Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (43 total)

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, barabara ya Sumbawanga, Mpanda inafanana na barabara ya Magole, Mvomero - Turiani ambayo nayo ipo katika mapango wa Serikali wa kuweka lami na kwa kuwa kilomita nane za mwanzo zilishawekwa lami baada ya kuteuliwa na kuchaguliwa kuwa Mbunge nimefuatilia na nimeambiwa fedha za kumalizia mradi huo zinatafutwa na kwa kuwa kipindi hiki mvua kubwa zimenyesha barabara hiyo imeharibika.


Je, Serikali ipo tayari kufanya kazi ya dharura, huku tukisubiri fedha za lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara nyingi hapa nchini sasa zimeharibika kutokana na hali ya mvua inayoendelea kunyesha. Lakini TANROADS imetenga pesa maalum kwa ajili ya kufanya ukarabati kwenye barabara zote ambazo zimeharibika ili tuhakikishe wananchi wanaweza kupata mawasiliano kama kawaida.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara hii imetumia muda mrefu takribani miaka sita kutoka Sumbawanga mpaka Mpanda haijakamilika na wakandarasi wanaingia na kutoka mpaka hatima yake sasa hivi barabara ile imeharibika kupita kiasi na pale Mpanda Mjini kuna shimo ambalo mkandarasi alilichimba katikati ya Mkoa halieleweki lile shimo litazibikeje.

Je, Serikali ina mikakati gani kwa ajli barabara hii imekaa muda mrefu mno mpaka wananchi wa Katavi wamechoka, itakwisha?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili sasa hivi Mkoa wa Katavi mawasiliano hayapo, barabara ya kutoka Mpanda kuelekea Tabora haipitiki kabisa na wananchi wa Katavi wanategemea kwenda kuchukua bidhaa zao Tabora, Mwanza, maisha ya Mpanda yamekuwa magumu kutokana na hali ya hewa jinsi ilivyo.

Je, Serikali ina mikakati gani ya dharura ili kuwaokoa wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa ajili ya barabara hizo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu barabara hiyo kuchukua muda mrefu ni kweli baadhi ya barabara zimechukua muda mrefu lakini siku kumi zilizopita Serikali imetoa takribani shilingi bilioni 200 kwa ajli ya kuwalipa Wakandarasi mbalimbali hapa nchini. Tunaamini sasa, nachukua fursa hii kuwaagiza Wakanarasi wote kama nilivyowaagiza wataalamu wetu wa TANROADS kwamba sasa hivi waanze kwenda kwenye site ili kazi hizo zianze mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kweli kuna changamoto kubwa huko sehemu ya Katavi, Mkoa wa Katavi kwa sababu barabara zimekatika. Lakini wataalamu wetu wa TANROADS sasa tumewaelekeza huko ili waweze kuzikarabati barabara hizo. Pia sasa hivi tumefungua njia yetu ya reli kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa huko baina ya Katavi, Tabora na Dodoma ili waweze kupata huduma kama kawaida, asante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mwaka jana Bunge lililopita mwezi wa nne niliuliza swali hili hili la kufuatilia ujenzi wa minara hii na jibu nililopewa lilikuwa kwamba, kazi ya ujenzi imeanza na mpaka Waziri wa Mawasiliano wakati ule alinipa barua ya commitment ambayo nilikwenda kuwaonesha wananchi lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote ambacho kimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nataka kujua inakuaje makampuni ya simu...
MWENYEKITI: Swali la pili eeh?
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Inakuwaje Makampuni ya Simu pamoja na ruzuku wanayopewa kutoka kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa wote yanashindwa kukamilisha ahadi zao?
Swali la pili, Serikali ilituambia kwamba imebaini Makampuni ya Simu yanakuwa reluctant, ni wazito kwenda kujenga minara vijijini kwa sababu ya kifaida kwamba hakuna faida wanapoweka minara vijijini na wakasema kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watahakikisha kwamba, minara ya vijijini inajengwa kwa ruzuku ya 100%.
Je, mpango huo upo? Unaendelea na kama unaendelea ni vijiji gani ambavyo wameshabaini na vitanufaika kwa mpango huo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwenye Bunge hili mwaka 2014/2015, tulisemea maeneo hayo na ni kweli kwamba Makampuni mengi ya Simu, Airtel, Tigo, Vodacom, Zantel wanachelewesha kupeleka mawasiliano vijijini. Kwa mantiki hiyo ndiyo tuliamua kuleta Halotel au Viettel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini haraka. Kwa mtazamo huo huo kuanzia mwezi Mei mwaka huu mpaka mwezi Oktoba mwaka huu, Kampuni ya Halotel au Viettel itajenga takribani mawasiliano kwenye vijiji 1800. Tunaamini na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge vilevile vitapata huduma hiyo.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; kwa kuwa tatizo la Kahama la mawasiliano ya simu linafanana na tatizo la Mvomero na kwa kuwa tumepeleka maombi kwa kampuni mbalimbali za simu, na kampuni hizo zimeahidi kujenga minara katika Kata ya Luale, Kikeo, Kinda, Pemba na Kibati. Kwa kuwa minara hiyo hadi leo bado haijajengwa, je, Serikali iko tayari kupeleka ruzuku ya Mfuko wa Mawasiliano katika Kata hizo ili wananchi wa Mvomero sasa wapate mawasiliano ya uhakika? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko tayari kupeleka ruzuku lakini tatizo kubwa sio ruzuku, tatizo kubwa tunatoa ruzuku, lakini makampuni yenyewe hayako tayari. Kwa mtazamo huo, kama nilivyosema kwamba Serikali iliingia na mkataba na kampuni ya Halotel au Viettel kwa ajili ya kupeleka mawasiliano kwenye maeneo hayo. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, eneo lake litakuwepo kwenye mpango wa kupelekwa mawasiliano mwaka huu.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la Bukene linafanana kabisa na Korogwe Vijijini hasa kwenye Kata ya Kizara. Mwaka 2012 tulimchukua Naibu Waziri hapa alikwenda mpaka kule akawaahidi wananchi wa Kizara kwamba mwishoni mwa mwaka 2012 mnara utapatikana. Cha kushangaza mpaka leo hii hakuna cha mnara wala namna ya kupata mnara. Je, ni lini sasa Serikali itawapelekea wananchi wa Kizara mnara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tutagawa fomu kwa ajili ya Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanahitaji mawasiliano kwenye vijiji vyao ili na sisi tuwe na database ya uhakika. Pia nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kijiji chake kama nilivyosema mwaka huu kitapelekwa mawasiliano, kupitia kwa kampuni ya Viettel au Halotel Tanzania. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina swali dogo tu, najua kuna juhudi nzuri sana za kufufua Shirika letu la Ndege hili la ATCL, lakini lipo tatizo kubwa la wafanyakazi wasiokuwa na tija. Ndege hizo mbili zinazotarajiwa kununuliwa kuna wafanyakazi zaidi ya 200, ni lini sasa au mna mkakati gani wa kupunguza wafanyakazi wasiokuwa na tija ili hizo ndege mbili zitakazonunuliwa ziwe na manufaa kwa Shirika la ATCL?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli ATCL kuna wafanyakazi takribani 200 na sasa hivi kuna ndege moja, tunalolifanya sasa hivi ni kuhakikisha wafanyakazi wote tunawaajiri upya kuhakikisha tunakuwa na wafanyakazi ambao wanaendana na ndege zilizopo. Hatutaki kuchukua watu ambao wanakaa wanapiga maneno, lakini hakuna kazi ambayo inafanywa.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Nyakato – Buswelu - Mhonze ina urefu wa kilometa 25 ambapo kilometa 6 ni urefu wa barabara kutokea Nyakato National kuelekea Buswelu Wilayani. Serikali pamoja na kutoa kilometa 2.4 ambapo katika hizo kilometa 1 ilitengwa shilingi milioni 500 na sasa wametenga shilingi bilioni 1.16. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza kilometa 4 ili kuweza kuifanya barabara hiyo kufika Wilayani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Rais aliyepita wa Awamu ya Nne aliahidi kuijenga barabara ya Kamanga – Sengerema kwa kiwango cha lami na barabara hiyo inawasaidia wanawake wa Vijiji vya Katungulu, Kasomeko pamoja na Nyamililo kufanya kazi zao za kiuchumi. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa kuongeza fedha ili kuhakikisha ile barabara inafika Makao Makuu ya Wilaya, Wizara inautambua na ndiyo maana hata katika mwaka wa 2016/2017 tumeongeza kiwango cha fedha tulichotenga. Nimhakikishie Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma kwamba juhudi zake hizo zitazaa matunda kwa kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana mwaka hadi mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili kwa barabara ya Kamanga – Sengerema, naomba tu nimjulishe kwamba yale ambayo tuliyaeleza katika swali kama hilo hilo hapo nyuma tulidhamiria. Tuna dhamira ya kujenga hiyo barabara na tutaendelea kwa hatua zile ambazo tulizieleza. Tutaanza na masuala ya feasibility study pamoja na detail design kama ambavyo Wizara imepanga.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo.
Kwa kuwa, katika swali la msingi suala zima linaloongelewa ni juu ya elimu na faida inayotokana na faida na ulipaji wa kodi. Kwa kuwa tumekuwa mashuhuda katika baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa tukipata fedha kutoka kwa wafadhili nikitolea mfano wa barabara iliyojengwa kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga unakuta kuna vibao ambavyo vimeandikwa kwamba pesa hii imetokana na walipa kodi wa Marekani.
Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kwa ile miradi ambayo inakamilishwa kwa pesa ya ndani, vikawekwa vibao ili kuhamasisha ulipaji wa kodi kwamba miradi hii inatokana na ulipaji kodi ya Watanzania?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazo zuri na tutalichukua na tutalifanyia kazi. Hili ni jambo jema nafikiri.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri nazoendelea kuzifanya za Taifa letu. (Makofi)
Swali la kwanza kutokana na umuhimu wa barabara hii katika Mkoa wa Geita; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutembelea katika Mkoa wa Geita na kuipitia hii barabara ili aone uwezekano wa kuiingiza barabara hii katika kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?
Swali la pili, Mheshimwia Rais wetu kwa nyakati tofauti akiwa Waziri wa Ujenzi na alipoteuliwa kuwa mgombea wa Chama chetu cha Mapinduzi, aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa tatu katika Mji wa Masumbwi; je, Serikali ina mpango gani sasa kutimiza ahadi hizi za Mheshimiwa Rais wetu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Masele amenialika nitembelee katika mkoa wake, nataka kumuhakikisha nitatembelea nitatembelea mkoa huo na kuangalia barabara anayoisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kipindi kifupi nilichoingia kwenye Wizara hii, tumetembelea takribani mikoa kama 23 ya Tanzania Bara kuangalia barabara mbalimbali. Tunaamini baada ya miezi miwili inayokuja tutatembelea mikao yote ya Tanzania na kuangalia barabara zetu kuhakikisha kwamba tunazitengeneza kama tunavyopanga mikakati yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, alitaka kufahamu Mheshimiwa Rais, aliahidi kujenga kilometa tatu (3). Ni kweli Mheshimiwa Rais ameahidi maeneo mbalimbali kujenga, kwingine kilometa tatu (3), kwingine kilometa tano (5); sisi kama Wizara tumezichukua ahadi zote hizo za Mheshimiwa Rais na tumeziweka kwenye mpango wetu na tunahakikisha kwamba barabara hizo tutazijenga kwa awamu, itategemea upatikanaji wa fedha.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia muda wa kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema amefika mikoa hii 23, kwanza nimshukuru sana kwa kuweka plan ya kujenga barabara ya Mbulu - Karatu, Mbulu - Haydom - Singida kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kuanzia na upembuzi yakinifu? Ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwenye mpango wetu tumeweka barabara hii na hatua inayofuata sasa hivi ni kufanya feasibility study na detail engineering design tutafanya tu pale tutakapopata hela sasa hivi tupo katika mchakato wa kutafuta hela mara hela hizo zitakapopatikana nataka kuhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutakuja kuifanya kazi hiyo ili hatimaye tuijenge kwa kiwango cha lami.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Nakusukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara kutoka Kitosi kwenda Wampembe na barabara kutoka Nkana kwenda Kala na alitoa ahadi kwamba barabara hizi zitapandishwa hadhi ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka, na kwa bahati mbaya sana katika mwaka huu barabara hizi bado hazi bado hazikutengewa fedha za kutosha na Halmashauri haina uwezo wa kutosha kuzihudumia.
Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha kwamba ahadi ya Rais huyu inabaki na heshima na fedha ziweze kupatikana?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpatakama ifuatavyo:-
Ni kweli kuna barabara nyingi Tanzania ambazo zinahitajika kupandishwa hadhina tuna barabara pale ofisini, karibu 150 ambazo zinatakiwa kupandishwa hadhi. Barabara hizi ukizipandisha hadhi maana yake ni kutafuta fedha ili uweze kuweka katika viwango vya barabara za TANROADS.
Lakini nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, wakati tutakapoanza mchakato wa kuzipandisha hadhi barabara hizo na barabara zako tutaziangalia kwa sababu tunaamini kwamba barabara zako ni muhimu sana kwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wako.
MHE. DOTO M. BITEKO:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema mpango wa kujenga ile barabara ya Butengo Lumasa kwenda Masumbwe haupo kwa sasa na kwa sababu Mkoa wa Geita barabara ya Katoro - Ushirimbo ambayo inaunganisha Wilaya tatu za Mkoa wa Geita iko kwenye ngazi ya TANROADS.
Je, Serikali haioni muda umefika sasa barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Katoro - Lulemba - Ushirombo yenye kilometa 56 ni barabara muhimu ambayo inaunganisha Wilaya tatu za Mkoa wa Geita. Sisi kama Serikali tumeitengea pesa barabara hii kila mwaka; kwa mfano mwaka huu wa fedha 2016/2017 tumeitengea takribani shilingi bilioni 1.25 kwa matengenezo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge hapo baadaye tutakapopata fedha ya kutosha tutaifanyia feasibility study na detail engineering design barabara hii na hatimaye tuijenge kwa kiwango cha lami.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, alichokiuliza Mheshimiwa Sabreena ni kwa nini Serikali haitumii mawakala. Mawakala hawana gharama ni kama leo unaposema kwamba TANESCO iuze LUKU yenyewe badala ya kutumia ma-agent wa LUKU. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri na Mkurugenzi Mkuu wa TRL wakae, kwa sababu mimi na Mkurugenzi Mkuu wa TRL na Waziri tumekutana Kigoma, tumekwenda Stesheni, tumeona hali ilivyo na tumekubaliana kwamba the best way ni kuruhusu mawakala kuuza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtu yupo Ilagala, yupo Kibondo, yupo Kasulu, kama alivyosema Mheshimiwa Sabreena, mawakala wauze, tunakuwa tunajua idadi ya mabehewa yatakayokuja Kigoma, abiria watakaoondoka, tiketi zitolewe ziweze kuuzwa. Nashindwa kuelewa Mheshimiwa Naibu Waziri anazungumzia gharama gani hapa, sielewi kabisa, inabidi ujifunze kwa watu wa Nishati na Madini, TANESCO wanafanyaje kwenye LUKU.
Mheshimiwa Waziri tunaomba umsaidie Naibu wako bwana!
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikwenda pamoja na Mheshimiwa Zitto kule Kigoma na tuliona hali halisi na kupitia kampuni yetu ya TRL tuliamua kuanzia sasa hivi tunakwenda kufanya mfumo wa elektroniki ambao watu wanaweza kununua tiketi kwa simu popote pale walipo Tanzania. Tunaanzia na trial ya kwanza kuanzia Mpanda mpaka Tabora wakati wowote kuanzia sasa hivi, halafu tunakwenda Kigoma na Tabora. Ahsante sana.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa matatizo ya Itigi ni sawasawa na matatizo ya Wilaya ya Biharamulo hasa msitu tunaokatisha wa Kasindaga Muleba una matatizo ya mawasiliano na pale kuna barrier nyingi za maaskari ambao wanakaa pale saa zote. Ni lini Serikali itaweza kuwawekea mawasiliano pale hata mnara mmoja angalau wa Tigo au Vodacom?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALINO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 Serikali ina mpango wa kupeleka mawasiliano maeneo yote ambayo yana matatizo ya mawasiliano. Moja kati ya eneo hilo ni hilo alilosema Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na rubani kuwa mmoja na risk za ndege hizi zimewekwa kwa mazingira kwa Rubani mmoja anaweza kurusha hizi ndege kwa kitalaam, lakini liko tatizo la baadhi ya viwanja vyetu kutokuwa na mitambo ya Precision Approach Path Indicator, kutokuwa na mitambo ya Visual Approach Slope Indicator na hizi ni kwa Rubani licha ya kuwa anayo mitambo ya Eye Rescue ya ndege yake, lakini anahitaji Visual Support.
Je, Serikali sasa itafanya nini kuhakikisha System hizi za taa, visually kumsaidia Rubani kuweza kutua, kuokoa maisha ya watu na kumuokoa yeye mwenyewe?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna baadhi ya viwanja vyetu vina matatizo ya vifaa, lakini Serikali tumejipanga kuhakikisha viwanja vyetu vyote ambavyo vinatumika kwa sasa hivi viwe na vifaa vya kisasa kuhakikisha kwamba kuna usalama wa kutosha kwa ajili ya abiria wetu wanaosafiri katika viwanja hivyo vya ndege.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa simu fake mpaka sasa hivi zinaingizwa hapa nchini na wananchi wengi huwa wanazinunua kwa kuona kana kwamba sio simu fake, maana hazina utambulisho rasmi kuonekana hii ni fake ama hii si fake, unaweza ukaiona simu kubwa, ukaipenda kumbe hiyo ndiyo fake yenyewe. Sasa baada ya wananchi kuzinunua simu hizo hapo, TCRA wanazifungia kwa kuona kwamba ndiyo simu fake, mimi naomba kuuliza hivi; kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuwafungia wale wanaozileta badala ya kuwanyanyasa wananchi? Ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli bado zinaingia simu fake lakini mara ukienda kununua simu, ukiiwasha pale kama simu fake haiwezi kuwaka. Sasa kabla ya kulipia simu unaponunua hakikisha kwamba unamwambia yule muuzaji akutilie line pale na ujaribu, kama ni simu fake simu hiyo haiwezi kuwaka kwa sababu simu zote fake sasa hivi zinazoingia nchini haziwezi kufanya kazi.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri.
Kwa kuwa inaonekana hizi shilingi bilioni 2.5 zilizowekwa kwenye bajeti ya 2016/2017 zitalipwa tu pale uthamini utakapokamilika, sasa uthamini huo unatarajiwa kukamilika lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa katika majibu Mheshimiwa Waziri amebainisha kwamba uwanja mpya utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege za Airbus pamoja na Boeing, na uwanja wa sasa wa Bukoba hauwezi kuhudumia ndege za Airbus na Boeing, si kweli kwamba sasa uwanja huu wa Bukoba umeshafikia ukomo sasa jitihada ziharakishwe ili ndani ya miaka mitano uwanja wa Omukajunguti uwe umejengwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, tayari mthamini yuko pale kwa ajili ya kufanya uthamini tena na kazi hiyo imekamilika, na kesho anakwenda Dar es Salaam kumpelekea Chief Valuer thamani aliyoiona pale ili kazi ya ulipaji ianze mara moja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza je, sasa anaona kwamba huo uwanja wa Bukoba uwezo wake utashindwa baada ya miaka mitatu. Naomba kujibu swali hili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uwanja wa Bukoba ulipojengwa design capacity yake (uwezo wake) ulikuwa ni kuchukua abiria 300,000 kwa mwaka, hivi sasa tunavyozungumza Uwanja wa Bukoba unachukua abiria 25,000 tu kwa mwaka. Kwa vile tunaamini hapo itakapofikia mahitaji ya uwanja huo wa kuchukua abiria wengi tutakwenda kujenga uwanja mpya huo ambao anauulizia Mheshimiwa Mbunge.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza nipende tu kusikitika tu kwamba sijui Serikali inafanya kazi kwa upendeleo baadhi ya Wilaya zingine. Tumekaa RCC iliyokuwa Mkoa wa Mbeya na Mheshimiwa Mwambalaswa na Mheshimiwa Mary Mwanjelwa mashahidi hapa. Tumepitisha barabara za Chunya mbili kutoka Ngwala mpaka Kapalala na kutoka Gua ziende ziwe hadhi kwa Mkoa ziwe kwenye TANROADS, toka mwaka 2011 tulikaa RCC tukapitisha leo bado Serikali inasema tunafanyia kazi, miaka sita mnafanyia kazi? Mimi binafsi nimesikitika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti narudia tena, naomba Serikali inijibu kwasababu tayari Songwe imeshakuwa ni Wilaya mpya ni lini watatupatia fedha tupandishe hadhi barabara ya hiyo kutoka Kininga kwenda Ngwala ni kilometa 46. Nikitaka kufanya ziara kule nitembee kwa bodaboda na watu wananielewa hivyo na kuna wanyama wakali na kuna ndorobo nahangaika sana.
Naomba leo Serikali inipe majibu tunahangaika sana wenzenu. Mbona sehemu zingine barabara mnatengeneza? Kutoka mwaka 2011 mpaka leo hatujatengeneza barabara. Naomba Mheshimiwa Waziri uniambie hapa hapa, utaniletea lini barabara hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumfahamisha kwamba Serikali hii haifanyikazi kwa upendeleo. Watanzania wote sisi kwetu ni sawa na nia ya Serikali hii ni kuwajengea miundombinu ya kisasa Watanzania wote. Kama uko Mbeya, kama uko Mwanza, kama uko Shinyanga kazi yetu ni kuwajengea Watanznia miundombinu ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli imechukua muda mrefu na tatizo kubwa ambalo tunalo ilikuwa ni fedha, fedha, fedha, lakini Serikali yetu ya Awamu ya Tano sasa tumejipanga na tutahakikisha kwamba siyo muda mrefu barabara zote tutaanza kuzipandisha hadhi. Lakini naomba waelewe tu changamoto tuliyonayo ni fedha, fedha kwa sababu ukipandisha hadhi barabara maana yake ni fedha unataka utengeneze sasa kwa kiwango cha juu zaidi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
25
Kwa kuwa Serikali ilikuwa imeniahidi kupandisha barabara ya Gulwe, Berege, Chitemo, Mima, Chazima, Igoji mpaka Seluka Ufufu. Barabara hii ni mbaya, Halmashauri haina uwezo. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini sasa mtapandisha hadhi barabara hii pamoja na kuweka lami barabara ya Mbande - Kongwa - Mpwapwa na Kibakwe?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumemuahidi na tunalifanyia kazi mara tutakapopata fedha za kutosha barabara hiyo tutaipandisha kama nilivyosema mwanzo nia ya Serikali hii ni kuhakikisha kwamba barabara zote zinakuwa nzuri na zinapitika wakati wote na pale tunapokuwa na fedha za kutosha tutahakikisha kwamba barabara zote tunazijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ukiliangalia jibu unaona kweli fupi na linaridhisha.
Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, ni nini kinachochelewesha Wizara kuchukua hatua ya kujibu barabara zote ikiwemo hii ya Kakozi - Kapele mpaka Ilonga, kupata majibu mapema iwezekanavyo tofauti na jibu ambavyo limewekwa hapa?
Jambo la pili, barabara hii tulikuwa tunaiombea kupandishwa hadhi karibu mara tatu kukamilisha vigezo, mwaka 2011, mwaka 2013 na mwaka 2015 kupitia Road Board ya zamani tulipokuwepo ya Mkoa wa Mbeya. Wizara mlitushauri tuombe special funds kwa ajili ya kuikarabati barabara hii, tumeomba fedha na mpaka sasa hazijaja.
Kwa nini mnatushauri tuchukue maamuzi ambayo hamuwezi kutekeleza? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli inachukua muda mrefu, baadhi ya kati, kupandisha hizi barabara kwa sababu kuna mchakato lazima na tujiridhishe whether barabara hiyo imekidhi viwango au sivyo. Vinginevyo kila maombi tunayoletewa kama tutazipandisha itakuwa hatufanyi sahihi. Kuna utaratibu ambao umewekwa na vigezo ambavyo vimewekwa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inakidhi vigezo hivyo ndiyo ipandishwe.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara ya Mheshimiwa Silinde, ni kweli barabara hii inakidhi. Kwanza barabara hii inaunganisha mpaka baina ya Tanzania na Zambia; pili inaunganisha Mkoa wa Rukwa ambao kwa upande wa Mkoa wa Rukwa barabara hii ni ya Mkoa lakini kwa upande wa Mkoa wa Songwe ni ya Wilaya (District Road). Kwa vile tutaipandisha na baada ya kuipandisha, fedha hizo tutatoa ili kuikarabati barabara hii.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na kuwepo kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa lengo la kuchangia gharama za ujenzi wa minara maeneo ya vijijini, lakini bado speed ya ujenzi wa makampuni haya umekuwa mdogo sana, kulikuwa napendekezo kwamba sasa Mfuko wa UCSAF ugharamie asilimia 100 ya ujenzi wa minara katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto kwa biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefikia wapi katika kuona umuhimu huu wa kwamba Mfuko wa UCSAF ugharamie minara ya vijijini kwa asilimia 100 badala ya kuyaachia makampuni ambayo kwa kweli yamekuwa mazito kupeleka minara vijijni kwa sababu hakuna mvuto wa kibiashara?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko wa mawasiliano kwa wote unagharamia kuanzia asilimia kumi mpaka asilimia 100; inategemea eneo na eneo. Kama eneo hilo halina mvuto wa kibiashara kabisa mfuko wa mawasiliano kwa wote unagharamia asilimia 100. Kuna tatizo ambalo limejitokeza ni kweli makampuni ya simu yamechelewa kujenga minara ya mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali na kwa kulijua hilo sasa Serikali itapiga faini makampuni ya simu yote ambayo yamechelewa kupeleka mawasiliano kwenye maeneo hayo. Ahsante.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru.
Katika Awamu ya Nne, Serikali ya Ujerumani ilileta maombi nchini mwetu kutaka kufanya ukarabati meli ya MV Liemba ambayo ipo toka Vita Kuu ya Kwanza kama sentiment value ya Serikali ile walitoa offer ya kuitengeneza na kui-refurbish na kuifanya i-comply na sea worthiness kwa asilimia mia moja lakini hawakupewa jibu sahihi.
Je, Serikali mko tayari kukaa nao tena ili sasa offer ile iweze kufanywa na meli ile iweze kutengenezwa na ili iweze kutoa huduma kwa uhakika kwa wananchi wa Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulikuwa na mpango na sasa hivi mpango huo upo, mimi mwenyewe kama mwezi mmoja uliopita nilikuwa na mazungumzo ya kina na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, mpango huo upo na tunaendelea nao ili MV Liemba ambayo imedumu kwa muda mrefu iweze kufanya kazi kama inavyopaswa.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa kulikuwa na mpango ambao ulisemekana kwamba Serikali ilikuwa inanunua meli tatu Korea Kusini na sasa hivi katika majibu ambayo yanatolewa na Serikali ni kama mpango ule umekufa kabisa.
Je, Serikali ituambie ina mpango gani kuhakikisha kwamba hizo meli ambazo zilikuwa zinunuliwe kutoka Korea Kusini zinanunuliwa na kupelekwa katika maziwa yote matatu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mhimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tulikuwa na mazungumzo na Serikali ya Korea na mimi nilikaa miezi miwili iliyopita nilizungumza na Balozi wa Korea na mazungumzo hayo bado yanaendelea, lakini itategemea hasa Exim Bank ya Korea itaamua vipi ndiyo tutaendelea na utaratibu huo.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Waziri. Je, sasa ni lini wananchi hawa wa Delta watapata mawasiliano hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni lini Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana nami bega kwa bega ili twende kuangalia maeneo hayo na kuwapatia ufumbuzi wa mawasiliano hayo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni lini? Katika mpango wetu wa awamu ya pili, mpango huu utaanza mwezi Oktoba mwaka huu ambapo takribani vijiji 1,800 vitapelekewa mawasiliano. Kati ya vijiji hivyo na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge tumeviweka kwenye mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni lini tutakwenda, hiyo tutazungumza mimi na yeye kwenda kuangalia maeneo hayo pia na miradi mingine ya uchukuzi na ujenzi. (Makofi)
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini katika vivuko vilivyotajwa; Kivuko cha Chaulesi kilichopo Makande na Chamba kilichopo Wenje kinaunganishwa na barabara mbili za mkoa ambazo zipo chini ya barabara ya ulinzi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitengeneza barabara hizi kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika muda wote wa mwaka kwa ajili ya kutoa huduma hiyo ambapo watu wa Msumbiji na Tanzania wanatembeleana kwa ajili ya kupata huduma kutoka Tunduru Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa eneo la Chaulesi na Chamba watu wengi wanapita sana kutoka Msumbiji kuja Tanzania kufuata huduma za mahitaji ya muhimu kutoka Tunduru Mjini: Je, Serikali haioni haja ya kuweka Kituo cha Uhamiaji katika maeneo hayo mawili ili kuondoa kero ya Watanzania ambao wanapata tabu wanapovuka Msumbiji kwa ajili ya kukosa hati na kusumbuliwa na askari wa Msumbiji?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara zote za mkoa tunazitengeneza kwa kiwango kizuri ili ziweze kupitika wakati wote wa mwaka. Kwa hiyo, nitaongea na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tutaona mpango gani barabara hii tutaweza kuishughulikia, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu utaratibu wa kuweka Kituo cha Uhamiaji, tutaongea na Wizara ya Mambo ya Ndani kuona kama kuna uwezekano wa kuweka kituo hicho ambacho kitapunguza matatizo kwa wananchi wetu wanaovuka sehemu hizo mbili.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama ilivyo kwenye Jimbo la Busokelo kuna barabara ya Mbalizi kwenda Makongorosi ambayo inapitia kwenye Bonde la Ziwa Rukwa ambayo tumegundua neema ya gesi nyingi sana. Sasa ni lini Serikali itajenga barabara hiyo ya Mbalizi - Makongorosi kwa kiwango cha lami ambayo ni ya Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali tunaifahamu barabara hiyo na tuna mpango thabiti wa kuijenga. Lakini kwanza tupo katika mchakato wa awali hapo utakapo kamilika tutamtafuta mkandarasi ili tuweze kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza. Ni dhahiri kwamba Watanzania wengi wanapoteza maisha katika bahari au katika maziwa zinapotokea ajali na ni ukweli uliowazi kwamba hatuna wataalam wa uokozi wa kutosha kama divers ndani ya nchi yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kikosi kazi chenye wataalam kama divers na wakiwa na zana za kisasa za uokoaji ili kuepusha ajali zinazotokea na kuokoa maisha ya watu wetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tuna kikosi maalum kwa ajili ya uokoaji kama kumetokea ajali, kikosi hicho kinashirikisha pamoja na Jeshi la Wananchi, Marine Police, SUMATRA na wadau wengine mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kawaida ajali ikitokea baharini chombo kinatakiwa kipeleke signal maalum ambayo tunaita distressing signals, signal hiyo ikipelekwa meli zote zilizopo zinakwenda kusaidia kuokoa kwa sababu ukisubiri wewe mpaka wataalam watoke Dar es Salaam na meli imetokea pengine kilometa 200 ulipo itakuwa ni too late. Kwa ufupi tu tuna vikosi maalum ambavyo ikitokea tu vikosi hivyo vinakwenda na vinafanya kazi hiyo. Kwanza Polisi, Jeshi la Wanamaji na Zanzibar kuna KMKM na wataalam wengine wapo ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wale wanaopata ajali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kama Serikali kuwaimarisha hawa kiutaalam ili waweze kufanya kazi na teknolojia za kisasa za uokoaji.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kuwepo kwa mahitaji mbadala ya usafirishaji wa mizigo kutoka Mtwara - Dar es Salaam, Dar es Salaam - Mtwara; na kwa kuwa Kampuni ya Dangote peke yake ina magari 600 ambayo Mheshimiwa Rais aliyazindua na GSM ina magari 300 jumla yote ni magari 900 ambayo yanasafirisha saruji kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam; na kwa kuwa barabara hii inaenda kuharibika; Serikali ituambie ina mkakati gani wa dharura na wa makusudi inaopanga kuchukua ili kuinusuru barabara hii isiharibike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa inavyooneka mtazamo wa Serikali ni kwamba haitaki kufahamu ukubwa wa tatizo hili. Ikitokea Mheshimiwa Naibu Waziri kwa muda mrefu hamjampata mwekezaji kama mlivyosema na barabara hii inaenda kuharibika, je, Serikali haioni kwamba mtakuwa mmeanza kutafuta mkandarasi mwingine ambaye atatumia fedha nyingi kujenga barabara hii ya Dar es Salaam - Mtwara, jambo ambalo ni matumizi mabaya ya fedha za umma? Je, uko tayari kuwajibika kwa hili?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu kuwa na usafiri wa baharini hasa ukiangalia kwamba barabara zetu zinaharibika sana. Ukichukua kwa upande wa Bandari ya Mtwara, sasa hivi ipo meli ambayo inasafirisha saruji ya Dangote kutoka Mtwara kwenda Zanzibar. Takribani kila mwezi meli hiyo inasafirisha tani 6,000 sawa na magari 200. Sasa hivi Serikali ikishirikiana na Dangote na watu wengine tunaendelea kuhakikisha kwamba mzigo mkubwa wa saruji kutoka kwa Dangote unasafirishwa kwa meli ili kuhakikisha kwamba barabara yetu ile inadumu kwa muda mrefu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali la Mheshimiwa Masoud ambalo kwa masikitiko tu niseme Mheshimiwa Waziri hajalijibu kadri ya mahitaji ya watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali letu sisi ni kwamba kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita Serikali ilikuwa haijatengeneza barabara inayounganisha Mtwara na Dar es Salaam. Baada ya utengenezaji wa barabara hii na mara Kiwanda cha Dangote kikafunguliwa ambacho kina magari zaidi ya 1,500 yanayosafirisha cement kutoka Mtwara na kuzileta Dar es Salaam.
Sasa tunataka kufahamu Serikali kwa nini isizuie usafirishaji wa cement kwa kutumia magari ambayo yanaleta uharibifu mkubwa sana kwenye barabara za Mtwara, Lindi kufika Dar es Salaam na badala yake wanawaaachia wasafirishaji wale wale wa magari. Kwa nini wasizuie na wakapa uwezo watu wa kuleta meli wakasafirisha cement hiyo mpaka Dar es Salaam kwa distributors?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza na Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye jibu lake la msingi, kwanza barabara ile imekuwa designed kuchukua mzigo mkubwa, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili mzigo wote wa Dangote wa cement hauendi Dar es Salaam, unaenda sehemu mbalimbali za Tanzania na tatu, Serikali tunaendelea kufanya utaratibu na kampuni mbalimbali za meli kuhakikisha kwamba mzigo huo unakwenda kupitia vilevile upande wa baharini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mazingira ya barabara ya Mtwara yanafanana kabisa na mazingira ya barabara ya kutoka Masasi – Mangaka – Tunduru - Songea - Mbinga kutokana na machimbo yanayoendelea ya makaa ya mawe pale Ngaka, Mbinga. Makaa yale yanasafirishwa kwa malori makubwa yenye zaidi ya tani 30 kupitia barabara ya Tunduru – Mtwara
- Lindi - Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kujenga reli ili makaa yale yaweze kusafirishwa kwa njia ya reli kwa sababu magari yale yanahatarisha usalama wa barabara yetu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hiyo inasafirisha mzigo mkubwa lakini kila kwenye barabara tumeweka mizani ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba magari hayo hayazidishi mzigo ili kuhakikisha kwamba barabara hizo zinadumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuitumia barabara hiyo lakini tutahakikisha kwamba magari hayo hayazidishi mzigo ili kulinda barabara yetu.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kuuliza swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa Zanzibar Sheria ya Makosa ya Kimtandao (CyberCrime Act) bado haijapitishwa, je, inapotokea Mzanzibar kamtendea kosa Mzanzibar mwenzie yaani makosa ya mtandao, naweza kumfungulia kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Sheria ya CyberCrime au Makosa ya Mtandao ni sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria hii inafanya kazi pande zote mbili za Muungano kwa maana ya Zanzibar au Bara. Sheria hii tayari imeshaanza kufanya kazi na tunasimamia maeneo yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimuambie Mheshimiwa Rukia kwamba sheria hii ni ya Muungano na imeshapitishwa kwa taratibu zote.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, hayakosekani.
Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na muafaka. Nawaomba tu Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, wanapojibu maswali kwanza wafanye utafiti kabla ya kuja kujibu humu ndani. Tumekuwa na masikitiko sana back bencher huku na…
Mheshimiwa Spika, hewala!
Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi ni kuhusu meli za Zanzibar na meli hizi ni za local na zimekuwa zikiwa-charged kwa dola na rate ya dola huwa inapanda siku zote.
Je, Mheshimiwa Waziri haoni sababu sasa hivi tariffs zile za muda mrefu na hivi sasa kuchajiwa kwa shilingi ukizingatia zile meli ni za Tanzania na ziko katika sehemu ya local?
Mheshimiwa Spika, la pili, kumekuwa na kilio kirefu sasa bandarini, hata leo hii pana crane pale imekuwa ikisumbua watu, baada ya miezi mitatu leo ndiyo imeondolewa, ni jambo la kupongeza kwa kuwa nauliza swali humu ndani. Lini Mheshimiwa Waziri atafanya ziara pale kuona hali ilivyo? Kuna usumbufu wa malipo; inachukua masaa matatu au mawili kulipa shilingi 10,000? Ni lini Mheshimiwa Waziri atafanya ziara hiyo kwenda kuona hali halisi ilivyo? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa nini tuna-charge kwa dola? Bandarini pale sisi tunafanya biashara na watu wa kutoka nchi mbalimbali kama vile kutoka Tanzania, Rwanda, Burundi na pia Comoro. Lile eneo ambalo wanatumia wananchi hasa kutoka Zanzibar tunafanya biashara na watu wa Comoro ambao wote tunawa-charge kwa dola, lakini inategemea na exchange rate.
Mheshimiwa Spika, sasa kama mtu anataka kulipa dola anaweza kulipa kwa dola, kama anataka kulipa kwa shilingi anaweza kulipa kwa shilingi. Leo tunaona tu kwa sababu dola kila siku inapanda, lakini naamini uchumi wetu utakapokua iko siku currency yetu itakuwa iko nzuri na tutaweza tutamani tulipe kwa dola kwa sababu itakuwa ni cheaper zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu kufanya ziara, ni mara nyingi nafanya ziara kwenye Bandari ya Dar es Salaam na ninategemea hata wiki inayokuja Mungu akipenda, nitafanya hivyo. Naomba tu nimwalike Mheshimiwa Jaku tuwe pamoja katika ziara yangu ili tuweze kuzungumza na wadau wengine jinsi gani tunavyoweza kutatua matatizo ya Bandari yetu ya Dar es Salaam kwa maslahi ya uchumi wan chi yetu.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu lililotolewa na Mheshimiwa Waziri. Hata hivyo, namwomba sana, kwa kuwa Mheshimiwa Rais Magufuli ameagiza hii barabara ijengwe na mpaka sasa hivi anasema kwamba wanatafuta fedha ili ijengwe, naomba sana waitafute hiyo fedha barabara hiyo ijengwe. Pamoja na hilo, nataka niulize swali la nyongeza; kwanza; je, tathmini hiyo ni shilingi ngapi katika barabara hiyo iliyotathminiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika kampeni ya mwaka 2015, Rais Dkt. Magufuli alipokuja Kilwa aliwaahidi watu wa Kilwa kama atashinda Urais atajenga kilometa tano katika Mji Mdogo wa Kilwa Masoko. Sasa pamoja na kwamba ahadi za Rais hizi hazitekelezwi kwa wakati. Je, ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa sababu Urais alishaupata, na yule Bwana akisema jambo basi linakuwa hivyohivyo anavyosema. Je, ni lini itatimizwa ahadi hii ya kilometa tano katika Mji wa Kilwa Masoko?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wetu wa TANROADS walikwenda kufanya tathmini ya barabara hiyo na tukagundua kwamba inahitajika takribani bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha barabara hiyo. Mwezi huu uliopita tu Halmashauri zilipelekewa takribani milioni 400, sasa tunaamini kazi iliyopo mbele yetu ni kutafuta bilioni 2.6 kwa ajili ya kukamilisha barabara hiyo. Mheshimiwa Rais alinipa jukumu hilo na nitahakikisha kwamba pesa hizo tunazitafuta ili barabara hiyo iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kuhusu ujenzi wa kilometa tano Mjini Kilwa Masoko. Ahadi zote alizotoa Mheshimiwa Rais tumezichukua na tunazifanyia kazi na tutahakikisha hivi karibuni tutaanza kuzitekeleza moja baada ya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Barabara inayotoka Lushoto kwenda Mlalo, kilometa 42, ambayo ndiyo inayounganisha Majimbo haya imekuwa ikijengwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kilometa mbili mbili kwa kila mwaka. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuitengea fedha barabara hii ili iweze kurahisisha mawasiliano kati ya Mlalo, Mtae na Lushoto?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Lushoto – Mlalo ni barabara ambayo inahudumiwa na TANROADS Mkoa wa Tanga na inapitika siku zote, mwaka mzima, haina matatizo makubwa. Kazi iliyopo mbele yetu sasa hivi ni kutafuta fedha ili tufanye feasibility study na detailed engineering design ili huko baadaye tuweze kutafuta pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Shangazi kwamba, tutakaa pamoja tutazungumza ili kuhakikisha tunampa mpango mzima ambao tutaweza kuutekeleza ili kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa upande mmoja nakubali kwamba imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na inasubiriwa sasa watafute hela ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Msisitizo wangu, yeye amesema inapitika kipindicha mwaka mzima isipokuwa miezi michache, sasa mimi ndiye ninayetoka Mlimba na juzi tu mwezi Agosti nimetoka Mlimba, hii barabara imewekwa kwa kiwango cha inapitika angalau kwa miezi minne sikatai, kuanzia mwezi wa Septemba mpaka Desemba inapitika lakini kuanzia Januari mpaka Agosti hii barabara haipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna adha kubwa na hii barabara ina umuhimu wake siyo kwamba tu kusafirisha mazao lakini Hospitali ya Wilaya ya Rufaa, Mahakama na Kituo cha Polisi vipo Ifakara kilometa 231. Kwa hiyo, kipindi hicho akina mama, watoto na wazee adha inakuwa kubwa sana. Kwa hiyo, hii barabara licha ya suala la kiuchumi lakini watu wanakufa kwenye hiyo barabara na hakuna Hospitali ya Wilaya kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara hii inapitika kwa miezi nne na inatengenezwa kwa kiwango cha vumbi na hii hela iliyotengwa hapa ni ndogo na kuna madaraja mengi, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuitengea barabara hii pesa za kutosha ili ijengwe kwa kiwago cha changarawe wakati tunasubiri lami? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila siku naongea na Mheshimiwa Waziri Mbarawa, je, yupo tayari sasa kuongozana na mimi kwenda kuikagua hiyo barabara na kuonana na wananchi wamwambie adha halisi wanayoipata kwenye barabara hiyo ili awe na huruma ya kuweka hela ya kutosha? Je, yuko tayari twende tukatembee mpaka Madeke kule Njombe?
Mheshimiwa Spika, naomba maswali yangu haya yajibiwe. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii kuna changamoto hasa wakati wa kipindi cha mvua na sababu kubwa ambayo imesababisha hivi, kwenye maeneo yale hakuna changarawe za kutosha na tunatumia mawe laini (soft rock). Sasa ukiweka mawe laini wakati wa mvua unakuwa na changamoto.
Mheshimiwa Spika, tumeamua tubadilishe mpango ule, tuweke soft rocks pamoja na cement tuichanganye pamoja ili kuhakikisha sasa barabara hiyo inaweza kupitika wakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda kutembea na Mheshimiwa Susan, Mheshimiwa Susan ana speed kubwa kuliko mimi lakini tutakwenda pamoja tu. (Makofi/Kicheko)
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, changamoto zilizopo katika Jimbo la Chilonwa linafanana kabisa na changamoto zilizopo katika Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna ujenzi ambao unaendelea kutoka katika Mkoa wa Tabora barabara ya Inyonga - Ipole kuelekea Mpanda. Barabara hii inajengwa lakini wakandarasi hawaweki alama za ujenzi kwamba kuna madaraja yanajengwa, kuna mashimo yamechimbwa na jambo hili limekuwa linasababisha ajali nyingi kwa wakazi wa Mpanda, kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi.
Nini tamko la Serikali kuhakikisha inatoa maekelezo kwa hawa wakandarasi ili kupunguza ajali za barabarani katika Mkoa wa Katavi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge swali lake la ujenzi wa barabara ya kutoka Katavi mpaka Tabora. Ni kweli Serikali tumeanza ujenzi wa barabara hiyo na hatua tunayokwenda nayo sasa ni hatua ya mobilization yaani makandarasi kwa sasa wanakusanya vifaa vya ujenzi katika maeneo hayo, bado kabisa kazi ya ujenzi haijaanza. Mara itakapoanza kazi ya ujenzi tutaweka alama kuhakikisha kwamba watumiaji wote wanaotumia barabara hiyo wako salama.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hoja ya msingi ambayo inaonekana ni usalama wa raia wakati wakivuka. Mbunge wa Mafia alisema kutoka Nyamisati na Kilindoni, maboti yaliyoko pale ni maboti ya mbao, Serikali ina mikakati ya mrefu ufumbuzi haupatikani.
Swali la msingi sasa, Serikali ina mkakati gani wa ziada sasa kuhakikisha maboti haya yanayochukua abiria yamepewa uwezekano wa kuwa makoti ya kuokolea maisha (life jacket) ili kunusu maisha ya abiria?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukianzia na lile swali la Mheshimiwa Dau, Serikali ina mpango wa kupeleka kivuko eneo lile, kwanza kazi inayofuata ni kufanya feasibility study, baada ya kufanya feasibility study na kujua bei ya hicho kivuko then tutapanga pesa kwa ajili kununua kivuko hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Masoud ni kweli kwamba kuna tatizo hilo na tutahakikisha kwamba sasa hivi tunapeleka vyombo vyote kuhakikisha kwamba vinakuwa na life jacket ili ikitokea matatizo wananchi wale waweze kujisaidia. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la msingi linahusiana na usalama wa wasafiri, na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja maeneo ya Mbulu na kwa kuwa ile barabara ya lami ya kilometa tano ya Hydom na Dongobesh bado. Je, Mheshimiwa Waziri lini sasa atakuja Hydom kuangalia barabara ile ambayo haina usalama kwa wasafiri? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anavyosema Mheshimiwa Mbunge na niko tayari wakati wowote kwenda kutembelea eneo hilo. (Makofi)
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri na niipongeze Serikali kwa kununua boti ndogo ya MV Kuchele. Hata hivyo, MV Kuchele itatumika vizuri sana kama Serikali itajenga majengo katika pande zote mbili au itajenga upande wa Msangamkuu ili kuwezesha kuwa na mtu ambaye analala pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo sasa hivi kama kuna mgonjwa ni lazima ile simu ipigwe na Mganga wa kituo cha Msangamkuu na wakati mwingine mganga wa Msangamkuu anakuwa hayupo Msangamkuu hivyo kuleta changamoto kubwa sana kwa wagonjwa kuweza kuvushwa upande wa pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huu upande wa pili hakuna nyumba ambayo kuna mtu analala pale, huyo ambaye anavusha kwenye hiyo boti analala nyumbani kwake na yeye kama binadamu huwa inachukua muda mrefu sana kuweza kutatua changamoto hiyo. Swali je, Serikali ni lini itajenga hiyo nyumba ya kuwezesha kulala mtu pale upande wa Msangamkuu ili dharura inavyojitokeza iweze kutatuliwa kwa haraka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa nini upande huu wa Msangamkuu ambapo MV Kuchele na MV Mafanikio zinalala kwa nini kusiwe na mtu analala pale ili simu inapopigwa aweze kuvuka kwa haraka na kuweza kutatua changamoto inayojitokeza?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeingia Bungeni lakini wakati tunamaliza Bunge lililopita nilikuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji leo hii ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake nimeendelea kumwomba anielekeze na kuniongoza nitende yaliyo mema yanayompendeza. Pili nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini, lakini tatu, nijibu sasa hoja za Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kutokana na uzoefu alionao, aliyoyataja ndio ambayo sasa hivi tunayapanga, kwamba tuliona changamoto ya kivuko kilichokuwepo kwamba ni kikubwa na ule upande wa Msangamkuu wakati mwingine maji yanakuwa yapo chini sana, tukanunua kivuko kidogo ambacho kinabeba watu nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kivuko hiki usiku kina-park upande wa Mtwara Mjini, lakini ni kweli tunajipanga kujenga nyumba ili walinzi wakae upande wa pili kuweza kuondoa hili tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge analizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ndio nimeingia nitampa majibu Mheshimiwa Mbunge kabla hatujatoka katika hili Bunge kuangalia fedha ambazo tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ili nyumba iwepo askari wakae pale na kuangalia jinsi gani kile kivuko sasa kitakaa ule upande wa pili. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Itoni – Manda kuanzia eneo la Nundu kupitia Kata za Uwemba, Luponde na Matola, ni barabara ambayo imeahidiwa miaka mingi sana na Serikali kwamba itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Nataka kufahamu, ni lini hasa kazi hii itaanza kutekelezwa? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kuhusiana na Barabara ya Itoni – Manda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile tayari tumeshaanza kuitekeleza na ndiyo barabara pekee ambayo inajengwa kwa kiwango cha zege kilometa 50 kutoka Lisitu - Mawengi. Tumeanza na hilo eneo tukaacha kilometa 50 ambazo zinaingia kwenye jimbo lake, lakini nimhakikishie kwamba na hizo 50 nazo tuko kwenye hatua ya kukamilisha taratibu tuweze kuzitangaza ili iweze kuunga sasa kutoka kwenye lami kwenda barabara ya zege.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napongeza majibu mazuri ya Serikali. Lakini la pili nampongeza pia huyu Mhandisi Mshauri Kampuni ya KORAIL kwa kuona kile ambacho hata kufanya upembuzi yakinifu wa wakitaalamu sana kinaonekana.
Kwa kuwa tunazungumzia mradi ambao unakwenda kuhudumia au kutafuta au kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na madini chuma, lakini pia makaa ya mawe, lakini mazao ya kilimo lakini pia urani lakini pia fursa za Ziwa Nyasa zinazotokana na shughuli za uvuvi kutaja machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali mwaka 2016 mpaka leo ni takribani miaka mitatu tangu upembuzi yanikifu ukamilishe kazi yake utoe matokeo.
Sasa je, Serikali inajipangaje kuharakisha utekelezaji wa mradi huu katika hatua inayofuata? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Serikali naamini kwamba amesema mimi kama muuliza swali mmojawapo wa Wabunge na wenzangu wengine Bunge zima tuweze kushirikiana na Serikali kwa kutekeleza jukumu letu la kuisimamia na kuishauri Serikali; na mimi nilikusududia hapo mwanzo kabisa kwamba niweze kujiandaa kwa hoja binafsi kuhusiana na mradi huu. Lakini kwa wakati huu na kwa sasa hivi na majibu haya ya Serikali ya leo yakiniridhisha basi nitaondoa ile azma yangu ya kwenda kwenye hoja binafsi.
Je, inawezekana kuunda Kamati Ndogo ya Wabunge ili waweze kushirikiana kwa karibu kabisa na Serikali katika kutafuta huyo Transaction Advisor? Ama hata hao wawekezaji ili tuweze kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nikuambie kwamba Liganga na Mchuchuma zimekuwepo, mali hii ni ya nchi na kwamba sasa wakati muafaka umefika kwamba sasa mali hii lazima itumike kwa ajili ya manufaa ya nchi. Tayari kama ulivyosema tangu mwaka 2016 Serikali iliona kwamba wakati muafaka umefika, tunahitaji kutumia haya madini kutokana na mahitaji ya kunyanyua uchumi wa nchi. Taratibu zimeshafanyika, Transaction Advisor sasa hivi anatafutwa ili kwenda kwenye mwelekeo sasa ya kupata mwekezaji ambaye ni mzuri atayekubalika na taratibu zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwamba shughuli hii inafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu, ushauri wako ni mzuri Mheshimiwa Mbunge. Lakini sioni kwamba sasa hivi kwa vile mambo yanaendelea kwamba Bunge. Kwa hiyo, niombe tu kwamba uiachie Serikali kwa sababu imeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na inakwenda vizuri.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hii barabara inasuasua sana na ilisimama kwa takriban miezi minne mpaka mitano. Ikumbukwe kwamba Serikai iliingia mkataba wa ujenzi na wahisani wa EU na USAID kwa masharti kwamba Serikali italipia gharama za fidia pamoja na kuruhusu mashine na vifaa vingine viingie nchini bila VAT wala ushuru mwingine.
Mheshimiwa Spika, lakini hivi ninavyokwambia tayari mashine zimeingia lakini zimeshikiliwa na TRA. TRA wanadai kwamba hawatambui mkataba kati ya Serikali na Hazina, wao wanataka fedha zao tu na hii imesababisha hii barabara iende kwa kususasua sana. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri aniambie ni kwa nini TRA wanazishikilia mashine hizi wakati mkataba unaruhusu mashine ziingie bure? Hali hii inasababisha barabara iende kwa kususasua. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nijue kama itawezekana kwa yale madaraja ambayo yapo sasa hivi kama tunaweza tukayachukua tukayapeleka sehemu zingine zenye uhitaji hasa Mlimba na Kilombero kwa sababu sasa hivi huku kwetu barabara zile za mitaa ni mbovu sana. Kwa hiyo tunaomba baadhi ya haya madaraja yafanye kazi kwenye mitaa mingine. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na barabara ya Ifakara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa mgogoro uliokuwepo wa interpretation ya mikataba ukiwepo mkataba wa European Union, lakini pia Bunge hili lilipitisha msamaha wa VAT mwaka jana, kwa hiyo zile taratibu za Kanuni zilikuwa hazijakamilika. Kwa sasa tumeshamaliza kuchambua ule mkataba wa European Union pia na taratibu za VAT nazo zimekamilika. Kwa hiyo mgogoro huo Mheshimiwa Mbunge haupo tena ndiyo maana vile vifaa sasa vimetoka na mkandarasi anaanza kazi. Hilo tumelimaliza, hiyo sasa ni historia.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa yale madaraja ambayo yalikuwa yanatumika, baada ya kukamilisha sasa lile daraja kubwa la zege kiutaratibu yale madaraja huwa tunayapangia kwenda kujenga maeneo mengine kulingana na uhitaji. Kwa hiyo kama uhitaji utakuwepo na kwenye maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, nayo yatakuwa considered kwa ajili ya kupeleka hayo madaraja ili pia yakatumike eneo hilo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda niulize maswali mawili ya nyongeza. Nishukuru pia kwa majibu ya Mhshimiwa Waziri lakini nilikuwa na ushauri mmoja na swali moja. Ushauri kwa kuwa Serikali imeamua kutoa maji kutoka kwenye maziwa makuu kama Ziwa Victoria na maziwa mengine ili kuwapa wananchi wake maji ya kutosheleza ingekuwa vizuri sasa inapobuni miradi hii ikafikiria kuwapa maji watu wanaohusika, lakini pia ikafikiria mbele uhitaji wa maji jinsi ulivyo mkubwa kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Mradi wa Maji wa Ngudu kama ungebuniwa vizuri ungeweza kabisa kutoa maji kwenye vijiji na kata nilizozitaja. Kwa hivyo inapobuni miradi ifikirie kupeleka mradi kwa watu wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kwa kuwa pia nilishapeleka andiko kwaajili ya kupata maji ya Ziwa Victoria kutoka Wilaya Kishapu kwenda Kata ya Sengwa yenye vijiji vya Seng’wa, Mwanundi, Mandela, Mwabomba na Seng’wa yenyewe. Ni lini sasa wizara itaweka pesa kwenye mradi huu ili uweze kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya ziada ya Mheshimiwa Ndaki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni ushauri tumeupokea ambapo na ni mipango ya Serikali kwamba tukianza kutengeneza miradi mikubwa lazima tuangalie maeneo ya mbali ili kuhakikisha wananchi wengi wanapata maji safi na salama na ndio maana sasa hivi miradi yote tunayojenga tunaochukua maji kutoka Ziwa Victoria tunatoa maoteo au tunapeleka maji mpaka kilometa 12 inapopita bomba kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kweli tumepokea andiko lake na andiko hilo lina gharama takribani shilingi bilioni kwa ajili ya kutoa maji kwenye bomba kuu la Kashuasa na kupeleka maji kwenye vijiji vya Manawa, Sengwa, Mwabomba, Mandale na Mwanundi ambao tunalipitia sasa hivi na mara baada ya kulipitia tutafanya utaratibu wa manunuzi ili tuhakikishe kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama kutoka Bomba kuu la KASHUASA.