Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Philip Isdor Mpango (19 total)

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ripoti ya PAC ya Januari 2015 iliyojadili ripoti maalum ya CAG ikionesha upotevu kutokana na watu kukiuka utaratibu. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kuhakikisha watu waliokwepa kodi na kukiuka taratibu waweze kulipa pesa hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ripoti hazioneshi kiuhalisia faida ambazo Serikali inazipata kutokana na misamaha hii ya kodi na makampuni haya hayafanyi social responsibility kwa kiwango kinachoridhisha. Je, Serikali inafanya mkakati gani ili kuhakikisha kwamba makampuni haya yanaondolewa misamaha ya kodi, walipe kodi stahiki na wajibu wa huduma kwa jamii ubaki ni wajibu wa Serikali? Ahsante
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza misamaha ya kodi ambayo tumekuwa tunaitoa kwa makampuni ya madini imekuwa inapungua kutoka takriban asilimia 17.6 ya exemptions zote zinazotolewa za kodi, mpaka sasa imefika takribani asilimia tisa. Hatua ambazo tumekuwa tunachukua, moja ni kurekebisha Sheria za Kodi na Waheshimiwa Wabunge mlipitisha hapa marekebisho ya Sheria ya VAT ambayo iliondoa misamaha mingi ya kodi na VAT peke yake misamaha ya kodi ni takriban asilimia 56 ya mapato ya exemptions zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kurekebisha sheria hiyo, msamaha wa kodi umepungua kwa kiasi kikubwa. La pili, tunafanya jitihada kubwa kushughulikia mazingira ya biashara na uwekezaji, kwa kuwa uwekezaji hautegemei kodi peke yake, ndiyo maana Serikali imeelekeza nguvu kuongeza upatikanaji wa umeme ambayo ni malalamiko makubwa ya wawekezaji, lakini pia ulinzi kwa ajili ya wawekezaji na kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya kutoa leseni za biashara na vibali vya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeongeza kujenga uwezo wa kuchambua vipengele vya misamaha ya kodi, vile vitengo ambavyo ndani ya Wizara ya Fedha lakini pia ndani ya Mamlaka ya Mapato ili kuhakikisha kwamba misamaha inakuwa tu ile ambayo inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Waziri wa Fedha atakataa misamaha yote ambayo haina maslahi kwa Taifa. (Makofi)
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikwazo kikubwa sana cha biashara kuendelea katika Taifa letu ni riba kubwa inayotolewa na mabenki ya biashara ambayo sababu yake ni kiwango kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Je, Serikali ina mpango gani dhidi ya kusaidia wafanyabiashara dhidi ya riba kuwa inayotolewa na mabenki, kikwazo hicho ambacho BOT ndiyo imekuwa msingi mkubwa ili kuwezesha watu wengi kufanya biashara zenye sura ya miradi na siyo biashara za uchuuzi?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Benki Kuu itaendelea kusimamia sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba riba zinapungua na ndiyo maana katika mapendekezo ya Mpango tulioleta, moja ya hatua ambazo Serikali inachukua ni kuhakikisha kwamba, taasisi za umma sasa zinafungua akaunti Benki Kuu ili tuhakikishe kwamba fedha nyingi ambazo zilikuwa zinatumika na mabenki kwa ajili ya kufanya bashara, fedha za Serikali bila Serikali yenyewe kupata faida, sasa zinaweza zikatumika ili hayo mabenki sasa yaende huko kwa kupeleka huduma kwa wananchi vijijini. Hii ni hatua mojawapo ya kusaidia kupunguza riba ili wananchi wetu waweze kunufaika zaidi.
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Waziri hasa kwa baadhi ya wastaafu hao kusitishiwa zoezi wakati walikuwa watumishi wa halali. Hii inaashiria kuwa Serikali haikuwa na orodha sahihi ya wastaafu hao. Pia stahiki walizolipwa ilikuwa ni kusafirishia mizigo na wala siyo kiinua mgongo. Je, Serikali itawalipa lini kiinua mgongo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imeomba fedha ya kulipa madeni kwenye bajeti ya mwaka 2016, je, madeni hayo ni pamoja na ya wastaafu hao?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba hawa watumishi wa iliyokuwa Afrika Mashariki walipokuwa wanastaafu kazi, mafao yao ya kustaafu yalikuwa yanakokotolewa na kuunganishwa na kipindi ambacho walikuwa wanafanyia kazi Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi chote walichofanyia kazi kwenye mashirika husika. Pamoja na kulipwa mafao yao kwa namna hiyo, walikwenda wakafungua kesi Na.93 ya 2003, wakidai walipwe mafao ya utumishi waliyotumikia kipindi wakiwa Jumuiya ya Mashariki. Serikali iliwaomba tufanye mazungumzo nje ya Mahakama wakakubali na tulifanya mazungumzo na 2005 Serikali ndipo ilikubali kuwalipa wafanyakazi 31,831. Mwezi wa Septemba, tulifikia makubaliano (Deed of Settlement) kwamba baada ya kuwalipa wastaafu hao hapatakuwa na madai mengine tena na ndiyo tuliwalipa kama nilivyoeleza katika jibu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, swali la ni lini tutawalipa kiinua mgongo tulishamaliza na Serikali haidaiwi tena. Pia ni muhimu nieleze kabisa kwamba pamoja na kufikia Deed of Settlement bado tulitoa muda wa zaidi ya miaka saba ambapo wastaafu walikuwa wanakuja wanalipwa on a case by case basis. Kwa hiyo, Serikali hatudaiwi tena na wastaafu hao.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii, ninapenda kuuliza swali dogo la nyongeza.
TRA wanafanya kazi nzuri, lakini katika baadhi ya maeneo TRA hawa hawana ofisi; kwa mfano katika Wilaya ya Kasulu, Wilaya kubwa ya kibiashara, Wilaya ya mpakani TRA haina ofisi. Sasa ningependa kujua kupitia kwako je, wenzetu wa Wizara ya Fedha mna sera ipi ya kujenga ofisi za TRA katika maeneo hasa yale ya kibiashara ili mapato ya Serikali yaendelee kuongezeka.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, TRA imekuwa ikifanya uchambuzi wa mwenendo wa biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika Wilaya na Mikoa ya nchi yetu ili kuweza kuamua mahali ambapo panatakiwa patangulie katika kujenga ofisi za Mamlaka ya Mapato, ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Kasulu ambapo tumekuwa na mazungumzo na Mheshimiwa Nsanzugwanko na yeye ametuahidi kwamba atatupatia hata kiwanja. Tumemuahidi kwamba tupo tayari sasa kujenga Ofisi ya TRA katika Mji wa Kasulu. Vivyo hivyo kwa Wilaya nyingine tunaendelea taratibu, tutaanza na zile ambazo gharama zetu za kupata mapato zinakuwa ni ndogo zaidi kulinganisha na mapato. Lakini dhamira yetu ni kuwa na Ofisi ya TRA katika nchi nzima.
MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ambayo kwa kweli hayatekelezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili lilipitisha Mpango wa Miaka Mitano 2011/2012 hadi 2015/2016 na swali langu ndiko lilikoelekea, lakini kitu cha kushangaza ni kwamba, tuliamua kwamba Bunge hili shilingi bilioni 100 ziwe zinatengwa na zinatolewa kila mwaka kwa ajili ya benki hiyo kama mtaji ambapo ni shilingi bilioni 60 tu zilizotolewa katika benki hiyo kwa miaka mitano. Je, shilingi bilioni 440 ambazo hazikutolewa na Serikali hii, ziko wapi? Tunataka kujua, kama hamna huo mtaji, hiyo Benki ya Mikopo itafanyaje kazi kwa Watanzania ambao ni wakulima 98%? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nasikitika sana kuwadanganya Watanzania. Hii benki imeundwa kwa ajili ya kuinua uchumi wa wakulima wadogo wadogo. Wako wakulima zaidi ya 98% nchini. Leo tangu benki imeanzishwa imekwenda Iringa tu na kuwapa vikundi vinane tu shilingi bilioni moja: Je, kati ya zile shilingi bilioni 60, nyingine zilikwenda wapi kama ni shilingi bilioni moja tu zilitolewa kwa hao wakulima ambao ni wachache? Je, asilimia..
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kesho tunatarajia kwamba tutafanya negotiation na African Development Bank kwa ajili ya mkopo nafuu wa UA milioni 50 lakini pia UA milioni 25 ambao tunatarajia kwamba utakuwa ni mkopo nafuu ambao Serikali ita-own land TADB kwa ajili ya kuboresha mtaji wa benki hiyo iweze kuendelea kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha zote hizo zile 50 za kwanza ni takriban shilingi bilioni 150 na hizi nyingine ni takriban shilingi bilioni 75. Kwa hiyo, Serikali inafanya jitihada ya dhati kabisa kuongeza mtaji wa TADB.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; niseme tu kwamba, Benki hii imetoa mikopo kwa vikundi mbalimbali zaidi ya hivyo ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amevieleza, Mheshimiwa Rose Sukum naweza nikakupatia orodha ya vijiji ambavyo vimepatiwa jumla ya bilioni 5.9 kwa Mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga hadi hivi sasa na naweza nikatoa hii taarifa ya mikopo iliyotolewa hadi kufikia tarehe 31 Oktoba.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kulingana na majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba, hivi karibuni tutapata mikopo kutoka Benki ya Dunia na sehemu mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha kuwa na unafuu, niseme tu kwamba, Benki hii ya TADB kwanza iko kwenye Kanda, kwa mfano katika Kanda ya Ziwa iko Mwanza. Wakulima kwenda mpaka Mwanza kufuatilia mkopo huu kwa kweli inakuwa ni tabu na wanatumia gharama kubwa.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati iweze kuhakikisha Benki hii inafika mpaka vijijini au kwenye Makao Makuu ya Wilaya ili kuwawezesha wananchi wengi kufaidika?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu niseme kwamba Serikali inaona umuhimu wa kupeleka huduma za benki hii kutoka kwenye Kanda mpaka katika ngazi za chini zaidi na ndiyo dhamira ya Serikali, lakini ni vema twende taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kwanza ambayo inafanywa na Serikali sasa hivi ni kuiongezea mtaji benki hiyo, kazi ya pili ambayo sikuisema mwanzo ni kuimarisha Management ya TADB yenyewe ili iweze kufanya kazi hiyo, yote mawili yakifanyika kwa pamoja hakika tutahakikisha kwamba benki hiyo inajitanua mpaka katika ngazi husika kuwafikia wananchi.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Dhamira ya Benki ya Kilimo ni kuwasaidia wakulima wadogowadogo, lakini kwa muda mrefu wanaokopa katika benki hii wengi ni wakulima wakubwa ambao pia wanakopesheka katika mabenki mengine.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itahakikisha benki hii inawanufaisha wakulima wadogowadogo ambao wengi wako vijijini na si wale wakulima wakubwa ambao wanaweza kukopesheka katika mabenki mengine?
ambao wanasemwa ni wakubwa ambao wanakopeshwa na Benki ya Kilimo, benki hii imewakopesha wakulima wadogowadogo katika mikoa ambayo nimeitaja katika vikundi. Mpaka sasa katika hiyo mikoa niliyotaja, vimekopeshwa vikundi 89 ambavyo vina wakulima wadogowadogo 21,526 na hawa wanaokopeshwa wanakopeshwa mikopo midogomidogo kutegemea, wengine wanapata mikopo miaka miwili, wengine miwili mpaka mitano na wengine mitano mpaka 15. Kwa hiyo, si kweli kwamba benki hii imekuwa inakopesha wakulima wakubwa tu. Tunawakopesha pia vikundi vya wakulima wadogowadogo.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, katika majibu ambayo Naibu Waziri ameyajibu amesema kwamba Benki Kuu haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya dhahabu. Nadhani swali la msingi hapa ni kuweka akiba (reserve) kama dhahabu, siyo kufanya biashara ya dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, Waziri atakuwa anakumbuka huko nyuma Tanzania ilikuwa inaweka reserve hii kwenye dhahabu. Kwa hiyo, uzoefu wa kuweka hivyo tunao na swali la msingi hapa ni kwamba kwa nini tusitumie na baadhi ya migodi tunaimiliki wenyewe, tusitumie sehemu ya uzalishaji kutunza kwa sababu bei ya dhahabu hata iwe nini bado huwa ni stable zaidi kuliko bei ya dola au fedha zingine za kigeni ambazo tunawekea akiba zetu.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Na baadae imepanda.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kuhusu uwezo wa Benki Kuu ya Tanzania ni kweli miaka ya 1980 tulikuwa na utaratibu huo lakini tulipigwa kweli, maana wakati ule bei ya dhahabu iliporomoka kutoka dola za Kimarekani 700 kwa ounce zikaporomoka chini mpaka kufikia dola 235 kwa ounce moja. Hiyo ndiyo ilifanya Serikali iamue kuuza hata ile dhahabu iliyobaki baada ya kupata hasara kubwa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Baadae imepanda ni sawa.
Lakini sasa uzoefu tunaouzungumzia ni pamoja na uwezo wenyewe wa pale Benki Kuu kusema hii ni dhahabu kweli na hii siyo…
Waheshimiwa Wabunge, tuelewane Mheshimiwa Spika amenipa nafasi.
Kwa hiyo, ni muhimu sana ule uwezo wenyewe uweze kujengwa ndani ya Benki Kuu, siyo tu kuitambua ile dhahabu yenyewe iliyo halali na sivyo, lakini na biashara yenyewe na kufuatilia mwenendo unavyoenenda duniani.
Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ni kwamba Serikali inalifanyia kazi ili kuangalia tena uwezekano wa kuweka akiba yetu katika dhahabu au madini mengine ya vito ambayo tunayo hapa nchini.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa suala hili linahusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, nilitaka kujua je, wastaafu wa Afrika Mashariki wa nchi nyingine walishalipwa lakini Tanzania imekuwa inasuasua na kuna sintofahamu wakati ambapo wengine wanasema wameshalipwa, bado tunatambua kuna wastaafu wengi wa Tanzania hawajalipwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka tamko la Serikali, je, wastaafu hao ni kweli wamelipwa wote na kama bado kuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wastaafu wao au warithi wao wanapata fedha zao? Ahsante.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu hao wamelipwa na kama kuna madai zaidi wayawasilishe Serikalini tutayashughulikia kwa mujibu wa taratibu.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wafanyabishara wengi wetu ni wadogo na wa kati na wengi wao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mitaji. Je, Serikali ina mkakati gani ya kuhakikisha taarifa ya fursa hii inawafikia? Lakini pia katika mwaka uliopita trend ya mauzo ya hisa katika soko letu la hisa la Dar es Salaam linaonyesha kushuka, na share nyingi ambazo zilizokuwa traded pia price zake zimeshuka. Je, ni nini mkakati wa Serikali katika kutatua changamoto hii?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa maana ya mkakati, kikubwa ni elimu kwa umma. Kwa kweli soko hili watu wengi hawalielewi, na tumeendelea kusisitiza kwamba Capital Market and Securities Authority na DSE wenyewe waongeze jitihada katika kutoa elimu kwa umma. Lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema katika jibu langu la msingi nao pia wachangie kutoa elimu, kwa kweli kuna fursa kubwa katika kuiongezea mitaji makampuni mbalimbali kwa wananchi wetu kununua hisa katika makampuni hayo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli trend inashuka lakini kilicho kikubwa kama nilivyosema ni kwa sababu ya uelewa mdogo na kwa hiyo, Serikali inafanya jitihada kupitia taasisi hizi kuongeza elimu kwa umma na fursa hizi zitaongezeka katika siku zijazo ndio matumaini ya Serikali.
MHE. FRANK MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio mimi, naitwa Frank George Mwakajoka. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa kipindi hiki cha miaka miwili kumekuwa na tatizo kubwa sana la malalamiko ya wafanyabiashara katika nchi hii na wafanyabiashara wengi sana wamekuwa wakifunga biashara zao, wafanyabiashara wa maduka pamoja wafanyabiashara wa hoteli, lakini pia wawekezaji wa kutoka nje, wamekuwa wakifunga shughuli zao na kuondoka. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaendelea kuwekeza katika nchi yetu?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba katika biashara yoyote ile kuna kupanda na kushuka. Kwa hiyo pamoja na kuwa tumeona kwamba baadhi ya biashara zimefungwa lakini ni ukweli pia kwamba baadhi ya biashara nyingine zimechipuka, hilo ni la kwanza. Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili mkakati wa Serikali ni kuendelea kuzungumza na wafanyabishara ili kuelewa changamoto ambazo zinawakabili, na zile ambazo zinahusu Serikali tutazitatua.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Waziri ametueleza kwamba shida kwenye kuwekeza hisa iko kwenye elimu kwa umma; na kwa kuwa ametutajia kwamba wanaonufaika na lile dirisha dogo zaidi ni makampuni. Nilikuwa naomba kuuliza kwa kuwa wengi wa wajasiriamali ni wadogo wadogo wakiwepo wale wamama wa Kilimanjaro na mpaka sasa elimu ya hisa inatoka tu labda kutokea Benki ya CRDB kupitia matawi yake, ni lini sasa mabenki mengine yaliyotajwa pamoja na TOL, TCC, NMB watatoa elimu ya hisa kupitia matawi yao yaliyo huko mikoani?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sikusikia vizuri jina la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza haya mashirika na taasisi ambazo nimezitaja, linalonufaika na dirisha dogo, mashirika haya, hisa zao zile wao ndio wanapopata faida wanawagawia wanahisa wao. Kwa hiyo, wananchi wadogo wadogo wananufaika kupitia hizo taasisi ambazo zinanufaika na hilo dirisha dogo. Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa swali dogo la pili nitumie nafasi hii kuyashauri mashirika yote yanayohusika na benki hizi kuongeza elimu katika matawi mbalimbali ili wananchi waweze kupata elimu na kunufaika na hilo dirisha.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hata hivyo, nieleze masikitiko yangu tu kwamba eti unapata majibu ya Serikali, yanakwambia Mpango wa Serikali kuliwezesha Bunge kufanya shughuli zake kwa ufanisi ni kutoa
fedha toka Mfuko Mkuu wa Serikali kupeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Bunge, Fungu 42 eti huo ndiyo mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sijaridhika na
majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu najua sisi wote hapa katika Bunge hili ni mashahidi, majukumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu na nyeti sana kuliko hiki ambacho Serikali inataka kutuambia kwamba
mpango wake ni kutoa fedha Mfuko Mkuu wa Serikali na kupeleka Mfuko wa Bunge. Ninyi wote ni mashahidi kwamba kwa mujibu wa kanuni, muda wa Kamati za kuelekea bajeti ni wiki tatu lakini this time wiki moja imeondoshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali langu la msingi nilichouliza ni kwamba, muda wa uendeshaji wa shughuli za Bunge umepunguzwa mno kiasi cha kufikia siku 10 hadi 12, lakini hata muda wanaopewa Mawaziri kujibu hoja za Wabunge na wananchi wa Tanzania nao
umepunguzwa kufikia kiasi cha dakika tano. Kwa hiyo, hatutekelezi wajibu wetu kama Bunge kwa sababu tunakimbizana na muda ingawa hili la muda naona halikuzingatiwa, lakini bado hoja ya bajeti mpaka mweziwa Pili mmetupa asilimia 68, tu kwa hiyo bado hata hilo ambalo mlifikiri ni kazi rahisi tu kutoa Mfuko wa Serikali kuweka
Mfuko wa Bunge bado hamjatoa kiasi kinachokidhi, bado mnatusafirisha kwenye Hiace, bado…
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa binafsi yangu, naomba nielezwe kabisa straight forward kama hili ndiyo jibu la Serikali basi swali hili halijajibiwa
naomba lijibiwe.
..
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza:-
La kwanza; kwa kuwa wapo watu wanaokopesha
kienyeji na hutoza riba kubwa inayofikia asilimia 30 kwa mwezi na inapotokea mkopaji akakosa kulipa maana yake mwezi unaohusika gharama hiyo hupanda kwa maana ya compound interest kwamba mtaji pamoja na asilimia iliyopaswa kutozwa hufuata kwa mwezi mwingine na hali
hii huacha wananchi katika hali ngumu sana. Je, Serikali inawajua vizuri hawa watu na ina mpango gani wa kutafuta njia ya kuimaliza kadhia hii? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa watumishi ndiyo walengwa
wakuu katika jambo hili pamoja na wastaafu ambao wako karibu kustaafu na kadhia hii huwafanya wapoteze hata ufanisi kazini; je, Serikali haioni umuhimu wa kulichukulia hili
jambo kama vita ya madawa ya kulevya kwa sababu watumishi wengi wanastaafu wakiwa hawana kitu chochote na familia zao zinasambaratika?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, ni kweli kabisa riba hizi kwa hawa wakopeshaji wa mitaani ni mzigo mkubwa kwa wale wanaolazimika kwenda kukopa huko
na ndiyo maana Serikali imekuwa inasisitiza kwamba kadri inavyowezekana wasiende huko, lakini jibu langu la msingi ni kwamba; sasa hivi Serikali tunafanya jitihada kubwa na tayari tumeshaandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri ili jambo hili baada ya kulifanyia kazi kwa mapana yake liweze kushughulikiwa kwa ukamilifu na maagizo maalum ya Serikali baada ya kuwa waraka huu umepitiwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lile la kusema kwamba
tuichukulie kama vita nafikiri tusiende huko kwa sasa kwa sababu waraka umeandaliwa, ni vizuri tupate nafasi ya kulichukulia maamuzi tukiwa tumetulia. Ahsante.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutupa moyo na kutuhakikishia kuwa tayari mikakati ya kutuwekea kituo cha forodha iko njiani. Hata hivyo, nataka vilevile nimtake
Mheshimiwa Waziri na Serikali kuharakisha mipango hiyo kwa sababu hivyo vituo vya jirani anavyovizungumza bila shaka anazungumzia Kasumulo iliyopo Kyela, anazungumzia Tunduma ambavyo vyote viko mbali sana na Ileje na Ileje
kama inavyofahamika hakuna barabara hata moja
inayopitika vizuri, kwa hiyo kutuambia sisi twende tukatumie vituo vile ni kama kutudhihaki. Pamoja na hayo, tayari ardhi imeshaanza kupimwa na inamaliziwa, tayari maeneo yameshaainishwa, tayari wahusika wameshakuja kukagua maeneo, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri anihakikishie
kuwa sasa hatua itakayofuata ni ujenzi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Malawi; Malawi
tayari wana kituo, wanatungojea sisi. Miundombinu yetu sisi ndiyo inachelewesha kile kituo cha Malawi kushirikiana na cha kwetu. Kwa hiyo, naomba sana hilo lifahamike na
atuhakikishie hapa ni lini sasa hatua hizo zitafanyika? Ahsante sana.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje kwamba maoni yake yatazingatiwa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika jambo ambalo wanafunzi wetu wanahimizwa sasa hivi ni kuondokana na dhana kwamba elimu yao ni kwa ajili ya kujipatia ajira rasmi Serikalini na hivyo waingie katika mtazamo kwamba elimu itawasaidia kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muktadha huo, benki ni chombo muhimu sana cha kuwasaidia vijana wetu wanapomaliza shule kuweza kukopa ili kufanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo linalowakwamisha ni dhamana. Vijana wetu wanaambiwa wapeleke hati za mashamba, majumba na vyombo visivyohamishika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaiagiza Benki Kuu iweze kurekebisha sheria zake ili kuwasaidia vijana hawa wanaomaliza vyuo vikuu waweze hata kutumia vyeti vyao kama dhamana kwa ajili ya kukopa ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kuwasaidia katika maisha yao? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana. La kwanza, ni muhimu sana kutambua kwamba benki zetu zinafanya biashara. Ni lazima benki hizi zipate faida kama mfanyabiashara yeyote ili shughuli za benki hizi ziweze kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba vijana wetu walioko shuleni wanakwamishwa na baadhi ya masharti ya mabenki yetu ikiwemo hili la dhamana ambalo Mheshimiwa Selasini anasema, lakini tumeanza kupiga hatua kuelekea huko ambako tunataka kwenda. Mathalani, vijana walioko Igunga walipomaliza masomo yao Chuo Kikuu cha Sokoine, kitu cha kwanza walijiunga pamoja wakaunda kikundi wakakiandikisha na wakaanza shughuli yao katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya CRDB ni moja ya benki ambayo ilijitokeza na kuwakopesha kufanya shughuli zao. Kwa hiyo, pole pole tunakwenda kuangalia, ni vyombo gani ambavyo vinaweza vikatumika kama dhamana kulinda mabenki yetu yasipate hasara, lakini wakati huo huo kuwawezesha vijana wetu waweze kupata mikopo. Kwa hiyo, hilo ni moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni muhimu sana niendelee kusisitiza kwamba vyombo hivi sisi wenyewe tunao mchango. Mara nyingi baadhi ya wakopaji wanakuwa na historia mbaya, hawalipi. Sasa wasipolipa maana yake ni kwamba zile benki nazo zitapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu nao wakopaji wakalinda ile credibility yao, ndio, maana tulianzisha Credit Reference Bureau kuhakikisha kwamba wakopaji wanakuwa na historia ya ukopaji. Wale ambao wana rekodi nzuri vyombo vyetu vya fedha viko tayari kuwakopesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko benki ambazo sasa hivi zimeanza hata kutoa mikopo kwa watu wasio na dhamana. Zipo benki ambazo zinakopesha kwa mfano vikundi vya akina mama, ikiwemo CRDB na NMB, vikundi vya walemavu, bila dhamana lakini sharti ni kwamba kiwepo kile kikundi credible kimeandikishwa ili fedha zinazokopeshwa zisipotee. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 1998/1999, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Katiba ya Sheria na Utawala, Serikali iliamua TRA ijaribu kukusanya kodi ya majengo na walianzia na Halmashauri za Manispaa tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni. Baadaye walishindwa, Serikali ikarudisha tena kodi hizo zikusanywe na Manispaa hizo. Sasa ni sababu gani za msingi tena Serikali imeamua kodi ya majengo ikusanywe na TRA na siyo Halmashauri zenyewe? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sababu ya msingi kwa nini Serikali ilifanya maamuzi kwamba sasa kodi hii ianze kukusanywa na Mamlaka ya Mapato, kwanza, niseme Mamlaka ya Mapato kazi yake ni kukusanya mapato yote wala siyo ya kodi peke yake.
Pili, tuliona udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato katika ngazi ile na ndiyo maana lengo la Serikali ni kusema tutumie chombo ambacho kina wataalam waliobobea kwa ajili ya kukusanya mapato haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili la kusema huko nyuma walishindwa kwani ukishindwa maana yake ndiyo basi tena. Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje tumepata uzoefu, tumejifunza kutokana na uzoefu, tumefanya maandalizi ya kutosha na tuna hakika awamu hii tutaikusanya kodi hii ipasavyo. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, msingi mkubwa wa Serikali iliyopo madarakani unatokana na ridhaa ya wananchi, lakini hali ya maisha ya wananchi wetu ni duni, mzunguko wa fedha ni mdogo sana, wananchi wanalalamika sana kwamba fedha imepotea/haipo mtaani na kasi ya ongezeko la maisha magumu imekuwa kubwa kupita kiasi. Kwa muda mrefu sana Serikali hii imekuwa ikijisifia wanakusanya zaidi lakini hali ya uchumi wa wananchi wetu imekuwa mbaya sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri atuambie leo fedha ambazo zilikuwa zinaonekana kwa muda mrefu katika mzunguko mtaani sasa ziko wapi na wana mkakati gani wa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema kwamba mwaka huu 2017 mnataka kujitathmini wenyewe, katika kujitathmini wenyewe mtaandika kweli? Kwanza mambo yafuatayo, haki ya kupata habari kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba yetu, Bunge haliko live, mikutano ya hadhara imepigwa marufuku…

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, swali sasa linakuja, kwa kuwa Bunge haliko live, mikutano ya hadhara imepigwa marufuku, katika kujitathmini wenyewe mtaandika kweli haya au kuna haja ya kutafuta chombo kingine huru APRM Number Two ili iandike uhalisia kwa sababu mambo kama haya kweli mtaandika wenyewe? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kwanza nalitaka nimuombe Mheshimiwa Masoud avute subira kidogo. Leo nitapata fursa ya kueleza kwa kirefu hali ya uchumi ambayo ni pamoja na masuala ya maisha magumu, mzunguko wa fedha, fedha imekwenda wapi, kwa hiyo, namuomba avute subira tu kidogo, asubuhi hii na mchana leo.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu kujitathmini, kila robo mwaka Serikali inajitathmini katika vigezo mbalimbali, kila robo mwaka, kila nusu mwaka na kila baada ya mwaka mzima. Taarifa zipo, ukienda kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha taarifa zipo, tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango taarifa zipo na sasa hivi mmeanza kugawiwa vitabu ambavyo vinatoa tathmini.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, katika ngazi ya Afrika Mashariki tunajitathmini ili kuweza kujua kama kweli tunaelekea kwenye vigezo ambavyo tulikubaliana tunapokwenda kwenye Umoja wa Shirika la Fedha. Kwa hiyo, tuna convergence criteria ambazo tunazitathmini nchi baada ya nchi na tunakwenda vizuri. Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo kwenye macro-economic convergence criteria tuko vizuri. Nikuhakikishie tu kwamba hizi taarifa ziko wazi na hakuna mahali popote zitaminywa. (Makofi)
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Naishukuru Serikali kwa majibu yao mazuri kabisa, sina wasiwasi na majibu kwani mmejibu vizuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa inavyoonekana future transport logistic kati ya Tanzania na Burundi itapitia Manyovu. Ameonesha kabisa kwamba Dar- es-Salaam – Kabanga ni kilometa 1330 na Dar-es-Salaam – Tabora – Manyovu ni 1273, kwa hiyo, katika mpango wetu wa Blueprint na Easy of Doing Business inaonesha kwamba siku za mbele wafanyabiashara watapitia Manyovu kupitia Tabora. Kwa kuwa iko hivyo, ni maandalizi gani sasa mmeyafanya kwa ajili ya kupokea biashara hiyo? Najua Serikali mtaendelea kujitahidi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa, amesema kuna changamoto ya barabara kwa ajili ya kurahisisha biashara kwenda Burundi. Je, Wizara ya Ujenzi ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hivi vipande vya barabara vinaisha haraka?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kitu cha kwanza Mheshimiwa Obama anawatetea kweli ndugu zetu kule, napenda tu nimjulishe kwamba katika utaratibu wa ujenzi wa barabara ambayo inatoka Burundi - Manyovu – Kasulu - Nyakanazi, moja ya vipengele vya barabara ile baadhi ya huduma ambazo zitajengwa kwa fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika ni pamoja na kujenga Kituo cha Pamoja cha Forodha pale Manyovu ambacho kwa hakika itakuwa ni mkombozi wa kuharakisha biashara kati ya Tanzania na Burundi.

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa upande wa Wizara ya Ujenzi pamoja na sisi kama Wizara ya Fedha karibu tumekamilisha jitihada za kupata fedha za kukamilisha vile vipande ambavyo vimebaki vya barabara ambayo inatoka Manyoni - Tabora - Kigoma. Fedha zimekwishapatikana, tunakamilisha taratibu za ujenzi kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi. Ahsante.