Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shabani Omari Shekilindi (69 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Waziri pamoja na timu yake yote kwa kuwasilisha vizuri hotuba yake nzuri iliyojaa matumaini ya kuinua Wizara hii katika Habari, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali yangu tukufu kuwekeza katika suala zima la michezo wala isichukulie mzaha kwani sekta hii ikisimamiwa vizuri itakuwa inaingiza mapato mengi katika Taifa letu pamoja na kutangaza utalii katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Lushoto, Radio ya Taifa haipatikani kabisa zaidi ya wananchi kusikiliza Radio za Kenya. Hivyo, naishauri Serikali yangu tukufu ijenge minara ya redio katika Wilaya ya Lushoto kwani wananchi wanakosa taarifa muhimu pamoja na mawasiliano muhimu ya kuhusu nchi yao pamoja na nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Lushoto kuna vijana wengi wana vipaji vya sanaa na michezo lakini vijana hawa wameachwa huko vijijini na kupoteza vipaji vyao. Kwa hiyo, naiomba Serikali hasa Wizara ya Michezo itoe timu kwa ajili ya kwenda vijijini ili kwenda kuibua na kuwanusuru vijana ambao wana vipaji na kuwajengea uwezo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Lushoto ni Wilaya kubwa ambayo ina vijana zaidi ya 250,000, lakini ndani ya Wilaya hakuna uwanja hata mmoja wa michezo. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijenge uwanja wa michezo Lushoto Mjini. Pamoja na hayo, kujengwe Chuo cha sanaa katika Jimbo la Lushoto ili kuendeleza vipaji hivi vya vijana wetu hawa wa Kitanzania. Niishauri Serikali ifundishe michezo mashuleni pamoja na kupewa vifaa vya michezo katika shule zote.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali yangu tukufu kwa wale wote ambao wapo vijijini, wanamichezo pamoja na wasanii Serikali iwasaidie ili waweze kukuza vipaji vyao sambamba na kuwa na ajira kupitia kazi yao hiyo kwani wasanii wa vijijini wanapata tabu sana mwisho wa siku wanakata tamaa na kuiona Serikali yao haiwajali.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, toka mwaka 2014/2015, 2015/2016 pesa za maendeleo hazijafika katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu ipeleke pesa hizi kwa wakati. Pesa hizi kwa kutofika imedumaza kabisa Sekta ya Kilimo pamoja na wakulima kutopata huduma hii muhimu ukizingatia 70% ya wananchi wa Tanzania ni wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa wataalam; katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuna wataalam 35 tu ambao wanahudumia vijiji 125. Hii inapelekea kila mtaalam kuhudumia wakulima 3,000 kitu ambacho ni vigumu kumfikia kila mkulima. Kwa hiyo, kuna upungufu wa wataalam 55 – 60. Niombe Serikali ipeleke wataalam hawa ili kuwanusuru wakulima wetu hawa. Kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na ina mpango mzuri wa kumuinua mkulima wa Tanzania, ni imani yangu wataalam hao watafika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ruzuku na pembejeo katika nchi hii bado ni tatizo kwani hazifiki kwa wakati pia mara kwa mara hazimlengi mkulima aliyekusudiwa kwani kuna udanganyifu mkubwa unafanyika. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto pembejeo hizi zinatolewa kwenye mazao ya nafaka tu yaani mahindi na mpunga. Niombe wakulima wa mbogamboga na matunda nao wafikiriwe. Kama inavyojulikana Lushoto ni ya wakulima wa mbogamboga na matunda, Serikali isiposaidia wakulima hawa itakuwa haijasaidia wakulima wa Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, miche bora ya kahawa. Kahawa iliyopo Wilaya ya Lushoto ni ya zamani mpaka imepelekea zao hilo kupotea. Hivyo, niombe Serikali ipeleke miche bora na ya kisasa ili kufufua zao hili ambalo ndiyo tegemeo kubwa la wana Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yako iwatafutie masoko wakulima wa Lushoto hapa nchini na nje ya nchi. Pia Serikali itoe ushuru kwenye mazao haya ya mbogamboga na matunda kwani unawakatisha tamaa wakulima wetu hao. Pamoja na hayo, nimshukuru Waziri wa Kilimo katika hotuba yake iliyoelezea kutoa ushuru kwenye vizuizi na hatimaye ushuru ukachukuliwe sokoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la nyanya limepungua sana katika Halmashauri ya Lushoto kwa kuwa kumezuka ugonjwa unaitwa Kantangaze. Ugonjwa huu umeathiri zao zima la nyanya na ugonjwa huu dawa yake inauzwa ghali mno. Kipimo cha dawa hii miligramu nne inauzwa sh. 4,500 ambayo ni bomba la nyanya lenye kuingia lita 15 wakati huo shamba la nyanya linaingia bomba 20 hadi 25. Kwa hiyo, mkulima wa kawaida hawezi kumudu gharama hizo. Niombe Serikali iwaangalie wakulima hawa kwa jicho la huruma ili mkulima yule wa hali ya chini aweze kumudu kununua dawa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaposema kilimo ni uti wa mgongo kinaenda sambamba na miundombinu ya barabara hasa za vijijini. Naomba Serikali yangu iangalie hilo nalo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia na mimi niweze kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais wangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya, kwani naamini kabisa mwenye macho haambiwi tazama. Pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kazi kubwa anayoifanya sambamba na kumpongeza Waziri Jenista pamoja na Timu yake Naibu Waziri Mheshimiwa Ikupa na Mheshimiwa Mavunde, kwani Watanzania wanaona kazi mnayoifanya hongereni sana. Sisi tunaamini hatuna cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye atajua cha kuwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika kuchangia sasa. Wenzangu wameshachangia mambo ya bomba kutoka Hoima Uganda kuja Tanga. Niendelee kupongeza juhudi hizo za Mheshimiwa Rais kwani Mheshimiwa Rais anatupenda sana, naamini kabisa Watanzania sasa itakuwa ni fursa ya kupata ajira katika bomba lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze kupanuliwa kwa Bandari au kuongezwa kina cha bandari pale Tanga, nimpongeze Rais wangu kwa kutupa pesa na kazi ile inaendelea kupanua bandari ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo niiombe Serikali yangu sasa Tukufu kwamba vitu vyote hivi viende sambamba na standard gauge hiyo ambayo itaanzia Tanga kwenda Arusha mpaka Musoma. Naomba Serikali yangu tukufu iende sambamba na reli hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tuna uwanja wa ndege wa Tanga. Kwa kuwa tayari tuna Bombardier, kwa hiyo niiombe Serikali sasa Bombardier ile iweze kufika Tanga. Ianze Dar es Salaam iende Pemba ije Tanga hadi Mombasa, naamini hiyo sasa ni fursa yetu pamoja na upanuzi wa uwanja ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupongeza hayo niende moja kwa moja sasa kwenye suala la afya. Nimshukuru Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kunitengea milioni mia saba kwa ajili ya Kituo cha Afya Mlola, milioni mia nne kwa ajili ya majengo na majengo yale tayari mpaka sasa hivi yako kwenye hatua nzuri, mengine yanapauliwa, mengine yanafanyiwa usafi na mengine yako kwenye mtambaa wa panya. Mheshimiwa Rais, ahsante sana Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hayo kuna juhudi za wananchi zinaendelea kufanyika kule, kuna vituo vya afya zaidi ya viwili vinajengwa pale; Kituo cha Afya Gare na Kituo cha Afya Ngwelo. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwa kuwa vituo vile vinajengwa kwa nguvu za wananchi…

T A A R I F A . . .

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo siikubali hata yeye anajua kwamba Rais ndiye Mkuu wa Nchi, ndiye mwenye maamuzi yote. Kwa hiyo wafu ngoja wakazike wafu wao, sisi tuendelee kutangaza injili. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vituo vya afya viwili ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi. Sasa niiombe Serikali iweze kupeleka pesa kwa ajili ya kumaliza vituo vya afya vile, ambavyo ni Kituo cha Afya Gare na Kituo cha Afya Ngwelo. Sambamba na hayo kuna Zahanati zaidi ya 19, zahanati zile ziko kwenye nanii tofauti tofauti. Kuna ambazo zinahitaji watumishi na kuna ambazo zinahitaji kumaliziwa, kwa hiyo niiombe Serikali yangu tukufu kwamba ipeleke mafungu sasa…

T A A R I F A . . .

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, saa nyingine hawa watu wakitoa taarifa usiwaruhusu kwa sababu Bunge ndilo linalotenga Bajeti Serikali inatekeleza. Kwa hiyo, mtu wa kwanza kabisa kutekeleza na kutoa maelekezo ni Rais.

T A A R I F A . . .

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Ulega naipokea kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema awali kwamba naomba sasa Serikali katika bajeti hii itenge pesa kwa ajili ya kwenda kumalizia vituo vile vya afya ambavyo ni Kituo cha Gare na Ngwelo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, niende kwenye suala la umeme. Kwanza nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Dokta Kalemani na Naibu Waziri, Mheshimiwa Subira Mgalu kwani wanafanya kazi kubwa sana. Watu wa REA, sisi tumepangiwa mkandarasi anaitwa DEM Contractors, huyu bwana alikuja mara moja tu mpaka leo hajaonekana na vijiji na vitongoji vyote ambavyo vimepangiwa bado hajavifanyia kazi, amekuja kupima kama vitongoji viwili, vitatu ameondoka moja kwa moja. Niiombe sasa Serikali Tukufu kwamba mkandarasi yule atafutwe popote alipo aende akatekeleze ile miadi ambayo wameahidiana na Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu.Kuna maboma mengi sana ya maabara yamejengwa lakini maboma yale mpaka sasa hivi yamekuwa ni magofu. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa ichukue hatua madhubuti kuhakikisha kwamba inakwenda kumaliza maboma yale kwani maboma yale yalikuwa yanajengwa na nguvu za wananchi, kwa hiyo tunapoyaacha vile yalivyo wananchi sasa hivi hata uwezo hawana. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu sasa imalizie maboma yale ili watoto wetu waweze kusoma elimu kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Wilaya ya Lushoto tangu iumbwe ina wananchi wengi sana lakini haijawahi kupata Chuo cha VETA. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu, hususan Wizara; Waziri wa Elimu naomba atakaposimama pale aniambie lini atanitengea pesa za kujenga Chuo cha VETA Lushoto. Kuna sekondari zaidi ya 105, kwa hiyo nimwombe Waziri wangu atakapo-wind up hapo basi aniambie kwamba ni lini atatenga mafungu hayo kwa ajili ya kujenga Chuo cha VETA Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, niende kwenye barabara; wenzangu wameongea mambo ya TARURA, ni kweli lakini mimi nilichoona TARURA ni watu wazuri sana ila naamini bado hawajatengewa mafungu kwenda kule. Mfano mimi ninachoongea, barabara zangu pale Lushoto Mjini bado ni tatizo, kuna mashimo makubwa sana, hata nikipita pale wananchi wananiuliza hivi Mheshimiwa Mbunge upo, hivi hii hali unaiona? Kwa hiyo niiombe sasa Serikali ipeleke mafungu kwenye Taasisi ya TARURA iweze kujenga barabara zile sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna barabara ambayo kila siku naiongelea hapa, Barabara kutoka Mlalo – Ngwelo – Mlola – Makanya – Mlingano hadi Mashewa ambayo ni kilometa 57.7, barabara hii imeshasemwa mara nyingi, kabla ya mimi kuingia Bungeni waliopita wameshaizungumzia barabara hii tangu 1995, lakini barabara hiyo mpaka sasa hivi bado haijapandishwa hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Waziri sasa, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, atakapo-wind up hapo anipe majibu barabara ile itapandishwa hadhi lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna barabara ya mchepuko ambayo ni kilometa 16, inaanzia Dochi – Nguli hadi Mombo. Nimwombe sasa Waziri barabara ile iweze kutengenezwa kwani barabara ile ni barabara mbadala ambayo barabara hii kubwa ya kutoka Soni – Mombo ikiziba basi barabara ile inatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye walemavu, ukurasa wa 24; nimeona walemavu wametengewa vitu vingi kidogo, lakini upande wa vijijini walemavu hawa wamesahaulika. Niiombe Serikali yangu sasa itakapotenga pesa hizi basi ipeleke vijijini kwani vijijini kuna walemavu wengi sana ambao wamesahaulika, kwa hiyo niiombe Serikali yangu tukufu iweze kutenga pesa ili iweze kuzipeleka vijijini. Ukizingatia mazingira ya vijijini miundombinu si rafiki, mnaifahamu wenyewe hata Mwenyekiti naamini unaifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji; kama unavyojua maji ni uhai na katika mwili wa binadamu maji ni asilimia 75. Kwanza niipongeze na niishukuru Serikali yangu kwa kunitengea milioni mia saba sabini kwa ajili ya Mamlaka ya Maji Mjini. Pia niendelee kuipongeza kunitengea milioni mia tano kwa ajili ya mradi wa Ngulu – Kwemashai na pia niipongeze Serikali kwa kunipa milioni mia nne hamsini kwa ajili ya maji Mlola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna mradi ambao una miaka mingi sana, mradi wa kutoka Mtumbi kuja Kwekanga, kuja Malibwi kuja Kilole kwenda mpaka Mbwei, mradi huu ni wa miaka mingi sana, kwa hiyo niiombe Serikali yangu sasa iweze kutenga pesa awamu hii ili tuweze kutekeleza mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, kuna mradi ambao unatoka Lushoto kwenda Mkuzi kupitia mpaka Kwemakande, mradi ule walishafanya feasibility study (upembuzi yakinifu), lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea ambapo mradi ule unagharimu shilingi bilioni moja na milioni mia sita, ambapo ukitekelezwa utatoa kabisa changamoto au utatatua matatizo ya maji katika maeneo hayo niliyoyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mimi niko kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii; tulienda Mkoa wa Geita tukaenda mpaka Mkoa wa Kagera, nilikuwa na rafiki zangu Mheshimiwa Kalanga, Mheshimiwa Nassari na wengineo, tuliona pale Chato Uwanja wa Ndege Chato. Kwa hiyo niendelee kumpongeza Rais wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine walikuwa wanasema uwanja ule hauna maana, uwanja ule una mapori matatu wanaita BBK (Biharamulo, Burigi na Kimisi), kwa hiyo uwanja ule naamini kabisa utatoa fursa kubwa sana. Ningetegemea wenzangu hawa wamuunge mkono Rais kwamba juhudi alizozifanya ni juhudi ambazo zinatakiwa tumwombee dua, lakini… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niiombe Serikali iwasimamishe kazi wakandarasi wanaojenga Mradi wa Maji wa Nguluma Mlola kwa sababu wakandarasi hawa walitoa ahadi mbele ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa Mradi wa Maji wa Ngulu ungekamilika tarehe 30 Aprili, 2017 lakini mpaka sasa hakuna hata dalili za kumaliza mradi ule pamoja na mradi wa Mlola. Miradi yote miwili imefikia asilimia 70 ya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali yangu iwasimamishe au wapewe deadline ya kumaliza miradi yote hii miwili maana imekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha afya na nguvu kuweza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza basi niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Lushoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kushukuru hotuba hii ambayo imejaa maudhui mema, niendelee kumshukuru Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Andiko linasema nimrudishie nini Bwana kwa wema wake alionitendea, kwani hotuba ya Waziri Mkuu imekuna wengi na inastahili kupongezwa hata Mwenyezi Mungu naamini ameibariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waislamu tunasema; maa yashkuru-nnasa laa yashkuru-llah (usiposhukuru watu basi hata Mwenyezi Mungu hutamshukuru). Basi nishukuru hotuba hii na pia niwashukuru Watanzania wote kwa kumchagua Rais wetu John Pombe Magufuli Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nijikite katika kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Hakuna asiyefahamu kwamba Wilaya ya Lushoto ni Wilaya ya kilimo cha matunda na mboga mboga. Wilaya ile na wakulima wanalima kwa zana ambazo ni dhaifu mno, wanalima kwa mbolea ya samadi yaani kinyesi ng’ombe. Wakulima wanapovuna mazao yao huwa wanapata taabu sana, wanunuzi wakati wa mvua barabara hazipitiki na inapelekea mazao yale yanauzwa bei rahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la ukusanyaji wa mazao wananchi wa Lushoto wanapata taabu sana. Mimi kama Mbunge wao ambaye wamenituma niwawakilishe kwao, kwani wakati wa kura za maoni walisema tunakutuma wewe mnyonge mwenzetu, mkulima mwenzetu ukatuwakilishe, basi na mimi ninawaahidi kutowaangusha na ndiyo maana mkulima mimi, mnyonge mimi nimesamama mbele ya Bunge hili Tukufu kwa ajili ya wananchi wa Lushoto hususani wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hotuba ya Waziri Mkuu iangalie wakulima wangu wa Lushoto hususan katika suala zima la pembejeo, suala zima la masoko, suala zima la kujenga maghala na kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji. Lushoto imezungukwa na vyanzo vingi vya maji, lakini miundombinu ya maji hakuna katika Jimbo zima la Lushoto. Ukianzia Kata ya Ngwelo, Gare, Mlola, Ubili, Makanya, Kwemashai, Mbwei, Ngulwi, Malibwi, Kilole, Kwekanga na Lushoto Mjini. Nakuomba katika bajeti hii basi uwafikirie watu wa Lushoto hususan katika suala zima la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la afya, tunashukuru tuna Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, lakini hospitali ile ina changamoto. Hospitali ya Lushoto hususani wodi ya akina mama wajawazito, ile wodi ni ndogo inastahili kuongezwa. Sambamba na hilo katika Kata za Ngwero, Gare, Magamba, Ubili, Kilole na Kwemashai tunahitaji kujengewa vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la miundombinu, Lushoto wenyewe tunaita Lushoto ya wazungu, kwani Wazungu Wajerumani walikuwa wanaishi maeneo yale, miundombinu ya barabara imejengwa tangu kipindi cha mkoloni. Kwa hiyo, niiombe Serikali ituangali katika vipaumbele vya barabara, hususan barabara ya kutoka Lushoto kupitia Soni hadi Mombo. Barabara hii ni nyembamba na mvua zikinyesha huwa kuna mawe yanaporomoka yanazuia barabara. Hata juzi kati tarehe 17 zaidi ya siku tatu magari yalilala pale mpaka hata maiti zinatoka Dar es Salaam, Tanga na sehemu zingine basi zilishindwa kupita pale kwa sababu ya mawe yaliyoshuka pale na makalvati kuziba, maji yanatiririka katikati ya barabara ilichukua takribani ya siku tatu, naomba katika bajeti yako hii basi waifikirie barabara ya Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo kuna barabara ya kutoka Mlalo kupitia Ngwelo, Mlola hadi Makanya kwenda kwa Mheshimiwa January, Mlingano kwa Mheshimiwa Majimarefu, Mashewa, barabara hii tunaomba sasa ipandishwe hadhi iwe ya Wakala wa Barabara TANROAD. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka Dochi kupitia Ngulwi hadi Mombo, kwa kuwa barabara hii ya Lushoto - Soni - Mombo, mara nyingi mvua zinaponyesha barabara ile mawe yanashuka yanaziba barabara ningeishauri Serikali iwe na barabara mbadala ya kutoka Dochi - Ngulwi hadi Mombo ijengwe kwa kiwango cha lami na iweze kupandishwa daraja ili iweze kuwa barabara mbadala kwa ajili ya matatizo yanapotokea na breakdown zinapotokea katika barabara ya Soni - Mombo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hawa ndugu zangu, vijana wenzangu siyo vijana wa Lushoto tu ni Tanzania nzima, vijana wanaojihusisha na bodaboda. Vijana hawa inapaswa walindwe maana bodaboda ni ajira kama ajira nyingine. Bodaboda hawa naomba kama kuna uwezekano watengewe fungu katika bajeti hii kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao kwani katika vipaumbele vinavyotoa ajira ni watu wa bodaboda. Wamepata ajira kwa kuwa watu hawa wana watoto, wanao wake zao na wanawasomesha watoto na bodaboda ndiyo kipato chao, ndiyo ajira yao, ninaomba askari wasiwanyanyase vijana wanaojishughulisha na bodaboda, siyo kwa Lushoto tu ni Tanzania tuwalinde vijana wetu wa bodaboda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la umeme. Nimshukuru Waziri Muhongo, alituma timu yake wakazunguka katika Wilaya nzima ya Lushoto siyo Jimbo la Lushoto tu, Wilaya nzima ya Lushoto alituma timu yake ikazunguka na kubaini maeneo ambayo hayana umeme na kuyaandika, kuyahakikisha kwamba ameyachukua then atayafanyia kazi. Kwa hiyo nampongeza sana Profesa Muhongo, Mungu akulinde na akuzidishie umri! (Makofi)
Kuna suala zima la michezo. Lushoto kuna vipaji vingi sana, kuna vijana wengi sana ni wanamichezo wazuri na hata timu za Simba na Yanga zinakuja Lushoto kwa ajili ya kufanya mazoezi. Kwa hiyo, niombe sasa, nimuombe Waziri wangu, mpendwa wangu Mheshimiwa Nape Nnauye katika bajeti hii aifikirie Lushoto kimichezo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Napenda kuchangia katika suala zima la nyumba za Walimu hasa wale wanaoishi vijijini.
Pia ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari na msingi hasa ukizingatia katika Wilaya ya Lushoto kuna maeneo mengi vijijini hayana shule kabisa. Watoto wanatoka zaidi ya Kilometa 20 hadi 25. Wakati wa mvua nyingi watoto hawa hawaendi shule mpaka mvua itakapopungua.
Naiomba Serikali yangu Tukufu ijenge shule kwenye maeneo hayo, mfano Lushoto Makanya Kagambe, Mazumbai, Ngindoi, Muheza na Mlola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wetu wanapata mishahara midogo sana ambayo haikidhi haja zao. Naiomba Serikali yangu Tukufu iangalie jinsi gani ya kuwaongezea mishahara Walimu wetu hawa. Pamoja na stahiki zao, walipwe kwa wakati hasa hizi za uhamisho. Sambamba na hayo, makato ya Walimu yamekuwa mengi. Naiomba Serikali yangu ipunguze makato hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la vitabu mashuleni pamoja na miundombinu kwa ujumla. Pia Walimu hawa wapandishwe madaraja kwa wale wote wanaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la VETA ni suala ambalo lipo kwenye ilani, kila Wilaya iwe na VETA. Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Chuo cha VETA. Naiomba Serikali ikafungue chuo cha VETA Lushoto na kwa bahati nzuri kuna majengo ambayo yako tayari, kwani ni kuongea na TAMISEMI wawape majengo waliyoyaacha na kuhamia kwenye jengo lao jipya. Nia na madhumuni ni kusaidia vijana wetu hawa ambao hawakuweza kuendelea na masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naishukuru Serikali yangu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi hao, lakini wanafunzi hawa wanapomaliza vyuo, Serikali haiwapatii ajira vijana wetu hawa. Hapo hapo Serikali inatangaza wote ambao wamesoma Vyuo Vikuu kwa mikopo wanatakiwa warejeshe mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe binafsi najiuliza, vijana hawa bado hawajapata kazi na huu mkopo wataurudishaje? Naiomba Serikali yangu Tukufu iwapatie Vijana hawa ajira ndiyo waanze kulipa mikopo hiyo. Pia Serikali ijue ya kuwa kuna kundi kubwa sana la vijana ambao wapo mtaani hawana ajira. Kwa hiyo, ni muhimu sana kujenga vyuo vya VETA vijana wetu wakimaliza waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aniangalie kwa jicho la huruma aniletee Walimu wa sayansi. Mungu akubariki mama yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anitembelee katika Wilaya ya Lushoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi wetu ufikie uchumi wa kati tunatakiwa tuwekeze katika viwanda vyetu vya ndani pamoja na kuvisimamia. Pia tukumbuke viwanda ndio njia pekee inayoweza kutoa ajira kwa vijana walio wengi nchini. Pia kuna vijana wengi ambao hawana ajira, niishauri Serikali iwawezeshe vijana hawa ili wasiwe wanatangatanga kwenda mjini kutafuta ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna vijana wengi waliomaliza vyuo na hawana ajira, papo hapo wanaambiwa walipe mkopo waliokopa, vijana hawa watalipaje mkopo kama Serikali yao haijawawezesha kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyefahamu kuwa Wilaya ya Lushoto ni ya wakulima wa matunda na mboga mboga. Hivyo niishauri Serikali iweke kiwanda cha kusindika matunda, kwani matunda na mboga mboga vinaharabika hali inapelekea wakulima kupata hasara katika mazao yao hayo na pia wakulima wetu tunawakatisha tamaa kwa kupoteza nguvu zao nyingi shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wamejitahidi kujiajiri kwa kufanya biashara lakini wanasumbuliwa sana na watu wa TRA hasa wafanyabiashara wa Jimbo la Lushoto. Maafisa wa TRA hawana elimu ya biashara, halii inapelekea Maafisa hawa kuwa ndio wamepata uchochoro wa kuwanyanyasa wafanyabiashara hawa. Imefikia hatua mfanyabiashara akutane na simba lakini sio Afisa wa TRA. Naomba Serikali iliangalie hili ili wafanyabiashara wale waweze kufanya biashara yao kwa amani na kujipatia kipato chao cha kila siku.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Habari Mheshimiwa Nape Nnauye kwa hotuba yake nzuri iliyojaa matumaini ya kuona tasnia ya habari ikisonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vipaji vingi vya vijana hasa Wilayani hadi Vijijini, lakini vipaji hivi vinapotea bure na vijana kushindwa kuviendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali hasa hii tasnia ya michezo ifike Wilayani mpaka Vijijini kwenda kuwanoa vijana hawa ili Serikali iweze kuwawezesha na vijana hawa waweze kutimiza ndoto zao. Sio kutimiza ndogo zao tu pia nchi yetu itakuwa ina kiwango kikubwa cha michezo, kwani kuna wakina Samatta wengi huko Wilayani na hasa Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule za habari, utamaduni na michezo. Niishauri Serikali ifungue shule kila Wilaya ili kuibua vipaji vya vijana wetu. Vijana hawa Serikali imewaacha kwa muda mrefu sana hivyo basi katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017 itenge pesa kwa ajili ya kuibua fani za vijana hawa pia niishauri Serikali ije iwekeze katika Wilaya ya Lushoto, katika shule ya michezo, Lushoto ni mji ambao una mazingira mazuri, mazingira haya mazuri iliwavutia timu ya Simba na Yanga kuja kufanya mazoezi yao Lushoto.
Pia niishauri Serikali iweze kujenga uwanja wa michezo katika Mji wa Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wasanii katika nchi hii hakuna asiyejua ya kuwa Tanga kuna vipaji vingi vya wasanii. Hivyo niiombe Serikali iweze kuwajengea uwezo wasanii hawa ili nao waweze kufahamika Kitaifa hata Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimuombe Waziri wa Habari na Michezo atenge muda wa kutembelea Lushoto. Mungu ambariki sana Waziri wetu Mheshimiwa Nape Nnauye.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu huyu aliyenijalia afya na nguvu kuweza kusimama katika jengo lako hili Tukufu. Pia niwashukuru wananchi wangu wa Lushoto kwa kuniamini ili nije niwawakilishe katika jengo lako hili tukufu. Niendelee kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake ya Mawaziri, aendelee kutumbua majipu na sisi Wabunge tutaendelea kuyapaka spirit ili yakauke haraka siku ya siku tuyapeleke mahakamani majibu haya ili wakome kuita nchi hii ni shamba la bibi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwashukuru Mawaziri wangu wawili Mheshimiwa Angellah Kairuki na Mheshimiwa George Simbachawene. Pia niendelee kuwapongeza ndugu zangu wapinzani maana leo naona wameanza kuchangia hoja, wamebakisha tu kusema naunga mkono hoja, lakini kwa uwezo wa Mungu naamini itafikia hatua hiyo sasa naona roho mtakatifu amewashukia leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchangiaji mmoja dada yangu Mheshimiwa Grace Kiwelu alisema kwamba tufute mbio za mwenge. Kufuta mbio za mwenge ni sawasawa na kufuta historia ya nchi, hiyo haitawezekana. Kama isivyowezekana kwa CHADEMA kufuta historia ya Edwin Mtei ndani ya CHADEMA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia hoja sasa. Niishauri Serikali iendelee kuanzisha vijiji, kata, Halmashauri, wilaya hadi mikoa kwani hii inapelekea kupeleka huduma karibu na wananchi. Historia ya Jimbo la Lushoto au Wilaya ya Lushoto kwa kweli ni kubwa sana na Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya Nne alivyotembelea Lushoto alituahidi Halmashauri ya Mji wa Lushoto na Mlalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongea juu juu hivi mtu huwezi ukaamini kwamba Wilaya ya Lushoto ni kubwa sana. Nataka niseme ili ujue uhondo wa ngoma uingie ucheze, namuomba Mheshimiwa Waziri wangu Simbachawene atembelee Lushoto ili tunapoongea maneno haya tuwe tunamaanisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto inapakana na Kenya. Kuna watu wanatoka kwa miguu kufuata huduma Wilayani Lushoto inashindikana wanatumia siku mbili. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sasa ituangalie kwa jicho la huruma ili kwenye bajeti hii ya 2016/2017 iweze kutupatia Halmashauri ya Mji na iweze kutupatia Halmashauri ya Mlalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye afya. Suala la vituo vya afya ni tatizo la nchi nzima na naamini Serikali yangu sikivu imejiandaa vyema kuweza kujenga vituo hivi vya afya. Pamoja na hayo kwenye mpango huo naomba sasa Waziri, Mheshimiwa Simbachawene tuangalie Lushoto kwa sababu Jimbo la Lushoto lina kituo cha afya kimoja na zahanati nane. Kwa hiyo, huduma hii ya watu wa Lushoto kwa kweli imekuwa na hali ngumu kiasi kwamba kwa kweli inatia masikitiko. Kituo hiki kiko sehemu moja inaitwa Mlola, kutoka sehemu moja wanaita Makanya kwenda Mlola kwanza hata miundombinu ya barabara hakuna, wananchi wa kule wanapata taabu sana.
Hawa wananchi ni wapiga kura wetu tunawategemea, hawa hawayumbi wala hawayumbishwi, hawajui CHADEMA wanajua tu CCM. Kwa hiyo, nikuombe Waziri wangu katika bajeti ya mwaka 2016/2017 hebu liangalie hilo tuweze kuongeza vituo vya afya. (Makofi)
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa....
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba unilindie muda wangu kwani mtoa taarifa, taarifa hiyo nadhani hajajielewa aipeleke Simanjiro lakini Lushoto ni kijani tupu. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Ulipata asilimia mia?
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Ndiyo ni asilimia mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongelea suala zima la afya. Kwa kuwa Serikali yetu ina mpango mzuri wa kujenga vituo vya afya katika Jimbo la Lushoto, niiombe sasa isimamie hawa watu wa MSD kwani dawa hazifiki kwa wakati. Nimechunguza kweli hawa watu wa MSD ni majipu kwani DMO anapeleka pesa za kununulia dawa labda shilingi milioni tano lakini akifika anapewa dawa za shilingi milioni mbili. Kwa hiyo, hili ni jipu naomba lifuatiliwe. Sisi tunalalamikia madaktari wetu kumbe kuna kidudu mtu hapa katikati anakwamisha huduma nzima ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la kilimo. Uti wa mgongo wa Taifa hili ni kilimo lakini huachi kuongelea pia na miundombinu. Miundombinu ya barabara ndani ya Jimbo la Lushoto hasa za vijijini ni tatizo. Wananchi walio wengi hususan wakulima wanakwamisha na miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu tukufu kwamba katika bajeti hii ya 2016/2017 ipeleke pesa za ruzuku za kutosha katika Halmashauri ili barabara hizi ziweze kutengenezwa kiwango cha kupitika ndani ya mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo kuna barabara za vijiji ambazo ni tegemezi hata katika Jiji la Dar es Salaam, barabara hii ni ya Mshizihii - Boheloi, inatoa mazao mengi sana. Barabara nyingine ni ya Kwemakame - Ntambwe - Mazumbai - Baga kwa Mheshimiwa January.
Kwa hiyo, hizi ni barabara ambazo zinatoa matunda na mazao mengi sana. Pia kuna barabara inatoka Malibwi – Kwekanga - Kilole - Ngwelo ni ya muhimu sana kwani inachangia pato kubwa la Taifa hili.
Barabara nyingine ni ile inayoingilia sehemu moja wanaita Kwaikileti – Dindira – Bandi – Kwaboli – Migambo. Barabara hii inatoa matunda mengi mno kiasi kwamba hata tukielezea uchumi wa matunda ya Lushoto basi chanzo chake kinatoka maeneo hayo niliyotaja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia suala zima la redio ya Taifa (TBC). Nimuombe Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Nape, kule kwetu tunasikiliza redio za Kenya tu. Kwa hiyo, ifikie hatua sasa kwenye bajeti hii ya mwaka 2016/2017 basi watutengee mafungu ili wananchi wale waweze kupata taarifa mbalimbali za Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wangu umeisha, naunga mkono hoja asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri kwa hotuba yake nzuri iliyojaa matumaini ya Watanzania kujitoa kwenye vibatari hadi kuwa na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Lushoto tunakushukuru baadhi ya vijiji vimepata umeme. Pia ametuma timu yake imeenda kupima maeneo yote ambayo yamekosa umeme wa REA II na kuwahakikishia wananchi wangu kuwa Jimbo la Lushoto litapata umeme kwa yale maeneo yote yaliyobaki. Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wananchi wangu wameshakuwa na matumaini makubwa juu ya suala zima la umeme, niendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutimiza ahadi yake hiyo ili ifikapo 2020 wananchi wangu waendelee kuamini Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi. Pia napenda kuorodhesha maeneo ambayo hayajapata umeme pamoja na kwamba maeneo mengine ya kata na vitongoji yameshapata umeme. Kata ambazo hazina umeme pamoja na vijiji vyake ni kama ifuatavyo:-
(i) Makanya yote;
(ii) Ngwelo baadhi ya vijiji;
(iii) Kilole baadhi ya vijiji;
(iv) Kwekanga baadhi ya vijiji;
(v) Gare baadhi ya vijiji;
(vi) Kwemashai baadhi ya vijiji;
(vii) Ubiri baadhi ya vijiji;
(viii) Magamba baadhi ya vijiji;
(ix) Kwai baadhi ya vijiji;
(x) Mgambo baadhi ya vijiji;
(xi) Mbwei baadhi ya vijiji;
(xii) Malimbwi baadhi ya vijiji;
(xiii) Lushoto baadhi ya vijiji;
(xiv) Mlola baadhi ya vijiji; na
(xv) Ngulwi baadhi ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa binafsi nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti ya Wizara yake pamoja na hotuba yake nzuri iliyojaa mazuri na mambo ambayo yametoa kiu za wananchi. Pamoja na style yake ya kutoa mabegi yaliyojaa mambo yote yanayohusu Wabunge na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri sina budi kumshukuru kwa kunipatia Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Lushoto ambalo lipo kwenye Jimbo langu kwani mchakato huu niliufuatilia wakati tupo kwenye Kamati yako ya Ardhi. Hivyo hujasita kuondoa kiu yangu na ya wananchi wa Lushoto kwa kiujumla na kuahidi kuja kufungua Baraza hilo mwezi wa saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi, Mheshimiwa Waziri migogoro ya ardhi ipo katika nchi nzima lakini ndani ya Jimbo la Lushoto kuna migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima hasa maeneo ya Bwei, Kilole na Mlola, yote haya yanasababishwa na eneo dogo lililopo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mwekezaji wa kiwanda cha mbao kinachoitwa Mombo Saw Mill. Kiwanda hiki kilikufa takribani miaka 20 iliyopita, lakini Mheshimiwa Waziri eneo hili linapakana na shule ya sekondari ya St. Mary’s - Mazinde Juu na shule hii ni ya boarding kwa ajili ya wasichana. Mheshimiwa Waziri eneo hili limekuwa ni kichochoro cha watu kuingia katika eneo la shule ukizingatia eneo hilo linapakana na shule hiyo na upande lilipo ndiyo mabweni ya wanafunzi. Father amemfuata mwenye eneo lakini hakuonesha ushirikiano kwa sababu mwenye eneo hili anashirikiana na watu wabaya ambao hawana nia nzuri ya shule hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima na taadhima na kwa unyenyekevu mkubwa, suala hili uliingilie kati, eneo hili liweze kurudi ili liungane na eneo la shule. Ninashauri hivyo kwa ajili ya kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, sambamba na hilo eneo hili halijalipiwa kwa muda mrefu sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ningeomba Mheshimiwa Waziri Mungu akikujalia kufika Lushoto kufungua Baraza la Ardhi, utembelee eneo hilo la Magamba na shule ya sekondari Mazinde Juu kwa ajili ya kupata maelezo ya kina kwenye uongozi wa shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Lushoto kuna muingiliano mkubwa wa watumishi wa ardhi, hii imepelekea ujenzi holela na urasimu wa kupata hati ni tatizo kubwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimtakie Mheshimiwa Waziri utumishi uliotukuka huku wananchi wa Lushoto wakiendelea kukuombea kwani wana imani kubwa sana na wewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Mchango wangu upo kwenye suala zima la utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto kuna vivutio vingi vya kitalii lakini vivutio vile havichangii Pato lolote la Taifa letu kwa sababu utalii ule unafanywa kienyeji. Hivyo basi niombe Serikali ifungue chuo cha kitalii Lushoto ili vijana wetu wapate elimu ya utalii ili wasiendelee kufanya kazi ile kienyeji na kuisababishia Serikali kukosa mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishauri Serikali, yale maeneo yote yenye vivutio yatengenezwe ili watu wasiingie kiholela, ikiwezekana kuwe na vizuizi. Niombe Serikali yangu Tukufu iwaangalie hawa watu wanaovuna mti mmoja mmoja, waweze kuchana mbao zao kwa kutumia chainsaw kwani wakulima hawa hawana uwezo wa kununua mashine za kuchana mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo walikuwa wanatumia misumeno ya mikono ambayo hakuna watu wanaoitumia kwa sasa maana walikuwa wanatumia wazee na wazee wengi wameshakufa na waliobaki wamezeeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pia imepelekea baadhi ya watu ambao hawana nia nzuri hasa polisi wanawakamata sana watu wanaokata miti kwa chainsaw, na askari hawa wameacha kufanya kazi zao nyingine, kazi yao kusikiliza maeneo yanayolia chainsaw ili wakakamate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la asilimia 20 kumekuwa na tabia ya Maafisa Misitu kuchukua asilimia hizo hata kama mtu anavuna mti wake kwa matumizi yake binafsi. Niombe Serikali yangu iwape Wabunge zile sheria za misitu ili Wabunge tukawaelimishe wakulima wetu wa miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi yaliyozungukwa na misitu mameneja hawatoi mgao kwa vijiji vilivyozunguka msitu pamoja na vikundi vya kina mama wajane, vijana pamoja na vikundi vya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hasa katika Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mungu amlinde na kumzidishia umri pamoja na kumpa afya nzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya na nguvu kuweza kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Naomba nimpongeze Waziri Maghembe na timu yake kwani hotuba yake ina vina, imegusa, lakini nimuombe isiwe ya maandishi tu iwe ya vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja katika kuchangia juu ya upandaji wa miti. Miaka ya nyuma misitu iliungua baadhi ya maeneo katika nchi hii, hususani Lushoto, mpaka sasa hivi maeneo yale bado ni mapori hayajapandwa miti. Niishauri Serikali yangu sikivu iandae mikakati kwa ajili ya kupanda miti katika maeneo yale kuanzia Korogwe, Lushoto mpaka kushuka maeneo ya Same kule ni jangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pamoja na kupanda miti iwasaidie pia wakulima mmoja mmoja wa miti waweze kupanda kwenye mashamba yao, kwani ukitaja Lushoto ndiyo kuna wahifadhi, watunzaji wa mazingira wakubwa sana. Leo hii maeneo yale ambayo ni vichaka yanatia aibu. Naiomba Serikali yangu tukufu ipange fungu kwa ajili ya kupanda miti katika milima ile ya Lushoto, pia iwasaidie wakulima hawa mmoja mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie moja kwa moja kwenye mgao na uvunaji. Tunashukuru tumepakana na misitu ya Shume, Mazumbai, Baga, Gare, lakini misitu ile bado haisaidii wananchi. Katika mgao wanaangalia wale watu ambao wana uwezo na kila mwaka watu wanaopewa mgawo ni wale wale. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu na nimuombe Waziri Maghembe kipindi hiki ahakikishe kwamba mgao ule aufuatilie waliopata ni wangapi na ni wa aina gani? Mimi kama Mbunge wao wamenituma baada ya kulalamika kilio hiki kwa muda mrefu sana. Mgao huu pia au uvunaji huu haujazingatia watu wanaochakata viwandani, kwa mtu mmoja mmoja na kwa vikundi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uvunaji kwa mtu mmoja mmoja. Misitu ya Serikali hii watu wanapeleka kuchakata kwenye viwanda, viwanda viko mbali sana na miti ile. Kuna sehemu wanaita Makanya, Ngwelo, Gare, Ubiri, Lushoto, Mbwei, Malibwi na Kilole, maeneo haya yako mbali sana na viwanda. Kitu cha ajabu na cha kushangaza watu hawa wameweka sheria moja kwa ajili ya kuvuna kwa vikundi au kwa ajili ya kuvuna na chainsaw, wamekataza kuvuna kwa chainsaw wavune kwa shoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana wakulima wangu wale wa miti sasa waruhusiwe kuvuna kwa chainsaw kwani ukitoa mti kutoka Makanya au mtu wa Makanya akivuna mti hawezi kupeleka moja kwa moja mpaka kiwandani, lakini Mheshimiwa Maghembe watu hawa anawakataza anasema kila mtu avune kwa shoka kitu ambacho ni kigumu, ndiyo maana nikasema ameangalia upande mmoja tu kwa ile misitu ya Serikali lakini hajaangalia kwa mtu mmoja mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Maghembe, atakaposimama ku-wind up basi aangalie vitu hivi. Ahakikishe kwamba watu wangu awaruhusu sasa wavune kwa chainsaw. Kwa sababu mtu yule hawezi kukata mti wake kule mpaka akapeleka kiwandani, itakuwa ni shida. Tunawaomba hata mbao za madawati wanashindwa kuvuna wanasema kwamba tumekatazwa kuvuna kwa chainsaw. Kwa hiyo, hili ningeomba baada ya kusimama Mheshimiwa Maghembe basi alitolee ufafanuzi, ili watu wangu waweze kuvuna kwa chainsaw.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mheshimiwa Maghembe alitembelea Jimboni kwangu kule Lushoto, alikuta changamoto, pamoja na kwamba sikuwa na taarifa za ujio wake kama angenipa taarifa, basi ningemwambia hali halisi ilivyo, yeye alienda moja kwa moja mpaka ofisini kwa wataalam wake tu, na alipofika kule alichukua maneno ya wataalam akayaacha ya wananchi. Ninamshauri siku nyingine akienda atafute na Wabunge, hii siyo kwa Waziri Maghembe tu, Waziri yeyote atakayeenda site basi atafute Wabunge kwa sababu Wabunge ndiyo wanajua changamoto zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Lushoto inapakana na msitu, ninamuomba Mheshimiwa Maghembe kuna akina mama kule wanatafuta kuni msituni wanakamatwa, shoka zao zinachukuliwa zinaenda kuhifadhiwa ofisini, mapanga na kila kitu, watu wale ni walindaji wakubwa wa misitu. Nashukuru Mheshimiwa Maghembe alienda pale akawaambia kina mama wale basi waendelee kutafuta kuni na waende na mapanga na mashoko, lakini wasije wakatafuta mti ambao ni mbichi. Kwa hiyo, nimuombe atakaposimama basi aliongelee hilo suala hapa ili liingie kwenye Hansard na watu wangu waweze kupata nguvu kwa ajili ya kutafuta kuni msituni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri wa Maliasili na Utalii, ashirikiane na Waziri wa Viwanda, kuna Kiwanda cha Ceiling Board pale Mkumbara; kiwanda kile kinakufa, hakina tatizo lolote, kina skyline inatoa magogo kutoka Shume kushuka chini. Lakini kwa sasa hivi kinakufa, na kinakufa bila sababu yoyote, ningemuomba sasa Mheshimiwa Waziri Maghembe na Mheshimiwa Mwijage wafike pale Mkumbara Ceiling Board, waone kiwanda kile jinsi kinavyonyanyasika, na watu wa pale jinsi wanavyonyanyasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa pale hata kulipa bili ya umeme wameshindwa, sambamba na hayo naamini kabisa Mheshimiwa Mwijage na Mheshimiwa Maghembe watakapofika Mkumbara basi moja kwa moja wataenda mpaka kwenye Kiwanda cha Chai Mponde, naamini Mheshimiwa Mwijage kama kweli ana hofu ya Mungu atatoa sauti yake na kufungua viwanda vile, wananchi wa kule wananyanyasika, hata kulipia karo ya shule wanashindwa, hata mlo ni mmoja kwa sababu ya chai yao kiwanda hakijafunguliwa wanashindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Mwijage, nitamwekea hata mafuta aende Mkumbara Ceiling Board kwa sababu itakuwa ni ziara yake hiyo basi aende mpaka Mponde pale aone wakulima wa chai wanavyonyanyasika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, huyu ambaye amenijalia afya na nguvu ya kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia bajeti ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nikupongeze wewe mwenyewe na tutaendelea kukuombea dua sisi Wabunge wote kwani unatosha. Kwa kuwa sisi wengine ni Masharifu basi naamini hakuna kitu kibaya ambacho kitakupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kumpongeza Waziri wa Fedha na timu yake kwani bajeti yake kwa kweli ni nzuri na inatia moyo. Tuna uhakika sasa kwamba tunakwenda kwenye Tanzania mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kuchangia suala la kilimo. Nchi yetu inasema kilimo ni uti wa mgongo, lakini inasikitisha tunaposema kilimo ni uti wa mgongo, kilimo hiki kimetengewa bajeti ya shilingi trilioni 1.56, bajeti ambayo ni ndogo sana, haikidhi haja. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sasa Tukufu iongeze bajeti hii kwani kama tunategemea uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda hautoki sehemu nyingine zaidi ya kwenye mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu zinanyesha mvua za msimu, niishauri Serikali yangu sasa ijenge mabwawa kila maeneo ili kuweza kukinga mvua zile na wakulima wetu waweze kulima kilimo cha umwagiliaji. Kama alivyosema viwanda vinategemea kilimo kwa maana kwamba malighafi zinatoka kwenye kilimo, kwa mfano kule kwangu kuna maeneo mengi sana lakini ni kame, kwa maana hiyo tukiyajengea sasa mabwawa ina maana tutalima kilimo cha umwagiliaji na tutaongeza mnyonyoro wa thamani kwenye mazao yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna asiyejua kwamba Lushoto ni ya kilimo cha mboga mboga na matunda lakini kilimo kile wanalima kwa mazoea. Niiombe Serikali yangu ipeleke ruzuku za pembejeo kwenye kilimo cha mboga mboga na matunda. Wenzangu wote wanaposema ruzuku basi mimi kwa Wilaya ya Lushoto kwa kweli mboga mboga zile na matunda hayajawahi kupata ruzuku. Niishauri Serikali yangu sasa kama ina nia ya dhati, basi iweze kuwezesha kilimo kile kiweze kupata pembejeo za ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niingie kwenye afya. Wakati tuko kwenye mchakato wa kampeni tulikuwa tunanadi Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwamba kila kijiji kitajengwa zahanati na kila kata itajegwa kituo cha afya. Leo hii katika bajeti nimeona tu mambo ya dawa na madeni ya MSD na vinginevyo lakini sijaona zahanati hata moja wala kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kuangalia wananchi wetu kule vijijini kwa kweli ni masikitiko makubwa sana. Laiti ningekuwa na uwezo ningemchukua Waziri wa Fedha akaenda moja kwa moja kwa wananchi wale awaone kwani kuna wananchi kule hawajui hata hospitali. Wananchi wale kwa kweli wako kwenye mazingira magumu, wanalala chini, leo hii ukimchukua ukisema umpeleke hospitalini, kwa kweli hata mwili wake umekakamaa kama mbao. Hata umchome sindano ina maana haingii, sasa huyo unategemea nini, lakini mtu yule amekosa huduma. Niiombe Serikali yangu iende moja kwa moja kwa wananchi wale ili waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumeongea suala la walemavu, lakini tumeangalia walemavu wa mjini wale ambao tunawaona lakini wa vijijini wala hawajafikiwa. Niombe sasa katika bajeti ya walemavu basi iende moja kwa moja kwa wale walemavu wa kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala zima la shilingi milioni 50. Tulikuwa tunapigia kelele kwamba jamani mkituchagua basi shilingi milioni 50 zitakuja tena kwa wakati kwa kila kijiji, lakini leo hii naona bajeti imetengwa tu kwenye mikoa 10. Niishauri Serikali yangu wasipeleke kwenye mikoa 10, watenge hata vijiji vitano vitano kwenye mikoa yote Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Sisi wengine tumeshajiandaa watu wetu tumeshaanza kuwapa pesa ya kufungulia akaunti mahsusi kwa ajili ya pesa hizi. Mpaka sasa ninavyoongea, nina vikundi zaidi ya 100 ambavyo nishavifungulia akaunti wanasubiri pesa hizi. Kwa hiyo, niiombe sasa Serikali yangu Tukufu iweze kupeleka pesa hizi kwa wakati ili nikirudi Jimboni wananchi wale wasije wakaniuliza maswali magumu ambayo nitashindwa kuyajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye kodi ya bodaboda. Wakati Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anapita alisema katika watu ambao nitawaangalia ni watu wa bodaboda, leo hii naona watu wale tunazidi kuwaongezea mzigo kwani walikuwa wanalipa Sh. 45,000/= sasa hivi wanatakiwa walipe Sh. 95,000/=. Hebu jamani hili tuliangalie kwa jicho la upendeleo kwani ndugu zangu itafikia hatua sasa bodaboda hawa hawatatuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuongelea ushuru wa mitumba. Mitumba hii imeajiri wananchi wengi sana. Leo hii ukifika pale Dar es Salaam au nimtume Waziri wa Fedha pale Dar es Salaam ataona ma-godown ya mitumba ambayo inasafirishwa mikoa yote Tanzania. Niiombe Serikali yangu iondoe ushuru huu ibaki VAT ileile ya mitumba iliyokuwepo siku zote ikiongezwa ina maana tumewapa mzigo watu ambao hawastahili kubeba mzigo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia moja kwa moja niende kwenye suala la mifuko ya nailoni. Unapopiga marufuku matumizi ya mifuko ya nailoni unakuwa umepiga marufuku utunzaji wa mazingira kwani miche inaoteshwa kwenye mifuko ya nailoni. Kwa hiyo, anaposema mifuko ile ipigwe marufuku isitumike ina maana atakuwa amewaambia wananchi wasipande miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii asilimia tano ya vijana na asilimia tano ya akinamama, tunaipeleka wapi kama wananchi wetu hawa hatuwasaidii ipasavyo. Tunawapa wananchi asilimia tano kwa ajili ya kupata mitaji ndiyo anakwenda kununua bodaboda ambayo ina kodi kibao, unategemea mwananchi huyu atafaidikaje? Mwananchi huyu tumembebesha mzigo ambapo ni sawasawa na kumpaka mafuta kwa mgogo wa chupa. Kwa hiyo, hebu ifikie hatua sasa Serikali yetu iliangalie hili kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Niiombe Serikali yangu ijipange katika suala zima la wafanyabiashara kwani hawa wanaongeza pato kubwa katika Taifa letu, lakini kunakuwa na ukiritimba wa passport pamoja na Visa. Sambamba na hayo VAT inakuwa ni shida kwa wafanyabiashara hawa, yaani mzigo unachajiwa mara mbili ya bei aliyonunulia mfanyabiashara huyu. Suala la utoaji wa passport unachukua muda mrefu kuipata kwa hiyo niishauri Serikali yangu iliangalie hili pass hizo zitoke kwa muda muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la Mabalozi wetu hawa imefikia wakati sasa watafute wawekezaji pamoja na wafadhili kwa ajili ya kujenga nchi yetu sasa kiuchumi zaidi.
Katika Jimbo la Lushoto kuna ma-sister wana miaka zaidi ya 60 na wamesaidia sana jamii inayowazunguka na mpaka sasa wanaendelea kusaidia. Wamejenga shule, wamejenga zahanati na wamejenga hosteli na pia wanajitolea kuwafundisha watoto wa maeneo hayo. Kwa kuwa ma-sister hawa ni wa muda mrefu sana na wanaendelea kulipia kodi kama kawaida, lakini kwa sasa hawa wamezeeka na shirika limefika hatua wanashindwa kuwalipia ma-sister wale. Niiombe Serikali yangu iweze kuwapa uraia kwani wakiondoka na kurudi kwao itakuwa ni hasara kubwa sana kwa wananchi wa eneo lile la Kifungilo sekondari pamoja na Kata ya Gare kwa ujumla itakosa huduma muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba Mheshimiwa Waziri atembelee Jimbo la Lushoto au atume Mjumbe ili akaone hali halisi kwa haya niliyoongea hasa kwa suala zima la misaada tunayopatiwa na ma-sister hawa, kwa maelezo zaidi Mheshimiwa Waziri naomba nimwone ili nimwelezee kwa undani zaidi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri wa Fedha na timu yake kwa kutuletea mapendekezo mazuri ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018. Naomba kuchangia suala zima la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu. Naomba niishauri Serikali yangu Tukufu tufungue viwanda vidogo vidogo ambavyo malighafi zake zinapatikana hapahapa nchini hasa kwa wakulima wetu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumeongeza mnyororo wa thamani katika mazao yetu pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi wetu. Pia pembejeo zifike kwa wakati kwa wakulima wetu na pia wakulima wa mbogamboga na matunda nao wapewe pembejeo za ruzuku kwani wakulima hawa wanachangia sana Halmashauri zetu kwa kulipa ushuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali yangu Tukufu kuwe na mkakati maalum kuhusu suala zima la maji. Suala la maji lingefanywa kama suala la madawati lilivyofanywa tungemaliza tatizo la maji kabisa hapa nchini na kusahau kabisa tatizo hili la maji. Hili ni tatizo kubwa sana hapa nchini na kila Mbunge aliahidi kutatua tatizo hili. Naamini kabisa kama tatizo hili halijatatuliwa, Wabunge wengine tutashindwa hata kurudi majimboni kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana katika suala zima la huduma ya afya upande wa dawa pamoja na kutokuwa na vituo vya afya na zahanati hasa wananchi wanaoishi vijijini wana hali mbaya sana. Sisi kama Wabunge tumehamasisha suala la CHF na wanaelewa na kuchangia, lakini wanapofika hospitali wanakuta hakuna dawa zaidi ya kuambiwa wakanunue dawa katika maduka binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maliasili na utalii, naomba niishauri Serikali yangu Tukufu kuhusu suala zima la misitu yetu kuchomwa moto kila siku hali ambayo husababisha uoto wa asili kutoweka na maeneo ya misitu kubaki vichaka. Nashauri Serikali inunue ndege kwa ajili ya kuzima moto katika misitu yetu inayopata majanga ya moto hasa ikizingatiwa jiografia ya misitu mingi kuna maporomoko makubwa ambayo watu hawawezi kuzima moto unapotokea. Pia maeneo yote yaliyoungua Serikali ipande miti ili kurudisha mandhari ya msitu husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na unyanyasaji mkubwa sana hasa kwa mama ntilie, bodaboda, akinamama wanaouza mbogamboga na matunda pamoja na watu wenye ulemavu. Halmashauri zetu hasa Wakurugenzi wanawatoza ushuru watu hawa bila huruma pamoja na kuwatolea maneno yasiyofaa, kubwa zaidi kuwaongezea ushuru kila uchao. Niiombe Serikali yangu Tukufu iwaonye Wakurugenzi hawa ili wasiendelee kuwanyanyasa wapiga kura wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, sisi Wabunge tunapowaambia Wakurugenzi hawa wanatudharau na kutuita wanasiasa hatuna lolote. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu sisi Wabunge tunapoleta matatizo ya Wakurugenzi, tunaomba yafanyiwe kazi haraka na ikiwezekana mhusika achukuliwe hatua, zaidi ya hapo, majimbo yetu yatakuwa hatarini kuyakosa. Kibaya zaidi Wakurugenzi wengi ni wanasiasa pamoja na hayo wanarubuniwa na baadhi ya wanasiasa walioshindwa ili amharibie Mbunge ambaye yupo madarakani ashindwe au aonekane hafai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mazao ya biashara kama pamba, kahawa, korosho, tumbaku pamoja na katani. Mazao haya yamesahaulika wakati ndiyo yanatoa pato kubwa katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali yangu Tukufu kuhusu TRA. Mzigo unapoingia kutoka nje huwa unatozwa ushuru/kodi, ukitoka bandarini ukifika sehemu kama Kariakoo, TRA tena wanachukua kodi, ukipakiwa kwenda mikoani TRA wanachukua kodi, mwisho wa siku biashara hii inamfikia mtumiaji kwa bei ya juu. Kwa hiyo, niishauri Serikali ipunguze mzigo huu wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la motor vehicle licence, huwa inakatwa au inalipiwa kila mwaka lakini kuna watu wana magari ambayo yameharibika kwa muda mrefu mpaka limefikia kuchakaa mtu anaamua kuliuza kama skrepa. Cha ajabu mtu huyu anapofika TRA kwa ajili ya kuripoti ili arudishe kadi ya gari anaambiwa unadaiwa lazima ulipe, hii inasumbua sana watu wengi na ukizingatia walio wengi hawana uwezo tena. Kwa hiyo, niishauri Serikali iliangalie suala hili upya ili wananchi wetu ambao hawana uwezo wasije wakachukua maamuzi ambayo hawajayapanga na kama kuna uwezekano ifutwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimtakie Waziri afya njema pamoja na timu yake kwa ujumla.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati wote wawili kwa kuwasilisha hoja zao vizuri. Pia ni-declare interest kwamba na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu tulitembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mji Mpya Kigamboni, lakini mradi ule haujatengewa hata shilingi tano. Sasa basi niishauri Serikali ili jengo lile lisiendelee kulipa kodi wala wafanyakazi basi nadhani mradi ule urudishwe sasa kwenye Halmashauri ya Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulitembelea mradi wa utafiti wa nyumba bora na vifaa vya ujenzi. Kwa kweli kama tuna nia ya dhati tuwezeshe wakala wale wa nyumba na vifaa vya ujenzi. Tulifika pale wataalam walikuwa hata sita hawafiki, lakini vitu wanavyofanya ni vitu vikubwa sana. Sasa niishauri Serikali yangu kwamba wataalam wale wapewe uwezo ili waongezeke, waende mpaka Wilayani, naamini kabisa kwamba wataalam wale wakiongezeka na wakifika Wilayani vijana wetu watapata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefika pale wanatengeneza vigae na tofali. Vigae vile wanatengeneza kwa nyuzi za katani, huoni sasa wataalam wale wakiwa wengi wataenda Wilayani mpaka vijijini na kwenda kufundisha vijana wetu wale na hao vijana wakishapata taaluma ile basi waende kwenye Halmashauri wajisajili ili kazi za Halmashauri zikitokea waanze kupewa kazi na kuanzakujenga majengo kama ya zahanati, maabara, shule na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi nimeuona ni mradi mzuri sana. Naamini kama kweli Serikali yetu tukufu ina nia ya dhati basi iwekeze kwenye mradi ule. Wakala wale ni wa kweli wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la migogoro ya ardhi. Migogoro ya ardhi ni kitu ambacho kimekithiri hapa nchini kwetu Tanzania. Sina imani kabisa kwamba migogoro hii inaweza kuisha kwa jinsi tunavyoenda sasa. Niishauri tu Serikali yangu kwamba kama tunataka migogoro hii iishe basi tuhakikishe kwamba tunaandaa utaratibu mzima wa maeneo yote ya hapa nchini yanapimwa na watu wanapata hati zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuhakikishe kwamba watu wetu wa Wilayani hususan Maafisa Ardhi wanapewa zana na vifaa vya kutosha kuweza kupima ardhi hii kwa haraka. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Dada yangu Naibu Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Angeline Mabula wanafanya kazi moja nzuri sana kiasi kwamba hata Watanzania walio wengi wanaimani kubwa sana nao. Walitutangazia kwamba wameshafuta mashamba zaidi ya 200 lakini kuna shamba la mwekezaji mmoja kule Mnazi anaitwa Renash Enterprises Plot No. 292, title deed 11,247 ekari 2,442; na title deed 1746 ekari 1,188; title deed 4144 yenye ekari 562.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza mwekezaji yule analima tu eneo hili tena eneo kidogo sana ambalo ni ekari 562. Eneo lote lililobaki amelitelekeza, ni vichaka, kuna mapori makubwa ambayo kwa kweli hayastahili kuwa pale wakati watu wana shida ya ardhi. Nimuombe Waziri wangu na Naibu Waziri wa Ardhi, title hizi zifutwe na mpaka sasa taratibu zilishafuatiliwa lakini naambiwa kwamba Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini bado hati ile haijafutwa. Sasa nimuombe Waziri wangu atakapoamka ku-wind up basi aniambie kwamba hati ile itapatikana lini ili Halmashauri yangu iendele kupata mapato yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye kilimo, naishauri tu moja kwa moja Serikali ijenge mabwawa mengi ya kutosha hapa nchini kwa ajili ya wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa na cha umwagiliaji. Pamoja na hayo, wapeleke pembejeo kwa wakati pia hakuna asiyefahamu kwamba Lushoto ni ya wakulima wa matunda na mboga mboga, wakulima wale wanachangia sana kwa kutoa ushuru mwingi Halmashauri, lakini Serikali sijawahi kusikia Serikali inatenga ruzuku za pembejeo kuwapa wakulima wale wa matunda na mboga mboga. Ninaishauri Serikali yangu kwamba iwatengee wakulima wale wa mboga mboga na matunda nao waweze kupata ruzuku ya pembejeo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maji. Kama inavyofahamika maji ni janga la Kitaifa basi nashauri kwa kuwa EWURA wanatoza pesa kupitia nishati hii ya mafuta, niiombe sasa EWURA itenge asilimia 50 kwa ajili ya kupeleka maji vijijini.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Mazingira na Muungano pamoja na timu kwa hotuba yake nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuishauri Serikali yangu Tukufu kuhusu suala la mazingira. Kumekuwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa mazingira hasa kwa wananchi ambao hawajui suala zima la utunzaji wa mazingira. Niishauri Serikali yangu Tukufu ije na mkakati wa kupanda miti, hasa yale maeneo ambayo misitu imechomwa moto pamoja na vyombo vyote vya maji vipandwe miti na viwe na usimamizi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na sheria maalum ya kupanda miti katika kila kaya, kijiji hadi kata na kuanzia Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji wapewe sheria hizo ili wazisimamie kikamilifu. Naamini tukifanya hivyo tutakuwa tumeboresha nchi yetu kwa kurudisha uoto wa asili uliokuwepo hapo zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo wananchi wapewe miche ya miti bure. Kwa hiyo, Serikali itenge mafungu kwa ajili ya kununua miti na kuwapa wananchi. Kwa mfano, katika jimbo langu la Lushoto wananchi wangu wapo tayari kupanda miti kwa wingi, shida ni uwezeshaji wa miche.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni mambo mazuri. Pia nipongeze Kamati zote tatu kwa maana ya Kamati ya UKIMWI, Kamati ya Katiba na Kamati ya Sheria na Bajeti kwa kuwasilisha vizuri maoni yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na ninyi, ambaye ametujalia afya na nguvu kuweza kuhudhuria na kusema chochote katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika kuchangia na nianze na afya. Kama unavyofahamu Chama chetu cha Mapinduzi ambacho ndiyo chenye Serikali Ilani inasema kila kata itajengwa kituo cha afya na kila kijiji itajengwa zahanati. Kwa kuzingatia hilo
sasa kwenye Jimbo langu la Lushoto nimebahatika kujenga zahanati kumi na tatu na vituo vya afya viwili. Zahanati karibia tatu zimeisha zinahitaji madaktari na nyingine kama tano zimepigwa bati lakini bado usafi na zilizobaki bado zinahitaji kumaliziwa. Kwa hiyo, sasa niombe Serikali yako Tukufu kwamba ipeleke pesa katika halmashauri ili iweze kumalizia zahanati zile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto ina Majimbo matatu na Hospitali ya Wilaya moja. Takribani Wilaya ya Lushoto ina wakazi zaidi ya laki sita lakini hospitali ile imehemewa yaani inajaza kiasi kwamba kwa kweli sijui nieleze nini. Niiombe Serikali na niishauri katika bajeti hii inayokuja basi watenge bajeti ya kutosha ili Hospitali ile ya Wilaya iweze kupanuliwa hususan chumba cha akina mama wajawazito na chumba cha mama na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielekee kwenye kilimo. Niiombe Serikali yangu tukufu ijielekeze katika sekta ya kilimo kwani kama tunavyofahamu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu hili na kimebeba takribani asilimia sabini. Niiombe Serikali yangu itenge mafungu ya kutosha katika
kilimo na pia iwawezeshe wakulima wetu wadogo wadogo hawa hususan wa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde, ni ya wakulima wa bustani mfano mbogamboga na matunda. Wakulima wale wanachangia asilimia kubwa katika Halmashauri zetu lakini cha kushangaza hawapati pembejeo. Niiombe Serikali sasa kwa jicho la huruma iwaangalie wakulima wale wa mbogamboga hususan wale waishio Lushoto waweze kupata pambejeo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo naiomba Serikali iweze kujenga mabwawa katika Wilaya ya Lushoto kwani mvua nyingi sana zinanyesha kule lakini zinaharibikia baharini. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa ijenge mabwawa ili wananchi wetu waweze kulima kilimo cha
umwagiliaji. Pia hii itakuwa ni fursa kwa vijana wetu na ili wasikimbilie mjini basi tuwajengee miundombinu ili waweze kujiajiri wenyewe na kulima kilimo cha umwagiliaji. Naamini hii italeta tija kwa vijana wetu na wala hawatakimbilia mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye miundombinu. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbarawa kwa kazi kubwa anayoifanya. Ila nimuombe sasa kuna barabara hiyo tangu ninasoma darasa la kwanza kila siku naambiwa itapanda hadhi, lakini haipandi. Barabara hiyo imeanzia Mlalo - Ngwelo - Mlola - Makanya ikaenda mpaka kwa mzee wangu Mheshimiwa Kitandula. Nimuombe sasa Mheshimiwa Waziri Mbarawa hebu afumbe macho tu barabara ile ipandishwe hadhi kwani ni muda mrefu sana na kila nikisimama kwenye Bunge lako Tukufu naisemea barabara ile. Kwa heshimiwa kubwa na taadhima niliyokuwa nayo kwake nimuombe basi barabara safari hii ipandishwe hadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara zetu za mchepuko. Kama unavyofahamu Lushoto ni ya milima na mabonde kwa hiyo Lushoto bila barabara kwa kweli hatuwezi kusafiri. Lushoto kuna barabara kuu moja tu ikipata breakdown basi sisi Lushoto tumekwisha hata mahitaji
tunashindwa kupata. Kwa hiyo, niiombe Serikali yako Tukufu sasa Mheshimiwa Mbarawa kwamba kuna barabara ambayo inatoka Dochi - Ngulwi mpaka Mombo ni ya mchepuko na itakuwa mbadala kwa ajili ya breakdown itakayotokea maeneo ya Soni - Mombo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara aliahidi Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kilometa nne mpaka sasa sijapata maelezo yake. Niiombe sasa Serikali yako Tukufu hebu tuweze kupatiwa kilometa nne zile angalau tuweze kutengeneza Mji wetu wa Lushoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali hususan Waziri wa TAMISEMI kwamba zile barabara ambazo zipo Halmashauri zirudi kwa Wakala wa Barabara yaani TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna hii Idara ya Ardhi kule Halmashauri nayo irudi kwa Mkuu wa Wilaya kwa sababu ndiye anayesuluhisha migogoro ya ardhi zaidi kuliko Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu; Wilaya ya Lushoto kama nilivyosema ina Majimbo matatu lakini haina chuo cha VETA. Kwa hiyo, nimuombe mama yangu mpendwa Waziri wa Elimu atujengee hata chuo kimoja cha VETA kwani maeneo yapo tayari, kuna karakana, gereji na majengo
mengine. Kwa hiyo, nimuombe Waziri wangu huyu aweze kuliona hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanikiwa kujenga maboma zaidi ya ishirini, lakini bado hayajaezekwa kwa maana ya kupigwa bati. Sasa basi niiombe Serikali yako na Waziri wa TAMISEMI apeleke pesa za kutosha kule kwenye Halmashauri ili maboma yale ambayo tumeyajenga kwa
nguvu za wananchi tuwape moyo wasije kukata tamaa juu ya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme; kwanza nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Muhongo kwa kazi kubwa anayoifanya na Naibu wake, ila nimuombe kitu kimoja maana tunapata maswali magumu sana kule vijijini, unakaa tu hapa Bungeni unapigiwa simu haya vijiji vingapi
vimepata umeme unawaambia jamani bado hata orodha hatujaipata. Kwa hiyo, nimuombe Waziri wangu sasa niweze kupata ile orodha ya vijiji ili niweze kuwajibu watu wangu wale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ajira kwa vijana; kama unavyofahamu sasa hivi vijana ni wengi mno hususan vijana wa bodaboda na wauza mitumba. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa wajengewe uwezo ili waweze kujiajiri wenyewe na kama unavyofahamu sasa hivi vijana wengi wemejiunga na vikundi na wana SACCOS zao. Pia hizi SACCOS naomba ziundwe kisheria ili zitambulike na kukopesha hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na team yake yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu sana naomba kupandishwa hadhi kwa barabara inayoanzia Mlalo - Ngwelo – Mlole – Makanya – Milingano hadi Mashewa. Kilio changu hiki mpaka sasa hakijapata ufumbuzi; na barabara hii ni barabara ya uchumi ambayo ikifunguka itakuwa inachangia pato kubwa katika Serikali pamoja na Halmashauri yangu. Pia kutoa ajira kwa vijana, maana vijana wangu wamejiajiri katika suala zima la kilimo. Mazao yao yanaharibikia mashambani kwa sababu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtaji huu, vijana wengi wanakata tamaa ya kulima na kukimbilia mjini. Barabara hii ina kilometa 58 tu ambayo inaunganisha Majimbo matano, yaani Jimbo la Mlalo, Lushoto, Bumbuli, Korogwe Vijijini mpaka Mkinga. Naiomba Serikali yangu sikivu itoshe sasa, naomba barabara hii ipandishwe hadhi. Pia siyo vizuri Mbunge kuwaahidi wananchi wake kuwa barabara hii itapandishwa hadhi, lakini mpaka sasa hakuna hata dalili. Kwa hiyo, naomba Serikali itoe majibu leo baada ya kuhitimisha taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kilometa 16 inayoanzia Dochi hadi Ngulwi mpaka Mombo. Nayo hii ni kilio cha muda mrefu sana na barabara hii ni muhimu sana. Kama unavyojua, Lushoto ina barabara moja tu ya kuingia Lushoto Mjini. Kwa hiyo, barabara hii ikipandishwa hadhi itasaidia sana Mji waLushoto, utakuwa unafikika kwa wakati wote. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu ipandishe hadhi barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, barabara inayoanzia Mombo, Soni hadi Lushoto. Alitokea kiongozi mmoja na kutoa tamko kuwa barabara hiyo ipite magari ya uzito wa tani 10 tu. Kauli hii imesababisha ugumu wa maisha kwa wananchi wa Wilaya ya Lushoto. Kwani biashara zilizo nyingi zinauza bidhaa kwa bei ya juu na wananchi wa Lushoto kununua bidhaa hizo kwa bei ya juu kutokana na kuingizwa kwa bidhaa hizo kwa bei ghali. Wakati huo huo magari yenye uzito wa tani 40 yanapita, bila kuathiri au kuharibu barabara hiyo. Kwa mfano, magreda, magari yanayobeba materials yanayoenda Mtwara kwenye kiwanda cha Sementi cha Dangote. Pamoja na hayo nilimuuliza Meneja wa TANROADs Mkoa wa Tanga na akaniambia barabara hiyo inaweza kubeba gari lenye uwezo wa tani 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri atoe tamko la kuruhusu kupita magari yenye uzito usiozidi tani 40 kwani suala hili limesababisha uchumi wa Lushoto kushuka na kunilalamikia mimi Mbunge wao kila siku. Naomba Waziri atoe tamko leo hii zaidi ya hapo nitashika shilingi ya mshahara wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona bajeti ya daraja la Mshizii pamoja na bajeti ya barabara yake ya kutoka Nyasa kupitia Gare hadi Magamba. Kwani barabara hii ni mbadala, kukitokea breakdown ya Magamba Lushoto, magari yanatoa huduma kupitia njia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde, kwa hiyo, minara ya simu baadhi ya maeneo hakuna. Kwa hiyo, naiomba Serikali itujengee minara hasa katika Kata ya Makanya, Malibwi, Ubiri, Ngwelo, Kwekanga na Kilole.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la upimaji wa barabara, yaani kutoa kilometa 30 kila upande, yaani jumla mita 60. Hili naomba niishauri Serikali yangu Tukufu kwamba iangalie maeneo mfano, maeneo ya Lushoto, Serikali ikisema itoe mita 60 itapata hasara kubwa. Ushauri wangu ni kwamba kuna baadhi ya maeneo kama Lushoto yajengewe kulingana na yalivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kilometa nne za lami. Mpaka sasa hivi bado ahadi hiyo haijatekelezeka na ni takriban miaka minne sasa imepita. Naomba Serikali yangu itupatie ahadi hiyo ya Rais ili Mji wetu wa Lushoto angalau nao upendeze na tuwe tunajivunia na kumkumbuka Mstaafu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Naomba pia nipatiwe majibu haraka iwezekanavyo, maana wananchi mpaka sasa wanakosa uvumilivu kwangu, kwani wanadai nimewadanganya kwa muda mrefu sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Lushoto ni Wilaya yenye wakazi zaidi ya 600,000 na Wilaya yenye majimbo matatu ya uchaguzi. Hata hivyo Wilaya ile haina Chuo cha VETA tangu nchi hii ipate uhuru. Pamoja na hayo kuna vijana wengi sana ambao wanamaliza elimu ya msingi na sekondari lakini vijana hawa wanakimbilia mijini kwa sababu hawajaandaliwa juu ya suala zima la kupata stadi za maisha. Hivyo basi, niiombe Serikali yangu tukufu kuanzisha Chuo cha VETA haraka iwezekanavyo katika Wilaya ya Lushoto ili kuwanusuru vijana wetu na kutokukimbilia mijini. Pamoja na hayo Lushoto kuna majengo ambayo yapo tayari kwani kuna karakana ya seremala na jengo kubwa la gereji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri Serikali yangu iwawezeshe hawa wakaguzi wetu wa elimu Wilayani. Watu hawa wanapata taabu sana kwa kuwa hawapati bajeti yoyote hivyo kushindwa kufanya kazi zao za kutembelea shule na hii pia inachangia kushuka sana kwa elimu. Kwa mfano, Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde, kwa hiyo, Wilaya ile inahitaji miundombinu ya magari pamoja na mafungu ya rasilimali fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya na Jimbo la Lushoto kuna shule za msingi zaidi ya 90 na seondari 35 lakini shule hizi zinakabiliwa na changamoto za walimu hasa wa masomo ya sayansi pamoja na nyumba za walimu. Pamoja na hayo walimu wetu watengenezewe mazingira mazuri pamoja na kuwapa motisha pale wanapofanya vizuri, lakini pia Serikali iboreshe miundombinu ya shule zetu kwani shule zilizo nyingi zinahitaji kukarabatiwa pamoja na kujenga matundu ya vyoo yaliyojaa, na yaliyobomoka yafanyiwe ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haya maboma yanayojengwa kwa nguvu za wananchi, niiombe Serikali yangu ipeleke nguvu ya kumalizia majengo yake, pamoja na hizi maabara nyingia ambazo zimesimama kwa sababu wananchi wamejenga mpaka mtambaa wa panya yaani (kwenye lenter) na mengine yamepigwa mpaka na bati. Niombe Serikali yangu sasa imalizie maabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe Serikali ipeleke vitabu vya kiada na ziada kwa wakati kwani hii nayo ya kutokupeleka huduma hii kwa wakati kunasababisha kushuka kwa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu Tukufu, hili suala la chakula cha mchana ilichukue kwani wazazi walio wengi hawana uwezo na hii inasababisha wanafunzi hasa kwa wale ambao wazazi wao hawajachangia, hujisikia vibaya na kuathirika kisaikolojia, na kumsababisha mwanafunzi kutozingatia masomo anayofundishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Wizara, Waziri Mheshimiwa Ummy pamoja na timu yake yote kwa taarifa iliyosheheni na kukidhi kiu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Wizara ningeomba kujenga au kuboresha vituo vyetu vya afya nchini. Kwa mfano, Jimbo la Lushoto lina kituo cha afya kimoja tu ambacho kipo katika kata ya Mlola. Kituo cha afya hiki kiliahidiwa kupata huduma ya upasuaji lakini mpaka leo huduma ile haipo. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ipeleke huduma hiyo mapema ili kuzuia vifo hasa vya akina mama na watoto.

Pia niiombe Serikali yangu tukufu ipandishe hadhi zahanati ya Makanya kuwa kituo cha afya, pamoja na kujenga kituo cha afya katika kata ya Ngwelo kwani maeneo yote haya yapo mbali sana na huduma za afya ukizingatia hata miundombinu ya barabara ni mtihani, hali hii inasababisha vifo vya wananchi walio wengi pamoja na vifo vya akina mama na watoto.

Sambamba na hayo wananchi wamehamasika kwa kujitolea nguvu zao kwa kushirikiana na Mbunge wao, wameanzisha ujenzi wa vituo vya afya viwili ambavyo vipo maeneo ya Ngwelo na Gare. Hiki cha Gare kina vyumba kumi bado wananchi wanaendelea kujenga. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu tukufu ichukue majengo yale ili iweze kuyamalizia na wananchi waweze kupata huduma kwa ukaribu zaidi kuliko hii adha wanayoipata sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sabamba na hayo pia kuna zahanati zaidi ya 13, zipo kwenye hatua tofauti, nyingine zimeisha lakini hazina vifaa wala watumishi, nyingine zipo kwenye hatua za kufanyiwa usafi. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali yangu ipeleke watumishi katika zahanati zilizoisha na zile ambazo hazijaisha Serikali izichukue ili imalizie ili wananchi tusiwavunje moyo kwa kazi yao kubwa waliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kauli ya Serikali inavyosema kila Jimbo itajenga kituo cha afya kimoja, mimi katika Jimbo langu kituo hicho kijengwe katika kata ya Ngwelo kwani wananchi hawa ndiyo wanaopata taabu zaidi hasa katika kipindi cha mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu Wilaya ya Lushoto ina Majimbo matatu na yote hayo yanaangalia hospitali moja ya Wilaya na Hospitali ile ni ndogo inahitaji kupanuliwa hasa vyumba vya mama wajawazito, vyumba vya mama na watoto. Pamoja na hayo x-ray na ultra sound ni ndogo sana hazina uwezo, ndiyo maana inafanya kazi kwa muda mfupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu sasa ipeleke vifaa hivi ili hospitali iweze kutoa huduma inayoendana na kazi ya hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma hii ya afya ya uzazi na mtoto naiomba ifike vijijini hasa katika Jimbo la Lushoto wananchi wengi wanaishi ndani sana yaani vijijini mno. Kwa hiyo, naomba huduma hii ifike huko. Huko ndiko kuna wapiga kura wenye imani kubwa sana na Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niishauri pia Serikali yangu haya mafungu yapelekwe vijijini, mfano, hizi asilimia tano hazifiki kabisa vijijini. Pamoja na hayo katika Mikoa ambayo itapelekewa mafungu, Mkoa wa Tanga sijaiona, naiomba Serikali yangu iangalie Mkoa wa Tanga nao uwe kwenye list ya kupata fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu iweze kutoa ajira hasa kwa hawa maendeleo ya jamii, kwani hawa ni watu muhimu sana, wanahamasisha maendeleo vijijini kuliko ilivyo kuwa sasa ni wachache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niongelee suala la magari katika vituo vya afya pamoja dawa, vitu hivi ni muhimu sana kuwa katika vituo vyetu vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia elimu ya UKIMWI ipelekwe zaidi vijijini kwani bado mpaka sasa kuna maeneo ya vijijini hawajapata elimu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ambariki Rais wetu wa Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na timu yake yote kwa ujumla kwa hotuba yake nzuri inayoonesha matumaini makubwa na zana nzima ya Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika kuwa Wilaya ya Lushoto ni ya Wakulima wa matunda na mbogamboga, na ndiyo biashara inayoipatia Halmashauri mapato makubwa. Pamoja na hayo asilimia kubwa ya matunda yale na mbogamboga vinaoza kwa kukosa soko. Kwa hiyo, niombe pamoja na kuishauri Serikali yangu iwakumbuke wakulima wa Lushoto kwa kuwawekea kiwanda angalau hata kimoja tu ili mazao ya wakulima yasiharibike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika Tanga ni Mkoa wa Viwanda lakini viwanda vilivyokuwa Mkoa wa Tanga vyote vimekufa, mfano kiwanda cha nondo, kiwanda cha sabuni, kiwanda cha nguo, kiwanda cha katani, kiwanda cha Mkumbara, kiwanda cha mbolea, kiwanda cha chai cha Mponde kimefungwa mpaka leo. Wakulima wa chai wanapata tabu hawajui hatma ya kiwanda kile na maisha yao yamekuwa ya tabu mno na ukizingatia kiwanda kile hakina tatizo lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara ya mwisho Waziri alisema kiwanda cha chai Mponde ameshakikabidhi kwenye Mfuko wa Jamii (LAPF), lakini mpaka sasa Mfuko huu wa Jamii haujaonekana na wala hawajaonesha nia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba Mheshimiwa Waziri, uwafuatilie watu hao then utupe majibu ya kuaminika wawekezaji hawa watakwenda kufungua kiwanda kile. Pamoja na majibu hayo utakayoyatoa pia tungeomba ukayatoe wewe mwenyewe kwa wakulima wale kwani imefika hatua hawatuamini kabisa sisi viongozi wao. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu kiwanda kile mpaka sasa kina miaka minne sasa hakuna muafaka, leo tusipopata majibu ya kuridhisha tutashika shilingi juu ya hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Mwisho kabisa nimwombe Mheshimiwa Waziri, aikumbuke Tanga na aikumbuke Wilaya ya Lushoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja na timu yake kwa ujumla na hotuba yenye mtazamo chanya na iliyojaa matumaini mazima katika sekta ya utalii, pamoja na matumaini makubwa ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu Tukufu katika suala zima la upandaji miti katika maeneo yote yaliyozungukwa na misitu pamoja na watu binafsi. Sambamba na hayo, pia tuna misitu iliyoungua, kwa mfano, misitu ya Wilaya ya Lushoto, imeungua toka mwaka 1994, lakini mpaka sasa misitu ile haijaota tena. Kwa hiyo, naishauri Serikali ipande miti maeneo hayo ya misitu iliyoungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wakala wa Mbegu yaani TTSA na TAFORI. Wakala hawa ni muhimu sana, kwani hawa ndiyo watakuwa wakombozi katika kurudisha uoto wetu wa asili uliotoweka, lakini Mawakala hawa hawana mafungu ya kutosha, pamoja na vifaa vyao wanavyotumia ni vya zamani.

Kwa hiyo, naisisitizia Serikali yangu kama kweli ina nia ya dhati ya kupata miche kwa ajili ya kupanda miti katika nchi hii, basi wawape mafungu ya kutosha mawakala hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hawa TFS wanafanya kazi yao nzuri sana ya kuhakikisha misitu yetu haihujumiwi hovyo. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu iwawezeshe kwa vifaa vya kutosha, kama magari pamoja na ma-grader kwa ajili ya kuchimba barabara za msituni ili kurahisisha kupitika kwa haraka wakati wa majanga ya moto yanapotokea kuliko ilivyo sasa, tunategemea wananchi kuzima moto, pamoja na vifaa vya kuzimia moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wana mwamko wa kupanda miti, lakini wananchi wanapangiwa kuvuna miti yao waliyopanda wenyewe. Naiomba Serikali iitoe sheria hiyo, kwani inakandamiza wakulima wa miti. Hii imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwawezeshe vijana waliojiunga kwenye vikundi hasa katika Wilaya ya Lushoto, kuna vijana wamejiunga kwenye vikundi vya upandaji wa miti, lakini hawana support yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la utalii katika Wilaya ya Lushoto; kama unavyojua, Wilaya ya Lushoto ina vivutio vingi kama malikale, milima yenye vivutio, maporomoko (waterfalls). Pamoja na hayo, Wajerumani waliishi sana Lushoto. Kwa hiyo, Serikali ifuatilie na itambue vivutio hivi ili tusikose mapato, kama inavyofanyika sasa kienyeji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, wapo vijana wengi pale Lushoto wanaotembeza watalii. Naiomba Serikali yangu iwajengee uwezo na kuwatambua ili wasifanye kazi kienyeji na kuhakikisha mapato yanapita katika Serikali yetu pamoja na kuwajengea uwezo wa kuwaendeleza kielimu na kama siyo kufungua Chuo cha Kitalii Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama inavyojulikana, Lushoto ni eneo lililozungukwa na misitu ya asili na misitu ya kupandwa, lakini barabara ya kuingia Wilaya ya Lushoto ni moja tu. Kama ilivyo sasa hivi, mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja. Hii imepelekea uchumi wa Lushoto kurudi nyuma pamoja na Serikali kukosa mapato kwani magari yanayopitisha mbao hayapiti, watalii hawafiki Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna kilio kikubwa sana cha barabara katika Wilaya ya Lushoto. Kwa hiyo, Serikali lazima ichukue hatua za haraka kujenga barabara nyingine na mchepuo, ambayo inatakiwa ijengwe eneo la kuanzia Dochi kupitia Ngulwi hadi Mombo. Kwani ikijengwa barabara hii ya mchepuo itakuwa barabara mbadala na kumaliza tatizo la maliasili zetu kupita kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mgogoro wa Ngorongoro, naomba niishauri Serikali yangu kuwajengea wafugaji wale mabwawa, visima na malambo ili kunusuru uharibifu wa hifadhi zetu unaotaka kutokea. Pia naishauri Serikali yangu iunde WMA katika eneo la Loliondo na kuwa na sheria kali za kusimamia eneo lile, kwani kuna vyanzo vya maji vinaharibiwa siku hadi siku na mwisho wa siku wananchi na wanyama wetu wa porini watakosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tulinde, tutunze hifadhi zetu ili na sisi tuweze kurithisha kama waliopita walivyoturithisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kutumikia Watanzania hasa wanyonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu tukufu itoe ajira kwa Balozi zetu hasa wachumi, kwani inavyoonesha kwenye Balozi zetu wachumi ni wachache mno, hii itapelekea kukuza na kuitangaza nchi yetu kiuchumi katika mataifa ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna vijana wengi wanaomaliza Chuo cha Diplomasia lakini wanakaa kwa muda mrefu bila kupata ajira, ni ushauri wangu vijana hawa Serikali iwachukue kwa mkataba wa muda wakati huo huo wakiendelea kupata uzoefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu, kuna hawa wageni kutoka nje na wamekaa kwa muda mrefu na kuwekeza hapa nchini na wakati huo wanasaidia misaada mbalimbali. Mfano kujenga shule, kujenga zahanati na kujenga hosteli kwa njia ya kusaidia wananchi wanaoishi maeneo yanayowazunguka. Pamoja na hayo wafadhili hawa kwa sasa wamezuka na wanataka kurudi makwao, sababu ya kurudi kwao wanasema kwa sasa wamezeeka na pia kodi ya makazi ya kuishi nchini ni kubwa hivyo labda Serikali iwasaidie kupunguza fee hiyo au kuondoa kabisa kwa sababu bado wanaendelea kusaidia jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali watu hawa wangepewa uraia wa Tanzania ili waweze kusaidia jamii yetu, ukizingatia watu hawa wamechoka na wamezeeka.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais wetu, uzidi kumpa afya na nguvu na umzidishie umri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. SHABANI O. SHELIKINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hotuba iliyoko mbele yetu. Kwanza nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya kwani Watanzania wanaiona kazi yao kubwa lakini sisi hatuna cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu mwenyewe ndio atajua cha kuwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja kwenye ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Mimi niko kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, tulitembelea wakala wa kuuza vifaa vya ujenzi na ujenzi wa nyumba za bei nafuu. Kwa kweli inasikitisha sana kama kweli Serikali ina nia ya dhati kujenga nyumba za bei nafuu basi wawezeshe wakala wale, kwani wakala wale vifaa vyao wanauza bei nafuu sana, just imagine kigae kimoja kinauzwa Sh.500/= halafu ukiuliza unaambiwa bado wako kwenye utafiti. Kwa nini sasa Serikali isitenge mafungu ya kutosha kuwawezesha wakala wale ili wakasambaa kwenye mikoa hadi wilayani sambamba na hayo waendelee kufundisha vijana wetu ili waweze kupata elimu na kujiajiri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mtandao wa ILMIS. Huu mtandao ni mzuri sana lakini nimuombe Mheshimiwa Waziri Lukuvi huu mtandao usiishie Dar es Salaam tu, huu mtandao uende kwenye majiji makubwa kama Mwanza, Arusha, Tanga, Mbeya na majiji mengineyo hapa Tanzania, kwani mpango huu ni mzuri ambao utarahisisha kabisa hata ile kazi ya kupata hati au kubaini kiwanja cha mtu. Pia ikiwezekana nimwombe Mheshimiwa Lukuvi kwa heshima na taadhima mtandao huu hebu auzambaze kwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye upimaji wa ardhi. Kama Mheshimiwa Rashid Shangazi alivyosema kwamba Lushoto kuna uhaba sana wa ardhi na watu wa Lushoto wako tayari kupimiwa ardhi lakini wanapohitaji kupimiwa ardhi basi kunakuwa na figisufigisu nyingi sana. Nashindwa kuelewa tatizo liko wapi? Ukizingatia Wilaya ya Lushoto pamoja na kwamba ni ya milima, milima lakini ina watu wengi sana ambao wana uhitaji, wanahitaji hati ili waweze kukopa benki, wanahitaji pia na hati za kimila. Kwa hiyo tatizo liko wapi Mheshimiwa Lukuvi kwa wananchi wa Lushoto? Hivi kwa nini wanapata tabu kiasi hicho? Wanapohitaji kupimiwa au kupata hati inakuwa ni shida kubwa sana kiasi kwamba mpaka wawapigie watu magoti? Nashindwa kuelewa kwa ajili gani inakuwa hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo huyu mtu wa shamba, mwekezaji shamba la Mnazi, huyu mtu anasema ameishika Serikali kwa hiyo hatambui viongozi zaidi ya yeye na pesa zake. Kwa hiyo nimuulize Mheshimiwa Lukuvi tatizo liko wapi hapa na yeye ameshikwa? Eeh tunataka kujua kwa sababu mtu huyu anatusumbua sana kiasi kwamba sijui yeye anajiamini vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Lukuvi, nawaamini sana na dada yangu Mheshimiwa Mabula, naamini hii ni issue ndogo sana mpaka kesho naamini taarifa hii tutaipata. Tunataka mtu huyo tumjue ni nani na ana uwezo gani katika nchi hii? Mheshimiwa Lukuvi najua kazi yake, natambua uwezo wake naamini hili sasa limefika kwake sasa. Tunahitaji ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo wananchi wa Lushoto kama Mheshimiwa Shangazi alisema kwamba wanahitaji sana kupima ardhi lakini kunakuwa na tabu moja kubwa sana. Sasa sijajua kwamba pale hakuna vifaa au wataalam hakuna? Mheshimiwa Lukuvi mimi ndiyo maana nikampongeza sana kwa sababu naamini kazi yake na sidhani kabisa kwamba kazi hii itamshinda. Naomba sasa wananchi wa Lushoto waweze kupata hati kwa mapema na wapimiwe kwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Rais wangu kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuwatumikia wananchi hasa wale wanyonge. Pia nimpongeze Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na timu yake kwa hotuba yake nzuri iliyojaa matumaini makubwa yenye nia ya dhati na yenye kugusa na kuondoa kero zote za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri Serikali iwape fedha Wakala wauzaji wa vifaa vya ujenzi vya bei nafuu. Kama kweli Serikali inataka Watanzania wenye kipato cha chini wawe na uwezo wa kununua nyumba za bei nafuu. Basi tuwawezeshe Wakala wa vifaa vya Ujenzi. Pamoja na hayo, wakala wawe wanatoa elimu ya ufundi. Kwa hiyo, wakala wale wapewe uwezo ili wafike mkoani hadi wilayani kutoa elimu kwa vijana wetu wa Kitanzania ili vijana wetu wakishapata elimu waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niishauri Serikali yangu, iharakishe na kutoa mafungu katika Wilaya ili mafungu haya yaendane na kasi ya upimaji na upatikanaji wa hati kwa haraka. Kwa mfano, Wilaya ya Lushoto wananchi wapo tayari kupimiwa na kupewa hati lakini kuna ukiritimba katika idara ya ardhi. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri afuatilie hili suala katika Ofisi ya Ardhi Lushoto ili wananchi wangu wasinyanyasike pindi tu wanapotaka kupimiwa shamba na hao wananchi wameshajua umuhimu wa kupima ardhi na ukizingatia watu wanahitaji kupata mikopo kwenye mabenki. Pamoja na hayo kuna rushwa sana katika Idara ya Ardhi, maana wananchi wengi wametoa fedha zao ili wapate hati lakini fedha zinaliwa na hati hawapati. Naomba Mheshimiwa Waziri aondoe tatizo hili katika Wilaya ya Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu Tukufu ili migogoro katika nchi hii iishe ni kupima ardhi yote ya nchi hii. Naamini maeneo yote yakipimwa na kila mtu akamiliki ardhi kihalali migogoro hii itakwisha. Pia niiombe Serikali yangu itenge mafungu ya kutosha yaende katika kupima ardhi kuliko kutegemea wafadhili. Mheshimiwa Waziri nimependa sana zoezi lile linaloendelea katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilombero. Kwani ni mpango mzuri na wenye tija. Kikubwa wapewe mafungu ya kutosha ili kuharakisha zoezi lile. Pamoja na kuwaongeza wataalam ili kumaliza zoezi kwa haraka na ikiwezekana ifikapo 2020 Ardhi yote ya Tanzania iwe imeshapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja kwa asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/ 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijaalia afya njema na mimi niweze kuongea katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote nianze kumpongeza kipenzi cha Watanzania, mtetezi wa wanyonge, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Hii ni tunu tuliyopewa na Mwenyezi Mungu na kama huamini hilo au kama kuna wale ambao hawaamni hilo basi wangeangalia leo jinsi anavyotoa somo pale Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Waziri Mpango kwa kuja na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2018/2019. Na mimi nijikite katika kuchangia hususan katika kilimo. Hatuwezi kuzungumzia mapinduzi ya viwanda bila kuzungumzia mapinduzi ya kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo katika taifa hili, lakini mimi ninachoamini au nilichoona uti wa mgongo unaelezewa tu kwenye vitabu lakini sio kwa vitendo. Kama kweli tunataka twende kwenye mapinduzi ya viwanda ni lazima tuhakikishe kwamba tunaboresha kilimo chetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima walio wengi hapa nchini wanategemea jembe la mkono. Kwa hiyo, nimuombe sasa Mheshimiwa Mpango, hebu panga mipango yako mizuri sasa kuhakikisha kwamba unaweka mipango mizuri katika wakulima wetu hawa kuwawezesha ili waweze kulima kilimo cha kisasa na kuweza kuzalisha malighafi ambayo itasababisha kujenga katika viwanda vyetu. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kuna suala la maji. Maji ni uhai na Tanzania yetu hii bahati nzuri imezungukwa na miito na maziwa makubwa sana. Lakini kuna changamoto sana ya upatikanaji wa maji. Mheshimiwa Waziri Mpango sasa aje na mpango kabambe, naamini kabisa kwenye vitabu hivi kwa kweli mpango wake ni mzuri kuhusu maji lakini apeleke pesa za kutosha katika suala zima la maji kwa sababu maji ndiyo kila kitu. Ukizungumzia kilimo lazima uzungumzie na maji, kwa hiyo naomba sasa katika mpango wake Mheshimiwa Mpango ahakikishe anaandaa pesa za kutosha kupeleka kule kwa wakulima hususan katika suala zima la kujenga mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuingie kwenye suala la barabara. Barabara ndio uti wa mgongo, ndiyo uchumi katika taifa hili. Ili uchumi wa nchi hii ukue unahitaji barabara. Kwa mfano kule kwetu Lushoto, kuna barabara ambazo zinatakiwa kupandishwa hadhi lakini mpaka sasa ni miaka mitano barabara zile hazijapandishwa hadhi, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri huyu katika mpango wake huu basi zipandishe barabara zile hadhi. Kuna barabara ya kutoka Mlalo – Ngwelo – Mlola – Makanya – Mlingano hadi Mashewa ambapo barabara hii kwa kweli ni barabara ya kiuchumi endapo itafunguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala tena la barabara kutoka Mombo – Soni – Lushoto – Mlalo – Mlola, barabara hii ni nyembamba mno kiasi kwamba hata juzi mwezi wa nne tulipopata mafuriko kwa kweli wananchi wa Lushoto walipata taabu sana, walikaa zaidi ya wiki mbili bila kupata huduma za msingi. Kwa hiyo, nimuombe sasa Mheshimiwa Mpango katika mipango yake hii basi apange pesa za kutosha ili barabara ile iweze kupanuliwa. Pamoja na hayo kuna barabara za kupandisha hadhi ziweze nazo kupandishwa hadhi. Pia nimshukuru Dkt. Mpango au niishukuru Serikali yangu kwa kuja na TARURA, Mheshimiwa Dkt. Mpango nakuomba sana TARURA ni jambo zuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati kwa kuwasilisha hoja nzuri na zenye tija na Serikali ichukue hoja hizo na izifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia uti wa mgongo wa Taifa hili ina maana umezungumzia kilimo. Naomba niishauri Serikali iwekeze kweli kweli kwenye kilimo kwani ukizingatia zaidi ya asilimia 75 ni wakulima. Kwa hiyo Serikali ipeleke pesa za kutosha katika sekta hii ya kilimo na ukizingatia sekta hii ikikaa vizuri hata vijana wengi hawatakimbilia mijini zaidi ya kubaki vijijini na kuendeleza kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe inaweka miundombinu, hasa kujenga mabwawa ili wakulima walime kilimo cha umwagiliaji. Serikali iongeze Maafisa Ugani katika kila kata na kuwapa vitendea kazi pamoja na kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii ili waweze kuwapa elimu ya kilimo wananchi waliopo vijijini, ndiyo maana inafikia hatua wanauza ardhi ili wahamie mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukifanya hivyo hawatauza maeneo yao. Pia kuwapatia pembejeo wakulima kwa wakati hata wale wakulima wa mbogamboga na matunda, kwani hii tutakuwa tumeinua kilimo na wakulima hawa watalima kilimo chenye tija na kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Maji; ukizungumzia maji katika nchi hii kila mtu atakuunga mkono kwa asilimia mia moja, lakini yote haya yanafanywa na watendaji wetu ambao si waaminifu katika sekta hii. Kwa hiyo niishauri Serikali kuwe na Mamlaka ya Maji Vijijini kama ilivyokuwa TARURA. Hii itasaidia sana hata wale watendaji wetu wasiokuwa na nia nzuri na nchi yetu hawatapata nafasi tena ya kuchakachua miradi hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto kuna mito mingi sana inayotiririsha maji kutoka milimani na kuelekea baharini, lakini tukitumia kwa kujenga mabwawa hii itasaidia sana kwa wananchi wetu kupata maji safi na salama pamoja na kutunza vyanzo. Hata hivyo unakuta maeneo kama Lushoto kunakuwa na shida kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama na yapo maeneo mengi tu yenye mito na vyanzo vya kutosha lakini mito hii haitumiki ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi kusimama kwenye Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake kwa hotuba nzuri ambayo siku ile ya kusoma hotuba Watanzania wote naamini walikuwa kwenye luninga na kwenye redio kusikiliza hotuba na walifurahi mno. Kwa hiyo, hotuba hii kwa kweli imejibu kiu ya Watanzania hususan wale wa hali ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais wangu, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli kwa kazi anayoifanya kwani sisi katika upande wetu wa dini unasema kwamba Mwenyezi Mungu anapomchagua mtu wake anamtuma Jibril. Jibril anapeleka majibu kwa Mwenyezi Mungu kwamba Mwenyezi Mungu nimeleta jina la Joseph John Pombe Magufuli kwamba huyu ndiyo anakubalika kwa watu, Mwenyezi Mungu anaidhinisha. Mwenyezi Mungu anapoidhinisha anatuma malaika, malaika wanakuja kwetu sasa kusambaza kwenye mioyo ya wananchi kwamba mchagueni John Pombe Magufuli huyu ndiyo Rais wa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni tunu ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu ambaye hamuungi mkono Rais wetu kwa juhudi hizi anazozifanya, basi apimwe akili kwa sababu naamini kabisa huu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu, ameletwa na Mungu huyu. Kwa hiyo, kama mtu hatamuunga mkono tunaita ni kizazi cha shetani. Mara nyingi viongozi wazuri wanapofanya kazi vizuri basi wale ambao ni mlolongo wa shetani huwa wanapinga. Kwa hiyo, usione watu wanapinga ujue ni mlolongo wa shetani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niendelee kuchangia, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mpango na timu yake kwa ujumla hasa kwa kutoa hii tozo ya Road Licence. Hata hivyo, nimuombe tu sasa kwamba amekula ng’ombe mzima amebakisha mkia, kuna hii fire extinguisher na sticker zake ni kodi kandamizi ambayo kwa kweli naomba aiangalie na ikiwezekana nayo iondoke. Kwa sababu yeye mwenyewe naamini anakiri kwamba gari ikipata ajali ule mtungi wewe abiria, dereva au turnboy huwezi kuamka na kuzima gari ile au hao watu wanaokata sticker hizi za fire extinguisher hawawezi kuzunguka barabarani na kukuta gari inaungua na wakazima sijawahi kuwaona. Kwa hiyo, naona hii ni kodi kandamizi itolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna hawa vijana wetu wa bodaboda wameamua kujiajiri na hili ni kundi kubwa sana, nao ikiwezekana hii SUMATRA itoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa niende kwenye suala zima la viwanda. Nashukuru kwenye hotuba ya Waziri ameainisha mikoa ya viwanda ikiwemo Tanga lakini cha kushangaza Mheshimiwa Mpango kwenye hotuba yake anasema atatengeneza viwanda vipya wakati Tanga kuna viwanda vimekufa mfano Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Afritex na Kiwanda cha Foma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna Kiwanda cha Chai cha Mponde hakifanyi kazi na hapa lazima niseme, tumeongea vya kutosha, kiwanda kile hakina tatizo lolote ni kizima kabisa, kinaendelea tu kulipiwa bili za umeme. Wananchi, wakulima wa Mponde wanapata tabu sana. Imefikia hatua sasa hata ule mlo mmoja kwa siku hawaupati, hawapeleki watoto wao shule, hawana ada, hata bili ya umeme wameshindwa kulipa. Kwa hiyo, nimwombe Waziri Mpango kwa unyenyekevu na heshima kubwa aliyokuwa nayo atenge hata shilingi bilioni nne akafungue kiwanda kile ili tuweze kuokoa maisha ya wananchi wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala zima la maji. MWewe ni shahidi wakati unaniona nimevaa mabuti niko kwenye barabara ya Soni – Mombo - Lushoto, kumenyesha mvua nyingi mno. Nashindwa kuelewa nimeshaongea sana mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Wizara sasa ipeleke wataalam wa kutujengea mabwawa ili yatumike kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji cha mboga mboga na kuwapa wananchi maji. Vilevile mabwawa haya yatazuia uharibifu wakati wa mafuriko hata kama yatashuka, yatashuka kidogo sana. Niiombe Serikali hebu itenge fedha za kutosha ili ipeleke vijijini ili wananchi wa vijijini waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, hizi fedha zinazoenda Halmashauri kwa ajili ya maji naomba sasa mfumo ubadilishwe. Kuna watu wanaitwa DCCA wapewe kazi hawa au kuundwe Mamlaka ya Maji Vijijini, naamini hawa wataenda sawia kabisa na kuboresha huduma na kwenda kwa kasi zaidi ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zangu zimeharibika mno. Nimeomba kwa muda mrefu sana barabara ya kutoka Mlalo - Ngwelo – Mlola – Makanya - Milingano - Mashewa ipandishwe hadhi lakini mpaka sasa hivi bado haijapandishwa. Nimwombe Waziri Mheshimiwa Mpango ikiwezekana barabara ile sasa ipandishwe hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua barabara yetu ile inashuka matope na mawe, inafunikwa kutokana na mafuriko, kwa hiyo, ningeomba sasa tupate barabara mbadala. Kuna barabara inaanzia Dochi - Ngulwi - Mombo kilometa 16 tu, niiombe Serikali yangu tukufu, sikivu iweze kunisaidia barabara ile ili wananchi wangu wa Lushoto wasiishi kisiwani. Pamoja na hayo, Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kilometa nne, nizikumbushie kwa Waziri Mheshimiwa Mpango aweze kutupa hizo kilometa ili tuweze kutengeneza Mji wetu wa Lushoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la vituo vya afya, wananchi wangu nimewahamasisha wamejenga vituo vya afya zaidi ya vinne, vimefikia hatua ya lenta lakini kama ilivyo ada Serikali imesema kwamba wananchi wakijenga ikifikia hatua ya lenta basi Serikali inachukua. Kwa hiyo, niombe Serikali sasa nimeshafikisha hatua ya lenta hebu wanipe pesa ili niweze kumalizia vituo vile ili wananchi wangu waweze kupata huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, usambazaji umeme vijijini. Nishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ina kasi sana ya kusambaza umeme vijini lakini imetoa vijiji vichache sana. Niiombe sasa Serikali yangu, sisi tumeshaahidi kule kwamba jamani umeme unakuja kama Ilani ya chama inavyosema, sasa unapopata vijiji hata 10 havizidi sijui tutawajibu nini wananchi wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, milioni 50…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunijalia afya na nguvu na mimi niweze kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya kwani mwenye macho haambiwi tazama. Pia nimshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ndugulile na watendaji wote, kwani kazi wanayoifanya Watanzania hakika wanaiona. Mimi naamini hakuna cha kuwalipa ila Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiyo atajua cha kuwalipa ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye vituo vya afya. Kwanza nimshukuru Waziri, Serikali yangu tukufu kwa kunitengea shilingi milioni 700 kwa ajili ya Kituo cha Afya Mlola, sasa hivi naamini mambo ni mazuri kabisa, tumetengewa shilingi milioni 700 kwa maana hiyo shilingi milioni 400 kwa ajili ya majengo na milioni 300 kwa ajili ya vifaa tiba, kwa hiyo naishukuru Serikali yangu Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Lushoto, Halmashauri ya Lushoto, Jimbo la Lushoto lina kituo cha afya kimoja tu ambacho kiko Mlola. Kwa hiyo, kituo kile hakitoshelezi kabisa mahitaji ya wananchi. Kwa hiyo, niiombe sasa Serikali yangu kwa kuwa wananchi wa Gare, wananchi wa Ngwelo wamejitahidi wenyewe wamejenga vituo vya afya mpaka kufikia mtambaa wa panya na majengo mengine yamepauliwa, niiombe Serikali sasa safari hii itenge pesa za kutosha kwa ajili ya kumalizia vituo vile kwa maana ya Kituo cha Gare na Kituo cha Ngwelo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo, hospitali yetu ya Wilaya imeelemewa. Wilaya ya Lushoto ina takribani Majimbo matatu, Halmashauri mbili, kwa maana ina wakazi zaidi ya 600,000, ultra sound na x-ray ya Lushoto ni ndogo sana haikidhi mahitaji. Kwa hiyo, tunakosa wananchi wengi sana pale, wanapoteza maisha kwa sababu ya x-ray ile ni ndogo sana, ikihudumia watu watano tu inakufa. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu tukufu na sikivu ipeleke x-ray yenye uwezo ili kuweza kuhudumia wananchi wale, hususan kuokoa maisha ya mama na mtoto pamoja na wananchi wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, gari la wagonjwa niiombe Serikali, Mheshimiwa Ummy anajua kwamba Wilaya ya Lushoto jiografia yake ni mbaya sana, ni ya milima na mabonde. Kwa hiyo, chondechonde, kwa kweli hali ni mbaya. Juzi nikiwa niko Jimboni nilishuhudia vifo vya akina mama watatu wamekufa kwa ajili ya kifafa cha mimba kwa sababu ya kukosa usafiri kufika katika Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, nimuombe dada yangu Mheshimiwa Ummy, naomba Land Cruiser, siyo vile vigari vidogo maana naamini anajua barabara za kwetu, nimuombe atupatie Land Cruiser ili kuweza kuhudumia hususan wananchi wa Mlola, Makanya, Bwelo, Mlalo, Mbwei, Malibwi pamoja na Kwai. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala zima la walemavu. Kule kwetu ni vijijini mno kiasi kwamba walemavu hawapati huduma. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa ipeleke hususan vifaa kwa walemavu hususan walioko vijijini, hasa kule Lushoto maeneo ya Makanya, Mavului, Manolo pamoja na Mbwei, kwani ukiangalia hali halisi ilivyo takwimu zinazoletwa na wataalam kutoka Halmashauri ni potofu siyo sahihi, kwa hiyo niiombe Serikali yangu sasa ipeleke vifaa vya kutosha hususan vya walemavu katika maeneo yale ya Lushoto.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Kwanza kabisa nimpongeze Waziri Mheshimiwa Dkt. Kalemani, Naibu wake, dada yangu Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kazi anayoifanya, lakini pamoja na timu yao yote, wanafanya kazi kubwa sana kwa kweli mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye mada moja tu, hususan katika kutaja vijiji vyangu vyote ambavyo havina umeme, pamoja na shule, pamoja na zahanati. Ni imani yangu kubwa kwamba Mheshimiwa Kalemani alifika Lushoto na akatoa maelekezo kwa Wakandarasi, lakini Mkandarasi yule, bado hajatekeleza ahadi ya Waziri mpaka leo. Sasa kwa kuwa leo timu nzima leo ipo hapa basi nami nianze Kijiji kimoja baada ya kingine ili wataalam wake wakusaidie kusukuma mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na vijiji ambavyo havina kabisa umeme katika Jimbo la Lushoto ambavyo ni Vijiji vya kwanza Miegeo, Handei, Ngulwi, Kwemashai, Gare, Yamba, Kongei, Masange, Makanka, Milungui, Kireti, Kigumbe, Bombo Kamgobore, Kilole, Mazumbai, Ntambwe, Mavului, Mazashai, Mdando, Kweulasi, Bombo, Kwetango, Mbwaya, Kigulunde na Kwai. Hivyo ni vijiji kabisa ambavyo havina umeme kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vinavyofuata ambavyo ni vya kujaziliza ni Vijiji vya Chumbageni, Ngulwi, Kizara, Yoghoi, Magamba, Kilangwi, Kwemashai, Boheloi, Migambo, Kwefingo, Kwemakame, Malibwi, Mbwei, Mshangai, Makole, Mlola, Ungo na Mhezi.

Mheshimia Naibu Spika, nimeamua kuyataja maeneo yangu kwa sababu Mheshimiwa Waziri alikuwa kila siku ananiambia nimletee orodha, kwa hiyo leo nimeamua kutaja orodha hii moja kwa moja kwa sababu wataalam wake wote wapo, basi waichukue na waendelee kumsukuma sana yule Mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na sekondari ambazo hazina umeme ni Sekondari za Balozi Mshangama, Masange, Gare, Mkuzi, Kwai, Kwekanga, Mariam Mshangama, Makole, Mdando, Kweulasi na Mazashai. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo bila kupumzika niendelee na Vituo vya Afya na Zahanati. Kituo cha Afya Gare, Zahanati ya Makanka, Kituo cha Afya Ngwelo ambayo ni Kigulunde, Zahanati za Miegeo, Mavului, Mazumbai, Mbelei, Kweulasi na Mdando. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyafanya hayo, maana nimechoka kuandika na hansard nayo ichukue ili Waziri akihitaji basi atachukua tu kiurahisi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyataja hayo maeneo yote hayo lakini kila eneo nililolitaja hapo lina shule, lina Msikiti na Zahanati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipongeze Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hasa kwa Waziri na timu yake yote kwa hotuba yao nzuri ambayo imejaa matumaini makubwa ya Watanzania hasa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Wizara kwa kupunguza tozo hasa kwenye zao la kahawa. Serikali kutoa tozo 17 siyo kitu cha mchezo. Sambamba na hayo, Wilaya ya Lushoto inalima kahawa na kutoa tani zaidi ya 300 kipindi cha nyuma, lakini sasa hivi ni tani 40 tu ndiyo zinazopatikana. Hii yote ni kulitupa kabisa zao la kahawa ambalo linaipatia Serikali pesa za kigeni na zao hili Wilaya ya Lushoto limeonekana ni zao ambalo linalimwa na wazee tu na siyo vijana, yote hayo ni kutowawekea vijana miundombinu mizuri na kuhamasisha kupenda kahawa na zaidi vijana kukimbilia mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo Idara ya Kilimo ilikuwa inapanda miche ambayo walikuwa wanaipata au kununua TACRI N39, miche hii inakaa muda wa miaka mitatu inazaa na kila mbuni wa mbegu hii unatoka kilo tatu lakini Idara ilishindwa kutokana na ukosefu wa fedha. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu itoe tamko katika Halmashauri zile pesa za kahawa wanazotoza ushuru wazirudishe zinunue miche ile ili kuokoa zao la kahawa linalokufa katika Wilaya ya Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kutenganisha Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Ujenzi. Kule Lushoto kuna mvua nyingi zinazoendelea kunyesha na zimeleta madhara makubwa na kuharibu miundombinu ya barabara pamoja na madaraja kuvunjika. Hivyo, kusababisha mpaka sasa hivi ninavyoandika mchango wangu huu mazao ya wakulima yanaozea shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niishauri Serikali yangu itoe pesa za dharura ili kwenda kutengeneza barabara zile ili wananchi wasiendelee kupata hasara ya mazao yao maana ukitegemea Halmashauri zetu hazina pesa za kutengeneza barabara zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo kuna barabara ya mchepuo ya kuanzia Dochi – Ngulwi hadi Mombo barabara ile niliisemea sana kuwa iwe mbadala lakini mpaka leo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na kama ingetengenezwa kusingekuwa na upatikanaji wa hasara ya mazao ya wakulima. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu itengeneze barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wakulima wa chai Mponde, takribani miaka minne sasa kiwanda kile cha chai kimefungwa, kwenye hotuba inaonesha kiwanda kile kimepewa mfuko wa jamii (LAPF) lakini mpaka sasa mfuko huo umefika mara moja tu kuona kiwanda kile. Kwa heshima na taadhima naiomba Serikali yangu hasa Waziri wa Kilimo aende Lushoto eneo la Mponde ili akaone wakulima wanavyonyanyasika na chai yao. Wakulima wale wamefikia kula mlo mmoja kwa siku na kushindwa kulipa mpaka bili za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mbogamboga; kilimo hiki kimetupwa pembeni kabisa wakati kilimo hiki ndicho kinachochangia mapato makubwa katika Halmashauri. Naishauri Serikali yangu iwaandalie wakulima hawa miundombinu ili waweze kulima kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, mvua hizi zinazoendelea kunyesha kungejengwa mabwawa yangenufaisha wakulima wetu na kulima kilimo chenye uhakika na chenye tija kuliko ilivyo sasa, mvua zinaendelea kuharibu miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niishauri Serikali yangu ifufue kiwanda cha mbolea Tanga ili kuwezesha mbolea kupatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu. Naishauri Serikali yangu ipeleke Benki ya Wakulima Mikoani hadi Wilayani kwa sababu huko ndiko kwenye wakulima au wahitaji kuliko Benki hiyo kuwa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri pamoja na team yake yote kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto ni eneo lenye milima na mabonde mengi na kwa hiyo tuliomba mnara kwa ajili ya kupata matangazo ya Redio ya Taifa yaani TBC. Hivyo basi tunaomba mnara huo ujengwe haraka. Pamoja na kwamba Serikali imetuahidi kutujengea mnara katika maeneo ya Kwebusani katika Kijiji cha Kwemashai, na tuliambiwa ujenzi huo umeanza lakini mpaka sasa bado ujenzi huo haujaanza. Naomba tufanyiwe haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba kuna vijana wengi sana ambao wana vipaji mbalimbali hasa katika michezo, sanaa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Lushoto ina vijana wengi ambao ni wachezaji wa mpira wa miguu. Cha kusikitisha vipaji vya vijana vinapotea bure na Serikali kupoteza nguvu kazi ya vijana hao. Hivyo basi niiombe Serikali ijenge chuo cha michezo katika Wilaya ya Lushoto pamoja na kiwanja hata kimoja tu. Sambamba na hilo kuna hawa vijana ambao ni wanasanaa na utamaduni. Lushoto ni Wilaya ambayo imebarikiwa kwa vipaji mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu Tukufu itume wataalam kwenda vijijini na wilayani kwa nia ya kwenda kuwabaini vijana wenye vipaji na kuwapa au kuwajengea uwezo ili waweze kutoka vijijini na kuwaleta mjini na kuwapa msaada ili nao waweze kujiajiri. Kama inavyojulikana kuwa michezo ni ajira, kwa hiyo tukiwasaidia vijana hawa Serikali itakuwa imepunguza asilimia kubwa sana ya tatizo la ajira hasa kwa vijana wetu hawa wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuwekeza katika michezo kuanzia shule za msingi hasa kwa kupeleka vifaa vya michezo katika shule zetu. Sambamba na hayo niiombe Serikali itoe VAT katika vifaa vya michezo ili vijana wetu waweze kumudu gharama za kununua vifaa hivyo vya michezo, kwa sababu ukizingatia Tanzania imeamka sana katika tasnia hii ya sanaa na michezo. Ni imani yangu kubwa kuwa tukiwatumia vizuri wasanii wetu hawa tutakuwa tunaingiza pesa nyingi hasa kwa kuwatumia kutangaza utaliii wetu nje na ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe Serikali kuwasimamia wasanii wetu ili wasidhulumiwe na matajiri ambao hawana nia nzuri na wasanii wetu. Msisitizo, tunaomba mnara wa Lushoto ufanyiwe bidii ili uweze kuisha haraka kwa sababu tumechoka kusikiliza redio za Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yake yote kwa ujumla kwa kazi nzuri na hotuba nzuri yenye mtazamo wa kukidhi na kufikia matarajio ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kuchangia katika suala zima la maji hasa vijijini. Hakuna asiyefahamu kuwa Lushoto ni Wilaya ya milima na mabonde na yenye vyanzo vingi vya maji; lakini tunu ile tuliyopewa na Mwenyezi Mungu hatuitumii ipasavyo, tena ndio sehemu kubwa ya wananchi wanaokosa maji. Kuna tatizo kubwa sana la maji katika Kata za Makanya, Mbwei, Kilole, Ngwelo, Malibwi, Kwekanga, Kwai, Migambo, Ubiri, Gare, Ngulwi, Kwemashai.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote haya yana uhaba mkubwa wa maji na ukizingatia maeneo yote haya yana vyanzo vikubwa vya maji, lakini Serikali haijapeleka hata nguvu za kusaidia wananchi hao, kwani kilio chao ni cha muda mrefu sana. Pamoja na kuleta suala hili katika Ofisi za Wizara ya Maji lakini mpaka sasa hatujatengewa pesa yoyote ya maji vijijini na katika Jimbo langu sijawahi kupewa hata mradi mmoja mkubwa, zaidi ya kurukwa kila mwaka. Kwa hiyo, naomba Serikali yangu Tukufu itufikirie watu wa Jimbo la Lushoto na sisi tuweze kupata maji kama wenzetu wa maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, naishukuru Serikali yangu Tukufu kwa kunitengea shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya maji katika Mji wa Lushoto, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naungana na wenzangu kwa hoja ya kuongeza tozo ya mafuta ya sh.50/= ili iwe sh.100/= kwa kila lita ya mafuta, kwani hii itapelekea upatikanaji wa maji kwa haraka kwa wananchi wetu. Pamoja na hayo, Serikali iweke msisitizo katika Halmashauri zetu na ufuatiliaji madhubuti kuhakikisha wanatenga pesa hizi za vyanzo vya ndani ili pesa hizo nazo ziweze kusaidia maji vijijini kuliko ilivyo sasa, kwani Halmashauri nyingi zinadharau mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali yangu Tukufu kujenga mabwawa kwa ajili ya kusaidia wakulima pamoja na wafugaji. Kama nilivyosema, mvua nyingi sana zinanyesha katika Wilaya ya Lushoto, lakini maji yale yanaharibika na kuleta maafa pamoja na kuharibu miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali yangu Tukufu baada ya kuyaachilia maji haya ya mvua kwenda kuharibu miundombinu, tujenge mabwawa ili maji haya yaweze kusaidia wananchi. Sambamba na hayo, katika Vijiji vya Wilaya ya Lushoto kuna maeneo ambayo mpaka sasa wananunua ndoo ya maji sh.500/= hadi sh.1,000/=. Vijiji hivyo ni vya Kwemakame, Kweulasi, Mbwei, Kilole, Mshangai, Malibwi, Handei, Miegeo, Kizara, Masange, Kongei na Gare.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu, katika bajeti ya mwaka huu nitengewe pesa kwa ajili ya vijiji hivi. Kama unavyojua, tuliwaahidi wananchi tena kwa kujigamba kwa kujiamini kwamba mkinichagua mimi pamoja na Rais wa Chama cha Mapinduzi tatizo la maji tutalimaliza, lakini mpaka sasa naulizwa na wananchi kuhusu maji, nakosa majibu ya kuwapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niihakikishie Serikali yangu Tukufu, wananchi wanayo imani kubwa sana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ninachokiomba kwa heshima na unyenyekevu mkubwa katika Wizara hii initengee pesa ili nikamalizane na wananchi wangu hawa, pamoja na kuendelea kujenga imani kwa wananchi na viongozi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali yangu kuhusu hawa Wahandisi walio wengi, hawafanyi kazi kwa weledi, kwani hawa ndio wanachangia kurudisha nyuma miradi hii kwa kutosimamia vizuri. Kwa hiyo, wataalam hawa ambao hawana uwezo wasimamiwe na Mainjinia wa Mikoa ili kusukuma miradi hii ya maji kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 nami ndiyo nitakuwa miongoni mwa Wabunge watakaoipitisha bajeti hii kwa kusema ndiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Lushoto lina zaidi ya shule za msingi 33 nasekondari 26 za Serikali, lakini katika shule hizi kuna changamoto nyingi kama:-

(i) Ukosefu wa nyumba za walimu wa shule ya sekondari na msingi;

(ii) Ukosefu wa hostel katika sekondari zetu;

(iii) Fedha za ukarabati wa shule za msingi za Kilole, Kwemashai, Malibwi, Kwembago, Ngulwi, Ubiri, Milungui, Kwemakame na Yogoi;

(iv) Kumalizia maabara zilizojengwa kwa nguvu za wananchi;

(v) Upungufu wa walimu wa shule ya msingi na sekondari;

(vi) Walimu kutolipwa posho zaonakuwekewa miundombinu rafiki;

(vii) Watumishi kutopandishwa madaraja; na

(viii) Ukosefu wa fedha za kumalizia maboma yote ambayo hayajakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niipongeze Wizara ya Fedha kwa hotuba yao nzuri iliyojaa matumaini makubwa. Naomba niishauri Serikali katika suala zima la road license, ni ukweli usiopingika kwamba Serikali inatakiwa ikusanye mapato ya kutosha ili nchi iweze kujiendesha yenyewe, lakini mimi kama Mbunge nimegundua tunakosa mapato mengi kwa kulipia kila gari, ikizingatia magari mengi yamekufa na mengine yamekatwa skrepa, Serikali inayavizia iyaone barabara ili yakamatwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa ukusanyaji huu tutakuwa tunapoteza mapato mengi sana. Niishauri Serikali iongeze hata shilingi tano kwenye kila lita ya mafuta, ukipigia hesabu ya kila gari kwa mwaka itakuwa imelipia fedha nyingi sana, itakuwa mara kumi ya ukusanyaji huu unaotumika sasa, kwa kufanya hivyo Serikali itagundua ilikuwa inapoteza fedha nyingi sana kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali yangu kuhusiana na TRA. Kila TRA hasa za Wilaya zipandishwe hizi ziwe zinatoa huduma zote mfano TIN namba road licence.

leseni za udereva, motor vehicle na kadhalika. Serikali ikifanya hivi itaongeza mapato mara dufu kuliko ilivyokuwa sasa ukizingatia wananchi walio wengi wanaishi vijijini, anaona ngumu kwenda kukata leseni mkoani hivyo yupo tayari aendeshe chombo cha moto kwa kujificha ili mradi asitumie gharama kwenda kutafuta vitu hivyo. Kwa hiyo, Serikali imekosa mapato kwa kutopeleka huduma karibu na wahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu wafanyabiashara. Mfanyabiashara anakadiriwa mapato wakati hata hajafungua biashara. Niishauri Serikali ishawishi watu wafungue biashara kisha baada ya mwaka ndipo anafanyiwe makadirio kama sheria inavyosema. Sasa hivi TRA na wafanyabiashara ni kama maadui wakati Maafisa hawa wanatakiwa wawape elimu wafanyabiashara ili Serikali iweze kupata mapato au kukusanya mapato mengi zaidi kuliko ilivyokuwa sasa Maafisa wa TRA wanawatisha mno wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mashine za EFD, mashine hizi hazitumiki kama ipasavyo hasa katika Halmashauri zetu, kuna wizi mkubwa sana unafanyika katika Halmashauri baadhi kwani watendaji wengi wa Halmashauri wanatoa maelekezo kwa maafisa wanaokusanya ushuru kuwa kuna sehemu za kutumia risiti za EFD na sehemu nyingine wanatumia manual, hii inasababisha upotevu wa makusanyo na kuitia Serikali hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika Halmashauri nyingi hapa nchini hasa zile zinazotiliwa mashaka zifanyiwe ukaguzi wa mara kwa mara (special auditing), mfano Halmashauri yangu Lushoto inakusanya mapato mengi lakini mwisho wa siku unaambiwa mapato yameshuka. Mimi kama Mbunge napata mashaka sana na kama mnavyojua Halmashauri ya Lushoto ina wakulima na wafanyabiashara wengi, haingii akilini ukiambiwa kwa mwaka Halmashauri imekusanya asilimia 38 tu wakati huo unaona kuna vitu vya hovyo vinafanyika bila kufuata taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Halmashauri ya Lushoto ikafanyiwe special auditing, mimi kama Mbunge nimeliona hilo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjaalie afya njema na umzidishie umri ili aendelee kuwatumikia Watanzania hasa wanyonge wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SHAABANI D. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hoja ya Katiba na Sheria kwa asilimia mia moja. Pia nampongeza Waziri Mheshimiwa Balozi Dkt. Mahiga na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Lushoto ina Majimbo matatu na Halmashauri mbili, na jiografia yake ni ya milima milima na mahakama zilizopo ni chache mno ambazo hazikidhi huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu itujengee Mahakama za Mwanzo hasa katika maeneo ya Malibwi na Ngwelo. Pamoja na maeneo hayo ambayo hayana mahakama, kuna mahakama ambazo zinahitaji ukarabati. Mfano, Mahakama ya Gare na Mahakama ya Mlola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Gare pamoja na kuomba kukarabatiwa, pia haina watumishi, wakati Mahakama ya Gare ilikuwa inafanya kazi, lakini nilishangaa mahakama ile imefungwa, kuuliza sababu nikaambiwa hakuna watumishi. Mahakama ile inasaidia zaidi ya kata nne, yaani Kata ya Kwemashai, Gare, Migambo, Kwai, Kata jirani ya Baga na Malibwi. Kwa hiyo, kufungwa kwa mahakama hii imesababisha usumbufu mkubwa sana kwa wananchi hao. Naiomba Serikali irudishe huduma hii haraka pamoja na ukarabati wa haraka ili wananchi wasipate usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo. Pia niiombe Serikali yangu Tukufu itoe ajira kwa watumishi katika mhimili huu wa mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mahakama hizi zote mbili hazina vifaa kama photocopy machine, computer kwa ajili ya kurudufu nakala za hukumu na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya ya Lushoto ni ya zamani sana, kwa hiyo, niiombe Serikali yangu kama siyo kukarabati basi kujengewa mahakama nyingine ili na sisi wananchi wa Lushoto tuwe na mahakama ya kisasa na inayoendana na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Wilaya ya Lushoto tuna bahati ya kuwa na Chuo cha Mahakama Lushoto (IJA), lakini wananchi walio wengi hasa wa vijijini wanadhulumiwa haki zao na kutokana na wananchi hawa kutojua sheria. Sasa basi niiombe Serikali yangu Tukufu kwa kuwa tuna Chuo cha Mahakama, niiombe Serikali yangu wakati wanafunzi wanakwenda field basi waende vijijini hasa katika Vijii vya Lushoto ili wananchi wa Lushoto waweze kufaidika na fursa ya kuwa na Chuo cha IJA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia kuwe na dawati la kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wa Lushoto na elimu hiyo itolewe na Uongozi wa Chuo cha Mahakama (IJA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais wetu Dkt. John Joseph Magufuli.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Waziri Mpango pamoja na timu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia mapinduzi ya viwanda pia hutoacha kuzungumzia mapinduzi ya kilimo. Niishauri Serikali yangu ipeleke wataalam wa kutosha katika sekta nzima ya kilimo kama Maafisa Ugani pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii washirikiane kuhakikisha kuwa wanatoa elimu yenye tija kwa wakulima wetu pamoja na Serikali kupeleka pembejeo na mitaji kwa walengwa ambao ni wakulima kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya ni kutaka kuboresha kilimo chetu ili kuwezesha malighafi nyingi zitoke kwenye kilimo ambazo zitatumika katika viwanda vyetu kuliko kutegemea malighafi kutoka nje. Pia katika viwanda vyetu Serikali ihakikishe inasimamia viwanda vyetu vizalishe bidhaa bora zenye viwango kuhakikisha tunashindana na ubora wa masoko ya ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ndiyo njia kuu pekee ya kiuchumi. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu Tukufu ipeleke fedha za kutosha na kuhakikisha barabara zinaunganisha Mikoa hadi Mikoa na Wilaya hadi Wilaya. Pamoja na barabara hizi muhimu ambazo ndiyo zinazotoa malighafi kutoka vijijini, Serikali ipeleke pesa za kutosha na kuwa na usimamiaji wa karibu kwa kuhakikisha zinapatikana kwa mwaka mzima kuliko ilivyo sasa hasa barabara za Jimbo la Lushoto zimeharibika sana. Kwa hiyo, niiombe Serikali katika Mpango wake huu iangalie kwa jicho la huruma barabara za Lushoto ili wakulima wetu mazao yao yasiozee shambani kama ilivyokuwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila afya hakutakuwa na maendeleo katika sekta zote hapa nchini. Wananchi wengi wameitikia wito wa kujitolea kujenga zahanati pamoja na vituo vya afya, lakini Serikali haipeleki mafungu kwa ajili ya kumalizia majengo hayo. Niishauri Serikali yangu ipeleke pesa za kutosha ili majengo yale yaweze kukamilika na Watanzania waweze kupata afya njema na kuweza kulitumikia Taifa lao. Hii iende sambamba na kupeleka vifaa vyote vya afya ili kupunguza mlundikano mkubwa katika hospitali zetu za Mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo kila kitu katika maisha ya binadamu. Kwa hiyo, niiombe Serikali katika Mpango wake huu wa mwaka 2018/2019 ihakikishe inamalizia maabara zote ambazo zimeanza kujengwa bila kumaliziwa pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa, kujenga vyoo pamoja na kujenga nyumba za walimu na elimu hii iendane na kujenga vyuo vya VETA kila Wilaya. Wilaya ya Lushoto tokea mkoloni hakujawahi kujengwa Chuo cha VETA. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango katika awamu hii naomba utenge pesa za kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia mazingira tuwe tunahakikisha tunapanda miti nchi nzima pamoja na kusimamia sheria kikamilifu ili wananchi wetu wawe wanatunza vyanzo vyetu vya maji na Serikali ihakikishe inawawezesha wananchi kwa kuwapatia miche ili wapande
katika mashamba yao. Kwa mfano, katika Jimbo la Lushoto kuna misitu imeungua moto lakini kuna kikundi cha vijana kinaitwa Friends of Usambara mpaka sasa kina miche zaidi ya milioni 10 na wao wenyewe wameamua kupanda miti katika maeneo yote ya misitu yaliyoungua. Kwa hiyo, niishauri Serikali iweze kusaidia vikundi kama hivi ambavyo vipo hapa nchini na vikundi hivi ikisimamiwa vizuri tutarudisha uoto wetu wa asili uliopotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoanzishwa TARURA, niishauri Serikali ije na mpango wa kuanzisha pia wa Wakala wa Maji Vijijini na Serikali ipeleke kwa wakati umeme vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Lushoto ina wasanii wengi mno, lakini wasanii wale hawajulikani kwenye tasnia ya vyombo vya habari na ukiangalia Serikali pamoja na kupoteza mapato mengi ya kuchangia Taifa letu unakuta tunazikosa, lakini pia wasanii hawa kupoteza taaluma yao na mwishowe hujiingiza kwenye mambo ambayo hawana fani nayo na kupoteza mwelekeo wa maisha yao. Kwa hiyo niishauri Serikali yangu tuwawekee miundombinu rafiki ili tusipoteze vipaji vya wasanii hawa kwani mwisho wa siku Taifa letu litaongeza mapato kupitia wasanii wetu hasa wasanii wa Lushoto.

Mheshimiwa Spika, pia Wilaya ya Lushoto ina vijana wengi wana vipaji vya mchezo hasa mpira wa mguu, lakini pia kuna changamoto kubwa ya kiwanja cha mchezo. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu itujengee uwanja wa michezo katika Jimbo la Lushoto ili tuweze kuwapata kina Mesi kutoka Lushoto. Pamoja na hayo niishauri Serikali yangu hasa Waziri mwenye dhamana, michezo ifundishwe mashuleni ili kubaini vipaji toka mashuleni.

Mheshimiwa Spika, najua upo UMISHUMTA na UMISETA, hii haitoshi, kuwe na ratiba ya vipindi katika shule zetu. Pia, niiombe Serikali yangu hasa Waziri mwenye dhamana wakati wanawatafuta wachezaji hasa hawa wa chini ya miaka 17 waende mpaka wilayani kwani kuna wachezaji wazuri mno wanakosa tu kuonekana katika vyombo au hakuna wa kuwasemea.

Mheshimiwa Spika, Redio ya Taifa ni shida katika Wilaya ya Lushoto. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu itujengee mnara wa TBC 2 ili wananchi wa Lushoto waweze kupata mawasiliano ya matangazo ya habari kuliko ilivyokuwa sasa. Booster imefungwa kwenye mnara wa redio, kwa hiyo kusababisha usikivu wa TBC kuwa mdogo yaani usikivu hauendi mbali na kama tunavyojua TBC ndio redio yenye uhakika wa taarifa zake.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nisisitize kuwekewa mnara wa TBC ni muhimu mno hasa kwa maslahi ya wananchi wa Lushoto.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niipongeze Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kuwasilisha vyema. Pia niishauri Serikali ichukuwe taarifa yote ya Kamati na kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wimbi kubwa sana la migogoro ya ardhi hapa nchini; na migogoro hii itaendelea kama tu Serikali haijachukua hatua za haraka juu ya suala zima la kupima ardhi katika maeneo yote ambayo ni mipaka ya ardhi ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi na wafugaji na watu binafsi wenye mashamba au viwanja kuvamia maeneo ya watu hasa wale ambao hawana uwezo. Kwa hiyo niishauri Serikali yangu Tukufu kuharakisha mchakato huu hasa kwa kupeleka fedha za kutosha na kwa wakati ili maeneo yote yapimwe na kuanishwa ili makundi yote hayo yatambue mipaka yao hasa kwa kuweka mawe ya mipaka (beacon).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuajiri watumishi wa kutosha kwani kwa sasa Wizara ina watumishi wachache sana ambao hawakidhi mahitaji ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kupima miji na majiji kwa vile vifaa vya kisasa ambavyo vimetumia Satellite, hivi vifaa visambazwe kwa kasi vifike mpaka kwenye wilaya kuliko ilivyo sasa ambapo vipo tu kwenye baadhi ya majiji kwani hii itafanya wananchi wapate hati kwa haraka kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Misitu. Maeneo mengi hapa nchini hayana miti ya kutosha na kuna maeneo mengine hayajapandwa miti kabisa. Naomba niishauri Serikali iwape pesa za kutosha hasa Wakala wa Mbegu ambao ni TTSA,TAFORI, DANIDA pamoja na hawa Wakala wa Misitu Tanzania TSF na kuwasimamia na kuhakikisha wanazalisha miche ya kutosha na kupanda maeneo yote yenye ukame pamoja na yale ambayo misitu yake imeungua kama vile Misitu ya Lushoto takribani maeneo mengi ya Misitu ya Lushoto imeungua na kubaki vichaka tu. Kwa hiyo, niiombe Serikali maeneo hayo yapandwe miti haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kuwashirikisha watu binafsi wenye bustani za miti pia kuwapa support ili nao wawe wanachangia katika suala zima la kupanda miti. Pamoja na kusimamiwa Sheria Ndogo hasa hizi zinazotoka Halmashauri na kuwaelekeza mpaka Wenyeviti wa Vitongoji wasimamie zoezi hili. Serikali ikifanya hivyo, naamini nchi nzima hii itakuwa ya kijani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapango ya Amboni. Tulitembelea Mapango ya Amboni tumekuta Serikali inapoteza pesa nyingi sana kwani mapango yale ni ya asili ambayo huwezi kuyapata popote pale hapa duniani lakini mapango yale yanaendeshwa kikawaida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali iyaboreshe maeneo yale ya Ambaoni kwani inapoteza fedha nyingi sana, patangazwe na kuwe na miundombinu ya barabara, waajiriwe watumishi wenye taaluma . Pia tutangaze mbuga zetu ndani na nje ya nchi kwani hii ndiyo secta inayoingiza pesa nyingi za kigeni. Pia nashauri kuundwe Tume hapa Bungeni itakayochunguza migogoro ya wafugaji na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwani hali si nzuri, kuna malalamiko ya wafugaji pamoja na wadau, yaani watu wanaomiliki vitalu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri Mheshimiwa Lukuvi kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na timu yake kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze kwa hotuba yake iliyojaa matumaini makubwa ya kupelekea kwenda kumaliza upimaji pamoja na kupunguza kama sio kumaliza kabisa migogoro hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto imekuwa ni Wilaya ambayo ipo chini sana hasa katika suala la upimaji ardhi na sijajua hili suala la kutopima ardhi Lushoto inasababishwa na Maafsa Ardhi ambao sio waaminifu, kazi yao maafisa hawa ni kula pesa za wananchi na kuwadanganya kuwa mtapata hati. Mpaka sasa hivi ninavyoandika ujumbe huu kuna wananchi ambao wameshalipia gharama zote za kupimia viwanja vyao, lakini mpaka sasa ni miaka saba sasa hawajapata hati zao wala kupimiwa viwanja vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya Ardhi iende Lushoto kwenda kuwanasua wananchi wale waliodhulumiwa na Maafsa Ardhi wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro ya ardhi kwa wananchi na Serikali pamoja na mipaka ya vijiji na vijiji, kata kwa kata na hata wilaya kwa wilaya. Hivyo basi ili migogoro hii imalizike Wizara iendelee kukopesha Halmashauri ili ziweze kupima maeneo haya hasa ya wakulima na wafugaji. Jambo hili linachelewesha sana maendeleo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali ianzishe sera ya nyumba kwani sera hii itakapoanzishwa itakuwa ni sheria yenye manufaa hasa katika ukusanyaji wa kodi za nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo niendelee kuishauri Serikali yangu tukufu hasa Wizara ya Ardhi itenge bajeti kubwa zaidi ili imalize kupima ardhi yote hapa nchini, kwani ardhi itakapopimwa kwanza kabisa migogoro ya ardhi itaisha, pili, Serikali itapata pesa za kutosha ambazo pesa hizo hazipatikani kwa kutokupimwa kwa viwanja vingi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunipa uwezo nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia uhai na kunipa nguvu niweze kuchangia katika hotuba yako hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ambayo imetukuka ambayo haina mfano. Hata hivyo, nataka nimwambie kaza buti, watasema sana na watochonga sana, lakini kaza buti mwendo uwe uleule. Kuna hadithi ya Mtume inasema: basi wapendelee wenzako vile vitu ambavyo unavyovipendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Mathayo 22:34–39 inataja upendo, wapende au mpende jirani yako kama vile unavyoipenda nafsi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba, Rais anawapendelea Watanzania kuliko hata familia yake. Huu ni ukweli ambao haujafichika na watu ambao wanabeza basi, ujue hawa wana lao jambo, lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu atamjalia Rais wetu, atamjalia miaka mingi na atatimiza kazi hii na wao watasema baada ya Mheshimiwa Rais kustaafu ndio watajua kwamba, Rais wetu anafanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake, Naibu Waziri Mheshimiwa Nditiye na Naibu Waziri Mheshimiwa Kwandikwa kwa kazi kubwa wanayoifanya, Mungu atawalipa, sisi hatuna cha kuwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika kuchangia sasa. Nimshukuru Rais wangu na niishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaongozwa na Rais wangu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kunipatia barabara ya lami kilometa moja kila mwaka. Kwa hiyo, nimwombe sasa Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa, kilometa hii ni chache sana, kwani naamini kabisa inaenda kwa kusuasua, niombe iongezwe hata iwe kilometa mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila ninapopata nafasi naongelea barabara kupandishwa hadhi, barabara ya kutoka Mlalo – Ngwelo – Mlola – Bakanya – Bilingano hadi Mashewa na ikitoka Mashewa inaenda kwa Mheshimiwa Kitandula mpaka Chongoleani Tanga, kule Mabokweni. Barabara hii Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa aliniahidi kwamba, itapandishwa hadhi mwaka huu na niliongea nae na akajiridhisha kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga akaambiwa kila kitu kiko vizuri. Nashangaa kwenye bajeti hii siioni barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Mbarawa hebu aniambie, nitumie style gani, ili barabara yangu aweze kuipandisha? Watoto wa mjini wanasema nitoke vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana, unaposema barabara ya Lushoto ina maana umesema uchumi wa Lushoto. Barabara hiyo ambayo nimeitaja sasa hivi hata ng’ombe anapita kwa tabu. Nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa, niko chini ya miguu yake, naomba barabara hii wakati wa ku-wind up basi aipandishe hadhi kwani naamini kabisa hata wananchi wangu wanashindwa kwenda hospitali, akinamama wanajifungulia njiani maana hata gari halipiti wanawabeba kwenye machela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mbogamboga, viazi, matunda, ina maana hayafiki kwa wakati, wakati barabara ile ni barabara ya mkakati, barabara ya kiuchumi. Nilishaongea siku nyingi sana, namwomba Mheshimiwa Profesa Mbarawa asije aukawa masuula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna barabara ambayo inaanza Dochi kwenda Nguli mpaka Mombo, kilometa 16... (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei, kwani hajui analolifanya na tabia zake zinajulikana kabisa hapa Bungeni na Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Dochi kupitia Ngulwi hadi Mombo, kilometa 16.1 barabara hii Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja, Mheshimiwa Kwandikwa, akashuhudia barabara ile na akaongea na wananchi. Barabara ile ni barabara ya kihistoria, barabara ile ilitumika tangu mkoloni mpaka sasa hivi kuna sehemu inaitwa Kalimasumni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kalimasumni ina maana mababu zetu walikuwa wanabebeshwa mizigo na wazungu kutoka Bondeni Mombo mpaka hapo Kalimasumni sehemu wanaita Ngulwi kwa hiyo, analipwa senti 50 ndio maana panaitwa Kalimasumni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Serikali yangu Tukufu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake, naomba barabara ile itengenezwe kwa sababu barabara ile ni barabara mbadala. Nimeshaiongelea sana barabara ile kila wakati nachangia. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa sasa, barabara hii naomba kabisa aiweke kwenye mkakati wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitengenezewa barabara mwaka 1984 na JBG. JBG baada ya kutengeneza barabara kutoka Mombo mpaka Lushoto kilometa 32, walikabidhi majengo yale kwa halmashauri ya Lushoto, lakini RRM wakayachukua majengo yale mpaka sasa hivi majengo yale ni ya TBA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa, nimwombe Waziri wangu, chonde-chonde, naomba majengo yale sasa yarudishwe halmashauri, ili tuweze kufungua Chuo cha VETA pale kwa sababu, majengo yale tayari yana karakana, yana garage na chuo cha seremala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Waziri wangu Mheshimiwa Profesa Mbarawa atakapohitimisha hoja yake basi, nimwombe karakana ile iweze kurudi halmashauri yetu tuweze kufungua Chuo cha VETA, Lushoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara za TARURA. Inasikitisha sana, inasikitisha mno unapozungumzia barabara za vijijini ni nyingi mno kiasi kwamba, TARURA hata haiwezi. Hebu angalia barabara ambayo nimemwambia, hiyo barabara ya kutoka Dochi – Ngulwi mpaka Mombo, barabara ile tangu mafuriko ya mwezi wa Nne mwaka 1917 haijawahi kupitika, matokeo yake TARURA naona wamepanga eti ukarabati sehemu korofi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Profesa Mbarawa, barabara haipitiki halafu inapangiwa pesa eti sehemu korofi, hivi inakuwaje? Basi nimwombe barabara hizi nazo ziweze kupatiwa fedha ziweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kitandula alisimama akasema kwamba, kuna Kampuni ya Kichina inawekeza kiwanda kikubwa sana ambacho kinatumia trilioni saba, lakini kuna baadhi ya watu au mtu ambaye amekwamisha Wachina wale wasijenge gati maeneo yale ya Mkinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Mheshimiwa Profesa Mbarawa mtu huyu anamfahamu, kama sio mmoja basi ni wengi anawafahamu. Nimwombe atakapo-wind up basi mtu huyo ampigie simu awaachie, atoe kibali, ili wananchi wa Mkinga au Mchina yule aweze kujenga gati pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara ya Ardhi. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na nguvu mpaka kuweza kuchangia katika Hotuba hii ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Lukuvi na timu yake kwa ujumla, pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa mama Angelina Mabula kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Waziri na timu yake wanafanya kazi kubwa sana, na-declare interest kwamba mimi nipo kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Tulitembelea juzi miradi ya NHC pale Dar es Salaam, tuliona mambo makubwa sana. Wakati huku ndani watu walikuwa wanasema kwamba Mradi wa NHC, Mradi wa nyumba unakufa, lakini mradi upo vizuri. Nikupongeze Waziri endelea na kasi hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona mfumo wa upimaji ardhi mpya ambao unaitwa ILMIS, mfumo ule ni mzuri, naamini kabisa utaondoa ile zana ya kudhulumiwa hati au wale wajanja wajanja sasa wanaotaka kuuza viwanja vya watu itakuwa sasa haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niendelee kuchangia sasa katika suala la upimaji ardhi. Lushoto ni eneo ambao lina wakazi wengi sana, wanahitaji kupimiwa ardhi na wanahitaji hati. Hata hivyo upatikanaji wa hati katika Halmashauri ya Lushoto, tuseme Wilaya kwa ujumla ni mgumu sana. Nimwombe Waziri sasa, pamoja na kwamba ana mpango mzuri wa kupeleka vifaa vya kisasa kupima maeneo ya Lushoto, basi nimwombe aharakishe ili wananchi wa Lushoto waweze kupata hati zile. Maana kupata hati Lushoto ni sawasawa na kuokota dhahabu chini ya mchanga, ni ngumu sana, lakini kwa mfumo huu Waziri anaokuja nao naamini kabisa sasa mambo yatakuwa ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nimwombe sasa Waziri katika mfumo huu wa ILMIS usiishie Dar es Salaam tu, hebu uende kwa Kanda, wagawe Kanda ndani ya Tanzania hii ili uweze kwenda kwa kasi kwani mfumo huu ni mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la hati. Nilienda Dar es Salaam kwenye mtaa mmoja wanaita Kilungule A na B. Tulikuta wananchi wa Kilungule A walioomba hati ni 600, lakini ambao wameenda kuchukua hati ni 176, kumuuliza Waziri akasema hati zote 600 zipo. Baada ya kuwauliza wananchi wale wakasema kwamba hawana pesa za kulipia gharama ya hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri hizi gharama za kulipia hati hebu ziangaliwe upya maana ni gharama kubwa, wananchi wale wanasema kwamba kupimiwa ni Sh.300,000 wakajumuisha pamoja na hati kwamba gharama yote ni Sh.300,000, matokeo yake kufika kule katika kuchukua hati wanaambiwa kuwa, kuna gharama za hati na kuna gharama za upimaji. Kwa hiyo hili niiombe sasa Serikali iangalie upya ili ipunguze wananchi wale waweze kupata hati kwa bei rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye Mabaraza ya Ardhi. Kule Lushoto namshukuru Waziri Lukuvi alituwekea Baraza la Ardhi, lakini Baraza la Ardhi lile mpaka sasa hivi halina Mwenyekiti, Mwenyekiti anatoka Korogwe. Kwa hiyo nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri apeleke Mwenyekiti katika Baraza lile la Ardhi kwani kuna msongamano mkubwa sana katika Baraza la Ardhi la Lushoto na wananchi wengi wanatoka maeneo mbalimbali na maeneo ambayo kwa kweli wanafika pale huenda kwa siku moja au siku mbili. Kwa hiyo nimwombe sasa Waziri anisaidie kupeleka Mwenyekiti katika Baraza lile la Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mipaka. Sisi na Kamati yetu tulienda maeneo ya Mtukula kule mpakani mwa Uganda na Tanzania; tuliona vile vigingi vya mkoloni ni vizuri kuliko vigingi vinavyowekwa na Serikali. Kwa hiyo ningeomba Serikali yangu sasa itumie modal ile ya vigingi vile vya mkoloni. Kwanza vigingi vile viimarishwe then viwekwe vya kutosha katika maeneo yote ya mpakani katika mipaka yetu yote ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna mipaka kwenye maziwa; mipaka yetu kwenye maziwa haijulikani, kwa hiyo niiombe Serikali yangu iweke maboya yale sasa kwenye maziwa ili wananchi wetu wanapoenda kuvua katika maziwa yale wasiingie katika maeneo ya watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Kilimo pamoja na timu yake kwa kazi nzuri na yenye tija wanayoifanya, na kwa hakika vipaombele vyote hivi vikifanyiwa kazi nchi yetu itakuwa imetimiza malengo yake ya asilimia 75.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina asilimia 75 ambayo ni wakulima, lakini kinachoonekana wakulima hawa hawapati huduma kama inavyotakikana. Ushauri wangu kwa Serikali ijipange kuhakikisha inapeleka pembejeo za kutosha na kwa wakati, mfano nchi yetu ina mazao ya kibiashara zaidi ya sita ikiwemo kahawa; na kahawa hii inalimwa pia katika Milima ya Usambara ila cha kushangaza na kusikitisha zao hili la kahawa linakufa, hivi ninavyoandika Lushoto kahawa imekufa.

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hii naomba niishauri Serikali yangu tukufu iende ikafufue zao la kahawa katika Wilaya ya Lushoto kwani zao hili lilikuwa linainua sana uchumi wa Lushoto. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali iende kufufua zao hili la kahawa pamoja na kupeleka wataalam wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Lushoto ni ya wakulima wa mbogamboga na matunda, na mazao haya ndio mazao tegemezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, lakini sijawahi kusikia wakulima hawa wanapelekewa pembejeo, lakini pamoja na hayo mazao ya wakulima hawa mengi yanaozea mashambani. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu iwapelekee wakulima hawa wa mbogamboga na matunda pembejeo pamoja na kuwatafutia masoko wakulima hawa.

Mheshimiwa Spika, pia Wilaya ya Lushoto ina milima na mabonde mengi, hivyo wakati wa msimu wa mvua kunakuwa na maporomoko makubwa ambayo yanaleta asali kwenye mashamba pamoja na kuharibu miundombinu ya barabara na kupelekea hasara kubwa kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kujenga mabwawa kwa ajili ya kukinga maji hayo ili wakulima wetu hasa wa Wilaya ya Lushoto waweze kulima kilimo cha umwagiliaji kuliko ilivyo kuwa sasa ardhi yote yenye mbolea inasombwa na maporomoko yanayosababishwa na mvua?

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali itenge pesa za kutosha ili iwajengee mabwawa wakulima wa Jimbo la Lushoto.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono kwa asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo ndiyo iko mbele yetu. Kwanza kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake, Mheshimiwa Jenista pamoja na Mheshimiwa Mheshimiwa Kairuki kwa kazi kubwa wanayoifanya, hakika mwenye macho haambawi tazama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende kwenye suala zima la afya. Kwanza niendelee kuipongeza Serikali yangu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa wanayoifanya kwani hivi karibuni tumeshuhudia karibia Hospitali za Wilaya 67 zimekarabatiwa. Sambamba na hayo, Hospitali yangu ya Wilaya ya Lushoto sijaiona na hospitali ile ni kongwe, ni ya zamani sana. Hospitali ile inachukua karibia Wilaya tatu ambazo zimezunguka pale, naamini inahudumia takribani watu 500,000. Niiombe sasa Serikali yangu Tukufu watakapokuja ku-windup basi waingize hospitali hii iweze kukarabatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kama nilivyokwishasema hospitali hii ni kongwe lakini pamoja na ukongwe wake majengo pia ni ya zamani sana, hayaendi na wakati, inapitwa mpaka na kituo cha afya. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu sasa itengee fedha kwa ajili ya Hospitali hii ya Wilaya ya Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hospitali hii haina X-Ray kwa muda mrefu, sasa hivi ni takribani miezi sita. Hata Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi wakati anakuja Lushoto nilimlalamikia kuhusu X-Ray hii. Kwa hiyo, niiombe sasa Serikali yangu Tukufu iweze kupeleka X-Ray ile wananchi wangu waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vituo vya afya ambavyo vinaendelea kujengwa. Niishukuru Serikali yangu Tukufu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwani tumepewa Kituo cha Afya kimoja cha Mlola, tumepewa takribani shilingi milioni 700; shilingi milioni 400 kwa ajili ya majengo na shilingi milioni 300 kwa ajili ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nguvu za wananchi tumeshajenga vituo vya afya viwili ambavyo viko hatua tofauti tofauti. Kituo cha Afya Gare tayari kina maboma zaidi ya matatu na vyumba zaidi ya 20. Kama ilivyoahidi au kama ilivyo ada wananchi wanapojenga maboma yale basi Serikali inamalizia maboma yale, kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu ipeleke fedha tuweze kumalizia maboma yale na wananchi wa Gare na wa Lushoto kwa ujumla waweze kupata huduma hiyo na kupunguza msongamano ambao upo katika Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kituo cha Afya Ngwelo tunaanza kukijenga na kiko hatua ya lenta kwenye OPD. Kwa hiyo, niiombe pia Serikali yangu Tukufu kwamba ipeleke fedha pale tuweze kukamilisha kituo kile cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zahanati kama Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inavyosema kwamba kila kijiji kitajengwa zahanati. Wananchi wa Lushoto kwa nguvu zao wamejenga zaidi ya zahanati 12. Zahanati sita ziko tayari zinahitaji vifaatiba na watumishi, zahanati sita ziko kwenye lenta. Kwa hiyo, niombe Serikali yangu kama ilivyoahidi au kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyosema kwamba mnapofikisha kwenye mitambaa ya panya basi Serikali itachukua. Niombe sasa Serikali iwaunge mkono wananchi wa Jimbo la Lushoto ili waweze kumalizia zahanati zile ambazo zimebaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la TARURA. Kwa kweli TARURA ni watu wazuri sana na wanafanya kazi kubwa sana ambayo kwa kweli inafaa kuigwa lakini haina fedha za kutosha. Kama unavyofahamu Lushoto ni ya wakulima wa mbogamboga na matunda na kahawa lakini wanapata hasara kubwa sana hususan mvua zinaponyesha mazao yao huwa yanaozea shambani kwa sababu ya kukosa miundombinu ya barabara. Niiombe Serikali yangu Tukufu iangalie namna ya kuiwezesha TARURA waweze kupata fedha nyingi ili waweze kutengeza barabara zile za Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ambazo ni critical issue, mfano barabara ya kutoka Mlalo – Ngwelo – Mlola – Makanya - Milingano – Mashewa. Barabara hii ni ya kiuchumi na kila siku, kila mwaka na kila wakati naisemea lakini mpaka leo haijatengezwa. Kwa hiyo, niombe Serikali yangu Tukufu kwamba barabara ichukuliwe na TANROADS kwa sababu inaunganisha wilaya hadi wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto kuna barabara moja kuu tu ambayo inatoka Mombo - Soni – Lushoto, kwa hiyo, Wilaya nzima ya Lushoto barabara ya kuingia Wilayani ni moja tu. Kuna barabara moja ya mchepuko ambayo inatoka Dochi - Ngulwi - Mombo, hii ni barabara muhimu sana na kwa kweli itaenda kutatua kilio cha wananchi wa Lushoto kwa sababu ni njia fupi, ni kilometa 16 tofauti na barabara ya kutoka Mombo - Soni - Lushoto ambayo ni kilometa 32, ni nusu ya barabara hiyo. Niiombe Serikali kutenga fedha ili barabara ile iweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye suala zima la umeme, kwa kweli tumekuwa tunajibu maswali magumu sana ambapo na sisi tunashindwa kuyajibu. Niiombe sasa Serikali yangu Tukufu, dada yangu Mheshimiwa Subira Mgalu na Mheshimiwa Medard ameshafika Lushoto na ameona hali halisi ilivyo, ameona jinsi wananchi wa Lushoto wanavyopenda umeme na anajua kabisa Lushoto hakuna nyumba ya nyasi hata moja na wananchi wa Lushoto tayari wameshafanya wiring kabla hata hawajatangaziwa mambo ya umeme. Kwa hiyo, niiombe sasa Serikali ipeleke umeme kwa wananchi wangu wa Lushoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye suala la kilimo, Lushoto kuna zao moja la kahawa ambalo hata wadau wa mkutano juzi walikaa pale LAPF wakasema kahawa ya Lushoto ni bora kuliko kahawa ya sehemu nyingine. Kwa hiyo, niombe sasa Serikali yangu ipeleke pembejeo na miche kwa ajili ya kupanda kahawa katika milima ile ya Usambara ili tuweze kupata kahawa bora tuweze kuimarisha kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kumalizia niongelee uwekezaji. Hebu tuangalie ni namna gani ya kuondoa changamoto zinazowakwaza wawekezaji wetu. Mheshimiwa Kairuki naamini ni jembe, unafanya kazi iliyotukuka, kuna Kiwanda cha Sementi kule Mkinga, mwekezaji yule anaweka shilingi trilioni 7.7 lakini leo hii ni mwaka wa tatu hajafanikiwa. Naomba Mheshimiwa Kairuki kwa sababu Wizara hii umeshakabidhiwa naomba kabisa uanze na hili tuhakikishe mwekezaji anafungua kiwanda kile. Kiwanda kikishashafunguliwa inamaana wananchi watapa ajira, uchumi wa Taifa utakua na mambo mengine yataenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali yangu Tukufu Uwanja wa Ndege Tanga sasa upanuliwe ukizingatia sasa hivi tuna bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda. Tanga sasa inaku,a tunaongeza kina cha bahari, ina maana wawekezaji na wanachi wengi watakuja kwa ajili ya fursa zilizopo Tanga. Kwa hiyo, niombe Serikali yangu Tukufu iweze…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Shekilindi.

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu kuweza kuchangia Wizara hii ya maji. Pili, nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya hakika sisi hatuna cha kumlipa ila Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiyo atajua cha kumlipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru kwanza Waziri Mbarawa, Naibu wake Aweso, Katibu Mkuu pamoja na timu nzima kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwakweli Watanzania wanaona kazi kubwa mnayoifanya. Endeleeni kufanya hivyo, naamini na Mungu atawasimamia na malengo tutayafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukuru kwa kupewa milioni 500 kwa ajili ya mradi wa Ngulu. Mradi ule umekamilika na sasa nimuombe Waziri au Naibu Waziri aende sasa kwenda kuufungua. Lakini sambamba na hayo, nimepewa milioni 770 kwa ajili ya maji mjini, milioni 770 hizi zimepan giwa zijenge tenki la lita 650 ambalo tenki hilo liko sehemu ya Magamba na tenki lile linaendelea kujengwa mpaka sasa hivi, na banio la sehemu m oja inaitwa Kindoi na banio hilo bado linaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kwa kuwa kuna kata mbili ambazo ziko chini vyanzo vyake viko juu Lushoto basi nilimuomba Waziri baada ya kufika Waziri Mheshimiwa Prof. Mbarawa baada ya kufika Lushoto kuangalia hali ile halisi ilivyo. Basi nikamuomba kwamba pamoja na kujenga tenki hili, kulijenga, basi kuna banio linajengwa sehemu ya Kindoi niombe banio lile litolewe matoleo mawili kwa ajili ya kata mbili, kwa ajili ya Kata ya Ubiri na Kata ya Ngulwi. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu tukufu kwamba Mheshimiwa Waziri, naomba sasa unipangie fedha au unipe fedha kwa ajili ya kata zile ambazo nimeshazitaja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, hili tenki la lita 650 naishukuru sana Serikali lakini hakuna mabomba ambayo yanatakiwa kuanza kwenye chanzo kuja kwenye tenki na kutoka kwenye tenki, kwenda Lushoto mjini. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sasa kwamba pamoja na kupata fedha hizi lakini bado hakuna fedha za miundombinu ya bomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu initengee fedha hizo ili tuweze kukamilisha miundombinu ya bomba. Sambamba na hayo, miundombinu ya bomba ambayo iko Lushoto Mjini ni ya zamani sana, ni ya tangu mkoloni. Bomba zile ni za chuma Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nikuombe sasa unitengee pesa nyingine kwa ajili ya kutoa miundombinu ile ya zamani ili tutoe miundombinu chakavu, tuweke miundombinu mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pamoja na banio hilo niombe sasa kwamba nipate fedha kwa ajili ya kupeleka maeneo yale ambayo nimeyataja kata zile mbili ambazo ni Ubiri na Ngulwi maana nikikosa kwenye eneo hili basi ujue kabisa kwamba wale watu wa Ngulwi na Ubiri hawataweza kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe tena, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwamba kuna mradi mkubwa ambao umeshafanyiwa upembuzi yakinifu. Mradi huo unaitwa chanzo cha wanaitwa mstari namba tisa ambao uko Magamba. Chanzo kile kikienda kutekelezwa kitaenda kutatua tatizo la maji katika kata 12 ambazo kata hizo ni Kata ya Makanya, Mbwehi, Malibwi, Kwekanga, Kwahi, Migambo, Kilole, Gare, Ngwelo, Ubiri, Ngulwi pamoja na Kata na Kwemashao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua Lushoto, jiografia yake ni ya milima kwa hiyo vyanzo vya maji viko Lushoto. Sisi tumekosa miundombinu ya maji na maeneo haya ina maana yako mlimani, vyanzo viko mlimani, maeneo yako bondeni. Kwa hiyo, kwenye maeneo haya niliyotaja nikipata miradi miwili tu basi ina maana tunaenda kutatua tatizo kubwa katika kata ile. Cha kushangaza na cha kusikitisha, wenzangu wanaongelea vijiji havina maji lakini mimi naongelea kata hazina maji, hebu angalia distance iliyopo hapo. Nimuombe Waziri aliangalie hili kwa jicho la huruma ili niweze kuongelea vijiji, sio kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri anafahamu kabisa Lushoto na Waziri mwenyewe Mheshimiwa Prof. Mbarawa anafahamu Lushoto. Lushoto kule wananchi wanapata taabu sana hasa katika Kata ya Kwai, Makanya, Malibwi, Mbwehi, Kilole, Kwekanga wananchi wanapata taabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mistari ya dini inasema kullukum rai wakullukum masuul. Hii ni dhamana, viongozi tutakwenda kuulizwa juu ya jinsi tunavyolinda mali zetu au tunavyowaongoza wananchi wetu. Kwa hiyo, sisi tusije tukawa masiula, Mheshimiwa Waziri usije ukawa Masiula, Naibu Waziri usije ukawa Masiula. Hakika, wewe Mheshimiwa Naibu Waziri unafahamu Lushoto. Dada zetu wanapata tabu sana, wanatoka mpaka vipara, hakuna hata wa kuwaoa angel face hazikai usoni, carolite hazikai usoni hata lipstick hazikai mdomoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe usije ukawa masiula, hebu angalia suala hili kwa makini, tusije tukaulizwa na Mwenyezi Mungu kwamba umewatendea nini wananchi wa Lushoto hususan akina mama. Nikuom be upeleke fedha katika Jimbo la Lushoto na maene haya niliyoyataja ili wananchi wangu hususan akina mama tuanze kuwatua ndoo kichwani kuliko ilivyokuwa sasa hali ni m baya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, pia niende kwenye suala la kujenga mabwawa. Kama walivyosema, Lushoto ni ya milima milima lakini laiti Serikali ingekuja na mpango wa kujenga mabwawa naamini tusingepata taabu ya maji. Lushoto kuna maji ya mserereko, kwa hiyo, niiombe Serikali sasa itenge fedha kwa ajili ya kujenga mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, waati tunasubiri miradi mikubwa, hebu sasa tupatieni fedha za kuchimba visima virefu ili wananchi wale waanze kupata maji, wananchi wale wasipate taabu san a na ukizingatia sasa hivi wananchi wetu wanatoka asubuhi hususan akina mama. Wanatoka asubuhi saa kumi na mbili wanarudi saa saba. Hivi hawa watoto watawahudumiaje kwenda shule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri na timu yake iliangalie ili kwa jicho la huruma. Nimeongea sana kwa muda mrefu hususan katika Bunge hili kuhusu mambo ya maji. Kwa kweli kama tumedhamiri akumtua mama ndoo kichwani basi kweli tumtue mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, watumishi Wizara ya maji mpaka kule chini kwenye idara hawatoshi ni wachache sana ndiyo maana unakuta mambo yanazorota. Pamoja na hayo, kuna hii sheria ya manunuzi, hii sheria inakandamiza sana na ndiyo inapelekea miradi inakuwa miradi inatengwa kwa gharama kubwa sana. Mfano unaweza ukaona get valve ya inchi sita inauzwa 1,000,000…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wetu ndiyo huo.

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunipa afya na nguvu ya kuweza kuchangia katika Wizara hii. Niwapongeze Waziri, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, Naibu Waziri Mheshimiwa Nditiye na Naibu Waziri Mheshimiwa Kwandikwa kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishukuru Wizara hii kwa kunitengea fedha za kujenga kilometa 1 kila mwaka ambapo zinajengwa katika barabara ya kutoka Magamba – Mlalo na Magamba - Mlola. Nashukuru Serikali kwa kilometa 1 waliyotutengea lakini ni chache sana ambapo sasa hatuendi na ile kasi ya kujenga viwanda na kwenda kwenye uchumi wa kati. Nimuombe Waziri aweze kututengea hata kilometa 4 ili pande zote mbili ziende kilometa 2, Mlalo kilometa 2 na Mlola kilometa 2. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo pia kuna barabara ambayo kila siku nilikuwa naionglea, inaanza Mlalo - Ngwelo - Mlola – Makanya – Milingano - Mashewa. Barabara hii inaenda mpaka kwa Mheshimiwa Kitandula Mkinga kule, inaenda mpaka Chongoleani, kwa hiyo, barabara hii ni ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara hii nimeiongelea sana na hii ni bajeti ya nne. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kwamba, itoshe sasa, mimi siyo mtoto wa kufikia, mimi ni mtoto wako kabisa, sijawahi kushika shilingi, sijawahi hata kukataa bajeti, ifikie hatua sasa Mheshimiwa Waziri hebu barabara hii uichukue ili tuweze kunusuru watu wa Makanya na maeneo mengine niliyoyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo Mheshimiwa Waziri anafahamu fika kwamba barabara ile ni ya kiuchumi. Barabara ile kuanzia Makanya au Mlola kwenda maeneo niliyoyataja hakika tutakuwa tumekuza uchumi. Kwa hiyo, nikuombe sana itoshe, kwa kweli sijui niingie kwa style gani au nije kwa style gani ili uweze kunielewa barabara ile iweze kupandishwa hadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna barabara nyingine ya kutoka Dochi – Ngulwi - Mombo ambayo ni kilometa 16. Barabara ile Mheshimiwa Waziri niliripoti kwako 2017 wakati barabara ile inapata mafuriko. Kwa hiyo, nikuombe nayo barabara hii Mheshimiwa Waziri hebu iingize sasa iweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii walisema kwamba TARURA inaweza lakini TARURA haina fedha za kutosha kila mwaka inatengewa kilometa 1 au 2, kwa hiyo, ni kama vile barabara hii imetelekezwa. Mheshimiwa Kwandikwa ni shahidi amefika mpaka pale kwa wananchi wa Ngulwi ameongea nao akawaambia kwamba barabara hii sasa itatengenezwa lakini mpaka leo hii barabara ile haijatengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile pia ni ya kiuchumi. Halafu ni barabara ya mchepuko, kama unavyofahamu Lushoto kuna barabara moja tu kubwa ambayo ni ya Mombo – Soni - Lushoto kilometa 32. Kwa hiyo, kukitokea matatizo kama yalivyotokea 2017 na kuziba barabara ile ya Soni – Mombo basi Wilaya ya Lushoto tunakosa huduma kabisa. Kwa hiyo, niombe sasa barabara hii iwe barabara mbadala na inawezekana hata barabara hii sasa ikawa ni barabara kwa ajili ya kushuka tu magari na hii ya Soni - Mombo kwa ajili ya kupandisha magari. Hiyo, naamini kwa kweli ukiipanga vizuri Mheshimiwa Waziri inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja sasa kwenye minara (mawasiliano). Mheshimiwa Nditiye wewe ni shahidi nimekuja mara kadhaa kwako kwa ajili ya kukuomba minara. Mfano maeneo yangu mengi ya Wilaya ya Lushoto hayana mawasiliano, mfano, Ubiri, Mazumbai, Magului, Makanya, Kireti, Kigumbe na maeneo ya Mlalo ya Makose, Longoi, Mavumo na Kikumbi. Nikuombe chondechonde kaka yangu hebu sasa peleka mawasiliano katika maeneo haya ili wananchi wetu waende na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye Uwanja wa Ndege Tanga, wenzangu wameongea sana kuhusu uwanja huu. Uwanja ule wa Ndege kweli tumeona tumetengewa mashine zile lakini ziende sambamba sasa na kuongeza uwanja ule. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri ni shahidi wakati wa bajeti wakati ana-wind-up alisema kabisa kwamba uwanja ule utaletewa bombardier lakini mpaka leo hii bombardier hatuioni, Tanga kumekucha, Tanga kuchele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu sasa Tanga ionekane, safari hii tuweze kupata bombardier inayotoka Dar-es-Salaam kuja Tanga mpaka Pemba ikiwezekana hata iende mpaka Mombasa. Hili naomba sasa nalo ulichukue wakati wa ku- wind-up naamini kabisa utalisemea na ukizingatia Tanga tayari tunaongeza kina cha bahari, Serikali imetuona, tuna viwanda pia kama unavyojua.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda umeisha. Naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SHAABAN O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na mimi kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza kabisa nimshukuru mwenyezi mungu mwingi wa rehma kwa kunipa afya na nguvu na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wangu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, then nimpongeze Waziri Philipo Mpango na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ashatu Kijaji na timu yake ya wataalam kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli bajeti hii ni nzuri na imeenda kujibu matatizo ya Watanzania, ile kiu ya Watanzania naamini sasa imepata suluhu kwa bajeti hii. Wale ambao wanasema kwamba asiyepigia kura bajeti hii basi atamshangaa mimi nataka nisema atajishangaa yeye mwenyewe, kwa sababu bajeti hii haijawahi kutokea Mwenyezi Mungu anasema: :Man laa yashkur kalila laa yashkur kathira”; maana yake usiposhukuru kwa kidogo, basi hata kikubwa hutoshukuru. Ina maana mambo yote yaliyofanyika katika nchi hii hawa ndugu zangu wanataka waniambie hawajayaona? Nataka niseme basi tumwachie Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye ndiyo mwenye majibu sahihi, lakini Mwenyezi Mungu anajua ameona na Watanzania wameona.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika kuchangia, nianze na barabara. Ni ukweli usiopingika kwamba barabara za vijijini ndiyo kila kitu ndizo zinazotoa mazao, ndizo ambazo wakulima wanazitegemea kuliko barabara nyingine. Sasa niiombe Serikali yangu Tukufu kwamba badala ya kutenga asilimia 30 kwa ajili ya TARURA basi watenge asilimia 40; niishauri Serikali yangu Tukufu; mimi naamini Mheshimiwa Mpango hili linawezekana. Wewe mwenyewe unajua kwamba barabara hizi za TARURA ni nyingi kuliko hata hizi za TANROADS. Nikuombe Mheshimiwa Mpango hili uliangalie kwa jicho la huruma ili sasa twende kukidhi haja za wananchi wetu, hususan wale waishio vijijini. Kwa kweli fungu hili la TARURA ni dogo sana ambalo kwa kweli haiwezi kabisa kukidhi barabara za vijijini.

Mheshimiwa pamoja na hayo kuna barabara ambazo zinaunga wilaya hadi wilaya; niishauri au niiombe Serikali yangu sasa ichukue barabara hizi ziingie kwenye TANROADS. Kwa mfano barabara zangu za kutoka Mlola, Makanya, Milingano hadi Mashewa, barabara hii ni barabara ya kiuchumi; nikuombe Mheshimiwa Mpango barabara hii ipandishwe hadhi. Bado kuna barabara ya Dochi, Ngulwi hadi Mombo kilometa 16; barabara hii siyo ya kiuchumi tu, barabara hii sasa itakuwa ni barabara ya mchepuo, hususan barabara yetu ya kuanzia Mombo, Soni hadi Lushoto. Kwa mfano mwaka juzi iliharibika mafuriko yaliingia kule maporomoko yakaziba barabara zaidi ya takriban wiki mbili na wananchi wale walipata tabu sana mpaka mazao yao yakaharibika. Kwa hiyo nikuombe barabara hii angalau ipandishwe hadhi ili ichukuliwe na TANROADS na iweze kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, niende kwenye kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu na asilimia 65 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima. Kwa hiyo niombe sasa hawa Wakala wa Pembejeo wapeleke pembejeo kwa wakati. Wakati wa palizi anapeleka mbolea za kupandia wakati wa kuvuna anapeleka mbolea ya kukuzia; sasa hii jamani tutafika kweli ilhali tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo tuangalie na masoko yetu, tuwatafutie wakulima wetu masoko. Mimi naamini kabisa kwamba Serikali hii ni sikivu na inaweza kabisa kutafuta masoko. Ni imani yangu kubwa kwamba kipindi hiki cha 2019/2020 wakulima wetu watapatiwa masoko ya kutosha ili waweze kujikimu katika hali hii, waondokane na hii hali ya kuhangaika huku na kule kutafuta masoko wao wenyewe

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye elimu. Tunaenda kwenye uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda huu naamini kabisa unaendana sambamba sasa na kumalizia maabara zetu. Hizi maabara naamini kabisa zikimaliziwa tutaanza kupata watu ambao ni wataalamu kuliko ikifikia hatua tukaenda kutafuta wataalamu nje ilhali sisi wenyewe tuna watoto wetu ambao tukimaliza maabara hizi watasoma elimu kwa vitendo, moja kwa moja wataenda kuhakikisha kwamba wanasimamia viwanda hivi ambavyo vitafunguliwa; mimi naamini hii inawezekana. Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Mpango sasa twende kumalizia maabara hizi, lakini sambamba na hayo lazima tuyamalizie pia haya maboma ya madarasa kwa shule zetu. Pamoja na hayo tujenge nyumba za walimu pamoja na hosteli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye pensheni kwa wazee. Wazee hawa wamesahaulika kwa muda mrefu sana, wazee hawa ndio ambao wametufanya mpaka leo hii tunasimama mbele yenu hapa tunaongea na nyinyi tunaongea na Bunge lako Tukufu, tunaongea na Watanzania. Niombe sasa kwamba wazee hawa kwenye ile asilimia 10 inayotoka halmashauri na wazee nao wawepo pale inaweza kuwa asilimia tatu kwa vijana, asilimia tatu kwa akinamama, asilimia mbili kwa walemavu, na asilimia mbili kwa wazee, hiyo inawezekana

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja niende kwenye suala la faini za magari zinazotozwa na traffic. Nikuombe Mheshimiwa Mpango; faini hizi ukizilinganisha kati ya basi au pamoja na pikipiki ni vitu viwili tofauti sana.

Nikuombe sasa Mheshimiwa Mpango kwamba hizi faini 30,000 zinazotozwa kwenye bodaboda zipungue, angalau zifikie 10,000 kwa sababu hawa ndugu zangu kipato chao wanachokipata ni kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende tena kwenye suala la kitengo cha manunuzi. Hiki nilikielezea kipindi cha nyuma lakini ikawa nimeishia katikati. kitengo hiki kwa kweli kinakwamisha sana maendeleo. Ninaomba, ikiwezekana kitengo hiki kama si kufutwa basi kirekebishwe; kwa sababu mradi ambao unahitaji milioni 500 ukipeleka kwenye kitengo cha manunuzi utaambiwa labda bilioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitengo hiki kwa kweli mimi ni imani yangu kabisa kwamba kinazalisha rushwa moja kwa moja. Kwa mfano unaweza ukanunua hata koki au gate valve ya shilingi 50,000, lakini wao wakileta quotation yao wanakwambia hii inauzwa shilingi 500,000 sasa kweli utafika, kwa hiyo niombe tuangalie ikiwezekana tutumie force account katika suala hili; na hiki kitengo ikiwezekana kifutwe kabisa maana naamini kabisa kinakwamisha juhudi za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niende moja kwa moja kwenye suala la viwanja vya ndege. Ni imani yangu kubwa sana kwamba Serikali hii imejitahidi kwenye ukarabati wa viwanja vya ndege. Niombe kwamba kile kiwanja cha ndege; kwa kuwa Tanga sasahivi imefunguka kibiashara basi ongeza fedha. Naamini umetenga fedha lakini fedha zile hazitoshi; ongeza fedha sasa ziende zikatengeneze uwanja ule kwani uwanja ule sasa hivi ndege haziwezi kutua usiku kwa sababu hauna taa. Kwa hiyo ni imani yangu kubwa; nikuombe uhakikishe kwamba unapeleka fedha za kutosha ili kwenda kujenga uwanja ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la watumishi. Watumishi wetu wana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa ahsante sana, Mheshimiwa Lucy Magereli atachangia kwa dakika saba, tutamalizia na Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki

MHE. SHAABAN O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema ambaye ameniwezesha kusimama mbele yako, mbele ya Bunge Tukufu hili kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kumpongeza Waziri Mkuu pamoja na timu yake kwa hotuba nzuri iliyojaa matumaini, iliyosheheni kila kitu. Naamini kabisa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu ikienda kutekelezeka hii naamini kabisa kwamba, tayari sio hatuko kwenye uchumi wa kati, tuko kwenye uchumi wa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwenye suala zima la afya. Niipongeze Serikali yangu tukufu kwa kujenga vituo vya afya vingi nchini pamoja na zahanati. Ombi langu, hebu sasa Serikali ione namna gani itapeleka vifaa tiba na dawa katika hospitali zile ili, naamini kabisa Serikali ikishapeleka dawa na vifaa tiba naamini kabisa wananchi wetu watapata huduma stahiki na wataishi na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye tiba asili. Enzi za mababu zetu walikuwa wanatumia dawa hizi za asili, lakini mababu zetu wale walikuwa wanaishi miaka mingi sana tofauti na sasa. Kwa nini sasa sisi hatuwezi kuwaenzi mababu zetu kwa kutumia tiba zetu za asili?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii watu wanasema tunaenda kidigitali. Ushauri wangu niombe sasa tiba zetu za asili hizi zitumike. Mfano mzuri mwaka jana, nakumbuka ilikuwa mwezi wa tatu, Taifa letu lilikumbwa na ugonjwa wa corona, lakini Rais wetu Hayati Dkt. Magufuli alisimama kidedea na kutamka kwamba, taasisi za dini waombe misikitini pamoja na makanisani. Pamoja na hayo akasisitiza nyungu ziendelee na wale ambao wana fani zao za tiba za asili waendelee nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli ilifanyika vile, nadhani umeona mafanikio makubwa sana; hivyo basi, kwenye mpango huu, kwenye hotuba hii sijaona hata bajeti ya tiba ya asili. Nikuombe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, baada ya hotuba hii…

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shekilindi kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mariam Ditopile.

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda kumpa Taarifa muongeaji. Ni kweli kwa dhahiri tumeona mchango wa dawa za kienyeji kwenye kutibu gonjwa hili la Covid 19, hasa dawa ambayo yeye mwenyewe ndio ameibuni ya Shekilindi Bosnia Covid 19 Anti-Covid. Naomba nimpe Taarifa hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shekilindi unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea Taarifa hiyo, lakini nataka nimwambie sio dawa za kienyeji ni tiba ya asili, tiba mbadala tiba ya asili. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia hususan katika suala hili. Dawa hii imefanya vizuri sana, imefanya vizuri kiasi kwamba, hata wataalamu wetu wa dawa hawa wa kisasa naamini wali-appreciate kwamba, dawa Hii ni safi na salama. Niombe sasa, huoni sasa umefikia wakati wa kupaisha dawa zetu? Huoni sasa umefikia wakati Serikali i-support watu wa tiba asili na tiba mbadala kwa ajili ya kunusuru Taifa letu? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, na nikuhakikishie dawa zetu hizi zinafanya vizuri, lakini nataka nikuhakikishie kwamba, wataalamu, watafiti nikiwemo mimi, tumegundua dawa zenye kutibu magonjwa mengi.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Kwanza kabisa inatibu corona, inatibu UKIMWI, inatibu cancer, inatibu kisukari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Asante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi kubwa wanayoifanya. Pia niendelee kuwapongeza kwa kuwaagiza Wakandarasi wawe wanawasiliana na Waheshimiwa Wabunge. Nawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Lushoto lina Kata 15 na baadhi ya Kata, umeme umepita maeneo ya barabarani tu. Kwa hiyo, kumekuwa na malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Lushoto. Hata hivyo, namshukuru Waziri kwa kutoa maagizo yake ya kuhakikisha vijiji vyote vya Jimbo la Lushoto vipatiwe umeme. Wasiwasi ni Wakandarasi: Je, watafanya hivyo kweli? Kama hivyo ndivyo, naomba niorodheshe vijiji vyangu vyote ambavyo havina umeme kabisa, pamoja na vitongoji vilivyorukwa.

Mheshimiwa Spika, hivi ndiyo vijiji ambavyo havina umeme kabisa. Gare, Yamba, Kongei, Masange, Boheloi, Kwemashai, Ngulu, Miegeo, Handei, Milungui, Kireti, Kwemakame, Mazumbai, Ntambwe, Kigumbe, Bombokamgobolo, Kilole, Mbelei, Mavului, Mazashai, Kigulunde, Mdando, Kweulasi, Bwaya, Kwetango, Bombo na Ngulwi Chumbageni.

Mheshimiwa Spika, hivi ndiyo vijiji ambavyo havina umeme kabisa. Pamoja na hayo, kuna Vitongoji zaidi ya 27 navyo vimerukwa. Kwa hiyo, naomba Serikali ivipatie Vitongoji hivyo vilivyorukwa na umeme ili kuepuka malalamiko ya wananchi waliokosa umeme na wakati huo huo wanauona umeme unawaka kwa jirani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, wananchi wa Lushoto wana uwezo mkubwa wa kuweka umeme, lakini wanakwamishwa na watu wa TANESCO, kwa kuwaambia umeme bado ni shilingi 177,000. Hili suala linawakatisha tamaa wananchi wa Lushoto. Kama hivyo, basi naiomba Serikari itoe waraka wa kutoa bei elekezi kwa wananchi ili kuepuka usumbufu kwa wananchi wanaoupata kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa nimpongeze Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na timu yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kwangu nitatoa tu ushauri wa kuongeza mapato katika Wizara hii. Nchi yetu hii imejaliwa misitu mingi sana na misitu hii imejaa miti dawa na mimea dawa. Ndiyo maana hata imefikia hatua ina maana tumekabiliana na ugonjwa huu wa Covid-19. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana, Wizara imeangalia mali hizi bila kuzifanyia kazi, hata katika taarifa yake hotuba ya Mheshimiwa Waziri hakuna sehemu iliyotaja miti dawa, hakuna sehemu iliyotaja dawa zetu za asili. Nimwombe sasa, naamini ametaja tu eneo ambalo kwa kweli ni la vinyago, kwamba vinyago viwekwe kwenye maduka ya utalii. Nishauri kabisa na dawa za asili ziwekwe kwenye pharmacy za kitalii. (Makofi)

MHE: FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niende moja kwa moja …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shekilindi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Flatei Massay.

T A A R I F A

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa ndugu yangu Shekilindi asisahau ku-declare interest kwamba yeye pia ni mtalaam na ana madawa hayo kupitia hiyo miti mishamba, hiyo ya Covid na sisi tumetumia humu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Kwa ile kanuni yetu hawezi kusema hayo kwamba yeye ana maslahi kwenye hilo jambo, kwa sababu yeye anachangia kuhusu misitu yote, maana ukisema una maslahi lazima ututajie kiasi gani, sasa yeye si anauza dawa yake jamani inaitwa Shekilindi, watu wakanunue huko.

Mheshimiwa Shekilindi malizia mchango wako.

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, mimi sikutaka kufanya hivyo kama Massay anavyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kuishauri Serikali sasa, kwamba watalaam wetu washirikiane na watalaam kama sisi kuhakikisha kwamba tunaanzisha viwanda vya kutengeneza dawa zetu hizi. Pia kama unavyofahamu nchi za wenzetu Ulaya kule wanakuja kuchukua miti yetu huku na anaenda kutengeneza dawa, sisi ndugu zangu tupo wapi na nchi hii ina watalaam ambao ni wabobezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali yangu Tukufu kwamba, hebu sasa watalaamu wakae na sisi tuhakikishe kwamba tunaenda kujenga viwanda, then tunaenda kutengeneza dawa zetu, ukizingatia sasa hivi deni, Wizara ya Afya inadaiwa na MSD mamilioni ya fedha, karibu asilimia 93 za dawa zinatoka nje, lakini tukishajenga viwanda vyetu hivi kwa sababu raw materials zetu tunazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi niishauri Serikali kwa kweli isichukulie jambo la mzaha kwamba asilimia 93 hizo hatuwezi tena kwenda kuzichukua nje tuna uwezo wa kujenga viwanda vyetu hapa na dawa za kutosha zikatengenezwa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo niiombe Serikali iwe serious juu ya jambo hili, kwa sababu watu wanasema sijui nini taharuki ndiyo maana sasa hivi hapa hatuvai barakoa kwa sababu dawa za Corona zipo kwa watu ambao ni watalaam wa dawa za asili. Kwa hiyo, Serikali iwashike mkono watu hawa, iwaboreshee ili pato la Serikali hususan Wizara hii kama inaingiza asilimia 17, basi naamini itapiga mara mbili asilimia 34. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali iwe serious juu ya jambo hili, iwashike mkono watu hawa ili wazungu nao washike adabu kwetu, wajue kabisa kwamba Watanzania nao kumekucha, siyo wachukue mizizi yetu, waende wakatengeneze dawa then waje watuuzie sisi. Mfano, nchi ya Nchi ya China, Bara la Asia inatengeneza dawa zao za asili, lakini sisi tunakimbia kivuli chetu, kwa nini? Hivi tumerogwa na nani, namwomba sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili ili akae na wataalaam kama sisi na watalaam hao tunaamini wa nchi hii ni waelewa na wana uwezo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu sasa ingekuwa Wizara haina…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imegonga.

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, pia nimpongeze Waziri na timu yake yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi katika kada zetu mbalimbali, kwa Wilaya ya Lushoto kuna upungufu kwenye kada ya afya na elimu zaidi ya watumishi 11,000 hawa ni katika kada mbili, bado kada nyingine. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwa kipindi hiki cha bajeti Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto iweze kupata walimu hao niliyoorodhesha hapo juu, hasa ukizingatia Wilaya ya Lushoto ina shule nyingi pamoja na vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa TASAF unasaidia sana wananchi wetu, lakini kunakuwa na changamoto hasa kwa watu wa vijijini wengi wao kutopata fedha hizi za TASAF na ukikuta baadhi ya wanaopata unakuta wengi wao sio walengwa, hii inatutupia lawama sisi Wabunge. Lakini pia pesa za TASAF ziwe na account yake tofauti na ilivyo kwa sasa na pia inaleta mkanganyiko hasa pale pesa zinapoingia, zinachukua muda mrefu kuzipeleka kwa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niiombe Serikali ipeleke pesa hizi vijijini kwani huko vijijini ndiyo kuna wahitaji zaidi kuliko mjini, pia fedha hizo ziongezwe kiwango wanachopewa ni kidogo mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko mengi kwa wastaafu wetu hawapewi stahiki zao kwa wakati pindi wanapostaafu, unamkuta mstaafu anafuatilia mafao yake zaidi ya miaka miwili mwisho wa siku anafariki bila kupata mafao yake na ukizingatia wengi wanaostaafu hawana kazi nyingine ya kufanya. Kwa hiyo, mstaafu huyu unamkuta maisha yake yanakuwa ni ya taabu na mwisho wa siku humpelekea kuiaga dunia. Niiombe Serikali yangu tukufu iwalipe wastaafu wetu hawa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wengi wanahama kwenye Halmashauri kwa sababu ya kupata mshahara mdogo tofauti na idara nyingine, mfano sasa hivi watumishi hao wanakimbilia kwenye mashirika kama TANESCO, TARURA, TPDC na TASAF, kwa hiyo huku wanapata mishahara mikubwa kuliko hawa wa Halmashauri, ukizingatia elimu zao ni sawa.

Kwa hiyo, niiombe Serikali iweke uwiano sawa wa mishahara ili kuondoa ubaguzi na sintofahamu na kufanyakazi kinyoge kwa hawa watumishi wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia afya na nguvu ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu na kuweza kuchangia.

Pili, niunge mkono hoja taarifa zote mbili kwa maana Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nijikite sehemu moja tu; Bunge la Bajeti la mwaka jana Tume ilipewa shilingi bilioni nne, lakini baada ya Kamati yetu kuangalia fedha zile hazionekani. Kama unavyojua ipo haja kubwa sana na changamoto sana katika kupima ardhi yetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi sijajua zimekwama wapi, fedha sijajua zimekwama wapi kwa sababu fedha hizi zingetolewa kwa wakati zingeenda kupima zaidi ya vijiji 600. Hata hivyo kwenye vitabu fedha hizi hazionekani. Niiombe Serikali au Wizara ifuatilie fedha hizi ili ziweze kutolewa ziende kufanya kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye fedha walizopewa Wizara ya Ardhi ambayo ni pesa ya uimarishaji wa usalama wa ardhi. Pesa hizo ambazo ni shilingi bilioni 345, fedha hizi ni nyingi sana, lakini ukiangalia walichopanga hapa ambayo ni KKK yaani Kupima, Kupanga na Kumilikisha, wamepewa asilimia asilimia 25 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweke legacy na tuweke historia katika Bunge hili la Kumi na Mbili chini ya Spika wetu makini Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika Mheshimiwa Mussa Zungu na ninyi Wenyeviti wawili yaani wewe Mheshimiwa Najma Giga na Mheshimiwa Kihenzile, lazima fedha hizi sasa zifanyiwe review ili fedha hizi ziende kupima ikiwezekana kupima nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani naongea hivyo, ukiangalia sasa hivi migogoro ya wakulima na wafugaji ni mingi sana, lakini ukienda mbali zaidi ni kwamba nchi hii haijapimwa, lakini ukikusanya pesa hizi zote zikaelekea kupima ardhi nchini, tayari tutakuwa tumesaidia wananchi wetu kwa asilimia 100 na hili suala wala hatutalirudia tena katika kupima, kupanga na kumilikisha tutakuwa tumekwisha maliza kazi kama Mheshimiwa Chege alivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yako tukufu, Bunge hili la Kumi na Mbili, Waheshimiwa Wabunge kwa pamoja tuombe hata kwa Mwenyezi Mungu mapendekezo haya yaridhiwe, pesa hizi ziende katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchini ili tuondokane kabisa na tatizo hili kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye TANAPA; ni kweli TANAPA wanafanya kazi moja nzuri sana na kwa kweli watu hawa wanastahili kuongezwa fedha na ukizingatia mwaka 2017 waliongezewa hifadhi sita kwa maana ya 16 ongeza sita ni 22, bado ina maana fedha walizotengewa bado bajeti ni ile ile. Lakini bila kusahau TAWA hawa watu wa TAWA wanafanaya kazi kubwa sana. Watu hawa ukiangalia ndio wanapambana na wanyama wakali na waharibifu, lakini watu hawa hawajapewa fedha na wameongezewa mapori tengefu zaidi ya matano, lakini ceiling bado ni ile ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Bunge lako hili lipendekeze TAWA kuongezwa fedha ili waende kufanya kazi hii ambayo ni kujenga vizimba maeneo yote, kwa mfano sasa hivi tunavyoongea katika Kamati yetu mwaka 2019 mpaka sasa hivi wamejenga vizimba 15 tu, just imagine, wakati huo vizimba vile vinasaidia wanyama wakali na waharibifu kutoingia kwa wananchi wetu. Wananchi wetu wanadhurika. Niiombe Serikali itenge fedha za kutosha wapewe TAWA watu hawa wana kazi kubwa sana, wanafanya kazi nzuri mno. Waongezewe fedha ili tutoe migogoro ya wakulima, wanyama wakali kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo twende kwenye mahoteli yetu; kuna hoteli 23 na lodge ambazo nne ziko katika hifadhi, lakini hoteli zinazofanya vizuri ni zile ambazo zimebinafisishwa tu. Hata hivyo zote zaidi ya hoteli 10 hazifanyi vizuri. Ina maana hoteli zile zinaenda ku-corrupt kabisa, nyingine zimebaki kama magofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua mama yetu Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Royal Tour yake imejibu. Kuna wazungu, kuna watalii chungu nzima, lakini ukija kuangalia kwenye hoteli zetu hizi zime-corrupt hazifanyi vizuri, zimekufa, kwa maana hazipo. Wakati watalii wale wanahitaji hoteli nyingi, hoteli zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi niliombe Bunge hili lipitishe mapendekezo wanyang’anywe wawekezaji wale ambao wamehodhi hoteli hizi wapewe watu wengine ambao wana uwezo wa kuendeleza hoteli hizi. Ukiangalia kwenye Kamati yetu hoteli hizi zimepewa watu ambao hawana uwezo. Unakuta mtu amepewa hoteli halafu anaandika kukarabati zaidi ya miezi sita. Kukarabati zaidi miezi sita hii sio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ipitishe mapendekezo haya hoteli zile wale wawekezaji wananyang’anywe na wapewe watu ambao ni wenye uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na mfumo wa ILMIS; mfumo wa ILMIS tangu mwaka 2018 nadhani mpaka sasa hivi uko katika mikoa miwili tu kwa maana ya Dar es salaam na Dodoma, lakini bado mfumo ule haufanyi vizuri, niiombe Serikali yako sasa itoe fedha za kutosha ili mfumo huu ukae vizuri ili kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji; vijiji na vijiji; migogoro ya Wilaya na Wilaya; migogoro ya Mikoa na Mikoa na hata migogoro ya Taifa na Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri Ummy pamoja na Naibu Waziri wake pamoja na timu yote kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwatumikia Watanzania bila kuchoka. Mwenyezi Mungu atawalipa ujira wao huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lushoto kuna Kituo cha Afya kimoja tu ambacho kipo Mlola na kituo kinahudumia zaidi ya kata nane, na hii imepelekea mrundikano wa wagonjwa. Hivyo basi niiombe Serikali yangu tukufu ipandishe hadhi Zahanati ya Makanya kuwa Kituo cha Afya kwani hii itapunguza mrundikano wa wagonjwa na kuokoa vifo vya wananchi hasa vifo vya mama na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana ya gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Mlola. Niiombe Serikali yangu katika bajeti hii mtutengee pesa kwa ajili ya kununua gari la wagonjwa kwani tunapoteza wananchi wengi hasa akina mama wajawazito pale wanapohitaji usafiri kwenda katika Hospitali ya Wilaya na kama unavyojua miundombinu yetu ya barabara sio mizuri kabisa. Kwa hiyo kunahitajika gari la wagonjwa ambalo ni kwa ajili ya kubebea wagonjwa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kuwa Jimbo la Lushoto kuna kituo cha afya kimoja lakini wananchi wamejitolea na kuanza kujenga vituo vya afya viwili ambavyo ni Kituo cha Afya Gare na Kituo cha Afya Ngwelo. Hivyo basi, naomba safari hii Serikali ivitengee pesa ambazo zitatosha kumalizia vituo hivyo ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya na ni pamoja na kuendelea kuokoa vifo vya mama na mtoto ukizingatia vituo hivi vipo mbali na Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto za vifaatiba katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto ambavyo ni ultra sound, x-ray machine ni ndogo haina uwezo. Kwa hiyo, inaharibika mara kwa mara hii imepelekea wagonjwa wengi kukosa huduma na kupata usumbufu wa kwenda na kurudi na ukizingatia wagonjwa wengi wanatoka mbali. Kwa hiyo, niiombe Serikali ipeleke vifaa hivyo ili kuokoa vifo vya wananchi ambavyo vinaweza kuzuilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la watumishi katika kada ya afya, niiombe Serikali ipeleke watumishi wa kutosha katika zahanati zetu pamoja na vituo vya afya pamoja na Hospitali ya Wilaya. Wananchi wengi wamejenga zahanati kwa nguvu zao mpaka nyingine zimeisha, lakini watumishi ni shida mpaka zahanati hizi kuelekea kuwa magofu na hii inapelekea kuwavunja nguvu na kuwakatisha tamaa. Naomba Serikali iajiri watumishi haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiofichika kuwa katika vituo vyetu vya afya na katika hospitali zetu za wilaya chanjo ya kichaa cha mbwa ni gharama, na siyo gharama tu pia haipatikani. Kwa hiyo, niiombe Serikali ipeleke chanjo hiyo ya kichaa cha mbwa katika hospitali zetu pamoja na vituo vya afya mpaka kwenye zahanati ili kuokoa wananchi wanaopata ajali ya kung’atwa na mbwa. Tumekosa na kupoteza wananchi wengi waliopata ajali hizo za kung’atwa na mbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa muhimu hazifiki kwenye zahanati zetu vituo vya afya pamoja na hospitali ya wilaya, kwa mfano dawa za kisukari hizi ndio kabisa. Mimi kama Mbunge nimepata malalamiko mengi sana hasa kwa wale wazee ambao wanatibiwa bure. Niishauri na kuiomba Serikali yangu ipeleke dawa hizi muhimu hasa katika zahanati, vituo vya afya na katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na hotuba yake nzuri iliyojaa kutatua kero za elimu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali yangu tukufu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Ili kuendeleza juhudi hizi niishauri Serikali iwape vitendea kazi wakaguzi wa elimu katika Wilaya kwani idara hii ndiyo ambayo itakayoweza kusimamia hili suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali ijenge vyuo vya VETA katika kila Wilaya kwani itakuwa mkombozi kwa watoto wetu wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari walioshindwa kuendelea na masomo, kwani watoto hawa wakipitia kwenye vyuo vyetu vya VETA walio wengi watakuwa wanajiajiri wenyewe kupitia maarifa waliyoyapata kwenye vyuo vyetu vya VETA. Hii itakuwa mwarobaini kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali iangalie stahiki zote za walimu. Kuna malimbikizo makubwa ya walimu ambayo bado hawajapewa na walimu hawa wananung’unika, hili si jambo zuri kwa walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo walimu wanaoishi vijijini wanaishi katika maisha magumu sana. Kwa sababu hiyo, niiombe Serikali yangu tukufu ijenge nyumba za walimu hasa waishio vijijini pamoja na kumalizia madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na maabara. Wananchi wameshajenga maabara hizo na kazi iliyobaki ni upande wa Serikali pamoja na kuongeza walimu wa kutosha katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na baadhi ya watendaji katika Halmashauri kuingilia kazi za wakaguzi. Niiombe Serikali itoe tamko kwa watendaji hawa kutoingilia kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kuwa wanafunzi wote wakatiwe bima ya afya, hasa kwa wale wambao wanaishi boarding. Serikali ihakikishe watoto hawa wanapata bima hiyo ili waweze kupata matabibu bure kwani hii inaleta usumbufu mkubwa hasa kwa walimu, maana inatokea mtoto anaumwa na mwalimu mnamkuta hana hela na mwalimu hawezi kumuacha mwanafunzi kumpeleka hospitali atakopa au atatumia maarifa yake kuhakikisha mtoto anapata matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali yangu ipunguze masharti ya kusajili shule hasa hizi za msingi. Hata ikiwa shule hizi zina madarasa mawili isajiliwe tu ili kuondoa usumbufu kwa watoto wetu hasa kwa wale wanaokaa mbali na shule na hii itapuguza watoto kutotoroka shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Elimu ya Watu Wazima; elimu hii ni muhimu sana kwani ilifika mahali watu wazima wasiojua kusoma na kuandika ilipungua mpaka asilimia sita ya Watanzania, lakini sasa hivi imeongezeka mpaka kufikia asilimia 30. Hii ni ishara ya kuwa elimu hii haitiliwi mkazo katika Taifa letu. Hivyo basi niiombe Serikali itilie mkazo elimu hii ya watu wazima, ukizingatia sasa hivi kuna mfumo mzuri wa kuwafundisha watu wazima na wale watoto ambao wameshindwa kabisa kusoma na kuandika, inaitwa Graph Game.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe ni shahidi kwani wadau wa GG walikuja mpaka kwako na wadau hawa wamesaidia sana katika Jimbo la Lushoto kwa baadhi ya shule kwani kuna watu wazima zaidi ya 200 kwa sasa wanaojua kusoma na kuandika. Pia kuna watoto ambao walishindikana kabisa kujua kusoma na kuandika, lakini walivyotumia mfumo wa Graph Game sasa hivi wanajua kusoma na kuandika na ndio wanaoongoza madarasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niishauri Serikali yangu tukufu iwasaidie wadau hawa ili waweze kukomboa watoto wetu pamoja na watu wazima hawa. Serikali iwajengee uwezo wadau hawa wa GG na hili Mheshimiwa Waziri ili ulione kuwa ni mkombozi wa Watanzania naomba upange ziara ya kutembelea Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la michezo shuleni, hii elimu ya michezo haitiliwi umuhimu wakati tunajua kama michezo ni taaluma kama taaluma nyingine. Kwa hiyo, kujengwe vyuo vya michezo au hivyo hivyo vya VETA vifundishe na somo la michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Lushoto hasa katika Kata za Kwai – Makanya, Kilole, Malibwi Kwekanga, Mbwei, Ngulwi, Ubiri Gare pamoja na Kwemashai. Maeneo yote haya yana shida kubwa mno ya maji. Hivyo basi, naomba Serikali yangu iangalie kwa jicho la huruma kabisa kutupatia fedha kwa ajili ya kunusuru wananchi hawa hasa akina ama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali yangu tukufu kwa kunipatia pesa shilingi milioni 770 kwa ajili ya maji katika Mamlaka ya Maji Lushoto, lakini pesa hizi hazitoshi kwani zinajenga banio moja na kisima kimoja chenye ujazo wa lita 600,000. Kwa hiyo, naiomba Serikali iongeze pesa ili kazi hii inayoendelea kufanyika iende sambamba na usambazaji wa maji yaani tupatiwe fedha kwa ajili ya kununua bomba na kutoa mabomba ya zamani ambayo ni ya tangu mkoloni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kuna Kata mbili za Ngulwi na Ubiri; kata hizi huwezi kuzitenganisha na Mradi wa Mamlaka ya Maji Lushoto, kwani kata hizi zipo chini ya mji wa Mamlaka ya Mji Lushoto na mradi huo unaelekea maeneo hayo ya kata hizo mbili. Hivyo basi, naiomba Serikali ituongezee fedha ili mradi huu uunganishwe na kata hizo mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu hasa waishio katika Mamlaka ya Mji hubambikiwa bili. Hivyo basi, naiomba Serikali ilichukue suala hili na kutoa hatua kali za kisheria maana watu hawa wa Idara ya Maji wananyanyasa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ngulu umefanyiwa hujuma na Mkurugenzi wa Halmashauri baada ya kumsimamisha mkandarasi wa kwanza bila kufuata utaratibu na akampa mkandarasi mwingine bila kutumia utaratibu kwa minajili ya kupewa asilimia 10. Hii imepelekea mpaka sasa hivi mradi ule kusimama na wananchi wamekosa huduma mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni shahidi, alikuja na kutoa maelekezo na baadhi ya Madiwani na Mwenyekiti wa Kijiji walimpongeza Mkurugenzi yule lakini akawaambia msimpongeze bado ni muda mfupi aliokaa. Hili limekuwa kweli. Hivyo basi, naomba Mheshimiwa Waziri atume timu yake ikatoe mwelekeo au yeye mwenyewe akamalize suala hili ili wananchi waweze kupata huduma hii muhimu ambayo wanaisubiri kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naunga mkono kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji Vijijini kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa Mtumbi, huu mradi ni wa muda mrefu lakini mpaka sasa mradi ule bado hauna hata dalili ya kuanza na sasa ni takribani miaka sita imeisha. Naiomba Serikali ipeleke pesa ili mradi huu uweze kuanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu tukufu itujengee mabwawa hasa katika maeneo ya Mazashai, Mbwei, Makanya Kwai, Kwemakame, Boheloi, Mshangai, Ubiri na Mazumba kwani katika Wilaya ya Lushoto kuna mito mingi sana inayopeleka maji sehemu za mabondeni na maji haya kuharibika tu wakati wananchi wana shida kubwa ya maji. Hivyo basi, kwa kujenga mabwawa, itasaidia wananchi kupata maji ya kunywa pamoja na kulima kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Lushoto wana hali mbaya sana hasa wananchi waishio Kwemakame, yaani mpaka sasa wananunua ndoo ya maji shilingi 1,000. Nakuomba eneo hili uliangalie kwa jicho la huruma kwani imekuwa ni kilio changu kila tunapokutana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwa kuhakikisha tunafikia uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali iwekeze sana katika kilimo ili tuweze kupata malighafi kutoka kwenye mazao yetu ambayo tunayalima sisi wenyewe, kwani bila kuwekeza katika kilimo tutakuwa tunachelewa sana kuwa na viwanda. Niendelee kuishauri Serikali yangu tukufu ipeleke pembejeo za kutosha kwa wakulima na kujenga mabwawa ya kutosha ili wananchi waweze kulima kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima tuhakikishe wananchi wanapata elimu ya ufundi hasa kwa vijana wetu wa Kitanzania ili wawe na uelewa wa kutosha katika suala zima la kusimamia viwanda vyetu tunavyo kusudia kuvijenga. Hivyo basi, Serikali ijenge Vyuo vya VETA kila Jimbo na sio kila Wilaya, kwa mfano Wilaya ya Lushoto tangu ianzishwe haina Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kupoteza rasilimali watu na sio hivyo tu pia tunakosa vijana wenye taaluma ambao hawataweza kusimamia viwanda vyetu. Lakini hatujachelewa tuanze sasa kujenga vyuo hivyo ili vijana wetu waende sawa na ajira ya ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kuanzisha Viwanda Vidogo Vidogo yaani SIDO kwani viwanda hivi kwanza vitainua kipato cha mtu mmoja mmoja, pili, uchumi katika sehemu husika kilipowekwa utakuwa na tatu, vijana wengi watapata ajira pamoja na kupata ujuzi hapo hapo. Kwa hiyo, niendelee kuishauri Serikali kuanzisha viwanda vidogo vidogo hivi katika kila Kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga ulikuwa ni Mkoa wa viwanda lakini sasa viwanda vingi vimekufa. Hivyo basi, niiombe Serikali iweze kurudisha viwanda vile vyote vilivyo kufa hasa kiwanda cha sabuni, nondo na kiwanda cha mbolea. Ni imani yangu viwanda hivi vikifufuliwa Tanga tutakuwa tumepiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuongelea uchumi wa viwanda kama barabara zetu ni mbovu, maji hakuna na umeme haupo. Kwa hiyo, hebu tupeleke miundombinu hii, kwani hii ndiyo itatufikisha katika uchumi wa viwanda bila hivyo tutachelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto ni Wilaya inayojulikana kwa kuzalisha matunda na mboga mboga lakini cha kushangaza Serikali haijawahi kufikiria kuweka viwanda Lushoto. Hivyo basi niiombe Serikali yangu iweke viwanda Lushoto hasa viwanda vya matunda na mboga mboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wawekezaji, wapo wawekezaji wazuri na wabaya kwa mfano Lushoto kuna Kiwanda cha Miwati. Lakini kiwanda kile hakifanyi vizuri kwa sababu hakiwalipi mishahara wafanyakazi wake. Kwa hiyo, hili linasikitisha sana, kwani sera ya sasa hivi ni ya viwanda lakini kiwanda hiki kimekuwa hakina manufaa kwa wananchi wa Lushoto. Zaidi ya kuwanyanyasa wafanyakazi wake. Kwa hiyo, niiombe Serikali ifuatilie suala hili kwa haraka ili wafanyakazi hawa waweze kulipwa stahiki zao. Pamoja na kujua mwenendo mzima wa uendeshaji wa kiwanda hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali yangu tukufu kwa kuwa tunahitaji wawekezaji kwa wingi na tunawapenda wafanyabiashara wetu. Hivyo basi, ipunguze haya malalamiko yanayo lalamikiwa na wawekezaji pamoja na wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na hotuba iliyojaa matumaini ya kuendeleza wakulima na hatimaye kuvuna mazao yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa ni zao kuu la biashara ambalo linaingiza pesa za kigeni, lakini zao hili sasa hivi ni zao ambalo haliangaliwi wala halina tija tena. Hivyo basi niishauri Serikali yangu ipeleke miche ya kutosha ya kahawa ili kuweza kufufua zao hili na pia zipelekwe pembejeo pamoja na zana zote zinazohitajika katika kilimo hicho. Pamoja na hayo Serikali ihakikishe inawapa miche bure kuisimamia kwa karibu. Pia Serikali inatakiwa itafute masoko ili mkulima huyu aweze kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua zao la kahawa lina hatua nyingi, mpaka kufikia kuvuna na kuuza inakuwa imegharimu pesa nyingi. Kwa hiyo, bila kutafuta soko zuri wakulima hawa watakata tamaa na kuacha kabisa kulima zao hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto ilikuwa inatoa zaidi ya tani 300,000 lakini zao hili limeshuka. Kwa sasa huwezi kupata hata tani 50 kwa msimu na bado uzalishaji unazidi kushuka. Yote haya yanasababishwa na kushuka kwa bei ya zao hilo na wakulima kuacha kahawa ife yenyewe mashambani. Pia mibuni mingi ni ya zamani kwa hiyo imezeeka na kufa na kuzaa mazao kidogo sana. Hivyo basi kuna uhitaji mkubwa sana wa kupeleka miche ya kutosha katika Wilaya ya Lushoto ili kufufua zao hili ambalo ndilo mkombozi wa wananchi wa Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto ni Wilaya ya wakulima wa mboga mboga na matunda na katika Halmashauri ya Lushoto mapato mengi yanatoka huko. Hivyo basi ipo haja kubwa ya kuwaangalia wakulima hawa ili nao waweze kupata pembejeo au kuwapunguzia bei ya dawa kwani wakulima wananunua dawa kwa bei ya juu sana na ukizingatia magonjwa ya mboga mboga yanaongezeka kila kukicha hasa huu ugonjwa wa kantangaze unasumbua sana wakulima hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mkulima aweze kulima kwa uhakika kama Ilani ya Chama chetu inavyosema, kwamba kilimo ndio uti wa mgongo, ni lazima tuwaandalie wakulima wetu mazingira ya kila hitaji.

Kwanza, lazima kujengwe mabwawa ya kutosha kila kijiji ili waweze kulima kilimo cha umwagiliaji; pili, lazima wapate zana za kilimo kwa wakati; tatu, pia lazima watengenezewe miundombinu ya barabara ili wasafirishe mazao yao kwa wakati na nne, kuwapatia pembejeo za wakati. Yakizingatiwa yote haya naamini yatatimiza ndoto yetu ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda na viwanda vyetu kupata malighafi katika mazao yetu haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la kurudisha vyama vya ushirika. Hili suala litakuwa ni gumu sana kusimamia kwani ushirika hawa ndio waliotufikisha hapa tulipo na ushirika hawa wana madeni makubwa sana na imefikia hatua benki zimefilisi baadhi ya mali za vyama hivyo. Leo hii mnataka ndio wanunue mazao ya kulima, hili ni suala ambalo wakulima wamelikataa, kuuza mazao yao katika vyama hivyo. Suala hili lingewezekana kama Serikali ingejenga imani kwanza kwa wakulima na kwa kutoa elimu mpaka hapo wananchi watakapoelewa. Lakini zaidi ya hapo naamini zoezi hili halitafanikiwa na Serikali itazidi kupoteza fedha bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo cha katani katika Mkoa wa Tanga, zao hili la katani ni zao ambalo kwa sasa lina soko zuri, lakini lina changamoto nyingi. Hivyo basi niiombe Serikali iliangalie zao la katani kwa jicho la huruma kwani zao hili tayari lipo vizuri sasa na litaingiza fedha za kigeni, pamoja na soko la ndani lipo kwa kufufua viwanda vyetu vya magunia, kwa hiyo, Serikali ipeleke vifaa vya kilimo katika zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali iunde vikundi vya vijana na kuviwezesha mitaji na kuwawekea miundombinu wezeshi ili vijana hawa waweze kulima katika vikundi. Hii itatoa fursa ya vijana kujiajiri na kuacha kukaa vijiweni. Pamoja na hayo niishauri Serikali ianzishe benki za kilimo katika kila mkoa kwani hii itarahisisha wakulima wetu kupata mikopo kwa wakati na bila kwenda mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya. Suala zima la upandaji miti katika maeneo yetu yaliyo wazi pamoja na maeneo yaliyoungua. Niishauri Serikali yangu kuwa na mpango mkakati wa kuhakikisha miti inapandwa kwa wingi na si kupanda tu pamoja na kuitunza mpaka ikue pamoja na kuwapa miche bure. Pia kuna misitu iliyoungua katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Lushoto.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali ikapande miti katika maeneo hayo hasa Lushoto katika Misitu ya Magamba, Shume, Gara, Irente; maeneo yote yameungua tangu mwaka 2004 mpaka sasa kumeota tu majani bila miti. Kwa hiyo maeneo haya ni muhimu sana yarudishiwe miti ya asili ili kurudisha mandhari na uoto wa asili uliopotea. Wananchi wa Lushoto wapo tayari kupanda miti isipokuwa hawana uwezo wa kununua miche hiyo. Hivyo basi niiombe Serikali itenge mafungu ya kununua miche ya miti ili kuwapa wananchi hao.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la kuungua kwa misitu hii inatokea kila wakati lakini uzimaji wa moto unategemea wananchi. Kwa hiyo, niiombe Serikali inunue ma-grader ili yakachimbe barabara maeneo ya msituni ili janga la moto linapotokea iwe rahisi kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, katika zao la misitu kuna tozo zaidi ya 32. Tozo hizi zimewaathiri sana wafanyabiashara kiasi kwamba mpaka sasa mgao wanaopewa umesimama kwa sababu gharama zenyewe zimepanda, ambapo kwa square meter 100 ni shilingi 10,000,000 tofauti na mwaka 2016 – 2017 ilikuwa square meter shilingi 6,000,000 ukichanganya na hizo tozo gharama inakuwa kubwa sana ambayo haiendani na bei ya soko.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali, zao la misitu ni sawa na mazao mengine, kwa hiyo tozo hizi zipungue kama mazao mengine ya kahawa, pamba, korosho na tumbaku kwa sababu hii imesababisha wafanyabiashara hao kununua miti kwa watu binafsi kwani huko bei ni nzuri. Changamoto yake ni kwamba wanauza miti ambayo haijakomaa na hii itasababisha nyumba zetu hatimaye kwenda na upepo maana mbao zilizoezekea si imara.

Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali kwa kuziacha hizi mashine ndogo za kuchania mbao ziendelee mpaka hapo zitakapoisha zenyewe. Hivyo basi nikuombe Waziri wetu utakaposimama na kujibu hoja naomba hili ulisemee kwani kuna watu wengine wamezisimamisha na kazi zao kusimama. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba tamko juu ya hili. Mashine hizo zinaitwa Dindon.

Mheshimiwa Spika, pia wafanyabiashara hao wana group lao la LMDA, hili linatoa pesa kwa ajili ya kupanda miti lakini cha kushangaza mchango huu hautambuliwi.

Wadau hawa ni watu muhimu na wanastahili kupunguziwa pamoja na kuwaangalia kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, niunge mkono ushauri wa Kamati kuhusu kuweka miundombinu ya barabara katika mapori ya Biharamulo, Burigi na Kimisi pamoja na vifaa vya kazi, magari, wafanyakazi pamoja na nyumba za wafanyakazi bila kusahau kuweka mazingira mazuri kwa ujumla ili kuweza kuvutia watalii wetu watakaokuja. Hivyo basi niishauri Serikali iharakishe kazi hii ili Serikali iweze kuongeza pato la Taifa kupitia mapori hayo. Pia imekuwa ni jambo la furaha sana na la kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kujenga Uwanja wa Ndege wa Chato, uwanja huu utakuwa umepandisha hadhi mapori haya matatu, Mwenyezi Mungu ambariki sana Rais wetu kwani kazi anayoifanya ya kuwatumikia Watanzania inaonekana dhahiri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais wetu pamoja na Watanzania wote. Amen
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri Mheshimiwa Mwigulu pamoja na timu yake yote kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Lushoto kilijengwa toka mwaka 1890 na kimejengwa na mkoloni. Mpaka sasa hakijafanyiwa hata ukarabati lakini DC anayeitwa Majidi Mwanga alipata pesa kupitia wafadhili na kujengwa jengo moja la utawala ambalo limejengwa mpaka kufikia usawa wa lenta. Mpaka sasa ni miaka minne imepita bado jengo liko vile vile na linazidi kunyeshewa na mvua. Kwa hiyo, niiombe Serikali ipeleke pesa za kumalizia jengo lile ili lisije likaangushwa na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, kuna shida kubwa sana ya nyumba za watumishi. Nyumba zile za polisi ni za tangu mkoloni, zimechoka mno hazistahili kuishi askari wetu. Pamoja na hilo, askari wameamua kujenga nyumba za mabanzi ili waweze kuishi humo lakini kiuhalisia nyumba hizo za mabanzi hazistahili kuishi askari wetu ambao wanafanya kazi ngumu mno. Hivyo basi, niiombe Serikali angalau askari wetu wapate hata nyumba tano.

eshi la Magereza nalo gereza lao ni la muda mrefu pamoja na nyumba wanazoishi askari wetu siyo nzuri kabisa na hata nikisema hazistahili kuishi askari namaanisha. Hivyo basi, niiombe Serikali yangu Tukufu iiangalie Lushoto kwa jicho la huruma ili tuweze kuokoa maisha ya askari wetu. Kwani kwa maisha wanayoishi askari wetu wanaweza kupata magonjwa na kuhatarisha maisha yao ukizingatia nyumba zile walizojenga hazina hata sehemu ya kuchimbia choo kwa ujumla nyumba zile hazina vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jiografia ya Lushoto inajulikana kuwa ni ya milima na mabonde na wilaya nzima ina wakazi zaidi ya milioni moja lakini Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Magereza hawana vitendea kazi. Hivyo basi, niiombe Serikali yangu ipeleke magari kwa ajili ya askari polisi na askari magereza. Hasa hawa magereza hawana kabisa magari wanapata tabu sana hasa katika utafutaji wa kuni. Hii imepelekea wafungwa kutembea umbali mrefu kufuata kuni na hii ni hatari kwa askari wetu wanaweza kutorokwa na wafugwa. Kwa hiyo, Serikali ituangalie Lushoto kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tabia ya askari wetu wasio waaminifu kuwanyanyasa raia wetu kwa kuwalazimisha wawape rushwa. Wakikataa au kama hawana ndiyo wanaanza kuwabambikia kesi au kuwapiga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, askari wetu hawa hasa hawa askari trafiki wanawanyanyasa vijana wa bodaboda na vijana wanaoendesha Noah. Imefikia hatua hata kama dereva amepaki gari askari hutoa plate namba za gari tena kwa kuitoa kwa nguvu hadi ikatike na kusababisha uharibifu wa plate namba hiyo. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu ikemee kitendo hiki kinachofanywa na askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu Tukufu itujengee vituo vidogo vya polisi katika maeneo ya Makanya – Kwemakame na Gare, kwani maeneo haya yana watu wengi sana na pia ndiyo maeneo ambayo yana matukio mengi ya kihalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali yangu Tukufu, hizi pesa zinazokusanywa vituo vyetu vya polisi zote zisiende Serikali Kuu. Angalau zibaki hata 30% ili vituo vyetu viweze kukidhi mahitaji yao madogo madogo kama mafuta ya magari na kununua stationary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitambulisho vya Taifa, kazi hii inasuasua sana na huku wananchi wetu wanatuuliza kila siku. Hivyo basi, niiombe Serikali yangu ihimize mamlaka hii inayoshughulika na vitambulisho hivyo iongeze kasi hasa katika maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa TAMISEMI pamoja na Manaibu Mawaziri wake. Wananchi wengi wamejenga maboma mengi ya zahanati, shule, nyumba za Walimu pamoja na vituo vya afya na maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, maboma haya yamekaa muda mrefu bila kuendelezwa na kama Serikali inavyosema kuwa wananchi wanapojenga maboma na wakafikia kwenye mtambaa wa panya (lenta) Serikali inaendeleza, lakini mpaka leo kuna maboma mengine yanakuwa magofu. Kwa hiyo niiombe Serikali ipeleke fedha za kutosha ili kumalizia maboma haya ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna vituo vya afya viwili vinavyojengwa kwa nguvu za wananchi, vituo hivyo ni Kituo cha Gare na Gwelo. Kituo cha Gare tayari kimeshajengwa maboma manne ambayo yako kwenye hatua tofauti. Jengo la kwanza ni OPD hili limeshapigwa bati, ward mbili nazo zimeshapigwa bati na ward nyingine mbili zipo kwenye kujengwa msingi. Kituo cha Afya Nawelo hiki kina jengo moja la OPD ambalo lipo kwenye mtambaa wa panya (lenta). Kwa hiyo niiombe Serikali itupatie fedha kama vinavyopatiwa vituo vya afya vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lushoto lina kituo cha afya kimoja tu ambacho kipo Mlola na niishukuru Serikali yangu tukufu kwa kutupatia shilingi milioni 700 kwa ajili ya kupanua kituo pamoja na kupata vifaa tiba. Hata hivyo, kituo cha afya kile kina changamoto ya gari la wagonjwa na ukizingatia kituo cha afya kile kina zaidi ya kilomita 53 kufika katika hospitali ya wilaya. Kwa hiyo gari hii itakuwa ni muhimu ili kuokoa vifo vya akinamama na watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida kabisa kwa halmashauri kutotenga 10%. Kwa hiyo niiombe Serikali ihakikishe halmashauri zinasimamiwa ipasavyo kwa suala zima la kutoa 10%. Kwani halmashauri nyingi hazitengi pesa hizi kwa viburi walivyokuwanavyo watendaji wachache wasiolitakia Taifa letu mema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa zilizotengwa kwenda TARURA 30% ni ndogo sana wakati mahitaji ya barabara ni makubwa hasa kwa vijijini. Kama unavyojua uchumi mkubwa wa wananchi unatoka kwa wakulima ambao wapo vijijini kwa hiyo wananchi hawa wanatakiwa waboreshewe miundombinu. Serikali iongeze ifike 50% ili angalau barabara zetu ziwe zinatengenezwa kwa wakati muafaka na kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali 20% kikamilifu kwa ruzuku inayotengwa kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya mamlaka za chini yaani vijiji na Serikali za Mitaa. Kwani hii pesa ikitengwa itasaidia kuwalipa Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa. Niishauri Serikali ianzishe Bodi ya TARURA ili Bodi hii isimamie kuanzishwa kwa Mfuko wa TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe Serikali iwezeshe halmashauri fedha ili ziweze kununua magreda kwa ajili ya kutengeneza barabara zetu za vijiji hasa kukiwa na dharura kuharibika kwa barabara hasa vijijini. Niiombe Serikali pamoja na kuishauri ifanye haraka iunde haraka mamlaka ya maji vijijini, kwani kuna uovu mkubwa sana unaofanywa na watendaji wetu na ndio maana miradi hii ya maji haimaliziki kwa wakati na mingine haifiki hata kwa robo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni takribani miaka saba sasa toka iundwe Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lushoto, lakini cha kushangaza mamlaka ile haijapewa mamlaka ya kujiendesha mpaka leo. Niiombe Serikali itoe kauli ili mamlaka ile iweze kupewa madaraka yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliyotoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Lushoto lakini mpaka sasa kituo kile hakijakamilika. Nilipofuatilia nikaambiwa fedha zimeisha na wakati jengo lipo kwenye usawa wa lenta. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu ifuatilie fedha hizo ili jengo lile liweze kuisha na kama unavyofahamu Kituo cha Polisi Lushoto ni cha tangu Mkoloni, kwa hiyo ipo haja kubwa kumalizia kituo kile.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kuna tatizo kubwa sana la nyumba za Askari Polisi na Askari Magereza. Kama nilivyotangulia kusema kuwa Kituo cha Polisi pamoja na Magereza majengo haya ni ya tangu Mkoloni na hii imefanya Askari wetu kuishi katika mazingira magumu mno. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu ipange bajeti mwaka huu ili tupate hata nyumba kidogo za wafanyakazi wa Polisi pamoja na Magereza.

Mheshimiwa Spika, sambasamba na hayo, Gereza la Wilaya Lushoto lipo katikati ya mji ambapo siyo salama kwa Askari wetu wa Magereza, kwani wanakuwa na kazi ya ziada na hii inapelekea kutoroka kwa wafungwa. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu itenge fedha ili kujenga gereza lile eneo ambalo tayari limeshatengwa la Yogoi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na baadhi ya Askari wanafanya vitendo vya kihalifu lakini yote haya ni kutokana na kukaa kwa muda mrefu katika kituo kimoja, ndiyo maana Askari hawa wanatumika na wenyeji hasa wenye uwezo wa kifedha kufanyia matukio watu ambao hawana hatia, hasa kuwabambikia kesi, ili mradi tu hakupewa rushwa na mhusika. Kwa hiyo, niishauri kama siyo kuiomba Serikali kuwahamisha Askari hawa, hasa katika Wilaya ya Lushoto kuna Askari wanataka kuzeeka hapo hapo Lushoto.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wetu kucheleweshewa Vitambulisho vya Taifa, hasa wale waliopo vijijini kwani tumekuwa tukikosa majibu ya kuwajibu wananchi wetu. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu ifanye haraka iwezekanavyo, iwapatie wananchi vitambulisho hivyo na kama unavyojua vitambulisho hivyo ni muhimu katika usajili wa mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde, kwa hiyo, kwa jiografia hiyo wananchi wengi hasa wa pembezoni hawapati huduma hasa ile ya usalama pamoja na mali zao. Hii imepelekea wananchi kuvamiwa mara kwa mara na kupoteza maisha pamoja na mali zao au kujeruhiwa mwisho wa siku anakuwa ni mlemavu wa viungo. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu Tukufu ijenge vituo vidogo vya Polisi katika kila Kata ili kupunguza changamoto hizi zinazoendelea kujitokeza.

Mheshimiwa Spika, Askari wa Barabarani wamekuwa wakiwanyanyasa madereva wa magari hasa wa Noah, bodaboda pamoja na wa magari ya mizigo. Hali hii imekithiri katika Wilaya ya Lushoto. Nimuombe Waziri atume hata wataalamu wake ili wakajionee jinsi madereva wale wanavyonyanyasika, hasa hawa wa bodaboda, ukizingatia bodaboda hawa, pikipiki nyingi wamezaminiwa utakuta mwisho wa siku anarudi mtaani na kufanya vitendo vya kihalifu. Niendelee kuiomba Serikali yangu kuwasimamia vijana hawa wa bodaboda waweze kufanya kazi zao bila ya bughudha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Mheshimiwa Waziri alitoa tamko la zile pikipiki zilizokamatwa kwa makosa madogo madogo ziachiliwe lakini ukifika Kituo cha Polisi Lushoto, pikipiki hizo zimejaa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na hili ulifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwatumikia Watanzania. Ninaishukuru Serikali yangu Tukufu kwa kupata mgao wa walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Kama ujuavyo, Lushoto ni eneo lenye milima na mabonde na miundombinu yake siyo rafiki. Kwa hiyo, zipo changamoto nyingi mno za kielimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, walimu waliopangiwa Wilaya ya Lushoto katika Halmashauri ya Lushoto ni wachache sana kwani hawaendani na shule zilizopo katika Halmashauri ya Lushoto. Ukizingatia Lushoto kuna shule nyingi za msingi na sekondari zaidi ya 100 na zaidi. Kwa hiyo, naisihi Serikali yangu sikivu ituongezee walimu ili kuondoa zero katika shule zetu, kwani Lushoto tumekuwa hatufanyi vizuri lakini sababu kubwa ni ukosefu wa walimu. Kwa hiyo, kutotupa walimu wa kutosha ni kufanya watoto wetu waendelee kufeli. Naomba Lushoto iangaliwe kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Lushoto ni watu wanaojituma sana katika msaragambo, hasa wa kujenga maboma ya shule za msingi pamoja na sekondari. Wananchi wale wanakata tamaa kwani majengo mengi yamejengwa na kufikia usawa wa lenta lakini majengo yale mpaka sasa hivi hayajaezekwa na nguvu za wananchi kuharibika bure. Hii inawakatisha tamaa wananchi wetu. Kwa hiyo, naiomba Serikali ipeleke fedha kwa ajili ya kumaliza maboma yale yanayotokana na nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna changamoto za mabweni katika sekondari zetu. Lushoto kuna sekondari zaidi ya 20 hazina mabweni na hii pia inachangia sana watoto wetu kufeli, hasa kwa hawa watoto wetu wa kike kupata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu itujengee mabweni hasa katika shule za Gare Secondary, Mgambo Secondary, Malibwi Secondary, Kwemashai Secondary, Balozi Mshangama Secondary, Mdando Secondary, Mkunzi Juu Secondary; Prince Clous Secondary, Lushoto Secondary, Kitala Secondary, Ngwelo Secondary na Mariam Mshangama Secondary. Shule zote hizi hazina mabweni. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ilione hili ili tuweze kuboresha elimu katika Jimbo la Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kupandisha madaraja walimu wetu pamoja na kuwapa motisha, kwani walimu wanafanya kazi kubwa sana. Pia waboreshewe miundombinu ya nyumba zao, hasa ukizingatia Wilaya ya Lushoto shule nyingi zipo vijijini sana ambako hakuna mazingira rafiki ya kuishi watumishi wetu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Lushoto ni Wilaya kongwe, kwani wilaya hii ni ya tangu Mkoloni, lakini mpaka sasa hakuna Chuo cha VETA. Kwa hiyo, hii imechangia kurudisha watoto wetu nyuma, hasa wale wanaomaliza Darasa la Saba pamoja na wale wanaomaliza Kidato cha Nne. Hili limekuwa ni kundi kubwa linaloongezeka siku hadi siku. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu itujengee Chuo cha VETA katika Jimbo la Lushoto ili watoto wetu waweze kupata stadi za maisha. Sambamba na hilo, nimependekeza Jimbo la Lushoto kijengwe Chuo cha VETA kwani ndiyo katikati ya majimbo yote matatu ya Wilaya ya Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hizi shule shikizi, naiomba Serikali yangu sikivu iweze kusajili shule hizi, hata kama ina vyumba vinne. Nayasema hayo kwa kuwa wananchi wakiamua kuanzisha jambo lao huwa halirudi nyuma. Mfano, katika Jimbo la Lushoto nina shule shikizi mbili; Mgambo Primary School na Kaghambe Primary School. Shule hizi mpaka sasa zina vyumba sita, kwa hiyo, niombe shule hizi zisajiliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na team yake kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya. Mwenyezi Mungu awabariki sana ADDS - Head Radiology.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lushoto ni Wilaya isiyopungua takribani watu 800,000 na wote hawa wanategemea Hospitali ya Wilaya. Cha kusikitisha, hospitali hii haina huduma muhimu kama X-Ray mashine na hii imesababisha wananchi wengi kukosa huduma hiyo na ukizingatia wananchi wengi hawana uwezo wa kwenda mbali kupata matibabu. Kwa hiyo, naomba Serikali yangu Tukufu ipeleke X-Ray mashine ili wananchi wa Lushoto waweze kupata huduma hiyo kuliko iliyo sasa, kwani wananyanyasika mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu maendeleo ya jamii. Suala la huduma kwa wazee imekuwa ni mtihani sana, kwani wazee hasa wa Lushoto wanapata adha kubwa kwa kukosa vitambulisho, hasa wale ambao wapo vijijini ambako hakuna hata zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo, kuna wananchi wengi wanaoishi vijijini, hata wale ambao wanauhitaji maalum pamoja na walemavu hawapati mahitaji yao kabisa. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ipeleke dawa na vifaa tiba vyote vinavyohusika kwa watu hawa, ukizingatia vijijini hakuna zahanati wala kituo cha afya. Kwa mtaji huo, sasa Serikali itumie magari ya afya ili kufikisha huduma hii kwa walengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lushoto ni Wilaya yenye milima, kwa hiyo, hata wananchi wakitaka kufuata huduma za afya, ni lazima wafunge safari ya siku mbili au tatu hasa ikitokea mgonjwa amezidiwa na anahitaji usafiri wa gari. Hii imepelekea wagonjwa wengi kupoteza maisha hasa kwa akina mama wajawazito. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu tuangalie watu wa Jimbo la Lushoto hasa kwa Kituo cha Afya Mlola tuweze kupata gari la wagonjwa, kwani kwa sasa hali ni mbaya, wagonjwa wanapoteza maisha kila siku kwa ajili ya kukosa gari la wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naishukuru Serikali yangu Tukufu kwa kutupatia shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga majengo matano na vifaa tiba. Kwa sasa majengo yemekamilika, kwa hiyo, tunahitaji sasa vifaa tiba ili kituo chetu kianze kufanya kazi; na kwa kuwa mmeshatutengea fedha, shilingi milioni 300, naomba Serikali yangu ipeleke vifaa hivyo ili kuwahisha huduma kwa wananchi na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna upungufu mkubwa wa Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto pamoja na kwenye Vituo vya Afya na Zahanati zetu. Mfano, sasa hivi Jimbo la Lushoto nina zahanati zaidi ya sita, zote zimekamilika, zinahitaji vifaa tiba pamoja na watumishi. Hivyo basi, naiomba Serikali yangu ipeleke vifaa tiba pamoja na watumishi katika zahanati zilizopo katika Jimbo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lushoto kulikuwa na hospitali kwa watu wanaopatwa na vichaa ambayo ilikuwa inamilikiwa na Kanisa, lakini huduma ile kwa sasa haipo. Kwa hiyo basi, naiomba Serikali yangu ione ni jinsi gani ya kufufua huduma ile muhimu, maana sasa hivi watu wenye ugonjwa huo wana pata taabu kusafiri umbali mrefu; na kama inavyofahamika watu wenye kupatwa na ugonjwa wa kichaa kumsafirisha inakuwa ni shida sana. Nisisitize tana Serikali yangu irudishe ile huduma ya kituo cha watu wenye ugonjwa wa kichaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri pamoja na timu yake yote kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Wilaya ya Lushoto hasa katika Jimbo la Lushoto, barabara za Lushoto siyo siasa tu, ni zaidi ya maisha ya watu hasa barabara ya Mlalo – Ngwelo – Mlola – Makanya - Mlingano - Mashewa yenye kilometa 57. Barabara hii nimeizungumzia kwa muda mrefu sana kuwa ni barabara ya kiuchumi yenye wakulima wengi wanaozalisha mazao ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, barabara hii inapigwa danadana na TARURA wanasema ipo TANROADS nao TANROADS wanasema ipo TARURA. Naomba Mheshimiwa Waziri barabara hii muichukue iwe ya TANROADS ili wananchi wa maeneo hayo niliyotaja waweze kunufaika. Kama hili Mheshimiwa Waziri haliamini, atume timu yake iende ili ajue ukweli wa haya niliyoyaandika.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna barabara ya kuanzia Dochi - Ngulwi – Mombo. Kama unavyofahamu Lushoto kuna barabara moja kubwa tu na barabara hii ni nyembamba na imejaa mawe yanayoning’inia juu ya barabara na ndiyo sababu mvua ikinyesha mawe yanaporomoka na kuziba barabara.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017, barabara hii iliziba kwa siku zaidi ya 21 (wiki tatu) hali iliyosababisha usumbufu mkubwa sana na kupelekea wakulima wa mboga mboga na matunda kupata hasara kubwa sana pamoja na huduma za jamii kukosekana. Niiombe Serikali yangu Tukufu, kwa kuna kuna barabara hii ya Dochi - Mombo kilometa 16 tu itengenezwe ili iwe barabara mbadala lakini siyo kwa kupitika tu ila pia ni barabara yenye mazao mengi na pia kuna wananchi wengi wanaoishi katika maeneo hayo na kwa sasa wanakosa huduma za afya pamoja na za kijamii. Pamoja na hayo, barabara zote hizi mbili siyo lazima ziwe na lami. Wananchi wanataka zipitike tu kwa mwaka mzima yaani ziwe za changarawe tu.

Mheshimiwa Spika, pia kuna barabara ya TANROADS inayoanzia Nyasa – Mshizi - Gare - Magamba. Barabara hii kwa kweli nimshukuru Meneja wa TANROADS Ndugu Ndumbali kwa kazi kubwa. Barabara hii ina maeneo ya kujenga madaraja mawili; Daraja la Mshizi na Daraja la Kongei pamoja na kuweka zege maeneo hatarishi kama vile Mlima wa Yamba. Hili nalo niiombe Serikali yangu itenge fedha ili barabara hii iweze kurekebishwa na kujenga hayo madaraja mawili.

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kuipongeza Serikali yangu tukufu kwa kutupatia kilometa 1 kila mwaka kwa barabara iliyoanzia Magamba kwenda Mlola na Magamba kwenda Mlalo. Niiombe Serikali yangu ituongezee angalau kilometa 3 ili ziwe 4 ili kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Lushoto na huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu kuwa Tanga ni Jiji lakini tunayo changamoto za uwanja wa ndege. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu iupanue Uwanja wa Ndege wa Tanga ili ndege kubwa ziweze kutua.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, mwaka jana tuliomba Bombardier iweze kutua Tanga na Waziri alikubali lakini mpaka leo ndege haijatua. Naomba nikumbushie tena kuwa Bombardier itue Tanga sasa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia nimpongeze Waziri Mkuu pamoja na timu yake kwa kuwasilisha hutuba yake nzuri iliyogusa kila mahitaji ya Watanzania.

Mheshima Spika, naomba nianze kuchangia suala zima la afya na niendelee kuipongeza Serikali yangu tukufu kwa kujenga vituo vya afya zaidi ya 350 na zaidi pamoja na Hospitali za Wilaya, pamoja na hayo kuna maeneo mengine wananchi wamejitolea kujenga vituo vya afya kwa nguvu zao pamoja na zahanati na wamefikia hatua nguvu zimewaishia, hivyo wanahitaji Serikali yao tukufu iwaunge mkono kama maeneo mengine walivyopewa fedha kwa ajili ya kujenga majengo ya kisasa.

Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu iwapatie wananchi wa Jimbo la Lushoto fedha kwa ajili ya kumalizia vituo viwili vya afya ambavyo kimoja kipo Kata ya Gare na cha pili kipo Kata ya Ngwelo, kwani vituo hivi vikimalizika, vitapunguza usumbufu wanaoendelea kuupata kwa kutembea zaidi ya kilometa 50 mpaka 60 kufuata huduma za afya Wilayani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kuna zahanati nyingi zimejengwa kwa nguvu za wananchi na zimeisha lakini hazina vifaa tiba pamoja na watumishi, kwa hiyo niiombe Serikali yangu itenge fedha za kutosha katika bajeti hii ili zahanati zile ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi zianze kutoa huduma kwa wananchi wetu pamoja na nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Spika, nichangie suala la elimu, niipongeze Serikali kwa kujenga madarasa mengi ya sekondari na msingi, kwakweli madarasa yale yameleta tija na ufanisi mkubwa hasa kwa wananchi, kwa jitihada hizi naomba niishauri Serikali yangu tukufu kwa nini isitumie mfumo huu huu kumalizia maabara zilizojengwa kwa nguvu za wananchi, pamoja na kujenga hosteli katika mashule yetu ya sekondali ili wanafunzi wetu wa kike kuepuka kupata mimba za utotoni na zisizokuwa za lazima na watoto hawa kutimiza ndoto zao.

Kwa kuwa Jimbo la Lushoto lina shule za sekondari zaidi ya 30 na zenye hosteli ni sekondari tatu tu na hosteli hizo hazina ubora. Kwa hiyo niiombe Serikali yangu iweze kunipatia fedha ili tuweze kujenga hosteli angalau katika sekondari zifuatazo Malimbwi Sekondari, Mariam Mshangama Sekondari, Kwai Sekondari, Ubiri Sekondari, Claus Sekondari na Ngwelo Sekondari.

Mheshimiwa Spika, tutakapojenga hosteli katika shule hizi tutakuwa tumewaokoa watoto hasa wa kike katika janga hili la kupata mimba na pia ufaulu utaongezeka katika mashule yetu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara zetu hasa za TARURA kwa kweli chombo hiki kinafanya vizuri ila kina changamoto ya rasilimali fedha na ukizingatia chombo hiki kina barabara nyingi za vijijini ambazo ndizo zinazotoa mazao kutoka kwa wakulima, hivyo basi niishauri Serikali yangu iongeze asilimia kumi ili jumla wapewe asilimia 40 angalau wataweza kukabiliana na changamoto hizi za barabara kuliko ilivyo kuwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la umeme, niendelee kuipongeza Serikali yangu tukufu kwa kusambaza zaidi ya vijiji 9000 mpaka sasa, kwa kweli ni kazi kubwa sana imefanyika, ushauri wangu niiombe Serikali yangu itenge bajeti ya kumalizia vijiji vilivyobaki ili kuondoa manung’uniko kwa wale ambao bado hawajapata umeme,hasa katika Jimbo la Lushoto lenye vijiji 62 lakini vilivyopata umeme ni vijiji 30 tu.

Kwa hiyo bado vijiji 32 na hii imeleta malalamiko ya kila siku na sisi Wabunge kuulizwa maswali ya kila siku na kukosa majibu yake, pamoja na haya Waziri wa Nishati alitoa waraka wa gharama za umeme zisizidi shilingi 27,000 lakini maagizo hayo hayafuatwi, wananchi bado wanalalamika, kwani wanapofika TANESCO wanaambiwa hakuna kitu kama hicho.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu naomba Waziri atoe tamko tena na ufuatiliaji ufanyike pamoja na kutoa onyo kali kwa Mameneja wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono bajeti ya Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Waziri Mkuu wetu kwa hotuba yake nzuri yenye matumaini makubwa kwa Watanzania na pia niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutupa pesa nyingi za miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika jimbo la Lushoto lina changamoto kama ifuatavyo; kwanza kuna changamoto ya vituo vitatu vya afya ambavyo ni Kata ya Gare, Kata ya Kwai na Kata ya Makanya. Kata zote hizi wananchi wameshaanza kujenga kwa kutumia nguvu zao wenyewe, kwa hiyo wanasubiri tu Serikali nayo iingize nguvu zake kwa kuwapa pesa kama vituo vingine hapa nchini vilivyopata pesa. Takribani ni miaka sita sasa vituo hivi havijapewa pesa yoyote, hivyo basi niiombe Serikali katika kipindi hiki cha bajeti Serikali itenge fedha za kumalizia vituo hivi ili kuunga mkono juhudi za wananchi wetu na kama unavyojua ni ahadi tulizowaahidi kwenye kampeni zetu.

Mheshimiwa Spika, pili ni changamoto ya maji; katika Jimbo la Lushoto lina kata 15 kati ya kata hizo zenye changamoto ya maji ni kama ifuatavyo; Kata ya Gare yote, Kata ya Kwai hasa Kijiji cha Kwemakame, Kata ya Makanya yote, Kata ya Kwekanga yote, Kata ya Kilole yote, Kata ya Ubiri yote, Kata ya Malibwi yote na Kata ya Migambo yote.

Mheshimiwa Spika, kama inavyofahamika ya kuwa barabara nazo ndiyo zenye kuchangia pato la Taifa, lakini barabara nyingi za vijijini zina hali mbaya, pamoja ya kwamba TARURA wanajitahidi sana, lakini bajeti yao ni ndogo, ushauri wangu Serikali iipatie TARURA pesa za kutosha ili ikatatue matatizo ya barabara hasa katika Jimbo la Lushoto kuna changamoto ya barabara zifuatazo; Dochi - Ngulwi hadi Mombo; Mbwei hadi Mavului; Kibao cha Mazumba - Ntambwe hadi Ngaloi; Kizara - Ngulu hadi Kwemashai – Kwelugogo; Mmanyai hadi Kwezinga na Kwekanga hadi Mlola.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali yetu tukufu kwa kusambaza umeme katika kila Kijiji pamoja ya kwamba kuna changamoto ya mkandarasi kutoendeleza mradi, kwa maana mradi umesimama, sambamba na hayo katika Jimbo la Lushoto mpaka sasa kuna vijiji zaidi ya 15 na vitongoji ambavyo vimepitiwa na umeme 26 havijapata umeme mpaka leo, na kusababisha kero kubwa sana kwa wananchi. Kwa hiyo niiombe Serikali katika kipindi hiki cha bajeti, Serikali itenge pesa ili vijiji hivyo pamoja na vitongoji vyake viweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, kuna maboma mengi ya maabara yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi lakini mpaka sasa maboma yale yanaanguka na katika Jimbo la Lushoto kuna maboma ya maabara zaidi ya 26 bado hayajaendelezwa. Niiombe Serikali itenge pesa za kutosha ili kwenda kumalizia maboma haya ya maabara yaliyoko nchi nzima ambayo yametumia nguvu za wananchi. Sambamba na hayo Serikali isisahau kujenga nyumba za walimu ili kuwapunguzia kuishi katika nyumba zisizo bora na hatarishi pamoja na kuongeza watumishi wa kada zote.

Mheshimiwa Spika, kama inavyofahamika kuwa Wilaya ya Lushoto ni ya wakulima wa matunda, lakini mazao haya hayajapewa ruzuku za pembejeo wakati ni mazao ambayo yanaingiza pesa katika Halmahauri zetu, niiombe Serikali iangalie upya ili kuwapatia pembejeo wakulima hawa, sambamba na hayo Lushoto inazalisha kahawa lakini zao hili linakufa kwa sababu wakulima hawajawahi kupewa pembejeo pamoja miche bora. Niiombe Serikali iende Wilayani Lushoto ikafufue zao hili kwa ajili ya kuongeza pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mwisho naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni mpongeze na kumshukuru Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwa kutupatia fedha za miradi ya maendeleo katika majimbo yetu, Mwenyezi Mungu azidi kumbariki Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Waziri wa TAMISEMI pamoja na Katibu Mkuu bila kuwasahau wasaidizi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo katika Jimbo la Lushoto lina changamoto zifuatazo; nikianza na kada ya afya; katika Jimbo la Lushoto lina Tarafa mbili ambazo ni Tarafa ya Lushoto na Tarafa ya Mlola, Tarafa ya Lushoto haina kituo cha afya hata kimoja, hivyo kuna upungufu wa vituo vya afya vitatu ambavyo wananchi wameshaanza kujenga kwa kutumia nguvu zao wenyewe, vituo hivyo ni kama ifuatavyo; Kituo cha Afya Gare, Kituo cha Afya Kwai na Kituo cha Afya Makanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba katika bajeti hii Serikali itenge pesa kwa ajili ya kumalizia vituo hivi vinavyojengwa kwa nguvu za wananchi na vituo hivyo mpaka sasa vina miaka mitano bado tu mpaka sasa havijatengewa fedha, pamoja na nyumba za watumishi, vifaa tiba pamoja na watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kada ya elimu kuna changamoto kama zifuatazo; niaze na sekondari; sekondari nyingi zina upungufu wa maboma, ukarabati, mabweni, uzio pamoja na maabara. Sekondari zifuatao ndiyo zenye chagamoto za mahitaji tajwa hapo juu ni Sekondari ya Mlongwema, Sekondari ya Mdando, Sekondari ya Kweulasi, Sekondari ya Makole, Sekondari ya Balozi Mshangama, Sekondari ya Malibwi, Sekondari ya Ntambwe, Sekondari ya Kireti na Sekondari ya Kwai na Sekondari ya Kwemashai. Hizi ndiyo sekondari zenye changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi zenye uhitaji ni hizi zifuatazo; Shule ya Msingi Ungo, Shule ya Msingi Hondelo, Shule ya Msingi Ngulu, Shule ya Msingi Kilangwi, Shule ya Msingi Handei Boheloi, Shule ya Msingi Kwemashai, Shule ya Msingi Gare B, Shule ya Msingi Bombo Ngulwi, Shule ya Msingi Ngulwi, Shule ya Msingi Mbula B na A na Shule ya Msingi Kwembago. Hizi ndiyo baadhi ya shule za msingi zenye changamoto kubwa,kama nilivyo ainisha hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upannde wa TARURA katika Jimbo la Lushoto kuna changamoto ya barabara ambazo hazipitiki kabisa toka wakati wa mafuriko na hazijawahi kutengewa fedha, barabara hizo ni barabara ya Dochi - Ngulwi hadi Mombo kilometa 16, barabara ya Kwedaraja kupitia Kwemashai hadi Kwelushega kilometa nane, barabara ya Kwekanga, Makole hadi Ngwelo kilometa sita, barabara ya Kihitu - Ngwelo - Kaya hadi Kigulunde kilometa saba, barabara ya Kizara – Ngulu - Kilangwi hadi Kwelugogo kilometa 11, barabara ya Boheloi, Makanka hadi Masange kilometa tisa, barabara ya Kilole kupitia Ula hadi Ungo kilometa tisa, barabara ya Kilole hadi Kweboma kilometa nne na barabara ya Ntambwe hadi Kwalei kilometa saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi ndiyo zinazotoa mazao kutoka mashambani hadi mjini, kwa hiyo hizi ni barabara muhimu hasa kwa kuchochea uchumi wa sehemu hizo, niiombe Serikali yangu tukufu itenge pesa kwenye bajeti hii ili barabara hizi ziweze kuhudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali yangu tukufu iwatambue wazee wa nchi hii kwa kuhakikisha wanapata kadi za bima ya afya sambamba na kupata huduma inayostahili kuliko jinsi ilivyo sasa, kwani wanafika hospitali hawapati huduma zaidi ya kurudishwa au kuandikiwa dawa kwenda kununua kwenye maduka ya dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja ya kwamba Serikali imetenga dirisha la wazee, pia niishauri Serikali inapotoa pesa za vituo vya afya au zahanati kwenye ramani ya jengo waongeze chumba cha kuhudumia wazee tu, sambamba na hayo kuna haja ya Serikali kujenga kliniki za wazee na ikiwezekana wazee hao waende kliniki kila mwezi kwa ajili ya kuangalia afya zao, kwani katika nchi hii wazee ni hazina na ndiyo tunu ya nchi yetu, kwa hiyo lazima tulinde afya zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuongeza posho za Madiwani wetu, naunga mkono hoja iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wenzengu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja.