kwa Watanzania wanaofanya biashara katika Mji wa Guangzhou.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo unawataka Watanzania na wageni kutoka Mataifa mengine walioamua kuishi nchini China zaidi ya mwaka mmoja kuwa na kibali cha kuishi. Kibali hiki kinapatikana kwa kuwasilisha maombi kwenye Wizara inayoshughulikia na masuala ya mambo ya ndani ya China na iwapo watakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za China watapatiwa kibali cha namna hiyo.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya wananchi, watumishi wa umma na wafanyabiashara juu ya riba kubwa inayotozwa na benki zetu kwa wale wanaochukua mikopo hali ambayo inarudisha nyuma juhudi zao za kupunguza umaskini na kwa kuwa Benki Kuu ndiyo inayosimamia mabenki yote nchini.
(a) Je, ni lini Serikali kwa kupitia benki zetu nchini itaweka utaratibu wa kupunguza riba ya mikopo walau kufikia 10% -12% badala ya riba ya sasa ambayo ni 17% - 20%?
(b) Kwa kuwa mikopo inayotolewa kwa watumishi wa umma ni salama zaidi kwa mabenki, je, benki hizo haziwezi kuweka riba maalum?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki. Viwango vya riba za mikopo na riba za amana, pamoja na riba za mikopo kati ya benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, riba za dhamana za Serikali, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo, pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. Hivyo basi, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Serikali haina mamlaka kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na mabenki katika kupanga viwango vya riba za mikopo. Aidha, kwa sehemu kubwa gharama za riba za mikopo hutegemea zaidi gharama za upatikanaji wa fedha pamoja na gharama za uendeshaji.
Pili, ni muhimu kutambua kwamba kadri riba za mikopo zinapokuwa juu, ndivyo riba za amana zinapokuwa juu pia. Mfano; wastani wa riba za kukopa kwa mwaka mmoja mwezi Juni, 2016 ulikuwa ni asilimia 13.67 wakati wastani wa riba za amana za mwaka mmoja ulikuwa ni asilimia 11.52 ikiwa ni tofauti ya asilimia 2.25
MHE. SAADA MKUYA SALUM (K.n.y MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:-
Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri kiuchumi, kiafya na kisiasa na Jamhuriya Muungano wa Watu wa Cuba, lakini Tanzania haina Ubalozi katika nchi hiyo:-
(a) Je, ni lini Tanzania itafungua ubalozi wake nchini Cuba hasa ikizingatiwa kuwa Cuba tayari wana Ubalozi nchini muda mrefu?
(b) Je, Serikali inajua kwamba kutokana na Tanzania kutofunga Ubalozi nchini Cuba, imesababisha sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyeree kutowekwa katika uwanja wa Viongozi muhimu wa Afrika katika Jiji la Havana?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Tanzania na Cuba imekuwa na mahusiano mazuri ya Kidiplomasia, Kisiasa, Kiuchumi, Kielimu, Kiafya na Kiutamaduni kwa muda mrefu yalioanzishwa na waasisi wa Mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Fidel Alejandro Castro Ruz wa Cuba. Kwa ujumla mahusiano haya mazuri yamedumu kwa miaka mingi kutokana na kuwa na maslahi mapana na nchi yanayozingatia usawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya mafupi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua mahusiano mazuri na ya muda mrefu yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ina mpango wa kufungua ubalozi katika Mji wa Havana Cuba. Hivi sasa taratibu za kufungua Balozi hizi zinaendelea, mara zitakapokuwa zimekamilika ubalozi huo utafunguliwa kama ulivyopangwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa katika vita vya ukombozi wa bara la Afrika iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu kuenzi juhudi na harakati hizo pamoja uzalendo wa viongozi hao akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba Tanzania kutokufungua Ubalozi nchini Cuba kumesababisha sanamu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutokuwekwa katika Uwanja wa Viongozi Muhimu Afrika katika Jiji la Havana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sanamu hiyo haikuwekwa katika uwanja huo kutokana na muonekano wake kutokuwa na uhalisia wa sura ya Hayati Baba wa Taifa, hivyo utengenezaji wake kuanza upya. Matengenezo ya sanamu hiyo yanaendelea na Serikali inafanya juhudi ili sanamu hiyo ikamilike na kuwekwa sehemu iliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa mahusiano ya Tanzania na Cuba yataendelea kuwa mazuri katika nyanja mbalimbali hapa nchini kama vile diplomasia, afya, elimu, michezo, utalii na biashara.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa Kurugenzi nyingi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zimekuwa zikiongozwa na Makaimu, hali ambayo inapunguza ufanisi wa kazi.
Je, ni sababu gani za msingi zinazoifanya Serikali kushindwa kuwathibitisha makaimu hao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Kurugenzi mbili ambazo Wakurugenzi wake wanakaimu kwa muda mrefu. Kurugenzi hizo ni Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii na Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji.
Aidha, hivi karibuni Kurugenzi nyingine zinakaimiwa na Maafisa Waandamizi au Mabalozi kutokana na baadhi ya Wakurugenzi kustaafu, kuhamishwa na kuteuliwa kuwa Mabalozi kwenda kuwakilisha nchi katika Balozi zetu za Beijing, Paris, Oman, New Delhi. Khartoum na Brussels.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya msingi iliyoifanya Serikali kutothibitisha Makaimu Wakurugenzi ni pamoja na Wizara kuwa katika mchakato wa kupitia muundo wake ili kujua idadi halisi ya Kurugenzi zinazohitajika, hivyo kuleta, ufanisi katika kazi. Mchakato wa kupitia muundo huo umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa taratibu za uteuzi wa Kurugenzi kwa ajili ya kuthibitishwa na kujaza nafasi hizo zinakamilishwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y. MHE. MACHANO OTHMAN SAID) aliuliza:-
Katika utekelezaji wa bajeti ya 2017/2018 Serikali imekuwa ikitegemea msaada wa wafadhili (Basket Fund) ili kutunisha Mfuko wa Hazina katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kutoka Basket Fund
kimepatikana katika mwaka 2017/2018?
(b) Je, kati ya fedha hizo ni kiasi gani kimepelekwa Zanzibar kusaidia bajeti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Machi, 2018 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 182.92 sawa na asilimia 32.89 ya makadirio ya shilingi bilioni 556.08 kimepokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 pamoja na marekebisho yake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapokea misaada ya mikopo ya kisekta moja kwa moja kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Hivyo, basi kiasi cha shilingi bilioni 182.92 kilichopokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni kwa ajili ya Tanzania Bara tu.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-

(a) Je, ni Wizara ipi inayo wajibika kukusanya fedha za Viza na kusimamia utoaji wa Viza hizo?

(b) Je, kuna mgao wowote kwenda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia uwanja wake wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi lenye sehemu (a) na (b) yote kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji ndiyo inayowajibika kukusanya fedha za Viza na kusimamia utoaji wa Viza. Aidha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi za Tanzania ndiyo inayo kusanya fedha za Viza na kusimamia utoaji wa Viza katika Balozi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusanyo yote ambayo yanayokusanywa na Idara ya Uhamiaji Zanzibar kupitia vyanzo vya mapato ikiwemo mapato yatokanayo na Viza kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume huwasilishwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID aliuliza:-

Kwa muda mrefu kumekuwa na upungufu mkubwa wa Wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar hali inayopunguza ufanisi wa kazi katika Idara hiyo?

(a) Je, ni lini Serikali itaajiri Wafanyakazi wa kutosha katika Idara hiyo?

(b) Je, ni lini Serikali itaimarisha Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi ili kupunguza msongamano katika Ofisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Machano Othman Said Mbunge wa Baraza la Wawakilishi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Uhamiaji imetengewa Bajeti ya kuajiri Watumishi 505 katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mwaka wa fedha 2017/2018 Idara ya Uhamiaji limefanya upanuzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kuongeza vyumba vitatu kwa ajili ya kuimarisha huduma za Kiuhamiaji ikiwemo huduma ya pasipoti mtandao, pia katika Bajeti ya mwaka huo Idara ya Uhamiaji imetenga fedha kwa ajili ya upanuzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hiyo Idara itakuwa imeongeza wafanyakazi, pia Ofisi ya Uhamiaji Mjini Magharibi itaimarika ili kupunguza msongamano uliopo katika Ofisi kuu ya Uhamiaji Zanzibar.