Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omar Abdallah Kigoda (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji wake, pia kulitakia kila la kheri Baraza la Mawaziri katika kutekeleza Ilani ya Chama Tawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, napenda kujikita kwenye ushauri. Kwanza; Serikali ijitahidi kufuatilia kwa karibu fedha ambazo zinakwenda kwenye Halmashauri, bajeti nyingi sana zinapangwa vizuri, lakini inapokuja suala la matumizi huwa zinapotelea Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; kuwe na uwazi wa mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri. Hii itasaidia hata kwa Wabunge kujua ni kiasi gani kinapatikana na kiasi gani kinatumika kurudi kwenye huduma za jamii. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya huduma mbovu kwa jamii kama barabara za mitaa, vyoo na mahitaji mengine madogo madogo ambayo Halmashauri ina uwezo wa kuhudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu; suala la uajiri wa wafanyakazi ningeshauri pia kuwe na upendeleo wa baadhi ya wafanyakazi wawe wazawa ili kuwe na uchungu wa utendaji. Inaonekana watumishi wengi wa Halmashauri ni watu wanaokuja na kuondoka. Hili pia linasababisha kuzorota kwa maendeleo kutokana na ugeni wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne; napenda pia kumshauri Waziri mara kwa mara wawe wanapeleka wataalam kwenye Halmashauri zetu ili kufanya auditing kuangalia matumizi ya hela ambazo ni hela ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuwapongeza Serikali na mpango wa Tanzania wa Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa unapoongelea viwanda unahitaji infrastructure iliyokamilika ambazo ni umeme wa kutosha na barabara ya kupitika kwa urahisi ambazo tunaipongeza Serikali kwa kuliona hilo na mnalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya sasa hivi ni dunia ya processing, ni vizuri Serikali iweke utaratibu mzuri kwa wawekezaji wa ndani na wa nje, wakubwa na wadogo wa kuweza kuanzisha viwanda kwa urahisi ikiwezekana kuwe na one stop centre ya kumaliza taratibu zote za leseni na vibali mbalimbali. Vilevile Mheshimiwa Waziri lazima akae na taasisi zake na wawe na speed ya kuweka Mazingira mazuri kwa yeyote anayetaka kuweka kiwanda especially vya processing (processing Industry), napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri akija kwenye majumuisho ni vizuri awaeleze na kuwaelimisha Wabunge kwamba viwanda vya zamani huwezi kuvifungua, Hata mashine zilizopo sidhani kama zina vipuri vyake maana yake ni teknolojia ya zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha viwanda vya zamani vinapatiwa Wawekezaji ambao wataleta mitambo ya kisasa na kuanza upya. Hatuwezi kujadili yote haya kuhusu Viwanda bila umeme wa uhakika. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri awe na angalau taarifa za juu ni lini gesi yetu itakuwa tayari kuanza kutumika na kutoa umeme mwingi ambao utavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba pia Waziri aje atoe ufafanuzi kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali haifanyi Biashara na Serikali haijengi Viwanda, kinachofanywa na Serikali ni kuweka mazingira mazuri kwa Wawekezaji wa aina yote kuweza kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa kuwa wabunge wengi wanasimama na kuomba Serikali iwajengee Viwanda nadhani wakieleweshwa nia ya Serikali wataweza kuwa katika mstari mmoja wa kauli yetu ya Tanzania ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mungu kutuamsha salama. Na mimi naomba nitoe ushauri wangu kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Lukuvi kwa maamuzi yake mazito ya kubomoa lile ghorofa kubwa pale mjini, ila napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri asiishie hapo, azidi kupambana kwa kuwa majengo ambayo hayana ubora yatakuwa mengi sana, hivyo katika kuokoa maisha ya watu, napenda kuhimiza wataalam wetu wasikae ofisini, waende site na kukagua kila hatua ya ujenzi inayojengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri kuangalia watumishi wake kwa karibu zaidi ili kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua kwa kiwango kikubwa. Malalamiko ya ardhi yanasababishwa na watumishi wa Wizara ya Ardhi kwa uuzaji holela maeneo ya wazi, utoaji wa hati mara mbili mbili ambayo siyo ya kujengea. Tukirekebisha hili, hali hii ya migogoro mijini na vijijini itakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, nadhani wengi hawana elimu ya sheria especially wafugaji. Utakuta mfugaji mmoja ana ng‟ombe 5,000. Kwa idadi hii lazima atagombana na wakulima kwa kuwa eneo lake haliwezi kumtosha. Elimu ya sheria ya kuwa na idadi ya mifugo inatakiwa itolewe sana na isimamiwe kwa makini na kwa ukaribu. Pia wafugaji wapewe elimu ya kupanda nyasi, ikiwezekana Serikali ianze kwa mashamba ya mfano. Hii itapunguza kasi ya wafugaji kuhamahama kwa kutafuta malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri na watumishi wake, nyumba nyingi zinazojengwa mijini hazifuati sheria ya parking, ni vizuri sheria kali ikatipitishwa kwa yeyote asiyefuata kanuni ya ujenzi mijini. Pia napenda kuishauri NHC kuangalia upya mpango wa kodi zao na hili linaweza kurekebishika kwa kupunguza kodi na linawezakana kama watasimamia vizuri ukusanyaji wa kodi za sasa hasa katika taasisi kubwa ambazo zinaongoza kwa kutolipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jedwali Na. 2 page ya 83, marejesho ya asilimia 30 ya makusanyo ya Halmashauri kwenye mkoa wa Tanga kuna Handeni tu; na sasa kuna majimbo mawili; Handeni Mjini na Handeni Vijijini. Naomba unisaidie ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kutufikisha salama katika Bunge hili. Pia niwape pole wafiwa na majeruhi wa ajali, pia naipongeza Serikali kwa maamuzi yake ya kuhamia Dodoma. Pamoja na juhudi zake za Kasi katika kuinua uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumedhamiria kuwa na Tanzania ya viwanda, ni vyema sasa Serikali ikajikita kwa kina katika kuhakikisha kuwa umeme wa kutosha unapatikana ili tuweze kuendesha viwanda vyetu especially kwenye umeme wa gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kujitahidi kutatua changamoto ambazo zinagusa kwa kiasi kikubwa wananchi, mfano maji, afya na elimu, hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kunyanyua jamii yetu na kuifanya jamii yetu ishiriki vyema kwenye maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la maji pamoja na jitihada kubwa za Serikali kuhakikisha tunapata maji safi na salama, bado kuna changamoto kwa upande wa watendaji hususan katika maeneo ya vijijini. Hii inatokana na utendaji wa mazoea kwa wataalam wa Idara husika.
Mfano unakuta Mhandisi wa Maji amekaa eneo moja kwa zaidi ya miaka kumi na pamoja na kukaa miaka yote hiyo tatizo la maji bado lipo palepale pamoja na kulipwa mshahara na mahitaji mengine. Nashauri kuwe na uhamisho kwa watendaji ambao wamekaa sehemu moja kwa muda mrefu na pia ni vizuri wakaangaliwa performance yao kila mara ili kuona ni jinsi gani wanafanya kazi ya kutatua kero hii ambayo inagusa
kila jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Elimu; ni vizuri Serikali ikatoa mwelekeo mzuri kwa Halmashauri ni jinsi gani wanasaidiwa na wananchi katika ujenzi wa madarasa mfano kuna mkanganyiko kati ya Halmashauri na wananchi. Tunaambiwa kama wananchi tujenge boma na Halmashauri itaezeka juu. kuna maboma mengi yameshajengwa na wananchi lakini bado Halmashauri zinasuasua katika mpango wao wa kumalizia juu na ukizingatia idadi ya wanafunzi inaongezeka kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya, pamoja na jitihada, kubwa kuhakikisha huduma ya afya inaimarika, bado kuna changamoto kwenye ununuaji wa dawa na upungufu wa Madaktari. Nashauri Serikali ihakikishe MSD wanapata dawa ya kutosha ili kuepuka kuonekana
kulemewa na order kwenye hospitali zetu au kuweka utaratibu wa kuziwezesha hospitali kununua dawa maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa Madaktari na Wauguzi ni kubwa sana na lipo nchi mzima. Ningependa kuiomba Serikali ifanye haraka kulishughulikia suala hili, mfano katika jimbo langu, kuna upungufu wa karibia asilimia ishirini ya Madaktari na Wauguzi na ukizingatia hospitali yetu inahudumia majimbo manne. Upungufu huu, unasababisha vifo vya mara kwa mara kutokana na kuchelewa kuhudumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kuipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuyaondoa maduka yote ya watu binafsi (ya dawa) ila iharakishe kuhakikisha maduka ya Serikali yanaanzishwa haraka.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa January Makamba kwa hotuba yake nzuri ya Mazingira na Muungano,
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwa ufupi sana katika suala zima la mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira bado wananchi wanalichukulia kama ni option na sio lazima. Hili linatokana na kutosimamiwa vizuri sheria zake. Naiomba Serikali izingatie kusimamia na kuelimisha watu kuhusu mazingira. Bado elimu inahitajika. Mfano; kuna Sheria ya Kutotiririsha maji machafu kutoka viwandani, lakini mpaka sasa kuna viwanda vingi tu ambavyo vinatiririsha hayo maji bila hata kuyachuja. Hii inaonesha ni jinsi gani sheria bado haisimamiwi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sheria ya kutokukata miti lakini bado maeneo makubwa nishati inayotumika kwenye kupikia ni mkaa, hakujasisitizwa wale wote wanaozalisha mkaa wawe na vitalu vya miti ili tukamilishe ile panda miti, kata mti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, napenda kuisisitiza Serikali kuwa, kuna wale watu wanaozalisha miti mbalimbali, iwawezeshe wanapohitaji msaada kwani wao ndio watunzaji wazuri wa species za miti mbalimbali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa jitihada wanazofanya katika kuimarisha miundombinu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mikakati ya nchi ni kuhakikisha barabara za kufungua mikoa zinafanyiwa kazi kwa kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuinua uchumi wetu katika Sekta ya Usafirishaji.

Mheshimiwa barabara ya Magole - Mziha - Handeni ni moja ya barabara zilizopo kwenye mpango huo. Licha ya kuwa kwenye mpango mkakati, pia ni barabara iliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara kwa kutengea fedha kipande kilichobaki ambacho ni kidogo sana. Mwaka 2016 katika bajeti tuliambiwa Mkandarasi anadai; naomba Mheshimiwa Waziri akija kujumuisha, atufafanulie ile shilingi milioni 100 iliyotengewa ile barabara ni ya matumizi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kupata ufafanuzi, shilingi milioni 500 iliyotengewa barabara ya Handeni – Kiberashi – Kibaya – Singida ni kwa matumizi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kuunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuwapongeza Waziri, Naibu pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa utendaji mzuri wa kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu ambalo nalirudia mara kwa mara katika Wizara hii ni upungufu wa Madaktari na Wauguzi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Handeni. Hili ni tatizo kubwa sana na mara kwa mara hutokea vifo wagonjwa wakiwa wanasubiri huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishaliongelea kwenye kipindi cha maswali na majibu, Hospitali ya Wilaya ya Handeni inahudumia takribani majimbo manne na ukiangalia hakuna bajeti yoyote ya kujenga hospitali nyingine hivi karibuni. Kutokana na hilo, hospitali inaelemewa na uhitaji wa vifaa tiba. Namwomba Mheshimiwa Waziri na kwa vile ameshatutembelea na anajua hali yetu, basi atuangalie kwa jicho la tatu kwenye vifaa tiba na madaktari. Namwomba Mheshimiwa Waziri katika majumuisho aizungumzie na Hospitali yetu ya Handeni ili hata wananchi wetu wapate imani kwamba matatizo yetu yatafanyiwa kazi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kuleta maendeleo katika nchi yetu, bila ya kusahau kumpa pongezi kubwa sana Rais wetu, Mheshimiwa John P. Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango endelevu inahitaji kwanza kabisa kutokuwa na watu wajinga, maradhi na maskini. Lazima mipango hii iendane na kuwanyanyua watu na kuwasaidia katika utendaji wao wa kulinyanyua Taifa. Serikali ihakikishe huduma ya ukusanyaji kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki inakuwepo nchi nzima. Hii itasaidia ukusanyaji wa haraka na kutopoteza muda wa kutoa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni lazima Serikali ihakikishe huduma za jamii kama maji, umeme na mengineyo zinapatikana kwa wingi ili muda mwingi watu tuutumie kwenye kujenga nchi yetu. Maendeleo ya nchi lazima tuwe na manpower ya kutosha, kwa hiyo, tukihakikisha huduma za jamii zipo itasaidia kuwa na manpower ya kutosha kujenga uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima ihakikishe inazingatia suala la afya ya kila mwananchi inakaa sawa na inatibika kwa urahisi, ili kutokuwa na Taifa la wenye maradhi; hii itadhoofisha ukuaji wa uchumi wetu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni suala la amani. Lazima nchi iwe na amani, ili kila mtu awe huru katika kutekeleza kazi zake za kulijenga Taifa. Lazima Serikali isisitize watu kufanya kazi ili tuweze kukwamuka kutoka tulipo, twende mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, infrastructures zetu lazima tuhakikishe zinatumika na lazima tuweke mazingira mazuri kwa watumiaji. Mfano, gesi lazima itumike kwenye viwanda vyetu ili kuwa na uzalishaji wa kutosha. Lazima barabara zetu ziwe za kupitika muda wote, hii itasaidia kwa wakulima na wafugaji hata waoa huduma kufika kwenye point haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu ni muhimu sana. Taifa la wajinga haliwezi kuwa na maendeleo au kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jiografia ya nchi yetu kuna infrastructures ambazo ni za mkakati especially kiuchumi, kwa mfano, barabara ya Handeni – Mziha – Dumila na nyingine nyingi. Hizi infrastructures lazima tuzitengeneze ili ziweze kutumika katika mzunguko wa biashara kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Taifa lililoendelea bila kuwahusisha wafanyabiashara wakubwa, pia na kuwahusisha katika uwekezaji. Hivyo, ni lazima Serikali iwe karibu na wafanyabiashara na kusikia matatizo yao na kujadiliana ili kuweka mambo sawa.

Mhershimiwa Mwenyekiti, miaka 30 iliyopita South Korea tulikuwanao almost sawa, lakini kwa sasa wamepiga hatua sana kimaendeleo. Walichofanya ni kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na Serikali ilibaki kuchukua kodi kutokana na uwekezaji huo, pia kuhakikisha hiyo kodi inatumika ipasavyo kwenye huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda kumshauri Waziri, hii mipango tunayopanga ni mizuri tu endapo utekelezaji wake utapewa kipaumbele na msisitizo wa kila mtu katika sekta yake lazima afanye kazi. Hakuna uchumi unaopanda kwenye Taifa la wavivu, lazima msisitizo wa uwajibikaji usemwe mara kwa mara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Serikali yake. Pili, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu wake kwa mapambano makubwa ya kuhakikisha ufumbuzi wa maji unapatikana. Vilevile nampongeza Katibu Mkuu na Naibu wake kwa kuongoza Wizara vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kidogo kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Lazima sasa tubadilike na kuhakikisha watendaji wote wa Wizara na Idara za Maji hawafanyi kazi kwa mazoea. Mfano, kwenye Jimbo langu kuna watu wana zaidi ya miaka 30 wako eneo moja; kwa vyovyote mtu kama huyu hawezi kuwa na performance nzuri. Lazima sasa hivi watu wote walioajiriwa wapimwe utendaji wao (performance) ikiwezekana kwa kila mwaka kwamba wamefanya engineer katika Wilaya, unakaa miaka kumi hakuna chochote ulichofanya, lazima wapewe performance time.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelewa kuna tatizo la upatikanaji wa fedha, ila hata hiyo hela ndogo inayopatikana kama tunapata watendaji wabunifu, inaweza kupunguza shida ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaambia Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwamba haya malalamiko wanayopata leo ni kwa sababu ya utendaji wa mazoea uliopita. Mfano, ni juzi Mheshimiwa Rais alivyompigia Katibu Mkuu wa Wizara mpaka leo tumeambiwa wataalam wameshakwenda na kazi imeanza. Hii inaonekana kabisa watendaji wa kwenye eneo husika hawakuwa makini (ufanyaji kazi kwa mazoea).

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawapongeza sana kwa kupata hela ya fidia. Hakika kuna miradi mingi itanyanyuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuipongeza Serikali inayoongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri wake Mheshimiwa Kangi Lugola kwa ufanisi wake.

Mheshimiwa Spika, hali za Magereza yetu nchini ni mbaya, lazima kuwe na mkakati wa kufanya ili kunusuru hali hii. Ndani ya Magereza kuna wafungwa wenye vipaji vyao ambao wanaweza kutumika kama sehemu ya uzalishaji na sehemu ya kipato. Mfano, kuna wafungwa wenye taaluma ya carpenter (utengenezaji wa furniture), wengine ni wajenzi. Hao hao wangetumika kwenye matengenezo ya furniture za Magerezani au hata ujenzi wa ndani lakini pia furniture zingeuzwa kwenye Taasisi za Serikali ili waweze kupata mapato. Hii ingesaidia sana kuongeza hela ya bajeti mnayoomba, ingesaidia kwenye matatizo mengine kama kununua vitendea kazi kwa ajili ya wale wenye vipaji vya kuzalisha.

Mheshimiwa Spika, hii ingetumika kwa taasisi zote kwa kuwa hata Polisi wapo wenye vipaji vya ujenzi, wawezeshwe kwa kupatiwa vifaa. Hizi nyumba tunazolalamika wanaweza kuzijenga wenyewe kwa kiwango kizuri. Tutumie sana vipaji vyao kuzalisha na kuingiza vipato. Ni aibu mtu anasimama hapa anaombea Askari mafuta. Tubadilike, hizi hela zinazopatikana zipelekwe kwenye maeneo ya uzalishaji na kujiwekea mazingira mazuri.

Mheshimiwa Spika, tuzipe hizi taasisi uhuru wa kuonesha vipaji vyao katika maendeleo na kujiweka wenyewe katika mazingira mazuri. Tuachane na mawazo ya kunufaisha watu wengine kwa kutumia neno tenda. Taasisi hizi zina uwezo wa kufanya vitu wenyewe na kuleta tija, tuwape nafasi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali na Wizara kwa jitihada kubwa za kuinua elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuinua elimu basi ni lazima Serikali iwe na mkakati wa kuongeza idadi ya walimu hasa maeneo ya vijijini, hii inaendana na kuboresha miundombinu ya maeneo ya vijijini. Walimu wengi wanaondoka maeneo ya vijijini kwa sababu tu ya miundombinu mibovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wengi wanadai haki zao, hili pia ni tatizo. Serikali lazima ijitahidi kuhakikisha stahiki za walimu zinalipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pale Handeni kuna Chuo cha FDC. Chuo hiki kina msaada mkubwa sana kwa Mkoa wa Tanga. Naiomba Serikali ikiangalie kwa jicho la karibu kwa kuwa hali yake ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda kuwapongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Handeni Mji ni ya zamani na kwa sasa inaelemewa sana na idadi ya wagonjwa. Inahudumia majimbo almost manne na mpaka sasa hakuna utaratibu wa kupata hospitali katika majimbo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, tuna zahanati eneo la Kwamagome ambalo Mheshimiwa Waziri Ummy alifika kwenye ufunguzi, tumefikia pazuri na ikiwezekana tunaweza kupafanya pale na kuwa kituo cha afya. Naomba Waziri aliangalie eneo hili ili kuondoa msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kule kwetu hatujapata mgao wowote kwenye kuongeza au kujenga kituo cha afya. Tunaomba Wizara itufikirie na sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niipongeze Wizara na Mawaziri wake kwa kazi bora.

Mheshimiwa Spika, kipande kilichobaki cha Mziha - Handeni kwenye majibu ya Waziri kilitengewa shilingi bilioni 2, katika kitabu cha hotuba ya Waziri ukurasa wa 29-30 ameeleza Serikali bado inatafuta hela. Naomba kwenye majumuisho nipate ufafanuzi wa suala hili hasa akizingatia wananchi wa Handeni na Tanga kwa ujumla wamepata faraja baada ya kusikia imeshatengwa shilingi bilioni 2 kutokana na majibu ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, barabara nyingine yenye umuhimu mkubwa ni ile ya Handeni – Kiberashi. Hii barabara ndiyo litakapopita bomba la mafuta. Naomba ufafanuzi wa Serikali kuhusu barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami hata tukianza kwa vipande vipande itasaidia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. OMAR A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja, pili niwapongeze Mawazili wote wawili na watendaji wao kwa bajeti zuri waliyowasilisha. Mimi nataka kujikita kwenye ushauri kuhusu suala la mwananchi kutoa mizigo bandarini mwenyewe. Niimpongeze Serikali kwa kuleta utaratibu huu, hii itasaidia sana kwa mwananchi kupunguza gharama kubwa zitokanazo na makampuni ya clearing.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Serikali lazima itafute utaratibu au mpango ambao utamsaidia huyu mwananchi kutoa mizigo yake. Ikiwezekana kuwe na one stop center kwa huyu mwananchi aweze kufanya utaratibu wote eneo moja na kumaliza kila kitu na kupata mzigo wake. Niliona utaratibu kama huu Oman.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa jitihada kubwa za kuinua elimu nchini. Pia niwapongeze sana kwa kuleta Muswada huu ili kuweza kuupitia na kutoa maoni yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi hii kwa kweli itakuwa na msaada mkubwa sana kwa upande wa Walimu ambao watakuwa na weledi mzuri kwenye shule ngazi zote, kuanzia awali mpaka vyuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningemshauri Waziri katika haya majukumu ya bodi kwa upande mkubwa yanaonesha kumweka Mwalimu katika uadilifu na kuepuka kupatikana kwa Walimu wasiofaa, ambao ni utaratibu mzuri sana. Pia ukiangalia kwamba itasimamia maadili ya ualimu, hii itasaidia kudhibiti Walimu ambao wana tabia zisizofaa shuleni, mfano, kuna wimbi kubwa la wanafunzi kupigwa mpaka kufa; kwa bodi hii hili litatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine Waziri angeweka majukumu kwenye bodi ya kumsaidia Mwalimu endapo atakuwa na uhitaji fulani, kama haki zake stahiki, pia kumwekea mazingira mazuri ili awe na ari na moyo wa kufundisha; Walimu wengi wana mazingira magumu, especially vijijini mpaka inasababisha wengi wao kuacha kazi.