Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (41 total)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanywa na Manispaa ya Mpanda ni dhamira chanya ya kuthubutu, lakini ujenzi wa chuo nafahamu ni kazi kubwa. Je, ni kwa nini Serikali Kuu isiungane na Manispaa hii, kwa maana ya kulichukua zoezi zima la ujenzi huo wa Chuo Kikuu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi nikizingatia kwamba tunapozungumzia habari ya kuifungua mikoa ya pembezoni katika maeneo ya barabara na kilimo, huwezi ukaacha kuifungua mikoa hiyo kwa maana ya eneo hili la elimu. Elimu ndiyo chanzo cha mambo mengine yote. Je, Serikali haioni kwamba wakati umefika wa zoezi hili ikalichukua? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunaposema Manispaa ikaliweke wazi suala hili…
MWENYEKITI: Kwa kifupi, tafadhali!
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Zoezi hili lilichukuliwa na Bodi. Baadhi ya watendaji waliokuwa kwenye Bodi, Serikali hii hii imewahamishia maeneo mengine kwenda kufanya utumishi. Je, ni kwa nini Serikali isije na hatua za makusudi kuhakikisha nyaraka muhimu zimerudishwa katika Manispaa ya Mpanda ili Manispaa ya Mpanda iweze kuendelea na mchakato mwingine ikiwa ni pamoja na fidia kwa watu waliotenga eneo lao?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Ufundi, ningependa kumjibu Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-
Kwanza kuhusu sababu ni kwa nini Serikali isichukue ujenzi huu, ningependa kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba swali lake la msingi, lilikuwa ni lini ujenzi utaanza. Ujenzi huu ulikuwa ni mchakato ambao Manispaa, ilikuwa imeomba ijenge na Wizara yangu ilikuwa kazi yake ni kutoa support ambapo TCU ilipitia kulingana na mchakato. Kwa hiyo, naona kama anachokisema ni swali jipya ambalo haliendani na swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwamba kuna baadhi ya wajumbe walihamishwa na wameondoka na nyaraka, huo sio utaratibu. Taratibu ni kwamba mtumishi anapohama nyaraka za Serikali zinatakiwa zibaki mahali husika. Kwa hiyo, bado naiomba Halmashauri kama kuna watumishi wanapopata uhamisho wanahama na nyaraka za Serikali ni kinyume cha utaratibu na Halmashauri inatakiwa kuchukua hatua husika.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake kimesema kwamba shule ni bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuyaachia matokeo ya wanafunzi ambao wanadaiwa na NECTA kwa sasa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa hoja yake, niseme kwamba hilo suala tumelipokea, tutalifanyia kazi, halafu tutakuja kutoa majibu
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na matatizo makubwa ambayo wanayo Walimu na nia ya Serikali kuyatatua ipo kada nyingine ambayo ni kama inasahaulika na hii ni kada ya Wakaguzi wa Elimu. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba kada hii nayo inatazamwa ili kwa pamoja na kwa kushirikiana na walimu waweze kusaidiana katika kuboresha elimu ya watoto wetu katika nchi yetu?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali tayari imeshaanza mkakati wa kuboresha ukaguzi wa shule na sasa hivi hata kuna muundo mpya wa wakaguzi, ambapo hata jina la ukaguzi limebadilishwa, wanaitwa Wathibiti wa Ubora wa Elimu, na yote hii ni katika lengo la kuhakikisha kwamba tunaimarisha zaidi ukaguzi wa shule kwa kuangalia wakaguzi wanavyoweza kufanya kazi zao kwa kufanisi zaidi. Ukaguzi umeimarishwa mpaka katika ngazi za Wilaya, na huu muundo unaendana pia na maslahi bora kwa wakaguzi. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la ubora wa elimu ni muhimu kusimamiwa na Wizara ya Elimu yenyewe; je, Serikali inasemaje kuhusu kuimarisha macho yake ambayo ni ukaguzi ili ijue kinachoendelea katika shule hizo ambazo naona mimi pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kugatua madaraka, lakini kule chini kumezidiwa, mmewapelekea kazi kubwa.
Je, Serikali ipo tayari kuimarisha ukaguzi kwa kuifanya iwe SU yaani chombo kinachojitegemea ili kifanye kazi kikamilifu?
(b) Serikali inasemaje kuhusu hizi shule maalum; inazisimamiaje baada ya kugatua madaraka? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kuhusu Serikali kuboresha ukaguzi, hilo suala la kuboresha ukaguzi ni dhamira ya Serikali kwa sababu tunatambua kwamba wakaguzi ndio jicho letu, ndio wanaotuwezesha kubaini changamoto zilizopo na utaona hata katika bajeti yetu kuna mambo mengi ambayo tumefanya ya kuboresha ukaguzi. Sasa suala la kufanya ukaguzi uwe ni wakala hilo suala tunaliangalia na kuona kwamba je, kuna changamoto gani katika muundo uliopo na kama Serikali itaona kuna umuhimu wa kubadilisha mfumo hakuna tatizo lolote kwa sababu lengo letu sisi ni kuhakikisha kwamba ukaguzi unafanya kazi yake kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la shule za wanafunzi wenye vipaji maalum, kama alivyojibu Mheshimiwa Jafo kama Serikali tunafanya kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, usimamizi wa shule upo kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI lakini bado Wizara yangu inahusika katika kuangalia ubora kinachoendelea shuleni na kuhakikisha kwamba mitaala inafundishwa kama inavyokusudiwa. Kwa hiyo, bado Wizara ya Elimu ina shirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kwamba hizi shule zenye vipaji maalum zinaendelea kufanya vizuri.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa majibu ya Serikali yanaeleza wazi kuwa kufaulu kwa mtoto kunategemea mwanafunzi mwenyewe, Mwalimu, mazingira ya kufundishia pamoja na wazazi. Sasa, je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba mazingira ya kufundisha na kufundishia yanakuwa bora na pia kutoa elimu bora kwa wazazi kwamba wao ni wajibu wao pia kuwasimamia watoto wao?
Swali la pili, kwa kuwa hakuna Mwalimu anayefanya kazi kubwa kama Mwalimu ya KKK wa darasa la kwanza na la pili kwani yeye ndiye anayetoa msingi wa elimu au mwelekeo wa mtoto wa maendeleo yake ya baadaye. Je, Serikali imejipanga vipi kuwapa motisha Walimu wa KKK kutokana na kazi kubwa wanayoifanya?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi kwa ufuatiliaji mzuri. Anawajali sana Walimu na ndiyo maana maswali yake kila siku yanalenga katika kuangalia Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na ndiyo maana katika majibu yangu ya msingi nimeeleza kabisa kwamba, Serikali imekuwa inatoa mafunzo kwa walimu kazini na tumetoa mafunzo kwa walimu 22,697 kwa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, hii yote ni katika kujenga mazingira mazuri na kumwezesha mwalimu. Vilevile Serikali imeandaa vitabu na iko inasambaza vitabu katika kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwamba Serikali inafanya nini ili wazazi waweze kutambua wajibu wao. Serikali imekuwa ikihamasisha wazazi na ndiyo maana hata kupitia Bunge lako naomba pia Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika maeneo yenu tuhamasishe wazazi ili watambue kwamba elimu ndiyo kila kitu katika maisha ya watoto wao na hivyo Serikali itaendelea kutoa uhamasishaji kwa wazazi ili waendelee kutambua wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la mwisho la nyongeza anauliza kwamba, Serikali imejipanga vipi kutoa motisha kwa walimu wa darasa la kwanza na la pili ambao wanakuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha watoto. Serikali inatambua mchango wa walimu na ndiyo maana nasema ukiangalia vipaumbele vyetu katika mafunzo kwa Walimu kazini tumejikita zaidi kwa Walimu hao kwa sababu tunatambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nitumie nafasi hii kusema kwamba tunakusudia na kesho nitasimama hapa mbele yenu kueleza mipango yetu ijayo lakini tunakusudia kuweka utaratibu wa kuweza pia kuwatambua Walimu wa darasa la kwanza na la pili wanaofanya vizuri kwa sababu tumekuwa na utamaduni wa kuwatambua kwenye darasa la saba, kidato cha nne, lakini tunaweka utaratibu mahsusi wa kuweza pia kuwatambua kwa sababu nayo pia ni motisha.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na uwepo wa Tume ya Vyuo Vikuu yaani TCU (Tanzania Commission for Universities), lakini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya kuzalisha wahitimu wasiokuwa na uwezo wa kutosha katika mustakabali wa ujenzi wa uchumi wa nchi ya Tanzania. Swali, je, Serikali imejipangaje katika suala zima la kuzalisha wahitimu wenye uwezo, weledi wenye tija na maarifa kazini? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali imejipanga vizuri kabisa kuhakikisha kwamba watu wasiokuwa na uwezo wanachukuliwa hatua stahiki na katika hili niseme tu wazi kwamba, Serikali itafanya uhakiki wa wanafunzi au tunaangalia upya vigezo vya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu ili tuweze kuchukua hatua mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kesho nitakuwa nawasilisha hotuba yangu, haya yote nitayaeleza kwa kina, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Ester upokee hili jibu lakini tumejipanga vizuri na mikakati yote nitakuja kuieleza hapa kesho.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, suala hili ni nyeti na linagubikwa na mambo mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo imani mbalimbali za kidini, mila na desturi. Je, ni lini sasa White Paper hiyo itapitishwa katika makundi mbalimbali ya jamii, ili iweze kupata maoni yake mbalimbali na kuweza kutungwa Sheria inayoweza kumlinda mtoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili; chini ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuwa, mpaka sasa hivi elimu yetu ya mpaka sekondari ni bure. Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu wa kuongeza elimu ya kidato cha bure ikawa mpaka form six ambayo ni elimu ya lazima, ili tuweze kuvuka ule umri wa miaka 18 ukizingatia sasa hivi watoto wameanza kusoma wakiwa chini ya miaka minne mpaka mitano? Je, Serikali inasema nini kuhusiana na hilo?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru kwa swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge, napenda kumjibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba, kila safari tunaanza kwa hatua kwa hiyo, Serikali imeanza kutoa elimu bure na hatua ya kwanza tumeanza na elimu msingi mpaka kidato cha nne. Kuna changamoto ambazo zinajitokeza katika kutekeleza hii, kwa hiyo, tupate nafasi tutatue changamoto, lakini mawazo na mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge ni jambo la msingi ambalo Serikali italiangalia baada ya kuwa tumeweka vizuri hii ambayo tumeanza nayo kwa awamu ya kwanza.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imetangaza kwamba nchi yetu sasa masomo ya sayansi ni lazima kwa wanafunzi wetu; lakini hakuna maandalizi ambayo yamefanyika mpaka sasa, hatuna walimu hao kabisa. Nitolee mfano katika Jimbo langu la Babati Mjini, walimu wa mathematics katika shule kumi za sekondari, ni shule moja tu ndiyo ina mwalimu wa hesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu, Serikali haioni kwamba inawachanganya wananchi wa Tanzania katika kutoa kauli zao wakati hawajajiandaa kukabiliana na tatizo hilo? Ni lini wanaajiri walimu hao wa sayansi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba wanafunzi kusoma sayansi kama somo la lazima halijaanza, lakini Serikali iko katika maandalizi. Hatua muhimu ambayo imefanyika ni kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na maabara ambapo hizi maabara tunashukuru kwamba zimejengwa kwa ushirikiano na wananchi hatua inayofuata, sasa hivi Serikali ipo katika utaratibu wa kuhakikisha kwamba maabara zote za sayansi zilizojengwa kwenye shule za sekondari zinakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali wa kwamba masomo ya sayansi yatakuwa ni ya lazima, unaendana sambamba na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambapo elimu inakuwa ya msingi kwamba wanafunzi wanasoma kuanzia msingi mpaka sekondari. Kwa hiyo, Serikali bado ipo katika maandalizi ya kuhakikisha kwamba inatengeneza mazingira mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mafunzo kwa Walimu ni kwamba sasa hivi kuna vyuo 10 ambavyo tumeviangalia na tunaviimarisha maabara zake ili ziweze kutoa mafunzo zaidi kwa masomo ya sayansi. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba sasa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, ni lini sasa Serikali itaanza kutekeleza kwa vitendo, Waraka namba tatu (3) wa mwaka 2014 unaoelekeza kwamba kutakuwa na posho ya madaraka kwa ajili ya Walimu Wakuu wa shule za Msingi, Walimu wa Sekondari, Waratibu wa Elimu wa Kata na Wakuu wa Vyuo? Sasa utekelezaji wake utaanza lini maana ni mwaka wa pili sasa unakwenda?
Mheshiminiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza; kwa kuwa umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari hapa nchini maarufu kwa jina la TAHOSSA ulikuwa ukitumia sehemu za michango, kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo pamoja na kufanyisha mitihani ya mock na ujirani mwema ambao ililenga sana kuimarisha na kuboresha taaluma. Sasa, kwa kuwa tunaenda na mpango wa elimu bila malipo, je, Serikali iko tayari kuisaidia ruzuku TAHOSSA ili iendelee kufanya kazi zake kwa ufanisi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu suala la utekelezaji wa waraka namba tatu wa posho ya madaraka. Hili ni swali jipya halina uhusiano na swali la msingi kwa hiyo majibu yake yataandaliwa na kuletwa katika kipindi kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la TAHOSSA ambalo linaendana na utekelezaji wa Sera ya Elimu Msingi ya Mwaka 2014, ni kwamba katika mwongozo waraka namba sita umebainisha wazi mgawanyo wa fedha na hivyo basi kama kuna mahitaji yanayohusiana na mitihani, fedha zinazotolewa kwa ajili ya elimu bure kuna kipengele cha mitihani. Kwa hiyo, napenda kuchukua nafasi hii kusisitiza kwamba matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya elimu msingi yazingatie mwongozo uliotolewa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua elimu shirikishi kuhusiana na wanafunzi wenye uhitaji maalum, kwa sababu shule yetu ya Lugalo iliyopo katika Mkoa wa Iringa ina wanafunzi ambao wana uhitaji maalum, lakini utakuta hawa wanafunzi hawana vifaa vya kujifunzia wala Walimu hawana vifaa vya kuwafundishia. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na hilo?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na elimu shirikishi na changamoto za elimu maalum, nadhani nimeeleza wazi dhamira ya Serikali ya kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Ritta Kabati pengine anaona mikakati ambayo tumeiweka kwenye bajeti haitaweza kuondoa changamoto mahususi, ambazo ziko kwenye shule katika eneo lake, nimhakikishie kwamba, niko tayari kuongozana naye ili nione matatizo halisi ili tuweze kuyatatua, kwa sababu hiyo ndiyo dhamira ya Serikali.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wanafunzi hawa wa awali pia ni elimu ambayo ni msingi na sehemu nyingi wamekuwa wakifundishwa na Walimu waliosomea kufundisha wanafunzi wa shule za msingi na kuna baadhi ya maeneo wamekuwa wakifundishwa na Walimu ambao hawajapata mafunzo. Sasa kwa kuwa tuna chuo ambacho kinatoa Walimu, au tuna vyuo ambavyo vinatoa Walimu wa shule za awali, ni kwa nini Serikali isiajiri Walimu wa shule za awali katika shule zote nchini ili waweze kufundisha vizuri kwa sababu hawa wana mafunzo maalum kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Walimu wa elimu ya awali wanahitaji kuwa na mafunzo maalum, lakini napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Walimu wote wanaofundisha shule za msingi wanakuwa na course ya lazima ambayo inahusiana na ufundishaji wa elimu ya awali. Kwa hiyo, kwa sasa hivi ambapo wale walimu ambao wamefanya kama course maalum (specialization) hawapo wa kutosha, bado Walimu wa shule za msingi wana uwezo wa kufundisha kwa sababu ni somo la lazima kila Mwalimu wa shule ya msingi lazima achukue somo la elimu ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumfahamisha Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, sasa hivi tayari Serikali imepanua wigo wa utoaji wa mafunzo ya elimu ya awali kwa Walimu na sasa hivi tuna vyuo tisa ambavyo vinatoa mafunzo na Walimu hawa watahitimu mwaka 2018, ndipo watakamilisha masomo yao.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa vile suala la elimu ya juu ni suala la Muungano na kuna watu kama sisi yaani kama mimi, wazazi, hasa wa kike tulio majumbani, huwa hatuwezi kwenda directly kusoma kwenye vyuo vikuu kwa kujiendeleza. Kwa mfano kama mimi mwenyewe nimesoma distance learning kwenye Chuo cha ICM cha Uingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa hili si tatizo kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, wenzetu hawa ambao wamesoma distance learning wanaajiriwa kwenye taasisi za muungano na Serikali kwa ujumla lakini tatizo lipo kwa upande wa Zanzibar; sisi ambao tumesoma distance learning, hasa wanawake tunaoishi majumbani tunakuwa hatuwezi kwenda vyuoni, tunaonekana kwamba vile vyeti vyetu vya distance learning si chochote isipokuwa wale ambao wamekwenda direct kusoma wanakubaliwa.
Sasa je, kwa nini Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazikai pamoja zikakubaliana mfumo ulio bora ili na sisi wazazi hasa wa kike wa Zanzibar tuweze kujiendeleza kimasomo kupitia distance learning?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Niseme tu kwamba, ni kweli suala la elimu ya juu ni suala la muungano na taratibu za kujiunga na vyuo na kuhakiki watu wanaosoma nje zinafanywa na TCU. Lakini pia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina taratibu zake za ajira na ndiyo maana kabla ya kuajiri wana taratibu zao za kuhakiki vyeti. Kwa hiyo, niseme kwamba na mimi nilipokee ili kama sehemu ya masuala ambayo ni ya muungano tunakaa tunayajadili na lenyewe tuangalie kwa pamoja na Waziri mwenzangu wa Elimu wa Zanzibar ili tuangalie namna ya kulipatia ufumbuzi. Nashukuru sana.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja tu la nyongeza. Taifa lolote duniani ili lisonge mbele linahitaji watu waliosoma kada mbalimbali, iwe ni sanaa, sayansi au biashara.
Je, Serikali ina mpango gani wa ku-balance wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, pamoja na wanafunzi wanaosoma sanaa ili isitokee kama sasa tuna ziada ya wanafunzi wa sanaa zaidi ya 7,463 na inapelekea kutokuwa na ajira. Serikali ina mpango gani kwa miaka ya hivi karibuni na baadaye? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Serikali, imekuwa ikiendelea kuweka mazingira mazuri na kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi. Katika mwaka 2015 mpaka 2016 Serikali ilijikita zaidi katika kuhamasisha Shule za Sekondari kujenga maabara. Katika mwaka 2016/2017 tunasambaza vifaa vya maabara. Hizo zote ni jitihada za kuongeza wanafunzi wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba wanafunzi wanayo hiari ya kuchagua masomo. Kwa hiyo, kama Serikali tunatoa mazingira mazuri. Nangependa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kuwahamasisha wanafunzi pia kuona kwamba masomo ya sayansi na teknolojia nayo ni muhimu ili waweze kuyachukua kwa wingi zaidi. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naitwa Mashimba Mashauri Ndaki hivyo ukisema Mashauri Ndaki bado ni sawa. Niulize swali moja la nyongeza, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa, tuna chuo kizuri cha VETA pale Maswa Mjini na kwa kuwa pia, tuna Chuo cha Maendeleo ya Jamii Malampaka, wakati huu ambapo matayarisho ya kujenga Chuo cha VETA cha Mkoa yanaendelea, Je, Serikali ina mpango gani wa kuviboresha vyuo hivi viwili ili viweze kuanza kuchukua vijana wakati tunaendelea na mpango wa kujenga Chuo cha VETA mkoani?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwamba Serikali ina mpango gani wa kuviboresha vyuo vya ufundi vya Malampaka na Chuo cha Ufundi cha VETA niseme tu kwamba, Serikali itafanya mapitio ya uendeshaji wa mafunzo ya ufundi stadi nchini. Nimekuwa nikisikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge na maswali ambayo wamekuwa wakiuliza kuhusiana na suala la mafunzo ya ufundi stadi VETA ni kwamba, Wizara ya Elimu inaona kuna umuhimu wa kufanya tathmini ya mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa katika vyuo vyote nchini kwa lengo la kuangalia upya aina ya mafunzo yanayotolewa, kuangalia teknolojia inayotumika, na niseme tu kwamba hili ni zoezi ambalo baada tu ya kufunga Bunge lako hiyo ndiyo kazi agenda namba moja ambayo tutafanya tathmini kwa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikiwasikiliza sana Waheshimiwa Wabunge michango yao mizuri na maswali yao kuhusiana na VETA wamekuwa pia wanahoji kuhusiana na teknolojia, kwa mfano baadhi ya vyuo vya ufundi vinaendelea kutumia labda cherehani za miguu, wakati zimepitwa na wakati kwa hiyo hiyo ni tathmini ya ujumla ambayo itahusisha nchi nzima ikiwa nii pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyauliza. Baada ya hapo hatua mahsusi zitachukuliwa katika kuhakikisha kwamba VETA zinatoa mafunzo ya kisasa, mafunzo ambayo yanaendana na mahitaji ya sasa hivi ya viwanda tunavyotarajia kuvianzisha.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Sera ya Serikali ni kuwa na chuo cha ufundi VETA kila Wilaya lakini hadi sasa ipo baadhi ya Mikoa haina hata chuo kimoja cha ufundi VETA kwa mfano Mkoa wa Rukwa.
Je, Serikali ina mpango gani, wa kiuwiano wa kuhakikisha Mikoa yote ambayo haina vyuo vya ufundi VETA inapewa kipaumbele kwanza?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba kila Wilaya inakuwa na VETA na kila Mkoa inakuwa na VETA bado uko palepale. Niseme tu kwamba kwa mfano Mkoa wa Rukwa aliyosema changamoto iko ndani ya Mkoa katika kutoa kiwanja, kwa hiyo tungeomba kwamba zile changamoto ambazo zinajitokeza za upatikanaji wa eneo Mkoa wakamilishe ili ahadi ya Serikali iendelee kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais ameipatia Wizara yangu, vyuo vya Folk Development College‟s Wizara kama nilivyosema kwenye majibu ya awali itafanya tathmini ya VETA, itafanya tathmini ya hizo Folk Development College‟s ambazo ni 53 tumekabidhiwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba tutatoa kipaumbele kwenye yale maeneo ambayo yalikuwa hayana vyuo vya ufundi ili kuhakikisha kwamba hii ahadi ya Serikali inatekelezwa kwa vitendo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Kwa kuwa, katika Wilaya ya Mkalama wako wafadhili wa Marekani wanaitwa Family Community Connection wana pesa takribani zinazozidi shilingi bilioni moja, wamejitokeza kujenga kituo cha VETA Nkungi kwa masharti kwamba Halmashauri ipeleke maji na umeme, na Halmashauri haina pesa. Je, Wizara inasema nini, katika mazingira kama hayo na pesa ziko mkononi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningemwomba kama fedha ziko mkononi anikabidhi basi niwe nazo mfukoni, zisiishie kuwa mkononi ziingie mfukoni kwangu. Lakini ningependa tu kusema kwamba kama suala ni upatikanaji wa maji na miundombinu, nadhani hayo ni mambo ambayo yanazungumzika na Wizara yangu haikuwa na taarifa na hili jambo basi atuletee tu rasmi tutalifanyia kazi, lakini naomba hiyo hela ije iingine mfukoni kwa Waziri wa Elimu ili tuweze kufanyia kazi.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Karagwe tuna kituo cha ufundi stadi cha KVTC Kayanga. Serikali iliandaa mchoro wa kupanua hiki chuo kwa muda mrefu sasa miaka mingi. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kupanua hiki chuo cha KVTC Kayanga.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali imetenga fedha za kufanya ukarabati wa vyuo viwili. Chuo cha Ufundi Stadi cha Korogwe pamoja na Karagwe kwa hiyo fedha zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwanza ningependa kutambua jitihada kubwa sana zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli katika vita dhidi ya madawa ya kulevya na ningependa kuwatia moyo na waweze kuendelea na jitihada hizi. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuweka katika mitaala ya elimu ya msingi pamoja na sekondari mafunzo kuhusu athari ya dawa za kulevya?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, hawa vijana 3,000 waliopatiwa tiba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kwa kushirikiana na wadau, je Serikali inafahamu vijana hawa wako wapi katika muda huu, yaani kwa sasa na wanafanya nini?(Makofi)
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ningependa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainab Katimba kuhusiana na kipengele cha mpango wa Serikali kuweka kwenye mitaala masuala ya madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Spika, ningependa kusema kwamba mitaala ya kuanzia shule za msingi, Sekondari pamoja na masuala ya kitaaluma lakini pia inakuwa imebeba masuala mtambuka. Kwa hiyo, masuala yanayohusiana na masuala ya madawa ya kulevya, masuala ya jinsia, masuala ya UKIMWI yapo katika mitaala yetu na tutaendelea kuyaimarisha ili kuhakikisha kwamba tunaenda sambamba na azma ya Serikali ya kupambana na hili janga la madawa ya kulevya nchini. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Serikali za kusambaza vifaa saidizi kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inajenga shule moja ya mfano ambayo itawajumuisha watoto wenye ulemavu pamoja na watoto wengine ambao hawana mahitaji maalum, ili basi shule hiyo iweze kuwasaidia kwa kiwango kikubwa watoto wenye mahitaji maalum?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inakamilisha mapitio ya michoro kwa ajili ya shule maalum ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kujenga shule ya Kisasa ambayo itakuwa ni ya bweni, shule ya msingi na sekondari kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo shule hiyo itajengwa kwenye maeneo ya Chuo cha Ualimu cha Patandi ambacho ni chuo mahususi kwa ajili ya kufundisha walimu wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi huo utaanza mara moja mara baada ya kukamilisha mishoro kwa sababu fedha kwa ajili ya ujenzi zipo.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Walimu ndiyo wanaowalea watoto wetu shuleni na ndiyo wanaotegemewa zaidi kuwa walinzi wa watoto hawa wanapokuwa shuleni. Hata hivyo, baadhi ya Walimu ndiyo wamekuwa na tabia za kuwadhalilisha watoto kwa vitendo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa kuna suala la elimu, mtoto yule anakuwa mwoga kutoa taarifa pale anapodhalilishwa na Mwalimu. Serikali ina mkakati gani wa kuwapa watoto elimu ili wawe na ujasiri wa kuripoti vile vitendo ambavyo wanafanyiwa na baadhi ya Walimu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali imeweka utaratibu shuleni wa kuwawezesha watoto wa kike kuwa na ujasiri wa kuripoti matukio ya udhalilishaji ambayo yanafanyika yaani life skills na pia tumeanzisha club mbalimbali za kuwawezesha watoto kuwa na ujasiri wa kuweza kuripoti matukio hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuomba na kuwasihi watoto wasiwe na uwoga wowote kwa sababu Serikali yao inawalinda. Pale ambapo anafanyiwa vitendo ambavyo ni kinyume na matakwa ya Serikali, watoe taarifa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaodhalilisha watoto na kuwasababishia wasisome shuleni kwa amani. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani haijawahi kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma, lakini Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ambacho ni chombo cha Serikali kimeongeza makato kutoka asilimia nane hadi asilimia 15. (Makofi)
Je, Serikali iko tayari sasa kusitisha nyongeza hiyo ya makato hadi pale ambapo itaongeza mshahara kwa Watumishi wa Umma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa ongezeko la makato kutoka asilimia nane hadi 15 limewaathiri sana watumishi wa umma maudhurio kazini kwa kukosa nauli.
Je, Serikali haioni kwamba ni muda muafaka sasa kusitisha makato haya ya kutoka asilimia nane hadi 15 kwa kuwa watumishi wengi sasa hawana nauli na suala hili limeweza kuathiri maudhurio watumishi kazini na kupunguza ufanisi wa kazi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza katika majibu yangu ya msingi Serikali haina mpango wowote wa kusitisha makato ya asilimia 15 ya wanufaika wa mikopo. Naomba kwamba watu wasichanganye mambo kwa sababu unapokata asilimia ya mshahara italipwa kulingana na kiwango chako cha mshahara wewe kama unapata shilingi 100,000 asilimia 15 itakuwa ni ya 15,000 na anayepata milioni moja atalipa 150,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, makato haya yanazingatia uwiano na ukubwa wa mishahara, lakini Serikali haitasitisha kama ambavyo nimesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaasa na kuwaonya watumishi ambao wanataka kusingizia makato ya asilimia 15 kwa kuchelewa kazini Serikali itachukua hatua za kinidhamu. Kwa sababu watumishi wote wa umma wanapaswa kuzingatia sheria kanuni na taratibu zinazoongoza utumishi wa umma.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza hapo hapo awali tulikuwa na chombo ambacho kilikuwa kinapitia hivi vitabu na vifaa vya elimu EMAC kabla ya kwenda mashuleni. Na kwa kuwa EMAC ilifutwa rasmi, sasa niulize Serikali ina mpango gani wa kuanzisha chombo kingine au chombo mbadala ambacho kitakagua vitabu na vifaa vya elimu kabla ya kwenda mashuleni? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni dhahiri kwamba sasa hivi kuna upungufu mkubwa sana wa vitabu kwa shule za msingi hasa darasa la kwanza mpaka la tatu; je, Serikali ina mpango gani wa haraka ili kutatua changamoto hii?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli Serikali ilivunja EMAC ambayo ni Education Management Approve Committee iliyokuwa inahusika na kupitisha machapisho na vitabu vya elimu baada ya chombo hicho kushindwa kutekeleza wajibu wake vizuri na tulishuhudia kwamba pamoja na kuwepo kwa chombo hicho, lakini bado vitabu vilikuwa na makosa mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba sasa hivi kazi ya kupitisha vitabu inafanywa na Taasisi ya Elimu Tanzania, lakini niseme kwamba Serikali itaangalia namna ya kuangalia utaratibu mwingine, baada ya kuondoa EMAC kwa sababu pia Taasisi ya Elimu inakuwa inaelemewa na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa vitabu, naomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba sasa vitabu vimekwishafanyiwa marekebisho na zaidi ya nakala 9,000 za vitabu vya kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu vimekwishasambazwa shuleni, kwa hiyo, sasa hivi tatizo hilo Serikali imekwishasambaza vitabu vilivyorekebishwa.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Waziri hususan anaponieleza mkakati wa Serikali katika kuinua kiwango cha elimu ya awali. Namshukuru sana kwamba ametamka wazi kwamba kuna vitabu vya kiada vinachapishwa na kuna vitabu vya ziada viko katika mchakato wa kutolewa. Sasa swali langu la kwanza ni kwamba, je, vitabu hivi vitasambazwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa inaonekana Serikali imejikita kupeleka madarasa ya elimu ya awali katika shule za msingi kwa kuzingatia kwamba jamii nyingi za kifugaji wanaoishi katika Wilaya kwa mfano Wilaya yangu ya Longido, Simanjiro, Kiteto, Ngorongoro na Monduli hata Siha wanaishi mbali na shule kutokana na jiografia. Sasa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba elimu hii bora katika ngazi ya awali inawafikia watoto hawa wadogo ambao hawawezi kufikia hizo shule zenye madarasa ya awali?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusiana na vitabu katika jibu langu la msingi nimesema kwamba tayari vitabu sita vya kiada; na vitabu vya kiada ni vile ambavyo ni lazima kwa mujibu wa muhtasari mwanafunzi awenavyo tayari vimekwishachapwa ambavyo viko katika hatua ya uchapaji ni vitabu vya ziada yaani vya nyongeza zaidi ya vile ambavyo ni vya lazima katika muhtasari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na umbali wa shule, kama nilivyosema Serikali imetoa maelekezo kwamba kila shule ya msingi ni laizma iwe na darasa la awali. Kwa hiyo, nitoe wito kwake nafahamu kwenye jamii za wafugaji kunakuwa na changamoto kwamba Halmashauri ishirikiane na Serikali Kuu kuona kwamba kama kuna utaratibu wa tofauti na uliowekwa na Serikali wa kuchukuliwa kwa ajili ya jamii za wafugaji Serikali iko tayari. Lakini Halmashauri ndiyo ina jukumu la kutoa mapendekezo pale ambapo wanaona utaratibu wa kisera ni mgumu kulingana na mazingira yao.
MHE. ASHA ABDALLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, bado vijana wengi wanaomaliza darasa la saba wanakuwa hawajapata nafasi kwenye vyuo vya ufundi au kuendelea na masomo ya sekondari. Ni lini Serikali itaboresha elimu ya msingi kuhusisha mafunzo ya ufundi ndani yake ili kuwaasaidia wale wanaobaki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mtaala wa VETA ni mmoja nchi nzima wakati mahitaji yanatofautiana sehemu na sehemu. Kwa mfano, mikoa yenye gesi wangefundishwa mambo yanayotokana na gesi, mikoa ya uvuvi wangefundishwa taaluma za uvuvi na mikoa ya madini vivyo hivyo. Sasa Serikali ina utaratibu gani kuhusu kuingiza component hiyo katika mitaala yake?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu suala la wanafunzi ambao wanamaliza darasa la saba lakini hawapati nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inafanya kazi kubwa ya kuongeza nafasi za udahili kwenye vyuo vya ufundi kwa kujenga vyuo vipya vya ufundi pamoja na kuboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme kwamba katika mtaala wa elimu ya msingi kuna somo la stadi za kazi ambalo limewekwa mahsusi kwa ajili ya kuwapatia vijana wetu angalau ujuzi ili hata yule anayemaliza elimu yake ya msingi awe tayari ana uwezo wa kufanya jambo katika mazingira yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu mtaala wa VETA kwamba unafanana, kimsingi masuala ya ufundi yanatakiwa yaangalie mazingira halisi ya mahali ufundi unapofanyika. Kwa hiyo, suala la kuangalia masuala ya gesi au masuala ya uvuvi ndiyo jambo ambalo limekuwa likifanyika. Kwa hiyo, niendelee kutoa wito kwa wote wanaotoa mafunzo ya ufundi stadi wahakikishe kwamba mitaala yao inazingatia mazingira halisi ya pale ambapo wanatoa mafunzo ili kuwawezesha wananchi wa eneo husika kuongeza tija katika shughuli wanazozifanya.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa sasa wa kutumia VETA na vyuo vya FDC kutoa mafunzo ya ufundi stadi umekuwa ni wa polepole sana na idadi kubwa ya vijana wanamaliza shule za sekondari hawana ujuzi kabisa. Je, Serikali inaonaje sasa ikaanza kubadilisha baadhi ya shule za sekondari ambazo tumezijenga katika Halmashauri zetu kuwa shule za ufundi ili kusudi zisaidie vijana hawa kupata elimu ya ufundi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwalongo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba Serikali tayari imeshaona hiyo changamoto na ndiyo maana zile shule za ufundi ambazo awali zilikuwa zimebadilishwa mafunzo ya ufundi yaliondolewa tayari Serikali imeshachukua jukumu la kuzikarabati zile shule saba za ufundi za Kitaifa na kuziimarishia vifaa vya kufundishia na karakana zake zote zimeimarishwa. Nitoe wito kama alivyosema Mheshimiwa Mwalongo, Serikali itafurahi sana kama kuna Halmashauri ambayo ina shule na wanaona kwamba inakidhi vile vigezo vya kutoa mafunzo ya ufundi tuko tayari watuambie ili twende kuikagua na tutapenda tu kuongezea idadi ya wanaofanya mafunzo ya ufundi.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya shule za msingi zina vituo vya ufundi stadi, mfano, katika Wilaya ya Chamwino, vituo hivyo viko katika Shule ya Msingi Mvumi Mission na Shule ya Msingi Chamwino lakini hakuna vifaa wala walimu wa kutosha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifufua vituo hivyo siyo kwa Wilaya ya Chamwino tu lakini katika shule zote za msingi ambazo ziko Tanzania hii? Ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLIJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Fatma Toufiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kwa swali lake zuri kwa sababu ni kweli zile shule zipo lakini kwa kweli hali yake haijakaa vizuri, niliona nilipozitembelea. Kwa hiyo, tayari Serikali imeliona na kwa kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi hapa Nchini (ESPJ) ambao Wizara yangu inautekeleza kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, tutafanya tathmini ya shule hizo na kwa awamu tutaanza kuzifanyia maboresho kwa kuzipelekea vifaa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tunaamini na tunajua kwamba elimu ndiyo msingi wa kila kitu katika maisha ya mwanadamu na mafanikio ya elimu ni pamoja na kuwa na zana za kufundishia pamoja na kujifunzia. Kwa kuwa, vitabu vyetu vya kiada huchapishwa nje ya nchi yetu na tukiamini kwamba elimu ni jambo tete katika ustawi wa Taifa letu, je, ni lini vitabu hivi vya kiada vitachapishwa hapa nchini ukizingatia Serikali yetu ni ya viwanda? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru sana kwa kuleta swali hili hapa Bungeni na nitumie nafasi hii kuonyesha masikitiko yangu makubwa sana kwa makampuni ya Kitanzania ambayo yanafanya kazi ya uchapishaji. Haya Makampuni yametuangusha kweli kweli, tumelazimika kwenda kuchapa vitabu nje kwa sababu unapoyapa makampuni ya Kitanzania kwanza kuna mengine ambayo yamekuwa yanachapa vitabu, kitabu kimekaa kama sambusa yaani wanakata hovyo hovyo lakini pia wanatumia muda mrefu kuvichapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu swali lake kwamba Serikali ina mpango gani, kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeamua kununua mashine ya uchapaji na hapa tunapoongea tayari tumekwishaiagiza. Kwa hiyo, tunategemea hilo suala sasa tutakuwa tunalifanya wenyewe.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni ianze kujitathmini kwa upya aina za adhabu zinazotolewa kwa wanafunzi wetu kwa sababu adhabu hizi mara nyingi huwa zinadhalilisha na zinaleta madhara ya kisaikolojia na katika mwili. Sasa ni bora Serikali itathmini kwa upya hizi adhabu hata kama ni kiboko kinatolewa sehemu gani, unakuta adhabu mtoto anaambiwa azomewe mbele ya darasa, achapwe mbele ya darasa tayari unamu-affect kisaikolojia na mwili wake. Kwa hiyo, tuangalie na tutathmini hizi adhabu ni katika kujenga na sio kumbomoa yule mwanafunzi. Kuna umuhimu wa kujitathmini hizi adhabu tunazowapa wanafunzi, ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niongelee hili suala. Kwanza niseme kwamba suala la utoaji wa viboko lengo lake si kuongeza ufaulu, adhabu inakuwa inarekebisha nidhamu au dosari ambayo imejitokeza. Kwa hiyo, tutofautishe haya mambo ya kurekebisha nidhamu na suala la ufaulu. Suala la adhabu linatolewa pale mtu anapoenda kinyume na taratibu.

Mimi ningependa kuchukua nafasi hii, kuwahimiza wanafunzi wote nchini kufanya utii wa sheria bila shuruti, kwa sababu watakapotii sheria hakutakuwa na sababu ya wao kupewa adhabu. Lakini pale ambapo inakuwa ni lazima mwanafunzi apewe adhabu kwa sababu hajatii sheria zilizowekwa, ni muhimu sana kwa walimu kuhakikisha kwamba wanazingatia taratibu ambazo zimewekwa na mwalimu yeyote ambae anakwenda kinyume na zile taratibu za kuadhibu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Serikali kwamba kuna mikakati fulani inafanywa kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Vilevile sehemu kubwa ya kukosekana kwa ajira za vijana inatokana na mitaala mibovu. Tunakubaliana kwamba zamani tulikuwa na elimu ya kujitegemea ambayo ilikuwa inawasaidia vijana kuwa na skills baada ya kumaliza shule, lakini hilo sasa halipo:-

Je, Serikali iko tayari kuangalia upya mitaala ya vijana wetu ili wanapomaliza shule wawe tayari wana utaalamu wa namna fulani ambao utawasaidia kujiajiri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba, wako vijana wanaomaliza Vyuo Vikuu wana uwezo wa kufanya kazi lakini wanakosa mitaji; na nilishaomba hapa Bungeni, ni kwa nini Serikali isitengeneze utaratibu au sheria ambapo vyeti vya hawa vijana vitatumika kama dhamana ili vijana hawa wakopesheke waweze kuwa na mtaji wa kuanzisha mambo ambayo yanaweza kuwategemeza kama kilimo, biashara na kadhalika?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selasini. Kwanza napenda kutoa ufafanuzi kwamba bado Elimu ya Kujitegemea inaendelea shuleni. Kwa hiyo, kama kuna sehemu ambazo Elimu ya Kujitegemea haifanyiki, ni kwa sababu tu labda wahusika katika maeneo husika wanalegalega. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa walimu kuhakikisha kwamba elimu ya kujitegemea inaendelea shuleni.

Mheshimiwa Spika, katika mitaala yetu, tunalo somo la stadi za kazi ambapo lengo la somo hilo ni kujenga utamaduni wa watoto wadogo (wanafunzi) kupenda kazi na kuweza kufanya shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa wanafunzi kujifunza kujitegemea na tunayo katika mitaala yetu. Kwa hiyo, cha msingi ni kuhakikisha kwamba inatekelezwa kama ilivyopangwa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Selasini Mbunge wa Rombo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja kati ya mikakati ya Serikali kwenye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana wahitimu wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu, mkakati tulio nao hivi sasa, tumeanza kuwahamasisha vijana kupitia fani zao kukaa katika vikundi na kuunda makampuni na Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikiwasaidia kufikia katika hatua hiyo.

Mheshimiwa Spika, lengo ni kwamba baada ya kuhitimisha hatua hizo za awali, waweze kuwezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kupitia asilimia 10 ya mapato ndani ya Halmashauri na Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili ipo kampuni moja ya vijana wahitimu wa Chuo Kikuu pale Sokoine, Morogoro ambao walihitimu katika kilimo wakakaa pamoja, Serikali tukawawezesha. Hivi sasa, juzi kampuni hiyo imeshinda tenda katika Ofisi ya Waziri Mkuu ya kiasi cha shilingi bilioni nne katika masuala ya kilimo. Huo ni mfano ambao upo hai. Kwa hiyo, nitoe rai kwa vijana wengine wote nchi nzima kujikusanya kwa pamoja Serikali tutakuwa nao kuhakikisha kwamba wanafikia malengo yao.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Elimu amejibu kwa kutumia sera, lakini swali langu mimi hapa lilitumia sheria na bahati nzuri sana amelielezea vizuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Kiswahili kimekuwa na kuwa moja ya lugha mashuhuri sana Duniani ambayo chimbuko lake ni Tanzania. Je, Serikali haioni umuhimu wa Kiswahili kutumika sasa kuwa lugha ya kufundishia katika elimu yetu kwa ngazi zote? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Kiswahili sasa kimekuwa na kuwa bidhaa muhimu sana ya kuuza nchi za nje na hivyo kuingiza hela kupitia walimu wa Diaspora. Je, Serikali ina mpango gani wa kukikuza Kiswahili na kukiuza nje ya nchi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante ningependa kumjibu Mheshimiwa Almas Maige maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na lugha ya Kiswahili ambayo hakika ni ligha adhimu na imeendelea kushika kasi, suala la kutumia lugha hiyo kufundishia kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi lugha hiyo inatumika katika kufundisha katika shule za elimu ya awali, msingi na vyuo vya ualimu ngazi ya kati na bado Serikali inaona kuna umuhimu wa kutumia lugha ya kiingereza kama ambavvyo nilisema katika majibu yangu ya msingi na ndio maana ukiangalia hata Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani wanawapeleka watoto wao kwenye english medium kwa sababu wanatambua umuhimu wa lugha hiyo, kwa hiyo Serikali itaendelea kutumia lugha zote kama ambavyo imeelezwa katika sera ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kukuza Kiswahili, kwanza nshukuru kwamba lugha yetu ya Kiswahili imeendelea kupendwa na baadhi ya nchi wamekuwa wakiomba Tanzania kuweza kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi zao kama vile Sudan Kusini, Afrika ya Kusini pamoja na nchi nyingine. Kwa hiyo ni lugha ambayo Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha na suala la lugha ya Kiswahili sio suala tu la kujua kuzungumza, lakini pia lina suala la usanifu wa lugha ya Kiswahili, kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha ili fursa zinazojitokeza Watanzania waweze kunufaika zaidi. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali la nyongeza kama mwalimu kwa mwalimu mwenzangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako.

Kwa kuwa umezungumza kwamba Wabunge wengi, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Mawaziri na watumishi wengi tu wa Serikali, sasa hivi wanapendelea sana kuwapeleka watoto wao shule za english medium. Lakini kwa kuwa hizi shule za english medium zimekuwa zikitoa malalamiko mengi kwamba Serikali haijajenga chuo cha kufundishia walimu special kwa ajili ya kwenda kufundisha hizi shule za english medium.

Ni lini Serikali itajenga Chuo cha Serikali ili walimu wa Tanzania waweze kusoma na kwenda kuwafundisha walimu hao kwa sababu tunatumia walimu wa Kenya na Uganda? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana ningependa kujibu swali la nyongeza la mwalimu mwenzangu Mheshimiwa Phillipo Mulugo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake ni la msingi kwamba Serikali iandae walimu ambao watafundisha katika shule ambazo zinatumia lugha ya Kiingereza, na niseme suala hili si lazima tujenge chuo, nimwambie kwamba suala hilo Serikali imelipokea na tutangalia utaratibu ambao tunaweza ndani ya muda mfupi tukaanza kuwa hata kuwa tunatoa hayo mafunzo katika vyuo ambavyo vipo hapa nchini. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Waziri yameonesha kweli Kiswahili kimekua, lakini nchi ya Afrika Kusini wanafundisha Kiswahili na walitupa tender kama Tanzania ili tuweze kuwaandaa walimu wa kuwapeleka katika nchi ile. Lakini mpaka sasa hakuna jambo hilo limetekelezeka na hata nchi ya Kenya sasa wametupiku wamepeleka kule.

Je, Tanzania ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwamba wana walimu wa kutosha wa kuwapeleka nchi hizo? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie kwamba Serikali au nchi yetu ya Tanzania inao walimu wa kutosha wa Kiswahili ambao ni wabobezi, kwa hiyo suala la upungufu wa walimu wa kutosha ambao wanaweza kwenda kufanya kazi katika nchi za nje hamna tatizo lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la nchi kuamua kwamba inafanya kazi na nani hilo ni suala la hiyari ya nchi yenyewe, lakini kama Tanzania tuko tayari kupeleka walimu wetu wa Kiswahili mahali popote katika dunia hii kwa sababu tunao walimu wa kutosha mahiri na Serikali inaendelea kuimarisha ufundishaji wa somo la Kiswahili kwa sababu kama ambavyo tumeona lugha ya Kiswahili imeendelea kuheshimika na imeendelea kutumika sehemu mbalimbali katika Afrika na hata nje ya Bara la Afrika. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa swali la msingi linazungumzia suala la kufundisha Kiswahili na kwa kuwa Mheshimiwa Rais John Joseph Pombe Magufuli anakitangaza Kiswahili dunia nzima na kwa kuwa Serikali inajua umuhimu wa kukitangaza Kiswahili.

Je, kuna mkakati gani wa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika kukitangaza Kiswahili, kwani nchi jirani wanachukua nafasi ya kuonekana wao ndio wamejipanga katika kuuza soko la lugha ya Kiswahili? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli hakika amekuwa ni Balozi mzuri sana katika kuhakikisha kwamba Kiswahili kinatumika na amekuwa akikitumia katika mikutano hata nje ya nchi na ameongeza chachu ya Kiswahili kutumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata katika Mikutano ya Umoja wa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeendelea kukitangaza Kiswahili kwa kuhakikisha kwanza kinatumika katika shughuli mbalimbali za kiserikali, lakini vilevile hili suala la kwenda kufundisha katika nchi za nje ni mojawapo ya hatua muhimu ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili na hata katika mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tumeona kimekuwa kinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba fursa yoyote inayopatikana ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili tunaendelea kuitumia, lakini vilevile Wizara yangu itaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha ufundishaji wa somo hili la Kiswahili kwa sababu kadri ambavyo tutakuwa na watalaam wengi wa Kiswahili hiyo pia ni sehemu moja wapo ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, wote tunatambua lengo kubwa la vyuo hivi ni pamoja na kuondoa ujinga lakini vilevile kufanya watu waweze kujiajiri wenyewe na lengo kubwa nilikuwa na mimi nashangaa ni kwa sababu gani what is the uniqueness ya hiki chuo mpaka hiki kiwe chini ya Wizara ya TAMISEMI wakati tunajua vyuo vyote vya maendeleo vilikuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na vyote vikapelekwa Wizara ya Elimu.

Sasa nataka kujua what is uniqueness yaani nini upekee wa chuo hiki kuwa chini ya TAMISEMI wakati tunajua Wizara ya Elimu ndiyo ingeweza zaidi kuhakikisha kwamba vinajengewa labda hata hizi changamoto zisingekuwepo? Nilitaka kujua hilo.
WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI kwa majibu yake mazuri kuhusiana na swali hili.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo; ni kweli kwamba vyuo vyote vya maendeleo ya wananchi viko chini ya Wizara yangu na Wizara imekuwa ikivifanyia ukarabati vyote 54 ambavyo viko chini ya Wizara na hapa katika majibu ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea historia ya hicho chuo. Lakini historia inaweza ikabadilika, naomba kama Serikali tulipokee hilo wazo tuangalie ni namna gani hiki chuo kinaweza tukakifanyia utaratibu ili kiweze kupata huduma vizuri zaidi kama ambavyo vyuo vingine 54 vinapata huduma. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni dhahiri kwamba Watanzania wengi ambao unakuta wamemaliza kidato cha sita na wengine ambao wanasifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo ya elimu ya juu ili tuweze kuwa na wataalam wa fani mbalimbali. Mikopo hii inapotolewa tumeweka riba kubwa sana ya asilimia kumi na tano ambayo ipo katika sheria ya 2016 na penati ya asilimia sita. Hivyo, tunakuta wanufaika wengi ambao ni watoto wa familia maskini wanashindwa kulipa au kubeba huu mzigo. Je, ni lini sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria hii angalau tupeleke kwenye singledigit kwa maana ya asilimia nane au tano ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuza kama chanzo cha mapato? Ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la nyongeza ukiangalia kwa kiasi kikubwa haliendani na swali la msingi, lakini kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya Bodi ya Mikopo, ningependa kwanza kuonesha kwamba mwombaji wa kwanza anasema wanafunzi wote wapate mikopo, lakini mwombaji wa pili anasema makusanyo wapunguze.

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha Mfuko huu wa mikopo ilikuwa ni kwamba watu wafanye marejesho, mikopo ijiendeshe yenyewe kama vile revolving fund yaani yale marejesho yakikusanywa yatosheleze kuwapatia wanafunzi wengine. Kwa hiyo, ukiangalia hata sasa makusanyo ya mikopo yanachangia asilimia 46 ya bajeti ya mikopo. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kurejesha mikopo upo na asilimia 15 ambayo mwanafunzi anakatwa, anabaki na asilimia 85 ya mkopo wake, tukumbuke kwamba mkopo wa Bodi ya Mikopo ndiyo uliotangulia kabla ya mikopo mingine na Kanuni za Utumishi makato ni kwamba mtumishi anatakiwa abaki na theluthi moja ya mshahara.

Mheshimiwa Spika, nawasihi wanaochukua mikopo, waone umuhimu wa kulipa na wale wenye fedha wasisubiri kukatwa hiyo asilimia kumi na tano, kumi na tano ili wanafunzi wengine waweze kunufaika kama wao walivyonufaika, wakaweza kupata ajira. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watusaidie kutoa elimu kuonesha umuhimu wa kurejesha mikopo kwa sababu marejesho hayo ndiyo yanawasaidia wengine kupata mikopo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni dhahiri kwamba Watanzania wengi ambao unakuta wamemaliza kidato cha sita na wengine ambao wanasifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo ya elimu ya juu ili tuweze kuwa na wataalam wa fani mbalimbali. Mikopo hii inapotolewa tumeweka riba kubwa sana ya asilimia kumi na tano ambayo ipo katika sheria ya 2016 na penati ya asilimia sita. Hivyo, tunakuta wanufaika wengi ambao ni watoto wa familia maskini wanashindwa kulipa au kubeba huu mzigo. Je, ni lini sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria hii angalau tupeleke kwenye singledigit kwa maana ya asilimia nane au tano ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuza kama chanzo cha mapato? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la nyongeza ukiangalia kwa kiasi kikubwa haliendani na swali la msingi, lakini kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya Bodi ya Mikopo, ningependa kwanza kuonesha kwamba mwombaji wa kwanza anasema wanafunzi wote wapate mikopo, lakini mwombaji wa pili anasema makusanyo wapunguze.

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha Mfuko huu wa mikopo ilikuwa ni kwamba watu wafanye marejesho, mikopo ijiendeshe yenyewe kama vile revolving fund yaani yale marejesho yakikusanywa yatosheleze kuwapatia wanafunzi wengine. Kwa hiyo, ukiangalia hata sasa makusanyo ya mikopo yanachangia asilimia 46 ya bajeti ya mikopo. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kurejesha mikopo upo na asilimia 15 ambayo mwanafunzi anakatwa, anabaki na asilimia 85 ya mkopo wake, tukumbuke kwamba mkopo wa Bodi ya Mikopo ndiyo uliotangulia kabla ya mikopo mingine na Kanuni za Utumishi makato ni kwamba mtumishi anatakiwa abaki na theluthi moja ya mshahara.

Mheshimiwa Spika, nawasihi wanaochukua mikopo, waone umuhimu wa kulipa na wale wenye fedha wasisubiri kukatwa hiyo asilimia kumi na tano, kumi na tano ili wanafunzi wengine waweze kunufaika kama wao walivyonufaika, wakaweza kupata ajira. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watusaidie kutoa elimu kuonesha umuhimu wa kurejesha mikopo kwa sababu marejesho hayo ndiyo yanawasaidia wengine kupata mikopo.
MHE. DKT THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa mara ya kwanza mimi naona amelitendea haki sana swali hilo, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ili kuendelea kupunguza uhaba wa wahadhiri;

Je, Serikali haiwezi kurudisha utaratibu wa kuwafanya wahadhiri hao wafundishe hata baada ya miaka 65 kama nchi nyingine za Marekani na Ujerumani?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wahadhiri wetu kufundisha zaidi ya miaka 65 ni suala la kiutumishi kwenye kanuni zetu za kiutumishi. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua suala hili, tutakwenda kukaa na wenzetu wa Wizara ya Utumishi ili tuweze kuangalia namna gani ya kurekebisha sheria zetu zile ili ziendane sasa na mahitaji haya muhimu ya soko letu la wahadhiri nchini. Ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Taifa letu la Tanzania linatambulika kabisa kwamba kilimo ni uti wa mgogo, na tangu uhuru tunatambulika kwamba taifa hili ni taifa la wakulima na wafanyakazi. Serikali imesema somo hili linafundishwa kwenye somo la maarifa ya jamii na stadi za kazi. Kimsingi ni mada wala si somo la kilimo ni mada zinafundishwa huko.

Mheshimiwa Spika, swali langu, swali langu, ni lini sasa...

SPIKA: Anayeuliza maswali haya ni mwalimu jamani enhee Endelea Mheshimiwa.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, swali langu, ni lini sasa Serikali itaweka kipaumbele kuhakikisha kwamba somo hili la kilimo linafundishwa na linakuwa la lazima, kwa maana compulsory dhidi ya masomo mengine kama general study, develop and study ambayo kimsingi tija yake ni ndogo ukilinganisha na tija hii ya somo la kilimo? Serikali inasema ukienda sekondari unachagua maana yake ni option, sasa una opt nini ilhali kwenye msingi hujatengeneza somo?

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali, ikubaliane na mawazo haya kuhakikisha kwamba inalianzisha somo hili la kilimo kuanzia ngazi ya msingi mpaka chuo kikuu?

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, Serikali imeanza mchakato wa mabadiliko ya mtaala wa elimu, na nichukue fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu alipoamua kwa dhati na kusema kuna haja kufanya mabadiliko ya mtaala wa elimu. Sasa swali langu hapa, ni lini Serikali itatuletea mchakato huu hapa Bungeni ili sisi tukachakata na kuhakakisha kwamba tunakuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu yetu hii tunaiwekea msingi ulio bora ili watoto wetu waweze kujiajiri na kuajiriwa kupitia na ujuzi huo? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kujibu muhimu kabisa la mwalimu mwenzangu, Mwalimu Sima. Kwa kweli maswali aliyouliza ni ya msingi. Tunatambua kwamba asilimia kubwa ya wananchi wetu ni wakulima. Kwa sasa hivi, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri wangu, somo la kilimo liko kwenye sekondari kama options na kwa upande wa shule za msingi tunafanya stadi za kazi; na tunafanya mapitio ya mitaala.

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu umetuwekea semina, lakini kabla hujatutangazie ile briefing mimi nilikuwa nimepanga tarehe 6 Novemba, 2021 nifanye semina, ingawa nilikuwa sikupanga kwa Bunge lote lakini nilikuwa nimepanga nifanye na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, niwapitishe mpaka sasa hivi Serikali imefikia wapi kwenye mapitio ya mitaala, wadau wanasema kitu gani na uchaguzi wa Wizara ni nini kutokana na maoni ya wadau na mwelekeo wa Serikali kutokana na maoni ya wadau ni nini, ili sasa Waheshimiwa Wabunge wapate nafasi ya kuweza kuweka maoni yao wakati tayari maoni ya wananchi wao tumeshayaweka Pamoja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, labda niahidi tu kwamba hili nitalifanyia kazi kiutawala kuangalia kwamba tarehe 6 ambayo nilikuwa nafikiria kuwa na semina na Waheshimiwa Wabunge tayari Mheshimiwa Wangu Spika kiongozi wetu umeishaichukua hiyo tarehe kwa hiyo tutaangalia utaratibu. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na hatua mbalimbali ambazo, tayari wameshaanza kuzichukua kwa kuona umuhimu wa kufanya mapitio ya mitaala yetu ya elimu.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nikufahamu kwa sababu kimsingi wameshafanya makongamano kadhaa ya wadau na marafiki wa elimu kwa ajili ya kukusanya maoni. Lakini wamepitia elimu ya awali, msingi na sekondari kimsingi vyuo na vyuo vikuu bado. Kwa hiyo, niulize sasa Wizara ama Serikali ina mpango gani wa kutuletea pia kufanya mapitio ya kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kuna maoni ya watanzania wametoa mbalimbali kuna masuala ya kilimo, kuna masuala ya ujasiriamali pamoja na stadi za kimaisha na mambo mengine mengi yote yamejadiliwa. Lakini vyuo na vyuo vikuu ambavyo ndio kimsingi vinatoa watu ambao ndio watenda kazi kwenye nchi. Ni lini sasa Serikali italeta kufanya marekebisho pia ya mtaala na masuala ya kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo hivyo. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nitoe ufafanuzi na kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Hanje. Utaratibu wa vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu wana taratibu zao za kuanzisha mitaala.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano katika vyuo vikuu seneti ndio chombo kikuu ambacho kina mamlaka ya kuangalia mitaala katika vyuo vikuu na vyuo vya kati vina nyanja tofauti, vyuo vya kilimo viko chini ya Wizara ya Kilimo, vyuo vya utalii viko chini ya Wizara ya Utalii, vyuo vya afya viko chini ya Wizara ya Afya na wote wana taratibu zao. Wizara husika ndio zinakuwa na mabaraza kwa mfano Wizara ya Afya, Baraza la Madaktari ndio linaangalia mitaala ya madaktari, Baraza la Wauguzi linaangalia mitaala ya manesi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kiasi fulani hili jambo labda nilipokee kama Serikali tuangalie namna ya kuliratibu. Kwa sababu, kwa sasa hivi sio vyuo vyote vya kati vinasimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Elimu na wala Wizara haihusiki moja kwa moja na kuidhinisha mitaala. Ila imekasimisha mamlaka kwa seneti za vyuo vikuu pamoja na vyombo ambavyo vimewekwa, kwa mujibu wa sheria katika vyuo husika kushughulika na mitaala.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu tuangalie namna gani labda kwa kuongezea kabla sijamalizia. Ni kwamba nako pia tumeelekeza wafanye mapitio ya mitaala na katika huu Mradi wa Higher Education tuna fedha ambazo tumetenga, kwa ajili ya kufanya mapitio makubwa na ndio maana mradi unaitwa mageuzi ya kiuchumi na yanajikita katika kuimarisha uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, mapitio ya mitaala yanafanyika kwa hiyo tutaangalia utaratibu mzuri wa kuratibu tupate mapitio yanayofanyika. Ili tuweze kuja kutoa taarifa kwenye chombo muhimu, ambacho ndio kinasimamia sheria na kusimamia utendaji wa shughuli za Serikali. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kulingana na majibu ya Serikali, inaonesha kwamba mafao yanayolipwa hayazingatii asilimia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa kulingana na michango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, je, kwa mujibu wa sheria ambayo imepitishwa hivi karibuni mwaka 2022, inasema mstaafu atalipwa asilimia 33 katika mafao yake kama pensheni yake ya mkupuo; kama analipwa asilimia 33 ina maana kwenye asilimia 100 inabaki asilimia 67 kwa ajili ya pensheni limbikizi; sasa kwa mujibu wa majibu haya, kwanini hawa wastaafu pindi anapofariki, ile asilimia 67 iliyobakia kama pensheni limbikizi wasilipwe wategemezi wake au warithi wake pindi ambapo tunajua kabisa kwamba huyu mtumishi kipindi chote cha utumishi wake ame- contribute kwenye mfuko fully? Kwanini wasilipwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; tunaona kwamba sasa hivi kuna mfumuko wa bei, maisha yamepanda sana, lakini wastaafu waliostaafu kuanzia miaka ya 2000 na kurudi nyuma pensheni yao ni ndogo sana; ile monthly pension, Serikali haioni sababu au umuhimu wa kuongeza pensheni kwa hawa watu ambao pensheni yao haikui? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kumjibu dada yangu, Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, maswali yake mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, ni kwamba malipo ya mafao yanazingatia kanuni. Mstaafu anapostaafu, kama alivyoeleza, analipwa mafao ya mkupuo na kunakuwa na wastani wa umri wa kuishi. Sasa kwenye majibu ya msingi kama nilivyoeleza, anapofariki haijilishi kama alishavuka ule wastani wa umri wa kuishi au hajavuka, lakini analipwa ile miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kiasi ambacho anakisema cha asilimia 67 kinawekwa kama makisio, lakini mstaafu analipwa kwa kadri anavyoendelea kuishi, anaendelea kupata pensheni ya mwezi. Kwa hiyo, sasa hivi tunalipa kwa miaka mitatu anapofariki bila kujali kama alikuwa ameshazidi ule umri wa wastani wa kuishi baada ya kustaafu.

Mhelshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Migilla kwa kweli ni la msingi la kuhusu Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza mafao kwa wastaafu. Utaratibu wa mifuko ni kwamba inafanya tathmini (actuarial evaluation) na kulingana na ile tathmini ndivyo ambavyo inaweza ikaangalia uhimilivu na uendelevu kuwaongeza wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kufanya tathmini ya mifuko katika mwaka fedha 2022/2023 na baada ya tathmini hiyo ndiyo tutaona uwezekano wa kuongeza kulingana na uwezo wa mifuko yetu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwanza sina budi kuishukuru Serikali kwa jibu lake zuri lenye mafanikio kwa wananchi. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inafanya juhudi kubwa kusomesha vijana wake ili kufaidika nao; je, baada ya kuhitimu masomo hayo, Serikali inafaidika kitu gani wakati vijana hao wanabakia vijiweni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa Serikali haina ajira kwa watu wote, na vijana hawa tayari wamesoma; je, Serikali inawatengenezea mazingira gani vijana hawa ili nao waweze kuishi maisha bora? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba, Serikali inapata manufaa makubwa sana kwa kupeleka vijana kusoma nje ya nchi, kwa sababu licha ya ujuzi na maarifa ambayo wanapata, lakini vijana hao pia wanapata uzoefu kutoka nchi nyingine; kutoka nchi ambayo wanafunzi wanasoma lakini pia na nchi ambazo zinakuwa zimepeleka wanafunzi katika chuo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwamba Serikali haina ajira na je, inatengeneza mazingira yapi kwa vijana hawa wanaotoka nje ya nchi: Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeendelea kuwa inatoa ajira kupitia ajira zinazotangazwa na Sekretarieti ya Ajira na pia kupitia sekta binafsi ambayo inakua kwa kasi kubwa. Vile vile, Serikali imeendelea kutengeneza mazingira kwa kuwapa nafasi za kupata mafunzo ya uzoefu kazini wakati wakiwa wanasubiri kupata ajira.