Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Constantine John Kanyasu (22 total)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu ilijengwa na mradi wa GGM kusaidia kundi kubwa la wasichana wasome Wilayani Geita, shule hii ina hosteli za kutosha na nyumba za walimu.
Je, ni kwa nini shule hiyo imebaki kuwa shule ya kutwa wakati mazingira yake yanafaa kuwa sekondari ya bweni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kanyasu Constantine John, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Wasichana Nyankumbu ilijengwa chini ya mradi wa Geita Gold Mining na kupata usajili Na. S. 1942 mwaka 2006 ikiwa ni shule ya kutwa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne. Aidha, mwaka 2012 iliongezewa kidato cha tano na sita. Hivyo shule hiyo imesajiliwa kuwa ya kutwa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na bweni kwa kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu zinazotumika ili kuisajili shule kuwa ya bweni, ni Halmashauri yenyewe kupeleka maombi Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ili kupata kibali.
Aidha, kabla ya kupata usajili huo, Kamishna wa Elimu atatuma timu ya wataalam katika shule husika kwa ajili ya kuhakiki uwepo wa miundombinu inayohitajika ili shule iweze kusajiliwa kuwa ya bweni.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Je, Serikali ina uhakika gani na usalama wa nchi yetu katika mpaka wa Pori la Akiba la Kimisi na Burigi na Mto Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constatine John Kanyasu Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inaendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori zilizopo ndani ya Mapori ya Akiba yakiwemo ya Kimisi na Burigi katika kukidhi malengo ya uhifadhi endelevu kwa maslahi ya Taifa. Hii ni pamoja na kupambana na uvamizi wa mifugo, shughuli za kilimo, uharibifu wa mazingira na ujangili ndani ya hifadhi hizo. Aidha, pamoja na ulinzi wa ndani ya hifadhi, eneo la mpaka wa Mto Kagera na Pori la Akiba la Kimisi na Burigi limeonesha kuwa na changamoto zaidi zikiwemo za uhamiaji haramu na uingizaji wa silaha ambazo zinatumika kwa ujangili na ujambazi hivyo kulifanya eneo hilo la mpakani kuhitaji ulinzi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ngazi za Wilaya na Mkoa, kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi kwa upana wake katika eneo hii mpakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itaendelea kuimarisha doria ndani ya mapori ili kuboresha uhifadhi wa wanyamapori na kuhakikisha usalama katika maeneo hayo. Aidha, wavamizi wa hifadhi kwa shughuli za mifugo wanaweza kutumiwa kuhatarisha usalama wa nchi. Hivyo tunatoa rai kwa wananchi na wadau wengine kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika dhana nzima ya ulinzi shirikishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama itaendelea kuimarisha ushirikiano na nchi jirani kuhakikisha ulinzi na usalama wa mipakani unakuwa madhubuti ili kudhibiti madhara yanayotokana na uvamizi wa mifugo na wahamiaji haramu.
MHE. VICKY P. KAMATA (K.n.y MHE. CONSTATINE J. KANYASU) aliuliza:-
Mgodi wa GGM - Geita umepewa eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 192 kwa ajili ya kuchimba dhahabu wakati wananchi wamenyang‘anywa maeneo yao.
Je, ni lini maeneo waliyonyang‘anywa wananchi yatarudishwa kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constatine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Vicky Kamata Likwelile, Mbunge wa Geita Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ya Geita Gold Mine Limited yaani GGM inamiliki leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini kupitia leseni namba SML45/99 yenye ukubwa wa kilometa za mraba 196.27 iliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maeneo ambayo mgodi GGM waliyahitaji ndani ya leseni yao kwa ajili ya uchimbaji walifanya mazungumzo na wamiliki wa maeneo hayo na kulipa fidia kwa mujibu wa Sheria Namba Nne ya Madini ya 2010 pamoja na Sheria Namba Tano ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaomiliki ardhi ndani ya leseni ya GGM kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali ambazo siyo shughuli za uchimbaji wanaendelea na shuhguli zao kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo baadhi ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo ambao hawakufikia makubaliano na mgodi wa GGM bado wanamiliki leseni zao za uchimbaji mdogo. Baadhi ya wananchi hao ni pamoja na Bwana Jumanne Mtafuni mwenye leseni ya uchimbaji mdogo PML0001044 pamoja na Bwana Leonard John Chipaka mwenye leseni namba PML0001331 wachimbaji wadogo hawa wanaendelea na shughuli za uchimbaji katika maeneo yao kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na maelezo haya sasa wananchi ambao wamepisha maeneo baadhi yao walilipwa fidia kwa mujibu wa taratibu za nchi hii.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kupitia mtandao wa Twitter alitangaza kuzuia timu yoyote katika kundi „C‟ la Ligi Daraja la Kwanza kupanda daraja kabla ya mechi zao kukamilika na kabla ya vikao halali vya uchaguzi kufanyika:-
Je, Serikali haioni kwamba, maamuzi yalifanywa kinadharia na uonevu mkubwa kwa Timu ya Geita Gold Sport?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Costantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) dhidi ya Timu ya Geita Gold Sports ya kuishusha Daraja kutoka la Kwanza kwenda la Pili hayakuwa ya kinadharia au uonevu. Yalizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika kushughulikia malalamiko yanayotokana na mwenendo wa mashindano husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa TFF baada ya kupata malalamiko kutoka timu za Kundi „C‟ kuhusu timu ya Geita Gold Sports kukiuka Kanuni za Mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza kwa kujitangazia kuwa ni washindi katika kundi hilo hata kabla haijakamilisha kucheza mechi moja, iliielekeza Kamati ya Nidhamu kufanya uchunguzi wa suala hilo na kuchukua hatua stahiki. Kupitia vikao vya maamuzi vilivyokaa kujadili suala hilo ilionekana kuwa, timu ya Geita Gold Sports imekiuka Kanuni za Ligi na hivyo ilistahili kupewa adhabu ya kushushwa kutoka Daraja la Kwanza hadi la Pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa TFF anao utaratibu wa kuvitahadharisha vilabu vinavyoshiriki mashindano ya ligi katika ngazi mbalimbali kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima hivyo, taarifa aliyoitoa kupitia mtandao wa twitter ilikuwa ni sehemu ya tahadhari hiyo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuvitaka Vyama vya Michezo, Mashirikisho, Vilabu na wadau kwa ujumla kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango, maamuzi, chaguzi mbalimbali kwa maslahi ya vyombo hivyo na Taifa kwa ujumla.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:- Wananchi wa Mtaa wa Katoma na Magema katika Kata za Mtakuja na Kalangalula kwa muda mrefu wamezuiwa kuendeleza ardhi zao kwa sababu Mgodi wa GGM ulipima na kuweka vigingi vya mpaka ndani ya makazi yao.
Je, ni lini mgodi huo utawalipa fidia ili kupisha shughuli za mgodi huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 huwataka wamiliki wa leseni za uchimbaji wa madini kuzingatia umbali uliowekwa kisheria kutoka sehemu ambako shughuli nyingine za kijamii zinaendelea. Kwa kuzingatia sheria hiyo, mgodi hulazimika kuwalipa fidia na kuhamisha wananchi wanaoishi ndani ya umbali wa mita 200 kutoka katika shughuli za uchimbaji ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na uchimbaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa GGM mwaka 2007, 2010, 2013 na 2014 ulilipa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 9.67 kwa wananchi 733 wanaoishi ndani ya mita 570 katika maeneo ya Katoma na Nyamalembo. Hata hivyo, kwa kuwa mgodi haujaanza kutumia eneo hilo kwa shughuli za uchimbaji, baadhi ya wananchi waliopata fidia pamoja na wengine wapya, wamejenga tena katika maeneo hayo kwa ajili ya kudai fidia nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa eneo la Magema, mgodi hauzuii wananchi kuendesha shughuli za kilimo na kuendesha shughuli za kimaisha kwa sababu eneo hilo halihitajiki na mgodi kwa sasa. Mgodi utalazimika kulipa fidia kwa kuzingatia sheria husika iwapo mgodi utahitaji kuendeleza eneo hilo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. CONSTANTINE J. KANYASU) aliuliza:-
Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hivi karibuni alitoa agizo la kuwakamata wanawake wanaojiuza:-
Je, zoezi hili limefanikiwa kwa kiasi gani nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa kumekuwa na vitendo vya wanawake kujiuza katika sehemu mbalimbali nchini, hasa maeneo ya mijini. Tatizo hili limekuwa kubwa zaidi katika Mikoa na Miji mikubwa kama vile Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa vifungu vya Sheria Na. 146A, 176(a) na 176A vya Sheria ya Makosa ya Jinai, (Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002), kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, katika kuhakikisha kuwa sheria hii inatekelezwa ipasavyo, viongozi katika mikoa mbalimbali ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wanawake wanaojiuza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inaendelea kufanya operesheni ya kuwabaini na kuwakamata wamiliki wenye madanguro yanayotumiwa na makahaba hao. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutahakikisha wanawake wanaojihusisha na biashara hii wanaendelea kukamatwa ili kulinda heshima, utu na hadhi ya wanawake wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nitumie fursa hii kuwataka wanawake wanaofanya biashara hii kuacha mara moja na kutafuta shughuli nyingine ya kujipatia kipato cha halali. Pia napenda kuwaasa wanaume kuacha kujihusisha katika biashara hii yenye madhara kwa familia zao kiuchumi na kijamii, kwani wao wakiacha wanawake hawa watakosa soko. Aidha, kwa mwanaume kuwa mteja wa biashara hii nalo pia ni kosa kisheria. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Mgodi wa GGM - Geita umekuwa ukitumia milipuko mikubwa wakati wa kulipua miamba ya dhahabu na kusababisha madhara makubwa kwa wananchi jirani na maeneo hayo, kama wale wa eneo la Katoma.
• Je, Serikali inafahamu kwamba nyumba za wananchi zinapasuka na baadhi ya watu huzimia kutokana na mshtuko?
• Je, Serikali inalitatua vipi tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tangu shughuli za ulipuaji zianze katika eneo la Katoma tarehe 23 Septemba, 2014 kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho kuwa milipuko inayofanywa na Kampuni ya GGM imekuwa ikisababisha sauti na mitetemo mikubwa na hivyo kuleta usumbufu na athari mbalimbali kwa wananchi na majengo yao.
Mheshimiwa Spika, kufuatia malalamiko hayo, mwaka 2014 Serikali kupitia Idara ya Madini na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kushirikiana na wananchi wa Mtaa wa Katoma pamoja Geita GGM, waliunda Kamati shirikishi ya kushughulikia malalamiko ya wananchi hao, ijulikanayo kama Blast Monitoring Committee (BMC). Kazi kubwa ya Kamati hiyo ilikuwa ni kukutana kila siku ya ulipuaji na kupokea malalamiko wakati wa mlipuko.
Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2016 Wizara ilituma timu ya wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania – GST kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina ya nyufa za nyumba ambazo zimesababishwa na GGM. Timu hiyo ilibaini uwezekano wa milipuko ya mgodi huo katika shimo la Katoma kuchangia nyufa katika nyumba na maeneo mengine ya Katoma pamoja na Nyamalembo Compound.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa hiyo ya GST, Wizara iliunda timu ya wataalam iliyojumuisha wawakilishi wa wananchi wa maeneo hayo ili kufanya utambuzi wa nyuma zenye nyufa. Kutokana na utambuzi huo, takribani nyumba 890 katika maeneo hayo zilibainika kuwa na nyufa. Hivi sasa uchambuzi wa kina unafanywa kuhusiana na hatua stahiki za kuchukua uchambuzi huo utatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2017 na taarifa yake itatolewa kwa wananchi.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Liko tatizo la uhaba wa dawa na madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.
Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa dawa na Madaktari wa kutosha wanakuwepo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kanyasu Constantine John, Mbunge wa Geita Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu zilizopo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto zinaonyesha kuwa Hospitali ya Mkoa wa Geita ilipandishwa hadhi kutoka iliyokuwa Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018. Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya walengwa wa huduma kwenye hospitali hiyo, hospitali ya Wilaya ya Geita imekuwa ikipata mgao mkubwa wa fedha za kununulia dawa, vifaa tiba na vitendanishi kuliko hospitali za Mkoa isipokuwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga na ile ya Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia hali hiyo, Hospitali ya Geita katika mwaka wa fedha 2015/2016 ilitengewa fedha za Kitanzania shilingi 141,939,184 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 ilipokea kiasi cha shilingi 278,666,525 kiasi ambacho ni takribani mara mbili ya mgao wa mwaka wa fedha 2015/ 2016. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Hospitali hii baada ya kupandshwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, mgao wake umeongezeka na kufikia fedha za Kitanzania shilingi 368,287,841; hadi kufikia mwezi Desemba 2017, Hospitali hii ilikuwa imepokea kiasi cha milioni 168,609,586.94 kwa ajili ya kununua dawa kupitia bohari ya dawa. Hali ya upatikanaji wa dawa kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita ni asilimia 90 kwa zile dawa muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kuna jumla ya Madaktari Bingwa 451 nchi nzima. Wizara imeweka utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo ya Uzamili kwa Madaktari Bingwa kila mwaka wa fedha kwa uwiano wa wanafunzi 100 ndani ya nchi na 10 nje ya nchi. Jumla ya madaktari 236 wanaendelea na masomo na tunataraji ndani ya miaka mitatu watakuwa wamehitimu na kurudi vituoni. Wizara imeanzisha utaratibu wa kuwatawanya Madaktali Bingwa ili kuweka uwiano katika Mikoa yote nchini na sasa jumla ya Madaktari Bingwa 74 ambao walikuwa wakifadhiliwa na Wizara walihitimu masomo ya udaktali bingwa kwenye fani mbalimbali, taratibu za kuwapandisha vyeo na kuwatawanya kulingana na uhitaji katika Mikoa zinaendelea. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Zao la Pamba limeendelea kupoteza mwelekeo kila kukicha na hivi karibuni mbegu walizoletewa wakulima wa Geita hazikuota kwa asilimia 30. Je, ni nini juhudi za Serikali katika kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO allijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba ulibadilika kuanzia miaka ya 1990 baada ya soko huria kuanza. Kutokana na kutokuwepo mfumo rasmi wa utayarishaji wa mbegu za pamba kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003, wakulima walikuwa wakiendelea kutumia mbegu aina ya UK 91 ambayo kwa mara ya kwanza ilitolewa mwaka 1991 na imekuwa ikitumika kwa zaidi ya miaka 25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuwepo kwa magonjwa na wadudu, aina hii ya mbegu ya UK 91 imekwisha poteza sifa za kuendelea kutumika hivyo kuendelea kutumia aina hii ya mbegu ndio chanzo kikubwa cha uzalishaji na tija duni ya zao la pamba. Aidha, kwa kuwa mbegu hiyo hutunzwa na viwanda vya kuchambulia pamba, mara nyingine utunzaji wake huwa duni, hali ambayo hufifisha ubora wa mbegu na kusababisha utoaji wake pia kuwa hafifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kurekebisha mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba kwa kufuata vigezo vyote vya ubora kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu Na. 18 ya mwaka 2003. Aidha, juhudi zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika sasa ni kuzalisha kwa wingi mbegu aina ya UKM 08 chini ya uratibu wa Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru kwa kushirikiana na sekta binafsi na Bodi ya Pamba. Vilevile aina mbili za mbegu mpya za UK 171 na UK 173 zitaanza kupatikana kwa wakulima kuanzia msimu wa 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa tulizonazo ni kwamba mbegu iliyosambazwa kwa wakulima Mkoani Geita haikuwa na tatizo lolote la kuota na hatukuwahi kupokea malalamiko kutoka kwa mtu yoyote kuhusu kutoota kwa mbegu hizo. Tumuombe Mheshimiwa Mbunge pia kama anao ushahidi wa mbegu wa hizo kutoota utupatie ili tufanye utafiti kujua tatizo hilo litakuwa limetokeaje. Aidha, maoteo ya uzalishaji wa pamba msimu huu wa 2017/2018 yanatarajiwa kuwa makubwa sana ambapo kiasi cha tani 600,000 zinatarajiwa kuvunwa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-
Moja ya sababu zinazochelewesha kuanza kwa Mgodi wa Kabanga Nickel ni umeme na reli:-
Je, ni lini reli ya Isaka – Keza kuelekea Burundi na Rwanda itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constatine Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia ushirikiano baina ya nchi za Afrika Mashariki inatambua umuhimu wa ujenzi wa reli ya Isaka – Keza kuelekea Burundi na Rwanda, siyo kwa sababu tu ya kuanza kwa mgodi wa Kabanga Nickel, bali pia kuchochea kasi ya usafirishaji wa mizigo na shughuli za kibiashara na hivyo kuinua uchumi wa nchi yetu na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inatambua kuwa kila nchi ina wajibu wa kutekeleza mradi wa kujenga reli hii kwa sehemu yake. Hivyo, ni wajibu wa kila nchi kukamilisha mradi huo ili kuchochea maendeleo yanayotokana na ujenzi wa reli hiyo kwa kukidhi mahitaji makubwa ya ubebaji mizigo kwenda nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Aidha, hali hii itasaidia pia usafirishaji wa wananchi kwenda mikoani na nchi hizo za jirani kwa wingi na kwa kasi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Tanzania, tayari imeshaanza kujenga kwa kipande cha kuanzia Dar es Salaam – Morogoro kilometa 202 na Morogoro – Makutupora kilometa 336, ikipitia Makutupora – Tabora kilometa 294, Tabora – Isaka kilometa 133 na Isaka – Mwanza kilometa 254 ikikamilika kwa urefu wa kilometa 1,219; na sehemu nyingine ni kutoka Tabora hadi Kigoma kupitia Mpanda – Kalemela – Tabora na Uvinza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga reli kutoka Isaka kupitia Kabanga hadi Rusumo na kuingia Kigali nchini Rwanda, Serikali inakamilisha maandalizi ya kujenga reli hiyo. Mkataba wa usanifu na matayarisho ya zabuni umesainiwa mwezi huu wa Mei, 2018 na Kazi itaanza mwezi Juni, 2018 na zabuni itatangazwa ndani ya mwaka huu wa 2018.
MHE. CONSTATINE J. KANYASU aliuliza:-
Watanzania tuliaminishwa kwamba iwapo Tanzania ikiunganishwa na Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa, tutaimarisha mawasiliano na kupunguza gharama za mawasiliano:-
Je, taarifa hizo zilikuwa sahihi kwa kiwango gani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constatine John Kanyasu, Mbunge mahiri wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi kabisa kuwa kujengwa kwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kumeimarisha mawasiliano na kuleta faida ya kushuka kwa gharama za mawasiliano nchini, pamoja na faida nyinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkongo umewezesha kushuka kwa gharama za kusafirisha masafa kwa umbali unaozidi kilomita 1,000 kwa kiwango cha 2Mbps kutoka Dola za Kimarekani 20,300 mwaka 2009 hadi Dola za Kimarekani 160 kwa mwaka 2015. Hilo ni sawa na punguzo la zaidi ya asilimia 99. Hii imewezesha gharama za huduma za kupiga simu kwa mtumiaji wa mwisho kushuka kutoka Sh.147 kwa dakika mwaka 2009 hadi wastani wa Sh.56 kwa dakika mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya simu na internet kutoka watumiaji 17,642,408 mwaka 2009 hadi kufikia watumiaji 40,080,954 mwaka 2017 kwa watumaiji wa simu; na kutoka watumiaji 520,000 mwaka 2009 hadi kufikia watumiaji 22,995,109 mwaka 2017 kwa watumiaji wa internet. Vilevile gharama za maunganisho baina ya mtandao mmoja na mwingine (interconnection fee) zimeshuka kutoka Sh.115 kwa dakika mwaka 2009 hadi Sh.15.6 kwa dakika mwaka 2018, ambapo imesababisha watoa huduma kuwa na huduma za vifurushi vinavyoruhusu mtumiaji kununua kifurushi kinachomwezesha kupiga simu katika mitandao yote na kutumia internet kwa bei nafuu kuliko ilivyokuwa hapo awali.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU Aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi na Vitendea kazi vya kutosha katika Zahanati mpya 24 zilizojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita?

(b) Je, ni lini Serikali itadhibiti upotevu wa mapato katika Zahanati, Vituo vya Afya hadi Hospitali za Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu Mbunge wa Geita Mjini lenye sehemu (a) and (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Geita ina jumla ya watumishi 162 wa kada mbalimbali ya afya na upungufu wa watumishi 469. Mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali iliajiri watumishi 2,726 na kupanga katika vituo vilivyokuwa na upungufu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri imeomba jumla ya watumishi 126. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya katika kuendelea kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi, ikiwemo watumishi kwenye Halmashauri ya Mji Geita.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudhibiti upotevu wa mapato kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambapo hadi Februari 2021, mfumo wa GoTHOMIS umesimikwa katika hospitali 21 za Mikoa, Hospitali 82 za halmashauri, hospitali teule za Wilaya 22, Vituo vya Afya 385 na zahanati 411. Aidha hatua za kinidhamu na kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa watumishi wanaothibitika kuhusika na upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji Geita inaendelea kufunga mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za Afya na fedha ili kuboresha ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi milioni 28.2 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa Mfumo wa ukusanyaji wa mapato (GoTHoMIS) katika Zahanati 11 kati ya Zahanati 13 zilizopo ambazo hazina Mfumo wa GOT- HOMIS. Hospitali ya Geita pamoja na Vituo viwili vya Afya vilivyopo tayari vimefungwa mfumo wa GoTHOMIS. Ahsante sana.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, nini kinakwamisha ujenzi wa stendi mpya ya Geita Mjini na lini sasa ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi kwenye eneo la ukubwa wa hekta
6.9 unaendelea na upo katika hatua ya usanifu ambapo unafanyika pamoja na usanifu wa miradi mingine ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami nzito zenye urefu wa kilometa 15.4.

Mheshimiwa Spika, kazi za ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi imepangwa kuanza mwaka wa fedha 2022/2023, baada ya kukamilika kwa usanifu. Mradi huu umepangwa kutekelezwa na Serikali kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia. Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, ni zipi sababu za Kiwanda cha Pamba na Mafuta cha Kasamwa kusimamisha uzalishaji kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Pamba na Mafuta cha Kasamwa kilisitisha shughuli za uzalishaji mwaka 2012 kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo teknolojia iliyopitwa na wakati, ukosefu wa vipuri, gharama kubwa za uendeshaji hususani maji na umeme, uhitaji wa idadi kubwa ya wafanyakazi na ukosefu wa malighafi. Ninakushukuru.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, ni upi mchango wa Serikali Kuu katika ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Geita?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 Ibara ya 7(1) mpaka (7), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa na watu binafsi. Hata hivyo, tunaipongeza Halmashauri ya Geita Mji kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu ambao umefikia asilimia 75. Hivyo napenda kutoa wito kwa halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Geita Mji kwa kujenga fedha kutoka mapato yao ya ndani kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo tayari kutoa mchango wa ushauri wa kitaalamu katika ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo unaojengwa katika Halmshauri ya Geita Mji, pale itakapohitajika kama ilivyofanya katika halmashauri kadhaa nchini ikiwemo Halmashauri ya Chalinze, Tunduma, Ruangwa na Taasisi kama vile Bandari na Gymkhana. Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga upya Bwawa la Kasamwa na kutenganisha mwingiliano wa binadamu na mifugo?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Kasamwa lilijengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa huduma za maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, viwanda, kunyweshea mifugo pamoja na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itafanya usanifu kwa ajili ya kukarabati bwawa hilo ambapo pia itajumuisha miundombinu kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha za ukarabati wa Madarasa, Mabweni na Usafiri katika Shule ya Sekondari ya Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Mji Geita ilitumia fedha za ndani shilingi milioni 50 kukarabati mabweni matatu ya Shule ya Sekondari ya Geita. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, shilingi milioni 20 kutoka fedha za CSR zilitumika kukarabati mabweni mawili, shilingi milioni 100 zilitumika kujenga bweni moja na shilingi milioni 40 zilitumika kujenga madarasa mawili mapya. Vilevile katika mwaka 2022/2023, Serikali imepeleka shilingi milioni 360 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mapya matatu katika shule hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kupeleka fedha za ukarabati kwa shule za kitaifa ikiwemo Shule ya Sekondari ya Geita pamoja na ununuzi wa magari kwa ajili ya shule za mabweni kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, Serikali inatambua utaratibu wa Mgodi wa GGML wa ku-blacklist vijana nchini na ni vijana wangapi wapo blacklisted?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imewahi kupata malalamiko kuhusu Mgodi wa GGML ku-blacklist vijana ambao wamesitishiwa ajira zao na Mgodi huo kwa sababu mbalimbali. Ufuatiliaji uliofanyika haukubaini suala hili. Kilichobainika ni kuwa mgodi umeweka utaratibu wa kutunza taarifa za kiutendaji na mienendo ya wafanyakazi wake ikiwemo matendo/matukio ya ukiukwaji wa kanuni na taratibu ambayo mfanyakazi anakuwa amefanya katika kipindi cha ajira yake.

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa kuajiri, Kampuni/Waajiri karibu wote hufuatilia taarifa za utendaji wa waombaji wa kazi kwa waajiri wao wa awali. Hivyo, GGML imekuwa ikitoa taarifa za utendaji na mienendo ya wafanyakazi waliowahi kufanya kazi nao pale inapoombwa kufanya hivyo. Aidha, pamoja na kutoa taarifa hizo, GGML haizuii kwa namna yoyote Mgodi husika kuwaajiri waombaji.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwataka vijana ambao wana uhakika utumishi wao katika Mgodi wa GGML haukuwa na dosari na wanaweza kuthibitisha kuwa wamekuwa black-listed katika kampuni hiyo kuwasiliana na Ofisi yangu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Aidha, nichukue nafasi hii kuwasihi vijana wote kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kujiepusha na athari za kuwa kwenye kumbukumbu mbaya za utumishi wao hali inayokwamisha jitihada zao za kujikwamua kiuchumi na kushiriki katika Ujenzi wa Taifa letu.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kupata viwanja vya michezo na kuvilinda kwani baadhi ya shule zimetumia kujenga madarasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Costantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya vigezo vya kuanzishwa shule ni pamoja na uwepo wa viwanja vya michezo. Michezo ni muhimu kwa kuwa husaidia kuimarisha afya za wanafunzi na kujenga akili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) itafuatilia jambo hili na kujiridhisha, endapo kuna shule ambayo imetumia viwanja vya michezo kujenga madarasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule pamoja na Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia kanuni na taratibu zote zinazohusu usajili na uendeshaji wa shule ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu iliyopo shuleni kama viwanja vya michezo.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, ni lini mianya ya majadiliano yanayopelekea rushwa kwenye mfumo wa ukadiriaji wa kodi kwa Wafanyabiashara itaondolewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ukaguzi na makadirio ya kodi huongozwa na Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438 na Kanuni zake, pamoja na miongozo inayotolewa na Serikali kupitia TRA. Hivyo, mawasiliano yote yanayofanyika baina ya TRA na Mlipakodi kabla ya makadirio ya kodi kutolewa yanaongozwa na misingi iliyotajwa hapo juu. Aidha, TRA inachukua hatua mbalimbali ili kuondoa mianya ya rushwa kama ifuatavyo: -

(i) Kutoa elimu kwa walipa kodi kujua haki na wajibu wao;

(ii) Kuimarisha usimamizi wa sera ya maadili kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania;

(iii) Kurahisisha utoaji wa taarifa za watumishi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kupitia tovuti na kupiga simu kupitia namba za simu zisizo na gharama; na

(iv) Kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika kuelimisha, kuzuia na kushughulikia vitendo vya ukiukwaji wa maadili ndani ya mamlaka.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kuunda, kutumia na kuimarisha utendaji kazi wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kupunguza vitendo vya ubadhilifu na rushwa vinavyosababishwa na utaratibu wa kuonana ana kwa ana kwa Afisa wa Kodi na Mlipa Kodi wakati wa ukadiriaji wa mapato. Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza:-

Je, ni lini Mji wa Geita utakuwa Manispaa kwa kuwa taratibu zote zimekamilika na imefikia viwango vya kupewa hadhi ya Manispaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilipokea mapendekezo ya kupandisha hadhi Halmashauri ya Mji Geita kuwa Manispaa. Mapendekezo hayo yalifanyiwa uhakiki na timu ya Wataalam Kutoka OR-TAMISEMI, kati ya vigezo 21 Halmashauri ya Mji wa Geita ilikuwa imekidhi vigezo 18 sawa na asilimia 85. Vigezo ambavyo havikuwa vimefikiwa na Mji wa Geita ni pamoja na kutokuwa na Mpango Kabambe wa uendelezaji Mji, eneo lililopimwa lisipungue asilimia 75 ya eneo lote kutofikia asilimia 75 zinazohitajika za wakazi waliokuwa wameunganishwa na huduma ya maji. Hivyo, Halmashauri hii haikuweza kupandishwa hadhi kwa kuwa ililazimu kukidhi vigezo vyote kwa pamoja kwa mujibu wa mwongozo wa kuanzisha maeneo ya utawala wa mwaka 2014 ili kupandishwa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Manispaa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, kwa nini NHIF inazuia matibabu ya baadhi ya wagonjwa wenye Bima za Afya wakiwa hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwa na zoezi la uhakiki wa uhalali wa wanufaika wa Mfuko wa Bima ya Afya. Zoezi hilo lilileta usumbufu ambao ungeweza kuzuilika kama wahakiki hao wangetumika wataalamu wenye miiko ya taaluma ya tiba. Wizara ilipopata malalamiko hayo ilifuatilia mara moja na kufanya maboresho ambayo yaliyoondoa usumbufu kwa wateja.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuielekeza Menejimenti ya Mfuko wa Bima ya Afya katika kipindi cha miezi mitatu, ihakikishe inaboresha mifumo ya TEHAMA itakayoweza kuondoa usumbufu na pia kudhibiti udanganyifu pasipo kuwa kero kwa wanufaika wa Mfuko, naomba kuwasilisha.