Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hawa Subira Mwaifunga (24 total)

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali madogo ya nyongeza. Nashukuru Serikali inatambua kwamba kuna msongamano hasa katika gereza la Manispaa ya Tabora. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kupanua mahabusu ya Kwa Zuberi ili kuweza kupunguza msongamano wa mahabusu walioko katika gereza la Tabora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwasaidia mahabusu ambao wamepelekwa magereza bila kuwa na hatia na kusababisha msongamano usiokuwa na sababu eti kwa sababu upelelezi haujakamilika; wanaendelea kuwekwa tu katika mahabusu hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuleta jambo hili na bahati nzuri na mimi nilishazungukia Mkoa wa Tabora. Tunachokifanya tunakubaliana naye kwamba kuna msongamano katika gereza la Tabora na mapendekezo yake ya kufanya upanuzi katika gereza la Kwa Zuberi ni jambo la msingi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tunapokea maoni yote haya, lakini tunachofanya tunaweka vipaumbele katika kuongeza ukubwa wa magereza katika maeneo ambayo magereza yale yana kazi za kufanya ili wafungwa wanapokuwepo waweze kuwa na kazi za kufanya ili waweze kulisaidia Taifa katika kurekebishwa kwao kuliko kuwa na wafungwa wengi, tunatumia kodi za walipa kodi kuwatunza, halafu wakawa hawana kazi za kufanya na wala hawana namna ambayo wanarekebishwa. Kwa hiyo tumepokea na tutaweka vipaumbele kulingana na jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuwasaidia mahabusu ambao wamerundikana na wapate msaada wa kisheria. Serikali tumekuwa tukifanya hivyo na katika kipindi cha tangu Julai, binafsi nimezunguka, Waziri wa Katiba na Sheria amezunguka na katika vipindi tofauti aliambatana na Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na zoezi hilo limekuwa endelevu na kuna wakati maafisa wenyewe wa ngazi ya juu kutoka katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wamekuwa wakipita katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma hiyo na kushughulikia kesi zile ambazo si za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nilipopita Rukwa nilikuta kwenye gereza moja kulikuwepo na vijana kama 11 hivi, nilipowahoji kwamba kwa nini wapo pale, waliniambia makosa yao. Kumi walikuwa wana makosa ya kunywa supu. Walikunywa supu wakashindwa kulipa, walishakaa karibu mwezi hivi na mmoja alikuwa amekunywa soda ya kopo. Sasa nikawambia muda waliokaa umeshazidi gharama ya soda ile ya kopo na ile supu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumewaelezea na wenzetu kule waweze kuchukua hatua za kurekebisha kulingana na makosa watu waliyofanya na wale ambao wanastahili kurekebishwa na kuondoka, wasirundikwe mle, wapate dhamana waweze kuondoka na kuendelea kufanyiwa hatua zingine.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tabora Mjini lina kata 29, katika kata hizo kata 11 hazipati maji kabisa. Ni tatizo linalotokana na Serikali kudaiwa kiasi cha shilingi bilioni mbili na mkandarasi. Je, ni lini Serikali italipa pesa hizo ili hizi kata 11 ziweze kupatiwa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza bahati nzuri kwenye sherehe ya Pasaka nilienda Jimboni kwangu nimepita Tabora, nimekuta Mamlaka yetu ya Tabora imenunua mabomba mengi kuhakikisha kwamba katika hizi kata zilizosalia ni kata tisa ambazo zimebaki hazipati huduma ya maji mjini. Kwa hiyo, kata moja tayari inawekewa miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi ambao tarehe 22 Mheshimiwa Waziri anakwenda kushuhudia kusaini mikataba ya mradi wa kutoa maji Solya kupeleka Nzega, Igunga na Tabora, kata zote zilizobaki sasa zitapata huduma ya maji kutoka kwenye huu mradi mpya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge baada ya mwaka mmoja au miwili Mji wa Tabora tutakuwa tumemaliza kabisa matatizo ya maji.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri ambayo hayaridhishi vizuri, napenda nimuulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kwenda kutoa elimu kwa wakulima hawa ili badala ya kutumia hayo magogo ambayo wanasema, basi waweze kutumia hayo matawi ili kuweza kukausha tumbaku zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuhakikisha wakulima hawa hawatumii tena kuni kwa sababu wanakata sana miti na badala yake walete hiyo nishati mbadala kwa haraka ili wakulima hawa waweze kuacha kukata miti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia majiko sanifu na vilevile athari za mazingira zinazotokana na ukataji wa miti. Kwa hiyo, ni kitu ambacho kimekuwa kikiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namsihi tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine wanaotoka maeneo yanayolima tumbaku, waendelee kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira katika kilimo cha tumbaku kwa sababu tumbaku yetu inaweza ikawa na bei nzuri kwenye soko kama tutakuwa na tabia ambazo zinahifadhi mazingira. Inaitwa compliance, ni moja kati ya vigezo vinavyoangalia ubora wa tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa sasa Serikali inahimiza matumizi ya majiko sanifu na kuanzia msimu huu unaokuja, haitaruhusiwa tena kutumia majiko ya aina nyingine; itakuwa ni lazima kila mkulima atumie majiko sanifu wakati wa kukausha tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na nishati mbadala, kama nilivyosema, tayari tafiti zimeshafanyika kuangalia kama umeme na makaa ya mawe yanaweza yakawa nishati mbadala, lakini kwa sasa ilionekana kwamba nishati hizo zinakuwa na gharama kubwa kwa mkulima. Kwa hiyo, njia ambayo inaoneka ni ya gharama nafuu lakini vilevile ni rafiki kwa mazingira, ni kutumia majiko sanifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine waisaidie Serikali kuendelea kuhimiza wakulima wetu watumie njia hiyo wakati wa kukausha tumbaku.
MHE. HAWA S. MWAIFUGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo lililopo Morogoro Kusini Mashariki ni tatizo ambalo linafanana na Jimbo la Tabora Manispaa katika Kata 11 za vijijini ambapo mpaka sasa hazijaanza kupelekewa umeme wa REA III. Je, ni lini Serikali itaanza utaratibu huo? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwanza mkandarasi yupo Tabora na ameshakamilisha kazi ya survey na wiki iliyopita amekamilisha Igunga. Kwa hiyo, nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema tarehe 20 na bahati nzuri tunaanza kuwakagua ujenzi wa wakandarasi kuanzia Tabora na Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi atakuwa site kuanzia tarehe 20 baada ya kumaliza Igunga na ataendelea na ujenzi wa vijiji vyote 16 katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo lililopo Handeni linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete, ina upungufu mkubwa wa madaktari na wauguzi. Je, ni lini Serikali itapeleka madaktari na wauguzi katika Hospitali ya Mkoa ambayo inategemewa na mkoa mzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la swali la msingi, ni kweli tunatambua kuna upungufu mkubwa wa wauguzi pamoja na madaktari na hasa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, kwa kadri ambavyo ikama inahitajika kutokana na bajeti, ni vizuri basi niwatake Mkoa wa Tabora kwa ujumla wake waanze kwa haraka kuiga mfano mzuri wa Handeni kwa kutumia own source za kwao ili kuweza kuziba hilo pengo lililopo wakati tunasubiri bajeti iruhusu kwa ajili ya kuajiri hao wengine ambao watatoka Serikali Kuu. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia sugu ya wazazi hasa wababa kutelekeza watoto na kuwaachia akina mama walee watoto hao peke yao.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kudumu wa kuyapa nguvu Madawati ya Jinsia na Mabaraza ya Usuluhishi katika kata zetu ili waweze kuweka sheria ngumu ambayo itawafanya wababa hawa wasiweze kutelekeza watoto wao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kuzileta Bungeni Sheria za Ustawi wa Jamii ili tuweze kuzibadilisha kama siyo kuziondoa zile za zamani ili ziweze kuendana na hali ya maisha ya sasa? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga kwa maswali yake mazuri, lakini vilevile kuwa mtetezi mzuri wa haki za watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali imeandaa na kuzindua Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Jinsia dhidi ya akina Mama na Watoto wa mwaka 2017/2018 na utaisha mwaka 2020/2021. Sambamba na hilo, utekelezaji wake umeshaanza kwani hivi tunavyoongea sasa hivi tumezindua madawati 417 katika vituo vyetu vyote vya polisi ambavyo vinasimamia masuala yote yanayohusiana na ukatili wa kijinsia kwa akina mama na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, sasa tunakwenda mbali zaidi na kwamba tunaanzisha Kamati za Ulinzi wa wanawake na watoto ambapo Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Wajumbe wa Mabaraza watakuwa ni sehemu ya mkakati huo, kuwajengea uwezo, kuwapa elimu kusimamia haki za wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri katika swali lako la pili kwamba viwango vya sasa haviendani na hali halisi, sasa hivi tu katika mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Ustawi wa Jamii ambayo itazingatia hali ya sasa.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa la ardhi katika Wilaya ya Sikonge, Mkoa wa Tabora, eneo kubwa ni eneo la hifadhi kuliko eneo ambalo wanaishi binadamu na inabidi wale wanadamu wafanye kazi kwenye eneo la hifadhi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza eneo la hifadhi na kuwapa wananchi ili waweze kufanya shughuli zao za kibinadamu kuliko ilivyo hivi sasa ambapo wananyanyasika, wanadhalilika na kuteseka? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli na mimi naomba niungane naye kusema kwamba Mkoa wa Tabora ni mojawapo ya mikoa ambayo ina sehemu kubwa sana ya Hifadhi ya Taifa, kwa kweli hilo Serikali tunakubali na tumeona kabisa juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nchi yetu kama tulivyokuwa tunasema kila siku na tumekuwa tukisema, ardhi haiongezeki, idadi ya watu inazidi kuongezeka, shughuli za kibinadamu zimezidi kuongezeka, mambo mengi yamezidi kuongezeka. Kwa kweli mpango wa kupunguza maeneo ya hifadhi hautatusaidia kutatua matatizo, tatizo linaweza kutatuliwa kwa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na mipango mizuri ya kutumia ardhi iliyopo hiyo itatusaidia kuliko kupunguza hifadhi. Leo hii tutapunguza kesho idadi ya watu itaongezeka zaidi, je tutazidi kupunguza? Mwisho hifadhi zote zitaisha.
Kwa hiyo hatuna mpango wa kuweza kupunguza bali ni kuwashauri wananchi watumie muda wao vizuri wapangilie vizuri ardhi yao ili ile ambayo ipo kwa ajili ya shughuli za kilimo na makazi itumike kama ambavyo imekusudiwa. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Tatizo lililopo katika Jimbo la Bunda linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Jimbo la Tabora Manispaa, chanzo cha maji cha Mto Gombe kinasumbuliwa sana na tatizo la mazingira katika eneo hilo.
Je, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira ina mpango gani wa kusaidia wananchi wale kunusuru afya zao za maji ambayo wanatumia wakati tukisubiri maji ya Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nchi yetu ina changamoto ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira, kwenye vyanzo vingi vya maji. Ndiyo maana mkakati mmojawapo wa kunusuru vyanzo vya maji nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa January Makamba alishatoa agizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaorodhesha vyanzo vyote vya maji katika maeneo yao, vikiambatana na changamoto ambazo zinakabili vyanzo hivyo ili Serikali ijipange katika kunusuru vyanzo hivyo, hili la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, katika Ilani hii ya CCM ambayo naamini Mheshimiwa Hawa Mwaifunga anaiamini na kuisimamia itekelezwe katika maeneo yake, katika ukurasa wa 212 mpaka 213 Ilani hii inaagiza Halmashauri zote katika nchi yetu, kuhakikisha kila mwaka wanapanda miti ya kuhifadhi mazingira na kwenye vyanzo vya maji isiyopungua milioni 1.5.
Hivyo kupitia swali hili, naziagiza Halmashauri zote nchini, zitekeleze Ilani hii na baada ya Bunge hili wajue wana deni ambalo dawa ya deni ni kulipa nitaenda kukagua kuona sasa miaka miwili kwamba wana miti si chini ya milioni tatu.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa niseme kwamba majibu ya Waziri yanaonesha kana kwamba suala la bodaboda limeanza juzi ama jana.
Suala la bodaboda ni la muda mrefu na kero za watu wenye bodaboda zimekuwa ni kubwa kwa wananchi lakini bado Serikali inasema inajipanga kufanya haya na yale wakati bodaboda ni suala la muda mrefu. Ni dhahiri traffic police wameelemewa na usimamizi wa kudhibiti uvunjifu wa Sheria Barabarani kwa waendesha bodaboda. Kwa mfano; bodaboda zina…

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Kwa mfano; Bodaboda zimekuwa zikipita kwenye traffic lights wakati wowote bila kufuata taa. Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kubadili ama kuboresha mikakati yake ili kuimarisha usalama barabarani hususani jinsi ya kusimamia hawa wenye bodaboda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nchini Rwanda wenzetu wana utaratibu mzuri wa kusajili madereva wa bodaboda na kusajili vituo ambavyo wanafanyia kazi. Je, ni lini Serikali itasajili hawa vijana wenye bodaboda na maeneo wanayofanyia kazi ili kuweza kubaini watu wanaofanya uhalifu kwa kutumia bodaboda?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali haya yaliyoulizwa nilishayajibu kwenye jibu la msingi. Ninachosema siyo kwamba Serikali inajipanga, ni Serikali imeshachukua hatua hizi na mambo haya yamefanyika kwa mfano, swali la msingi linauliza Dar es Salaam. Pale Dar es Salaam hatua kubwa sana imeshafanywa ya kusajili waendesha pikipiki na haikuishia hivyo tu wamewapa mpaka jezi za kuwatofautisha na mtu mwingine ambaye hakupangiwa katika vituo hivyo. Lakini siyo hilo tu, ukisema tunajipanga ni kama vile pikipiki ni zile zile ambazo zilishasajiliwa. Kama tulishasajili wakija wapya inabidi pia tuendelee kuwasajili ndiyo maana utaona kwamba zoezi hilo linaendelea kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hii ya waendesha bodaboda kupita kwenye taa, hilo ni jambo la tabia ambalo tumeendelea kuchukua hatua, lakini elimu imeshatolewa na utaratibu ambao wanatakiwa wafuate ulishatolewa, kwa hiyo, tunaendelea kuchukua hatua kwa wale wanaovunja sheria hizo.
MHE. HAWA B. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Serikali ya utengaji wa maeneo, lakini je, mpaka sasa ni waombaji wangapi ambao tayari wameshapewa maeneo hayo kwa ajili uwekezaji wa viwanda vya kuchakata korosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Tabora ni moja kati ya Mikoa ambayo inalima tumbaku kwa wingi; je, ni lini Serikali itatenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya korosho/ulimaji wa tumbaku ili wakulima wetu waweze kunufaika na tumbaku yao? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, anauliza ni wangapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaungana na mimi kwamba suala la kitakwimu linahitaji kupata data mapema. Namwomba Mheshimiwa ili apate jibu la uhakika, angeleta kama swali la msingi ili tuweze kumtafutia takwimu ili tumpe majibu ambayo yanastahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya Mkoa wa Tabota kutenga eneo kwa ajili ya wakulima wa korosho; kasema korosho na wakati mwingine kasema tumbaku, sasa I am not so sure ni kwa ajili ya nini? Kwa sababu hata ukienda Tabora pia korosho zinastawi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama msingi ni kwa ajili ya wakulima wa tumbaku, namwomba Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri yeye ni Diwani katika eneo lake, mchakato ni vizuri ukaanzia kwenye Halmashauri, maana yeye analifahamu vizuri eneo la Mkoa wa Tabora ili wahakikishe kwamba maeneo kwa ajili ya wajasiriamali yanawekwa na yanatunzwa ili watu wetu waweze kupata maeneo hayo.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri ambaye na yeye pia ni mkazi wa Mkoa wa Tabora katika Jimbo la Sikonge anafahamu hali halisi ya elimu za watoto wetu na ndugu zetu katika mkoa wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea hapa na takwimu zinazooneshwa ni shule chache ambazo zimefaulu kwa kiwango kikubwa zinatengenezewa takwimu na zinaonekana kwamba ndiyo takwimu halisi; lakini uhalisia uliopo katika Mkoa wa Tabora, elimu yetu imeshuka kutokana na miundombinu hakuna walimu. …

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha wa kuboresha miundombinu ya elimu katika Mkoa wa Tabora ili watoto wetu waweze kufanya vizuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika shule za sekondari ambazo ni shule zilizokuwa zinafaulisha vizuri miaka ya nyuma ambapo watu wengi humu ndani wamesoma katika shule hizo leo shule hizo zimekuwa na changamoto za vitanda, changamoto za viti na changamoto za miundombinu mbalimbali. Serikali ina mpango gani pia wa kuweza kuhakikisha maeneo yale yanaboreshwa ili shule zile ziweze kufanyavizuri kama ilivyokuwa hapo awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimsifu san binamu yangu kwa kufuatailia sana sekta ya elimu. Nakubaliana nae kwamba kuna baadhi ya shule hususani za pembezoni kabisa hazifanyi vizuri lakini mara nyingi tunapozungumzia mkoa huwa tunajumlisha kupata matokeo ya kimkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, Serikali ina mpango gani kuboresha miundombinu? Kama tulivyowasilisha bajeti yetu vizuri ya juzi, tumejidhatiti kweli kweli. Mwaka huu tumepeleka walimu 112 katika shule za msingi, walimu wa sayansi tumepeleka walimu 20 katika Mkoa wa Tabora lakini kwa mwakani 2018/2019 tutajenga vyumba vya madarasa 207, matundu ya vyoo 689, nyumba za walimu 123 na kwa upande wa sekondari tutajenga nyumba za walimu 179, vyumba vya madarasa 159, matundu ya vyoo 166 na kukamilisha maabara 163 kwa ajili ya masomo ya sayansi. Tunaamini kuwa mchango huu utasaidia kuboresha sana hali ya ufaulu wa vijana wetu katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; shule maalum ambazo zilikuwa zinafaulisha sana zamani. Kwanza naendelea kuzipongeza shule hizo ikiwemo Tabora Boys ambayo imekuwa ikichangia sana kuinua ufaulu wa Mkoa wa Tabora na ni kweli kwamba baadi ya miundombinu yake iko katika hali ambayo inahitaji sana msaada na naomba niungane nae katika kuzifuatilia shule hizo ili tusaidiane katika kuzitendea haki.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Mradi wa Maji wa Ziwa Viktoria ni mradi mkubwa na ni mradi wa muda mrefu. Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa ambayo wananchi wake wana matatizo makubwa ya maji. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Tabora wanapata maji safi na salama? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimuulize kweli, yupo? Kwa sababu, katika Mkoa wa Tabora tumekamilisha mradi mkubwa kutoka lile bwawa kubwa la pale Tabora, Bwawa la Igombe, ambao sasa hivi unatoa lita milioni 30 kwa siku na mahitaji ya maji kwa Tabora ilikuwa lita milioni 24 na kwa hiyo tulikuwa na excess ya lita milioni sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo tunatekeleza mradi mkubwa wa maji ambao tumepata fedha kutoka Serikali ya India. Ndiyo maana tumeamua sasa, kwa sababu maji yatakuwa mengi tutapeleka mpaka Sikonge, tutapeleka mpaka Urambo na tunaweza tukayafikisha mpaka Kaliua. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge sasa hivi tayari kuna mradi mwingine unaendelea pale Tabora kwa sasa, tunasambaza maji kupeleka kwa wananchi, maji yapo, Ilani ya Chama cha Mapinduzi inafanya kazi yake.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Serikali imetoa majibu kwamba na wamekiri kwamba kweli sheria ya mtoto ya kuolewa kwa maiaka 15 ipo na inaendelea kuwepo na wanasema kwamba wanataka kumlinda mtoto huyu asiolewe akiwa na umri huo wakati sheria inasema kwamba anaweza kuolewa akiwa na umri huo. Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa ambayo ndoa nyingi za utotoni na watoto kujifungua watoto wenzao wakiwa na umri mdogo na kusababisha vifo vingi vya watoto. Serikali ina mpango gani wa kuibadilisha sheria hii ili watoto hawa waweze kuendelea na masomo yao kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, asilimia 63 ya wanaoathirika na ndoa za utotoni ni watoto wa kike, kesi nyingi zimekuwepo mahakamani kuhusiana na suala hili, lakini kutokana na sheria kuwepo ya watoto kuolewa na umri wa miaka 15 wanaofanya makosa hayo wamekuwa hawaadhibiwi kwa sababu sheria haisemi ni adhabu gani wanaweza wakapatiwa, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili ili kunusuru watoto wetu wanaolewa wakiwa na umri mdogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) : Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la kwanza amezungumza kuhusu mkinzano na kuitaka Serikali kubadilisha sheria. Suala hili limekwishazungumzwa sana na Serikali mkishatoa maelezo yake na ikumbukwe kwamba yalitolewa maamuzi ya kesi Na.5 ya mwaka 2016 ambayo ni kesi kati ya Rebeka Jumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Serikali imekata rufaa, kwa hiyo tunasubiri maamuzi ya kesi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache anachokisema Mheshimiwa Mbunge kama mkinzano, mkinzano huu haupo kwa sababu suala la umri, umri wa mtoto unatafsiri katika sheria tofauti na katika maeneo tofauti. Kuna umri biological, kuna umri contextual na kuna umri situational.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana tunasema hapa katika sheria zetu hizi sheria ambayo anahisi yeye inakinzana hakuna upinzani wowote, Kwa sababu mwanafunzi yoyote ambaye yuko shuleni ambaye akipata ujauzito pale Hatuangalii biological age yake tunaangalia umri wa muktadha, ndio maana tunasema hata kama akiwa yupo form six ana miaka 18 akipewa ujauzito sheria ambayo tulifanya wenyewe marekebisho hapa Bungeni ukienda kwenye Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kifungu imeongezwa kifungu cha 60A imeweka adhabu ya kwamba mtu anayefanya akosa hilo adhabu yake ni miaka 30. Kwa hiyo hakuna mkinzano katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusu Serikali ifute sheria na amesema kwa sababu ndio sehemu pekee ya kuweza kulinda haki ya mtoto wa kike hasa katika eneo ambalo ametokea yeye kutokana na kwamba kulikuwa na idadi kubwa sana ya watoto ambao wanapata ujauzito na akasema ni sheria gani ambayo inamchukulia hatua mtu huyu ambaye anafanya kosa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii imesema dhahiri kabisa ukienda kwenye Sheria Na. 21 ya mwaka 2009, sheria ambayo inalinda haki ya mtoto imezungumza juu ya kosa hilo la mtu yoyote ambaye anatenda kosa la kuzuia haki ya mtoto, baadaye sheria hiyo inaweza kuchukua mkondo na kuhakikisha kwamba mtu huyo anatiwa katika mikono ya sheria. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa kwamba si kweli kwamba Serikali hatu fahamu na hatulindi haki za mtoto na ndio maana tumechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba tunalinda haki ya mtoto na watupe muda tuendelee kufanyia kazi suala hili. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Chama cha Msingi cha Imalamakoye AMCOS kimesababishia hasara kubwa wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ya zaidi ya Dola 19,500 sawa na Shilingi za Kitanzania milioni 40 na zaidi na hivyo kusababisha kushindwa kununua pembejeo kwa ajili ya kilimo chao cha tumbaku. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima hawa ili Chama hiki cha Imalamakoye kiweze kuwalipa pesa zao waweze kupata pembejeo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii pia na yeye kumpongeza kwa jinsi anavyofuatilia suala zima hili la tumbaku. Ni kweli kwamba hii AMCOS ya Imalamakoye ambayo ameisema imekuwa ina matatizo, kumekuwa na ubadhirifu katika na mpaka sasa hivi tunapozungumza ni kwamba Mwenyekiti wa Bodi ameshashtakiwa na kesi hii iko Polisi, uchunguzi unaendelea kufanyika. Mara itakapobainika basi hatua kali sana za kisheria zitachukuliwa.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Kitete ina wodi ambayo inalea watoto njiti, lakini wodi hiyo ni finyu na vifaa vilivyopo ni duni. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha wodi ile na vifaa kuongeza, ili kuweza kuendana na kasi iliyopo pale?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya awali moja ya mkakati ambao tunao Serikali baada ya kukabidhiwa hospitali za rufaa za mikoa tumejielekeza katika maeneo makubwa matano;

(i) Kuhakikisha tunaboresha huduma za dharura;

(ii) Huduma za upasuaji; na

(iii) Masuala ya theatre, vilevile tunataka tuboreshe huduma za mama na mtoto ikiwa ni pamoja na huduma za ICU pamoja na ICS za watoto.

Kwa hiyo, tumeshafanya tathmini za kina hospitali zote, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Kitete na tumeshaweka Mpango Kazi wa kuboresha huduma hiyo katika Hospitali ya Kitete.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Waziri amesema kwamba ugonjwa huu ni tatizo kubwa nchini lakini katika Mkoa wa Tabora hasa Wilaya za Sikonge, Kaliua pamoja na Uyui umekuwa ni mkubwa zaidi hadi kusababisha kila siku watoto 40 kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete. Watoto hawa ni wengi sana na ndiyo hawa ambao wamejitokeza kuja hospitalini, hatujui hawa ambao hawajaja hospitalini. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wazazi kuhusu ugonjwa huu wa mguu kifundo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Daktari aliyepo katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete yupo tayari kufanya kliniki kwenye Wilaya hizi ili angalau kuwafuata wazazi ambao hawana uwezo wa kuwapeleka watoto wao Kitete?

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti kidogo ili Daktari huyu aweze kufika kwenye Wilaya hizi na kuweza kutibu watoto wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge kutoka Mkoa wa Tabora, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba mguu kifundo kwa lugha ya kitaalam tunaita Talipes ni ugonjwa ambao hutokea kwa baadhi ya watoto; mmoja kati ya watoto 1,000. Niseme tu kwamba mtoto akibainika mapema anaweza akapata matibabu na zaidi ya asilimia 80 ya hawa watoto miguu hurejea kuwa katika hali ya kawaida. Nitumie fursa hii kuongea na jamii ya Watanzania kusema kwamba wazazi wote ambao wana watoto ambao wana tatizo hili la mguu kifundo wawafikishe katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya ili waweze kupata huduma za utengamao. Kama nilivyosema hapo awali, ugonjwa huu unaweza ukatibika kwa kutumia utaratibu wa hizi huduma za utengamao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, sisi kama Wizara hatuna shida kama tuna mtaalam pale katika hospitali yetu ya Kitete kumpa usaidizi ili kuweza kufanya kliniki katika Wilaya zote. Hili Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukakaa tukaangalia utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba hii huduma inaweza ikapatikana katika Wilaya nyingine ambapo si rahisi kufika katika hospitali yetu ya Kitete pale Tabora.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kumekuwa na utaratibu mbovu kwa baadhi ya viongozi wanaogawa fedha hizi, wakitumia itikadi za kisiasa, ikiwepo ukiwa mwanachama wa chama fulani, unaweza ukapewa fedha hizo, lakini ukiwa mwanachama wa chama kingine hupewi fedha hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba Serikali itoe tamko fedha hizi wanaotakiwa kupewa ni watu wa aina gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haina ubaguzi. Ni Serikali ya Watanzania wote. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba pesa hizi zinazotokana na Mpango wetu wa TASAF ni kwa walengwa wote wanaotokana na zile kaya masikini sana na hakuna ubaguzi wowote. Nitoe rai na agizo kwamba yeyote atakayeleta ubaguzi katika kuhakikisha kwamba walengwa wanaotokana na mpango huu wa kunusuru kaya masikini wanasaidiwa, watoe taarifa na watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, Bwawa la Igombe katika Manispaa ya Tabora limejaa tope hivyo kusababisha upungufu wa maji katika manispaa hiyo. Aliyekuwa Waziri wa Maji Mheshimiwa Eng. kamwelwe aliahidi kupeleka fedha TOWASA ili kuweza kusaidia kuondoa tope na kufanya kina cha maji kuendelea kuwa kama kilivyokuwa hapo awali. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo ili wananchi wa Tabora tuweze kupata maji kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri lakini nimtoe hofu, ahadi siku zote ni deni, sisi kama Wizara ya Maji tutatekeleza deni lile katika kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji. Lakini pia ninataka nimfahamishe kwamba sisi kama Serikali tunatekeleza zaidi ya mradi wa bilioni 600 ambao tunatoa maji Ziwa Victoria kupeleka Tabora pamoja na Miji ya Igunga na Nzega yote ni katika kuhakikisha tunasaidia Mji wa Tabora uweze kupata huduma ya maji. Lakini kuhusu suala zima la ahadi ya kupeleka fedha, ahadi iko pale pale tutatekeleza katika kuhakikisha bwawa la Igombe tunatatua tatizo lile.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria umeshafika Mkoani Tabora. Jimbo la Tabora Mjini ni moja kati ya wanufaika wa mradi huo. Je, ni lini Serikali itaanza usambazaji wa maji katika Jimbo la Tabora Mjini ili wananchi wa maeneo ya pembezoni ambao hawana maji kabisa waweze kunufaika na mradi huu? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Moja ya ahadi kubwa sana kwa wananchi wa Tabora ni kuyatoa maji ya Ziwa Victoria na kuyaleta Tabora. Ni jambo kubwa ambalo amelifanya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na ahadi hiyo imetimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ni wa zaidi ya shilingi bilioni 600, nasi kama Wizara mradi huu tumeukamilisha na tume-save zaidi ya shilingi bilioni 25. Fedha zile zilizobaki zote zitatumika kwa ajili ya usambazaji wa maji, wananchi wote ambao hawana maji katika Mkoa wa Tabora wataweza kupata huduma ya maji. Kazi hiyo imekwishaanza na wakandarasi wako site kwa ajili ya uendelezaji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; pamoja na majibu ya Serikali naomba kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao kuu la biashara katika Mkoa wa Tabora ni tumbaku je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mazungumzo na kampuni kubwa za kununua tumbaku ili kuweza kuongeza kilo zaidi wakulima wengi waweze kupata manufaa na kilimo hiki?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia wakulima wa Mkoa wa Tabora ili waweze kulima kilimo cha kisasa na waweze kupata zao bora la tumbaku ambalo linaweza kununuliwa katika soko la dunia? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mwaifunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali imekuwa ikichukua jitihada za kuongea na kampuni mbalimbali za ndani na nje na ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wakaelewa. Ni hatari sana kama nchi kuruhusu sekta kama ya tumbaku kuwa dominated na kampuni za nje peke yake. Hatua ya kwanza tuliyoichukua kama Serikali kwa mara ya kwanza tumeruhusu ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika kununua tumbaku na tunazisaidia kupitia Balozi zetu za nje kuya- connect moja kwa moja na masoko ya Kimataifa. Sasa tuna kampuni nane ambazo zimeingia katika msimu uliopita na wamenunua tumbaku ya zaidi ya bilioni 12 kutoka kwa wakulima na wamekuwa na baadhi ya changamoto ambazo Serikali imekuwa ikiwasaidia. Lakini jitihada za kuongea na kampuni kubwa duniani, tuna maongezi na kampuni ya British American Tobacco, ambayo tunaendelea nayo maongezi. Tunajadiliana nao mfumo wa wao kuingia sokoni. Wao ombi walilolileta Serikalini ni kutaka kununua kupitia kampuni zilizoko hapa hapa za wenzao za nje na sisi hilo tumewazuia kwa sababu ita-restrict competition. Tunawataka waende moja kwa moja sokoni kushindana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ubora nataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kati ya wakulima wanaofuata best practice za kilimo katika nchi hii ni wakulima wa tumbaku na wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Tabora na mikoa mingine hasa Mbeya maeneo ya Chunya wanajitahidi sana kufuata utaratibu mzuri na hatua hii imesababisha hadi kupunguza madaraja ya mazao mabovu. Tumefuta madaraja kumi kwa sababu ya wakulima kufuata best practice. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba ubora wa tumbaku ya Tanzania hauna mashaka katika soko la dunia.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ujenzi wa barabara inayotoka Tabora Mjini kuelekea Mambali Bukene, imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu. Barabara hii ilikuwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 lakini mpaka sasa barabara hii imekuwa ikisuasua hivyo kusababisha wananchi wanaotoka Tabora kuelekea Shinyanga na Mwanza kupata usumbufu mkubwa kuzunguka:-

Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wa Tabora kuhusu barabara hii ili kurahisisha usafiri katika mikoa hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Bukene – Tabora ni barabara ambayo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, tayari Serikali imeshaonesha commitment kwamba ni barabara ambayo iko kwenye mpango wa kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na vipindi vya bajeti, lakini bado tuna mpango wa miaka mitano wa kuzijenga hizi barabara. Kwa hiyo, wananchi wa Tabora na wote wanaonufaika na barabara hii wawe na uhakika kwamba barabara hizi zitajengwa kama zilivyoahidiwa na kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Changamoto ya upatikanaji wa dawa haiko kwenye zahanati na vituo vya afya peke yake bali hata katika Hospitali za Rufaa. Hospitali ya Rufaa ya Kitete Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa Hospitali ambazo zinachangamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa; na hii inatoka na…

NAIBU SPIKA: Swali, swali!

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA:…je? Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiwango cha dawa katika Hospitali ya Rufaa ili iweze kuwapatia wananchi wa Tabora huduma iliyobora ya dawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tunafahamu kwamba pamoja na uboreshaji wa upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu katika Hospitali za Halmashauri na Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora kwa maana ya Kitete bado tunachangamoto ya upungufu wa dawa baadhi ya vituo. Ndio maana Serikali imeendelea kwanza kuongeza bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba kila mwaka. Kwa mfano kwa miaka mitano iliyopita tulikuwa na bilioni 30 sasa tuna bilioni takribani 270. Pili, tumeendelea kuboresha sana ukusanyaji wa mapato ya fedha za uchangiaji wa huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kwanza tunapunguza utegemezi wa vituo vyetu kwa bajeti ya Serikali Kuu kwa kuviwezesha kukusanya vizuri mapato ya uchangiaji lakini pia kununua dawa na vitendanishi vya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Hawa kwamba jambo hili Serikali tunalichukua, na tumeweka mpango mkakati wa kwenda kuboresha upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu, zikiwezo Hospitali za Rufaa, ikiwepo Hospitali ya Kitete. Nimhakikishie kwamba tutahakikisha kadri ya bajeti na taratibu ambazo zimepangwa tunaboresha sana upatikanaji wa dawa kwa wananchi wa Tabora na katika Hospitali ya Kitete na nchini kote kwa ujumla.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimsahihishe kidogo Naibu Waziri majengo yale yalianza kujengwa mwaka 2012, mwaka 2015 majengo yalikuwa yameshasimama.

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni umuhimu wa kutuongezea fedha badala ya bilioni moja ili tuweze kukamilisha majengo yale tuondokane na adha ya kufanyia vikao madiwani na watumishi kwenye maeneo vyumba vidogo sana ambavyo hata hewa nzuri havina. Majengo yale yameshakuwa ni ya muda mrefu mpaka yanatoa ule ukungu wa kijani Serikali haioni umuhimu wa kutuongezea fedha ili tuweze kumaliza kabisa majengo yale ili tuachane nao waendelee kwenye maeneo mengine? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mhesimiwa Spika, nchi yetu ni kubwa na kwenye jibu langu la msingi nimeongea namna ambavyo Serikali imeelekeza nguvu kubwa kwenye ujenzi wa majengo ya utawala kwenye halmashauri takribani 100 hivi sasa. Kwa hivyo, safari ni hatua tumeanza na bilioni na tutaendelea kadri ya fedha zainapopatikana tutakwenda kwa awamu kupeleka fedha hizo ili kukamilisha majengo hayo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba ni kipaumbele cha Serikali na tutahakikisha tunakamilisha jengo hilo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, changamoto ya wanawake kutelekezewa watoto imekuwa kubwa sana; je, Serikali haioni umuhimu wa kubadilisha kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ustawi wa Jamii Bungeni ili iendane na hali halisi ya maisha ya sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo ili wanawake waweze kupata haki zao kikamilifu. (Makofi)