Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hawa Subira Mwaifunga (12 total)

MHE. ANTONY C. KOMU (K.n.y. MHE. HAWA S. MWAIFUNGA) aliuliza:-
Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili ya utumishi ndani ya Jeshi la Polisi kutokana na hilo Askari wengi wanaonekana kukosa weledi kwa kujihusisha na matendo yanayokinzana na maadili ya utumishi wa umma:-
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa Askari wasio na sifa wanachukuliwa hatua?
(b) Je, zoezi la kuhakiki vyeti vya Askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi limefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi lina utaratibu wa kuwachukulia hatua za kisheria askari wachache ambao wanachafua taswira na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu pamoja na kujihusisha na vitendo vinavyokinzana na maadili ya utumishi wa umma. Aidha, tumeamua kusitisha kwa muda ajira zote kwenye vyombo vyote vilivyomo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwemo Jeshi la Polisi na kupitia utaratibu wa kutoa ajira ili kuondoa uwezekano wa watu wasio na sifa kujipenyeza na kupata ajira ndani ya vyombo vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la uhakiki wa vyeti vya askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi linaendelea. Mpaka sasa jumla ya askari 19 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora unakabiliwa na tatizo kubwa la msongamano wa mahabusu kiasi cha kutishia afya zao kwa sababu magereza hayo yana uwezo wa kuchukua takribani mahabusu 1200, lakini mpaka sasa kuna zaidi ya mahabusu 2500 kinyume kabisa na haki za mahabusu:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa hali ya magereza katika Mkoa wa Tabora zinaboreshwa na idadi hiyo ya mahabusu inazingatia haki za msingi za binadamu?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kesi zilizopo mahakamani zinaharakishwa kwa kuwa wapo mahabusu wengi ambao wana kesi za kubambikiwa au kughushiwa tu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba hali ya magereza katika Mkoa wa Tabora pamoja na mikoa mingine nchini zinaboreshwa ili kuzingatia haki za binadamu, Serikali inaendelea kufanya upanuzi wa magereza kwenye magereza ya zamani na kujenga magereza mapya ya mahabusu katika kila Wilaya ambapo mpango huu ni endelevu na utekelezaji wake umekuwa ukifanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni tatu katika bajeti ya fungu la maendeleo kwa ajili ya ukarabati na upanuzi na umaliziaji wa ujenzi wa mabweni mapya na majengo ya utawala katika baadhi ya magereza nchini likiwemo Gereza la Nzega na Gereza la Mahabusu Urambo. Kati ya fedha hizo, milioni 150 ni kwa ajili ya kuanza upanuzi wa gereza la Nzega kwa kujenga mabweni mawili ya wafungwa yenye uwezo wa kuchukua wafungwa 50 kila moja na milioni 35 ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni moja la wafungwa ambalo linatarajiwa kujengwa liwe gereza la mahabusu huko Urambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa kuna msongamano wa mahabusu katika gereza la Tabora kama ilivyo katika magereza mengine hapa nchini. Kwa kutambua hilo, Serikali kupitia Jukwaa la Haki Jinai imekuwa ikifanya vikao vya kuharakisha kesi ambazo bado upelelezi wake ulikuwa haujakamilika ili kupunguza msongamano magerezani. Aidha, mafunzo yamekuwa yakitolewa kwa askari wapelelezi ili ukamataji wa watuhumiwa uzingatie uzito wa ushaidi wa mhusika kuepusha malalamiko ya kubambikiwa kesi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza:-
Tumbaku ni moja ya zao la biashara ambalo ni muhimu sana kwa Mkoa wa Tabora, lakini ukaushaji wake umekuwa mgumu sana kwa wakulima kutokana na kulazimika kutafuta kuni kwa ajili ya kukaushia tumbaku jambo ambalo linaathiri afya za wakulima hao pamoja na mazingira.
Je, ni lini Serikali itawasaidia wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kupata nishati mbadala kwa ajili ya kukaushia tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la…(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumbaku ni zao muhimu sana kwa Mkoa wa Tabora na Taifa kwa ujumla, kwani huwapatia wakulima kipato kikubwa na huchangia zaidi ya shilingi bilioni 14 kwa mwaka Mkoani Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kupata nishati mbadala kwa ajili ya kukausha tumbaku badala ya kuni. Utafiti wa awali uliofanyika ni ule wa kutumia makaa ya mawe na umeme uliofanyika mkoani Iringa ambapo ilibainika kuwa na gharama kubwa kwa mkulima.
Aidha, kuanzia msimu wa kilimo wa 2015/2016, utafiti wa matumizi ya nyasi maalum umeanza kufanyika Mkoani Mbeya na Songwe katika wilaya zinazolima tumbaku. Utafiti huo umeanza kuonesha mafanikio na unatarajiwa kuwasaidia wakulima kwa kupunguza gharama na kutunza mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasisitiza kuwa wakulima wa tumbaku nchini kutunza mazingira kwa kupanda miti ya kutosha na inayoendana na kilimo chao kwa mujibu wa sheria na kuacha kukata magogo na kutumia magogo kukaushia tumbaku badala yake watumie matawi ya miti. Pamoja na wito huo, Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku imeagiza wakulima wote wa tumbaku kwa msimu 2017/2018 watumie majiko sanifu yanayotumia kuni kidogo na yenye ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majiko haya sanifu yanatumika katika nchi za Malawi na Zimbabwe na yanapunguza sana uharibifu wa mazingira na hayana athari kwa wakulima sababu moshi unapungua sana.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko la watoto wa mtaani katika miji na majiji mengi hapa nchini.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na sheria zitakazoibana jamii kuwa na wajibu wa kulea watoto hawa badala ya kuwaachia majukumu Mashirika yasiyo ya Kiserikali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna ongezeko la watoto wa mitaani katika miji na majiji mengi hapa nchini. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatekeleza Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 ambayo inabainisha majukumu ya familia, jamii pamoja na Halmashauri za Miji na Majiji hapa nchini katika kutekeleza wajibu wa matunzo na malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu cha 95(1) cha Sheria ya Mtoto kinaelekeza na naomba kunukuu; “Ni jukumu la kila mwanajamii ambaye atakuwa na ushahidi au taarifa ya kuwa haki za mtoto zinavunjwa na wazazi, walezi au ndugu ambao wana jukumu la kumlea mtoto lakini wameshindwa kufanya hivyo au wameacha kwa makusudi kutoa huduma za chakula, malazi, haki ya kucheza au kupumzika, mavazi, haki ya matibabu na elimu atatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Halmashauri husika.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 95(2), kinamuelekeza Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri husika kupokea taarifa ya malalamiko na kumwita mlalamikiwa ili kujadili tatizo hilo. Maamuzi yatatolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kwa kuzingatia maslahi mazima ya mtoto husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mlalamikiwa atapuuza maamuzi yalyotolewa na Afisa Ustawi wa Jamii, shauri hilo litafikishwa Mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 95(5) ambacho kinaelekeza na naomba kunukuu; “Mtu yeyote atakayekiuka kifungu cha 95(1) atakuwa ametenda kosa, na akitiwa hatiani atahukumiwa kulipa faini isiyopungua shilingi elfu hamsini za Kitanzania au kifungo cha miezi mitatu jela au vyote viwili”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kuzielekeza Halmashauri zote nchini kutunga Sheria Ndogo zitakazodhibiti watu wanaosababisha watoto kuishi na kufanya kazi mitaani. Aidha, Waheshimiwa Wabunge na sisi tutoe elimu ya uwepo wa sheria hii kwa wapiga kura wetu.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA alijibu:-
Kumekuwa na wimbi kubwa la uhalifu unaofanywa na baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji katika maeneo mengi Jijini Dar es Salaam.
(a) Je, Serikali mpaka sasa imechukua hatua gani kudhibiti wimbi hili linalokuwa tishio kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri?
(b) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakiki na kutambua mmiliki, dereva na mahali zinapopaki bajaji na bodaboda?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na ongezeko la uhalifu unaofanywa na waendesha bodaboda ama bajaji katika maeneo mengi Jijini Dar es salaam. Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kama kufanya doria za magari, doria za pikipiki na za watembea kwa miguu lakini pia kuanzisha na kushirikiana na vikosi vya ulinzi shirikishi ili kubaini na kuzuia uhalifu katika maeneo ya makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Serikali za Mitaa, Halmashauri na Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuhakiki pikipiki hizo ikiwa ni pamoja na kuwapangia maeneo ya kuegesha (ku-park). Aidha, kupitia usajili wa TRA na Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imeendelea kuhakiki pikipiki hizo ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuzisajili katika maeneo ya maegesho ili kupata kumbukumbu za mmiliki, dereva na eneo maalum wanaloegesha pikipiki hizo.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Kiwango cha elimu katika Mkoa wa Tabora kimeshuka sana, Mkoa umefanya vibaya katika mtihani wa darasa la saba, kidato cha nne na cha sita. Kufanya vibaya kunatokana na changamoto mbalimbali kama walimu, upungufu wa madawati na idadi kubwa ya wanafunzi katika madarasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kero hizi zinatatuliwa ili kurejesha hadhi ya elimu Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, ambaye ni mtoto wa shangazi yangu na Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto zilizotajwa katika swali, si kweli kwamba kiwango cha elimu kimeshuka sana Mkoani Tabora kwa kufanya vibaya kwenye mitihani. Takwimu zinathibitisha hali tofauti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, katika mitihani ya darasa la saba ya mwaa 2016 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 71.35 ambapo Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya 10 kitaifa, lakini mwaka 2017 ufaulu ulipanda hadi asilimia 73.61 na Mkoa ukaendelea kushika nafasi ya 10 kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2016 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 71 ambapo Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya 10 kitaifa, lakini mwaka 2017 ufaulu ulipanda hadi asilimia 84 na Mkoa kushika nafasi ya 3 Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kwa upande wa kidato cha sita, ufaulu mwaka 2016 ulikuwa asilimia 97.8 na Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya 11 kitaifa. Kwa mwaka 2017 pamoja na takwimu kuonesha kuwa ufaulu ulikuwa asilimia 87, nafasi ya mkoa kitaifa ilipanda hadi nafasi ya 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka yote miwili mfululizo, Mkoa wa Tabora umekuwa juu ya wastani wa ufaulu kitaifa, hilo ni jambo la kujivunia. Kwa hali hiyo hatuwezei kusema kiwango cha elimu katika Mkoa wa Tabora kimeshuka bali kimepanda. Serikali ina kila sababu ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Aggrey Mwanri na viongozi wote wa Mkoa wa Tabora wakiwemo viongozi wa wilaya zote na hamashauri zote kwa juhudi zao zilizowezesha matokeo hayo mazuri.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa inayokabiliwa na tatizo kubwa la ndoa za utotoni na kusababisha watoto wengi wa kike kushindwa kumaliza elimu ya msingi au ya sekondari. Aidha, hivi karibuni Serikali ilikata rufaa juu ya ndoa za utotoni ikitaka iruhusiwe watoto wa kike kuolewa na umri kuanzia miaka 14 ambapo hii ni kinyume cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia watoto wa kike wa Mkoa wa Tabora angalau wengi waweze kwenda kupata elimu ya msingi na sekondari kwa kupunguza ndoa za utotoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wote wa kike na kiume wa Tanzania. Hii inadhihirishwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuifanya elimu ya msingi na ya sekondari kuwa ni elimu ya lazima na kutolewa bila malipo. Lengo la mpango huu ni kuhakikisha watoto wetu wote ikiwa ni pamoja na watoto wa kike wanaipata elimu hiyo bila kikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Elimu ambayo inalinda haki za mtoto kusoma hadi sekondari. Kupitia marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Elimu na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016, ni marufuku kwa mtu yeyote na katika mazingira yoyote kuoana na msichana au mvualana anayesoma shule ya msingi au sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kosa kumpa mimba msichana anayesoma au sekondari na kwa yeyote anayesaidia msichana au mvulana anayesoma kuoa au kuolewa anakuwa ametenda kosa. Marekebisho haya yameweka adhabu kali kwa yeyote anayetenda makosa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kumlinda mtoto wa kike na ndoa za utotoni, licha ya Sheria ya Ndoa kuweka mazingira na vigezo vya mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuhakikisha mtoto huyu analindwa. Katika kulisimamia hilo, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo pamoja mambo mengine imeainisha haki za mtoto ikiwemo haki ya kupata elimu na kutoa wajibu wa haki hizo kulindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuzuia vitendo vya kuwaozesha watoto wa kike. Si tu kwa mkoa wa Tabora bali katika nchi yote ili kuwawezesha watoto wetu wa kike kupata elimu ya msingi na sekondari na pale ambapo vitendo hivyo vinajitokeza wananchi wana wajibu wa kutoa taarifa na kushirikiana na vyombo vya Serikali ili kuhakikisha wanaofanya makosa hayo wanachukuliwa hatua za kisheria.
MHE. ESTHER N. MATIKO (K.n.y. MHE. HAWA S. MWAIFUNGA) aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Tabora inakabiliwa na changamoto kubwa za majengo, Wauguzi, Madaktari na Wahudumu wengine wa Hospitali, pia kuna uhaba mkubwa wa vitanda hali inayosababisha wajawazito kuzalia chini:-

(a) Je, katika mwaka huu wa fedha Serikali imejipanga vipi kuwasaidia Wananchi wa Tabora kupata ahueni kwa kutatua kwa kero za Hospitali hiyo inayotegemewa na zaidi ya robo tatu ya wakazi wa mji wa Tabora?

(b) Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kuwa Wilaya ya Tabora Mjini na Uyui nazo zinapata hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora katika ajira mpya za mwezi Julai, 2018 imeajiri watumishi wapya wapatao 49 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kati ya hao wakiwemo wauguzi, wateknolojia, wafamasia na madaktari na kufanya hospitali kuwa na jumla ya watumishi 357 kwa kada zote kati ya watumishi 468 wanaohitajika kulingana na ikama ya hospitali ambayo ni sawa na asilimia 76.3 ya mahitaji halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hospitali haina tatizo la vitanda na magodoro lakini kuna ufinyu wa majengo unaopelekea kuwa na vitanda vichache. Hivyo basi kwa kuwa hospitali za rufaa za mikoa zimekabidhiwa rasmi chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 wizara imetenge bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ambapo itaweza kupunguza uhaba wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka fedha 2018/ 2019 Serikali imepanga kujenga hospitali za wilaya 67 nchi nzima katika jitihada za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kwa upande wa Wilaya ya Tabora Mjini na Uyui nazo zimepatiwa fedha kiasi cha bilioni 1.5 kwa kila moja kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imeboresha vituo vya afya 13 katika Wilaya ya Uyui DC, Tabora MC, Nzega TC, Kaliua DC, Igunga DC, Skonge DC, Urambo DC na Nzega DC. Kukamilika na kuanza kutumika kwa hospitali na vituo vya afya hivi vitapunguza sana msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-

Ugonjwa wa Mguu Kifundo unatibika katika Hospitali ya Rufaa Kitete – Mkoani Tabora ambapo hupokea zaidi ya Watoto 40 wenye tatizo hilo kila mwezi:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa vya kutosha kama vile POP, bandeji, pamba, kiatu na gongo-pinde ili kusaidia watoto hao?

(b) Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo kwa watoto Mkoani Tabora na familia nyingi hazina uwezo wa kufika Hospitali kupata huduma; je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ili watoto wengi zaidi waweze kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utoaji wa huduma hizi, vifaa tiba vya huduma za utengemao vimeingizwa katika mfumo wa ununuzi wa Bohari ya Dawa (MSD) kuanzia mwaka 2018/2019 na hivyo kufanya upatikanaji wa POP bandeji, pamba na viatu na gongo- pinde kupatikana kwa uhakika. Aidha, Wizara imeagiza waganga Wafawidhi na Wafamasia katika vituo vya kutolea huduma za afya kupeleka mahitaji yao mapema Bohari ya Dawa ili pasiwepo na upungufu wa aina yoyote wa vifaa tiba ikiwa ni pamoja na vifaa hivyo vinavyotumika katika kutoa huduma za utengamao.

(b) Mheshimiwa Spika, kutokana na ukubwa wa tatizo hilo hapa nchini, Wizara yangu imeandaa Mpango Mkakati wa muda wa Kati (Medium Term Strategy: 2017-2021) unaolenga kufikisha huduma za utengemao hadi ngazi ya Wilaya ifikapo Juni 2021, ambapo kwa sasa huduma hii hupatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali zote Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. HAWA S. MWAIFUNGA) aliuliza:-

Ajali za barabarani bado zimekuwa tishio kubwa kwa maisha ya Watanzania, kutokana na ajali hizo tunapoteza nguvu kazi ya Taifa na familia nyingi zinabaki zikitaabika.

Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na ajali hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na athari kubwa za ajali za barabarani kwa Taifa Serikali ina mkakati madhubuti wa kupambana na tatizo hili. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza wigo wa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo hivyo kwa njia ya redio, luninga na machapisho na vipeperushi.

Aidha, mikakati mingine ni kuboresha mifumo ya utendaji kazi maeneo ya ukaguzi wa mabasi na maroli, mfumo wa ufuatiliaji wa magari barabarani na mfumo wa uwekaji nukta katika leseni za madereva utakaodhibiti tabia za madereva wazembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Serikali ilibuni na kutekeleza mikakati hii ya kupunguza ajali barabarani ambao katika awamu tatu zilizotekelezwa mpaka sasa umefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 43. Aidha, awamu ya nne ambayo inaendelea kutekelezwa tumejipanga kupunguza ajali kwa asilimia 35.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza: -

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Tabora kuwa na soko la uhakika la zao la tumbaku?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuruhusu soko huria kwa zao hilo ili wakulima wanufaike?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo mfumo wa sasa wa uuzaji wa tumbaku nchini ni wa soko huria ambao unaruhusu kampuni yoyote yenye sifa kuingia mkataba na mkulima kabla ya uzalishaji wa tumbaku ambapo mkulima anakuwa na uhakika wa soko, ubora na bei ya kuuzia tumbaku yake. Wizara inaendelea kuboresha mfumo huo ili uwe mfumo wa uwazi na kuleta mfumo wa flow market competition.

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la tumbaku linategemea mahitaji ya dunia. Katika soko la dunia ambapo mahitaji ya tumbaku katika soko la dunia yamekuwa yakishuka kwa wastani wa asilimia sita mpaka saba katikamsimu wa mwaka 2019/2020. Hali hiyo, imetokana na mambo mengine ikiwemo janga la Corona na na kampeni ya kidunia ya kupunguza matumizi ya bidhaa za tumbaku. Lakini msimamo wa Serikali ni kuendelea kulijenga soko la tumbaku nchini na kuongeza transparency katika soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua zingine ili kuongeza ushindani katika soko la tumbaku. Serikali imeruhusu kampuni nane za Kitanzania ambazo zimeshiriki katika msimu wa 2019/2020 na katika msimu huu wa 2020/2021 kampuni hizi zimetoa jumla ya mikataba yenye uzito wa jumla ya kilo milioni 17 kati ya hizo kilo milioni 9.7 zitatoka kwa wakulima wa Mkoa wa Tabora kutokana na jitihada hizo za kutafuta masoko. Sasa uzalishaji wa tumbaku katika Mkoa wa Tabora utaongezeka kutoka kilo milioni 16 katika msimu wa mwaka 2019/2020 hadi kufika kilo milioni 32 katika msimu wa mwaka 2020/2021.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Jengo la Manispaa ya Tabora ambao umesimama kwa muda mrefu sasa huku shughuli za Manispaa zikiendelea kufanyika kwenye majengo ya zamani yaliyochakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mhesimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa baadhi ya halmashauri nchini ambazo hazina majengo ya utawala na uwepo wa majengo chakavu. Serikali kwa kutambua hilo, inaendelea na ujenzi wa majengo ya utawala ya Halmashauri 100 nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa Tabora kwa kutumia mapato ya ndani, mwaka 2015 ilianza kujenga jengo la utawala la ghorofa nne ambalo lilikadiriwa kugharimu kiasi cha shilling bilioni 5.7 mpaka litakapokamilika. Ujenzi wa awamu ya kwanza unaohusisha boma la jengo hilo umekamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja ili kuendeleza ujenzi wa jengo hilo ambapo ujenzi wa awamu ya pili utatumia utaratibu wa force account ili kupunguza gharama za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, imeelekezwa kukamilisha taratibu za kuwasilisha maombi ya fedha za ujenzi huo Wizara ya fedha na Mipango ili ujenzi uanze mara moja.

Mheshimiwa Spika, aidha, halmasahuri imeelekezwa kuanza ukamilishaji wa baadhi ya maeneo ya jengo hilo ili watumishi waweze kupata ofisi wakati ukamilishaji ukiendelea.