Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rashid Mohamed Chuachua (22 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa weledi wake katika kuhakikisha juhudi za kujenga Tanzania ya Viwanda zinafanikiwa. Kusini mwa Tanzania ni eneo ambalo viwanda vya korosho vilijengwa kwa kuwa ndiko mali ghafi hii inakozalishwa kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa juhudi za Serikali zinahitajika katika kufufua viwanda hivi kwa ajili ya kuinua uchumi wa nchi yetu pamoja na wakazi wa maeneo husika. Jimbo la Masasi lina kiwanda cha kubangua korosho ambacho hakifanyi kazi kwa muda mrefu sasa. Naomba majibu ya Serikali kuhusu mpango wa kuhakikisha kuwa kiwanda hiki kinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakusudia kutoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri ikiwa katika majumuisho Serikali haitatoa kauli kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Microphone yangu haiwaki hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Serikali kwa mwaka 2016/2017. Kabla sijaanza kuchangia, kwa heshima kubwa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika katika Bunge hili, lakini pia nawashukuru Watanzania wote kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa kishindo kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Masasi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kampeni takribani miezi mitatu, minne hivi katika uchaguzi mdogo. Hawakukata tamaa walifanya kazi usiku na mchana hatimaye CCM imeshinda kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa namna ya kipekee, naomba nitumie fursa hii kuwaambia wananchi wa Masasi chaguo walilolifanya ni chaguo sahihi kukichagua Chama cha Mapinduzi, lakini kunichagua mimi mtoto wao ili niwapiganie na tutatekeleza tuliyo waahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali iendelee kuweka nguvu kubwa katika kukusanya mapato. Iendelee kuweka nguvu kubwa katika kuhakikisha kwamba wanakusanya kodi na kuwachukulia hatua wakwepa kodi wote pamoja na kuongeza juhudi zake za kupambana na ufisadi. Haya ni mambo ambayo tukiyafanya kwa nguvu kubwa tunaimani kwamba tunaweza tukasonga mbele kiuchumi.
Vile vile niwashukuru sana wale walioandaa mapendekezo haya na niseme tu mapendekezo haya yameakisi kwa kiasi kikubwa Hotuba ya Mheshimiwa Rais, lakini pia yameakisi kwa kiasi kikubwa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa mchango wangu katika sekta ya kilimo, kila mmoja wetu hapa anafahamu umuhimu wa sekta hii, namna ambavyo sekta hii ina uhusiano mkubwa sana na Sekta ya Viwanda. Hata hivyo, niseme tu Serikali ina mzigo mkubwa sana kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inasonga mbele na lazima tuelezane wazi kwamba hatuwezi kusonga mbele katika viwanda kama sekta ya kilimo haitapewa uzito mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba niishauri Serikali lakini pia nimshauri Waziri mwenye dhamana kuwa ana kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba kilimo kinasonga mbele. Tunapozungumzia kilimo tunazungumzia sekta tofauti tofauti, lakini pia tunazungumzia suala la mazao ya biashara. Kwa kweli hali ya manunuzi na mauzo ya mazao yetu ya biashara haijafikia kwenye kiwango cha kutembea kifua mbele. Nasema hivi nikiwa naakisi Jimbo langu la Masasi ambapo mchakato mzima wa ununuzi wa zao la korosho kama zao kuu la biashara umegubikwa na mambo mengi ambayo yanamkandamiza mkulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ihakikishe kwamba kama tunataka kusonga mbele katika viwanda basi ni lazima kuhakikisha kwamba tunaondoa kero zote zinazomkandamiza mkulima wa zao la korosho. Zipo kero nyingi, kuna makato yasiyo na sababu za msingi, kuna sheria ambazo kimsingi zinapaswa zifanyiwe marekebisho ili kusudi korosho imnufaishe mkulima na iwe ni zao lenye tija. Pia mchakato mzima wa pembejeo na usambazaji wake nao umegubikwa na mambo ambayo kimsingi yanamkandamiza mkulima. Wapo wanaopata pembejeo ambao hawakustahili pembejeo. Namwomba Waziri mwenye dhamana aliangalie sana eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo deni kubwa kwa Watanzania na tusingependa kusikia tena Watanzania wakiendelea kulalamika kuhusu mazao yao ya biashara. Kero hizi namwomba Waziri mwenye dhamana na Serikali ihakikishe kwamba inaziondoa na tutaisaidia Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakiona kilimo chao kikiwa kina tija. Pamoja na mambo mengine wakati wote wakulima wetu wamekuwa hawana dhamana ya kuweza kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itoe nguvu kubwa kuhakikisha Benki ya Kilimo inawafikia wakulima, lakini tuhakikishe kwamba rasilimali zao zinarasimishwa ili waweze kupata mikopo, waweze kupata hati miliki na waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Jimbo la Masasi tunacho Kiwanda cha Korosho, kiwanda hiki ni cha muda mrefu tungependa pia kiwanda hiki kiweze kufanya kazi ili wananchi waweze kubangua korosho zao na kuzisafirisha zikiwa zimebanguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengine ya msingi nitazungumzia kuhusu barabara, tunapozungumzia Kusini na mchango wake katika uchumi ni lazima tukumbuke kwamba wakulima wanaweza kurahisishiwa shughuli zao za kusafirisha mazao kama barabara zetu zinapitika. Tunalo tatizo kubwa tumeona katika mpango kuna kilomita kadhaa zilizotengwa kwa ajili ya barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningeomba Serikali safari hii iangalie Mikoa ya Kusini ambayo imekuwa ikisahaulika sana kwa ujenzi wa barabara zetu. Zipo barabara zina umuhimu mkubwa kama waliotangulia kusema wenzangu kama vile barabara ya Ulinzi inayotokea Mtwara inakwenda Tandahimba na Nanyamba - Newala inakuja kutokea Nanyumbu, hii ni barabara muhimu sana. Ipo barabara nyingine ya kutokea Mtwara unakwenda unatokea mpaka Jimbo la Lulindi unaingia Jimbo la Masasi hii ni barabara muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee tunaiomba Serikali itutengenezee barabara ya Masasi kwenda Nachingwea, tunaomba Serikali itutengenezee barabara inayotoka Jimbo la Masasi inaelekea Jimbo la Ndanda na inakwenda kukutana na Jimbo la Nanyumbu kupitia katika Kata za Mwengemtapika Kata za Mlingula, Kata zote hizo mpaka tunafika katika hayo Majimbo mawili. Hizi ni barabara muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango mwingine kwa upande wa elimu, tunalo tatizo kubwa. Katika elimu tunazo changamoto lakini pia tunakila wajibu wa kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya. Sisi ambao tumeishi katika Ualimu takribani miaka 15, 16; tunajua namna ambavyo Wananchi wameguswa na suala la Serikali kufanya elimu bila malipo. Hili ni jambo la msingi sana na sote tunapasa kuipongeza Serikali kwa kazi yake kubwa iliyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Waziri mwenye dhamana pamoja na Serikali iangalie namna ambavyo tunataka kuboresha elimu isisahau elimu nje ya mfumo rasmi. Tunapotaka kuboresha elimu, tusifikirie tu kuboresha elimu kwa upande elimu iliyo rasmi, tuangalie pia elimu nje ya mfumo rasmi. Ningeiomba Serikali ifanyekazi pamoja na Wizara husika, kukaa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, ione namna ambavyo inaweza, ikatoa mchango mkubwa katika kuelimisha watu nje ya mfumo ulio rasmi wa elimu. Ni lazima tukubali kwa sasa kwamba tunao Watanzania wengi wasiojua kusoma na kuandika, tunao Watanzania wengi wenye hitaji la elimu lakini wako nje ya mfumo rasmi wa elimu; hawa wanahitaji msaada mkubwa tusije tukawasahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la maji, Mapendekezo ya Mpango yameonesha namna ambavyo Serikali inakwenda kulitatua tatizo la maji. Niseme tu, niishukuru Serikali kwa namna ya kipekee kwa kujumuisha mradi mkubwa wa maji wa Mbwinji na kutaka kutengeneza mipango ya kuuendeleza kwa sababu mradi huu ni muhimu sana, kwa wananchi wa Jimbo la Masasi, lakini pia ni muhimu sana kwa Watanzania. Nawashukuru sana Serikali kwa kuweka mpango huu ili kusudi maji sasa yafike katika vijiji vyote vya Jimbo la Masasi, ambavyo havina maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza kuhusu suala la barabara, lakini ni muhimu kuelewa kabisa, tunapoizungumza Mtwara na miundombinu yake lazima tuzungumzie pia uwanja wa ndege. Uwanja huu umekuwa ukiimbiwa mara nyingi kwamba unahitaji marekebisho ya kina, lakini marekebisho haya yamekuwa hayafanywi. Si jambo zuri mpaka leo tukiwa tunazungumzia uwanja ambao ni uwanja wenye sifa za kuweza pengine kuwa wa Kimataifa, lakini hauna taa. Uwanja huu haujafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu. Tunaiomba Serikali yetu sikivu ifanye kazi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa katika huduma zetu za afya, katika Jimbo la Masasi zipo zahanati saba tu. Tunajua Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba kila Kijiji, kila Kata kinakuwa na zahanati, lakini lengo hili halijafikiwa ipasavyo katika baadhi ya maeneo. Tunaiomba Serikali wakati inataka kupiga hatua mbele kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda, tuangalie pia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Chuachua.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe kwa kazi kubwa na nzuri inayopendeza ya kuandaa hotuba hii ambayo kimsingi inatafsiri kwa kina Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme tu kwamba kazi kubwa inayofanywa na Serikali iliyopo madarakani ni kazi ambayo inapaswa kuungwa mkono na sisi Wabunge. Tuiunge mkono Serikali yetu ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisahau kusema kwamba wakati tuna harakati za kisiasa, wananchi wangu hawakunituma ili nije kuonekana kwenye tv. Wamenituma nije kufanya kazi kwa sababu wao hawahitaji tv, wanahitaji maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda niiambie Serikali kwamba wakati tunajiondoa kwenye hali ya utegemezi lazima tufahamu kwamba maendeleo haya tunayoyataka ni vita kubwa sana. Hili ni jambo la msingi sana, maendeleo ni vita. Nachukua kauli ya Profesa wangu Mheshimiwa Norman Sigalla King ameandika maendeleo ni vita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo viongozi wengine ni waandamizi, wanazungumza kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Rais wake wanapofanya kazi kubwa ya kuwawajibisha watumishi ambao kimsingi wanatenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma wanakosea, hili ni suala la ajabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ni suala la ajabu kwa sababu viongozi hao wanafikia hatua ya kudiriki kuzungumza kwamba wanaowajibishwa ni watu wa mkondo fulani wa kisiasa, ni jambo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais tunamuona anavyofanya kazi na Waziri Mkuu akiwa anawawajibisha viongozi ambao kimsingi wengine ni waandamizi katika Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, lazima tuzungumze mambo ambayo hatuwapotoshi Watanzania. Tukisema hivi maana yake tunataka kuwaaminisha Watanzania kwamba hao wanaoharibu wao ndiyo wamewatuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba wakati Serikali inakwenda kwenye hatua ya maendeleo ya viwanda, naomba waendee katika hatua hiyo wakijua kwamba maendeleo haya ni vita. Unapokwenda kwenye viwanda unahitaji rasilimali kubwa inayozalishwa nchini iende kwenye processing industry, lakini wakati huo huo tunawakwaza Watanzania wenzetu ambao kimsingi tuliwategemea watusaidie, wao kazi yao ilikuwa ni kusafirisha malighafi, wanakwazika na kitendo cha Tanzania kutaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda na kuziwezesha sekta zinazotegemea viwanda, wapo Watanzania wenzetu wanaishi hapahapa, wanakwazika na ununuzi wa ndege kwa sababu wana hisa kwenye makampuni mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kuboresha reli tunawakwaza Watanzania wenzetu kwa sababu wengine wana malori, wanataka bidhaa zisafirishwe kwa malori wapate faida hata kama tunadidimia katika uchumi wetu. Maendeleo ni vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ikaze buti kuhakikisha kwamba inasimamia yale ambayo wameyasema na sisi tutawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, niseme tu kwamba wakati tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda tunategemea sana kilimo lakini mipango yetu inaonyesha wazi kabisa kwamba mchango wa sekta ya kilimo ni asilimia 25 tu katika Pato la Taifa wakati nguvu kazi iliyopo katika kilimo ni zaidi ya asilimia 74.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kwamba kiasi kikubwa cha nguvu kazi kipo kwenye kilimo lakini tija ya kilimo bado haiwezi ku-support uchumi wa viwanda. (Makofi)
Naiomba Serikali iliangalie hili na ihakikishe kilimo kinatengewa pesa za kutosha. Wakati wa kuondoa kero kwa wakulima wetu ni sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, alipotembelea maeneo ya Kusini. Amefanya uamuzi mkubwa wa kufuta baadhi ya makato ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa wakulima. Huu ni uamuzi mkubwa sana. Wakulima wetu wamelalamika kwa miaka mingi na tunaendelea kuitia moyo Serikali kwamba iendelee kuona namna ambavyo inaweza kuondoa kero kwa wakulima wa mazao yote yanayotegemewa kukuza uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, tunategemea pia Serikali sasa itoe kipaumbele katika suala zima la pembejeo. Katika bajeti iliyopita, Serikali ilitoa voucher za pembejeo kwa takribani voucher milioni tatu. Mkoa wa Mtwara peke yake ulipata voucher 10,000 tu na Jimbo la Wilaya ya Masasi lilipata voucher 3000. Hili ni jambo ambalo linaweza kuwakatisha tamaa wakulima kwa sababu voucher hizi hazikutosha. Naiomba Serikali iongeze mkazo mkubwa sana katika kuhakikisha kwamba voucher zinatoka za kutosha ili wakulima wetu wapate pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze haraka haraka kwenye suala la elimu. Tunazo changamoto kubwa na Serikali imefanya juhudi kubwa. Mimi naamini kwamba changamoto hizi ni sehemu ya maendeleo. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali iendelee kufanya juhudi kubwa, lakini naiomba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, iweke msisitizo mkubwa sana kwenye suala la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi. Ukiangalia historia ya elimu ya nchi hii, toka Serikali ya awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, alifanya kazi kubwa katika eneo la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa sababu tunahitaji nguvukazi kwenye Sekta ya Viwanda, hatuwezi kuhakikisha kwamba tunawaelimisha Watanzania wengi kwa wakati mmoja kwa kutegemea waingie madarasani. Pia naiomba Serikali ifahamu kwamba kiwango cha Watanzania kutokujua kusoma na kuandika kinaongezeka na vijana wetu wengi hawana elimu ya kutosha. Kwa hiyo, tunaweza tukawa na viwanda vya kutosha lakini tukaishia kwenye kuwa wabeba mizigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana, Serikali yangu ihakikishe kwamba inapanua wigo wa elimu ili wale ambao hawana uwezo wa kwenda kwenye sekta rasmi ya elimu waweze pia kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa katika ardhi, lakini juhudi za Serikali za kutaka kuwapimia wananchi tunazipongeza ila tunamwomba kwa heshima kubwa Waziri wa Ardhi afike Jimbo la Masasi ili atatue kero za wananchi wa Masasi. Wananchi wa Masasi wana matatizo mengi katika ardhi na bahati nzuri tumezungumza na Waziri, amesema atapanga muda. Naomba baadaye atuambie ni lini atakwenda ili kusudi wananchi waweze kutatuliwa matatizo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo katika eneo la afya, lakini pia Serikali imepiga hatua katika kutatua kero za afya kwa wananchi wetu, isipokuwa katika Jimbo la Masasi matatizo bado yapo. Tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba katika bajeti ya mwaka huu inatoa pesa za kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze tu suala la ulinzi na usalama. Tunaishukuru Serikali kwa juhudi zake, tunashukuru Serikali kwa kuhakikisha kwamba inawajali Askari Polisi. Isipokuwa katika Jimbo la Masasi, kuna tatizo kubwa. Jeshi la Polisi wanaishi katika maeneo ambayo hayana nyumba. Tunaomba Serikali iangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nizungumze tu kwamba Askari wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, tunaomba wapatiwe Bima ya Afya. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Maana naona Walimu tuko wengi sana, nami nimefundisha zaidi ya miaka 15, ni muhimu sana kutoacha bajeti hii ipite hivi hivi bila ya kuwasemea Walimu na elimu kwa ujumla. Kwa nini? Kwa sababu, kimsingi elimu ndiyo injini ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la kwanza ni kuzungumzia maslahi na madai ya Walimu. Tulitoa ahadi na tunaendelea kuitoa ahadi hiyo kwamba tutawatetea Watumishi wa Umma na hili ni jambo la msingi ambalo ni lazima tulifanye. Tumewaahidi tutawatetea na sisi tutafanya kazi hiyo, ila Serikali nayo itimize wajibu wake katika kuhakikisha inatimiza ahadi inazozitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wana changamoto kubwa. Wapo Walimu ambao wanadai kupandishwa mishahara katika maeneo mbalimbali nchi nzima. Kwa mfano, tu katika Jimbo langu la Masasi Walimu zaidi ya 50 bado wanadai kupandishwa mishahara. Hili ni jambo la msingi na ni lazima Serikali iwajibike kuhakikisha kwamba watu hawa wanapata fursa ya kulipwa mahitaji yao ili waweze kufundisha vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jambo hilo, kimekuwa kilio cha Walimu cha muda mrefu cha kupata posho ya madaraka (responsibility allowances). Tunao waraka ambao umetolewa na utumishi, Waraka Na. 3 wa mwaka 2014, unaotoa maelekezo, toka mwaka 2015/2016 maelekezo hayo yalipaswa kutimizwa kwa bajeti iliyopita, kwamba Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi alipaswa kulipwa shilingi 200,000/= kila mwezi kama posho ya madaraka; Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari shilingi 250,000/=, Mkaguzi wa Elimu Kata ni shilingi 250,000/= lakini Mkuu wa Chuo cha Ualimu ni shilingi 300,000/= kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno mazuri tu, tumwambie Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atupe mkakati ukoje katika kutekeleza mahitaji ya waraka huu unaotaka Walimu walipwe responsibility allowances.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ni muhimu tuliweke wazi suala ambalo kimsingi nchi yetu imepita katika mtikisiko wa kutoka kufanya mabadiliko makubwa ya namna ya kutoa vyeti vyetu kwa wanafunzi wetu wa Kidato cha Nne. Hili ni jambo la msingi sana! Sasa hivi tunao vijana wetu ambao tumeshatikisa standard ya vyeti vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali, sasa iandae utaratibu na Waziri atuambie utaratibu anaokuja nao, tufute vyeti vyote vyenye GPA, badala yake watoto hawa wapewe vyeti ambavyo vina division.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tumeamua kufanya mabadiliko, tumetoka tena kwenye GPA tunakwenda kwenye division, tayari tumeshaathiri watu katika kundi kubwa sana ambao mpaka sasa hivi wanashindwa kutambulika wana standard gani ya elimu katika vyeti vyao. Naomba tuliangalie sana hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusu Elimu Maalum. Kama kuna eneo ambalo limesahaulika katika nchi hii, ni Elimu Maalum. Ninajua tukisema Shule za Sekondari na Shule za Msingi tutasema ziko katika eneo la TAMISEMI, lakini acha tu tuseme, nami ninaishauri Serikali, iangalie uwezekano wa kuchukua shule hizi za Elimu Maalum na kuzipeleka kwenye Wizara badala ya TAMISEMI ili ziweze kupata jicho maalum la kuziangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika katika hizi Shule za Msingi na Shule za Sekondari ambazo zinawasaidia vijana wetu wenye mahitaji maalum, unaweza ukatokwa na machozi. Vijana hawa wanasoma katika mazingira magumu sana. Nadhani hata kama tukienda kwenye theories of learning tunajua kabisa miongoni mwa shule ambazo zilitakiwa ziwe na mazingira rafiki na ya kuvutia ni hizi zenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu kuna shule mbili za msingi; Shule ya Msingi Masasi na Shule ya Msingi Migongo. Watoto hawa wamesahaulika! Naomba Serikali iangalie namna invyoweza kuziboresha shule hili ili na hawa wenye mahitaji maalum wajione ni sehemu ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mambo hayo, napenda tu kuelezea jambo la msingi kwamba tunaposhughulikia elimu katika nchi yetu, hatuwezi kuweka mkazo moja kwa moja kwenye formal education pekee, yaani kwenye elimu ndani ya mfumo rasmi. Hili nimekuwa nikilisema na leo nalirudia tena. Ninaposoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri sioni inapojitokeza non formal education.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo takwimu kwamba kama asilimia 50 ya Watanzania ni watoto; na kama asilimia 50 ni watoto, maana yake ni takriban milioni ishirini na kitu. Kama waliopo katika mfumo rasmi wa elimu ni milioni 12 tu, ni wazi kabisa kuna kundi kubwa la watu ambalo haliwezi kufikiwa bila ya kushiriki nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie, hatuwezi kutumia madarasa yetu pekee kutoa elimu ya sekondari. Naiomba Wizara iangalie namna ambavyo inaweza ikazitumia taasisi zake kama vile Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha kwamba watoto wengi ambao wanakosa kuingia katika elimu rasmi, waende nje ya mfumo rasmi wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ya kuyaangalia katika hilo. Nimekuwa nikisema, Waziri naye sasa hivi atakuwa na dhamana kubwa ya kuhakikisha tunakuja na mikakati ya kupunguza kiwango cha watu ambao wako nje ya mfumo wa elimu, wasiojua kusoma wala kuandika, wengine ni watu wazima; nao pia tuwaelimishe, tusizingatie tu elimu rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ya kuzungumza, lakini niseme tu kwamba hali ya elimu tunaendelea kujikokota, tunakwenda, lakini yako mambo ambayo bado ni changamoto. Katika Jimbo la Masasi tuna tatizo kubwa la Walimu wa Shule za Msingi. Tunahitaji Walimu takriban 252; hatuna hata Mwalimu mmoja wa kufundisha Shule ya Awali, katika Walimu wa sayansi kiwango cha sekondari tuna matatizo makubwa. Tunapungukiwa Walimu zaidi ya 60, haya ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto tulizonazo, pamoja na juhudi kubwa tunazofanya za kutoa elimu bila malipo, lakini pia tuongeze nguvu katika kutatua changamoto zinazotukabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi, huo ndiyo mchango wangu. Naunga mkono hoja. Naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ambayo yatatupa imani. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia kwenye Wizara hii adhimu kwa mustakabali wa afya za Watanzania. Nitumie pia fursa hii kumpongeza Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri waliyoitoa, inayoonesha mwelekeo wa suala zima la utekelezaji wa sera ya afya katika awamu hii.
Mheshimiwa Spika, ninapoiangalia Wizara ya Afya, nashindwa kabisa kutenganisha majukumu yake na TAMISEMI na kwa maana hiyo basi kama majukumu hayo tunaweza tukayatenganisha katika actual practice, acha tuseme katika kiwango hiki cha kuchangia, ili tuweze kueleza matatizo na changamoto zilizopo katika Wizara ya Afya, halafu hao wenyewe kwa sababu Serikali ipo, watagawana, watajua hiki ni cha TAMISEMI na hiki ni cha Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya, niseme tu kwamba kama ningekuwa napata fursa ya kuangalia changamoto za Wizara zote, basi Wizara ya Afya ningesema namba moja, inawezekana katika Majimbo mengine ni tofauti, lakini katika Jimbo langu Wizara ya Afya ni Wizara ambayo ina changamoto kubwa sana kuliko Wizara nyingine zote.
Mheshimiwa Spika, jambo hili kwanza linatupeleka katika kuhakikisha kwamba, fedha wanazoomba zinapatikana na zinafika kwa wakati. Pili, ni jambo ambalo nadhani linatakiwa liwekewe msisitizo maalum na Serikali ili kila mwaka tusiendelee kuimba changamoto za Watanzania katika eneo hili la afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa kuakisi moja kwa moja Jimbo la Masasi ambalo kimsingi Jimbo hili kabla halijagawanywa na hata kabla ya Wilaya haijagawanywa tulikuwa tuna Hospitali moja tu ya Wilaya inaitwa Hospitali ya Mkomaindo. Tumegawanya Wilaya na sasa tuna Wilaya ya Nanyumbu, Hospitali kubwa ni ile ile. Tumegawanya Majimbo, lakini bado tunategemea hospitali moja. Hospitali ambayo inahudumia watu wa Wilaya takribani mbili, pamoja na watu wanaotoka nje ya nchi ya Tanzania kwa upande wa Msumbiji. Ni hospitali iliyoelemewa sana.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tunapozungumza, hospitali hii ina changamoto kubwa ya dawa, hospitali hii ina changamoto kubwa ya vifaa tiba na hospitali hii ina changamoto kubwa ya majengo. Labda tu nitoe mfano, tunayo wodi ya wazazi ambayo kwa mwaka hospitali hii inapokea takriban wazazi 4,200, ina vitanda 10 tu. Hii ni changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, nina imani kwamba, mwanamke ndiye kiumbe anayekwenda hospitali mara nyingi zaidi kuliko mtu yeyote. Kama hatutaangalia kwa jicho la kipekee huduma zinazowagusa wanawake, hatuwezi kusema tumepiga hatua katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali liwe suala hili linahusu TAMISEMI au liwe linahusu Wizara ya Afya, waje na majibu, ni lini upanuzi wa wodi ya akinamama katika Hospitali ya Mkomaindo utafanyika ili kusudi akinamama hawa wasilale chini au wasilale wawili wawili? Mheshimiwa Ummy amefika Hospitali ya Mkomaindo ameiona. Mheshimiwa Jafo pia amefika, ameiona na changamoto zake. Tunaomba tupate majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba huduma zinasogea karibu na wananchi, tunaiomba Serikali izipandishe hadhi baadhi ya zahanati zinazozunguka Jimbo la Masasi ili kusudi kuisaidia Hospitali ya Mkomaindo. Naomba ipandishwe hadhi zahanati ya Mwengemtapika, zahanati ya Mombaka na zahanati nyingine ya Chisegwe, tuwe na vituo vya afya. Wenyewe mtagawana majukumu mjue ni nani ambaye anahusika na kupandisha zahanati hadhi na nani anahusika na kuwepo kwa zahanati hizo. Naiomba Serikali iangalie eneo hili.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza hapa, Jimbo la Masasi lina takribani ya mitaa na vijiji 60 na zaidi, lakini tunazo zahanati tano tu. Tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi wa afya, tunapungukiwa na watumishi 400 na kibaya zaidi kama wiki mbili zilizopita watumishi 19 tena wamesimamishwa kazi kwa kosa la kughushi vyeti na kwa maana hiyo, hatuna kabisa watumishi. Naomba Serikali iliangalie hili na ilifanye kama jambo la dharura, hali sio nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote niliyoyaeleza, lakini tuna magari mawili tu kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa. Haiwezekani, mambo hayawezi kwenda. Tunaiomba Serikali na hili nalo iliangalie.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 kuna ubadhirifu wa fedha ulifanyika na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mkomaindo, fedha za dawa. Naiomba nayo Serikali itoe majibu, hatua gani mpaka sasa zimeshachukuliwa? Shilingi milioni 29 hazijulikani zilitumika vipi. Naomba Serikali itoe majibu hatua ambazo imezichukua ili wale wanyonge waendelee kupata matibabu.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala la utekelezaji wa huduma za afya bure kwa wazee, nalo jambo hili ni zito na gumu sana katika Jimbo langu. Hapa ninapozungumza toka mwezi wa Kwanza hakuna hata shilingi iliyopelekwa kwa ajili ya kuwahudumia wazee katika Jimbo la Masasi. Wazee hawa wanapata shida, wanawaona madaktari kwa shida na wakiwaona hawapati dawa. Kwa hiyo, tunakosa kuona umuhimu wa kuwepo hilo Dirisha la Wazee. Naomba pia Serikali iliangalie hili kama ni suala la Serikali Kuu au kama ni suala la Serikali za Mitaa, lakini sisi shida yetu watu wa Masasi, wazee wapate huduma zao.
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi katika Wizara hii hatuwezi kuyamaliza yote, lakini kimsingi na kwa namna ya kipekee tuone namna ambavyo Serikali inatoa msisitizo maalum katika kuboresha vyuo vyetu vya maendeleo. Tunavyo vyuo takribani 55 ni vyuo vichache nchi nzima, tunahitaji vyuo hivi viongezwe, lakini kikubwa zaidi vyuo hivi havina wataalam na havina vifaa vya kutosha.
Mheshimiwa Spika, nadhani umefika wakati sasa pamoja na pendekezo la vyuo hivi kwenda Wizara ya Elimu, lakini lazima utoke msisitizo maalum kuhakikisha kwamba vyuo hivi ndivyo ambavyo tutakuja kuvitegemea kwa ajili ya kutengeneza vijana watakaoingia kwenye soko la ajira tunapokwenda kwenye uchumi wa viwanda. Vyuo vilivyopo chini ya mamlaka ya VETA havitoshi na kwa maana hiyo, vyuo hivi vina nafasi kubwa sana. Naomba Serikali itazame vyuo hivi, kikiwemo chuo kilichopo katika Jimbo langu cha Masasi FDC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema yako mambo mengi, nimeongea kwa kifupi. Naunga mkono hoja, lakini naiomba sana Serikali ije na majibu ya maswali niliyoyauliza. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RASHIDI M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na nzuri ya kusambaza na kusimamia nishati ya umeme. Hata hivyo, naomba ufafanuzi Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa chanzo cha nishati ya umeme wa gesi katika Mkoa wa Mtwara, hali ya usambazaji wa umeme hairidhishi. Pale ambapo umeme umefika hali ya kukatikakatika kwa umeme inaendelea kuwakatisha tamaa wananchi wa Mikoa ya Kusini hususani Wilaya ya Masasi. Kwa kweli ikiwa nishati ya mwanga wa kibatari inayoweza kuzimika kwa upepo wakati wowote inapaswa iwe tofauti na ile ya umeme. Kwa sisi watu wa Masasi inatuwia vigumu kutofautisha kutokana na kukatikakatika kila wakati bila ya taarifa yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atueleze hali hii itakwisha lini? Je, Serikali haioni sababu ya kuwa na njia mbadala ya umeme ambayo kwa sasa umeme unaokuja Masasi unapitia Tandahimba, Newala - Masasi kuelekea Nanyumbu? Matatizo yoyote ya umeme katika maeneo hayo yanatuathiri mara kwa mara wananchi wa Masasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo tatizo kubwa la kutofanyiwa marekebisho au matengenezo ya nyumba za wafanyakazi wa TANESCO zilizopo katika Kata ya Migongo, Jimbo la Masasi. Nyumba hizi zinageuka kuwa magofu wakati watumishi wanahangaika mahali pa kukaa. Naomba nijue mkakati wa Serikali kuhusu nyumba hizi ?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakushukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia leo tarehe 21 Mei kwenye hotuba ya Wizara ya Ardhi, inayoongozwa na Mheshimiwa William Lukuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 143. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake anaonyesha kwamba maeneo ya ardhi yaliyonunuliwa na Shirika la Nyumba la Taifa hadi Aprili, 2016 katika Wilaya mbalimbali nchini, Jimbo langu linajitokeza katika Wilaya ya Masasi ambapo Shirika la Nyumba limejenga nyumba chache pale na inaonekana eneo hili ni la ekari 16 na kwamba walilinunua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho, aweke sawa taarifa hizi, kama kulipa fidia ya shilingi milioni 22 katika eneo la ekari 16 ndio kununua eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, naomba pia Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake, atuambie ni vigezo gani Shirika la Nyumba wanavitumia katika kulipa fidia ya eneo lililopo katika mji kwa shilingi 22,500,000 kwa eneo la ekari 16 za wananchi ambao wamehamishwa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lililopita, Mheshimiwa Waziri alituelekeza tuorodheshe migogoro iliyopo katika maeneo yetu. Mimi binafsi niliunda kikosi kazi na tukaorodhesha migogoro mbalimbali iliyopo katika maeneo ya Mji wa Masasi wakati wananchi wa eneo la Kata ya Mtandi, Migongo, Napupa, Mkomaindo, Jida, Mkuti na Mwenge Mtapika, wamekuja wakaleta malalamiko yao mengi, tukapata orodha ya wananchi takribani 1,123. Kwa pamoja wananchi hawa wanadai fidia ya zaidi ya shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha migogoro, jambo hili halipo. Sasa naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni mgogoro mkubwa kwa kiwango gani unatakiwa uoneshwe kwamba ni mgogoro ambao umedumu kwa takribani miaka kumi kwa sasa, wananchi hawa wanaendelea kuhangaika, wamehamishwa kwenye maeneo yao na hawajapewa fidia?
Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu ametupa documents za kusoma, nataka pia tujaribu kuangalia hizo sheria ambazo zinawaruhusu watumishi wa Idara ya Ardhi kupima maeneo ya wananchi, kuwahamisha maeneo hayo, kuyauza kwa watu wengine na kujenga nyumba zao, halafu wananchi hawa wanaendelea kuidai Serikali fidia. Hizi ni sheria za kutoka wapi? Tunaomba pia Mheshimiwa Waziri aweze kutupatia ufafanuzi wa jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Masasi wanakusubiri. Sisi Wabunge tunapofikia hatua ya kuleta migogoro kwako, maana yake migogoro hii imekuwa ni sugu na viongozi waliopo katika Halmashauri zetu wameshindwa kuishughulikia, ndiyo maana yake! Kwa sababu hatuwezi kuwa na migogoro miaka kumi, kila siku tunazungumza haya haya, mpaka leo hayajapatiwa ufumbuzi.
Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufanya hitimisho, utuambie utakuja Masasi lini ukae na wananchi wa hizi Kata nilizozizungumza hapa waweze kulipwa mahitaji yao? Hali yao siyo nzuri na wanasubiri kauli yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Masasi limepitiwa na barabara ya kutoka Masasi kuelekea Nachingwea. Pambezoni mwa barabara hii ambayo kwa sasa inasubiri upanuzi, wapo wananchi ambao tayari wameshafanyiwa tathmini ya eneo hili. Kwa maana hiyo, wanatakiwa kupisha upanuzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini hii imefanywa muda mrefu na sasa ni miaka mingi imepita, wananchi hawa wameambiwa watalipwa fidia zao ili watafute maeneo mengine ya kukaa, lakini mpaka sasa hivi wananchi hawa wapo stranded hawajui wafanye nini kwa sababu hawajalipwa fidia zao. Mheshimiwa Waziri kwa sababu eneo la fidia linakuhusu wewe, naomba utoe ufafanuzi, ni lini Serikali itawalipa fidia zao wananchi hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nilipokuwa napitia makabrasha ya Wizara ya Ardhi, sijaona mipango ya upimaji wa miji hususan Mji wa wa Masasi. Naamini kwamba harakati za upimaji wa mji na kuyarasimisha makazi ni jambo muhimu sana kwa sababu kadri tunavyozidi kusonga mbele ndivyo wananchi wetu wanavyozidi kujenga kwenye makazi holela na kwa maana hiyo, hatua zetu za upangaji wa miji zinazidi kuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atoe pia ufafanuzi, mpango huu hasa ukoje? Ni maeneo yapi na ni lini Mji wa Masasi nao utaingia katika mpango huu wa upimaji ili kusudi wananchi wakae katika maeneo yaliyorasimishwa waweze kupata umiliki wa maeneo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya machache, namuomba Waziri akija hapa atoe ufafanuzi wa maeneo hayo niliyoyaeleza na mimi naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kusema kwa kifupi ili nitoe mchango wangu kwenye mapendekezo ya mpango. Kwanza kabisa tuipongeze Serikali kwa sababu kilicholetwa hapa ni mapendekezo na kama tukitoa mapendekezo mazuri yatafanya mpango wetu uwe bora zaidi kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumza katika maeneo mawili; kwanza nitazungumzia suala la kilimo, katika kuzungumzia suala la kilimo nitajikita kwenye miradi ya kimkakati. Katika ukurasa wa 43 tumeelezwa kwamba mradi namba saba utakuwa ni kuimarisha kilimo cha mazao ya chakula na malighafi nakadhalika. Mimi ninaomba niishauri Serikali eneo hili lisomeke kuimarisha ushirika na kilimo, tusiache ushirika, nikiangalia mpango huu sioni namna unavyozungumzia kwa kina suala la ushirika. Katika kipindi kifupi na uzoefu tulioupata wa kuwatetea wananchi katika majimbo yetu tunaona kwa kiwango kikubwa kabisa wakulima wanategemea ushirika, lakini ushirika lazima uimarishwe na usimamiwe vizuri ili kusudi wakulima wetu waweze kupata tija ya mazao wanayolima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kusimamia vema suala la kilimo, mauzo na manunuzi ya zao la korosho kwa msimu wa mwaka huu, hili ni jambo kubwa kwa sababu bei ya korosho imepanda lakini bado kuna changamoto za hapa na pale ambazo kimsingi tunapenda Serikali iziangalie kwa kina. Nitazisema kwa kifupi, jambo la kwanza katika msimu wa korosho uliopita wananchi wa Mikoa ya Kusini wamepata shida kubwa baada ya vyama vya msingi kukata fedha kwa wakulima wetu. Fedha hizi ni nyingi na tunaomba Serikali ichukue hatua ya haraka ili wakulima walipwe fedha zao ambazo zilikuwa zimekatwa katika msimu uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ripoti iliyoandaliwa na TAKUKURU inaonyesha kwamba takribani shilingi bilioni 30 hazijulikani zilipokwenda, lakini bodi ya korosho imeeleza takribani shilingi bilioni 11 hazijulikani zilipokwenda katika Mikoa ya Kusini. Cha kushangaza bado wale wale waliohusika na wizi wa namna hii wanaendelea tena kusimamia mfumo wa mwaka huu. Wakulima wanaendelea kuuza korosho zao, lakini jicho lao lipo kwa Serikali ni namna gani watu hawa watachukuliwa hatua ili fedha zao zirudishwe na hatua zichukuliwe kwa ajili ya ubadhilifu mkubwa uliofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine la msingi ambalo linapaswa kuangaliwa katika ushirika, katika msimu wa mwaka huu mazao mchanganyiko yameuzwa kwa bei holela mno. Tunaiomba sasa Serikali ije na mpango madhubuti wa kuona namna gani mazao mchanganyiko kama vile mbaazi, ufuta, choroko zitauzwa kwa bei inayofaa na kwa utaratibu unaoeleweka ili wakulima wetu waweze kupata manufaa makubwa, tunaiomba Serikali ilisimamie jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi ninapochangia katika eneo la elimu nimekuwa nikisema jambo ambalo na leo nitalisema, nina imani Serikali yangu sikivu italisikia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoiangalia elimu tunapaswa kuiangalia elimu kwa jicho pana sana tusiiangalie elimu kwa mtazamo wa elimu rasmi peke yake. Nimekuwa nikilisema hili mara nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia utaratibu wenyewe wote wa kuendesha elimu rasmi uliowekwa katika mpango wetu unaonesha wazi kabisa kuna kundi kubwa la watu tunaowaacha, ambao kwa msingi huo hawatapata elimu kwa muda mrefu sana na baadaye tutakuwa na kundi kubwa la watu ambao hawajaelimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia sensa ya watu ya mwaka 2012 tunaona kwamba takribani watu wazima milioni 5.5 hawawezi kusoma na kuandika. Lakini pamoja na hilo tukiangalia tena idadi ya watu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia muda wa kuchangia eneo hili la TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Waziri wa TAMISEMI kwa kazi kubwa anayoifanya na wasaidizi wake, hongera sana Mheshimiwa Waziri. Kazi unayoifanya Watanzania wanaiona na hotuba yako inaonesha kabisa mwelekeo wa bajeti yetu, lakini pia mwelekeo wa mambo
ambayo yamefanywa katika bajeti iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia eneo la elimu. Ni kweli kabisa kuna tofauti kubwa kati ya elimu bila malipo na elimu bure. Hii tofauti ipo na Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kufafanua majukumu ya Serikali ni yapi, lakini pia majukumu ya jamii au wananchi ni yapi. Ni kweli kwamba tofauti kati ya elimu bila malipo na elimu bure inapaswa ifike kikamilifu kwa wananchi wetu kule chini.
Mheshimiwa Spika, ni jukumu letu sisi kama wanasiasa kuwaeleza wananchi, lakini pia ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wetu wa kawaida wanajua majukumu yao. Uelewa wa wananchi bado haujakaa sawasawa na kwa maana hiyo, ninaishauri Wizara ifikishe
elimu hii kwa kutumia Idara ya Elimu kwa ngazi ya chini kabisa ili wananchi wajue majukumu yao ni yapi kama yalivyofafanuliwa na miongozo ya Serikali.
Kimsingi suala la elimu bila malipo lina changamoto zake na ndiyo maana tuko hapa kwa ajili ya kutatua changamoto hizo. Serikali ilipoamua kupeleka fedha katika shule za msingi na sekondari imekwenda sambamba na kubana matumizi ambayo yanasababisha baadhi ya maeneo kutotekelezwa vizuri katika utoaji wa elimu.
Mheshimiwa Spika, naomba niliongelee eneo moja tu la mitihani. Ni kweli kabisa ili mwanafunzi aweze kujifunza, anahitaji kichocheo cha kuwa na majaribio na mitihani ya mara kwa mara. Kwa maana hiyo basi, pamoja na kwamba tunakwenda vizuri katika kutoa elimu hii bila malipo, lakini tunaiomba Serikali iongeze fedha ambazo zitawasaidia walimu kutoa majaribio ya mara kwa mara ili tuweze kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine muhimu ni eneo la miundombinu ya shule zetu. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaonesha wazi kwamba tunalo tatizo kubwa la miundombinu katika shule zetu, tuna matatizo ya vyoo, tuna matatizo ya majengo na matatizo ya nyumba za walimu.
Nadhani sasa umefika wakati wa Serikali kutenga fedha ya kutosha na kuzisimamia vizuri Halmashauri zetu ili fedha nyingi itengwe katika maeneo haya kuondoa hizi changamoto ambazo tumekuwa tukizieleza kila siku.
Mheshimiwa Spika, suala la kuboresha miundombinu ya elimu liende sambamba na kuangalia shule zenye mahitaji maalum hasa zile zinazopokea watoto wenye mahitaji maalum yaani watoto wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Masasi kuna shule mbili; shule moja ilipata fedha katika mwaka wa fedha uliopita na kuboresha kwa kiwango kikubwa shule moja kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, lakini shule ya msingi Lugongo hali ni mbaya na hakuna vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine muhimu tunapozungumzia elimu ni suala zima la idadi ya walimu katika shule zetu. Umefika wakati Serikali iseme, wanapofanya majumuisho Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI atuambie, ni lini hasa wanaajiri walimu wa shule za msingi na ni lini hasa
wanaajiri walimu wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Spika, hata tufanye vipi, kwa uelewa wangu na kwa uzoefu wangu wa eneo la elimu, ni afadhali mwanafunzi asomee kwenye mwembe lakini mwalimu awepo. Mwalimu ndiye ambaye ana msaada mkubwa wa kumpa maarifa mwanafunzi. Tuna changamoto kubwa na
tumekuwa tukisema muda mrefu sana kwamba pamoja na kwamba tumetatua changamoto ya madawati, pamoja na kwamba tunaendelea kujenga majengo, lakini kama walimu hawapo wa kutosha, hali haiweze kuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna shule nyingine zina walimu wanne, wanafunzi 600. Hali haiwezi kuwa sawasawa katika kujifunza kwa watoto. Katika Jimbo la Masasi tunapungukiwa na walimu takribani 219 wa shule za msingi, tunapungukiwa na walimu 60 wa masomo ya sayansi; wanatakiwa walimu 84, wapo walimu 24 tu. Hatuwezi kuongeza ufaulu wa watoto katika mazingira ya namna hiyo. Kwa hiyo, lazima Serikali ifike wakati iajiri walimu hawa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo mambo haya yanatakiwa tuwianishe. Tunajenga mazingira mazuri ya kujifunzia watoto, lakini pia tunatengeneza mazingira ya maslahi kwa walimu wetu. Ni kweli kwamba Serikali inalipa madeni, hasa madeni yaliyo nje ya mshahara kwa walimu wetu. Pia ni kweli kwamba walimu bado wana malalamiko, tuendelee kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto zinazowakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 Serikali iliwapandisha baadhi ya walimu madaraja. Katika Jimbo langu, walimu 397 wa Masasi walipandishwa wakapokea mshahara mmoja baadaye wakashushwa. Hawa ni walimu wa Jimbo moja tu, eneo moja tu, walimu wana malalamiko, wanakata tamaa. Ulishapewa mshahara, baadaye unashushwa. Tunaomba Serikali iangalie namna gani inaweza kuyaangalia mazingira haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wapo walimu ambao walitakiwa kupanda madaraja kutoka mwaka 2014 mpaka leo hawajapandishwa madaraja. Mwaka 2010 Serikali iliondoa annual increment kwa walimu na ilikuwa pengine ni tofauti na mazingira ya mikataba waliyosaini wakati wanaajiriwa,
lakini mpaka leo walimu hawa hawajaambiwa kwa nini annual increment imeondoka, lakini hata kama wanaambiwa, bado wanabaki kuwa na malalamiko.
Tuangalie mazingira ya walimu ili tuone namna gani walimu hawa wanaweza kuwa na motisha pia ya kufundisha.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo eneo la uratibu katika shule zetu. Ipo changamoto hasa maeneo yale ambayo yana changamoto ya usafiri. Waratibu wa Elimu wa Kata wanashindwa kufanya kazi yao ya uratibu vizuri kwa sababu wengi hawana usafiri. Tunasikia kuna baadhi ya maeneo, waratibu wana usafiri, lakini tungeomba sasa tuyaangalie na maeneo ya kusini hususan katika Jimbo langu la Masasi, waratibu wetu wapewe usafiri angalau wa pikipiki ili waweze kuyafikia maeneo ya shule zao mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo katika eneo la afya. Kama kuna eneo lina changamoto kubwa sana ni eneo la afya. Tuna tatizo kubwa. Katika Jimbo langu, tuna tatizo linaloendana na upungufu mkubwa wa watumishi, hili ni tatizo kubwa sana!
Mheshimiwa Spika, tuna zahanati lakini hazina watumishi wa kutosha; tuna upungufu na tumeomba kupatiwa watumishi wa hospitali, takribani watumishi 56 wa huduma ya afya lakini hakuna hata mmoja aliyeajiriwa mpaka sasa. Huu ni wakati ambapo Serikali inatakiwa kusema ni lini inaajiri watumishi wa afya ili tuweze kupata rasilimali watu katika maeneo yetu ya huduma za afya?
Mheshimiwa Spika, katika eneo la afya hususan katika Jimbo langu bado kuna changamoto kubwa. Pamoja na kupungua kwa watumishi, lakini hatuna magari ya wagonjwa. Wilaya nzima kuna magari mawili tu ambayo moja ni bovu na moja ndiyo linalofanya kazi; siyo rahisi kuweza kuwapeleka wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka hospitali.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tungependa katika eneo la huduma za afya kuwe na upatikanaji wa dawa kwa wakati; hili pia limekuwa ni eneo lenye changamoto kubwa sana. Katika Hospitali yetu ya Mkomaindo mwaka 2014 ulifanyika ubadhirifu wa fedha za dawa.
Mheshimiwa Spika, niliwahi kuuliza swali, niliwahi kueleza masuala haya mara nyingi, lakini kila Waziri anapotoa majibu hapa, sijapata majibu ambayo yanaridhisha ni kwa nini hatua hazichukuliwi kwa watu ambao walihusika na ubadhirifu huu wa dawa mwaka 2014?
tunaomba Serikali ichukue hatua katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni ujenzi wa jengo la utawala. Jimbo langu la Masasi halina jengo la utawala lakini kwa bahati mbaya sana, fedha ambazo zilikuwa zime…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo. Pia nielekeze mchango wangu kwenye eneo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema lolote, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwatetea na kuwasimamia wakulima. Ni kweli kwamba kilimo kinachukua nafasi kubwa ya Watanzania, lakini pia ni kweli kwamba tunaendelea kuimarisha mifumo ya kutetea haki na maslahi ya wakulima kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pia kwamba kuna umuhimu mkubwa wa Wizara ya Fedha kuangalia uwezekano wa kutoa fedha za kutosha kwa Wizara hii. Ukiangalia ukurasa wa 25 wa hotuba ya Waziri, unaonesha wazi kwamba fedha zinazotolewa ni kidogo sana hadi kufika Mei mwaka huu. Haitawezekana kutekeleza mipango na mikakati ya Wizara hii ambayo inabeba msingi wa uchumi wa nchi yetu kama fedha zinazotolewa hazitoshi mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kufikiria utaratibu mpya wa utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa 100% kwa wakulima. Hili ni jambo kubwa sana na ni jambo ambalo linaweza likachochea maendeleo katika sekta ya kilimo, hususan sisi tunaotegemea kilimo cha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie utaratibu wa namna ambavyo mazao mchanganyiko yanaweza kununuliwa mwaka huu. Katika msimu uliopita wa mazao mchanganyiko kwa upande wa Mikoa ya Kusini, nazungumzia mbaazi na choroko, bei ya kilo moja ilikuwa shilingi 400 hadi shilingi 600. Ukweli ni kwamba bei hii haitoshelezi na haifanani na gharama za uzalishaji wa mazao haya kwa kilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza tayari wanunuzi wa choroko wameshafika kwa wakulima na wanaanza kununua choroko kwa shilingi 900; hii bado ni bei ya chini sana. Tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kusimamia uuzaji na ununuzi wa mazao haya ili kuwafanya wakulima wetu waweze kuona mazao yao yana tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa na Serikali kwamba wametafuta soko nchi za India, Vietnam na nchi nyingine ambazo wanatumia mazao haya kwa wingi, lakini hali halisi ya ununuzi wa mazao haya haiendani na kauli ya Serikali. Tunaomba sana, jambo hili liweze kusimamiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo kuhusiana na suala la kilimo cha korosho pamoja na suala la ununuzi na uuzaji wa zao hili. Naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuondoa tozo katika zao hili, kupunguza baadhi ya tozo. Tozo hizi baada ya kupungua zinapandisha bei, lakini zinatoa matumaini zaidi kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo katika zao la korosho zinawagusa kabisa wakulima. Zinawagusa na wanaziona zina tija kubwa, lakini yapo mambo ambayo Serikali inapaswa kuyatilia mkazo zaidi. Tunashukuru mwaka 2015/2016 ulifanyika ubadhirifu na Serikali katika mwezi huu inaendelea na imepiga hatua kubwa kuhakikisha kwamba wale waliofanya ubadhirifu katika tasnia hii ya korosho wanachukuliwa hatua kwa kuondolewa kwenye uongozi. Hili ni jambo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali, katika msimu wa 2016/2017 korosho zimenunuliwa kwa bei nzuri na wale waliofanya ubadhirifu mpaka sasa hivi tunavyozungumza kesi yao iko mahakamani. Haya ni mambo ya msingi yanayoendana kabisa na kasi ya Serikali ya kutetea maslahi ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo la kujiuliza, kuna ambao walifanya ubadhirifu mwaka 2015/2016 na kuna ambao wamefanya ubadhirifu mwaka 2016/2017 na mpaka sasa tunapozungumza wakulima wa korosho wanadai fedha zao hata kwa msimu huu uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa korosho 2016/2017 katika Wilaya ya Masasi peke yake wakulima wanadai zaidi ya shilingi bilioni 1.5. Umefika wakati sasa wa Serikali kuhakikisha wakulima hawa wanalipwa. Serikali inaweza kuangalia uwezekano wa kutumia hata fedha ambazo zilikuwa ni michango yao wakulima, fedha ambazo zimewekwa katika Mfuko wa Pembejeo. Je, Serikali haiwezi kutumia fedha hizi kuwalipa wakulima wakati wanaendelea na utaratibu mwingine wa fedha hizi kurudishwa? Kwa sababu hali ya wakulima wetu ni mbaya na wakulima wanaendelea kudai, na sisi tumechoka na huu mzigo wa kuwasemea kila siku wakulima kwa mambo ambayo hayatatuliwi. Fedha zao zinatakiwa zipelekwe, walipwe kwa sababu korosho hizi zimeshauzwa, fedha zimekwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kero imezidi kuwa kubwa. Tunaomba Serikali itoe tamko na Waziri anapofanya majumuisho atuambie na asiposema nitashika shilingi kuhakikisha kwamba Waziri anaeleza commitment ya Serikali katika jambo hili. Korosho za wananchi bado hazijalipwa katika msimu uliopita, Serikali inaendelea na huo utaratibu, lakini ituambie ni lini jambo hili litakwisha? Wananchi wameuza korosho toka mwaka 2016 mwezi Oktoba, wengine mwezi Novemba. Kwa hiyo, Serikali ituambie inafanya nini katika hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la ushirika. Tunalo tatizo na Serikali ina jukumu kubwa sana la kuimarisha ushirika. Sekta ya Ushirika kwanza inakabiliwa na rasilimali watu ambayo haina weledi wa kutosha wa kusimamia ushirika. Serikali tunaomba iliangalie hili kuanzia katika vyama vya msingi mpaka katika Chama Kikuu cha Ushirika ili kuwa na watu wenye weledi wa kutosha wa kusimamia hasa yanapofika masuala ya fedha za wananchi. Kwa hiyo, Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo lingine la ziada. Tunao watendaji wa Serikali, tunao watumishi ambao wana maslahi ndani ya mfumo wa ushirika na wana maslahi ndani ya biashara, hususan biashara ya korosho. Tumeeleza mambo haya kwa muda mrefu na Serikali baadhi ya mambo inaendelea kuyafanyia kazi; lakini tunaeleza wazi hatutakuwa tena tayari kuendelea kufanya kazi na watumishi ambao kwa namna moja ama nyingine wana maslahi ndani ya mfumo wa ununuzi na uuzaji wa korosho. Kwa kweli hawawezi kusimamia mfumo huu kwa kutetea maslahi ya wakulima wetu. Tunaomba Serikali iendelee kuchukua hatua na iwaondoe wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wanashiriki katika biashara ya korosho na kushindwa kuwasimamia wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo ya kuzungumza. Naunga mkono hoja ya Serikali. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Serikali kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kutoa pongezi kwa Waziri pamoja na Mawaziri wote kwa sababu mpango ni shughuli shirikishi, wamefanya kazi kubwa katika kuandaa dira hii ambayo sasa tunaichangia ili tuweze kuiimarisha zaidi, iweze kutupeleka kule tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ambayo inaendelea mpaka sasa. Mradi wa reli kwa kiwango cha standard gauge ni kazi kubwa, kuimarisha pia Shirika letu la Ndege ni kazi kubwa, kuendelea kuisimamia na kuimarisha sekta ya madini nayo ni kazi kubwa inayohitaji pongezi kubwa sana kwa Serikali, kuimarisha sekta ya usafirishaji pia ni kazi kubwa sana kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, pia kusimamia nidhamu kazini na kuendeleza ujenzi wa viwanja mbalimbali vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti nianze kwa kusema tu kwamba tunaingia katika utaratibu wa utekelezaji wa bajeti wa mwaka 2017/2018 ambao tumeshauanza, lakini pia tunazungumzia mpango kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka unakuja. Lipo jambo ambalo tunapaswa pia tuliulize na Serikali iendelee kulifanyia kazi kutokana na utekelezaji hafifu wa bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma mpango katika ukurasa wa 20 inaonesha kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 ni asilimia 55 tu ya fedha ya miradi ya maendeleo zilizokwenda kwenye miradi yetu. Hii inaleta picha ifuatayo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tunapaswa kuongeza upya vyanzo vyetu vya mapato, lakini inawezekana pia kuna mahali ambapo tunazo sheria zinazotukwaza katika usimamizi wa fedha lakini tunahitaji kuongeza juhudi kubwa katika kusimamia na kudhibiti matumizi na mapato ya Serikali. Naikumbusha Serikali kwamba katika bajeti ya 2016/2017 ilikuwa ime-allocate fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Baadhi ya fedha bado hazijafika katika miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali iweke msisitizo mkubwa katika mpango huu kwa kuhakikisha kwanza tunakwenda kuimarisha au kutatua kero za wananchi kwa ile miradi ambayo inagusa huduma za jamii, hususani maji, umeme na afya. Haya ni mambo ambayo napenda Serikali yangu iyape kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuikumbusha Serikali kwamba bado ina kazi ya kuendelea kusambaza fedha za miradi ambayo iliahidiwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Katika mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Mji wangu ilitengewa fedha shilingi milioni 599 kwa ajili ya uchimbaji wa mifereji na usambazaji wa maji ya bomba, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi tunavyozungumza fedha hizo hazijafika katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inachelewaesha kuanza kwa mradi lakini inaongeza kero kwa wananchi kwa sababu tayari wameshachimba mifereji na sasa wanasubiri fedha. Nimezungumza na Waziri wa Maji amesema kwamba fedha hizo tayari ameshazi-approve kutoka Wizarani lakini zimekwama Hazina. Namwomba Mheshimiwa Mpango ahakikishe fedha hizi zinakwenda haraka kwa sababu mvua zikinyesha mifereji ambayo walichimba wananchi kwa njia ya kujitolea itaziba, hatimaye tutaanza tena kupigizana kelele na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na suala la maji kuna suala la umeme, kila Mbunge anayetoka Kanda ya Kusini lazima azungumze kuhusiana na suala la umeme. Tuna kero kubwa sana katika eneo hili tumezungumza mara nyingi na Waziri, tumezungumza mara nyingi na Watendaji wa TANESCO. Ukweli ni kwamba hali ya umeme katika Mikoa ya Kusini ni mbaya sana na ubaya zaidi kwamba ni kipindi sasa cha takribani miaka miwili ahadi ambazo tumekuwa tukipewa ili kuondoa tatizo la umeme hazikamiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Naibu Waziri amezungumza kwamba mwisho itakuwa mwezi wa Disemba tatizo la umeme litakuwa limekwisha. Tunaomba Waziri wa Fedha, tunaomba Waziri wa Nishati ahakikishe kwamba tatizo hili kweli linakwisha kwa sababu wananchi wanashindwa kufanya biashara, wananchi wanashindwa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa sababu tatizo la umeme ni kubwa sana. Kitu kikubwa kinachowaumiza wananchi wa Mikoa ya Kusini ni kwamba Kusini ni chanzo cha gesi ambayo pia inatumika huku katika miji mingine kwa ajili ya kusambazia umeme, kwa nini tuna shida kubwa kwa kiwango hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa napitia mpango, sioni mahali ambapo kuna mpango wa kuimarisha au kufufua viwanda vyetu vya korosho. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza, binafsi nimemwandikia barua Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na pia nimepeleka barua Wizarani kwake na kumkabidhi Katibu, tunaomba maelezo ya kina kwa nini Kiwanda cha Korosho cha Masasi hakifufuliwi? Nani kapewa kiwanda kile na mamlaka gani imemfanya akifanye kuwa ghala la kuhifadhia korosho badala ya kuleta mitambo na kubangua korosho. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inalitatua na inalishughulikia kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niseme kidogo katika suala la kilimo, tunashukuru Serikali watu wa Kusini tukizungumzia kilimo tunazungumzia korosho, tunaishukuru sana Serikali kwa hatua iliyofikia, korosho inauzwa vizuri lakini zipo changamoto ambazo tungependa Serikali iziangalie. Kwa mfano, tumepata changamoto kubwa ya uhaba wa pembejeo katika mwaka wa fedha uliopita lakini ninaposoma mpango huu sioni mahali ambapo Mheshimiwa Mpango ameonesha usambazaji wa pembejeo aina ya sulphur utakavyokuwa kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. Tunaomba eneo hilo liingizwe ili tuweze kuona namna gani sasa Serikali inawasaidia wakulima wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo eneo lingine ambalo ningependa kuikumbusha Serikali, tunayo miradi ya barabara ambayo inaendelea na mengine inaendelea kwa taratibu mno, tunayo barabara yetu ya kutoka Nanganga kuelekea Nachingwea – Masasi, barabara hii hatuoni kazi inayofanyika kwa kweli, tungeomba Serikali iongeze juhudi na kutoa fedha za zakutosha barabara hii ikamilike ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ya kutokea Mtwara inakwenda Tandahimba, inakwenda Newala, inakuja Masasi nayo hii hatuoni Serikali kama ina kasi kubwa ya kutaka kuimaliza tunajua kazi imeanza, tunaomba Serikali iongeze fedha za kutosha katika mwaka wa fedha ujao na mwaka wa fedha huu ili tuweze kukamilisha barabara hizi kwa ufanisi zaidi na kwa haraka ziweze kupitika tuwe tumetekeleza tuliyowaahidi wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wetu kuna eneo la kufunganisha maendeleo ya watu na shughuli za kiuchumi. Nataka niseme kidogo katika eneo la elimu, mwaka wa kwanza nilichangia na jambo hili nililisema halikuwepo katika mpango mpaka last version, mwaka wa pili nilichangia tena na mwaka wa tatu huu nachangia. Hakuna nchi inayoweza kuendelea duniani katika sekta ya elimu bila ya kufikiria namna ya kuendeleza sekta ya elimu isiyo rasmi, elimu nje ya mfumo rasmi. Jambo hili nalieleza mara nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo matamko yanatolewa na viongozi wetu, kwa mfano mtoto akishapata mimba haruhusiwi tena kusoma, tunajiuliza mtoto yule anatakiwa aende wapi? Wapo watoto ambao wanashindwa kumaliza elimu ya Sekondari kwa sababu mbalimbali zikiwemo za utoro, umaskini uliotopea na mambo kadha wa kadha. Wapo ambao pia wameacha kusoma shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pamoja na wingi wa wanafunzi tulionao katika elimu rasmi watu ambao wanahitaji elimu walio nje ya mfumo wa elimu rasmi ni wengi zaidi. Nataka nikupe tu mfano mdogo, kwamba katika sensa ya watu iliyofanyika mwaka 2012 watu milioni 5.5 sawa na asilimia 22.4 ya Watanzania walionekana hawajui kusoma na kuandika. Ukisoma ripoti ya UNESCO ya mwaka 2014 inaonyesha kwamba tatizo hili linaendelea siku hadi siku...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya mimi kuchangia kwa muda wa dakika tano, nitazitumia vizuri. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri pamoja na wasaidizi katika Ofisi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwa kifupi, nataka nichangie kwenye hifadhi ya jamii. Watumishi waliostaafu wa Jimboni kwangu Masasi wameniagiza niseme kwamba kutoka mwaka jana mwezi Juni mpaka leo hawajalipwa mafao yao lakini pia wananchi hawa ambao wamestaafu hawajapewa hata fedha za kuhamisha mizigo kurudi majumbani mwao. Jambo hili linahuzunisha sana kwa sababu watu hawa wamekwishatumikia nchi hii na wameshafikia umri wa kustaafu, Serikali inapaswa kuwalipa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kidogo pia kwenye kilimo. Niishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha sekta hii lakini pia sisi watu wa Kusini tunazo changamoto ambazo lazima tuziseme. Moja, toka tumepata tatizo la wakulima wa mbaazi kwa kutokupata bei mpaka leo Serikali haijasema kama iko tayari na imeshatafuta soko la mbaazi. Mpaka sasa hatuna majibu kwa wakulima kwa sababu mbaazi ziko mashambani tena, mwaka huu utaratibu ukoje katika kupata soko la mbaazi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tukumbuke Serikali katika msimu wa korosho uliopita ilitoa sulphur bure kwa wakulima na sisi tulifanya kazi kwenye mikutano kuwashawishi wakulima wapate sulphur hiyo na Serikali ipeleke. Sasa tumebadilishiwa utaratibu tunaambiwa wakulima wanatakiwa wanunue sulphur.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaiomba Serikali itoe kauli haraka ili wakulima wajue sulphur hiyo inapatikana vipi tena kwa kudhibiti bei ya soko la sulphur. Kwa sababu mpaka sasa hivi tunavyozungumza bei ya sulphur ni Sh.70,000, Sh.80,000 kwa mfuko ambao walikuwa wananunua kwa Sh.27,000. Kwa hiyo, Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti bei hii ili wakulima wetu wamudu kuinunua na ipatikane mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kidogo kuhusu suala la maji. Tunalo tatizo kubwa katika nchi yetu na Serikali kweli inafanya kazi ya kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapata maji. Hata hivyo, katika Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Masasi na Nachingwea tunategemea chanzo cha maji cha MANAWASA. Hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo haya ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema mbaya sana kwa sababu hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja tulimwambia kwamba, MANAWASA wana tatizo kubwa la kutokwepo chujio la kuchuja matope, kiasi kwamba katika kipindi hiki chote wanafunga maji kwa sababu maji yale yanakuja yakiwa machafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika randama tumeona mmepanga shilingi bilioni mbili kuwapa MANAWASA lakini kwa sababu mara nyingi bajeti ya MANAWASA inakuwa haitoki, tunaomba sasa Serikali kwa kipindi hiki kilichobaki bajeti hii ya shilingi hizo bilioni mbili ipelekwe kwa ajili ya kufanya usanifu wa chujio la kuchuja tope ili wananchi wetu wapate maji na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni umeme. Wabunge wengi wamezungumza, pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali lakini bado Mkoa wa Mtwara tuna tatizo la umeme, umeme unawaka kama indicator ya gari, unawaka unazimika, unawaka unazimika. Tumekwishaambiwa juhudi zinazofanywa na Serikali kwamba sasa hivi wanataka kufunga mashine nyingine ambayo itaongeza kiwango cha umeme. Tungependa Serikali ifanye jambo hili haraka kwa sababu linaharibu utaratibu mzima wa wananchi wa Jimbo langu pamoja na Mkoa mzima wa Mtwara kutokana na kukatikakatika umeme bila sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni REA. Nimezungumza na Waziri, nimezungumza na viongozi wa TANESCO, Jimbo la Halmashauri ya Mji wa Masasi vijiji vingi vimesahaulika. Tunaomba Waziri atakapokuwa anahitimisha atoe kauli ni vijiji gani sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Mheshimiwa Nabu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya mimi kuchangia angalau dakika tano. Nataka niseme tu kwamba naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake inayoonesha kwamba tumepiga maendeleo makubwa sana katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo ningependa kuzungumza ni kuishukuru tena pia Serikali kwa kunipatia uhakika wa kupata fedha kwa ajili ya kujenga kituo kimoja cha afya cha miongoni mwa kata zangu, kwangu mimi hili ni jambo kubwa sana katika kuboresha afya za wananchi wetu wa Masasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee pia suala la Hospitali ya Kanda ya Rufaa. Ni muda mrefu sasa Serikali imekuwa ikizungumza na ikiwa na utaratibu wa kutaka kujenga Hospitali ya Kanda ya Rufaa katika Mkoa wa Mtwara, lakini kwa bahati mbaya sana jambo hili linakwenda taratibu mno. Tunasikia kwamba NHIF wamepewa dhamana ya kutaka kumalizia hospitali hiyo, lakini mpaka sasa hatujui kwa sababu hatuoni kinachofanyika. Tungependa kusikia kauli ya Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake, ni kwa vipi wamejipanga kukamilisha Hospitali hii ya Kanda ambayo itakuwa inahudumia mikoa ya Ruvuma, Lindi pamoja na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini nizungumze kidogo kuhusu suala la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Wabunge wa Mtwara wamezungumza jambo hili na sisi katika jambo hili ni wa moja sana nataka kusema miongoni mwa mambo ambayo ni magumu na ni mazito sana kwetu kuyatolea maelezo ni hali ya hospitali yetu ya mkoa. Hospitali hii ina hali mbaya sana kwa upande wa watumishi natoa tu mfano; kwa mfano tunatakiwa na Madaktari Bingwa 24 lakini tunao Madaktari Bingwa wawili tu, tunatakiwa tuwe na madaktari wa kawaida 30 tunao saba, Madaktari Masaidizi (AMO Assintant Medical Officers) tunatakiwa tuwe nao 23 tunao wanane tu, nursing officer wanatakiwa wawe 37 tunao wanne.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa ma-nurse wengi kwa sababu wanatakiwa wawe 131 tunao 44 tu. Hali ya hospitali hii ni mbaya na inajhitaji jicho la kipekee la Serikali ili kuhakikisha kwamba hospitali hii inaimarishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatukuishia hapo tu katika changamoto za hospitali hii kuna miundombinu chakavu sana. Tuna matatizo ya vifaa tiba, kwa mfano tunayo x-ray zeefu na ni ya kizamani sana na inaharibika mara kwa mara, tungependa Serikali sasa itupatie digital x-ray ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi wetu kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika katika chumba cha upasuaji hata mashine ile ya kuchemshia vifaa nayo imezeeka sana, lakini pia inaharibika mara kwa mara na inakwamisha sana shughuli za hospitali. Mashine ya kufulia nguo pamoja na mashuka ya wagonjwa ni mbovu na imezeeka sana, tungependa Serikali iangalie mambo haya. Kwa bahati mbaya sana tunalo gari moja tu la kusadfirisha wagonjwa na gari hilo nalo limezeeka sana, tunasikia kwamba Serikali ina mpango wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua gari lingeni la wagonjwa yaani ambulance, tungependa Serikali ikamilishe jambo hili haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Mji wangu wa Masasi hatujapata bado fedha kiasi fulani cha fedha katika mfuko wa afya. Tulitengewa shilingi milioni 187 tumepata shilingi milioni 76 tu. Tunaimani Serikali sasa inapaswa kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakwenda haraka iwezekananvyo ili tuweze kupata nasi fursa ya kununua dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze kidogo kuhusu huduma ya tumaini la mama; hii ni huduma nzuri na naipongeza sana Serikali kwa hatua iliyofikia. Hata hivyo nataka niseme kitu kimoja tu, kabla Serikali haijaanza jambo hili katika jimbo langu mimi nilikuwa natumia mfuko wa jimbo kununua package hizi kwa ajili ya akina mama kujifungulia. Hata hivyo hata baada ya Serikali kuanzisha utaratibu huu bado ninalazimika kutenga baadhi ya fedha kutoka kwenye mfuko wa jimbo kwa ajili ya kununua vifaa vya akina mama kujifungulia kwa sababu huduma ya tumaini la mama haitoi vifaaa vyote tunaomba sasa Serikali kwa sababu huu ni mpangao ambao umeamua kuianzisha kwanza mpango huu uwe endelevu, lakini pili u-accommodate vifaa vyote ambavyo vinahitajika kwa ajili ya akina mama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye eneo letu hili la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa juhudu kubwa inazofanya kwenye sekta hii, pia kwa namna ya kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako kwa kazi kubwa anayoifanya katika elimu pamoja na watendaji wake wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nilipokuwa ninasimama kwa ajili ya kutoa mchango kwenye wizara hii muhimu nimekuwa nikizungumza kuhusu non formal na adult education, yaani elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi. Nina hamu sana ya kuiona Wizara ya Elimu, kisera ikiwa inatambua kwamba ina jukumu la kuwaelimisha Watanzania wote bila ya kuzingatia wale tu ambao wako madarasani kwa sababu Watanzania wote wanategemea wizara hii ili kupata elimu kwa namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza hili ninaiona kabisa Serikali yetu ilishaamua kuiunda taasisi maalum ambayo itafanya kazi ya kusimamia elimu nje ya mfumo rasmi pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Hapa ninaitaja Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na ninaitaja hii kwa makusudi kwa sababu miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanajua kusoma na kuandika hata kama wako nje ya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha kutojua kusoma na kuandika kinaongezeka sana kwa wananchi wa Tanzania. Katika kipindi kilichopita katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilisimamia sana hili la kuhakikisha kwamba ni lazima kumuelimisha kwanza mtu mzima halafu mtoto baadaye kwa sababu mtu mzima tunamtumia sasa hivi wakati mtoto tuna muda wa kusubiri kumtumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema, ukiangalia Ripoti ya Adult Literacy Survey ya mwaka 2014 inaonesha kwamba kutoka mwaka 1986 Watanzania asilimia 9.6 walikuwa hawajui kusoma, lakini sasa katika mwaka 2012 wameongezeka mpaka asilimia 31, sasa leo ni mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inao mkakati ambao inapanga kuutekeleza, mkakati huu unaitwa National Literacy and Mass Education Strategy. Huu ni mkakati madhubuti waliouandaa kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma pamoja na kutoa elimu na hamasa maalum kwa wale watu ambao hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuishauri na kuiomba sana Serikali kwanza iangalie Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, lakini pia ihakikishe inatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huu unakwenda mbele ili Watanzania waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine ambalo ni lugha, nimekuwa nikisema kila siku. Kama kuna jambo ambalo linatatiza mfumo wetu wa elimu ni lugha tunazozitumia. Hili lazima niliseme wazi. Ukiwasikiliza baadhi ya wataalamu wanaozungumza kuhusu elimu wanazungumza kuhusu tatizo kubwa la ufaulu katika sekta yetu ya elimu, lakini wanapozungumza jambo hilo hawazungumzi kama tuna mkanganyiko mkubwa sana katika matumizi ya lugha, hawasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza ripoti za TWAWEZA, ukiwasikiliza Haki Elimu pamoja na mashirika mengine wanaofatilia michakato ya kujifunza katika mfumo wetu wa elimu hawasemi wazi kama tuna tatizo kubwa la matumizi ya lugha. Hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea na kupata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu kwa kutumia lugha za watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili mimi nalisema wazi. Ninaweza nisieleweke kwa sababu hata pengine wasimamizi wa mfumo huu tumepita katika mfumo ambao bado kwetu ni kikwazo. Kwa hiyo, ukiambiwa leo tujifunze kemia au fizikia kwa kutumia kiswahili utaona shida lakini kujifunza kemia au fizikia kwa kutumia kireno, kifaransa, kichina, kijerumani tunaona inawezekana. Kwangu mimi hili ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hakuna lugha iliyo bora kuliko lugha nyingine, na hii ni kwa mujibu wa Profesa Noam Chomsky ambaye ni mtaalamu wa isimu ya lugha, anasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ndiyo inayotufundisha namna ya kutazama na kuutafsiri ulimwengu wetu. Hakika tuna mkanganyiko mkubwa. Leo hii katika zile shule ambazo wanatumia lugha ya kiingereza kujifunza kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la tatu hautakiwi kugusa kiswahili. Katika shule wanazotumia kiswahili kama lugha ya kufanyia mawasiliano ya kujifunza hawatakiwi kugusa kiingereza mpaka wanafika darasa la tatu. Lakini wakifika darasa la nne wanafanya mtihani mmoja hawa wanafanya kwa kiingereza, hawa wanafanya kwa kiswahili, lengo letu ni nini? Lengo letu ni kuwashindanisha wanafunzi kwenye umahiri wa lugha au kuwashindanisha wanafunzi kwenye umahiri wa maudhui ya masomo yetu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana katika jambo hili na ni lazima Serikali ifike wakati wa kufanya maamuzi magumu. Mimi nataka nikwambie kama Serikali inaamua leo, kwa mfano wanafunzi wajifunze kwa kutumia lugha yetu inawezekana kabisa wakajitokeza watu wakasema tunataka tusisaidie mfumo wa elimu ya Tanzania kwa sababu tunaondokana na kujifunza kwa lugha ya wakoloni, hili ni jambo gumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie kwamba ni vyema sasa hivi tukafikiria namna bora ya kujifunza, kwa sababu watoto wetu wana kikwazo kikubwa sana katika kujifunza wanajifunza kwanza kukielewa kiingereza halafu wanajifunza kuelewa maudhui ya somo. Lakini hivi ni kitu gani kinaweza …

T A A R I F A . . .

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kukataa ni kwamba ni Wabunge wote na Mawaziri wote, lakini wapo ambao watoto wao wanasoma katika mfumo huo wa kukwepa kiswahili na kwenda kwenye kiingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja, kwamba umefika wakati wa Watanzania kufanya maamuzi. Tunawaweka watoto wetu katika mfumo wa lugha ya kiswahili mpaka wanafika darasa la saba, tukitoka darasa la saba tunakwenda form one mpaka form four tunabadilisha ghafla wanasoma kwa kiingereza, halafu baadaye wanakwenda tena chuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nchi gani duniani inafanya mambo haya? Tumebakiwa ni nchi za kiafrika ambazo tunalazimika kutumia aidha kifaransa au kiingereza kwa sababu ni lugha ambazo tuliachiwa. Tufanye maamuzi, nchi nyingi ambazo zimeendelea wanatumia lugha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa kuwe na chombo maalum kitakachoangalia na kusimamia mfumo wetu wa ubora wa elimu, hili ni tatizo pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli kabisa ni kwamba zipo shule binafsi ambazo zinaanzishwa na zinasimamiwa vilivyo na Serikali ili kukidhi mahitaji, lakini pia tunazo shule za Serikali ambazo nazo pengine zingeweza kusimamiwa na chombo kinachojitegemea ili kuziongezea ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tufike wakati wa kuona tuwe na chombo maalum ambacho kinaangalia pia shule zetu za Serikali, kwa sababu shule za private kukiwa kuna walimu watatu kuna uwezekano wa kusema tunafunga shule, lakini katika shule za Serikali ili ku- maintain ubora wa elimu mimi naishauri Serikali ione umuhimu wa kuwa na independent board ambayo inaweza pia kuzisimamia shule hizo. Lengo ni kuondoa pia matabaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matabaka makubwa wapo watoto ambao wanaonekana wanasoma shule bora sana wanatumia lugha bora sana lakini wapo watoto ambao wanaonekana wanasoma shule za chini sana. Ili kuondoa haya matabaka pia kingekuwepo chombo kinachoweza kuiangalia Serikali na kuisimamia ili tuweze kwenda vizuri na shule zetu pia nazo ziwe shule bora kama ilivyo katika shule zingine za private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya nashukuru sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kupata nafasi ya kuzungumza kidogo kuhusiana na Wizara hii muhimu kwa uchumi wa Taifa letu, Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Serikali pamoja na Mawaziri kwa kazi wanayoifanya kwa sababu changamoto katika kilimo zipo lakini yapo mambo ambayo hata wakulima wa korosho tunaona wameyafanya katika kupiga hatua mbele ya kutetea wakulima wetu. Changamoto zipo nasema lakini yapo mambo ambayo yamefanyika niwapongeze sana katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 80 ya chakula kinachozalishwa Sub-Saharan African pamoja na Asia kinazalishwa na wakulima wadogo wadogo ambao wanatengeneza ajira takribani kwa watu bilioni mbili. Sambamba na hilo asilimia zaidi ya 70 ya watu wanaoishi kwenye Bara la Afrika ni wakulima wadogo wadogo, Tanzania tuna asilimia zaidi ya 60 ya wakulima wadogo wadogo. Hakuna ubishi kwamba this is the largest private sector on earth, lazima Serikali iangalie namna ya kutetea, kuwasimamia na kuwasaidia wakulima wadogo wadogo. Hata mjadala wetu katika Bunge kuanzia jana unawagusa wakulima wadogo wadogo. Ni muhimu Serikali sasa iangalie namna ambavyo inajikita sawasawa katika kupunguza au kuondoa kero zinazowakabili wakulima wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao utaratibu unaosemekana wa kuanzishwa kwa mabenki kwa ajili ya kuwakopesha wakulima wetu, ukweli unabaki pale pale kwamba wakulima hawa hawakopesheki. Inawezekana hawakopesheki kwa sababu miundombinu yetu ya kisera, kwenye sera ya kilimo au sera ya fedha lakini inawezekana hii inatokana na sababu ya miundombinu ya utaratibu mzima wa kuangalia namna gani mabenki haya yanaweza yakawa- favor wakulima wetu haijakaa sawa. Tunahitaji kubadilisha taratibu zetu za kifedha au sera zetu ili wakulima hawa waweze kukopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umefika wakati wa Serikali kuangalia kwa kina ni namna gani inaweza kusimamia matumizi bora ya ardhi zetu. Ukweli uko wazi kabisa kwamba Tanzania ina ardhi kubwa, lakini yapo maeneo ambayo yanakabili sawa wakulima wadogo wadogo kutokana na kuingiliana na wafugaji kwa ajili ya migogoro inayotokea hapa na pale. Migogoro ya ardhi pamoja na migogoro ya vyanzo vya maji haya ni maeneo ambayo Serikali inatakiwa ichukue hatua ili mkulima aweze kufanya kazi yake kwa tiza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sasa umekwishafika kwa ajili ya Serikali kuangalia namna ambavyo wakulima wanaweza wakawa na bima katika shughuli zake za kilimo, hili ni jambo la muhimu sana. Ni jambo muhimu kuanzia mkulima anakwenda kuandaa shamba mpaka anapeleka mazao yake sokoni. Kwa sababu tunapoweza kuangalia mnyonyoro mzima wa thamani ndivyo tunavyoweza kuboresha maisha ya mkulima kwa kupunguza athari au risk inayoweza kumpata katika shughuli zake za kilimo. Haya ni mambo ambayo ni ya muhimu Serikali yetu ya Awamu ya Tano iangalie ili kuimarisha wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo pia eneo lingine, kilimo cha sasa lazima kiende sambamba na kisukumwe na haja ya soko la ndani na soko la nje. Ni lazima wakulima wetu wasimamiwe vizuri kabisa, namna gani wanaweza wakafanya kilimo chao kuwa biashara, wakati huo huo Serikali iangalie namna ya kupanua soko la ndani. Wabunge wengine wamekwishazungumza kwamba ili kutengeneza soko la ndani liwe na fursa ya kutosha ni lazima tuangalie namna ambavyo tunapanua uwekezaji katika viwanda vyetu ili Serikali iweze kuona namna gani wakulima wanaweza kuuza raw materials kwenye viwanda, wakati mnafikiria soko la nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la nje ni muhimu kwa sababu tunahitaji fedha za kigeni, lakini soko la ndani ni muhimu zaidi kwa sababu tunahitaji wakulima hawa waweze kupata soko la uhakika. Leo hii tunauza asilimia zaidi 95 nje ya nchi. Leo hii tunauza pamba zaidi ya asilimia 80 nje ya nchi, hivi Wahindi ambao kwa mfano ambao ni wanunuzi wakubwa wa korosho pamoja Vietnam, wakisema sasa korosho ambazo wanalima huko zinawatosheleza tutauza wapi hizi korosho? Kwa hiyo, ni muhimu kuimarisha viwanda vyetu vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye masuala mengine ambayo Wabunge wameyazungumzia kwa kina. Mwaka huu Serikali kupitia Bodi ya Korosho ilifanya kazi ya kuingia mikataba na vikundi vya ujasiriamali pamoja na watu binafsi kwa ajili ya kuzalisha miche ya korosho. Katika mikataba ile Serikali iliwaahidi kuwalipa asilimia 30 kabla ya kuanza kufanya kazi na baadae kumalizia asilimia 70 ya malipo yao ili waweze kusambaza miche ya korosho. Ile advance payment haijalipwa, lakini kwa bahati mbaya sana mpaka leo hao waliosambaza miche kwa ajili ya mikorosho nao hawajalipwa. Hili ni jambo serious sana, kwa sababu ikiwa kila ambao wanajitolea na wanaonyesha uzalendo wa kusaidia sekta hii ya kilimo wanachelewa sana kulipwa fedha zao, utafika wakati watu wataona Serikali yetu haiko serious katika kuhakikisha kwamba wakulima wanapata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo jambo lingine la muhimu na wengine wamekuwa wakilisema, mwaka 2015/2016 walitokea watu ambao walikuwa wanasambaza pembejeo mawakala. Hili jambo kila Mbunge amekuwa akilisema na mimi nasema umefika wakati sasa unajua ukiwaona hawa mawakala wako very loyal na wanaonesha kabisa kwamba fedha ambazo wanaambiwa na Serikali ndizo zinadaiwa kama deni siyo fedha sahihi. Inaonekana kwamba ni bilioni 35 tu ambazo ziliidhinishwa lakini ukizungumza na mawakala wanaonyesha wazi kabisa kuna vocha zilibaki na zilirudishwa kutoka katika Mikoa hawajui vocha hizi ziko wapi? Deni linaonekana ni shilingi bilioni 64, ukweli ni kwamba madai ya mawakala wetu ni tofauti na fedha zilizoandikwa na watendaji waliosimamia zoezi hili.

Kwa hiyo, ni aibu sana miaka karibu miaka mitatu, minne tunazungumzia tunawahakiki, tunawahakiki kitu gani? Wale walioiba tunawafahamu tukamate tuweke ndani na hawa watu wengine walipwe. Hili ni jambo muhimu sana ambalo tunapaswa kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mpaka leo wananchi wangu wa Masasi wameniagiza sana niseme sulphur haijafika na ile ambayo inauzwa kwa bei ambazo siyo rasmi na siyo halali zinauzwa zaidi ya shilingi 70,000 kwa mfuko mmoja. Ni lazima sasa Serikali...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi nashukuru kupata fursa ya kuchangia kidogo katika maeneo ambayo nilipata nafasi ya kuyamakinikia wakati ninapitia vitabu vilivyotolewa na Serikali kwa ajili ya mjadala wetu wa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na kutoa pongezi kwa Serikali kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutekeleza miradi katika kipindi ambacho wameikiainisha, lakini niseme tu wakati najaribu kumakinika zaidi kwenye taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2016/2019 sikuona kazi zilizofanywa na Wizara ya Maji kwenye kitabu hiki. Kama itampendeza Waziri Mpango basi atupatie miradi hiyo tuione maana tuna wajibu wa kujua Wizara yetu ya Maji imefanya kazi kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine nilitaka kufahamu utekelezaji wa suala la maji kwa Serikali kwa upande wa Mradi wa Maji wa Mbinji ambapo tulitengewa shilingi bilioni mbili katika kipindi kilichopita kwa hiyo, tungepeta fursa ya kuona utekelezaji huo tungeweza kujua kama fedha hizo zimetoka au zimefikia katika hatua gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapopitia mapendekezo ya mpango pamoja na utekelezaji wa miradi bado naona kuna kazi kubwa na Serikali inapaswa kuona umuhimu sasa wa kutenga fedha za kutosha kwenye miradi ambayo inatoa huduma za jamii, huo ndio mtazamo wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya umeme, tuna miradi ya maji, lakini pia tuna suala la elimu, hayo ndio maeneo matatu nitakayoyazungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na umeme, suala la usambazaji wa umeme wa REA kwa kweli, haliendi sambamba na matarajio ambayo sisi kama Wabunge tunayo. Kwa hiyo, kwa mfano ukisoma kitabu cha utekelezaji ukurasa wa 55 inaonesha kwamba takribani vijiji kama 5,000 ndivyo ambavyo vimefikiwa katika mpango huo. Tukumbuke tunao mpango wa utekelezaji wa REA kwa awamu ya tatu sasa na zaidi ya vijiji 7,000 mpaka sasa bado havijafikiwa. Ukienda kwenye mapendekezo ya mpango, katika mapendekezo ya mpango ukurasa wa 30 inaonesha kwamba mwaka kwa 2019/2020 matarajio ni kufikia vijiji 557.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Mkoa wa Mtwara peke yake, Wilaya ya Nanyumbu, Wilaya ya Masasi, Wilaya ya Tandahimba, Wilaya ya Newala na Wilaya ya Mtwara DC utaona kwamba wastani wa utekelezaji wa mpango huu wa REA kwa jumla ukitafuta wastani ni kama vile ni 23.6% jumlisha na bajeti ya 2018/2019. Katika mkoa huu peke yake vijiji 497 vimeachwa mpaka sasa bado havijafikiwa, lakini 2019/2020 tuna mpango wa kufikia vijiji 557, vijiji vingine hivi tunavifikia lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda unakwenda na hapa mimi napendekeza sasa kama tatizo linaloonekana katika utekelezaji wa miradi ya REA ni fedha, basi napendekeza Serikali ione umuhimu sasa wa kupunguza fedha katika baadhi ya miradi mikubwa ambayo tunataka kuitekeleza ili tupeleke fedha hizo kwenye miradi inayowagusa wananchi, hususan miradi ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la maji, tatizo liko palepale, fedha katika utekelezaji wa miradi. Ukisoma hotuba ya Waziri ukurasa wa 31, inaonesha kwamba tumeshawafikia Watanzania milioni 31 kuwawekea maji ya bomba. Hii ni kama 50% tu ya Watanzania wote, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika hili na bado nashauri, ili kuweza kufikia miradi mingi kwa pamoja na kuwafikia wananchi wengi ni muhimu Serikali ikaona umuhimu wa kupeleka fedha za kutosha kwenye miradi hii na ikibidi kupunguza fedha kwenye baadhi ya miradi mikubwa, ili kufika katika miradi ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la elimu, kila nilipokuwa nachangia mpango nimekuwa nikisema kwamba mipango inayoletwa na Serikali pamoja na mambo mazuri mengi yanayofanywa, lakini haigusi elimu nje ya mfumo rasmi na leo nitarudia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, tangu tumeanzisha kutoa elimu bila malipo, kwa mfano katika shule ya msingi wanafunzi wengi sasahivi wanaandikishwa na wengi wanamaliza, lakini bado najiuliza wanafunzi hawa ambao kimsingi shule za msingi ni nyingi sana kuliko shule za sekondari, wanapomaliza, ni wazi kabisa watoto hawa kwanza wengi wao ni watoto wa wanyonge na hawawezi kwenda shule za sekondari za kulipia au shule za binafsi, lakini katika shule za sekondari za Serikali wanachukuliwa wachache, wengi wanabaki, wanakwenda wapi? Hili ni swali ambalo najiuliza kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa tu mfano, ukisoma Ripoti ya UNICEF ya mwaka 2018 inaonesha kwamba walifanya utafiti kwenye watoto milioni 3.7 wakabaini kwamba katika watoto wale milioni 3.7 wenye umri wa miaka 14 mpaka miaka 17 ni watoto 59.1% ndio ambao walikuwa shuleni, takribani 40.9% hawakuwa madarasani, hawakuwa shuleni, walikuwa mitaani na wapo katika umri wa kupata elimu. Na watoto hawa walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili tu, kulikuwa kuna watoto ambao hawakwenda kabisa shuleni na kulikuwa kuna watoto ambao wameacha shule. Hivi kweli Serikali inajua kwamba inalo jukumu la kutoa elimu hata kwa watot ambao wako nje ya mfumo wa elimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba ni muhimu Serikali itambue kuwa pamoja na juhudi inazozifanya za kuhakikisha kwamba Watanzania waasoma bila ya kulipa, lakini hata tufanye nini hatuwezi kuwa- accommodate Watanzania wote kwenda form one kwa sababu shule hatuna za kutosha. Kwa hiyo, kwa namna yoyote lazima tuwe na alternative means ya kuhakikisha kwamba, hawa watoto wanapata elimu kwa sababu wapo wanaoacha shule kwa sababu ya mimba, utoro, migogoro ya kifamilia na wapo wanaoacha kwa sababu ya uyatima. Baada ya kuacha shule ambazo ni shule rasmi za Serikali sisi kama Wabunge tunao wajibu wa kuiambia sasa Serikali ichukue majukumu haya ya kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanapata elimu kwa sababu, nao ni watoto ambao wanahitaji kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nizungumze kitu kimoja, tunayo Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ambapo inaonesha takwimu zake kutoka mwaka 2004 mpaka mwaka 2017 imepitisha takribani watoto 159 kumaliza kidato cha nne, 159,000 yaani 150,000 kumaliza kidato cha nne. Hawa watoto ni wachache, maana yake Serikali katika watoto karibu milioni ambao tunawaacha kila mwaka wasioweza kuingia shuleni au wanaoacha shule tunawaacha wakiwa mtaani. Hii ina maana kwamba kila tunavyozidi kwenda mbele ndivyo kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kinaongezeka. Ndivyo kiwango cha watu ambao hawamalizi kidato cha nne kinaongezeka, ndivyo kiwango cha watu ambao hawamalizi hata darasa la saba kinaongezeka. Jukumu letu ni nini Serikali katika jambo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawataja bado vijana ambao hawapo katika umri wa shle ya msingi, wapo katika umri wa shule ya sekondari, wako mtaani. Wana ari ya kutaka kusoma, hawawezi kwa sababu ya umaskini, tunafanyaje kama Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu tunayoitoa kwa wanyonge kwa walio ndani ya shule inapaswa pia, tuitoe kwa wanyonge kwa walio nje ya shule kwa kupitia mfumo wa elimu ya watu wazima pamoja na kwa kutumia nje ya mfomo rasmi. Naomba Serikali iangalie maeneo haya, lakini pamoja na mambo mengi niliyozungumza kama sehemu ya kupata marekebisho katika mpango wetu, naunga mkono hoja ya Serikali. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba Serikali anayoiongoza inatimiza na kutekeleza ahadi ambazo imeziweka kwa wananchi hususan kwenye sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri, kumpongeza Naibu Waziri, pamoja na Makatibu wake, Manaibu Katibu Mkuu lakini kwa namna ya kipekee nimpongeze sana Dkt Pilap ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hii. Kwa jumla watu hawa wanafanyakazi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Elimu kwenye upande wa kuimarisha miundombinu ya shule zetu naitambua, lakini natambua pia kazi hiyo wanashirikiana vizuri na TAMISEMI. Sikupata fursa kuchangia wakati wa TAMISEMI lakini lazima niseme hapa kwamba halmashauri ya mji wa Masasi ambayo ndiyo Jimbo langu, limepata fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na shule za sekondari. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika fedha hizo tumepata pia bahati ya kupata fedha za kujenga shule mpya, shule ya msingi, shule ya kisasa kabisa yenye thamani ya zaidi ya milioni mia saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara tena kwa kazi kubwa ya kuimarisha vyuo vyetu vya maendeleo kwa kweli vyuo vya maendeleo ya wananchi vilikuwa vimeachwa kwa muda mrefu bila ya kufanyiwa matengenezo yoyote kiasi kwamba hata wale waliokuwa wanakwenda kusoma pale kwa kweli walikuwa hawapo katika wakati mzuri. Lakini niseme tu kwamba vyuo hivi ni vyuo vya wananchi masikini wananchi wa kawaida kabisa ambao kimsingi wanavitegemea sana katika kujenga stadi zinazoweza kuwafanya waweze kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi, katika awamu ya pili kimetengewa fedha zaidi ya shilingi milioni mia tano katika kuimarisha miundombinu yake. Niipongeze sana Wizara kwa uamuzi huu wa kukiboresha chuo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwaombe sasa Serikali waone namna wanavyokwenda kwenye stage nyingine ya kuimarisha sasa ujifunzaji wa vijana wetu katika vyuo hivi. Kuna tatizo kubwa sana la walimu katika vyuo hivi, lakini pia kuna tatizo kubwa sana la vifaa vya ufundi katika kujifunza vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Masasi, kinahitaji walimu 24 lakini kina walimu sita tu kina upungufu wa walimu 18. Nilikitembelea Chuo hiki nikakisaidie kompyuta chache lakini hazitoshi hawana vifaa vya kufundishia, hawana vifaa vya kufundishia aina mbalimbali za ufundi hata baadhi ya vifaa vinakuja vinakuwa ni mali tu ya waalimu na wanafunzi kwa kweli hawapati muda wa kushirikishwa kikamilifu katika kujifunza. Wizara ione namna ambavyo inaboresha vyuo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo wazo tunavyo vyuo vya watu wenye ulemavu, watu wenye ulemavu watu wasioona tunavyo vyuo. Nchi hii ina sita sita tu vyuo hivi viko chini ya Wizara yenye dhamana inayoshughulikia walemavu. Lakini ninaushauri kwamba ni vema sasa Serikali ione kwasababu Wizara hii ndiyo yenye Sera ya Elimu na ndiyo yenye methodology, nashauri vyuo vyote vile sita ambavyo tunavyo ambavyo kwa kweli vipo katika hali mbaya sana vichukuliwe na Wizara ya Elimu ili viweze kupata huduma inayostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vyuo hivi sita vilivyopo katika nchi hii chuo kimoja kipo katika Jimbo langu la Masasi, kinaitwa Chuo cha Wasioona cha Mwengemtapika, Chuo hiki sasa kimebaki majengo tu hali ni mbaya sana, naomba Waziri Serikali ione namna ambavyo Wizara ya Elimu inaweza kupewa dhamana ya kuviendesha na vyuo hivi navyo ili viweze kutoa mafunzo yanayostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kama alivyosema Mbunge aliyetangulia ni muhimu sasa hata katika vyuo hivi kufanya elimu jumuishi tufanye inclusive education tuungane wale wasioona na watu wenye maumbile mengine ya kawaida ili waweze kufanya kazi zao kwa vizuri zaidi, tusiwatenge na huko ndiko dunia inakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la elimu ya ufundi, Mheshimiwa Mbunge aliyepita amezungumza kwamba miongoni mwa mambo ambayo yanatusumbua sana ni kutoona kwamba kila level ya education lazima iwe level of exit. Lazima iwe level ambayo inaweza kumfanya ajitegemee, hili ni jambo la msingi sana kuliko mambo mengine yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu ina mambo mengi, lakini miongoni mwa mambo hayo ni kuwajenga vijana wetu kifikra na kuwajenga vijana wetu kiustadi ili waweze kujitegemea. Katika shule za msingi katika miaka ya 70 mpaka miaka ya 80 karibu na 90, ukisoma malengo ya shule ya kuhitimu shule ya msingi, ilikuwa ni kumuwezesha mtoto anayehitimu shule ya msingi na kushindwa kuendelea mbele aweze kufanya kazi za kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la msingi sana kipindi kile tulikuwa tuna shule ambazo ni shule za msingi lakini ni shule za msingi zenye fani za ufundi, tulikuwa tuna shule za msingi zenye fani za kilimo. Ni lini tumefanya utafiti tukaona ni dhambi kuendelea na shule za msingi zenye mashamba? Ni lini tumefanya utafiti tukaona ni dhambi kuendelea na shule za msingi zenye karakana ya ufundi wa kawaida kama ufundi seremala, ili baadhi ya watoto watakaotoka pale ambao wameshindwa kuendelea au hata kama waliweza kuendelea wanaendelea katika elimu ya sekondari huku wana skills wana-study zinazoweza kuwafanya waweze kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ione namna ambavyo itarudisha elimu ya ufundi na kuimarisha vyuo vya ualimu ambayo vilikuwa ni vyuo vya ufundi kutoka katika elimu ya msingi mpaka katika elimu ya Chuo Kikuu. Wabunge wengine wamezungumza inawezaje unamfundisha mtu Bachelor degree ya Education ukitegemea aende kufundisha baadaye unataka ajitegemee wakati hakuna msingi wowote huku chini uliojengwa wa kumfanya aweze kujitegemea hapo baadaye ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya shule za private zipewe mwongozo wa kuwa shule za private za msingi ambazo zinatoa elimu ya ufundi, na elimu ya kilimo, lakini baadhi ya shule zetu za zamani ambazo zilikuwa zinatoa mafunzo ya ufundi ziendelee kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nieleze suala la elimu nje ya mfumo rasmi, tangu 2016 katika hotuba zote nilizochangia kwenye Wizara ya Elimu nimezungumza kuhusu non formal education, nashukuru leo Mheshimiwa Ngombale naye amezungumza. Nimekuwa nikisema kwamba Wizara ya Elimu siyo Wizara ya wale waliopo madarasani ni wizara ya watanzania wote. Wapo watanzania wengi sana ambao wanauhitaji wa elimu lakini hawajajengewa fursa za makusudi za kuipata elimu hiyo, wapo watanzania wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alitoa tamko la kwamba watoto ambao wanapata ujauzito hawataendelea kusoma katika mfumo rasmi, tamko lile lilikuwa linamaana sana lakini halikuwa linamaanisha kwamba watoto hawa hawawezi tena kupata fursa ya elimu. Fursa zipo lakini wizara ina mikakati gani kusaidia watu hawa? Wizara ina mikakati gani kuwasaidia watoto hawa wanaopata ujauzito nje ya mfumo rasmi waweze kusoma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunafahamu kwamba tunawasajili watoto wa miaka sita, miaka saba kwenda shule za msingi tunajua watoto wangapi wa miaka minane na miaka tisa wapo huko mitaani na hawapati fursa ya kwenda katika mfumo rasmi wa elimu? Tunajua kwamba kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kinaongezeka kila siku? Serikali inakuja na mkakati gani? Tukipata majibu ya Waziri anayoweza kutuambia kuna program ya MEMKWA na nilikuwa ni mwezeshaji huko wakati wangu, tunaweza tukaambiwa kuna mukeji …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa mimi kupata fursa ya kuzungumza kidogo kwa ajili ya kuchangia hotuba ya bajeti hii ya Wizara ya Afya. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuisimamia Wizara hii, lakini kusimamia na kupigania afya za Watanzania. Tunao ushahidi, tunaona kwa macho, Hospitali zinajengwa, hospitali za rufaa na vinajegwa vituo vya afya kila kona. Kwa kweli, kazi kubwa inafanyika, lakini nimpongeze sana mama yetu mama Ummy, Watanzania wanamwona namna anavyofanya kazi na hakika Mwenyezi Mungu atamlipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikumbushe mambo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, Mheshimiwa Ummy alikuja Mtwara wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais katika Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Ummy alisikia kilio cha Wabunge wa Mtwara na Wabunge wa Kusini kwa ujumla pamoja na wananchi kuhusiana na suala zima la Hospitali ya Kanda ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy kwa kweli moyo wake mwema, uendelee hivyo hivyo kwa kuhakikisha kwamba hospitali hii inajengwa na inakamilika kwa sababu kwa muda mrefu ujenzi ule umesimama na sisi tunaisubiri kwa hamu sana hospitali hiyo ili tuweze kupata huduma za afya kubwa kubwa kama wanavyopata katika maeneo mengine waliopata Hospitali za Kanda za Rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie fursa hii kumkumbusha Mheshimiwa Ummy alipokuja Masasi katika ziara yake ya kikazi, alipata fursa ya kufanya mkutano wa hadhara. Katika mkutano ule tulimwomba ambulance moja na aliahidi kutupatia, tunaomba moyo wake mwema, uendelee hivyo hivyo atusaidie tuweze kupata ambulance hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbusha tena Mheshimiwa Ummy kwamba alipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Mkomaindo, aliona changamoto kubwa tuliyonayo kwenye upande wa x-ray, x-ray ni chakavu na haifanyi kazi. Tunamwomba moyo wake uendelee kuwaangalia kwa jicho la kipekee watu wa Masasi atuletee x-ray mpya ya ki-digital kama katika maeneo mengine ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tena dada yetu Mheshimiwa Ummy, kwamba ameona hali halisi ya Hospitali yetu ya Mkomaindo na namna ambavyo chumba cha upasuaji hakiwezi hata kuchukua zaidi ya mgonjwa mmoja katika kutoa huduma. Tunaomba mabadiliko makubwa ya chumba hiki ili wananchi wetu waweze kupata huduma inayostahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tena Mheshimiwa Ummy, kwamba kama ilivyo katika maeneo mengine, tuna uhaba mkubwa wa Madaktari na wahudumu wa afya katika Jimbo la Masasi, tunaomba pia atuangalie kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hoja ya kuwarudisha watoto wajawazito waliojifugua shuleni; turejee mifumo ya elimu duniani yaani formal education na non-formal education. Fursa ya elimu kwa waliopata ujauzito ipo kupitia non-formal. Serikali iimarishe non formal system.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu lugha ya kufundishia; Sera ya Lugha ya Kufundishia inakinzana na ukuzaji wa fikra za kibunifu na kujiamini. Kiswahili kama lugha ya kwanza kwa walio wengi ndiyo lugha sahihi ya kufundishia. Kiingereza na lugha nyingine zibaki kuwa masomo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuta ujinga au kuongeza idadi ya wanaojua kusoma na kuandika, Serikali izingatie umuhimu wa kuwa na Taifa lililoelimika kwa kuwatazama wasio na fursa ya kujiunga na formal education. Inakadiriwa watu milioni sita hawajui kusoma na kuandika. Hii ni hatari kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabadiliko ya mitaala, kuna umuhimu wa kuimarisha dhana ya uzalendo ndani ya somo la uraia. Watoto au Watanzania wajifunze kuwa kuzaliwa Mtanzania ni jambo bora zaidi kuliko kuzaliwa mahali popote pale duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wajifunze falsafa hususan kipengele cha namna ya kufikiri (systemic and systematic thinking)logical reasoning na kadhalika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Bima ya Afya kwa wanajeshi, kuna malalamiko ya wanajeshi kuhusu kutibiwa kwenye hospitali zao pekee bila ya kuwa na Bima ya Afya, ni lini Serikali itawapatia bima za afya wanajeshi na familia zao
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Korosho Masasi kina mwekezaji aliyepaswa kukifufua, lakini kimegeuzwa ghala la korosho; tafadhali tunaomba majibu juu ya hoja hii. Mheshimiwa Waziri mfumo uliopo sasa hauwezi kuwafanya wajasiriamali wenye viwanda vidogo vya ubanguaji kupata malighafi, wasiliana na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ili kuchochea ukuaji wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kusini kuna malighafi ya juisi (mabibo na maembe mengi) mpango wa Serikali ni upi katika uwekezaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, wa Mwaka 2016
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii na mimi nichangie kidogo kwenye Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Ni imani yangu kwamba tukiwa na good legal framework na good institution framework kwa pamoja tunaweza tukafikia malengo yetu. Kwa maana hiyo basi, lazima sheria zetu zitupeleke katika kujenga msingi mzuri wa namna ya kuziendesha taasisi zetu. Nasema hivi nikiwa na maana kwamba sheria hii inapaswa ituongoze katika kuzisimamia pia taasisi zetu na kuzijengea misingi imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sheria hii tunaambiwa kabisa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kumteua Mwenyekiti wa Bodi. Kuwa na mamlaka ya kumteua Mwenyekiti wa Bodi siyo tatizo, lakini tatizo linatokea pale ambapo sheria haoinyeshi sifa za Mwenyekiti wa Bodi. Nimesoma sheria mbalimbali zinaonesha wazi vigezo ambavyo Mwenyekiti wa Bodi anatakiwa awe navyo ili aweze kuchaguliwa hususani tunapowaweka Wenyeviti wa Bodi ambao wanakwenda kuongoza Bodi zinazolenga weledi wa namna fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo basi, ni muhimu sheria yetu ifikirie Mwenyekiti wa Bodi awe na sifa zipi ili awe Mwenyekiti wa Bodi husika. Nitaleta schedule of amendment mezani na nina imani Wabunge wataunga mkono namna ambavyo tunatakiwa tuangalie vigezo vya kuwateua Wenyeviti wa Bodi kwa sababu wana mamlaka makubwa ya ku-influence maamuzi ya Bodi hizi. Kwa hiyo, ni vyema wakawa na weledi wa eneo ambalo wanaliongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, Kamati husika imeeleza namna ambavyo kuna mgongano wa kimajukumu kati ya Tume ya Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi hii tunayoitengenezea sheria. Kwa maana hiyo basi, napenda kama kuna uwezekano sheria hii itambue kuwepo kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma sheria yetu hii hakuna mahali ambapo Tume ya Sayansi na Teknolojia inatambuliwa. Ni lazima tujiulize, je, kuna umuhimu wowote wa taasisi hii ya utafiti katika kilimo kutoa taarifa angalau za mwaka au kila mwaka kwa Tume kuhusiana na tafiti inazofanya au inazozisimamia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine la msingi, kuna taasisi hii ambayo ina vituo vya utafiti. Vituo hivi vya utafiti vimetajwa kwenye sheria lakini havijawekewa majukumu yake ya msingi. Nimesoma sheria ya Uganda, Kenya, Malaysia na nchi nyingine vituo vya utafiti vya namna hii majukumu yake yamekuwa stipulated kwenye sheria husika. Jambo hili limesaidia sana kuhakikisha kwamba vituo hivi vinakuwa na majukumu yaliyoko kwenye sheria hata kama wanatekeleza majukumu mengine wanayopewa na Bodi au Director General lakini wakati huo huo wanayo majukumu yao ya msingi. Ni muhimu tuyataje katika sheria ili vituo hivi viweze kufanya kazi zake kwa weledi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo lipo tatizo kubwa la kutopelekwa kwa taarifa za matokeo ya utafiti kwenye grass roots, hili nalo ni jambo la msingi sana. Sheria yetu haioneshi ni wakati gani vituo hivi vya utafiti vinalazimika kupeleka matokeo ya utafiti walioufanya kwa wananchi ambao kimsingi ndiyo consumer wa matokeo yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo manne nadhani kama yatazingatiwa tutakuwa katika mstari mzuri wa kuendelea kuiboresha sheria yetu. Ahsante sana.