Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Machano Othman Said (5 total)

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Shirika la Kazi Duniani na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho vya Mabaharia Na. 185 wa Mwaka 2003 wa Shirika la Kazi Duniani.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba niishukuru Serikali kwa kuleta Azimio hili la kuridhia Mkataba wa kazi wa Mabaharia, Mheshimiwa muda ni mchache sana, kwa hivyo nitazungumza kwa haya mambo mafupi tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, imekuwa ni kawaida kwa Tanzania kutohudhuria vikao vingi vya IMO na pia Shirika la Kazi Duniani kuhusu Mabaharia. Bahati nzuri nchi yetu ina bahari kubwa na ina fursa nyingi sana katika eneo hili, kwa hiyo naomba Serikali isidharau. Mimi mwenyewe nilishawahi kuhudhuria vikao kama vinne vya IMO lakini upande wa Bara hawakushiriki.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tukiridhia Azimio hili la mkataba huu tutanufaika sana, kwa sababu tuchukulie mfano Zanzibar kwa kupitia mamlaka ya usafiri baharini wamesajili meli karibu 400 duniani na kila meli sasa hivi wanatozwa dola 500 kwa sababu bado Tanzania hatujaridhia mkataba huu na kiasi kama dola 200,000 kila mwaka zinalipwa na ZMA kwa ajili ya suala hili. (Makofi)Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo nafurahi kwamba Serikali inaridhia itatuwezesha Tanzania kwa ujumla kuongeza idadi ya Mabaharia lakini pia kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la ubaharia ni eneo pana sana na linaweza kutusaidia. Bahati nzuri Tanzania tuna vyuo viwili vinavyotambulika duniani, tuna Chuo cha DANAUSE kiko Zanzibar na tuna chuo cha DMI Dar es Salaam. Vyuo hivi wanatoa certificate na zinatambulika na vinatoa ajira kwa vijana wetu. Kwa hivyo niiombe Serikali kwamba ni wakati muafaka sasa tuseme kwamba tumechelewa kidogo, lakini maadam leo limeletwa hakuna tatizo, nafikiri Waheshimiwa Wabunge wote tutaridhia na sisi ili kuwezesha nchi yetu isonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba nimalizie hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuchangia mchana huu wa leo. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Mheshimiwa Masele na Mheshimiwa Mboni kwa nafasi ambazo wamezipata katika Bunge la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka nizungumzie baadhi ya majukumu ya Wizara hii na umuhimu wake. Wakati wa bajeti ya Wizara ya Maji Mheshimiwa Waziri wa Maji alizungumzia pia kuhusu mradi wa maji ambao tunatarajia kutoka India. Sasa mradi huu karibu ni mwaka wa tatu naomba Wizara hii nayo itusaidie kutupa maelezo ya ziada kuhusu hatima ya mradi huu wa maji ambao pia na Zanzibar ipo katika mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni kuhusu Wizara ya Mambo ya Nje katika ofisi za Zanzibar. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na Kamati naipongeza sana wamezungumzia umuhimu wa kufanywa matengenezo ya jengo la Zanzibar au kujenga jengo jipya. Kwanza nikiri kwamba lile eneo ni nzuri na liko katika sehemu nzuri na niiombe Wizara ijenge au ifanye matengenezo makubwa kwa jengo lile lakini pia na vitendea kazi kwa ofisi ya Zanzibar. Pamoja na watenda kazi wenyewe bado ni tatizo kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, natarajia Mheshimiwa Waziri hili nalo atalitilia mkazo na kutuletea majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze uamuzi wa Wizara wa Serikali wa kufungua ofisi ndogo au Council katika Mji wa Guangzhuo na Lubumbashi. Vile vile pia niipongeze sana Serikali kwa kuamua kufungua ubalozi mjini Havana, Cuba kwa masilahi ya Tanzania. Cuba ndio nchi ya kwanza kutambua Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 64, kwa hivyo kwa Cuba, Tanzania ni rafiki wao wa kudumu kwa hivyo nimefurahi nawashukuru na kuwapongeza Wizara kwamba mwaka huu pengine tunaweza tukafungua Ubalozi nchini Cuba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine suala la Mahujaji, Mheshimiwa Masoud alizungumza lakini mimi kidogo na tofautiana naye. Ni kweli tunazo fursa na uhuru wa makundi kupeleka mahujaji Makka, lakini mwaka jana kupitia makundi haya haya mahujaji wa Tanzania walipata tabu sana nchini Saudi Arabia. Wengine walitapeliwa na imefikia hatua Serikali ya Saudia kuagiza mahujaji wa Tanzania mwaka huu walipiwe mwanzo kabla ya wakati wa Hija ili kuepusha tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo ambalo limewasababisha baadhi ya mahujaji kuwa katika wakati mgumu kwa sababu kwa utaratibu Mahujaji wanachanga fedha kidogo kidogo ili wawahi nao kutekeleza ibada. Sasa kwa uamuzi huu imekuwa kazi kubwa sana na ngumu. Nimwombe Waziri pia kwa sababu masuala haya ya dini pamoja na kwamba ni Tanzania lakini yanashughulikiwa sehemu mbalimbali, kulikuwa na wazo kwa mahujaji wa Zanzibar kufunguliwa akaunti yao peke yao na mahujaji kutoka Bara wawe na akaunti yao. Sasa sijui Serikali ya Jamhuri ya Muungano imefikia wapi katika suala hili la kuweka sawa ili kupunguza hili suala la utapeli kwa mahujaji wetu na kuweza kupata huduma nzuri katika mji wa Maka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu Ubalozi wetu Msumbiji. Msumbiji ukiacha lile jengo kubwa ambalo tumejenga la ghorofa tisa liko kwenye sehemu nzuri lakini pia tunayo majengo mengine yasiyopungua mawili mpaka matatu. Maeneo ambayo tumepewa Msumbiji ni mazuri na wenyewe Msumbiji wanaona wametuheshimu sana kutupa maeneo yale, lakini kwa bahati mbaya tumeshindwa kuyaendeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara kama ingewezekana wangebadilisha matumizi ya lile jengo jipya badala ya kulitumia kwa Ofisi ya Ubalozi, tungelitumia kwa kituo cha biashara na yale majengo mengine tukayajenga na tukatumia kwa shughuli za kibalozi ambayo yanatosha sana. Yaani pale fedha nyingi tumetumia lakini tuna maeneo mazuri tunaweza tukawa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata wao Msumbiji Tanzania yapo maeneo bado wanadai kwamba walipewa na wamenyang’anywa katika utaratibu ambao hauko wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia hotuba hii lakini wiki moja ijayo tutakuwa tunaadhimisha miaka 54 ya Muungano wetu. Kwa hiyo, jambo hili ni jema sana kwa leo kulizungumza katika Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumzia mambo matatu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nchi kwa kitabu chake hiki kizuri, nikienda katika ukurasa wa sita amezungumzia jinsi ambavyo wamefanya vikao vya kuzungumzia kero za Muungano. Kwa bahati nzuri vikao hivi vimeanza muda mrefu sana na kwa bahati mbaya hapo hapo matokeo ya vikao hivi utekelezaji wake unakuwa mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pande mbili za Muungano yaani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walifikia makubaliano kuhusu ajira za taasisi za Muungano kwamba katika taasisi za Muungano asilimia 21 za ajira zote zitengwe kwa ajili ya Zanzibar kwa watu ambao wana elimu na weledi wa kazi ambazo zitatangazwa kwa upande wa Bara. Ukiacha taasisi za ulinzi kama Jeshi la wananchi wa Tanzania, Polisi na Uhamiaji, taasisi zote zilizobakia hazijatekeleza suala hili.

Naomba Mheshimiwa Waziri akija kufanya majumuisho atuambie ni sababu gani za msingi zaidi ya miaka mitano sasa suala hili halijatekelezwa. Suala hili linaleta kero, manung’uniko kwa watu ambao wana sifa, baadhi ya Wizara wanaziona za Muungano lakini Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi mpaka watumishi wote hamna. Siyo jambo jema na linaleta ukakasi sana katika shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika makubaliano ambayo yamefanywa pia pande mbili zilikubaliana kwamba Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ifanyiwe marekebisho katika Bunge hili ili iweze kuridhiwa na Zanzibar kwa kupitia Baraza la Wawakilishi. Hadi leo sheria hii haijafanyiwa marekebisho na bado suala la uvuvi wa bahari kuu linaleta tabu na haliwezi kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili ambalo Mheshimiwa Pondeza alilizungumzia la vyombo vya usafiri au vyombo vya moto. Ni kweli kwamba vyombo kutoka Zanzibar vikija Bara vinatozwa fedha na havipati permit vizuri. Hata hivyo, nalo hili wamekubaliana Serikali mbili kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wafanye marekebisho kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kifungu kimoja tu cha sheria ili sheria hii iwe vizuri, lakini mpaka leo bado haijafanyiwa marekebisho. Hili nalo nataka ufafanuzi wa Mheshimiwa Waziri wakati akija kuhitimisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika kitabu hiki imeelezewa kwamba pamoja na kuimarisha Muungano ofisi hii imejenga makazi na Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, lakini hadi leo wajenzi wa Ofisi zile hawajamaliziwa malipo yao karibu mwaka wa nne au wa tano sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuomba Mheshimiwa Waziri nalo hili alione kwamba ni kero pia kwa wale ambao wamejenga ofisi hizi. Ni vizuri kwa Makamu wa Rais kuwa na Ofisi nzuri Zanzibar lakini pia kuwa na staff wazuri Zanzibar ili kuweza kushughulikia masuala haya ambayo ni sehemu ya Muungano wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala ya Muungano ambayo yamekubaliwa nje ya Muungano ni kutoa fursa kwa upande wa Zanzibar kupata soko kwa Tanzania Bara. Jambo hili utekelezaji wake umekuwa mgumu sana hata bidhaa ndogo ndogo ambazo zinazalishwa Zanzibar kuingia Bara ni jambo gumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linaambatana na sheria ya kwamba ukianzisha kiwanda Zanzibar lazima upate leseni kutoka Bara yaani BRELA. Kwa hiyo, tunafikiria kwamba ni vyema kwa upande wa Jamhuri wangefikiria kuanzisha wakala ama Ofisi ya BRELA Zanzibar ili Wazanzibar waweze kuanzisha viwanda kukidhi mahitaji ya Zanzibar na kukidhi soko la Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni ahadi za viongozi. Viongozi wetu wa Kitaifa wanatembelea Zanzibar na Bara na kote huko wanatoa ahadi, lakini utekelezaji wa ahadi kwa upande wa Zanzibar unakuwa mgumu na wa muda mrefu. Zipo ahadi tangu Awamu ya Nne ambazo
zimetolewa Zanzibar ikiwemo ahadi ya barabara ya Fuoni mpaka leo bado haijajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili kwamba ni changamoto katika Muungano wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nisilalamike tu pia niwapongeze sana kwa kupitia mradi wa TASAF. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imefanya vizuri sana katika mradi huu na kwa upande wa Zanzibar mradi huu unafanya vizuri. Tunaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na tunasema kwamba ni vyema miradi kama hii iwe inapelekwa Zanzibar kwa kiwango kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa kwa upande wangu mimi ni kuhusu fursa za kibiashara kama nilivyozungumza mwanzo, lakini pia Zanzibar ni sehemu ya kisiwa kwa hivyo shughuli nyingi za kibiashara zinakuwa katika huduma. Huduma za kibiashara ndiyo ambazo zinaingiza fedha nyingi Zanzibar kama mitandao ya kijamii, simu na kadhalika.

Kwa hiyo, fursa hizi zifunguke zaidi ili Zanzibar waweze kufaidika. Wenzangu asubuhi walizungumzia utalii na majengo ya kisasa ya airport na bandari haya ni msingi mkubwa katika uchumi wa Zanzibar. Tunaomba sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano iwaunge mkono Serikali ya Zanzibar katika utekelezaji wa miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii na sina mengi zaidi ya hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Pili nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima na kuweza kufika leo katika Bunge letu Tukufu. Pia napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa uchapakazi wao, wamefanya kazi nzuri katika kulitumikia Taifa kwa kipindi chote tangu Mheshimiwa Waziri ameteuliwa.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maeneo matatu ambayo ni Polisi, Uhamiaji na NIDA. Kwanza nianze na Jeshi la Polisi na kwa upande huu pia niwapongeze sana polisi na zaidi kwa upande wa Zanzibar Kamishna wa Polisi kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. Kwa miaka karibu mitatu sasa hali ya utulivu katika Mji wa Zanzibar na maeneo mengine ni nzuri. Maeneo ya ujambazi yamepungua sana na vitendo vya uhalifu pia vimepungua, tatizo ambalo bado lipo kwa polisi na kwa upande wa Zanzibar ni mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, tunamuomba Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Maafisa wao waendelee kupambana na suala hili ambalo ni janga la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwa upande wa polisi yapo matatizo ambayo tunaomba wayatatuwe na moja ya tatizo kubwa la polisi ni makazi miundombinu ya makazi kwa polisi kwa upande wa Zanzibar bado ni madogo sana. Katika maeneo mengi ya vituo vya polisi, askari polisi hawana makazi, wanakaa katika hali ngumu, lakini hata vituo vyenyewe vya polisi vimechakaa sana. Mfano, kwa Mkoa wa Mjini Magharibi ambao wananchi wa Zanzibar karibu nusu wanaishi Mjini Magharibi, hali ya vituo ni vichache na vichakavu sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulifurahi sana Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Zanzibar na kuzungumza na Maafisa wa Polisi na tunaomba Mheshimiwa Waziri afanye tena ziara kutembelea baadhi ya maeneo ya vituo vya polisi ili ajionee hali halisi ya uwepo wa vituo hivyo katika hali mbaya. Tunashukuru kwamba wameanza kujenga nyumba za askari katika Kituo cha Polisi cha Fuoni, lakini waangalie na maeneo mengine zaidi ya Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo hali ya uchakavu ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwa polisi Zanzibar ni ukosefu wa vitendea kazi kama magari na uniform ambazo zinawakabili kwa muda mrefu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, jambo hili nalo alifikirie sana na aweze kulipatia ufumbuzi zaidi magari katika maeneo ya vituo vya polisi.

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, naomba nizungumzie Uhamiaji; namshukuru na kumpongeza Kamishna uhamiaji Zanzibar Ndugu Sururu kwa kufanya kazi vizuri sana, lakini naomba hapa nimshukuru Waziri wa Utawala Bora kwa tamko lake ambalo amelitoa hivi punde kuhusu kupandishwa vyeo kwa madaraja. Maafisa wengi wa Uhamiaji Zanzibar walikuwa wanalalamika kwamba wameshakwenda kozi kwa muda mrefu, lakini bado kwa miaka mitano hawajapandishwa vyeo. Nafikiri hili tangazo la Mheshimiwa Waziri leo litawapa nafuu na mategemeo kwamba hali hii itamalizika na wataweza kupandishwa vyeo kama ilivyo kawaida.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupandishwa vyeo na kuisifu Uhamiaji, ukizungumzia kwa ujumla Uhamiaji Tanzania tatizo ambalo naliona ni biashara ya binadamu. Biashara ya binadamu kila siku tunaisikia na tunaomba Serikali ijitahidi sana kukabiliana na changamoto ya biashara ya binadamu. Pia kuna uhaba wa wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji ambao hawajaajiriwa kwa kipindi cha miaka mitatu, minne hivi. Sasa baadhi ya Taasisi za kiaskari kama Polisi, Jeshi na wengine wamepata fursa za ajira, lakini wa Uhamiaji bado hawajapata nafasi za ajira, kwa hiyo, naomba nalo hili liangaliwe sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuendelea naomba nizungumzie NIDA; Taasisi hii ina umuhimu mkubwa katika maisha ya wananchi wa Tanzania, kwa sababu ndiyo inashughulika na kutoa vitambulisho vya Mtanzania, vitambulisho vya Taifa lakini naomba sana Mheshimiwa Waziri na watendaji wako, hii NIDA naiomba sana ishirikiane na Wakala wa Usajili wa Zanzibar ambao nao wanatoa vitambulisho vya Mzanzibari, vitambulisho hivi vina umuhimu sana kwa watu wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla. Jambo ambalo lipo hivi sasa ni kwamba kama vile vitambulisho vya Mzanzibari havitambuliki, tukienda kwenye passport havitambuliki, katika usajili wa simu havitambuliki, kwa hiyo tunaomba NIDA wafanye mashirikiano ya karibu na Mamlaka ya Usajili wa Mzanzibari.

Mheshimiwa Spika, nataka kuzungumzia NIDA ni deni la JKU, Zanzibar Mamlaka hii ya NIDA inadaiwa karibu milioni 489 na JKU Zanzibar kutokana na ulinzi wa ofisi zao mbalimbali. Kule Pemba sehemu ya Micheweni wanadaiwa milioni 82, lakini ukija Ofisi Kuu ya Idara wanadaiwa milioni 222, Mwanakwerekwe wanadaiwa milioni karibu 110 na Gamba hivyo hivyo. Madeni haya yamemalizika tangu Julai, 2018, kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Waziri akija hapa aje atueleze kuna mpango gani wa kulipa madeni haya ya JKU kwa upande wa NIDA.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na uzima, na pia niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa kuwasilisha maazimio haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia hili Azimio la WTO. Kwanza naunga mkono uamuzi wa Serikali wa kulileta hapa Bungeni, lakini pia naomba Waheshimiwa Wabunge tulipitishe azimio hili kama maazimio mengine ambayo tumeyapitisha Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azimio hili lina umuhimu mkubwa kwa Tanzania katika uendelezaji wa biashara, lakini pia kuzalisha bidhaa bora. Ni vyema kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya mashauri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili, pamoja na kwamba Bunge linaridhia azimio hili, lakini pia kwa upande wa Zanzibar nao waelewe na wafahamu faida ambazo zitapatikana kwa kuridhia azimio hili kwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipowasilisha alieleza faida za azimio hili kwa kuzitaja baadhi ya ibara ambazo zitaleta na kuimarisha mshikamano na mtengamano wa kibiashara kwa Tanzania. Kwa mfano Ibara ya 10 inatoa fursa kwa kuweka forodha ya pamoja na mambo mengine ambayo yatasaidia katika uendelezaji wa biashara, lakini pia kulinda na kuimarisha wataalam wetu katika shughuli za uzalishaji na kuweka viwango bora vya uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kwamba tulichelewa kidogo kwa sababu kati ya nchi nyingi tu sisi tulikuwa miongoni mwa nchi 18 ambazo zilichelewa kuridhia azimio hili, lakini leo ni furaha kwamba tumekubaliana na tumeridhia azimio hili. Hivyo kama ulivyozungumza, hatutakiwi kuzungumza sana isipokuwa kuunga mkono azimio hili, na mimi naliunga mkono kwa asilimia mia. (Makofi)