Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Asha Abdullah Juma (24 total)

MHE. ASHA A JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mwingiliano baina ya wananchi na kambi ni mkubwa, sasa pamoja na hatua za miti na kuta, ni kwa kiasi gani au ni tahadhari gani ya ziada zilizochukuliwa kukabili matokeo ambayo hayatarajiwi ya bahati mbaya kama yale yaliyotokea Gongolamboto na Mbagala? Na nataka nithibitishiwe hapa kwamba wahanga wote wa Gongolamboto na Mbagala kama walishapata fidia?
Swali la pili, ni kwamba Jeshi linapopanua sehemu zake hizo huwa linatoa fidia. Je, katika suala hili limejipanga kiasi gani katika mpango wa kulipa fidia kwa wananchi ambao inawahamisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (Kn.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali kwa swali lake la kwanza ni kwamba mpaka hivi tunavyoongea hapa tayari ndani ya Jeshi kuna mikakati ya kujenga maghala mapya na kwa kiasi kikubwa maghala mapya ya kuhifadhia ilaha yamekwisha kamilika kwenye vikosi mbalimbali, kambi mbalimbali. Japakuwa sitovitaja ni vikosi gani kwa sababu za kiusalama, lakini tayari mabomu na vifaa vyote vya milipuko vya Jeshi vimekwishahamishwa kwenye kambi ambazo zipo karibu zaidi na wananchi na kuwekwa kwenye maghala hayo mapya ili kuondoa uwezekano wa matatizo kama yale yaliyojitokeza pale Mbagala na kule Gongolamboto.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa fidia tayari naamini utakuwa ulishaanza na pengine ulishamalizika sina uhakika sana na hilo, naomba nisiseme lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili, kuhusiana na wananchi kupatiwa fidia kwenye maeneo ambayo Jeshi linaonekana limevamia. Kiukweli ni kinyume chake. Jeshi limekuwepo katika maeneo haya ya makambi kwa kiasi kikubwa lakini wananchi ndiyo wamekuwa wakivamia maeneo ya majeshi. Lakini kwa kuwa Jeshi hili ni la wananchi na ni rafiki kwa wananchi, japokuwa wananchi wanavamia Jeshi mara kadhaa limekuwa hata likilazimika kuhamisha mipaka yake kutoka kule waliko wananchi na kuingiza ndani zaidi kwenye maeneo yake. Pamoja na kwamba wanayahitaji hayo maeneo lakini Jeshi kwa sababu ni la wananchi na ni rafiki kwa wananchi limekuwa likifanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwasihi wananchi wote ambao wapo karibu na maeneo ya Jeshi wasiendelee kuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya majeshi na tayari sasa hivi Serikali imeshaanza kubaini mipaka yote ya kambi za majeshi na kupanda miti kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi na kwenye kambi hizi ndogo ndogo kuweka fence aidha ya wavu ya ukuta. Ninaamini tunapoelekea matatizo kama haya ya mwingiliano baina ya wananchi na Jeshi hayatojitokeza.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu na kwa kuwa mimi ni msema kweli daima napenda niseme sijaridhika na majibu hayo; na kwa kuwa, Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano imejikita zaidi kuwaondolea dhiki wanyonge na wanyonge wa Zanzibar pamoja na Tanzania Bara bado wanapata dhiki katika suala hili, nipende kusema na kumwambia Waziri kwamba ni kwa kiasi gani Serikali itaongeza udhibiti wa mamlaka husika kwa kuhakikisha kwamba bei hizi zinapungua na wananchi wanapata nafuu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa haiingii akilini Mhesimiwa Waziri anaposema kwamba mtu anayetaka kufanya safari afanye booking siku nne au siku ngapi hizo zote anazoziona yeye; kwa kuwa safari nyingine ni za dharura sana. Kwa mfano, watu wanapokuja huku Bara ni kwa ajili ya kupata tiba katika Hospitali ya Rufaa, pengine Muhimbili, pengine Kituo cha Cancer Ocean Road na mambo mengine ya dharura mtu anapoumwa unapomwambia akafanye booking ya siku nne ili apate nafuu ya ndege nafikiri hiyo siyo sahihi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, Mheshimiwa Waziri bado atilie mkazo katika mamlaka hizi pamoja na hivyo vyombo vya pwani, bado nauli hii bado ni kubwa sana kwa wanyonge…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka majibu ya maswali yangu hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kukubaliana na maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Asha Abdullah Juma na ninamhakikishia kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwamba tutafute muda twende wote Zanzibar tukakutane na Zanzibar Maritime Authority, ili tukalijadili hilo kwa undani, hatimaye mamlaka hizo mbili za Muungano, mamlaka iliyoko upande wa Zanzibar na mamlaka iliyoko upande wa Tanzania Bara ziweze kutekeleza majukumu yake kama ambavyo Mheshimiwa Asha Abdullah Juma amependekeza. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mashaka ya vijana wetu yamekuwa yakizidi siku kwa siku, vijana wanajihusisha katika michezo hii ambapo muda mwingi unapotea hata muda wa masomo, muda wa kufanya kazi …

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Maadili yamepotea, kuna masuala ya betting ambayo yanachukua muda mwingi wa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waziri kuniambia kwamba kuna Sheria Namba 4 inayoruhusu mambo hayo lakini udhibiti wake ukoje? Je, mpaka sasa ni wafanyabiashara wangapi wamekamatwa na maduka yao kufungwa ambao hawakuzingatia taratibu za kuzuia vijana wenye umri mdogo kuingia sehemu hizo na je, wamepelekwa kwenye vyombo husika na kuchukuliwa hatua?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza aliuliza udhibiti wake ukoje, kama nilivyosema sheria yetu imeweka wazi na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha iko makini kusimamia michezo hii yote ndani ya nchi yetu ili kuhakikisha sheria hii iliyotungwa na Bunge letu Tukufu inafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, ni watu wangapi na maduka mangapi yamefungwa, naomba nilichukue swali hili tuweze kulifanyia kazi kwa sababu linahitaji data mahsusi ili tuweze kumjulisha Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ila nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa nyendo zimekuwa nyingi, watu wanakwenda sana kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kiuchumi na mengineyo, kwa hiyo ajali za majini, baharini na kwenye maziwa yawezekana zikatokea. Serikali imejipanga hivi ilivyojipanga; Je, Serikali inaonesha vipi shughuli zinazofanywa na SUMATRA na kule Zanzibar, kwa sababu bado ajali zitakuwa zinatokea tunafanyaje?
Swali la pili; Serikali ina mpango gani kwa wale waliopatwa na msiba na kupoteza ndugu zao wakati ilipopata tatizo MV Bukoba, MV Spice Islander iliyozama kule Nungwi na ajali nyingine. Je, watu wote hawa wameshalipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mahusiano ya MRCC na upande wa Zanzibar, naomba nimhakikishie kwamba MRCC ni ya masuala ya Muungano na yanasimamiwa na SUMATRA, kwa hiyo Zanzibar Maritime Authority watashirikiana na taasisi yetu katika kusimamia hii MRCC iweze kuhudumia pande zote za Muungano mara ajali inapotekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili nimuombe tu Mheshimiwa Asha Juma kwamba ajali ya MV Bukoba na ajali nyingine zote zimeshughulikiwa na Serikali kwa kiwango kikubwa sana, maadam sina takwimu hapa nisingeweza kumpa undani wa nini kilifanyika, lakini ni masula ambayo yalishughulikiwa na Idara yetu ya maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ukamilifu kabisa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nashukuru kwa majibu, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa pamoja na mikataba na vipengele vingi vilivyoratibiwa vizuri hali bado kwenye eneo hili siyo nzuri. Bado wananchi wetu wengi wanaendelea kupata matatizo hasa wanawake wanaokwenda kufanya kazi nchi za Urabuni. Serikali kupitia Ubalozi wetu inalazimika kutumia gharama nyingi za kifedha ambazo zingeweza kutumika katika shughuli za maendeleo, kwa mfano, miundombinu, standard gauge na kutununulia ndege nyingine ya Bombadier. Je, Serikali haijaona kwamba sasa wakati umefika wa kuwakatibisha hawa ma-agent, wafanya mikataba ili kuweza kuweka deposit ya fedha ambazo zitatumika kuwashughulikia wananchi wetu hawa inapobidi kurudishwa wanapokuwa wagonjwa wakati wanapokuwa wametelekezwa na waajiri wao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa zipo taarifa na malalamiko kwamba baadhi ya wananchi wetu hawa wanaokwenda kufanya kazi huko huambiwa, kwa mfano, wanakwenda kuuza duka wakafika kule wakafanyishwa kazi nyingine kinyume na hilo duka na kinyume na ridhaa yao na pengine kusababisha hatari kwenye afya zao. Je, Serikali inalisaidiaje jambo hili katika kudhibiti na kuhakikisha kama wananchi wetu hawaendi kuongezewa udhalilishaji huko nchi za Kiarabu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Spika, la kwanza, Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua namna ambavyo Serikali tutaweka mfumo mzuri wa kuweza kuwabana mawakala hawa. Kazi hii ya kuwapeleka Watanzania kufanya kazi nje ya nchi inaratibiwa kwa mujibu wa sheria zetu na mawakala hawa wanasajiliwa katika utaratibu ambao umewekwa. Wakala yeyote ambaye anavunja masharti na matakwa ya sheria hizi tumekuwa tukimchukulia hatua kwa kufuta pia usajili wake ili kumtaka ufuate taratibu za nchi ambazo tumeziweka katika kupeleka wafanyakazi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika eneo hili nitoe rai tu kwa wafanyakazi wote ambao wanafanya kazi nje ya Tanzania hasa katika nchi za Kiarabu hususani Oman kufuata taratibu tulizoziweka kupitia Ofisi ya Wakala wetu wa Huduma za Ajira (TAESA) ambapo tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kabla ya mfanyakazi wa Tanzania hajatoka nje ya nchi tunafanya kwanza mawasiliano kufahamu kazi anayokwenda kufanya lakini na mkataba na malipo yake. Matatizo mengi yanakuja kwa sababu asilimia kubwa ya wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi hawapitii katika utaratibu ambao tumeuweka na ndiyo maana wakipata matatizo huwa inakuwa ngumu sana kuweza kushughulikia kwa sababu hawajapitia katika mfumo wetu na hawapo katika kanzidata yetu ya watumishi ambao wanafanyakazi nje ya nchi. Nitoe rai kwa Watanzania wote wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kufuata taratibu ili wapatapo matatizo iwe rahisi kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumza kuhusu kwenda kufanyishwa kazi kinyume na utaratibu uliowekwa, haya yote yanatokana na iwapo tu wafanyakazi hawa hawatakuwa wamepitia katika ofisi zetu. Sisi tunawabana mawakala ili waje na mikataba ambayo tutaipitia wote kwa pamoja na Ubalozi utabaki na nakala yake ili kuweza kufuatilia. Inapotokea Mtanzania anafanya kazi tofauti na ile ambayo ilisemwa katika mkataba ni rahisi kwenda kuripoti katika Balozi zetu na sisi kuweza kuchukua hatua.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, napenda niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mashaka, matatizo, huzuni na gharama kubwa za matibabu zinaendelea kuwakabili vijana wetu hawa kutokana na hizi ajali za bodaboda. Je, ni lini Serikali itaongeza usimamizi na udhibiti wa kuhakikisha kwamba helmet na reflector zinavaliwa na vilevile kudhibiti upakianaji wa kimishikaki ambao unasababisha watu wengi zaidi kuumia kwa wakati mmoja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu maelekezo tulishatoa na tunachukua hatua kwa maswali yote mawili aliyoyauliza. Moja likiwepo hili la kuvaa kofia ngumu, tumeweka hiyo ni sheria na tumeenda mbali zaidi tunataka si tu mwendesha bodaboda tunataka hata abiria naye atimize wajibu huo wa kuvaa kofia ngumu. Pamoja na hilo, hili lingine la ubebaji wa mishikaki kama alivyoita, abiria zaidi ya moja na lenyewe tumeelekeza popote pale yanapotokea lichukuliwe kuwa ni kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo kwamba jambo hili ni vema likaongelewa kwa ngazi ya kijamii na familia kwamba tuendelee kuwaelekeza vijana wetu. Mara nyingi vijana wetu wakielekezwa kwa mkono wa Serikali wanaona kama wanaonewa lakini wakielekezwa kuanzia ngazi ya familia, tunapokaa tuwaambie vijana wetu tunawapenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe niliwahi kuwapa vijana bodaboda kule Jimboni, niliwahi kuwapa wadogo zangu, watoto wa dada zangu lakini jambo la kwanza nililowaambia, niliwaambia nawapa chombo hiki cha moto lakini chombo hiki kinauwa. Wakiambiwa mkono ambao usio wa kisheria ambao ni wa kifamilia linawakaa zaidi kutambua kwamba ukikosea masharti ya uendeshaji ukaenda kasi, ukakosea sheria za uendeshaji barabarani, gharama yake ni kupoteza maisha ya mwendeshaji mwenyewe na abiria aliyebebwa kutoka kwenye hicho chombo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mashaka na madhila yatokanayo na matumizi ya vipodozi hatarishi yanazidi kuwaathiri wananchi wetu waliokuwa wengi, japokuwa Mheshimiwa Waziri umegusia kama mtatoa elimu, lakini nataka kujua kuna mkakati gani madhubuti kwa elimu hii ya umma ili wananchi hawa wafahamu na wasiweze kutumia vipodozi hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali iwe na mkakati wa kuwawajibisha na kuwalazimisha kulipa gharama za tiba kwa maradhi yanayosababishwa na matumizi ya vipodozi hivi kwa vile kila siku tunaambiwa tusitumie na wao hawasikii. Kwa hiyo, sehemu ile ya tiba walipe wale kwa sababu Serikali ina maradhi mengi sana ya kushughulikia, lakini bado…
inashughulikia maradhi ya makusudi ya kutafuta weupe. Kwa hivyo, Serikali ina kauli juu ya hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Asha Mshua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza mkakati wa kutoa taarifa na elimu katika vyombo vya habari, mihadhara, matangazo ya redio, mafunzo kwa njia ya mada, maonyesho pamoja na huduma kwa wateja.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 tumeweza kutoa elimu kwa wanafuzi 73,323 katika vyuo saba na shule za sekondari 170 katika mikoa yote 21 nchini. Nitaendelea kusisitiza kwamba tunapokea ushauri wako Bi. Mshua na tutajaribu kuzingatia wakati tunafikiria kuongeza adhabu zinazohusiana na uingizaji na matumizi ya vipodozi haramu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Anthony Mavunde, Naibu Waziri anayehusika na masuala haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, kutokana na kwamba bado hakujawa na udhibiti wa kutosha wa kuzuia madawa ya kulevya yasipenye na kutokana na tulivyomsikia Mkuu anayeshughulika na udhibiti wa madawa ya kulevya kwamba kule Zanzibar bado kunatumika kama kipenyo cha kupitisha madawa haya ya kulevya. Je, Serikali imejipangaje kuongeza ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ili kudhibiti na kuhakikisha kwamba kule Zanzibar hakuwi mlango wa kupitisha madawa haya ya kulevya? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli baada ya jitihada na juhudi kuwa kubwa sana Tanzania Bara, hasa kazi kubwa sana ambayo ilifanywa na Mamlaka ambayo imewafanya wafanyabiashara wengi sana wa dawa za kulevya nchini na wengine kukimbilia Zanzibar, ni kweli sasa Zanzibar imeanza kutumika kama sehemu ya uchochoro wa wafanyabiashara ambao wanakimbia kutoka Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayofanyika hivi sasa ni kuhakikisha kwamba tunaanza kufanya kazi kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kwanza kutengeneza mfumo mzuri wa kusaidia katika kuhakikisha kwamba tunawabaini wafanyabiashara hata hao wanaokwenda nje Tanzania Bara ambao wanakwenda Zanzibar. Pia vimekuwepo vikao vya mara kwa mara kati ya Mamlaka na wataalam kutoka kule Zanzibar, lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza mfumo mzuri wa udhibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hiyo inaendelea na tayari tatizo hilo limebainika, naamini muda siyo mrefu sana maridhiano yakikamilika basi tutafanya kazi pia kuhakikisha kwamba tunazuia na upande wa Zanzibar.(Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa bado hali ya upatikanaji maji katika baadhi ya mabweni hasa vyooni haujarekebishwa pamoja na kutengewa hizo shilingi bilioni mbili na kupatikana hizo zilizopatikana. Je, ni lini Serikali itafanya zoezi la dharura kuhakikisha maji yanapatikana hasa hizi sehemu za vyooni wakati ukarabati mkubwa ukiendelea?
Swali la pili, nilitaka kufahamu katika ukarabati huo, je, Serikali ina huo mpango wa kuyabomoa kabisa yale majengo yaliyochoka na kuyaweka mengine yenye sifa na haiba ya Chuo hiki Kikuu cha Mzumbe na lini jambo hili litatekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. la kwanza; katika kufanya marekebisho ya dharura tayari tumeshawaelekeza na hatua zinachukuliwa kuhakikisha kwa kutumia fedha zao za ndani Chuo cha Mzumbe kitaanza mara moja katika ukarabati wa miundombinu hiyo ya maji.
Lakini vilevile katika mpango wa kudumu kuhusiana pia na majengo ambayo yana hali mbaya, kwa mwaka huu wa fedha unaoanza Wizara yetu imejipanga vizuri sana na kwamba tuna fedha taslimu takribani shilingi bilioni 56 hizo tunazo mkononi kwa ajili ya kuboresha vyuo vyetu mbalimbali ikiwemo Mzumbe ambayo itapatiwa mabweni ya kutosha wanafunzi 3,000 pamoja na kumbi za mihadhara na majengo mengine ya utawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vingine ni pamoja na Chuo Kikuu Huria ambacho kitapata jengo hapa Dodoma, Chuo cha Ushirika-Moshi lakini pia mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pale DUCE.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyeki, ahsante kwa majibu mazuri. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa usumbufu umekuwepo kwa watumiaji wa hizi cable hasa hii Cable ya Dodoma, mtu ushaharibikiwa inabidi uende trip mara mbili, mara tatu kuripoti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu aliyonijibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba inabidi uende tena Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano ukatoe ripoti, hizo ni gharama na ni usumbufu. Kwa nini Serikali isiweke kitu kama hotline ikiwa mtu unaposumbuliwa na mambo kama hayo unapiga ukapata ripoti ili kuhakikisha kwamba mtumiaji anapata haki kwa ile pesa yake aliyoitoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, swali langu lingine ni vile unavyokwenda kutaka kujiunga na hizi cable unaahidiwa utapata channel kama 200 au 300. Inapokuja kwenye hali halisi ukijaribu kutafuta channel nyingi unaambiwa access denied, sasa huu kweli si wizi wa kiwaziwazi? Je, Serikali inadhibiti vipi kuhakikisha kwamba mtumiaji anapata haki yake kwa pesa aliyoilipia? Nahisi bado Mamlaka ya Mawasiliano inatakiwa izidishe udhibiti kwenye vyombo hivi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyeki, napenda kumtaarifu tu Mheshimiwa Asha kwamba huwa zipo hotline lakini kwa kweli sasa hivi sipo nazo kichwani. Baada ya muda tukikuta tu hata pale canteen nitakuwa nimeshazipata kutoka kwa watu wa TCRA CCC na kumpatia ili kuweza kuwasiliana na watu ambao wako pale kwa ajili kuhudumia wateja.
Mheshimiwa Mwenyeki, swali lake la pili ni kuhusu channel chache kuliko zinavyopaswa, hiyo inahusika na masuala ya ving’amuzi. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Asha kwamba Serikali kupia TCRA tunaendelea kuwahakiki hawa wanaotoa huduma za TV. Kuna leseni mbalimbali, leseni kama DSTV wale wako wazi kabisa kwamba channel za bure ni mbili au tatu lakini kwa mfano hivi ving’amuzi vingine kama Dodoma Cable, sijapata uhakika Mheshimiwa Asha wana channel za bure ngapi na kwa zipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakapopata uhakika nitakuwa na nafasi nzuri sana ya kukujibu lakini tuna uhakika na kama Serikali tunafahamu kwamba kuna baadhi ya cables ambazo zinatakiwa zitoe channel za bure na zile ambazo hazitoi channel za bure tunazifuatilia kwa karibu ili tuweze kuzifungia kama zinakiuka masharti.
MHE. ASHA ABDALLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, bado vijana wengi wanaomaliza darasa la saba wanakuwa hawajapata nafasi kwenye vyuo vya ufundi au kuendelea na masomo ya sekondari. Ni lini Serikali itaboresha elimu ya msingi kuhusisha mafunzo ya ufundi ndani yake ili kuwaasaidia wale wanaobaki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mtaala wa VETA ni mmoja nchi nzima wakati mahitaji yanatofautiana sehemu na sehemu. Kwa mfano, mikoa yenye gesi wangefundishwa mambo yanayotokana na gesi, mikoa ya uvuvi wangefundishwa taaluma za uvuvi na mikoa ya madini vivyo hivyo. Sasa Serikali ina utaratibu gani kuhusu kuingiza component hiyo katika mitaala yake?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu suala la wanafunzi ambao wanamaliza darasa la saba lakini hawapati nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inafanya kazi kubwa ya kuongeza nafasi za udahili kwenye vyuo vya ufundi kwa kujenga vyuo vipya vya ufundi pamoja na kuboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme kwamba katika mtaala wa elimu ya msingi kuna somo la stadi za kazi ambalo limewekwa mahsusi kwa ajili ya kuwapatia vijana wetu angalau ujuzi ili hata yule anayemaliza elimu yake ya msingi awe tayari ana uwezo wa kufanya jambo katika mazingira yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu mtaala wa VETA kwamba unafanana, kimsingi masuala ya ufundi yanatakiwa yaangalie mazingira halisi ya mahali ufundi unapofanyika. Kwa hiyo, suala la kuangalia masuala ya gesi au masuala ya uvuvi ndiyo jambo ambalo limekuwa likifanyika. Kwa hiyo, niendelee kutoa wito kwa wote wanaotoa mafunzo ya ufundi stadi wahakikishe kwamba mitaala yao inazingatia mazingira halisi ya pale ambapo wanatoa mafunzo ili kuwawezesha wananchi wa eneo husika kuongeza tija katika shughuli wanazozifanya.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, na mimi nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja kumbe, haya. (Kicheko)..... Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ziko sababu kadhaa ambazo nyingine hazizuiliki zinazosababisha watoto hawa kuzaliwa mapema, je, Serikali ina utaratibu gani wa kuziimarisha na kuziboresha hizi special care intensive nurseries zilizopo na zipo ngapi katika mikoa yetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi huduma kwa mtoto yeyote ambaye anatarajiwa kuzaliwa inaanza katika mahudhurio ya kliniki. Ninaendelea kusisitiza na kutoa rai kwamba wanawake wajawazito na baada ya kubaini wameshapata ujauzito ni muhimu sana kwenda kliniki mara nne, kwa sababu katika mahudhurio haya ya kliniki ndipo hapo ambapo tunaweza tukabaini changamoto kama hizo na uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa njiti. Sambamba na hilo nimesema kwamba tumetoa elimu kwa watoa huduma wetu wote katika ngazi zote kuhusiana na jinsi gani wanaweza wakawahudumia watoto njiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali sasa hivi katika bajeti ambayo mmetupitishia katika moja ya kipaumbele ambacho tumesema tutaweza kuweka katika hospitali za rufaa za mikoa ni pamoja na huduma za Neonatal ICU. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kupata majibu hayo ya kina ambayo yameelezea vizuri sana juu ya miradi muhimu kama hiyo REA, Standard Gauge na bomba la mafuta lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni kwa nini Serikali isije na utaratibu wa kuwachukua vijana hawa moja kwa moja kutoka kwenye vyuo ili kuwapunguzia mihangaiko ya kuzunguka na barua za maombi na kushinda mitandaoni kama ilivyokuwa kwenye sekta nyingine, mfano, afya na elimu ambapo watu hupata ajira kwa wepesi zaidi kutokana na taaluma zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Wizara hii na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ina mikakati gani kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo Incubation Centres za uhakika za kutosha, mitaji, vitendea kazi kwa wahitimu hawa ili waweze kupata wepesi wa kujiajiri na vilevile kwenda na Sera yetu ya Tanzania ya Viwanda, Inawezekana? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza la kuwachukua vijana hawa wahitimu wa vyuo vya ufundi moja kwa moja, tunachokifanya kama Serikali kwanza kabisa kwa kushirikiana na sekta binafsi ambazo pindi nafasi zinapopatikana huwa tunawaunganisha moja kwa moja na vyuo vyetu vya ufundi ili vijana hawa waweze kupata nafasi za ajira za moja kwa moja. Pia baadhi ya vyuo, kwa mfano, Chuo cha Don Bosco kimekuwa kina utaratibu wa kila mwaka kuandaa Kongamano la Waajiri ambapo wamekuwa wakiunganisha wahitimu hawa moja kwa moja na waajiri na vijana wengi wameajiriwa kwa kupitia mfumo huo. Kwa hiyo, naamini kabisa wazo la Mheshimiwa Mbunge ni jema, nasi kama Serikali tutaona namna ya kuweza kuviunganisha vyuo vyetu vya ufundi pamoja na waajiri ili vijana hawa wapate nafasi za ajira za moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, suala la incubation kwa ajili ya kuwandaa vijana hawa, kuwalea na kuwapatia mitaji, sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tunavyo Vituo vya Vijana. Kipo Kituo cha Vijana Sasanda-Mbozi, Ilonga pale Kilosa na Kilimanjaro. Vituo hivi viko kwa ajili ya kuwalea vijana na kuwandaa kuwa na sifa za kuajiriwa. Pia vijana hawa wanawezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana ambao umekuwa ukitoa mikopo kwa vikundi vya vijana lakini vilevile na asilimia 5 za mapato ya ndani ya Halmashauri yamekuwa yakisaidia katika kuwakomboa vijana kwa kuwapatia mitaji.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu hayo yaliyotolewa na Serikali na kwa kuwa bado stesheni zetu nyingi hasa ikiwemo hii ya Makao Makuu bado hazina sura ya kuvutia na kwa kuwa huduma za vyoo na maji ni muhimu sana kwa afya, majibu ya Serikali yameeleza kwamba itategemea upatikanaji na vyanzo vya ndani, ambavyo vinaweza vipatikane au visipatikane au vitengwe au visitengwe. Je, ni kwa nini Serikali isitenge ikahaulisha kwenye mafungu mengine kufanyia matengenezo huduma hizi muhimu kwa afya ya wananchi wengi hasa wenye uwezo mdogo ambao wanatumia reli hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa watoaji wa huduma wengi kwenye reli hii ni wajasiriamali wadogo akinababa lishe, akinamama lishe na vijana. Kwa nini Serikali isiwafanyie utaratibu wa kujenga sheds au miavuli iliyopangika kwa utaratibu unaolekeweka wakafanya shughuli zao kuliko kutawanya masufuria, majungu, majiko, kuni along the railway lane? Na kwa nini Serikali…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hali ya Shirika la Reli Tanzania halijaimarika sana; lakini tukumbuke tu kwamba Shirika la Reli nalo linafanya biashara na linao wajibu na jukumu la kuhudumia wateja wake. Pale watakapoona kwamba wameshindwa tutataarifiana ndani ya Wizara halafu tutajua namna ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli kwamba wajasiriamali wapo wengi kwenye station zetu mbalimbali hapa nchini na wamekuwa wakifanya shughuli pamoja na Shirika letu la Reli. Ni jukumu sasa la Shirika la Reli wakae na hao wajasiriamali waweze kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na napongeza juhudi kubwa za Serikali kwa kujenga Kituo kipya huko Chukwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Chukwani ni nyuma kidogo, Mazizini ni barabarani na ni centre na karibu na Shehia nyingi kama vile Shakani, Kombeni, Maungani na kadhalika. Sasa kile Kituo cha Wilaya kwa nini hiki cha Mazizini mnataka kukiua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, kwa nini msifanye taratibu kama hivyo mnavyoshirikiana na wadau kufanya kampeni ya kuboresha vyoo na vyumba vya mahabusu kwa nchi zima mkianzia na hapo Mazizini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hatutarajii kukiua Kituo cha Mazizini, kitu ambacho tunafanya ni kuhamisha kuwa Kituo cha Wilaya, kuhamishia Chukwani. Kwa hiyo Kituo cha Mazizini kitaendelea kutumika tu, tutafanya jitahada ya kukikarabati na kwa kuwa kiko barabarani kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tunaamini kwamba kinahitajika kuendelea kutoa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu ukarabati wa vituo vyetu kwa ujumla wake ikiwemo mahabusu, ni jambo ambalo tunakwenda nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake kuhusu kuwatumia wadau ndiyo tumekuwa tukiufanya kazi, wako wadau ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa dhamira ya kurekebisha mazingira ya Vituo vyetu vya Polisi ikiwemo mahabusu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaandaa jedwali la kuonyesha miradi mikubwa ya barabara zinazounganisha miji mikuu ya mikoa ili kuonyesha hali ilivyo na hivyo kuweza kuwaanika wakandarasi wanaochelewesha kazi hiyo kwa makusudi na kuwapa wananchi dhiki mfano barabara ya Nyakanazi – Kabingo - Kidahwe - Kasulu ambazo kwa muda mrefu hazikamiliki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi mingi sana ya ujenzi wa barabara inatekelezwa kote nchini. Nawaona Waheshimiwa wa Kigoma wanatabasamu kwa sababu wanafahamu fika kwamba miradi hii ambayo ilikuwa inatekelezwa katika Mkoa wa Kigoma ukianzia Nyakanazi – Kibondo - Kidahwe – Kasulu inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie wananchi wa Kigoma kwa ujumla kwamba ipo miradi mingi sana ambayo kwa hapa siwezi kuitaja inaendelea vizuri. Mheshimiwa Nsanzugwanko na Mheshimiwa Zitto wanafahamu kwamba sasa appetite ya matengenezo ya barabara kwenye Mkoa wa Kigoma ipo juu sana na barabara karibu zote zina fedha kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Asha asiwe na wasiwasi. Hata eneo hili lililokuwa linasuasua kutoka Nyakanazi - Kakonko tumeendelea kulisimamia. Mimi mwenyewe nimekwenda mara kadhaa na tumezungumza na mkandarasi na zile changamoto zilizokuwa zinamkabili kama Serikali tumezitatua. Tunaendelea kusukuma na nitahakikisha barabara hii inakamilika ili wananchi wa Kigoma nao wapate faraja ya kuwa na miundombinu kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya mkoa wao.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu niliyopatiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la watoto wetu wanaoendelea kupata mimba bado limeshika kasi. Ni juzi tu tumepata habari kwamba kuna mwalimu amewafanya wake zake watoto wa primary karibu 10. Wako wanaopata mimba kwa kubakwa, wako wanaopata mimba kwa kushawishiwa na wako wanaopata mimba kwa bahati mbaya yoyote ambayo inatokezea lakini huwa siyo dhamira, dhamira hasa ni watu hawa wapate haki ya kielimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni zito sana…

MWENYEKITI: Swali sasa.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Sheria Na. 5 imetoa adhabu ya miaka 30 kwa yule mharibifu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abdullah, nipe maswali.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, nataka niiulize Serikali ni lini hasa itakaa chini itizame upya kadhia hii inayowakuta watoto wa wanyonge, wafanyakazi na wakulima, wasichana ambao wanakosa haki yao kielimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, lini Serikali itatafuta mbinu mbadala ya kuwasaidia watoto hawa ambao wanakosa haki yao ya kimsingi? Hili jambo linauma sana, lazima Serikali itazame upya.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu kwenye swali la msingi, Serikali inachukua hatua kadhaa kuhakikisha inadhibiti tatizo hili. Kubwa ambalo limezungumziwa ni mabadiliko ya sheria ambapo imekuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari. Tunachoomba na Waheshimiwa Wabunge ni mabalozi wazuri katika hili, Serikali ina dhamira ya kuhakikisha kwamba wale wote wanaokutwa na makosa haya wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sharia na kama tulivyosema tumeweka kifungo cha miaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kinachotokea ni kwamba ushirikiano kutoka kwa wazazi wa wanafunzi ambao wameathirika unakuwa siyo mkubwa. Pindi tutakapopata ushirikiano na ushahidi ukiwepo, Serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba wale wahusika wote wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili tunachukua hatua zipi kuhakikisha kwamba wale wanafunzi wanaoathirika wanaendelea na safari ya masomo? Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwanafunzi kupata mimba haimaanishi kwamba ndiyo mwisho wa safari yake ya masomo. Serikali imeweka taratibu kadha wa kadha ili kuhakikisha wanafunzi wale bado wanapata fursa nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa hiyo ipo katika maeneo matatu makubwa; moja Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ina utaratibu wa kutoa elimu nje ya mfumo rasmi. Napenda kutoa taarifa kwamba kwa mwaka jana kuna wanafunzi 10,000 ambao wamehitimu kidato cha nne kupitia utaratibu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na 6,000 ni wasichana. Tunaamini kwamba baadhi yao ni wanafunzi wale ambao walikatisha masomo kwa sababu ya mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na UNICEF tunaendesha Mradi wa Elimu Changamani kwa wanafunzi ambao wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu ya kupata ujauzito. Pia, Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya ufundi, kwa hiyo, wanafunzi ambao hawajaweza kwenda sekondari au ambao wameshindwa kuendelea kwa sababu ya kupata ujauzito kuna fursa vilevile ya kupata elimu ya ufundi na tumeendelea kuimarisha na elimu hiyo sasa hivi ni bora.

Kwa hiyo, tunachosema kimsingi, hata kama mwanafunzi amepata ujauzito sio mwisho wa safari yake ya masomo kuna fursa nyingine na kuna wengi ambao wamenufaika. Nina hakika hata baadhi ya Wabunge kwenye Bunge hili wamenufaika na mipango hii ya Serikali.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa hali ya maumbile ya mwanadamu, hasa mwanamke yanapelekea kujifungua au kupata watoto: Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti utungwaji mimba ndani ya Magereza ili kupunguza shida ambazo watoto hao watapata katika kulelewa katika mazingira ambayo siyo rafiki kama Magereza; kwa kuwa bado inasemekana kwamba kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume na wanapata access ya kukutana? Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie atadhibiti vipi utungwaji mimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza wakati najibu swali la msingi kuhusiana na uwezekano wa mwanamke kupata mimba ndani ya Magereza. Nimezungumza hivyo kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Magereza yametenganishwa, hakuna mchanganyiko kati ya Magereza upande wa wanawake na wanaume; hata Askari ambao wanahudumia wafungwa na mahabusu wa kike basi wanakuwa ni Askari wa kike. Kwa hiyo, mara nyingi tunapozungumzia upataji mimba wa Magereza inakuwa ni kwa wafungwa ama mahabusu ambao wameingia tayari Magerezani ikiwa mimba zimeshaanza kutungwa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi napongeza sana Serikali kwa hatua zake za kusambaza na kusimamia mawasiliano pamoja na kujenga minara sehemu zote. Pamoja na hayo nataka niulize Serikali ina mikakati gani na ya haraka kwa kiasi gani katika kudhibiti au kuimarisha kikosi kazi cha kupambana na hawa wahuni kila siku wanaosumbua wananchi katika kuwaibia pesa zao kupitia mtandaoni kwa kuwaambia tuma hela hii kwa namba hi, tuma hela hii kwa namba hii, Serikali inafanya nini kuwadhibiti wahuni hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ipo mikakati mingi ya kupambana na hali hii ambayo inajitokeza kwa sababu ya ukuwaji wa teknolojia pia changamoto nazo zinakuwa zipo nyingi, tunao mkakati kwanza wa kuelimisha wananchi ili kuwaokoa na hii hali ambayo inajitokeza lakini pia mara kwa mara mnaona tunaendelea kuboresha Sheria na Kanuni hata hili zoezi la uandikishaji wananchi kwa kupitia alama za vidole kufanya usajili wa simu ni hatua hizo madhubuti za kuhakikisha tutaendelea kumbambana nah ii changamoto ambayo ipo. Kwa hiyo, ni kuahakikishie tu kwamba kila wakati changamoto inapojitokeza kama sisi Serikali tunachukuwa hatua hii kuwafanya wananchi wetu kuwa salama.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nashukuru sana kwa majibu mazuri, ya kina na yenye maelezo ya kutosha na kwa kiasi kikubwa suala langu limepata ufafanuzi kwa swali la aliyeuliza kabla yangu lakini nitakuwa na maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti baadhi ya utawala wa shule ambao huwa unawazuia watoto wenye uwezo mdogo au uwezo wastani kufanya mitihani yao ya mwisho na kuwalazimisha waende wakajiandikishe kama private candidates kwenye vituo vingine wakati wakijua kufanya hivyo ni kuwapunguzia moral na kuwavuruga kiasi kwamba wanawazidishia kutofanya vizuri lakini pia ni kuwabagua watoto hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kushirikiana na wazazi na walezi kuona kwamba Kamati za Ahule zinasaidia kupunguza kadhia hii kwa watoto hao wenye uwezo pungufu katika masomo yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdulla Juma kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watazania kwa ujumla kwamba ni kosa kumbagua mtoto yeyote kwa sababu yoyote. Wote ni watoto wa Kitanzania na tena Serikali inatoa msisitizo zaidi kwa wale ambao wana changamoto mbalimbali za ujifunzaji. Kwa hiyo, ikibainika kwamba kuna mwalimu au kiongozi yeyote wa elimu ambaye anawabagua watoto wenye changamoto ya uzito katika kujifunza kwa kweli ni kosa na atachukuliwa hatua za kisheria. Naomba nimtake Mhshimiwa Mbunge kama ana ushahidi kuhusu hili alete kwetu na sisi hatutasita kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu nafasi ya Kamati na Bodi za shule katika kutatua changamoto hii, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba lengo zima la kuanzisha Kamati za shule katika Shule za Msingi na Bodi katika Shule za Sekondari ni pamoja na kuangalia changamoto kama hizi ili kuhakikisha kwamba sheria, taratibu na miongozo ya Serikali inatiliwa mkazo katika usimamizi wa elimu. Kwa hiyo, tuendelee kuwaunga mkono kwa sababu ndiyo kazi yao hasa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nashukuru kwa majibu hayo yaliyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wananchi wengi waliofanya mambo ya muhimu na ya kuandika historia. Mfano Meja Jenerali Mrisho Sarakikya aliyepandisha bendera ya siku ya Tanganyika ilivyopata uhuru. Hivi Serikali haioni umuhimu wa kuandaa sera ya kushughulikia viongozi kama hawa ikasaidia kuamsha ari ya uzalendo kwa nchi yetu ya Tanzania kuliko kusema kwamba tutawaonea huruma, tutawatazama wako hawa na hawa? Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri, naomba nijibu swali la nyongeza lililoulizwa nikijumuisha pamoja na majibu yaliyotolewa kwa swali lililopita kwamba nchi hii inayo watu wengi sana waliofanya mambo makubwa katika historia ya nchi yetu na Serikali imekuwa ikitambua michango yao kwa namna mbalimbali. Hawa wanne tunaowazungumzia waliochanganya udongo wa Tanzania Zanzibar na Tanganyika na kufanya alama ya Muungano ni moja tu ya wazee wengi ambao wengine hata kuwatambua bado hatujawatambua. Wako wazee waliopigana vita ya Kagera, wako watu waliofanya shughuli mbalimbvali zilizofanya Tanzania hii ya leo tunayoiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili ni lazima tujipe tahadhari kuhusu ukubwa wake lakini pia hatuwezi tukaliacha hivi hivi ni lazima tutafakari kwamba je, tunapotaka kuchukua tuchukue kada ya namna gani au watu wa namna gani. Naomba tu niseme kwa niaba ya Serikali kwamba kwanza tunatambua na kuheshimu na kuenzi michango ya wazee waliofanya mambo makubwa hapa nchini lakini tunahitaji muda wa kutafakari sana mwisho wake yaani limitation na scope yake iwe wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. ASHA ABDULLA JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyosheheni vigezo.

Mheshimiwa Spika, askari wa Jeshi letu la Polisi wanafanyakazi nzuri sana ikiwepo usalama barabarani, usalama wa raia na mali zao na kutuelimisha kutii sheria bila shuruti.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wako baadhi ya askari ambao hawakupandishwa cheo mpaka wamefikia kustaafu, na kwa kuwa kutokupandishwa huko si kosa lao, ni kosa la mfumo; je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia ili wasiwe wamepoteza haki zao na hasa kwa vile sasa hivi wako wastaafu wanahitaji sana fedha hizo?

Mheshimiwa Spika, swali langu lingine; Je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mfumo na utaratibu uliowazi kabisa unaoonyesha namna gani na vigezo gani vya kuweka nafasi ya kwenda course ili uweze kupandishwa cheo na utaratibu huo uwe wazi na haki kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asha Abdalla Juma, Mbunge wa Viti Maalum kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mfumo ambao tunao sasa hivi wa upandishwaji askari vyeo uko vizuri; na nimeeleza katika jibu la msingi vigezo ambavyo vinatumika. Hata hivyo kulingana na wingi wa askari tuliokuwanao na uchache na ufinyu wa nafasi hizo inasabbaisha wakati mwingine askari wengine kutumia muda mrefu zaidi katika kupata vyeo.

Hata hivyo tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba wale askari ambao wanatimiza vigezo wanapata fursa ya kupandishwa vyeo; kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Asha Abdalla Juma kuhusiana na hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na hoja yake, kama nitakuwa nimemuelewa vizuri, ya kuwafidia, nadhani hilo halipo katika utaratibu. Kimsingi tu ni kwamba tutaendelea kuhakikisha tu kwamba askari ambao wenye sifa wanapandishwa vyeo. Katika kipindi cha mwaka huu mmoja, hivi karibuni tulipandisha vyeo askari kwa upande wa Jeshi la Polisi pekee kwa haraka haraka nadhani ni zaidi ya askari 9000 ukiachilia mbali majeshi mengine yaliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Utaona kwamba tunafanya jitihada kama Serikali kuona askari hawa ambao wanafanyakazi vizuri wanapata fursa ya kupandishwa vyeo kadri ya hali na uwezo wa Serikali unavyoruhusu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kupongeza Serikali kwa jitihada kubwa za maboresho kwenye magereza na pia tumeona juhudi za Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pale alipo tembelea Gereza na Butimba na maelekezo aliyotoa na hatua zinazochukuliwa na Serikali nzima katika kupunguza kadhia ya magereza. Kama tunavyofahamu kwamba gerezani siyo kuzuri. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka takwimu, data ya wakosaji makosa na adhabu wanazozipata wakiwa magerezani na kuziweka wazi takwimu hizi ili kuona kwamba udhibiti upo na kwamba haya makosa yanaendelea yamedhibitiwa au yanapungua?

Swali la pili, Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kufikiria kuweka wigo wa kutoa adhabu za kutumikia ndani ya jamii kwa wale ambao wanamakosa ambayo si ya kuleta dhara kwenye jamii zaidi, kuliko kuwarundika kwenye magereza kwa kuwa kufanya hivyo itaweza kupunguza mzigo mkubwa wa mkusanyiko magerezani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ya kwanza ilikuwa ni ushauri ambao tunaupokea kuhusiana na takwimu kuziweka wazi. Lakini swali la pili ambalo aliuliza kimsingi jambo hilo tunalo tuna utaratibu ambao unaitwa kwa lugha ya kiingereza extramurally labor ambao utaratibu huu kwa kawaida unatumika kutoa adhabu kwa maana ya adhabu za vifungo vya nje kwa baadhi ya watuhumiwa kulingana na masharti na vigezo vilivyowekwa. Kwa hiyo, utaratibu huo tunao na tunaendelea nao. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi hii, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa majibu yako mazuri lakini nitakuwa na suala moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muingiliano umekuwa mkubwa na watu wamekuwa wengi, kwanini hiki kituo kisitafutiwe sehemu nyingine, kikajengwa huko, kikawa na nafasi kubwa kikaelekea kama kituo kweli cha polisi kuliko pale kilivyokaa, hakijapendeza wala haifai. Huku kituo, huku soko, nafikiri Serikali ifikirie kukihamisha kikapate nafasi kubwa zaidi na majengo ya kisasa yaliyokuwa bora zaidi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kuhamisha kituo hiki kwa sababu ya ufinyu wa nafasi kiusahihi ni kwamba eneo la kituo lile ni kubwa mno, labda Mheshimiwa Mbunge tukipata nafasi tukatembelee ili nimuoneshe. Ni juzi tu hapa kuna eneo ambalo liliwahi hata kupewa mwekezaji na kutokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kwamba maeneo ya vyombo vya usalama yabakie kwa matumizi ya vyombo hivi tulitoa maelekezo na kuhakikisha kwamba tumemhamisha yule mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, lakini utakumbuka pia hata eneo ambalo liko pembeni ya kituo cha polisi ambacho kimetumika kama soko kama alivyozungumza kwenye swali la msingi ni eneo pia la polisi ukiachia mbali eneo la nyuma ambalo ni kubwa. Kwa hiyo, kimsingi kuhamisha kituo hiki kwa sababu ya ufinyu wa eneo nadhani haitakuwa sahihi kwa sababu kuna eneo la kutosha. Cha msingi ni kuendelea kutoa wito kwa wananchi kutumia nafasi yao yoyote ya kuvamia maeneo ya polisi kuacha maeneo ya polisi yaendelee kutumika kwa ajili ya shughuli za kiusalama.