Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Omar Abdallah Kigoda (11 total)

MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, kwa kuwa, Wakandarasi wakipewa kazi huwa wanapewa na time frame ya kumaliza ile kazi, hii barabara imeshafanyika kwa asilimia 69, naomba Mheshimiwa Waziri anipe jibu asilimia 31 iliyobaki atakabidhiwa lini na Mkandarasi?
Swali la pili, kwa kuwa, Wataalam wamethibitisha tairi za super single zinazofungwa kwenye malori zina uharibifu mkubwa sana wa barabara zetu. Je, ni lini Serikali itatoa maamuzi kuhusu hizo tairi ambazo zinaharibu barabara zetu zinazo-cost hela nyingi sana za wananchi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, time frame ya kukamilisha barabara hii hivi sasa iko katika majadiliano kutokana na kuchelewa kwa Serikali kumlipa Mkandarasi kulikotokea katika kipindi kilichopita na hivyo, alivyorudi sasa tutapata muda kamili wa kukamilisha barabara hii kutokana na majadiliano yanayoendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la matairi ya super single, Serikali hivi sasa inangalia uwezekano wa kubadilisha kanuni zinazotumika kwa sasa ama kupunguza kiwango cha uzito utakaotumika kwa super single badala ya kutumia kile kiwango cha matairi mawili, kipungue chini ya matairi mawili ama kupiga marufuku kabisa. Kwa hiyo, hilo tunalishughulikia na mara Kanuni hizo na baada ya kujadiliana na wadau kutakapokamilika, tutalijulisha Bunge lako maamuzi yatakayotokea.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwa kuwa Serikali imeshatoa kibali cha kupeleka wauguzi kule na ukizingatia kwamba hospitali ina upungufu wa wauguzi zaidi ya asilimia 60. Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kupeleka hao wahudumu ukizingatia kwamba hali ya kule siyo nzuri kwa sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema wenzetu wa Handeni waliomba kibali. Naomba niseme kwamba ni vibali katika kada mbalimbali zimeombwa, lakini naomba niwahakikishie wazi kwamba, kwa sababu mchakato wa utoaji wa vibali ulishaanza katika sekta ya elimu hasa katika suala zima la walimu wa sayansi, kwa kadri Serikali itakavyoona inafaa tutajitahidi kuhakikisha tunapeleka nguvu na hasa vile vibali ambavyo vimebainishwa.
Ofisi ya Utumishi ikishatoa go ahead katika maeneo mbalimbali, tutashiriki kuona ni jinsi gani tutafanya kuongeza watumishi, tukijua kwamba siyo sekta ya afya peke yake isipokuwa kada mbalimbali zina matatizo makubwa sana na hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba tunafanya kila iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata huduma inayostahiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Omari naomba ondoa hofu katika hilo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda kwamba Serikali za Vijiji chini ya TAMISEMI zinasimamiwa vizuri na sasa wenzetu TAMISEMI wanataka kuweka mpango wa kuhakikisha kwamba mikataba yote inayoingiwa kati ya vijiji na wawekezaji tunakuwa na wataalam wa sheria kutoka Halmashauri wanaohakikisha kwamba maslahi ya wanavijiji yanalindwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge masuala haya na sisi tunayafuatilia kwa sababu yanatuletea picha siyo nzuri sana kwa wawekezaji wetu tunaowapeleka maeneo mbalimbali ya vijiji wanakojenga minara. Tutayafuatilia na baadaye tutakuja kukuletea mrejesho kupitia wenzetu wa TAMISEMI.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa swali hili la mawasiliano linafanana sana na matatizo katika Jimbo la Kilindi katika Kata za Saunyi, Kwekivu na Tunguli. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini kampuni za mawasiliano zitaweza kuweka minara katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi? Ahsante.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kila kitu karibia kimeshakamilika, wananchi wa Handeni, Kiberashi, Kijungu, Kiteto na Nchemba wao wanataka kujua ni lini huu mradi utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kuwahakikishia wananchi wa maeneo hayo yote aliyoyataja kuanzia Handeni – Kiberashi – Kijungu – Kiteto – Nchemba - Kwamtoro hadi Singida ambako barabara hii itapita, Serikali imedhamiria kwa dhati kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Mwaka huu wa fedha ndiyo tunaanza kufanya maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami na tumetenga shilingi milioni 500 kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi. (Makofi)
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Handeni inahudumia karibia majimbo manne; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekubali hili ni suala la dharura haoni kwamba kuna umuhimu wa sisi kupata ambulance badala ya kutumia haya magari ya kawaida ambayo muda mwingi vifo hutokea njiani kwa sababu sio magari special ya kusafirisha wagonjwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba uko uhitaji mkubwa sana wa gari la wagonjwa na pia ni ukweli usiopingika kwamba uwezo wa Halmashauri kuweza kununua gari jipya kwa sasa hivi ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulitambua hilo ndiyo maana Halmashauri ya Handeni imetuma ombi maalum Wizara ya Fedha ili kuomba gari la wagonjwa liweze kununuliwa. Naamini hali ya bajeti ikitengemaa ombi lao litaweza kujibiwa na wagonjwa waweze kupata gari ambalo litakuwa linamudu kwa mazingira ya Wilaya ya Handeni.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya maji Handeni na Kilindi ipo kwa muda mrefu sana na sababu kubwa nyingi ni miradi ambayo imefanywa chini ya kiwango. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge twende wote tukakague miradi ile na Serikali iweze kuwatolea maamuzi kwa wahusika wote walioshiriki katika kutekeleza miradi hiyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Omari Kigua na kaka yangu Mheshimiwa Kigoda kwa namna ya kipekee wa ufuatiliaji wao wa maendeleo ya majimbo yao kwa wananchi wa Handeni pamoja na Kilindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya maji lakini wapo baadhi ya wajanja wajanja kwa maana ya wakandarasi na wahandisi wanahujumu fedha hizi za Serikali. Huruma hailei mwana. Sisi kama viongozi wa Wizara hatutomuonea haya mtu yeyote. Yapo maneno yanayosema kwamba eti huyu ni mtu wa kigogo tutamuonea haya, hata awe mtoto wa kigogo cha namna gani tutatumia chainsaw kulicharanga awe kuni wananchi waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya halmashauri bado zinalalamikiwa kwamba utekelezaji huu ni mdogo au wakati mwingine haufanyiki kabisa. Je, malalamiko haya yanapotokea katika baadhi ya halmashauri, hawa vijana, walemavu na akina mama, ni wapi wanapaswa waende kulalamika ili kuhakikisha utaratibu huu unafanyika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema hapo awali, ni kweli kwamba hatua ya kwanza kabisa ya kusemewa ni kwa Mheshimiwa Diwani, lakini vilevile kupitia Baraza la Madiwani ambacho ndicho kikao cha kwanza kabisa kuhoji kuhusu mgawanyo wa fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Spika, lakini katika ukaguzi ambao wamekuwa wakiufanya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali amekuwa akionesha kwamba halmashauri ambazo hazitengi fedha kikamilifu kama ambavyo mapato ya ndani yanaonesha zimekuwa zinaandikiwa madeni. Kwa hiyo, uwajibikaji unaanzia hapo na hatua hizi tutaendelea kuzifuatilia. Kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba tunatarajia kuweka kipengele kwenye sheria ambacho kitalazimisha sasa kila halmashauri itenge asilimia 10 ya mapato yake ya ndani na itoe fedha hizo kwa ajili ya vikundi vya vijana na wanawake. (Makofi)
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na suala la elimu bure, imeleta changamoto ya kuwa wanafunzi wengi sana ambao wamejiandikisha, lakini kuna uhaba mkubwa sana wa Walimu ambao unasababisha hawa wanafunzi wasipate elimu bora: Je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kuajiri Walimu wengi zaidi ili hawa wanafunzi waweze kupata elimu bora?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kwamba elimu ya msingi bila malipo imeleta chachu ya maendeleo na mwamko mpya na wanafunzi wengi wamejiandikisha na kuingia katika mfumo wa elimu Tanzania. Hili ni jambo jema na kupongezwa kwa maamuzi thabiti ya Mheshimiwa Rais kwa Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, mpango uliopo ni kwamba tunao Walimu zaidi ya 11,000 katika Shule za Sekondari, ambao hawa tunaona kwamba mzigo wao siyo mkubwa sana, tumeomba kibali washushwe waje kufundisha Shule za Msingi ili waweze kuziba gap la uchache wa Walimu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kumekuwa na wale Walimu ambao wanastaafu na wengine wanapata makosa ya kinidhamu kazini na wengine wanafariki dunia, lakini hapa katikati kumekuwa na mkwamo kidogo, Mheshimiwa Rais amesharuhusu kuajiri angalau kila mwaka kupunguza gap hili.

Mheshimiwa Spika, mpango wa tatu, tumepata kibali cha kuajiri Walimu zaidi za 6,000 ambao wakiajiriwa watapunguza upungufu wa Walimu katika Shule zetu za Msingi. Ahsante sana.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza kabisa napenda kuishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha Wanahandeni cha muda mrefu kwa kuitengea hela hiii barabara. Barabara ya Mziha - Handeni matatizo yake ni sawasawa na barabara inayotoka Handeni kwenda Kilindi. Barabara hii inaunganisha mikoa karibu minne ambayo ni Tanga, Manyara, Dodoma mpaka Singida. Barabara hii asilimia kubwa wanayoitumia ni wakulima na huwa wanapata tabu sana…

MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swali sasa.

MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni lini barabara hii inayotoka Handeni kwenda Kilindi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inayo mpango wa kujenga barabara hiii kutoka Handeni kilometa 461 inapita katika maeneo ya Handeni, Kivirashi, Kijungu, Kibaya, Njoro, Mrijo chini inakwenda Chemba hadi Singida. Tunao mpango wa kujenga barabara hii na tayari imeshasanifiwa. Niseme tu kwamba katika mwaka huu wa fedha unaokuja tutapendekeza kwenye Bunge lako ili tuanze kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii muhimu kwa sababu barabara hii itakwenda sambamba na bomba la mafuta ambalo litajengwa. Kwa hiyo ni barabra muhimu sana, kwa hiyo nimwombe tu Mbunge avute subira kwamba tutakuja kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwenye maeneo ambayo ni korofi ambayo yanapita eneo la Kilindi, kwa mfano, eneo la kutoka kwa Luguru kwenda Kibirashi ni eneo ambalo kidogo lina ukorofi, tumepanga katika mwaka unaokuja kwamba wakati tuna harakati za kujenga kiwango cha lami tutaiimarisha eneo hili kwa kujenga daraja katika eneo la Kigwangulo. Mheshimiwa Kigua naona anapiga makofi pale anafahamu eneo hili lina changamoto, kwa hiyo tutakuja kuimarisha wakati huo Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga kiwango cha lami.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Bunge lililopita niliuliza kuhusu suala la ambulance na Mheshimiwa Waziri aliniambia tuendelee kutumia magari ya kawaida mpaka ambulance itakapopatikana. Tatizo la magari ya kawaida hayana vifaa maalum vya huduma ya kwanza kwa hiyo wagonjwa wengi wanaotoka pale hospitali kwenda hospitali nyingine wengi wanapoteza maisha njiani. Sasa nauliza tena, je, ni lini tena Serikali itaona umuhimu wa kuipatia Hospitali ya Handeni ambulance, asante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kipekee kabisa nitumie fursa hii kuwapongeza Wabunge wa Mkoa wa Tanga maana maswali ya kuhusiana na afya wiki hii yamekuwa kila leo yakiulizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake ambalo anauliza juu ya umuhimu wa Serikali kuhakikisha kwamba inapatikana ambulance kama ambavyo tulishawahi kujibu hapa, naomba niendelee kumsihi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kwa kupitia Wizara ya Afya ipo kwenye mchakato katika hatua za mwisho kuhakikisha kwamba ambulance zinanunuliwa. Na naamini katika maeneo ambayo yatakumbukwa kuhakikisha kwamba kile tulichoahidi kama Serikali tunatekeleza na yeye atapata.
MHE. OMARY A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Handeni - Mziha na barabara ya Handeni- Kibirashi kutokana na mvua hazipitiki sasa hivi. Je, ni nini uamuzi wa Serikali kuhakikisha kwamba wanaokoa zile barabara ziweze kupitika wakati tunasubiri ziwekwe lami ili wananchi waweze kusafirisha mali zao na wao waweze kusafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omary Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu niwape pole sana wananchi pamoja na Mheshimiwa Mbunge Kigoda kwa sababu maeneo yale nilitembelea walipata shida kubwa sana wakati wa mvua ilipokuwa kubwa na maji yalikuwa mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake tumechukua hatua za dharura kurejesha miundombinu katika maeneo haya. Kulikuwa na uharibifu mkubwa daraja lilikatika pale Nderemi pamoja na bwawa kubwa ambalo lilisababisha pia kukatika kwa daraja hili, tumerejesha kwa kushirikiana na Jeshi na sasa panapitika na maeneo mengine pia tumeweza kutengeneza barabara ya kilometa 24 kuunganisha Mji wa Handeni pamoja na Mziha na sasa panapitika.

Pia tumeiunga barabara ya Handeni pamoja na Korogwe, niseme kwa ujumla tumejipanga kuimarisha maeneo yote yaliyoathirika na mvua na Bunge lako limetenga fedha kwa ajili ya kumudu dharura zinazojitokeza, tutaendelea kutumia fedha za dharura katika maeneo yote nchini ambapo tutakuwa tunapata uharibifu wa mvua, kurejesha miundombinu ili wananchi waendelee kupita wakati wote.