Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Godbless Jonathan Lema (1 total)

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu yake. Kwa sababu TRA ina sheria zake na kwa sababu amekiri kwamba hii task force inakuwa-engaged kwa wale wafanyabiashara ambao ni wadeni sugu wa TRA. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa vile kuna sheria zinazoendesha shirika hili la kodi, ni kwa nini sheria hizo zisitekelezwe kwa kina na kwa uthabiti kuliko kutumia task force ya Jeshi la Polisi, TAKUKURU pamoja na Usalama wa Taifa kitu ambacho kinatia hofu sana wafanyabiashara hao.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba TAKUKURU, Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi hawafahamu mambo yanayohusu kodi. Sasa hata kama ni task force kwa nini isiwe inahusisha TRA wenyewe pamoja na sheria zao za kodi ambazo zinajulikana nini kitafanyika iwapo mfanyabiashara ataendelea kukaidi kulipa kodi katika Taifa hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Godbless Lema kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema task force ni kwa ajili ya wale ambao kwa makusudi hawataki kutekeleza sheria ya ulipaji wa kodi kwa kuwatembelea kwenye maeneo yao, siyo wote ni wachache wale sugu. Nimeeleza kwamba task force hii imejengwa na TRA wenyewe Polisi na TAKUKURU na hapa kila mmoja ana wajibu wake. Kama mlipa kodi anaamua kulipa mpaka afuatwe na kwa sababu wanakusanya fedha Polisi yeye yuko pale kwa ajili ya ulinzi wa fedha ambayo inakusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TAKUKURU yuko pale kuona kwamba hakuna nafasi ya rushwa kutokea. Kwa sababu pale inakwenda kumuuliza na wakati mwingine mlipa kodi sugu anaweza kudhani kwamba anadaiwa fedha nyingi akatamani kufanya makubaliano na Afisa wa TRA kwa lengo la kutoa rushwa. Kwa hiyo, mtu wa TAKUKURU yuko pale kuhakikisha kwamba hakuna jambo lolote linalohusiana na rushwa linalofanywa kati ya mdaiwa sugu ambaye hakutaka kulipa yeye mwenyewe labda angeweza kushawishi alipe kidogo ili jambo lake liweze kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kila mmoja ana wajibu wake lakini mwenye dhamana kubwa pale ni TRA kukumbushia sheria, kuonyesha kipindi ambacho amekaa bila kulipa na kwamba sasa anatakiwa kulipa kodi na kwa kuwa ni mdaiwa sugu basi pale inaonekana kwamba hataki kuchukua hatua hiyo wanatakiwa kumpeleka Polisi hata kama itakuwa alikuwa hana notisi. Kwa hiyo, timu ile inalenga zaidi kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya uovu vinavyoendelea kwenye uendeshaji wa zoezi lile lakini halilengi kumtisha mfanyabiashara. Polisi hawajibiki kumtisha wala TAKUKURU hausiki na mfanyabishara isipokuwa ni TRA mwenyewe kama ambavyo nimeeleza.
Mheshimiwa Spika, kwa hili nataka niwahakikishie wafanyabiashara, pamoja na haya yote yanayoendelea kwamba task force inapita kwenye maeneo haya haina nia mbaya kabisa na wafanyabiashara wetu na wawe na amani. Cha msingi zaidi kila mmoja sasa aone umuhimu wa kulipa kodi bila shuruti ili shughuli zetu ziweze kwenda kama ambavyo tumekubaliana.