Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jerome Dismas Bwanausi (14 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii ya Waziri wa Fedha.
Kwanza, niwashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Lulindi ambapo katika uchaguzi uliopita nilishinda Ubunge kwa asilimia 87. Siri kubwa ya ushindi katika uwakilishi kwa wananchi ni kupunguza maneno na kufanya kazi na kuondoa kero kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zote anazoanza katika kuhakikisha Taifa hili linaelekea kwenye uchumi wa kati, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapa pole sana wapiga kura wangu kwa maafa waliyopata kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika vijiji vya Matogoro kule Msanga, Mkangaula, Lupaso na maeneo mengine ambayo sikuyataja, nawapa pole sana na nataka kuwahakikishia kwamba nipo pamoja nao katika mkasa huu uliowapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda moja kwa moja katika hoja, nianze kuzungumzia kuhusu mapato. Kwanza, nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa jinsi ambavyo imejipanga kuhakikisha kwamba tunakusanya mapato ya kutosha ili tuweze kwenda kuondoa kero za wananchi ambapo kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri huduma kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Wizara ya Fedha na watendaji, baadhi ya watendaji wengi hapa nchini wanashindwa kuwa wabunifu wa vyanzo ni kwa sababu wenyewe wanaendelea kupata riziki yao kwa maana ya mshahara na wanaendelea kupata pensheni baada ya kustaafu, wako tofauti kabisa na taasisi za binafsi ambapo wenzetu wamekuwa wabunifu sana. Mimi naomba sana tuhakikishe tunakuwa wabunifu na kupata vyanzo vipya vya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho chanzo kikubwa sana cha mapato ambacho hatukitumii cha property tax. Mheshimiwa Mnyika atakubali kule Dar es Salaam tunazo nyumba nyingi sana kama zingeweza kulipa property tax vizuri na tukawaweka katika makundi mawili, wale ambao tunaweza kutathmini nyumba zao lakini wale ambao tunaweza kuwaweka katika kundi la ukadiriaji na tukakadiria katika kiwango ambacho mwananchi anaweza akalipa, ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Naomba Wizara na Halmashauri ziweze kuona ni jinsi gani tunaweza tukakusanya mapato kutoka kwenye chanzo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuziwezesha halmashauri zetu kuweza kukusanya mapato ni jambo lingine. Kwa mfano, Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi, tarehe 23 Januari, 2013 nilipata janga kubwa sana la watu waliovamia Halmashauri na kuchoma magari 11 lakini pia kuchoma ofisi tano. Serikali ilituahidi kwamba halmashauri yetu ingeweza kupata fidia ya shilingi 1,337,000,000/= lakini tangu mwaka 2013 hadi sasa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo, hata viwango tunavyopangiwa kukusanya tunapata ugumu mkubwa sana. Namwomba Waziri wa Fedha, namuona Naibu yupo, hebu chukueni jambo hili ili kuhakikisha kwamba Halmashauri hii inapata fidia ili tuweze kununua magari, tuweze kutengeneza majengo yale ili ifanye kazi yake inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala zima la barabara. Barabara ni jambo muhimu sana na sisi wote tunajua. Kwa mikoa ya Kusini sisi ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho na moja ya barabara ambayo ni ya kiuchumi ni ile inayotoka Mtwara – Newala - Tandahimba - Masasi kupitia Lulindi. Barabara hii imeahidiwa na Mheshimiwa Rais na ipo kwenye Ilani na tayari kuna dalili za kuanza kujenga barabara hii.
Naiomba sana Wizara ya Fedha na Wizara ya Miundombinu kuhakikisha katika miaka mitano barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni barabara ya Ulinzi. Katika miaka mitano iliyopita tumezungumza sana juu ya barabara ya Ulinzi ambayo inapita kwenye zaidi ya Majimbo manne. Jimbo Mtwara Vijijini kwa Mheshimiwa Hawa Ghasia, kwa Mheshimiwa Mkuchika, kwa Mheshimiwa Katani kule Tandahimbi, kwangu kwenye Jimbo la Lulindi na kwa Mheshimiwa Dua kule kwenye Jimbo la Nanyumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ilikuwa na madhumuni makubwa mawili, kwanza ilikuwa ni barabara ya ulinzi. Wakati ule tunapigana na Mreno kule Msumbiji barabara hii ndiyo ilitumika vizuri sana kuhakikisha kwamba tunapambana naye. Pia tulianzisha vijiji vya ulinzi katika barabara yote hii lakini vijiji vile vyote havipati huduma ya barabara kwa sababu tuliiombea iingizwe kwenye TANROADS lakini hadi sasa Wizara haijakubali. Namuomba sana Waziri anayeshughulika na Wizara hii ya Miundombinu tuhakikishe kwamba barabara ile tunaiweka TANROADS ili iweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka nilieleze ni suala zima la umeme. Nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Muhongo, tulikuwa wote kwenye Kamati ya Nishati na Madini, kwa kweli kazi yake kila mmoja wetu hapa tunakiri ni kazi iliyotukuka, hongera sana Mheshimiwa Profesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa ameeleza hapa kwamba wanatagemea kwenda Mtera kufanya tathmini ya REA I na REA II, yako mambo ambayo ningeomba mkayazungumzie. Kwanza, ni kwamba kwenye REA I na REA II idadi ya wananchi wanaotakiwa kupewa umeme kwa bei ya shilingi 27,000/= ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji. Kwa hiyo, jambo hili ni muhimu sana mkalizungumzie ili kuhakikisha kwamba idadi ile inaongezeka kulingana na hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ambalo limejitokeza ni kwamba wakati vijiji vinavyowekwa kwenye mradi wale wanaokwenda kufanya survey wanaacha vijiji vya katikati bila kuviingiza kwenye mpango, jambo ambalo linatusumbua sana wakati mpango ukiendelea. Ningeomba sana Profesa hili mkalishughulike kwa nguvu zenu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari kengele ya kwanza imeshagongwa, nichukue fursa hii kuzungumzia suala la viwanda. Kule Kusini zao letu la korosho linahitaji kuongezewa value lakini itategemea na jinsi ambavyo tutaanzisha viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri mwenye dhamana afanye juhudi katika miaka mitano hii kuhakikisha kwamba viwanda vya korosho vinafufuliwa katika Mikoa ya Kusini ili korosho ipewe thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuokoa muda, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nianze tu kwa kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze kwenye sekta ya kilimo ambayo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imo kuanzia ukurasa wa 26 hadi 32. Nijikite kwenye zao la korosho. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, ndugu yangu Majaliwa Kassim, kwa kazi kubwa sana aliyoifanya wakati alipofanya ziara kule Ruangwa na kutoa tamko la Serikali la kuondoa tozo tano ambazo zilikuwa ni kero za wananchi, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tatizo la korosho ambalo ni zao la pili kwa kuiingizia pato Serikali yetu, ukiacha tumbaku ambayo ni ya kwanza. Lakini hali ya wakulima wetu Mheshimiwa Waziri Mkuu anajua, hali za wakulima wetu ni hali mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna sakata linaloendelea katika Wilaya ya Masasi ambalo wakulima hawajalipwa fedha zao kati ya shilingi 200 hadi shilingi 400 kwa kila kilo, lakini hadi sasa kuna wingu ambalo halieleweki wakulima wale watalipwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linawafanya wakulima wetu wawe katika mazingira magumu sana. Wanahangaika, wanapalilia, wanapulizia, wanakwenda kuokota korosho zao, wanapeleka kwenye Vyama vya Msingi, vinakwenda kwenye Vyama Vikuu na hadi pale kupata soko, lakini baadhi ya wachache wakiwemo baadhi ya Maafisa Ushirika ambao siyo waaminifu wanashirikiana na baadhi ya Viongozi wa Bodi za Wakulima wa Vyama vya Msingi kuwaibia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa Wilaya ya Masasi safari hii tumesema tunahitaji fedha walipwe wakulima, nani amechukua, ameziweka wapi, hiyo siyo hoja yetu! Ninamshukuru sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Mwigulu baada ya mazungumzo naye amekubali kufanya ziara kwenda Masasi kujionea hali halisi na ninaamini kabisa kwa utendaji wake mzuri ataweza kuwaridhisha wakulima wale na kuwapa matarajio na mategemeo makubwa jinsi ambavyo Serikali inajitahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ili kuwasaidia wakulima wa korosho katika mikoa yote ambayo inalima korosho ni lazima kufanya reshuffle ya Maafisa wa Ushirika. Maafisa wa Ushirika waliokaa katika Mkoa wa Mtwara sasa wamekaa wengine zaidi ya miaka 10 wengine miaka 15, katika mazingira hayo wanatengeneza mtandao wa kutengeneza hata Bodi za Wakulima kule kwenye Vyama vya Msingi na kuhakikisha wanajipatia kipato kutokana na hali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanyie kazi hili kwa nguvu zake zote ili kumfanya mkulima sasa ajengewe matumaini kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ni Serikali inayowajali wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sekta ya afya. Nimesoma kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesisitiza sana jinsi ambavyo Serikali itajitahidi sana kuhakikisha kwamba inaboresha sekta ya afya, nimueleze tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa hivi ameelekeza kwenye ukurasa wa 55 kwamba tujitahidi sana tuhakikishe tunawahamasisha wananchi waweze kujiunga na Bima ya Afya. nimthibitishie tu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo zimeshaanza kufanywa na wananchi wamehamasika lakini nina mashaka juu ya jambo hilo, kukakatishwa tamaa wananchi kwa sababu wamekata Bima, lakini wanapokwenda kwenye zahanati zetu hakuna dawa! hivyo hawaoni umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kama hawapati dawa kwenye zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ijikite kuhakikisha kwamba haya yote yanakwenda sambamba, tunahamasisha suala la Bima ya Afya, lakini tunaongeza dawa kwenye zahanati zetu na watendaji wetu ili wananchi wawe na uhakika kwamba wakienda zahanati wanapata dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka niliseme ni juu ya suala la barabara. Mheshimiwa Waziri Mkuu umeelezea juu ya jitihada ya Serikali jinsi ambavyo itaimarisha sekta ya barabara lakini nataka tu nikuhakikishie Mheshimiwa kwamba wananchi wanaimani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano sana, haya yote mnayoyasema na mnayotuambia tunakubali kwamba awamu hii mambo mengi yatatekelezwa, lakini nasisitiza suala la barabara kutoka Mtwara - Newala - Tandahimba hadi Masasi ambayo ni barabara ya uchumi. Napenda Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ujenzi atekeleze agizo la Mheshimiwa Rais alilolisema ataweka wakandarasi wanne ili kuhakikisha barabara hiyo inamalizika kwa haraka ili kutatua tatizo lililoko pale. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maelezo hayo ambayo umetupa matumaini lakini kuna suala la barabara ya kutoka Masasi kwenda Nachingwea ambayo inaunganisha hadi Ruangwa hadi Nanganga kwenye Jimbo la Mheshimiwa Waziri Mkuu. Barabara hii tumeisemea muda mrefu, kwa kweli kuna kila sababu barabara hii ijengwe. Ni barabara muhimu inaunganisha mikoa miwili, ni barabara ya uchumi na kwa hakika wewe mwenyewe huwezi kujisemea, sisi lazima tuseme kwamba barabara hii sasa tunataka ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nijikite katika eneo hilo lakini pia nimalizie kwenye sekta ya elimu. Mimi niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu bahati nzuri alikuwa mwalimu. Naamini kilio cha walimu sasa kitapewa kipaumbele. Kilio kile ambacho kwa kweli muda mrefu wao wamekuwa wakilalamikia kuhusu marupurupu yao, kuhusu nyumba, kuhusu stahili zao nyingine, hatutegemei Serikali ya Awamu ya Tano walimu wawe ni sehemu ya manung’uniko kama ilivyokuwa miaka mingine.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hili lipewe kipaumbele ili Walimu waweze kupewa umuhimu katika jamii na ndiyo sekta ambayo inaajira pekee kuliko sekta nyingine na Walimu ni wengi naamini kabisa Serikali hii na Walimu wameshaanza kuwa na imani, tuendelee kuwapa imani zaidi ili wafanye kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hotuba ya Waziri Mkuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kunipa nafasi na mimi ili ukayasikie tena mambo ya korosho.
Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, lakini pia Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Watendaji wa Wizara kwa jinsi ambavyo mmejipanga kurudisha imani katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua juhudi za Mheshimiwa Waziri Mwigulu ambazo anazifanya na wananchi wana imani kubwa sana kwa jinsi ambavyo ameonyesha njia na mipango thabiti ya kuhakikisha kwamba wakulima na wavuvi wanaanza kuneemeka kwa kupata kipato kizuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sakata la korosho Masasi. Mheshimiwa Waziri, mimi niendelee kukushukuru na ninamshukuru sana Mrajisi, namshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara, ndugu yangu Turuka kwa kuanza kulichukulia kwa umakini mkubwa suala la sakata la korosho katika Wilaya Masasi. Mheshimiwa Waziri, sakata hili ambalo wewe mwenyewe umeahidi kwenda kulisikiliza kule, takriban zaidi ya shilingi bilioni tatu, wakulima wale hawajuwi watazipata lini. Mchezo huu wa kuwadhalilisha wakulima na kuwanyima haki zao haujaanza leo. Ni wa miaka mingi, lakini mwaka huu Mheshimiwa Waziri wamekufuru kuchukuwa hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa umakini wa Serikali ya Awamu hii ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye amesema Serikali hii ni ya kuwajali wanyonge na watu ambao wako kule chini, ninao uhakika kabisa kwamba Serikali itaingilia kati suala hili na kuhakikisha wakulima wale wote ambao wanaelekea kudhulumiwa wanalipwa stahili zao inavyostahili! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelipokea sana kwa shangwe kubwa tamko la Waziri Mkuu juu ya kupunguza zile tozo, lakini nataka kutoa angalizo, wananchi wamefurahi sana kuona jinsi ambavyo korosho sasa zitaweza kuuzwa kwenye maghala yao. Kama hatukujipanga vizuri kuhakikisha bodi inaweka watalaam wa korosho kule katika kila ghala kuangalia ubora wa korosho kwa kuziweka katika grade zinazostahili na kuhakikisha zinawekwa vizuri, tutajikuta baadaye tunakwama katika suala zima la soko la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni imani yangu katika miezi hii michache iliyobaki, Bodi ya Korosho kwa kushirikiana na Mfuko, lakini pia kwa kushirikiana na Wizara, ijipange vizuri. Umebaki muda mfupi, tujipange vizuri ili azma ya Serikali ya kumfanya mkulima wa korosho apate bei nzuri mwaka huu iweze kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana Wizara hii ijielekeze sana katika kuhakikisha kwamba Mfuko wa Wakulima wa Korosho unajielekeza kutumia zaidi kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya korosho kuliko matumizi ya kawaida. Ingewezekana kabisa, bodi kwa kushirikiana na Mfuko ikaongeza fedha kwenye ruzuku ya mbolea na kuwafanya wakulima wengi zaidi wapate punguzo la bei ya pembejeo kuliko ilivyo sasa. Na mimi naomba sana Mfuko wa Wakulima wa Korosho ni lazima ufanye kazi yake kwa uwazi zaidi kuliko ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotolewa kupelekwa kwenye Mfuko wa Wakulima wa Korosho ambayo inatokana na export levy ni fedha nyingi sana, lakini sijuwi kama Serikali inaziangaliaje fedha zile tunazozipeleka kule kwa maana ya kuzikagua, lakini kuhakikisha kwamba matumizi yasiyo ya lazima yanaepukwa ili ule Mfuko ufanye kazi yake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye suala zima la kilimo katika Bonde la Mto Ruvuma. Kama kuna maji ambayo hatuyatumii mpaka yanaelekea baharini ni maji ya Mto Ruvuma. Yale maji tungeweza kuyatumia kwa kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili bonde lile litumike kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula, lakini yale maji yote yanatiririka kwenye bahari na wala hatuna mpango wala scheme kubwa ya kuhakikisha kwamba maji yale tunayatumia. Naomba sana Mheshimiwa Waziri katika mipango yako hebu tujaribu kuangalia uwezekano huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu Maafisa Ugani. Katika kipindi changu cha siasa nimefanya kazi kwenye ngazi za chini, kuanzia chini kabisa; Mwenyekiti wa Mtaa, Diwani, Meya hadi sasa. Nilichobaini ni kwamba Maafisa Ugani wengi tunawalipa mishahara bila kufanya kazi. Ni lazima wale Maafisa Ugani tunaowapeleka kwenye Kata, Maafisa Kilimo na Maafisa Mifugo, waonyeshe mpango wa kazi. Unamkuta wakati mwingine baadhi ya maeneo, siku Mheshimiwa Mbunge unakwenda ndiyo na yeye anajitambulisha mbele ya wananchi. Wananchi hawamjui! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima Wizara isimamie kuhakikisha wale Maafisa Ugani kule chini kwa kweli wanafanya kazi, lakini kuwe na utarabu hata wa kwenda kuwakagua shughuli gani ambazo wanazifanya za kila siku katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika wananchi wangependa sana kuendelea na mfumo huu ambao hivi sasa upo wa pembejeo za ruzuku. Naiomba Wizara, kama haijajipanga vizuri, utaratibu huu wa kusambaza pembejeo za kilimo kwa maana ya ruzuku usitishwe mpaka mtakapojipanga vizuri! Hakuna sababu Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuwapa wachache wanaoweza kutumia zile fedha kwa njia za udanganyifu! Hakuna sababu! (Makifi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawakala wengi sio waaminifu hata kidogo! Wenyewe wanashirikiana na baadhi ya wachache ambao sio waaminifu katika vijiji kusaini kwamba wamepokea mbegu pamoja, ambapo hawakufanya hivyo, yaani hawapokei! Wanakwenda kuziuza tena zile pembejeo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia. Wizara ya Kilimo kama haijajipanga vizuri kwa muda huu mfupi kabla ya msimu ujao wa kilimo, iache, isubiri mwakani ikijipanga vizuri! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja Masasi. Naomba katika mahitimisho yake atuthibitishie Wanamasasi kwamba lini tunakwenda ili kukutana na wananchi wale ili tuwaondelee matatizo waliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru nami kuwa miongoni mwa Wabunge ambao wanachangia hotuba hii ya Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu wake na watendaji wa Wizara ya Maji kwa jinsi ambavyo mnafanya kazi sasa kwa kujituma ili Watanzania waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wengine wanaosema kwamba tatizo siyo Waziri, tatizo ni upatikanaji wa fedha katika Wizara hii. Katika bajeti ya mwaka jana 2015/2016 ni asilimia 19 tu ya fedha ambazo zilipangwa kwenda Wizara hii zilipelekwa. Niwaeleze Waheshimiwa Wabuge kwamba hata hizi fedha mnazoziona sasa hazitokani na fedha za miradi ya maendeleo zilizopangwa, hizi ni fedha zinazotokana na Mfuko wa Maji ambao Waheshimiwa Wabunge tuliopita tuliuanzisha mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kama kweli tunataka maji yapatikane na tuweze kupata fedha zetu kutoka Wizara ya Fedha bila vikwazo ni lazima tuongeze fedha kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetoa ushauri na mapendekezo kwamba angalau mwaka huu tozo ya kwenye mafuta kutoka shilingi 50 iwe shilingi 100, kwa hakika Waheshimiwa Wabunge, tuunge mkono hili ili tuhakikishe Mfuko wa Maji unapata fedha za kutosha, hizi ndiyo fedha za uhakika ambazo zinaweza kututoa na kutuhakikishia kwamba tunapata maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyejua umuhimu wa maji katika Taifa letu, maji ni muhimu na hapa Mheshimiwa Gekul amesema maji kwanza na kwa vyovyote vile lazima tuhakikishe kwenye bajeti hii tunapata fedha za kutosha ili fedha zipelekwe kwenye miradi na tunapata maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Jimbo langu la Lulindi, kwanza ninaishukuru sana Wizara kwa kuutengea fedha mradi wa Chiwambo, ambao upo kwenye Jimbo langu la Lulindi kule Masasi, bahati mbaya mradi huu hii ni bajeti ya tatu mradi haujakamilika, ni imani yangu Serikali hasa Wizara kwa kipindi kilichobaki cha miezi miwili kuelekea mwisho wa bajeti na ziko kila aina ya dalili kwamba Wizara ya Fedha huenda ikakusanya kufikia asilimia 100 kwa fedha za ndani. Ningeomba mradi huu sasa ukamilike ili wananchi wa Kata saba na vijiji zaidi ya 30 waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya vijiji kumi ambapo kila Jimbo tunalo, kila Mkoa ipo. Katika Jimbo langu kuna mradi wa Chipingo, mradi wa Shaurimoyo, mradi wa Mkululu, ningependa kuona miradi hii Wizara inaitekeleza ili kuhakikisha kwamba wimbo wa vijiji kumi au mradi wa vijiji kumi sasa unakwisha ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona kwenye miradi ya umwagiliaji katika Mkoa wetu wa Mtwara, nina uhakika hata Mkoa wa Lindi, ningeomba tuhakikishe kwamba tunakuwa na scheme za umwagiliaji kandokando mwa Mto Ruvuma, maji ni mengi, yote yanaingia baharini, ni imani yangu kabisa kwamba Wizara tukijipanga vizuri kwenye suala la umwagiliaji, kilimo kinaweza kukuzwa kandokando ya Mto Ruvuma na kuwafanya wananchi wanaoishi katika Mikoa hii hasa kandokando ya Mto Ruvuma wanufaike na kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie kwamba wote tunakuombea na Wizara tunaiombea ili ikamilishe azma ya kuhakikisha kwamba kila eneo ambalo linahitaji maji liweze kupatiwa maji. Hata tunapozungumzia suala la viwanda, maendeleo ya kilimo, suala la maji ni la kipaumbele cha kwanza. Kwa hiyo, Wizara ijipange upya ihakikishe kwamba inakuwa na usimamizi bora wa fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri. Hivi sasa miradi ile inasimamiwa na Halmashauri kwa asilimia kubwa zaidi kuliko Wizara, ninaomba Wizara iweke kitengo cha usimamizi wa miradi ya maji katika Halmashauri zetu, isisitize suala la ubora wa vifaa vinavyonunuliwa kwenye suala zima la maji. Kwa sababu yako maeneo, miradi imefanyika, lakini inadumu kwa muda mfupi kwa sababu vifaa vilivyotumika, mabomba, viunganishi na mambo mengine yanakuwa hayako katika kiwango kinachostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na fedha hizi zinazotengwa tunapeleka kule safari hii zaidi ya shilingi bilioni 900, lakini kama hakuna usimamizi, na hakuna uangalifu kuhakikisha kwamba vifaa vinavyonunuliwa vinakuwa kwenye kiwango kinachostahili, hakika hatuwezi kupata mafanikio kama tunavyotarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie pia mradi mkubwa ulioko Masasi, mradi wa Mbwinji. Mradi huu umeigharimu Serikali zaidi ya shilingi bilioni 51, ningeomba shilingi bilioni moja iliyotengwa kila mwaka ihakikishe ile shilingi bilioni moja ipelekwe, tunataka tuone kwamba katika bajeti hii inayoishia ya 2015/2016 kiasi kile cha shilingi bilioni moja kilichopangwa kiende ili kiweze kufanya kazi ya kusambaza maji vijijini.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niyaeleze hayo lakini msisitizo mkubwa ni kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwa kauli moja tuhakikishe tunaunga mkono, suala la kuongeza shilingi 100 ili iwe tozo ya kuhakikisha kwamba tunapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa kupata fursa hii kama mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.
Nianze tu kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya na kuonesha uzalendo wa hali ya juu katika kuhudumia Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, la pili, namshukuru sana mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa jinsi alivyotoa hotuba yake na jinsi alivyojaribu kuchambua maeneo mbalimbali yanayohusiana na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, labda niende moja kwa moja, lakini pia bila kuwasahau Waziri anayeshughulikia Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu wake, ndugu yangu pale Mheshimiwa…
SPIKA: Mavunde!
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hiyo.
Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye kilimo na hasa kwenye ukurasa wa 23 wa kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu, alipozungumzia zaidi suala la stakabadhi ghalani. Nianze tu kwa kusema, kwa kweli Sheria ya Ushirika inabidi tuombe mamlaka zinazohusika zilete sheria ile tena, tuifanyie marekebisho kwa sababu sheria ya ushirika ina upungufu mwingi sana na kusababisha wananchi wetu
kupata athari mbalimbali katika kupata haki zao katika mazao yao.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana kabisa na hoja ya Waziri Mkuu kwamba maeneo mengi, stakabadhi ghalani imeonekana moja kwa moja kuwa ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya masoko katika mazao yetu mbalimbali, ikiwemo kahawa, chai, tumbaku, pareto, korosho na mengineyo.
Nitolee mfano zao la korosho; tatizo kubwa lililojitokeza kufanya wakulima wetu wasipate haki vizuri ni tatizo la vyama vya msingi na vyama vikuu wakati mwingine kufanya kwa makusudi kabisa hujuma ya kuiba fedha za wakulima.
Mheshimiwa Spika, nikitolea mfano, wananchi walipeleka zao lao la korosho kwenye maghala tangu Septemba mwaka 2016, lakini ninavyosema hivi sasa, kwenye Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi kiasi cha zaidi ya sh. 1,200,000,000/= hazijalipwa kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, jambo hili linawakatisha tamaa wananchi na ndiyo maana nimesema ile Sheria ya Ushirika inabidi tuitazame upya, kwa sababu wenzetu wanaopata mamlaka kwenye vyama vya msingi na vyama vikuu wamegeuka kuwa miungu watu na kuona kwamba wao
wana uhuru uliopitiliza kana kwamba wanaishi kwenye himaya tofauti na Watanzania wengine.
Kwa hiyo, ombi langu kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni kwamba hebu iingilie kati kuona jinsi gani wananchi hawa wanavyoweza kupata haki zao, kwa sababu kwa kweli ni jambo ambalo wananchi hawalielewi, kwa sababu hakuna korosho zilizopo kwenye maghala lakini fedha zao
hazionekani zipo wapi.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la tozo kama alivyozungumzia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Serikali mwaka huu imepania kuhakikisha kwamba inaondoa baadhi ya tozo kwenye mazao mbalimbali ya biashara yakiwemo tumbaku, chai, kahawa pamoja na korosho.
Bahati nzuri mimi ni miongoni mwa wanaotoka kwenye maeneo yanayolima zao la korosho; Masasi ni Wilaya ya pili kwa uzalishaji ukiachia Tandahimba. Kwa kweli tunampongeza sana Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wameshiriki katika kufanya zao la korosho kwa
mwaka huu liweze kufikia kilo moja sh.3,800/=. Naamini kabisa Serikali ikiendelea kukaza uzi korosho zinaweza kuwa na uwezo wa kuuzwa sh. 5,000/= kwa kilo katika misimu ijayo.
Mheshimiwa Spika, naomba sana katika tozo zile ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu amezisema, lakini napenda kwa mfano tozo ya magunia ambayo kwa kweli inatozwa kwa wakulima, nadhani iondolewe pamoja na zile nyingine ili kumfanya mkulima aweze kupata unafuu zaidi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningetaka niliseme, ni juu ya masuala ya umeme. Bahati nzuri ameelezea Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake kwamba Serikali ina nia nzuri ya kusambaza umeme, lakini napenda sana ieleweke kwamba wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa sababu ambazo hata Mawaziri wanazijua kwamba maeneo haya yaliachwa kupewa huduma za umeme tangu mwanzo kwa sababu kulikuwa na tetesi kwamba Mkoa huu wa Mtwara na Lindi ulikuwa uhudumiwe na kampuni ambayo ilianza pale kusambaza gesi. Kwa hiyo, baadaye Serikali iliamua kusitisha makubliano yale na TANESCO kuendelea kuhudumia mikoa hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tatizo ambalo lipo ni kwamba maeneo, vituo au Wilaya za Mkoa wa Mtwara na Lindi hazina magari. Hata magari yaliyoletwa hivi karibuni, hayakusambazwa tena katika mikoa hii vizuri na kufanya utendaji wa kazi katika Mkoa wa Mtwara na Lindi hasa Wilaya ya Masasi kuwa mgumu sana kiutendaji kwa sababu hawana usafiri. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali
ione kwamba eneo hili linahitajika kutazamwa vizuri zaidi. Naipongeza suala la REA Awamu ya Tatu, kwamba linazinduliwa katika mikoa, lakini nataka tu nitoe angalizo kwa Serikali kwamba kama Mkoa wa Mtwara na Lindi haukutazamwa vizuri, unaweza ukajikuta maeneo mengine
yote nchini yamemaliza vijiji vyake, lakini Mtwara na Lindi vikabaki kwa sababu kule hatukuwahi kupata ile phase one
na wala zile fedha za MCC kwa ajili ya umeme hazikupatikana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukienda kwa uwiano ulio sawa, basi mikoa hii bado itabaki nyuma. Kwa hiyo, naomba sana hata katika usambazaji umeme, katika maeneo ambayo umeme ulipita muda mrefu, utakuta maeneo ya Mkoa wa Mtwara na Lindi bado maeneo mengi
sana umeme umepita lakini wananchi hawajanufaika.
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la reli. Naomba sana hii reli ya kutoka Mtwara kwenda Mchuchuma na kama Mheshimiwa Nape alivyokuwa analalamika kwamba maeneo mengi yamewekwa ‘x’ lakini hatuoni zile juhudi za hasa za kuhakikisha kwamba kweli reli hii inataka ijengwe
hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Maliasii na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumpongeza sana Profesa Maghembe; Naibu Waziri, Injinia Makani; Katibu Mkuu na Watendaji wa Wizara kwa kuanza kuonesha sura mpya ya Wizara na kuanza kuleta matumaini mapya kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Wizara, Mheshimiwa Waziri Profesa Maghembe na wenzake kwamba juhudi zinazoendelea hivi sasa za kutatua migogoro walioyoikuta ziongezwe kasi ili kuwe na mahusiano mema kati ya Wizara na wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Pia niitahadharishe Wizara siyo vema kuanza kutafuta migogoro mipya kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakala wanaoshughulika na mambo ya misitu wamepewa jukumu la kwenda kutathmini mipaka ya hifadhi za misitu, lakini nimwombe na kumkumbusha tu Mheshimiwa Waziri kwamba zoezi hili halikuwa limefanyika kwa zaidi ya takribani miaka 20 iliyopita,
kinachotokea hivi sasa ni baadhi ya maeneo kuanza kuzalisha migogoro kutokana na zoezi hili. Mheshimiwa Waziri nitolee mfano tu kwenye Jimbo langu la Lulindi tunayo hifadhi ya msitu ya Njawala, lakini tunavyo vijiji vinavyozunguka katika eneo hili, ambavyo Vijiji hivi vya Njawala, Mchoti na Mtona ni vijiji ambavyo vipo tangu miaka 20 iliyopita, katika zoezi hili vijiji vile vinaambiwa vimo ndani ya msitu, sasa inaleta kero kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha basi ni vizuri kueleza wataalam wetu wasiende kuanzisha migogoro mipya. Nilipokuja katika Bunge hili nimemletea Mheshimiwa Waziri barua na wamenituma nimwombe Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge atembelee maeneo ya Jimbo la Lulindi ili akajionee hali halisi katika maeneo haya, naamini atanikubalia ili tukayasikilize na kuyatatua matatizo haya tukiwa kule site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kulichangia ni tatizo kubwa sana la wanyama hatarishi na wanyama ambao wanawadhuru wananchi. Tangu niingie katika Bunge hili 2010 nimekuwa nikilalamika sana juu ya Wizara kutotilia maanani matatizo yanayotokana na mamba wanaoshambulia wananchi katika Jimbo langu la Lulindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuliwahi kufanyika utafiti kama miaka minne iliyopita na utafiti ulifanywa na wenzetu wa Wizara ya Maliasili, wakabaini kwamba katika Mto Ruvuma hasa eneo langu la Jimbo la Lulindi, mamba ni wengi zaidi ya 300 wapo katika eneo lile. Kulitolewa ahadi, ya kuwapunguza mamba wale lakini kwa masikitiko makubwa katika miaka minne tu wananchi wa Jimbo langu na Watanzania 35 wameshapoteza maisha na zaidi ya watu 50 wamekwishajeruhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tunayo Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), nichukue fursa hii kuilalamikia sana TAWIRI, najiuliza labda makao makuu yapo mbali sana na Mtwara yako Arusha, katika kipindi chote cha Ubunge wangu sijawahi kuwaona TAWIRI wakija kutembelea maeneo yaliyoathirika katika Majimbo yetu. Kikubwa ambacho wanakatisha tamaa ni kwamba sisi tunasikiliza maelekezo yanayotolewa na Shirika la Wanyama Duniani kwamba lazima tuwalinde wanyama wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hebu awape matumaini wananchi wale ambao wanaishi kandokando ya Mto Ruvuma, vijiji hivi ni vijiji vya ulinzi, kuna Vijiji vya Mapili, Mduhe, Maparawe, Mkoo, Sindano na Mgwagule wananchi hawa katika kipindi chote hiki wameishi kwa maisha ya shida mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshafika ofisini kwa Mheshimiwa Waziri mara nyingi na tumezungumza, kwamba moja ya suluhisho la kuwasaidia wananchi wale ili wasiathirike na tatizo la mamba ni kupunguza idadi ya wananchi wanaokwenda kuchota maji na huduma zote za maji kutoka kwenye mto ule. Tunao mfuko hapa unaoshughulika na wanyama pori, tunayo mifuko mingi inayoshughulika na wanyama pori, inazo fedha, kwa nini Wizara isihakikishe kwamba inasaidia vijiji vile kupata maji ili tupunguze idadi ya watu wanaokwenda kutumia maji kutoka Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namfahamu Mheshimiwa Profesa Maghembe, Naibu Waziri Engineer Makani na Katibu Mkuu kwamba ni wasikivu sana, naamini atakapokuwa anahitimisha kwenye hotuba yake atawaambia ndugu zangu wale Lulindi ni jinsi gani Wizara yake itakavyolichukulia suala hili kwa uzito mkubwa na kuhakikisha katika bajeti hii ya 2017/2018, tunatenga fedha kwa ajili yakuchimba visima vinane kwenye vijiji hivi ili kuwasaidia wananchi wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaacha kusema aliyosema aliyetangulia kutoa maoni yake. Mheshimiwa Waziri hili tamko tunalotaka kuendelea kupewa msisitizo la kuzuia mkaa kutoka eneo moja kwenda lingine ni lazima litazamwe upya. Bado hatujafika wakati ambapo nishati mbadala zinaweza kutosheleza badala ya mkaa. Namwomba sana hili jambo la kuhifadhi misitu ni jambo muhimu sana, nakubaliana nalo sana kwa asilimia mia moja, lakini twende taratibu, kuagiza tu mamlaka zote zianze kuzuia mikaa kuingia mijini kwenda wapi, wakati mitandao ya gesi hatujaikamilisha, ni jambo ambalo hapana, hili jambo tutaonekana tunakurupuka na litaleta athari kubwa sana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana kwa sababu hili jambo linagusa maisha ya wananchi wetu wengi wa vijijini na maisha ya wengi wa mijini, jambo hili lisitishwe mpaka pale ambapo tayari tutakuwa na nishati nyingine ambayo wananchi hawa wanaweza wakatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa sina tabia ya kupenda kugongewa kengele, naamini haya ambayo nimeiambia Wizara, nimeiambia Serikali na hasa kwa wananchi wale ambao wanapoteza maisha, yatazamwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki cha mvua huwa hakuna matukio makubwa ya mamba kuwavamia wananchi, kwa sababu maji yamejaa, wako katikati ya maji marefu, lakini kuanzia Julai hadi Desemba kila siku tunapokea taarifa ya vifo vya wananchi. Mheshimiwa Waziri wale ni Watanzania sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kuwaambia Watendaji kwamba, wakiwa wanang’ang’ania taarifa zinazotolewa na jumuiya ya Kimataifa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Serikali. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Mpango na Dada yangu Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kazi nzuri wanazozifanya na kutuletea bajeti ambayo imejenga matumaini makubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano kwa jinsi anavyofanya kazi. Nami nataka niseme tu, hii ni zawadi kwa Watanzania. Kama ambavyo nchi nyingine wanatamani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais katika nchi nyingine, sisi wote kwa pamoja tunatakiwa tuienzi hii tunu ambayo tumepata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoeleza Mjumbe aliyetangulia kusema hapa Mheshimiwa Bura, kwamba ziko taarifa kwamba yako matumaini makubwa ya kupata zile fedha ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anazisema, nashauri hizi fedha zikipatikana, basi baadhi ya sehemu kubwa ya fedha hizi zielekezwe kwenye mradi wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuzungumzia suala la uchumi bila kuhusisha suala la upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu. Tulipendekeza kuanzia kwenye Kamati ya Bajeti lakini pia kwa Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba tungeweza kupata Sh.50/= kwa kila lita ya mafuta ili iende kwenye maji, lakini bahati nzuri imetengwa Sh.40/= kwa kila lita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa hizi fedha sasa zielekezwe kwenye maji ili ziweze kwenda kutusaidia kuwafanya Watanzania waweze kufanya kazi nyingine na kuhakikisha kwamba maji yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye uti wa mgongo wa Taifa letu ambao ni kilimo. Naishukuru Serikali kwamba imefanya juhudi sana za kuondoa tozo na kwenye korosho Serikali imeamua kwa mara ya kwanza kabisa kutoa sulphur bure kama ruzuku kwa wakulima wa korosho. Sasa isiishie tu kwenye kuondoa tozo, ni lazima tuelekee pia kwenye kuwatafutia masoko bora wakulima wetu ili waweze kupata masoko mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitembelewa na viongozi wengi hapa nchini akiwemo Waziri Mkuu wa India; na alipokuja alizungumza na Serikali na alizungumza na Mheshimiwa Rais, akatoa matumaini kwamba Serikali ya India iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kununua aina zote za Kunde kwa maana ya choroko, kunde na mbaazi. Naomba Serikali iharakishe suala la mazungumzo na Serikali ya India. Hivi sasa Wakulima wa Wilaya ya Masasi na Mkoa mzima wa Mtwara kwa ujumla, waliitikia wito wa kulima mazao haya na choroko sasa ndiyo zinavunwa lakini bei imeshuka kutoka Sh.1,200/= hadi Sh. 400/= kwa kilo. Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na juhudi ya kuondoa tozo kwenye mazao, lakini ihakikishe tunapata soko zuri la mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ninaotaka kuutoa kwa Serikali; hivi karibuni Kamati ya Bajeti ilipata nafasi ya kuzungumza na wenzetu ambao wanatusaidia misaada kutoka nje. Jambo ambalo limeonekana kuchelewa kupata misaada ya nje ni kwamba tunawatoza VAT, fedha zinazoletwa hapa nchini kwa misaada ya maendeleo, jambo ambalo Mataifa yanayotoa misaada yanakataa, kwamba sisi tunatoa misaada kuwaleteeni ninyi kwa maendeleo, kwa nini mtukate VAT? Kwa hiyo, naiomba Serikali hili suala liondolewe ili kuwafanya wafadhili wetu walete zile fedha zao bila vikwazo. Sasa tunalalamika kwamba fedha haziji kumbe tatizo ni kwamba Serikali zile wamesita kuleta kwa sababu sisi tunawatoza VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nichangie ni juu ya Serikali kuona umuhimu wa kupeleka milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizi zinahitajika sana kule, lakini iko haja ya kutazama pia upya jinsi ya kuzipeleka fedha zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri badala ya kwenda kuwagawia mmoja mmoja kwa ajili ya miradi midogo midogo, ni vizuri kuchagua mradi mmoja katika Kijiji na zile fedha zikatumika shilingi milioni 50 kwa ajili ya kusaidia kwenye maendeleo ya kile kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka nichangie kwenye bajeti hii, lakini kabla sijamaliza kuchangia nirudi kwenye kilimo kuwapongeza sana Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ole Nasha, wanafanya kazi kubwa sana na Watanzania wana imani nao sana kwenye Sekta ya Kilimo. Naamini kabisa wataongeza bidii ili kuhakikisha wakulima wanaweza kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye Sekta ya Viwanda. Ni lazima Serikali sasa tujielekeze kwenye suala la viwanda kwa moyo wa dhati kabisa na dhamira ya kweli. Tunavyo viwanda ambavyo kama tungevifufua tungeweza kuongeza uchumi wetu kwa kiasi kikubwa sana likiwemo zao la korosho. Tunavyo viwanda ambavyo vilijengwa, viwanda vile vikachukuliwa na baadhi ya watu wakisema watavifufua, lakini hadi sasa hawajafufua. Ni vizuri tukavifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naipongeza Serikali kwa kuwasaidia wakulima wa zao la tumbaku ambao kwa muda mrefu walikuwa wanalia, lakini naamini sasa wale wa Urambo, wale wa maeneo yote yanayolima tumbaku sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango na Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa hakika kwa Wizara hii kutupiwa lawama ni jambo la kawaida kwa sababu ni Wizara ngumu na hasa ukizingatia kwamba fedha tunazozipata hazitoshelezi kufanya kila jambo kwa wakati tunaohitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye suala la mapato. Naona bado kabisa tuna mianya ya ukusanyaji wa mapato. Nikianza na mfano mdogo tu, bahati nzuri niliwahi kuwa Dar es Salaam pale, suala la Property Tax, kiwango tunachokusanya hakifanani na hali halisi ambayo tungeweza kupata. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, akae vizuri na watu wa TRA ukusanyaji wa fedha hizi ni mdogo sana. Pia hata suala zima la kukadiria, suala la malipo ya hizi fedha za Property Tax haziko katika kiwango kinachostahili. Kwa hiyo, naomba sana kwamba suala la ukusanyaji mapato katika kila eneo ambalo linatakiwa zikusanye lifanywe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sasa hivi ukienda katika petrol stations zetu nyingi, kila petrol station karibu wiki nzima hii nikipita wanasema zile mashine zimeharibika. Kwa hiyo, kuna kila dalili kwamba katika miezi hii tutakosa mapato mengi. Naomba tu nimshauri Mheshimiwa Waziri, hivi haiwezekani badala ya kufunga zile mashine wale wafanyabishara wakubwa wa mafuta wanaomiliki vile vituo wakatozwa kodi moja kwa moja kule wanakonunulia mafuta ya jumla badala ya kuweka hizi mashine ambazo kila wakati zitakuwa zinaonekana zimeharibika. Nadhani tuangalie mfumo bora utakaosaidia ili huyu mlipa kodi alipe vizuri na Serikali ipate kipato chake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nichangie kuhusiana na mapato ni suala la kilimo. Tunakwenda kuua zao la korosho ambalo lilikuwa linaipatia Serikali fedha nyingi sana. Nina mashaka sana inawezekana walioko Hazina pale kuanzia Katibu Mkuu na wengine ambao wana mamlaka hawaijui korosho vizuri. Ndiyo maana zile fedha zikija wanaona hakuna sababu ya kurudisha kule. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, fedha hizi zirejeshwe kwa wahusika wakulima ili ziweze kuzalisha tena. Kwa sababu fedha hizi kama hazitoki kwa ajili ya pembejeo, unategemea msimu ujao wakulima wale watazalishaje zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kule suala la kuanzisha vitalu vile vya kupata mbegu mpya. Wale wote walioandaa zile mbegu bora za korosho ambazo zimesambazwa hawajalipwa hata senti tano na walitumia fedha zao na wengine walikopa benki. Mimi nakubali kwamba ni kweli kuna baadhi yao inawezekana hawakuwa wakweli katika jambo hili lakini huo uhakiki ukishamalizika, basi wale ambao wanatakiwa kulipwa waweze kulipwa fedha zao, sasa uhakiki unafanyika lakini fedha hazirejeshwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza hapa kwamba zao hili linahitaji utafiti na zile fedha zilikuwa zinarudi kule zinakwenda kwenye utafiti. Kwa maana hiyo Chuo cha pale Naliendele kitakufa, hawawezi kufanya utafiti kwa sababu hawapati fedha ambazo walikuwa wanapata kutoka kwenye Bodi ya Korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kabisa kwamba kuna baadhi ya fedha zilikuwa zikirudi kule hazitumiki vizuri. Nashauri uhakiki ufanyike ili zile fedha zirudishwe ili ziweze kuleta tija katika zao hili la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka nizungumzie ni juu ya viwanda. Bahati nzuri na Waziri wa Viwanda yupo, suala la kubangua korosho na kuweka thamani ya korosho ni jambo muhimu sana. Hili jambo tumelizungumza sana sioni progress, sioni kama kuna jambo la msingi linafanyika, tunawanufaisha wenzetu wa nchi za India ambako tunapeleka korosho ghafi, sisi tunategemea kuuza korosho ghafi. Viwanda vipo na ilitakiwa kwanza wale ambao wamechukua wavirejeshe Serikalini ili tupate wawekezaji watakaobangua korosho, lakini hivi sasa hakuna suala lolote la msingi ambalo linafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumzia ni juu ya ugatuaji wa madaraka kurejesha kwenye Serikali za Mitaa. Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi ambazo zimefanya vizuri sana katika Afrika katika suala zima la kushusha madaraka kwenye Serikali za Mitaa. Hivi sasa naona kila Wizara inataka kuchukua mamlaka zote zilizoko kwenye Serikali za Mitaa zirudi Wizarani kwao. Kwa hali hii, Serikali za Mitaa zinakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, enzi ya Mwalimu waliwahi kuzivunja Serikali za Mitaa lakini baadaye umuhimu wa Serikali ya Mitaa ulionekana na zilirejeshwa. Tusifike huko kuziua tena Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nilikuwa nashauri kwamba kama tunawaondoa Maafisa Ugani wote kule na wanarudi katika Wizara zao, lazima tutengeneze muundo mpya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutengeneze muundo mpya ambao utafanya Mabaraza ya Madiwani yafanye kazi, lakini kwa sasa katika utaratibu huu Mabaraza yale hayatafanya kazi vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nishiriki katika mjadala wa hotuba hizi za Mawaziri wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana kwanza kumpongeza Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Selemani Jafo na Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Kakunda na Kandege kwa kazi kubwa sana wanayoifanya. Sifa kubwa waliyonayo Mheshimiwa Selemani Jafo na Mzee George Mkuchika, ni kwamba ninyi ni wasikivu sana kwa Waheshimiwa Wabunge. Wanawasikiliza lakini pia ni wafuatiliaji wazuri katika shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Watendaji wanaofanya nao kazi Mhandisi Iyombe, Naibu Makatibu Wakuu wanawasaidia, lakini pia na Ndugu Seif ambaye ndiye mteule katika kusimamia TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa ku-declare interest kwamba nimekuwa sasa Mwakilishi wa wananchi kwa miaka 22. Katika miaka 22 hii nimekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kwa miaka mitano, nimekuwa Diwani kwa miaka kumi, Nimekuwa Meya kwa miaka mitano na sasa ni Mbunge kwa miaka saba. Kwa hiyo nimekuwa TAMISEMI kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye kada ya Wenyekiti wa Serikali za Mitaa na Vijiji na Madiwani. Naishauri Wizara kwamba msingi wa Serikali ni kuanzia kwenye ngazi za vijiji na mitaa, lakini uboreshaji wa maeneo haya umekuwa siyo kwa kasi kubwa. Nashauri kwamba posho za Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ni muhimu sana, kwa sababu viongozi hawa wamekuwa wakifanya kazi kwa masaa 24 na ndiyo viongozi wanaokaa na jamii. Maeneo mengine ambako Maafisa Watendaji wa Vijiji ama Mitaa hawapo wao ndio walinzi wa amani, kwahiyo ni muhimu sana tukazingatia kuhakikisha na maeneo ya hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye maeneo ya Madiwani. Waheshimiwa Madiwani ndiyo wasimamizi wa mabilioni ya fedha tunayoyapeleka kwenye Halmashauri zetu,
lakini posho wanazozipata zinafanya wakati mwingine Waheshimiwa Madiwani sasa wawe ombaomba hata kwa Watendaji. Kwa hiyo, inakuwa ngumu sana kusimamia kikamilifu katika maeneo hayo, nashauri kwamba ni vizuri sana tukaangalia. Pia suala zima la mafunzo ya viongozi hawa wakichaguliwa wanakaa miaka miwili au mitatu hawajapata semina yoyote. Ni vizuri sana viongozi hawa wakapata semina ili kuhakikisha watende kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili napenda kuchangia ni sekta ya afya. Waziri Mheshimiwa Jafo na Watendaji wake na Wasaidizi wako nadhani wameandika na wanaendelea kuandika historia ya kwamba ni Viongozi waliosimamia kikamilifu katika suala zima la kuhakikisha ujenzi wa vituo vya afya, lakini pia ujenzi wa hospitali 67 za Wilaya, lakini pia upatikanaji wa dawa katika mahospitali yetu na zahanati zetu. Haya ni mambo ambayo wote tunayaona na tumpongeze Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimkushukuru sana Mheshimiwa Jafo na Serikali kwa kuwakumbuka wananchi wa Wilaya ya Masasi hususani Jimbo la Lulindi kwa kupata hospitali ya Wilaya, tunawashukuru sana. Katika hilo nina ombi kwa Mheshimiwa Jafo na Serikali kwamba katika kituo cha afya cha Nagaga ambacho nilikielezea kwamba kilipata tatizo la gari lake la wagonjwa kuungua moto miaka saba iliyopita, hakijapata gari tena, hivyo kupelekea tatizo kubwa sana katika maeneo hayo hasa wagonjwa kuwapeleka mbali katika hospitali ya Wilaya. Naomba sana katika mgao ujao wa magari, hebu tufikirie kupeleka gari katika kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye TARURA. nampongeza Mkurugenzi ama Mtendaji Mkuu wa TARURA Ndugu Seif kwa maandalizi ambayo yanaendelea kwenye TARURA. Hata hivyo, nitoe angalizo tu kwamba kama hawatapata fedha za kutosha itakuwa ni wakala pekee hapa nchini tuliouanzisha ambao hautaleta tija. Tumeshuhudia wakala zote REA, TANROAD zinafanya vizuri, lakini hapa tunahitaji papatikane fedha za kutosha ili waweze kukidhi haja na matarajio ya Watanzania kuhusu eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la watumishi mpaka sasa wameazimwa tu kutoka kwenye Halmashauri wawe pia na watumishi wao ambao wataweza kukidhi kusimamia suala hili. Vile vile kama TARURA hatukuwapa fedha za matengenezo ya kawaida za barabara kwa sababu barabara hizi ambazo TARURA wanakwenda kuzifanyia kazi ni barabara ambazo nyingi ni za changarawe na mvua ikinyesha huwa barabara hizi nyingi hazipitiki. Kwa hiyo kama hawatapata fedha za maintenance maana yake barabara nyingi hapa nchini hazitaweza kupitika hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni eneo la migogoro na kero mbalimbali za wananchi kwenye maeneo yetu. Uzoefu wangu mdogo ndani ya TAMISEMI unaonesha kwamba baadhi ya Halmashauri zetu Watendaji hawafuatilii kero za wananchi na matokeo yake sasa hivi Waheshimiwa Mawaziri wakienda kutembelea, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais ni mabango chungu mzima yanayoonesha matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba sana Mheshimiwa Jafo aimarishe kitengo cha ufuatiliaji wa kero za wananchi ili zipungue hata yeye anapokwenda kule asianze kukumbana na mabango kwa sababu huo ni upungufu unaoonesha kwamba watu hawajawajibika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo nataka kuchangia ni juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Uzoefu unaonesha kwamba liko tatizo kweli la kucheleweshwa fedha na Serikali imejitahidi kwamba wamefikisha asilimia hizo 49,asilimia 50, lakini tukumbuke tu kwamba bado mwaka wa fedha haujausha bado tuna miezi mitatu, tuiombe Wizara ya Fedha ikamilishe ule upungufu wa fedha ambazo zilikuwa hazijaenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa pia kwa miradi kunatokana na baadhi ya Watendaji kutoharakisha michakato ya kupelekea uanzishaji wa miradi. Kwa mfano, suala zima la kutangaza tender, kuhakikisha kwamba Mzabuni anakuwa awarded inachukua muda mrefu sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba za hizi Kamati ambazo zimewasilishwa hapa. Nianze tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyofanya kazi na kwa kweli ni mfano wa Marais bora katika Afrika ambao wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwenye afya, pongezi hizi ambazo nimempongeza Mheshimiwa Rais na sisi sote hapa pande zote mbili, upande wa Chama Tawala na wale wenzetu wa Upinzani ni mashahidi kwamba katika miaka ya nyuma haijawahi kutokea tukaweza kutenga fedha kwa ajili ya hospitali 67 na vituo vya afya 350. Hii haijawahi kutokea, tunahitaji kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama walivyochangia wengine haya majengo tunayoyajenga, hospitali 67 na vituo vya afya 350, kama havikupata watumishi, kwa kweli vituo hivi vitabaki kama white elephant, yatabaki majengo ambayo hayana tija. Nisisitize sana wanaohusika na maandalizi ya kuwapata watumishi wa Idara ya Afya waweze kufanya jambo hili kwa haraka sana ili tuweze kupata tija katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, pia niiombe tu Serikali, sisi wa Mkoa wa Mtwara kuna ujenzi unaoendelea wa Hospitali ya Rufaa lakini unasuasua sana. Nipongeze kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu wake ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Ndungulile, mnafanya kazi kubwa sana na wala hatuna mashaka na utendaji wenu wa kazi lakini naomba sana mlitupie macho suala la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa pale Mtwara. Kwa sasa wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi wakihitaji kumpeleka mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa wanawajibika kuja Dar es Salaam. Kwa hiyo, naomba sana hili jambo lipewe kipaumbele, najua Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa mchango wake ataeleza kuhusu jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilitaka kusema, ni kweli huu utaratibu wa Serikali tuliouanzisha wa kuwaondoa watumishi kwa mfano wa kilimo, maji na ardhi na kuwapeleka kwenye Serikali Kuu ni mzuri. Jambo hili ni jema kwa sababu inawezekana likawa linasaidia kuweka udhibiti wa watumishi wetu. Hata hivyo, kwa maana ya uwakilishi (Madiwani na Wabunge), nikubaliane na hoja na Mheshimiwa Mwamoto kwamba kweli tulipitisha hapa hizo sheria lakini kuna wakati mwingine unaweza ukakuta liko jambo ambalo lina umuhimu sana.

SPIKA: Waheshimiwa wenye kikao pale, nawaombeni sana.


MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, napendekeza Usirudishwe utaratibu wa zamani wa kwamba kila jambo linaongelewa kwenye Baraza lakini lazima kuwe na baadhi ya vikao hata kama ni kwa miezi sita au kwa mwaka ambavyo vitafanyika kwenye Halmashauri ambapo mchango wa Waheshimiwa Madiwani na Wabunge kuhusu barabara, maji na kilimo unaweza kupewa umuhimu. Kwa sababu kama wataachiwa tu watendaji peke yao wakafanya maamuzi sasa ule uwakilishi wa wananchi kutoka kwenye ngazi mbalimbali hautakuwa na maana kabisa. Kwa hiyo, hili naomba sana litazamwe Serikalini na tuone mfumo gani mzuri utakaosaidia kuhakikisha kwamba na wale wawakilishi wa wananchi wanapewa fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa pia suala la TARURA kwenye Kamati ya TAMISEMI na mimi naunga mkono kabisa yote yaliyomo katika taarifa ya Kamati ile. Hata hivyo, kama TARURA haikupata fedha za kutosha, watu watakuja kusema afadhali ya Halmashauri kuliko TARURA. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwenye bajeti ijayo TARURA wapate fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna tatizo kubwa sana la barabara vijijini na madaraja ambayo yanahitaji kujengwa lakini kwa fedha wanazopata TARURA hawawezi kujenga madaraja hayo kabisa. Kwa hiyo, ni vizuri sana TARURA iweze kupata fedha za kutosha ili washirikiane na TANROADS kuhakikisha kwamba suala la barabara na madaraja linapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu sana ni juu ya kuziwezesha Halmashauri zetu zijiendeshe zenyewe. Hali kwenye baadhi ya Halmashauri ni mbaya sana na nitatoa mfano wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi na Halmashauri nyingi ambazo zaidi ya asilimia 80 ya mapato yake zinategemea kutokana na ushuru wa korosho, hali ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Madiwani hawajapata posho zao za mwezi sasa takribani miezi nane hata posho za vikao hazijatolewa na miradi mbalimbali hakuna kinachofanyika. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshalieleza kwamba Serikali ipo kwenye mpango sasa wa kuhakikisha kwamba ushuru wa korosho kwa ajili ya Halmashauri unapelekwa, kwa kweli fedha zile zinahitajika zipelekwe haraka sana ili kunusuru hali ya Halmashauri zetu ambazo hivi sana hali ni mbaya kuliko maelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kusisitiza ni kwenye Kamati ya UKIMWI. Wafadhili wetu wamekuwa wakitusaidia sana kwenye eneo hili lakini baadhi ya wafadhili wetu wamekuwa wakijiondoa taratibu katika kuchangia kwenye janga hili la UKIMWI. Niiombe Serikali sasa ione uwezekano wa kuanza kutenga fedha zetu za ndani ili zisaidie katika kupambana na janga hili. Kama hatuwezi kutenga fedha zetu za ndani itatusumbua sana mbele ya safari pale wafadhili wetu watakuwa wameachia kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kulinda muda wako, niunge mkono hoja za Kamati zote zilizowasilishwa, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kwenye hotuba ya Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Waziri wa Nchi anayeshughulikia mambo ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Nimemshangaa sana ndugu ya Mheshimiwa Ngombale pale alipotamka kwamba anaitaka Serikali iwaombe radhi wakulima wa korosho. Mimi nasema Serikali haiwezi kuomba radhi ila inapaswa kupongezwa kwa hatua iliyoichukua kwa kuwanusuru wakulima wa korosho. Mheshimiwa Ngombale yeye analima ufuta, nimeshangaa sana anaposema habari ya korosho na Wilaya Masasi ambayo natoka mimi ndiyo Wilaya ya pili kwa uzalishaji nchini baada ya Tandahimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyolishughulikia suala la korosho na kuwasamehe wale ambao walinunua kinyume na utaratibu almaarufu kama ‘kangomba’. Tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tunashuhudia jinsi wananchi wanavyojitokeza kwa wingi, nimeona mkutano wa pale Mufindi, Iringa, Mtwara, Namtumbo, kwa kweli Watanzania wana imani kubwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Nadhani vyama vya upinzani mwakani itabidi wajitafakari kuona kama kuna sababu ya kumweka mgombe Urais kwa sababu kwa hali ile navyoiona sidhani kama kutakuwa na mgombea yeyote atakayeweza kushindana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

WABUNGE FULANI: Aaaaaa.

MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana jirani yangu Waziri Jafo na wasaidizi wake ndugu yangu Mheshimwa Kandege na Mheshimiwa Waitara kwa kazi kubwa mnayoifanya TAMISEMI, hongereni sana. Mheshimiwa Jafo namfahamu siku nyingi sana na wengi tunamfahamu pale alipokuwa Plan International aliwahi kuwa mfanyakazi bora lakini Bunge lililopita tulimchagua Mheshimiwa Jafo kutuwakilisha kwenye Bunge la SADC. Mheshimiwa Anne Makinda aliwahi kusimama hapa akasema anatuwakilisha vyema baada ya kupewa Kamati kule kwenye SADC, tunakupongeza sana. Kwa hiyo, haya unayofanya TAMISEMI ni mtiririko wa utendaji kazi wako uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri, Kapteni Mstaafu George Huruma Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa, msaidizi wake katika Wizara hii. Tunapongeza tuna maana, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, yeye ni kati ya wachache ambao wapo madarakani waliowahi kuteuliwa kwa nafasi mbalimbali kuanzia DC, RC hadi Waziri katika vipindi vyote vya Marais watano walioongoza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Baba wa Taifa alimteua kuwa DC na Mheshimiwa Rais Mwinyi akamteua kuwa DC baadaye Mzee Mkapa akamteua kuwa RC. Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete na Mhehimiwa Dkt. Magufuli wote wammeteua Mzee huu kuwa Waziri katika awamu zao. Kwa hiyo, kwa kweli tunampongeza kwa utendaji wake mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la TAMISEMI, hii ni Wizara ngumu sana. Bahati nzuri nimekulia TAMISEMI, nimekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Diwani kwa miaka 10, Meya na sasa Mbunge, naifahamu TAMISEMI ni ngumu sana. Kwa mfumo Mheshimiwa Jafo, Manaibu, Katibu Mkuu na watu wa TAMISEMI kwa ujumla sasa haitembei bali inakimbia kwa utendaji wenu wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya elimu wengi wamezungumza sitaki kurudia sana lakini nikuombe Mheshimiwa Jafo pamoja na juhudi ambazo zimeendelea kufanywa hasa katika Jimbo la Lulindi kama nilivyokuwa nikieleza mara kwa mara kwamba sasa hivi kituo kinachofanya kazi ni kimoja tu cha Nagani. Namshukuru Mheshimiwa Rais nilipomuomba suala la gari amenikubalia na wananchi wa Lulindi wanashukuru sana kwa jinsi ambavyo amesikiliza kilio kile. Bado nikombe Mheshimiwa Jafo na Naibu Katibu Mkuu Afya na timu nzima ya Naibu Mawaziri, Mungu akiwajalia mkapata fedha za kuongeza vituo vya afya tunahitaji kituo muhimu sana cha afya cha Mnavila kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naomba kituo hiki kwa haraka sana? Tunalo tatizo kubwa sana la wananchi wetu kupoteza maisha na viungo kutokana na wimbi kubwa la kuzaana kwa mamba katika Mto huu wa Ruvuma. Tatizo lililopo ni kwamba hatuna kituo cha afya karibu, hivyo, kukitokea majanga ya namna hiyo wananchi wetu wanapata tatizo la kupoteza maisha ama kupata ulemavu kwa sababu hakuna huduma ya haraka katika eneo hilo. Kutoka pale Mnavila kwenda kwenye kituo cha afya ni zaidi ya kilomita 50. Kwa hiyo, nikuombe sana kwa huruma yako kwa kweli kituo hiki ni muhimu sana kipatikane ili tuweze kuwanusuru wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili hili la ujenzi wa hospitali, nishukuru kwa kunipatia Hospitali ya Wilaya ambayo inajengwa hivi sasa pamoja na kituo pale Chingutwa. Nashauri kitengo kile kinachohusika na gharama za majengo haya wawe waangalifu katika kutoa fedha aidha shilingi milioni 400 au 500 kwa sababu kuna baadhi ya maeneo ambapo upatikanaji wa vifaa ni mgumu inapelekwa shilingi milioni 400 lakini eneo ambalo halina tatizo inapelekwa shilingi milioni 500. Kwa hiyo, nadhani hili ni suala tu la marekebisho la kuangalia eneo ambalo lina changamoto nyingi basi ndiyo lipelekewe fedha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nishukuru kwa jinsi unavyoiongoza TARURA lakini bado Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa mchango wako.

MHE. JEROME D. BWANAUSI: Ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie mapendekezo ya Mpango wa Serikali ambao umewasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Na mimi niungane kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, Naibu Waziri na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa jinsi ambavyo mmeuandaa Mpango huu, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunapokuwa na Mpango ni lazima tuwe fedha za kuutekeleza Mpango. Kwa hiyo, nianze tu kupendekeza katika mipango ya Serikali kuhakikisha vyanzo vya mapato vinaimarishwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya chanzo cha mapato ambacho hatufanyi vizuri sana ni cha kodi ya majengo (property tax). Kwa kweli eneo hili tukiliimarisha, Serikali inao uwezo mkubwa sana wa kupata fedha. Naomba Wizara ihakikishe katika Mpango ujao na bajeti iliyokuja basi eneo hili la ukusanyaji wa kodi za majengo uweze kuimarishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni muhimu sana ni suala zima la nyumba za Serikali ambazo zilikuwa za Wizara na taasisi zilizopo Dar es Salaam hivi sasa hazitumiki. Naomba Serikali katika mpango na bajeti ijayo itoe mipango ya kuhakikisha majengo yale sasa yanageuka kuwa ni vitega uchumi vya kuisadia Serikali kupata fedha. Majengo yale ni mengi na baadhi ya maeneo tunalo tatizo kubwa sana la hosteli za wanafunzi kwa Dar es Salaam, kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano wa baadhi ya majengo aidha kuyakarabati na kuwa hosteli kwa sababu wanafunzi wale watachangia na kuiingizia Serikali mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza sasa Mheshimiwa Job Ndugai umekuwa ni mfano wa kuigwa katika Maspika na Bunge hili mzee unalimudu, unaliendesha vizuri na kwa kiwango. Moja ya ishara hiyo ni jinsi ambavyo umeamua sasa kutuweka kwenye Bunge Mtandao, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa jitihada hizi ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na Katibu wa Bunge, juzi tulikuwa tunapata takwimu ya jinsi ambavyo tutaokoa fedha nyingi sana za Serikali ambapo tulikuwa tunatumia karatasi nyingi sana, niIombe Serikali kwa kuwa tumeanzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao basi mawazo haya mema ya Spika na Bunge letu yahamie kwenye maeneo ya taasisi zote za Serikali pamoja na Halmashauri ziachane na mambo ya kutumia karatasi. Hii itakuwa imeokoa fedha nyingi sana za Serikali na kufanya fedha hizo zitumike katika shughuli zingine za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kuchangia kwenye suala zima la ununuzi wa ndege. Naipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo tumeionyesha dunia kwa kauli ambazo anatoa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwamba Tanzania ni matajiri, hii imedhihirishwa kwa jinsi ambavyo tunanunua ndege zetu kwamba sisi tunao uwezo kuliko hata nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, najua dhamira ni kutaka tuongeze mapato kwa maana ya watalii lakini pia kusaidia usafiri wa ndani. Baadhi ya maeneo mengine yanahitaji uboreshaji wa viwanja vya ndege. Kwa mfano, Uwanja wa Ndege wa Masasi tunatumia Uwanja wa Ndege wa Mtwara kwa abiria kutoka Tunduru, Liwale, Nachingwea na Newala. Hata hivyo, kwa kuuboresha Uwanja wa Ndege wa Masasi itakuwa ni kituo kimoja muhimu sana kwa wasafiri wa kutoka maeneo haya na kuweza kuhakikisha tunaboresha usafiri katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba uwanja huu ndio unaotumiwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa. Uwanja huu uko katika hali mbaya sana na niiombe Serikali katika mipango ya uboreshaji wa viwanja vya ndege basi tuboreshe uwanja ule ili pia hata anapotua Rais wetu Mstaafu basi uwe ni uwanja wenye usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye reli, nishukuru sana mpango huu umeainisha kwamba tutakuwa na ubia kati ya Tanzania na wabia wengine katika ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara hadi Mbambay lakini pia matawi ya Mchuchuma na Liganga. Niombe Serikali jambo hili ni la muda mrefu basi sasa ifikie kwenye utekelezaji wa kuingia makubaliano na hao wabia ili reli hii iweze kuleta matunda na tija katika mapato ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kilimo, Waheshimiwa wengi wamezungumza kuhusiana na kilimo cha umwagiliaji. Wewe ni shahidi umezunguka nchi hii sana, nchi hii ina utajiri mkubwa sana wa kuwa na mito ambayo maji yake yake hayakauki. Tunao Mto Simiyu, Mto Mara na Mto Ruvuma lakini maji yake yote yanakwenda baharini bila sisi kuyatumia. Kwa hiyo, mii niiombe Serikali tuimarishe sana kwenye suala zima la kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo kwenye kilimo nilitaka kuishauri Serikali kwamba tunayo mazao ambayo yanatuingizia fedha za kigeni ikiwemo korosho, chai, pamba, pareto, tumbaku lakini unapokuwa na ng’ombe wa maziwa ni lazima uhakikishe kwamba baadhi ya fedha zinazopatikana kwenye maziwa ziende zikanunue nyasi na maboresho mengine ili tupate maziwa zaidi.

Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba lazima itenge fedha tunazozipata kurudisha kwenye mazao haya ili kuyaendeleza vinginevyo itafika wakati tutakuwa tunapata kiwango kidogo sana cha mazao kwa sababu hayapati fedha kutoka Serikalini kama ruzuku ya kusaidia kwenye uimarishaji wa mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi ni mchangiaji wa mwisho nataka niokoe muda wako, naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia, kwenye bajeti hii ya Wizara ya Nishati, nianze pia kwa kumpongeza Waziri wa Nishati na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii. Waziri na Naibu wake wamekuwa wakizunguka nchi nzima na ziara zao zimekuwa na tija kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye Jimbo langu kwanza, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri hivi karibuni amefanya ziara katika Jimbo langu la Lulindi kule Wilayani Masasi ziara ambayo imeleta matumaini mapya kwa wakazi wa Jimbo la Lulindi. Lakini nimuombe tu Mheshimiwa Waziri kuweka msisitizo kwa yale aliyoyasema alipokuwa Jimboni Lulindi na hasa pale alipotoa maelekezo kwamba vijiji vile takriban tisa ambavyo viko katika Jimbo langu ambavyo vimepitiwa na umeme kwa miaka mingi lakini havijashushwa TANESCO uliwaagiza wafanye hiyo kazi katika vijiji hivyo vya Dagaga, Mkangaula, Mpita, Guluni, Maugura na vijiji vile vingine vyote ambavyo uliviainisha vikiwemo na cha Chanika ili kuhakikisha kwamba vijiji hivyo vipatiwe umeme haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Lakini pia nikumekupongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwa jinsi ulivyotoa maelekezo kwamba maeneo ambayo tayari yana umeme, yasisubiri tena mpango mwingine wa REA hakikisheni wananchi lipeni walipie ili nguzo Serikali iwapelekee kwa kweli huu ni mpango mzuri na tunaupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naushauri Mheshimiwa Waziri, kuhusiana na usambazaji wa umeme vijijini tunalo tatizo kubwa sana kwamba tunatakuwa kuwa na vijiji vingi sana tunavigusa lakini matokeo yake wakandarasi wanakwenda kuweka umeme katika kijiji robo tu ya kijiji na eneo lingine linabaki. Hili jambo linatuletea mgogoro mkubwa sana tunategemea kwenye REA awamu ya tatu mzunguko wa pili hili jambo liangaliwe sana kama tunakwenda kwenye kijiji tuhakikishe kijiji chote kinapewa umeme badala ya kuwekewa katika eneo dogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia suala la kuruka vijiji, kijiji kimoja kinapata kingine kinarukwa kingine hakipati hili jambo Mheshimiwa Waziri umelisisitiza sana lakini wakandarasi wamekuwa hawatekelezi kama vile unavyowaagiza.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho nimemsikia dada angu Mheshimiwa Peneza kuhusiana na mradi wa Rufiji mimi nilikuwa nadhani ingekuwa busara kwa sasa kwa upande wa wenzangu kule ndugu zangu kutouzungumzia sana juu ya kana kwamba huu mradi usitekelezwe Serikali imekwishaamua na katika ukurasa wa 23 wa hotuba ya Rais…

SPIKA: Mheshimiwa Upendo unaelimishwa huku!

MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Upendo nilikuwa nasema kwamba hivi sasa si vizuri sana kupoteza nguvu kubwa sana kujadili jinsi gani huu mradi utatekelezwa Serikali imekwisha dhamiria, imeshasema haiyumbishi na utatekeleza kwa wakati na historia jinsi mnavyoona sasa Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt John Pombe Magufuli inatekeleza kwa wakati miradi yake yote. Kwa hiyo, huu mradi hauyumbishwi na mtu wa ndani wala wa nje kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye bajeti yetu ambayo imewasilishwa kwa umakini mkubwa sana na Waziri wetu wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mpango na kwa kuanza tu niwatoe mashaka juu ya utendaji wenu wa kazi Dkt. Mpango na Naibu Waziri na mimi nataka niwape moyo kwamba ukiona watu wa upande wa pili wanawashambulia basi mjue mnafanya kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri imejaa hali ya matarajio makubwa sana kwa Watanzania na sisi wote tunaunga mkono juhudi ambazo Serikali inazifanya chini ya uongozi wa Rais wetu Jemedari Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kwa hakika wananchi wengi wamekuwa na imani kubwa na bajeti ya mwaka huu hasa pale ambapo mlijikita sana katika kuhakikisha kwamba mnapunguza kodi mbalimbali, lakini kuweka utaratibu mzuri wa wafanyabiashara kutozwa pale TRA, kwa hiyo, mwaka huu mmeweka maelekezo mazuri ambayo wafanyabiashara wengi wameunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nijikite kwenye Serikali kwanza Serikali za Mitaa. Uongozi wa Serikali unaanzia kwenye kijiji na pia kwenye mtaa. Mimi niiombe Serikali, Wabunge wengi wamekuwa wakilalamikia juu ya kutoona umuhimu kwa sasa wa kuwalipa walau kifuta machozi Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa. (Makofi)

Mimi nataka niseme ni-declare interest kwamba ni nafasi ambayo niliitumikia niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa pale Dar es Salaam, nimekuwa Diwani, nimekuwa Meya, hadi sasa nimekuwa Mbunge, hakuna nafasi ngumu kuiongoza kama ya kuwa Mwenyekiti wa Kijiji au Mwenyekiti wa Mtaa. Kwa hiyo kwa kweli ningeomba sana kama haiwezekani kuwapa hizo posho kila mwezi basi tunapofika mwisho wa kipindi cha miaka mitano nafasi hii ifikiriwe kama wanavyofikiriwa Madiwani na wanavyofikiriwa Wabunge walau wanapata chochote kutokana na kazi waliyofanya katika miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije pia katika suala zima la umuhimu wa afya ya Watanzania; kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi ambavyo imesaidia sana kwenye sekta ya afya. Tumejenga vituo vya afya zaidi ya 350, tumejenga hospitali zaidi ya 67 sasa hivi na bado mahitaji yapo ni makubwa. Mimi niiombe tu Serikali sasa pia ielekeze katika maeneo mahususi ambayo huduma hii ya afya inahitajika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenda jimbo langu pale Jimbo la Lulindi Wilaya ya Masasi kuna maeneo mawili ambayo yanahitaji kwa kiasi kikubwa sana Serikali itazame macho kuwapelekea kituo cha afya na maeneo hayo ni Mnavira pamoja na Kata ya Lipumburu. Kata ya Mnavira iko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, eneo hili limekuwa likikubwa na matukio mbalimbali ya wananchi kupoteza maisha, lakini kupoteza viungo kutokana na wimbi kubwa la mamba ambao mara nyingi nimekuwa nikilisema ndani ya Bunge. Hivyo wakipata majeraha wengi wanapoteza maisha kwa sababu kutoka Mnavira hadi kufika kwenye Hospitali ya Wilaya ni kiometa 50 kufika Masasi Mjini, kwa hiyo, pale panahitajika na bahat nzuri wananchi wa pale pamoja na Halmashauri imejitolea kujenga Jengo la OPD. Kwa hiyo, majengo mengine tu yaliyobaki ili pale pawe na kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kwenye ile Kata ya Lipumburu ambayo pia ndio kata ambayo Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anatoka kwa kweli lile eneo linahitaji kuwa na kituo cha afya ambacho kitahudumia kata ile ya Lupaso pia na Kata ya Lipumburu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la ukusanyaji wa mapato ya property tax. Bahati nzuri mimi nilishuhudia wakati nilipokuwa kwenye ngazi hizi zingine za Serikali za Mitaa jinsi ambavyo Halmashauri tulikuwa tunafanya vizuri katika ukusanyaji wa property tax. Lakini baada ya kuchukua TRA naona kama kuna hali ya kushuka kwa kiwango cha ukusanyaji wa kodi hii. Mimi niseme tu wananchi wapo tayari kabisa kulipa lakini mamlaka zinazopewa kazi hii ya ukusanyaji haziko makini katika kuhakikisha zinafuatilia suala hili la kodi ya majengo, ni sehemu ambayo likizingatiwa tutapata kipato kikubwa na kuisaidia Serikali kutimiza wajibu wake katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nilitaka niliseme ni juu ya suala zima la umuhimu wa mitandao na ujenzi wa minara katika maeneo yetu. Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikisema kwamba kama kuna maeneo muhimu ya kuhakikisha minara inajengwa ni mipakani yaani kati ya nchi na nchi na mimi jimbo langu linapakana na Msumbiji. Lakini hadi sasa hivi ninavyosema wananchi wa maeneo yangu ya Nanyemyo, Mnavira, Chipolopola, Sindano wanatumia mitandao kutoka Msumbiji. Kwa hiyo, mimi ningeomba sana Serikali kwamba badala ya wananchi kwenda kununua vocha za mitandao ya Msumbiji basi fedha zile zingetumika kununua mitandao ya hapa nchini na kuiingizia mapato Serikali yetu. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ihakikishe kwamba maeneo haya ya mipakani ambayo Serikali ilishaeleza umuhimu wa kujenga minara hiyo iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningeomba sana ni kwamba bahati nzuri tuna Daraja la Umoja kati ya Tanzania na Msumbiji, lakini eneo kubwa la kiuchumi ambalo linafanya biashara kati ya Msumbiji na Tanzania halipo kwenye eneo lile ambalo daraja limejengwa. Ningeomba sana Serikali tunapoteza mapato mengi sana kutokana na jinsi ambavyo hatuzingatii suala la ukusanyaji mapato katika nchi ya Tanzania na Msumbiji. Vifaa vingi vinatoka Msumbiji kuingia hapa lakini hakuna ushuru wowote uliotolewa. Pia Serikali iangalie kwamba uwepo uwezekano wa kujenga daraja lingine pale Mtwara maeneo ya pale Chilambo ambapo tukijenga daraja lile pale tutaweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa sana mapato kati ya Tanzania na Msumbiji. (Makofi)

Kwa hiyo, hili jambo ningeomba sana sana Serikali ilitazame kwa macho mawili kuhakikisha kwamba tunapata mapato kutoka Msumbiji kama tulivyopata mapato kutoka nchi zingine zinazopakana na Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa na mchango huo na najua muda ni mfupi kwa hiyo naunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)