Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli (28 total)

Vinguguti ina wakazi wengi na mpaka sasa hivi Kata ya Vinguguti haina zahanati yoyote.
Swali la Pili, kwa kuwa Kata ya Kipawa, Kata ya Minazi mirefu, Kata ya Kiwalani pamoja na Kata ya Kisukuru na Kimanga zina matatizo kama haya haya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inashirikiana na Manispaa ya Ilala ili Kata hizi ziweze kuwa na zahanati lakini pia tuweze kuwa na vituo vya afya ili kuondoa msongamano katika Hospitali ya Amana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, Vinguguti kweli ni eneo ambalo lina wakazi wengi sana na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba eneo hili lazima lipatiwe kipaumbele. Lakini naomba nimwombe Mheshimiwa Mbunge japokuwa juhudi kubwa zinafanyika needs assessment wakati mwingine zinaanza katika Mabaraza yetu ya Madiwani.
Kwa hiyo, kwa sababu nia yako ni njema na Serikali tutakuunga mkono katika eneo hilo. Lakini kikubwa zaidi tutaweka nguvu zaidi katika lile eneo letu la Kituo cha Afya cha Mnyamani, kwa sababu ni eneo ambalo wenzetu wa Plan International walifanya juhudi kubwa sana kujenga kituo kile, jukumu letu kubwa ni kwamba kwanza kuwekeza vya kutosha kituo kile angalau kiweze kua-accommodate hii demand iliyokuwepo hivi sasa, wakati huo tukiangalia mtazamo wa mbali jinsi gani tutafanya, eneo lile la Vinguguti tuwe na sehemu ya kujenga zahanati kubwa na siyo zahanati kwa hadhi ya Vingunguti, kujenga moja kwa moja kituo cha afya kutokana na mahitaji ya idadi ya watu waliokuwa katika maeneo yale.
Mheshimwa Spika, eneo la Kipawa, Kiwalani na maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema ni kweli, ukiangalia yana sifa zinazofanana na maeneo ya Vingunguti kwamba watu ni wengi.
Mheshimiwa Spika, naomba nisema kwamba mimi nipo radhi kabisa kukutana na Mheshimiwa Mbunge kubadilishane mawazo, kwamba tutafanya vipi na kwa sababu nikijua Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wana mikakati mikubwa sana ya ujenzi wa sekta afya ukiangalia demand ya sasa hivi iliyokuwepo hivi sasa hospitali yetu ya Amana inazidiwa, hata Hospitali ya Taifa ya Muhimbili idadi ya wagonjwa imekuwa wengi, ni kwa sababu katika ngazi ya chini tunakosa facilities za kuwasaidai wananchi kiasi kwamba kila mngojwa anaona kwanza aende Hospitali ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI jukumu letu kubwa ni kwamba katika mpango unaokuja tuhakikishe tufanye kila liwezekanalo. Huduma ya afya tuipeleke chini zaidi kupunguza ile referral system inayoenda juu ili kuhakikisha hospitali zetu za ngazi za juu ziweze kupata fursa nzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, hili kwa sababu Waziri wa Afya kesho ata-table bajeti yake hapa, tutaona mipango mipana katika Wizara Afya ambayo ina lenga moja kwa moja kutatua tatizo la suala la afya katika jamii yetu.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilitaka nimuambie Mheshimiwa Naibu Waziri wa Miundombinu kwamba sasa hivi wakazi wanaodai fidia siyo 800 ni wakazi 1,600. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yake mazuri aliyonipa, lakini nilitaka niongeze maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tathmini iliyofanyika ilifanyika 1995 na wakati huo mfuko wa cement au vitu vyote ambavyo vinavyohusisha ujenzi vilikuwa viko bei ya chini, je, Serikali ina mpango gani wa kuwafanyia tathmini tena hawa wakazi 1,600 ili waweze kupata fidia yao kutokana na bei za vifaa vya ujenzi kupanda?
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nalotaka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba commitment ya Serikali, iseme itawalipa lini hawa wakazi wa Kipunguni, ambao wamebaki 1,600, kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali haijasema itawalipa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILINO: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu concern ya Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kipunguni 742 ambao bado hawajalipwa fidia. Kwanza, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba itabidi tuwasiliane ili tuwe na takwimu sahihi. Kwa mujibu wa takwimu zetu waliobakia ni 742 na sio 1,600 aliowataja. Hata hivyo, kwa sababu yeye anafahamu ni 1,600 tutalisawazisha hilo. Naomba atuletee orodha ili tuweze kuangalia hatimaye tuone kuna tatizo gani katika hizo takwimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwalipa hao 742 waliobakia, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi, Serikali itawalipa kama ilivyodhamiria. Kuhusu kwamba wafanyiwe tathmini upya, nadhani Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba hakuna sababu ya kufanya tathmini upya kwa sababu tathmini ile iliyofanyika na kwa kipindi ambacho kinachelewa tuna utaratibu wa kuhuisha viwango kwa maana ya kuongeza riba inayotakiwa kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba suala la tathmini upya wala siyo la msingi sana. La msingi ni sisi kupata fedha na kuwalipa hawa waliobakia 742 na tutalifanya hilo mara tutakapopata fedha.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru
Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake. Kwa kuwa, Wizara ya Maliasili imelitelekeza
hili eneo kwa muda mrefu na hili eneo limekuwa ni eneo hatarishi na lipo katikati
ya makazi ya watu, watu wamekuwa wakipita hapo wanavamiwa na wengine
wameumizwa. Je, Wizara haioni sasa umefikia wakati muafaka kulirudisha hili
eneo Manispaa ya Ilala ili liweze kutumika kwa maendeleo ya Watanzania wote.
(Makofi)
Swali la pili; Jimbo la Segerea lina wakazi wengi lakini ndio Jimbo mpaka
sasa hivi halina kituo cha afya, halina soko, halina viwanda vidogovidogo
ambavyo wananchi au vijana wanaweza wakajiendeleza. Je, Wizara ya Maliasili
haioni kwamba umefika wakati ilirudishe hili eneo kwa wananchi wa Jimbo la
Segerea ili sisi tuweze kujenga kituo cha afya na mimi Mbunge wa Jimbo la Segerea nitatoa milioni 50 katika Mfuko wa Mbunge ili tuweze kuanzisha kujenga
kituo cha afya.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu
swali lake la kwanza Wizara haijatelekeza eneo la Msitu wa Kinyerezi na badala
yake miongoni mwa maeneo ambayo tayari yana maboya kwenye mipaka na
ambayo yana mabango na usimamizi wake unaendelea kwa kufuata mipaka
hiyo niliyoitaja ambayo imeshawekwa alama kama nilivyotangulia kusema eneo
la msitu huu ni mojawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema eneo hili ni la hekta 4.4 tu.
Eneo la hekta 4.4 ni dogo sana, tunapata changamoto kubwa sana kama Taifa
ya kwamba Miji inaonekana kama vile ili uone mahali kuna mji ni sawasawa
kwamba panatakiwa pawe mahali palipo wazi kabisa hapatakiwi kuwa na miti
hata kidogo. Hii ni dhana ambayo tunapaswa kuondokana nayo twende katika
mwelekeo ambao Miji yetu itakuwa pamoja na majengo na vitu vingine
unavyoweza kuviona kama miundombinu, misitu iwe ni sehemu mojawapo. Tuwe
na miti, bustani ndiyo tunaweza kuwa na miji ambayo itakuwa endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la mahitaji ya eneo;
nimesema kwenye swali la msingi, Ilala ina eneo kubwa bado kwa mujibu wa
sensa iliyopo ina jumla ya hekta 21,000. Kwa hiyo, hakuna uhaba wa ardhi, tuna
changamoto ya matumizi bora ya ardhi. Haya mambo mawili ni tofauti. Kukosa
ardhi au kuwa na uhaba wa ardhi na kukosa mbinu za matumizi bora ya ardhi ni
mambo mawili tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu narudia tena Mheshimiwa
Mbunge kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani na Halmashauri ya Wilaya
inayohusika, waende wakakae wajaribu kuangalia Ilala kwa ukubwa wake na
eneo lake lote, miundombinu iliyopo na fursa zingine zilizopo za matumizi ya
ardhi, wafanye mpango bora wa matumizi ya ardhi ili waweze kupata maeneo
ya kuweza kujenga miundombinu aliyoizungumzia.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba nimekuwa nikiuliza hili swali na leo hili ni swali la tatu; lakini pia Naibu Waziri alikuja kuongea na wananchi wa Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni kuhusiana na mambo ya fidia na akawaahidi atarudi. Mpaka sasa hivi ni mwaka mmoja Mheshimiwa Waziri hajawahi kurudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini mwaka 1995, leo ni miaka 22: Je, atawalipa kwa kutumia tathmini gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, namwuliza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hawa wananchi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nabadilisha la kuja…
Mheshimiwa Spika, nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba, hawa wananchi wamesimamisha maendeleo kwa muda mrefu; aseme hapa leo katika Bunge hili kwamba: Je, waendelee na maendeleo yao mpaka watakapopata hizo pesa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli niliahidi nitarudi, lakini nilimwambia nitarudi nikiwa na majibu sahihi. Sikusema mwaka mmoja, niliwaambia ni katika kipindi cha miaka mitatu tatizo hilo tutalitatua. Naona umeshaona tofauti, toka pale nilipofika, mwaka huu tumeshatenga shilingi bilioni tano na mwaka ujao tumeshatenga shilingi bilioni 30. Unaona kabisa kwamba nitakaporudi kule, nitarudi kwa kishindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili kwamba tunalipa kwa tathmini gani? Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalipa kwa tathmini ile iliyofanyika pamoja na interest ya miaka yote hiyo. Ndivyo sheria za fidia zinavyotuongoza, kwamba kuanzia mwaka uliofanya tathmini ukizidisha miezi sita hujalipa, kuna interest inaingia na kadri utavyoendelea kuchelewa ndivyo interest inavyoingia. Ndiyo maana kama umeona gharama inayodaiwa iliyopo katika kitabu kile cha tathmini ni shilingi bilioni 19, lakini fedha tutakazolipa ni zaidi ya shilingi bilioni 35, ina maana ni kwa sababu ya kuongeza interest ambayo ni kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri. Wananchi wa Jimbo la Segerea, Kata ya Kinyerezi, Mtaa wa Kifulu nao pia walitoa maeneo yao kwa ajili ya kuipisha TANESCO na mpaka sasa hivi hawajalipwa tangu Machi, 2016. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri ni lini wananchi wa Kinyerezi watalipwa pesa hizo kwa ajili ya maeneo yao waliyotoa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tathmini ya maeneo ya Kinyerezi ambapo maeneo yao yametolewa kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Kinyerezi imekamilika na kiasi cha Sh.10,475,603,000 zinahitajika. Kwa hiyo, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake kwamba fidia hii italipwa kwa bajeti zinazokuja. Ahsante.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutuletea maji Segerea, lakini nilitaka nimuulize Waziri, pamoja na kwamba tunapata maji asilimia 70, lakini kumekuwa na matatizo ya Kata kama Bonyokwa, Kipawa pamoja na Kiwalani na Minazi Mirefu. Sasa Serikali ina mpango gani kwa hizi Kata zilizobaki kuziletea maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii, lakini kubwa napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mbunge wa Segerea kwa namna anavyowatetea wananchi wake. Moja ni Mbunge shapu ambaye alishafika ofisini kwetu katika kuhakikisha kwamba tunaenda kufanya ziara katika Mkoa wa Dar es Salaam katika Jimbo la Segerea. Sisi mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwapatia maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari baada ya Bunge kwenda kuongea na wananchi wa Segerea katika kufanya mpango wa haraka ili wananchi wake waweze kupata maji.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri kutokana na tamko lake la juzi, Jimbo la Segerea katika Kata ya Kipawa kuna wananchi 1,800 wanasubiri malipo tangu mwaka 1992 na juzi alisema kwamba waondoke. Sasa nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa atawafanyia malipo yao watu wa Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni na wanahusika vipi kuondoka kabla hawajalipwa malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna wananchi wanatakiwa wapishe eneo la uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere International Airport ambao walivamia miaka ya nyuma, lakini Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kwamba walipwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya hao kuna wananchi 59 ambao tayari wamekwishapokea malipo yao kwa ajili ya kupisha upanuzi wa uwanja huo. Tunaowazungumza na ambao nilitoa agizo waondoke ni hao wananchi 59 na bado naendelea kusisitiza kwamba hao wananchi 59 ambao tayari wamekwishakupokea malipo yao ya fidia, wanatakiwa waondoke wapishe upanuzi wa uwanja wetu wa ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikiri kwamba kuna baadhi ya wananchi ambao hawajalipwa kwa sababu mbalimbali, kuna baadhi walifungua kesi na kuna wengine ambao hawajafungua kesi lakini hawakuridhika na fidia, hao bado tunaendelea kutafuta utaratibu mwingine wa kuwashawishi kwa njia moja au nyingine ili waweze kupisha upanuzi wa uwanja huo wa ndege.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri, kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha Dar es Salaam na Mheshimiwa Waziri alishafanya ziara Jimbo la Segerea na kuona barabara nyingi ambazo zimekatika na nyingine zimekata kabisa mawasiliano.
Sasa Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba hizo barabara zinarudi kwenye matumizi ya kawaida hasa katika Jimbo la Segerea, Kata ya Kimanga, Segerea pamoja na Kinyerezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kwamba tumekuwa na mvua nyingi na maeneo mengi nchini yameharibika. Kwa Jiji la Dar es Salaam kuna hali mbaya sana naye mwenyewe kwa sababu anatokea Jijini Dar es Salaam kwa kweli miundombinu ya barabara imeharibika sana na kwa sababu mvua ni nyingi na zimeendelea kunyesha na ile mito mikubwa inaendelea kumomonyoka na kufuata makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu ni kwamba tunatazama kwa macho mawili Jiji la Dar es Salaam kwa maana kwamba mvua zitakapopungua tuweze kwenda kufanya marekebisho makubwa. Niseme tu na niendelee kurejea kwamba upande wa TANROADS na upande wa TARURA wamekuwa wakifanya uratibu wa kuangalia uharibifu mkubwa uliofanyika. Kwa sababu uharibifu unaendelea kutokea, nawaomba tu kila kukicha waendelee kuona kama kuna ongezeko la uharibifu, tufanye makadirio kuona namna gani tutafanya ili kurejesha miundombinu iliyoharibika kwa sababu bado mvua zinaendelea kunyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, aendelee kufuatilia na tuendelee kupeana taarifa, Serikali iko macho kuangalia na kufanya marekebisho.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri pale Segerea kuna pori moja linaitwa Msitu wa Nyuki, walikuwa wanafuga nyuki zamani lakini naona Wizara imeshaachana na huo mpango wa kufuga nyuki.
Sasa Wizara ina mpango gani na hilo pori maana yake wameliacha tu, na kama hawana mpango nalo kwa nini wasitupe sisi Manispaa ya Ilala ili tuweze kulitumia katika matumizi ya soko na mambo mengine ya huduma za kijamii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba tuna msitu katika lile eneo ambalo lilikuwa linatumika kwa ajili ya kufuga nyuki, lakini si kwamba lile pori tumeliacha tu, kuliacha tu bado linaendelea kuhifadhi ule uoto wa asili.
Kwa hiyo, bado ni pori linalotambulika vizuri kabisa na bado tutaendeleza jitihada za kufuga, lakini pia inasaidia sana katika kuweza kupunguza carbon dioxide ambayo inatokea katika viwanda mbalimbali pale Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lile eneo tutaendelea kulihifadhi na litaendelea kuhifadhia na kuendelezwa.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, ni lini sasa watamalizia barabara ya Kimanga ambayo inajengwa sasa kwa muda wa miaka miwili, mpaka sasa imeleta usumbufu mkubwa katika Kata ya Kimanga na mpaka sasa haijamalizika imesimama na mkandarasi hayupo, ni lini Serikali itamalizia hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kaluwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, baada ya Bunge hili nitatembelea mradi huu niangalie pamoja na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuona changamoto zilizopo ili tujue hatua za kuchukua kwa haraka ili barabara iweze kuboreshwa.

MWENYEKITI: Kwa hiyo unakwenda jimboni kwake?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mradi.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ambayo ameyajibu Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Serikali imeanzisha miradi ya kimkakati katika mikoa mingine na ukizingatia katika Jimbo la Segerea kuna wananchi wengi sana ambao wanakaribia 1,300,000; je, Serikali ina mpango gani kujenga masoko ambayo yatakuwa yanawasaidia wananchi ili wasiweze kwenda mbali kama hivyo alivyosema Kisutu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nimemsikia Mheshimiwa Waziri anaongelea kuhusiana na Soko la Kinyerezi. Kutokana na kwamba nilifanya ziara mwezi uliopita, hilo soko mpaka sasa hivi kwanza linavuja, halafu pia halijamaliziwa vizuri. Kwa hiyo, haliwezi kuzinduliwa mwaka 2019 kama anavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna Kata nyingi ambazo hazina masoko kama Kata ya Kisukulu, Kata ya Kipawa na Kata nyingine: Je, Serikali ina mpango gani kuhusiana na hizo Kata nyingine kuhakikisha kwamba zinapata masoko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuelewa, nakushukuru. Swali la kwanza ningeomba niseme tu kwamba utaratibu unaotumika kuibua miradi ya kimkakati ni Halmashauri husika, inakaa na wataalam wake, wanaandika andiko, wanaliwasilisha Ofisi ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha; wataalam wa Wizara ya Fedha wanaenda kufanya tathimini ya andiko lenyewe, gharama zake na mrejesho kwa maana ya faida itakayopatikana na baada ya hapo wataruhusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ya kuwa na masoko ya Kinyerezi na maeneo mengine, itategemea Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilitaka tu niseme kwamba inawezekana ni kweli Mheshimiwa Mbunge anasema, sasa nimwelekeze Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala aende akafanye utaratibu wa kukarabati na kurekebisha soko hilo ili liendane na ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi, kwamba Kinyerezi ilizinduliwa mwaka 2017 na Mbio za Mwenge wa Uhuru lakini Mei mwaka huu linatakiwa lianze kufanya kazi. Mkurugenzi aweke pesa pale ili liweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja anayoizungumza Mheshimiwa Mbunge hapa, soko la Kisutu ni kweli lipo kwenye mkakati, limesharuhusiwa na Serikali na fedha imeshatolewa. Naomba nimhakikishie, kwa kadri anavyojua kwamba lazima lisimamiwe; na Mheshimiwa Mbunge nimridhishe kwamba yeye katika Manispaa ya Ilala ana ujenzi wa machinjio ya kisasa kabisa ya Vingunguti ambayo ipo pia kwenye mpango mkakati katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niulize, Serikali ina mpango gani kuhusiana na barabara za Mkoa wa Dar es Salaam hususan barabara ya Vingunguti - Liwiti ambapo kuna mradi mkubwa wa machinjio lakini barabara yake ni mbovu sana, ina mahandaki makubwa? Sasa Serikali ina mpango gani kuhusiana na hizo barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama jana nilivyozungumza ni kwamba kati ya maeneo ambayo yamepata athari kubwa hasa kwa mvua za mwezi Oktoba na Novemba ni Mkoa wa Dar es Salaam. Nilisema kwamba katika hatua zile za awali, kama mkakati wa kunusuru hali ya uharibifu wa barabara katika Jiji ni pamoja na kupeleka fedha za dharura. Kwa hiyo, tulitumia takribani shilingi milioni 500 kurejesha maeneo ambayo yalikuwa yameharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha, bado uharibifu unaendelea kutokea. Nasi kama Serikali tunajipanga na kila wakati tumetoa maelekezo kwa Mameneja wa Mikoa, waendelee kutuletea hizo taarifa za uharibifu unaotokea ili tuendelee kufanya uratibu kwa sababu suala la kurejesha miundombinu hasa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha ni endelevu. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana, watupe taarifa za maeneo ambayo yanaendelea kupata uharibifu na sisi tulivyojipanga tutaendelea kuwahudumia wananchi katika maeneo haya ili kwanza waweze kupita, lakini mvua zikipungua tutakuja na mkakati wa kuona tunafanya maboresho makubwa.
MHE. BONAH KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mheshimiwa Waziri Serikali ina mpango gani kuhusiana na Barabara ya Kimanga, kwa sababu last time Naibu Waziri alienda kufanya ziara lakini ile barabara mpaka sasa hivi imeachwa kutengenezwa. Pia nauliza kuhusiana na daraja la Segerea Seminari ambalo limechukuliwa na maji tangu mwaka 2012 lakini pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais mpaka leo halijatengenezwa ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anapigania sana barabara za eneo la jimbo lake. Lakini niseme tu ile barabara ya Kimanga kulikuwa na mradi unaendelea nitafuata tu ufuatiliaji nione nini kimetokea kama ule mradi unasua sua na tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge tukatembelee mradi tuone changamoto iliyokuwepo ili tuweze kuitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu lile daraja la upande ule wa Seminari, nilitembelea eneo hili tunahitaji kuweka daraja kubwa pale, Serikali bado inajipanga kutafuta fedha za kutosha hili tuweze kuboresha katika eneo hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba uvute Subira tutajipanga vizuri tutaporesha eneo hili kwa sababu linahitaji fedha nyingi ili kuweza kuboresha mahali hapa ambapo ni sehemu korofi ahsante sana.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nataka kujua ni lini Serikali italipa fedha hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu mradi huu umekaa sasa ni miaka minne, je, Serikali ipo tayari kuwapa kifuta jasho wananchi ambao wamesubiri kwa muda wote huo wakati wakisubiri malipo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Bonnah, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nieleze kidogo kwamba fidia inayotakiwa kufanyika katika maeneo haya ni fidia ambayo ni ya miradi ambayo tunaweza kuiita miradi ambatanishi. Kimsingi umeme unaozalishwa katika Bwawa letu la Mwalimu Nyerere megawatt 2,115 unatakiwa utoke Mwalimu Nyerere kuja kuingia katika Gridi ya Taifa na unaingilia kwenye Gridi ya Taifa pale Chalinze. Kwa hiyo, itajengwa hiyo njia ya kutoka Mwalimu Nyerere kuja Chalinze, lakini Chalinze kwenda Kinyerezi na Chalinze kuja Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuhusu exactly fidia italipwa lini ni tusema ni kabla ya kufika mwezi wa kumi mwaka huu, kwa sababu lazima kwanza tulipe fidia ndiyo tutaweza kujenga njia hiyo ya kupeleka umeme. Njia hiyo ya kupeleka umeme lazima ikamilike kabla ya tarehe 14 Juni, 2022 ili iweze kusafirisha ule umeme utakaozalishwa pale Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fidia itatolewa kwa wakati na haitochelewa kwa sababu kuchelewa kwa fidia hiyo kutasababisha mradi wa Mwalimu Nyerere usiweze kuingiza umeme wake kwenye grid.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili kama Serikali ipo tayari kuwapa kifuta jasho, niwahakikishie waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoendeshwa na Mama yetu Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni Serikali sikivu na isiyoonea mwananchi taratibu za fidia zipo na zinafahamika kwamba inalipwa kwa namna gani na ndani ya wakati gani. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa fidia stahiki italipwa kwa kila anayestahili kulipwa kwa mujibu wa viwango vya kisheria vilivyowekwa na muda uliowekwa kwa ajili ya hesabu hizo.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili nyongeza. Swali la kwanza: Je, ni lini Serikali itaanza kupanga vituo vya afya kutokana na wingi wa watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Sera ya Serikali ni kila Kata kuwa na Kituo cha Afya na Kila Mtaa uwe na Zahanati: Je, ni lini Serikali italeta vituo vya afya katika Kata ya Kimanga, Kisukuru, Buguruni pamoja na Minazi Mirefu ili hawa wananchi waweze kuondokana na matatizo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ni kweli kwamba tunajenga Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali za Halmashauri katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia: kwanza, ukubwa wa kijiografia wa maeneo hayo; na pili, idadi ya wananchi katika maeneo husika ili kuhakikisha vituo vile vinasogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Bonnah kwamba Serikali imeendelea kujenga vituo vya afya kwa kuzingatia vigezo hivyo viwili; kigezo cha ukubwa wa jimbo au halmashauri na pia kigezo cha idadi ya wananchi. Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam, miaka miaka mitano iliyopita, zaidi ya vituo vya afya 12 vimeendelea kujengwa na Hospitali za Wilaya zimeendelea kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha ujao wa 2021/2022 katika Manispaa ya Ilala kwa maana ya Jiji la Dar es Salaam peke yake, kuna vituo vya afya vipatavyo sita vitakwenda kujengwa, pamoja na Hospitali ya Halmashauri na katika Halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam zitakwenda kujenga angalau vituo vya afya vitatu. Kwa hiyo, tunaona Serikali imeendelea kuhakikisha inaongeza idadi ya vituo vya afya katika Manispaa na Jiji la Dar es Salaam kwa kuzingatia idadi ya wananchi; na suala hili linafanyika kwa utaratibu huu nchini kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Sera ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo ya Msingi ni kuhakikisha kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya na Zahanati katika Vijiji. Sera hii imeendelea kutekelezwa kwa vitendo na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa mashahidi kwamba Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa sana katika ujenzi wa zahani na vituo vya afya katika kata zetu. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi kwa vituo vya afya ambavyo tayari Serikali imeanza kujenga na katika kata hizo ambazo Mheshimiwa Kamoli amezitaja. (Makofi)
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza tunaunga mkono jitihada za Serikali. Hata hivyo, kuna wananchi ambao wanafanya shughuli zao za kilimo cha mbogamboga ambazo zinawaingizia kipato, wako ndani ya mita 60; na shughuli zao hizo haziathiri mazingira.

Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao au kuwalinda ili wazidi kujiongezea kipato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa eneo hili linaweza likageuzwa kuwa vivutio au sehemu ambazo ni center ambazo wananchi wanaweza wakatengeneza, kama vile Coco Beach au sehemu nyingine, wakaweza kupata shughuli za kujiendeshea maisha yao.

Je, Serikali iko tayari kuwasiliana na Halmashauri zetu ili wananchi wetu ambao wanaweza kufanya shughuli hizi waweze kupewa maeneo haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la mita 60 ni jambo la kikanuni kabisa. Lakini kingine tunaweza tukawaruhusu wakaendelea ndani ya mita 60; lakini changamoto iliyopo, athari za kimazingira si athari za kuonekana leo na kesho. Huwezi ukachimba mgodi leo, ukawa unachimba dhahabu au chochote ukaziona athari leo. Huwezi kukata miti ukaona athari leo, huwezi ukaendesha viwanda ukaona athari leo. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo na kesho inawezekana wananchi wa Segerea wanaweza wasione athari za kimazingira, lakini baada ya muda watakuja kuona athari za kimazingira. Hicho ndicho kitu ambacho sisi Serikali tunakihofia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni vipi tutawasaidia, tuko tayari kuwasaidia kwa kuendelea kuwapa taaluma ili sasa waweze kufahamu mambo haya ili wajue athari za kimazingira. Kwa sababu tusipoyalinda mazingira hayataweza kutulinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine kwamba je, Serikali iko tayari kuwatengenezea creation centers kwa ajli ya angala ya kuweza kujiendesha. Hilo jambo wala hatuna tatizo nalo kwa sababu lengo letu ni kwasaidia wananchi; lakini nadhani watupe muda kwanza ili tutafute fedha kwa sababu hili jambo linahitaji fedha. Kupageuza pale ili tutengeneze sehemu ya kivutio yenye garden nzuri tunahitaji tupate fedha za kutosha. Lakini pia watupe muda ili tuweze kufanya ushauriano na baadhi ya wadau wengine maana pale Wizara za Maji, Maliasili na Ardhi, pamoja na sisi na Halmashauri zinahusika. Kwa hiyo jambo hilo linawezekana, lakini watupe muda kidogo ili tujue namna ambavyo tunafanya. Nakushukuru.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri: Je, ni lini Serikali itamalizia barabara ya Bonyokwa – Kimara ambayo tangu mwaka 2021 ilikuwa kwenye bajeti ambayo ni kilomita 3.5? Ni lini itawekwa lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoisema ya Bonyokwa ipo kwenye mpango wa TANROADS wa kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Serikali bado inaendelea kutafuta fedha kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Segerea kwamba hii barabara ni muhimu sana ambayo inaunganisha Segerea na Kimara; na tutaijenga kwa kiwango cha lami mara fedha itakapopatikana. Ahsante. (Makofi)
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Kipawa ambao walipisha Airport terminal three tangu mwaka 1997 na sehemu hiyo mpaka sasa hivi shughuli za maendeleo zimesimama. Je, ni lini Serikali itawalipa hawa wananchi fidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Kamoli, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi aliowasema wa Kipawa Airport ambao walipisha ujenzi wa uwanja wa ndege, suala hili nimwombe Mheshimiwa Mbunge aweze kutuletea maelezo sahihi kwa sababu ambao walilipwa na hawa ambao hawakulipwa ili tuweze kujua ni wapi ambao hasa anawasimamia ili tuweze kuwa na majibu sahihi kwa upande wa Serikali. Ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri ni lini barabara ya Bonyokwa - Kimara itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba amefika mara kadhaa Wizarani na Mheshimiwa Waziri pamoja na TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam wamemuahidi na mimi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo kutoka Bonyokwa kwenda Kimara ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itakarabati daraja la Kimanga ambalo linazunguka Tabata, pamoja na Kata zingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Kamoli Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa barabara hii upo kwenye usanifu na mara usanifu utakapokamilika daraja hili litajengwa. Ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Kwa kuwa hii ni Wizara ya Ujenzi, Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini TANROAD wataenda kutengeneza barabara ambayo wameiparua pale Kata ya Segerea kwa muda wa Miezi Mitatu sasa na wananchi wanapata vumbi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Kalua Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hii barabara imekuwa inatengenezwa kwa vipande na kipande anachokisema kweli tulikuwa tumeanza kufanya maandalizi lakini kulikuwa na shida ya kupata msamaha wa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba msamaha huu umeshatolewa na mara moja Mkandarasi atakuwa yuko site kuondoa lile vumbi ambalo linaleta shida kwa wananchi wa Jimbo la Segerea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu kupitia nafasi hii pia nimjulishe ama kumuagiza Meneja wa TANROADS kwamba kwa kuwa msamaha umeshatolewa basi Mkandarasi aende site ili aweze kukamilisha kazi ambayo anatakiwa aifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kuna pesa ambazo zinakuja sasa hivi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Swali la kwanza; je, ni kwa nini Serikali wakati inaleta hizo pesa ilete pamoja na hizo pesa za kujenga ofisi za walimu kwa sababu kumekuwa kuna tofauti kubwa kati ya madarasa ambayo yanakuja kujengwa lakini Walimu wanakuwaqa hawana ofisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je ni lini Serikali itanunua furniture za ofisi ambazo zimejengwa na manispaa zipo tu na hazina furniture za walimu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa sasa wa Serikali ni kujenga na kuongeza madarasa katika maeneo ambayo yana uhitaji na ndio maana katika miradi mikubwa ambayo tunayo sasa kwa maana Mradi wa SEQUIP pamoja na BOOST yote miwili kwa pamoja ina thamani karibU trilioni 2.35.

Mheshimiwa Spika, katika yale madarasa maeneo mengine wanajiongeza, ukipeleka madarasa mawili wanajenga na ofisi katikati ambalo ni jambo jema. Tumekuwa tukipeleka fedha kwa ajili ya majengo ya utawala. Kwa hiyo sisi tutaendelea tu kuziagiza halmashauri kutenga fedha kujenga maeneo ya utawala, lakini ofisi nyingine waendelee kujiongeza kwa kuweka ofisi katikati ya madarasa ambayo tumekuwa tukiyapeleka huko. Kuhusu fanicha nafikiri ni maelekezo yetu pia kwa halmashauri zote nchini kuwapatia furniture kwenye staff rooms zote za shule katika maeneo yao, ahsante sana.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, Serikali ina mpango gani na barabara ya Kisukulu - Maji Chumvi ambayo imeharibika sana sasa hivi na wananchi hawawezi kupita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bonnah Kamoli, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo ameianisha Mheshimiwa Mbunge inafanyiwa tathmini kwa wakati wa sasa na watakapomaliza tathmini tutampatia taarifa Mheshimiwa Mbunge, ni lini sasa tunaanza rasmi ujenzi katika eneo hilo.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilikuwa nataka commitment ya Serikali ni lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilikuwa nauliza kwa kuwa sasa hivi mfumo ndiyo unaochagua wapi nyumba ziende. Kwanini sasa Wizara isipeleke hizi nyumba kwa majimbo badala ya mfumo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali imeshaweka commitment ya kwa kutenga fedha katika bajeti yake, na ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha ambao tumepitisha bajeti ya TAMISEMI, tumetenga jumla ya bilioni 81.48 ambazo zitatumikwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za misingi na sekondari.

Kwa hiyo, ni commitment kubwa ya Serikali. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba tutafanya hivyo katika maeneo yote nchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, ni kwamba amekuja tu mfumo kwamba tupeleke katika majimbo. Niseme tutaendelea kuzingatia maeneo yote yenye uhitaji mkubwa ikiwemo katika jimbo lake kama ambavyo ameainisha. Kwa sababu lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba tunamaliza hii kero kwa kadri fedha itakavyokuwa inapatikana. Ahsante sana.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; je, Serikali imejipangaje kutokana na miradi mikubwa ambayo inaendelea hapa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini pia na Miradi ya SGR; ili kuhakikisha vijana wetu wa Tanzania wanaenda kusimamia hii miradi pindi itakapokamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Ili kuendana na Uchumi wa Bluu; je, Serikali imejipangaje kufundisha vijana wetu kwenye mambo ya uvuvi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali ilimeshaliona hilo na kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ile miradi wakati inaanza tayari tulishatambua vijana ambao walipaswa kuchukuliwa na kwenda kupata mafunzo zaidi. Katika Mradi wa Reli ya Kisasa, vijana 3,526 tayari walishaajiriwa. Kati ya hao, tumewatambua vijana 1,916 ambao wataenda kwenye vyuo vyetu mbalimbali na ndio watakaofanya succession plan kwenye maeneo hayo kwa ajili ya masuala ya teknolojia na ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, likiwa sambamba na Bwawa la Mwalimu Nyerere ambapo ni zaidi ya vijana wa Kitanzania 10,228 ambao tumewaajiri, kati hao 146 tumeshawatambua na tutawasajili kuweza kuwajazia na kuwajengea ujuzi na skills za kuweza kuendelea hata baada ya watalamu wa kigeni wale kuondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili katika succession plan; sheria yetu inaendelea kusimamia seccession plan ya local content ili ilete faida zaidi kwa Watanzania hasa katika kununua bidhaa za ndani na pia kupata wafanyakazi wa Kitanzania kwenye miradi hii ya maendeleo na kuweza kujeza kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kuhusiana na Blue Economy, tayari kupitia Wizara yetu ya Uvuvi, wapo vijana ambao wanapata mafunzo na ufugaji wa samaki umeshaanza, ufugaji wa vizimba kule Mkoa wa Mwanza, pia tunafanya kwenye maeneo ya bahari ikiwa ni pamoja na Tanzania Zanzibar, tayari programu hii ipo, imeshaanza kufanya kazi na Mheshimiwa Rais ameendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana hawa kwa kujiandaa na uchumi wa kisasa, ahsante. (Makofi)
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, barabara ya Bonyokwa – Kinyerezi walisema itaanza mwezi wa sita mpaka sasa hivi hajiaanza, je, ni lini itaanza hiyo barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba hiyo barabara tumeitengea bajeti kwenye bajeti ya mwaka huo wa 2023/2024 na kama nilivyosema kwenye barabara zingine ambazo zimepewa fedha kwa mwaka huu taratibu zipo zinaandaliwa ili zianze kujengwa ikiwa ni pamoja na hiyo barabara ya Bonyoka – Kinyerezi. Ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itaanza kujenga Mto Msimbazi ukizingatia sasa hivi wataalam wa hali ya hewa wamesema kwamba kuna mvua kubwa inanyesha; je, ni lini wataanza kutujengea ili wananchi wetu wawe salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ujenzi wa Mto Msimbazi umeanza, na nimwambie tu Mheshimiwa kwa kuwa ujenzi huu...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri umeanza au uko katika maandalizi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hatua tuliyofikia maana yake sasa tunakwenda kuanza.

NAIBU SPIKA: Haya, endelea.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo namwambia Mheshimiwa kwamba uanzaji huu unakwenda kwa hatua. Hatua hizi zinakwenda kadri tutakavyokuwa tunapata fedha. Tutahakikisha kwamba maeneo yote yatajengwa na tutahakikisha kwamba tunapata usalama wa wananchi.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante nilikuwa naomba pamoja na majibu mazuri na mambo yanayoendelea katika hii Wizara kwa hawa wananchi, nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri; ni lini hawa wananchi watapata barua ya kuwaambia kwamba sasa wanakwenda kufanyiwa tathmini upya, ni lini maana yake mlikuwa mkiongea kila siku?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilikuwa nataka nijue ni lini hiyo tathmini itaanza kufanyika, wapate barua rasmi lakini pia wapate tarehe na mwezi ambao wataanza kufanyiwa tathmini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bonnah Kamoli, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini barua tutapeleka kwa wananchi ili wajue, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshakwisha andika barua kwenda Jiji na Jiji wao watachukua wajibu wa kwenda kuwajulisha na kuwahabarisha wananchi kwamba zoezi hili la tathmini linaanza rasmi, na ninaamini na kwa kuwa Jiji tumeshawaandikia tangu mwezi Aprili naamini watakuwa wamelifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, zoezi lenyewe swali lako la pili linaanza lini? Linaanza mwezi Julai na litakamilika mwezi Septemba, 2022. (Makofi)