Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jaku Hashim Ayoub (30 total)

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nimuombe kumuuliza maswali madogo sana ya nyongeza.
Kwa masikitiko makubwa sana suala hili limeleta gumzo sana katika chombo cha Baraza la Wawakilishi, limeleta gumzo muda mrefu na hatimaye likatua katika chombo hiki muhimu kwa wananchi.
Mwaka 2014 Serikali mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliunda kamati ya wataalam na kamati hiyo ya wataalam iliongozwa na wanasheria wazito wa nchi hii akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar…
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio swali hili nakuja nalo; imeunda Kamati iliyokuwa inaongozwa na Wanasheria Wakuu wawili kutoka Zanzibar na Bara ili kutatua changamoto zilizokuwepo katika mafuta na gesi ikiwemo ya Kisiwa hiki cha Latham na ripoti hii wakaikabidhi kwenye Serikali zote mbili. Je, ni lini Serikali imetoa ripoti ya suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Zanzibar ina mipaka yake ninachokifahamu hapa kama ni Serikali moja ni majibu yaliyojibiwa hapa; Zanzibar mipaka yake na hili eneo Zanzibar na swali lao. Tukamate wapi ambapo pana ukweli?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tangu mwaka 1968 ambapo suala la gesi na mafuta liliingizwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano; baada ya hapo kwa muda mrefu kumekuwa na hoja na haja ya kuliondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano; na zimefanyika jitihada mbalimbali ili kufikia azma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2010 ilikubalika baina ya Serikali zote mbili kwamba suala hilo liondolewe. Kamati anayoizungumza Mheshimiwa Jaku ya wataalam iliundwa ili kutafuta namna kwa sababu suala hili lipo Kikatiba na lingeweza kuondolewa Kikatiba; lakini kamati hiyo iliundwa mahususi ili kuwezesha jambo hilo lifanyike wakati mchakato wa kubadilisha Katiba unafanyika na matokeo ya kamati hiyo ilipelekea sasa kuapata mwanya ambapo Sheria ya Mafuta tuliyopitisha Bungeni mwaka jana iliruhusu Zanzibar iweze kuchimba na kutafuta mafuta na sasa kuna sheria inatungwa katika Baraza la Wawakilishi ya kuruhusu Zanzibar ichimbe na kutafuta mafuta hata kabla Katiba haijabadilishwa rasmi na kuliondoa suala hilo kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunafahamu kwamba katika Katiba Inayopendekezwa suala hilo limezingatiwa na litaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho napenda kusisitiza ni kwamba sisi Jamhuri yetu hii ya Muungano kama nlivyosema kwenye lile jibu la msingi ni watu wa ndugu na jamaa moja; hakuna mgogoro wowote unaohusiana na mipaka au umiliki wa eneo lolote katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Na sisi pia kama ndugu tumejenga utaratibu wa kiutamaduni na kitaasisi wa kushughulikia na changamoto za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachopenda kutoa rai ni kwamba kwa wenzetu ambao wanapenda kutumia masuala ya Muungano kukabiliana na matatizo yao ya kisiasa, aidha, upande wa Bara au Zanzibar waache hayo mambo na watoe nafasi kwetu sisi ambao tumepewa dhamana ya kushughulikia mambo ya Muungano na Serikali iweze kufanya shughuli zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa kutokana na mchango mkubwa wa maendeleo wa Taifa wa Baba Hayati Mwalimu Nyerere ni mkubwa nikiri hivyo, lakini nataka kuweka Hansard sawa. Rais Marehemu Aboud Jumbe ni Rais aliyefungua demokrasia mwanzo Zanzibar ikiwemo Baraza la Wawakilishi la Katiba ya Zanzibar. Lakini kumbukumbu nyingi zinaonyesha Baba Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anazo ikiwemo Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa, Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kuitwa jina lake, Mfuko wa Taasisi ya Fedha, kuna barabara hata Zanzibar zipo zinaitwa Baba Nyerere. Leo kweli tunamtendea haki Hayati Aboud Jumbe Mwinyi mtu aliyeishi karibu miaka 32 na kila mmoja Mtanzania anajua aliishi kule Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuteleza siyo kuanguka, kutokuwa na meno siyo uzee, je, Serikali imesema ipo tayari kuchukua mapendekezo yangu na kubadilisha jina hilo? Hilo la kwanza.
Pili, je, kwa nini Serikali haikutafakari mapema na badala yake Serikali inasubiri mapendekezo kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge. Lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano itawaenzi viongozi wetu kwa kuweka historia katika kumbukumbu ili vizazi vijavyo vikaja kuwa na historia hiyo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ambaye hatambui michango ya viongozi wetu wa Kitaifa wote, nimwombe tu, bahati nzuri yeye ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi na nina hakika anafahamu kwamba tuna forum kati ya Serikali hizi mbili, tuombe tuzitumie zile forum kama kuna kitu anadhani kina tatizo, tuweze kukijadili na kukirekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana kama kuna daraja lingine, kama kuna barabara nyingine, tafadhali wewe tuambie ili tuweze kuangalia uwezekano wa kutumia hilo jina kwa hilo eneo ambalo hata ninyi watu wa Baraza la Wawakilishi mtaridhika nalo.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa fursa hii na nimshukuru Mheshimiwa Faida kwa swali zuri alilouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi linahusu matumizi ya dola, hivi sasa kumekuwa na kilio cha wanafunzi wengi wa vyuoni kulipishwa ada kwa malipo ya dola na baadhi ya taasisi, ikiwemo taasisi hii ya TRA inayoongozwa na Waziri na Naibu Waziri wa Fedha. Je, kuna Sheria yoyote iliyopitishwa humu kuhusu suala hili na amesema tokea 1992 hakuna utaratibu huo? Je, hatua gani zinazochukuliwa kwa taasisi hizi zinazolipisha ada ya dola kinyume na sheria?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekiri na nimesema kwamba, tunafahamu zipo taasisi zinazotumia dola katika kufanya transaction. Nimesema pia, ni mojawapo ya chanzo cha Serikali yetu kupata fedha za kigeni moja ya faida ni hiyo, lakini kama nilivyosema ni asilimia 0.1 tu ya transaction zinazofanyika nchini zinazotumia dola ya Kimarekani. Kama nilivyosema Sheria ilipitishwa na Kanuni zake zimepitishwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba tunawachukulia hatua gani, bado hatuoni kwamba, inahatarisha na kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, siyo sababu inayopelekea thamani ya pesa yetu kupungua.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali ya nyongeza, mji umebadilika, je, Serikali haioni haja nayo ibadilike kuleta sheria nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa baadhi ya watendaji wake wanaokusanya zile shilingi mia moja hamsini, mia mbili wamekuwa na kauli ambazo haziridhishi kwa wananchi, je, anatoa wito gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mji umebadilika lakini kama nilivyosema kwamba Halmashauri ya Jiji kuna sheria ambayo inaongoza utaratibu katika maeneo hayo nayo ni Sheria Ndogo yenye GN Na.60. Naamini kwa sababu kuna wadau mbalimbali na Mheshimiwa Jaku najua ni mdau wa Jiji la Dar es Salaam lakini na Wabunge na Waheshimiwa Madiwani wa maeneo hayo kama wakiona kuna haja ya kurekebisha Sheria Ndogo hiyo basi wafanye hivyo na sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI ambao ndiyo wenye jukumu la kufanya mchakato huu uweze kukamilika tutalishikia bango jambo hili liweze kuwa mahali pazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine alilosema ni kuhusu kero ya ukusanyaji wa fedha hizo lakini hata uaminifu wa upelekaji fedha zile haupo. Kwa bahati nzuri sasa hivi katika Jiji la Dar es Salaam tuna Mkurugenzi makini sana naamini kwa hizi changamoto ndogondogo zinazobainika tutazisimamia kwa pamoja ili kuzitatua. Lengo ni wananchi wanaoegesha magari yao katika Jiji lile kupata huduma bora bila kupata usumbufu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na kutotaka kuniona naomba niulize maswali madogo sana mawili ya nyongeza na niombe Waziri wa Fedha awe tayari kumsaidia Naibu Waziri. Ninachozungumza ni Kiswahili wala si Kihindi. Waziri wa Fedha ningeomba akainuka yeye maana hili swali linamhusu yeye. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge ni chombo kizito cha Tanzania na Watanzania wametutuma ili tuyasemee matatizo yao. Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri atakuwa yuko tayari kujiuzulu pindi nikimletea ushahidi wa kutosha juu ya suala hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kujiuzulu pindi nikimletea ushahidi wa kutosha juu ya kadhia hii kwa vijana wa Tanzania kutozwa fedha za kigeni katika vyuo hivyo na anajibu hapa hamna? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, amefanya utafiti kwenye vyuo gani mpaka akatueleza hakuna utaratibu wa kutoza fedha za kigeni ili Bunge lako liweze kuridhia tatizo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, swali la tatu, hakuna sheria…
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote anayekuwa hatendewi haki kwa mujibu wa sheria anayo fursa ya kuchukua hatua. Hatua mojawapo ni pamoja na kutoa taarifa kwa ngazi zinazohusika. Ndiyo maana nimesema kwamba kwa kipindi chote hiki Wizara yetu haijaweza kupata taarifa na hata wewe ulivyoendelea kuuliza umeshindwa hata kutuambia mfano wa chuo ambacho kinafanya hivyo. Kwa misingi hiyo, mimi nachukulia hilo suala halipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na kufanya utafiti, ni sawa, ni jambo jema, hilo nalichukua kuendelea kulifanyia kazi.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili limekuwa likijirudia mara nyingi na naomba nitoe maelezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 inamruhusu mtu yeyote kupokea na kumiliki na kutumia fedha za kigeni kwa shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, hao wenye shule siyo kwamba hawaruhusiwi, hilo la kwanza tuelewane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inaweka bayana kabisa kwamba legal tender ya nchi yetu ni Shilingi ya Kitanzania. Nilikwishalieleza Bunge lako Tukufu kwamba ni makosa kwa mtu yeyote kukataa Shilingi ya Tanzania kwa malipo hapa nchini. Kwa hiyo, narudia tena, pale ambapo kuna Mtanzania yeyote anakwenda kulipa ada au malipo mengine akadaiwa kwa dola lakini yeye akatoa Shilingi za Kitanzania akakataliwa, atoe taarifa mara moja ili tuchukue hatua za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine Benki Kuu tumeshafanya utafiti na nilikwishalitolea taarifa hapa ni 3% tu ya shughuli mbalimbali ambazo wana-quote bei zao kwa dola. Kwa hiyo, kosa ni kukataa shilingi kosa sio ku-quote bei zao kwa dola.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami kwanza kabla ya yote niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kumtakia afya njema Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na
familia yake kwa jinsi alivyotuongoza kipindi chake. Pamoja na hayo, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Basi nitauliza swali moja la nyongeza lenye kifungu (a) na (b).
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri wake kwa kuwa makini wakati wa kujibu suala hili lakini kuna kadhia kama hii imetokea kwa baba kufariki na watoto kubaki na huyu mtu akaenda kulalamika Ustawi wa Jamii nao wakapendekeza kwamba
watoto hawa ikifika muda waende kwa babu yao na ukitazama chimbuko la hawa watoto ni babu. Leo kwa nini babu ananyimwa haki yake ya kuwasomesha watoto wale? La kushangaza, baadaye bibi huyo akakimbilia mahakamani
nayo ikaamua kuwa shule zikifungwa wakatembelee tu watoto asiweze kuwachukua. Haki ya mtoto iko wapi hapo katika vifungu ulivyotaja 21 na 7?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mtoto iko wazi katika kifungu cha 37 ambacho kinahusu custody of the child. Katika kifungu hicho utaratibu unawekwa kwamba pale mtoto anapokuwa amefika umri wa miaka saba utaratibu unabadilika badala ya kubaki tu kwamba atakuwa chini ya usimamizi wa mama yake sasa mahakama inaweza ikaamua mtoto ama aende kwa baba au kwa mama kwa kuzingatia mahali ambapo huyo mtoto atapata malezi bora.
Mheshimiwa Spika, lakini kama imetokea sasa mzazi ambaye ni baba amefariki, maana yake mzazi anayebaki automatically ni yule mmoja kwa sababu mtoto ni wa wazazi wawili. Kwa hiyo, kama mama yupo maana yake naturally tu mama anapata haki ya kumlea yule mtoto siyo tena kwa
babu mzaa baba, hapana! Kama mama yupo lakini baba amefariki haki inabaki kwa mama.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama inatokea
kwamba mama anaonekana hana uwezo wa kumlea yule mtoto ama mtoto hapati haki ama mtoto anafanyiwa vitendo vya ukatili kwa namna yoyote ile na wazazi na jamii ipo, basi hao wazazi kama babu wanaweza wakaenda mahakamani kwenda kushtaki na shauri hili likajadiliwa pale
na hatimaye mahakama itaamua kutafsiri kifungu hicho in the best interest of the child.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kutokuwa na afya naomba kuuliza maswali mawili madogo
ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri kuna ushahidi ambao kama utakuwa tayari kuja kuueleza kuwa kuna kodi zinalipwa Bara, je, utakuwa uko tayari kupokea ushahidi huo ili Zanzibar nayo inufaike kibiashara kupata mapato hayo ili imalize deni lake la umeme inayodaiwa? (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuna Tume ya Fedha iliyoundwa mwaka 2007 mpaka leo hiyo Tume ya fedha haijakutana kutatua matatizo hayo, je, ni lini kama Naibu Waziri utachukua hatua hizo ili kutatua tatizo hili la Tume ya Fedha ya Pamoja iliyoundwa nafikiria mwaka 2007 hadi
leo karibu miaka 16 haijakutana?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari kabisa kupata huo ushahidi anaosema na ikiwa tutajiridhisha ni kodi iliyotakiwa kukusanywa Zanzibar imekusanywa Bara tuko tayari kuirejesha Zanzibar, kwa hiyo, naomba tupate ushahidi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Tume ya Fedha ya Pamoja najua imeundwa kama alivyosema na inafanya vikao vyake sasa pia nimeshangaa kusema kwamba tangu imeundwa haijawahi kufanya kazi. Nalichukua suala hili na kama Serikali tunalifanyia kazi.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ningeomba tu Mawaziri na Naibu Mawaziri wakafanye utafiti kwanza wa kina kabla ya kujibu maswali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu aliyojibu Naibu Waziri, haoni wakati umefika sasa ukiona kuwa mizigo iliyokuwa inapimwa kwa tani hapo mwanzo na hivi sasa kuchanganywa na CBM haoni ipo haja kwa hivi sasa mzigo wote ule ukapimwa kwa tani badala ya CBM ukizingatia
Wazanzibari wanategemea chakula sana kutoka Tanzania Bara kwa ndugu zetu wa damu na vilevile biashara kubwa iliyopo kati ya Zanzibar na Tanzania Bara ndiyo uchumi mkubwa wa Zanzibar ukiacha zao la Karafuu kuzaa mwaka hadi mwaka?
Swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri utakuwa tayari kufuatana na mimi mguu kwa mguu na tarehe unipe ili Hansard zikae sawa kwenda kuona kama alivyofanya Waziri aliyepita Mheshimiwa George Harrison Mwakyembe na
akaona matatizo yaliyopo pale na mengine akayapatia ufumbuzi lakini kwa bahati mbaya akaondoka Wizara ile, ikiwemo umeme uliopo pale ni hatari chini, mabonde ya mpunga yaliyopo pale hivi sasa bila kukusudia baada ya bandari na wakati wenye meli wanalipa gharama zile.
Je, ni lini tutafuatana mimi na wewe ili kwenda kuona kadhia zilizopo pale ikiwemo na Kampuni ya Hisab kushindwa kufanya majukumu yake?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, hivi vyote viwili ni vipimo vinavyotumika kutegemeana na aina ya mzigo ulivyopakiwa, ni lazima vyote hivi viwili vitumike the Cubic Bank Metres pamoja na tonnage. Kutaka itume tonnage peke yake kuna
aina ya mizigo itatoa hali siyo nzuri kwa TPA namna ya kuihandle kutokana na namna ilivyopakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kutokana na
swali lake la pili na ukijua wazi kwamba Waziri wangu ni mdau mkubwa wa bandari zote za kule Zanzibar nitaomba niwasiliane nae tukubaliane yeye au mimi na tukishakubaliana nitakupangia tarehe, tutakupigia siku ya kwenda huko Zanzibar kulishughulikia hili.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, hayakosekani.
Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na muafaka. Nawaomba tu Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, wanapojibu maswali kwanza wafanye utafiti kabla ya kuja kujibu humu ndani. Tumekuwa na masikitiko sana back bencher huku na…
Mheshimiwa Spika, hewala!
Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi ni kuhusu meli za Zanzibar na meli hizi ni za local na zimekuwa zikiwa-charged kwa dola na rate ya dola huwa inapanda siku zote.
Je, Mheshimiwa Waziri haoni sababu sasa hivi tariffs zile za muda mrefu na hivi sasa kuchajiwa kwa shilingi ukizingatia zile meli ni za Tanzania na ziko katika sehemu ya local?
Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na kilio kirefu sasa bandarini, hata leo hii pana crane pale imekuwa ikisumbua watu, baada ya miezi mitatu leo ndiyo imeondolewa, ni jambo la kupongeza kwa kuwa nauliza swali humu ndani. Lini Mheshimiwa Waziri atafanya ziara pale kuona hali ilivyo? Kuna usumbufu wa malipo; inachukua masaa matatu au mawili kulipa shilingi 10,000? Ni lini Mheshimiwa Waziri atafanya ziara hiyo kwenda kuona hali halisi ilivyo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa nini tuna-charge kwa dola? Bandarini pale sisi tunafanya biashara na watu wa kutoka nchi mbalimbali kama vile kutoka Tanzania, Rwanda, Burundi na pia Comoro. Lile eneo ambalo wanatumia wananchi hasa kutoka Zanzibar tunafanya biashara na watu wa Comoro ambao wote tunawa-charge kwa dola, lakini inategemea na exchange rate.
Mheshimiwa Spika, sasa kama mtu anataka kulipa dola anaweza kulipa kwa dola, kama anataka kulipa kwa shilingi anaweza kulipa kwa shilingi. Leo tunaona tu kwa sababu dola kila siku inapanda, lakini naamini uchumi wetu utakapokua iko siku currency yetu itakuwa iko nzuri na tutaweza tutamani tulipe kwa dola kwa sababu itakuwa ni cheaper zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu kufanya ziara, ni mara nyingi nafanya ziara kwenye Bandari ya Dar es Salaam na ninategemea hata wiki inayokuja Mungu akipenda, nitafanya hivyo. Naomba tu nimwalike Mheshimiwa Jaku tuwe pamoja katika ziara yangu ili tuweze kuzungumza na wadau wengine jinsi gani tunavyoweza kutatua matatizo ya Bandari yetu ya Dar es Salaam kwa maslahi ya uchumi wan chi yetu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa umakini wake, ufuatiliaji wake na utendaji wake na hasa kwa wapiga kura wake vilevile Jimboni kwake ingawa majukumu ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza kwa kukiri na hii ni mara ya pili kukiri, katika wakati wa bajeti na leo hii. Nafikira baada ya kupitisha bajeti yake ataniambia labda kesho au kesho kutwa tufuatane. Naomba kumwuliza maswali mawili madogo sana ya nyongeza.
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni zinafunguliwa na Serikali, iweje leo hii uhakiki ufanyike wakati mradi umeshafanyika na kukamilika karibu miaka mitano? That is (a).
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mhusika amemaliza kazi, kwa nini Serikali isimlipe fedha yake na uhakiki huo ufanyike kwa watendaji waliosimamia tender hizo ili kuwawajibisha? Hii ni sawa sawa na kumchukua kuku aliyechinjwa kisha akaliwa, ushahidi huwezi kuupata. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Jaku kwa kufuatilia masuala yanayohusu wananchi wake. Hili siyo jambo moja ambalo Mheshimiwa Jaku amefanya hivyo, nawaomba na Wabunge wengine tuige mwenendo wake. Panapotokea jambo linalohusu wapiga kura wake, Mheshimiwa Jaku huwa anafuatilia Ofisini, Wizarani na hapa Bungeni. Nampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba suala la uhakiki ni utaratibu ambao tulijiwekea Serikalini kwa ajili ya; moja, kuwa na uhakika wa madeni ambayo yanatakiwa kulipwa; pili, kuweka kumbukumbu sawa ili kuondokana na ulipaji wa madeni mara mbili. Hii ina faida pia hata kwa anayedai kuweza kuhakikisha kwamba haki yake haipotei. Kwa maana hiyo, kwa sababu ni utaratibu ambao una-cut across kwa wazabuni wote kwa madeni yote ya Serikali na suppliers wengine wote, ni lazima na sisi kama Wizara, ni lazima tufuate taratibu hizo kwa wazabuni wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa taratibu hizo zilishafanyika kama nilivyokwambia, sasa hivi ni suala tu la upatikanaji wa fedha. Sehemu kubwa ilikuwa ni kukubalika kwa deni hilo, kukubalika kwa kazi ambavyo hivyo vyote vimeshafanyika na tunampongeza kwamba amefanya kazi nzuri.
MHE. JAKU HASHIM JAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri wake kwa majibu yao ya umakini kabisa. Naomba kuuliza maswali madogo tu ya nyongeza yenye fungu (a) na (b):-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yako Mheshimiwa Naibu Waziri, swali la msingi umesema Waziri amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Jeshi la Polisi limetenga jumla ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa huu wa Kituo cha Mkokotoni. Umetenga shilingi milioni 200 na kutenga maana yake ni kitu tayari umekiweka pembeni na huyu mtu ni mgonjwa, hili suala nimelisemea karibu mara nne katika chombo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini nije naye mguu kwa mguu ili asije akapata usumbufu apate haki yake hii, ili akamalize kituo hiki na yeye mwenyewe apate matibabu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa vile deni hili lina muda mrefu kwa nini, Serikali au Wizara haitoi priority ikammalizia deni hili, ili kumaliza ujenzi huu wa vituo vyetu vilivyokuwa huko Unguja na Pemba? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali kumpa pole sana huyu mkandarasi kutokana na maradhi ambayo ameyapata na tunamuombea Mwenyezi Mungu amjalie aweze kupona haraka. Nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge hana haja ya kumhangaisha mkandarasi kuja naye hapa mguu kwa mguu, asiwe na wasiwasi wowote fedha hizi shilingi milioni 200 zimetengwa kwa ajili yake katika bajeti ya mwaka huu na kwa hiyo basi, fedha hizo zitakapokuwa zimeingia tu atalipwa bila hata kumsumbua mkandarasi kwa kuja naye hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba lisiwe kipaumbele. Ni kipaumbele na ndiyo maana tukatenga hizo fedha kwa ajili ya kumlipa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunaomba vile vile awe na subira wakati tukisubiri fedha hizi wakati zitakapokuwa zimeingia na tutamlipa mara moja.
MHE. JAKU HASHIM AYUBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza mnyonge mnyongeni, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kitendo alichoonyesha asubuhi hii leo cha uungwana na ungwana ni vitendo. Nikupongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa, tena makubwa, tena makubwa kwa mara ya tatu. Wizara yake anayoiongoza Mheshimiwa Waziri imekuwa ikiwaonea wananchi wa Zanzibar, Unguja na Pemba. Nipo tayari kumthibitishia hilo kwani mafuta yanayouzwa Zanzibar sasa hivi ni ghali kuliko hapa Dar es Salaam. Nimwombe tu kwa unyenyekevu, ni lini atakaa na watu wa upande wa Zanzibar kutatua tatizo hili? Kama anavyojua mafuta ni nguzo muhimu. Mafuta Zanzibar yanauzwa ghali, kodi zimekuwa nyingi na amekiri, nimpongeze kuwa Zanzibar wamechaji Dola 10, wakaiacha Rwanda Dola tatu, Zambia Dola tatu Burundi Dola tatu, kwa nini wanaionea Zanzibar kwa Dola 10? Mawaziri wengi husema Muungano huu wetu …
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima ujenge hoja kwanza. Bila kujenga hoja hawezi kuja kufahamu Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri, nimwombe ni lini atakaa na upande wa Zanzibar maana kuna barua mpaka leo Katibu wake Mkuu hajawajibu Wazanzibari, je, kalamu ya kuandikia hana au anaandika spelling moja moja? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uonevu, mafuta Zanzibar yanauzwa ghali, sisi tunaumia. Mafuta ni nguzo muhimu …
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Kwanza nikiri kweli kwamba kuna changamoto katika hizi tozo ambazo zinatozwa na bandari, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Jaku kwamba tupo tayari kama Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi ya Zanzibar lakini vilevile na Mamlaka ya Mapato kukaa na kuangalia hizi tozo ambazo ni kero sana kwa wananchi wetu wa Tanzania, tuweze kuzitatua kwa pamoja. Katika hilo, nitamkaribisha Mheshimiwa Jaku tukae pamoja tulijadili kwa kina tuliondoe tatizo hilo ambalo linasumbua wananchi kwa njia moja au nyingine. Hili linatatulika kwa mustakabali wa nchi yetu ya Tanzania. Ahsante.
MHE. JAKU H. AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza lenye kifungu (a) na (b).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa akijibu swali la msingi alisema Tume imekuwa ikiongeza jitihada kila mwaka kukagua vituo vya polisi na magereza. Je, katika kukagua vituo hivyo hasa vya polisi wameona makosa gani na hatua gani zimechukuliwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili Kikatiba wanafunzi walioko magerezani…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mheshimiwa Jaku anataka kufahamu baada ya kaguzi hizi ni makosa gani yameonekana. Nirudie tu majibu yangu ya msingi niliyoyasema kwamba ripoti hii ikikamilika itawasilishwa. Nachelea kusema moja kwa moja kwa sababu iko ndani ya ripoti na ripoti hii itawasilishwa. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira ripoti hii ikiwasilishwa ataona ukaguzi uliofanyika na matokeo ya ukaguzi huo.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, lakini kabla ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza aliyekuwa Kaimu Waziri Mkuu Mheshimiwa Mwakyembe kwa kazi nzuri aliyoifanya Kukaimu Kiti cha Waziri Mkuu.
Baada ya hapo nichukue fursa hii swali la msingi linahusu mwanamke na mwanaume, je, kuna sheria gani iliyopitishwa na Bunge kama mtu kafanya kosa mume akakamatwa mke kuna utaratibu gani au kuna sheria iliyopitishwa? Vilevile ninavyojua mimi utaratibu…
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jaku anataka kujua kama kosa la mwanamke anakamatwa mwanamume. Kosa aliyefanya ndiye atakayekamatwa, kwa hiyo, haiwezekani Mheshimiwa Jaku kosa akafanya mtu mwingine ukakamatwa wewe.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru kwa kuniona. Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa akijibu swali la msingi hapa alitaja Balozi, sasa nataka kujua Balozi zote za Tanzania duniani ziko ngapi na Zanzibar wamegaiwa ngapi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, Balozi za Tanzania ziko 40 na Mabalozi wanaotoka Zanzibar wako tisa na hiyo ni asilimia 22.5 ya Mabalozi wote waliopo. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kuniona. Nina swali dogo sana la nyongeza. Swali la msingi linahusu vituo na nilikuwa nikipigia kelele huu mwaka wa tatu au wa nne kuna mjenzi wa kampuni ya Albatina na Mheshimiwa Waziri amekuwa akiahidi sana ndani ya jengo hili muhimu kwa wananchi. Kesho kutwa tarehe mosi mwezi wa Tano Mungu akijalia tunapitisha bajeti; na nilimwambia huyu mzee mpaka leo asubuhi tumezungumza, huyu mzee bado anaumwa anadai ng’ombe kama 30; na amekiri si mara ya kwanza si mara mbili, si mara tatu, kesho kutwa sitakuja kuizuia shilingi Mungu akinijalia. Je, lini atalipwa mjenzi huyu karatasi zake na lini nimlete?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba Mheshimiwa Jaku amelifuatilia sana jambo hili Ofisi na hata kwenye masuala ya anapopata fursa ya kusemea hapa kwenye bajeti. Kama nilivyosema, tutaonana naye ili tuweze kukubaliana, kwa sababu kitu ambacho kimetuchelewesha hapa katikati ilikuwa ni kwamba lazima madeni yote yafanyiwe uhakiki kabla hayajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa yalikuwa yanafanyiwa uhakiki, nitaomba Mheshimiwa Jaku aridhie tuwe na kikao mimi pamoja na yeye na watendaji wangu ili tuweze kupata kwanza status ya upande wa uhakiki umefikia hatua gani. Tukishajua kwamba limeshahakikiwa liko tu kwenye hatua za kulipwa tutaweza kulifanyia uharaka kwa sababu kama anavyosema Meshimiwa Jaku mhusika anahitaji sana fedha kwa ajili ya matibabu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kutokuwa na afya kwa upande wangu, niwapongeze sana Naibu Mawaziri; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye na Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, kwa kupokea simu kwa wakati, niwapongeze sana kwa hili na wengine naomba wafuate mfano huu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, hizo Kanuni nani anazisimamia ili hao Mawaziri ambao wamo humu ndani, hawapokei simu zikiwemo za Wabunge, mbali na za wananchi, ili hatua zichukuliwe? Ikiwa namba za ma- RPC ziko hadharani na ziko katika mtandao, sababu gani zinazosababisha Mawaziri hao namba zao zisiwe hadharani? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri kabla ya kupata Uwaziri hapa, Mheshimiwa Spika ni shahidi, alikuwa mkali kutetea wananchi wake na akawa ngangari kwelikweli. Ni lini Mawaziri namba zao zitatangazwa hadharani ili wananchi na Wabunge watakapowapigia simu wapokee?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, maswali yake kwa kweli ni moja lilelile limejirudia lakini pia nafikiri kuna mchanganyiko kidogo katika swali lake. Analalamika kwamba Mawaziri hawapatikani kwa simu lakini wakati huohuo analalamika kwamba namba zao haziko hadharani. Sasa hao ambao huwapati kwa simu ni wapi kama simu zao hunazo? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kujibu swali lake, nani anazisimamia hizo Kanuni nilizozitaja? Kanuni zinasimamiwa na Serikali, kila Wizara kuna viongozi wake na Wizara ya Utumishi inasimamia Kanuni zote za watumishi wa umma.
Mheshimiwa Spika, sasa ilimradi tumeshasema katika jibu la msingi kwamba hatuna ushahidi wa Waziri ambaye kwa makusudi hataki kupatikana, ndiyo maana hatujamchukulia hatua maana hatuna taarifa hizo. Kila Waziri hapa ana mkubwa juu yake, akizileta kama mimi siyo size yangu nitazipeleka juu, lakini atuletee na siyo kwako wewe tu, Mtanzania yeyote yule ambaye anaona kwamba hakutendewa haki, hampati Waziri kwa makusudi, hilo kwa makusudi naliweka kwenye, Wazungu wanasema inverted commas, maana yake mimi sina ushahidi nalo hilo.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kila Wizara kuna sanduku la maoni. Sanduku lile una jambo la kuishauri Wizara, una jambo umetendewa vizuri na Wizara unaandika unawapongeza, una jambo umefanyiwa vibaya na Wizara unaandika unawasema.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimkumbushe tu kidogo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa vile alikuwa ni mwalimu wangu kullu-kum rai, wakullu-kum mas-ul alayhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliokuwa wafanyakazi wa benki ambayo waliondolewa kazini na wasimamizi wa Deposit Insurance Board (DIB) ndio wakasimamia ufilisi wa benki hiyo. Hawajalipa wafanyakazi hao mpaka sasa hivi na ukizingatia ni wapiga kura wetu, ni wananchi wetu kwa muda mrefu sasa hivi. Je, haioni sheria hiyo aliyoitaja kuwa imepitwa na wakati na inawakandamiza wananchi na lini ataleta sheria hiyo? That is (a).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili katika majibu yake alisema kukusanya madeni pamoja na fedha za benki zilizopo kwenye benki nyingine nje ya nchi na kulipa amana za benki, nataka nimwambie tu FBME correspondence bank ni Dutch Bank hebu tuambie kiasi gani ambazo ziko huko na lini zitaletwa ili wananchi hao na Serikali kukosa mapato. Na hivi juzi tumeshuhudia makontena kupigwa mnada wananchi wanataka kununua makontena hayo ili wapate biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza ni swali la wafanyakazi wa iliyokuwa Benki ya FBME. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, taratibu za wafanyakazi zinashughulikiwa na sheria za kazi za Taifa letu. Kwa hiyo, wafanyakazi wale walipoajiriwa na benki hii walisaini mikataba na hivyo sheria za kazi za Taifa letu zinaendelea kusimamia haki ya wafanyakazi wote waliokuwa wa benki hii ya FBME.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili napenda kumwambia Mheshimiwa Jaku Hashim kwamba avute subira tunaendelea kufuatilia kama anavyofahamu yeye kwamba benki hii ilikuwa ni benki ambayo asilimia 10 ya uendeshaji wake ulikuwa ndani ya Taifa letu na asilimia 90 ulikuwa nchini Cyprus. Kama Wizara na Benki Kuu tunaendelea kulifuatilia jambo hili kwa ukaribu na tunawahakikishia wateja wetu watapata fedha zao kwa muda muafaka.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimuombe tu Mheshimiwa Naibu Waziri anisikilize kwa makini kabisa, ninachokizungumza ni Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri, Muungano wetu huu tumeungana watu nchi mbili, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa Tanganyika ndiyo maana jina likapatikana likaitwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenkiti, kati ya mambo waliyokubaliana yalikuwa ni biashara na viwanda na swali la msingi linahusu viwanda vilevile. Nataka sababu za msingi nijue Kiwanda cha Sukari cha Mahonda hata Wabunge tungesimama mara nyingi mjue kuwa hili suala limetukwaza ndani ya moyo wetu. Bidhaa zinazotoka Tanzania Bara zinakwenda Zanzibar bila kigugumizi, leo viwanda vya Zanzibar kuzalisha na hii Jamhuri inaitwa Tanzania hebu tuelezeni ukweli Kiswahili tuweze kufahamu kwa nini maziwa ya Bakhresa hayawezi kufika hapa yanakwama na huku tukishuhudia wakati mwingine sukari inatoka nje mnaacha kununua kutoka Zanzibar. sababu gani zinasababisha bishaa hizo kupata kigugumizi. Za Tanzania Bara zinaingia Zanzibar, za Zanzibar kuja huku imekuwa kitendawili? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Kamati kati ya Waziri wa Biashara wa Tanzania (mimi) na mwenzangu wa Zanzibar. Yamekuwepo malalamiko ya wafanyabiashara na kupitia vikao hivyo tunakaa chini na kujadili suala la Kiwanda cha Maziwa cha Bakhresa kilichopo Zanzibar mimi mwenyewe nimekwenda nikakiangalia. Nikakitembelea kiwanda kile, nikaangalia uzalishaji wao ni mzuri na maziwa yamekuwa yanaingia. Tulichokubaliana ni kwamba mtu anapopata tatizo la kukwazwa na watendaji ilitolewa namba maalum na kikao cha Mawaziri wawili kwamba anayekwamishwa awasiliane na mamlaka. Kama kuna tatizo kuhusu maziwa mnijulishe mimi kusudi mimi niende kuwa-task wale wanaohusika. Lakini hao wawekezaji wenye viwanda napenda nikiri kwamba ninashughulika nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye Kiwanda cha Sukari cha Mahonda. Serikali imeamua kusimamia Sekta ya Sukari kwa sababu kupitia sukari tunataka kuzalisha ajira. Kwa sababu ya nia ya kuzalisha ajira na kwa sababu ya fursa ya ajira katika sekta ya sukari hii sukari ni classified product na sasa hiyo Tume ninayowaeleza ikimaliza kazi ndiyo mtakuja kujua maana ya classified product kwamba sukari inakuwa classified. Kiwanda cha Mahonda wake wa kuzalisha ni tani 4,000 mahitaji ya Zanzibar ni tani 20,000. Mimi nawasiliana na watu wa Zanzibar, Waziri wa Zanzibar kwamba azalishe 4,000 auze kwao. Ndiyo!
…ninachozungumza ndiyo…, ngoja niwaeleze…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waheshimiwa Wabunge wanataka kujua ninachokisema.
Ningeomba muwape fursa wale wanaotaka kunisikiliza niwaeleze suala la Mahonda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niku-address wewe Mahonda inazalisha tani 4,000. Itakapokuwa imezalisha tani 4,000 inataka kuziuza katika soko la Tanzania Bara haitazuiliwa, tutakaa chini tuzungumze, lakini huwezo kuwa unazalisha tani 4,000 lakini wewe soko lako ni tani 20,000 halafu wewe unakwenda kuuza tani 4,000 nje hizi nyingine unazipata wapi? Kwa hiyo, ndiyo utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa taarifa katika Bunge, tunataka ku-classify sukari. Mafuta ya kula ni classified, sukari itakuwa classified kwa sababu tunataka ajira. Niko tayari kulisimamia hilo mpaka nitakapoambiwa vinginevyo. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa akijibu swali lake, alisema mazungumzo yamefanyika na Serikali ya Kenya. Namwomba tu Mheshimiwa Naibu Waziri, mazungumzo hayo yamefanyika Tanzania au Kenya? Yamefanyika lini na yatamalizika lini ili wananchi wetu wapate nusura ya kutokuhenyeka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mazungumzo tunafanyia wapi, siwezi kueleza hapa kwamba tunafanyia wapi kwa sababu inategemea na sisi wenyewe tutakavyokuwa tumeamua. Nimesema mazungumzo yanaendelea kati ya Serikali hizi zote pamoja na Ubalozi baada ya kujua kwamba hili tatizo linafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu ni kuhakikisha kwamba changamoto hii inatatuliwa. Mimi kama Serikali nataka kumhakikishia kwamba mazungumzo yameshaanza, sisi kama Wizara tayari tumeshawaandikia Wizara ya kisekta ambayo inahusika na uvuvi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tayari tumeshakubaliana kwamba sisi kwa upande wetu pamoja na Ubalozi wetu na Ubalozi wa Kenya tutashughulikia hilo jambo. Sasa tunafanya wapi? Hayo ni maamuzi ya Serikali.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kukiri kuwa Tanzania hakuna uhaba wa sukari katika majibu yake na amesema baada ya miaka mitatu au minne uhaba huu utapungua hiki ni kiswahili alichokiandika.
Mheshimiwa Spika, mara kadhaa tukifika katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani pamekuwa na kadhia hii ya upungufu wa sukari. Haioni Serikali imefika wakati ipunguze punguzo hili ili kuwalinda wananchi ukizingatia wananchi ndiyo waliyoweka Serikali hii madarakani na si aibu viongozi wetu Zanzibar hao Marais wetu mara nyingi ikafika mwezi Mtukufu wa Ramadhani huondoa ada hii na Tanzania Bara imeiga mambo mengi kutoka Zanzibar ikiwemo vyama vingi vimeanzia Zanzibar, haki za binadamu zimeanzia Zanzibar, matumizi ya dola yameanzia Zanzibar si aibu kuiga. (Makofi)
Je, haioni imefika wakati kuiga formula hii mara kadhaa unalinda viwanda, viwanda hivyo haviwezi kulindika wakati huu?
Mheshimiwa Spika, la pili tumo kwenye Tume ya Afrika Mashariki, lakini mpaka leo bidhaa za Zanzibar haziwezi kufika kwenye soko hilo mpaka upitie Tanzania Bara. Je, haijafika wakati Tanzania Bara mkatamka kwa Zanzibar sasa hivi isiingie katika soko hili kwa kupitia mgongo huo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimeeleza kwanini, sukari inayozalishwa Tanzania Bara inakuwa na gharama kubwa. Nimesema tumeamua kusimamia viwanda hivi ili tuweze kuzalisha ajira. Sasa kuhusu kupunguza nimeeleza kwamba ushuru kwa makubaliano yetu ya East Africa ni asilimia 100, tumepunguza kutoka asilimia 100 kuja 25 tumeshapunguza kuja asilimia 25. Kuhusu bidhaa ya Zanzibar kama kuna mfanyabiashara ana matatizo awasiliane na Waziri wa Zanzibar ambaye mimi na Sekretarieti inawasiliana naye. Mimi Zanzibar sina matatizo bidhaa zinakuja zinaingia nchini kama mtu hafuati viwango ana matatizo yake. Lakini TBS ya Tanzania Bara na Viwango vya Zanzibar wanawasiliana haya mambo madogo madogo myawasilishwe kwa watendaji kule na watendaji watayashughulikia, ahsante.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kwa dhati kabisa kumshukuru Naibu Waziri huyu ambaye amekuwa akishughulika sana kwa suala la Muungano, mara utamkuta Pemba mara Unguja na mambo mengi ni sare ya Muungano anaileta Baraza la Wawakilishi, ni Waziri Naibu wa pekee na niombe Manaibu Mawaziri wengine mfuate nyayo zake huyu bwana na hana kiburi hata kidogo. Mheshimiwa Naibu Waziri sikusifu kwa kuwa upo mbele yangu lakini kiburi huna na Manaibu Waziri na Mawaziri wafuate nyayo zake.

Mheshimiwa Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ndege kuondoka kule Ijumaa na Jumapili nimwambie kuwa ndege kule inaondoka saa mbili na kufika hapa 2.30 kutoka saa tatu mpaka saa 10 jioni huoni ni fatigue na ni adhabu hii kwa Wazanzibari: Sasa, swali la kwanza, je, ni lini atafanya utaratibu huu wa kujipanga upya kuona Zanzibar ni haki yao ya msingi katika Shirika hili la Ndege la Air Tanzania na hii Tanzania ni mmiliki kutokana na muungano wa Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania?

Mheshimiwa Spika, ATCL tokea mwaka 2007 inadaiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar shilingi milioni 241 na amekiri humu ndani kuwa watalipa na mpaka hii leo ikiwa mimi ni mjumbe wa Kamati hii hawajalipa deni hili? Pia je, ni sababu gani zilizopelekea Wajumbe wa Bodi ya ATCL hata upande mmoja…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba abiria wa kutoka Zanzibar kuja Dodoma wakipitia Dar es Salaam huwa wanachukua muda mrefu sana wakisubiri ndege ya kuwaunganisha, hilo tumeliona na kwa kweli tunalifanyia kazi, kama mnakumbuka juzi wakati tunapokea ndege yetu nyingine tumeahidiwa na Mheshimiwa Rais kuwa tutakuwa na ndege za Viongozi ili tuziweke kwenye ATCL ili tuweze kuhudumia.

Mheshimiwa Spika, lengo la ATCL ni kuhudumia Watanzania wote bila usumbufu wowote. Kwa hiyo, tukapozipata hizo tutahakikisha wasafiri wa Zanzibar kuja Dodoma hawachukui muda mrefu sana pale uwanja wa ndege.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Jaku ameuliza kuhusu deni la shilingi milioni 241 ambayo ATCL inadaiwa kama landing fee na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar. Ni kweli hilo deni tunalikumbuka na tunalifahamu na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa linafanyiwa kazi na Mamlaka za Ukaguzi; tukishalihakiki tutalipa. Tunaendelea kulipa madeni kwasababu ATCL ina madeni mengi na inaendelea kuyalipa baada ya kuyahakiki.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimpongeze sana Mheshimiwa muuliza swali Mheshimiwa Mwatum Dau. Kwa kweli hawapati stahili zao Polisi na waliojenga Vituo vya Polisi pamoja na Ofisi zao. Swali la Msingi linahusiana na kwamba hawapati stahili zao, karibu mwaka wa sita au wa saba….

MWENYEKITI: Swali swali.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili limeahidi kwa kampuni ya Albertina kumlipa pesa zake milioni 200 kwenye bajeti iliyopita ya nyuma yake na mpaka leo hajalipwa na Mheshimiwa amekuwa akitembea na ilani ya chama cha Mapinduzi. Je, ni lini stahili hizi atapata kwa ajili ya kituo hiki cha…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Jaku amekuwa akifuatilia sana suala la huyu Askari ambaye amezungumzia. Nimuhakikishie kwamba yale ambayo nimeyajibu kwenye swali la msingi, huyu anayemsema ni baadhi ya wale Askari ambao wako katika hatua za mwisho mwisho kumaliza matatizo yao. Ni kweli kabisa katika Ilani hii ya CCM, Ibara ya 146 imezungumzia stahiki za askari na ndiyo maana sisi kama Wizara tunawajibika kuhakikisha kwamba stahiki za askari hazichezewi kwa namna yoyote ile.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpe pole sana Mheshimiwa Waziri kwa kuvamiwa Kituo chake cha Polisi cha Madema…

MWENYEKITI: Waheshimiwa, muda wetu umekwisha. Mheshimiwa Jaku.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tarehe 25 Julai, 2017, naomba kunukuu Hansard, “taratibu hizo zilishafanyika kama nilivyokwambia sasa. Tarehe 9 Novemba, “Serikali inatambua deni hilo.” Tarehe 8 Novemba, 2017 mwaka wa Fedha 2017, “Jeshi la Polisi limetenga jumla ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ikiwemo mkandarasi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona ni aibu kwa Serikali yangu kupata aibu na hili deni ni la muda mrefu. Je, Mheshimiwa Waziri, hesabu hata ulipochaguliwa wewe Jimboni kwako ulianzia kwa kura moja ukafika hapa. Kama mimi, Serikali yangu kupata aibu nami ninaipenda niko tayari…

MWENYEKITI: Mheshimiwa, uliza swali.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …niko tayari kuanza kuchangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kituo. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuchukua shilingi milioni moja, kupokea mchango huu ili tufuatane kupeleka deni hilo na hizi hapa? Maana yake deni limeshakuwa la muda mrefu. Yuko tayari kupokea shilingi milioni moja kufuatana nami kupeleka hizi fedha za deni?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ilani hii ya CCM ujenzi wa vituo vya Polisi na makazi ya Askari tumeweka utaratibu kwamba tutahusisha wadau. Ninashukuru sana wewe Bungeni kujitokeza kuwa mdau kwa mujibu wa ilani hii. Hivyo naomba mchango wako uuwasilishe kwa Inspekta Jenerali wa Polisi ili tuendelee na ujenzi wa vituo vya Polisi hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kweli kabisa kwamba deni la huyu Mkandarasi limekuwa la siku nyingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Jaku, ambaye najua akifuatilia jambo lake ni king’ang’anizi, ni moto wa kuotea mbali; na kwa kweli siku siyo nyingi hatutakubali jambo analolisema kwamba Serikali yetu inatiwa aibu. Ndiyo maana Wakandarasi wengi nchini wanapenda kufanya kazi na Serikali na Serikali yetu inalipa madeni yake na deni lake limeshahakikiwa, awe na subira wakati wowote tutaweza kumlipa Mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali hili karibu kwa ufasaha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri alikiri kuwa dawa hizi ni ghali na zina gharama kubwa na Serikali isiogope gharama kwa wananchi wake, wananchi ndio Serikali na Serikali ndio Wananchi na Mheshimiwa Lyimo alizungumza karibu watoto 9000 wanakufa kwa mwaka. Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itajaribu kuiga lini formular kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya utawala wa Dkt. Ali Mohamed Shein, kutoa dawa zote Unguja na Pemba bure? Na Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeiga mambo mengi kutoka Zanzibar, dawa…

MWENYEKITI: Swali moja, swali moja tu Mheshimiwa Jaku.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Je, ni lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano itafuata nyayo za Mheshimiwa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein kutoa dawa bure kutoa dawa bure kwa wananchi na sio kwa mdomo, dawa zipo Unguja na Pemba.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kwamba, Serikali itatoa dawa bure kwa Watanzania wote milioni 55 haitawezekana. Kwa hiyo, sasa hivi sisi kama Serikali kuleta nafuu kwa wananchi kuweza kumudu gharama za matibabu tunajielekeza katika mpango wa bima ya afya kwa wananchi wote, ili wananchi waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Waziri hebu tueleze Bunge hili, tokea mwaka 2009 sheria hii haijaridhiwa Zanzibar na kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam na kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar inachukua siku ngapi kutatua tatizo hili? Huu mwaka karibu wa 10; huoni Serikali mnaikosesha mapato kwa jambo ambalo halina msingi wowote?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, katika hii miaka Kumi aliyoitaja Serikali imepata jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 22 ambapo mgawanyo wa pesa hizi asilimia 50 huwa inaenda Mamlaka ya Bahari Kuu ambayo ni sawa na Bilioni 11, bilioni Sita ilienda katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Bilioni Nne ilienda katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhiwa kwa sheria hii kwa upande wa Zanzibar ni mchakato ambao tunautazama na tunaamini kwamba iko siku moja mchakato huo utakamilika. Kama nilivyosema katika jibu la msingi la awali ya kwamba ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wadau wetu wote juu ya kukwama kwa biashara hii ya Uvuvi wa Bahari Kuu na tunayachakata na hatimae tuweze kutoka na suluhu ya kuhakikisha tunaendelea kuvuna na kulinufaisha Taifa letu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, subira ina mipaka yake, nisubiri hadi lini maana hata kuna wimbo umeimbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni lini mtairuhusu Zanzibar kujiunga moja kwa moja katika soko la Jumuiya la Afrika Mashariki kwa nchi zile za Uganda, Burundi na Rwanda kwa vile soko la Tanzania Bara limefungwa kabisa, Zanzibar hairuhusiwi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile Jamhuri ya Muungano ndiyo yenye nguvu katika sekta ya fedha, sera za kodi na ndiyo mhimili mkubwa wa uendesha wa biashara na nchi. Je, hamuoni mnaendelea kuikandamiza Zanzibar kiuchumi kwa vile bidhaa za Tanzania Bara zinaingia Zanzibar bila vikwazo kwa maana kwamba saa 24 milango iko wazi na zinapokelewa na kupigiwa salute? Je, lini mtaondosha pingamizi hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza hapo awali masuala yanayohusu Muungano wa nchi yetu hii ni muhimu na sensitive na ndiyo maana yamewekewa utaratibu maalumu wa namna ya kujadiliana. Kwa hiyo, niseme tu kwamba hayo yote ambayo yanaonekana yanahitaji kufanyiwa maboresho mbalimbali ni vema yakajadiliwa kupitia vikao hivyo ambavyo tumeona ni muhimu sana na vimekuwa vikifanya kazi nzuri sana katika kutatua changamoto za Muungano.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nizungumze kidogo kidogo ili nifahamike nisiende haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina sehemu mbili ambazo ni Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Nilichouliza ni mipaka ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, kisiwa kile kiko sehemu gani, hicho ndicho nilichouliza. Kisiwa kile kiko Zanzibar au Tanzania Bara. Swali langu la kwanza nafikiri limefahamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni sababu gani iliyopelekea Tanzania Bara kudai kisiwa kile ni chao na Zanzibar kudai ni chao? Hata hivyo, kuna ushahidi wa kutosha na naomba nikuletee nakala hii na kuweka record ya Bunge hili ni sababu gani iliyopelekea kuvutana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 Serikali mbili zilikutana, ya Mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania Bara na ikaundwa Kamati ya Wajumbe wawili wazito akiwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Bara. Je, ni lini ripoti ile italetwa ili kuondosha fitina hii?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Jaku kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Jaku majibu niliyoyatoa katika swali lako la msingi yamejitosheleza kuelezea kisiwa hiki kiko wapi. Hata hivyo, nyongeza yake, kwa kuwa tayari unayo taarifa, nadhani ni jambo jema sana tukakutana ili uweze kunikabidhi tuone namna gani tunaweza kulifuatilia jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kwamba kila jambo lina utaratibu, hata kama Wanasheria wamekutana lakini ni lazima viko vikao maalum, iko Sekretarieti lakini wako Makatibu Wakuu, iko level ya Mawaziri mpaka zije zikutane Kamati zote mbili za SMZ na Jamhuri ya Muungano ili kuweza kuona ni namna gani mambo haya yanaweza kufikiwa muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Jaku wala asiwe na wasiwasi. Serikali iko kazini tukutane tuone taarifa aliyonayo ili tuone ni namna gani tunaifanyia kazi. Ahsante.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichouliza Mheshimiwa, Je, Kati ya wanafunzi hao ni wangapi waliotoka Zanzibar pamoja na majina yao. Swali hili limeletwa zaidi ya mwezi mmoja na, kwa maana hiyo wizara haijawa tayari kutaka kujibu na ninaomba utumie kanuni yako swali hili lije tena. Baada ya hayo, tuendelee hivyohivyo, kwa kuwa suala hili la Muungano wala siyo hisani wala fadhila, ni la Muungano, kwa mujibu wa Katiba ambayo umeisaini wewe bwana Chenge, ukurasa mwisho 124. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo inayoshughulikia masuala yote ya elimu ya juu, Wizara ya Elimu ya Zanzibar kukosa fursa hii. Je, ni lini watakaa kuweka utaratibu huu Zanzibar vijana hawa wakapata masomo kuhusu Elimu ya Juu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tokea kuanza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kweli karibu mwaka wa nne, vikao hivyo vimefanyika mahali gani na wapi, kama Mheshimiwa Waziri ni mkweli wewe. Tuwe wakweli, hii si fadhila wala hisani, kwa mujibu wa Katiba hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jaku kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, kwamba nafasi za ufadhili zinazotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hutolewa kwa Watanzania wote bila kujali wanatoka upande gani wa Muungano. Wakati tunatangaza nafasi hizo, kawaida hakuna sifa au hakuna hitaji la wewe kusema kwamba unatokea upande gani wa Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anaponitaka mimi nije na orodha ya wanafunzi wangapi wamenufaika wanaotoka Zanzibar, ananipia kazi ambayo kawaida hatuifanyi, kwa sababu sisi tunachofanya tunapopata nafasi, tunakaa na wenzetu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kupitia sifa zile halafu tunawachagua wanafunzi wa Kitanzania, bila kujali wanatoka wapi. Kwa hiyo, hatuwaambii waandike kama wanatoka Zanzibar au wanatoka Bara. Kwa hiyo, orodha ambayo ananiomba sisi hatuna! Kwa sababu hatuchukui wanafunzi kwa kuzingatia sifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimhakikishie kwamba Wizara yangu inashirikiana vizuri sana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kila wakati tunahakikisha kwamba pande zote za muungano zinapata manufaa sawa bila ubaguzi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima afahamu kwamba nafasi hizi hutolewa na wale wanaoomba wanatakiwa washindane. Kwa hiyo, mara nyingine ukisema tuanze kukaa na kusema tuanze kuchukua watu kulingana na wametoka wapi, tunaweza tukashindwa kwa sababu kule wanakwenda kushindana na wanafunzi wa nchi zingine. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba, asijenge ubaguzi kichwani, sisi hatuna ubaguzi, tunakaa na wenzetu na wala hakuna malalamiko yoyote ambayo yameshakuja kwamba kuna Wazanzibar ambao washindwa kupata nafasi hizi.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, haya ndiyo majibu ya muda mrefu, lakini anavyoanguka ndivyo anavyochinjwa. Nami nitakuja hivyo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nakupongeza na miongoni mwa Manaibu Waziri wanaopigiwa simu wewe na Atashasta Nditiye mnapokea kwa wakati tofauti na Mawaziri wengine, hilo hongereni sana. (Makofi)

Mheshiniwa Naibu Waziri, swali hili limeulizwa karibu mara tano humu ndani nikiwemo mimi mwenyewe tarehe 6 Septemba, 2018 na leo ni tarehe 12 Septemba, 2019, ni mwaka mmoja na siku kidogo. Kama mwaka mmoja hivi tulifanyiwa semina hapa Ukumbi wa Msekwa, walikuja Ma-deputy governor karibu watano, Wakurugenzi na Watendaji na niliuliza swali hili, wakasema hizi fedha ziko Dutch Bank zitaletwa muda siyo mrefu. Sasa swali langu ni: Je, tokea muda huo zinaletwa kwa baiskeli ama kwa mguu? Maana ni muda mrefu hazijafika. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi juzi hawa jamaa walishinda kesi yao huko Uingereza: Je, ni kweli na kwamba waliambiwa waliofungua kesi hiyo walipe gharama za kesi? Ni kweli wameshinda kesi? Kama wameshinda, ni hatua gani zinazofuata? Wengine tukumbuke Mheshimiwa Naibu Waziri, cheo ni dhamana…

SPIKA: Maswali yasiwe mengi, nataka maswali mawili tu Mheshimiwa Jaku.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza, amekuwa mfuatiliaji mzuri sana tangu benki hii ilipofutiwa usajili wake hapa nchini akifuatilia amana za wateja ili waweze kulipwa. Kwa dhamira njema na nia njema ya Serikali yetu, ndiyo kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa shilingi milioni 1.5 wateja ambao walikuwa na amana hiyo ndani ya benki, yatari tumeshalipa zaidi ya asilimia 83 ya wateja wote. Asilimia 17 iliyobaki ni wateja ambao hawajajitokeza wao wenyewe kuja kuchukua amana zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba dhamira ya Serikali yetu ni njema na ndiyo maana tumeanza kulipa hawa wateja wote ambao walikuwa na fedha zao ambazo hazizidi shilingi milioni 1.5 kama sheria inavyotuelekeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza naomba niyajibu yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza fedha hizi hazitakuja kwa baiskeli, wala kwa gari, wala kwa meli, ila ni taratibu za kisheria zitakapokalimika. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha amana za wateja wetu wote ambao wako ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania zinabaki kuwa salama na wanazipata pale ambapo tumemaliza majadiliano na Benki Kuu ya Cyprus.

Mheshimiwa Spika, tayari mwezi wa Tisa baada ya Mahakama za nchini Cyprus kurejea na kuanza kufanyakazi yao, kesi zote zilizokuwa zimefunguliwa, tumekubaliana zitafutwa na tayari sasa fedha hizo zitafika ndani ya nchi yetu na watu wetu wote wataweza kulipwa fedha zao.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba tu nitoe majibu ya nyongeza kwa swali la nyongeza alilouliza Mheshimiwa Mbunge na hasa kuhusu ile kesi ya Uingereza.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wamiliki wa iliyokuwa Benki ya FBME walifungua kesi Uingereza. Lakini lengo la kesi ile ilikuwa ni ku-challenge mwenendo wa mchunguzi aliyekuwa anachunguza masuala ya FBME kule Uingereza, ni kweli kwamba Mahakama kule imetoa hukumu yake lakini kwa namna yoyote hukumu au matokeo ya kesi ile haiathiri suala zima la liquidation ya ile benki huku. Kwa maneno mengine, hukumu ile haina athari yoyote wala haigusi jambo lolote katika mchakato unaoendelea kwa upande wa Tanzania na Cyprus.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)