Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jaku Hashim Ayoub (13 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, unapokuta maji yakoge, mwanzo hujui mbele kama utayakuta tena.
Kwanza nichukue fursa hii kukushukuru wewe kunipa hizi dakika nne au tano hizi zilizobaki kumalizia ngwe hii iliyobaki na nitakuwa si mwingi wa fadhila kama sikumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyeniwezesha kusimama hapa na kuvuta pumzi zake na kurudi tena kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo Mheshimiwa Waziri kipindi kilichopita mwaka jana, nilikigusia sana na nikazuia shilingi, na hii leo hii nafikiri Mheshimiwa Waziri kuna vijana 13 kutoka Zanzibar. Nazungumza kuhusu maslahi ya Zanzibar kuhusu Wizara hii, kutokana na mambo yanayohusu masuala ya Muungano.
Kuna vijana 13 mmewasomesha Chuo cha Diplomasia, bahati mbaya mkawachukua saba, lakini kwa masikitiko makubwa na unyonge na huruma kubwa mpaka hii leo vijana hao saba hamjawaajiri. Mwaka jana nilihoji kwenye bajeti na Mwenyezi Mungu si Athumani kanirudisha tena leo hii, nipo hapa, kwa hiyo, nitahitaji maelezo ya vijana saba hawa wa Zanzibar mpaka leo hamjawaajiri na hii ilikuwa si hisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni makubaliano katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Vijana hawa hamjawaajiri hadi hivi leo, nataka maelezo ya kina kuhusu suala hili na umri wao unakwenda, na mmechukua barua Zanzibar kama kuwaazima, si kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka hapo kwa haraka haraka nitahitaji maelezo lakini haya vilevile ni ya kusikitisha, Wizara hii huko nyuma au uzoefu unaonesha Waziri anatoka Bara, Naibu Waziri kutoka Visiwani. Lakini kwa masikitiko Wizara hii wote wazee mmekalia kiti chenu, lakini si maamuzi yangu ni maamuzi ya Mheshimiwa Rais. Lakini kama hapatoshi hapo, hata Wizara ya Fedha haya mambo ya Muungano tulikuwa tupokezane, hapatoshi hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa umakini wake na Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu, alikuwa akijitahidi katika safari za nje, kuwachukua Mawaziri kutoka Zanzibar katika safari zake, je, mpango huu utaendelea tena vilevile au utalala?
Mheshimiwa Mwenyikiti, nitoke hapo nataka kuulizia haya maslahi ya Mabalozi wangapi wa Zanzibar waioajiriwa, huu ni wimbo wa Taifa wa muda mrefu. Wimbo huu umekuwa wa muda mrefu, kuhusu ajira katika Wizara hii nataka kujua Mabalozi kutoka Zanzibar ni wangapi wanaowakilisha hivyo? Vilevile senior officer kutoka Zanzibar, katika Mabalozi wako wangapi, wimbo huu umekuwa ni wa muda mrefu lakini hautoshi...
MWENYEKITI: Ahsante,
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Bila kupoteza muda wala kurembaremba sana, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na baadhi ya watendaji wake, maana wengine siwajui kwa umakini wao na utendaji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumsifia Mheshimiwa Waziri, ikiwa yeye ana pumzi zake, na mimi nina pumzi zangu. Watu wengi baada ya mtu kuondoka ndiyo humsifu mtu kwamba alikuwa mzuri; lakini namsifu nikiwa niko hai na yeye yuko hai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni miongoni mwa Mawaziri wa Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa bora katika utendaji wake, bila kuficha! Mheshimiwa Waziri ni msikivu, utendaji wako tumekuwa tukiuona ambao hautaki torch. Ni Waziri unayeshindana kidogo na Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba, kwa muda mfupi amechukua Wizara mbili kuongoza na huo ni kutokana na umakini wako Mheshimimiwa Waziri. Waziri ambaye hana Jimbo, akitokea Ikulu mara nyingi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana na elimu yake, utendaji wake, umakini wake na busara zake, ndiyo maana Marais wengi huvutiwa na wewe kutokana na umakini wako. Mheshimiwa kuna usemo usemao; mgema akisifiwa, tembo hutia maji, unatokea Zanzibar. Hata Mheshimiwa Kishimba anatamani kuwa Mzanzibari Mbunge wa Kahama, lakini Mungu hajamjalia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaigusa Bandari ya Dar es Salaam na nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe kwa kazi aliyoifanya pale. Mabenki yale baada ya kuchangia kipindi cha mwaka uliopita, akafungua benki na tumeziona. Mheshimiwa Dr. Mwakyembe keep it up! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hapa, kidogo Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa umakini kabisa; na ball pen iwe karibu kuandika; yatamgusa Engineer Kakoko wa bandari ile na Port Manager ambaye ana-act, Fredy John Liundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyo katika bandari ya Dar es Salaam bado kuna matatizo, kauli siyo nzuri na sisi Waislamu tunasema maneno mazuri ni sadaka au methali inayosema, kauli nzuri humtoa nyoka pangoni. Sasa Mheshimiwa Waziri anza kuandika mwanzo. Customer care kwanza haipo katika bandari ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, customer care katika bandari ile haipo. Mheshimiwa Kakoko siyo kila anayepepesuka ni mlevi. Kazi zote hizi Mheshimiwa Kakoko huwezi kuzifanya peke yako. Kama yupo juu, basi nafikiri utakuwa unasikia huko. Madaraka haya lazima mgawane na wenzio, utakuja kuumia, sisi bado tunakuhitaji. Huu ni ushauri wangu, bado tunakuhitaji. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, ndungu yangu, trend ya mizigo ya miaka kumi au saba ya nyuma, mizigo iliyoingia na iliyotoka na sasa hivi, kaiangalie. Tuelezane ukweli, mizigo iliyoingia na kutoka imeshuka. Ni ushauri wangu. Kaangalie trend ile ya miaka saba au sita ya nyuma au mitano iliyotoka hivi sasa, utaona ukweli ulipo. Hali siyo nzuri kusema ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni declare interest, mimi ni mfanyabiashara, siwezi kudharau dafu kwa embe la msimu. Hii siasa kesho Mungu akijaalia haipo, lakini dafu siku zote unaweza kulipata. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna VAT on transit hivi vitu wananchi wanalalamikia sana. Ajira mnavyotangaza, hivi juzi mmetangaza ajira, sijui kama mmezitangaza, lakini kuna watu mmewaajiri. Tuwe wawazi, tuwe wakweli katika bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, DG baadhi ya wafanyakazi wanamwogopa sasa hivi. Kama wanapita njia hii wafanyakazi wanamwogopa, wanapita njia nyingine. Liandike, ulifuatilie kama nasema ni ya kweli ama siyo ya kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wengine wanaomba muda wao wa kustaafu kabla haujafika, wanaogopa bandarini kutokana na matukio yanayotokea. Suala za wizi limekuwa wizi tu. Ndiyo yale niliyosema, siyo kila anayepepesuka ni mlevi. Muda wa kustaafu wafanyakazi haujafika, watu wanataka kustaafu kuondoka, wameshachoka. Tena wale wazoefu; tutakuja kutafua rasilimali hiyo wakati huo hatuna. Huu ni ushauri wangu, Mheshimiwa Waziri fuatilia niliyokwambia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije DMI (Chuo cha Baharia). Kuna eneo pale limekaa miaka nane au kumi, kibanda kimeshaanguka. Unafanya biashara; mimi mwenyewe binafsi nilishapeleka barua pale, lakini hakuna majibu, hakuna kilichofanyika. Nafikiri wenyewe wapo hapo. Imekuwa kama nyoka wa mdimu Mheshimiwa Waziri. Nyoka wa mdimu hukaa kwenye mdimu, yeye hana kazi nazo na ukienda kuchuma, anakurukia, faida iko wapi? Siyo kitu kizuri!
Kodi zingesaidia! Wengine wamekodishwa maeneo yale, wengine hawajakodishwa, wako kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika Bandari ya Letakii, hapa pana dhambi na maonevu makubwa. Wafanyabiashara wa Zanzibar na Zanzibar tegemeo lake kubwa ni biashara. Leo viazi, cabbage, pilipili ina-megati nane inapekuliwa. Vipo hapa hapa, local food hiyo, hatutendi haki. Kama unataka, nitakutajia; kuna geti namba tatu Mheshimiwa Waziri. Malindi pana geti pale pale, mita 50 haijafika, pana mizani, halafu unakuta mizani yenyewe. Usumbufu, mnasema mnapunguza foleni, huku mnazidisha foleni. Umefunga mlango wa mbele wa nyumba wa nyuma umefungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanalipa ada za bandari pale kwa muda mrefu, lakini charge zimekuwa nyingi. Bandari zimekuwa na mapote; ikija mvua tope, likija jua, vumbi; wafanyakazi wana mazingira magumu katika kazi ile. Nampongeza sana Acting Port Manager, John Liundi, kazi anayofanya pale nitakuwa sijamtendea haki na nitakuwa mtovu wa adabu wa mwisho kama sikumshukuru kwa mazingira ya kazi anayofanya pale. Hongera Port Manager unayekaimu kwa muda. Pengine Mungu atakujalia muda siyo mrefu utatoa fupa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna yule mlinzi pale anayeshughulikia ulinzi wa bandari. Kwa muda mrefu ulinzi umeimarika bandari ya Dar es Salaam. Tuwape haki zao. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Jamaa wa pale anaitwa Twange, amefanya kazi nzuri ya ulinzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla muda haujamalizika, nije kwenye ndege, Bombardier sasa.
Mheshimiwa Waziri chukulia mfano Pemba kule Makombeni kuna mabonde ya mpunga, umelima, umeshaotesha mpunga wako, kuna ndege wanaitwa tongwa wale, ukishauacha unakuja kuuvuna. Hawa wana malalamiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, umenunua baiskeli, leo unashindwa kununua pump tu kujaza upepo baiskeli! Hebu waingizeni pesa tusije tukawalaumu, baadaye tukawa tunasema Tanzania wanafanya vibaya. Wanahitaji mtaji hawa. Kama hamuwezi, wakopesheni five billion. Leo tunafanya vitu vizuri, baadaye tutakuja ku-fail.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu msikivu sana yule CO hata jina lake silijui mimi. Ni rasilimali kubwa sana yule. Maneno yake tu ukisikia akizungumza utafikiri asumini zinatoka mdomoni, harufu yake. Ndiyo yale walisema, maneno mazuri ni sadaka. Ongeza mtaji wa Mtanzania. Hawawezi kufanya kazi wale bila kuwa na mtaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka hapo utaratibu wa Bombardier jamani, kuja usiku sisi kama walinzi tumechoka. Jaribuni kupanga utaratibu, Bunge linaanza Jumanne. Pangeni Jumatatu angalau saa 10.00 tuondoke kule. Badilisheni utaratibu huu. Halafu bei zake zikoje? Leo unanunua bei nyingine, kesho bei nyingine, kiti ndiyo kile kile. Hebu jaribuni kufanya utaratibu (format) mwingine. Bunge hapa linaanza Jumanne, Jumatatu angalau ndege ingeondoka saa 10.00 pale.
Hayo ni maoni yangu, nanyi kama hamtaki mtachangia. Kila mmoja ana uhuru wake wa kusema.
Nije kwa SUMATRA. Mheshimiwa Branch Manager, sheria hii inaumiza watu...
Mheshimiwa Branch Manager, sheria hii inaumiza (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi bila kupoteza muda nichukue fursa hii kukupongeza wewe kwakuniruhusu kuchangia. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa muda mfupi kuwa Waziri katika Wizara mbili tofauti, hii ni kutokana na utendaji wake na umakini wake Mheshimiwa Waziri. Nikupongeze vilevile kwa timu ya Singida United kupanda daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze Kamishna Hamdani Omar Makame kwa kutuongoza vizuri Zanzibar katika kipindi chake na nimtakie kila la kheri na mapumziko mema ya kikazi. Nitakuwa sijamfanyia haki Kamishna Johari Masoud Sururu waImmigration Zanzibar kwa kazi anayoifanya Zanzibar, amekuwa makini katika utendaji wake bila ya kujali mvua, jua, usiku, mchana anapiga kazi, nimpongeze sana Kamishna Sururu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa sijamfanyia haki Kamishna Musa Ali wa Zanzibar, kwa kujenga vituo vingi Zanzibar vya polisi zikiwemo nyumba. Amejenga nyumba na vituo vya Polisi Paje katika Jimbo langu ninakotokea.Vilevile amejenga vituo cha polisi karibu saba kikiwemo cha Jambiani, Nungwi, Bumbwini, Kiboje, Meli Nne, Fumba, Jozani na Pemba – Chokocho. Mheshimiwa IGP huyu mtu nafikiri ni hazina kubwa sana unisikilize kwa makini Mheshimiwa IGP, amefanya kazi vizuri sana na kubwa zaidi kujenga Kituo cha Afya Ziwani katika Makao Makuu ya Polisi, kituo cha kileo kabisa, huyu ni mtendaji kazi kupita kiasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri hapa unisikilize kwa makini vinginevyo shilingi nitaizuia. Kuna mjenzi nimeshakwambia mara mbili/mara tatu, amejenga nyumba na Kituo cha Madungu anadai shilingi milioni 220, leo mwaka wa tano anahangaika,mpaka akapata maradhi anafanya mazoezi bila kutaka kupata ngazi kwenda na kushuka.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nitakuwa mkaidi sana kama hujamlipa haki yake na Mwenyezi Mungu kamjalia kapata maradhi ya mitihani sasa hivi. Mtu anadai shilingi milioni 220; ameshajenga vituo, leo miaka mitano na baya zaidi hata kwenda kukaguliwa hazijaenda kukaguliwa, hilo ni jambo la kusikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na IGP naomba mnisikilize, kumekuwa na kilio cha Wabunge humu ndani kunyanyaswa na wanaambiwa baada ya miaka mitatu muda wao wa Ubunge umekwisha, kuna Mbunge wa Ulanga yumo ndani humu, anaonesha kitambulisho kwa traffic anaambiwa wewe baada ya miaka mitatu Ubunge wako unaisha, siyo kauli nzuri hiyo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tunalipigia kelele katika vikao vyetu siku zote. Traffic wamekuwa wameshika mpini, Mbunge hana thamani mbele ya traffic. Leo Mbunge wa Ulanga yule anaambiwa baada ya miaka mitatu na kitambulisho anatoa, hatuwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu hali za uchakavu wa nyumba, Mheshimiwa Waziri ulikuwemo Ziwani umeona askari wetu wanaishi vipi, mchana haendi kujisaidia, anakaa mtu upande huo huko anamwambia nitizamie mtu anakuja huko, ili apate kwenda chooni! Hali hairidhishi, mazingira siyo mazuri wanayofanya askari, vitendea kazi havipo, tunafanya nini? Hali ya Ziwani ndiyo Makao Makuu ya Polisi hairidhishi.(Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile askari wanakaa muda mrefu kupandishwa vyeo, anafika miaka 15 mpaka mtu anakaribia kustaafu hajapanda cheo! Hii siyo halali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya vituo vya polisi vimekuwa vichakavu sana, ulikaja Pemba, pia wale wanaojenga mbona hamuwalipi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nichangie kuhusu mahabusu.Polisi wanapata shida wanatoa pesa zao mfukoni kuwahudumia mahabusu.Pia hali ya bajeti Zanzibar kupiga doria, umekuwa mtihani vilevile mafuta.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sitaunga hoja mkono mpaka jamaa apate haki yake.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kukupongeza kwa dhati kwa kuniruhusu kuchangia hoja hii. Bila kuniruhusu nisingeweza kuchangia hoja hii kwa hiyo nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada anazochukua kwa wananchi wake na kwa jinsi anavyowatumikia. Nichukue fursa hii tena kuwapongeza wale Mawaziri na Naibu Mawaziri waliopanda hivi juzi kwa kupata vyeo hivi na niwape pole waliokuwa wakitegemea, lakini hawajapata nafasi hizi mpaka muda huu. Niwaombe wasikate tamaa, Mwenyezi Mungu siyo Athumani lakini niwaambie tu uteuzi wao huu wanaujua nini maana yake? Uteuzi huu Mheshimiwa Rais aliotoa Mawaziri na Naibu Mawaziri ili wamsaidie kutumikia wananchi kinyume chake Mawaziri na Naibu Mawaziri simu mnazifunga, hamuwatumikii wananchi, siyo kitu kizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaziteua Wizara kama Wizara ya Afya wenye matatizo ya afya waende afya, Wizara ya Elimu waende wenye matatizo na elimu, Wizara ya Ardhi waende wenye matatizo ya ardhi lakini kwa masikitiko simu ukimpigia Waziri hapokei, ukimpigia Naibu Waziri hapokei, humu ndani tumo sawasawa haya mambo yanageuka. Aliyeko mbele mngoje nyuma, aliyeko juu msubiri chini atateremka tu. Hivi vyeo ni dhamana na tutakwenda kuulizwa siku ikifika tumewatumikia vipi wananchi. Kuna milango mitatu ya kuingilia humu ndani ya Bunge hili, kuna Jimbo kutoka Ikulu, kuna Viti Maalum na uchaguzi wa wananchi, hiki chombo kina uzito kutokana na wananchi. Wananchi ndiyo waliopotupa dhamana ya kuja kusema matatizo yao humu ndani. Kuna siku tutakwenda kuulizwa hizi dhamana zetu tumezitumia vipi, haya mambo ya kupita tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika mchango wangu sasa kuhusu TRA. Mheshimiwa Waziri kwa masikitiko na unyonge mkubwa sana kitendo ulichokifanya cha kutatua kero ya Kenya na Tanzania kuhusu maziwa na cigarette umechukua muda mfupi sana, lakini kero ya Zanzibar bado kila Waziri kinamshinda. Leo Muungano wetu huu tunasema kwa mdomo tu tunataka uendelee kudumu kwa vitendo. Mali inayotoka Uganda, Kenya, Burundi, Zaire, Zambia ikiingia Tanzania wala huulizwi kitu, leo mali inayotoka Zanzibar ukiingia nayo Dar es Salaam utafikiri umeleta unga, huu uonevu wa aina gani? Dkt. Mpango Wazanzibari hamtufanyii haki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mzanzibar kachukua gauni zake tatu anakuja hapo bandarini anaambiwa weka chini, tv tu moja, mbili anaonewa, hii haki ikoje? Nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Saada Mkuya, kazungumza vizuri sana lakini huu Muungano tunaosema ni wa upande mmoja tu jamani? Tunasema huu Muungano uendelee kudumu na mimi nasema uendelee kudumu, Zanzibar ukiacha zao la karafuu tegemeo kubwa ni biashara. Wenzetu Tanzania Bara Alhamdulillah, endeleeni kushukuru tuna madini, mbuga na neema nyingi tunazo lakini leo biashara ile nguo tatu au nne, miche mitatu ya sabuni unasumbuliwa pale mwisho mchele unaonunua pale bandarini unalipishwa pana kimizani kidogo kimewekwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala siyo la upande mmoja Mheshimiwa Saada kazungumza bado hujafika Zanzibar, mimi nikuombe ufike. Pindipo utakapokusanya mapato Mheshimiwa Rais atakusifu, tuangalie biashara, huku kidogo, huku kidogo, kuku anataga yai moja ukamlazimisha mayai matatu utamuua, utakosa kuku. Chukua huku kidogo, huku kidogo pishi inajaa lakini kuku yule anataga yai moja, unamlazimisha leo leo atage matatu atakwenda wapi, tutaua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu twende Kariakoo ukaangalie milango ya maduka nani anaitaka saa hizi? Samora mlango ulikuwa unakodishwa bei kubwa sasa hivi milango imefungwa. Fikiri Mheshimiwa Waziri huu ni ushauri wangu wa bure wala sitaki kulipwa mimi. Kaa na wafanyabiashara utazame nini tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muungano Zanzibar tunauhitaji kwa kila hali miongoni mwao ni mimi kutokana na udogo wetu, lakini mzigo utoke Kenya, Rwanda, Burundi hauulizwi kitu, mzigo ukitoka Zanzibar ukifika hapa aibu. TRA ni moja, formula yake ni moja, vigezo vyake ni vimoja, Waziri nikuombe kwa masikitiko makubwa, Wanzanzibar ukiacha karafuu wanategemea biashara. Juzi umetatua tatizo la Kenya kwa muda mfupi tu, leo unatuaacha sisi ndugu zako wa damu. Umetatua juzi tu tumekupongeza lakini litatue na hili pia. Taa huwashi nje, unawasha kwanza ndani ya nyumba yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawashaje nje kabla ya kuwasha ndani huwezi kuona na sadaka sisi tunasema inaanzia nyumbani ndipo utoe nje. Kwa hii kero dada yangu kazungumza sana hapa, fanya uwaite wafanyabiashara, wanafunga milango wanaanza kuondoka. Tembea na kama uko tayari tufuatane nikakuoneshe mlango huu umefungwa, huu umefungwa utahesabu milango mingapi. Tufike wakati tupunguze, tujihurumie jamani mapato tunahitaji wewe kusanya mapato mazuri uone Mheshimiwa Rais atakavyokusifu. Nchi inataka kwenda kwa mapato lakini tukianza kubana kwa marungu, leo watu wananyang’anywa komputa zao wanavamiwa na TRA, polisi imekuwa TRA sasa hivi watu wanasumbuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri sisi sote humu ndani vyeo vyetu vimoja tunaitwa Waheshimiwa tofauti tu ni Waziri na Waheshimiwa na haya mambo yanageuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba kukaa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nisikupotezee muda, mimi nitahitaji maelezo maana nikichangia itachukua muda mrefu, nitahitaji maelezo kwenye mambo kama manne Mheshimiwa Waziri. Nikupongeze tu juzi nilikuona katika sherehe za Siku ya Sheria Duniani na ulihimiza sana Mheshimiwa Waziri, mahabusu sheria ya kesi zao zile haraka, hebu tueleze kuna tatizo gani Arusha kule watu wana miaka sita mpaka leo wanachunguzwa nini? Kesi mpaka leo au kunatakiwa ushahidi wa Kinyamwezi mpaka ukamilike? Watu wanateseka, wana familia zao, wana watoto, wengine wanataka kuthubutu kuachwa, hebu tueleze tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kumejitokeza tatizo hivi sasa Zanzibar watu kuchukuliwa wakaja kushitakiwa huku Bara, je, Zanzibar hawana Mahakama? Hawana wanasheria? Tatizo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sheria inavyosema unapokamatwa ndipo unapohukumiwa. Leo sijaona mimi mtu kakamatwa Pakistan akaletwa Tanzania, kakamatwa Mascut akaletwa huku, hebu tueleze utaratibu gani wa sheria huu, ukoje? Mimi si mtaalamu wa sheria, lakini haya mambo yanajitokeza sasa hivi na yanazidi kuendelea, keshokutwa usije ukanichukua mimi ukanileta huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini na lingine nikuombe, hebu katika hiyo orodha ya mambo ya Muungano, na hii Mheshimiwa Chenge ulikitunga wewe kitabu hiki ukiwa Mwanasheria mwaka 2005. Kuna orodha hii ya mafuta na gesi, mali pamoja na mafuta yasiyochujwa na matokeo ya mafuta aina ya petroli na aina nyingine ya mafuta, limo humu na sheria hii ilivyoelezwa, angalia Ibara ya 64 Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria; “Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa ni batili na itatanguka na pia endapo sheria yoyote itakayotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa ni batili na itatanguka.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni vichekesho, kwa hiyo bado tuna mtihani wa mafuta Zanzibar. Pamoja na jitihada zilizochukuliwa, niwapongeze Marais wote wawili, lakini bado, na ulijibu hapa, ulimjibu Mheshimiwa Juma Ngwali kuwa bado mafuta ni tatizo. Hebu lipate kuliondoa ili Muungano ulete sura nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na lingine, mara nyingi waislamu wamekuwa wakiahidiwa Mahakama ya Kadhi humu ndani hebu tueleze imefikia wapi? Hata katika Katiba Iliyopendekezwa na wewe ulikuwa ni Mjumbe katika Tume ya Warioba, hebu tuelezeni juu ya Mahakama ya Kadhi nayo ina mambo matatu, ndoa, mirathi na talaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamekuwa wakilalamikia suala hili, na hili Bunge hili ukifuata Hansard limezungumza ndani wakati wa Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa, utaratibu fulani utaletwa, lakini mpaka leo? Imekuwa kama mtoto wa kuku anayetaka kunyonya, kesho, keshokutwa mpaka anakuwa kuku, maziwa hayaoni. Hebu tuelezeni lini utaratibu huu utaletwa wa Mahakama ya Kadhi? (Kicheko)

Mheshimiwa Waziri ulikuwa Mjumbe katika Tume ya Warioba na waislamu wengi walizungumzia suala hili. Kuna mambo ya ndoa, talaka na kuna mambo ya mirathi, hebu tuendelee na utaratibu wa kulieleza suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisikupotezee muda. Naomba nafasi hii umpe mtu mwingine achangie dakika zilizobaki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru, ntakuwa mchoyo wa fadhila kama sikukushukuru kwa kupata nafasi hii. Niyakumbuke maneno ya Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Salmin Amour Juma, almaarufu Komando, alikuwa na maneno mawili akisema urafiki na nchi, kwanza nchi urafiki baadae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa January Makamba, Waziri wa Wizara hii jinsi anavyojituma bila kujali mvua, jua, usiku au mchana, anapoitwa Zanzibar wakati wote anatii amri; nimpongeze sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu cha kupendeza sana Wizara hii, hasa Naibu, angetoka angalau Zanzibar, ingeleta sura nzuri sana ya Muungano, ndiyo Wizara ya Muungano, ingeleta sura ya Muungano. Hata hivyo, siwezi kuingilia mamlaka ya Mheshimiwa Rais, nataka kujua nini Muungano, nini definition ya Muungano; what is union? Umuhimu wa kuungana watu, kuwa pamoja, kushirikiana katika nyanja mbalimbali kiuchumi, ulinzi, ajira, huu ndiyo Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini Muungano, definition yake ni hii; umuhimu wa kuungana watu kushirikiana, kuwa pamoja kiuchumi, nchi, ulinzi, ajira. Hata Tume ya Mheshimiwa Jaji Warioba ilisisitiza sana umuhimu wa Muungano huu kuwepo, katika watu 1,000 labda watu wawili watakataa Muungano huu kuwepo. Lakini kuna mambo muhimu au fomula gani ya kuendesha Muungano wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mheshimiwa Jaji Warioba haikukataa Muungano huu kuwepo, katika watu1,000 labda watu wawili watakataa Muungano huu. Kwa hiyo Muungano huu tunauhitaji na ukizingatia keshokutwa, Mheshimiwa Machano amezungumza, tunatimiza miaka 54 ya Muungano wetu huu. Hata hivyo, kuna baadhi ya watu mnawalea vibaya, wanachafua Muungano huu bila kuwaonya. Tatizo tutafute formula ya kuendesha Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, nije kwenye changamoto za Muungano, akiwemo Mheshimiwa Keissy. Ya nini kusema … (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)

T A A R I F A . . .

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, narudia yaleyale, ni mzee wangu, adabu kitu cha bure, nitaendelea kumheshimu hata tukatoka nje. Mimi ni jirani yangu, nikianguka leo ataniokota yeye na akianguka leo nitamuokota mimi, sisi sote Waislamu, sisi ndugu moja lakini ukweli utabaki ukweli; moja moja mbili mbili, kavu kavu mbichi mbichi, mimi naendelea kukuheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye changamoto mwaka jana Mheshimiwa January alizungumza zimebaki changamoto tatu, nimpongeze. Hata hivyo, changamoto hizo mpaka leo nafikiri zipo ICU, hazijapata ufumbuzi, wanakaa vikao lakini zinafika mahali zinapata kigugumizi. Angalia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ukurasa wa sita Sura ya Saba, vifungu 133 na 134, huu ndiyo mzizi wa fitna yetu ya Muungano, ni Joint Finance Commission, ukamaliza huu Muungano umekwisha, Mungu atuweke hai. Joint Finance Commission, Jamhuri ya Muungano Katiba 1977, nafikiri ukurasa wa sita, kifungu 133 na 134, huu ndiyo mzizi wa fitna uliobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza humu katika mahali palipokuwa nidhamu yake siwezi kusema nzuri bandarini. Watu wamekuwa wanapata mpaka maradhi. Waziri wa Fedha hayupo hapa, Naibu Waziri ampelekee salamu Mheshimiwa Waziri. Huu Muungano tumeungana kwa nia njema, isiwe kama Lugha ya Kiarabuukiandika unavutia kwako tu, maandishi ya Kiarabu ukiandika unavutia kwako tu. Naibu Waziri wa Fedha, Waziri wa Fedha hayupo hapa, lakini mahali wanapoteseka watu, Mheshimiwa Tauhida kazungumza, mtu kavunja TV kwa uchungu, ule ni uchungu, tunaumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara Rais wetu tumemuona shahidi anawatetea wanyonge, anasimamisha misafara njiani kuwasikiliza wananchi, Wamachinga kaachia huru wafanye biashara. Leo mtu katoka Zanzibar, Zanzibar uchumi wake ukiacha karafuu ni biashara, tuwe wakweli. Imefika mahali kero hizi hazijafika mahali, double standard, VAT imekuwa kupita kiasi, tutaendelea kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna msemo usemao asemaye hachoki…

T A A R I F A . . .

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa aliyonipa nimeipokea kwa mikono miwili. Taarifa nzuri, taarifa ambayo inaleta sura ya Muungano wetu; nimshukuru sana Mheshimiwa Mattar kwa umakini wa hali hiyo. Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukizingatia kuna mambo matatu ya uchumi haya yako Tanzania Bara, sera za kodi ziko Tanzania Bara, sera ya sarafu iko Tanzania Bara. Hebu tufike mahali haya madogomadogo wenzetu mtuachie au tubadilishane, miaka mitano mchukue ninyi, miaka miwili tupeni sisi. Sera hizi muhimu, nyenzo hizi muhimu mnazo ninyi, Sarafu ya Tanzania, Benki Kuu, kodi hizi, mna mbuga nyingi za kuendesha, mna madini mengi. Zanzibar uchumi wake ni biashara, mambo madogo madogo haya ifike mahali… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nikushukuru kwa kunipa fursa hii, jioni hii kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Hata Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akihimiza sana viwanda na kasi yake. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, maneno mazuri sisi Waislam tunasema ni sadaka au maneno mazuri humtoa nyoka pangoni. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, uongozi ni dhamana, ni jambo la kupita, leo lipo kesho halipo na baada ya siasa kuna maisha nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, biashara ni nini? Biashara haifanywi na mtu mmoja, biashara lazima iwe na monopoly. Biashara haiwezi kufanywa na mtu mmoja hata kidogo. Uzuri wa Wizara ya Biashara haiwezi kwenda bila ya fedha. Fedha ndiyo biashara, biashara ndiyo fedha, kwa hiyo, hivi vitu kidogo vinaoana. Hapa kidogo Mheshimiwa Waziri nataka unisikilize kwa makini, hasa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango, nikuombe sana, kuomba siyo kosa, kuiba ndiyo kosa, kama kuna watu wanateseka, Benki ya FBMEwatu wanateseka, nimepiga kelele, nitaendelea kupiga kelele mpaka pumzi yangu ya mwisho. Watu wanaweka haki zao kule, wananyanyasika, wengine wameshaanza kutangulia mbele ya haki, hakuna harufu yoyote na Benki Kuu ndiyo dhamana na kama nilivyosema cheo ni dhamana na tutaenda kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu au mbele ya haki, tumetumia vipi dhamana zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanataka kusomesha, fedha zao zimekwama benki. Mnawaambia nini? Benki Kuu iko chini ya Wizara ya Fedha, Bureau de Change zote mna-control ninyi. Tumeona Greenland Bank imefungwa na wakati huohuo mnasema fedha za wateja ziko salama, salama iko wapi? Au Salama jina la mtu? Maana kuna jina la mtu Salama. Kuna wawekezaji Zanzibar pesa zao zimekwama, wafanyakazi wa benki pesa zao zimekwama, mishahara yao haipatikani.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa huruma na unyenyekevu, sijawahi kukuambia hivi Mheshimiwa Dkt. Mpango. Wewe binadamu na mimi binadamu, tuwe na jicho la huruma. Je, ungefanyiwa wewe au mimi tungekubali? Tuwaonee huruma wananchi. Wananchi ndiyo walioweka Serikali hii madarakani. Mtu ana shilingi milioni 200, unampa milioni moja na laki tano ni sawasawa na kumpa peremende baadaye ukamnyang’anya, haifai hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika kero za Muungano, biashara ndogondogo bandarini. Hii tuliambiwa moja kati ya kero ya Muungano. Msijali mtu wa mbali, jirani yako ndiyo mtu wa karibu. Tumetimiza miaka 54 ya Muungano huu na tuombe uendelee kudumu. Wafanyabiashara bandarini Mheshimiwa Mwijage wanateseka na hesabu inaanza moja ndipo ije mbili na tatu. Hawa wote wafanyabiashara wameanzia biashara ndogondogo wakafika kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi wa Zanzibar amechukua TV moja, amechukua mashati yake matatu, amechukua kilo zake sita za sukari akafika pale ananyanyaswa. Imefika wakati watu wakathubutu kuvunja TV zao, huu siyo ubinadamu wala siyo uungwana. Nikuombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Waziri wa Biashara mliangalie hili suala. Leo imekuwa mali inayotoka Zambia, Uganda, Burundi na Kenya inaingia hapa iko salama, inayotoka kwa ndugu zetu upande wa pili utafikiri umeleta bangi au unga, kwa nini tunafanya hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema na nitaendelea kusema, baada ya siasa kuna maisha nje, haya mambo ni ya kupita na cheo ni dhamana lakini hatuwatendei haki. Zanzibar inategemea zao la karafuu, uchumi wake wa pili ni biashara. Leo bandari imezuiwa usajili wa meli, kuna matatizo hatujui kinachoendelea, lakini tusiwanyanyase wafanyabiashara. Mtu ana TV moja, mbili, atakula nini? Anakuja na boti yake asubuhi, jioni apate kuuza aondoke lakini anakuja mzigo unaoza ndani mle, ndiyo lengo hilo? Katika moja ya kero kubwa ya Muungano hili ni moja, tuwe wakweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Kiwanda cha Sukari cha Mahonda, hapa nisikilizeni vizuri. Kiwanda hiki kipo Tanzania, Tanzania hii imeitwa na Zanzibar ikiwemo. Tunalinda viwanda vya Tanzania, je, Zanzibar haipo Tanzania? That is my question. Tunalinda viwanda vya Tanzania, Zanzibar haiko Tanzania? This is my question au hailindwi Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalinda viwanda vya Tanzania Bara kwa hiyo Zanzibar haipo? Pombe, nondo, saruji, unga wa ngano unaingia Zanzibar lakini bidhaa kutoka kule kuleta huku imekuwa mtihani, tuwe wakweli. Ndiyo yale nimemwambia Mheshimiwa Keissy, moja iwe moja, mbili iwe mbili, mbichi iwe mbichi, kavu iwe kavu. Kama tunalinda tuseme tunalinda viwanda vya Tanzania Bara siyo Tanzania, tuwe na vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. au Prof. Mwijage maana cheo chao kikubwa, juzi ulijibu swali la 205. Mheshimiwa Spika aliona udhaifu wa swali hili, ningesema mimi ingekuwa mtihani, huku unakataa Tanzania hakuna uhaba wa sukari, huku unasema baada ya miaka mitano sukari itakuwa ya kutosha, tukamate wapi? Huku unakataa, uhaba wa sukari haupo, baada ya miaka mitano unasema uhaba wa sukari utakuwa umekwisha. Sasa tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Waziri toka kaangalie bandarini, hiyo sukari imeshafika usije ukauziwa mbuzi kwenye gunia. Uende ukapate ushahidi, usije ukapata ushahidi wa Kinyamwezi. Nenda kaangalie hii sukari uliyowapa vibali imefika? Isije kufika Ramadhan hapa tukawasumbua au kuwatesa wananchi. Narudia tena, Serikali hii isingekuwa madarakani bila wananchi. Hata Uwaziri wako huu,Mheshimiwa Waziri ungekuwa mtihani tungetawala nini, miti au barabara? Wananchi ni kitu muhimu. Hata Mheshimiwa Rais mwenyewe anawajali wananchi, tumpongeze kwa dhati kabisa hasa wananchi wa chini, credit yake kubwa iko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isiogope kula hasara kwa mambo madogo madogo kama haya na wewe mshauri Mheshimiwa Rais usiogope kuwa hiki kiko hivi, hiki kiko hivi, mueleze tuna upungufu huu. Tuliwapa vibali vya sukari, mimi na ninyi, twende mguu kwa mguu kama sukari mliyotumbia imeshaingia tani 135,000, twende tukaiangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijamaliza lakini itabidi nishukuru hivyo hivyo kwa muda ulionipa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kwanza kukushukuru kwa kuniruhusu kusimama hapa na kama si jitihada zako baada ya Mwenyezi Mungu kuniruhusu, nitakuwa sijakufanyia haki lakini nikushauri tu na nikuombe, tunapoomba Mwongozo ungejaribu kutusikiliza kuna nini wewe ndio Mwenyekiti na unatoa ruling. Kuliwahi kutokea moto humu ndani wa simu, pengine lilikuwa jambo la hatari huwezi kujua, usidharau wito, dharau unaloitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi asubuhi, katika kipindi cha maswali na majibu nilitetea Kampuni karibu mara sita na Naibu Waziri akajibu alivyojua mwenyewe, lakini yule jamaa sasa hivi ni mgonjwa ka-paralyze na yote hii kutokana na mazoezi ya kupanda ngazi na kushuka kwenye Maofisi. Anafanyishwa mazoezi bila kutaka mwisho wake kapata mtihani, kwa hiyo niombe Serikali hili suala iliangalie katika madeni na huyu umuangalie na Hansard zipo haya sio maneno yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye ukurasa wa 3 na 17 naomba uangalie maana nisijefika mahali nikawa nazungumza labda kitu sio. Niangalie kwenye hiki kitabu ukurasa wa 3 na 17 angalia halafu kama nitakosea nikosowe wewe ni mwalimu mzuri wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kwa ushauri, maoni yatakayotoka katika kikao hiki cha Bunge yatazingatiwa kikamilifu katika kuandaa rasimu ya mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu naomba kuisoma hii Hansard na juzi ulikuwepo tena ili iwe record katika Bunge hili nitakapokuja kufa angalau historia itanihukumu au itanikumbuka; “Sasa kwa sababu ahadi ilikuwa ni Bunge hili basi, tutasogeza ahadi kwa Bunge lijalo, Bunge lijalo halipo mbali sana, kwa hiyo ni vizuri kwa kweli mtakapotoka hapa basi mjitahidi Bunge lijalo tusikie lugha nyingine ili tuendelee na mambo mengine, tunajua ni kubwa na lina mambo mengi, lakini umuhimu kwa sababu ya interest kubwa ya zaidi ya Muungano.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 17 miradi ya umeme. Utekelezaji wa miradi ya umeme na kufufua kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo maji na gesi, kuendeleza miradi ya umeme ikiwemo sakata hili la Zanzibar la VAT umeme mara mbili, na sheria ya VAT mradi wa mwisho unaotakiwa alipe VAT ile hili sakata la muda mrefu.

Kwa hiyo imefika mahali hili Bunge na haya maneno ni mazito katika chombo hiki, lilifika hili suala Serikali itoe kauli, tulishaambiwa Bunge linalokuja, linakuja linakwenda, linarudi tunafika wapi? Kwa hiyo, hili suala liangaliwe, Mheshimiwa Waziri nilishajitahidi sana kumfuata anavyotaka yeye na Mwenyezi Mungu shahidi, nilishampa mpaka viongozi wakuu si vizuri kuwataja hapa kuzungumza nao hili suala linatusokota, hatutendewi haki na si suala hili tu la VAT la umeme bidhaa yoyote iliyotoka Tanzania Bara ikaingia Zanzibar VAT mara mbili. Nini maana ya VAT, nini formula yake tupeni definition ya VAT. Imekuwa tunasokotana tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitabu cha mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa kujumuisha mapitio ya hali ya uchumi, utekelezaji mipango na maendeleo ya mwaka 2017/2018 robo ya kwanza ya mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa uchumi ikiwemo mabenki uchumi, leo FNB Bank ina mwaka wa tatu, watu wanateseka tumeuliza kwenye chombo hiki mara nne, mimi mwenyewe mara mbili, tumefanya semina na watu wa Benki Kuu humu ndani wakatuambia muda si mfupi pesa zitapatikana wengine wameshatangulia mbele ya haki kwa Mwenyezi Mungu, sasa huku wanataka kuhujumu uchumi pesa zimebaki tu kule, na pesa dhamana ni Waziri wa Fedha kupitia Benki Kuu, hebu toeni ufafanuzi hizi pesa na sio kama benki imefilisika, pesa ziko wapi, Dutch Bank ya Ujerumani. Tunaambiwa zinaletwa, zinaletwa kwa mguu au kwa baiskeli na hazifiki mpaka leo, wananchi wanaumia Serikali ndio wananchi na wananchi ndio Serikali, hebu fikeni mahali mliamue hili suala.

Lakini jambo lingine wafanyabiashara wadogo wadogo wa Zanzibar wenye hata tv moja, simu tatu za mkononi wakafika Bandarini Dar es Salaam wanapata fatiki, wananyanyaswa na hesabu inaanzia moja hata hao matajiri wakubwa walianza na hesabu hii moja, wakafika mbili, wakafika tatu. Mtoto akizaliwa haendi mbio siku hiyo hiyo, hutambaa akaokotwa, akaanguka, akakamata ukuta. Sasa mfike mahali wafanyabiashara wadogo muwathamini. Bandarini Dar es Salaam kumekuwa usumbufu maana utafikiri unakwenda wapi, hakuna mvua, hakuna jua, hakuna usiku, hakuna mchana. Tufike mahali Waziri wa Fedha uwaonee huruma, na wao wanataka kupanda V8 hawa. Eeh hesabu inaanzia moja, mtoto hazaliwi akaacha ziwa siku hiyo hiyo. (Kicheko)

Mheshimwa Mwenyekiti, nije habari ya viwanda ukurasa wa 42 kama sikosei katika kitabu hiki maana itabidi twende kwa data sasa hivi. No! no! naomba Hansard ikae sawa 42 kuhusu udhibiti wa matumizi ya fedha za umma sio viwanda, matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar niipongeze sana Benki Kuu sana unajua tuseme ukweli penye ukweli tuseme ukweli katika watu wanaolipa kwa wakati 4.5 Benki Kuu, hili niwapongeze sana Waziri wa Fedha nakutuma unipelekee salamu kwa Gavana hili lazima tushukuru. Lakini hii 4.5 toka urembo ungali tunguja wazee wetu walikuwa wakijifunga vile vitu vya ajabu ajabu kwenye masikio sasa hivi dunia imekuwa, population ya Zanzibar imekuwa 4.5 hii haikidhi, ifike mahali izingatiwe barabara zimeongezaka, watu wameongezeka, vituo vya afya vimeongezeka, population imekuwa. 4.5 imepitwa na wakati, kwa hiyo, mfike mahali mzingatie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda vya Zanzibar. Nadhani itakuwa kengele ya kwanza kama sikosei.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana kwa kuniruhusu kuchangia bajeti hii muhimu ya Waziri Mkuu. Kabla sijaanza kuchangia kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu za kuweza kusimama hapa na kuchangia, uwezo huu si wangu, wala maarifa yangu, wala nguvu zangu, ni neema zake yeye Mwenyezi Mungu. Ndio pale aliposema katika kitabu chake kitukufu “Wakhulka l-insaanu dhwaif” maana yake tumemuumba mwanadamu kuwa ni dhaifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa dhati kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake kwa umakini wa hali ya juu kwa kutuletea ripoti hii. Namjua Mheshimiwa Waziri Mkuu umakini wake, lakini mchango wangu utalenga katika sehemu tatu: Kwanza sehemu ya Muungano; pili, sehemu ya Bunge; na tatu, TRA. Nitajikita zaidi kwenye Muungano ukurasa wa 81 ambapo tunakaribia kutimia miaka 55 ya Muungano wetu huu ambao ni mfano kwa dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muungano wetu huu ni matokeo ya mahusiano kihistoria kwa pande zote mbili, kwa hiyo hatuna budi kuheshimu na kulinda ili kuendeleza kudumu kwa faida ya watu wetu. Katika kuimarisha Muungano wetu Serikali zote mbili zinaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoukabili. Tarehe 21 Januari, 2019 kilifanyika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichohusu utozwaji wa kodi wa thamani (VAT) cha 0%. Hili jambo niendeleee kulishukuru tena kwa mara ya pili ndani ya chombo hiki na huu ndio Muungano, sio upande mmoja. Limepata suluhu na kiana yake niendelee kumshukuru sana Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa aliyofanya pamoja na Mawaziri

Mheshimiwa Naibu Spika, sitawafanyia haki Mheshimiwa January Makamba na Naibu Waziri wake katika sekta hii ya Muungano, Mheshimiwa Mussa Sima kama sitawapongeza kwa jitihada walizozifanya. Hata hivyo, kuna baadhi ya hizi kero za muda mrefu za 4.5%, kwanza naishukuru Benki Kuu kwanza hapa Waziri wa Fedha naomba a-take note hapa kidogo kwa faida ya wananchi wa Zanzibar; 4.53 toka dunia ilipoanza mpaka muda na mwanzo ilipokubaliana IMF, formula hii ni ya muda, sasa Zanzibar imekua, watu wameongezeka, mahitaji ya barabara yamekuwa makubwa, hii muingalie tena upya na hii ilikuwa ya muda 4.5. Zanzibar ishakuwa kubwa kupita kiasi kwa muda huu, ifike mahali walitatue tatizo hili, ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ajira katika sekta ya Muungano, upande wa Jeshi, upande wa Mambo ya Ndani, Migration, Polisi na Mambo ya Nje wanawashirikisha Zanzibar lakini waangalie formula nyingine, sasa hivi ajira imekuwa ngumu, pamoja na kuwa Tanzania bara ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la kusikitisha, formula iliyokuwepo zamani Marais wengi wamekuwa wakitumia, viongozi waliokuwa wakifika Tanzania Bara walikuwa wakifika Zanzabar, sasa hivi hatuwaoni. Hili niliombe, viongozi sitaki kuwataja, ni wengi wamefika Tanzania Bara, viongozi mashuhuri, lakini wengine hawafiki Zanzibar. Hili halileti picha nzuri, hili naomba sana ifike mahali viongozi wanaofika huku wawapeleke Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu bidhaa za Zanzibar kuingia katika soko hili la Tanzania bara, hiki ni kilio cha muda mrefu sana na wengine wameanza kufunga biashara zao. Itafutwe formula, maziwa hayafiki huku, sukari ipo Tanzania Bara, huku hailetwi, tunalinda viwanda vya Tanzania, sio vya Tanzania Bara. Tanzania ikiwepo Zanzibar, tuwe wakweli, tutafute formula itakayoweka sana. Zanzibar inategemea karafuu, ndio uchumi wake, ukiacha karafuu, pili ni utalii.

Mheshimwa Dau alizungumza pale hajui watalii wanaofika Zanzibar ni wangapi karibu laki saba kwa mwezi au zaidi ya hapo kama sikosei.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ifike mahali tuangalie formula hii inavyokwenda. Zanzibar kipato chake kikubwa sasa hivi ni utalii, tufike mahali tuangalie, watusaidie. Bidhaa inayitoka Zanzibar ikafika huku, suala hili tumepiga kelele muda mrefu jamani, waitafutie formula, TRA ni moja Tanzania. Leo hesabu inaanza moja ndio ije mbili. Mtoto akizaliwa leo hatembei siku hiyo hiyo hutambaa, akakamata kibambaza akaanguka, hili halileti picha nzuri jamani. Niombe sana suala hili liangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Tanzania mambo mengi Tanzania Bara imeiga Zanzibar bila kuficha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa nataka aliangalie na Benki Kuu awafahamishe, formula inayokuja ya Bureau De Change nasikia itakuwa ngumu na Zanzibar ni ndogo na inategemea sana utalii itawasumbua. Vigezo vya formula hii Tanzania Bara wameiga toka Zanzibar, waangalie masharti yatakayokuwepo yawe na uwiano.

Narudia tena Zanzibar itategemea utalii, watalii watapata shida, kwa hiyo formula ya Bureau De Change zinazokuja waziangalie ili angalau kuwe na uwiano, nafikiri hii formula itawasokota sana wananchi. Kwa hiyo, jambo hili waliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake tunamhitaji Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara angalau na sisi atutembelee, roho ina choyo, tunaomba sana. Kachanguliwa na Tanzania ikiwepo Zanzibar tunamwona kwa wenzetu, hili tunaliomba sana, tupelekeeni salam kwa wahusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jaku, lakini umezungumza lugha moja hapo kuhusu mtoto kushindwa kukimbia naamini hukukusudia kuita Zanzibar mtoto. Kwa kuwa hukukusudia hayo maneno kwenye Taarifa Rasmi za Bunge yasi…

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke hansard sawa unajua Kiswahili cha kwetu pwani mtoto akazaliwa haendi mbio siku hiyo hiyo hutambaa akakwetwa, maana yake haya mambo yawe na formula maalum kwa upande wa Zanzibar.

NAIBU SPIKA: Hiyo hiyo kauli ndio sitaki iingie kwenye taarifa rasmi za Bunge kwa kuwa Zanzibar sio mtoto wala hajaanza jana Muungano ni wa muda mrefu.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni hivyo au kama imefahamika hivyo nafuta kauli hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, nianze kwa ni-declare interest kwamba mimi ni mmoja wa wanaohitaji Muungano na Wazanzibar wengi wanauhitaji, lakini niformula tu ya kuuendesha muungano huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nichukue fursa hii kuwashukuru sana viongozi wetu wawili wakubwa; Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ushirikiano mkubwa wa kutatua tatizo la mazingira ya hali ya VAT ya umeme na tumefikia mahali muafaka; mwezi huu wa Aprili, aliwahi kuzungumza Mheshimiwa Najma hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa January Makamba, pamoja na kuambiwa na Mawaziri wenzake ni Mzanzibar, akubali hivyo hivyo. Ameonesha uwezo mkubwa sana katika Mawaziri ambao wameitwa Zanzibar wakafika kwa wakati, mmojawapo ni yeye. Haya ndiyo malezi mazuri binadamu anatakiwa kulelewa. Ameonyesha ushirikiano kwa hali na mali bila kujali mvua wala jua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitamfanyia haki Mheshimiwa Naibu Waziri wake tumemshuhudia sana katika kutatua matatizo hayo. Pia nitakuwa sijamfanyia haki ndugu yangu, jirani yangu Mheshimiwa Keissy. Nakushukuru sana kwa utulivu wake alioonesha kwa kipindi kirefu baada ya kero hizi za Muungano. Ametulia sana Mheshimiwa Keissy, namshukuru sana na huu ndiyo uungwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …nataka kuuliza…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …nini Muungano?…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Taarifa.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …maana ya formula ya Muungano?

MHE. ALLY K. MOHAMED: Nataka nimpe taarifa huyu.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …umuhimu wa kuungana ni watu kuwa pamoja, kushirikiana katika nyanja mbalimbali katika kuungana kiuchumi…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …ulinzi,…

MWENYEKITI: Taarifa

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: …maendeleo

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji, anasema mimi nimetulia muda mrefu. Mimi sikuwa napinga Muungano, nilikuwa napinga habari ya bidhaa kutoka Zanzibar ambazo hazilipiwi ushuru, ndiyo nilikuwa napinga. Mambo mengine mimi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jaku, unapokea taarifa hiyo?

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba afute kauli yake. Kule Wazanzibar wanalipa ushuru, vinginevyo kwa vyovyote vile kungekuwa hakuna Serikali pale bila kulipa ushuru. Naomba umruhusu afute kauli yake kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Siyo kauli ya kiungwana aliyoitumia. Hiyo siyo kauli ya kiungwana, yeye atetee mambo yake kule Nkasi; maji hakuna, barabara ndiyo vya kutetea. Wazanzibar wapo wenyewe wasemaji.Wakuu wa Dunia walishirikiana katika Jumuiya za Afrika Mashariki waliomba European Union kwa mashirikiano makubwa sana, lakini jambo la kushangaza na la kusikitisha, nije katika bidhaa za biashara hasa kutoka upande wa Zanzibar kuja kutafuta soko hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni geti kubwa la Bandari ya Tanzania Bara na ndiyo soko kubwa lenye walaji wengi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kati. Hili suala limekuwa ni la muda mrefu, vinginevyo labda ifutwe hii kauli. Kuna mahali Kenya inataka kwenda, Rwanda inataka kwenda na Burundi inataka kwenda, lazima ipite katika gateway kubwa hii ya Bandari ya Dar es Salaam. Sasa patafutwe njia. Hili suala limekuwa la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar wapo katika Jukuiya ya Afrika Mashariki, vinginevyo, watumwe Wabunge wetu wa Afrika Mashariki na Kati wapeleke hoja binafsi Zanzibar itolewe katika hili. Hili ni soko lenye walaji karibu milioni mbili na kuendelea. Hili ni jambo la kufikiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango lilitokea tatizo la Kenya, bidhaa za Kenya kuja huku ilikuwa maziwa sijui na cigarrete na bidhaa za hapa kwenda kule, tatizo likatatuliwa mara moja. Sisi ndugu wa damu. Mheshimiwa January utapa kazi kubwa sana haya mambo, lazima ufuatilie; na yote utakuwa masuuli hata kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni mambo ya kuyafikiria. Mmetatua kero za mbali za karibu mmeziacha! Lah, hii siyo halali, mlifikirie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, Mheshimiwa Dada yangu Mheshimiwa Saada aliyazungumza Mashirika ya Muungano. Kwanza naipongeza sana Benki Kuu. Katika Shirika linalotoa pesa wakati, BoT; 4.5 ile inapatikana kwake tofauti na Mashirika mengine. Mheshimiwa Naibu Waziri yupo, Waziri wako hayupo, hii 4.5 tulikuwanayo ya mkataba tu, ni ya muda. Zanzibar imekua, population imekua, IMF walitumia kutokana na kigezo cha watu lakini mlifikirie. Mheshimiwa January lifuatilie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mapato ya NBC, Zanzibar imo. Kuna Benki ya NMB, Zanzibar imo; kuna Postal Bank, Zanzibar imo; kuna TTCL, Zanzibar imo; kuna TCRA, Zanzibar imo; kuna TCAA, Zanzibar imo; imepata nini? Haya ni matatizo. Zanzibar imepata lini? Haielekei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira za mambo ya Muungano Mheshimiwa January; kuna Jeshi, kuna migration, kuna Polisi, kuna Mambo ya Nje. Mnapogawa hizi kazi mfikirie mtapeleka namna gani Zanzibar, zinahitajika, Ajira imekuwa issue. Muungano wetu keshokutwa Mungu akijaalia unatimiza miaka 55, twende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uchumi siyo suala la Muungano, ndiyo hoja yangu ilipo; Zanzibar ina haki yake ya kutumikia Wazanzibar wake na Tanzania Bara ina haki ya kutumikia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwanza na mimi kukushukuru kuniruhusu kuchangia mjadala huu ambao ni muhimu na ndio afya ya Serikali yetu, bila ya fedha huwezi kufanya kitu. Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake pamoja na Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mchango wangu kwa Serikali zetu hizi mbili ni sikivu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Bila kupoteza muda nianze na TRA, kwa kweli siku zote Mheshimiwa Rais kama hatukujipanga watendaji wa TRA nafikiri mko ndani mnasikiliza mchango huu, siku zote atabadilishwa Kamishina, itakuwa kama kubadilisha shati siku zote. Hapa pana uwajibikaji na utendaji, siku zote suala hili lina kazi. TRA mmekuwa midomoni mwa watu/ wafanyabiashara sana lakini niwaombe panapo haki ya mtu jaribuni kuangalia haki ya mtu, tusifikie TRA kutumia nguvu za ziada kumlazimisha mtu, kuku anataga yai moja huwezi kumlazimisha kutaga mayai matatu utamkosa mpaka yule kuku, kwa hiyo hili mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Murad alizungumza sana kuhusu Kariakoo, sasa hivi haipo limebaki jina tu, kutengeneza jina kuna kazi kuchafua ni mara moja. Kwa hali ya Kariakoo haipo, kurejesha kuna kazi sasa hivi, wafanyabiashara wengi washafunga virago kutafuta maslahi kwingine. Hili mkae na mliangalie TRA, hali si nzuri, kodi hizi zinakusanywa kwa viwango vyake na utendaji wake, tusitake kumuonea mtu wakati hana hatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wengine wanalazimishwa wasaini kabla hajaja kupelekwa mahakamani, kosa halijulikani, kuna mtu ana kesi ya mwaka 2010 mpaka leo, sheria ya TRA inasemaje miaka mingapi kufunga file? Tusifufue maiti wakati ilishaoza, hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu kubwa kuhusu Zanzibar kukopa hapa tutapiga kelele mpaka dakika ya mwisho Waheshimiwa Wabunge hasa kwa upande wetu wa Zanzibar. Kuna sheria ambayo ilipitishwa naomba kuinukuu ya tarehe 03 Machi, 2017; The Written Law Miscellaneous Amendment Act 2017; hii sheria kama Mwanasheria Mkuu yupo naomba akaiangalie haiko vizuri sana. Nasema kwa sababu zangu ninazozijua pamoja na kuwa na elimu yangu ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, amendment section two “The principal Act is amended in section 2, by (a) adding appropriate alphabetical order the following of definitions:

“Consolidated Fund” means Consolidated Fund of Government refered to in the Constitution;

“On-lending” means an arrangement whereby the Government borrows from the external or domestic source and thereafter passes on the loan of another entity such as Revolutionary Government of Zanzibar, parastatal organizations, local Government of any other public body corporate.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sheria haiko vizuri kwa maslahi ya Zanzibar na imepitishwa hapa sijui tulikuwa wapi. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hii tuliangalie, maana yake kwa haraka SMT inaweza ikakopa SMZ kama ni mashirika au halmashauri za mjini kukopeshwa, kwa hiyo ile ndoto yetu ya Mpigaduri pana kazi kubwa sana, tuwe wa kweli wajumbe hii angalieni sheria hii ikoje? Mimi elimu yangu ni ndogo. Kwa hiyo, mkopo ule kujenga bandari ile pana kazi kubwa kwa sheria hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, haitoshi nakwenda tena mbele; The principal Act is amended by repealing section 12 and replacing for it the following; Revolutionary Government of Zanzibar may, where arrangement between the Government and the lender requires on-lending arrangement enter into on-lending arrangement with...

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili; on-lending arrangement under subsection (1) shall be effected through on-lending agreement which shall, amongst other things, contain the terms and conditions of the primary kuna high and equally. Hii sheria bado ina kazi kubwa, vinginevyo tutapata matatizo sana Serikali ya Mapinduzi kukopa.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda hautoshi lakini hii sheria ina mambo mengi huko mbele angekuwepo Mwanasheria Mkuu hapa ningemkabidhi hii ingekuwa vizuri, lakini huko mbele ina marekebisho mengine, lakini nitakuletea copy moja ili uione kuna nyingine za Government, Loans, Guarantees and Grants Amendment Act ya mwaka 2003 nayo haiko vizuri kama nitaruhusiwa kuja na hoja binafsi nitakuja nayo na naomba kuinukuu; “The Minister shall, within three months prior to the commencement of fiscal year other than the fiscal year in which this Act comes into operation, cause to be prepared for approval by the Government; an annual Debt Strategy and borrowing plain ambayo sheria hii ni ni mazonge matupu, kwa hii sheria naomba iangaliwe vizuri ili Zanzibar waanze kujikomboa na si vibaya Serikali ya Jamhuri Muungano kutokana na uwezo wako wakaifikiria Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa na kilio tulipitisha sheria hapa ya TASAC (ya meli) lakini ninavyojua mimi mtu anapokamatwa, anatakiwa afuate sheria za sheria kama meli imekamatwa China itafuata sheria za nchi ya China, Zanzibar uchumi wake umekuwa mdogo, sasa ZMA imekuwa pale haina kazi kipindi hiki na usajili wa meli umeanza nafikiri Zanzibar kabla ya Tanzania Bara.

Kwa hiyo, mambo mengi narudia tena yale yale kwa Zanzibar imeanza mapema, kwa hiyo ifike pahali muangalie uchumi wa Zanzibar umekuwa ni mdogo, tufike pahali sheria tuiangalie ZMA imekwama kutokana na sheria ile, lakini sheria inasema meli inapokamatwa inahukumiwa na sheria za nchi, siwezi mtukakamatwa Oman akaletwa Tanzania akahukumiwa, anahukumiwa kule kule sheria na nchi hiyo, tufike pahali ili tuliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini njie na lingine niendelee kushukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondoa VAT na hatimaye kuwa sifuri na unaweza kuomba mambo mengi, lakini ukafanikiwa moja mengine yakaja baadae, niendelee kuomba tena umeme ule walionunua Tanga Cement, Twiga Cement na baadhi ya kampuni nyingine na bei niliyonunua Zanzibar karibu almost sawa, ukizingatia Zanzibar miundombinu ni yake mwenyewe ya baharini na ikaharibika anatengeneza kwa pesa zake. Kwa hiyo, hilo nalo mlifikirie na mlichukue, huwezi kuomba mambo yote kwa mpigo ukaja ukafanikiwa kwa wakati mmoja, hili mkae na mlifikirie, hali iko mashaka na duniani kote kuna bei ya rejareja na jumla kwa hiyo hili nalo mlizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nije kwenye suala la bidhaa za Zanzibar kuingia katika soko la Tanzania Bara; imekuwa kizungumkuti cha muda mrefu tufike pahali, hapa rafiki yangu Mheshimiwa Mwijage alipokuwa Waziri wa Viwanda na Biashara tulikuwa tukipigana vikumbo sana, leo tufikieni sukari ile ya Zanzibar pamoja na udogo wake kwani kuleta hapa kuna tatizo gani? Leo bidhaa za Zanzibar zimeingia kule hakuna question mark yoyote, leo bidhaa zinatoka Uganda, zinatoka Congo, zinatoka Zaire zinaingia bila vikwazo vyovyote. Zanzibar inategemea biashara tufike pahali napo hili mlizingatie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwnye suala la ajira za Muungano; hapa nilikuwa nikiomba kidogo papangwe formula maalum kuhusu ajira kwa sekta za Muungano, hiki ni kilio cha muda mrefu hakujawa na formula maalum mpaka muda huu. Kama ipo nafahamishwa ipo, kwa hiyo naomba nifute kauli yangu hiyo naambiwa ip, kwa hiyo ipo naomba kufuta kauli yangu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye mgao wa mashirika ya Muungano iiwepo TCRA, Posta, benki NBC na kadhalika nyingine mpaka muda huu hayo mashirika hayajatoa gawio.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizi nije kwenye suala la Zanzibar inategemea zaidi uchumi wake karafuu, Mungu ajalie ziweze kuzaa, lakini kukikosekana karafuu ni utalii; sasa hivi utalii umekuwa ukigwaya gwaya maana yake, ikiwemo sheria ya Wizara ya Fedha za Tanzania sheria mnazozitunga Tanzania Bara baadhi ya sheria muwashirikishe ndugu zetu wa Zanzibar, kuna sehemu zinawagusa, haziko sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kengele yako imelia, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama hapa. Huu sio uwezo wangu wala nguvu zangu wala ubabe wangu ni neema yake hii, na pumzi alizonipa hapa za kuniazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa fursa hii kuchangia muswada ulio mbele yetu, muswada muhimu na sijui niseme niilaumu Serikali kidogo kwa kuchelewa kuleta muswada huu. Muswada muhimu kwa wananchi, umechukua muda mrefu haujafika hapa, wananchi wakaendelea kuumia.
Mheshimiwa Nibu Spika, lakini vilevile nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Msaidizi wake Naibu Waziri, Dkt. Hamisi Kigwangalla, team captain wa timu ya Bunge kwa muswada huu.
Mheshimiwa Nibu Spika, lakini mimi ni mdau wa Kamati hii, lazima ni-declare interest. Sifa pekee za aina yake ziende kwa Mkemia Mkuu wa chombo hiki. Mkemia Mkuu amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu bila kujali mvua, jua, usiku mchana. Mkemia Mkuu hongera sana na usitegemee malipo kwa binadamu, tegemea malipo kwa Mwenyezi Mungu. Kazi uliyofanya Mheshimiwa Mkemia Mkuu ni kazi nzito sana katika mazingira mazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape pole sana watendaji wa kitengo hiki, wamekuja Kamati karibu mara nne, kwenda na kurudi hawapungui watu 20. Ndipo pale Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nilipotaka Mwongozo wako kwa vitengo hivi kwenda na kurudi, gharama ya mafuta, kulala, kula, kunywa, inakuwa ni gharama kuliko Bunge likabaki pale Dar es Salaam, ndicho kilio change hiki nilikiona muda mrefu na nilikuwa na Kamati jirani palepale, Wizara ya Ulinzi walikuwa wanakuja kwa ndege, gharama ni kubwa, tulifikirie hili suala kwa ajili ya kubana matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa nisichangie, nimekaa sana kwa kipindi kirefu kusikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge, lakini kazi hii yote mwisho wake ingekuwa bure. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize kwa makini hivi sasa na ukaanza ku-note hizi point ninazozungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, DNA Tanzania nzima ni moja. Tanzania na ukubwa wake tuliokuwa nao ni moja kwa utambuzi wa vipimo vya binadamu. At least Serikali itafute angalao DNA sita kwa Tanzania ili baadhi ya Kanda ziwekwe. Huwezi mtu kumtoa Mtwara kuja kufuata kipimo Dar es Salaam. Huwezi kumtoa mtu Arusha kuja kufuata kipimo Dar es Salaam! Kweli tunaitendea haki? Niliyazungumza haya Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwenye Kamati haya na yote ukayakubali kwa mdomo, si vitendo, sijui vitendo viko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mashine moja inahitaji angalao shilingi milioni 700 kwa utafiti niliofanya, lakini Serikali isiogope hasara kwa ajili ya wananchi wake. Serikali hii isingekuwa madarakani bila kuwa wananchi, wananchi ndio Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili, kwanza Serikali ibanwe itoe fedha haraka, ije sheria maalum ya kuibana Serikali kuhusu vyombo hivi vya DNA. Hatuwezi kuja kuzungumza maneno yote hapa wakati vitendea kazi hatuna, hii ni sawa sawa na kutwanga maji kwenye kinu, kazi yote hii itakuwa bure. Kama hawajawezeshwa hawa tunapitisha muswada huu kwa malengo gani? Ndiyo yale tunayosema tuna huruma kwa mdomo, sio kwa vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hapatoshi changamoto ya tatu, watumishi ni kidogo. Waliopo hivi sasa kwa mujibu wa taarifa niliyokuwa nayo kwenye Kamati ni 192, at least wapatikane watumishi 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio pale niliposema nilikuwa sitaki kuchangia, lakini kama sikuzigusa changamoto hizi tukiwa tunachangia muswada huu, wale watenda kazi watafanya kazi katika mazingira gani? Watu sita watafanya kazi gani? Watu 12 watafanya kazi gani Tanzania kutokana na ukubwa wake? Hata sisi Zanzibar tunaitegemea DNA hii, ndio ukweli ulivyo; mtu avuke bahari aje apime kipimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mazingira wanayofanya kazi ukiyaona utalia. Hiyo wafanyakazi 208 wapatikane hivi sasa tukijaliwa. Hapa nitahitaji maelezo Mheshimiwa Waziri, watu 400 wanahitajika, wafanyakazi wako 192, hapa nitahitaji maelezo yakutosha, majengo ya Kanda hayapo. Kama mfano Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, huu mji mpya mnaotaka kuufanya sasa hivi, Dodoma, hatujawa tayari. Changamoto hii Mheshimiwa Waziri nitahitaji maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, nimuombe Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini Waheshimiwa kama nitawakera kidogo niombe radhi hasa akinamama kuhusu nywele zetu hizi kidogo za kubandika, zina mitihani jamani, zina maradhi. Nazungumza kwa nia njema kabisa, haya mambo nimeyapata mimi kwenye Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali kama itawezekana kabla ya kuondoka kesho ukatupa semina bure siku ya Jumamosi kuhusu namna ya kubandika hizi nywele, zina maradhi Waheshimiwa. Niombe radhi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa dakika hizi za majeruhi. Mchango wangu utakuwa mdogo sana kwa hizi dakika ulizonipa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Balozi Seif Idd na Waziri Mkuu kwa jitihada alizozichukua lakini vilevile nitakuwa sijamtendea haki dada yangu Jenister Mhagama kwa suala hili. Nizipongeze kabisa Serikali mbili hizi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kukiondoa kifungu cha 2(2). Ni jambo la kulipongeza sana tena sana kabisa kwa usikivu, vinginevyo kingepita hivi wananchi wale wa Pemba na wa Darajani wangeumia kwenye majahazi yao na wana majahazi wale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wangeshindwa kusajili hata uwakala ule ungekwenda zake, wangeumia sana sana na unajua ajira zilivyo. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri hiki kifungu kweli hamkukiona? Hii ofisi ina Wanasheria wangapi? Kuna Makatibu wangapi Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Spika, ahsante nimekusikia. Huu Muswada nathubutu kuapa kwamba Zanzibar hawakushirikishwa, lakini kuna Miswada mingine muifikirie kama wa TTCL umekuja dakika za mwisho kwenye Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo jambo hili lifikiriwe.

Mheshimiwa Spika, lakini nije katika kifungu cha sita (6), hiki kifungu kinafanana na cha 11, NASACO huyu huyu atakuwa Wakili, NASACO huyuhuyu atakuwa Jaji? Hebu iangalieni sheria hii, huyu ndio atazikagua meli huyuhuyu atakuwa wakala wa meli, patakwenda kweli, ni kitu cha kuzingatia sana, haiwezekani mtu mmoja ukampa majukumu mawili, hata kanuni zetu za uchaguzi zinasema kule kuwa mtu mmoja huwezi kumpa kazi mbili.

Mheshimiwa Spika, Zanzibar wana Zanzibar Maritime Authority ambayo imepitishwa mwaka 2006, lakini SUMATRA wana kifungu chao kinaitwa Shipping Act ya mwaka 2003, kila mmoja ana sheria yake sasa kufika mahali na hapo nakumbuka mimi, walikuwa wakishirikiana lakini cha kusikitisha cha kutia huruma hizi sheria zikifika na za Wazanzibari washirikishwe kwenye mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo kuna suala la bandari, tumelipigia kelele humu juzi. Bado Wazanzibari wanasumbuliwa bandarini, ule mchele pale ukafika unapokewa, utafikiri unapewa heshima, pana kitu unapimiwa lakini nafikiri kipo kisheria, hebu aliangalie Mheshimiwa Waziri, mwenzetu angalau anapanda bombadier lakini pale pana usumbufu bandarini, pembeni ukifika unapewa heshima zote na wafanyakazi. Ule mzigo wako unapimiwa kisha unalipishwa, kitu cha ajabu kwelikweli.

Mheshimiwa Spika, kutengeneza jina kuna kazi, kuliharibu ni mara moja’ kutengeneza jina kuna kazi lakini
kuharibu ni mara moja. Hizi sheria tuziangalie, hapo zamani meli pale Msasani zilikuwa zikijaa kuja kwenye bandari ya Dar es Salaam, tulikuwa tuna kazi nzuri kupita kiasi lakini sasa zimeshaanza kupungua hebu tujiulize kulikoni kuna tatizo gani? Tusiwe tunatengeneza sheria tu baadaye zikaja zikatubana wenyewe, tuangalie nini athari yake na nini faida yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kuunga hoja mkono hoja.