Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Goodluck Asaph Mlinga (46 total)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Ulanga kuna mradi mkubwa wa maji wa Mahenge Mjini ambao tayari umeshakamilika. Tatizo la huo mradi umeshindwa kuanza kwa kuwa tu, Idara ya Maji haina mita za kuwafungia wateja, kwa kisingizio cha fedha zikipatikana, fedha zikipatikana. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa ili Idara ya Maji iwafungie mita wananchi wa Mahenge Mjini ili waanze kufaidi matunda ya Mbunge wao kijana machachari?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetekeleza mradi na mradi ule umekamilika; kilichobaki ni mita. Sasa naomba anisaidie awasiliane na Halmashauri kuna tatizo gani, hatuna taarifa kwamba wana hilo tatizo la mita, watuletee taarifa. Hata hivyo, katika Mwaka huu wa Fedha tumemwekea bajeti, kwa nini wasiangalie hiyo bajeti ili wakaweza kufunga mita, halafu waendelee kupata mapato. Kwa sababu najua kwamba wananchi watakuwa wanapata maji, lakini tatizo Halmashauri haipati mapato. Kwa hiyo, kwanza Mheshimiwa Mbunge aangalie bajeti ambayo tumempatia, kama haitatosha, basi tuwasiliane ili tuweze kuliondoa hili tatizo la mita.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyama vya Upinzani vimekuwa vikileta vurugu, kutotii amri ya halali za Serikali na Jeshi la Polisi na wakati mwingine kuleta vurugu, kwa mfano, katika Jimbo langu la Ulanga kwenye kijiji cha Iputi - Nambuga walichoma nyumba sita za wananchi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na suala hili, ili kutokomeza kabisa tabia hii.
Pili, kumekuwa na Wabunge, wakileta uchochezi wa kisiasa katika maeneo yetu ya makazi. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na Wabunge kama hawa?(
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni kama ambavyo nimeeleza katika jibu la msingi. Kwa maana hiyo basi, katika kutekeleza wajibu wake huo Jeshi la Polisi halibagui mtu yoyote na lina thamini vilevile maisha ya Watanzania wote kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na limekuwa likichukua hatua stahiki mbalimbali kwa uhalifu wa aina yoyote iwe kutoka katika Vyama Vya Siasa ama raia wa kawaida.
Kwa hiyo, nilitaka nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mlinga kwamba kuna hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa na viongozi ambao wamekuwa wakitoka katika vyama vya siasa wakishiriki katika vitendo vya uhalifu. Mfano halisi ni katika matukio ambayo yanajitokeza sasa hivi Pemba, miongoni mwa watu ambao wameshikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuchochea vurugu Kisiwani Pemba wapo ambao walikuwa na nafasi kubwa za uongozi katika vyama vya siasa na katika chombo cha kutunga sheria.
Kwa hiyo, hiyo inadhihirisha kwamba Jeshi la Polisi halibagui mtu na atashughulikiwa mtu kwa mujibu wa matendo yake na siyo kwa mujibu wa affiliation yake ya siasa ama rangi, dini, kabila la mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na Wabunge kushiriki katika vitendo vya kihalifu ni kama nilivyozungumza katika swali la nyongeza la mwanzo kwamba iwe Mbunge, mwanachama wa kawaida, kiongozi wa chama cha kisiasa kitakachoamua hatua za kuchukuliwa ni matendo yake na niseme tu kwamba kwa kuwa umegusia suala la Wabunge wao wana haki zao kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge yanamlinda Mbunge kwa kila ambacho anakisema Bungeni lakini haimlindi Mbunge kwauhalifu wa aina yoyote wa jinai iwe ndani ya Bunge ama iwe nje ya Bunge.
Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwasihi sana wanasiasa hasa viongozi ikiwemo Wabunge kuwa makini sana na kauli zao na matendo yao kwani yanaweza kuchochea uvunjifu wa amani katika nchi yetu.
Lakini pia nichukue fursa hii kuwanasihi wananchi kuwa makini sana na kauli za wanasiasa ikiwemo viongozi wa siasa katika kuhakikisha kwamba wanafuata misingi ya sheria ya nchi yetu ili waweze kuepuka madhara yanayoweza kuwatokea katika maisha yao.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu sahihi na majibu yanayokidhi. Niongezee tu kipengele kile alichosemea kuhusu Wabunge na viongozi wa vyama vya kisiasa kuwa vyanzo vya vurugu na nieleweke wazi kwamba utaratibu ambao tutautumia kuanzia sasa kwa kupima kwamba kila kiongozi anawajibu wa kuhimiza amani katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea uchochezi wa aina yoyote ambao na kiongozi yupo tutashughulika na kiongozi aliyewapeleka watu wengine kwenda kwenye matatizo hayo. Kwa sababu mara nyingi viongozi wamekuwa wakiwatanguliza watu wengine na kupata madhara kwa sababu wao hawaguswi na madhara yale. Kwa hiyo, tutakachofanya na nitaaambia vijana wangu kwamba kunapotokea na uchochezi hangaikeni na mzizi wa tatizo ambaye ni kiongozi aliyesababisha watu waende katika matatizo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisema kwamba watanzania pamoja na hao ambao hawajasoma vitabu vya historia vinavyoelezea udikteta ni nini wasichanganye udikteta na msimamo wa kusimamia sheria. Mimi niwape taarifa tu kama hawawajui madikteta niwape kwa taarifa zao dikteta huwa hatoi fursa hata ya kuambiwa wewe ni dikteta, huwezi ukamsema mtu wewe ni dikteta na ukaendelea kutembea kwenye disco upo, kwenye unywaji upo, kwenye sherehe upo, yaani kile kitendo kwanza cha kupewa fursa za aina zote zile zinaonyesha kwamba nchi yetu inafuata utawala wa sheria na demokrasia. Wale waliozoea maisha ya deal deal wanatakiwa tu waachane na mambo ya deal deal na wafuate sheria na wataishi kwa usalama.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri napenda kuongezea kama Waziri ninayesimamia utawala wa sheria (rule of law) nchi hii kwamba kimsingi swali hili halikutakiwa hata kuwemo kwenye Order Paper kwa kuwa linakiuka masharti ya Kanuni ya 40 ya Kanuni zetu za Kudumu.
Kanuni ya 40 inasema; “Swali lolote la Bunge halitaruhusiwa kuulizwa Bungeni kama (d), limekusudiwa kupata maoni ya kisheria ya kinadharia au kutoa mapendekezo juu ya jambo la kubahatisha tu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ukilisoma hili swali la msingi ni nadharia tupu na hoja zakubahatisha, linasema kumekuwepo na vifo vyenye utata wa kisiasa, vifo vipi hivyo vilivyothibitishwa kitaalamu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kifo kikitokea, vijana wetu wa polisi wakishirikiana na mamlaka nyingine kama Mkurugenzi wa Mashtaka wanatumia muda mrefu kufikiri hiki kifo kimetokana na nini, wanatafuta ile blameworthy state of mind au unavyopeleka mahakamani kinachotafutwa ni malice aforethought sio tu unakaa kwenye jukwaa unasema hii ni siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, (b) inasema; linatokana na habari za kubahatisha tu, linasema inapotokea mpinzani kupoteza maisha suala halipewi kipaumbele. Ushahidi upo wapi tuletee huo ushahidi hapa sisi kama Serikali tutajibu, lakini sio maswali generalized, yanaleta tu hisia mbovu katika jamii ya Watanzania.
(f) inasema linaulizwa kwa njia inayoonyesha jibu lake au kutambulisha mkondo fulani wa maoni na hapa unaona bayana mkondo fulani wa maoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusisitiza tu kwamba Watanzania siasa zisitufikishe huko; kibaka anakamatwa tunaanza kukimbilia kwenda mfukoni ana kitambulisho cha CHADEMA au cha CCM, hatutajenga Taifa hili kwa njia hiyo, ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kutuangalia sisi kambi mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha afya cha Lupilo ndiyo kama Hospitali ya rufaa katika kata tano za Ilagua, Lupilo, Kichangani na Milola. Je, ni lini serikali itaifanyia ukarabati kituo hiki cha afya maana kina hali mbaya ya majengo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze kwa sababu ni kweli kwamba Mbunge amekuja amejipanga kweli katika Bunge hili na mimi naomba nikuhakikishie, naelewa wazi kwamba ukarabati unaanza pale Baraza la Madiwani linapoweka vipaumbele. Na mimi nilivyopitia katika database wakati wa mchakato wa bajeti ya mwaka huu niligundua kwamba hata eneo lako la Ulanga ni kweli kuna mahitaji, isipokuwa tatizo kubwa lilikuwa katika budget ceiling.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa zaidi naomba nikuhakikishie, ni kwamba sasa hivi ukiwasiliana na Mkurugenzi wako; kama nilivyosema siku mbili zilizopita hapa; kwamba tumewaagiza wabainishe magofu yote na maeneo yote katika eneo la afya yanayotakiwa kufanyiwa ukarabati ili Ofisi ya Rais - TAMISEMI tuangali tunapeleka wapi nguvu. Katika hilo naamini kwamba eneo lako la Ulanga katika kituo hicho cha afya ni miongoni mwa takwimu ambazo zitakuja tuweze kuzifanyia kazi. Na nikuhakikishie kwamba zitakapofika ofisini kwetu tutapanga mpango mkakati kuweza kukusaidia ili uendelee kuleta heshima katika Jimbo la Ulanga kama ilivyokuwa toka zamani.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba ni-declare interest, na mimi ni mchimbaji mdogo japokuwa sijawahi kunufaika kutokana na mfumo mbovu wa Serikali. (Kicheko)
Tatizo lililoko Mpanda Mjini linafanana na lililoko katika Jimbo langu la Ulanga. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwaelimisha na kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo la Ulanga ili waweze kuyathaminisha madini haya wanayoyapata ili waweze kuyauza katika thamani halisi inayoendana na soko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona umuhimu, hilo la kwanza. Tunaona umuhimu wananchi wako Mheshimiwa Mbunge kuendelea kuwaelimisha, lakini siyo kuwaelimisha tu, hata kuwapatia ruzuku wakikidhi vigezo. Napenda tu kusema katika Jimbo la Ulanga, maeneo ya Mvomero, maeneo ya Iringa, maeneo ya Singida, yote kwa pamoja tunaendelea kuyatathmini tuwatengee wananchi. Kwa hiyo, pamoja na kutoa elimu, tunawahamisha Waheshimiwa Wabunge wawahamishe wananchi washirikiane na Waheshimiwa Wabunge ili kunufaika na rasilimali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kwanza mwaka huu, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amekaa sana na wachimbaji wadogo Wawakilishi wao wa Katavi, Singida pamoja na kwa Mheshimiwa Mbunge wa Ulanga. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mlinga nakuhakikishia tutaendelea kusaidiana na wananchi wako kuwaelimisha waweze kunufaika na mapesa haya.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Japokuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema majibu yatakuwa ni yaleyale na mimi naomba nikumbushie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Maswa linafafana na tatizo lililoko Ulanga katika Kata ya Ilagua, Lupilo, Minepa na Milola ambapo Mheshimiwa Rais aliahidi kuhalalisha hili eneo la buffer zone ili wananchi hawa wafaidi tunu ya pekee ya ardhi tuliopewa. Je, ni lini Serikali itahalalisha na itatekeleza ahadi hii ili wananchi hawa wafaidi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante. Kwanza nimshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba maswali haya mengi yanayohusiana na migogoro ya mipaka na hasa pale yanapogusa Wizara zaidi ya moja tulikwishayazungumzia na kuyatolea maelekezo. Kama alivyojibu Naibu Waziri wa Maliasili Wizara tutakwenda kukaa, tutafika kwenye maeneo ambayo yanahusika baada ya wataalam kuwa wamepitia maeneo hayo na kujua ile mipaka inayolalamikiwa kuona kama kweli mpaka ulipanuliwa na kufuata watu au mahitaji ya watu yamekuwa ni makubwa kiasi kwamba sasa inahitajika kuangalia upya mipaka iliyowekwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala hili ningeomba sana Waheshimiwa Wabunge wawe na uvumulivu kwa sababu ni maeneo mengi yana mgogoro huo na maeneo mengi yanahitaji pia kupitiwa upya ili kuweza kukidhi ile haja ambayo Waheshimiwa Wabunge wanaiona kwamba inafaa kwa wakati huo. Ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wangu wa Ipanko, usiku wa leo kuvamiwa na Polisi na kupigwa sana na kuumizwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sasa hivi taasisi za kifedha zimeleta ugumu kukopesha taasisi za Serikali kwa sababu ya ugumu wao wa kulipa haya madeni. Je, sasa Serikali haioni kuwa inahitajika ifanye mpango wa dharura kwa ajili ya kutengeneza barabara za vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachozungumzia kwamba Serikali kufanya mpango mbadala ndiyo maana mwanzo nimesema, katika kuhakikisha tunafanya mpango mbadala Ofisi ya Rais, TAMISEMI inafanya mambo makubwa sana. Leo hii ukitembea katika Manispaa zetu maeneo mbalimbali tunatengeneza barabara za kiwango cha lami tumeanza katika miji mikubwa, tumekuja katika Manispaa baadaye tunakwenda katika Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu kubwa takribani miaka mitano itakayokuja tutaona mabadiliko makubwa sana ya miundombinu ndiyo maana mwaka huu ukiangalia zile fedha tulizotenga katika maeneo mbalimbali takribani bilioni 200 zitaenda kupakwamua sehemu korofi ambazo barabara zetu za Halmashauri zimekuwa hazipitiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili la Mheshimiwa Goodluck niseme kwamba huu ni mpango wa Serikali na naomba nikwambie kwamba tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kama ombi lako linavyosema tutaendelea kuweka mkazo ili wananchi wapate huduma.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kutupa kipaumbele sisi Kambi mbadala.
Kwa kuwa matatizo ya mawasiliano yaliyoko katika Jimbo la Nanyamba yanafanana na Jimbo la Ulanga, Kati ya Kata ya Ruaha, Chilombola, Ilagula, Ketaketa na Ilonga; je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu za mkononi katika Kata hizi ili na wananchi hawa wafaidi mawasiliano ya simu za mkononi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maswali yako tutayashughulikia, tumeyachukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate ufafanuzi zaidi wa hayo maeneo aliyoyaeleza ili tuweze kuyafanyia kazi na kuwatendea wananchi wake kwa namna inavyotakiwa. Naomba tukutane ofisini tuelezane kwa undani zaidi kuhusu hilo eneo ili hatimaye tutende kile ambacho wananchi wanakihitaji.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wangu wa Lupilo wanaopata misukosuko ya kubambikiziwa kesi na Jeshi la Polisi, nalaani vikali matumizi mabaya ya nguvu za Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, mradi huu tangu uanze una miaka mitatu sasa hivi; upembuzi yakinifu sijui nini vinafanyika. Sasa Mheshimiwa Waziri anawaambia nini wananchi wa Lupilo wanaotarajia mradi huu uwe mkombozi wa maisha yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu wa kuiunganisha ofisi yake ya kanda na Mkurugenzi wangu wa Ulanga ili iwe rahisi kwa ajili ya ufuatiliaji na utekelezaji wa mradi huu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuweka uzito katika masuala ya umwagiliaji kwa sababu huu ndiyo ukombozi wa huko tunakokwenda kuhakikisha Watanzania watakuwa na chakula cha uhakika kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuhusu mradi huu, ni kweli kwa mwaka huu wa fedha tumeamua kwamba katika bajeti iliyokuwa imetengwa ya bilioni 35, bilioni sita ndizo fedha za ndani. Sehemu kubwa ya kazi hii ilikuwa ni kufanya upembuzi yakinifu na kufanya mapitio ya mabwawa mbalimbali ambayo tumelenga katika miaka mitano tufikishe hekta milioni moja. Kwa,hiyo, ni pamoja na bwawa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fedha zinazohitajika kwa bwawa hili peke yake ni bilioni 40, bajeti ya Wizara kwenye umwagiliaji ni bilioni 35. Kwa hiyo, ni fedha nyingi tunahitaji tu-mobilize fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali ili tuweze kupata fedha za uhakika. Naomba niwahakikishie wananchi wanaoishi kwenye eneo hili la Lupilo kwamba mradi huu Serikali itakwenda kuutekeleza na katika mwaka wa fedha 2017/2018 tutaweka fedha kuanza kujenga skimu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, mapendekezo yake kwamba Ofisi ya kanda iweze kuunganishwa, naomba hili nilichukue tutakwenda kuangalia uwezekano wa kufanya hivyo.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; kwanza naomba nioneshe masikitiko yangu kwa kiwango cha juu kwa Waziri kijana kujibu majibu ambayo hayaendani na kasi ya Serikali kwa sasa hivi. Haya
mashirika ambayo ameyataja TRA, BOT, ANESCO, NHC na TPA mimi mwenyewe binafsi nilitembelea wakati nipo NHIF lakini ni tofauti ya anavyosema Waziri sasa hivi. Je, katika michakato ambayo imeshawahi kutokea nchini kwetu
mchakato mgumu ulikuwa wa kuhamia Dodoma, Rais alisema mwaka jana mwezi wa Saba lakini sasa hivi Mawaziri wote wamehamia Dodoma.
Swali la kwanza; je, ni nini kinashindikana mashirika haya ya umma kuhamia NHIF wakati ni kitendo cha muda mfupi tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ofisi yako ni
shahidi Wabunge tulipotoka mashirika ya private insurance kwenda NHIF tuliweza ku-save kiwango kikubwa cha pesa mpaka tukanunua madawati nchi nzima. Kumekuwepo na ubadhirifu mkubwa wa pesa za Serikali kwa haya mashirika ya umma through private health insurance. Je, Serikali
itakubaliana na mimi sasa hivi kufanya mchakato wa kuangalia kiwango gani cha pesa kinachopotea iwapo mashirika ya umma yataendelea kutumia private health insurance badala ya NHIF?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naweka sawa, mimi sio Naibu Waziri kijana, mimi nimeshavuka umri wa ujana mimi ni mtu mzima na yeye bado kijana mdogo wangu lakini mimi sio kijana, mimi ni Naibu
Waziri. Kumjibu ni kwamba, hakuna kinachoshindikana kwa mashirika kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa na kinachofanyika sasa hivi ndani ya Serikali ni mapatano baina ya shirika letu la NHIF na haya mashirika mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ambapo tunatarajia
watakapokubaliana kama ambavyo Katibu wa Bunge amekubaliana na Shirika letu la NHIF kuliingiza Bunge huko na haya mashirika mengine taratibu yataendelea kufanyiwa kazi kama ambavyo alikuwa akifanya yeye wakati ameajiriwa na NHIF. Aliendelea kuwashawishi kwa sababu
sio suala la kulazimishana. Yeye amekuwa akienda kule kuwashawishi miaka yote ambayo amekuwa akifanya kazi kule hakufanikiwa kuwa-convince wakajiunga na mfuko; leo hii anataka tu hii miezi miwili, mitatu tuwe tumeshawaconvince sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pengine mfupa uliomshinda yeye anatarajia sisi tutauweza kwa haraka zaidi wakati yeye mwenyewe ulishamshinda. Kwa hiyo wataalam wetu, kama alivyokuwa yeye mtaalam wa NHIF – wanaendelea kupatana na haya mashirika taratibu
kuyashawishi yajiunge na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu yake ya pili; mpaka sasa hatujajua ni kiasi gani cha pesa ambacho pengine kinapotea kwa mashirika mbalimbali ya umma kuwa yamejiunga kwenye mifuko ya private health insurance na sio kujiunga katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Hata
hivyo, natoa rai kwa mashirika haya na Mawaziri ambao wanayasimamia mashirika haya kutoa maelekezo kwenye mashirika haya ili huu mchakato wa negotiations ambao unaendelea uweze kuongezwa kasi ili mashirika yote ya
Serikali hatimaye yajiunge na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya badala ya kuwa kwenye mifuko hiyo mingine.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nimshukuru sana Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nataka kuwathibitishia suala la mashirika ya umma kujiunga
na NHIF sio suala la hiari. Tayari kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanatumia NHIF kwa hiyo hatuoni kisingizio kwa mashirika ya umma kutumia NHIF. Nimetoka kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na yeye alipowasilisha mpango wa bajeti na mwongozo wa sera za matumizi, Serikali imetoa maelekezo tutumie huduma na bidhaa zinazozalishwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutakaa na
mashirika haya tuweze kuona, wengi tumeongea nao wana mikataba na mashirika haya ya bima binafsi kwa hiyo hatuwezi kukatisha lakini nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mlinga, tutafanya kazi pamoja kuhakikisha mashirika yetu haya yote yanajiunga na bima ya afya NHIF. Nitoe wasiwasi, NHIF sasa hivi inakubalika katika hospitali kubwa zote, kama Wabunge wanatumia sioni ni sababu gani mtumishi wa TRA na BoT asitumie huduma
za NHIF. Mheshimiwa Mlinga, nakushukuru sana na tutafanya kazi pamoja kuhakikisha tunalitatua suala hili.
MHE.GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Sasa hivi ninavyoongea barabara ya Ifakara - Mahenge haipitiki kabisa, wananchi wanakosa huduma za muhimu kama petroli, dizeli na dawa kwa ujumla. Je, wananchi wa Ulanga wanataka kusikia kauli ya Serikali nini kitafanyika sasa hivi ili watu hawa wa waweze kusafiri kwenda Mahenge? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kuitaka TANROADS Taifa na TANROADS Mkoa wa Mogororo washughulikie ufunguzi wa barabara hii iliyokatika.(Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wapogoro tunajulikana dunia nzima kuwa chakula chetu kikubwa ni wali na kambale, kwa kuwa Ulanga tunalima sana mpunga.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga kiwanda ili sasa wakulima wasiuze mpunga wauze mchele ili kuwaongezea kipato? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kukoboa mpunga ni viwanda vidogo na viwanda vya kati. Ni viwanda vyenye thamani kati ya shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakachofanya kwa ajili ya wajomba zangu, ni kuwahamasisha wananchi. Matajiri wa shilingi milioni 200 tunao, badala ya kuwekeza kwenye malori, ni kununua dryer. Nitoe taarifa, kwa nini mchele wetu wa Tanzania unakataliwa nje? Ni kwamba tunashindwa ku- control moisture content. Nimeshamweleza hata rafiki yangu pale Mheshimiwa anayependa kula sana pepeta, nimeshamweleza kwamba control moisture content. Kwa hiyo, moisture content inauzwa dola 50,000, kinu kinauzwa dola 100,000. Tunaweza kufanya hivyo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nitasaidiana na wewe na tulishafika pazuri, sitaki kukurudisha kwenye historia; tutaweza kuhamasishana. Hivi viwanda vya shilingi milioni 200, shilingi milioni 300 au shilingi bilioni moja, msitafute wageni, tunavimudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amezungumza hapa, ziko benki, tunavimudu na tutawasimamia. Ndio nyie wenye kuwekeza. Wale wengine watakuja baadaye, lakini watu wa kuwekeza ni sisi. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, katika ngo’mbe milioni 28 ni ng’ombe 700,000 tu wanaozalisha maziwa, hii inatokana na wafugaji kutokuwa na watetezi katika nchi wakiwemo wafugaji wa Iragua. Je, Wizara sasa iko tayari kuhakikisha wafugaji hawanyanyaswi na watu wa maliasili? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Serikali itahakikisha kwamba wafugaji nchini hawanyanyaswi na mtendaji yeyote wa Serikali na inapotokea tukapata ushahidi kwamba mtendaji yeyote wa Serikali amekiuka maadili ya kazi, basi Serikali haitasita kuchukua hatua mara moja.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jimbo langu la Ulanga tumebahatika kuwa na mto mkubwa sana, Mto wa Kilombero lakini wananchi wanaoisha maeneo yale hawajawahi kunufaika na chochote kile kuhusu uvuvi.
Je, sasa Wizara iko tayari kutoa ushauri wa kitaalam na vifaa ili wananchi wanaoishi karibu na mto ule wanufaike na shughuli za uvuvi na Serikali ipate mapato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara na Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi wake waweze kuvua katika Mto Kilombero. Nimhakikishie tu kwamba huduma hii inapatikana katika Halmashauri ambapo yeye mwenyewe ni Diwani na vilevile niwashauri Waheshimiwa Wabunge wote kwamba huduma za namna ya kuwasaidia wananchi katika sekta ya uvuvi na sekta zote za Wizara yangu yaani kilimo na mifugo, sehemu nzuri ya kuanzia ni kwenye Halmashauri na sisi wenyewe tunashiriki lakini kama nilivyosema kwa Mheshimiwa Aweso, hata Mheshimiwa Mlinga anaweza akaja nikamuelekeza zaidi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa nafasi ya pekee napenda nikipongeze Chama changu cha Mapinduzi kwa kutimiza miaka 41 ya utawala bila kung’oka, na kwa utendaji huu tuna miaka 41 mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri atakuwa shahidi tangu hili pori lianzishwe ni miaka mingi sasa na watu wameongezeka kwa kiasi kikubwa, sheria hizi zilizoanzisha mapori ndiyo sheria hizi hizi zilizoanzisha vijiji, inapotokea maeneo wanayoishi wananchi yakagundulika madini wananchi wanatolewa, lakini wananchi wanapohitaji kulima maeneo ya mapori wanaambiwa sheria zizingatiwe. Kwa nini sheria ziko bias upande mmoja kwa kuwaonea wananchi ambao ni wanyonge?
(b) Mheshimiwa Waziri tulikuwepo nae Ulanga wiki mbili zilizopita ameona jiografia ya Ulanga ilivyo ngumu maeno yote ya matambalale ambayo wananchi wanaweza wakalima ni Mapori Tengefu, ni Hifadhi na Bonde la mto Kilombero, naomba busara zitumike ili wananchi wapate maeneo ya kilimo kwa sababu wameongezeka kwa kiasi kikubwa.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wakati tunapata Uhuru idadi ya wananchi wa Tanzania ilikuwa haizidi milioni tisa na ardhi ilikuwa hivi, lakini miaka karibu 56 ya Uhuru wananchi wa Tanzania wameongezeka kwa kiwango kikubwa sana, sasa tuko karibu milioni 52 lakini ardhi haijaongezeka. Kwa hiyo naomba nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutokana na ongezeko la watu ndiyo maana kumekuwa na presha kubwa sana katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo naomba nimhakikishie kwamba sheria zilizotungwa sio kwamba ziko bias, sheria ziko vizuri kabisa, sheria zinaainisha maeneo yaliyohifadhiwa, maeneo ambayo yanafaa kwa makazi, maeneo yanayofaa kwa ufugaji, maeneo yanayofaa kwa kilimo kwa hiyo hili lazima tulisimamie ipasavyo. Siyo kwamba sheria zinapendelea labda kitu fulani na Serikali yetu itaendelea kuhakikisha kwamba wananchi wanapatiwa maeneo ya kulima yale yanayostahili na yale yaliyohifadhiwa yaendelee kuhifadhiwa kwa mijibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali lake la pili ni kweli kwamba tutatumia busara kubwa sana katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo hili la Ulanga wanapata eneo la kulima, kufuatia hatua hiyo na ziara ambayo tumeifanya hivi karibuni kama alivyosema yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ameunda Kamati ya Wajumbe 22 kwa sababu ya ukubwa wa Bonde lenyewe la Kilombero lilivyo ili kuweza kubainisha, kuweza kupitia maeneo yote na waone ni maeneo gani yahifadhiwe, maeneo gani yatafaa kwa kilimo ili kusudi wananchi wapate kuelekezwa ipasavyo. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Swali langu ni hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ajali zinaendelea kutokea kwa wingi, hata hivi sasa hivi ninavyoongea ukipita barabara ya Morogoro – Dodoma kuna ajali nyingi sana, lakini traffic wamegeuka agent wa TRA kazi yao ni kusimamisha magari na kutoza faini. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba atoe tamko kuanzia leo hii matrafiki waache kutoza faini wakazane na kutoa elimu kwa kutoa elimu kwa watumia vyombo vya moto na wasafiri ili wajue ni haki gani watapata pindi ajali zinapotokea. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja, sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi, kutoza faini ama kukusanya faini si kipaumbele chetu; sisi kipaumbele chetu ni maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa imepita miaka mingi sana ya kutoa elimu na tunaendelea kuona kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alisema uzembe bado uko mwingi sana ndipo tunapokwenda kwenye hatua hiyo ya kutoza faini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Watanzania watazingatia kwamba wamebeba dhamana kubwa ya maisha ya Watanzania na maisha yao wao wenyewe, wakawa waangalifu hili suala la faini litakuwa limeisha, lakini kwa kuwa tunawapenda zaidi na tunapenda zaidi maisha yao ndiyo maana tunakuwa hatuna njia nyingi zaidi ya kuchukua sheria kali ili kuweza kuokoa maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitoe rai kwa Jeshi la Polisi kuendelea kuwa strictly, kuendelea kuwa wakali punde watu wanapofanya mzaha na huku wakiwa wamebeba abiria ili kuweza kuokoa maisha yanayopotea kutokana na ajali nyingi zinazotokea barabarani. Jambo hili ninalolisemea ni kwa vyombo vya moto vyote, ukianzia magari ambayo si ya abiria pamoja na bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisisitiza sana hili kwa sababu tumeshuhudia vifo vikiwa vimetokea na pale tunapokwenda kwenye kuokoa miili tunakuta watu walikuwa tayari walishaandikiwa faini ikiwa ni kwamba wameambiwa kwamba wanakwenda mwendo kasi. Hata hivyo, pamoja na faini wanaendelea na mwendo kasi ama na uzembe na baadaye inagharimu maisha ya Watanzania.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, asante sana, Wilaya ya Ulanga pamoja na kuwa na Mbunge kijana machachari lakini haina Mahakama ya Wilaya. Je, wananchi wa Ulanga wanaisikiliza Serikali yao ya hapa kazi tu inawaambia nini kuhusiana na jengo la Mahakama ya Wilaya? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU:
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika miaka ya hivi karibuni Serikali imeendelea kujenga Mahakama tofauti na miaka iliyopita na kwa mwaka huu wa fedha unaokuja 2017/2018, tumetengewa kiasi cha shilingi billioni 46 kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge na kwamba ninacho kitabu hapa kinachoelezea Mahakama zitakazojengwa, kwa hiyo nimwombe tu afike katika Ofisi yetu aangalie, ni orodha ndefu sana ya Mahakama na naamini kabisa eneo lake la Jimbo la Kilombelo lilitakiwa pia liwe limezingatiwa ili nao waweze kupata huduma hii.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Wanaulanga kwanza naomba niishukuru Serikali kwa ukamilishaji wa Daraja la Mto Kilombero, haya ndiyo matunda ya Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yanazunguka Mto Kilombero yana shida kubwa sana ya maji…
Mheshimiwa Spika, Daraja la Mto Kilombero la kwenda Ulanga, limelamilika.
Mheshimiwa Spika, lile limekamilika, lile kubwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, kabisa na tunapita pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu ni hili, maeneo ambayo yanazunguka huu Mto Kilombero yana shida kubwa sana ya maji kwa upande Wilaya ya Kilombero, kwa maana ya Ifakara Mjini, pamoja na Tarafa ya Lupilo. Je, sasa Wizara ina mpango gani wa kubadilisha matumizi ya Mto Kilombero ili uwe unatumika kwa matumizi ya binadamu, kwa maana ya maji ya kunywa na kupikia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri nimetembelea Morogoro kwenye Majimbo yote na Halmashauri zote, nimefika mpaka Mto Kilombero. Kwanza baada ya kuvuka Kilombero, Lupilo pale tayari tulishaweka mfumo wa maji na wananchi wanapata maji safi na salama. Maeneo mengi tunaendelea kuhudumia kwa kutumia Bonde la Mto Kilombero, lakini mawazo yako pia pale itakapofika sasa inahitajika tutajenga bwawa kulingana na uwekezaji uliopo na idadi ya watu waliopo. Tutajenga bwawa kubwa Mto Kilombero ili tuweze kuwahudumia wananchi. Lakini kwa sasa bado tunaendelea kutumia Bonde la Mto Kilombero, wananchi wote wanapata maji safi na salama.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niishukuru Serikali kwa kuitupia sekta ya afya jicho la pekee katika Jimbo langu la Ulanga. Kituo cha Afya cha Lupilo karibu kinakwisha, sasa wananchi wa Ulanga wategemee nini katika huo mgawo? Siyo kwamba Madaktari ni wachache tu lakini ni pamoja na kuwa na watumishi wa afya wasio na sifa. Ulanga inakusikiliza sasa hivi Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ulanga limepewa kipaumbele sana kwenye sekta ya afya, hilo naishukuru Serikali, hicho ndiyo kipaumbele cha Mbunge wao, kipaumbele cha kwanza afya, cha pili afya, cha tatu afya. Shida kubwa iliyopo ni watumishi wachache, Mheshimiwa Waziri katika majibu yake haya ya kugawa watumishi wa afya wananchi wa Ulanga wanamsikiliza sasa hivi anawaambia nini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nitangulie kupokea shukrani anazozitoa, lakini naomba nimhakikishie nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati zetu zote zinafanya kazi iliyokusudiwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, litakuwa ni jambo la ajabu tukamilishe kituo cha afya kizuri halafu kisiwe na watenda kazi. Katika wilaya ambazo zitapata watendaji kwa maana ya wahudumu wa afya pamoja na Waganga, nimhakikishie kwamba wale wenye sifa ndiyo ambao watapelekwa kwake, kwa hiyo, wananchi wategemee mambo mazuri kuhusiana na suala zima la afya.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ushoga usagaji na kutukuna matusi mithili ya bomu la nyuklia siyo maadili yetu na desturi ya Mtanzania, lakini vitendo hivyo vimekithiri kartika mitandao yetu ya kijamii. Kwa mfano, wapo mashoga maarufu wanajitangaza katika mitandao yetu ya kijamii na siyo utamaduni wa Kitanzania; kwa mfano kuna mtu mmoja maarufu anaitwa James Delicious.
Mheshimiwa Spika, kuna vikundi vya matusi kabisa katika mitandao ya kijamii. Mfano kuna team Wema, team Zari, team Diamond, team Shilole, hawa wamekuwa wakitukana matusi katika mitandao ya kijamii.
Je, nini kauli ya Serikali kutokana na hili kwa sababu linachangia kwa kiwango kikubwa sana kuharibu maadili na utamaduni wa Kitanzania? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Tulitunga Sheria ya EPOCA mwaka 2010 lakini tulikosa Kanuni za kuweza kubana hasa maudhui upande wa mitandao. Tumeshatunga hizo Kanuni na sasa hivi hizo Kanuni zimeanza kufanya kazi. Naomba nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna baadhi ya wasanii wetu ambao walianza kufanya uhuni uhuni ndani ya mitandao, jana tumeweza kumkamata mwanamuziki nyota Tanzania, Diamond tumemfikisha polisi na anahojiwa kutokana na picha alizozirusha. Vilevile imebidi hata Binti Nandy naye apelekwe polisi kuhojiwa. Tunaangalia namna ya kuwapeleka mahakamani.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe wito kwa vijana wote nchini, mitandao siyo kokoro la kupeleka uchafu wote ambao umezuiwa na sheria zingine. Hii nchi ina utamaduni wake. Tunahitaji kulinda kizazi cha leo, kesho na kesho kutwa cha Taifa hili. Ahsante. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri machachari na kijana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo kuongezeka kwa wingi Ulanga limeanza tangu miaka ya 90 na tumepiga kelele lakini Serikali kwenye ujenzi wa majosho wako nyuma lakini kwenye kupiga chapa kwa sababu inawaingizia mapato wamekuwa wako mbele. Naomba commitment ya Serikali iseme kuwa mwaka huu 2018/2019 tutajenga majosho. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa kuwa kumekuwa na tatizo la masoko ya mifugo, masoko yaliyoko ni minada ya kienyeji ambapo wafugaji wanauza mifugo kwa bei nafuu. Je, lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa masoko ili wafugaji wauze mifugo yao kwa bei ya faida? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga kwamba tutajenga josho katika jimbo lake mwaka huu ujao wa fedha pamoja na kisima, siyo josho tu ni pamoja na kisima cha kunyweshea mifugo maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunajua kuna tatizo la uanzishaji wa masoko ambapo watu wengine wanaanzisha masoko bila utaratibu na wengine wanakosa mwongozo. Kwa hiyo, hili tunalisimamia vizuri na katika mwaka huu wa fedha tutayamaliza yote haya. Tutahakikisha kwamba miongozo ipo ya kutosha kuhakikisha kwamba masoko mahali popote yanapoanzishwa yanazingatia miundombinu mahsusi inayotakiwa na eneo mahali linapohitajika.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri wakati akijibu hoja zangu za kuhusu fine kwa madereva wa bodaboda alikiri kweli haiwezekani bodaboda anabeba abiria mmoja, anatozwa fine Sh.30,000 wakati basi linalobeba abiria 60 fine ni ile ile Sh.30,000. Tunaomba atuhakikishie katika hayo mabadiliko ya sheria, je, hii sheria ya fine kwa ajili ya madereva bodaboda itakuwepo? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimempata vizuri mwakilishi na msemaji/mtetezi wa vijana, Mheshimiwa Mlinga. Niseme tu suala la fine sheria yake inapitishwa na Bunge kupitia Finance Bill ambayo itakuja kwenye mapendekezo ya Wizara ya Fedha. Sisi kama Wizara tumependekeza hivyo hivyo kwamba kwa kweli, ni vyema fine ya bodaboda itofautishwe na fine ya mabasi na coaster kwa sababu fine ya bodaboda kuwa sawasawa na ya magari makubwa yanayobeba abiria wengi ndiyo inayosababisha bodaboda nyingi zinarundikana kwenye vituo vya polisi kwa kushindwa kulipia fine zile. Kwa hiyo, tuliona ni vyema ikawa fine inayoweza kulipika ili kuweza kuwa na mantiki ile ya kutoa onyo badala ya kuwa chanzo cha fedha.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, Shule ya Msingi Iputi iliyoko Kijiji cha Mbunga katika Jimbo langu la Ulanga ina msongamano mkubwa sana wa wanafunzi. Sisi tumejenga wenyewe shule nyingine, tumejenga ofisi ya mwalimu kwa kushirikiana na Mbunge wao, tunachoomba usajili na kutuletea walimu. Je, Serikali ipo tayari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA TAWALA ZA MIKOA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ametupa habari hapa Bungeni kuhusu Shule ya Msingi Iputi ambayo tayari wananchi kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wao wameshaanza ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo katika Kijiji cha Mbuga. Nataka nimhakikishie kwamba, naomba ushirikiano wake tukitoka hapa Bungeni leo tuwasiliane na wenzetu wa Wizara ya Elimu ili shule ile tuanze taratibu za kuisajili na tukishaisajili tutaipatia walimu. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Ulanga ya sasa hivi tumeanza uchimbaji wa graphite ambayo tutakuwa tunasafirisha tani 350,000 hadi 500,000 kwa mwaka wastani wa malori 150 hadi 170 kwa siku kwa barabara ya vumbi hatuwezi Serikali peke yake itapata kodi ya mrahaba bilioni 61 hadi 100 kwa mwaka lakini bila barabara ya lami biashara hii hatuwezi kuifanya.
Sasa basi maswali yangu je, Serikali haioni umuhimu wa kukamilisha barabara hii haraka kabla ya mwaka 2020 ili tusizikose hela hizi ambazo tunazihitaji sana kwa sasa hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili Serikali ipo tayari kushirikiana na Mbunge kutafuta wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kuangalia ni namba gani wataharakisha ujenzi wa barabara hii unafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimeeleza hatua ambazo tumekwishaanza kuzifanya kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizo hatua zitakapokamilika ujenzi wa kipande hicho cha barabara utaaanza mara moja kutegemeana na upatikanaji wa pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ninazo taarifa kwamba tarehe 16 Juni, 2018 kutakuwa na kikao kati ya wadau mbalimbali wanaotaka kushirikiana na Serikali katika kujenga kipande hicho cha barabara ambako Mheshimiwa Mbunge naye atakuwepo kwa hiyo tutasikiliza mapendekezo yao kama Serikali kama yana tija kwa ajili ya nchi tutayapokea, lakini ninaamini kwamba Serikali ina mpango madhubuti wa kuhakikisha kwamba kisehemu hicho kinajengwa kutokana na hali ya uchumi iliyoko maeneo hayo. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Ulanga Kijiji cha Gombe kuna mradi mmoja mradi wa kiinimacho. Mawaziri wote anapokuja Waziri maji yanajazwa kwenye tanki usiku kucha, akija Waziri asubuhi anakuta yanatoka. Kaja Waziri kafanyiwa hivyo hivyo, kaja Naibu Waziri kafanyiwa hivyo hivyo. Sasa Mheshimiwa Waziri anatoa kauli gani kuhusiana na mradi huu kiini macho ambao unafanya wananchi wanashindwa kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nilifanya ziara katika Jimbo la Ulanga na tumefika katika eneo lile tumeona hali ya utekelezaji na moja ya majukumu nilichukua hatua ya kuhakikisha yule Mkandarasi anakamatwa kwa sababu ya kusuasua kwa utekelezaji wa mradi ule. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge nipo tayari kukutana naye leo baada ya saa saba tuangalie wapi walikofikia ili mwisho wa siku na sisi tuendelee kuongeza nguvu wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika mkakati wa Serikali kuhakikisha mikoa yote inaungana inakuwa na mtandao wa barabara; kuna barabara inayoanzia Mahenge – Mbuga kupitia Mbuga ya Selous mpaka Liwale. Rais aliahidi wakati wa kipindi cha kampeni, lakini sijaona mahali popote katika Wizara kama kuna mchakato wa kutoboa barabara hii kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Lindi. Je, Serikali inatoa kauli gani kutokana na hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inafanya utaratibu na ni sera kwa kweli kuunganisha mikoa yote. Mheshimiwa Mlinga tumezungumza kwamba barabara hii niliyojibu swali la msingi pia urefu wa kilometa alizozitaja unaunganisha pia sehemu ya Mahenge kuja pale Lupiro. Pia iko haja ya kuunganisha Mahenge na wenzetu wa kule Liwale, lakini kunahitaji logistics nyingi sana kwa sababu inapita katika hifadhi ya mbuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mlinga avute subira, tutaendelea kuzungumza wakati tunaangalia logistics nzuri ili tuweze kuwaunganisha wananchi wa Mahenge na eneo la Liwale kwa maana ya Mkoa wa Lindi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, mgogoro uliopo Manyara unafanana na mgogoro uliopo Ulanga kati ya Selous Game Reserve na wananchi wa Kata za Ketaketa, Ilonga na Mbuga, Mheshimiwa Waziri analifahamu vizuri. Sasa wananchi wameendelea kukamatwa na kupigwa, huku siyo tu kuwachokoza wananchi, ni kunichokoza hata na mimi mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri, lini yuko tayari kwenda kwa ajili ya kumaliza huu mgogoro kati ya Selous Game Reserve na wananchi wa hizi kata?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, niko tayari kuongozana naye kwa sababu tulishakubaliana kwamba baada ya wiki hii Jumamosi inayofuata twende tukaangalie hali halisi katika eneo lile ambako kuna mgogoro. Kwa hiyo, tutakwenda, tutabainisha na tutakaa na wananchi ili tuone kwamba tatizo ni nini na tulipatie ufumbuzi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, mimi nakubaliana na wewe kuwa bila viboko wanafunzi hawawezi wakaenda. Lakini kwa nini Serikali isitoe aina ya mfano wa kiboko ambacho kinatakiwa kitumike kuchapia wanafunzi? Tumeshuhudia walimu wakikata kuni kwa ajili ya kwenda kuwachapia wanafunzi; kwa hiyo watoe kiboko cha mfano.l
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kuhusu ni aina gani ya kiboko kinaruhusiwa kanuni ile ya mwaka 2002 (The Corporal Punishment Regulations) inasema kwamba fimbo au kiboko kinachotumika ni kile ambacho kiko flexible yaani hakijakakamaa ndicho kinasema hivyo, kwa hiyo, sio kwamba ni fimbo yoyote unaweza ukachukua ukamchapa nayo mtoto. Kwa hiyo, tayari sheria imeeleza kwamba ni kiboko cha aina gani ni kiboko ambacho ni kilaini, hakija kakamaa.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wananchi wengi hasa wa Ulanga wamekuwa na muamko mkubwa wa kujiunga na CHF liyoboreshwa, lakini wamekuwa wakilipa hela wanapoenda hospitali huduma zimekuwa haziridhishi, na hii inatokana na usimamizi mbovu wa CHF iliyoboreshwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali mwezi Aprili, 2018 imetoa mwongozo kuwa mtumishi atakayepangiwa kuwa CHF Manager asiwe na majukumu mengine yoyote, lakini huu mwongozo umekuwa haifuatwi. Je, kauli ya Serikali ni ipi kwa watumishi hawa wanaopangiwa kuwa Mameneja wa CHF, lakini wanapangiwa na majukumu mengine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, tunakiri kwamba, mfumo huu wa CHF umekuwa na changamoto na sisi kama Serikali tumeiboresha, kuongeza mafao, zamani CHF ilikuwa unapata huduma katika kituo kilekile ambacho ulikatia, lakini sasa hivi unaweza kwenda mpaka katika ngazi ya mkoa. Hili tunalipokea, hii changamoto ambayo Mheshimiwa Goodluck Mlinga ameitoa kwenda kuboresha mfumo wa usimamizi wa CHF iliyoboreshwa ili iwe na matarajio na makusudio ambayo yamelenga.

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo sasa hivi mwelekeo wa Serikali ni kwenda katika One National Health Insurance Scheme kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunakuwa na bima moja ya afya kwa wananchi wote. mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tutakapoleta muswada huo Bungeni, basi mtusaidie kuunga mkono.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu linahusu barabara ya Kidatu – Ifakara; barabara yenye urefu wa kilometa 69.9. Mradi wake wenye thamani ya shilingi bilioni 109 ambao unafadhiliwa na DFID na European Union.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilifunguliwa tarehe 5 Mei, 2018. Wakati inafunguliwa vifaa viliwekwa vingi na Mheshimiwa Rais lakini Mheshimiwa Rais alipoondoka na Mkandarasi akaondoa vifaa vyake. (Kicheko)

Je, Serikali inatuambia nini kuhusu barabara hii? Ina maana ndiyo tumepigwa changa la macho sisi pamoja na Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) : Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mlinga kwa sababu mara zote amekuwa ukifuatilia sana ujenzi wa barabara hii. Niseme tu kwamba tunawaambia nini wananchi na Watanzania kwa ujumla kuhusu barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulivyoanza ujenzi wa barabara hii kulikuwa na changamoto kuhusu vifaa na material kwenye ujenzi wa barabara hii. Hii ilitokana na mabadiliko ya Sheria ya VAT, kwa hiyo, tulichelewa kidogo. Niwaambie wananchi na Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya changamoto hizi kutatuliwa, sasa Mkandarasi atakwenda kwa kasi kubwa na wananchi wategemee kupata barabara ya lami, bora na itakayowahudumia wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ukiacha Wakuu wa Wilaya ambao wanafanya vibaya wako Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanaofanya vizuri. Kwa mfano, kwa Wakuu wa Mikoa yupo Salum Hapi wa Iringa amekuwa mbunifu kupita kiasi, Ndugu Alexander Mnyeti, Ndugu Mrisho Gambo na Ndugu Paul Makonda... (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, uliza swali Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu ni hili, je, Wizara ina mkakati gani wa kuwaandalia motisha ama tuzo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawa ambao wanafanya kazi vizuri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema hapo awali mwanzo tulikuwa na matatizo mengi sana, sasa hivi matatizo haya kwa kweli kwa kiwango kikubwa yamepungua sana. Ni kweli nikiri wazi kwamba kuna Wakuu wa Mikoa hivi sasa wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, tulianzisha programu ya ujenzi wa viwanda, katika kila mkoa viwanda 100, matarajio yetu ni kupata viwanda 2,600 lakini tumepata viwanda 4,877 ni outstanding performance, lakini kazi hii imesimamiwa na Wakuu wa Mikoa.

Kwa hiyo, agenda ya kuwapa appreciation baadhi ya Wakuu wa Mikoa tumeshaanza kuifanya katika vikao vyetu na juzi-juzi baadhi ya Wakuu wa Mikoa tumeshawakabidhi vyeti vyao kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikish mambo ya Serikali yanaenda vizuri. Kwa hiyo, hilo tutaendelea kulifanyia kazi, ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kata yangu ya Mahenge Mjini ambapo ndiyo Mji wenyewe ulipo, kuna shida kubwa ya soko. Wananchi walijitolea wakajenga soko, Serikali ikatia hela zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 Mwenge ulikuja ukafungua hilo soko, lakini mpaka leo hii soko hilo halijaanza kutumika. Kwa hiyo, Mwenge umedanganywa, Mbunge kadangaywa, wananchi wamedanganywa. Je, lini Serikali itasimamia ufunguaji wa soko hilo ili wananchi wapate kulitumia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhsukuru. Hili jambo tumelipokea, tutalifanyia kazi tuone tatizo liko sehemu gani ili liweze kufanya kazi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ugonjwa wa kifafa una mahusiano makubwa sana na ugonjwa wa akili, kwa sababu mgonjwa wa kifafa akikosa zile dawa zake anakuwa amechanganyikiwa na anakuwa mkorofi na kibaya zaidi mgonjwa wa kifafa huwa anaanguka, kwa hiyo, anaweza kuangukia kwenye moto ama kwenye maji.

Mheshimiwa Spika, Ulanga ni miongoni mwa maeneo kinara duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kifafa na Serikali kwa uzito huo ikaamua kutoa dawa hizo bure kwa nchi nzima, lakini mgao tunaoupata Ulanga haukidhi mahitaji na Serikali inalitambua hilo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuipa Ulanga kipaumbele kwa upatikanaji wa dawa hizi za kifafa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mikoa ndani ya nchi yetu ambayo inaonekana kuna wagonjwa wengi wa kifafa ni pamoja na Ulanga. Nasi kama wataalaam wa afya tunajaribu kufanya utafiti kubaini chanzo, kwa nini Mkoa huu wa Morogoro na hususan katika Wilaya hii ya Ulanga kumekuwa na wagonjwa wengi.

Mheshimiwa Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dawa za wagonjwa wa kifafa pamoja na wagonjwa akili tunazo za kutosha, tutafuatilia katika Wilaya hii ya Ulanga kwa nini hizi dawa hazifiki ili kuhakikisha kwamba wale wote ambao wana ugonjwa huu wa kifafa katika Wilaya ya Ulanga wanapata tiba sahihi.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpongeze Mkuu wangu wa Wilaya kwa jitihada zote za kunyanyua elimu ya Ulanga Bi. Ngoro Malenya.

Mheshimiwa Spika, chuo anachoongelea Mheshimiwa Waziri ni cha mission na kinachukua wanafunzi wachache sana na fani chache ambazo haziendani na rasilimali zinazopatikana Ulanga kama madini, misitu na uvuvi. Wanafunzi wanaomaliza Ulanga kidato cha nne kwa mwaka ni 1000 hadi 1200 na hiki chuo kinachukua wanafunzi chini ya 150.

Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa Serikali isishirikiane na misheni ili kuongeza kukipanua chuo hiki ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna eneo ambalo tulilitoa kwa ajili ya VETA wajenge Chuo cha Ufundi eneo la Mwaya. Je, Serikali inasemaje ipo tayari kutoa hela kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo hiki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama tulivyosema kwamba Wilaya ya Ulanga kwa sasa ina chuo kimoja tu cha binafsi lakini tumeshauri kwamba wananchi wa Ulanga waendelee kutumia vyuo vingine vilivyopo, kuna vingi vipo katika Mkoa wa Morogoro lakini vilevile nchi nzima kwa sababu ndio utaratibu tunaoutumia kwa sababu sio kila Wilaya ina vyuo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na Serikali kushirikiana na wa-misionari wanaoendesha Chuo cha Mtakatifu Francis, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kuendesha vyuo kwa utaratibu wa PPP. Tupo tayari kuona ni namna gani tutajenga Chuo cha Ufundi Stadi Ulanga kwa sababu hata hivyo ni mpango wa Serikali kujenga chuo cha Ufundi Stadi kila Wilaya na Mkoa.

Kwa hiyo, kuhusu eneo ambalo limetengwa, wizara yangu haina shida ya kushirikiana na Wilaya ya Ulanga kuangalia namna gani kile chuo kitajengwa kwa sababu tayari ni mpango wa Serikali kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko la matumizi ya dawa za nguvu za kiume, enzi zenu nakumbuka kulikuwa na mkuyati, lakini sasa hivi, kuna super moringe, mundende, super gafina, gasosi mix, super shafti, sado power, amsha mzuka, Kongo dust na hii Kongo dust imeonesha kuwa mafanikio makubwa. Je, Serikali imeshafanya utafiti nini kinasababisha tatizo hili la watu kutokuwa na nguvu za kiume kupelekea kutumia sana hizi dawa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zinazopelekea kupungua kwa nguvu za kiume ni nyingi, ikiwemo magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, msongo wa mawazo na kadhalika, kwa hiyo kuna sababu nyingi zinazopelekea matatizo haya na ndio maana watu wengi wamekuwa wakitafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Ninachoweza kusema hapa ni kwamba ziko dawa zenye maada ambazo sio za kikemikali, ambazo ni bora zaidi zitumike kuliko kemikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili kama nilivyosema awali TFDA wanao uwezo wa kubaini ni dawa gani ambazo zinasababisha madhara na zile ambazo zinasababisha hakuna budi kutolewa taarifa mapema ili ziweze kuondolewa kwenye soko, lakini tunatambua kwamba sasa hivi kuna dawa zilizopitishwa na Mamlaka za Udhibiti ambazo zinauzwa kihalali kabisa za kuweza kuongeza nguvu za kiume na ambazo hazijaripotiwa kuwa kuna matatizo kama ya athari zinazopelekea kutokana na matumizi ya dawa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wetu ni kwamba wanaotaka kutumia dawa hizi waendelee kutumia zile ambazo zimethibitishwa kitaalam na wasitumie zile ambazo hazina uthibitisho ili wasiweze kupata madhara.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa vinara wa kuwa na viwanda vingi na imekuwa ikitoa ajira nyingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro enzi hizo za ujana wetu.

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vilikuwepo viwanda vya maturubai, magunia, ngozi, mafuta ya kupikia, vipuli vya mashine, mazulia hata Ulanga tulikuwa na kiwanda cha pamba lakini baada ya ubinafsishaji viwanda vyote vikawa kushne, vikawa magofu ya kufugia mbuzi na Serikali imekuwa ikipiga mikwara mara kwa mara…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kwa magofu hayo ambayo yamegeuzwa na wawekezaji badala ya kufanywa kuwa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Goodluck, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali ni kwamba wale wote waliokuwa wamebinafsishiwa viwanda na hawajaweza kuviendeleza kama ambavyo mkataba wao ulikuwa na ambavyo Serikali ilitarajia, tunatarajia viwanda hivyo vitarejeshwa. Mpaka sasa Serikali imesharejesha viwanda 15 na tunaendelea na zoezi hilo ili hivi viwanda viweze kufanya kazi kwa tija iliyokusudiwa.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ukiacha Taasisi nyingi kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake lakini Benki ya Kilimo ndiyo yenye dhamana ya kutoa mikopo. Benki ya Kilimo imekuwa na tabia ya ubaguzi, inatoa mikopo kwa wale wanawake ambao wana uwezo au wake za vigogo, lakini wale wanawake ambao wana uwezo mdogo na wamejiunga kwenye vikundi wamekuwa wakipewa masharti magumu.

Je, Serikali inatoa kauli gani hususan kwa wanawake wa Ulanga, Kilimanjaro na juzi nilikuwa Mbeya kule, hamna hata mmoja aliyepata mkopo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mlinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza siyo kweli kama Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tunatoa mikopo kwa kibaguzi. Hii kama nilivyosema ni benki ya maendeleo, ni benki ya kimakakati na tumeianzisha maalum kwa ajili ya kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini. Kwa hiyo hizi ni pesa za umma, kama pesa za umma lazima zina taratibu zake na zina masharti. Labda hao wanaoona wanapata maana yake ni wanawake waliotimiza vigezo vinavyohitajika na benki ili waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kumshauri kama nilivyosema kwenye jibu letu la msingi, tumewaelekeza wanawake hao hususani wale wa vijijini wajiunge kwenye vikundi, vile vikundi vyao ndiyo vitatumika kama dhamana na benki hii itaendelea kutoa mikopo. Hivi ninavyozungumza, pamoja na maelekezo ya Serikali tuliwaambia kwamba mikopo wanayotoa asilimia 20 watoe kwa akinamama, lakini benki hii imeweza kutoa mpaka leo tunavyozungumzia zaidi ya asilimia 33 ya mikopo yote waliyotoa imekwenda kwa akinamama.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ugonjwa wa dengue ni ugonjwa hatari sana na umekuwa ukiwa kwa kasi sana katika nchi yetu, lakini ugonjwa huu ni mgonjwa wa mlipuko kama magonjwa ya kipindupindu na magonjwa mengine, na Serikali imekuwa na utamaduni wa aidha wa kutibu bure au kwa gharama ya chini za matibabu.

Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kutibu ugonjwa huu bure kwa wananchi ili waweze kupambana nao na usisambae katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna mlipuko wa ugonjwa wa dengue ndani ya nchi yetu na hadi kufikia wiki hii tuna cases 1901 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Kilimanjaro pamoja na Singida ambayo imetambuliwa; na hawa mikoa mengine wengi walikuwa ni wagonjwa ambao wamepitia mkoa huu wa Dar es Salaam. Sisi kama Serikali tumeshaanza kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba tunaudhibiti ugonjwa huu wa dengue

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama nilivyosema hapo awali na katika taarifa zetu, ugonjwa huu hauna tiba, tunachokifanya ni kutibu zile dalili ambazo mgonjwa anakuja nazo ikiwa ni pamoja na matibabu ya homa, maumivu pamoja na upungufu wa maji ambao anakuwa nao. Changamoto kubwa ilikuwa katika katika upatikanaji wa vipimo. Sasa hivi niwahakikishie kwamba katika vituo vyetu vya umma vipimo vimepatikana na tumevisambaza katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na hapa Dodoma. Kusudio letu ndani ya wiki moja ijayo tutapata vipimo tena ambavyo tutataka sasa tuvisambaze nchi nzima ili kuhakikisha kwamba tunaweza kubaini hizi cases za ugonjwa huu wa dengue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hoja kubwa katika maswali mengi ambayo tumekuwa tunayapata ni ugharamiaji ugonjwa huu wa dengue na husasan kwa wale wagonjwa wa bima. Niseme tu kwamba wagonjwa wa ugonjwa huu wa dengue wanapata matibabu kwasababu huu ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine, na wanatibiwa na pale lilikuwa ni suala sasa la vipimo. Kwa wale wagonjwa ambao ni wagonjwa wa dengue ambao wanakadi ya bima za afya wanapokwenda katika vituo vya umma huduma ile ya vipimo wataipata bure. Tutazitoa hizi huduma za vipimo katika hospitali zetu za umma na kwasababu tumeshasambaza vipimo katika hospitali zetu za Umma.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe kuwa tarehe 24 Januari, 2020 Serikali imesaini makubaliano ya kuchukua asilimia 16 kutoka Barrick Gold Tanzania, kwa hiyo sasa hivi Serikali ina 16%, maana yake watu wengi hawajaisikia hiyo, kwa hiyo inabidi tuongeze sauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Gereza la Ulanga mwaka wa tano sasa hivi mahabusu wanapelekwa mahakamani kwa kutumia bodaboda. Hii ni hatari sana kwa mahabusu kutoroka. Naomba kuuliza swali la nyongeza, je, ni lini Serikali itapeleka gari la mahabusu Gereza la Ulanga? (Makofi/ Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mlinga kwa jinsi ambavyo anaweza kujenga hoja zake kwa msisitizo, sisemi kwamba anatia chumvi, lakini anajenga hoja kwa msisitizo na anatukumbusha mambo muhimu kama ambavyo ametukumbusha hili suala la mafanikio kwenye sekta ya madini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mlinga kwamba najua anapozungumza bodaboda alitaka tu kuongeza uzito wa hoja yake, lakini tunatambua juu ya changamoto ya usafiri katika baadhi ya magereza yetu nchini na nimhakikishie pale ambapo gari mpya zitakapopatikana, tutampelekea katika gereza hilo la Jimboni kwa Mheshimiwa Mlinga ili kukabiliana na changamoto hiyo ya usafiri.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vitendo hivi vinasikitisha sana. Huwezi ukakuta ng’ombe dume anapanda ndama, huwezi ukakuta jogoo anapanda kifaranga lakini binadamu aliyepewa utashi anafanya vitu hivyo. Ukiangalia trend ya matukio yanaongezeka kwa kiasi kikubwa. Matukio 13,457 mwaka 2018 yameongezeka kwa 1,000 lakini ukienda Mahakamani hukuti hizi kesi. Je, Wizara ina mkakati gani kuhakikisha haya matukio yote inasimamia upatikanaji wa ushahidi na kuhakikisha yanakwenda Mahakamani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sehemu kubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinasababishwa na mila na desturi potofu. Kwa mfano, katika mila za Kihehe kuna utamaduni unaitwa Nyangusage, katika tamaduni za Kisukuma kuna mila inaitwa Chagulaga na Kigoma kuna Teleza. Wizara ina mkakati gani wa kutoa elimu kuhakikisha mila na tamaduni potofu zinatokomezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matukio haya yamekuwa yanaongezeka na changamoto kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba asilimia zaidi ya 60 ya matukio haya yanafanywa na watu ambao wako karibu na familia na tumekuwa tunapata changamoto kama Serikali kuyafikisha na kuchukua hatua kwa wale wahusika kwa sababu ndugu na jamaa wanakaa vikao vya familia wanaamua kumalizana kwa kutozana faini au kwa kumtorosha yule mwathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii kuhakikisha kwamba haya mambo hayamalizwi katika mazingira ya nyumbani na badala yake mkondo wa sheria uruhusiwe kuchukua hatua. Kama Serikali ama kama Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto tunafanya kazi kwa karibu sana na Idara ya Mahakama, tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Mambo ya Ndani na tuna mpango unaitwa MTAKUWA ambao ni mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha 2021/2022. Katika mpango mkakati huu, taasisi zote za kisekta ambazo zinashirikiana kwa pamoja tuna lengo la kuhakikisha kwamba suala hili la ukatili wa kijinsia tunaweza kulidhibiti ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mlinga ameuliza swali lake la pili kuhusiana na mila na desturi potofu. Hili kama Wizara tunaendelea kulifanyia kazi na tumekuwa tunafanya kazi kwa karibu sana na viongozi wa kidini, kimila, wanazuoni na sasa hivi tumeanza hata kufanya kazi na wasanii mbalimbali kuhakikisha kwamba tunafikisha ujumbe huu kwa jamii. Suala lililotokea kule Kigoma la Teleza, lile siyo mila, ni suala la uhalifu, nasi kama Serikali tulichukua hatua na kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa ninavyoongea wako Mahakamani na mkondo wa sheria unachukua hatua zake. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niipongeze Serikali kwa dhati kabisa kwa juhudi zake za dhati za kuboresha utalii katika nchi yetu. Kama Mbunge, nimesikitishwa na kauli za baadhi ya Wabunge wa Upinzani kubeza juhudi za Serikali za kuboresha utalii na kuchochea kwa kutumia wasanii wa ndani. Niwaambie tu wasanii, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua mchango wao mkubwa katika kuijenga nchi yetu. Kwa hiyo iwapuuze hao, hii ni tabia yao na ndivyo walivyo.

Mheshimiwa Spika, swali langu namba moja, maeneo au halmashauri nyingi ambazo zimezungukwa na National Park hawanufaiki na shughuli za utalii kwa kuwa hoteli zile zimejengwa ndani ya zile mbuga. Sasa je, Seriakli haioni sasa umefika wakati wa kuweka utaratibu wa kujenga hoteli zile za kitalii nje ya zile hifadhi ili wananchi wa maeneo yale waweze kunufaika kama kodi na vitu vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, tunafahamu nyamapori ni tamu sana. Mtalii anapoona akatamani na akala, itavutia watalii wengi sana kuja hasa wa ndani. Je, Serikali haioni sasa umefika wakati iweke utaratibu wa kuweka vigenge vya nyama choma ndani ya mbuga zile ili mtalii anapoona nyama ile anaitamani halafu anaila sio aone, atamani, aondoke. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, MALIAISILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza kipekee kabisa naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mlinga, watu wengi wanapomuona hapa Bungeni huwa wanafikiri ni mtu wa vituko lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mlinga ni mfuatiliaji mkubwa sana wa masuala ya uhifadhi lakini na masuala ya kiuchumi yanayohusu wananchi wake na halmashauri yake. kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Mlinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hivi karibuni tumefanya mabadiliko ya Kanuni na tunaandaa Kanuni ili kuruhusu matumizi ya nyama ya wanyamapori kwa watu wengi na katika kufanya hivyo tunapitia upya kanuni ili tuweze kuruhusu uwindaji wa ndani lakini pia kufunguliwa kwa mabucha ambayo yatakuwepo katika maeneo mbalimbali na kuyasajili. Kwa hiyo, taratibu hizo zitasaidia pia kuhakikisha kwamba nyama hii ya wanyamapori inapatikana katika maeneo yote yaliyoko katika hifadhi na maeneo ya mapori ya akiba ambapo wafanyabiashara watataka kupeleka nyama hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Mlinga anataka kujua maoni ya Serikali ni kwanini hoteli zisijengwe nje ya hifadhi. Nakubaliana na Mheshimiwa Mlinga kwamba hivi sasa kwa mfano katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, nafasi ya kujenga hoteli ndani zimejaa na uzoefu tulionao ni kwamba kadri hoteli nyingi zinavyozidi kujengwa ndani ndivyo uharibifu wa mazingira unazidi kuondoa uhalisia wa hifadhi yenyewe ya Serengeti.

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana kwa sasa kwamba wawekezaji wote wapya tutawapeleka nje ya Hifadhi ya Serengeti na hifadhi zingine za Taifa ili kuvutia pia wananchi wanaozunguka maeneo hayo kuweza kujishughulisha na biashara ndogondogo moja kwa moja na hoteli hizo. Kwa hiyo, tunauchukua huo kama ushauri ingawa hauwezi kutumika hivyo katika hifadhi zote kwa sababu zipo hifadhi ambazo bado zina nafasi ambazo zimetengwa kwa ajili ya uwekezaji. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kumekuwa na matumizi ya hovyo kabisa katika halmashauri zetu na kupelekea halmashauri hizo kupata hati chafu. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imepata hati chafu kwa mwaka mmoja, mimi najiona kama natembea bila nguo, lakini halmashauri kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri ya Ujiji ambayo inaongozwa na ACT anapotoka Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, miaka minne mfululizo imepata hati chafu wakati yeye akishinda twitter na instagram. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifuta halmashauri hizi? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Ulanga, alikuwa anasema maneno mengi sana hapa Bungeni wakati mwingine akaonekana kwamba ni kituko, lakini naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kauli ya Mheshimiwa Mbunge wa Ulanga imetusaidia sana TAMISEMI na watu wengi wamewajibishwa katika halamshauri ile na uchunguzi mahususi umefanyika tukagundua kuwa ni kweli kwamba watumishi wetu wamwekuwa wabadhilifu, fedha nyingi zililiwa, kama alivyokuwa analalamika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, ni kweli, Kamati ya Bunge ya LAAC wapo, Mwenyekiti yupo hapa na Wajumbe wenzake wanafamu. CAG alipopitia baadhi ya halmashauri, hata mimi nilishangaa, halmashauri mbili, wamepoteza fedha zaidi ya shilingi bilioni kumi na kitu, lakini Halmashauri ya Kigoma Ujiji, halmashauri hii imekuwa na hati chafu mfululizo miaka minne, lakini tulipowahoji viongozi wa pale, wakatuambia viongozi wetu wa kisiasa, wanaingilia mpaka manunuzi ya kisheria, mpaka tenda ambazo zinagawanywa pale Kigoma Ujiji, wanapewa kwa itikadi za kivyama, hizi ni taarifa rasmi za Bunge, ninazozitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumetoa maelekezo, ni kweli kwamba, ile halmashauri ikiendelea kupata hati chafu ya tano na itapewa ukaguzi mahususi, kuna uwezekano mkubwa Mheshimiwa Zitto halmashauri yako kufutwa kwa sababu husimamii vizuri, na wewe ni mtaalam wa mahesabu. Ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ukatili mkubwa wa Wanyama unafanywa pindi Wanyama wanaposafirishwa, tumeshuhudia malori yakipita matani na matani yanatoa ng’ombe Karagwe Kanda ya Ziwa yanapeleka Dar es Salaama.

Mheshimiwa Spika, Sasa kwa nini Serikali isitoe agizo ijengwe Kiwanda huko, ng’ombe zichinjwe ndiyo wasafirishwe wapelekwe Dar es Salaam? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Swali la pili, ukatili mbaya kuliko wote ni upigaji chapa wa ng’ombe, tumeshuhudia ng’ombe wakiteswa kwa kupigwa chapa, Serikali imeshindwa kubuni mbinu nyingine tofauti na hiyo, Je, Serikali inatoa kauli gani na upigaji chapa wa hovyo kabisa na utesaji wa mifugo yetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunajenga Viwanda vya kutosha vya kuchakata mazao ya mifugo, na ndiyo maana katika baadhi ambapo mifugo inapatikana kwa wingi kama vile Mkoani Arusha katika Wilaya ya Longido tumefanikiwa kujenga Kiwanda ambacho kipo katika hatua nzuri ya kumalizika na hatimaye kuweza kuchakata mifugo.

Mheshimiwa Spika, rai yake ni kwa nini tusafirishe mifugo kutoka Karagwe na Mikoa mingine kama Kigoma na kupeleka katika machinjio, hali ambayo inapelekea kurundikana kwa mifugo katika magari na hatimaye kuitesa mifugo hiyo. Sisi tutaendelea na jitihada ya kuhakikisha mpaka kule Karagwe Kigoma na kwingineko Viwanda hivi vinaenea. Lakini ndiyo maana Serikali inaendelea kuboresha pia vilevile miundombinu yetu ili kusudi hata hizi hali za ukusanyaji wa mifugo kwa wingi katika magari wakati mwingine ni kwa sababu ya miundombinu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Mkoa wa Kigoma, ile harakati ya ujenzi wa barabara ile, itarahisisha mifugo inayotoka katika Mkoa huo ili iweze kufika katika soko na hatimaye kuwanufaisha wafugaji na wananchi wa Mikoa hii ambayo ina mifugo kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni suala la upigaji chapa ng’ombe, kwanza naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kuwa tunayo Sheria mahsusi kabisa ya utambuzi wa Wanyama katika Sheria za nchi yetu. Sheria hii inatuelekeza kila ng’ombe lazima atambuliwe na hii ni katika kuhakikisha kuwa tunakwenda sambasamba na mahitaji ya Sheria za Kimataifa ya soko la Kimataifa na nyingenezo.

Mheshimiwa Spika, rai yake ni kwa nini tusitafute njia nyingine mbadala, badala ya kuchoma ng’ombe moto, rai hii ya Waheshimiwa Wabunge tunaichukua na tumeanza kufanya kazi ya kuhakikisha tunatumia teknolojia ya hereni, earrings kwa upande wa ng’ombe wa maziwa, kwa kuwa Wabunge wengi wanaonekana kuwa wangependa kuona tunabadilisha utaratibu huu wa kuchoma moto tumelichukua jambo hili na tutalifanyia kazi kwa ajili ya kuweza kuitekeleza vyema Sheria ile ya utambuzi wa mifugo yetu.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante wananchi wangu wa Epanko tangu wafanyiwe tathimini ni miaka miwili mpaka sasa hivi hawajalipwa, na Mheshimiwa Waziri alishafika huko na anajua shida, sasa sheria inasema mtu akifanyiwa uthamini baada ya miezi sita anatakiwa alipwe na ikizidi hapo analipwa fidia na uthamini ukizidi miaka miwili unakuwa cancelled unafanywa upya, nataka kusikia kauli Serikali. Je, hawa wananchi waliofanyiwa uthamini wao lini watalipwa ni miaka miwili imeshapita?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli uzuri kwenye sheria ya uthaminishaji na kulipa fidia iko wazi tunataka makampuni yote yakishafanya uthamini walipe ndani ya muda uliokubaliwa, mtu ambaye hatalipa ndani ya miezi sita sheria inasema atalipa lakini atalipa na interest yaani kwa maana ya usumbufu na asipolipa ndani ya miaka miwili, sheria inasema kwamba tayari ule uthaminishaji una- expire kwa mujibu wa sheria kwa hiyo ni lazima mrudi mfanye uthaminishaji upya.

Mheshimiwa Spika, nipende kutoa tu wito kwa makampuni yote walipe kwa muda ambao umepangwa wasipofanya hivyo inaleta mtafaruku, mfano mzuri uko kule Mara Tarime, kuna watu ambao hawakulipwa ndani ya muda matokeo yalivyokuja kuonekana ni kwamba sasa wale wenye zile nyumba waliona kwamba baadaye wataonekana watakuja kuondolewa wakawa wanajenga nyumba za kutegesha, nyumba za gharama nafuu ili waje walipwe fedha nyingi. Sasa hii imetokea maeneo mengi, kwa hiyo tunaomba sana makampuni yote tunawahasa mkishafanya uthaminishaji lipeni kadri ya sheria inavyosema usipofanya hivyo inaleta mtafaruku. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kwa niaba ya wananchi wa Ulanga, naomba niishukuru Serikali ya CCM kwa kutupa kipaumbele kwenye Sekta ya Afya. Maana yake tumepata shilingi milioni 400, Kituo cha Afya cha Lupilo kimeisha na shilingi milioni 400 imeingia juzi.

(a) Hospitali hii ya Wilaya wakati inajengwa, mwaka 1905 wilaya ilikuwa na watu 23,000, leo hii wilaya ina watu zaidi ya 200,000: Serikali haioni kiasi hiki cha fedha, shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa hospitali hii ni kidogo sana?

(b) Hospitali yetu ya Wilaya ya Ulanga imekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi wachache na wasio na sifa: Je, lini Serikali italeta watumishi wa kutosha na wenye sifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza tunapokea pongezi za Serikali kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge na kwa niaba ya wananchi wa Ulanga. Mheshimiwa Mbunge ana maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, tumepeleka shilingi milioni 400, anadhani kwamba ni pesa kidogo.

Naomba tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni awamu ya kwanza, tunapeleka fedha katika maeneo mbalimbali ya nchi hii kama alivyosema kwa kuzingatia kipaumbele cha afya. Baada ya awamu hii kwisha tutaangalia pia kutokana na uwezo wa Serikali tutaongeza fedha nyingine. Lengo ni kuimarisha hospitali hii iweze kutoa huduma inayostahiki na hata kadri ambavyo wananchi wapya wataendelea kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mlinga anauliza habari ya watumishi. Muda uliopita Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Kandege, alitoa taarifa kwenye Bunge hili Tukufu kwamba tumeshapeleka barua kuomba kupata kibali cha kuajiri watumishi kwa upande wa Sekta za Elimu na Afya. Kwa hiyo, wakati wowote tukipata kibali hicho, tutakapoajiri tutazingatia maombi ya Mheshimiwa Mbunge lakini pia na maeneo mengine ya nchi hii. Ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ujenzi wa reli uendane sambamba na ujenzi wa barabara hasa kwa maeneo yenye misongamano mkubwa wa abiria na mizigo. Kwa mfano barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro, ile barabara ina hali mbaya sana, ina msongamano mkubwa wa magari na inatumia masaa matano hadi sita kwa basi la abiria. Serikali ilikuwa na mpango wa kujenga barabara (highway) barabara sita, kutoka Dar es Salaam mpaka Chalinze – Morogoro na sasa hivi imesitisha.

Sasa nataka kusikia kauli ya Serikali, je, lini itafufua tena mpango huu wa ujenzi wa hii barabara ili kuondoa kadhia hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, Serikali haijasitisha ujenzi wa barabara njia sita ya kutoka Dar es Salaam kuja Chalinze, isipokuwa ujenzi unaendelea kwa hatua na hata juzi tu nimefanya ukaguzi wa barabara. Ile barabara ya kutoka Kimara kuja Kibaha sasa tuko 28% na mkandarasi anaendelea kulipwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Mlinga uvute tu subira kwamba tumejipanga vizuri kadri tunavyopata fedha, tunaendelea na harakati za ujenzi wa barabara hiyo. Hata hivyo, tunaendelea kufanya maboresho mbalimbali maeneo ambayo yanakuwa na uharibifu kwa sababu ni kawaida maeneo ambayo yanaharibika Serikali tunaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho mbalimbali ili barabara ipitike wakati tunaendelea na hatua upanuzi wa barabara.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Uwepo wa kundi kubwa la watoto wazururaji kunasababishwa na wazazi kutofuata njia bora ya uzazi wa mpango. Njia bora kabisa ya uzazi wa mpango isiyo na madhara yoyote ni matumizi ya mipira ya kike na ya kiume.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa katika jamii yetu kumekuwa na tatizo kubwa la watu kutotumia mipira ya kike na ya kiume licha ya watengenezaji kuweka vionjo mbalimbali katika dhana hii kwa mfano strawberry, ndizi, chocolate na hivyo kusababisha siyo tu kuwa na watoto wa mitaani bali ongezeko kubwa la magonjwa ya zinaa na HIV. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu inayoendana na wakati ya watu kutumia mipira hii ya kiume ili kuondokana na changamoto hii ya watoto wa mitaani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, moja ya kisababishi ambacho kinapelekea kuwepo na watoto wa mitaani, ni wazazi kutojiandaa kupata watoto na labda na lingine ni moja ni kwamba watu kupata ujauzito wakiwa na umri mdogo pasipokuwa na uwezo wa kulea.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tumekuwa tunahimiza sana suala la uzazi wa mpango na katika suala hili la uzazi wa mpango kuna njia mbili, kuna matumizi ya dawa, lakini hata hii mipira ya kiume kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema.

Mheshimiwa Spika, kKwa hiyo rai yangu kwa jamii ni kwamba kabla hatujaanza kuingia katika suala la kupata watoto ni muhimu ni vizuri tukajitafakari katika masuala mazima ya malezi na matunzo ya watoto. Suala siyo kuzaa tu ila ni kuhakikisha kwamba watoto wale tunaweza tukawalea na kuwapa matunzo ambayo yanastahiki na njia zote hizi tunazo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa kondomu tunazo za kutosha ndani ya nchi.