Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Asha Abdullah Juma (26 total)

MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. ASHA ABDULLAH JUMA) aliuliza:-
Majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo yamechakaa sana:-
(a)Je, Serikali ina mpango gani wa kuyafanyia ukarabati au kuyajenga upya?
(b)Je, Serikali haioni kama Mahakama ya Mnazi Mmoja - Dar es Salaam imeelemewa na kesi nyingi hivyo iangalie namna ya kupunguza kesi?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama wa miaka mitano 2015 - 2020 na hivi sasa inaufanyia marekebisho ili kukidhi mahitaji sahihi ya wakati husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015/2016, Serikali lilitoa fedha ya kiasi cha shilingi bilioni 12.3 za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 100% ya fedha zilizopangwa. Fedha hizo zitatumika katika ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Wilaya 12 ambazo ni Mahakama za Bariadi, Kilindi, Kasulu, Kondoa, Bukombe, Makete, Sikonge, Nkasi, Bunda, Chato, Nyasa na Namtumbo. Aidha, fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa Mahakama mpya za mwanzo 10 za Longido (Manyara), Terati (Simanjiro-Manyara), Machame (Hai), Makongolosi (Chunya-Mbeya), Unyankulu (Urambo-Tabora), Sangabuye (Ilemela-Mwanza), Mtowisa (Sumbawanga), Njombe Mjini, Gairo (Morogoro) na Mangaka (Mtwara).
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, itakamilisha ukarabati wa Mahakama Kuu Shinyanga, Mtwara, Tanga na Mbeya. Maandalizi ya utangazaji wa zabuni za ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na Mahakama Kuu Mara yanaendelea.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ina mpango wa kujenga Mahakama mpya ya Kinyerezi na Ilala. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa kukamilika kwa miradi hii kutawezesha kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Mnazi Mmoja.
MHE. ASHA A. JUMA aliuliza:-
Kumekuwa na muingiliano wa wananchi kuishi karibu, ndani au pembezoni mwa maeneo ya Kambi za Jeshi kama ilivyo kwenye Kambi ya Chukwani.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha maeneo hayo na makazi ya wananchi kwa kuweka mipaka madhubuti?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia suala hili mapema ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea baina ya Jeshi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (Kn.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Jeshi, yale ya makambi, ya mafunzo au vikosi yana mwingiliano mkubwa na wananchi au taasisi zingine. Mwingiliano huu husababishwa na wananchi wenyewe kutoelewa mipaka vizuri, lakini walio wengi huingia kwa kujua na wakati mwingine husaidiwa na wataalam wa Ardhi wa Manispaa na Halmshauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili linashughulikiwa kupitia marekebisho ya sheria ili kuimaliza migororo hiyo.
(a) Serikali inaona umuhimu mkubwa kuyatenganisha maeneo hayo yasiwe na mwingiliano na wananchi au taasisi zingiene. Hatua zinazochukuliwa ni kujenga kuta au uzio wa waya kwenye maeneo madogo lakini kuna mpango wa kupanda miti kwenye maeneo makubwa sambamba na kuweka mabango makubwa ya tahadhari.
(b) Serikali kupitia Jeshi, tayari imeanza mikakati ya kupanda miti kwenye maeneo ya kambi. Hivi sasa upo mkakati kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 wa kuanzisha vitalu vya miti kwenye baadhi ya kambi kwa ajili hiyo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Gharama za usafiri wa vyombo vya baharini na angani kwa safari za Zanzibar na Dar es Salaam ni za juu sana licha ya bei ya mafuta kupungua.
Je, Serikali inachukua hatua gani kusaidia wananchi hao kudhibiti nauli hizi za meli na ndege kwa kushirikiana na mamlaka husika toka pande zote mbili za Muungano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuunguza nauli Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ina jukumu la kujenga ushindani katika sekta ndogo ya usafiri wa ndege na hi ni kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Sheria ya Usafiri wa Anga (Civil Aviation Act [Revised Edition 2006]). Panapokuwa na ushindani katika njia moja nauli hutokana na soko. Aidha, mamlaka huingilia kati kisheria kuweka kiwango kikomo pale tu inapotokea kuna ukiritimba na wananchi wanaumia.
Mheshimiwa Spika, mamlaka imejitahidi kuhusu ushindani kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ambapo zaidi ya makampuni kumi ya ndege yanatoa huduma katika njia hiyo kwa nauli kati ya shilingi 140,000 na shilingi 278,000 kwenda na kurudi pamoja na kodi endapo msafiri atanunua tiketi mapema zaidi kabla ya safari. Kwa mfano, tarehe 4 Aprili, 2016 nauli ya juu kwa kampuni kumi za ndege zilizokuwa zinatoa huduma katika njia hiyo ilikuwa shilingi 139,000 na ya chini ilikuwa shilingi 75,000 ambapo wastani wa nauli kwa makampuni yote kumi kwenda tu pamoja na kodi ilikuwa shilingi 88,700.
Mheshimiwa Spika, utaona kuwa wastani wa bei ya nauli ya kwenda Zanzibar pamoja na kodi ni wa chini na unaendana na gharama halisi za uendeshaji na faida kidogo kwa mtoa huduma ukilinganisha na sehemu ambazo hakuna ushindani kabisa au hakuna ushindani mkubwa kama ilivyo Songwe na Mwanza. Hivyo, nashauri kwa mtu anayehitaji kusafiri afanye mipango ya safari yake mapema ili kupata unafuu wa nauli, maana kadri anavyonunua tiketi yake mapema kabla ya safari, ndivyo nauli inavyokuwa chini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vyombo vya usafiri wa bahari kwa safari za Zanzibar na Dar es Salaam, kwa sasa kuna jumla ya vyombo sita vya majini vinavyotoa huduma hiyo. Vyombo hivyo vyote vimesajiliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Bahari Zanzibar (Zanzibar Maritime Authority). Hivyo, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekwishafanya mawasiliano na ZMA ili viwango hivyo vya nauli za vyombo vya majini baina ya Dar es Salaam na Zanzibar vitathiminiwe kwa kuzingatia taratibu za mamlaka ya usajili wa vyombo hivyo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Kuna ongezeko kubwa la maduka ya kucheza kamari yanayotaitwa Jack Pot katika miji nchini ikiwemo Dodoma; maduka hayo huchezesha kamari mchana na usiku na wateja wengi ni vijana ambao hutumia mbinu mbalimbali kupata fedha ndani ya familia ili wakacheze kamari hali ambayo husababisha uvunjifu wa maadili:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mchezo wa kamari ambao huwakosesha amani wazazi na jamii nzima?
(b) Je, Serikali haoni kuwa kuna uvunjifu wa maadili na nguvu kazi ya vijana inapotea kwa kucheza kamari badala ya kushiriki katika uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo yote ya kubahatisha ikiwemo kamari inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Namba 4 ya mwaka 2003, Sura 41 pamoja na kanuni zake. Kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha biashara ya michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka zingine za biashara. Pia, sheria inakataza watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote atakayeruhusu mtoto chini ya miaka 18 kushiriki, kuingia au kukaa karibu na eneo la mchezo wa kubahatisha anahesabika kufanya kosa na anastahili kulipa faini ya sh. 500,000 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au vyote kwa pamoja. Aidha, endapo kosa hili litafanywa na mwendesha mchezo wa kubahatisha, Bodi ina mamlaka kisheria ya kumfutia leseni. Hivyo basi, wajibu wa Serikali ni kuzuia watoto na vijana walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha. Hata hivyo, natoa rai kwa wazazi na walezi kuwazuia vijana wao kucheza michezo ya kubahatisha pale wanapoona kuwa uchezaji wao unakuwa na matokeo hasi.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ya kubahatisha ni moja ya shughuli za kiuchumi inayoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama shughuli nyingine zozote. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, wote wanaoendesha michezo ya kubahatisha wanazingatia sheria na kanuni zilizowekwa. Pili, ni wajibu wetu kama wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa vijana wetu wanazingatia mila na desturi zinazolinda maadili ya Kitanzania pindi wanapokuwa wanajishughulisha na shughuli halali za kiuchumi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA Aliuliza:-
Majanga ni mambo yasiyotarajiwa ila huwa yanatokea tu, majanga kama ajali za baharini, ziwani, barabarani, matetemeko, vimbunga, majanga ya njaa na kadhalika yamekuwa yakitokea:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha na kuimarisha nyenzo na ujuzi kwa Kikosi cha Uokoaji wa Majini kinachojulikana kama Coast Guard kwa ajili ya uokoaji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina utaratibu wa namna ya kushughulikia masuala ya utafutaji na uokoaji majini. Kituo maalum kijulikanacho kama Dar es Salaam Maritime Rescue Coordination Center (MRCC) kimeanzishwa na kimekuwa kikitoa huduma kwa saa 24 kila siku. Kituo hiki kinasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). Aidha, kwa kuzingatia ukubwa wa shughuli za usafiri, uvuvi na nyinginezo katika maziwa, kituo kidogo cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji (MRCC) kimeanzishwa Jijini Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha utaratibu wa utafutaji na uokoaji, Wizara yangu imeandaa rasimu ya sheria ya utafutaji na uokoaji (search and rescue) inayozingatia miongozo ya Kimataifa ya Utafutaji na Uokoaji (International Air and Maritime Search and Rescue Guidelines) na wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu rasimu hiyo na sasa kazi ya kurekebisha rasimu ya sheria hiyo ili kuzingatia maoni ya wataalam mbalimbali inaendelea ili kuruhusu hatua zaidi za kupitisha sheria hiyo kuendelea.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Watanzania wengi hasa wanawake wanaokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za kiarabu kama Oman na nyinginezo wamekuwa wakifanyiwa ukatili mkubwa sana unaosababisha wengine kufariki na wengine kujeruhiwa vikali.
(a) Je, Serikali ina utaratibu gani madhubuti wa kudhibiti safari za Watanzania hao wanaokwenda katika nchi za Kiarabu na pia kuwabana Mawakala na kuwawajibisha inapobidi?
(b)Je, ni wanawake wangapi wa Kitanzania wameuawa katika Nchi za Kiarabu na fidia kutolewa katika familia zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na Wizara inayoshugulikia masuala ya kazi Zanzibar na Balozi zetu zilizoko nchi mbalimbali huko Mashariki ya Kati.
Serikali imeweka miongozo itakayosaidia siyo tu kuwabana mawakala bali pia kuwasaidia Watanzania kutumia fursa za ajira zilizopo nje ya nchi ili kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana kwa kuelekeza kila mfanyakazi kuwa na wakala rasmi na kupata mkataba kutoka Ubalozini.
Mheshimiwa Spika, Ubalozi unakuwa na taarifa katika kila hatua ambayo Watanzania wanapitia wakati wa maandalizi ya kwenda kufanya kazi hivyo kulinda maslahi yao. Aidha, mwajiri anayetaka kuajiri wafanyakazi kutoka Tanzania atatakiwa kusoma na kuelewa mwongozo na baada ya kukubaliana nao anatakiwa kujaza fomu ya kuomba kumwajiri Mtanzania na kuwasilisha Ubalozini kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Maombi hayo yatafuatiwa na mkataba wa kazi.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu una vupengele vikuu vitano ambavyo mwajiri na mawakala wanapaswa kukidhi mahitaji yake ili Serikali itoe idhini kwa Mtanzania aliye tayari kufanya kazi aendelee na taratibu za ajira katika nchi hizo. Vipengele hivyo ni kama ifuatavyo:-
(i) Taarifa za mwajiri.
(ii) Taarifa za mwajiriwa.
(iii) Mshahra wa mwajiriwa.
(iv) Masharti ya mkataba.
(v) Maelezo ya mawakala wa Tanzania na Oman.
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Watanzania zaidi ya 12,000 ambao Balozi unawatambua wanafanya kazi katika kada mbalimbali nchini Oman. Kati ya hao, wanawake watatu wamepoteza maisha kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, ajali na kadhalika. Katika vifo vilivyowahi kuripotiwa ambapo Serikali ilifuatilia hadi kujua vyanzo halisi vya vifo hivyo, hakuna taarifa kuhusu vifo vilivyosababishwa na mauaji ya makusudi.
Aidha, mara zote tunapopata taarifa za vifo katika nchi hizo, Serikali huchukua jukumu la kufuatilia kwa kushirikiana na mamlaka za nchi husika kujua hatma za familia zilizopoteza mwenzi wao ikiwa ni pamoja na malipo ya fidia kutoka kwa mwajiri wa marehemu.
Mheshimiwa Spika, wakati wote Serikali imekuwa makini katika hatua za awali za maandalizi ya safari hizo kwa kuwabana mawakala na kuhakikisha kuwa mikataba inakuwa ni mizuri ili kuwezesha kuziba mianya yote ya kukwepa majukumu kwa pande zote inayoweza kusababisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi katika nchi hizo kupoteza haki zao.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Baadhi ya majengo na mabweni katika campus ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro yana uchakavu mkubwa sana ikiwemo miundombinu ya maji vyooni.
Je, kuna utaratibu gani wa kuyafanyia ukarabati majengo haya na hasa kuwapunguzia shida wasichana wanaohitaji matumizi zaidi ya maji kuliko wengine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu swali namba 22 tarehe 1 Februari, 2017 Serikali imeshaanza ukarabati wa Miundombinu na majengo katika campus kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa gharama ya shilingi bilioni mbili. Hadi kufikia terehe 31 Mei, 2017 jumla ya shilingi milioni 884,634,366 zilizotengwa zilikwishatolewa na Wizara yangu inaendelea kufuatilia fedha zilizobaki ili zitolewe kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa juhudi hizi za ukarabati unaoendelea kutekelezwa chuoni hapo ni dhahiri kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuinua hadhi ya chuo hiki na hivyo kuweka mazingira stahiki ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuwapunguzia shida wasichana wanaohitaji matumizi zaidi ya maji.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Kumekuwa na kero kubwa kwa wananchi wanaotumia huduma za Cable TV hasa Dodoma Cables; wananchi wanalipia lakini hawapati huduma ipasavyo:-
Je, ni lini Serikali itawadhibiti na kwa namna gani baadhi ya Service Providers kama hawa ambao wamekuwa wakiwadhulumu wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa leseni ya kutoa huduma za Cable kwa kituo cha Dodoma Cables ambapo kinatakiwa kiendeshwe kwa kufuata sheria na kanuni zinazohusu masuala ya utangazaji. Ili kukidhi ubora wa huduma za cable, TCRA imekuwa ikifuatilia maudhui na inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo hivi kuangalia kama mitambo inakidhi vigezo vya utoaji wa huduma bora na ya uhakika kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyeki, kwa kuwa suala la Cable TV linahusu kuwepo kwa mtandao wa waya kutoka kwa mtoa huduma (cable operator) kwenda kwa wananchi, kuna wakati kumekuwa na changamoto za kukatika kwa nyaya ambapo wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa mtoa huduma ili apate msaada wa kiufundi pindi anapokuwa hapati huduma za matangazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, TCRA imeweka mfumo wa kupokea malalamiko ambapo kama mwananchi atakuwa hapati huduma bora na stahiki anatakiwa kutoa taarifa kwa mtoa huduma na pindi asipopatiwa huduma kama alivyoahidiwa na mtoa huduma, mwananchi anatakiwa kupeleka malalamiko yake katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambayo kawaida huyapokea na kuyafanyia kazi ili kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki kwa malipo waliyotoa kwa mtoa huduma.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Wapo wahitimu wengi sana kutoka Vyuo mbalimbali vya Ufundi nchini ambapo hadi sasa hawajapata ajira wala hawajaweza kujiajiri, ikiwa pia tuko kwenye wakati wa kuanzisha uchumi wa viwanda ambapo taaluma za wahitimu hao zinahitajika sana:-
Je, ni lini Serikali itafanya juhudi za dhati za kushughulikia suala hili kwa lengo la kuongeza tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha tatizo hili linapungua kwa kiasi kikubwa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo kama ifuatavyo:-
(a) Kuhakikisha kuwa vijana wahitimu wa Vyuo vya Ufundi wanapata fursa za ajira katika miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya Standard Gauge, ujenzi wa bomba la mafuta, mradi wa usambazaji wa umeme vijijini, mradi wa kufufua umeme na mingine. Mathalan, katika ujenzi wa bomba la mafuta, uchambuzi umeonyesha kutakuwa na fursa za ajira zaidi ya 11,000 za aina mbalimbali. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) inaratibu upatikanaji wa Watanzania wenye sifa za kuajirika katika miradi hiyo.
(b) Kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, Serikali imeainisha aina ya ujuzi unaohitajika katika ujenzi wa miradi husika na imetenga fedha za kugharamia kuziba ombwe la ujuzi lililopo kati ya wahitimu na mahitaji ya soko la ajira kuwezesha Watanzania wakiwemo wahitimu wa Vyuo vya Ufundi kupata sifa na kuajirika.
(c) Kuendelea kuhamasisha na kuwawezesha vijana kujiajiri kwa kuanzisha makampuni na vikundi vya uchumi vilivyosajiliwa kisheria ili kutumia taaluma zao kuzalisha na kujipatia vipato halali. Kwa mfano, Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) umetoa fursa za ajira kwa vijana wengi wenye ufundi. Aidha, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Taasisi nyingine za Serikali, Serikali imeendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana ili kuwajengea mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kuwa tunapoelekea katika uchumi wa viwanda taaluma za wahitimu wa vyuo vya ufundi zitaendelea kuhitajika sana kwa ajili ya uendeshaji endelevu wa viwanda vitakavyoanzishwa. Serikali imeona jambo hilo na kwa kushirikiana na vyuo vya ufundi imeanza kutoa mafunzo kwa kuzingatia mahitaji.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Stesheni Kuu, vituo vidogo vidogo na maeneo yanayozunguka Stesheni za reli ya kati vimechakaa sana:-
Je, Serikali haioni haja ya kukarabati majengo ya Stesheni za reli ya kati na kuweka miundombinu ya maji safi na maji taka katika majengo hayo na maeneo yanayozunguka stesheni hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASHTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lina jumla ya stesheni 124 katika mtandao wake wa reli hapa nchini. Aidha, shirika lilishaanza ukarabati wa stesheni za treni ambao pamoja na mambo mengine umezingatia uboreshaji wa mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na sehemu za kukaa abiria wakati wa mvua kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, stesheni zilizokwisha kukarabatiwa ni pamoja na Kigoma, Kaliua, Pugu, Malindi na Mwanza ambapo ukarabati bado unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, shirika linatambua changamoto ya ukosefu wa baadhi ya huduma katika stesheni zilizobakia za reli kutokana na kuwa na miundombinu chakavu na hivyo kuweka mpango mkakati wa kukarabati na kuboresha stesheni hizo hatua kwa hatua kadri hali ya kifedha itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Kuna harufu mbaya inayotoka kwenye chumba cha Mahabusu katika Kituo cha Polisi Mazizini Zanzibar na kuwa kero kwa Askari na wananchi wanaofika kupata huduma kituoni hapo.

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati kituo hicho ili kuondoa harufu hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bi. Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa hali ya jengo la Kituo cha Polisi Mazizini hairidhishi. Kwa kutambua hilo, Serikali ikishirikiana na wadau wa usalama inaendelea na ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha kisasa katika eneo la Chukwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hili jipya lipo katika hatua za mwisho za umaliziaji na mara ujenzi utakapokuwa umekamilika shughuli za kiusalama za Jeshi la Polisi za Kituo Kikuu cha Wilaya ya Magharibi ‘B’ katika Mkoa wa Mjini Magharibi zitahamishiwa kutoka Kituo cha Mazizini na kwenda Chukwani.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na ongezeko la wasichana wanaokatishwa shule kwa sababu ya mimba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijua:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la wasichana wanaokatishwa shule kwa sababu za mimba, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 78. Katika marekebisho hayo ya mwaka 2016, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari atahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kudhibiti ongezeko la mimba kwa wanafunzi, kama vile ujenzi wa mabweni, hosteli na shule katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu. Aidha, huduma za ushauri na unasihi hutolewa kwa wanafunzi ambapo mwongozo wa ushauri na unasihi umeandaliwa. Vilevile mafunzo mbalimbali juu ya stadi za maisha, elimu na afya na uzazi hutolewa kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti mimba kwa wanafunzi, ili kuhakikisha kuwa, wanafunzi wote wanakamilisha mzunguko wa elimu bila kikwazo.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA (K.n.y. MHE. ASHA ABDULLAH JUMA) aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kuwasadia wananchi walioweka amana zao katika Benki ya FBME.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge Vitib Maalumu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39(2) na (3), amana au akiba za wateja katika benki au taasisi ya fedha, zina kinga ya bima ya amana ya kiasi kisichozidi shilingi za kitanzania 1,500,000 tu. Endapo mteja hana salio la amana la kiasi kilichozidi shilingi 1,500,000 atapata fidia ya asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, wateja walio na amana zaidi ya shilingi 1,500,000, wanalipwa shilingi 1,500,000 kama fidia ya bima ya amana, na kiasi kinachobakia kinalipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufirisi. Aidha malipo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufirisi yanategemea makusanyo ya fedha kutoka kwenye mauzo ya mali pamoja na fedha zilizowekezwa na benki katika taasisi mbalimbali za fedha za ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, zoezi la kukusanya mali na fedha zilizokuwa zimewekezwa na za benki ya FBME katika taasisi mbalimbali za fedha, hususan nje ya nchi, limekumbwa na changamoto za kisheria kati ya Tanzania na nchi ya Cyprus ambako benki ya FBME ilikuwa na tawi lililokuwa linaendesha sehemu kubwa ya biashara zake, na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa ukusanyaji na ugawaji wa fedha za ufilisi. Hivyo basi tarehe ya kuanza kulipa fedha zinazotokana na ufilisi haijulikani kwa sasa kutokana na uwepo wa kesi zinazokwamisha zoezi la ukusanyaji mali na madeni ya benki ya FBME. Serikali kupitia Bodi ya Bima ya Amana, Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipo katika mazungumzo na Serikali ya Cyprus ili kulipatia suala hili ufumbuzi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Wapo watoto wengi wenye uwezo (ubongo) mzito kufahamu kusoma au kuandika na hatimaye kubaki shule kwa muda mrefu:-

Je, Serikali ina mkakati gani juu ya kundi hili kubwa la watoto katika kuwaendeleza kielimu ili waweze kujitegemea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Eilimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Asha Abdulla Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa watoto wenye uelewa tofauti wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na watoto wenye uwezo mzito wa kusoma na kuandika. Uwezo huu mzito wa kusoma na kuandika husababishwa na sababu mbalimbali zikiwemo, mazingira yasiyo rafiki nyumbani na shuleni, migogoro ya kifamilia hasa ya wazazi na walezi, kuugua kwa muda mrefu, hofu na kutojiamini. Kwa sababu ya uelewa wao mzito, watoto hao huchukua muda mwingi katika kujifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua changamoto hii, Serikali imeendelea kutekeleza Mitaala ya Mafunzo ya Ualimu inayomwezesha mwalimu kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wanafunzi katika ujifunzaji. Kwa mfano, kuwabaini watoto wenye uwezo mzito katika kujifunza, kupata mbinu mbalimbali za kufundishia na kujifunzia ambazo husaidia watoto hao kujifunza. Vilevile, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu ili kuimarisha mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kuzingatia mahitaji halisi katika darasa. Kwa mfano, mafunzo endelevu ya ujenzi wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa Darasa la Kwanza hadi la Nne pamoja na Usimamizi wa Elimu ya Awali kwa walimu waliopo kazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imeandaa Mitaala na Vitabu kwa ajili ya Elimumsingi ili kuboresha maudhui na njia za ufundishaji zinazomwezesha mwanafunzi kushiriki kikamilifu katika tendo la ujifunzaji. Naomba kutoa rai kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa walimu ili kuweka nguvu ya pamoja katika kusaidia wanafunzi wenye uwezo mzito katika kujifunza kusoma na kuandika.
MHE. ASHA ABDULLA JUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mfumo gani wa kupandishwa daraja askari wenye vyeo vya chini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdulla Juma, Mbunge wa Viti Maalumkama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vina mfumo wa Upandishwaji wa madaraja kwa askari wa vyeo vya chini ambayo huzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo umbele kwa maana ya seniority, miaka mitatu ya cheo alichonacho, tabia njema, nidhamu, utendaji mzuri, umahiri wa kazi, elimu au utaalamu mahsusi, uwezo wa kumudu madaraka ya cheo anachopandishwa, kutokuwa na tuhuma zinazochunguzwa wala mashtaka ya Kijeshi katika kipindi cha miaka mitatu na bajeti tengefu kwa mwaka husika.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaendeleza kimasomo watoto wa kike waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwaendeleza wanafunzi wanaoacha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo wasichana waliopata ujauzito. Mikakati hiyo ni pamoja na Mpango wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi. Katika mpango huu wanafunzi wanaruhusiwa kufanya mitihani ya Kidato IV na cha VI. Kwa sasa kuna Vituo 753 vya Elimu nje ya mfumo rasmi vilivyosambaa katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo, Serikali imeendelea kutoa fursa za wanafunzi kujiendeleza wakiwemo wale waliopata ujauzito. Fursa hizo ni pamoja na:- Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA), mpango wa elimu kwa vijana uitwao Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (Integrated Program for Out of School Adolescents - IPOSA). Serikali pia inatoa fursa za kujiendeleza kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) ambapo maeneo Manne ambayo ni; Taaluma (Academic skills), Stadi za Ufundi wa awali (pre-vocational skills), Ujasiriamali na Stadi za maisha (Generic Skills) kusisitizwa katika ujifunzaji. Ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa mafunzo ambao utahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapangiwa moja kwa moja maeneo ya kwenda kujifunza badala ya utaratibu wa sasa wa mwanafunzi kutafuta mwenyewe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mitaala ya vyuo vikuu huwataka wanafunzi kukamilisha masomo kwa kufanya mafunzo kwa vitendo katika taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi. Utaratibu uliopo ni kwamba vyuo vikuu vinaainisha maeneo wanayokusudia kupeleka wanafunzi na kuomba nafasi za kufanyia mazoezi kwa vitendo. Baada ya maeneo ya kufanya mazoezi kwa vitendo kupatikana, vyuo huwapatia wanafunzi barua za kuwatambulisha kwenye taasisi husika ili waweze kupokelewa.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi wana uhuru pia wa kutafuta maeneo ya kufanyia mafunzo kwa vitendo na kukijulisha chuo kwa taarifa rasmi. Baada ya wanafunzi kupata nafasi katika Taasisi husika vyuo huwapa barua za utambulisho ili waweze kupokelewa na kuendelea kufanya mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa vyuo vikuu nchini kudumisha mahusiano na taasisi mbalimbali vikiwemo viwanda na kuwa na mikataba ya makubaliano ya kupeleka na kupokea wanafunzi kwenye mafunzo kwa vitendo. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, ni hatua gani zitachukuliwa kwa walipa kodi walioshindwa kulipa na kuwa na malimbikizo makubwa lakini wapo tayari kulipa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Usimamizi wa Mapato, Sura 438 Kifungu cha 70 na Kanuni zake kinampa mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kusamehe adhabu na riba kama kuna suala na sababu maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais, Serikali kupitia TRA inaendelea kujadiliana na wafanyabiashara wenye malimbikizo ya kodi ili kuwapa unafuu wa kulipa malimbikizo ya kodi kwa awamu bila kuathiri ukwasi, mwenendo na uendeshaji wa biashara. Ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kushughulikia huduma za afya kwa uchunguzi tiba na kujikinga katika Shule za Msingi na Sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya afya kinga na tiba shuleni ni afua muhimu inayotekelezwa na Serikali kuwajengea watoto uelewa wa kujikinga na magonjwa. Huduma hii inahusisha utoaji wa elimu ya afya, utambuzi wa magonjwa katika hatua ya awali pamoja na uratibu wa kupata matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri imeendelea kuratibu utolewaji wa elimu na huduma za afya kwa watoto walioko shuleni, hususani kwenye magonjwa ya malaria, minyoo, kichocho, saratani ya mlango ya kizazi, afya ya kinywa, meno pamoja na macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya iligawa vyandarua 3,104,401 kwenye shule za msingi 7,639 kwa uwiano wa chandarua kimoja kwa kila mtoto. Pia, chanjo ya kuzuia maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi ilitolewa kwa wasichana 623,501 dozi ya kwanza na 472,460 dozi ya pili. Aidha, kila mwaka hufanyika kampeni ya utoaji dawa za minyoo na matone ya vitamini ‘A shuleni, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kudhibiti magari yanayopakua na kupakia mizigo katika maeneo ya Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi na Barabara ya Morogoro ili kupunguza kero kwa wakazi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti magari makubwa yanayopakia na kupakua mizigo katika maeneo ya Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi na barabara ya Morogoro, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka utaratibu wa kudhibiti magari hayo kwa kutoa vibali Maalum vinavyowaruhusu kuingia mjini kama ilivyotamkwa kwenye kifungu cha 8 cha Sheria Ndogo za Matumizi ya Barabara za Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (ambayo ndiyo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa sasa) za mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, mtu yeyote atakayeingiza lori au kontena bila kibali atakuwa ametenda kosa, na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua Shilingi elfu hamsini hadi laki tatu kulingana na uzito wa gari, au kifungo kisichozidi miezi 12 jela, au vyote kwa pamoja. Hata hivyo, halmashauri kwa kushirikiana na vyombo vingine, ina utaratibu wa kutoa elimu kwa madereva, wamiliki wa magari makubwa na kwa umma ili kuwapa uelewa wa athari zinazotokana na uingizaji wa magari makubwa kiholela.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ina mpango wa kujenga maegesho ya kisasa katika eneo la Mnazi Mmoja kwa ajili ya magari mbalimbali yakiwemo magari ya mizigo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha mapitio ya kubaini madawa na vihatirishi vinavyosababisha madhara na vinaendelea kutumika katika Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania hutekeleza utaratibu wa kubaini viuatilifu na vihatarishi vinavyosababisha madhara kwa mazao, mimea na afya ya binadamu na wanyama. Utaratibu huo hufanyika kulingana na kifungu cha 54 cha Sheria Na. 4 ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020 kinachompa Mamlaka Msajili wa viuatilifu nchini kufuta usajili wa viuatilifu vinavyosababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 hadi 2021, Serikali ilifanya mapitio ya kubaini viuatilifu vyenye madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira vijulikanavyo kama Highly Hazardous Pesticides. Mapitio hayo yalibaini aina ya viuatilifu 44 vyenye viambata amalifu vyenye madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hatua hiyo, Serikali kupitia TPHPA imeanza kuchukua hatua za kusitisha matumizi ya viuatilifu 44 vilivyobainika na inaendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maghala na maduka ya viuatilifu ili kubaini uwepo wa viuatilifu vingine vyenye madhara.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha kimaendeleo vijana wa skauti nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa vijana wengine wote wa Tanzania wakiwemo vijana wa Skauti ambao wapo kati ya miaka 15 hadi 35, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania, imeendelea kutekeleza programu mbalimbali kama vile Klabu za Skauti katika shule za msingi na sekondari ambapo vijana hupatiwa mafunzo ya ujasiri, kutatua matatizo katika jamii, kujitolea na uzalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, vijana wa skauti ni miongoni mwa vijana ambao hunufaika na programu mbalimbali zinazosimamiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na fursa za mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha miradi ya uzalishaji mali inayowawezesha kujiajiri pamoja na mafunzo ya fani mbalimbali kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya mapitio ya bei ya nauli za Shirika la Ndege Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kawaida nauli za safari za ndege hupangwa na soko kulingana na aina ya huduma inayotolewa. ATCL kama ilivyo kwa mashirika mengine ya ndege yanayotoa huduma zake kibiashara, nauli zake zinapangwa na soko kwa kuzingatia matakwa ya sheria za ushindani ambapo vigezo vinavyotumika katika kupanga nauli hizo ni pamoja na gharama za uendeshaji ili kuhakikisha kuwa mashirika ya ndege yanahimili ushindani wa soko na kujiendesha kwa tija na ufanisi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, Serikali inawasaidiaje Wanafunzi wenye mahitaji maalum katika huduma za vyoo kwenye shule za msingi na sekondari nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiboresha ramani za ujenzi kwa shule za msingi na sekondari ili kukidhi mahitaji ya makundi maalum ya wanafunzi. Kwa sasa Serikali imeelekeza kwamba kila panapojengwa matundu ya vyoo lazima kuhakikisha kwamba mahitaji ya watu wenye mahitaji maalumu nayo yanaangaliwa.

Mheshimiwa Spika, Maelekezo yalishatolewa kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwemo Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuwa ujenzi wa shule mpya, ujenzi wa matundu ya vyoo uzingatie ramani ilyotolewa tarehe 20 Februari, 2023, ambayo ndani yake mahitaji ya watu maalum yameangaliwa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na ajali za majini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeanza kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Uratibu wa Shughuli za Utafutaji na Uokoaji Majini (Regional Maritime Rescue Coordination Center – MRCC) kupitia mradi unaoendelea katika Ziwa Victoria na vituo vidogo vinne vya uratibu wa shughuli za utafutaji na uokoaji majini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za ndani pamoja na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambapo katika mwaka 2023/2024 umetengewa Shilingi bilioni 1.74. Aidha, kupitia mradi huo zitanunuliwa boti tatu kwa ajili ya shughuli ya utafutaji na uokoaji ambazo kwa sasa zipo katika hatua za manunuzi, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga daraja katika eneo la Jangwani barabara ya Morogoro Jijini Dar es Salaam ili kuondoa usumbufu na adha wanazopata wananchi hasa wakati wa mvua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa daraja jipya la Jangwani chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ili kutatua tatizo la mafuriko imekamilika na Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia ili kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Ahsante.