Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asha Abdullah Juma (22 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii leo ya kuweza na mimi kuchangia.
Awali ya yote, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataala, aliyenijalia uwezo na satwa ya leo kuwa mimi Asha Abdullah Juma kuwa Mbunge na kuweza kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi ya kwanza kabisa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuweza kuwa Rais na kuongoza kwa speed hii ambayo anakwenda nayo, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana.
Vilevile nachukua nafasi ya kipekee kupongeza hatua iliyochukuliwa na chama chetu ya kuweza kumpendekeza Mheshimiwa Samia Sukuhu Hassan akawa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Napongeza pia uteuzi wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, anao uwezo wa hali ya juu sana na anakubalika na tuna matumaini atafanya kazi nzuri sana. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote mliopata nafasi hii, nawapongeza pia wale waliopata nafasi ya Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa nampongeza Mheshimi Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar na kwa kushinda uchaguzi. Mheshimiwa Ally Saleh nakuona hapo, nakuambia kwamba Mheshimiwa Dkt. Shein ndiyo Rais wa Zanzibar na amechagua cabinet nzuri naamini itamsaidia kufanya kazi nzuri. (Makofi)
Kwa kupitia Bunge hili, nilaani kitendo alichofanyiwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein cha kuzomewa lakini lile halikumrudisha nyuma yeye ameendelea kuwa Rais wa Zanzibar kwa kura nyingi na sisi tunamuunga mkono kwa sababu ndiye tegemeo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kitu kimoja, hii tabia ya kususasusa si nzuri, tabia ambayo inaoneshwa hapa kwa sababu inavunja demokrasia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Anajijua mwenyewe aliyesusa. Inavunja demokrasia, watu wamewachagua mje hapa muwawakilishe, muisemee Serikali au muikosoe, mnakuja hapa kisingizio hiki, kile, mara kutoka nje, mara uzomee, mara unune, mara ugome, sasa ndiyo umechaguliwa kwa ajili hiyo? Ilimradi hakuna lililo zuri kwa upande wenu. Usichukue mshahara wa kutwa bila kufanya kazi ya kutwa.
Baniani mbaya ila kiatu chake dawa. Mshahara, posho yote mazuri mbona hamyakatai?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asha…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya dibaji hiyo, sasa niende kwenye hoja.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asha naomba ukae.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu mia juu ya mia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba pia unilindie muda wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia kwanza kwa kupongeza safu nzima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba niseme kwamba kwenye Ofisi yako ukianzia na Mheshimiwa Jenista Mhagama, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi na Mheshimiwa Anthony Mavunde, hawa ni vifaa, tumewapima kupitia Kamati yetu ya Katiba, wanafanya kazi nzuri sana. Naamini watatusaidia sana kwa maendeleo husika katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze rasmi na naanza na eneo la Tume ya Uchaguzi. Naanza kwa kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Uchaguzi kuanzia Mwenyekiti wake Jaji Lubuva…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Kailima na Jecha pia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume hii ya Uchaguzi imethibitisha demokrasia, kama tulivyoona vyama 22 vimeshiriki na vimeshinda vingine na sasa hivi tupo hapa kuwawakilisha wenzetu. Hivyo, ukipata wapiga kura waliofikia 15,596,110 sawasawa na 67.3% ni hatua nzuri. Tuiombe Serikali iiongezee Tume ya Uchaguzi nguvu ili kudhibiti wizi wizi na vitendo vya kuivurugia kazi Tume hii ambayo inafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nataka kuligusia ni hili linalohusu vijana ambalo kwenye hotuba hii limezungumzwa vizuri la kuwapatia mafunzo. Tunajua vijana wanatuzidi kwa namba, ni wengi, kwa hiyo inahitajika mikakati na imara zaidi ya kuwahusisha ili wasitutoke wakawa kundi la wanaofanya vurugu na fujo. Kwa hiyo, mipango hii iliyopangwa nafikiri ingekuwa vizuri pia ikaelezwa waziwazi kila Wilaya watapata mafunzo kiasi gani na mafunzo gani ili kujua hawa watu wanashughulikiwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nalotaka kuligusia ni hili la bandari. Tumeridhishwa na mpango ulioelezwa hapa lakini tuongeze kuoneshwa kwamba kunaongezwa vifaa vya kisasa zaidi ili kuharakisha upakizi na upakuaji na pia kudhibiti bila kutumia nguvu zaidi na pesa nyingi huu uvujaji na wizi katika bandari zetu. Pia nadhani kama ingekuwa vizuri kwenye eneo hili la bandari kukaimarishwa masuala ya uokoaji inapotekea disaster katika maeneo ya bandarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jicho pia liongezwe katika kuimarisha bandari ya Mtwara na Tanga. Naona kama hii mipango iliyopangwa haijatosha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali hii ione umuhimu huo na hasa kwa vile kule Mtwara tuna mategemeo ya kupata shughuli nyingi za kupokea na kusafirisha mizigo. Kwa hiyo, ni vyema jitihada ikaongezwa kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la muhimu kabisa ambalo linatakiwa lipewe nguvu ya ziada ni elimu. Pongezi pia kwa Serikali kwa kuweza kuboresha elimu ya awali. Naomba tuendelee kuunga mkono juhudi hizi, kama tulivyofanya kwa kutenga pesa tukaziweka kwenye madawati hivyo na kila anavyofikiria mtu kuna namna nyingine ya kufanya ili kuweza kuiboresha elimu hii basi na tufanye.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja hii leo. Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuweza kutoa mchango wangu kwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Naanza kwa kuunga mkono hoja, napongeza juhudi na kazi nzuri inayofanywa na Profesa Joyce Ndalichako na timu yake akiwemo Engineer Stella Manyanya, pamoja na timu nzima ya Wizara na wakati huo huo nampa pole Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kuondokewa na mama yake mzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wizara hii ya Elimu ina umuhimu wake kipekee, hapo hapo naunganisha na kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kupitisha lile azimio la kupatia elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka sekondari. Jambo hili lina maana sana, kwa sababu linatoa nafasi na fursa kwa wanyonge wengi kupata elimu kwa watoto wao. Wote tunajua umuhimu wa elimu, kwa hiyo zinahitajika juhudi zetu za pamoja kuunga mkono Wizara hii, ili vijana wetu wote wapate elimu stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa elimu mpaka sekondari, ni bure kwa hivyo ningependekeza kwamba kidato cha tano na cha sita, vilevile tufanye jitihada, ili iweze kuwa bure vilevile. Kwa kuwa pale kuna watoto wa wanyonge wengi, ambao wameweza kupita kuanzia kutoka kwenye shule za kata mpaka wakafika pale.
Kwa hiyo, Serikali ifanye vile inavyoweza katika kuongeza ukusanyaji wake wa kodi au mbinu nyingine inakojua itapata pesa ili vijana hawa wasije wakakwazwa. Kwa kuwa vijana wa chuo kikuu wanapata mkopo, na hawa nao wapate, kwa kuwa form five na sixndio chimbuko la wataalam wetu, naamini juhudi za ukusanyaji wa kodi zitatuwezesha kufika hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara pia iangalie na ipitie ihakikishe kwamba angalau Wilaya zote zina shule za A-level za kutosha, kwa mfano Wilaya kubwa kama Rufiji ina shule moja tu yaA-level pale Mkongo na hii Wilaya ni kubwa kuliko Mkoa mzima wa Kilimanjaro, kwa hivyo Wizara ifanye ranking kuhakikisha kwamba Wilaya zote zina shule hizi la A-level.
kusimamia kujenga shule za sekondari za kata katika Kata zote, na maabara na madarasa. Hili jambo limefanikiwa kwa juhudi za wananchi na Serikali
pamoja.
Dhana ya elimu bure inapata mtikisiko kidogo, hii dhana imelenga kuondolea wazazi wanyonge, kuweza kuwasaidia vijana wao wapate elimu, maeneo mengi maabara zimesimama kujengwa, madarasa yamepungua kasi ya kujengwa, maeneo mengi wazazi wamepunguza kasi ya kujitolea kushiriki kwa kisingizio kwamba elimu ni ya bure, naomba sana tusiieleleze Serikali, tuendelee na spirit ile ile ya kuunga mkono jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kusisitiza wananchi waendelee kuelimishwa umuhimu wa kutimiza wajibu wao, tunakiri kwamba katika jambo hili la elimu bure ziko changamoto, na hilo ni jambo la kawaida kwa sababu jambo lolote la maendeleo huwa linavikwazo vikwazo, lakini tutashinda na tutafika tunakokwendea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumza zaidi kuhusu masuala ya shule hizi za kata, naomba kwa ruhusa yako nizungumzie kidogo kuhusiana na sheria. Naomba nitanabaishe kuhusiana na Sheria za Shule za Kata, Sheria ya Elimu Namba 25 kama ilivyorekebishwa mwaka 1978, kwa Sheria Namba 10 ya mwaka 1995, imeweka utaratibu wa Kikanuni wa kuanzishwa shule za sekondari na msingi, kwa utaratibu wa sasa, tuna shule za kata ina maana sheria hii haizungumzii shule za kata, kwa hivyo kunahitajika marekebisho ya sheria, kujumiuisha shule ya kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sheria na kanuni inayounda bodi za shule, inatoa maelekezo ya uteuzi wa wajumbe wa bodi katika mkoa; kwa kuwa sasa tuna shule za kata, tunahitaji malekebisho ya Kanuni ili tuweze kutoa wajumbe hao wa bodi kutoka kwenye kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilijitahidi sana kuanzisha Sekondari karibu 3,500 za kata kama sikosei, sasa niiulize Serikali hii inashindwaje kujenga vituo vya VETAkwa kila Wilaya ili hawa vijana wetu ambao ni wengi wakapate elimu ya amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia ina vitu ambavyo tunategemea vijana wetu wafanye. Lakini tulifuta somo la elimu na elimu ya kujitegemea, kwa mfano kila Ijumaa iliku wakati wa mchana watu wanakwenda kufanya mambo ya bustani, kama ilivyokuwa setup ya Mwalimu Nyerere wakati ule. Sasa vijana hawa wanapomaliza, wanaishia kwenda kucheza pool kwa sababu ile elimu ya bustani haipo, kwa mfano siku hizi kuna elimu ya bustani katika sehemu ndogo inaitwa permaculture ingeweza ikaanzishwa kwenye shule mbalimbali kule, watu wakajipatia mboga, viazi na vitu vidogo vidogo. Kwa hiyo lazima tuchanganue zaidi kutafuta, utaalamu na teknolojia sasa wa kuweza kuzalisha katika sehemu ndogo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliziwa muda wangu, basi niombe Wizara ya hii ilekebishe curriculum,ili tuweze kupata masomo ya kilimo na biashara, michezo, ufundi, katika ngazi zote na masomo haya yatiliwe mkazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala kubwa sana la kupata mimba wasichana, hili ni suala linaleta matatizo, linaleta unyonge, kwa sababu Wizara ifikirie na izingatie kwa kina kwa uharaka ikiwezekana kuwarudisha watoto hawa kwenye madarasa. Hatusemi hivyo kama tunawatia washawasha ili wakapate mimba laa! Ilamimba nyingine zinakuja ni kwa accident, nyingine ni kwa kubwakwa, kwa hivyo tufikirie, unapomuadhibu kijana huyu asiendelee kusoma, umemuadhibu na mtoto atakayezaliwa, umeiathiri familia yake nzima, umeongeza umaskini, hujauondoa umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini uadhibu mtoto ambaye hana makosa, na yule ambaye mhusika mwingine mara nyingi anakwenda wanaposema wazungu anakwenda scot free, kwa sababu huwezi kumpata na hivyo anapata nafasi ya kwenda kufanya uharibifu, kuwawekea mimba watoto wengine.
Sasa tuone Wizara, sisi Wizara ya Elimu kule Zanzibar kwa mfano wameliona hili na wasichana wanaopata mimba kwa bahati mbaya, wanaendelea na masomo yao na imeonekana kwamba wengine hawa wanatokea kuwa wataalam wakubwa, wakatoa na mfano mzuri katika jamii, na mchango mzuri katika jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara yangu wakati nilipokuwa nahudumu kama Waziri, nilifika Bahamas. Nikatembelea darasa zima nikakuta watoto wote ambao wana miaka 16 hivi nakuendelea wote darasa zima wana mimba matumbo kiasi hiki. Lakini wameandaliwa darasa lao na wanafundishwa, kwa sababu huwezi kum-penalized huyu mtu, ile mimba inatokana na hali ya maumbile, saa nyingine huna nguvu za kumshinda mwanaume. Mimi baba yangu alisema usiende ukaa faragha na mwanaume itakuwa taabu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Kwa dhati kabisa nakupongeza kwa umahiri na uhodari wako kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili na hivyo ndivyo tunavyotegemea, hutishwi wala hubabaishwi. Mimi ikiwezekana nataka ukae asubuhi na jioni uoneshe kama wewe uko fit kweli kweli. Maana hapa tuko katika sehemu ya kutunga sheria na kuondolea wananchi dhiki zao waliotutuma halafu tunakuja kufanya michezo ya kuigiza hapa kuingia na kutoka kama biharusi aliyekuwa hana kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo niseme kwanza naunga mkono hotuba hii ya Waziri wa Fedha kwa asilimia mia moja. Naamini kwa kupitisha bajeti hii basi yale mambo yote yaliyokuwa yanapata utatanishi au ugumu kidogo chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango yatakwenda sawa kwa sababu ni mchumi mahiri na anaweza kuongoza Wizara hii na naamini atafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme katika kusimamia uchumi wa nchi yetu hii basi ni lazima uchumi huu uwe na udhibiti mkubwa, tutengeneze mikakati ya kudhibiti uchumi wetu. Kwa mfano, kwenye nchi hii sasa hivi mtu anatumia currency yoyote anayotaka na kwa sehemu yoyote anayotaka, hapa udhibiti unaonekana umekuwa hafifu. Unaenda sehemu saa nyingine unaambiwa ulipe kwa dola na wewe Mtanzania uko hapa, kwa nini? Kwa nini kule tunakokwenda kuwakilisha ukitaka kununua chochote kama kule South Africa, hata kama unayo hiyo dola au Euro unatakiwa ukanunue kwa pesa za kule ambazo ni rand. Sasa na sisi tuudhibiti uchumi wetu, Wizara ya Fedha ifanye kazi hiyo, shughuli ya kudhibiti currency yetu ifanywe kwa bidii zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya maendeleo inasema kwamba uchumi wetu kama sikosei umekua kwa 7% lakini ni kwa kiasi gani mtu wa kawaida anaweza kupata reflection hiyo? Unamfaidia vipi au mtu wa kawaida anaonekana vipi hali yake kunyanyuka kiuchumi? Kwa sababu haya maelezo tunayopewa hapa ni ya kisomi zaidi lakini tunataka aje chini hata yule mtu wa chini ajue anafaidika nini na ukuaji wa uchumi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nalotaka kuzungumzia ni hili la ukusanyaji wa kodi. Tunapongeza hatua zilizofikiwa za kuweka mashine za electronic sehemu nyingi lakini bado kuna uvujaji katika ukusanyaji huo, hii efficiency iko kwa kiasi gani? Kwa mfano, inawezekana na imeshatokea unakamatwa na traffic njiani anakwambia mashine ya kutolea risiti haifanyi kazi, sasa unamlipa nani au ile pesa ukiitoa inakwenda kwa nani? Hapa inaonekana ni vema udhibiti uzidishwe pamoja na kwamba tunakuwa na digital lakini udhibiti kwenye hivi vifaa vya kukusanyia kodi uwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kukuza sekta binafsi. Sekta binafsi tumeambiwa inachangia uchumi kwa kiasi kikubwa na tunaunga mkono, jambo hili ni zuri. Hapa hapa inaonekana wadau wazalendo ambao wanashiriki kwenye hii sekta binafsi wanapata vikwazo kwa sababu wageni wanaleta bidhaa zao japokuwa hafifu, sisemi kama zote lakini nyingi ni hafifu, kwa bei ndogo ambayo wanaiuza hapa; mzawa na mwekezaji wa sekta binafsi anashindwa ku-compete. Hii binafsi na holela sana haifai, uwepo udhibiti wa bidhaa na tuwaunge mkono kweli kweli hawa wawekezaji wa binafsi ili waweze kushamiri. Kwa sababu nchi hii itajengwa na wenyewe wazawa, hao wengine wanakuja kuchuma kisha wanaenda zao. Itakuwa kama hii hadithi ya kudai mjusi, mjusi kachukuliwa tunadai hapa kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, naamini bado kuna kazi kubwa ambayo inatakiwa ifanywe na hii Wizara yetu ya Fedha na ninaamini itawezekana. Sina maneno zaidi kwa sababu mimi si mtaalamu wa fedha lakini kidogo mwanga ninao na naamini kwa kupitia Waziri wetu huyu kazi kubwa sana itafanyika. Nawapongeza wote na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi hii kwa leo ili kuweza kuchangia katika Muswada huu wa marekebisho ya Sheria mbalimbali, Sheria Na.3 ya mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa dhati kabisa kuipongeza Serikali kwa kupitia kwa AG na timu yake kwa kuweza kuleta marekebisho haya. Inaonyesha dhahiri kwamba Serikali imejipanga kuondoa mapengo pengo, mashimo shimo yote yaliyokuwemo kidogo kidogo katika Sheria. Unapoleta marekebisho ina maana kuna upungufu fulani na hii ni nzuri. Kwa hivyo nipongeze hiyo timu ya AG pamoja na Kamati yetu ambayo pamoja na wadau wengine wamefanya kazi kubwa sana ya kuchambua Muswada huu na kuweza kuuleta hapa, ambao utakidhi kwa kiasi kikubwa kuondoa zile kasoro ambazo zilikuwepo.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kutazama marekebisho katika ile Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sura ya 141 hapa kwa kweli inaonekana Serikali hii imedhamiria kushughulikia tatizo katika usikilizaji wa mashauri na kuweka urahisi.

Mheshimiwa Spika, kuchapisha bila kupitisha kwenye Ofisi ya Mtakwimu Mkuu ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuona hizo takwimu ndiyo stahiki, mtu yeyote yule atabidi apitie huko. Hilo ni jambo nzuri kwa ustawi wa nchi, kwa sababu vinginevyo zinaweza kupatikana takwimu ambazo siyo sahihi na mtu akaweza kuzichapisha zikaweza kuitia nchi yetu katika matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile iko Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura 11. Hapa Serikali ilipendekeza mobile courts ambazo kwa kweli tumeridhika sana, baada ya ushauri, Serikali imeondoa mapendekezo haya ya kutaka kuleta mobile courts, kwa sababu kwa kweli kwa sasa hivi zingekuwa mzigo zaidi, kwa sababu hizi Mahakama zilizopo ni nyingi pia. Hizo gharama ambazo tuliona kama zingetumika kutengeneza hayo magari ya mobile courts zingekuwa kubwa. Ni bora kujenga majengo ambayo yanaweza yakatumika kwa Mahakama au kama Mahakama kesi zimemalizika, tumeshakuwa watu wazuri, basi zitatumika kwa kazi nyingine kama vituo vya afya au libraries kuliko kutumia fedha nyingi hivi kuanzisha mobile court. Kwa hilo, Serikali tunaipongeza, ilikubaliana na Kamati ikaliondoa pendekezo hilo. Sasa siku za mbele sijui tena kama itaona kuna haja, itakuja kuirudisha lakini itatuambia hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria nyingine ni hii ya Baraza la Michezo, Sura 49. Kwa kweli kulikuwa hakuna sheria ya kusimamia vyama vya michezo. Serikali imeona hilo na ni kweli kwa sababu michezo siku hizi ni tija na ni kitega uchumi, kwa hiyo, lazima kuwe na watu watakaokuwa wanasimamia.

Mheshimiwa Spika, vilevile hili suala la sportingbet siku hizi imeenea sana na inaonekana kupata pesa nyingi sana, lakini hakuna sheria inayoidhibiti. Kwa hiyo, Serikali pale ikiingiza mkono wake, itaweza kuyachunga vizuri mapato na kuchunga haki za wenye sheria hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri kwa mchango wangu huo, naona kama inatosha, niwaachie wenzangu wengine. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii leo. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia uzima na afya leo nikapata fursa hii ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nasisitiza na nakupongeza na nakuombea dua Mheshimiwa Naibu Spika, Tulia Ackson. Mungu akupe nguvu uendelee kuhudumu katika Bunge hili kwa umahiri kama hivi unavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, umesimamia kanuni na taratibu bila kusita, hukubagua kama huyu mtu katoka chama gani wala nini. Mimi binafsi siku moja nilikatisha hapo ndivyo sivyo, ulivyomaliza kikao tu ukatoa mwongozo kwamba, siyo ruhusa kukatisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wetu wa Fedha ambaye anapanga na anajua kupanga. Wizara hii amepewa kusudi kwa kuwa anajulikana anaimudu, uchumi wake unaonekana hapa na nimtie nguvu. Watu wengi humwita kaka yao, mdogo wao, sijui nani wao, mimi ni shemeji yangu na namwamini sana. Najua ataupeleka uchumi wetu kule tunakotaka kwenda kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya pongezi hizo na kutia nguvu huko, nianze kuzungumzia utaratibu wa kodi ya ongezeko la thamani. Hapa nataka kuhusisha ile section iliyozungumzia kuhusu bidhaa zitakazotoka kwenda pande mbili za nchi yetu za Muungano yaani Zanzibar na Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijue tu, je, kodi hii itahusisha vyakula? Nauliza kwa sababu kwenye ukurasa wa 48 wa hotuba, kifungu 67 namba moja mpaka mbili kimeondoa kodi kwa baadhi ya vyakula. Hali halisi ni kwamba Zanzibar inaagiza vyakula na mboga mboga kwa kiasi kikubwa sana. Sasa naendelea kutaka kujua kwa ufafanuzi, vyakula ambavyo havikutajwa kodi yake itakuwaje? Kama kuna uwezekano iandaliwe orodha ya vyakula ambavyo havitatozwa kodi ili kuepusha migongano.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi mwingine juu ya kodi hii inayopendekezwa, kwamba je, pande hizi mbili zote zimeshirikishwa kupanga ili kuepuka kuwapa shida wananchi? Napendekeza pia kabla ya utaratibu huu yafanyike majadiliano ya kina kwa wadau wanaohusika na kwa kujua kiasi gani pande mbili hizi zimekutana na kutafakari mambo hayo ambayo kwa sehemu kubwa yasije yakasababisha kile kilichokuwa kinaitwa kero za muungano. Kwa sababu kwa spirit hiyo hiyo ya kuunganisha na kuboresha udugu wetu baina ya nchi yetu hii, kati yetu, basi ni lazima majadiliano ya kina yafanyike. Natambua kwamba Zanzibar ina bajeti yake na Bara ina bajeti yaken lakini ningeshauri hilo liwepo kwa spirit hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika sasa nataka kugusia uchumi wa viwanda ambalo ndilo tuliloambiwa na tulilotangaza kwenye ilani yetu na Mheshimiwa Rais wetu alisema kwamba Tanzania hii itakuwa kwenye uchumi wa viwanda na huko ndiko tutakopata manufaa. Naomba nijielekeze huko na naomba nilihusishe suala hilo na uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Bagamoyo ambacho kinajulikana kama Basic Bagamoyo Sugar Infrastructure and Sustainable Community Program. Hii ni program ambayo kwa bahati mbaya imepata mkwamo na imeanza siku nyingi sana, lakini ukichunguza kwa kina, mradi huu ni wa kipekee na unaendeshwa na mfadhili na Mwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango yote imepangwa. Mradi huu umeanza tangu 2005 na ungekuwa na faida kubwa kwa wananchi wetu kwa ujumla na hasa wananchi wa Bagamoyo. Wafadhili walikuwa tayari na washafanya study zao zote ni African Development Bank na IFAD na Mwekezaji ni ECO-ENERGY. ADB katika mradi huu ilivyojipanga ni kushughulikia miundombinu ya maji kuwafikia wakulima wadogo wadogo pamoja na barabara za mashambani. Pia kujenga bwawa la kuhifadhi maji litakalosaidia maji wakati wa kiangazi na kuzuia mafuriko.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu ambao umepatwa na vigingi vingi ungewasaidia sana. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za sukari na tunajua sukari ni tatizo na tunajua pia kwamba Kiwanda hiki kinge-take off, kingeweza kuwa na 140,000 CDM za Ethanol na 90,000 megawatts za surplus ya electricity. Kiwanda kitazalisha ajira, na ndicho tunachopigania kwamba vijana wetu wengi hawana ajira; hapa zingetegemewa kupatikana ajira 2,500 hadi 3,000 za moja kwa moja na karibu ajira 13,000. IFAD inasaidia wakulima wadogo wadogo wa miwa na kusaidia vijiji 27 vitakavyozunguka na pia wananchi karibu 91,444 watafaidika na kujiendeleza na ukulima wa kisasa (smart agriculture). Halikadhalika pia wafanyabiashara wadogo wadogo watafaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana kwamba mpango wa awamu ya nne wa BRN ulikusudia kuanzisha viwanda 10 ndani ya maeneo ya corridor ya kusini lakini mpaka sasa bado. Wafadhili wako tayari, gharama, project study zote zimeshafanywa, kitu gani kinachozuia?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo nigusie ile pesa ambazo tunaweza kuzikosa mradi huu ukitutoka. Ni USD milioni 450 kwa ajili ya maandalizi, preparedness, USD milioni 10 kwa uhifadhi wa mazingira za kingo za Mto Ruvu na Wami, USD 350 kwa ajili ya monitoring na evaluation. Sasa sisi tunafikwa na nini? Nafasi hizi na fursa hizi tunazipoteza, wenzetu kwa mfano kule Swaziland wamefadhiliwa na watu hawa hawa, African Development Bank na IFAD na sasa hivi wanazalisha sukari nyingi na wanapata faida kubwa, humo humo wamepata kumwagilia maji, wanapata mahindi ya kutosha, sisi tunakwazwa na nini? Kwa nini fursa tunachelewa kuzishika? Kila kitu bureaucracy.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afikirie sana tija itakayopatikana katika mradi huu. Inawezekana kuna watu ambao hawataki kwahivyo tutazame kwa kina faida inayopatikana….
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya, nikasimama mbele ya Bunge hili Tukufu ili kuweza kuchangia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati pamoja na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyosimamia, kuiendesha Serikali hii na kwa lengo la kuwapatia wananchi wote ustawi na maendeleo. Mheshimiwa Magufuli amefanya kazi nzuri na katika kazi yote hiyo iliyonifurahisha, moja inathibitisha kudumisha Muungano na inanifurahisha zaidi ni hii ya standard gauge nchini, Bombadia hewani, wabadhirifu, wafujaji na mafisadi kwapani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pongezi hizo za Dkt. Magufuli zinaenda pia kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa jinsi anavyoendeleza kazi zake, Mheshimwa Samia kwa kushirikiana na timu yake na vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yote nzima ya Mawaziri na Watendaji, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nasimama kifua mbele hapa kutoa tena pongezi nyingine kwamba watu kule Uyui katika Uchaguzi Mdogo tumewabandika matokeo Chama cha Mapinduzi, katika Vijiji 14 tumepata na CHADEMA moja, Vitongoji 51 na kwa CHADEMA saba, CCM mbele kwa mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa unaposema wewe wanakuwa wanaumia, wanakiherehere, lakini kila ukipigwa ngumi ndiyo unazidi kuwa imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua umuhimu wa Muungano na ndiyo maana leo mimi niko hapa bila ya Muungano nisingekuwa na sauti hii ya kusimama hapa kusema. Umuhimu wa Muungano unajulikana, una tija, unaleta mshikamano, unaleta udugu. Sisi wengine tuna watoto mwisho wa reli huko, kwa sababu ya Muungano, hivyo hatuwezi kukubali Muungano huu ukatawanyika na Muungano huu una faida nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru mpaka sasa hivi kwenye ripoti hii tumeambiwa kero nyingi sana zimemalizika, zimebaki kama kero tatu hilo ni jambo la kupigiwa mfano, hongereni sana Wizara ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea sana lazima niseme hapa maana yake mimi bila ya kuletwa na Zanzibar haiwi. Natoa pongezi za dhati kwa Dkt. Shein kuendelea kuishikilia na kuiongoza Serikali ya Chama cha Mapinduzi bila wasiwasi, maendeleo yanaonekana, kazi nzuri inafanyika na wale wanaongoja zamu yao wangojee mpaka hapo 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mazingira ambalo limeonekana kuwa ni tatizo kubwa sana. Mazingira yanaharibiwa vibaya sana, vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo, ukataji mikoko ya baharini. Kwa mfano, kama sehemu za visiwa ile mikoko iko pale kwa kazi maalum ya biodiversity kulinda maji yasiingie zaidi, sasa inapokatwa maji yanasogea ardhi ambayo ingeweza kuwa ya kilimo inakuwa ya chumvi, kwa hivyo tija inapungua. Nafikiri iko haja ya kuendelea kuimarisha zaidi udhibiti wa maeneo haya au vilevile kutangaza maeneo ya hifadhi zaidi ya hayo yaliyopo ili kuzuia mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba kuna tabia ya watu kuchukua maji kutoka kwenye mito kupeleka kwenye sehemu zao wanazozitaka matokeo yake ni kuleta shida, kwa nini na sisi hatufanyi kama vile walivyotangaza wenzetu kule India ule Mto Ganges na mito yetu na sisi tukawa tunaiangalia kwamba mtu atakayechafua chafua
au atakayeharibu anakuwa sawa na ku-temper na uhai, kwa hivyo lazima kuwa na udhibiti muhimu, tuziimarishe hizo sheria zetu za kudhibiti kwa sababu tunajua mazingira yakiharibika ndiyo uhai unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka niligusie kwa haraka haraka ni suala la ajira. Tunajua kwamba yalikuwepo makubaliano ya tutapata asilimia ishirini na moja ya share ya ajira kwa Zanzibar kwa nafasi za kutoka kwenye Taasisi za Muungano, sasa nimeambiwa nafasi hizo zipo lakini nataka Waziri akija hapa atuambie katika nafasi hizo wamepata Wazanzibari wangapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba kwa nafasi ya Majeshi na Polisi huko hatuna tabu vijana wetu wengi wanapata ajira. Kwa hivyo, tunaomba tufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kuhusu hizo nafasi kwa sababu katika kuzipata hizo nafasi kwa vijana wetu yako malalamiko ya kusuasua katika kupatikana nafasi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni hili la kuhusu makazi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais kule Zanzibar bado hayajawa katika hali nzuri sana yamechoka, nafikiri iko haja ya kufikiria kufanya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nataka nizungumzie ukiunganisha na hiyo kwamba bajeti inayotolewa kwa Ofisi hii naona haitoshelezi, iko haja ya kuongezwa. Kwa mfano, Ofisi binafsi ya Makamu wa Rais kupata 3.7 kwa mwaka mzima bado ni ndogo sana. Kwa mwaka jana Wizara hii ilipangiwa billioni nane lakini imeweza kupata millioni mia mbili, sasa inawakwaza watendaji wa Wizara hii, pamoja na Mawaziri ambao wanafanya kazi nzuri sana, lakini tusipowapatia pesa za kutosha inakuwa ni kikwazo. Tunawapa kazi lakini hatuwapi nyenzo za kufanyia kazi za kutosha, hivyo iko haja ya kufikiria ili kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kusema, ni muhimu kuhakikisha Muungano huu unadumu na
unaendelea kudumu kwa sababu ziko tija tunazozipata na usalama tunao na tunaona faida zake. Kwa hivyo siyo Muungano wa kufanyia masihara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuwa na maneno mengi, maneno yangu ni kwamba Muungano udumu na tunaona kazi inayofanywa na viongozi wetu kwa hivyo tuwape support. Wanawake kwa upande wetu tunashukuru viongozi wetu wametupa nafasi za kutosha, lakini tunataka zaidi lakini kila tukisema tunataka zaidi Mheshimiwa Rais anasikia na anatuongezea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima kubwa kupitia Bunge hili Tukufu naomba nitoe shukurani za dhati kwa Mheshimiwa David Silinde, Mbunge wa Momba mwanatimu ya mapambano kwa mashirikiano na juhudi zake amefanya kazi kwa moyo wa kijasiri na kwa kujitolea mpaka kuhakikisha ushindi wa Mheshimiwa Mboni Mhita, Rais wa Caucus ya vijana, Mheshimiwa Stephen Masele, Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika wamepata ushindi na kuIletea nchi yetu heshima kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa taarifa yako kamanda wa jeshi hilo la ushindi si mwingine isipokuwa ni mimi mwenyewe Asha Mshuwa na nampelekea salamu Mheshimiwa Dkt. Magufuli japokuwa mimi hakunialika mimi na Mheshimiwa Silinde lakini sisi ndio tuliofanya mapambano ya infantry na ya air wing.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la heshima kwa viongozi hawa wawili tulioweza kupata ni vile wameahidi kwamba watatumia lugha ya Kiswahili katika kuendesha shughuli katika Bunge la Afrika. Hii ni turufu kubwa na heshima kwa Tanzania yetu. Tanzania hoyee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nakubali. Katika hotuba Waziri amezungumza sana kuhusu diaspora na vile wanavyoweza kuchangia. Ni kweli wana-diaspora wameongezeka na uchumi wao huko waliko ni mzuri, hivyo wana nafasi kubwa kuchangia hapa kwetu. Sasa Serikali irahisishe mazingira ya wao kuweza kuwekeza hapa nchini Tanzania, kwa hili bado halijawa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko mifano kadhaa ya nchi ambazo zimeweza kuwatumia diaspora na kuendeleza na kunyanyua uchumi wa nchi hizo na kipato cha familia zao. Hasa kwa kuzingatia kama watu hawa wana uchumi mzuri na wanapata experience na exposure za kutoka katika nchi zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo linanikereketa na naomba Serikali inisaidie na tuweze kupata ufumbuzi ni hili suala la uraia pacha (dual citizenship). Suala hili tuiombe Serikali ilifanyie tafakari upya na kulipatia utekelezaji japo kwa masharti. Ikiwezekana basi kama wasiwasi wa kiusalama basi tuweke vipengele ambavyo vitazuia watu hawa wasiingie katika mistari ya kupiga kura au kuhatarisha usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nafikiria na napendekeza kwamba, basi tutazame uwezekano wa kufanya kama ule mfano ambao wanatumia India. India wao hawana duals citizenship lakini wanao utaratibu unaotiwa Person of India Origin, Wahindi hao wanapewa utambuzi ambao unawapa haki sawa isipokuwa hawawezi kupata uraia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jambo kama hili kwa kutumia watalaam wao watafute namna kama kuwa na timu kabambe kama zile za makinikia ili tuweze kuwasaidia hawa vijana wetu ambao wako nje huko na wanapoteza nguvu kazi nyingi sana, ambao wana nia hasa ya kuendeleza rasilimali katika Tanzania yetu na hasa hivi tunavyotaka Tanzania ya viwanda hawa watu naamini wanao uwezo sana wa kutengeneza viwanda hata vidogo vidogo. Mbona hamnipigii makofi, hamtaki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ombi hilo la kuiomba Serikali, sasa naomba tena suala la pass ya diplomatic. Diplomatic Pass imetoka agizo kwamba wasipewe wenza. Sasa naomba Serikali ifikirie jambo hilo kwa sababu inakuwa haipendezi unasafiri na mkeo au na mumeo japo mimi sina mume l akini nawasemea wenzangu wenye waume. Wewe mke unakwenda huku, mume anakwenda kwingine inakuwa haipendezi na haijengi heshima ya nchi. Hata hivyo, tutazame kwa wale watu ambao wanaongeza wake wengi waliozidi, waliozidi wanne au ishirini, basi waambiwe awekewe wake zake wawili tu. Kwa sababu tukisema apewe mke mmoja hapa nitaingilia utaratibu hata Mzee Ally Hassan nitakuwa nimemwingilia kwa hivyo atakuwa haweze kuwachukulia wake zake wote wawili.

Sasa nasema kwa sababu ukisema apewe mke mmoja tu au mume mmoja inaweza kuleta tatizo kwa sababu mzee wetu wa heshima baba yetu Rais wetu Ali Hassan anao wake wawili. Sasa utakuwa upendeleo ukisema mmoja aende. Kwa hivyo wakae watazame namna gani wata-sort out jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu viwanja vya ubalozi. Nchi yetu tulipata heshima kubwa na viwanja vingi tulipata kwa heshima ya mwenyewe hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, lakini viwanja vingi mpaka hivi sasa hivi bado havijaendelezwa. Sasa tubadilike tutafute namna hata kushirikiana na investors wengine sio tu haya majengo yawe kwa ajili ya ubalozi lakini tuweze kufanya shughuli nyingine kwenye majumba yale kujenga ofisi, kupangisha na kufanya ubalozi. Maana yake hiyo tunu tuliyopewa mwisho itapotea, nyota ile tuliondoka nayo itapotea, majengo yetu mengi hayako katika hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutumie hii nafasi ya kidemokrasia ya kiuchumi kushawishi ili tuweze kuviendeleza viwanja hivyo, lazima kuwe na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa fedha zilitengwa kwa mfano wa kujenga jengo la Oman lakini hazikuweza kupatikana. Sasa nataka nishauri kwa vile Oman ni rafiki zetu sana na nimeona hapa kwenye hili ripoti wanasaidia kukarabati Bete la Jaibu basi tutafute namna kwa kushirikiana kwa mazungumzo kama vile wafalme wengine wanaweza kuja kutujengea uwanja au kama marehemu Gadafi alivyojijengea misikiti na hao watusaidie kujenga hili jengo la ubalozi pale Oman itatusaidia sana.

Naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uwezo na nguvu za kuweza kusimama katika Bunge hili leo, na kuweza kuchangia Hotuba hii ya Bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Antony Mavunde, Mheshimiwa Stella, Katibu Mkuu na Watendaji wote wanaoshirikiana katika ofisi hii ya Waziri Mkuu, kwa jinsi walivyoiandaa Bajeti hii na jinsi walivyokuwa wanafanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naanza kwa kuunga mkono hoja hii ya bajeti. Napenda kutumia nafasi hii katika Bunge lako hili Tukufu kuandikisha masikitiko yangu ya moyoni na ya dhati kabisa kuhusiana na kwamba, ninavyofahamu hili Bunge ni sehemu ya mhimili mkubwa sana na muhimu sana katika ujenzi wa nchi yetu. Ni mahali pa heshima, tunapotakiwa tufanye kazi zetu kwa taratibu na kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha sana, kuna Mheshimiwa aliamua kwa kupitia kwenye Bunge hili kwa kinywa kipana kabisa kusema kwamba Rais analalamika lalamika. Nasikitika sana kwamba Mbunge huyu alivyofanya siyo sawa. Mheshimiwa Rais halalamiki, ameapa kusimamia maendeleo na ustawi wa nchi hii kwa kiapo. Kwa hiyo, ni kazi yake kukosoa, kukemea, kuelekeza na kufuatilia. Ndiyo maana unaona mambo yamechukua sura hii yaliyochukua. Sasa napenda jambo hilo lisije likajirudia hapa kusema kiongozi wetu mkubwa, Amiri Jeshi kwamba yeye kazi yake ni kulalamika. Hiyo siyo kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile namwomba sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli azidishe na aendelee kuwashughulikia wezi, wabadhirifu, wala rushwa na wale wote wanaokwenda kinyume na maagizo ya maadili ya maelekezo ya Chama chetu na misingi yetu. Chama chetu kwa wale wasiokijua ni Chama cha Mapinduzi, ndiyo ninachokikusudia, ninachokisemea hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazofanyika kwa usimamizi wa Rais wetu huyu zinatambuliwa hata nje ya mipaka yetu. Sasa kama huku ndani kuna mtu hatambui, huyu ndio anapanda mgomba changaraweni hauwezi ukamea. Tabia na dhamira inayooneshwa baadhi ya wenzetu humu kwa lengo la kutoka walikotoka kwamba nia ya kuivuruga Serikali na kuitifua humu sio mahali pake, kama wanataka kuitifua waende wakatifue malundo ya mchanga huko nje na ndio maana Spika juzi aliwaona akawaambia, wakafanye mambo ya huko nje Bunge. Nipende kusisitiza kwamba tukitunze chombo chetu hiki Bunge kama inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye mchango na napenda kuchangia kwenye Tume ya Uchaguzi. Tume ipo imara na imepangika vizuri na kama mlivyoona kwenye hotuba hapo, imefanya kazi zake kwa vizuri na imeweza kuongeza vituo na kuboresha madaftari ya kupiga kura, kwa hiyo suala kusimamia demokrasia ya uchaguzi limekaa vizuri. Tumeona hapo kuna ongezeko la vituo 27 kwa upande wa Zanzibar, jambo ambalo ni zuri na nahakikisha kwamba Tume yetu hii pia kwa upande wa Zanzibar iko vizuri vile vile hakuna tatizo na demokrasia ya vyama itakwenda vizuri na uchaguzi utasimamiwa vizuri na ni matumaini yangu pia uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa utakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kutoa idhari kweli Tume yetu ya Uchaguzi ipo vizuri na ipo imara kwa sababu mimi ni moja kati ya wale waliobahatika kwenda changuzi zinavyofanyika nchi zingine, huko inakuwa hali si hali. Tume ya ya Uchaguzi ni mashaka, tume si tume kwa mujibu wa maadili na itifaki hatuwezi kusema ni wapi na nini, lakini sisi tushukuru tume yetu ipo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye Ofisi ya Msajili, Ofisi hii ya Msajili kwa sasa badala ya kupitisha ile Sheria Na.5 kuifanyia marekebisho ile ya mwaka 95, naona hali itakuwa nzuri zaidi kwa sababu itapata meno ya kudhibiti wa hivyo wale ambao wamekusudia kufanya vurugu ya aina yoyote, ofisi hii ya msajili ipo tayari kwa ajili yao. Dhamira ya kuhakikisha kwamba hesabu za chama zinaangaliwa vizuri masuala yote yanayohusiana na demokrasia ya vyama vingi kwa msajili kwa imara hizo alizopata itakuwa vizuri. Kwa hiyo napenda kusema kwamba fungu alilopewa Msajili kama kuna namna yoyote ya kuweza kumwongezea, basi aongezewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ninalotaka kuzungumzia ni mahakama, kama tunavyojua huu mhimili ni muhimu sana na unahitaji kuimarishwa zaidi kwa kuwekewa nyenzo za kufanyia kazi. Kuimarisha mfumo wa utoaji haki ni jambo la lazima. Tumeona katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mashauri kadhaa yameweza kufanyiwa kazi na vile vile tumeweza kuelezwa na kuona kwamba kuna ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufaa na kuweza vile vile kuweka haya mabadiliko yote. Sasa unapoweza kupata Majaji ushauri wangu ni kwamba lazima uende sambamba na uboreshwaji wa majengo ya mahakama yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadri mahitaji yanapoongezeka majengo vile vile ya mahakama inabidi yaongezeke. Napongeza sana kazi zinazofanywa na hasa Kitengo cha Kusimamia Majengo ya Mahakama, hiki kitengo kimefanya kazi nzuri sana, sisi tuliopata bahati ya kukagua majengo haya tumeweza kuona majengo ya kileo kabisa ya Mahakama ya Rufaa kule Mara na kule Kigoma, kwa kweli Kitengo hiki kinafanya kazi nzuri sana. Kuna sehemu nyingi ambazo bado majengo ya mahakama hayajafikia, lakini tunaamini kwamba fungu likiwekwa hawa watu watapata spidi ya kumaliza kazi ambayo imepangwa na nyingine ambayo itaweza kuzuka. Kwa hiyo upande wa mahakama kwa kweli umejiweka vizuri sana. Naomba kama kuna ziada ya fedha hapo waweze kuongezewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka sasa kuzungumzia kilimo cha mchikichi, japokuwa kilipata msito kidogo, kilisita kwa sababu kilianzishwa siku nyingi, lakini kama watu wengine walivyosema kuchelewa sio tatizo, nia ni ile kuhakikisha unataka kufika kule unakokwenda. Kwa hali tuliyoiona ya Kigoma na sehemu nyingine na sehemu nyingi za Tanzania, hii miche inaweza kustawi sana na tukapata mazao mazuri sana. Vile vile lazima twende sambamba na viwanda vya kuchakata hizi chikichi. Tumeweza kuona wananchi kule Kigoma wanajitahidi sana kutumia matunda haya ya chikichi katika kujipatia kipato zaidi kwa kutengeneza sabuni na vitu vingine. Lakini vifaa wanavyotumia bado duni. Kwa hiyo Serikali ingefaa kuwaona watu hawa ambao wengi ni wanawake wanaojishughulisha kwa ujasiliamali kwa kutumia zao hili ili waweze kufanya shughuli zao kitaalam zaidi na kuleta tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na zao hilo la chikichi kwa mikoa kama Kigoma lakini naweza hapa kuingizia tu kwamba bado barabara kule haijakaa vizuri, inabidi litupwe jicho la ziada kuweka barabara kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nalipenda na linanikosha sana ni hili la wazo la kuanzisha SGR - Standard Gauge Railway na ninapoona kwamba itakapofika 2019 itakuwa imeshafika Morogoro, basi inanipa matumaini kwamba inaweza kufika Kigoma hatimaye Mwanza na kwingine na kwa kupitia kwenye reli hiyo ndio pale ambapo uchumi wa maeneo ya pembezoni utaweza kukua kwa sababu watu watasafirisha huku na huku bidhaa zao. Kwa hiyo, hili wazo ambalo champion wetu Rais Jemedari Mkuu amelivalia njuga, napenda nimpongeze linakwenda vizuri sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya bajeti. Naanza kwanza kwa kuunga mkono hoja hii, nachukua nafasi hii kupongeza juhudi zinazoendelea kufanywa juu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Kiongozi wetu mahiri Dkt. John Pombe Magufuli, akisaidiwa na viongozi Waandamizi wake, Mama Samia Suluhu, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Ashatu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha walioweza kufanya kazi nzuri hii leo inatuweka hapa ambayo ndiyo roho ya Taifa letu, Wizara ya Fedha ndiyo roho, wakaweza kuwasilisha bajeti shirikishi na kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Esther ananikera. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu ujikite zaidi katika hii sekta ya uchumi, ukurasa wa sita hali ya uchumi. Kukua kwa uchumi ni jambo zuri kwa Tanzania. Pato la Taifa tumeona limekua kwa asilimia 7.0 kutoka asilimia 6.8 ya mwaka 2017. Namuuliza Waziri Je, uchumi huu na ukuaji huu ni shirikishi, yaani inclusive? Ambao umezingatia umaskini kwa kina? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukuaji mkubwa umerekodiwa katika sekta ya sanaa ambayo tumeona hapa ni 13.7 ukilinganisha na sekta ya kilimo umepata kukua asilimia 5.3 ambao hautoshi. Kama tunavyotambua sekta hii ya kilimo ina watu wengi wanaoitegemea kwa ajira, kuzalisha chakula, biashara, mazao, kwa ajili ya viwanda. Kwa maoni yangu, sekta hii ya kilimo ndiyo inauhitaji mkubwa kukua zaidi, ili iweze kuongeza, uzalishaji zaidi (productivity) ili iweze kulima kisasa, (modern agriculture) na kupanua wigo kwa kuongeza malighafi. Mheshimiwa Waziri tuangalie kwa jicho la ziada namna gani ya kuongeza bajeti kwenye hii sekta ya kilimo na je, tunaona kwa hii tuliyoipangia sasa hivi inaweza kukidhi kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kwamba, sekta ya sanaa tumeona imebeba ajira kwa vijana wengi, lakini naamini sekta ya kilimo vilevile ikifanyiwa ubora zaidi, hasa kwenye mambo ya organ, research, pamoja na kuongeza malighafi itaweza kuajiri, kupanua wigo kwa vijana zaidi watavutiwa hasa tukitia hiki kitu wanaita agri-business. Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango, ninataka kufahamu kwamba, hii asilimia Saba ya ukuaji uchumi Kitaifa kwamba, je, imeoanisha na takwimu za Zanzibar za ukuaji uchumi, maana imesema Taifa? Sasa Taifa hili ni Taifa Tanzania au Taifa upande gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri uchumi ni mkubwa. Nataka niulize huu uchumi mkubwa ambao umeanza kukua kwa zaidi kwa kasi kubwa, je, unaushikaje mkono uchumi mdogo wa Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba kutayarishwe mkakati wa pamoja (strategic growth), baina ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuweza kuangalia mambo haya. Katika hali ya uchumi wa Taifa ya mwaka 2018, ukurasa wa 118 kitabu kimeonesha viwango vya umaskini Tanzania Bara kwamba umepungua, mapato na matumizi 2017/2018 basic needs property survey imeonesha kutoka 28.2 hadi kufikia 26. Kwa sasa, kama mnavyojua tunatekeleza malengo endelevu ya SDG 2030 na agenda ya 2063 Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, umasikini kupungua ni hali nzuri. Tunataka tuchukue hatua, ili umasikini huu uweze kupungua zaidi. Tunaweka mikakati ipi madhubuti ya kuongeza tija kwenye kilimo tuweze kutumia bahari yetu kikamilifu, tuendeleze kujenga miundombinu, tuendeleze human development, kustawisha elimu na afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba taarifa hizi za ofisi zetu za takwimu ziweze kufanywa pamoja baina ya Zanzibar na Tanzania bara. Kama vile tunavyofanya kwa sensa ya watu kwa vile taarifa hizi zinatumika kwa pamoja na zikiwa zimefanywa kwa pamoja zitaleta picture yenye faida zaidi. Nafahamu pia kwamba, tunakwenda kuwasilisha report ya hiyari ya utekelezaji wa SDG UN mwezi Julai. Pande mbili najua zinashiriki katika matayarisho, nasisitiza uanishwaji wa data na taarifa muhimu za uchumi na umasikini, napendekeza bajeti survey ifanywe mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mikopo nafuu, ukurasa wa 10 makadirio na mapato. Natambua kwamba, Serikali inatayarisha mwongozo wa ushirikiano baina ya Tanzania na washirika wa maendeleo. Katika kufuatilia kwangu nimefahamu Zanzibar imeshiriki kikamilifu katika matayarisho ya mfumo, frame work, ingawa katika utekelezaji kumekumbwa na changamoto na nina imani kubwa Serikali hii inafanyia kazi changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Zanzibar ina miradi ambayo kwa utaratibu inapitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mpaka sasa iko miradi kadhaa ambayo imekwama ikiwemo miradi ya maji, barabara, kwa mfano Barabara ya Wete – Chake, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na Bandari ya Mpigaduri, mingine imekwama kutokana na vipengele vya misamaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii barabara na hospitali ilitarajiwa kupata mkopo wa Saudi Fund. Kadhia kubwa ni hii ya mradi wa Zanzibar Airport, mkopo kutoka Exim Bank, mradi huu umekwama muda mrefu sana na kipingamizi kikubwa kwa maendeleo na ustawi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba mazungumzo yaendelezwe kwa speed na yakamilishwe kwa manufaa ya pande zote mbili ili Zanzibar nayo iweze kufaidi na kutumia Airports zake maana upo wivu wa maendeleo kwa sababu Airport ya huku Dar-es-Salaam imekamilika na hii yetu iliyoanza mwanzo haikukamilika, tunachukua kwamba, Zanzibar ni kisiwa na uchumi wa kisiwa unategemea zaidi bandari na uwanja wa ndege. Sasa tunaomba kwamba jitihada za ziada zichukuliwe baina ya Serikali zetu hizi mbili ili hili jambo liweze kukwamuka. Sekta hizi mbili, bandari na uwanja wa ndege, ndiyo sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo nafuu na misaada. Misaada ya kibajeti, mifuko ya kisekta, miradi ya maendeleo, ningependa kujua katika jedwali hili kwenye ukurasa wa 103, Zanzibar imepata kiasi gani? Pendekezo kwa mbele ni bora itakuwa vizuri kui-desegregate na kuchanganua takwimu za Tanzania Zanzibar na Bara zioneshwe waziwazi, ili tuweze kujua kila mtu anapata nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naanza kwa kumshukuru Mungu aliyenipa uwezo na nguvu ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa na kwa sauti kubwa, naomba nichukue nafasi hii ya kwanza kabisa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kusimamia maendeleo ya wananchi na uchumi wa nchi yetu Tanzania. Vilevile niwapongeze wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa jinsi walivyosimama na kuwajibika katika kusimamia maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo mambo mawili makubwa ya kuanza nayo. Jambo la kwanza ni hili lililotokea hivi karibuni lililoikumba nchi yetu nalo ni mafuriko. Mvua zimekuwa nyingi na zimeleta uharibifu kwenye makazi, mashamba, watu wanahangaika, mifugo inapotea na mazao yanaharibika.

Naamini Serikali inachukua hatua za kutosha katika kuwasaidia hawa waliopatwa na madhara haya. Nawapa pole kwa sababu hili jambo ni kubwa lisipochukuliwa vizuri watu wetu wengi wanaweza wakapata shida baadaye. Kwa hivyo, nina imani Serikali inafanya kazi yake kama inavyostahili kuli-address jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni kubwa na ni tishio kwa dunia nzima ni hili la Covid19, hii Corona ambayo kwa kweli imeangamiza maisha ya watu wengi hapa duniani na inatia wasiwasi na taharuki sana. Niombe tuendelee kusikiliza na kutekeleza yale ambayo tunashauriwa na Serikali katika kudhibiti maradhi haya yasienee. Naamini kwamba Serikali yetu pamoja na wale ambao walipewa dhamana ya kushughulia jambo hili akiwemo Waziri, Mheshimiwa Ummy, Naibu Waziri wake na wote wale ambao wanashughulika kwamba wanafanya kazi nzuri na watajipanga vyema katika kuhakikisha vifaa vyote vinavyohusika vinapatikana pamoja na hizo ventilators ambazo tumekuwa tukiona katika taarifa za habari huku duniani hata Marekani hazipatikani kwa hiyo watu wenye tatizo la kupumua inakuwa shida. Hii ikienda sambamba na kuwaandaa madaktari na wahudumu wote watakaowasaidia watu wanapopatwa na matatizo haya ya pumzi. Tunamwomba Mungu atusaidie balaa hili litokomee mbali kabisa.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, nataka kuchukua nafasi hii ya kipekee pia kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Ally Mohamed Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utekelezaji wake wa Ilani kusimamia mapinduzi na kuyalinda na kuulinda Muungano ambao umepelekea nchi yetu kuwa na amani na utulivu na sisi wengine tuko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, nije kwenye Wizara hii ya Waziri Mkuu. Natoa pongezi kwa Mawaziri Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Antony Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa. Hawa wote wamefanya kazi nzuri sana kusimamia utekelezaji wa majukumu katika Wizara hii. Hongereni sana ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea na mchango wangu, nije kwako wewe special. Wewe unatisha, umesimamia mabadiliko makubwa katika Bunge letu hili (Bunge mtandao). Pongezi nyingi sana kwako, leo Wabunge tunafanya kazi zetu kwa njia ya kisasa zaidi, kwa wepesi zaidi kwani taarifa zote ziko katika finger tips, huu ni ukombozi mkubwa. Vilevile hii itaokoa pesa nyingi ambazo zilikuwa zinatumika kuzalisha makaratasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi pia kwa Naibu Spika, Wenyeviti, Katibu wa Bunge na watendaji wote wa Bunge kwa jinsi tulivyoweza kushirikiana katika kufanya kazi mpaka Bunge letu hili ambalo ni la mwisho.

Mheshimiwa Spika, vilevile siwezi kusahau watu wetu ambao wametufanya tukakaa hapa Bungeni vizuri, hawa ni wahudumu wa sekta ya afya. Nayo hii ni timu kubwa ikiongozwa na mwenyewe Dkt. Temba na madaktari wenzake Dkt. Nuhu na Dkt. Ruge; Wauguzi, Sister Disifa, Sister Farida; Mfamasia Salma; Madereva wa Ambulance; Wahudumu wa Hospitali na Technician wa Lab. Hawa wote wametufanya sisi tumekuwa imara kuliko tulivyokuja. Mimi hapa mnavyoniona niko imara kuliko Halima Mdee na ninyi mnaniona leo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimefurahishwa sana na utekelezaji…

SPIKA: Mheshimiwa Asha na bahati nzuri hajabisha kabisa, kwa hiyo, endelea kuchangia. (Kicheko)

MHE. ASHA ABDALLUH JUMA: Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongelee miundombinu, hii Standard Gauge inanipa raha sana na kwa kweli ni ukombozi mkubwa kwa sekta ya usafiri. Hii ni reli ambayo inatoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Mwanza na Kigoma. Reli hii itakuwa msaada mkubwa kwa usafirishaji wa bidhaa, abiria, mazao na kuunganisha miji na vilevile kusaidia katika uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, mbali na hayo lakini reli hii inaweza kuja kuzalisha ajira nyingi sana zipatazo 13,177. Ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Naamini itakamilika kwa muda na ni jambo ambalo nchi yetu hii tutajivunia.

Mheshimiwa Spika, wakati Waziri Mkuu anazungumzia suala la bajeti yake lakini kuna wananchi na wao wanafikiria bajeti zao. Kuna kadhia moja kubwa imewakumba baadhi ya wananchi wale ambao walikuwa wateja na wafanyakazi wa FBME Bank. Watu hawa suala lao lilikuwa likiletwa hapa Bungeni mara kadhaa lakini limekuwa likipata majibu mepesi, mepesi. Watu hawa fedha yao iko kule hawapati msaada wowote, wengine wanakufa, familia zao bado zinateseka na jambo hili haliishi.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu wafanye utaratibu wa kuandaa Kamati, kama ile iliyokwenda kuzungumzia kuhusu madini yetu ikapata suluhu. Namna gani Kamati hiyo itakuwa wanajua wao. Kama wataweka Maprofesa wao waliobobea katika sheria pamoja na wadau lakini watu hawa ni kweli wana dhiki kubwa kwa sababu pesa zao nyingi zilikuwepo kule. Najua Serikali yetu ni sikivu na iko hapa kuwatetea wanyonge ambao pesa yao ya maisha iko kule na sasa hivi kazi imekuwa ngumu, kila kitu kimekuwa kigumu. Waziri Mkuu naomba alione jambo hili liweze kufikia mwisho wake kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kuchangia katika miradi ya Mahakama. Utekelezaji wa miradi hii umekuwa mzuri sana (first class), majengo ya Mahakama yamekuwa mazuri mno, kila mtu anayekwenda kule hawezi kusema katoka kule kaonewa. Majengo ya Mahakama Kuu Kigoma, Chato yamejengwa vizuri sana na Mahakama za Wilaya zote zimekarabatiwa na nyingine zimejengwa upya ziko kwenye hali nzuri sana pamoja na kupata furniture nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, ila kuna baadhi ya majengo haya ya Mahakama hayana uzio (fence) kitu ambacho ni hatari. Hii ni kwa sababu imeshawahi kutokea incident Mahakama ya Wilaya ya Uyole ilipigwa mabomu. Kwa hiyo, nashauri Serikali ijitahidi iweze kujenga uzio kwenye Mahakama hizi.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika pia katika watendaji ambao wamesimamia kazi hizi ni huyu Injinia Katunzi. Injinia huyu kwa miradi ya Mahakama amefanya kazi nzuri sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Asha, naona muda hauko upande wako.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, naam.

SPIKA: Muda wako umeisha.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, hapana, ndiyo kwanza kengele ya kwanza.

SPIKA: Leo sijui Katibu ana matatizo gani Mheshimiwa Asha.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, basi naunga mkono hoja lakini uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ni huru. (Makofi/Kicheko)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-wataala aliyenipa uwezo na afya njema leo hii nikaweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani zangu za dhati ziende kwa Chama changu cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kwamba mimi Asha ambaye najulikana zaidi kama Mshua kuwa Mbunge wa Jimbo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Mjini Zanzibar kwa imani waliyonionyesha. Niwahakikishie mbele yako kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya iliyopelekea kupata ushindi wa kishindo wa uchaguzi uliopita. Hiyo ni kuonyesha kwamba utekelezaji ulikuwa wa kuridhisha katika awamu aliyohudumu. Ni matumaini yangu pia huko mbele tunakokwenda mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa sababu yale mambo yetu muhimu; Standard Gauge, Stiegler’s Gorge na mengineyo yote yatakuwa in full operation. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. John Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nachukua nafasi hii adhimu sana kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuwa Rais wa Zanzibar na kuweza kuhudumu kwa style yake ya umahiri, umakini na uhodari na kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unapaa na neema tele kwa Wazanzibar. Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia habari ya Mpango. Nimeusoma na nimeuelewa na watu wengi wameuchangia. Kwa kweli Mpango umepangika, hongera sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na timu nzima mlioandaa Mpango huu. Kwa ujumla wake mipango ya humu inaleta matumaini kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia sekta ya afya na hasa Mpango wa Bima kwa Watanzania wote. Taarifa ya Serikali ilionesha kwamba asilimia 33 tu ya Watanzania wanashiriki fursa za Bima ya Afya. Hadi kufikia 2019, Watanzania walionufaika na huduma hiyo ilikuwa 13,029,636 sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iharakishe mchakato wa kuhakikisha kwamba Mfuko wa Bima kwa Watanzania wote unakuwa tayari na mchakato huo wa sheria ukamilike mapema iwezekanavyo. Hii itasaidia kuwa na mfuko mmoja wa Bima ya Afya ili kuwezesha Watanzania wengi kufaidika na huduma hiyo kwani wakiwa na afya njema, watachangia katika shughuli za maendeleo kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya pili ambayo nataka kuizungumzia ni hii ya Hifadhi ya Jamii. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria. Nimejengewa uelewa juu ya Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii inayochangia uchumi kwa kiasi kikubwa. Mifuko hii inachangia uchumi wa viwanda na nachukua nafasi hii kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa utaratibu wa Mifuko yetu NSSF, PSSSF na WSF. Nakupongeza sana Mheshimiwa Jenista, wewe na Kamanda wako Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa, mmejipanga kweli kweli kuchangia maendeleo na ustawi wa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu, tuongeze ubunifu wa maeneo ya uwekezaji kama vile viwanda vya kilimo vyenye uhakika wa soko, pamoja na kupanua huduma zake kwa Watanzania walio kwenye sekta isiyo rasmi kama vile wakulima, vikundi mbalimbali vya kijamii ambapo huko ndiko kuna Watanzania wengi Zaidi. Tukifanikiwa kuchangia mapato basi mifuko yetu hii itazidi kunona na Watanzania wetu watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo, ahsante sana, nyote nawapongeza. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii kuweza kuchangia leo hii katika Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Na. 2 ya mwaka 2021. Awali ya yote naipongeza Serikali kwa kuleta marekebisho haya hasa kuhusu usimamizi wa cheti cha kifo marehemu kama ilivyosemwa katika Sura 108.

Mheshimiwa Spika, tunajua kifo faradhi na kitatokea na hatujui wakati gani lakini ni lazima na hata kikitokea basi maisha lazima yaendelee.

Kwa hiyo, umuhimu wa upatikanaji wa cheti ni wa lazima kwa wale watakaosalia kuendelea na shughuli na vilevile kwa kuweka record kwa sababu hata takwimu zinataka kujua nani aliyekufa na nani aliyezaliwa na ndiyo maana kule nchi zilizoendelea hata ukiwa umekwenda kule umejifungua ukitaka ku-register mtoto huwezi wewe peke yako lazima wataulizwa na ile fomu watajaza na baba yake mtoto ili yote kuweka mambo sawa, na ukifungua tu record unamkuta. Fulani mtoto wa Mshua, baba yake fulani siyo hii tena leo huyu leo 10, hawa wapo 20 kila kitu kinatakiwa kiwekwe kwenye mstari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo mimi na Kamati yetu tuliona haya marekebisho Na. 19(a) yanayoanzisha mfumo wa electronical wa kuweka record za vifo na amini pia zitakuwa pamoja vizazi utasaidia sana kuoanisha hizi taarifa na kufanya utambuzi. Kwa hivyo, inapotokea unataka cheti au unataka record yoyote itakuwa umepunguza urasimu wa kuhangaika kutafuta hizo record. Kwa hili likifanyika litasaidia ndugu wa marehemu kupata hati za kifo bila kusumbuka na vile vile kwa sababu record zipo vizuri zitasaidi kudhibiti mtu asiyestahili kuweza kuchukua hicho cheti.

Mheshimiwa Spika, lakini Kamati yetu pia iliona endapo ikitokea mjane, mgane au mtoto kutokuweza kufika kuchukua hiki cheti basi yule mtu ambaye atathibitishwa na jopo la kifamilia ataweza kuchukua cheti hicho cha kifo na hivyo kuendelea na shughuli nyingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ufupi Kamati yetu ilifanya kazi kubwa sana na kama alivyosema Mheshimiwa Hadija, Kamati hii ni ya kuitegemea maana yake nchi bila sheria haiendi na hii kamati ndiyo inabeba Bunge hili. Kwa hiyo, sina makubwa sana lakini nimekubaliana na haya mapendekezo ya marekebisho yaliyoweza kuletwa mbele yako. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nashukuru sana kwa kuweza kupata nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia nguvu, uwezo, uhodari na umahiri wa kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutambua Tanzania yetu jinsi tulivyoweza kuridhika na kujidai na kujivuna kwa kuweza kupata Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Jemedari Mkuu mwanamke kuiongoza nchi yetu. Yeye ni Rais mwanamama wa mwanzo katika block hili la Afrika Mashariki. Niseme kwamba Mheshimiwa Jemedari wetu Mkuu Mheshimiwa Rais Samia ninaweza ku-quote ‘is one of our own’ ni mwenzetu. Anatoka kwenye block ya akinamama. Uhodari wake na umahiri wake na ujasiri wake kwenye kazi tunamjua tangu asubuhi. Kwa hivyo niwatoe wasiwasi kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu viatu hivi vimemfaa sawasawa, tena vimekuwa high heels atakwenda mdundo wa kuchumpachumpa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kumpa ushirikiano kama vile tulivyokuwa tunampa kipenzi chetu Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye ametangulia mbele ya haki. Kwa nukta hiyo, namwombea rehema. Mungu ampumzishe kwa amani na natoa pole sana kwa familia ya Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na mchango wangu kwa kugusia program za kukuza ujuzi wa vijana ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Ni dhahiri vijana wengi wanapotoka vyuoni wanakuwa hawana ujuzi wa kutosha katika kufanya kazi zao na hivyo kuweza kushindwa kuhimili ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi. Programu hii inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu imetumia gharama kubwa sana kwa kuwawezesha vijana hawa kupata nauli, fedha ya chakula wakati wanapokwenda kufanya mafunzo ya uanagenzi katika mashirika mbalimbali. Kwa sababu baadhi ya wanufaika hawalipii gharama hizi, lakini ni hii programu imewawezesha vijana wengi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uko umuhimu wa kuongezwa bajeti ili kuweza kuwafaidisha vijana wengi waweze kupata hii programu ya uanagenzi. Katika Ofisi hii ya Waziri Mkuu iko shida moja ambayo tumeiona sisi na hii nayo inatokana na tatizo la kukaimisha watumishi kwa muda mrefu na tatizo la kutoajiri watendaji wakuu wanaostahili na hivyo kuleta shida katika kuchukua hatua wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, shida hii ya kukaimisha kwa muda mrefu iko kwa taasisi mojawapo naweza kuitaja ni ya OSHA. Mkurugenzi anayekaimu OSHA amefanya kazi muda mrefu tangu sisi tunaingia hapa, tulipowezeshwa kipindi cha mwanzo, huyu anakaimu na anafanya kazi nzuri mpaka sasa hivi. Niulize, hivi huyu Mkaimu mwanamama tena wa OSHA ataendelea kukaimu mpaka lini? Awamu ya Tano Mkaimu huyu alikuwepo, Awamu hii tulivyoingia kwa bahati ya kuwezeshwa na wajumbe wetu watu wazuri sana tumemkuta tena anakaimu. Sasa nishauri Ofisi ya Waziri Mkuu ichukue hatua ya kuwa-sort out hawa watu mapema sana, ingawa shida hii ipo pia kwenye taasisi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nigusie masuala ya watu wenye ulemavu. Ofisi ya Waziri Mkuu imechukua hatua za dhati kuimarisha kitengo cha kuratibu masuala haya na jambo zuri nipongeze Wizara hii imeongeza bajeti kutoka milioni 978.50 kwenye mwaka 2019/2020 hadi bilioni 1.29 kwa mwaka 2021/2022. Hili ni jambo zuri na hili kundi litafaidika kwa programu mbalimbali zitakazoandaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko shida nyingine inayoikumba ambayo haijafanyiwa kazi ambayo ni kutokuanzishwa kwa kanzidata. Kwa hiyo tunashauri kuanzishwe kanzidata ili kuweza kuwajua watu hawa wenye ulemavu kwa nchi nzima. Hii itasaidia kuratibu vizuri mipango kwa kuwatambua na kujua nini shida zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye jambo letu hili ambalo linatuadhibu sana katika Taifa hili, nalo ni maambukizi ya maradhi ya UKIMWI. Tunahitaji huduma kukabiliana na kadhia hii, kwa hivyo Mfuko huu wa UKIMWI lazima uweze kutunishwa. Hapa nazungumzia Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI wa ATF, Serikali ichangamkie kutenga fedha zaidi za ndani na kuzitafuta kama tozo kutoka sehemu yoyote ambayo itaona inafaa mradi Mfuko huu uweze kutuna kwa sabbau kazi yake ni muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba kusisitiza kampeni ya kuwezesha wanaume zaidi kufanyiwa tohara. Kwa sababu ugunduzi wa kisayansi umegundua maambukizi ya UKIMWI yanatokana na shida hiyo. Kwa hivyo hilo jambo lifanyiwe kazi, kampeni tuipige, tuhakikishe na kama itabidi pia basi tutakwenda kujifunza namna gani ya kucheza jando kwa watu wa Mtama huko. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la dawa za kulevya; hii ni kadhia kubwa sana inayolikumba Taifa letu. Fedha za kutosha inabidi zitengwe ili kudhibiti na kuhakikisha kwamba kundi hili, Mfuko huu wa Kudhibiti Dawa za Kulevya unafanyiwa kazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ASHA ABDULLA JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mungu kunipa uwezo leo wa kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kuweza kutoa mchango wangu mdogo kwa Wizara hii. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Ndumbaro na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii pamoja na wahifadhi kwa sababu bila wao hakuna Wizara hii. Wote wamefanya kazi nzuri sana kusaidia kunyanyua kipato katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwanzo nataka nianze kwa ile staili ya kuunganaungana, yaani nioanishe utalii huu unaofanyika bara na wa Zanzibar ili watalii wanapokuja kwa mfano huku, wanaoshukia huku moja kwa moja waambiwe vivutio vilivyokuwepo kule Zanzibar na kwa utaalam maalum ili waweze kwenda na kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, na wale wanaokwenda kule vilevile waambiwe vivutio gani vya ziada vilivyopo huku ili waje. Kwa sababu utalii wa visiwani ni tafauti na utalii wa bara; huku kuna wanyama, kule kuna samaki, fukwe nzuri na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hilo naomba lioanishwe vizuri zaidi kama tulivyoungana kwenye Muungano tukaweza kupata watoto, mpaka Kakonko tuna watoto sisi wengine, kwa hiyo na utalii uje kwa staili hizo hizo. Hilo ndilo langu la mwanzo ninalopenda kulisemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kulizungumzia ni hili la malikale na uhifadhi ambalo lina mchango mkubwa katika kuendeleza sekta hii ya utalii. Ukweli tumeona kuna sehemu hizi ambazo zimeainishwa kama zinahifadhiwa, kwa mfano Kilwa Kivinje, Songo Mnara, Bagamoyo, Kaole na Kolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, huku baadhi kwa mfano kama Kilwa Kivinje mimi mwenyewe nimeona yale majengo yanapotea kabisa. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, Wizara ifanye jitihada ya kufanya ukarabati kwa staili ileile ili haya yasiweze kupotea wala yasiweze kuvamiwa. Hasa haya ya Kilwa Kivinje ambayo nimeweza kuyaona, haya yanapotea, hata madirisha, milango, yote yanachomolewachomolewa. Kwa hiyo Wizara waliangalie jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia sasa hivi ni hili la kusafirisha baadhi ya wanyama. Nafikiri kuwe na control kwa sababu wanyama inaonekana wengi tunasafirisha tembo, chui na wengine, kwa hiyo tuwe na control ili wasije kwisha, halafu hizi tunu zikahamia huko katika nchi nyingine sisi tukawa hatuna kitu. Kwa hiyo, Wizara waongeze control katika jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano zamani hapo nilikuwa nasikia sana vipepeo, ndege na nini, sasa siku hizi sijasikia, hata vyura walipelekwa kule. Kwa mfano vyura kutoka Kihansi walipelekwa kule, hatusikii tena chochote. Mwisho na sisi wenyewe tutapelekwa tukazae kule huku hakutakuwa tena watoto. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu lingine ninalotaka kulizungumzia ni hili la kuhakikisha kwamba utalii wa ndani unaongezeka kwa kuwashawishi wananchi wetu kufanya hizi ziara za kutembelea vivutio mbalimbali kwa kuwawekea excursion. Kwa mfano, niliwahi kwenda Kigoma nikataka kwenda kutembelea kule kwenye wale masokwemtu, nilishindwa. Bei ya kule ilikuwa ni kali sana. Kwa hivyo angalau kwa Watanzania ambao wana midomo mirefu wale ndiyo wa kuwapeleka, wa kuwapunguzia bei ili wakasemee kwengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine kwa Wizara hii ambayo inafanya kazi vizuri, ni kwamba mshiriki kwenye makongamano ya kimataifa kwa sababu huko ndiko tutakakojiuza zaidi. Ingawaje wanatuambia wamefungua app, wachangiaji wangapi sijui wameonekana ku-click au kufanya nini, hii haitusaidii bwana. Tutoke, tuvae masks zetu, tupige sindano za COVID, twende tukaitangaze Tanzania yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi hawa watu wanavyofanya kazi hii vizuri, na huyu jamaa Waziri anavyokuwa vizuri, sina la kusema zaidi ila apewe hiyo bajeti yake aliyoomba afanye kazi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi tena ya kuweza kuchangia kwenye marekebisho ya sheria mbalimbali namba nne mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, kwenye ile hoja ya Posta ninalo dogo tu la kukazia kwa sababu Mheshimiwa Rais alikuja hapa akahutubia akasema kwamba anafungua fursa ya ushindani wa biashara. Kwa hivyo, kuipa Posta kufanya zile shughuli peke yake ingekuwa tunakwenda kinyume na hilo lakini Serikali imesikia na hilo limetekelezwa. Natoa pongezi sana.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utakuwa ni kuhusu ufifilishaji wa makosa ya Sheria ya Madini Kifungu
28. Muswada huu ulitoka kwa mapendekezo ya Kamishna wa Madini. Kufifilishwa kwa makosa kwa wale waliovunja Sheria na kukubali kulipa. Kifungu hiki hakikueleza faida za ufifilishaji na kutoa kinga za kutoshtakiwa kwa mtu aliyekubali kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya majadiliano katika Kamati Serikali ikakubali kueleza faida za ufifilishaji na kutoa kinga kwa waliokiri kosa kwa kulipa faini wasipelekwe Mahakamani. Hili ni jambo zuri na litatuweka vizuri kwa hivyo, litapunguza msongamano kwenye Mahakama, watu watajifahamu na pengine itasaidia wakashughulike na mambo mengine ya kimsingi badala ya kwenda na kurudi Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu ulikuwa huo tu. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii kwa siku hii ya leo. Awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu kuweza kusimama hapa kwa heshima ya kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Rais wetu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi endelee Jemedari mkuu Mheshimiwa Mama Samia kwa jinsi anavyosimamia kuiendesha Serikali yetu hii na leo hii bajeti yake katika Awamu hii ya Sita. Bajeti ambayo imegusa wananchi wote na bajeti ambayo imeakisi na kulenga mambo muhimu yote ya maendeleo ya kila mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukubali kwamba lazima tuwe na mbinu yoyote ya kupata kodi ili kuendesha Serikali na kuendesha nchi. Kwa hivyo kuna sehemu itaumauma lakini hakuna nchi inayoendeshwa bila kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu leo nataka niunganishe pale Mheshimiwa Rais Jemedari Mkuu Mama Samia alipokwenda kufungua tawi la Benki kuu Tanzania na kuonyesha jinsi nchi yetu inavyotarajiwa kufanya kwa kutumia sekta hii ya kifedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo ambalo limekua likisemwa humu bungeni kwa muda mrefu nalo ni la benki ya Federal Bank of Middle East. Tokea tarehe 8 Mei, 2017, FBME benki ili wekwa chini ya ufilisi kwa DIB deposit insurance board na Benki Kuu ya Tanzania. Leo ni miaka minne na mwezi moja hakuna majibu ya utatuzi kwa suala hili.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wateja wa benki hii hawajapata amana zao Zaidi ya kulipwa shilingi milioni moja na laki tano licha ya ramana yao kuwa kubwa. Uwe na milioni mia mbili, uwe na milioni mia tatu kwa mujibu regulation uwe unalipwa 1500, wafanyakazi licha ya kuwachishwa kazi hawajapata stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki wenye amana mauti imewakuta bila kupata haki zao na familia zao zinaendelea kuteseka. Kwa ruhusa yako naomba niwataje baadhi ya hao waathirika ili Serikali na watu wengine wote wapate kuona jambo na uzito wake; mfano Marehemu Ally Juma Shamuhuna, aliyekuwa Waziri na Naibu waziri kiongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme hili jambo nina interest nalo mimi nausika nalo sana pia. Marehemu Dkt. Maliki Abdallah Juma, alikuwa mkurugenzi mkuu wa wizara ya afya, marehemu Mohamed Toll Suleiman, Marehemu Shaibu na wengine kadhaa na baadhi wengine walio hai sasa hivi wameshafika kustaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ruhusa yako niwataje; Mzee Buruani Sadati ambaye alikuwa Waziri na mshauri katika Ofisi ya Rais ya Dkt. Shein, Dkt. Mohamed Sale Jidawi, Dkt Nafisa Dkt. Mwatima na wengine kadhaa ambao hao wa sasa na wenzao wengi wamestaafu wanategemea amana yao hiyo waliyoweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Bunge lililopita 2018 walisemea jambo hili mara kadhaa halikupata majibu, Mawaziri, Naibu Mawaziri mpaka Mwanasheria Mkuu lakini bado jambo hili limekwama. Ushauri wangu kwa vile Benki Kuu ndiyo custodian na ndiyo guarantor basi waone namna ya kulimaliza jambo hili. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Mwanasheria wakutane na makundi ya wadau husika bila kubagua na mbili kutafuta njia bora kuhakiki haki za wadau hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu chini ya jemedari wetu Samia Suluhu Hassan iweje kulitatua jambo hili, hichi ni kilio akisikie Mheshimiwa Rais kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ninalotaka kulizungumzia hapa ni hili la suala ya VAT kwenye bidhaa, natoa shukrani sana kwa Serikali kulifanyia kazi jambo hili, kuamua mfumo wa marejesho kama ilivyokuwa zamani. Ombi marejesho yafanywe moja kwa moja baina ya TRA na ZRB kwa sababu wanayo mifumo ya risiti kila mmoja anamuona mwezake, zoezi likifanywa na Hazina patakuwa na urasimu na Hazina zetu Hazina mifumo wanayoonana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nimelifurahia na kweli limetia moyo vijana wetu ni hili la biashara za bodaboda. Ni ukweli usiopingika biashara hii inafanywa na vijana wetu wengi na inawasaidia sana lakini wamekuwa wakipata mkwamo mkubwa katika kufuatia tozo za faini kubwa ya elfu 30, lakini Serikali yetu sikivu imeona na imeweka kiwango kizuri cha Shilingi elfu kumi huu ni uamuzi wa kupongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ninataka kulisema hapa ni mkopo nafuu kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, Bunge la Kumi na Moja lilitunga sheria kuzitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya mikopo nafuu kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu. Ni ukweli usiopingika utaratibu umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za ukosefu wa ajira hivyo kuyawezesha makundi haya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Halmashauri zote ziongeze usimamizi na udhibiti wa makusanyo na migawanyo yake ili kuhakikisha fedha za mikopo zinawafikia makundi stahiki na mikopo itolewe bila upendeleo. Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI wakae pamoja kuona namna bora ya uratibu wa mikopo hiyo ya makundi maalum lengo la kuhakikisha makundi yanajiendeleza kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni nafasi ya taasisi ya OSHA kuchochea uchumi wa viwanda nchini. Kupitia Kamati yetu ya Katiba na Sheria nimeona usimamizi wa afya mahali pa kazi (OSHA) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na chini ya jemedari anayeendelea kusogea mbele Mheshimiwa Jenista anapambana kweli kweli kazi hapa inafanyika vizuri, mazingira yamekuwa mazuri sana kutokana na ufanisi wa shughuli zao kusimamia mazingira rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na michango mizuri ya taasisi ya OSHA bado narudia hoja yangu kwamba kumekuwepo na tatizo la kuwakaimisha watumishi kwa muda mrefu, kwa hivyo niombe ofisi hii ilifanyie kazi watu wasikaimu kwa muda mrefu ili wapate kufanya motisha na ninaamini kwa uhodari wako Mheshimiwa Jenista jambo hilo kwako siyo tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanisi wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF mfuko huu uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka mitano tangu ulipoanzishwa 2015 umekuwa mfuko wenye tija kubwa kiuchumi na ustawi wa waajiriwa katika sekta binafsi na sekta ya umma. Mfuko umeonyesha uwezo wa kujiendesha kwa kuendelea kukua kiuchumi kimfumo mwaka hadi mwaka kiasi kwamba mfuko umeipatia Serikali kodi ya Shilingi bilioni 10 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kufanyia kazi ushauri wa muda mrefu wa Kamati na Wabunge kuhusu michango, mwaka wa fedha inakwenda kupungua endapo waajiri wataanza kuchangia.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, waajiri wataanza kuchangia 0.6 kwa msingi huo naomba kuunga mkono hoja, nawapongeza Waziri, Naibu Waziri na wote waliochangia katika hotuba hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima leo nikaweza kusiamama mbele ya Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumpongeza sana Jemedari wetu Mama Samia Suluhu kwa jinsi anavyochapa kazi na kutuongoza vizuri na mambo yetu yanaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nawapongeza Mawaziri ambao wanatuongoza kwenye Wizara zetu hasa hii yetu ambayo tunashughulika nayo moja kwa moja kuanzia kwa Waziri Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria. Kwa kweli tumekuwa tunafanya kazi kwa mashirikiano na masikilizano makubwa, naweza kusema ni Kamati ambayo tunajiona kama tunafanya kazi heaven on earth, tunafanya kazi peponi katika dunia jinsi tunavyoweza kufanya kazi na ku-deliver.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kwa kupongeza sana Wakala wa Usalama na Afya Sehemu za Kazi. Kwa kweli wakala huu umeweza kufanya kazi vizuri sana kwa mujibu wa sheria iliyoianzishwa ya mwaka 2003; kwanza jambo la muhimu sana lile la kupunguza tozo na kuwaondolea wadau kero, halafu urasimu wa kupata huduma kwa kutumia nyenzo hizi za kisasa kwa matumizi ya TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine waliloweza kufanya watu hawa ambalo ni la heshima sana ni lile la kusimamia kumaliza jengo la Wakala na Usalama Sehemu za kazi hapa Dodoma. Jengo la uhakika lenye viwango lenye kutimiza masharti yote, lenye kurahisisha watu wa aina yoyote kuweza kutumia, kwa hivyo wale wote walioweza kusimamia katika kazi nzuri hii nawapa kongole zao.

Mheshimiwa Mwneyekiti, ziko changamoto katika OSHA nayo ni uhaba wa watumishi, sijui kwa nini; kwa sababu tunaona huko nje tunaona wamezagaa ma-graduate, mechanical engineering, ma-electrical engineering, watu wa afya na nini, sielewi inakuaje mpaka watumishi ikawa tabu kuchukuliwa kwenye Wizara hiyo kwenda kufanya hiyo kazi. Kwa upande wa OSHA nawapongeza sana na waendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sehemu yangu ya pili ninayotaka kuzungumzia ni hii ya Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo; hii nayo imepiga hatua kweli kweli kwa sababu zamani ilikuwa shida kidogo, lakini wameweza kuongeza vituo kutoka 139 ambayo ilikuwa kwa kupitia kwa Mkuu wa Wilaya hadi vituo 8,817 katika vituo vya tiba, huko kote watoto wanaandikishwa. Kwa hiyo hii imewapunguzia wananchi usumbufu na vilevile Watoto wanaweza walokuwa chini ya miaka mitano wanaandikishwa bila ya kutoa ada yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo changamoto ambazo RITA imewakabili ni zile za kushindwa kuandikisha watoto wanaozaliwa nje ya nchi, kwa sababu bado sheria haijatoa mamlaka kwa RITA kutekeleza hiyo. Sasa ninaushauri na ushauri wangu kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo Nchi za Nje, waje na mpango mkakati wa kutatua changamoto hii haraka iwezekanavyo ili hili jambo liweze kufanyaika na watu wapate vyeti vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vilevile liko jambo moja ambao linawasonenesha sana, ni hili watendaji wa RITA kuwa wanakaimu miaka kadhaa, yuko mwanadada pale tangu tumeingia sisi Bungeni hapa yeye anakaimu, kaimu, kaimu, sasa kama hafanyi kazi vizuri huyu kwa nini mnamuacha na sisi tunaamini anafanya kazi vizuri kwa sababu ripoti zinapokuja kwenye Kamati yetu tunaona anafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe mamlaka husika dada huyu apewe nafasi yake kwa sababu anaweza kufanya kazi vizuri. mwisho utamkuta anastaafu yupo pale pale, sasa hivyo ndio nini mnafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ninachotaka kuzungumzia sasa hivi ni kuhusu dawati la kuwasaidia kwenye sheria. Kuna watu wanapata taabu sana, sasa imetolewa huduma na Wizara hii ya kuwapa watu training wakawasaidie watu kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama ya mwisho. Wasiwasi wangu kama hawa watu waangaliwe vizuri isijekuwa tunatengeneza vishoka vyengine kwenye Mahakama. Wapate training nzuri ili waondolewe, kwa sababu wananchi wengi wa Tanzania hawana uwelewa mzuri wa mambo ya kisheria, kwa hivyo nifurahie kwa hili na ninaunga mkono na ninaomba Serikali izidishe iwaondolee wananchi shida zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo ninaunga mkono hoja hii, ahsanteni. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru Mungu kutujalia sote tukawa wazima hapa ili kujadili bajeti hii ya Katiba na Sheria kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, napenda sana nianze kwa kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na wasaidizi wako kwa jinsi mnavyoliendesha Bunge letu hili la Bajeti kwa ustadi na umahiri na uhodari.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na mchango wangu kwa ruksa yako nichukue nafasi hii kumpongeza Mama yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopambana kuhakikisha kwamba Tanzania yetu hii inashamiri kiuchumi, uhusiano wa kimataifa na ustawi wa Tanzania yetu. Vilevile kusimamia utawala wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Katiba na Sheria na Msaidizi Waziri, pamoja na watendaji na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii. Na kwa dhati kabisa nampongeza AG, Dkt. Feleshi kwa jinsi anavyokuwa makini na kushirikiana na sisi muda wote, he is never missed kwa kweli, AG ni kiboko yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kuzungumzia kuhusu utendaji na maboresho kwenye Mahakama. Pongezi za Serikali kwa hatua ya kuboresha Mahakama. Kusema kweli Mahakama za kileo. zimejengwa, Mahakama za kwa mfano Mahakama Kuu Shirikishi Arusha ni Mahakama ya kupigiwa mfano, facilities zote za kisasa, za ki-digital, za kimaendeleo yote. Maana hata kama utataka kwenda washroom basi utatamani usitoke kwa jinsi ya hali ilivyokuwa nzuri pale Arusha.

Mheshimiwa Spika, na vilevile tumeweza kuona kwamba, nchi yetu inakwenda kama vile supreme courts za Marekani. Jengo letu la supreme court litakapokamilika hapa Dodoma litakuwa ni jengo la mfano kabisa. Nashukuru sana, kwa kuwa kazi nzuri inafanywa pia chini ya usimamizi wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna maendeleo makubwa sana. Bado kama wilaya 19 tu ndizo hazijapata majengo ya kileo. Sisi wenyewe na kamati yetu tumeshuhudia majengo ya kisasa kabisa ambapo hata mtu ukipelekwa huko hukumu itakayotoka unaweza ukaridhikanayo. Ukitizama siku za nyuma Mahakama zilivyokuwa utafikiri vijumba vya ndege, lakini sasahivi wilaya zote zimepata Mahakama nzuri na furniture za kileo. Unakwenda unapambana na ki-dock kile anachowekwa mtumiwa, mninga safi kabisa, ni kazi nzuri sana imefanyika. Samani za kileo na nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, lakini maboresho kwenye Mahakama yameweza kustawi zaidi kwa vile imetolewa huduma nyingine inayosema, Sema Na Mahakama Saa 24, ambapo watu wataweza kupeleka malalamiko yao na kujua status ya kesi zao na mambo yao mbalimbali. Kwa hivyo haya nasema ni maendeleo makubwa kwa sekta ya Mahakama ambapo mtu atapiga simu saa 24 na ataweza kupata maelezo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande huu wa uboreshaji masuala ya Mahakama ni kweli fedha iliyotumika, wanasema wazungu ni value for money, tumeweza kuona sasa fedha iliyotumika ni kweli. Kwa sababu, kwa mfano Mahakama ile ya Mwanga ni ya kileo kabisa; kwa hivyo, tunapongeza jitihada hizi zinazofanywa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nataka sasahivi niizungumzie Ofisi ya Mashitaka ambayo ni kilio kikubwa kwa kuwa imekuwa inapata fedha kidogo za kufanyia kazi zake. Kama tulivyosikia kwenye ripoti, kwenye ofisi hii kuna upungufu wa ofisi 125 ambazo haziko. Na tunaona jinsi watu wanavyopata malalamiko ya kucheleweshewa uchambuzi katika kesi zao na hivyo kubaki mahabusu kwa siku nyingi. Kwa hivyo, Serikali haina budi kuongeza fedha na kuongeza watendaji ili waweze kufanya shughuli hizi za ofisi ya mashitaka ziende kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ninataka kuzungumzia ni Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kilichopo Lushoto. Chuo hiki kina mchango mkubwa kwa sekta ya sheria nchini, tumeona. Na mpaka sasahivi ni chuo ambacho hata majaji wapya wakiapishwa wanakwenda kule kupigwa msasa. Hata hivyo, chuo hiki kina majengo machakavu sana, miundombinu yake si mizuri na si friendly hasa kwa wale watu wenye mahitaji maalum. Kwa hivyo, tungependa Serikali ifikirie kuongeza fungu pale kukiboresha hiki kiwe cha kileo zaidi, ikiwezekana cha namna yake kwa Afrika.

Mheshimiwa Spika, mabweni yamechoka sana. Tunayahitaji, tungependekeza kwa sababu, wanafunzi pale ni wengi na hivyo wanalazimika kwenda kupanga mitaani. Kwa hivyo, ni bora pakafikiriwa kuongezwa hostels mpya ili wanafunzi wapate malazi. Pamoja na hayo tunapongeza tumeweza kushuhudia jingo la hostel ya wavulana zuri sana ambalo linakidhi hata hawa watu wenye mahitaji maalum. Kwa hivyo, napongeza jitihada hizi zinazofanywa, na nalazimika tena kumpongeza sana mtendaji mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante, anafanya kazi nzuri. Prof. Elisante yeye ni mtendaji, yeye ni mhamasishaji, yeye vilevile ni kila kitu. Thank you very much Professor. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningependa kwa ujumla wake Serikali iongeze mafungu kwenye mambo hayo mawili. Chuo hiki cha usimamizi huku Lushoto na Mkurugenzi wa Mashitaka.

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi hayo ndio yangu. Ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) ningependa kwanza kuanza kwa kupongeza kazi kubwa sana iliyofanywa na Kamati yetu ushiriki uliowakilishwa na wadau katika kuja kutoa maoni yao, walishiriki vizuri

Mwanasheria wetu naye kasimamia vizuri mambo hayo ya sheria naye kabobea na hii kazi anaiweza sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuongelea juu ya hili rekebisho la sheria kwenye Usajili wa Vizazi na Vifo Sura
108. Marekebisho haya ni muafaka na yamekuja wakati ndiyo sana, kwa sababu tumeona kwamba vifo na vizazi vingi vinakuwa havisajiliwi mpaka sasa tatizo hilo bado lipo na imani yangu kwamba nchi haiwezi kuendelea kama haiwezi kujua idadi kamili ya watu wake wale ambao wanaishi na wale ambao wanazaliwa kwa hivyo mipango inaweza kupata ugumu. Kwa nini sijui hampigi makofi wakati mimi nasema maneno ya maana.(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwakabidhi rekebisho hili linalowapa nafasi Watendaji wa Vijiji kuweza kufanya hii kazi itarahisisha sana kwa sababu itarudisha ile huduma chini sana kwa hivyo kutapunguza kuhangaika kwa wananchi wetu katika kutafuta huduma hii. Hili vilevile litaendana na agizo la kidunia Convention on the Rights of the Child ya mwaka 1989 inalooana na sheria ya The Child Act Sura Na. 13 pamoja na Kanuni zake zote zilizoko pale. Kwa hivyo, tutakuwa tunakwenda kama dunia inavyotaka twende lakini ningeshauri tu kwenye hili hawa watendaji waweze kupewa mafundisho au maelekezo rasmi ili hili zoezi liweze kufanyika kwa wepesi. Nikisema hivyo nina maana kwamba waweze kurekodi hali halisi kama inavyokuwa kwa sababu hili ni jambo ambalo litakaa na ni jambo ambalo tunalihitaji kwa kupanga mipango yetu ya baadaye

Mheshimiwa Mwenyekiti, rekebisho lingine katika haya ambayo nataka kuyazungumzia ni hili la mapato la kushughulikia mapato ambayo yanatokana na uhalifu Sura 256. Hili limekuja wakati muhimu sana, tunakumbuka sote kwamba kumekuwa na desturi ya kupiga, kupiga maana yake kuiba kwa kitaalamu watu kujilimbikizia mali kwa njia wanazozijua wao halafu baadaye wazungu wanasema wakaenda scot free kwa sababu baada ya muda hakuna sheria inayowaba kuweza kuzirudisha zile mali na kuikosesha Serikali mapato yake ambayo ni muhimu katika maendeleo ya nchi hii. Kwa hivyo, sheria hii itawabana kama wewe umeiba basi utabanwa siyo unaiba halafu unakwenda kumpa mkeo Ester Bulaya haifai, tutambana huko huko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tushughulike nao hawa wapigaji kama mkubwa wetu anavyosema. Rais kila siku anasema nchi hii imepigwa na imepigwa kweli kweli, kwa hivyo marekebisho haya yamekuja wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haki yako ipo na sheria tunaamini ipo inazingatia basi utaipata, hata kama ukiwa mke wa mtu lakini ikiwa ile mali imesemekana wewe umeipata kwa kupiga basi utathibitisha kama kweli wewe ni mke wa fulani lakini mali hii hukuipata kwa kupiga, kwa hivyo itarudi kwako hamna wasiwasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwe na wasi wasi tuiamini Serikali yetu sheria hizi na wasimamizi wa sheria zetu hizi wako vizuri na wamebobea kisheria, ndiyo maana tunaona kwa sababu sheria ni msumemo inakata kote na ndiyo maana kwa jitihada na ubobezi wa wanasheria wetu ndege yetu imerudi, ingekuwa hakuna sheria na hakuna wabobezi wa sheria wa kusimamia basi ndege yetu ingepotea. Kwa hiyo, niwapongeze Wanasheria wa nchi hii mnafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Na wewe ukipiga?

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Nishughulikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuzungumzia ni hii Sheria ya Kurejesha Wahalifu Sura Na. 368 ikiongeza Kifungu Na. 8 (a) inamwezesha Waziri Mamlaka kumkabidhi yule mhalifu aliyekimbilia huku kwetu, kama umeharibu lazima uende ukawajibishwe huko huko, nasi tutakuwa siyo kama kisiwa tunaishi peke yetu dunia nzima tunaona. Tunakumbuka pia Manuel Noriega alichukuliwa huko kwa sababu alifanya uhalifu fulani akarudishwa, yule alikuwa ni Rais wa Panama lakini alirudishwa. Kwa hivyo, hii mimi naona sawa sawa na ninawaamini Mawaziri wetu hawa wana uwezo wa kutosha siyo kama akiwa Waziri ndiyo yeye ataamua tu hata hazingatii, kwa hivyo nchi yetu hii inaendeshwa kwa utawala wa sheria hovyo, itazingatia mambo yote hayo

Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho mengine ni ya Sheria ya Msalaba Mwekundu sheria ya msalaba mwekundu Sura 66 ambayo imeweka Ibara ya 45 na 52 ni jambo zuri kwa sababu sharia itaweza kutumika bila matatizo yoyote kwa pande zote za Muungano. Vilevile sheria hii inaweza kutoa ufafanuzi kabisa kwa sababu watu wengi mara nyingi wakiona msalaba mwekundu wanafikiria wanapelekea upande mwingine lakini hii ni organization ambayo iko kushughulikia wakati wa maafa. Maafa ni mambo ambayo unpredictable yanaweza yakatokezea wakati wowote, kwa hivyo kuiwekea nafasi nzuri ili iweze kuhudumu vizuri hii Jumuiya ya Msalaba Mwekundu ni jambo zuri sana hizi sheria zote naona zimekuja kwa wakati mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria nyingine ni hii Sura ya 341 ya Kazi za Mawakili. Nafikiri ni wakati muafaka Serikali kuweza kudhibiti Mawakili wake, kama wewe unatumwa na Serikali basi ukatumike na Serikali vizuri, laa kama unataka kufungua Firm yako mwenyewe fungua ukashughulike huko, lakini haiwezekani nchi yetu saa nyingine watu wetu ndani ya Serikali yetu, badala ya kuitetea Serikali wanakwenda kuiangamiza Serikali hilo halikubaliki katika uongozi huu wa John Pombe Magufuli hatutakubali tunataka wewe uitetee Serikali ili tuweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri narudia tena ni huu uliofanywa na Mawakili wetu kutetea mpaka ndege yetu ikarudi hongereni sana Mawakili wa Serikali, nakupeni kongole kubwa sana endeleeni hivyo iteteeni Serikali yenu, teteeni mali zetu wapigaji wasipate nafasi, wakitaka kupiga wakapige majumbaji kwao, kwa wake zao huko na wapenzi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nikiwa kama Mwanakamati kuweza kuchangia mambo mawili, matatu ambayo ninayo. Ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tunashukuru sana Serikali kutuwezesha kutukusanyia wadau na kututolea taaluma mbalimbali ili tuweze kuchangia katika maboresho ya sheria hizi saba ambazo zililetwa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani sana kwa hii Sheria ya Uhifadhi wa Wanyama Pori, Sura ya 283 ambayo ina lengo la kuongeza Uwekezaji na kuongeza Pato la Taifa, hapa kwa kweli, kusema kweli watu wengi kati yetu tulikuwa hata hatujui vitalu ni nini, vitalu tunavyojua sisi vya Athuman, vya Asmini na Mawaridi ndio vitalu tulivyokuwa tunavijua. Lakini hapa kama alivyosema mwenzangu Maalim pale Mheshimiwa Ally Saleh, tulipata elimu ya kutosha kuonyeshwa namna gani hii minada itakavyofanywa na tukaona kwa taaluma hii ya elektroniki inavyokuja na itakavyokuwa Serikali yetu itapata faida kubwa sana kwa matumizi ya kufanya minada hii kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ni kusema kwamba tumekubali na tunaunga mkono rekebisho hilo na kwamba lengo letu katika nchi yetu hii kuhakikisha kwamba Pato la Taifa halipotei, haliibiwi na Sheria hii ni moja katika measures ambazo zitasaidia. Na zabuni kama tulivyoambiwa katika Kifungu 38(2) za vitalu hivi vitafanywa kwa uwazi kabisa. Jambo jingine zuri ni lile la kuhakikisha kwamba katika hizi Kampuni za Uwindaji basi wazawa nao wamewekewa sehemu yao wataweza kuhodhi share kiasi fulani kwa hivyo, naunga mkono sana marekebisho haya kwenye Sheria hii ya sura 283.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine nililotaka kugusia kidogo ni kuhusu marekebisho kwenye Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki ya Posta, Sura 306, kwa kweli kwa hali tuliyonayo sasa na utundu walionao watu wengi katika masuala ya ki-digital, wizi umekuwa mwingi, na hasa kupitia line za simu, kwa hivyo udhibiti huu ambao umeanishwa katika sura hii utasaidia kwa sababu hali duniani inakuwa tete na watu wengi wanatumia mawasiliano ya simu kufanya ukorofi wao wa wizi na kupeana habari zingine. Sasa ukidhibiti kwa kusajili inakuwa ni vizuri, na vilevile bila kusema kama kutakuwa na adhabu fulani kwa wale ambao watakuwa hawajatimiza masharti itakuwa hujafanya kitu, lakini kwa hivyo marekebisho haya kwenye Sheria hii yamekuja ni wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jambo la usalama na kutokuibiwa pesa zetu kama inavyofanyika siku hizi kwa kupitia mitandao na simu ni jambo linalotuuma sana. Sheria hii, lakini tuangalie namna gani itaweza kuhakikisha kwamba kwa kuwalazimisha hawa watu wenye Makampuni ya simu na wauzaji line kwamba kila mtu ambaye ana simu kabla hawajampa hiyo simu basi awe amesajiliwa kibiometria. Sijui kwa namna gani wataweza kufanya hivyo kama kutafuta ki-biometric kidogo kidogo wakawa nacho pale kama kile watu wanavyolipa wanavyopata kulipa kodi, lakini jambo hili tusilifanyie masikhara na ni wakati wake, lazima tuwabane sana, vile tunavyochukuliwa pesa zetu kidogo kidogo lakini wahakikishe kwamba hili ni jukumu lao hawa service provider, kuhakikisha kwamba wanarahisisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, kwa upande wa Serikali nao tunashauri NIDA nayo inajitahidi ndio kama jana mlisikia pale tunasema kwamba Watendaji wa Vijiji na wa Kata wapewe Mamlaka na wao ya kuweza kurahisisha usajili wa watu wapate hivi vitambulisho vya NIDA ili hili jambo liwezekane na kwa kweli sasa ni wakati wetu sisi kutoka nyuma, huko kwa wenzetu mtu akizaliwa tu anakuwa ameshasajiliwa, sasa hapa unapiga kelele kumuharakisha mtu akasajiliwe itolewe adhabu kali kwa muda unaotolewa, ukipita kwamba mtu hajasajili mtoto, hajajisajili mwenyewe, apate adhabu ndugu zangu, sasa hali imekuwa nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho mengine niliyotaka kuyazungumzia ni haya ya sura 204 ya Baraza la Sanaa, tumeona kwamba, sote tunajua kwamba kwenye sanaa vijana wetu, watu wazima kama sisi, na wengine wote wameweza kupata ni sehemu yao ya kupata kiuchumi na kwa hivyo Taifa limeweza kunyanyuka sana kipato chake kwa kupitia sanaa hii. Kwa hivyo, hivyo Vifungu vilivyoongezwa pale ni tafsiri kama hiki Kifungu cha Na. 2 cha kuongeza tafsiri ya misamiati kama modeling, mitindo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, humo pia kutakuwa na udhibiti mzuri kwa sababu hilo jambo liko Kisheria na kwa hivyo tutaweza kuongeza mapato kwa kupitia wasanii wetu hawa na jambo jingine ambalo kwenye hii Sheria tumeliona na linafaa ni hili uteuzi wa mabaraza kwenye wilaya na mkoa ambayo yatasimamia sanaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jambo lolote ambalo litakuwa halisimamiwi linakuwa haliwezi kwenda vizuri, lakini kukiwa na usimamizi kwa hivyo wataweza ku- tape sanaa nyingi ambayo iko nje kule chini vijijini, wilayani kwenye tarafa na kwenye kata ambayo inapotea yaani inakuwa –wasted kwa sababu haina msimamizi wa kwenda ku-tape.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, kuweka eneo hilo la wasimamizi wa mikoa, wilaya ni jambo ambalo naona ni muafaka sana. Vilevile kuna jambo hapa ambalo linatuweka katikati, hili la maadili la uvaaji, lakini naona kila mtu atajilinda kwa namna anavyoweza lakini kukosa kusemea lazima tuseme kama maadili yetu ni muhimu ni kuyalinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu jana hapa tumeona kadhia iliyotukuta sisi Wabunge kwa sababu mtu mmoja tu kwenda kinyume na maadili kwa hivyo ile escudo tulihangaika nchi nzima kuipata kwa sababu tu watu hawatambui, lakini ukijilinda na kujiweka vizuri ni jambo zuri, tegemea wapi unakwenda, kwa sababu mtu hakutegemei wewe uende kuogelea na manguo yako kama haya hivi nilivyovaa mimi si utazama? Eehe! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda kuogelea lazima uvae bikini, eehe, unategemea wapi unapokwenda, huwezi kwenda unategemea nini unakwenda kufanya na wakati fulani. Kwa hiyo, pale mtu ambapo anakosea anafanya sivyo ni wajibu wetu sisi kama Viongozi mahiri na hodari kumuelekeza, eheh, lakini huwezi kuogelea na mkanzu kama huu utazama. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ambayo nilikuwa nataka niizungumzie ni kuhusu Baraza la Mitihani sura 107, kweli ni Sheria muafaka imekuja kwa sababu wizi wa mitihani ndiyo baadaye umepelekea kule ambapo watu wengi sana wali-suffer kutokana na kukosa vyeti, walitumia vyeti vilivyokuwa si vyao, sasa ukianza kudhibiti mapema, ni vizuri. Kwa hiyo, hii Sheria ni muafaka ili kuwadhibiti wanafunzi na kwa sababu watu wengine wanaiba mitihani wanakuwa wanajitajirisha, ndio wale wale kundi niliyo wasema jana, hafanyi chochote anaiba mtihani anaurusha electronically yeye kapata pesa zake, sasa Sheria hii huyu akibanwa atashughulikiwa ipasavyona itapunguza, itakuwa elimu yetu pia ni credible ya faida sana na kwa sababu imepita kwenye michujo hakuna wizi wizi wa mitihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, jambo ambalo watu wa Makundi maalum kwenye Baraza la Mitihani ni jambo ambalo kwa sababu wanafunzi wengi waliopo wana mahitaji maalum, kwa hivyo wakiwa na mwakilishi wao naona ni jambo litakuwa muafaka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hivyo, kwa upande wangu, siwezi kuwa na mengi sana, ila niseme ninaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yetu hii hasa kuleta marekebisho na mwenyewe Mzee wetu, Mzee Baba, Rais wa Jamhuri hii Dkt. John Pombe Magufuli kasema wakiona tu walete haraka na wakikosa kuleta marekebisho haraka haraka yeye atashughulika nao ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu Mawaziri Marekebisho leteni Kamati yenu ya Katiba na Sheria tuko tayari tutapitia na kurekebisha, ahsante sana naunga mkono. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, 2022
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nikiwa kama Mwanakamati kuweza kutoa mchango wangu katika Muswada wa Sheria hii ya Kukabiliana na Kudhibiti Maafa kama ilivyoletwa.

Mheshimiwa Spika, kwanza natoa pongezi kwa Serikali kwa kuleta Muswada huu wakati muafaka kwa sababu tumeona matokeo huko nyuma yalivyokuwa yanatupata kukitokea maafa, watu wanavyohangaika na Serikali inavyohangaika, inakuwa mpata mpatae, kakamate kule, kashike kule. Sasa hivi unapokuja na sheria hii ambayo inashirikisha ngazi zote kuanzia chini mpaka hapa ilipofika, ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kusema kweli Serikali ilijiandaa vyema na kutuletea wadau, nao wenyewe kutuletea mabingwa waliobobea katika sheria hii, na Kamati yetu ilishirikiana na kushauriana kwa dhati kabisa. Kwa kweli huko hukuwepo lakini moto uliwaka wakati wa kujadili sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri kwa kuwa watu wote ni waelewa; wadau ni waelewa, wanasheria ni waelewa na sisi ni waelewa, tumeweza leo kusimama mbele yenu kuomba Bunge letu hili liweze kupitisha Muswada huu uwe sheria kamili kuweza kutusaidia katika hayo. Kwa sababu ni jambo la hakika kwamba unapotaka kupigwa ukiwa unajua ngumi itakupiga kwa wapi itakuwa haikuumi sana. Kwa hiyo, tunapojiandaa kwa lolote ni jambo ambalo litaisaidia Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria hii kwa kweli inatekeleza mambo ya Jamhuri ya Muungano, lakini kwa vile maafa yanaweza kugusa pande zote za Jamhuri, tumeona umuhimu wa ushirikiano wa pande hizi mbili yanapotokea matatizo makubwa, kwa sababu huenda yakatokea hata maradhi au dhoruba huko baharini yakakumba Zanzibar. Kwa hiyo, ule ushirikiano utakaokuwepo wakati wa dharura ni jambo zuri sana. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iendelee na jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tumejadili na tumeliona lina umuhimu wake, kwa sababu bila fedha hakuna utakaloliweza. Kuanzishwa huu mfuko maalum wa maafa, tunashawishi upate udhibiti mzuri, utekelezaji wake na uendeshaji wake uwe na uwazi zaidi ili tuweze kufikia yale ambayo tumedhamiria. Kwa sababu, bila kuwa na fedha hakuna kitu utakachoweza kukifanya na tunajua inapotokea maafa, basi fedha nyingi kweli huhitajika. Kwa hiyo, vile Serikali ilivyoona kwamba iweke kama ni sheria kwamba Serikali itie fedha kiasi fulani katika mfuko huu, ni jambo ambalo tunasema lilikuwa la maana sana.

Mheshimiwa Spika, sasa suala la majanga kama tunavyosema linaweza likatokea na maafa. Kitu cha muhimu ni kuhakikisha kwamba hii elimu inatolewa hasa shuleni, kwa wananchi kwa ujumla, kila mtu afahamu inapotokea dhoruba niiname chini. Kama vile tunavyoambiwa, ukisikia risasi zinalialia, basi wewe inama chini ili isije ikachukua sikio lako. Kwa hiyo, watu watakuwa wanajua mapema namna gani wafanye. Kwa hiyo, tunashauri Serikali iendelee kutoa elimu hii kwa ngazi zote tena kwa namna ya hali ya juu, kwa sababu kama alivyosema mwenzetu mmoja hapa Mheshimiwa Abdallah kwamba early warning inatusaidia sana; yaani tahadhari ya mapema ni jambo la muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali pia iimarishe kitengo hiki cha kuweza kuhabarisha wananchi; tuna-expect hiki kwa hiyo, ni lazima tujiandae kwa namna hii ili kupunguza yale madhila au madhara yatakayotokea, kwa sababu, ukijua namna gani ukimbie, yale maafa yatakuwa yamepunguza ukali wake.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kuliongelea hapa ni hili ambalo tulishauriana kwenye Kamati la kwamba siyo Waziri aamue tu kukamata mali za watu halafu afanye vile anavyofanya, ni kwamba ikitokea shida kutaka kutumia zitumike mali za Serikali, lakini kama itatokea mtu mwenyewe atataka kujitolea, kwa sababu wakati wa maafa kuna watu wana moyo wa imani wanapenda kujitolea. Tumefurahishwa sana na Serikali kukitengeneza kifungu hiki cha Ibara ya 6(C) ambacho kilikuwa kinakwenda kinyume na Katiba yetu ya kutaka kuchukua mali za watu kwa lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunashukuru kwamba Serikali imekubali kupunguza ule msururu mkubwa wa Kamati zile za Maafa. Kwa hiyo, yale yote ambayo tumeshirikiana tukashauriana na kuweka utaratibu maalum ambao utakuwa rahisi katika utekelezaji, kwa sababu ukiweka kundi kubwa mara nyingine kama walivyosema wenzangu, wengine; huyu atakuwa hapatikani, huyu hapatikani, kwa hiyo jambo linapotaka dharura, kwa hiyo, mmoja Mwanakamati hakupatikana.

Mheshimiwa Spika, kwa kiasi kikubwa nampongeza sana Waziri Simbachawene na Mheshimiwa Ummy, kwa kweli wamekuwa maridhawa sana mpaka wakatuletea CBD ndani, kila mtu kaletwa pale ili pande zote zipate kushirikishwa. Kwa hiyo, hawa ndugu zetu wamefanya kazi kubwa sana nasi tunashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lililopo tuiunge mkono Serikali sheria hii ipite ikatusaidie wakati tunajiandaa vizuri ili yakitokea maafa, tuwe na namna ya kukabiliana nayo na kupunguza machungu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, yangu yalikuwa ni hayo tu. Ahsante. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 2) Act, 2022
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Nami nimepata heshima ya kuweza kuwa mwanakamati na kushiriki katika kuchambua muswada huu ambao uliletwa na Serikali, na tukachambua kwa kina na tukafikia maamuzi ya pamoja na tunashukuru Serikali kwa kukubaliana na michango yetu Wanakamati.

Mheshimiwa Spika, fursa niliyo nayo leo nataka kugusia sheria zilizoletwa. Katika Muswada huu wa kubadilisha sheria mbalimbali una marekebisho udhiti na kupambana na madawa za kulevya Sura Namba 95, pia usafirishaji haramu wa binadamu Sura 432 Ibara ya 3 hadi 9, vilevile Sheria ya Kanuni ya Maadili ya Viongozi wa Umma Sura 398.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama tunavyojua, hii biashara haramu ya watu inaleta matatizo makubwa nchini kwetu. Kwa hivyo tuliona kwamba zile adhabu zilizopangwa zilikuwa hazitoshi. Tukapendekeza kwamba adhabu ile ya kulipa milioni 100 hadi 200, na kama mtu itatokea kurudia tena kosa lilelile basi apate kifungo cha maisha. Kwa sababu shughuli nyingi zinaharabika, kuwarundika watu kama wanyama kwenye magari kuwasafirisha kuwapeleka sehemu mbalimbali wakatumika kinyume na matakwa yao hapo tunaona haki za binadamu zinakiukwa. Kwa hivyo kwa Serikali kuleta jambo hili pengine litasaidia kwa kiasi kikubwa kuwavunja kasi wale ambao wanashughulika na biashara hii.

Mheshimiwa Spika, katika Ibara ya 13 tulipendekeza kufuta kifungu cha 32 na kuandika upya, kuchunguza makosa chini ya sheria hii. Binafsi katika sehemu hii tuliona kwamba hii mamlaka ya kudhibiti na kuzuia dawa za kulevya ipewe meno ya ziada. Na kwa hivyo ikapendekezwa kwamba, wawe na fursa ya kuwa na mahabusu ambazo watazisimamia wao wenyewe ili kuweza kuzuia kutovuja katika mtiririko wao wa kufanya uchunguzi. Kwa sababu kwenye mahabusu hizi za kawaida unachanganya watu wenye kesi za dawa za kulevya, walioiba kuku, walioiba mbuzi, waliotuhumiwa tu; ambapo taarifa pale zinaweza zikachanganywachanganywa mtu akamwambia hebu nipelekee taarifa yangu hii ili hata mzigo kama umefichwa mahala ukaondoka.

Mheshimiwa Spika, lakini hao watu wakipewa mamlaka hii ya kuwa na uwezo wa kumudu masuala yao wenyewe itatusaidia sana. Kwa sababu tunajua hasara ya dawa za kulevya taifa linaangamia na wachache wanatajirika kutokana na biashara hii, lakini sehemu kubwa ya wananchi watoto wetu wanaharibika, hali si nzuri na udhibiti unakuwa mgumu.

Mheshimiwa Spika, na hata ukiangalia unakuta kwamba jinsi ya kuweza kuwapata wale wenyewe, mapapa wakubwa inakuwa vigumu lakini wakipewa maeneo ya ziada hawa mamlaka na kwa walivyo hao wenyewe, na kamanda wao, kama mlivyomwona pale alivyosimama kupokea tension yake mambo yanaweza yakabadilika sana na hawa wahalifu wa mambo haya tunaweza tukawakamata kwa kirahisi sana.

Mheshimiwa Spika, marekebisho mengine tuliyoweza kuyazungumzia na tukayakubali ni juu ya mamlaka haya ya Sheria ya Maadili. Kwenye sheria hii tuliona mambo mengine ambayo tulishauriana tukakubaliana nayo lakini yale ambayo tumeshauri kama kutoa ripoti baada ya miezi mitatu tumeona kwamba ni jambo la kufaa, kwa sababu watu tuweze kuwadhibiti, tuweze kujua mali umepata kwa namna gani, ili utaratibu uliokuwepo uweze kufahamika nafikiri tutakapoweza kuweka vizuri mambo haya, hamna shaka mambo yetu yatakuwa vizuri, kwa sababu lazima tukishakuwa kwenye Sheria kwamba tuna- declare mali zetu, kwa hivyo ukiwa unafahamu mapema itakuwa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, napendekeza pia haya mamlaka kuweza kuupa nguvu zaidi ili waweze kuchunguza wenyewe mambo yao na kuendesha kesi wenyewe na haina maana kwamba hatutambui kazi nzuri inayofanywa na Polisi ila tutataka ushirikiano zaidi na Polisi. Tunatambua sana kama Polisi wanafanyakazi nzuri, kwa hivyo vyombo hivi viwili vifanye Pamoja.

Mheshimiwa Spika, vilevile tukaona pia kwa sababu madawa ya kulevya yanatembea sehemu nyingi, ukanda wa pwani na nini, tukaomba pia kuwe na ushirikiano zaidi baina ya Zanzibar na Bara ili kuweza kudhibiti, kwa sababu hili shauri la dawa ya kulevya haliwezi kuwa udhibiti wake hauwezi kuwa wa upande wa mtu mmoja tu.

Mheshimiwa Spika, kazi hii ya kuimarisha mamlaka hii siyo kama tunapora mamlaka ya Polisi na kazi zake lakini tumeona iko haja ya kufanya hivyo. Madawa ya kulevya kama tunavyoona ni tatizo kubwa kwa hivyo tushirikiane na maelekezo ya Serikali na tuupitishe Muswada huu ili tuweze kupunguza kadhia hii. Ahsante sana.(Makofi)