Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Omar Abdallah Kigoda (14 total)

MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya barabara ya Handeni – Mzika – Dumila na ile ya Handeni – Kiberashi, hasa ikizingatiwa kuwa upembuzi yakinifu umeshafanyika tangu kipindi cha uongozi wa Awamu ya Nne?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni hadi Mzika yenye urefu wa kilometa 70 ni sehemu ya barabara ya Handeni – Magole – Turiani – Dumila, yenye urefu wa kilometa 154.6. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii ulishakamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii unafanywa kwa awamu kwa kuanza na sehemu ya Magole hadi Turiani yenye kilometa 48.8 ambapo ujenzi wake unaendelea na umefikia asilimia 69. Ujenzi wa sehemu ya Turiani – Mzika hadi Handeni wenye urefu wa kilometa 105.8 utaanza baada ya kukamilika sehemu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni hadi Kiberashi yenye kilometa 80 ni sehemu ya barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwamtoro hadi Singida yenye urefu wa kilometa 461 ambayo iko katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi yakinifu wa barabara hii umekamilika na usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni uko katika hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara hizi zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mikoa ya Tanga, Morogoro na Manyara na kuinua uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:-
Kufuatia kukamilika kwa barabara za Handeni – Korogwe na Handeni – Mkata:-
Je, ni lini Serikali itafungua Vituo vya Mizani katika barabara hizo ili kuokoa barabara hizo na kukusanya mapato hasa ikizingatiwa kuwa miundombinu hiyo imeshatengenezwa lakini inaendelea kuharibika na haijawahi kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda barabara ya Handeni - Korogwe pamoja na Handeni - Mkata zisiharibiwe Serikali imeshafungua vituo vya mizani vya Kwachaga kilichopo barabara ya Handeni hadi Mkata na Misima kilichopo barabara Handeni hadi Korogwe. Mizani zote zimefunguliwa na kuanza kazi mwezi Desemba, 2015.
MHE. OMARI A. KIGODA Aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Handeni inahudumia wagonjwa kutoka Kilindi, Mziha, Wegero na Handeni yenyewe.
Je, ni lini Serikali itaipatia vifaa tiba na wauguzi wa kutosha hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mahitaji ya vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Serikali imetenga shilingi milioni 181.9 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Fedha zote zimeshapokelewa na zimetumika kununulia vifaa tiba vinavyohitajika kusaidia utoaji wa huduma vikiwemo BP machine, vifaa vya kupimia kiwango cha damu, vifaa vya kujifungulia na kupima upumuaji wa watoto, pamoja na kulipia gharama za manunuzi ya jokofu katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Halmashauri imeomba mkopo kutoka Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) ili kununua ultra-sound yenye thamani ya shilingi milioni 75. Halmashauri imeahidi kurejesha fedha zote kupitia makusanyo ya Tele kwa Tele ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi katika Hospitali hiyo ni 359, watumishi waliopo ni 170 na upungufu ni watumishi 189. Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi 118 katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo baadhi ya watumishi hao watapelekwa katika Hospitali ya Wilaya. Kati ya watumishi hao walioombwa, watumishi 49 ni wauguzi, watumishi 25 ni madaktari na kada nyingine ni watumishi 44.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni lini Kampuni ya Simu iliyofunga mnara wake katika kijiji cha Kwamatuku itauwasha ili wananchi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uliikabidhi Kampuni ya Simu ya MIC (Tigo) kazi ya kujenga mnara katika kata ya Kwamutuku yenye vijiji vya Komsala, Kwamatuku, Kweingoma na Nkale. Ujenzi huo ulikamilika mwishoni mwa mwaka 2015 na kuanza kutoa huduma katika kata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa za Kampuni ya Simu ya Tigo, mnara huu wa Kwamatuku uliwashwa na upo hewani ukitoa huduma za mawasiliano tangu tarehe 4 Desemba, 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tumetuma wataalamu wetu waende na vifaa vya kupima mawasiliano ili kuhakikisha kwamba taarifa hii ya Tigo iko sahihi.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Serikali iliahidi kutoa kipaumbele kwa barabara zinazounganisha mikoa.
Je, ni lini barabara ya Handeni – Kiberashi – Kiteto –Nchemba na Singida itaanza kujwengwa ili kuunganisha mikoa minne ambayo ni ya kiuchumi hususan kilimo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa Barabara ya Handeni – Kiberashi –Kijungu – Chemba – Kwamtoro hadi Singida yenye urefu wa kilometa 461 umekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii unatekelezwa ili kuunganisha mikoa inakopita na maeneo mengine hasa ukizingatia hivi sasa tuna mradi wa kujenga bomba la mafuta linalotoka Uganda kwa maana ya Hoima hadi Tanzania kwa maana ya Tanga.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapaleka madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni hasa ikizingatiwa kuwa hali ya hospitali hiyo kwa sasa sio nzuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupokea kibali cha ajira mwezi Julai, 2017 Serikali imepanga watumishi katika maeneo mbalimbali ili kupunguza tatizo la watumishi. Katika mgao huo Halmashauri ya Mji wa Handeni imepokea jumla ya watumishi 10 waliopangiwa vituo vya kazi Novemba, 2017. Watumishi waliopangiwa ni Daktari Daraja la II 1, Tabibu Wasaidizi wawili, Tabibu Meno mmoja, Wauguzi wawili, Afisa Muuguzi Msaidizi mmoja na Wateknolojia Wasaidizi Maabara wawili. Watumishi wote wamesharipoti na wanaendelea na kazi kama walivyopangiwa. Mgawanyo huu umefanyika ili kila eneo lipate wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na watumishi hao wapya, Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa afya inao watumishi 13 wanaofanya kazi kwa mikataba ya muda mfupi ambao wanafanya kazi katika Hospitali ya Wilaya Handeni. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuajiri watumishi wa kada za afya 182 ili kukamilisha Ikama ya Idara ya Afya ya Halmashauri ya Mji Handeni. Serikali itaendelea kupanga watumishi kadri bajeti ya mishahara itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ambazo zimeathirika kwa kiwango kikubwa kinachoathiri utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kutokana na zoezi la uhakiki wa vyeti fake zinaelekezwa kuwasilisha maombi ya ajira mbadala moja kwa moja Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuweza kutatua changamoto hiyo.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa (ambulance) kwenye Hospitali ya Wilaya ya Handeni hasa ikizingatiwa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wengi kutoka takribani majimbo manne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda Mbunge wa handeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji Handeni ina gari moja la wagonjwa lenye namba za usajili SM 11322 ambalo linatoa huduma kwa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni. Gari hilo kwa sasa liko katika matengenezo Mjini Tanga baada ya kupata hitilafu. Taratibu za matengenezo zinaendelea kufanyika ili liendelee kutoa huduma kwa wagonjwa. Katika hali ya dharura, Halmashauri inatumia magari ya kawaida kutoa huduma kwa wagonjwa hadi hapo gari la wagonjwa litakapotengemaa.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni kwa kiasi gani Serikali inasimamia suala la asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya vijana na akina mama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha halmashauri zote nchini zinatenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, jumla ya shilingi bilioni 56.8 zilitengwa na halmashauri zote nchini na jumla ya shilingi bilioni 17.5 sawa na asilimia 31 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 61.6 zilitengwa na hadi kufikia Februari, 2018 jumla ya shilingi bilioni 15.6 sawa na asilimia 27 zilikuwa zimetolewa, ambapo jumla ya vikundi 8,672 vya wanawake na vijana vilipatiwa mikopo. Katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, shilingi bilioni 53.8 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uwajibikaji katika kutenga na kupeleka fedha za Mfuko wa Wanawake na Vijana kwa vikundi husika, Serikali itaweka utaratibu katika Sheria ya Fedha (Finance Bill) ya mwaka 2018/2019 utakaohakikisha kwamba halmashauri zote zinatekeleza kikamilifu agizo hilo. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OMAR A. KIGODA) aliuliza:-
Kumekuwa na utekelezaji hafifu wa kusaidia akinamama na vijana kutoka kwenye ile asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri:-
Je, Serikali ina tathmini yoyote ya jinsi gani agizo hilo limetekelezwa kwa kila halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hufanya ufuatiliaji na tathmini kila robo mwaka, nusu mwaka na mwaka kuhusu utekelezaji wa agizo la kila Halmashauri kutenga asilimia 10 kwa ajili ya vikundi vya vijana na wanawake. Taarifa za ufuatiliaji na tathmini ndizo zimesaidia Serikali kubaini changamoto za usimamizi na uendeshaji unaotokana na upungufu wa kisheria, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanufaika wa mikopo kuwa wagumu kurejesha mikopo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 yatakayompa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa nguvu ya kutunga kanuni bora zaidi zitakazolazimisha halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya akinamama na vijana, Serikali inaamini taratibu za utoaji wa mikopo hiyo, usimamizi na urejeshaji wake zitakuwa nzuri zaidi ukilinganisha na hali ilivyo sasa.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali kupitia Halmashauri itakamilisha majengo ya madarasa yaliyotokana na nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Abdala Kigoda, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua juhudi za wananchi na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Elimu ikiwa ni pamoja na kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule kama vile vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo, nyumba za Walimu, mabwalo na maabara.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Handeni ina maboma yapatayo 15 ya vyumba vya madarasa yaliyoanza kwa nguvu za wananchi na kati ya hayo, maboma sita yako katika hatua ya lenta. Hadi Januari, 2019 Halmashauri imepokea jumla ya shilingi 46,600,000/= kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma yaliyoanza kwa nguvu za wananchi ili yaanze kutumika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wadau kupitia Programu ya Lipa kwa matokeo (EP4R) na Programu ya kuimarisha ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-T) itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.

Aidha, Halmashauri zinahimizwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma yaliyopo kabla ya kuanzisha miradi mipya. Naomba kuwasilisha.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-

Je, ni lini hatma ya kipande cha barabara ya Handeni- Mziha ambacho Serikali iliahidi kwamba Mkandarasi akishalipwa ujenzi utaanza, hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo inaunganisha mikoa miwili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Handeni- Mziha yenye urefu wa kilometa 70.1 ni sehemu ya barabara ya Handeni- Mziha-Turiani-Dumila yenye urefu wa kilometa 154.7. Sehemu ya Handeni –Mziha (kilomita 70.1) iko katika Mkoa wa Tanga na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Handeni – Mziha-Turiani umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Handeni- Mziha- Turiani kilometa 104 kwa kiwango cha lami. Aidha, katika mwaka wa Fedha 2019/2020 tumepanga kuitengea barabara hii fedha za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Handeni –Mziha-Turiani ili kuiunganisha Mikoa ya Tanga na Morogoro kwa lengo la kuchochea na kuinua uchumi wa maeneo husika.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-

Hospitali ya Handeni inahudumia karibu Majimbo manne lakini ina upungufu wa vifaa ambao unasababisha wagonjwa wengi kupewa rufaa:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza vifaa ili watu wengi wapate huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayofaa katika Hospitali ya Mji Handeni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018 Serikali imeongeza vifaa tiba muhimu ambavyo ni; ultra sound, urine chemistry analyzer, gene expert machine na cryotherapy machine. Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya vifaa tiba kila mwaka na katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 fedha zitakazotumika kununua vifaa tiba katika Hospitali ya Handeni ni shilingi milioni 96 ikiwa ni ongezeko la shilingi milioni 20 ikilinganishwa na bajeti ya vifaa tiba kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kuondoa msongamano kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni, Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Handeni. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na 2018/2019 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Vituo vya Afya vya Kabuku na Mkata vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 300 ili kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma bora. Serikali inazielekeza halmashauri kuendelea kutenga fedha kwenye bajeti zake kwa ajili ya ununuzi na ukarabati wa vifaa tiba.
MHE. OMARY A. KIGODA aliuliza:-

Barabara ya Handeni – Mziha ni barabara ya mkakati na ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Je, ni lini Serikali itamalizia kipande kilichobaki kutoka Handeni mpaka Mziha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omary Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Handeni – Mziha yenye urefu wa kilomita 70 ni sehemu ya barabara ya Handeni – Mziha – Turiani – Dumila yenye urefu wa kilomita 154.6 ambayo inasimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mikoa ya Tanga na Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Tanga imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo sehemu ya Handeni – Mziha (kilomita 70) kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 1,160 kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. OMARI M. KIGUA (K.n.y. MHE. OMARI A. KIGODA) aliuliza:-

Kuna mgogoro mkubwa wa ardhi unaondelea katika Wilaya ya Handeni ambao kama hatua za haraka hazikuchukuliwa unaweza kusababisha ugomvi mkubwa kati ya wananchi.

Je, nini tamko la Serikali katika kuzuia tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawaagiza viongozi na watendaji wote wa Serikali katika Wilaya ya Handeni kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendelezaji wa ardhi ili kuzuia migogoro ya ardhi. Aidha, wananchi wanasisitizwa kuzingatia sheria za ardhi na kujiepusha kuvamia maeneo yasiyoruhusiwa ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima. Tathmini inaonesha ipo migogoro inayohusisha mipaka baina ya halmashauri moja na nyingine, migogoro baina ya wamiliki wa ardhi na wananchi na baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya ardhi yasiyoruhusiwa. Viongozi wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Handeni wanaelekezwa kutatua migogoro hiyo kwa kushirikisha wananchi na kwa kuzingatia sheria za ardhi. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa viongozi na watendaji watakaobainika kukiuka sheria za ardhi na kusababisha migogoro ya ardhi. Ahsante.