Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Constantine John Kanyasu (82 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa lakini niwashukuru sana wapiga kura wangu kwa kunipa ridhaa hii ya kuwawakilisha. Niseme kwamba nitajitahidi kutimiza wajibu wangu kadri Mungu atakavyoniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya nikasema kidogo kuhusu tukio lililotokea hapa kwamba limenisikitisha. Kwanza kwa namna ambavyo niliamini baada ya wewe kutoa amri kwamba sasa watu hawa washughulikiwe na baadaye nikaona watu hawashughulikiwi wanabembelezwa, haikunifurahisha sana. Mimi nilitarajia askari wakiwa nje wangepanga mkakati wao wa namna ya kuwashughulikia na wanapokuja ndani wanakuja straight wamekwishajua wanawashughulikia namna gani. Matokeo yake wameanza kutukanwa hapo, vyombo vya dola vinatukanwa na vyombo vya habari vinachukua. Nataka niseme, matukio haya hayawezi kukoma katika mfumo wa Jeshi legelege namna hii. Mwenyekiti anapotoa amri wanaoingia ndani kutimiza amri wanapaswa waache mjadala na wahalifu. Ipo siku watu watakuja hapa wamekamia kufanya maovu na watakuja kuchukua hatua tayari wamekwishaua mtu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wakati mchangiaji mmoja anachangia aliwashambulia sana Wakuu wa Wilaya akasema yeye angetamani kuona Wakuu wa Wilaya wanafutwa. Pengine inawezekana yeye katika Jimbo lake haoni umuhimu wao kwa sababu anatazama zaidi vyeo vyao vile vya kisiasa na namna wanavyoshughulikia wahalifu lakini wananchi wa kawaida nafasi ya Mkuu wa Wilaya ni ya muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya, kwa siku nilikuwa naweza kumaliza migogoro mingi ambayo ingeenda yote Mahakamani, Mahakama ile isingeweza kufanya kazi. Tuna migogoro mingi ya ardhi, kuna watu wanaonewa huko hawawezi hata kufika polisi wakajieleza, hawawezi kwenda mahakamani wakajieleza hata kama haki ni ya kwake akifika mahakamani hawezi kujieleza, kwa Mkuu wa Wilaya wanaongea kwa uhuru na matatizo yao yanasikilizwa.
Kwa hiyo, mimi nasema wananchi waache kupokea hizi propaganda ambazo zinaweza zikawafanya wakashawishika kufikiri kwamba Mkuu wa Wilaya siyo mtu muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumefika hapa watu wanaongea hovyo kwa sababu mwanzo watu wametumia sana vyombo vya habari kupata publicity. Mimi naunga mkono TBC isirushe live na sababu za msingi ziko kwamba watu wametumia vibaya sana nafasi hii na matokeo yake badala ya kuzungumzia vitu vyenye manufaa kwa wananchi, wamekuwa wakiitukana Serikali na wananchi. Kwa hiyo, naomba kusema kwamba msimamo huo ulikuwa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie sasa kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ana vision ya kuona Tanzania inaelekea kwenye viwanda, mimi pia naunga mkono na nafikiri vision yake iko sahihi. Hata hivyo, yapi ni mahitaji muhimu ya kuwa na viwanda na viwe wapi. Tunachokitazama sasa hivi, ikitokea bahati mbaya likatokea tatizo, karibu 75% ya nchi itakuwa giza kwa sababu source ya umeme iko sehemu moja. Katika nchi hizi ambazo tunafikiri tunataka kuanzisha viwanda, kama viwanda vyote vitawekwa sehemu moja basi siyo ajabu siku moja Tanzania tukajikuta zaidi ya 30% ya watu walioko kwenye viwanda wamekosa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba tuanze kwanza kwa kutambua maeneo yapi tunataka kuweka viwanda. Ningetamani kuona tunaanzisha miji ya viwanda. Kwa mfano, kama tutasema tunafanya Singida kuwa mji wa viwanda na likatambuliwa eneo kubwa kuwa la viwanda, basi eneo hilo lipelekewe kila aina ya miundombinu ambayo itasababisha wawekezaji waweze kufika. Hatuwezi kuweka viwanda Singida tukategemea umeme unaotoka Dar es Salaam, ipo siku njia hii ya umeme wa kutoka Dar es Salaam itapata matatizo na viwanda vyote vitasimama. Lazima tuwe na alternative route ya umeme kutoka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, pamoja na wingi wa gesi, tunavyo vyanzo vingine vya umeme. Pale Singida tuna upepo, hadithi hii imeongelewa kwa muda mrefu sana lakini kule Ngara tuna mto Ruvuvu, haukauki, una maji mengi sana. Tuna mradi wa umeme pale ambao Tanzania, Rwanda na Burundi wameamua kufanya kwa ubia, wamekadiria kutengeneza megawatts 70 peke yake lakini wataalamu walisema wangeweza kupata megawatts 300 kama wangewekeza vizuri. Mimi nafikiri ule mto kwa sababu ni source ya Mto Kagera na una maji mengi, badala ya Tanzania kulazimisha kutegemea mpaka kuingia ubia na nchi nyingine tungefikiria namna ya kupata umeme mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda inawezekana wawekezaji wakawa wanakuja lakini wanatukimbia kwa sababu hata waliopo wanalalamika uzalishaji gharama zake ni kubwa sana, tuna kodi nyingi na urasimu mwingi. Kama haya yote tutayarekebisha na tukapata maeneo ambayo ni industrial na yakawekewa kipaumbele cha kuwekewa kila aina ya miundombinu, vision ya Mheshimiwa Rais ya kuweka viwanda inaweza ikatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu ninalotoka tunachimba madini. Limekuwepo tatizo kubwa sana la wawekezaji wakubwa kuchukua maeneo yote mpaka ambayo walikuwa wanachimba wachimbaji wadogo wadogo. Ni kweli, tunaunga mkono wawekezaji wakubwa wapewe maeneo lakini kama Serikali itaendelea kupata pesa wananchi wanaendelea kuwa maskini tutaendelea kuona uchumi unakuwa kwenye Serikali lakini wananchi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu hawana sehemu ya kuchimba. Kila wanapogundua madini anakuja mjanja anawahi Dar es Salaam analipia PL watu wanafukuzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Geita Mjini, Mgodi wa Geita umepewa kilometa za mraba 192 lakini hata katika maeneo ambayo walikuwa wanachimba wananchi kabla hawajapewa walifukuzwa wakapewa wao. Matokeo yake mji ule umedumaa na hauwezi kukua tena kwa sababu kazi ya asili ya watu wa pale ni kuchimba dhahabu. Naomba Serikali, wakati tunafikiria namna ya kuyafanya madini haya yawe na maana zaidi katika uchumi wa kwetu lazima tufikirie namna ya kuwafanya Watanzania waweze kupata maeneo ya kuchimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la namna ambavyo Tanzania haifaidiki na mifugo na madini. Wakati miji hii ikiwa midogo wananchi wenye mifugo walikuwa wanaishi karibu na miji hii. Kadri miji inavyopanuka maeneo ya kuchungia mifugo yanazidi kupimwa na kujengwa nyumba, Serikali haijawahi kutenga eneo kwa ajili ya wafugaji ambao inawaondoa. Matokeo yake maeneo yote haya ambayo tunapima watu wanahamia ambayo zamani yalikuwa machungio ya mifugo sasa hivi kuna nyumba, sehemu zenye majosho kuna nyumba, hivi tunatarajia mifugo hii iende wapi? Hata kama tunasema mifugo hii ipunguzwe, huyo anayekuja kuweka kiwanda hapa Tanzania atapata wapi mifugo ya kulisha kiwanda chake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri Serikali haijatimiza wajibu wake hapa. Tunayo mapori mengi ambayo hayana faida kwa nchi hii. Tukimuomba hapa Waziri wa Maliasili atuletee taarifa ya Pori la Biharamulo limeingiza shilingi ngapi, inawezekana tukachukua wazo la Mheshimiwa Waziri wa Mifugo la wafugaji kulipia wakawa na faida kuliko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyanza Cooperative Union wameshindwa kuendesha viwanda vya pamba kutokana na kuwa na madeni makubwa Benki. Pia kutokana na kupitwa na teknolojia ya viwanda walivyonavyo ambavyo sasa haviwezi kushindana katika soko kutokana na gharama za uzalishaji, kwa kuwa Serikali hivi sasa inataka kufufua viwanda vyote. Napenda kushauri Serikali kwanza kuwasaidia Nyanza kupata mbia ambaye atasaidia mitaji na teknolojia mpya katika ginneries.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita tunalima mananasi bora kabisa hapa Tanzania. Kwa muda mrefu zao la nanasi halijatumika kama kivutio cha uwekezaji na hivyo kupunguza uzalishaji kwa kuwa wakulima hawana soko la uhakika. Naiomba Serikali kupitia agenda ya Tanzania ya viwanda kutupatia mwekezajiwa Kiwanda cha Nanasi Geita na soko la nje la zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda, nashauri kila Mkoa upewe maelekezo ya kupima maeneo maalumu ya viwanda, yaani industrial area. Maeneo haya yatengenezewe hati na yamilikiwe na Halmashauri ili mwekezaji akifika usiwepo usumbufu wa kupata maeneo. Maeneo haya yapewe miundombinu ya umeme, barabara na maji ili kumfanya mwekezaji kuvutika na hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa mitaji, naomba kushauri kwamba Serikali mara itakapokuwa imefanya utafiti katika eneo fulani na kuona panafaa kiwanda, lakini hakuna wawekezaji, utumike mtindo uliotumika Rwanda ambao ni kwamba watu wenye mitaji ya wastani wanaunganishwa kwa hisa na kupewa access ya kukopa kwa collateral kwenye Benki maalumu kama TIB na kuwafanya wazawa kadhaa kumiliki kwa pamoja kiwanda. Haya yamefanyika Rwanda na viwanda vingi vinafanya kazi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Waziri aangalie upya ongezeko la kodi eneo la mapato ya ndani. Kila mwaka tunapoongeza budget projection ya nchi matokeo yake kila biashara inaongezewa kodi. Kuongezeka kwa kodi katika biashara ileile, mtaji uleule na mauzo yaleyale au yaliyopungua kwa zaidi ya asilimia 50, kunasababisha wafanyabiashara wengi kushindwa kulipa kodi, kufilisika na kufukuza wafanyakazi. Serikali iangalie vyanzo vipya kama kuanzisha malipo au tozo kwenye pikipiki zote kwa kuwa wanaoziendesha siyo wamiliki wake. Kuruhusu biashara hiyo kuwa bure maana yake wapo matajiri wengi hawalipi kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali iongeze uwekezaji katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula. Kwa kuwa kama wananchi watawezeshwa vizuri katika kilimo tatizo la fedha litapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iweke mpango mahsusi kuhusu maji. Mpango huo uhusishe ongezeko la Sh.50 kwenye lita ya mafuta ambayo yanaingia nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa ulipaji wa Road Licence uwe tofauti na sasa na nashauri kodi hiyo iunganishwe kwenye bei ya mafuta ambapo kila lita moja iwekewe ushuru maalum wa mafuta kulipia kodi hii. Mfano gari moja linatumia lita 20 kila siku zidisha kwa mwaka mmoja (20x360=7,200 lita). Ukichukua lita 7,200x50% tu ambayo itaongezwa kwa gari ndogo (tax) italipa ushuru wa Sh.360,000. Ushauri wangu hapa ni kwamba Road Licence fixed ikiondolewa na kuwekwa kwenye mafuta Serikali itapata pesa nyingi zaidi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni desturi wawekezaji wa madini kupewa Mining License katika maeneo ya hifadhi ya misitu. Katika maeneo mengi wanayopewa hufyeka miti ovyo na kuchimba humo na kuharibu kabisa mazingira ya asili ya eneo hilo. Mfano katika Mkoa wa Geita maeneo ambayo yalikuwa na misitu mikubwa yote yamefyekwa na sasa ni jangwa. Aidha, sheria inawataka kufanya recovery (reforestation) baada ya kumaliza kazi (exit plan).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba katika kipindi ambacho mgodi unaendelea kuleta madhara ya uharibifu huwapata wenyeji. Hivyo, madhara hayo huwezi kuyafidia baada ya mika 20 kwa kupanda miti. Maoni yangu ni kuwa:-
(i) Serikali ianzishe Sheria mpya ambapo mmiliki wa mgodi awajibike kutunza Maliasili zote katika eneo lake la license tangu siku ya kwanza ya kutoka, kwani kwa utaratibu hivi sasa mwenye license huangalia madini pekee (ardhini) na kutowajibika na uharibifu unaofanywa na wananchi katika eneo lake, isipokuwa kama watagusa madini. Mfano mzuri Geita Mjini msitu wote katika eneo la GGM umekwisha.
(ii) Serikali ianzishe mfumo maalum (Nature Resources Extract Fund) kama ulivyo Norway, USA na nchi za Kiarabu, maalum kwa ajili ya kuja kushughulika na rehabilitation kwenye maeneo yote yanayoathirika na miradi ya wawekezaji ambayo huvuruga kabisa mfumo wa maisha ya watu na wanyama wa eneo husika. Hivyo mfuko huo utasaidia kutoa elimu, majanga ya asili na kurudisha maisha yanayohusika kama kawaida baada ya miradi kukoma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami naomba nianze kwa kutoa pole sana kwa familia zote ambazo zimeguswa na msiba ambao umetokea mjini Arusha kwa kipekee kabisa. Kwa kweli msiba ule ni pigo kubwa kwa nchi yetu, na tunafahamu kwamba kuna tukio linaendelea pale Arusha tunawatakia kila la heri na kwa kweli tunawapa pole nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yupo rafiki yangu mmoja yuko Marekani jana alinipigia simu akaniuliza na nikashindwa kutoa jibu na nilikuwa nataka watu wa Kiswahili watusaidie kutafuta, inawezekana likawa ni neno jipya ambalo linaitwa “Bashite” kutafuta maana ya Kiswahili ili liwekwe kwenye Kamusi. Kwa sababu kuna wakati walioko nje wanashindwa kupata connection ya mazungumzo hayo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwanza kwa kutoa shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwanza kwa kuonesha kwamba anajali michezo, lakini pili kwa upendeleo kabisa wa kuleta uwanja mkubwa wa michezo hapa Dodoma. Mikoa mingi sana haina viwanja vizuri vya michezo na ni nafasi pekee hii katika Mkoa wa Dodoma kupata uwanja ambao unaweza ukawa ni uwanja wa pili wa Kimataifa baada ya uwanja wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, maoni yangu katika suala hili, naiomba Wizara ihakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na vitu vingi vya lazima. Hapa tunapoongea Tanzania hata pamoja na mchango mkubwa wa wasanii wa muziki, wasanii wa ngumi na aina nyingine za michezo, tuna maeneo machache sana ya michezo ya aina hii ambayo yapo. Hatuna ukumbi wa kisasa wa muziki, hatuna ukumbi wa kisasa wa ngumi, tuna maeneo tu ambayo ni ma-hall ambayo ni ya kawaida hayawezi kuhamasisha michezo hii ya Kimataifa. Kwa hiyo kuja kwa uwanja huu niombe wale ambao wanasaidia kwenye mipango wahakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na complex ili uweze ku-accommodate michezo mingi na ya aina mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana wanamichezo wetu wengi, nianze na under 17 ambao kipekee sasa wanaelekea Gabon kwa ajili ya michezo hiyo ya Afrika; niwatakie sana mafanikio mema.

Vilevile niwapongeze sana wachezaji wetu wa Kimataifa walioko nje ambao wanacheza mpira wa kulipwa kama Samatta, Ulimwengu na wengine, niwapongeze sana Mwanariadha Simbu, Cecilia, Ginoka, Magdalena, Emmanuel, hawa wameendelea kuiuza Tanzania kwenye ramani ya Kimataifa. Wasiwasi wangu ni mmoja tu; ni mchango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba mafanikio haya yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, ni bahati kubwa leo tunao akina Samatta, tunao hawa wanariadha wengine na kwa kweli kimsingi nchi hii kwa ukubwa wake na idadi yake ya watu, tungeterajia iwe na watu kama hawa zaidi ya 100.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa kinachoendelea ni kwamba anajitokeza mmoja na yeye anakuwa kama wa dawa. Hii maana yake ni kwamba maandalizi ya kuwapata ha watu huku chini yamekuwa ni madogo na matokeo yake kila anayechomoza anachomoka kwa bahati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye eneo hili, miaka ya nyuma tulipata wanamichezo wengi sana walitokea kwenye Majeshi hasa JKT, Polisi na JWTZ. Nadhani sasa Serikali inapoelekeza kwenye kuchagua vijana hawa kutoka kwenye maeneo mbalimbali kwenye Wilaya iweke kipaumbele sana katika suala la michezo ili kuwapata vijana hawa wanaopelekwa kwenye maeneo haya waweze kuandaliwa vizuri waweze kuiwakilisha nchi yetu. Ni kwa sababu tu kwamba zamani pia tulikuwa na mashirika ya umma ambayo yalikuwa yanaweza kuwa na timu hizi za michezo. Baada ya mabadiliko ya sera, mashirika haya yakabadilisha mfumo matokeo yake ni kwamba hayana tena nafasi ya kuandaa wanamichezo wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani kwamba vyombo hivi vya dola ambayo kimsingi bado vina uwezo mkubwa wa kuwa na bajeti ya kutosha lakini na nafasi ya kuwaandaa vingeendelea.

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kwa kweli niseme ni hotuba nzuri sana, nampongeza yeye pamoja na Naibu wake na Katibu wake Mkuu ambaye ni Mwalimu wangu, lakini napenda kusema upungufu kidogo ambao nimeuona hapa. Kwanza nilitarajia katika taarifa hii nione kwa kina inazungumzia uongozi mbovu na migogoro mingi iliyopo TFF. Kwa sababu ni kupitia mpira nchi yetu inaweza ikatengeneza wanamichezo wengine wapya kama Samatta.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa kabla timu ya Taifa ya Vijana haijaondoka, tulishuhudia vijana wale wanateremshwa kwenye basi kwa deni kubwa la kodi ambalo wanadaiwa TFF pamoja na TRA. Nikatarajia kuona ni namna gani sasa Wizara inaondoa aibu hii.

Mheshimiwa Spika, tuliona mwaka 2016 vyombo hivi vya mpira kama FIFA, CAF na TFF vilikuwa haviingiliwi na chombo chochote cha uchunguzi cha Serikali, lakini mwaka 2016 FIFA, FBI waliingia ndani, miaka kama kumi huko nyuma chombo cha Italia cha Usalama kiliingia ndani kuchunguza.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu sasa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, wakati nachangia katika ripoti yangu mwaka 2016 na hasa nilipogusia suala la rushwa katika Chama cha Mpira cha Tanzania, nilimtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge na awaeleze Watanzania ni chombo gani independent ambacho kilifanya uchunguzi kama ilivyo FIFA, kama ilivyokuwa Italia na kama ilivyokuwa kwenye CAF hapa juzi, Rais mpya wa CAF alipochunguzwa kwa tuhuma za rushwa ambacho kiliihakikishia TFF kwamba sasa ilikuwa na uhalali wa kufanya maamuzi ya kuzishusha timu tatu za Majeshi ya Polisi na JWTZ, lakini pia na timu moja ya Geita Gold Sport ambayo ilishushwa daraja na kupandishwa timu nyingine kutoka nafasi ya tano kwa sababu za kuhisia.

Mheshimiwa Spika, mpaka leo tunazungumza na nimetazama sijawahi kupata hiyo taarifa, pamoja na uchunguzi huo mkubwa uliofanywa na PCCB.

Mheshimiwa Spika, niliahidiwa hapa na Mheshimiwa Waziri, kwamba baada ya uchunguzi huo wahusika watapelekwa mahakamani na hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo hapa kwa Serikali, mahakamani mara nyingi tunashindanisha maneno na inawezekana kabisa kwamba mwenye haki akakosa haki mahakamani kwa sababu ameshindwa kujenga kesi. Hii maana yake ni kwamba pamoja na uchunguzi mzuri wa PCCB na ushahidi wote waliopewa na wahusika kwamba palikuwa na harufu ya rushwa kubwa TFF, mpaka leo inavyoonekana wale watu ambao walituhumiwa na ushahidi wote wanaelekea kuokoka.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nipate ushauri wa Mheshimiwa Waziri, ni kwa namna gani, ameitaja TFF, amezungumzia namna ambavyo anafikiria itaweza kusimamia michezo, lakini hajasema ni kwa namna gani anafikiria kuimarisha utawala bora kwenye TFF? Tunafahamu kwamba kwa mujibu wa sera, hizi ni taasisi ambazo zinajiendesha zenyewe, lakini kimsingi kama kuna rushwa, kama maamuzi yanayofanyika pale siyo ya haki, inakatisha tamaa wadau wa michezo.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, leo ni mwaka mmoja na nusu tangu Geita Gold Sport walipoomba review ya kesi yao baada ya kukata rufaa, TFF hawajawahi kutoa maamuzi wala hawajawahi kusema rushwa alitoa nani? Alipewa nani? Shilingi ngapi? Wameishia kwenda kumfungia mchezaji miaka kumi, wamemfungia kocha miaka kumi ambaye haijulikani pesa alitoa wapi, kwa sababu viongozi wake wote wanaonekana hawana hatia.

Mheshimiwa Spika, nilitaka pia Mheshimiwa Waziri aje atuambie hapa, inapotokea suala kama hili, ni nini hasa nafasi ya Serikali? Kwa sababu tukiruhusu hali hii kuendelea tutafika mahali tutajikuta kwamba michezo ambayo inasemekana ni ajira haiwezi kuwa ajira tena. Wapo Watanzania wengi ambao sasa hivi wanafikiria wafike level ya Samatta, lakini kwa kukatishwa tamaa na matukio yanayoendelea katika TFF unaweza ukajikuta kwamba baadaye watu wote wanaona ni bora waachane na michezo wafanye kitu kingine.

Mheshimiwa Spika, nimelisema hili kwa muda mwingi kwa sababu ni suala ambalo linaigusa timu ya Geita Gold Sport ambayo ni timu inatoka Geita, ambapo wananchi wa Geita waliipandisha kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka kusema, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais kuhusu kiwanja cha michezo, tumeona kwenye bajeti hii, lakini pia bajeti ya TAMISEMI, ni sehemu ndogo sana ya pesa ambayo inaelekezwa kwenye kuimarisha michezo. Kule kwetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na nimepata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba nitoe pongezi kwa hotuba nzuri na kwa kweli ninaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kushiriki katika tukio la uwashaji wa Mwenge pale Geita Mjini, nimpongeze sana kwa hotuba yake nzuri, lakini niwapongeze sana Wizara pamoja na watendaji wote ambao tulishirikiana nao kwa kiwango kikubwa na kwa kweli niwapongeze pia wananchi wa Jimbo la Geita Mjini ambao walijitokeza kwa wingi sana na kuvunja record katika siku ile ambapo Mwenge ulikuwa unawashwa na watu wa Geita hatuna cha kuwalipa tunawashukuru sana kwa sababu ni tukio la kihistoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mliona tulipeleka sherehe zile za kuwasha Mwenge sehemu ambapo ni katikati kidogo ya msitu, lile ni eneo maalum la hekta 12 ambalo tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo na wananchi wa Mkoa wa Geita kama wangepewa nafasi ya kusema neno moja kupitia mwakilishi wao, basi ombi lao kubwa lilikuwa ni msaada wa kupata namna ya kujenga uwanja wa michezo wa Mkoa wa Geita. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba sana hilo lisikike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niende kwenye suala la uvuvi, ninaunga mkono zoezi la kupiga vita uvuvi haramu na tangu nimeanza kuzungumza Bungeni hakuna sehemu niliwahi kukosoa au kuunga mkono uvuvi haramu. Tatizo langu kubwa limekuwa ni approach iliyotumika kupambana na operation yenyewe lakini pia na namna ambavyo huko chini linavyotekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unakumbuka katika matukio tulipokuwa hapa Bungeni niliomba mwongozo baada ya majibu ya Mheshimiwa Waziri alipokiri kwamba nyavu ya dagaa ya milimita nane inaweza ikakamata samaki aina ya Sangara ambao wako chini ya sentimita 55 na akakiri kwamba nyavu ya dagaa inaweza ikaja na samaki wadogo wadogo. Naibu Spika baada ya Naibu Waziri kukiri aliiagiza Serikali tangu siku hiyo iache kusumbua wananchi wanaokamatwa hovyo, wanaopigwa faini hovyo kwa sababu ya kukutwa na samaki wadogo wadogo, kumbe nyavu zina uwezo wa kukamata samaki wa aina mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maagizo hayo ya Bunge hili, wananchi waliendelea kukamatwa, wameendelea kutesema na hali ya maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa ni moja tu tumefikiria sana size ya samaki wa kuuza nje wanaoanzia sentimita 50 kwenda juu wa sangara tukaacha kufikiri kwamba samaki ni maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa. Samaki sangara ambae anauzwa nje anaanzia sentimeta 50 lakini sato ambae hauzwi nje anaanzia sentimeta 25; sasa samaki sangara ambae analiwa Tanzania lazima aanzie sentimeta 50 sawa na anayeuzwa nje kitu ambacho hakiwezekani kwa sababu nyavu zilizoruhusiwa na Serikali zinaweza kukamata samaki size ndogo kuliko ambao wameruhusiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mateso wanayoyapata wananchi ni makubwa sana hivi sasa tunavyozungumza Mtendaji wa Kijiji anakamata samaki, Mgambo anakamata samaki, Polisi anakamata samaki na matukio mabaya kabisa ambayo yanaendelea. Siku moja nilikuwa Geita mama mmoja anakwenda kumsalimia mwanae hospitali ana samaki wanne wamebanikwa amebeba kwenye box ndani ya hiace, ikakamatwa hiace, akakamatwa na mwenye samaki, kosa la mwenye hiace ni kwa nini amesafirisha samaki wanne kwenye box na kosa la mwenye samaki kwa nini amesafirisha samaki wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria haisemi hivyo, sheria inataja kama unataka kusafirisha samaki uwe na usafiri maalum wa samaki, lakini samaki wale ni wa biashara siyo samaki wa kula. Kuna matumizi mabaya sana ya sheria. Tulipotunga kanuni za uvuvi tuliweka Sheria ya Adhabu inasema kuanzia shilingi 50,000 mpaka shilingi 2,000,000, Waziri amekwenda amechukua Sheria za Mazingira akaziingiza kwenye Sheria za Uvuvi, akasahau mukhtadha wa uvuvi ni wa watu maskini anapiga faini kuanzia shilingi 50,000 mpaka shilingi 50,000,000, matokeo yake mtu mwenye mitumbwi miwili; mwenye mtaji wa milioni sita anaambiwa faini ya milioni tano, matokeo yake wavuvi wote wamefilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi tulikamata nyavu mpya tukazichoma moto. Katibu Mkuu wa Wizara wakati anachoma moto alikuwa anasikitika anasema ninachoma moto huku roho inaniuma nyavu za bilioni mbili. Mimi nikajiuliza, mimi nimesoma Mbegani Fisheries, kwa nini hakuchukua nyavu zile akapeleka chuoni wale wanafunzi wakajifunza kukata, kutengeneza single au akawapelekea Nyegezi Fisheries wakajifunza kutengeneza single ili wawape vijana wafanyakazi za uvuvi. Unachukuaje mtaji wa bilioni tatu unachoma moto nyavu mpya halafu unasikitika huku unafanya unachotekeleza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho angefanya angechukua zile nyavu akasema kumbe nyavu iliyoungwa mara tatu inaweza kukatwa ikapatikana single akawapelekea chuoni, akawaambia ninyi chuoni jifunzeni kushona, jifunzeni kukata, wapeni watu wanaohitaji mitaji ingewasaidia. Sasa mtu huyu aliyechomewa nyavu amekubali masharti, amepata hasara. Amendika kibali cha kuomba kuagiza nyavu nje mwezi wa kwanza, leo mwezi wa nne barua zake ninazo hapa hajaruhusiwa, kule wavuvi hawana nyavu, wamekaa, Serikali imekaa, wanaangaliwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kambi ilikuwa na wavuvi 50 hakuna mvuvi hata mmoja, viwanda vile vya samaki vya Mwanza vime-paralyze, wananchi wame- paralyze, Waziri hafanyi maamuzi nini tatizo hapa? Maagizo tukilalamika hayachukuliwi hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana inawezekana Waziri hafahamu yanayoendelea kule chini. Alichokisema Mheshimiwa Musukuma hebu tuunde tume tukasikilize watu. Kuna watu wamekufa kwa sababu ya kukimbia, wanawakimbia mgambo wanakufa kwenye maji na huu ni uonevu wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Kanda ya Ziwa maisha yetu ni uvuvi na ufugaji. Kwenye ufugaji kilichotokea mnajua, kwenye uvuvi kilichotokea mnafahamu, tunakwenda wapi sasa? Kwa sababu bahati mbaya sana Waziri wa Kilimo naomba nikuambie hata pamba tuliyokuwa tunaitegemea juzi imeanza kuliwa na wadudu na bahati mbaya sana matunda nayo yanaliwa na wadudu inawezekana isipatikane. Tunawasababishia umaskini Watazania.

Mheshimiwa iti, tunalolisema hili mimi ninazo karatasi hapa za watu walioomba vibali mwezi wa kwanza mpaka leo hakuna kinachoendelea. Inatuuma sana kwa sababu hatukuingia humu kwa bahati mbaya, tuliingia humu kuja kutetea wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni suala la Watendaji, nilifunga safari nikaenda kwa Katibu Mkuu wa Utumishi kwenda kumuuliza hivi ni kwa nini tangu mwaka 2004 mpaka leo 2018 walikuwa hawajachukua hatua akaniambia mwaka 2004 ilipotolewa maelekezo na Katibu Mkuu Utumishi tuliwapa miaka mitatu, ilipoisha tukawapa miaka mitatu, ilipoisha waliokuwepo wakakaa kimya. Busara ya kawaida ya waliokuwepo kukaa kimya waliona zoezi hili halitekelezeki, ndiyo maana walikaa kimya kwa sababu kama ingekuwa yule aliyekuwepo wakati ule anajua hili suala ni gumu, tangu mwaka 2010 angeagiza watu wafukuzwe kazi, sasa baada ya hapo watu walipata barua za ajira, watu wengine ni pensionable leo unawafukuza kazi unasema hawa wameiingizia Serikali hasara, hili siyo la kweli na halikubaliki na hatuwezi kulikubali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo naomba niliongee ni la wananchi wangu wa Geita. Geita tuna mgogoro na watu wa GGM. Tangu miaka mitatu, minne iliyopita Mawaziri walikuja karibu sita, nyumba za wananchi karibu 800 zimepasuka kwa sababu ya milipuko ya GGM, leo ni miaka mitatu Serikali ikitoa maagizo GGM hawatekelezi. Kuna wananchi pale wanakaa ndani ya vigingi vya GGM miaka 18 hawalipwi fidia, Serikali inatoa maagizo hayatekelezwi. Kuna wananchi Nyakabale, kuna wananchi Mgusu, kuna wananchi Manga wako ndani ya vigingi vya GGM hawaruhusiwi kufuga, hawaruhusiwi kulima, wanakamatwa na maliasili, wanakamatwa na mgodi lakini Serikali ilitoa maagizo mgodi hautekelezi. Nilitaka kufahamu ni nani…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara muhimu kabisa kwetu sisi tunaotoka kandokando ya ziwa, lakini pia maeneo ambayo kwa sasa kilio cha wananchi ni kwa kweli unyang’anyi mkubwa unaoendelea kufanywa na Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kusikitika kidogo, kuna bahati mbaya kwamba tunazungumza hapa kwa nguvu kubwa sana tukiwa tunazungumza maoni ambayo tunaamini waliotutuma ndiyo tunaleta, lakini majibu mepesi yanayokuja ni kwamba tumekamata Wabunge, tumekamata Madiwani ndiyo maana wanalalamika. Kama ziko kumbukumbu za Mbunge aliyewahi kukamatwa anavua samaki au na zana haramu, tungeomba sana leo wakati Waziri anahitimisha aseme ni Mbunge gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu hili linatia woga watu kuchangia kwa kuogopa kutuhumiwa na wengine wanaamini kila anayesema anasema kwa sababu ana maslahi. Kauli hii ilienda mbali zaidi, Mheshimiwa Waziri alikuwa na kikao na viongozi 260 akiandaa Operesheni yake ya Sangara awamu ya tatu. Kauli walizozitoa viongozi aliokuwa nao ni kwamba wanasiasa wanapotosha zoezi hili kwa sababu wana maslahi binafsi na kwa maana nyepesi wanasiasa ni sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ili kuliweka vizuri hili, kwanza ni vizuri sana akaweka kumbukumbu hizi sawa; anawazungumzia wanasiasa wapi wanaopotosha? Kwa sababu tunayoyazungumza sisi tunayazungumza kwa sababu tunayafahamu. Hata hivyo, ni vizuri sana pia viongozi wenzetu huko waliko kwa kuwa tunazungumza kuwawakilisha wananchi, wakafahamu kwamba sisi tunapokuja hapa tunakuja tumetumwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kuchangia; kwanza nianze na suala la operesheni ambayo inaendelea hivi sasa. Tulizungumza hapa na tukaomba mwongozo na tatizo kubwa halikuwa kupinga operesheni ya wavuvi haramu. Naomba niweke kumbukumbu vizuri; naunga mkono operesheni ya kupambana na uvuvi haramu, naunga mkono operesheni ya kupambana na zana haramu, naunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza kipato kinachotokana na uvuvi na mifugo, yote ninaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, unapotaka kufanya operesheni lazima uiwekee mipaa, lakini pawe na ile sense of humanity, kwamba ninaokwenda ku-deal nao ni binadamu. Tunao wavuvi kule ziwani, niliuliza swali na halijawahi kujibiwa mpaka leo. Unapotumia nyavu ziwani ya inchi sita iliyoruhusiwa na Serikali ambayo siyo zana haramu, ukaenda nayo ziwani ikiwa single ina uwezo wa kukamata samaki wanaozidi sentimita 50 na wanaopungua sentimita 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na watu wake wote wanakiri kwamba nyavu hiyo kwa kawaida ratio inaweza ikawa mpaka ten percent ya nyavu ambazo ziko under size. Ni kwa nini operesheni ya Mheshimiwa Waziri inaendelea kukamata watu hata wenye samaki wawili? Kwa nini inaendelea kupiga watu faini ya mamilioni ya shilingi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye sheria, sheria zote za mambo ya uvuvi ambazo zipo kwenye Sheria ya Mwaka 2003 na regulations zake, zinazungumzia faini na ziko very clear. Hata hivyo, kwa sababu operesheni ililenga kukusanya pesa, ililenga kwenda kuhakikisha kwamba watu wanatoka barabarani, mtu anapigwa faini mpaka ya milioni 50 kwa kosa la kukutwa na samaki 10, 15 kwenye mtumbwi, na operesheni hii inalenga wavuvi wakubwa peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza wanakwenda kwenye mwalo wanaangalia mvuvi mwenye mitumbwi zaidi ya 30, wakifika wanamkamata, wakimkamata wanam-detain kwenye gari tangu asubuhi mpaka jioni yuko chini ya ulinzi. Wanamwambia faini ni milioni 20 wanatembea naye, akikosa wanamweka ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye wanasema wewe bila kuleta milioni 20 tutakufungulia kesi ya uhujumu. Watu wanakwenda kuuza nyumba, wanakwenda kuuza ng’ombe. Kwa nini tunafanya hivi kama tuna nia njema na operesheni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliposema maneno haya, majibu yaliyotoka mepesi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri anasema ni kwamba nikiondoa hiyo exemption ya ten percent zoezi zima la operesheni halina maana. Maana yake ni nini kama wataalam wake wamekiri kuna kasoro na lazima iwepo, kwa nini anasema akiondoa haina maana; maana yake ni kwamba lengo la Mheshimiwa Waziri ni kufilisi watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua nyavu ya dagaa ukaenda nayo ziwani leo, ukizungusha ile nyavu ya dagaa utapata sangara, utapata furu na sangara utakaowapata ni wadogo wadogo na watakufa kabla hujawatoa ziwani. Nataka kujua Mheshimiwa Waziri, anawapeleka wapi hao samaki? Kwa sababu hao samaki atakapovua lazima waje na kokoro na dagaa, unawapeleka wapi? Wavuvi wote wa dagaa sasa hivi wanaogopa kuvua samaki, tulikuwa tunanunua kisado cha dagaa Sh.2,500, sasa kimepanda mpaka Sh.15,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niikumbushe Serikali, pamoja na lengo la kutafuta pesa kwenye samaki, samaki ni chakula kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa. Yaani kwa sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa, samaki ni chakula namba moja. Wewe unapofikiria mapato ya nje, fikiria kwanza watu ambao wanafaidika na samaki hao. Kinachoendelea katika zoezi hili ni uonezi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la nyavu; hivi tunavyozungumza, nyavu hakuna madukani. Nyavu za dagaa license amepewa mtu mmoja, yuko Arusha, alikuwa anatengeneza neti za mbu, anatengeneza nyavu za dagaa, matokeo yake nyavu ikiingia ziwani miezi miwili imepasuka. Wavuvi wameacha kununua nyavu za Tanzania wananunua nyavu za magendo kutoka Kenya na Uganda, Serikali inakula hasara. Waziri amezuia nyavu zisiingie Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyavu za sangara; nilizungumza hapa wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu, wafanyabiashara wamelipia nyavu tangu mwezi wa kwanza ziko bandarini, wanaomba kibali nyavu ziingie Tanzania. Wengine wamelipia na ushuru miezi miwili, Waziri hasemi kwa nini anazuia, hasemi ataruhusu lini, watu wanaenda kupigwa storage. Hebu tuwaambie Watanzania tunataka nini hapa kwenye nyavu, nyavu zile Mheshimiwa Waziri anazozitaka ziko bandarini hataki ziingie kwenye soko. Tunataka watu wavulie nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nafahamu na elimu yangu ndogo ya uchumi inaniambia ukitengeneza mazingira ya kupunguza supply kwenye soko ukasababisha demand ambayo haitarajiwi, bei ya nyavu itapanda na matokeo yake watu hawatanunua; ndiyo elimu yangu ya uchumi inavyoniambia. Sasa matokeo yake ni kwamba nyavu imepanda kutoka Sh.16,000 mpaka Sh.45,000 piece moja. Hiyo ambayo imepanda vifaa vyake vimepanda mara nne zaidi kwa sababu wanaoleta wote mali zao zimezuiliwa mpakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka Mheshimiwa Waziri aniambie, anazuia kwa maslahi ya nani? Sielewi. Kwa sababu kama anataka ku-control, apeleke mtu akakague kontena, kama anataka kuzuia atangazie watu wasilete nyavu. Watu wamelipa kodi wanamwomba kibali hataki, wanamwambia hiki, hataki, anataka nini, aseme. Kwa sababu ni rahisi sana kuwatangazia Watanzania wasiingize nyavu kutoka nje
tunategemea viwanda vya ndani, watu hawataleta. Sasa hasemi chochote, amekaa kimya, watu wanakula hasara, nyavu ziwani hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema hapa, nyavu sasa watu wanaanza kuendea nje ya nchi kwa sababu wanaona kuna urasimu; tunakula hasara. Kwa nini hili linatokea; tunamlinda nani? Kwa sababu lengo ni kulinda viwanda vya ndani, wakati huu viwanda vya ndani havina uwezo lazima uvuvi uendelee. Hiki ninachokizungumza ninavyo vielelezo; Mheshimiwa Waziri nimemwomba zaidi ya mara tatu hataki kusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, tulifanya semina akasema amezuia mitungi ya gesi na yenyewe ni uvuvi haramu. Kwenye uvuvi wa bahari, tulipozuia trolling tuliruhusu wavuvi waende zaidi ya mita 50 deep, deep sea ya mita 50 kwa pumzi ya kawaida lazima utumie mitungi ya gesi. Hii inatusaidia sana kwa sababu uvuvi pekee siyo majongoo bahari. Kama lengo ni ku-control majongoo bahari, tungeweka mfumo wa kuweka season fishing kwenye maeneo unasema kuanzia sehemu hii mpaka sehemu hii tutavua kwa miezi mitatu, kuanzia hapa tutavua kwa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya burning totally wale wanaotumia mitungi hawaendi tu kwenye majongoo bahari, kuna uvuvi ambao ni selective ndani bahari. Hii mitungi watu wanaitumia kuzamia chini, maana yake ni nini sasa, tunajielekeza kwenye kufikiri kwa jambo moja tu kwamba wavuvi wote wa mitungi wanakwenda kwenye majongoo bahari. Pia kuzuia kabisa wala sio economically, sio kitu ambacho nafkiri ni sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siungi mkono hoja kabisa, lakini namtaka Mheshimiwa Waziri kwa nia njema kabisa atakapokuja hapa aturidhishe na mateso makubwa wanayopata wavuvi wa Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na nimepata nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Madini. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake na Watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Serikali yangu kwa sheria ambayo tuliitengeneza mwaka 2017 ambayo imeenda kuboresha kabisa shughuli za madini na mpaka sasa tayari waombaji zaidi ya 5,000 kwa taarifa ambazo tunazo, waliyokuwa wamekaa zaidi ya mwaka mmoja kusubiri license wameshapata, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake kwenye suala la CSR, tulipitisha Sheria ya CSR hapa mwaka jana na tukaitengenezea utaratibu ambao utawahusisha Halmashauri ili ziweze kushiriki pamoja na migodi kwenye matumizi ya pesa hasa katika kuchambua miradi na kukubaliana na mgodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, nadhani kuna maeneo ambayo hatukuyaona vizuri, sisi katika maeneo ya migodi tulikuwa na tatizo la migodi hii kuja na mahesabu makubwa sana yanayoonesha wametumia kwenye miradi, wakati miradi iliyofanyika ni midogo na tatizo hili linaonekana bado linaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Geita akaomba watu wa Mgodi wampe orodha ya pesa ambazo zimetumika na miradi, hawakumwambia mradi huu wametumia shilingi ngapi. Nadhani angeona suala hilo angeshangaa sana. Mwaka huu baada ya vikao na Halmashauri tumeona tatizo hili litakuja kuwa kubwa zaidi. Kwa mfano, katika hesabu ambayo Halmashauri ya Mji wa Geita wametuletea kwenye miradi ambayo tumependekeza, cement wao wanasema ni Sh.48,000/= mfuko, wakati pale mjini mfuko ni Sh.18,000/=. Bati la gauge 28 wanasema ni Sh.78,000/=, wakati bati pale mjini ni Sh.22,000/= bati moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nondo ya milimita 16 wamewekwa Sh.52,000/= na kokoto trip moja wameweka Sh.80,000/=. Sasa unaona sheria hii imewapa loophole ya kuendelea kudanganya kama ilivyo kwenye transfer pricing, matokeo yake itakuwa ni Kampuni zao zile zile ambazo wanaziteua, zinawauzia material kwa bei kubwa mara nne zaidi. Mradi wa shilingi milioni 10 watajenga kwa shilingi milioni 80.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Sheria tutazame upya sheria hii ili ikiwezekana Halmashauri Kitengo chake cha Manunuzi kishiriki kwenye Procurement System nzima kwa bei ambazo ni shindani kwenye maeneo husika na kwa kutumia wazabuni na local contents. Bila kufanya hivyo tutarudi kule kule tulikotoka, takwimu zitaonesha mabilioni ya shilingi lakini miradi iliyofanyika ni midogo na pesa zote zinarudi kule zinakotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili, ni suala ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri pia alikuja Geita kulishughulikia. Pale Geita tunao mgogoro mkubwa wa Mgodi wa GGM pamoja na wananchi wa Geita pale, nyumba zaidi 800 zimepasuka kutokana na milipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi wengi ambao wanaishi kwenye vigingi vya migodi kwa zaidi ya miaka 18. Mheshimiwa Waziri alikuja akatoa maelekezo mazuri na kabla ya maelekezo yake Mgodi wenyewe ulifanya study kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Waziri aliyekuwepo, Waziri Kalemani alitoa maelekezo watu wa GST wakafanya study kuonyesha sababu za mipasuko kupitia GST, taarifa zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Ametoa maelekezo lishughulikiwe tangu mwezi wa pili, mpaka leo ninavyozungumza, wananchi wa Geita hawajui hatma ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu hawaoni kinachoendelea. Wenye nyumba zile, wengine wanakufa, nyumba zile zilizopasuka zinaanguka, ripoti zote mbili za Serikali zipo mezani, lakini mambo hayashughulikiwi na hayaendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri sehemu ambazo tuna migogoro ya muda mrefu kama Geita, kabla Mheshimiwa Waziri hajaja kwenye ziara ya Jimbo langu iwe ni vyema kupitia zile documents zilizopo mezani kwake na kujua wenzake walitoa maagizo gani; kuliko kuja kutoa maagizo yale yale yaliyotolewa na Waziri mwingine na yasitekelezwe, wananchi wanaona kama vile Mgodi huu unaidharau Serikali. Tunao wananchi katika maeneo ya Magema, tunao wananchi ambao wameteseka kwa muda mrefu sana na hawajapata haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la tatu. Katika eneo la Mgusu tunao wananchi watatu ambao wamekuwa na kesi na Mgodi tangu mwaka 1995. Majaji sita ambao wameshiriki kwenye kesi ambalo lilikuwa ni kosa la Serikali, Serikali ilikuwa imewapa license wananchi watatu; Felix Isidory Ngowi, Ezekiel Magese na Philipo Paskali na walikuwa wanaendesha leseni zao za utafiti na uchimbaji mdogo mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya, siyo kwa makusudi Kamishna akatoa leseni nyingine juu ya leseni zile zikiwa bado ziko hai, wananchi hawa wakakamatwa, wakapigwa, wakafungwa lakini wakaenda Mahakamani. Majaji sita wote wametoa hukumu iliyowapa haki wananchi kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2005.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Mgodi unaendelea kuonesha unakata rufaa. Jaji Matupa, Jaji Bukuku, Jaji Mero, Jaji Nyangarika, wote hawa wamewapa haki wale wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha sana ni kwamba hukumu nyingine ya mwisho ilitolewa mwaka 2016 na ikatoa permanent injunction ya kuzuia mgodi kuwaondoa wananchi hao kwenye eneo hilo. Kwa namna yoyote wanapokuwa wanaendelea na kesi nyingine, bado Mkurugenzi wa Mgodi na Polisi na wengine walioko pale wameendelea kuwakamata na kuwafukuza na eneo lile lina wachimbaji wadogo zaidi ya 5,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwanza ni aibu kwa Serikali. Majaji hawa wote wameonesha kwamba wachimbaji hawa wadogo wana haki na kosa ni la Kamishna, lakini bado wanaendelea kuonesha kwamba huyu mwenye Mgodi mtu mmoja ana haki ya kuwafukuza watu na kuwanyanyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wapewe haki yao, wamekamatwa zaidi ya mara 20, wanawekwa ndani miezi sita, Mgodi hauji kuendelea na kesi, wanatoka, wanapigwa, mali zao zinachukuliwa, wanafukiwa mashimo bila sababu yoyote ile ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa kwa kweli hawana sababu yoyote ile ya kuendelea kuteseka, kwa sababu vyombo vya Sheria; tuna mazoea wananchi wakifukuzwa huwa wanasalimu amri, wanaondoka. Hawa walikwenda Mahakamani wakafuata utaratibu kwa miaka 20 wameipigania haki yao na wameshinda na hukumu wanayo, lakini Mgodi unaendelea kuwafukuza. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala hili lishughulikiwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la nne, naomba kuishauri Serikali, tunao Mgodi wetu wa GGM pale awali ulikadiriwa kuchukua miaka 30 au 25, lakini baada ya sheria hizi mpya tulizozitengeneza, ule Mgodi unaanzisha pits nyingi na wanafanya kama lashing, matokeo yake ninayoyaona, baada ya miaka mitano watafunga Mgodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoendelea sasa, wakiona tu gharama za kupata madini zimeongezeka, wanahama wanaanzisha pit mpya. Matokeo yake wanakwenda wana-lash badala ya kuchukua miaka 30, tutaachiwa mashimo na mashimo yale ni makubwa, wataondoka kabla sisi wenyewe tuliotarajia kwamba tutachimba madini haya kwa miaka 30 hatujafaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie namna ya ku-control. Kuna maeneo migodi inachukua zaidi ya miaka 50 kwa sababu wanalazimishwa kufanya utafiti na kumaliza madini yaliyoko chini. Shimo lililokwenda milimita 200 ukiondoka leo anayekuja hawezi kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la GST. GST nawapongeza kwa kazi wanazozifanya, lakini nina tatizo moja na GST. Mwaka 2016 walikuwa kule Bukombe, nami nikaomba leseni kupitia wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo langu kama tulivyoshauriwa na Mheshimiwa Waziri, wakapewa leseni. Utafiti wa GST unaonyesha kuna dhahabu. Wamechimba wamekwenda mpaka mita 100 watu hawapati dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana GST, kabla ya kuishauri Serikali iwape wananchi maeneo haya yenye dhahabu, kwa sababu wananchi wanakopa, wanajichanga na pesa zao ndogo, nawaomba GST wahakikishe wanatoa elimu ya kutosha kwamba dhahabu hii ipo umbali gani kwa miamba iliyolala vipi? Tunafika mahali sasa tunaacha kuwaamini, ni bora ukatafute private watu wengine huko waje wakufanyie utafiti kuliko GST kwa sababu wanafanya utafiti wa kijanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, Mheshimiwa Waziri naomba sana wananchi wangu wa Geita Mjini na wananchi wa Mgusu waweze kupatiwa haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuja kusimama tena kwenye Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja. Naunga mkono pia miradi yote ya kimkakati ambayo Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wameileta. Naomba nitumie nafasi hii kuipongeza pia Serikali yangu kwa miradi yote ambayo imekuwa ikiendelea nchi nzima. Tumekuwa tukiona mambo mazuri yanaendelea kufanyika katika nchi nzima. Naamini kwamba haya yanayoendelea yanatokana na kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali nzima pamoja na Wizara yenyewe ambayo anaisimamia Mheshimiwa Dkt. Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na tatizo dogo ambalo lipo sasa hivi. Wakati tunahamasisha ununuzi wa EFD tulikuwa na makampuni mengi ambayo tumeyapa license ya kufanya kazi hiyo. Ipo kampuni ilikuwa inauza mashine za Prima, hawa walikuwa wanaitwa Boston Solution Ltd, mashine zao zinalalamikiwa kwamba hazifanyi kazi na inasemekana wamevunja mkataba na TRA na sasa wale walio na mashine hizo wanaambiwa wanunue mashine nyingine. Kwa hiyo, nataka kupata ufafanuzi kutoka Mheshimiwa Waziri na pia kuomba suala hili liangaliwe vizuri kwa sababu kama mzabuni amemaliza mkataba halafu mashine zile zinakosa kazi tutakuwa tunawarudisha nyuma wananchi wetu ambao wananunua mashine hizi bei ghali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze TRA kwa makusanyo mazuri ya kodi. Wameendelea kufanya vizuri na kuwa na lugha nzuri kwa wananchi katika maeneo yetu tunayofanya kazi. Nadhani speed ya ku-recruit new tax payers ku-enlarge tax base imekuwa ndogo kwa sababu tunaweza tukaendelea kukusanya hela nyingi kwa walipa kodi walewale na kama tax base haiongezeki basi tatizo letu la kuwa na bajeti finyu litaendelea kuwepo, nadhani hata mwaka jana nilijaribu kusema haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mpango kwenye Wizara ya Kilimo. Tunajenga viwanda na nilisema mwaka jana, lakini watumiaji wa bidhaa za viwanda zaidi watakuwa ni Watanzania ambao zaidi ya asilimia 70 ni wakulima. Tuna bahati mbaya sana kwamba katika nchi yetu jua likiwaka hasara ni ya mkulima, mvua zikizidi hasara ni ya mkulima, mazao yakipungua na yakizidi pia hasara ni ya mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema kuhusu Price Stabilization Fund, bado sioni kama ni solution namba moja hiyo peke yake. Nafikiri Wizara na wahusika wajaribu kufanya market intelligence kwani yapo maeneo ambayo wakati wakulima wanaingia kwenye kilimo unaweza uka-forecast ukaona mwaka huu tutakuwa na mahindi mengi, dengu nyingi na vitu vingi, unajaribu kuwatengenezea wakulima soko mapema kabla ya kwenda kwenye mgogoro huu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye vipaumbele vya kilimo pale, suala la kutafuta masoko kwa maana ya sehemu ya kuuzia mazao haya halimo, lipo suala la kujenga maghala na masoko ya mazao kwenye maeneo ya wakulima. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ikipatikana surplus, Serikali kwa sababu inaweka restrictions za kuuza mazao haya nje, tuwe na uwezekano wa kuchukua ile surplus ili isionekane ni laana tena mkulima anapovuna mazao yake. Inapoonekana kwamba sasa Serikali imetosha kununua yale mazao basi tuwe tayari na information kwamba wanaweza kupeleka wapi hawa wakulima mazao yao. Hivi tunavyozungumza watu wengi wanakimbia kilimo kwa sababu wanaona sehemu zote zina hasara, jua likiwaka na mvua zikinyesha kuna hasara na suala hili lina hatari sana siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye suala la bidhaa za viwanda. Sasa hivi tunapozungumza hasa sisi tunaotoka pembezoni mwa nchi kama Geita bidhaa zote hata zinazozalishwa Tanzania ni bei kubwa sana. Amesema hapa mchangiaji mmoja mimi nikawa nakumbuka bei ya nondo ya milimita 16 imetoka Sh.15,000 kwenda zaidi ya Sh.28,000 mpaka Sh.30,000. Sasa tunajiuliza hizi bidhaa zote zinazalishwa Tanzania, tatizo liko wapi? Ukiangalia bei ya bati imetoka Sh.160,000 mpaka Sh.450,000, tatizo lipo wapi na ni ndani ya miaka mitatu. Watumiaji wakubwa wa bidhaa hizi ni wakulima, kama wataendelea kuona bidhaa hizi zinapanda maana yake ni kwamba wataacha kulima na watahamia mjini. Kwa hiyo, tutaanza kutengeneza mgogoro wa watu kutoa vijijini kwenda mjini kwa sababu kile anachokifanya kijijini hakimlipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wenzangu wamesema inawezekana ni utitiri wa kodi, lakini inawezekana tunahamasisha wawekezaji waje na wakati huo huo hatujaangalia ni kwa namna gani huyu mtumiaji wa mwisho hii product inamfikia. Sasa hivi maeneo yetu yale ni rahisi kuagiza bati za kutoka Uganda na Kenya ukazinunua kwa bei rahisi kuliko kununua bati za Tanzania, sielewi tatizo lipo wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Naipongeza sana Serikali mwaka jana ilitenga pesa kwa ajili ya kukarabati shule kongwe, naipongeza sana. Lipo tatizo naliona kuhusu shule za msingi. Nilikusikia juzi unasema hapa ipo shule ina watoto zaidi ya 5,000, mimi kwangu Geita Mjini nina shule tatu ambazo zina watoto zaidi ya 4,500 kwa shule moja na madarasa yapo 16 au 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mmoja, kama inawezekana tuje na mpango kabambe kwenye mpango huu wa kuboresha miundombinu ya shule za msingi, halmashauri zetu haziwezi. Shule yenye watoto 5,000 maana yake ndani ya 5,000 kuna shule 7, lakini miundombinu iliyopo ni ya shule moja. Watoto wanaingia asubuhi wanatoka saa sita, wengine wanaingia saa sita wanatoka saa nane, mwalimu mmoja anafundisha watoto 400, hakuna uniformity. Huyu mwalimu hata angekuwa genius namna gani watoto hawawezi kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba kama tulivyofanya kwenye vituo vya afya na zile shule maalum, tuje na progamu maalum ya kuboresha hizi shule za msingi. Tuzitoe hizi shule kwenye watoto elfu moja na kitu twende kwenye watoto 800 au 1,200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hapa kwenye shule, lipo tatizo la watoto ambao wanamaliza sasa darasa la saba na hawawezi kuchukuliwa wote kwenda sekondari za Serikali na hata sekondari za Serikali zenyewe zimejaa. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Elimu, unajua zamani ilikuwa watu wote tunafanya mtihani unaambiwa haukuchaguliwa, si kwa sababu walikuwa hawapendi twende shule, walikuwa wanaangalia uwezo wa shule. Sasa siku hizi shule moja ya sekondari form one inapokea watoto 700, miundombinu iliyopo ni ya watoto 120, kwa hiyo, miezi sita ya kwanza yote Halmashauri inahangaika kuwatafutia watoto pa kusoma, hawa watoto watakuja kupimwa na mtihani ule ule wa watoto walioanza Januari, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tu-come up na mfumo, tujue kwamba Halmashauri hii ina nafasi 2,000, watoto watakaochaguliwa ni watoto 2,000 na watakaobaki watafute shule nyingine, ndiyo maana zamani watu walikuwa wanasoma kwa bidii. Hauwezi kuwa na mfumo wa kuchukua watoto wote, haiwezekani kwa sababu itakuwa kila mwaka hakuna halmashauri ambayo imekamilisha miundombinu. Tulikamilisha madawati mwaka juzi, sasa hivi hakuna shule yenye madawati ya kutosha na tulikamilisha madarasa hakuna shule yenye madarasa ya kutosha kwa sababu mfumo tulionao sekondari ni kuzoa watu wote, hauwezi kuwa na mfumo wa namna hiyo. Kwa hiyo, ni lazima tufike mahali tuseme kwamba nafasi tulizonazo ni hizi na kunakuwa na cutting point kwamba hapa tumekata cutting point, kama nafasi zipo ziende sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo pia la watoto sasa ambao inaonekana kwamba wanapomaliza darasa la saba au wanamaliza form four katika shule binafsi wanakwenda chuo kikuu halafu inaonekana kigezo cha kupata mkopo chuo kikuu unatakiwa uwe umesoma kwenye shule ya watu wanyonge, hiki kigezo si sahihi. Tunafahamu kwamba wapo watumishi ambao walikuwa na uwezo wa kusomesha watoto wake wawili kwenye shule nzuri lakini amestaafu, sasa kama kigezo ni hicho maana yake ni kwamba watoto wengi sana watakosa mikopo na ndicho kinachotokea sasa hivi, watoto wote wanamaliza darasa la saba wanakwenda kurundikwa sekondari ya Serikali kwa sababu anahofia mwanaye asikose mkopo chuo kikuu. Mimi nashauri, kama inawezekana mtoto yeyote aliyefaulu kwenda chuo kikuu apatiwe mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uvuvi, tulipiga kelele sana hapa Bunge lililopita kuhusu uvuvi. Tunashukuru kwamba Serikali ililifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Serikali ililifanyia kazi. Hoja yangu hapa ni ndogo, wavuvi wa sangara sasa hivi kwenye Kanda yetu ya Mwanza wanalalamika bei imepungua na kosa lilikuwa ni moja. Wakati sisi tunafanya operesheni kubwa wenzetu Kenya na Uganda walikuwa wanaendelea na kuvua na kuuza Ulaya. Kwa hiyo, matokeo yake walikamata masoko yetu kule na sasa hivi wavuvi wetu Kanda ya Ziwa wanakosa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri sasa Serikali, kwa sababu lipo tatizo la wamiliki wote wa viwanda vya samaki kuwa ni wa aina moja, wanafanya cartel, wanakaa wanapanga. Tutafute uwezekano wa kutafuta mtu wa kukaa katikati pale ili asiwe anakubaliana na lugha moja wanayozungumza wale wenye viwanda vya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, Mji wa Geita ulipewa ahadi na Mheshimiwa Rais kujengewa kilomita 10 za lami. Mwaka jana nilipoongea na Waziri aliahidi kuziweka kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2019/2020. Nimeangalia kwenye kitabu lakini hakuna barabara zangu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri anionee huruma hii ni ahadi ya Rais ambayo kwa miaka yote minne imekuwa inaonyeshwa kwenye vitabu lakini barabara hazijengwi. Kwa heshima kubwa, naomba jambo hili Waziri alipe umuhimu wake.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Kwanza naomba
kupongeza Kamati zote mbili kwa taarifa zao nzuri, lakini naomba nianze na tatizo la umeme
kwenye Mji wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku umeme Geita unakatika kila siku zaidi ya mara nne.
Nimezungumza mara nyingi sana na Waziri, nimezungumza na Naibu Waziri na tatizo hili kwa
zaidi ya miezi nane halipatiwi majibu. Nafahamu kuna mradi ambao unaendelea lakini nadhani
speed ya mradi huo ni ndogo sana, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Waheshimiwa Mawaziri
wanisikie kwamba kuna tatizo kubwa sana la umeme katika Mji wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, mji wenyewe wa Geita ule, ni nusu peke yake ndiyo
unaowaka umeme, sehemu zingine umeme hakuna. Tunaambiwa tunasubiri umeme wa REA na
niliongea na Naibu Waziri nikamuomba basi atupe ratiba ya mradi wa REA wa nchi nzima tujue
kwamba Geita unakuja lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, linguine pamekuwepo na malalamiko mengi sana kwamba
watu wanalalamika kwanini Geita uwanja wa ndege umejengwa Chato? Sisi watu wa Geita
ndiyo tunajua. Mheshimiwa Rais akitokea Geita kwenda Chato ni kilometa 160. Ili afike Chato,
magari yanayotangulia mbele yanasimamisha watu matokeo yake kwa saa sita watu
wamesimama Barabarani. Kwa hiyo, solution ni kumjengea uwanja karibu na nyumbani
kuondoa ule usumbufu. Kutoka Geita kwanda Chato ni kilometa 160 kwa hiyo, watu
wanaolalamika kujengwa uwanja Chato ni kwa sababu hawafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili, nilikuwa naiomba tu Wizara ya Mawasiliano isiondoe
sasa nafasi ya kutujengea uwanja wa Mkoa wa Geita kwa sababu hatuwezi kuzuia Mheshimiwa
Rais ule uwanja usijengwe kule. Hata usipojengwa kero yake ni kubwa sana kwa wananchi pale
barabarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu, Mheshimiwa Rais Mgodi ule wa Geita karibu
miaka kumi ijayo utakuwa umeshachimba dhahabu. Geita hii tunayoizungumza ambayo kwa
Mgodi ule ndiyo the leading gold producer hapa Tanzania na karibu ya pili Afrika, wananchi
bado ni maskini. Na ukitazama, sioni dalili za namna ambavyo huu mgodi utabadilisha maisha
ya Wananchi sasa hivi kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, wangeanzisha mfuko wa natural
resources rent extraction ambao unafanyika katika nchi nyingi sana. Kwa mfano, mfuko kama
huu upo Norway, mfuko kama huu upo Marekani. Wakati kazi za madini zinapokuwa
zinaendelea, mfuko maalum kwa ajili ya kuwafanya wananchi wa maeneo yale baada ya
shughuli za madini kuisha waweze kuendelea na mambo mengine unakuwa umeandaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyokwenda sasa hivi, kesho kutwa dhahabu zitakwisha
kama zinavyoisha Kahama, wananchi watabaki maskini, Geita hatuna hospitali, Geita hatuna
barabara, Geita hatuna maji, Geita hatuna kila kitu lakini dhahabu zipo nyingi. Kwa hiyo,
nilikuwa nafikiri kwamba kuna tatizo hapa, siyo suala la kwanza duniani ni tatizo ambalo watu
wengi wameshindwa kulisemea hili. Tukianzisha mfuko huu ambao utatusaidia watu wataweza
kusoma, utaweza ku-deal na humanitarian crisis lakini utaweza kushughulika pia na mambo
mengine ya development kwenye maeneo yale. Sasa hivi tunapata 0.7 CSR kwa miaka 17,
mgodi umejenga shule moja ya wasichana. Kila siku wanaonesha kwenye television, miaka 17
0.8 percent ya CSR wangeweza kuifanya Geita kuwa Ulaya, lakini kwa sababu wanaamua
wenyewe wafanye nini hakuna kinachooneka kimefanyika pale. Maisha ya wananchi wa Geita
inaendelea kuonekana kama vile hawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nashukuru kwa kunipa nafasi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. KANYASU J. CONSTATINE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia Ambulance na pia mgawo na Madaktari wanne ambao tayari wamefika Geita. Kwa bahati mbaya mmoja bado yupo masomoni China mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba yafuatayo:-

(i) Hospitali yetu ya Wilaya imekuwa ya Rufaa ya Mkoa, kwa sasa imezidiwa sana na wagonjwa, gharama za dawa na huduma ziko juu kwa level ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Naomba sana juhudi za kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mheshimiwa Waziri aipe kipaumbele ili kupunguza gharama kwa wananchi.

(ii) Bado tuna uhaba mkubwa sana wa Madaktari Bingwa, Madaktari wa kati na wahudumu wa Afya, kama Nurses na watu wa Maabara. Naomba sana mwaka huu wakati wa mgao wa Watumishi wa Afya, Wizara isaidie kuitazama Hospitali ya Geita kwa jicho la huruma. Pamoja na suala hili kuwa la TAMISEMI bado Wizara ndiyo yenye jukumu.

(iii) Bado hospitali ya Rufaa ya Geita tunahitaji Duka la Dawa la MSD. Kosa kubwa limefanyika Geita ni kupeleka Duka la MSD Hospitali ya Wilaya Chato ambapo hakuna wagonjwa wengi, matokeo yake mahitaji ya msingi yamesahaulika au kupuuzwa. Ombi langu, Duka hili la Makao Makuu ya Mkoa lifunguliwe.

(iv) Ufanisi duni wa MSD, Halmashauri zetu zimekosa dawa muhimu kwenye bohari ya dawa, mafunzo yake, pesa hiyo inatumika kununua vifaa ambavyo siyo vya lazima na kuacha uhaba wa dawa ukiwa pale pale, matokeo yake MSD wanatoa O/S release kwenda kwa Private Vendor’s ambao huuza dawa na vifaa tiba kwa gharama kubwa, mara kumi zaidi ya bei ya soko ambalo watu wa kawaida wananunua. Hii maana yake ni kwamba pesa ya kutosha kutoa huduma mwezi mmoja kwa gharama za Private Vendor’s inatumika siku 10 tu.

Mheshimiwa Mwenyekti, naishauri Serikali kuhakikisha MSD wanazo dawa wakati wote kuepuka kupoteza fedha za umma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Kwanza naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili naomba nimshukuru sana Mungu, kwa kunijaalia kufikia nafasi hii, na kwa kweli kwa kupata nafasi ya kushiriki katika Wizara hii, Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini kipekee kupata nafasi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika juhudi zake za kuwakomboa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa nafasi, na kufanya kazi hii, naamini sifa ya ziada kuliko watu wengine lakini ilimpendeza niweze kumtumikia katika nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ili kuyaweka vizuri maneno yangu, naomba wale ambao huwa wanasoma biblia watasoma katika zaburi ya 116 mstari wa 12 na inasema nimtumikie nini Bwana katika mambo yote aliyonijalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana viongozi wote, Makamu wa Rais, na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote ambao nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa. Kipekee naomba nitumie nafasi hii, kumshukuru sana Waziri wangu wa Maliasili na Utalii kwa namna ambavyo ananipa ushirikiano na kwa kweli kwa namna ambavyo ananipa miongozo mingi katika kufanikisha kazi yake. Ninaishukuru sana ofisi yako na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla, nimepata ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati na naishukuru sana Kamati kwa namna ambavyo imekuwa ikitusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niwashukuru pia wapiga kura wangu. Tulizoea siku zote baada ya Bunge nilikuwepo muda wote jimboni lakini sasa hawanioni lakini wameendelea kuwa na imani na mimi. Ninaishukuru pia familia yangu, kwa uvumilivu wote ambao wameupata hasa katika muda huu ambapo muda mwingi sipati muda wa kufanya kazi na familia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani zote hizo, naomba sasa nitumie nafasi hii kujibu maeneo machache ambayo naweza kupata nafasi kwa dakika hizi kumi na tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, nianze labda na tatizo la udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu. Serikali imechukua hatua nyingi za kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo, mamba na viboko. Kimsingi pamoja na hatua zote ambazo tulikuwa tunachukua, tulikuwa na tatizo kubwa la kanuni; kwa hiyo tumeanza kuandaa kanuni za shoroba na maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori kwa lengo la kuhifadhi na kupunguza migongano baina ya wananchi na wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kuendesha doria za kawaida za pamoja ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya mbinu tofauti kama vile kuweka mizinga ya nyuki, kulima pilipili kwenye mipaka ya mashamba, kuweka oil chafu kwenye maeneo ya mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kushirikiana na halmashauri kuunda na kuwezesha vikundi vya kijamii vinavyodhibiti wanyama waharibifu, kufatilia mienendo ya wanyamapori hususan tembo; na hivi karibuni tulimshuhudia Mheshimiwa Waziri akiwavalisha mikanda ya kielektoniki
yaani (callars) kwa lengo la kubaini mienendo yao. Pia kuendelea na mipango mikakati ya kitaifa ya namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba hivi karibu kumekuwepo sana na tatizo kubwa sana wanyamapori kuzagaa katika maeneo mengi, na hii inatokana kwa kweli na sasa wanyama wamekuwa huru. Mwanzo walikuwa wanawindwa hovyo na kwa sababu hiyo ulikuwa unaweza kufikiri kwamba sasa wanyama wamekwisha Tanzania, lakini baada ya udhibiti mkali, sasa wanyama imekuwa kila unapoamka asubuhi unasikia wanyama wako kila eneo wamezagaa. Kwa hiyo tumeendelea kuweka Mipango Mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo ambayo tunaamini kwamba baada ya mikakati hiyo Wizara yetu itafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika kukabiliana na changamoto ya watu ya kuuwawa na Mamba. Wizara imefanya sensa nchi nzima ambapo mwezi Oktoba mwaka jana mpaka Novemba taarifa ya sensa imeonesha kwamba, mamba wameongezeka katika maeneo yaliyohifadhiwa na mamba wamepungua katika maeneo ambayo hayakuhifadhiwa. Wizara itafanya utaratibu wa kuwavuna hawa mamba na utaratibu huu tayari tunauandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imefanya sensa ya Viboko katika maeneo ya Mafia na maeneo mengine. Takwimu zinaonesha kwamba katika Kisiwa cha Mafia viboko wako sasa kumi na sita na kuna mabwawa matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Changamoto ya wanyama hawa katika kisiwa hiki inaonekana kwamba inapanuka kwa sababu wanashambulia watu na kuvamia mashamba. Wizara itafanya juhudi za kutoa elimu kwa wananchi lakini pia tutawavuna viboko wakorofi ambao wamekuwa wakishambulia watu na mashamba ili kuwapunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu inafahamu kwamba ziko changamoto za malipo yanayotokana na shambulio la wanyama waharibifu. Ni kweli kwamba kifuta jasho kimekuwa ni kidogo lakini na kifuta machozi. Wizara inaendelea kufanya mapitio ya Kanuni za kifuta jasho na kifuta machozi na tayari wataalamu wa Wizara wameandaa andiko na mapendekezo hatua inayofuata ni kupeleka rasimu ya Kanuni ya hizo kwa wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya kanuni hizo yanakwenda sambasamba na mabadiliko ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009. Wizara pia inaendelea kulipa malipo ya kifuta jasho cha machozi kadiri madai yanavyowasilishwa, na kwa mwaka 2018/2019 jumla ya shilingi bilioni moja, milioni mia nne na ishirini sita, laki sita na thelathini na sita na mia tano zimelipwa kwa wananchi 7,320, hawa ni kutoka katika Wilaya 57. Kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni arobaini na mbili zimelipwa kwa wananchi 148 kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa. Malipo hayo yamefanyika tarehe 12 Februari.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba madai yako mengi na yanashughulikiwa; na Mheshimiwa Catherine alitaka orodha ya watu waliolipwa Serengeti, namuomba Mheshimiwa Catherine kama hatajari baada ya kikao hiki, tunaweza tukawasiliana tukampatia hiyo orodha kwa sababu ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, malipo ya kifuta jasho au kifuta machozi yalikuwa yanachelewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuchelewa kwa kuwasilishwa kwa taarifa kutoka kwa waathirika kwa sababu zipo taratibu nyingi ambazo zinatakiwa kupitiwa kabla ya kufikia hatua ya kupata malipo. Wizara kwa kushirikiana na Giz, inaboresha mfumo wa kuwasilisha taarifa kwa kuanzisha kanda nne ambazo zitakuwa zinapokea na kufanya tathimini ya athari zinazotokana na shambulio hilo, ambazo tunazipokea Wizarani kwa njia ya elektoniki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za kuwasilisha madai kwa mujibu wa sheria lakini pia ndani ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maeneo machache tu ya Waheshimiwa Wabunge ambayo walisema yalishatolewa maelekezo na Wizara yangu lakini hayajafanyika. Nikianza na Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, amezungumza kuhusu suala la watu wetu wa TANAPA kugonga mtu na baadaye hawakusimama na haijulikani malipo hayo. Suala hili ni la kisheria linashughulikiwa kisheria na ninaamini pale ambapo mfumo wa kisheria utakapokamilika haki za aliyegongwa zitapatikana kulingana na kheria kwa sababu gari zile ziko insured

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili amezungumzia kuhusu kisima; TANAPA tayari wameshatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Kanda hiyo kukamilisha kisima hicho kama nilivyonitoa maelekezo wakati najibu swali. Kwa hiyo kisima hicho kitakamilika na wananchi watapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Malocha, alizungumzia usumbufu wanaoupata wananchi wa Ziwa Rukwa wanapokwenda kuvua, na akaeleza kwa masikitiko makubwa kwamba wananchi wamekuwa wakinyang’anywa mali zao na mitumbwi yao kubomolewa na afisa wetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara yangu ilishachukua hatua, Katibu Mkuu wa Wizara alituma ujumbe wa maafisa watatu kwenda kuchunguza malalamiko haya ya kinidhamu, ambayo Mheshimiwa Malocha aliyaleta ofisini, pamoja na Mbunge wa Viti maalum na tayari taratibu za kiofisi zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Malocha, baada ya tu ya Bunge hili nilikuwa nimekuahidi kwamba tutakwenda katika eneo hilo kufanya mkutano na wavuvi na kuwasikiliza, na pale ambapo hatua italazimika kuchukua pale pale tutachukua kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Getere, amekuwa akilalimikia kuhusu Kituo chake cha afya ambacho kimejengwa na taasisi yetu ya TANAPA, kimekamilika kwa miaka miwili iliyopita lakini hakifanyi kazi. Ni kwamba tayari uongozi wa TANAPA umeshamwelekeza Mkurugenzi wa Kanda hiyo ya Magharibi kukamilisha kituo hicho ili kiweze kufanya kazi haraka, na tayari pesa za Kituo hiki zimekwisha tengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwepo ahadi ya Mheshimiwa Waziri katika eneo la Kihibu, Waziri alifanya ziara na akaahidi milioni thelathini kwenye jimbo la Mheshimiwa Getere. Tayari aliwaelekeza TANAPA kuhakikisha kwamba pesa hizo zinatolewa na zinatolewa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, kwanza kwa pongezi zao ambazo wametupatia katika Wizara, lakini kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupa. Tuwahakikishie kwamba sisi ni watumishi wao; kwa hiyo pale ambapo wanadhani tunahitaji kutoa ushirikiano tuko tayari muda wote masaa yote kufanya kazi hiyo bila kubagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru sana, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pia naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kupata nafasi ya kusimama mbele ya Bunge hili leo na kuweza kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo ilifanya marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 na tukaja na sheria mpya na kanuni zake ambazo kwa ujumla zimefanya mchango wa kampuni za madini hasa kampuni kubwa ya uchimbaji wa dhahabu pale kwangu Geita GGM kuonekana kwa macho kwa wananchi wa Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia marekebisho hayo ya sheria sasa katika kipindi cha miaka mitatu tu ambayo Bunge hili lilifanya marekebisho, ukifika Geita mjini unaweza ukagundua kwamba marekebisho yale yalikuja katika kipindi sahihi na tayari kuna mabadiliko makubwa na maendeleo makubwa sana ambayo wananchi sasa yanawatoa kwenye mgogoro ambao ulikuwepo awali wa kuona hawa wachimbaji, makampuni makubwa ya madini wanakuja kuchukuwa madini yetu na kutuacha watu maskini, ukifika katika Jimbo langu la Geita Mjini utaona kitu tofauti kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili liliwezekana kwa sababu lilisimamiwa vizuri na naamini katika Mpango huu wa miaka mitano ijayo, yako mambo nataka kuishauri Serikali iendelee kuyafanyia kazi. Kwa mfano, tulipotunga sheria tulizungumza habari ya local content nimsikia Mheshimiwa Rais juzi akisema inafanyika vizuri. Naomba niseme ukweli eneo hili bado halijafanya kazi vizuri, sio kwenye consultation peke yake bado local content katika mazingira ya bidhaa zilizotajwa katika sheria, section 102(2) na (3) tumesema vizuri juu ya bidhaa ambazo hazipatikani Tanzania na tukasema vizuri juu ya namna ambavyo Mtanzania au kampuni ya kitanzania inatakiwa iwe na asilimia ngapi kushirikiana na kampuni ya kigeni ili kuweza kuingiza bidhaa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado eneo hili halijasimamiwa vizuri, bado makampuni makubwa yanayo uza bidhaa za gari katika migodi ni makampuni ambayo yamesajiliwa nje na makampuni ambayo yanaleta bidhaa moja kwa moja kutoka nje kuingiza Tanzania. Maana yake ni nini? Kama mgodi matumizi yake makubwa ni kwenye services, maana yake asilimia zaidi ya sitini ya mapato ya mgodi ni kwenye services. Kama mgodi huo una mapato yake ya dola labda milioni 300, sixty percent ya dola milioni 300 ni kwenye gharama za uendeshaji, kama nusu ya hizi zinafanya manunuzi nje, maana yake Serikali inapoteza pesa nyingi sana. Kwa hiyo, ushauri wangu eneo hili lisimamiwe vizuri, ufanyike ukaguzi, sheria ime-provide, imetoa maelekezo migodi hii kila baada ya miezi miwili, kutangaza ni bidhaa gani ambazo inazitaka kutoka nje ili kuruhusu Watanzania waweze kuziingiza. Hata hivyo, bado zimekuwa hazifanyi hivyo na kama zinafanya inafanyika kwa kificho kiasi wafanyabiashara wengi wenye uwezo wanashindwa kupata nafasi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya sheria hii tulizungumza habari ya CSSR, inajulikana wazi, kwenye own source tunasema service levy watalipa 0.3 percent, lakini kwenye CSSR sheria imebaki kimya imeacha jambo lile liko wazi; wengine wanasema 0.7, wengine wanasema ni discretion ya investor. Sasa inatufanya tushindwe kuitumia vizuri hii sheria kwa sababu ni vizuri pamoja kwamba pesa hii ni ya mwekezaji iprovide iseme ita-range kutoka asilimia ngapi kwenda asilimia ngapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kuna shida moja kubwa ambayo naiona pamoja na kusifia tunafanya vizuri sana kwenye mahusiano na mgodi, lakini bado shida tuliyonayo kubwa na ambayo nafikiri Serikali inabidi inatakiwa ifanyie kazi ni kwamba pesa hizi za CSSR zinatumika unakuta gharama zake ni kubwa kuliko gharama halisi ambazo ziko kwenye maeneo ya masoko ambayo tunanunua bidhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa tu mfano, sisi tunapata CSSR ya bilioni 10, lakini gharama ya CSSR ile unaweza ukakuta mnabishana kuhusu ujenzi wa mradi ambao ungejengwa na halmashauri ungegharimu milioni hamsini, gharama ya ujenzi wa CSSR kwa sababu pesa ni ya kwao utajenga kwa milioni 150. Kwa hiyo nasema bado sheria hii haiweki wazi sana kwanza ni asilimia ngapi hii CSSR ambapo ni kichaka kinajificha, lakini pili ni matumizi ya CSSR, ni vizuri sheria ikasema wazi kwa kuwa ni pesa inakuwa declared kwenye kodi, basi pesa hii isimamiwe na Sheria za Manunuzi za Serikali ambazo tunazifahamu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya vizuri sana kwenye utalii kwa miaka takribani minne kabla ya covid na naomba niseme kwamba kipimo kizuri cha mafanikio kwenye jambo hili kimekuja kwenye kuharibiwa na mwaka mmoja baada ya kuingia kwa covid. Tunafanya nini ili tuweze kufanya ya tukio la covid.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia comment juzi hapa, habari ya hasara ya ATCL. Kulipima shirika la ndege changa lenye miaka mitatu kufikiri litapata faida hiyo sio biashara ya nyanya. Shirika la ndege lina-indirect vitu vingi sana ambavyo huwezi kuvipima kama unapeleka nyanya pale Soko la Karikoo kwenda kuuza unatoa gharama na vitu vingine. Kuna vitu vingi sana lazima CAG hapa angesema pamoja na kula hasara hapa lakini limesaidia one, two, three, four, five. Tunataka kuimarisha utalii dunia nzima wanayofanikiwa kwenye utalii wanafanikiwa kwenye mashirika ya ndege. Kwa hiyo maoni yangu kwenye jambo hili, kwanza tuendelee na mpango wa kuliimarisha shirika hili, lakini tujitanue vizuri Zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona tuna weakness moja, tunasubiri watalii wanaokuja wenyewe au wanaotafutwa na watu. Kiko kitengo kimoja ambacho nchi nyingi kinawapelelea watalii wengi sana hawa wanatumia sana mashirika ya ndege ya ndani cha mikutano lazima pale TTB, Wizara iweke kitengo maalum cha kufanya lobbying, mikutano mingi duniani inatafutwa haiji yenyewe. Wale ndugu zangu wa AICC pale wanasubiri mikutano ije, mikutano ile mikutano ile ya Afrika Mashariki haiwezi ikasababisha nchi hii iweze kuonekana inafanya mikutano. Ni lazima awepo mtu anafanya lobbying na mashirika makubwa duniani yanayoleta mikutano ya watu zaid ya elfu nne na anazunguka duniani kuitafuta hiyo mikutano.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema hapa Mheshimiwa Shangazi, kuna kinaitwa economic diplomacy, ukienda kwenye balozi zetu, nimeenda kwenye balozi karibu nane Tanzania, unakuta staffing ni watu wasiozidi kumi WTO mikutano peke yake iliyoko Ujerumani katika kipindi cha mwaka mmoja inayotangaza utalii iko zaidi ya hamsini, wale walioko pale watu sita, watatu wameweka brochures na vitu vingine kwenye meza na website yao ipo centralized Tanzania hawawezi kuleta watalii na kuongeza watalii Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tukubali kwamba tunatakiwa kama tunazungumzia hao wafanyakazi, tuwa- empower tupeleke watu wawe equipped na knowledge, wapewe pesa wazunguke kwenda kuwatafuta hao watu waje Tanzania vinginevyo tutaendelea kuzungumza habari hii na itaendelea kuwa shida kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, hapa katikati tulipata tatizo kidogo, tunao utalii wa uwindaji, watalii wa uwindaji ni matajiri sana duniani, lakini kuna gharama kubwa sana ya kuki-manage kitalu, tunayo sheria kila baada ya miaka mingapi unatakiwa kufanya mnada. Sasa unapofanya mnada, unakuta yule amekitunza kile kitalu kwa miaka mingi anaweza asishinde kulingana na mtu mwingine, anayekuja interest yake sio kutunza kile kitalu matokeo yake anapoteza wateja wale wa mwanzo, kitalu kinapoteza thamani na tayari tunandelea kupunguza idadi ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu hapa, wale wanaofanya vizuri waendelee kuaminiwa na Serikali, waendee kupewa na waendelee kulindwa. Nasema hivi kwa sababu shida kubwa tuliyonayo tunafikiri unataka uuze vitalu kwa mnada, sawa, utauza vitalu vinne, halafu vitalu sabini viko wazi maana yake nini, ningekuwa mimi ningeweza kuvigawa hata bure vyote, halafu ukataka utoze kodi kutoka kwenye vile vitalu kwa sababu kitendo cha kukaa wazi gharama kubwa ya Serikali ni kuvilinda na kuviendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza hapa mara nyingi kuhusu TRA, nashukuru sana Serikali Sikivu ya CCCM imesikia na imetoa maelekezo. Jambo moja hapa nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mara zote wanapoona tunazungumzia Habari ya mgogoro wa walipa kodi na TRA inayoweza kula hasara hapa ni Serikali, negotiation itakayokuja ulikuwa unalipa milioni tano na hili ndio jambo ambalo nataka kumshauri lazima tuwe waangalifu tunataka kumpa nani unafuu. Ulikuwa unalipa milioni tano unataka kulipa milioni tatu, wanaweza watu wakatumia vibaya hii loop aliyoisema Mheshimiwa Rais, matokeo yake watu wakawa wana-negotiate wanakwambia nipe milioni mbili halafu hapa tutaandika hela kiasi Fulani, tunapoteza pesa ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka kushauri, badala ya kila mwaka huyu mtu anakwenda kukadiriwa kodi ya kulipa TRA kwa nini ukikadiriwa mwaka huu usiachwe miaka mitatu unalipa constant ile ile halafu baadaye utakapo-provide zile audited accounts zako waweze ku- review hesabu. Kitendo cha kila baada ya miezi tisa unaweza kutengeneza hesabu kinafanya mazingira ya kukaa mezani kila mara kuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Kengele ya kwanza Mheshimiwa.

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na naomba nimpongeza waziri kwa hotuba yake nzuri na kimsingi ni kwamba ni mpongeze pia mtangulizi wake kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitano iliyokwisha, Jimbo langu la Geita Mjini, lilijenga shule mpya za sekondari 13. Na likajenga shule mpya za msingi 13, maana yake tulipata shule mpya 26. Lakini katika kipindi chote hicho, mgao wa walimu ajira mpya umekuwa mdogo sana. naipongeza Serikali kwa kuziba mapengo ya walimu waliostaafu hizi ajira 6,000 ambazo imesema itatangaza hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kama Jimbo langu peke yangu lina shule 26 na sasa hivi najenga shule zingine nane maana yake ni kwamba walimu wanaokuja hawawezi kwenda kumaliza tatizo la walimu katika halmashauri zetu. Niiombe Serikali kwa sababu tulikuwa na hizi ajira 6,000 lakini tuna ajira zingine ambazo zilikuwa zimetangazwa na zikaacha kuajiriwa ni vizuri Serikali ikaajiri walimu wa kutosha katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, madhara ya kutokuwa na walimu kwenye shule ni makubwa sana. Huku juu ambako tunakwena watoto wanakwenda Chuo Kikuu, wanashindanishwa kwa ufaulu na ufaulu wao hauangalii historia kwamba huyu mtoto kwa bahati mbaya hakupata elimu ya kutosha kutokana na uhaba wa walimu alipokuwa sekondari. Na hata wakati mwingine, mikopo inaangalia aliyefaulu vizuri sana, sasa utaangalia shule ambayo ina walimu wanne na ina Watoto 600 ametoa mfano hapa Mheshimiwa Mbunge asubuhi, ipo kata yangu mimi form one walioanza mwaka huu wapo 850, lakini shule nzima ina walimu 32, na wanafunzi wengine wapo zaidi ya 2,000 utaona shule hii kama wanafunzi hawa wataendelea kufika form 4 na baadaye waende Chuo Kikuu hata kama watafaulu, hawataweza kushindana na wale ambao walikuwa kwenye shule yenye walimu wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Watoto wana adhibiwa huko Chuo Kikuu kwa kuoneokana hawakufaulu vizuri lakini kwasababu ya mapungufu waliyoyapata walipokuwa sekondari. Niombe sana, wizara ituletee walimu wa kutosha. Kinachofanyika sasa tunaongeza idadi ya shule, tunaongeza idadi ya wanafunzi, tuna-deal na quantity na hakuna quality ya Watoto wanaomaliza shule. Tunaweza kufikiri tunafanikiwa lakini kimsingi tunapeleka kundi kubwa la watu ambao hawakupata elimu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa spika, tatizo hili lipo pia kwenye afya, tumejenga zahanati mpya 24. Zahanati 24, zahanati unakwenda unakuta nurse peke yake. Mwaka juzi na mwaka jana tuliajiri madaktari, nikaamini sasa Serikali inakuja kuajiri hizi kada za kati ma-clinical officer na ma-nurse hawa katikati, lakini hizi kada zimekuwa zinaajiriwa taratibu sana matokeo yake sasa tuna zahanati nyingi tunajenga kila Kijiji, lakini zahanati ina mhudumu mmoja na huyo mhudumu akiugua zahanati inafungwa. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri, najua hizi zinasimamiwa na TAMISEMI lakini inawezekana wanaoratibu ajira hizi wakawa ni wengine lakini uwepo tunahamasisha wananchi kujenga ni vizuri wakapata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kwenye mradi ambao ulikuwa unaitwa LGSP mradi huu ulikwisha na tukapata mradi mwingine unaitwa TACTICS wamesema wenzangu hapa. Taarifa tulizonazo ni kwamba fedha hizi tayari zipo, kinachotakiwa ni Serikali kutoa commitment ili pesa ziweze kutoka. Mazungumzo ya fedha hizi yalianza tangu mwaka jana tumeshirikishwa na wale wataalam waliokuwa wanakuja, ikaaminika zingesainiwa kabla ya bajeti hii haijapita, sasa tunaona mwaka wa fedha unaisha, hii miji 45 anbayo inahitaji pesa hizi ni muhimu sana Serikali ikatoa commitment ili tukaweza kupata fedha hizi zikaenda kusaidia watu wa TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pale kwangu pale Geita Mjini barabara zote ni mbovu lakini mradi huu ukianza utachukua sehemu kubwa ya barabara za pale mjini na TARURA wata-deal na barabara zingine sehemu za vijijini. Hatujui ni kwa nini mradi huu unachelewa kuanza kwasababu wanaotoa fedha hizi walishatoa, fedha ziko Serikalini, Serikali inatakiwa kufanya commitment tu fedha ziweze kutumika. Miji 45 Tanzania itapata fedha.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa ambalo tunalo hapa ni kuchelewa sana kufanya maamuzi. Kwa sababu tungechelewa kutafuta fedha, tumeshatafuta fedha tumepata, kufanya maamuzi ya kuzitumia fedha tunachelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TARURA ilichukua ma-engineer wote kwenye halmashauri, Tanzania nzima ma-engineer waliopo kwenye halmshauri ni 84. Halmashauri tulizonazo ni 180 na kitu, kwa hiyo utagundua kuna upungufu wa ma- engineer 100. Lakini niombe, kwenye majeshi yetu huko hasa Jeshi la Ulinzi la Wananchi kuna ma-engineer kuna ma- engineer wamejaa. Badala ya kutuletea washauri wa Mgambo ambao hawana taaluma wachukue washauri wa mgambo ma-engineer wawapeleke kwenye halmashauri huko, kwenye wilaya tunaweza tukawaazima kwenye miradi.

Mheshimiwa Spika, amesema Mheshimiwa mmoja hapa, tunatumia force account, ubaya wa force account hakuna retention kwa hiyo inapotokea mradi ule umekosewa usitegemee kuna mtu atakuja kurekebisha, kwa hiyo lazima ufanyike kwa usahihi tangu mwanzo. Tunajenga majengo makubwa milioni 500, milioni 400 hakuna engineer waliopo ni ma-technician. Niiombe sana wizara, kama kuajiri itashindikana vipo vyombo vina ma-engineer waazime walete hao watu wafanye kazi kule hii ndo maana ya Serikali moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoa ushauri kwenye TARURA. TARURA walipoundwa ilionekana kama chombo fulani hivi kinajitegemea, na matokeo yake kikajikuta huku halmashauri ni kama halmashauri hawahusiki. Kabla ya TARURA, Mkurugenzi alikuwa na uwezo wa barabara ikiharibika anatumia fedha zake kwenda kurekebisha barabara kwasababu kuna emergence. Leo mkurugenzi hawezi kwanini! kwasababu TARURA ni ka chombo fulani kanachojitegemea. Mimi nikuombe Mheshimiwa waziri, pitia upya muundo wa jambo hili, kama ni lazima hawa watu wapo halmashauri pale warudishwe halmashauri waendelee kuwa na pesa zao lakini warudishwe halmashauri waweze kushiriki, kusimamia na Madiwani na Kukaguliwa.

Mheshimiwa Naibu spika, Hii itawawezesha halmashauri wanapotoa fedha waweze kuamini kwamba tunawapa wenzetu. Leo mkurugenzi akitaka ripoti lazima aombe, Madiwani wakitaka taarifa lazima waombe, na huyu meneja wa TARURA wa wilaya ni kama karani kazi zote zinafanywa mkoani. Aliyeko pale hawezi kufanya chochote. Mheshimiwa hii imekata mawasiliano kabisa ya wawakilishi wa wananchi na matatizo ya barabara na unajua sehemu kubwa ya kura za Madiwani na Wabunge ziko kwenye barabara. Kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa utazame upya huu muundo.

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilipitia bajeti za mikoa, tumegundua kwenye asilimia 10 tumetunga sheria nzuri sana ya asilimia 10. Halmashauri nyingi zimetimiza agizo hilo, shida iliyopo hakuna ufuatiliaji wa kutosha wa fedha zilizokopeshwa, lakini hakuna utaalam wa kutosha kwenye halmshauri wa ku- manage fund kubwa.

Nataka kutoa tu mfano, Halmashauri ya Mji wa Geita inakusanya takriban shilingi bilioni mpaka bilioni 8, shilingi bilioni nane kwa mwaka. Fedha hizi ni nyingi sana, matokeo yake unatenga milioni 8 kwa miaka mitano unazungumzia takriban shilining bilioni 4, shilingi bilioni 4 tuliagiza kwenye Kamati zifunguliwe akaunti maalum zisiende kwenye general account maana yake kwa miaka mitano tuna 20 bilion. Lakini halmashauri zote, mikoa yote iliyokuja kuhojiwa hakuna continuation ya akaunti ya mwaka uliyopita na mwaka mwingine. Maana yake fedha hizi hazijulijani zikowapi? (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Constantine J. Kanyasu muda huu, malizia sentensi mbili, tatu.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa kuwa tulisema halmashauri zifungue akaunti inayojitegemea, tunachotarajia sasa akaunti hii itakuwa inakuwa at time five years tutakuta kuna 20 bilion, kuna 10 bilion na halmashauri zitaacha kusubiri makusanyo ya mwezi kukopesha wananchi. Lakini kwa sasa fedha hizi zinapotea, hazijulikani ziko wapi, wanaokuja wanakuja na hesabu za mwaka jana hawaji na collection ya mwaka wala haijulikani wana shilingi ngapi. Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nianze kuipongeza Wizara kwa bajeti yao nzuri, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Watendaji wote katika Wizara hii kwa kufanya kazi nzuri ambayo imeleta mapinduzi makubwa kwenye Wizara hii ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kusimamia vizuri suala la malipo ya mipasuko kwenye Jimbo langu la Geita. Tulikuwa na tatizo la mipasuko ambalo lilidumu kwa takribani miaka 20, lakini Mheshimiwa Waziri alikuja akaweka mguu chini na sasa GGM wamewalipa wale wananchi. Naomba kuwapongeza GGM na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa maelekezo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashukuru sana juhudi za Wizara. Pale Geita Mjini tumekamilisha refinery ya kisasa kabisa ambayo imejengwa na mwananchi Mtanzania na ninaamini kwamba Mheshimiwa Waziri atakuja na mpango mzuri ili kuhakikisha kwamba ile refinery yao ya Serikali isije ikawa inachukua mzigo wote Geita na kuupeleka kule, kwa sababu tunataka kuona ile refinery inaendelea kufanya kazi Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichosababisha mafanikio makubwa kwenye Wizara ya Madini ni baada ya Wizara hii kukaa na wadau na kuondoa utitiri wa kodi na kufanya watu kuwa walipa kodi wa hiari. Jambo hili limetufundisha kwamba kumbe siyo lazima kutumia nguvu nyingi, sheria nyingi, tozo nyingi ili tuweze kukusanya kodi. Sasa ni kwa mtazamo huo huo naiomba sana Serikali kuangalia maeneo yote ambayo wananchi wanalalamikia kuhusu tozo na kodi nyingi kuziondoa ili kufanya mazingira ya kufanya biashara kuwa mepesi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema hapa wakati wanachangia kwenye Mpango kwamba shida kubwa tuliyonayo sasa kwenye wachimbaji wadogo wadogo ni investment vis-a-vis production inayofanyika kwenye madini, kwamba uwekezaji ambao wachimbaji wadogo wanaweka ni mkubwa sana kuliko faida ambayo wanaipata. Watu wengi wanaweza kuona mauzo yameongozeka, lakini katika wachimbaji wadogo 100 wanaoweka pesa zao, ni wachimbaji watano au 10 ndiyo wanaoweza kurudisha gharama, the rest wote wanakula hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini? Kwa sababu wanachimba kwa kubahatisha, wanachimba kwa kupiga ramli, wanachimba kwa kufuata mkumbo. Jambo hili limezungumzwa vizuri na Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tuwape uwezesho GST wawe na league za kutosha. Hizi league nne ambazo wanazo, Tanzania ina madini kila mkoa na kila wilaya. Wawe na league za kutosha, tuajiri manpower za kutosha tuache kupeleka watu kwenda kupiga ramli na ndiyo maana msishangae kuona kwamba katika maeneo mengi ya machimbo ya madini Waganga wa Kienyeji wana soko sana kwa sababu wanapiga ramli sana na hii ni hatari sana katika nchi ambayo imepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Geita pale mitaa yangu na Vijiji vya Magema, Nyamalembo, Katumaini, Mizingamo na Katoma imekuwa kwenye mgogoro mkubwa na mgodi wa GGM kwa takribani miaka 20. Eneo la GGM ni Square kilometer 192, eneo wanalochimba ni kama asilimia 10 ya eneo hilo. Eneo hili la vijiji hivi limewekewa ulinzi sasa wa Polisi. Wananchi wakienda shambani wanakutana na Polisi, wakienda kukata kuni wanakutana na Polisi, akichimba choo, anakutana na Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sidhani kama Mheshimiwa Waziri, kule kwao Bulangwa wananchi wakiwa wanakutana na Polisi kila siku wanaweza kuishi kwa raha. Lile eneo wananchi wanasubiri fidia. Eneo lile ni kilometa zaidi ya 15 kutoka kwenye pit ya mgodi. Kama eneo lile ni potential kwa mgodi hakuna sababu ya kulundika Polisi pale kulinda raia wanaoenda kulima na kukata kuni, wawalipe wale wananchi waondoke pale. Hakuna sababu ya watu kuishi kwa tension wakiamka asubuhi kwa tension kwa sababu tu lile eneo lipo ndani ya leseni. Leseni ya mgodi ni kubwa lakini hawaja tayari kulitumia eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wananchi hawa wanaendelea kuishi kama vile ni wakimbizi wapo kwenye nchi ya vita. Hatuhitaji sisi kuja kuona Polisi wanajaa kwenye mitaa yetu, waje wakamate kama kuna wahalifu, hatuvamii eneo linalochimbwa, hatuna shida na kule na tunaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme ukweli, kama kuna mtu anafaidika na uwepo wa wachimbaji wakubwa ni Geita. Nasi tunataka waendelee kuwepo, tunawaunga mkono, tunawaomba wananchi waache kuvamia maeneo yao, lakini kwenye makazi yao ambayo hawajalipwa fidia. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana wananchi wapewe uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, Mheshimiwa Musukuma amezungumza hapa kuhusu CSR. Nilizungumza wakati nachangia Mpango kwamba tulitunga sheria nzuri sana, tukasema kwenye eneo la Service Levy 0.3 percent inalipwa Halmashauri. Haijulikani kwenye CSR ni percent ngapi? Shida kubwa nyingine tuliyonayo ni kwamba pesa hizi za CSR, sheria imebaki kimya kwenye manunuzi na kwenye matumizi. Sawa zinabaki kule GGM, tunashirikiana na Local Council, lakini matokeo yake zimekosa usimamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu supervision peke yake nilikuwa nacheki, imegharimu zaidi ya shilingi milioni 250 ambazo zinalipwa kwa viongozi wanaokuja kuangalia kazi zilizofanywa na CSR. Sasa Mheshimiwa hii ni pesa ambayo inakuwa declared kwenye kodi, kwa sababu anapotoa hii pesa mwisho wa siku anasema kwenye kodi nimepeleka hizi pesa kwa wananchi. Huyu Mtumishi wa Umma anaenda kulipwa supervision shilingi milioni 250 akiwa ndani ya eneo lake? Anatumiaje zile pesa namna hiyo. Naomba hii sheria iwekwe vizuri, hizi pesa zibaki kwa wenye mgodi, lakini matumizi yake yafuate sheria za matumizi ya pesa za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema hapa Mheshimiwa Iddi, nilisema wakati ule Local Content wamekudanganya kwamba wamefuata sheria. Pale logistic wanazotoa, ni kazi ndogo ndogo, lakini sheria inasema zile bidhaa ambazo hazipatikani Tanzania, waingize ubia na Watanzania, lakini halifanyiki hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunapigwa pesa kwa sababu kupitia Local Content kuna transfer pricing. Kama hakuna Local Content, akija mtu anayeuza kutoka nje, kinachofanyika ni kufanya gharama ya manunuzi kuwa makubwa na matokeo yake pesa hizi zinarudi kule kule zilikotoka. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat Hanje.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ni kweli tuna tatizo kubwa sana la uelewa kuhusu Local Content kwa sababu hatuna sheria inayoitwa Sheria ya Local Content ambayo ita-define ni vitu gani na vitu gani sisi kama nchi tunavi-regard kama local content? Ndiyo maana kuna mwingiliano wa kila namna mtu anavyo-define. Kwa hiyo, nimpe taarifa hiyo, lakini pia tunahitaji kama inawezekana kupata sheria maalum kwa ajili ya local content. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, malizia mchango wako.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria ipo na imeeleza vizuri sana na sheria ile shida yake kubwa ni kwamba hakuna compliance kwa wale wanaolengwa na sheria yenyewe, lakini sheria yenyewe ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jimbo langu lina wachimbaji wengi. Wafanyakazi wengi wa mgodi ni wa muda (contractual). Tulitunga sheria hapa tukasema kwamba mafao ya maeneo haya yanarudi kwenye mfumo ambao tulisema akishafutwa kazi anaanza kulipwa asilimia
80 sijui ya mshahara, lakini sehemu hii kubwa naiomba Serikali, wananchi wangu bado wanalilia sana Fao la Kujitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni nyingi zinafanya kazi kwa miaka miwili zinafunga na zikishafunga, wananchi hawa wanapoteza kazi kwa miaka mitatu mpaka minne. Hii fedha ilikuwa inawasaidia kwenda kuanzisha biashara na wengine walikuwa wanaweza kusomesha watoto wao. Sasa hivi muda wa kufuatilia mafao haya ni mrefu sana na kwa kweli wanakula hasara kubwa. Nilikuwa naomba sana maeneo haya yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara na Watendaji wake wote katika Wizara hii. Pia nawapongeza sana Kamati kwa taarifa yao nzuri na uchambuzi wao mzuri sana ambao wameufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa miongozo yake ambayo ameitoa na hasa katika eneo la kumaliza migogoro ambayo imewagharimu sana wananchi, wafugaji na wakulima katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kwenda kwenye Randama ya Waziri ukurasa sita na wa saba. Kwenye ukurasa wa sita kwenye item namba nne kwenye malengo mahsusi ya Wizara, Mheshimiwa Waziri amezungumza namna ambavyo maelekezo ya Serikali ya kumaliza migogoro ya ardhi ambayo inahusisha wananchi wanaokaa karibu na hifadhi na pia migogoro inayohusisha wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa saba wa randama ya Mheshimiwa Waziri na nikikariri hotuba ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. Magufuli, ambayo imeeleza vizuri namna ambavyo lengo la Serikali ni kufikia watalii bilioni tano na kuongeza mapato kutoka bilioni 2.6 za sasa za mwaka 2016 kwenda mpaka shilingi bilioni tano ndiyo malengo ya Wizara katika miaka mitano ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuangalia katika maeneo hayo mawili, naomba nianze kwa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba Mheshimiwa Rais, mwaka 2019, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua uwepo wa migogoro mingi sana nchini, mwezi wa Tatu, tarehe 15 aliagiza kuundwa kwa kikosi kazi cha Wizara saba kikiongozwa na Wizara ya Ardhi kushughulikia na kushauri namna gani Serikali inaweza kumaliza migogoro katika maeneo mengi ambayo yamekuwa yakiwakabili wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu, kazi kubwa katika eneo hili ilifanyika. Tulikuwa tunazungumzia maeneo yenye migogoro, vijiji 366, ikaja ikagundulika ni zaidi ya 1,000, lakini katika uchambuzi uliofanywa katika hiyo joint committee ilionekana karibu vijiji 975 vitaendelea kuwepo kutokana na mazingira na baadhi vilionekana vitashughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu hapa ni ya msingi kwamba nataka kufahamu maamuzi haya ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyatolea tangazo la Serikali na kuahidi utekelezaji; utekelezaji wake unafanyika lini? Kuchelewa kufanyika kwa utekelezaji huu kunawagharimu sana wananchi. Nataka nitoe mfano; katika Jimbo langu la Geita Mjini, msitu wa Hifadhi wa Usindwake na msitu wa Geita Kata ya Mgusu asilimia 80 wapo ndani ya eneo ambalo zamani na mpaka sasa linahesabika kwamba ni hifadhi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha asilimia 80 kuwa katika hifadhi maana yake ni kwamba makazi yamo ndani ya hifadhi, wakulima wamo ndani ya hifadhi na mifugo waliyo nayo inachungwa ndani ya hifadhi. Sasa wananchi hawa wanakamatwa kila siku na wanapokamatwa hawakamatwi kwa sababu ni makosa yao ni kwa sababu tayari kuna shule, tayari kuna zahanati, tayari kuna barabara, tayari kuna shughuli za kiuchumi zinaendelea maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali kumaliza tatizo hili. Tayari lilishatolewa maelekezo, sasa sielewi anatekeleza nani? Wizara yako Mheshimiwa Waziri Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi au Wizara gani? Ninachojua ni jukumu la Serikali kumaliza mgogoro huu ambao unawagharimu wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, faini katika maeneo haya ni kubwa sana. Anapokamatwa mfugaji ameingiza mifugo kwenye hifadhi, faini zake ni kubwa. Tuliona kwenye hotuba ya Wizara ya Kilimo na Mifugo, karibu ng’ombe milioni sita zimekamatwa, zimetaifishwa; na ni kwa mujibu wa sheria. Sasa lazima tumalize migogoro hii kwa maelekezo ya Serikali. Nataka kujua kwa nini utekelezaji wa maagizo haya unaendelea kuchukua muda mrefu? (Makofi)

MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Olelekaita.

T A A R I F A

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe tu mzungumzaji taarifa, kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii tarehe 1 Januari, 2021 alitoa tangazo lifuatalo: “Ninyi ni Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu, fanyeni kazi zenu za kulinda maeneo mliyokabidhiwa kama kawaida. Mkikuta kuna ng’ombe wanamilikiwa na Dkt. Damas Ndumbaro, ninyi kamateni, msije mkasema ng’ombe hawa ni wa Waziri, tuwaache, ninyi mkamate na mwapige mnada kama kawaida. Ng’ombe watakaokutwa ndani ya Hifadhi ni shilingi 100,000.” Nataka tu nimpe taarifa kwamba hili tangazo siyo kwa mujibu kwa sheria. Hakuna sheria inayosema ng’ombe atozwe kwa kichwa shilingi 100,000. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa John Constantine Kanyasu, unaipokea taarifa hii?

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo na ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri, pengine na Mheshimiwa Waziri wa Sheria watoe ufafanuzi kwenye hiyo sheria. Kwa sababu, hiyo sheria ukiitazama haimpi absolute right anayekukamata kupiga hiyo fine. Ina vipengele vyake ambavyo vinakuwa attested kufika kwenye fine hiyo. Kutokana na ignorance ya wananchi wetu huku, it is direct, ukikamatwa mara shilingi 100,000/=, sasa utatengeneza masikini wangapi katika nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja yangu ya pili ambayo lengo letu ni kufikisha watalii milioni tano. Kwanza niendelee kuwapa pole wahifadhi wetu Tanzania kwa sababu, kuja kwa COVID kumewarudisha nyuma. Walikuwa wanakwenda vizuri sana, nilikuwa ninaamini baada ya muda mfupi tungelikuwa ni nchi ambayo inaongoza kwa utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili katika Afrika, nchi ambazo zinafanya vizuri sana katika utalii, Morocco wanapata watalii milioni 12.3 ambao maeneo mengi sana wanachokwenda kuangalia kule ni cultural, pamoja na utalii ambao unahusisha sana mambo ya vyakula na maeneo mengine ambayo yamekuwa ni ya asili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Egypt milioni 11.3; huko nako ni cultural na maeneo makubwa hapa ni pyramids pamoja na kuangalia Pharaoh Tombs na kadhalika. Eneo la tatu, ni South Africa, hawa wanapata watalii milioni 10; most popular ni kwa sababu ya safari na kitu kinaitwa MICE, mikutano ambayo inafanyika South Africa. Katika Afrika kwa mujibu wa International Convention and Conference Association, South Africa wanaongoza kwa Afrika nzima kwa ku-host mikutano mingi sana ambayo inapeleka watu wengi kule nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya nne ni Tunisia ambayo inapata watalii milioni 8.3 na nchi ya tano ni Zimbabwe. Nini kinawapeleka watu Zimbabwe? Ni kwenda kuangalia Victoria Falls. Sasa hapa nataka kuzungumza nini? Katika orodha yote hii ya nchi tano, kimsingi nchi ambayo kidogo watalii wanakwenda kwa ajili ya kuangalia wanyama ni South Africa. South Africa ni kwa sababu ya improvement yake katika miundombinu na namna ambavyo wametengeneza mazingira ya kufanya watalii waweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi nyingi ambazo zinaongoza katika utalii, kinachowapeleka kule ni cultural pamoja na heritage centers ambazo ziko katika maeneo yale. Sasa ukiitazama vizuri Tanzania, ukaacha zile traditional products zetu zinazoleta watalii kwa maana ya safari, beach, labda kwa maana ya hunting na vitu vingine. Bado tuna- lack product ambayo inaweza kutuletea watalii wengi kwa mara moja na kufikisha watalii milioni tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka ni-emphasize jambo moja, katika Afrika Mashariki, Rwanda sasa hivi wamekuwa waki-host mikutano mikubwa sana kidunia. Kwa nini? Kwa sababu ya ile Kigali Convention Center. Wametengeneza Kigali Convention Center ambapo inafanyika mikutano mikubwa sana ya dunia. Nataka tu nitoe mfano; wamekuwa na Mkutano wa Force Agenda Summit, ambao ulikusanya maelfu ya watu; Mikutano ya Mo-Ibrahim, wamefanya mikutano ya GMSA ya Mobile 360, wamekuwa na mikutano mingi ambayo imeleta watu kutoka maeneo mbalimbali. Why Rwanda?

Moja, kwa sababu kwanza ni free VISA. ukiingia Rwanda unatoka dunia nzima, ukifika Kigali unakutana na VISA baada ya kufika, VISA on arrival. Hii imeondoa sana usumbufu, kwa hiyo, unaweza kwenda maelfu na maelfu ya mikutano pale na ukafika ukafanya mkutano wako lakini utapata VISA on arrival. Pia ni rahisi kupata VISA kwa masharti mepesi bila usumbufu wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, connectivity. Rwanda hana Shirika kubwa sana la Ndege, lakini anachokifanya ana ndege ndogo ambazo zinaweza kukupeleka kwenye activity nyingine. Kwenye eneo hili la mikutano anayeongoza ni South Africa, wa pili ni Rwanda; tatu hapa tuna Ethiopia, tuna Kenya, tuna Uganda. Why Kenya na Uganda na wenyewe hivyo ni connectivity. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa, tunayo haja kubwa; watu wanaokuja kuangalia Wanyama, anaweza akaja mara moja na asirudi tena, lakini anayekuja kuangalia cultural, anaweza kuja mara ya kwanza, akarudi mara ya pili. Kwa hiyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimalizie eneo moja kwamba kutoa ushauri wangu. Tunaomba kuishauri Serikali kutafuta uwekezaji mahususi kwa ajili ya kuhamasisha…

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: …utalii wa mikutano katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.(Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya Kanda ya Ziwa katika siku hizi tatu alizotembelea huko. Tunampongeza sana na kumshukuru sana kwa kazi kubwa aliyoifanya pale kwenye kivuko ambako tunajenga daraja. Kwa mtu ambaye hajawahi kufika anaweza kufikiri tunazungumzia daraja la mita 200, lile ni daraja lenye takriban kilometa 3 na pointi, lakini umuhimu wa daraja hilo ni pale unapokuwa una mgonjwa unampeleka Bugando kwenye hospitali ya Rufaa na ziwa limeziba water hyacinth unachukua masaa matatu unasubiri ferry. Umuhimu wa daraja hilo ni pale unapowahi ndege na ferry haziwezi kupita majani yameziba na umuhimu wa daraja hilo ni pale unapokimbizana na uhai wa mtu unataka kuvuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tumhakikishie Mheshimiwa Rais, wananchi wa Kanda ya Ziwa wanamshukuru sana na kumpongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa ambayo wameyasema weznangu. Kwanza nianze na msamaha wa kodi kwenye nyasi bandia. Mheshimiwa Waziri, nikupongeze sana kwa jambo hilo lakini nikuombe, nchi hii ina Majiji sita tu, unaposema umetoa msamaha wa kodi wa nyasi bandia kwenye majiji sita, maana yake unataka kupandisha michezo kwenye majiji sita na tayari majiji haya yana loopholes nyingi na uwezo mkubwa wa kujiendesha na kuendesha viwanja vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani kusikia kutoka kwako unategemea kupata hasara ya shilingi ngapi iwapo utaruhusu Makao Makuu ya mikoa yote Tanzania watapata viwanja vyenye nyasi bandia. Maana mpaka ninapozungumza leo kila nikiangalia kwenye viwanja tulivyonavyo Tanzania…

MHE. FESTO R. T. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Costantine kuna taarifa. Taarifa tafadhali.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. T. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuunga mkono mzungumzaji anayezungumza kwenye suala la nyasi bandia. Nataka kumpa Taarifa kwamba, kati ya hayo Majiji sita anayoyazungumzia, Dar es Salaam tayari wana viwanja, Mwanza tayari wana viwanja kwa hiyo kuna Majiji manne tu ndiyo ambayo hayana viwanja. Kwa hiyo, unachokizungumza ni kitu sahihi na sisi kama wadau wa michezo tunakuunga mkono. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Constantine, Taarifa hiyo.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa. Hapa ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Waziri ni kwamba, kwa mfano tukisema kwenye mwaka wa fedha ulioisha ni wangapi walioingizia pesa kwa kulipa kodi kwa kuleta nyasi bandia? Na unatarajia utakapofuta sasa hiyo misamaha Mikoa mingine utakuwa umeingia hasara kiasi gani? Mimi nikiangalia Mikoa ni miwili na walioweka nyasi bandia ni walewale na inawezekana kuna mwaka mzima utaisha hakuna nyasi bandia. Kwa hiyo, unachokifanya Mheshimiwa ni kuifanya nchi nzima iwe na mwamko wa michezo kuliko mikoa ambayo tayari imeendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi ninaunga mkono kabisa kodi ambayo umeileta kwenye LUKU ninaiunga mkono. Nadhani ni sahihi hata kama kiwanja kina apartment sita na apartment zote zikawa na LUKU yake n azote zikadaiwa kodi ni sahihi. Nataka nitoe mfano, sasa hivi ukiwa na low density umejenga apartment nane na kama zinatofautiana, unapokwenda kulipa TRA unalipa property tax ya kila apartment, sasa kwa nini unashindwa kulipa huo mchango ambao umeupendekeza, kodi ambayo imependekezwa kwenye kila apartment? Nafikiri ni sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili litaepusha sana kwanza makadirio ya hovyo hovyo yaliyokuwepo mwanzo ambayo Mheshimiwa wa Awamu ya Tano aliyaondoa, lakini uhakika wa ukusanyaji wa pesa yenyewe. Duniani kote maendeleo yanakuja kwa watu kulipa kodi na watu lazima walipe kodi ndiyo waone maendeleo yanakuja. Hatuwezi kupiga kelele hapa kila siku tunataka maendeleo wakati hatutaki kulipa kodi, lazima tulipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulisema hapa na kumshauri Mheshimiwa Waziri, bado pesa nyingi sana inapotea. Mimi nina uhakika TRA wanakusanya kama siyo asilimia moja ya tatu ya kodi basi ni nusu ya kodi. Mlifanya mpango mzuri sana pale bandarini kwamba, kodi za magari zinajulikana, kabla hujaagiza gari unajua kodi yako hii hapa, jambo ambalo unatakiwa ulibuni na kulifanya huku mtaani ni kuondoa utamaduni wa mtu anajaza zile audited accounts halafu tunaanza mjadala miezi mitatu, miezi minne, miezi mingapi, matokeo yake tunakuja kuishia kwenye kuelewana nikutoe ngapi ili tuweze ku- balance tunapoteza kodi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie upya namna tunavyoweza kufanya ili kuwafanya walipa kodi anapomaliza kulipa kodi zile instalments makadirio yake yaje genuine na anapolipa awe amemalizana na Serikali, kila mtu atalipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine tupitie upya orodha ya wamachinga. Machinga tumewapa vile vibali wengine wana maduka, wengine wanauza uji, mwingine anauza mchicha, tupitie upya tu-define tunafikiria machinga mwenye kibali ni mtu wa namna gani? Ili kundi fulani ambalo tunafikiri limevuka kwenye hiyo level tulitoe. Tutakuwa tumeongeza malipo ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo niende sasa kwenye idara moja ya uvuvi. Nimeangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anapendekeza kufuta kodi ya solar power. Hivi sasa kule kwetu Kanda ya Ziwa, solar panels ndiyo zinazo-charge taa za kuvulia dagaa, lakini nimeangalia sasa amefanya double standard, wakati amependekeza kufuta msamaha wa kodi amependekeza kuongeza withholding tax kwa mazao yote ya uvuvi yanayopelekwa kiwandani. Mheshimiwa Waziri this is too wrong.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ngoja niseme, samaki ambao mvuvi anawapeleka kwenye kiwanda production cost yake ni very expensive, unapomkata asilimia mbili utahamasisha smuggling. Nataka nikwambie mvuvi kwenye mtumbwi mmoja ana-invest about 20 million, siku moja ili aende ziwani anahitaji mafuta lita 30. Kuna wakati anapata kilo 10 tu na hizo kilo 10 ndiyo anazokusanya kwenye boti zifike tani mbili ziende zikauzwe, wewe unafikiri zote ni faida, huyu sio mkandarasi, utakapoingiza kiwandani ukakata 2% withholding tax kwa mvuvi utakuwa umekata mtaji tangu kwenye nyavu, kwenye mafuta na kwenye operation cost, sina uhakika kama watu wako wamelielewa vizuri suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimuona mtu yuko pale Mwanza ana boti la tani 10 la samaki amekusanya samaki hao wiki mbili na amekusanya kwa wavuvi wanaopeleka kilo 20, kilo 25 ambao kila siku wanatumia lita 30 za mafuta na ana boti investment yake ni milioni 20. Sasa unaposema unaenda kukata withholding tax kwa samaki aliowapeleka kiwandani maana yake nini, unakata mtaji. Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri hili practically tunakwenda kufilisi watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliishauri hapa Serikali mwaka 2017, ilikuwa inafanya operations nyingi kwa wavuvi na matokeo yake wavuvi wote wakubwa ziwani wamekwisha, wale waliokuwa wanakopesha wavuvi hawawakopeshi tena. Na tuliwaambia kwamba, mnafurahi mnakusanya pesa ya faini, lakini watu wanafilisika.

Sasa leo watu wamerudi kwenye kuvua wanavua illegal, matokeo yake sasa ni nini, hakuna tena mvuvi anakopeshwa nyavu, hakuna mvuvi ana mtaji. Sasa hivi mtakapoleta hii kodi watu watapeleka samaki Uganda na Kenya. Nakuomba Mheshimiwa Waziri liangalie vizuri sana jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Mheshimiwa Waziri unisaidie kupata ufafanuzi, kwenye ukurasa wa 34 umesema, nimeona kuna mambo mawili kama hapa yana- contradict, unazungumzia kuweka kiwango cha kutoza kodi kwa wachimbaji wadogo, kwenye (a) umesema kutoza kodi wachimbaji wadogo wa madini kwa kiwango cha asilimia tatu kwenye thamani ya mauzo ya madini, lakini nimeona tena kwenye sehemu ya nne unasema kutoza kodi kwa yule ambaye amenunua madini kwa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kwamba, anawalipia kodi sasa sijaelewa. Kwa sababu, huyu ulishamtoza kodi huku chini, huku tena unakuja kumtoza kodi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukumbuke pia huyu anayeuza madini hiyo siyo faida, hawa wanaochimba mashimo anachimba miezi mitatu anakwenda mita 100 hajaingiza hata 100. Shimo linamgharimu milioni 50, siku akianza kuzalisha mifuko 10, mifuko 10 anaitoa kwa one week, akiifikisha juu umeshachukua asilimia tatu, lakini bado unasema utahakikisha kwamba kuweka wajibu wa mchimbaji mdogo wa madini kama muajiri wa kukata kodi mapato ya ajira kutoka kwa wafanyakazi wake pale tu madini yanapokuwa yamepatikana na kuuzwa kwa masoko ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madini yametoka wapi? Yametoka kwa wachimbaji wadogo, umeshawakata kodi, huyu mchimbaji mdogo akienda kuuza unamkata kodi, tunapambana sana suala hili linafanana na kwenye samaki. Wenye viwanda wanalalamikia royality, umekwishaenda kukata asilmia mbili, umeshamkata mchimbaji mdogo, unamkata na huyo, Mheshimiwa hii si double taxation? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe Mheshimiwa litazame vizuri. Tukiamua kumkata yule mdogo kule chini basi tu-track source yake iko wapi ili kusudi hawa waliopo wabaki huku chini

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Constantine Kanyasu.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nami naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kunipa afya na kunijalia kufika siku ya leo niweze kuchangia kwenye huu Mpango.
Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kwa kasi kubwa ambayo ameanza nayo. Kasi hii inawatisha watu wote. Ukiona maadui zako wanaendelea kukusifia, basi lazima ujue kuna tatizo. Kwa hiyo, wale ambao wanaona hawafanyi kazi, nadhani wanaogopa kivuli chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais kwa kurudisha nidhamu ya Watumishi wa Serikali. Nchi yetu ilikuwa inarudishwa nyuma na mambo mengi sana, likiwemo suala la Watumishi wa Serikali kutokuwa na nidhamu; nidhamu ya muda, lakini hata nidhamu ya utendaji. Hili kama litasimamiwa vizuri, tunaanza kujenga spirit ambayo mtu akiingia ofisini, anafahamu kwamba yuko pale kwa ajili ya kufanya kazi ya wananchi. Hili ni lazima lisimamiwe vizuri pamoja na viongozi wengine walioko ngazi ya chini.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kurudisha nidhamu ya matumizi. Naamini tulikuwa ni nchi ambayo tunaweza angalau kujitegemea kwa kiwango fulani lakini matumizi yetu yalikuwa yanakiuka baadhi ya mambo na kuonekana ni nchi maskini sana. Nampongeza pia kwa zoezi lake la kuhakikisha kwamba Watanzania wanalipa kodi.
Mheshimiwa Spika, suala la kodi ni suala ambalo Tanzania ilikuwa inaonekana anayelipa kodi ni mshamba. Watu wengi walikuwa wanajisifu kwa kutokulipa kodi. Sasa hivi utasikia malalamiko ya watu wengi kwamba wamebanwa. Watumishi wa Serikali tulikuwa tunalipa kodi kubwa zaidi kuliko wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, ombi langu tu hapa ni kwamba, zipo lugha ambazo zinatuchonganisha; zinamchonganisha Mheshimiwa Rais. Wapo Watumishi wa Serikali wanakwenda kulazimisha watu walipe kodi kuliko ambayo inatakiwa kulipwa anasema na ni kwa sababu ya Serikali yenu. Naamini watu hawa wakifuatiliwa, kodi ni kwa manufaa ya umma.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Fedha kwa kuja na Mpango wake huu. Naamini kwamba hivi vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye Mpango huu kama vitasimamiwa, tunaweza tukaifikisha Tanzania sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, tunalo ongezeko la mapato ya TRA, mapato yetu ya kodi. Nawapongeza sana! Wasiwasi wangu ni mmoja tu hapa, yapo malalamiko sana kwa wafanyabiashara; hakuna uniformity pale bandarini. Leo atakuja mtu ana container, declaration inaonesha vifaa vilevile ataambiwa Shilingi milioni 20, lakini mtu yuleyule akirudi next time ataambiwa Shilingi milioni 50, lakini jana yake utaambiwa mtu mwingine amelipa Shilingi milioni tisa.
Mheshimiwa Spika, nadhani iko haja ya kuweka utaratibu, badala ya kuacha hii freelance ambayo mhusika anaweza aka-gamble nayo na kuhamasisha rushwa, uwekwe utaratibu ili kila mtu kabla ya kufanya importation, ajue kwamba mzigo huu nikiufikisha Tanzania anakwenda kulipa kodi ya shilingi ngapi.
Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo, tutaendelea kuruhusu watu kukaa mezani na kujadili na matokeo yake yatakuwa kama aliyosema Mheshimiwa Keissy jana kwamba gari ile ile unanunua Dola 10,000, ukija pale, mtu wa TRA analazimisha iwe Dola 50,000, anakadiria kodi anayoitaka. Matokeo yake, watu wanakimbia gari pale bandarini, halafu Serikali inauza gari zile kwa bei rahisi zaidi kuliko ambayo alikuwa ameisema mhusika. Mimi nasema Serikali inafanya kazi nzuri, tunaipongeza, lakini ni lazima itoe macho zaidi katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta. Kwanza nianze na suala hili la elimu. Nimekuwa napata tabu kidogo kuona Tanzania ina output ya wasomi wengi sana, lakini kila kona wasomi wanalalamika ajira. Tatizo ni kwamba hata anayemaliza Chuo Kikuu akimaliza hawezi kujitegemea, akimaliza hawezi kujiajiri, hata yule aliyesomea ufundi, ukimwingiza ukampa kiwanda leo, akifika mle ndani hawezi kufanya kazi aliyosomea. Nasema kwamba, katika kipindi hiki cha miaka mitano, ni lazima mfumo wetu wa output katika vyuo vyetu usimamiwe vizuri ili watu wanaotoka waweze kuwa ni material ambayo inakwenda kupata kazi kwenye soko.
Mheshimiwa Spika, niende mbali, tuna output kubwa sana ya darasa la saba na output kubwa sana ya form four na form six ambao hawapati bahati ya kwenda kwenda kwenye Vyuo. Nataka kushauri, katika nchi zote ambazo zimefanikiwa kupambana na tatizo la ajira hasa kwa vijana, wameimarisha sana kwenye Polytechnic Colleges ambazo ndiyo zinaweza zikasaidia kupunguza tatizo la ajira. Kama tunaweza tukaweka katika Mpango wetu huu wa miaka mitano, tuweke mpango kuhakikisha kila mtoto aliyemaliza kidato cha nne, anakwenda Chuo cha Ufundi na iwe ni lazima. Hawa watu wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tumepeleka umeme katika kila kijiji, lakini mafundi wa umeme wanatoka Makao Makuu ya Wilaya. Hii sasa ilikuwa ni wajibu wa Serikali kuona kwamba tunaweka vyuo vya kutosha. Tunavyo Vyuo vya VETA, bado vyuo hivi ni gharama kubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Chuo ambacho ulidhani angeenda mtu kusoma akapata ufundi, bado vyuo hivi vinachukua watu kwa kuchagua, wanakwenda watu 100 kati ya watu 10,000. Matokeo yake, bado kundi kubwa la vijana limezagaa mitaani, halina ujuzi wowote na Serikali nina uhakika hata tukizungumza kuwapa ajira, hawa sio sehemu ya kundi tunalofikiria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kushauri, pamoja na kuzagaa kwa vyuo, pamoja na mpango mzuri wa Serikali, tuweke mpango kabambe wa kuwa na vyuo vya ufundi ambavyo vitamlazimisha kila mtoto anayemaliza kidato cha nne, aende Chuo cha Ufundi ili apate kazi mbadala.
Mheshimiwa Spika, huwa nawaambia rafiki zangu tunaokwenda China; kule China ziko simu watu wanatumia hapa, zinatengenezwa mitaani tu, kwenye nyumba ya mtu. Ziko nguo zinashonwa mitaani, viko vitu vinatengenezwa hata ukitafuta kiwanda, huwezi kukipata kwa sababu kuna msambao wa viwanda vidogo vidogo katika kila kona na ndiyo namna tunavyoweza kupambana na tatizo la ajira kwa vijana, lakini na tatizo la viwanda.
Mheshimiwa Spika, kwenye Mpango kuna suala la viwanda. Tatizo langu ni kubwa. Hivi tunazungumzia viwanda vya namna gani? Viwanda hivi vitapata raw material wapi? Sehemu kubwa ya viwanda tunavyozungumza ni viwanda vya kilimo. Wilayani kwangu tuna Kiwanda cha Pamba cha Ginnery, kipo pale Kasamwa. Kile kiwanda hakijafanya kazi karibu miaka 15 sasa. Ukitazama uzalishaji wa zao la pamba umeshuka kwa kiwango ambacho kinatisha. Tatizo, kwa nini uzalishaji unashuka? Productivity ya uzalishaji inapungua wakati gharama za kilimo zinaongezeka! Viwanda tunavyozungumzia vinakwenda kupata raw material wapi?
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwenye suala la kilimo, kwanza tu- invest kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka maradufu ili watu watakaoanzisha viwanda wapate raw material. Leo watu wanalima pamba wanapelekewa mbegu feki, halafu mwisho wa siku kwenye uzalishaji mdogo waliopata, wanakwenda kudaiwa na kulazimisha walipe. Matokeo yake ni watu wote wameacha kulima pamba, wanahamia kwenye mazao mengine.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri katika Mpango huu tuwekeze kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji kwenye mashamba, uzalishaji wa mazao katika viwanda ambavyo tunafikiria tunakwenda kuvipeleka, lazima tufikirie namna ya kuongeza mazao yawe makubwa zaidi. Uzalishaji uwe mkubwa zaidi; na njia hapa ni rahisi tu!
Mheshimiwa Spika, cha kwanza ni kuwa na wataalam wetu katika kila kijiji na kuhakikisha wanafanya kazi; lakini kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati. Tulikuwa na tatizo la pembejeo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anajua. Pembejeo zinafika kwa wakulima mwezi wa kwanza. Wakulima wamekwishalima, wameshapalilia ndiyo pembejeo zinafika. Hawa watu wanalipwa!
Mheshimiwa Spika, tumeiambia Serikali kwamba kuna watu wanadanganya kwenye pembejeo, Serikali inatumia pesa nyingi sana, lakini haziwafikii wakulima; zinachelewa kufika. Ndiyo maana mtu analima heka tano za pamba anapata kilo 300. Ni kwa sababu pembejeo zinachelewa kufika. Kwa hiyo, nasema suala la viwanda liangaliwe vizuri kwenye suala la kilimo. Vile vile twende pia kwenye namna ambavyo tunaweza tukawaimarisha wananchi wa kawaida
Mheshimiwa Spika, sina tatizo sana na masharti ambayo yanayowekwa na watu wa Mazingira na kadhalika, lakini nadhani tume-copy sana mambo kutoka Ulaya kiasi kwamba tunashindwa kufikiria katika mtazamo wa Kitanzania, ni viwanda gani vinaweza vikasaidia wananchi wetu? Unaona kila siku tunapambana na watu wanaotaka kujikwamua.
Mheshimiwa Spika, kule Ulaya ukienda, mtu mwenye ng‟ombe wanne anaweza kuanzisha Kiwanda cha Siagi nyumbani kwake na akapeleka mazao yake kwenye Supermarket. Sisi kila siku tukienda kwenye mtu aliyeanzisha kiwanda, tunamfungia, huyu tunamfungia. Badala ya kuwasaidia hawa watu waimarike na wakue, tunawapunguzia uwezo. Utaona Serikali inapambana na watu wapunguze ng‟ombe, lakini haiwambii hao ng‟ombe wanaowapunguza itawasidiaje wabadilike kuwa na maisha tofauti.
Mheshimiwa Spika, mfugaji wa ng‟ombe anafanana sana na mtu mwenye mabasi kumi. Siku zote mtu mwenye mabasi kumi anataka afikishe mabasi 20. Hivi tuliwahi kumfuata mtu mwenye mabasi 20 tukamwambia apunguze idadi ya mabasi? Kwa nini tunafikiria kumwambia mwenye ng‟ombe apunguze, lakini hatumwambii apeleke wapi hizo fedha zake?
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwenye hili suala la viwanda, tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wa kawaida kuimarisha viwanda vidogo vidogo. Haijulikani SIDO ilifia wapi? Haijulikani kama ipo, inafanya kazi gani?
Nilitarajia tuone Tanzania ina Viwanda vya Sabuni kila Mtaa, Viwanda vya Nguo kila Mtaa na Viwanda vya kila kitu kila Mtaa. Sasa haya mambo hayafanyiki kwa sababu ya masharti mengi yanayowabana Watanzania na kuwafanya waendelee kutegemea bidhaa za kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze suala linguine. Kwenye Mpango naona kuna mpango wa kuongeza nishati. Nilisema wakati nachangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nikasema naipongeza sana Serikali na mkakati wake wa kuimarisha njia ya umeme inayokwenda Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa na wasiwasi sana ya kuwa na njia moja kuu ya umeme ya kupelekea robo tatu ya nchi. Napenda kushauri, katika Mpango huu, ile njia iliyotajwa katika Mpango; ya Nyakanazi, ni njia ya muhimu sana. Nchi nyingi zinapata majanga! Linaweza kutokea janga katikati hapa, nusu ya nchi ikawa giza na nchi hii inakwenda kuwa nchi ya viwanda. Ina maana tutasimama uchumi wetu siku hiyo hiyo. Ni lazima tutafute namna ya kuimarisha njia ya pili ya umeme.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Geita, bado umeme unazimika na kuwaka muda wowote kwa sababu njia iliyopo ni ile iliyokuwa inapelekea umeme Sengerema. Umeme ni mdogo sana. Wananchi pale kukatika kwa umeme kwao ni suala la kawaida, lakini umeme mzuri upo jirani tu Katoro pale.
Mheshimiwa Spika, nimezungumza na Waziri mara kadhaa na nimeomba sana katika mwaka huu wa fedha, umeme wa uhakika upelekwe Geita. Ni Mkoa mpya, Mkoa ambao tunatarajia utakuwa na viwanda vingi. Sisi katika Kanda ya Ziwa ni wakulima wakubwa sana wa nanasi, ingawa nanasi zile Mheshimiwa Mbunge mwenzangu alisema zinafaa kutengeneza madawa ya kienyeji, lakini tunapozungumzia viwanda, basi lazima wakulima waambiwe ni mananasi yapi yanayofaa kwa ajili ya kuuza kwenye viwanda, kwa sababu ardhi inakubali kulima nanasi, kahawa na mazao mengine. Ni lazima tukubaliane kwamba tunahitaji umeme ili huu umeme uweze kuwasaidia wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Spika, katika Mpango huu, naomba sana, sisi Kanda ya Ziwa kama walivyosema wenzangu, tunalo tatizo la bidhaa zote zinazotoka Dar es Salaam kufika Kanda ya Ziwa zikiwa zimepanda bei. Ukifika Geita leo, utakuta bandali moja ya bati inauzwa Sh. 280,000/= wakati bandali hiyo hiyo Dar es Salaam inauzwa Sh.160,000/=. Ni kwa sababu ya matumizi ya barabara. Tunaomba sana reli, reli ikiimarika, itasaidia kupungua gharama za vifaa vya viwandani ambavyo vinapanda bei kila siku Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, hata gharama ya mafuta iliyoko Geita ni kubwa kuliko iliyoko hapa, ni kwa sababu tatizo kubwa ni Usafirishaji. Hatuwezi kuendelea kujenga barabara zinazobomoka kila baada ya miaka miwili kwa sababu inabeba mizigo mikubwa. Tuwe wakweli! Kama barabara hizi zinatumia mamilioni ya shilingi, tunakopa, wenzetu wanakaa wanasema hawaoni faida ya mikopo na barabara hizo zinakufa, keshokutwa tutalazimika kuzijenga upya kabla ya kulipa madeni. Njia pekee ya kufanya suala hili ni kuimarisha sana mfumo wetu wa reli ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na bidhaa zinazopungua bei.
Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye Mpango, kuna mpango wa kujenga Uwanja wa Ndege Chato. Kutoka Geita kwenda Chato ni kilometa zaidi ya 150. Geita ni Makao Makuu ya Mkoa. Naomba sana Wizara hii itakapofika, tunataka kujua kama kutakuwa na mpango wowote kwa Geita kupata uwanja wake wa ndege. Watu hawawezi kutembea kilometa 160; tunakubali kwamba Mheshimiwa Rais anatoka Chato na sisi tunafurahi kuwa na Mheshimiwa Rais Chato, lakini Geita kama Makao Makuu ya Mkoa, tunataka uwanja wa ndege.
Mheshimiwa Spika, Geita tunayo machimbo mengi sana ya dhahabu. Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa inapambana zaidi na maskini kuliko inavyopambana na umaskini.
SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu, kama unaunga Mkono hoja, dakika zako zimekwisha.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOHN C. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niseme kwa kifupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niwaombe wahusika Mfuko wa Jimbo bado unakwenda Halmashauri ya Wilaya hauji Halmashauri ya Mji walishughulikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la TASAF, tatizo lililosemwa na Wabunge wengine liko kwangu pia, naomba litazamwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati yangu ya UKIMWI tulikutana na Group of Donors, wanasema ufadhili unaendelea kupungua na wanaitaka Serikali kuongeza uwezo wake kwenye mfuko wa AIDS Trust Fund. Kwa sababu kadri wanavyoonesha inaonekana mwaka huu itapungua zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa hapa kwamba jukumu la Ofisi za Wabunge liko chini ya TAMISEMI kwa maana ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunaomba watoe maelekezo tunapotoka hapa tupate ofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme lingine, katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Geita kuna madeni ya watumishi ya tangu mwaka 2007. Madeni hayo yamefanyiwa uhakiki zaidi ya mara tatu lakini fedha hizo haziendi na hawalipwi. Nilitaka kufahamu kwenye bajeti hii kama fedha hizo zimetengwa na wataanza kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Geita yalifanyika mazungumzo ya Serikali ya Mkoa pamoja na mfadhili COTECNA, ambaye walikubaliana kujenga diagnostic centre. Baada ya mabadiliko haya ya Mkuu wa Mkoa yule mfadhili amekwishaandaa fedha anakwenda pale anasema waliopo wote hawatoi ushirikiano. Naomba sana apewe ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo la ukusanyaji wa service levy. GGM wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi lakini 90% ya hizo kampuni ziko nje ya nchi. Nilitaka kupata mwongozo hizo kampuni zilizoko nje ya nchi ambazo GGM hawataki ku-disclose kwamba zinatoaje service levy, tunazipataje hizo fedha Halmashauri ya Mji wa Geita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu tulitembelea Buhangija, tukaenda kwenye kituo cha watoto albino. Tulipofika pale tulikuta kuna taarifa kwamba wake wa viongozi walifanya harambee kuchangia kituo kile miaka miwili iliyopita lakini fedha hizo hazijawahi kufika na tulikuwa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Possi. Tunaomba kujua waliofanya harambee hizo fedha zilikwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchangia kwenye suala la ujenzi wa ofisi. Nchi hii kila Halmashauri ina ramani yake, nataka kushauri pawe na common ramani ya Halmashauri zote. Halmashauri yangu ina fedha za kujenga ofisi miaka minne sasa fedha ziko ndani, ofisi haijengwi na kwa taarifa zilizopo wamepunguza karibu shilingi milioni 300 kuchoresha ramani mpya. Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo alikuwa amewaletea ramani ambayo tayari imechorwa na imejengwa sehemu zingine. Naomba Mheshimiwa Waziri afuatilie ili Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya iweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu ya muda nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu ada elekezi, Serikali iwaache wamiliki kupanga bei kwa kuwa gharama za uendeshaji wa shule hizo ni kubwa sana kutokana na michango mingi na kodi. Pia shule hizi hazifanani kutoka moja hadi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nizungumzie kuhusu vibali vya Walimu wa nje. Serikali iangalie namna ya kuondoa vizuizi vya Walimu wa kutoka nje kufundisha Tanzania hasa Walimu wa masomo ya hesabu na sayansi. Urasimu mkubwa wa Serikali wa kupata working permit na kodi kubwa inayotozwa na Serikali inakatisha tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Chuo cha VETA Geita. Naiomba Serikali kunipatia majibu ni lini chuo cha VETA kitajengwa katika Mkoa wa Geita ambao ni mpya na eneo la kujenga chuo hicho lilitengwa toka mwaka 2014. Kwa mujibu wa VETA, ujenzi wa chuo hicho ulikuwa umefadhiliwa na ADB kwa thamani ya 6.7 billion, leo miaka miwili hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu utitiri wa vyuo binafsi. Serikali ichunguze sana viwango vya elimu vinavyotolewa na vyuo mbalimbali vilivyosajiliwa na NECTA. Mfano ni Chuo cha Elimu ya Utalii Musoma kimefungua matawi katika wilaya za Kanda nzima ya Ziwa, je, ubora wa certificate na diploma hizi unafanana? Hii ni pamoja na matawi ya vyuo vikubwa na vidogo Tanzania ikiwemo CBE, Mipango na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, madeni ya wazabuni mashuleni. Serikali itoe taarifa ni lini itawalipa wazabuni fedha zao walizotumia kutoa huduma mashuleni. Hivi sasa hali ya huduma katika shule zetu ni mbaya kutokana na madeni haya ya wazabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, nyumba za Walimu vijijini. Naishauri Serikali kuanzia sasa itoe tamko la kuzuia kabisa halmashauri zote kujenga nyumba za watumishi wa mjini, kuacha kujenga ofisi za vijiji na kuacha kununua magari mapya na kuhamishia pesa yote kwa miaka mitatu kwenye nyumba za Walimu. Nashauri pia ramani ya nyumba simple iandaliwe kwa ajili ya nchi nzima mfano vyumba viwili vya kulala, sitting room na jiko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Nakushukuru sana Mwenyekiti, na naomba nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, niwashukuru pia wapiga kura wangu wa Jimbo la Geita Mjini na wananchi wa Geita kwa ujumla wake kwa uvumilivu wao mkubwa wanaoupata kwenye matatizo ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kusoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 ambapo amesema Serikali iliajiri kampuni ya Shaka Consult Group ya Misri kuwa mshauri mwekezaji wa kusimamia utekelezaji wa mradi wa Bulyanhulu - Geita KV-220 kwenye urefu wa kilometa 55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameendelea kusema hapa lakini interest yangu ni kule chini; anasema gharama za mradi huu ni dola milioni 23 sawa na takriban bilioni 41. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni shilingi bilioni sita, very interesting, na unatarajiwa kukamilika 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mradi huu ambao ameukusudia kuupeleka Geita. Ninaamini kwamba una nia njema, lakini natazama fedha zilizotengwa sasa na pia natazama muda ambao umejiwekea kutekeleza nayaona matatizo makubwa ya umeme katika Mji wa Geita kwa sasa yataendelea kuwa kero kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu nimsumbua sana mara kwa mara, umeme wa Geita Mjini unazimika kila saa, umeme wa Geita Mjini ambao unatokea Sengerema kuja Geita ni mdogo, ulikuwa umefikiriwa kwa ajili ya Mji wa Sengerema na baadaye ukapelekwa Geita. Umeme ule inapofika saa moja jioni unawaka lakini taa haziwaki. Nimemueleza hili Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri analijua, sasa nilitarajia kwenye taarifa yake hii atakuwa angalau na mpango wa dharura kwa sababu Geita pale ni Mji mkubwa, lakini ni Mkoa ambao tungeweza kuweka mpango mzuri wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninayo mapendekezo, tunao umeme kilometa 22 tu kutoka Geita Mjini ambao uko Katolo ambao ni umeme wenye nguvu. Wakati unafikiria mradi mkubwa huu ambao utaisha 2018, na inawezekana ukaisha 2020. Umeme huu ambao uko kilometa 22 tu kutoka Katoro kuja Geita, na ambao gharama yake inakadiriwa haifiki bilioni moja kuuvuta kuufikisha Geita Mjini, ingelikuwa ni suluhisho la kwanza la kupeleka umeme katika Mji wa Geita. Hivi ninavyozungumza na wewe kata zinazotengeneza Mji wa Geita wenyewe, kata za Nyankumbu, Bombambili, Buhalahala, Mtakuja zote hazina umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani umeme upo pale pale kati kati ya Mji lakini Vitongoji vyote vya Geita Mjini havina umeme. Pamoja na huo uliopo kutokuwa hautoshi lakini havina umeme. Kuna sehemu wameweka transfoma ambayo kila inapofika jioni saa moja umeme unazimika. Nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na nia njema ya mradi huu unaokwenda mpaka 2018 ambao pia naona fedha zake zimewekwa za kuanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe suluhisho la sasa, kwa sababu umeme uliopo Katoro una nguvu, utolewe umeme upelekwe pale. Bahati nzuri sana Geita tuna Meneja mzuri wa TANESCO, ana-respond haraka, hana matatizo makubwa, kinachosumbua pale sasa ni kumwezesha ili aweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye umeme wa REA. Katika Jimbo la Geita Mjini umeme wa REA bado katika kata zote 13 haujaenda, nimefanya mawasiliano na Meneja wa REA wa Kanda ile amesema ametuingiza kwenye awamu hii, lakini nilikuwa naomba sana, kwa sababu tatizo hili naliona hata katika Jimbo la Geita Vijijini, kazi ya mkandarasi imekamilika mpaka sehemu ya kutoka Nyamadoke tayari; pale panatakiwa tu kuunganishwa ule umeme, leo karibu miezi sita hapajaunganishwa. Nilikuwa naomba sana kwenye umeme wa REA Mheshimiwa Waziri suala hili lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni suala la wachimbaji wadogo wadogo. Mheshimiwa Waziri alikuwepo Geita, na nashukuru kwamba tulifanya mkutano naye na akatoa takwimu nyingi sana. Lakini anakumba nilitoa ushauri wangu pale sikumpinga nilitoa ushauri, ana takwimu nyingi sana zinazoonesha wachimbaji wadogo wamepewa maeneo lakini wanaopewa ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayepewa leo London – Singida, anayepewa leo Nyarugusu, anayepewa Kahama, majina ni yale yale. Nilimshauri atengeneze database, atagundua yako majina yale yale yanazunguka. Kila yanapogunduliwa madini wanakwenda wanafukuza wenyeji, wanaunda ka-SACCOS wananunua watu wanahamia pale. Nashauri kwamba wananchi wale wa kawaida bado hawapati maeneo, na ndio maana kelele za magwangala zitaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunazungumzia maeneo ya wachimbaji wadogowadogo lazima tuangalie watu wanaojirudiarudia, watu ambao kila mara yanapogundulika madini wanakwenda pale kwenda kutafuta maeneo mapya. Tulipokutana na Mheshimiwa Waziri kwenye ziara yetu Geita tulimgusia kuhusu milipuko. Mheshimiwa Naibu Waziri tulikuwa naye Geita, tulikwenda kwenye nyumba ambazo zimeathiriwa na milipuko, tulikwenda kwenye nyumba ambazo vigingi vya GGM viko ndani ya makazi yao, wale watu hawaruhusiwi kupima, hawaruhusiwi kuuza, wanaonekana eneo ni la mgodi lakini mgodi wanasema hawana kazi nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauriana na Mheshimiwa Naibu Waziri na akatoa muda, akawaambia wafanye declaration kama wanalihitaji lile eneo walipe fidia watu watoke na kama hawalihitaji, wawaruhusu watu waendelee na maisha yao mpaka leo hili suala halijafanyika, matatizo ya watu yanaendelea kuwa pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niseme kwamba kuendelea kukaa katika vigingi watu hawa wanaendelea kuwa maskini. Hawawezi kupima, hawawezi kukopeshwa, hawawezi kujenga nyumba za kudumu. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu atuambie anafanya nini kwa sababu hali hii inasababisha wananchi wangu wa Jimbo la Geita kuendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo kuhusu magwangala. Kama wanavyosema wenzangu magwangala inatokana na vijana wengi na wanotaka biashara za madini kukosa maeneo ya kuchimba; si suluhisho la matatizo ya wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu nina uhakika magwangala yale hata yakitolewa leo baada ya miezi miwili, yatakwisha na yatakapokwisha yale magwangala tutatengeneza tatizo jingine kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka kusema pamoja na nia njema ya kutoa magwangala haya ambayo wananchi wanayapigia kelele, wananchi walikuwa na maeneo yao walikuwa wanachimba ya asili pale Geita, kama Nyamatagata, Samina wakaja wakatolewa, lakini maeneo yale dhahabu yake iko juu juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa Geita akisema yeye hawezi kubadilisha hata mtu ampige risasi. Mimi nataka nimshawishi Mheshimiwa, sheria inasema kila baada ya muda, wanapofanya revision ya license kuna maeneo watu wanayaachia, ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo wanayaachia yawe ni maeneo ambayo wananchi wanaweza wakachimba wakapata dhahabu ya juu juu.
Mheshimiwa Mwnyekiti, matatizo tuliyonayo sasa hivi Geita ni kwamba hata kama watu wa GGM wangejenga hospitali, shule na barabara kama jamii inayowazunguka pale inalala njaa, kama jamii inayowazunguka pale bado wanaishi katika mazingira kama wako utumwani bado wataendelea kuwachukia wawekezaji na tutaendelea kuuchukia mgodi.
Kwa hiyo, mimi nilitaka niwashauri kwamba ni lazima wananchi wapewe maeneo ya kuchimba, na hili liko ndani ya uwezo wako kwa sababu maeneo tunayo. Tatizo kubwa ni moja walipelekwa maeneo ya Isamilo, wakapewa license karibu 17 za SACCOS wamechimba watu wameweka karibu milioni 200 madini hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechimba pale wanakutana na maji madini hakuna, kwa hiyo mara nyingi migodi inaachia maeneo ambayo imefanya utafiti imegundua kwamba dhahabu zilizopo pale ni ndogo na hazifai. Kwa hiyo nikuombe sana utakapotaka kutoa maeneo tuhakikishe kwamba maeneo haya yana madini ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la service levy. Mheshimiwa Waziti alipokuwa Geita, tulimwambia hatuna mgogoro na Geita Gold Mine ingawa mchango wao wa service levy ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita ule ni mgodi wa pili Afrika kwa dhahabu nyingi, wanatupa bilioni nne. Tuliuliza swali, hizi ni asilimia ngapi ya mapato yao? Kwa sababu tunaamini mapato yao ni makubwa sana, lakini la pili, wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi. Katika hizo asilimia 80 kampuni zile ziko Ulaya, Australia, New Zealand na Marekani, wanafanya nazo electronic business. Kwa hiyo, anampa Mkurugenzi wa Halmashauri aende akakusanye service levy kwa kampuni ambayo haina license Tanzania, hailipi kodi Tanzania, haina address Tanzania. Tulimwambia Mheshimiwa Waziri, watu wa mgodi walazimishwe kufanya kazi na kampuni za Tanzania ambazo tunaweza kuzi-trace na kujua zinapatikana wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wanakupa kampuni iko New Zealand halafu wanakwambia ukusanye service levy kampuni hii haijulikani, haina leseni, hailipi kodi za Serikali, hata Tanzania haina address na Mheshimiwa hili niliwahi kufika mpaka ofisini kwako nikakutana na Katibu Mkuu wa Wizara, nikamshauri, nikazungumza naye na akasema atalishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa watu pamoja na kuwaibia Halmashauri ya Geita, bado pia wanaiibia Serikali. Huwezi ukalipa mtu dola milioni moja kampuni yake iko South Africa, Tanzania haina leseni, hailipi kodi, haina ofisi na Serikali ipo inakubali hizo hesabu wakati wa kufanya Cooperate tax.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana hili liangaliwe vizuri. Na inawezekana kabisa haya yanafanyika kwenye makampuni yote katika nchi hii, kwa sababu visingizio ni kwamba kuna vipuri ambavyo vinaagizwa Ulaya na Watanzania wengi hawana uwezo wa kuviuza, yes tunakubali, lakini procedure za kufanya biashara Tanzania zinajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Watanzania hamuwaruhusu hata kufungua kibanda cha soda bila kupata TIN Number. Kwa nini huyo anayellipa mamilioni ya shilingi anaanza kufanya biashara na Mgodi na analipwa pesa na inakuwa declared kwenye hesabu wakati hana leseni Tanzania na halipi kodi? Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri asaidie kupata hizi fedha kwa sababu ni fedha nyingi na tunazihiitaji kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama unavyoitaza Geita sasa hivi, kuna mashimo makubwa, ambayo tayari dhahabu zimekwisha. Inawezekana kabisa miaka ishirini ijayo tukabaki na mashimo yale na wananchi wa Geita wakaendelea kubaki maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu ni kwamba wakati mgodi unafikiria kufanya CSR washirikiane na Halmashauri kuangalia miradi ambayo sisi tunadhani ina tija kwetu. Siyo wao wanabuni mradi wao halafu ule mradi wanaugeuza kuwa mradi wa wananchi wa Geita. Tunaunga mkono juhudi zao tunapenda waendelee kuwepo, tunataka wawekezaji zaidi lakini lazima waangalie mipango ya Halmashauri namna gani wataingia kwenye mipango hiyo kuliko kuja na mipango yao wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekwenda wameanzisha, chuo cha kushona cherehani wameanza na watu 90 sasa hivi wako watu kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba pia nitumie nafasi kukupongeza kwa namna ambavyo unaendesha Bunge letu na niwape pole wenzetu ambao wanasubiri siku ambapo utalegeza msimamo. Nadhani hii ndio namna bora ya watu kuheshimu taratibu na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kuchangia kwa hoja ya Mkoa wa Mwanza, Geita na Kagera kuonekana ni mikoa maskini zaidi Tanzania. Mwanzo ni kweli na nilikuwa napata shida, na nilikuwa sielewi mantiki ya suala hili linatoka wapi? Lakini nimekuja kugundua sababu za msingi ni kama ambazo wenzangu wamezieleza. Yapo mazao na kazi za msingi ambazo zilikuwa zinafanya maeneo haya yaonekane maeneo ambayo uchumi wake uko juu, yanaenda yanakufa polepole.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Geita, ambao miaka yote tulikuwa tunajivunia pamba, sasa hivi pamba imekufa hakuna dalili kuna mkakati maalum wa Serikali wa kurudisha zao hili kwenye chati na ukiangalia trend yake ya uzalishaji kwa miaka mitano, mwaka jana ilikuwa even worse. (Makofi)
Kwa hiyo, nadhani kwamba, hatuna sababu kwa nini tusiwe maskini. Mkoa wa Kagera walikuwa kahawa inakosa soko, walikuwa na migomba, migomba inaugua, ndivyo ilivyo katika mikoa mingine mingine ya Mwanza na Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaanza msimu wa pamba, lakini nataka kukuambia mpaka leo bei haijulikani na wananchi wana pamba iko ndani na ni haya haya ambayo mwakani zikija takwimu hapa itaonekana mikoa hii ni maskini sana. Kwa hiyo, nilikuwa nasema, Serikali pamoja na kutoa takwimu hizi bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha kwamba, ina-coordinate mazao haya na kazi hizi za wananchi ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia katika Mkoa wa Geita, ambao una dhahabu katika kila Wilaya, haijulikani mpaka leo wale wachimbaji wenyewe wa dhahabu wanauza wapi? Wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu haijulikani wanauza wapi? Wanaojulikana ni wanunuzi wa dhahabu wakubwa wakubwa. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba uchumi huu mdogo katika level ya chini hauko coordinated, haujulikani. Lazima wananchi hawa waonekane ni maskini, lakini influx inayosababishwa na machimbo katika Mikoa ya Geita na Mwanza na wapi ni kubwa sana na watu wote hawa wako bize kwenye kazi za kiuchumi. Nilikuwa nadhani watu wa uchumi wanatakiwa wafanye kazi vizuri zaidi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi kwenye bidhaa ambazo walikuwa wanauziwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Naweza nikaunga mkono suala hili, lakini naomba nitoe mapendekezo yangu kwamba bidhaa hizi zinaweza zikalipiwa kodi, lakini uwekwe utaratibu ambao utavifanya vyombo yetu vya ulinzi na usalama viwe na credit card wakati wa kufanya manunuzi. Kwa mfano kama askari hawa wataweza kwenda kwenye duka lolote bila kujali duka hili ni lile ambalo limetengwa, wakiwa na credit card au debit card na wakaweza kupata punguzo la kodi pale pale, mantiki ya maduka haya itaendelea kuwa ile ile na mantiki ya kuwapa huduma nyepesi wanajeshi watu itakuwa ile ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongeza mshahara au ukaongeza pesa kwenye mshahara wake haijulikani huyu mtu atanunua nini kwa mwezi, nina uhakika kwamba tutaendelea kufanya maisha ya vyombo hivi kuwa vigumu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na naomba nichangie pia kwenye suala la kufutwa kwa misamaha kwenye taasisi mbalimbali. Ni kweli kwamba, Serikali ilikuwa inapoteza karibu shilingi trilioni mbili kwenye kodi kwa sababu ya misamaha, lakini ninataka tu kutoa hoja hapa kwamba kama vyombo hivi vitalipa kodi, urasimu wa namna ya kurejeshewa kodi hii lazima Serikali ijipange vizuri. Kwa sababu nitapa wasiwasi namna wanavyokwenda kugagua na kujiridhisha kwamba, bidhaa hizi zilizoingizwa zimetumika kwa mujibu wa malengo yaliokusudiwa na matokeo yake tuta-demoralize hawa waliokuwa wanasaidia. Maana yake ni lazima tukubaliane nchi yetu mpaka leo, sehemu kubwa ya Hospitali zilizo kwenye Wilaya, sehemu kubwa ya taasisi ziliko hapa, shule pamoja na nini zinamilikuwa na taasisi mbalimbali. Kama watu hawa watakatishwa tamaa na wataacha tutakuwa tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa hiyo, lazima Serikali iangalie namna ya kulifanya hili ili lisije likatela usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yamefanyika marekebisho mbalimbali kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Waziri kwa kuondoa baadhi ya tozo kero kwenye maeneo mbalimbali. Lakini nilitaka kusema bado mazingira ya kufanya biashara kwenye nchi yetu ni magumu sana. Nitoe mfano sehemu moja tu. Sehemu ya hoteli, mtu akiwa na hoteli leo pamoja na kupata leseni, pamoja na kupata tax clearance kutoka TRA itaanza kulipa OSHA, atalipa Fire, atalipa hotel levy, ana aina ya tozo pale karibu kumi, ambazo zote hizi zinafanya mzunguko wa pesa kwa wananchi kuwa mdogo. Sasa inaonekana Serikali inajiaanda tu kukamata pesa kila kona na kuzirudisha kwake.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba bado kuna haja ya kuangalia vizuri, kwenye hoteli hapo utakuna na mtu wa afya, utakutana na mtu wa TFDA, utakutana na kila aina ya ushuru na wote hawa ni vyanzo vya mapato, nilikuwa nadhani kuna haja nzuri ya kuliangalia vizuri upya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi za majengo, naweza kusema kwamba nilikuwa naunga mkono watu wa Halmashauri waendelee kutoza hizi, lakini nitaunga mkono TRA iwapo Mheshimiwa Waziri, utatuambia ni kwa namna gani pesa zilizokadiriwa kwenye Halmashauri atahakikisha zinapatikana kama zilivyo kwenye bajeti, vinginevyo tutajikuta kwamba, wakishindwa kukusanya TRA madhara yakuwa makubwa sana kwenye Halmashauri zetu za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makato kwenye gratuity ya Mbunge; nilitaka tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, sisi Wabunge wa Bunge la Tanzania kwanza ni Wabunge tunaolipwa kidogo zaidi kuliko Mabunge yote Afrika Mashariki. Nataka nitoe takwimu hapa, ukichukua salary na allowance, Bunge la Kenya walipwa dola 11,000, Rwanda dola 9,000, Uganda dola 8,000, South Sudan dola 7,000, Burundi dola 6,000, Tanzania ni least pay dola 5,000, hii ni salary na allowance. Sasa atuambie baada ya kuingiza haya makato anakwenda kuboreha wapi ili tufanane na nchi zingine? Kama hilo halifanyiki nataka kumshawishi Mheshimiwa Waziri afikirie namna mpya ya kutanua hii tax base kwa sababu kinachomsumbua sasa ni kufikiri kwenye base ile ile wakati unaongeza projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na njia rahisi ya kutanua tax base, akumbuke kati mwaka 2007 na 2010, Serikali iliweka stimuli kwenye baadhi ya viwanda na mazao ili kuwa inalinda visife ili Serikali isipoteze walipa kodi. Sasa ushauri wangu hapa tunavyo viwanda vingi vimesimama, kama tunataka kuongeza kukusanya mapato tupeleke pesa huko viwanda vifufuke tuanze kukusanya kodi vinginevyo leo wataanza kukata kodi kwenye gratuity, kesho watakuja kwenye allowance, atakuja kwenye per diem baadaye pataisha pa kukata kodi wakati huo anaendelea kupanua projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba pia suala la polisi ambao wamewekwa kwenye chanzo cha mapato. Unapo-commercial raise service ukawambia polisi wakae barabarani ukawapa malengo ya kukusanaya shilingi bilioni moja, maana yake unawambia wakamate sana watu barabarani na kwa tabia ya polisi hawa-negotiate na wateja tutaanza kupata migogoro mingi kwa sababu watajielekeza kwenye kufikia malengo ya kukusanya shilingi bilioni moja kwa mwezi. Nilikuwa nadhani hawa wangeachwa watoe huduma na inapotekea wanatoa faini iwe ni faini ya kawaida, lakini wanapowekwa kwenye kikapu cha kuanza kukusanya pesa na kwamba lazima walete shilingi bilioni fulani lazima tunatengeneza mgogoro mkubwa kati ya watumiaji wa barabara na poilisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na lingine ni kuhusu kodi kwenye withdraw mbalimbali M-pesa na benki. Nataka tu kufahamu kwamba Serikali imejiandaaje kuweka regulatory board ambayo ita-control sasa wasipandishe hovyo hovyo. Walizoea hizi pesa zote kuzichukua wao, sasa tumepeleka kodi pale matokeo yake wataongeza, tutajikuta watu wanaogopa kupeleka fedha benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kunipa afya njema na kupata nafasi ya kusema machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini pia na Kamati ambazo ziliwasilisha maoni yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kwenye hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 21. Waziri Mkuu ametoa takwimu za upatikanaji wa chakula kwa mwaka uliopita na akagusia kwamba mwaka huu kuna maeneo ambapo hali ya hewa haikuwa nzuri sana. Nilichokuwa nakitegemea hapa kidogo na nitoe ushauri ni kwamba kutokana na hali hiyo kutokuwa nzuri, kwanza nilitarajia nione hapa kama kuna akiba kiasi gani sasa ya chakula lakini tunakitumia kwa namna gani ku-control bei inayoendelea kupanda kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza jana Mwanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 125,000 na wakati kelele za uhaba wa chakula zinaanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 80,000. Hii maana yake ni nini? Kadri tunavyokwenda kuja kufikia mwezi wa kumi kama hakuna
mechanism ya Serikali ku-control bei ya mahindi yatafika shilingi 160,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza hapa sio njaa, hatuzungumzi njaa tunazungumzia kwamba bei ya chakula inapanda kwa sababu Serikali ni kama haijachukua position yake ya ku-control bei ya chakula kwenye soko. Wakati tunazungumza wakati ule bei ya mchele ilikuwa
shilingi 1,200 leo ni shilingi 2,500, Mwanza ni shilingi 1,800. Maeneo yote haya ninayoyazungumzia hawakulima kwa sababu mvua hazikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama tunayo stock ya chakula kwenye godowns, Wizara ichukue position yake, chakula kingie kwenye masoko na bei elekezi itolewe ili kisiendelee kupanda, vinginevyo purchasing power ya wananchi
inapungua. Wananchi kipato ni kilekile, chakula kinapanda, matokeo yake watajikuta hata hiyo shilingi 2,000 ya kula kwa siku inakosekana. Hilo ndiyo lilikuwa ombi langu kwenye huu ukurasa wa 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 25 amezungumzia kuhusu hekta 38,567 za wachimbaji wa madini. Tatizo langu mimi sio utengaji wa maeneo, nilimwambia Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita akazungumza takwimu kubwa za
kuwapa watu maeneo ya kuchimba. Nikamwambia tatizo kubwa lililoko hapa wanaopewa ni walewale. Ukiingia kwenye database utamkuta Kanyasu huyu ana-appear kwenye karibu kila eneo dhahabu inapotokea wale ambao wanatakiwa kabisa wapewe maeneo haya hawapewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe tuna vikundi zaidi ya 100 Geita vimejiandikisha vinasubiri maeneo ya kuchimba havipewi, lakini ukienda kwenye takwimu za Wizara atakutajia kubwa ya watu ambao kimsingi ni walewale wachimbaji wakubwa ambao wanahama toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana, ni ahadi yetu kwenye Ilani ya CCM, tutawapa watu maeneo ya kuchimba, lini? Huu ni mwaka wa pili sasa. Kama yapo tunaomba yaanze kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 28 limeongelewa suala la umeme. Geita kila siku umeme unakatika. Hivi ninavyozungumza na wewe umeme hakuna, unakatika zaidi ya mara nne. Nimezungumza na Waziri na Naibu Waziri, wana matengenezo ya kutoka Busisi kwenda
Geita karibu miaka miwili hayaishi. Nataka kufahamu hili tatizo la umeme Geita linakwisha lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, kuna maeneo tumepeleka umeme wa REA baada ya umeme wa REA kufika kazi imeisha, jirani akiomba umeme TANESCO hakuna vifaa. Ina maana REA peke yake ndiyo sasa inafanya kazi ya kusambaza umeme, TANESCO wenyewe hawana uwezo? Naomba sana eneo hili lifanyiwe kazi vizuri kwa sababu linakatisha tamaa, kama umeme umefika kijijini, kuna watu wanne wamepewa umeme, jirani hapewi umeme kwa sababu TANESCO hana vifaa, nadhani hapa kuna mipango mibovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la fao la kujitoa. Mimi natoka Geita na naomba Waheshimiwa Wabunge wote wanisikilize vizuri sana. Geita pale karibu nusu ya watu wanaofanya kazi pale Geita Mjini ni watumishi wa mgodi. Kinachotokea kwenye mgodi pale ni kwamba
hakuna mwenye ajira ya kudumu. Kuna watu pale wanafanya kazi kwa mikataba ya miezi sita, miaka miwili, miaka mitatu. Anapofukuzwa kazi hawezi kupata kazi ya aina ile tena katika nchi hii, kuna wengi ni vibarua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu wanafukuzwa kazi, kwa sababu kandarasi iliyokuwa imempa kazi mkataba wake umekwisha, imeondoka imekwenda South Africa. Akienda kufuata pesa zake NSSF anaambiwa hizo pesa hawezi kupewa mpaka afike umri uliolezwa. Mtu leo ana
miaka 25 au 30 asubiri pesa hizi mpaka afikishe miaka 55 ndiyo aweze kulipwa na hana kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja ametoa hoja kwamba wapewe asilimia 25, hapana. Ziko kada ambazo wanaweza wakasubiri, ukimwambia mwalimu, polisi, daktari asubiri sawa. Pale mgodini kuna tabia supervisor akikuchukia anaku-blacklist,
akiku-blacklist huwezi kuajiriwa mgodi wowote duniani. Sasa unakaa unasubiri hiyo pesa mpaka utakapofikisha miaka 60 unaendelea kuwa maskini kwa misingi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri, sekta ya madini iangaliwe kwa jicho tofauti. Kuna watu pale wanaacha kazi kwa sababu ni wagonjwa. Mgodi ule hauchukui watu wagonjwa, ukitibiwa mara mbili unaumwa kifua wanakufukuza, Mheshimiwa Jenista unafahamu nilikuletea watu wanaumwa, walipokuwa vilema walifukuzwa kwenye kazi, wana miaka 25, 30 halafu wananyimwa zile pesa wanaambiwa wasubiri mpaka watakapozeeka, anazeeka hizo pesa aje atumie nani? Ushauri wangu ni kwamba sekta ya madini ichukuliwe kwa namna tofauti, hatuwezi kuwa na jibu moja kwenye maswali yote magumu, lazima tuliangalie hili suala tofauti. Kama tuna nia ya kuwekeza NSSF wana mitaji mikubwa waangalie sehemu nyingine, lakini haya maisha ya watu kwa pale Geita tutawafanya kuwa maskini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna gereza pale Geita Mjini, uwezo wake ni kuchukua watu 100 na zaidi, hivi sasa lina watu 800, sababu kubwa ni wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatafuta pesa ndogo ndogo ya kula, akikamatwa anarundikwa pale. Kuna tatizo sasa hivi kwenye Jeshi la Polisi na watu wa Idara ya Sheria, kesi ya madai inageuzwa inakuwa jinai wanarundikwa mle, matokeo yake watu wanalala wamesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu na nafikiri nilizungumza na wewe, pale kuna tatizo tuna OC-CID hafanyi kazi yake vizuri, kazi yake ni kukusanya pesa, anachokifanya yeye ni kuhakikisha kwamba kila anayetuhumiwa pale, iwe ni jinai, iwe ni civil lazima
abambikwe kesi ambayo itamuweka magereza zaidi ya miezi mitatu, gereza limejaa. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alikuja aliona, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ulikuja uliona, tunaomba mtusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hizi kesi ndogo ndogo za kupita tu mgodini anakamatwa mtu anawekwa ndani miezi sita. Unapita tu na baiskeli unakamatwa unawekwa ndani miezi sita. Serikali ina pesa za kuchezea, kwa nini hizi pesa ambazo zinakwenda kulisha watu humo
wasipewe hawa wanasheria wakapeleka hizi kesi haraka? Mimi nadhani kuna haja ya kuisaidia Wilaya ya Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni uwepo wa migodi mingi sana kwenye Mkoa wa Geita na tatizo la huduma za afya. Wilaya ya Geita peke yake ina watu 800,000 kwa sensa ya mwaka 2012, lakini hospitali yetu iliyokuwa ya Wilaya tuliigeuza kuwa ya Mkoa, matokeo yake hatuna tena Hospitali ya Wilaya. Sasa ufikirie population ya watu 800,000 wa Wilaya moja na ile hospitali imegeuka kuwa ya mkoa, watu milioni mbili matokeo yake ile hospitali imezidiwa kabisa uwezo. Tuna vituo viwili vya afya tumeanza kuvitengeneza, tunaomba support yako Mheshimiwa Waziri wa Afya, tunakushukuru ulitupa gari lakini hatuna madaktari. Daktari aliyepo pale kuna specialist mmoja ambaye ni surgeon waliobaki wote ni AMO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali, tulitaka kuleta muswada hapa wa kuwaondoa Madaktari Wasaidizi kwenye mfumo wa madaktari, lilikuwa ni kosa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule vijijini madaktari wetu ni ma-AMO na ndiyo wanaofanya kazi usiku na mchana. Ukiwaondoa wale kwenye mfumo wa madaktari waliobaki wengine wote ni mabosi wakienda kwenye wilaya kazi yao ni research, hawakai kwenye ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi namuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mtusaidie sana Hosptali yetu ya Mkoa wa Geita ianze ili Hospitali ya Wilaya irudishwe Wilayani ili gharama za matibabu ziweze kupungua. Hivi sasa navyozungumza na wewe gharama za matibabu ziko juu sana kwa sababu tunalipa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na mimi naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema kuweza kusimama hapa leo, lakini kipekee naomba nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayofanya ya kutuletea maendeleo Watanzania, lakini pia ya kuongoza Serikali vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba nikiri kwamba, Waziri anatupa nafasi ya kutosha kutusikiliza, anatoa ushirikiano mkubwa, lakini ni mtu ambaye yuko accessible, unaweza kumpata muda wowote unapomuhitaji. Kwa hiyo, yeye pamoja na timu yake nzima, Katibu Mkuu na wasaidizi wake tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasahau mdogo wangu Mheshimiwa Sanga amezungumzia mitambo ya kutengeneza barabara na akatamani Halmashauri ziruhusiwe kununua. Natamani sana aje ajifunze Geita, tulitenga shilingi bilioni 1.4 kila halmashauri kununua mitambo na ile mitambo haijawahi kuonesha value for money. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasikitika sana hiyo mikoa yote naweza nikakutajia Mwanza wanayo, Sengerema wanayo, yote yako grounded, kwa nini, na ni mapya? Yote ni kutoka CAT - Caterpillar, lakini huwezi ku-manage matumizi yake, wakienda site wale wanaoendesha wanabadilisha pump, anabadilisha roller, anabadilisha hiki, matokeo yake yale madude yanakuwa grounded siku mbili hayana kazi. Sasa ni vizuri kuja kujifunza kabla ya jambo hilo.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpe taarifa mzungumzaji, hatuwezi kuacha kufanya maendeleo kwa kuogopa uzembe wa baadhi ya watu ambao hawasimamii wajibu wao waliopewa na Serikali. Kwa sababu watu wa Geita kama hawasimamii hayo ma-caterpillar wanaachia watu wanaenda kuiba na kuchukua vitu haizuwii Halmashauri kama alivyosema Mheshimiwa Mheshimiwa Sanga kununua ma-caterpillar kwa halmashauri nyingine zinazofuata. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu, hiyo taarifa, umeipokea?

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia na Watanzania wamemsikia, lakini nimesema akajifunze Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili. Ntaka kuipongeza sana Serikali, ilisema katika Bunge hili kwamba, itatangaza ajira 30,000 na zimetangazwa…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba Makete tulinunua excavator toka mwaka 1998 na tunalo hadi leo. Anavyosema kwamba tukajifunze kwa watu ambao wame-fail, hakuna utamaduni wa kujifunza kwa watu walio-fail, tunajifunza kwa watu waliofanikiwa, kwa hiyo, hatuwezi kwenda kujifunza Geita kwa watu walio-fail. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Na mnaweza mkajifunza kwa Mheshimiwa Jerry Silaa mpaka leo analo bado. (Makofi)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa yake siipokei. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema naipongeza Serikali ilipotimiza ahadi yake ya kuajiri watumishi zaidi ya 32,000 na ninaipongeza kwa sababu tumekuwa na uboreshaji na uongezaji wa miundombinu katika maeneo mbalimbali kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mfano na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, tulipata fedha za UVIKO, tumejenga madarasa katika Halmashauri ya Mji wa Geita, madarasa zaidi ya 63, lakini kutokana na mapato ya ndani tumejenga shule karibu sita mpya, shule tatu za sekondari na shule mbili za primary. Tunahitaji walimu wa kutosha, lakini kwa bahati mbaya shule zile nyingi zina walimu wachache kwa sababu hapakuwa na staff, hatukuwa na walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaipongeza Serikali, lakini namuomba Mheshimiwa Waziri aje sasa na taarifa inayoonesha uwiano wa mahitaji pamoja na ajira iliyotolewa ili tuweze kujua tume-cover kwa asilimia ngapi. Kwa sababu tunaweza kuajiri 32,000; lakini mahitaji ya mpaka tunaahirisha Bunge mwezi wa pili ilikuwa ni walimu 120,000 lakini pia aje na mkakati tunaziba vipi hilo gape ambalo sasa litakuwepo?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri na tunashukuru kwa hizo ajira ambazo zimetangazwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nataka kuzungumza, Geita Mji imekuwa na ahadi ya kuwa Manispaa tangu mwaka 2018. Tumezungumza na Waheshimiwa Mawaziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wote waliokuwepo na ahadi mbalimbali zimetolewa. Nataka nitoe vigezo ambavyo vinasababisha Halmashauri kuwa Manispaa; la kwanza ni kuwa na watu wasiopungua laki moja sisi tuna watu takribani laki tatu, lakini la pili asilimia 30 ya wakazi wake wawe na ajira isiyohusiana na kilimo. Sisi pale asilimia 80 ni wafanyabiashara ya madini na biashara nyingine ambazo hazina uhusiano na kilimo, tuko mjini, lakini la tatu inasema kuwe na walau kiwanda kikubwa kimoja, tuna mgodi mkubwa pale ulioajiri zaidi ya watu 12,000; lakini la nne inasema tuwe na uwezo wa asilimia 70 ya uwezo wa kujitegemea Halmashauri, Halmashauri ya Geita Mjini ina uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 83, maana yake tumeshavuka hiyo habari, lakini lingine inasema kuwepo na huduma mbalimbali ya kwanza elimu ya watu wazima tunayo, hospitali ya rufaa tunayo, chuo kikuu tunacho, ukumbi wa mikutano tunao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kumwambia Mheshimiwa Waziri tunataka Geita ipewe hadhi yake ya kuwa Manispaa. Mlituongezea sharti moja tu la kupata master plan, tumekamilisha master plan na tayari Geita tunayo master plan. Sasa tunakuomba tupewe hadhi ya kuwa manispaa kwa sababu, mnatuchelewesha kuendelea, tunakusanya zaidi ya bilioni 15 kwa mwaka kwa hiyo, tunataka sisi tukimbie ninyi mnatusimamisha, tunaomba tupewe tuweze kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuongea ni jambo la TARURA. Kwanza naipongeza sana Wizara imefanya kazi vizuri, naipongeza sana Serikali, kwa mujibu wa takwimu kwa miaka minne yote mfululizo TARURA walikuwa wanapewa kwa wastani wa fedha wanazoomba; walianza kuomba mwaka 2019 shilingi bilioni 639 walipata fedha kwa asilimia 25 takribani, mwaka 2020 waliomba shilingi bilioni 699 wakapata asilimia 24 na asilimia 38 asilimia 35, lakini mwaka huu wa fedha unaoisha waliomba shilingi bilioni 717 wakapata kwa zaidi ya asilimia 96, naipongeza sana Serikali kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo nataka kusema hapa TARURA inasimamia mtandao wa barabara zaidi ya asilimia 90 Tanzania kwa hiyo, ni chombo ambacho lazima kitazamwe upya kiongezewe uwezo ili kiweze kusaidia miundombinu, lakini jambo moja Mheshimiwa Waziri Halmashauri zote uliziongezea pesa, ulitoa mwanzo milioni mia tano-mia tano fedha za jimbo za barabara ukapandisha bilioni moja, lakini Geita Mjini ukaiacha na milioni 500.

Mheshimiwa ninaomba hiyo pesa iongezeke ili tuweze kutengeneza barabara, barabara ni mbaya na Geita imekaa kwenye muinuko kila mvua inayonyesha maji yanaenda kwenye miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niipongeze pia Serikali kwa mradi wa TACTIC, tumeusubiri kwa miaka mingi sana, tumekaa tukiusubiri, lakini sasa unakuja. Hoja yangu hapa Mheshimiwa Waziri wakati ule tunatekeleza mradi wa LGSP tulijikuta mradi una- phase out fedha ziko kwenye account. Sasa tunataka tuiombe Serikali this time kwa sababu tunakwenda kwa pamoja tutakaposema tunaanza paa, miradi yote iliyotajwa kwenye mradi itangazwe ili tusiache fedha kwenye account, lakini barabara zitengezwe. Tumeipongeza sana Serikali kwa mradi huo na tunaomba jambo hilo liweze kufanyiwa mchakato mapema ili tuweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuchangia ni kuhusu Machinga Complex. Nampongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa kwetu wa Kamati amezungumzia kuhusu Dodoma, tulikwenda kutembelea machinga inayojengwa hapa Dodoma, mimi nikataka kukuuliza Mheshimiwa Waziri, hawa viongozi wetu wa mikoa wanakwenda kwenye semina tofauti?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia modal waliyoitumia Dodoma, namna walivyo-handle machinga ni tofauti na machinga nchi nzima. Ukienda mikoa yote machinga wamekuwa displaced, wamepelekwa kwenye maeneo ambayo wamefilisika, Dodoma wameachwa wanafanya kazi zao, mpaka leo tunavyozungumza wako barabarani, lakini wanajengewa miundombinu na miundombinu ile inaonesha wazi kwamba kuna mtu amekaa ame-plan. Sasa Dodoma walikuwa na formula tofauti na mikoa mingine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitu kingine cha mwisho Mheshimiwa Waziri, nimeona Dodoma Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kujenga machinga. Naamini tu sababu ni makao makuu, unakuja na package gani ya mikoa mingine ya Halmashauri nyingine ili kama hazina uwezo wa kutenga fedha hizo kwa sababu kundi hili ni muhimu ziweze kutengewa fedha kujenga kwa sababu, sasa hivi ninavyozungumza na wewe machinga almost wamefilisika na watu wengi sasa usije ukashangaa ujambazi ukaongezeka kwa sababu hawana kazi ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo nataka kuzungumza hapa ni hoja ya mifumo. Ilikuja moja ya idara zinazoshughulikiwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni eneo la uboreshaji wa mapato. Halmashauri yangu na Halmashauri nyingine wamebinafsisha ukusanyaji wa mapato, sasa nataka kutoa mfano; mmempa uzabuni wa kukusanya takataka mwananchi kwenye mitaa miwili ukamwambia kwa mwezi akusanye milioni tano, lakini asilimia 80 ya fedha ni za kwake, anakusanya anapata kwenye mashine yake inasoma alikusanya milioni 3.8, zile fedha unazikataa unasema hapana kalete milioni tano, akizikosa anawekwa ndani mpaka ifike milioni tano, lakini akishaweka milioni tano unamrudishia milioni nne na laki mbili. Kwa nini watu wa mifumo wasi-develop system ambayo computer iwe ina-tally ambazo zinatakiwa zipokelewe na Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kama ninatakiwa kwenye shilingi mia hela ya Serikali ni shilingi ishirini, computer imuoneshe mzabuni kupeleka shilingi ishirini kuliko kumng’ang’aniza apeleke milioni kumi anawekwa ndani, anakopa halafu baada ya siku mbili unamrudishia milioni tisa, kazi zimesimama mwezi mzima. Sasa hivi mji wangu wa Geita ni mchafu kwa sababu wazabuni wote wamekimbia, kwa nini, kwa sababu mwingine anadaiwa laki tano, anadaiwa laki nne, lakini katika milioni kumi hela ya kwetu ya Serikali ni shilingi milioni 1.2. Mfumo unaweza kutengenezwa ili kuweza kudhibiti suala hilo. Pesa inayopokelewa pale iwe ni ile ambayo kisheria inayotakiwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kushukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati zote mbili ambao wamewasilisha leo kwa taarifa zao nzuri. Pia kipekee niwapongeze Wajumbe wa Kamati hizo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala ya TAMISEMI na katika Kamati yetu tulipata bahati ya kuzikutanisha Kamati mbili. Kamati yetu ya Utawala ya TAMISEMI pamoja na Kamati ya Ardhi na tulikutanisha Kamati zote mbili baada ya karibu kila halmashauri tuliyokwenda kwenye ziara, tulikuta kuna migogoro mikubwa sana ya ardhi. Tulifanya kikao cha pamoja, lakini mwisho tulikuja na maazimio ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti ameyazungumza kwenye hotuba yake.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kuzungumza kidogo kuhusu migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma. Wananchi wa Jiji la Dodoma wanateseka sana na migogoro ambayo ilitengenezwa. Tunayo maeneo ambayo yalipimwa awali kama mashamba ya mjini. Waliopimiwa wakatoweka, baada ya miaka 30 Dodoma imetangazwa kuwa jiji, wakarudi lakini maeneo hayo yaliyopimwa kama mashamba Serikali haikuyafanya kuwa mashamba yakageuka yakawa vijiji. Dodoma ilipokuwa Makao Makuu likaibuka wimbi la kupima maeneo kupata viwanja. Dodoma wakaenda kupima maeneo kwenye hivyo, kupata viwanja, matokeo yake wanasema hayo maeneo ni mali yao kwa sababu walishayapima wakati wenyeji wa maeneo hayo walikuwa bado hawajalipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, haikuwa imefanyika land acquisition kabla ya kutengeneza hizo broad acres au hizo town farms ni mashamba ambayo ya mjini kuwapa hawa watu na hawa watu walitoweka hawakuyaendeleza. Wenye mashamba yao wananchi wenyeji wa pale wakaendelea kuishi kwenye maeneo hayo. Wamekuja wamepima wanasema haya maeneo sasa ni ya jiji.

Mheshimiwa Spika, ninao mfano mmoja, mwananchi mmoja alikuja anaitwa Daudi Samamba kwenye stendi hii ya kuelekea Bahi. Kushoto kwake kuna go down ya Banj, kulia kwake kuna stendi wamepima jiji. Yeye amebaki katikati ana heka 15, wamekwenda wamepima pale wamemnyang’anya wanasema haya maeneo ni ya jiji, lakini wote wa kushoto na kulia ambao tayari wamekwishabinafsisha, wamebinafsisha kwa kuuziwa na huyo huyo kama mwenyeji. Matokeo yake huyu mtu amekwenda kwa Mkuu wa Wilaya, amekwenda kwa Mkuu wa Mkoa, amekwenda kwa Kamishna. Kamishna ameelekeza kwamba wamtafutie eneo lingine mbadala.

Mheshimiwa Spika, huyu mwananchi akapelekwa Kikombo karibu kilometa 60 kutoka hapa mjini. Kule anaenda kuambiwa alipie tena ardhi kama mnunuzi mpya. Umemnyang’anya mwananchi kutoka kwenye prime area, hukumpa fidia heka 15, unampeleka kumpa viwanja vitano ambavyo havifiki heka moja halafu una mwambia anunue ardhi. Huu ni udhulumaji, huu ni wizi na huu ni uonevu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Kamati yetu imekuja na mapendekezo kwamba, hauwezi ukalitengeneza tatizo halafu ukaachwa pale pale kutafuta suluhu ya tatizo hilo. Maafisa waliohusika kwenye kutengeneza tatizo la migogoro mikubwa ya ardhi katika Jiji la Dodoma, bado wapo na ndiyo bado wanawasikiliza walalamikaji. Wizara ichukue hatua, hawa watu wawekwe pembeni, watafutwe watu ambao kutoka sehemu nyingine ambao hawana interest, waweze kuwasaidia hawa wananchi wa Dodoma ambao wanateseka wengi kwa sababu watu wanaoshughulika ni wale wale ambao wametengeneza tatizo hilo. Wananchi wapo na nadhani jambo hili linaeleweka vizuri kwenye Kamati.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tulikuwa na Kamati ya Mawaziri Nane. Walikuja Geita Mjini lakini mchakato unaujua vizuri. Tulianza kwa kutengeneza mchakato wa Wabunge kuleta maoni, Viongozi wa Wilaya kuleta maoni. Kwa hiyo yako maeneo ambayo sisi kama Wabunge na wawakilishi tuliamini kwamba haya yamekuwa sababu ya mgogoro wa kila siku. Wamesema baadhi ya Wabunge hapa kwamba watu wanakamatwa sana na Maaskari wa Maliasili na Maaskari wa Misitu. Nikisema maeneo haya tayari yamekwishakuwa sehemu ya makazi. Pale Geita Mjini tuna msitu wa Osindakwe. Msitu wa Osindakwe umepoteza sifa ya msitu kwa sababu tayari kuna watu wanakaa mle ndani.

Mheshimiwa Spika, tulipendekeza msitu ule urudishwe kwa wananchi kama yalivyo maeneo mengine hasa kwenye taarifa ambayo Mheshimiwa Rais ameidhinisha, eneo lile linazuiliwa kwamba ni chanzo cha maji. Hakuna kisima, hakuna bwawa, hakuna mto, hakuna chochote. Kwa hiyo kila siku wananchi wanakamatwa pale na kutozwa faini na kunyanyaswa kwamba kuna chanzo cha maji wakati ni katikati ya mji na hakuna kitu chochote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ombi langu hapa, kuna migogoro mingine tunaitengeneza wenyewe. Tunaleta manung’uniko bila sababu za msingi kwa sababu watendaji wengi wanalazimisha kushikilia maeneo ambayo tayari walishindwa kuyazuia yakapoteza sifa.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, Kamati yetu ilizungumza na Wizara ya TAMISEMI. TAMISEMI wanaisimamia TARURA. Tunaipongeza Serikali kwa kuongeza fedha kutoka shilingi bilioni 200 kwenda karibu shilingi bilioni 800. Bado kuna tatizo kubwa sana la barabara. Pale Geita mjini tunao mradi wa TACTIC. Tumeuzungumza sasa takribani mwaka wa tatu, wa nne. Kuwepo kwa mradi huu kunasababisha hata kwenye mgao wa fedha zingine za maendeleo, inapofika habari ya Geita Mjini unaambiwa kwamba ninyi mna barabara ya TACTIC, lakini mradi hauanzi, mradi haukamiliki. Nilianza kuuzungumza mimi wakati wa awamu ya kwanza ya ubunge wangu, sasa nakwenda awamu ya pili ya ubunge wangu, mwaka uko katikati.

Mheshimiwa Spika, ombi langu, jambo hili kama lipo, yafanyike maamuzi ya mradi huu uweze kuanza haraka ni pamoja na ujenzi wa Stendi ya Geita Mjini iko ndani ya mradi huu. Fedha tuliambiwa zipo, wamekwishakuja watu wa upembuzi yakinifu kutembea zaidi ya mara 10. Sasa mwisho unajiuliza, kama gharama hizi za kulipa posho watu njoo rudi, njoo rudi ni sehemu ya package hii, si mwisho itafika nusu wamelipana wao kwa ajili ya kuja kukagua eneo? Kwa sababu umeshakuja zaidi ya mara 10, kila siku unakuja unaenda, unakuja unaenda, mradi hauanzi.

Mheshimiwa Spika, ombi langu, mradi huu kama upo, uanze na kama haupo ijulikane kwamba huu mradi haupo. Hakuna kitu kinatesa wananchi kama unaambiwa mradi huu utaanza kesho halafu unachukua tena mwaka mwingine mradi haujaanza.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kusema ni jambo la ajira. Tunaishukuru sana Wizara ya Utumishi, Ofisi ya Rais, imerahisisha zoezi la interview. Tumepeleka kwenye kanda, lakini hoja yangu iko pale pale, kama tumeweza kupeleka kwenye kanda, zamani tulikuwa tunasafirisha watu kwenda mpaka labda Dodoma kutoka nchi nzima, tulizungumza hapa tukasema tuna watu wengi ambao wanatafuta kazi wenye sifa, shida imekuwa ni nafasi. Ile database ambayo imetengenezwa na Wizara ya watumishi ambao wamekwishafanya interview wasilazimike watu kufanya interview zaidi ya mara mbili au mara tatu.

Mheshimiwa Spika, tunaona, PCCB wanatangaza nafasi miezi mitatu, miezi mingine mitano wanatangaza tena, wanaoomba ni 8,000. Wanaochukuliwa ni 200, maana yake ni nini, wanao-qualify wapo zaidi ya 1,000.

Hatuna sababu ya kuendelea kila siku tunatangaza jambo lile llile kwa sababu tunaingizia watu gharama, hasara halafu unakuta mtu anafanya interview moja mara 20, maswali yale yale na wanakwambia ni very simple questions. Mtu anaulizwa maswali yale yale lakini hafaulu mtihani anafanya mara 10. Sasa tutengeneze hii kanzidata, mtu akifanya mtihani, aki-qualify pawe na cut off point ikitokea mahali kuna nafasi zimetangazwa na zipo, waitwe walio-qualify hata kama mwanzo walikuwa wameitwa watu 100, sasa zimepatikana 200, waulizwe je, bado una-interest na kazi hii? Kuliko kila tunapokuwa na ajira tunatangaza upya, tunaita watu wapya, tunaita new brains kutoka shuleni, watu wamekaa mtaani wana miaka minne, wamefanya mtihani mara 10, wakienda kupambana na vijana kutoka chuo kikuu juzi wanashindwa, watu wanazeeka na vyeti ndani.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa sababu ya muda naomba nizungumze mambo machache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Geita Mjini tulipopata bahati ya kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Geita karibu nusu ya eneo la upande wa Mashariki miaka ya 1954 lilikuwa declared kwamba ni hifadhi, hakuna msitu wowote kuna bushes. Nilimwandikia barua na kumuomba kwamba wananchi wa Geita ule mkoa hauwezi kutanuka kuelekea Kaskazini wala kuelekea Magharibi kwa sababu ni eneo ambalo limepewa mgodi, eneo pekee la kutanuka ni kuelekea Kusini, na Mkoa kupitia RCC wameomba katika vikao tangu mwaka 2012 kuomba eneo la Msitu wa Usindakwe na eneo ambalo lilikuwa Msitu wa Geita (Usindakwe) liwe eneo ambalo Mkoa uruhusiwe kutoa maeneo ya makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza karibu nusu ya Mji wa Geita ni eneo ambalo zamani lilikuwa declared kwamba ni hifadhi, sasa nilikuomba Mheshimiwa Waziri kwa maandishi lakini sasa ni karibu miezi sita naomba leo uniambie ni hatua gani zimefikiwa? Sababu moja ni kwamba mpaka leo watu wa TFS wanazunguka, wanaweka alama kwenye nyumba, wana-disturb watu, lakini hakuna mti, hakuna chochote. Katika maeneo ya Nyakabale na Mgusu wananchi katikati ya kijiji kuna vigingi na katikati ya eneo la vijiji hivyo tayari mgodi umepewa eneo hilo, hivyo, wanashindwa kufanya chochote kwa sababu eneo hilo linaonekana kama ni hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni TFS katika Mkoa wa Geita, limetoka tangazo kupitia kwa Waziri kwamba ni marufuku kutumia pikipiki, baiskeli kubeba mkaa wala kubeba chochote. Vijiji vyetu vyote ambako wananchi wanakaa hakuna magari, hakuna chochote, kwa hiyo matokeo yake watu wa TFS wamerundika pikipiki na baiskeli Makao Makuu ya Ofisi zao na wanategemea kuzipiga mnada. Baiskeli ambayo imenunuliwa shilingi 150,000 inauzwa shilingi 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo hili ni uonevu mkubwa kwa sababu wananchi katika maeneo hayo ya vijiji hawana usafiri mwingine wowote mbadala zaidi ya baiskeli. Sasa sheria inaposema kwamba ni lazima tutumie magari, kusafirisha mkaa, hivi wananchi kwenye vijiji wanapata wapi magari? Kwa sababu inavyonekana ni kama mkakati wa kuwadhulumu wananchi baiskeli zao, ananunua mtu baiskeli, anakamatwa anakimbizwa porini ananyanganywa na sasa hivi watu wa TFS wanakwenda kwenye masoko kusubiria watu. (Makofi)
Mimi nafikiri TFS wamesahau core function yao. Core function yao ni kulinda misitu, wanachokifanya sasa siyo kulinda misitu tena, ni kusubiri barabarani waendasha baiskeli na pikipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuambie na tangaza leo hawa wananchi wanatumia nishati gani? Tuambie tu mimi niko tayari kuwaambia wananchi sasa acheni, ni nishati gani mbadala ambayo Wizara yako imeandaa kwamba sasa hii ndiyo itakuwa nishati mbadala? Kinachoendelea sasa hivi na kwa wananchi ni kwamba wananchi wanalazimishwa sasa waanze kulala njaa kwa sababu mkaa unakamatwa sokoni, unakamatwa barabarani, anakamatwa mwenye baiskeli, pikipiki, gari haijulikani utaratibu huu sasa unatupeleka wapi.

Mheshimiwa Waziri inawezekana wewe huna taarifa, nguvu inayotumika kwenye suala hili kule kwenye maeneo ya wananchi ni kubwa kuliko hata thamani ya kitu kinachoenda kuzuiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikushauri Mheshimiwa Waziri, kwa nini unapata tatizo kubwa sana la kulinda misitu yako, unapata shida ya kulinda hifadhi? Kwa sababu ya mahusiano mabaya sana ya TFS na vijiji. Watu wa samaki walibuni kitu kinaitwa Beach Management Unit (BMU) kwa sababu wananchi wanatakiwa wajisimamie wenyewe. Ninyi mnatumia nguvu kubwa, amesema Mheshimiwa Mbunge asubuhi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua kuna maeneo ya wananchi katika Wilaya ya Ilemela ambayo Jeshi liliyapima ili kuyachukua kwa miaka mingi bila kulipa fidia na kuwaondoa wananchi katika maeneo hayo, Mheshimiwa Waziri naomba kufahamu uthamini uliofanyika maeneo ya Nyagunguku - Ilemela, Nyanguku, Lukobe kwa miaka miwili sasa umefutwa au bado upo valid?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lengo la JWTZ lilikuwa kufanya uthamini na baadaye kuwaacha wananchi katika maeneo yao kwa muda mrefu bila kujua hatima yao, naomba kujua watalipwa lini au Jeshi limejiondoa kwenye nia ya kumiliki maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatana na timu za Orjoro JKT na Kanembwa JKT kushushwa daraja kwa tuhuma za rushwa ambazo zimeshindwa kuthibitishwa na chombo cha kisheria cha uchunguzi wa makosa hayo (PCCB). Je, ni hatua gani Wizara yako imechukua kupigania haki ya vijana wako na heshima ya vyombo hivyo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kudorora sana kwa michezo ya aina mbalimbali, mfano, riadha, sarakasi, ngumi, mitupo, volleyball, nimetaja kwa uchache tu kwa nini kuanzia sasa kipaumbele cha kijana kujiunga na JWTZ na JKT au vyombo vingine isiwe ni kipaji kimojawapo cha michezo ili kuufanya umma wa Watanzania kupenda michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili vijana hao wawe competent ni vizuri Wizara yako ikatafuta wabia (marafiki) kutoka nje ya nchi kusaidia kuongeza taaluma, mfano, China, Cuba, Urusi na Korea, ambapo vijana wetu waweze kupata ujuzi mpya au nyongeza ya ujuzi walionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Wizara yako ina mpango mkakati upi wa kusaidia kuimarisha michezo nchini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi na naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanya. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi ambazo anaendelea kufanya; na wananchi na watu wema wa Jimbo la Geita Mjini wanamkumbuka na wanamshukuru kwa ziara yake ambayo aliifanya mwaka jana na wanaendelea kuitakia mema Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa taarifa yake nzuri kwenye bajeti aliyoisoma kwa utekelezaji wa shughuli mbalimbali. Wananchi wa Geita wanaishukuru Serikali kwa kukamilika kwa hospitali yao ya mkoa ambayo imeanza sasa kufanya kazi za nje, kazi za OPD, wanaomba tu ikamilike ili iweze kuingia kufanya kazi kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa mradi wa maji wa takribani bilioni 100 ambazo Mheshimiwa Rais alitupatia, na mkandarasi yuko site na anafanya kazi. Tunashukuru Serikali kwa fedha za barabara kupitia mradi wa TACTIC ambao tayari wakandarasi wametangazwa na wanaanza kufanya kazi. Wananchi wa Geita wanaishukuru sana Serikali kwa fedha za stendi ambazo taratibu za TAMISEMI zinaendelea. Wananchi wa Geita wamenituma nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu ombi lao la Mji wa Geita kuwa Manispaa, taratibu takriban zote zilikwishakamilika wanakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili likamilike kwenye mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais kule Kagera akizungumza kuhusu kuhamasisha watu kuwekeza na kulipa kodi alitoa maelekezo kwa TRA kuachana na madeni ya zamani na kuhangaika na kuhamasisha watu katika kukusanya kodi kwenye makadirio mapya. Sasa ilikuwa ni ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu; tunayo shida kidogo pale Geita. Mfanyabiashara anapofanya biashara na Mgodi wa GGM anapotoa invoice anatoa na risiti, anapotoa risiti inakuwa ina VAT lakini walipaji wanaweza kuchukua siku 30 mpaka 90 na wakati mwingine ikitokea dispute hawalipwi kabisa. Mfanyabiashara anaingia kwenye deni la TRA, inatokea mfanyabiashara anakamatwa wanawekwa ndani wanashtakiwa kwa fedha ambayo hajawahi kukusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili likienda sambamba na maagizo ya Mheshimiwa Rais; na ndiyo maana kuna madeni mengine yana miaka miwili miaka mitatu, wako wanye kesi mahakamani lakini kimsingi watu hawa hawajawahi kulipwa na GGM. Kwa hiyo ni ombi langu agizo hili la Mheshimiwa Rais liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili limezungumzwa hapa suala la BBT. Kwanza naipongeza sana Wizara kwa kuja na huo mkakati wa hayo makundi maalum kwa ajili ya kilimo. Nimeangalia malengi mahususi, kwamba ni kutoa mafunzo, kutoa mitaji, kutoa mashamba na kutafuta masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu kidogo juu ya sustainability ya zoezi hili. Kwanza, tumetenga heka 400, tumeziona pale Dodoma tunaanza. Natamani kujua kwenye mpango kila mwaka tutatenga shilingi ngapi ambazo zitakuwa zimetengwa kwa zoezi hili kwa nchi nzima? tunataka kuona katika halmashauri zote pana mashamba; kama alivyosema mchangiaji mwenzangu kutoka Itigi. Kwamba tunakuwa na mfumo ambao tutapata hao vijana katika halmashauri zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kinachofanyika ni collaboration ambayoo nina uhakika sustainability haiwezi kudumu kwa sababu tumekusanya watu waliokuwa wanatafuta ajira, tukawapa kazi lakini wamevutiwa wakiamini kwamba Serikali itaendelea kutoa pesa kwenye zoezi hili. Pale ambapo mrija huu wa Serikali utakapokatika hawa watu watarudi kwenye vijiji vyao. Nimeangalia kwenye orodha nzima watu walioko kwenye halmashauri yangu ni watatu, kule kwangu mashamba haya yako wapi? Kule kwangu mkakati wa kuja ukoje na mkakati wao umepangwa kudumu kwa muda gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano; zimeandaliwa takribani heka 47,000 lakini tatizo la ajira lipo leo, liko mwakani na liko mwaka unaofata. Kwa nini mashamba haya yasingebaki kuwa ya Serikali tukawa na vijana wanaofundishwa labda kwa program maalum kwa miaka mitatu, halafu wana-graduate wanaondoka wanakuja wengine kwenye kila halmashauri? Sasa hao uliowapa hizi ya miaka 60 au 90; kwanza sasa hivi wana miaka 30, sasa baada ya miaka 30 watakuwa wazee kuliko karibu watu wote tulioko humu ndani, halafu maeneo ya mashamba ya kuwapa vijana wengine itakuwa hayapo. Huo mpango uliopo wa kuwapa lease ya kudumu unawapa na hati halafu baadaye watakuwa na miaka 100 itakuwa shamba moja linamilikiwa na wajukuu 200 na hao wajukuu 200 wametoka Tanzania nzima kwa sababu bahati mbaya tunawachanganya kutoka mikoa yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni maoni yangu kwamba jambo hili ni zuri lakini liandaliwe katika mfumo ambapo litapelekwa kwenye kila halmashauri na halmashauri zile zitumiwe kama mashamba darasa lakini kuwe na mpango endelevu. Naitazama hii kama tulipoanza na ile kilimo kwanza ikaja big result. Vilikuja na presha sana halafu baadaye ikapita kwa sababu hatukuangalia sustainability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri jambo hili ni la msingi sana na liangaliwe vizuri. Kwenye ajira; ukiingia kwenye mfumo wa usajili wa ajira.com ukijaza zile credential zako zile za kwamba wewe una bachelor, ukirudi siku nyingine na umesema degree nyingine ule mfumo hakukubalii. Ukiwa umesoma diploma ule mfumo hakukubalii. Kwa hiyo siku ukijaza ule mfumo kwa mara ya kwanza ule mfumo kila unapotaka kuingia kurekebisha zile taarifa ulizonazo wewe mfumo unakataa. Vijana wengi kwenye soko la ajira ni mult- professional. Wanachokifanya, akisoma procurement, akasoma ualimu, akasoma project management akakosa anaamua kusoma profession nyingi. Sasa, ukishaingia mara moja ukajisajili ukirudi mara ya pili mfumo unakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo ombi langu ni kwamba mfumo huu uruhusu mtu kuingiza credentials zake hata kama ziko saba; kama amesoma certificate, diploma au amesoma digrii tatu aweze kuingia mle ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu VETA. Pale Geita Mjini tumejenga VETA, naishukuru sana Serikali. Mradi huu ulianza mwaka 2017/2018, leo ni 2023 Mheshimiwa Waziri Mkuu VETA haijakamilika. Majengo yapo, nyasi zimejaa na hakuna mwanafunzi. Tulio-target mwaka 2018 alipokuwa anamaliza form four, darasa la saba; sasa mwingine amemaliza chuo kuu, na kama yuko uraiani amekwishakata tamaa. Hivi mpango gani huu wa Serikali ambao hauna timeframe? Yaani mnataka tu kujenga tu ilimradi tu mnajenga haijulikani itafunguliwa lini, haijulikani vifaa vitakwenda lini, haijulikani training itaanza lini; ilimradi tuna taarifa tumejenga VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali; tulikuwa tunajenga mwanzo kwa mkopo wa African Development Bank hela ikarudi, tukachukua hela za Uviko tukapeleka fine, tumebadilisha design na mambo mengine. Naomba bajeti hii ije na bajeti ya vifaa ili chuo kile kianze. Kuna vijana wengi sana pale ambao wanatafuta kazi, wanakosa kazi kwenye migodi mbalimbali kwa sababu tuliazimia kuwa na VETA tuweze kufundisha zile skills ambazo zinatakiwa na mgodi pale na migodi mingine inayozunguka maeneo yale. Sasa leo mwaka wa sita tunazungumzia chuo ambacho hakikamiliki. Naomba sana jambo hili liweze kukamilika, lakini isiwe tu kukamilika iweze kukamilika kwa design iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne; juzi nilikuwepo kwenye uzinduzi wa upandaji miti ambao umeratibiwa na watu wa STAMICO, nawapongeza sana. Siku ile pia walikuwa wana-advocate makaa yao ya mawe ya Rafiki Briquettes. Kwanza napongeza sana juhudi hizo za watu wa COSTECH ambazo zimeendelea, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, shida yangu ni moja Rafiki Briquettes ni inatokana na mawe ambayo ni Wizara ya Nishati, watu wa STAMICO wanayo; lakini wanafanya kazi hiyo kwa ajili ya kusaidia kuongeza nishati, watu wa nishati wamo, wanasaidia kupunguza ukataji miti; watu wa misitu wapo kwa ajili ya kuokoa mazingira. Kwa hiyo jambo hilo linahusisha wizara nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu, hizi wizara nne zingetafuta namna ya kuli-coordinate hili jambo kusudi likapata mtu mmoja wa kulisimamia. Namna lilivyo sasa litapotea hewani halafu utabaki kuwa mtaa wa maonesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, na niseme tu tangu mwanzo kwamba mimi naunga mkono hoja. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameendelea kuifanya elimu kuwa kipaumbele kikubwa kwenye nchi, na hili tunaliona kwenye bajeti. Kwa mujibu wa bajeti ambayo tunayo takribani asilimia 17 imewekwa kwenye elimu, na haya ni maamuzi sahihi, na hakuna sehemu ambapo watu waliwahi kula hasara kwa kugharamikia elimu, kwa hiyo napongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kwanza kwa kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba pale Geita Mjini tuna Chuo cha VETA na kile Chuo cha VETA pamoja na kusua sua kwake kimefikia level ambayo naamini sasa tunaweza kuwa tayari kukifungua angalau tukaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu kumtaarifu mapema Mheshimiwa Waziri kwamba nimeunga mkono bajeti yake, lakini natamani kuona kwenye bajeti hii sasa ameweka mahitaji yote ya lazima ili kile chuo kiweze kuanza.

Tunahitaji walimu , vifaa na miundombinu mingine. Namna yalivyo sasa majengo yale yataanza kuharibika kabla hayajaanza kufanya kazi. Kwa hiyo nimesema naunga mkono hoja lakini namtahadharisha Mheshimiwa Waziri kwamba natamani kuona kwenye bajeti hii sasa chuo changu kinaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili Kamati imesema vizuri kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa walimu ; na jambo hili liko kwenye Halmashauri yangu. Mimi nina upungufu mkubwa wa walimu takribani walimu 500. Naipongeza sana Serikali imekuwa ikitupa walimu wachache; na hivi karibuni Mheshimiwa Waziri ametuma vishikwambi tunakushukuru sana kwa vishikwambi, amepelekea walimu .

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka anieleweshe vizuri; vishikwambi kama vilivyo havitawasaidia kama kwenye bajeti yake hatutaona ametenga fedha kwa ajili ya bundle kwa sababu watabaki na madude ambayo hayana kazi. Lakini nataka kujua sasa vitasaidiaje kupunguza upungufu wa vitabu? kwa mfano hata kishikwambi kimoja kikiwa kwenye shule kama kuna mfumo wa kuhamisha kufanya kishikwambi kuwa resource center na kuhamisha materials sasa kuyafanya yaweze kupatikana kwenye shule nzima ni jambo jepesi. Lakini shule zetu nyingi hazina printer, copier na umeme. Nataka kuona huo makakti vishikwambi hivi viweze kutumiaka vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu tuzungumzie habari ya mikopo. Naiomba Serikali, katika maeneo ambapo tumeendelea kufanya vizuri; tumeongeza fedha mwaka jana na nimeona mwaka huu pia wameongeza fedha kidogo kwenye mikopo lakini bado hatujatosheleza. Naiomba Serikali kapo kakundi kadogo sana ka walemavu, ambako kanahitaji tu kawekewe fungu maalumu, hata 1% au 2% ambao wanateseka sana. Ni moja ya kundi ambalo haliwezi kuhangaikia mikopo kama wanavyohangaikia watu wengine. Kwa hiyo kakundi hhiki kiwekewe kiwango maalumu kwamba aina yoyote ya mlemavu anapofanikiwa kwenda university habari ya mkopo kwake iwe granted, na jambo hili ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza NMB kwa kuja na package ya mikopo kwa ajili ya kukopesha wanafunzi. Shida yangu pale ni moja tu collateral ni nini? Huyu mwanafunzi collateral yake ni registration anaipata chuo kikuu? Nimeona, marejesho yake ni kama commercial, ni kama ya kibishara. Asilimia tisa ni hela nyingi sana kwa mtu ambaye hana uwezo wa kujisomesha.

Mheshimwia Mwenyekiti. kwanza registration iwe ni collateral number one, lakini cheti chake kiwe ndicho guarantee ya kumfanya huyu mtu aweze kuaminika. Familia nyingi hazina uwezo wa ku-service huu mkopo na riba ya asilimia tisa kwa mwanafunzi ambaye ameshindwa kujisomesha. Tunawapongeza sana kwa kuja na hiyo package, lakini bado naamini kwamba kuna haja ya kuapanua na kuona huyu anapopata udhamini peke yake iweze kumsaidia kwenda chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakwenda kwenye mambo yangu mawili ambayo nilitaka kusema. La kwanza, pamekuwa na double standard ya maelekezo kwenye ofisi ya Mheshimiwa Waziri. Unakuja waraka wa elimu. Kwa mfano kuna waraka wa elimu ambao umetoa maelekezo ya kuondoa darasa la kwanza mpaka darasa la nne kwenye bweni, na watoto wa bweni waanzie darasa la tano mpaka la saba. Mimi nataka Serikali inaisaidie; tunazo shule tayari ambazo zimefanya investment hii zaidi ya miaka 20 huko nyuma, na tuliwapa wenyewe leseni tukazisajili. Sasa tunapoleta waraka unaoanza sasa kuzuia tunafanya mambo gani? Maana yake tunazuia wale wasiandikishe watoto au tunawaambia wawekezaji wapya kwamba tunasheria double standard kwenye nchi moja kwamba ukienda shule B utakuta watoto wapo, ukienda shule C utakuta watoto hawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa mimi kwa maoni yangu Wizara itafute namna ambavyo itatoa waraka ambao utafanana kwenye usimamizi maeneo yote. Hata hawa wasimamizi wadhibiti ubora tutawapa kazi kubwa. Akienda kwenye shule A anakuta criteria tofauti, akienda kwenye shule B anakuta criteria ni tofauti, na wazazi pia tunawachanganya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja hapa; hakuna mtu aliyechagua, anayechagua kwenda kwenye shule ya gharama kubwa wala anayechagua kupeleka watoto bweni. Wako watoto wako kwenye bweni si kwa sababu wazazi wanapenda. Kuna mtumishi anaajiriwa leo, mke wake anaajiriwa Dodoma, baba anaajiriwa Lindi. Anakopelekwa baba hakuna shule, anakobaki mama nafanya kazi asubuhi mpaka saa kumi, solution ni kumpeleka mtoto bweni, kwa hiyo hawa wanapeleka mtoto bweni si kwa kupenda. Ninaiomba sana Wizara iliangalie jambo hili kwa mapana yake, isilichukulie jambo hili kama jambo ambalo watu wanaopeleka watoto kwenye shule za bweni wanapeleka kwa kupenda. Wengi wanapeleka kwa sababu mazingira ya malezi yanawalazimisha kutokuacha watoto na house boy ama na house girl, na matokeo yake Watoto hawa ni bora uwapeleke shule ambako unaweza kuwa na uhakika angalau na asilimia chache ya malezi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuwepo na utaratibu ambao ni uniform; tusije na utaratibu ambao unaanza kubagua sasa, watu waliowekeza mpaka miaka fulani wana masharti tofauti na wengine wanaokuja wana masharti tofauti. Hii itatuharibia sana kwa sababu inatuletea double standard kwenye eneo moja ambalo mimi naamini linahitaji kusimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na jambo ambalo ni la msingi kabisa katika maeneo haya, tunaamini kwamba, watu wote, hata kwenye shule za Serikali ambazo tunazo, kipimo kikubwa ni kuona kwamba wanafunzi na watoto tunaowapeleka wanapata elimu kwa mujibu wa mwongozo, sera na sheria za Serikali. Kinachoendelea sasa hivi ni kama vile kuna ushindani, sasa kunakuja ushindani, kwamba wanaotoa elimu binafsi ni washindani wa Serikali, lakini mimi Mheshimiwa Waziri nataka kusema hawa sio competitor wako shule binafsi ni partiners kwenye hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuikumbusha Serikali kwamba siku ikitokea shule zote za msingi za watu binafsi zikafungwa au ikatokea shule zote za Serikali zikafungwa mzigo huu mkubwa ambao umebebwa na wawekezaji binafsi utachukua miaka mingine 10 au 15 kufikia kwenye level ambayo tunayo sasa ya utoaji wa elimu Serikalini. Tuwachukulie hawa kama wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alizungumza hapa mzungumzaji mmoja jana kwamba, kwenye elimu ya sekondari na shule za msingi kuna kodi nyingi sana kiasi kwamba zingine zinakatisha tamaa wawekezaji wakifikiri kwamba tunawakomoa; lakini kimsingi jambo hili lilipaswa kubebwa na Serikali kwa sababu huu ni mzigo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananfunzi zaidi ya 200,000 ambao wako kwenye shule binafsi wakirudi ghafla Serikalini, iko miji ambayo haina maeneo ya kujenga shule. Nataka tu nitoe mfano, mimi nina shule yangu moja ya msingi inaitwa Mbugani ina watoto 4,500. Katika eneo lile tukisema tunafunga shule binafsi, tukaongeza watafika watoto 6,000; hakuna sehemu ambapo tutawapeleka hawa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ninaiomba Serikali, kutokana na upungufu wa walimu kuna michango mingi sana kwenye shule zetu huko chini. Kuna maeneo ambapo shule zinaamua kupeleka watoto kwenye kambi gharama zinakuwa kubwa. Kwa hiyo michango ile tuliyoifuta mwanzo imerudi kwa style kwa sababu ya ku-cover upungufu wa walimu. Sasa niombe itoe mwongozo ambao kama tumeruhusu kuajiriwa kwa mikataba, utolewe mwongozo na namna gani ya kufanya ili wazazi waweze kupunguziwa mzigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini pia kwa namna ambavyo hotuba imejielekeza kwenda kujibu kero za msingi ambazo zilikuwa zinasumbua hasa katika maeneo ambayo nimeona kwenye eneo la uvuvi ambalo nina interest nalo na eneo la madini. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais hasa kwa kuondoa kwa kweli utaratibu uliokuwa unatumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, pamoja na kazi yao nzuri ya kupitia mahesabu ya nyuma, hii watu wengi sana sio tu walikuwa wanapata tabu, lakini ukweli ni kwamba ukiniambia nitoe hesabu ya miaka kumi, miaka sita iliyopita lazima litaishia kwenye mazungumzo na ninayefanya naye hesabu. Kwa hiyo namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mwezi huu ilitoa bilioni mia moja kwa ajili ya ku-control bei ya mafuta na kusaidia kupunguza mfumuko wa bei. Naipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo, lakini kama ambavyo watu wengi wanataka kujua bado tuna hamu ya kufahamu ufanisi wa jambo hili. Mimi ambaye ninatoka katika Kanda ya Ziwa, pamoja na jambo kubwa hili ambalo Serikali imefanya bado hatukuona kimsingi ile impact kubwa ya hii fedha ambayo imewekwa na nadhani kuna haja ya kuwa na transport equalization fund ili kumfanya Mtanzania anayeishi Dar es Salaam, ugumu ya maisha na urahisi wa maisha yake usitofautiane kwa kiwango kikubwa sana na mtu anayeishi Kagera, Kigoma na Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mfano, kwamba pamoja na fedha hizi zote kuingia, lakini kule hazijasaidia sana kupunguza gharama za usafiri, zimebaki pale pale, bado mfuko wa sementi Geita Mjini ni Sh.24,000, lakini utaona Dodoma hapa ni Sh.15,500 kwa hiyo inaona katika nchi moja kuna tofauti ya Sh.9,000, lakini ukiuliza sababu ni gharama za usafiri. Kwa hiyo kuna haja ya kulitazama jambo hili vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri kwa kufuta ada ya kidato cha tano. Hili ni jambo kubwa sana na laiti Serikali ingejua namna ambavyo Wabunge inapofika muda wa kufungua shule tunavyohangaika kuwalipia watu, basi jambo hili limetusaidia sana. Hata hivyo, niombe ombi moja, bado tuna shida kwenye vyuo vikuu, bado tunatoa fedha kwenye vyuo vikuu kwa kutumia zile lettings na vigezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri kwa sababu mkopo wa chuo kikuu ni mkopo, madam nataka mkopo na nimejaza fomu ya kuomba mkopo habari ya kuangalia nani anastahili na mwingine hastahili kukopa hili jambo lingeangaliwa vizuri sana ili iwe ni haki ya Watanzania wote waliopata sifa ya kwenda kusoma wapate mkopo. Sasa hivi hiyo mean testing yao inamwacha mtoto yatima, ninao watoto wawili ambao ni yatima, lakini kwa bahati mbaya walipata wafadhili kusoma na wafadhili waliowafadhili walishakufa, kwa hiyo hawawezi tena kwenda kusoma na wameshindwa kusoma kwa sababu wamekosa mkopo. Nimejaribu sana kwenda kwa Mkurugenzi wa Bodi lakini ilishindikana, kwa hiyo jambo hili liangaliwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nimeliona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri, amezungumzia sehemu ambapo anaomba Bunge limpe ridhaa ya kusamehe baadhi ya kodi, niipongeze sana Serikali hasa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anazunguka huko nje na kutengeneza picha ambayo inavutia wawekezaji kuja Tanzania na hili ni jambo zuri sana. Hata hivyo, ni lazima twende na tahadhari kubwa, tumekuwepo na harmful tax incentives ambazo kimsingi hazijawahi kuisaidia nchi. Ukiangalia huko nyuma kote ambako tulikuwa tunalalamikiwa kwamba Serikali inapoteza trillions of moneys ni kwa sababu ya misamaha mikubwa ya kodi ambayo tulidhani inavutia wawezekaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wanakuja kwa mambo makubwa, yapo machache. La kwanza, wanakuja kwa sababu ya hali ya usalama. Pili, wanakuja kwa sababu ya kutabirika kwa nchi ile (predictability) yaani kama nchi inakuwa na sera zisizotabirika tabirika mwekezaji hawezi kuja. Tatu, anakuja kama infrastructure na energy supply ni kubwa. Nne, anakuja kama kuna masoko na human resource. Sasa unaweza ukaweka incentive ya fedha haijawahi kusaidia kumfanya mwekezaji aje, kwa sababu mwekezaji anakuja kwenye eneo hata ambalo wewe hujampa incentive kama anapata profit anakuja. Kwa hiyo hili ni angalizo ambalo inatakiwa kuliona. Kwa sababu juhudi kubwa hizi zinafanywa na Serikali, lazima pia tuangalie kwenye mianya ambayo tunaweza tukajikuta tunapoteza fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo ambalo sasa hivi linatupatia fedha nyingi za kigeni la madini. Tunafanya vizuri sana kwenye madini, lakini bado tuna shida moja kwenye madini. Niliwahi kusema hapa kwamba, haya madini tunayoona kwa wachimbaji wadogo wanayauza mpaka anapata labda gramu moja ameshakula hasara yenye thamani ya gramu 10. Sasa hapo niombe mambo mawili; moja tuimarishe sana GST na watu wa STAMICO ambao wanafanya mambo ya utafiti, lakini tubadilishe mfumo wa kutoa leseni kwa gharama ile ile. Unakuta mtu amepewa leseni anachukua leseni ya PML, SML, MML anaitunza kwa miaka 20 kwa kulipa fee tu kumiliki leseni. Wenye leseni walazimishwe kufanya utafiti halafu tuweke rates za leseni kulingana na deposit au value ya kitu kilichopo pale chini, ili huyu mtu kama akichelewa kulipa kwa miaka mitano aone gharama ya kutunza ile leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, niende kwenye utalii, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais hasa kwa filamu hii ya kuitangaza Tanzania. Ukweli ni kwamba Watanzania wengi hatufahamu kwamba nchi yetu huko nje ilikuwa haijulikani. Tulipata bahati hapa, Mheshimiwa Spika alitupeleka nje tulikwenda China, tumefika kule mtu ukisema Tanzania lazima a-google kuitafuta ilipo, halafu akitazama pale mtu wa kwanza anayemjua ni Nyerere, basi anasema Oooh! Nyerere’s country basi. Kwa hiyo, kuna watu duniani hawajui kama Tanzania ipo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuitangaza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa juhudi hizi za kutangaza Tanzania na kuvutia watalii zinakuja sambamba na maandalizi tuliyonayo. Jambo kubwa sana amesema hapa Mheshimiwa Sima asubuhi, duniani huko watalaii wanataka kwenda kwenye nchi ambayo usalama ni wa uhakika. Kwa hiyo, jambo la usalama ni la msingi sana. Tetesi zozote zinazoashiria kutokuwepo kwa usalama zinamfanya anayefikiria kuja Tanzania asije na ukiona kama jirani yako au mwenzako yeyote anatangaza sana ubaya wa usalama kwenye nchi yako, maana yake hiyo tayari ni vita ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa ni lazima tuangalie vizuri. Naiomba Serikali jambo hili isilichukulie poa, kwenye biashara ya utalii hakuna mtu atakwenda kwenye nchi ambayo ana taarifa za kwamba wananchi wanapigana na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili ni ukarimu. Tanzania lazima tujue kwamba ili tuweze kuwapokea watalii wengi lazima tufanye maandalizi. Maandalizi haya ni pamoja na kulinda maeneo yetu ya asili, na pili kuandaa sehemu za kuwapokea. Sasa ipo shida kidogo ambayo niliiona juzi hapa na ninaomba niseme vizuri, inaweza kuwa ni misconception au ni misleading ambayo imetokea kwa wananchi wa Loliondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotakiwa kufanyika kwenye eneo lile siyo kuigeuza Loliondo nzima ile ya square kilometa 4,000 kuwa game reserve. Ni kiini cha Lake Natron na sehemu ndogo ya square kilometa 1,500 kwa sababu kubwa mbili. Moja, lile ziwa kuna ndege ambao wanakuja kuzalia pale na wanakwenda Ulaya, lakini limeendelea kupata seriation kutokana na uingiliaji wa watu. Kwa hiyo, lazima tulinde nusu ya lile eneo. Naipongeza sana Serikali kwa juhudi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wanyama wote unaowaona, wana maeneo maalum ambapo huwa wanakwenda kufanya mazalia na maeneo ya mtawanyiko. Kwa hiyo, kale kaeneo lazima ukalinde. Sasa inawezekana kuna taarifa zisizo sahihi ambazo zinasambaa za kufikiri eneo lote lile zima wananyang’anywa wananchi na kupewa wawekezaji, jambo ambalo naamini siyo sahihi. Kwa sababu maandalizi ya andiko hilo yalifanywa na wizara na yakapelekwa kwa viongozi na yakafanyiwa kazi vizuri. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, elimu ya kutosha ipelekwe eneo hili, watu wasipewe picha ambayo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, ambalo nataka kuzungumza ni eneo la uvuvi. Miaka ya nyuma tulikuwa na TAFICO na nimeona hapa Mheshimiwa Waziri umeweka TAFICO unataka kuwapa fedha. Mimi nilipata bahati ya kusoma uvuvi na nilipata bahati ya kufanya field TAFICO, sielewi mnakwenda kufanyaje TAFICO ili ije kutusaidia kutoka kwenye mchango wa kiuchumi. Maana yake sasa hivi uvuvi unachangia chini ya 3% kwenye GDP.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu sana. Miaka ya nyuma, mwanzoni mwa mwaka 2000 uvuvi ilikuwa ni kwenye export; kwenye forex ilikuwa ni zao la pili Tanzania kwa kuingiza fedha za kigeni. Tumekuja tukavuruga wenyewe. Nimeona hapa umetoa exemption ya nyavu, hakuna kodi, lakini tulivuruga wenyewe. Wawekezaji wenye viwanda ndiyo walikuwa wanaleta nyavu. Wakileta nyavu, wanawauzia wavuvi. Sasa zote zikakamatwa, zikachomwa moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tutengeneze sera ambazo siyo kila atakayekuja kwenye Wizara hii atabadilisha ili wavuvi waweze kuvua vizuri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kanyasu. Ni kengele ya pili, ahsante sana.

MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri lakini na Serikali kwa ujumla, kwa kuchukua sehemu kubwa sana ya maoni ambayo tulitoa, lakini na kufanyia kazi malalamiko ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nilitaka niweke maelezo machache kwa alichosema Mheshimiwa Mathayo, wengi tunasema pikipiki inabeba mtu mmoja, lakini ukweli ni kwamba pikipiki ninazokutana nazo mimi barabarani zinabeba watu wanne mpaka watano. Sasa inawezekana kishawishi hiki cha kupunguza faini kisiposimamiwa vizuri tutatengeneza wodi 10 za majeruhi kule Bugando na kule Muhimbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kushuhudia pikipiki imeua watu watano. Iliingia kwenye trekta ikaua dereva wa pikipiki na abiria wake wanne. Sasa hapa tunazungumzia mtu mmoja, lakini nadhani kuna haja ya kusimamia vizuri sheria hapa ili kuwafanya madereva wa pikipiki kufaidika na punguzo la faini lakini kuheshimu sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, alitusikia kwenye uvuvi, lakini maelezo yake kwenye hotuba yake naona kama hayakueleweka vizuri. Amesema na ninaomba nimnukuu, alikuwa amezungumzia kutoza kodi ya zuio kwa kiwango cha 2% kwenye malipo yanayohusisha mauzo ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanapouzwa kwenye makampuni ya mashirika yanayojihusisha na usindikaji wa mauzo ya mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pendekezo hili halitahusisha wakulima akawaacha tena wavuvi hapa, hawapo kabisa; pendekezo hili halitawahusisha wakulima wadogo na wale wanaouza mazao yao kwenye Masoko ya Msingi, AMCOS na Vyama vya Ushirika. Yaani hapa hakuzungumza mvuvi kabisa, amemsahau. Huku juu amezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madhara yake ni kwamba mvuvi anapopeleka samaki kiwandani; ukiona samaki ziko kiwandani, pale katikati unaweza ukafikiri kuna mfanyabiashara au kuna Chama cha Ushirika. Hakuna Chama cha Ushirika cha Wavuvi, hakipo. Wavuvi wanaokusanya tani tano ni wavuvi wanaokwenda ziwani na kuleta kilo kumi kumi. Baadaye wanazikusanya na kuzipeleka kiwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maelezo yako hapa yasipokuwa wazi vizuri, yatamfanya huyo aliyepeleka kiwandani kutafsiriwa kama middlemen au kutafsiriwa kama mfanyabiashara mkubwa na kukatwa 2%. Mheshimiwa Waziri naomba uliweke vizuri kama ulivyokusudia huku juu ili liwataje wavuvi hawa tunaowazungumzia kwa sababu ni wale wale tunaowalenga ambao wanakusudiwa kuondoa tozo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea kwenye suala la cold rooms kwa maua. Nirudie kusema, kwamba Dodoma na miji mingine mingi tunakula samaki waliooza. Kwa sababu samaki unayemtoa kwa mvuvi mwenzangu hapa Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya kuwaleta Dodoma wakiwa kwenye lorry ambalo haliko refrigerated, wanafika wameoza. Samaki unaowatoa Mwanza wakiwa chilled kwenye barafu, halafu baadaye wanapelekwa kugandishwa, hawagandi kwanza, hawafikii freezing point ambayo ni recommended, wanakuja hivyo hapa na wengi wanafika wameoza. Maana yake ni nini? Hatuna refrigerated container wala refrigerated trucks ambazo zingeweza kusaidia kum-maintain quality ya samaki na kupunguza cost harvest loss. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakubaliana na hoja hii kwenye maua lakini naomba kumsisitiza Mheshimiwa Waziri atuombee msamaha kwenye refrigerated container ili tuweze kusaidia kwenye nyama na samaki. Hivi leo tunavyozungumza, ukikutana na nyama inasafirishwa kutoka machinjioni kwenda kwenye butcher utafikiri wanapelekewa labda mbwa; kwa sababu ni magari ambayo hayana quality na wala hayakuandaliwa vizuri. Ni kwa sababu ya sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sheria ya VAT 148 Sehemu ya Tisa Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu viwanja; misamaha ya nyasi. Amezungumza tu kuhusu Majiji na Mapispaa; mwanzo alikuwa kwenye Majiji sasa kaongeza Manispaa. Katika nchi hii tuna mikoa minne ambayo bado ni Halmashauri za Miji. Mkoa wa Geita ni Halmashauri ya Mji; Mkoa wa Katavi ni Mji, Mkoa wa Njombe sijui na wapi; hii ni mikoa ambayo umeiondoa kwenye misamaha yako, umepeleka kwenye Manispaa na kwenye Majiji. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwenye Mikoa hii Makao Makuu ya Mikoa uongeze kwenye msamaha wako wa kodi wa Nyasi Bandia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambao nataka kusema hapa, tulisema tunataka kuongeza uwezo wa Halmashauri kukopa. Zipo Halmashauri 34 tu ambazo zimefaidika na mikopo ya fedha kutoka Serikalini. Hizi Halmashauri 34, nyingine zimekopa mara nne, mara tano na mostly ni Dodoma na Dar es Salaam. Halmashauri zote Tanzania hazijafikia uwezo wa kujitegemea. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, masharti yaliyokuwa yamewekwa ni kama yalikuwa yanapunguza uwezo wa wakopaji badala ya kusaidia wakopaji kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri zote zilizoandika andiko zimeonekana maandiko yake hayana sifa kwa sababu walioandika hawana sifa, lakini waliotoa maelekezo ya kuandika ni Serikali na walioandika ni Serikali. Sasa mimi nimekuwa nikipata taabu, ambao hawana sifa ni waliotoa mafunzo ya uandikaji wa andiko au ni walioenda kuandika na kusahihisha andiko kwenda kwenye kukopeshwa? Kwa sababu fedha zipo kwa mujibu wa Serikali, lakini wakopaji hakuna na Halmashauri ni masikini. Kwa miaka mitano zimekopeshwa Halmashauri chini ya 30; na waliokopeshwa wanalazimishwa kubuni miradi ambayo Halmashauri hazina vipaumbele. Kwa mfano, usishangae kuona Halmashauri zote zinakopa kujenga stendi na masoko, ndiyo miradi ambayo inalipa kwenye Halmashauri husika. Ninyi mkija huku mnasema hapana, this is copy and paste. Ni copy and paste kwa sababu kule kwangu Geita stendi ndiyo mradi ambao unalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, aidha Kamati hii ambayo inasimamia na kuchambua ipeleke mafunzo sahihi kwa wakopaji au irekebishe masharti ya kukopa isionekane kama masharti yametengenezwa kupunguza wakopaji. Kwa sababu unaweza kutengeneza masharti ya kupunguza wakopaji na utashindwa kuisaidia Serikali kuongeza mapato. Jambo hili ni muhimu sana kwa sababu tunazungumzia Halmashauri ambazo nyingi hapa sasa umebeba mzigo wa kuzisaidia, lakini kuna mafungu ya fedha Serikali imeandaa kwa ajili ya kusaidia Halmashari kuweza kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuongeza fedha za mikopo hasa ya Elimu ya Juu. Zitaongezwa pale shilingi bilioni 70, lakini kilio ambacho tumekuwa nacho ni formula ile ya utoaji wa mikopo. Ile means test bado haiwezi kuwa very transparent. Mimi nina watoto hapa zaidi ya watatu ambao ni wapiga kura wangu; ni yatima na wemekosa mikopo. Yaani unamwona mtoto mpaka shule ameacha, chuo ameacha, lakini ana sifa za kukopeshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeongeza shilingi bilioni 70, ninataka kutoa ushauri; wachambuzi wale wanaokopesha wanasema wale wanaojaza fomu za maadili hawakopeshwi. Unajua wanaojaza Fomu za Maadili ni pamoja na Madiwani. Diwani analipwa shilingi 350,000/=, angekusanya posho zake zote, hazifiki shilingi 600,000/=, lakini ni sehemu watu ambaye mtoto wake akiandika kuomba kukopeshwa, siyo sehemu ya wanaokopeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa ushauri, kwa kuwa Serikali imeongeza fedha; na fedha hii ni ya mkopo, kila mtoto wa Kitanzania anayeomba kukopa maadam ni mkopo, apewe mkopo. Kama tatizo ni fedha, tuje na kiwango ambacho ni minimal rate. Kwa mfano, unaweza ukasema at minimal tutakupa 30% kwa sababu wewe baba yako ana uwezo wa kulipa; lakini as long nami mzazi nimesema mkopeshe huyu mtoto, ni kwa sababu nimeangalia may be nina watoto wengi wanaosoma, uwezo wa kuwasomesha sina na Serikali inakopesha na mtoto atalipa, aweze kukopeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, as it is now, as long as wewe ni Mbunge, haijulikani una watu wangapi unasomesha, watoto wako hawakopesheki; wewe ni Diwani, watoto wako hawakopesheki; wewe ni Mkuu wa Idara, watoto wako hawakopesheki. Mheshimiwa haka bado kanatengeneza ka aina fulani ka ubaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuondoa SDL kwenye hospitali, kwa watumishi wa Hospitali ambao kimsingi wanafanya kazi ya Serikali.

Sasa tuendelee taratibu, hata shule binafsi zinazofundisha watoto wetu zinafanya kazi ya Serikali. Watoto 20,000 walioko kwenye shule binafsi wakiondoka wakaenda kwenye shule za Serikali mtatengeneza madawati, mtajenga madarasa, mtaongeza walimu, mtanunua chaki, mtaongeza kila kitu kule ndani. Sasa kama umeweza kufanya huku, tulitazame hilo ili tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia na kwa niaba ya wapiga kura wangu wa Geita Mjini, naomba nitumie nafasi hii pia kuwataarifu kwamba lile tatizo lao la watu wa TFS kuweka alama kwenye nyumba ambazo zipo katikati ya Mji wa Geita wakidai ni hifadhi, nilishamjulisha Waziri wa Maliasili na kwamba tunachosubiri ni maombi ya RCC ili waweze kufikia maamuzi ya kuliachia eneo hilo. Maamuzi hayo yanachelewa sana na wananchi wanaendelea kusumbuliwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Geita wanaomba kuona unachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mbunge, Mheshimiwa Doto Biteko, nimesomeshwa na pamba, lakini pia nimesomeshwa na uvuvi. Nimesomeshwa na uvuvi, natoka kilometa mbili kutoka Ziwani ndiko nilipozaliwa; na eneo letu tulilokuwa sisi tulikuwa na mashamba makubwa sana ya Nyanza wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na pongezi nyingi sana ambazo nampatia Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwenye Wizara hii, hasa kwa kuondoa kero nyingi kwenye zao la pamba. Pia ninaomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba Nyanza Cooperative Union, mali zake ambazo zilihujumiwa kinyemela, zinarudi na hatimaye Nyanza iweze kusimama imara. (Mkofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mkataba inaoneka sasa hivi ni suala geni lakini sisi wakati tunakua wakati ule, pamba ndiyo lilikuwa zao la kujivunia kwenye Kanda ya Ziwa na umaskini wa wananchi wa Mkoa wa Geita na Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaonekana kudorora kwa zao la pamba. Wakati huo mashamba yote ya pamba makubwa na mazuri uliyokuwa unayaona, wananchi walikuwa wanalima yalikuwa aidha ni ya Nyanza au ni ya watu walikuwa wanakopa pembejeo. Mfumo wa kukopa pembejeo ulikuwepo tangu zamani wala siyo mgeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi walikuwa wanapewa mbegu bora, walikuwa wanapewa madawa na baadaye vyama vya ushirika kwa sababu vilikuwa vina nguvu, vilikuwa vinaweza kununua yale mazao kwa wakati na kuwalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri kuona namna ya kuimarisha vyama vya ushirika kwa sababu ndiyo reliable vinaweza kuwakopesha wakulima. Kama hilo haliwezekani, ni kuona namna ya kuwafanya hawa private buyers ambao mnawapa usajili waweze kuwa engaged namna ya kuwasaidia wakulima. Bila kutatua tatizo la kuwapatia pembejeo na mbegu bora wakulima, hatuwezi kulifanya zao la pamba likarudi kwenye nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna ambayo naiona hapa, kwanza wakulima sasa hivi wamekata tamaa kwa sababu ukiacha wastani wa heka moja kuzalisha tani mbili na kilo 200 wengi wanazalisha kilo 100 au kilo 200. Sasa kilo 200 hata kama ungempa kilo moja Sh.2,000/= bado hawezi kulipa gharama za kilimo, productivity imeshuka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mkulima kama ataweza kuzalisha tani moja kwenye heka, hata ukimpa kilo Sh.1,000/= utakuwa umemsaidia. Tatizo kubwa liko wapi? Tunao Maafisa Ugani wengi sana kwenye Halmashauri za Wilaya, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri hawa watu hawapewi target. Ameajiriwa, amepewa ofisi, amepewa Kata, hakuna mtu anayemsimamia. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu aweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba hawa watu wanakaguliwa, wanapimwa kwa kitu fulani ambacho wamekifanya kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wanaamka asubuhi, anakwenda anasaini, anarudi, analala, hata katika kijiji ambacho anakaa wakulima hawafahamu. Hata katika kijiji ambacho wanakaa hajawahi kutoa utaalam wa aina yoyote. Kwa hiyo, matokeo yake wakulima wameligeuza zao la pamba kuwa zao la pili na wengi wamehama. Wengi wanakwenda kwenye mazao mengine kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Geita watu wengi wanalima mpunga; na mpunga kwa sababu pia hata utaalam wa watu wengi wanalima kutokana na ulimaji wa asili, wamehamia huko kwa sababu ni zao la chakula na zao la biashara. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri Maafisa Kilimo, hata angeajiri wengi namna gani, kama waliopo hawasimamiwi, bado zao la pamba litaendelea kuwa chini kwa sababu hakuna uzalishaji ambao unaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba nilisomeshwa na samaki. Naomba hapa Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. Ipo sheria ambayo ilitungwa mwaka 2003 na kanuni yake ya mwaka 2009. Sheria ambayo inasema “it is illegal to manufacture, possess, store, sell and use or cause another person to use for a fishing gear of more than 26 mesh deep in the Lake Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha ya kawaida wanasema ni makosa kuzalisha au kukutwa una nyavu ambayo ina macho 26. Sasa macho 26 nikifanya mikono yangu miwili hapa, tayari ni macho 26 ya mtego.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatoka kisiwani, tumevua wote samaki. Naomba nimkumbushe, ukitoka Mwanza South pale ukaenda Nautical Mile 15, chini ni mita 70, hebu aende na hiyo nyavu ya macho 26 akavue samaki kama atapata kilo tano. Kinachofanyika sasa, imetungwa sheria, hiyo sheria imeipitishwa lakini inahamasisha watu waende kuvua samaki kwenye breeding areas. Wanakwenda kwenye zile breeding areas ambazo tungetarajia ziwe hifadhi, samaki wazaliane kwa sababu nyavu wanayopendekeza ambayo wanaiita illegal, ni nyavu fupi. Ni mikono yangu miwili hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Gozba ni mita 100 chini. Nataka nimpe challenge Mheshimiwa Waziri, nimefanya kazi ya samaki miaka 25. Kama ana wataalam wake wa uvuvi awaambie waweke nyavu 100 twende Gozba, wakirudi na kilo kumi naacha Ubunge. Naacha Ubunge kwa sababu wanachokifanya ni kuwaonea kabisa wavuvi. Wanaenda wanachukua zile nyavu, wanaita illegal wanazichoma moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mvuvi gani anatengeneza nyavu? Nyavu zimepita bandarini, zimelipiwa ushuru, mvuvi amekopa pesa benki, amekwenda kuweka kwenye mtumbwi, size ya nyavu anayotaka ni ile ile nchi tano au sita ambazo wameruhusu; lakini wanasema ikishazidi macho 26 ni illegal. Sasa wakati inapita bandarini watu wake walikuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu. Yeye kama ni mvuvi na anafahamu mambo ya uvuvi twende ziwani. Wavuvi wetu wengi ni local, wanafanya traditional fishing, hakuna mwenye fish finder; hakuna mwenye chochote. Kwa hiyo, hakuna anayeona samaki chini. Tuchukue hizo nyavu tuende nautical mile 50 tukatege, halafu turudi kesho tukavue; tukipata samaki kilo 50, mimi naacha Ubunge. Kwa sababu nimefanya kazi hii kwa miaka 20 na nimekimbia huko kwa sababu ya masharti mengi yasiyo na maana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachomaliza samaki Ziwa Victoria ni matumizi ya monofilament na matumizi ya makokoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri yafuatayo; Serikali iongeze bajeti kwenye fungu la maendeleo na pesa hii ipo kwenye mafuta, umeme na maji yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya umwagiliaji inakumbana na pingamizi kwa kuwa ujenzi wa miundombinu umejielekeza kujenga mabwawa kukinga maji. Hapa wananchi wanaogopa kupoteza ardhi zao, kwa nini tusitumie mfumo wa visima virefu na wind wheels kuweka maji kwenye matanki na kusambaza kwa gravity kwa kuwa gharama ni nafuu na eneo linalopotea ni dogo. Mradi kama huu upo kata ya Kanyalla Ibada na umepingwa na wananchi kwa sababu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tatizo la maji Mjini Geita, hivi sasa Mradi wa Maji wa LV-Watsan unasuasua sana mpaka leo miezi minne imepita, mkandarasi ameshindwa kumaliza kazi, nashauri mtu huyu afutwe kwenye orodha ya wakandarasi kwa kuwa hana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhaba wa maji katika Mji wa Kasamwe, naishauri Serikali kuunganisha mradi mpya wa maji wa fedha za India kwa Mji wa Geita ili maji yake yafike Kasamwa, kwa sababu kwa mujibu wa wataalamu hivi sasa kuna tanki kubwa la maji Buhalanda ambalo lipo kilometa 10 tu kutoka Kasamwa na ambapo maji yatafika kwa gravity na kwa kuanzia ziwekwe DP’s tu kwenye mitaa ili wananchi wapate maji, badala ya sasa kutumia bwawa ambalo gharama yake ni kubwa

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kunipa majibu maji katika Kata za Shiloleli, Bulela, Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Bung’wangoko yatafika kupitia mradi huu wa fedha za India? Kwa sababu hizi kata ni sehemu ya kata za Mji wa Geita Jimbo la Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ujasiri mkubwa na hasa kwa sababu mimi na Mheshimiwa Rais mwenyewe tunatoka kwenye mkoa ambao hawa wachimbaji wa dhahabu kwa kweli wanatuachia mashimo matupu na watu wanaendelea kuwa maskini. Kwa hiyo, hizi jitihada za Mheshimiwa Rais tunaziunga mkono, tunampongeza sana na wananchi wa Mkoa wa Geita kimsingi ambao wameshuhudia miaka 19 dhahabu inachimbwa lakini Makao Makuu ya Mji wa Geita hakuna barabara, Makao Makuu ya Mji wa Geita hakuna maji, hospitalini hakuna wodi, shule watoto wanakaa chini kilometa moja kutoka kwenye mgodi pale watu ni maskini sana; wanaona juhudi hizi za Mheshimiwa Rais zinatakiwa kuungwa mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nawashangaa sana wenzangu hawa ambao wanapinga kwa sababu kama walivyosema wenzangu huko nyuma, walikuwa kila siku wanalalamika wanasema kwamba nchi hii inaibiwa lakini nataka kusema kwamba Mheshimiwa Rais aendelee na ikiwezekana na aangalie pia katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mnyika katika ukurasa wake wa saba amezungumzia kwamba Serikali iliingia mkataba wa loyalty wa four percent. Hii ni four percent siyo ya force declaration. Unapofanya force declaration, four percent yeyote haina maana yoyote ile kwa sababu unazungumzia four percent ya value gani? Hawa watu wanafanya four percent ya uongo halafu wanakuja kuwatetea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine la pili; nilikuwa namshangaa sana Mheshimiwa Mnyika kwenye ukurasa wake wa tisa anasema kwamba taswira ya Tanzania kwenye jarida moja huko la Mining journal inasema trouble in Tanzania kwa sababu Rais ameanza kufuatilia wizi, so what? Trouble, yes kuna wizi unagundulika, unataka Rais asigundue wizi? Lazima Mheshimiwa Rais afuatilie kwa sababu unaposema trouble in Tanzania, kama kuna wizi umegundulika lazima Rais afuatilie sasa mimi nakushangaa unapo…

KUHUSU UTARATIBU .....

MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ulichosema ni sahihi na namshangaa sana ndugu yangu hapa mimi nazungumzia issue katika general yake yeye anajaribu kwenda katika eneo dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu ya muda, kuna mzungumzaji pia mmoja amezungumzia kwamba uzalishaji wa umeme umepungua, nilitaka aende kwenye ukurasa wa 21 ataona mahitaji ya umeme ndiyo yaliyoongezeka kutoka megawats 1,026 kwenda megawats 1,051, lakini uzalishaji wetu ni megawats 1,450.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuishukuru sana Wizara hii. Geita tulikuwa tuna matatizo makubwa sana ya umeme, unakatika kila siku; hivi ninavyozungumza sasa hivi umeme wa Geita haukatiki, umeme wa Geita uko imara na ninachowaomba tu sasa hivi ni kuhakikisha sasa umeme huu kama ahadi ambavyo ilikuwa kwamba vijiji ambavyo vilikuwa havijapata umeme wa REA vinapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kusema hapa ni kwamba pamoja na umeme wa Geita kutokatika, lipo tatizo ambalo nilimwambia Mheshmiwa Naibu Waziri kwamba TANESCO hawana vifaa. Kwa hiyo watu wanapoomba umeme wanachukua muda mrefu sana kupata connection ya umeme; hivyo nadhani pamoja na juhudi za REA TANESCO wakae upya wafikirie namna ambavyo wanaweza kuongeza mtaji. Kama TANESCO wameshindwa kuwa na vifaa vya kutosha kwenye store, ni vizuri wakaruhusu vendors wengine wakawa na vitu hivi kwenye maduka na wao wa-control quality kuliko ilivyo sasa, mteja ameomba umeme leo anafungiwa mwezi wa 10 kwa sababu wewe huna meter, kwa sababu wewe huna waya wakati soko hili ni soko huria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ushauri wangu. Nakushukuru sana kunipa nafasi.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kupata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya mwaka 2017/ 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wazungumzaji wengine waliotangulia wamesema, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao tunatoka kwenye maeneo ambayo uchimbaji wa dhahabu ni kazi kubwa kabisa ya maisha ya kwetu ya kila siku. Kwa hiyo, juhudi za Mheshimiwa Rais za kupambana na namna ambavyo madini haya yatakuwa na manufaa kwa wananchi sisi wananchi wa Jimbo la Geita Mjini na Mkoa mzima wa Geita tunazipa kipaumbele kikubwa na tunaziunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Wizara ya Fedha namna ambavyo inapoteza fedha nyingi kutokana na mikataba mibovu ambayo ilikuwepo. Nilipata nafasi ya kuchangia mwaka jana na sikuona mabadiliko yoyote yale wala hatua zilizochukuliwa. Kampuni nyingi zinazofanya kazi na migodi mikubwa ni kampuni za nje na migodi hii mikubwa imepewa uwezo inapotaka vipuli au bidhaa zozote inaweza kumpa yeyote aliyeko ndani au nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kampuni hizi zinazopewa kazi nyingi hazina ofisi Tanzania. Wanapokuletea orodha ya kampuni ili uweze kwenda kudai service levy wanakupa orodha ya kampuni ambayo ipo Canada, Australia, South Africa ambao hawana ofisi hapa, hawana license hapa wala hawana wafanyakazi. Lakini gharama ya manunuzi yao yameingizwa kwenye corporate tax, kwa hiyo, yanapunguza sehemu ya faida ambayo Serikali ingeweza kulipwa na ndiyo maana migodi mingi haiwezi kulipa kodi kwa sababu wanaweza ku-deal na kampuni iliyoko Canada ambayo ninyi Serikali hamna kumbukumbu nayo, haina ofisi, haina address, matokeo yake ni kwamba sisi tunapoteza pesa nyingi kwa sababu hatuwezi kwenda kudai service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, niliseme hili mwaka jana na miongoni mwa makampuni haya ni makampuni ya bima. Kampuni hizi za bima zime-insure wanafanyakazi lakini wana- insure strong room, processing, mgodi mzima. Kampuni hizi kubwa za bima unapoomba ile orodha ya makampuni ya service levy hawakuletei kwa sababu hazipo Tanzania. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri, hii ni sehemu kubwa ambayo tunapoteza pesa nyingi sana. Kama kampuni hii itakuwa ipo Dar es Salaam au ipo Mwanza watakuwa na ofisi, watalipa working permit, watalipia wafanyakazi wao na matokeo yake Serikali itapata fedha na itapata kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Halmashauri tunataka tupate hii service levy kama Serikali wanaona hii pesa ni ndogo hawana sababu ya kuyafanya makampuni yaje Tanzania, wayaache yakae nje. Sisi tunaomba watusaidie wawalazimishe sheria watu hawa wafungue ofisi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, mwaka jana nilishauri hapa nikasema tatizo kubwa tunakwenda kwenye viwanda lakini ili viwanda viweze kufanya kazi lazima kilimo kwanza kipewe kipaumbele. Watu wengi wamezungumza kuhusu kilimo. Tatizo ninaloliona kwenye kilimo tangu tumeanza kuzungumza unaona transformation inayotupeleka kwenye kilimo ambacho kitalipa inakwenda kwa kasi ndogo sana. Mtu anayehamasisha viwanda ana kasi kubwa. Viwanda vinahamasishwa kwa kasi kubwa, raw material ni products za kilimo, lakini transformation ya kufanya kilimo kiweze kusaidia viwanda inakwenda kwa kasi ndogo ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano, sisi Geita tunalima mananasi, mbegu ya nanasi ambayo ingeweza ku- supply au kuuzwa nje kwa sababu tunaambiwa mananasi tuliyonayo yanafanana sana na madawa ya kienyeji wala huwezi kuuza nje. Ili tuweze kupata product ya nanasi ambayo inaweza kuuzwa nje nilidhani kwa sababu nchi inajua tunalima nanasi, tayari wangekuwa wamepeleka wataalam wakatupa mbegu za kisasa zile mbegu ambazo tunaweza tukauza yale mananasi nje, tukawa na soko ambalo lingeweza kuwabadilisha wakulima wa mananasi katika Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tumeanza kuzungumza kuhusu kilimo, wakulima wa mpunga wanalima kienyeji vilevile walivyolima miaka kumi iliyopita. Tunafikiria kuongeza ukubwa wa mashamba, sio ukubwa wa uzalishaji. Kwahiyo, matokeo yake, mbegu za mpunga zile zile ambazo tulilima miaka kumi iliyopita ndizo tunazozungumzia kuendelea kulima kwenye mfumo wa viwanda. Kwa hiyo, haiwezekani viwanda tunavyovizungumza vikaja viwaka productive kama hatuwezi kufikiria kubadilisha kabisa namna ambavyo tunalima. Ukienda kwa wakulima wetu wengine wanalima ukubwa wa shamba. Anaweza kulima ekari kumi akapata gunia tano za mahindi, lakini kumbe angeweza kulima heka mbili akapata gunia 60 za mahindi na eneo lingine akalima kitu kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mabadiliko tunayotaka kwenye kilimo lazima yaendane na speed ya ujenzi wa viwanda tunavyovifikiria vinginevyo tunakwenda mahali tutajenga viwanda, halafu tutaagiza raw material kutoka nje. Alisimama hapa Waziri wa Kilimo akasema hata Bakhresa maziwa anayopaki kwenye pakiti mengine ni ya unga kwa sababu maziwa hakuna. Lakini leo utaona vita ya Serikali na mifugo, vita ya Serikali ya wafugaji ni kuhakikisha wale wafugaji wanafilisika badala ya kuwasaidia wale wafugaji waweze kutengeneza uzalishaji mkubwa wa maziwa ili Bakhresa apate maziwa. Bila kufanya hivyo, hata viwanda tunavyovihamasisha vije vitakuja vifungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili nilitaka kuona mchango wa Idara ya Uvuvi kwenye uchumi wa Tanzania. Ziwa Victoria miaka kama 15 ya nyuma tulikuwa tunapata pesa nyingi sana za kigeni kutokana na uvuvi, taratibu taratibu productivity imeendelea kushuka sasa tunabuni mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwalinda wale samaki. Lakini tatizo kubwa lililoko Ziwa Victoria, lile ni ziwa, uvuvi ni mkubwa hakuna juhudi za ziada za Serikali za kuhakikisha kwamba tunapandikiza vifaranga vya kutosha kwenye Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano, kuna maeneo mengi sana yemetengwa kwa ajili ya samaki kuzaliana na yale maeneo yaliyotengwa, Serikali ingeweza kuwa na mkakati kabambe wa kuingiza vifaranga hata milioni 100 kila mwaka vifaranga wa sangara unawaweka katika Ziwa Victoria, wakisaidiana na wale ambao wanazaliana kwa mfumo wa kawaida, samaki hawawezi kuisha katika Ziwa Victoria. Tatizo letu tunavuna tu, tunavuna tu matokeo yake badala ya kugundua kwa nini samaki wanapungua tunaweka masharti ya kuwaambia wavuvi wapunguze size ya nyavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hapa wakati nachangia kwenye Wizara ile na bahati nzuri Waziri hakutaka kulijibu. Amefanya operesheni ya kukamata wavuvi wanaovua samaki kwa nyavu ambazo zina macho zaidi ya 26 lakini hiyo nyavu ambayo inatumika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuzungumzia uwanja wa ndege wa Chato. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini na ninashangaa sana watu wanaoona uwanja wa ndege unaojengwa Geita/ unaojengwa Chato kwamba ni matumizi mabaya ya fedha. Watu wana-define uwanja mkubwa kwa urefu wa runway, lakini nadhani wanapungukiwa exposure. Uwanja mkubwa ni facilities na uwanja ule ili uwe mkubwa ungekuta linajengwa jengo la abiria kubwa, kwa hivyo ndipo ungesema uwanja mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe tu, wamesema uwanja wa ndege uko pale strategically, wanasahau kwamba kutoka Chato kwenda Rubondo ni kilometa 30 na tunahamasisha utalii. Pia wanasahau kutoka Chato kwenda Biharamulo ambapo kuna mbuga za wanyama za Buligi pamoja na Biharamulo pale ni kilometa
50. Wanasahau kwamba tuko karibu kilometa 100 kwenda mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaposema ni strategic airport watu wengi hawaelewi tunazungumza nini, wanawaza tu kwamba ni uwanja wa Rais kwenda nyumbani. Mimi nasema ule uwanja umejengwa sehemu sahihi na uwanja ule sisi tunauhitaji ungejengwa katika eneo lolote lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo jingine ambalo watu ni lazima walifahamu Rais alikuwa akitua Mwanza kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza kwenda Chato anatembea kilometa 270 anakwenda kupumzika. Akitua Bukoba anatembea kilometa 250 kwenda kupumzika. Sasa amejenga uwanja karibu anapokwenda kupumzika wanapiga kelele. Mimi nataka niwashauri, issue ya ukubwa si urefu wa uwanja, nenda kasome, issue ya ukubwa ni facilities za uwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya TRA, jengo la TRA watu wanafikiri kurudi nyuma unakwenda mbele unaenda wapi? Badala ya kusema tunajenga jengo likae miaka 50 mbele wewe unawaza kujenga slope.

Mimi nasema hata ofisi za Serikali tuache sasa, tuanze kujenga majengo ya ghorofa. Habari ya taa ni habari ya Halmashauri yenyewe hata kama wangepita punda tunaangalia usalama wa raia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la madini. Serikali ilipoanza kusimamia vizuri madini sisi watu wa Geita Mjini tumeona manufaa yake na nataka nitoe takwimu hapa. Kabla ya Serikali kuweka mikono yake kwenye madini, mapato ya Halmashauri yangu Januari-Machi ilikuwa shilingi milioni 514; Aprili-Juni shilingi milioni 750; yakaongezeka kidogo hapo. Ilipofika Julai-Septemba tumepata bilioni moja kasoro, maana yake ni nini? Kulikuwa kuna wizi mkubwa sana unafanyika hapa kwenye madini. Wito wangu hapa kwa Mheshimiwa Waziri ninashauri ufanyike uchunguzi kurudi nyuma kuona kwa nini baada ya Serikali kutuma wawakilishi kwenye hizi kampuni za madini mapato ya Halmashauri yangu yameongezeka kutoka shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni moja wakati kazi ni ile ile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, tulipitisha Sheria hapa ya Local Content, bado watu wa mgodi wanapiga. Bado wana walinzi kutoka nje, bado wana kampuni nyingi kutoka nje ambazo zinaweza kufanya kazi na Watanzania. Wakati wa Mpango wa mwaka uliopita nilishauri hapa kwamba tuna kampuni nyingi sana ambazo zinafanya kazi kwa remote, kampuni iko South Africa, iko Australia, inafanya services katika Mgodi wa Geita, hawalipi kodi! Bado halijafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kuwaomba hawa watu watulipe service levy wanakwambia hii kampuni haipo Tanzania. Naomba kushauri, sheria hii tuliyoipitisha hapa Bungeni, yaelekezwe haya makampuni ya madini yaweze kuisimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu tunajenga reli kuja Dodoma, mimi nasema fine, tunakopa, tunafanya nini, mimi nasema fine, lakini wasiwasi wangu ni mmoja tu, hii reli itakapofika Dodoma kabla haijafika Mwanza itakuwa haina msaada mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania. Nataka kushauri, badala ya kufanya vipande vipande kwa muda mrefu ufanyike uamuzi wa mara moja wa kuwekeza reli hii moja kwa moja kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ili itakapokamilika manufaa yake yaanze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi mimi na Waheshimiwa Wabunge wenzangu tulipata bahati ya kwenda China na tukaenda katika jimbo moja la Guangdong. Tulipotembelea pale, Meya wa mji ule anatuambia jimbo lile limejengwa na private sector, anasema Serikali haijajenga miundombinu katika jimbo lile. Airport, barabara, madaraja wamejenga private sector. Tuache kukopa kujenga miundombinu, tukaribishe… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampeni ya kuchoma kambi, kuvunjwa mitumbwi na kuchoma nyasi, haiwezi kuandoa uvuvi haramu kwa sababu mwisho wa siku itatengeneza maskini wengi ambao maisha yao yote ni uvuvi na watavua kwa sumu au njia mbaya zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampeni ya kukata nyavu kutoka double triple kuwa single, haijafanyiwa utafiti, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika vina vyake haviko sawa. Ukiwafanya wavuvi wote kutega single watavua kwenye mazalia ya samaki na iwapo itakuwa hivyo zoezi lote hili ni kupoteza muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyavu ya single; iwapo itatumika maji marefu ile ya nchi 7", 8", 10" inaweza kukamata samaki wa robo kilo, kilo moja mpaka kilo 100. Utaratibu wa kupiga watu faini ovyo ni sawa na kuwaagiza wavuvi kutupa samaki kwenye maji kwa sababu samaki akinasa hufa pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyavu ya single; haiwezi kuvua maji marefu kwa sababu nyavu ina kina cha mita nne wakati ziwa lina kina cha mita 84.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu faini, zitumike sheria za uvuvi siyo sheria za mazingira kupambana na wavuvi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika. Nashukuru kwa mgao wa magari ya ambulance, mgao wa Madaktari Bingwa na watumishi. Pamoja na pongezi hizi, naomba kutoa ushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu ya cancer - Bugando; zipo taarifa kwamba zaidi ya asilimia 30 ya wagonjwa wa cancer - Ocean Road wanatoka Kanda ya Ziwa. Kutokana na takwimu hizo ni vyema Serikali ikaongeza bajeti ya vifaatiba kwa hospitali hii ili kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaotoka Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam jambo ambalo litapunguza gharama na usumbufu lakini pia litasaidia kupunguza gharama kubwa kwa mgonjwa inayotolewa hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Geita; kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita. Hivi sasa wananchi wa Mji wa Geita wanapata taabu sana kwa kukosa hospitali ya level ya Halmashauri ya Wilaya kwa kuwa hospitali yetu ya Wilaya/Mji ndiyo Hospitali ya Mkoa kwa sasa.

Naiomba Serikali kuhakikisha ujenzi wa Hospitali ya Mkoa ambayo ipo Mjini Geita na inasuasua kutokana na uhaba wa fedha. Naitaka Wizara kutofautisha inapozungumza kuhusu Hospitali ya Mkoa inamaanisha hospitali ipi kati ya Hospitali ya Geita Mjini na Hospitali ya Chato. Ni vizuri kutofautisha ili kutoa uelewa mpana wa wananchi kufahamu ni kipi kipaumbele cha Wizara kati ya hizi hospitali mbili za Mkoa ndani ya Mkoa mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu wa watumishi; kwa muda mrefu Hospitali ya Mkoa wa Geita inaendelea kutokuwa na Madaktari Bingwa, hadi leo kuna Daktari Bingwa mmoja tu ambae ni surgeon, wale ambao Wizara iliwapeleka wote hawajafika. Pia kuna upungufu mkubwa wa manesi, wataalam wa kada za maabara, usingizi na madaktari wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana TFDA kwa kuendelea kusimamia viwango vya chakula kwa Watanzania. TFDA wanatoza ada kwenye kila leseni ya bar, grocery na migahawa ya shilingi 100,000 kwa mwaka. Ada hii ambayo ambayo ni sharti ya mfanyabiashara kupata leseni katika Halmashauri zetu, kwa ujumla hakuna kazi ambayo TFDA wanafanya kwenye bar kwa kuwa vinywaji vyote vinavyouzwa bar au grocery ni vya kununua na havitengenezwi na muuzaji. Hata kama lengo ni mamlaka hii kukusanya fedha ili iweze kujiendesha, busara ingetumika angalau shilingi 20,000 kwa hoteli kubwa zenye bar na shilingi 10,000 kwa grocery au bar za mitaani kwa kuwa ada hizi zinaongeza gharama kwa wananchi bila sababu yoyote.

Naiomba Serikali ifahamu pamoja na ada ya TFDA kuna ada ya leseni, ushuru, TRA, michango ya mwenge, majengo, ukaguzi wa watu wa afya, usafi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fedha za madeni ya watumishi; Jimbo langu kuna watumishi wengi Hospitali ya Mkoa ambao zamani walikuwa DC wana madeni makubwa na ya muda mrefu. Naiomba Wizara kulipa madeni yote kwa kuwa yameleta usumbufu mkubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kutoka Geita (Nyankungu) kwenda Kahama, barabara hii ambayo inapita Nyang’hwale kwenda Kahama ni kiungo kikubwa kwa Mkoa wa Geita na Shinyanga, na hii sasa inatumika sana kwa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika mgodini. Tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami kama ahadi ya Mheshimiwa Rais ilivyokuwa mwaka 2015. Hivi sasa barabara hii ni mbovu sana kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Uwanja wa Ndege Geita Mjini, Mheshimiwa Waziri kumekuwepo maneno mengi kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato. Sisi wananchi wa Geita hatuoni tatizo la ujenzi wa uwanja wa Chato. Tatizo tulilonalo ni umbali wa huduma hiyo kutoka Geita Mjini kwenda Chato, ndio utakuwa uwanja wa watu wa Geita Mjini; maana yake mtu atatakwa kusafiri kilometa 184 kutoka Geita kwenda Chato au kusafiri kilometa 120 kutoka Geita kwenda Mwanza Mjini na kwa sababu hiyo tatizo na uhitaji wa Uwanja wa Ndege Geita Mjini lipo pale pale. Ushauri wangu ni kwamba uwanja wa CCM uliopo hivi sasa ukarabatiwe na kuwa na uwezo wa kutumika kwa shughuli zote abiria wa Geita na CCM na kinachoweza kufanyika ni kutofautisha jengo la abiria peke yake hakuna sababu ya kuanza ujenzi wa eneo jipya.

Kuhusu barabara za Mjini Geita, Mheshimiwa Waziri tulipewa ahadi ya kilometa 10, ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni yake mwaka 2015. Kwa kuwa muda uliobaki, sasa ni miaka miwili tu naiomba Serikali kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuwa hali ya barabara za Mji wa Geita ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Geita ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubovu wa vivuko vya Kigongo Busisi, Mheshimiwa Waziri vivuko hivi vimechoka sana na vimekuwa vikisababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa kivuko, zipo nyakati feri inabaki moja tu magari na abiria wanakaa hapo zaidi ya masaa 10 kusubilia feri. Naiomba Serikali kuja na suluhisho lingine la mahali hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vya michezo. Serikali ije na mkakati kabambe wa kupatikana viwanja vya Serikali vya michezo. Mfano katika Mkoa mpya wa Geita, Mkoa mzima hakuna viwanja vya football, basketball, netball na hata riadha. Pia nataka kufahamu mkakati wa Wizara kuhusu bima ya wanamichezo wote kwa kuwa hivi sasa mchezaji anapopata tatizo dogo la kiafya maisha yake yanakuwa ya kuombaomba. Kwa nini Wizara isipitie upya sera yake ili kuwafanya wanamichezo wote kuwa na hifadhi maalum ya fedha na bima kwa afya zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina mbalimbali za michezo. Limekuwepo tatizo la Watanzania kuwekeza zaidi katika mpira wa miguu na kidogo ngumi ili kuongeza wigo au chaguo la aina ya michezo. Mfano shule ziache kuweka sharti la uwanja wa mpira wa miguu kama ishara ya kuwepo kwa michezo, ikiwezekana michezo kama kuogelea, ngumi, basketball, volleyball, table tennis na squash na mingine mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tushirikiane na Wizara ya Elimu kuratibu wamiliki wa shule kutoa proposal ya aina ya michezo ambayo shule itau-promote kwa nguvu zake zote kwa kuweka miundombinu yake badala ya kuweka mkazo kwenye masharti ambayo yamebaki kuwa mapambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vazi la Taifa, naishauri Serikali badala ya kulifanya vazi la Taifa kuwa moja kwa nchi nzima, vazi hili lianzie kwenye Wilaya, Mikoa na baadaye Taifa. Iwapo Wilaya kutakuwa na vazi lake na baadaye Mkoa mwisho wa siku Taifa litakuwa na vazi lenye kujumuisha Mikoa yote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nchi yetu bado inawahitaji wamiliki wa shule binafsi kama wadau wa elimu, ni vyema yafuatayo yakazamwa upya. Kodi nyingi zinazomwelemea mmiliki wa shule ambazo hatima yake ni kuwazidishia mzigo wazazi katika ada, ni vyema kodi nyingi hizi zikaondolewa kama ilivyo katika sekta ya afya. Serikali iendelee kudhibiti ubora wa elimu. Hoja ya shule binafsi kujitengenezea udhibiti isikubaliwe kwa kuwa imekuwa ikitumika vibaya kwa baadhi ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upungufu wa walimu wa sayansi. Naiomba Serikali iendelee kutafuta suluhu ya upungufu wa walimu wa sayansi na naomba kuishauri Serikali kuruhusu wahitimu wa kada za sayansi za vyuo mfano, engineering na kadhalika ambao wapo mtaani kuajiriwa kama walimu kwa kuwa masomo yanafanana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Maji Kasamwa ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Kasamwa kwa kuwa visima vyote huwa vinakauka wakati wa kiangazi. Hivi sasa Bwawa la Kasamwa limepasuka kutokana na mvua kubwa. Naomba Wizara
ifanye ukarabati mkubwa katika bwawa hili ambalo hivi sasa limepasuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hali ya maji Kasamwa, Mji wa Kasamwa una watu wanaokadiriwa kuwa 25,000 ambao wanategemea visima. Naiomba Serikali kupeleka maji ya bomba kutoka Geita Mjini kwa kuwa umbali uliopo kutoka Geita Buhalahala kwenda Kasamwa ni kama kilometa 10 umbali ambao ni mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya maji Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Bulela. Hizi ni kata ambazo ni sehemu ya Geita Mjini lakini hazimo katika hotuba ya Waziri na hali ya maji katika kata hizi ni mbaya sana. Naomba Serikali badala ya kufikiria kuchimba visima ni vyema kuweka mkakati wa kupeleka maji ya ziwa ya bomba ambayo yapo ndani ya kilometa 30 tu kutoka makao makuu ya mji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukaguzi wa TBS, NEMC, TFDA; Serikali kupitia mamlaka mbalimbali imekuwa ikifanya ukaguzi wa maeneo ya viwanda, bidhaa za viwanda na kutoa vibali au kuteketeza mali za wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la mamlaka hizi ni rushwa, urasimu na kutumia standards za Ulaya kwa kuwafanya Watanzania wengi kukwama kuanza biashara, kuchelewa kuanza biashara na kufilisika kutokana na matumizi mabaya ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kama tunataka viwanda viongezeke, nchi yetu lazima iondoe rushwa, urasimu na Europe Standards kwenye vigezo vya kufanya biashara au ubora wa bidhaa za Watanzania. Kwa sababu duniani kote kuna export quality na kuna internal consumption quality, lazima tuondoe masharti yanayokwamisha kuanza biashara na kujenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutumia TIC imekuwa ikihamasisha wawekezaji kutoka nje kuwekeza Tanzania. Wawekezaji wengi wanaokuja na mitaji yao na kununua ardhi na kumiliki kwa asilimia mia moja; nchi kabla ya kuingia kwenye mkakati huu wa viwanda haikuandaa sera itakayolinda wazawa na kuzuia utoroshaji wa faida zote kwenda nje. Mfano, viwanda vyote vikimilikiwa na wageni, maana yake faida yote ya uwekezaji mkubwa itakwenda kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kwamba tulitakiwa kuwa na sera ya kulinda maslahi ya nchi ili kuepuka matatizo tunayopata sasa kwenye uwekezaji mkubwa wa madini kumilikiwa na wageni watupu na kuruhusu wizi mkubwa, udanganyifu mkubwa kupitia transfer pricing na cheating kwenye contracts?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kutazama upya Sera ya Uwekezaji kwenye viwanda ili kuruhusu mgeni kuuza sehemu ya haki zake kwa wazawa, suala ambalo litasaidia kupunguza profit export kurudi kwao na kuiacha Tanzania maskini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia na naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu hii ukiitazama ina matatizo makubwa mawili; la kwanza ni tatizo la fedha ambalo limesemwa na kila Mbunge; lakini la pili kama walivyosema baadhi ya Wabunge ni tatizo la uwezo wa matumizi ya pesa zenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni mwa mwaka huu Mheshimiwa Waziri alifanya ziara na alikuja Geita na yeye mwenyewe akawa anashangaa kuona maji hakuna, anashangaa kuona malalamiko ya maji yako nchi nzima lakini anasema ana takriban shilingi bilioni 50 kwenye akaunti na tatizo ni kwamba hakuna mtu analeta certificate kuonesha kwamba kuna kazi zinaendelea.

Kwa hiyo, ina maana tuna matatizo mawili, la kwanza inawezekana tuna tatizo la pesa ambalo ni dogo lakini tuna tatizo la uwezo wa kutumia pesa kutoka kwenye Wizara yenyewe na pengine inawezekana ni uwezo wa watu walioko chini kwenye Wizara wanaoweza kusababisha pesa zitumike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kuimarisha sana uwezo wa watu wake huku chini. Kuna lugha mbili zinazungumzwa hapa, Mheshimiwa Waziri anasema msiangalie sana ring fence ya bajeti yenu kwenye Halmashauri, anzisheni miradi, tengenezeni certificate mlete tulipe, lakini walioko kule chini wanaangalia kile ambacho wamepewa na Serikali ndiyo wanatangaza na pengine hawatangazi mpaka waambiwe pesa zipo. Kwa hiyo, inawezekana kuna tatizo la mawasiliano kati ya ofisi ya Mheshimiwa Waziri na watu wake ndiyo maana malalamiko ni mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali, kwa miaka yote miwili mfululizo tumekuwa na tatizo kubwa sana la maji katika Mji wa Geita. Katika taarifa yake ukurasa wa 53 amekadiria kwamba hivi sasa upatikanaji wa maji katika Mji wa Geita ni kama takribani asilimia 37. Inawezekana takwimu hizi Waziri ameletewa lakini siyo kweli, Geita takwimu hizi ambazo nazipinga upatikanaji wa maji uko chini ya asilimia 15 na sababu ni kwamba maji yaliyoko Geita ambayo yanasukumwa na mgodi wa GGM, makubaliano ya uanzishwaji wa mradi ule ilikuwa Serikali ichangie asilimia 50 na mgodi asilimia 50, mgodi ukatumia shilingi bilioni 12; lakini Serikali ikatoa shilingi 400,000 peke yake. Kwa hiyo, matokeo yake ule mradi umekamilika lakini uwezo wake wa kufanya kazi unafikia kaya 1,700 peke yake. Mara nyingi Mji wa Geita hauna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hivi karibuni GGM wamesema wanajiondoa kwenye uendeshaji wa mradi ule na sasa hivi GEUWASA walikuwa wanakusanya mapato bila kuingia gharama ya kupeleka umeme wala kusukuma umeme kutoka kwenye chanzo cha maji. Maana yake ni kwamba muda mfupi ujao GGM wakijiondoa, GEUWASA wanatakiwa waanze kujilipia mwenyewe gharama ya uendeshaji na mradi ule uko category C.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ya namna gani tunamaliza tatizo la maji katika Mji wa Geita. GGM watakapoacha kusukuma maji kwa sababu wanasema gharama ni kubwa na walikuwa wanatumia pesa za CSR ambazo Serikali kupitia sheria tuliyorekebisha hapa Bungeni tumewanyang’anya sasa tumezipeleka halmashauri, kwa hiyo, hawana tena uwezo wa kutumia zile pesa na wao hawana fungu lingine kwa maelezo yao na kwa mwezi mmoja wanatumia milioni 70 maana yake ni kwamba GEUWASA hawana uwezo tena wa kusukuma maji, hata hii asilimia 15 tunayoipata sasa hivi haitakuwepo. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri aje na majibu ni namna gani ataondoa tatizo hili kwa sababu tumesubiri pesa za India leo mwaka wa tatu hazionekani na muda unakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi pale wa LV- WATSAN na kwa nini nimesema tunalo tatizo la matumizi ya pesa na usimamizi, huu mradi una pesa tayari shilingi bilioni sita, Waziri ametaja kwenye taarifa yake lakini mradi ambao ungekabidhiwa mwezi Novemba, 2016; leo Mei, 2018 mradi huu haujakamilika na mkandarasi hayuko site, maana yake ni nini? Amesema mradi huu utakabidhiwa Mei, namhakikishia Mheshimiwa Waziri sio kweli kwa sababu sisi tunatoka kule site tangu alivyoondoka matenki na mabomba yako vilevile na mkandarasi haonekani na kama anaonekana atakuwa anafanya kazi nje ya mkataba kwa sababu alishasimamishwa na Wizara na watu wanaomsimamia. Sasa kama pesa zilikuwepo shilingi bilioni sita na hakuna tatizo la pesa hapa lakini mradi hauendi leo mwaka wa tatu maana yake ni kwamba liko tatizo pia la uwezo wa kumsimamia huyu mkandarasi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri pengine leo atakuja na majibu sahihi kwamba huu mradi wa LV-WATSAN utakamilika lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita tunashangaa kuona tunapokuja na bajeti ya visima, sisi tuko kilometa nane tu kutoka ziwani. Watu wa Shinyanga, Tabora na sehemu nyingine wangezungumzia visima nisingeshangaa, sisi tunataka maji ya ziwa. Pale kama Serikali itawekeza maji kutoka ziwani ukapandisha kwenye ule mlima ulioko pale Geita, maji yatashuka yenyewe kwa gravity kwenda mpaka Kahama, kwa nini tunahangaika na visima katikati ya Mji wa Geita ambavyo kiangazi vyote vinakauka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini moja ya miji inayokuwa haraka sana kutokana na shughuli za madini na mwingiliano wa watu ni Mji wa Geita. Nimeona humu kwenye ripoti ya Waziri wamekadiria wanapeleka maji kwa watu 130,000, sisi Geita pale tunaamini kuna zaidi ya watu 300,000 sasa hivi na tunahitaji maji mengi sana ili tuweze kuendelea na shughuli zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii ametupatia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuongeza mtandao wa maji. Mwaka jana walitupatia tena shilingi bilioni mbili ambazo zilitupa kama kilometa 80 za mtandao wa maji. Tatizo kubwa tulilonalo ni maji machache ambayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya nishati ya mkaa na kuni kwa taasisi, nimesoma ushauri wa Waziri kwa taasisi kutumia nishati mbadala. Ushauri huu hauonekani kuwa ni msisitizo wa kuokoa misitu. Naishauri Serikali kuleta sheria ambayo itazilazimisha taasisi kuweka mkakati wa matumizi ya gesi badala ya kuni au mkaa. Pamoja na sheria hiyo Serikali itoe punguzo la kodi maalum kwa vifaa vya gesi yenyewe kwa taasisi zilizo tayari ambazo zitatambuliwa. Jambo hili iwapo litafanyika litasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Spika, suala la mipaka mipya ya hifadhi, naunga mkono maoni ya Kamati juu ya kuondoa kabisa mipaka mipya ya mbuga na hifadhi kwenye vijiji na nchi nzima kwa ujumla. Mipaka hii imeleta tafrani kubwa na imekiuka kabisa mipaka ya asili iliyowekwa kwa mujibu wa GN na sheria za nchi hii. Mipaka mipya isimame mpaka ushirikishwaji utakapofanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kesi za mifugo inayokamatwa, baadhi ya mifugo imekuwa ikikamatwa ndani ya hifadhi au mbuga za wanyama na Serikali kuzishikilia kwa muda mrefu. Kwa kuwa askari wa wanyamapori hawana utaalam wa mifugo, mifugo mingi huwa inakufa na Serikali na wananchi kupata hasara kubwa. Kwa mfano mwaka 2014/2015 huko Ngara Tanzania mifugo (ng’ombe) 887 ilikamatwa ndani ya hifadhi, mifugo 700 ilikufa kabla ya maamuzi ya Mahakama na hata waliobaki walikosa bei ya soko kwani walikuwa wamekonda sana.

Naishauri Serikali kubadilisha utaratibu wa kushikilia mifugo, badala yake iachwe kwa mtuhumiwa kwa uangalizi maalum mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naomba kuzungumzia kuhusu bajeti ya own source asilimia 40 maendeleo badala ya asilimia 60 ya awali. Halmashauri ya Mji wa Geita ilitenga asilimia 60 ya mapato ya ndani (own source) kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hivi karibuni Wizara yako imetoa maelekezo kwa Halmashauri yangu ya Geita Mjini kubadilisha mipango kutoka asilimia 60 ya own source kwenye maendeleo kwenda asilimia 40 na hivyo kufanya matumizi ya kawaida kuwa makubwa kuliko miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri yangu haioni sababu ya kubadili mipango yote ya bajeti ya fedha ambazo sisi wenyewe tumekusanya kwenye vyanzo vyetu wenyewe na tumekaa, tumeona tuzielekeze kwenye miradi ya maendeleo ambayo ndiyo vipaumbele vyetu. Naomba kupata ufafanuzi kuhusu sababu ya Wizara hii kutoa mwongozo ambao unaondoa vipaumbele vya maendeleo kwa matumizi ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, lingine ni madeni ya wazabuni mbalimbali. Pamoja na jitihada kubwa ya Serikali kulipa madeni, bado Wizara ya Fedha imeshindwa kuwalipa wazabuni wanaoidai Serikali kama wazabuni wa shule, magereza na taasisi za umma. Wazabuni wa pembejeo wanadaiwa na benki. Naomba juhudi za Serikali kupitia upya madeni hayo zifanyike mapema na kuleta orodha ya wauzaji wenye tuhuma za kuwapeleka mahakamani na kuwashitaki ili vyombo vya haki viweze kuona ni nani anastahili na nani hastahili kulipwa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu PRIDE kushindwa kulipa fedha za wateja na mishahara. Yapo malalamiko makubwa kuhusu PRIDE Tanzania. Ipo taarifa kwamba wafanyakazi wana miezi 18 bila kupata mishahara na wateja walioweka akiba ya fedha wamekosa huduma kwa kuwa fedha hakuna.

Mheshimiwa Spika, zipo taarifa kwamba management ya juu ya PRIDE imekimbia na zaidi ya shilingi bilioni 40 za fedha hii, kuna sehemu ni mali ya umma. Naitaka Wizara kutoa tamko kuhusu ukweli wa hali ilivyo PRIDE Tanzania na hatua zinazochukuliwa kulipa madeni ya wafanyakazi na wananchi walioweka akiba zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishaji vyeo Jeshi la Zimamoto; Askari walipandishwa vyeo baada ya mafunzo mwaka 2016 na walipewa barua za kupanda vyeo, lakini hawajabadilishiwa mshahara mpaka leo na badala yake kuna barua ya kufuta vyeo vilivyopanda. Naomba kujua lini Askari hawa watarejeshewa vyeo na mabadiliko ya mishahara yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Kituo cha Polisi Kati Geita; katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali iliahidi ujenzi wa kituo hiki. Naomba kufahamu lini ujenzi huu wa kituo cha Polisi Kati Geita Mjini utaanza, ikiwa ni pamoja na jengo la zimamoto na magari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa magari, lipo tatizo kubwa la usafiri kwa Jeshi la Polisi Mkoani Geita. Mfano OCD Geita anategemea gari la FFU Kasamwa inapotokea ugeni wa viongozi hali za doria zimepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mlundikano wa mahabusu na ubovu wa Magereza; hali katika Gereza la Geita ni mbaya sana, idadi ya mahabusu ni wengi na hii imetokana na utaratibu mbaya wa kesi za kawaida ambazo zingeweza kumalizwa na wahusika, kulazimu kupelekwa Polisi na Mahakamani ambapo matokeo yake mahabusu mwenye kesi ya kuku kutumia gharama kubwa bdala ya faida inakuwa hasara. Naishauri Serikali kuleta mfumo utakaoondoa watu kujazana mahabusu na magereza kwa sababu hili linasababisha mateso na rushwa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nitumie nafasi hii ingawa Mheshimiwa Mwambe amesema tusipongeze lakini niipongeze sana Serikali yangu kwa kuendelea kutekeleza vizuri Ilani ya Uchaguzi ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ili uvuke uende Geita lazima upite Busisi na juzi tumeona uzinduzi wa kivuko kipya ambacho kitakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuchukua abiria wengi na magari na ni njia hiyo pekee ambayo kwa kutokea Mwanza naweza kufika Jimboni. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kutimiza ahadi yake hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe Serikali walikuwa wanafanya feasibility study nadhani kwa ajili ya kujenga daraja kwenye eneo lile ambalo litapunguza sana vifo visivyo vya lazima ambavyo vinatokea wakati unasubiri ferry kwenda Bugando kwa sababu ndiyo hospitali pekee ya rufaa, kama upembuzi yakinifu ule umekamilika basi nimwombe sana Waziri wa Fedha kwamba wananchi wa Kanda ya Ziwa hasa wananchi wa Geita na Mikoa mingine wanasubiri kwa hamu kuona ujenzi wa daraja lile unaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri juzi amesema ameondoa kodi ya VAT kwenye taulo za kike, nampongeza sana kwa sababu ilikuwa ni ombi la kwetu wenyewe Wabunge. Wasiwasi wangu tu nataka aje anisaidie punguzo hili la VAT wamefanya utafiti litapunguza bei kwa kiwango gani kwa watumiaji. Nafahamu kwamba hizi exemptions mara nyingi mwisho wa siku zinawafaidisha zaidi wafanyabiashara na siyo watumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Kamati kwenye suala la maji, mwaka jana na mwaka juzi tulipendekeza kwamba iongezeke Sh.50 ili tutunishe Mfuko huu wa Maji na hatimaye tuongeze uwezo wa Serikali kwenye kuhudumia miradi ya maji. Kwa hiyo, nimwombe mwaka ule alikataa lakini mwaka huu na dalili ilivyo na kwa sababu tumemaliza mwaka mmoja na nusu kwenda kwenye uchaguzi nadhani sasa anafahamu kwamba bila kufanya hivyo suala hilo litakuwa gumu sana kutekeleza na kwa sababu ni Ilani yetu wenyewe ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala lenyewe la hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Hapa karibuni baadhi ya wachangiaji wameonesha sana wasiwasi wa kwamba bajeti yetu Tanzania ni ndogo kulingana na nchi ya jirani kwa mfano Kenya ambao bajeti yao ni dola bilioni 30 na nimeona Uganda wenyewe wana kama dola bilioni 8.5 lakini imeongezeka kwa asilimia 15, Tanzania imeongezeka kwa asilimia mbili. Nadhani sababu ya Waziri kutokuongeza bajeti kama alivyokuwa anafanya miaka ya nyuma ni kutokana na tax base yetu kuwa ndogo na tax base yetu imekuwa ndogo siyo kwa bahati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami kwamba Waziri wa Biashara anahangaika sana kuvutia wawekezaji waje, lengo lake ni kuongeza tax base ili Waziri Mpango aweze kukusanya kodi. Waziri wa Madini anahangaika kutengeneza sheria ili kuwarasimisha wachimbaji wadogo wadogo lakini kuhakikisha kwamba migodi yote inaweza sasa kulipa kodi ili kuongeza tax base.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata tabu sana kama Serikali inakwenda kwa kufikiri pamoja. Wakati Wizara hii inahangaika sana kuboresha tax base unashangaa kuona Wizara nyingine inatumia sheria na kanuni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara ambao wapo wanaendelea kulipa kodi wanafilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa mfano kwenye uvuvi, nimeangalia hapa kwenye taarifa ya Kamati, uvuvi umetengewa 0.06. Hivi ninavyozungumza tumepata taarifa hapa kutoka kwa Mheshimiwa anayeshughulika na uvuvi na mifugo kwamba amekusanya takribani bilioni nane kwenye faini na kodi mbalimbali kwa wavuvi haramu, lakini anasema amekuja kugundua asilimia 98 ya wavuvi wote Tanzania ni wavuvi haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba ameondoa walipa kodi asilimia 98 kwenye mfumo wa kulipa kodi ambao Mheshimiwa Dkt. Mpango alikuwa anakusanya kodi wote ni wavuvi haramu, amewaondoa kwenye mfumo bila kuja na mpango wowote wa kuhakikisha kwamba hiyo tax base anairudishia. Madhara yake ni kwamba tunaotoka kwenye maeneo ya uvuvi kabla ya Watanzania wengi kuingia ziwani kuvua samaki, wavuvi pekee walikuwa ni wale wenye viwanda na wenye viwanda walipewa kazi na Serikali ya kuwawezesha Watanzania kununua nyavu hizi ambazo ziliruhusiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waletaji wa nyavu wakalipa kodi, wakawakopesha Watanzania na wale Watanzania wakanunua wakaweka dhamana nyumba zao, nyavu ambazo zote ni haramu, zimekamatwa zote zimechomwa moto. Hawa wenye viwanda ambao leo hawawezi kuwakopesha tena Watanzania waliokuwa wanavua samaki na wale wote waliokuwa wanavua samaki hawana mitaji, maana yake ni kwamba hatuwezi tena kukusanya kodi lakini tumeua hiyo industry ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sishangai ninapomwona Waziri anaposema samaki wamekuwa wengi ziwani, ni kwa sababu anasahau there is no more industrial fishing tena kwa sababu asilimia 98 ya wavuvi waliokuwa mle ziwani ni wavuvi haramu kwa tafsiri yake, kwa nyavu alizopokea na alizoziruhusu yeye kuingia ziwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni mmoja, tunalalamika kwamba bajeti yetu ni ndogo lakini ukiangalia system nzima haifanyi kazi pamoja. Nilitarajia kwa kuwa kanuni hizi ni za Waziri na kanuni zinazomwongoza kufanya kazi hii amezitunga yeye, Sheria ya Uvuvi iko vizuri sana. Kwa kuwa nyavu hizi zililipiwa kodi na kwa kuwa tunahitaji industry ya uvuvi iendelee kuwepo ili tupate kodi, nimeangalia kwenye kwenye kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango makusanyo yote haya kwa miezi minne sasa ukienda Mwanza hayapo, angefanya mpango maalum wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na transition period kabla ya kuanza kuchukua hatua ambazo zinaondoa walipa kodi, karibu asilimia 30 ya walipa kodi wa Kanda ya Ziwa ni Wavuvi wote wanaondoka kwenye mfumo na wakirudi kukopa wataanza kulipa interest na interest ina gharama kwenye kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tunapotengeneza tax base, ukiangalia sasa hivi mwaka huu tumeshindwa kuongeza kwenye projection yetu ni kwa sababu tax base yetu ni ndogo. Tulikurupuka miaka fulani tukawa tunaongeza kila mwaka matokeo yake hatujawahi kukusanya kwa asilimia 100. Sasa kama tunatengeneza tax base leo kesho tunaibomoa, unaitengeneza kesho, kesho unaibomoa maana yake ni kwamba tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona juzi kwamba Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi amegundua kwamba operesheni ili iweze kufanikiwa sasa ni lazima twende kwa walaji na walaji ni kwenye hoteli na anatumia regulations hizo ambazo ni za uvuvi. Tatizo kubwa ambalo naliona, mimi nadhani Watanzania wengi hawajui kwamba source ya samaki siyo Ziwa Victoria peke yake, regulation iliyopo inazungumzia samaki wa Ziwa Victoria, sato na sangara lakini kuna watu wanafuga samaki, ambao hawafugi kwa masharti kwamba ili awavune lazima wafikie sentimita ambazo yeye anazitaka. Cost yake ya ku-run lile bwawa huwezi kusubiri mpaka samaki akae miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wa Mtera na Nyumba ya Mungu hawafanani na sato walioko Ziwa Victoria. Kwa nini Waziri akili yake anafikiri tu kwamba lazima hawa watakuwa ni kutoka Ziwa Victoria halafu ukikutana na sato species 50, Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukisema hapa ni kwamba unaweza ukaletewa sampuli ya sato 10 lakini wale sato 10 ni species tofauti, hawafanani na kadri wanavyotofautiana hawakui kwa kufanana. Kwa nini Waziri anakimbilia kwenda… kwa sababu kadri unavyochukua hatua una- demoralize watu wote wanaoshughulika na ile biashara una erode tax base. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kuleta mkakati wa kuboresha vituo vya afya. Naomba kujua awamu nyingine ya fedha hizi, Mji wa Geita utapewa? Hii inatokana na kutokuwemo katika awamu ya kwanza. Geita Mjini haina hospitali hivi sasa kwa kuwa hospitali yetu ya wilaya kwa miaka minne imebadilishwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kukubali kuwarejesha Watumishi wa darasa la saba kazini. Naomba sana suala hili liwe kwa watumishi wote waliokumbwa na kadhia hili ikiwa ni pamoja na Manesi, Dereva na Idara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kukabiliana na tatizo la upungufu wa Walimu, kwa kuwa hivi sasa tunapunguza Walimu wa sekondari kwenda msingi ni vyema taratibu za kuangalia kwa makini waliokusudiwa zifuatwe kwa kuwa hivi sasa kuna kukomoana. Pia ni muhimu sana wanaohamishwa wawe ni wale wenye Diploma kwanza kuepuka kutengeneza tatizo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubora wa elimu, naishauri Serikali hasa kwa elimu ya Sekondari kuacha kuchukua watoto holela wa darasa la saba. Kwa mfano, mwaka 2017 iwapo uwezo wa Serikali nchi nzima ni wanafunzi 200,000 wa mwaka wa kwanza basi mwaka unaofuata Serikali ichukue kwanza 200,000 na baadaye iongeze idadi iwapo tu inazo taarifa za uwepo wa nafasi zaidi kuliko hivi sasa kuchukua kama kokolo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira mpya; bado hakuna uwazi wa kutosha katika mfumo wa kuchuja watahiniwa kwa kuwa hivi sasa ni rahisi sana kwa Watendaji wa Idara ya Utumishi wanaokuja mikoani kuja na watu wao.
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipatia. Naomba niwashukuru wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia, lakini pia niwashukuru kwa sababu asilimia kubwa ya wachangiaji wameunga mkono hoja na sisi ambao tumeleta hoja hii tumefarijika kuona kumbe ulikuwa ni mtazamo wa kila mtu kuona umuhimu wa hifadhi hii kuwa National Park.

Mheshimiwa Spika, kama alivyomalizia kusema Mheshimiwa Angelina Mabula, watu wengi ambao hawajawahi kufika BBK hawaifahamu vizuri. Ukiwa BBK upande ambao tunapakana na nchi jirani kuna vijiji vinakwenda mpaka kwenye mto, mpaka wetu ni mto, lakini ukivuka mto peke yake unaingia kwenye BBK hizi ambazo tunazungumzia hii Kimisi, Burigi pamoja na Biharamulo. Maana yake ni kwamba, upande wa pili palikuwa na watu ambao wana access ya moja kwa moja na game reserve, lakini upande wetu huu kwa sababu, mpaka ni mrefu na kwa sababu ya uwezo ambao TAWA walikuwa nao tulikuwa tunshindwa kwa kweli kimsingi kusimamia ulinzi vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa tunafarijika kuona kwamba, baada ya kuwapatia TANAPA na kama walivyosema Wajumbe wengi ni kwamba, TANAPA kimsingi wanazo financial muscles ambazo zitatusaidia sana kwenye kuimarisha ulinzi. Katika kuhakikisha kwamba, hili linaungwa mkono na kauli hii, baada tu ya sisi kuonesha kwamba, tunataka kuichukua hii kuwa TANAPA, tayari TANAPA wamekwishatengeneza kilometa 121 za barabara, wamekwishapeleka magari matano kwa ajili ya kuimarisha doria, wamenunua maboti mawili kwa ajili ya usimamizi kwenye Ziwa Burigi na Ziwa Ngoma. Pia lakini tayari wametambua maeneo nyeti ya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na wameongeza idadi ya wafanyakazi katika eneo hili na kupeleka wafanyakazi 70. Kwa hiyo, utaona utayari wa TANAPA katika kuhudumia eneo hili ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ushirikishwaji; tangu tulipokuja na wazo hili tumezitumia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya, lakini Viongozi wa Vijiji wa maeneo husika. Wote hawa wametumika katika kutoa elimu na kuwaeleza faida ambazo zitapatikana kutokana na eneo hili kuwa hifadhi ya Taifa. Hata hivyo, elimu itaendelea kutolewa kwa sababu, elimu ni suala la kudumu. Naamini kwamba, wananchi wa maeneo haya wamejiandaa vizuri zaidi kupokea eneo hili kuchukuliwa na TANAPA kwa sababu za historia ya TANAPA yenyewe namna inavyofanya kazi, lakini faida ambayo wanaipata.

Mheshimiwa Spika, tunategemea watapata faida gani; la kwanza, tunaamini kwamba, eneo lile likishafanyika uwekezaji wa kutosha, ukiacha suala la usalama lipo suala la biashara. Maeneo yale yatachangamka sana kibiashara, kutajengwa hoteli za ndani na nje ya eneo hilo ambazo zitafanya mzunguko wa pesa katika eneo hilo kuwa mkubwa, lakini tutaimarisha zaidi cultural tourism. Maeneo mengi sana ukiwa unatoea Arusha ukija kufika Serengeti wananchi wa maeneo yale wanaona umuhimu wa uwepo wa Ngorongoro na Serengeti kwa sababu, wakati watalii wanaelekea kwenye kutalii Serengeti na Ngorongoro wanapita kwenye maeneo ya wananchi na kuona namna ambavyo wananchi wanashiriki kwenye utalii. Vile vile, tunaamini kwamba, usimamizi mzuri wa mazingira utaimarika ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Msigwa ameonesha dalili ya kwamba, nikitafsiri vizuri lugha yake ni kama anaona kunafanyika upendeleo kupeleka TANAPA sasa hivi BBK na kuacha REGROW, Mheshimiwa Waziri wangu atazungumzia vizuri kuhusu REGROW, Lakini nataka nimtoe wasiwasi kwamba, nchi hii ni moja, mtazamo ambao Serikali inao kuhusu Kusini ni mtazamo uleule ambao inao kuhusu Kaskazini,
kuhusu Magharibi na sehemu nyingine zote na kwamba, haya hayafanyiki ili kuondoa umuhimu wa eneo la Southern Circuit.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze kusema kwamba naunga mkono hoja na niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa maoni na ushauri kwa hoja ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye wasilisho lake mapori yetu yote Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba kinachotofautiana ni matumizi ya maeneo lakini yote yanasimamiwa na yanalindwa na yana ulinzi wa kutosha. Tunapopandisha hadhi pori la akiba la Selous na kuliita Nyerere National Park kinachobadilika pale ni matumizi tu ya eneo hilo, kwamba sasa tunakwenda kufanya zaidi utalii wa picha badala ya utalii wa awali ambao ulikuwa unaruhusu utalii wa picha na uwindaji, lakini matumizi mengine yote na namna ambavyo yanasimamiwa na ulinzi yanafanana. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kabisa Waheshimiwa Wabunge ambao wameonesha kana kwamba kubadilika kwa hadhi sasa Wizara iende kuanza upya kufikiri namna ya kuhifadhi eneo hilo lakini na kuondoa wafugaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wote ambao tumewaona kwenye maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba ni wavamizi na wamekuwa katika maeneo hayo kinyume cha sheria, kwa hiyo wawe ndani ya National Park au wawe ndani ya Game Reserve hawa wako kinyume cha sheria na wanashughulikiwa na sheria ile ya Uhifadhi ambao hawatakiwi kuwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, nijibu tu maeneo mawili matatu ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesema na Kamati, moja ni la kushirikisha wadau, wadau wameshirikishwa na mchakato huu tangu Mheshimiwa Rais alipotoa maelekezo pale wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa bwawa la umeme wadau mbalimbali wameshirikishwa wakiwemo hao wenye mahoteli lakini pia wakiwemo wadau wanaofanya biashara za utalii na wananchi wa Mikoa ya jirani ya maeneo hayo. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi kwamba suala hili halijakimbizwa kwa haraka, hakuna mdau ambaye hakusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, katika wadau wakubwa ambao walikuwa katika maeneo yale, hasa ambao wanaathirika na ujenzi wa bwawa, Wizara kupitia Serikali wapo ambao wameguswa na wamepata fidia na wamepewa maeneo mengine ya kwenda kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo limeonekana lina shida kidogo ni kwamba eneo la hifadhi hii ni kubwa sana na kwa sababu hiyo yako maeneo ambayo hayatatumika kwa leo kwa faida, ni kweli kilometa za mraba elfu 30 ni nyingi na huwezi kuziendeleza na kuzitumia kwa mara moja. Kama mnavyofahamu tumekuwa na traditional product mbili sana Tanzania ni mbili tu ya kwanza ni Safari ambayo ni ya kupiga picha, na nyingine ni ya kupanda Mlima Kilimanjaro sasa maeneo haya ambayo yalikuwa yanatumika zaidi kwa uwindaji ni maeneo ambayo terrain yake hairuhusu utalii wa picha na wakati mwingine utalii wa safari tuliouzoea, lakini huu ni muda muafaka wa ku-develop aina nyingine ya product kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tu nitoe mfano, ukienda leo Serengeti utakutana na balloons nyingi zipo mle ndani ambapo wawekezaji kadhaa wameingiza balloons ambazo zinaweza kutoa watu sehemu moja kwenda sehemu nyingine lakini pia tunafikiria hii milima mingi iliyomo katika pori la akiba la Selous tunaweza ku-introduce cable cars pamoja na maboti yanayopita kwenye maeneo ambayo sisi tunaona kwamba hayapitiki lakini kuna hiking na michezo mingi ambayo inatumika kwenye maeneo ambayo hayatumiki kwa utalii wa picha. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi kabisa Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tutakapolichukua litabaki bila matumizi.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, imezungumzwa hapa kuhusu vivutio vingi vya utalii vilivyopo mikoa ya kusini. Ni kweli kwamba mchakato huu unakwenda kufungua Mikoa ya Lindi na Mtwara na tunakwenda kufungua ukanda wote wa mashariki (ukanda wa bahari) na kwa sasa hivi baada ya mchakato huu kukamilika, kwanza nilitaka nitoe taarifa kwamba maeneo yale ya Mikindani na Kilwa yote haya mwanzo yalikuwa hayajiendeshi vizuri kwenye shughuli za utalii lakini Wizara ilikaa na kufikiri na kuona kwamba ili yaweze kuwa sehemu ya package ya watalii wanaotembelea maeneo haya na kwa juhudi za sasa za kupandisha hadhi eneo hili kuwa hifadhi ya Taifa ambazo zitaongeza miundombinu na kufungua maeneo haya yote, tuliyaunganisha pamoja na taasisi zetu zote kama TAWA.

Mheshimiwa Spika, na juzi nilikwenda Mafia nimekuta TAWA wapo pale wanaimarisha miundombinu lakini Mikindani pale wapo na hata maeneo yote ambayo ameyasema Mheshimiwa Hawa Ghasia ni maeneo ambayo tayari tumeyaweka kwenye mpango kazi wa kuyafungua.

Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba hata huu mradi wa REGROW ambao sasa ulikuwa sehemu ya juu ya Selous, awamu hii ya kwanza ya mradi huu wakati inaendelea kutekelezwa, Wizara imo katika mchakato kabambe wa Awamu ya II ya REGROW ambao sasa utaenda kuunganisha mikoa hii miwili ya huku chini na kuifungua kabisa na kuifanya iwe ni mikoa muhimu kwa ajili ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba tunatambua vivutio vingi vipo maeneo hayo, tunaamini kwamba tutakapoimarisha miundombinu na utangazaji wa maeneo hayo na tutakapokamilisha sasa uwekezaji, tutahamasisha biashara ya utalii ambayo imekuwa ni kivutio na chanzo kikubwa cha mapato kwa mikoa ya kaskazini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kurudi tena kwenye Bunge lako Tukufu. Nakishukuru sana chama change, Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua na baadaye kushinda uchanguzi Jimbo la Geita Mjini. Naomba kuwaahidi wananchi wa Jimbo la Geita Mjini kwamba nitaendelea kuwa mwakilishi mwaminifu sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kufungua Bunge ukurasa wa 41 alizungumzia madini na alisema sekta ya madini imekua kutoka mchango wake katika malipo ya pato la Taifa wa shilingi bilioni 168 mpaka 527 lakini katika pato la Taifa kutoka asilimia 3.4 mpaka 5.2. Naungana na Mheshimiwa Rais kuwapongeza sana Wizara ya Madini wanafanya kazi vizuri. Mimi ambaye natoka jimbo ambalo uchumi wake kwa asilimia zaidi ya 80 unategemea sana pato la madini, naona faida ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ambayo imeleta heshima katika matumizi ya fedha za CSR katika Halmashauri yangu ya Mji wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja tu hapa wachimbaji wadogo investment capital yao ni kubwa kuliko faida wanayoipata. Teknolojia wanayotumia na duni na bado mitaji ni midogo. Unakuta wachimbaji wadogo wanaendelea kubahatisha. Inaweza kutokea rush wataanza kuchimba mpaka wanafika mita 60 mpaka 100 hajaanza kufanya uzalishaji lakini tunazo teknolojia. Niiombe Wizara kama makampuni yanafanya CSR na yenyewe ifanye hivyo, ileta mitambo ya kutosha ili sehemu rush zinapotokea wawaambie wachimbaji kwamba eneo hili mnalochimba dhahabu zipo au madini yapo na yapo umbali gani na mlalo wa miamba. Namna tunavyokwenda sasa hivi utakuta ni kweli tunaongeza uzalishaji wa dhahabu lakini kimsingi gharama za uzalishaji wa dhahabu hizo ni kubwa kuliko faida ambayo wachambaji wadogo wanapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili katika eneo hilo, juzi Mheshimiwa Rais akiwa kule Mbogwe alisema kwamba siyo sahihi wachimbaji wakubwa wanapopata license kuamini kwamba sasa wamenunua haki ya wananchi ya ardhi na kukiuka sheria ambazo zipo. Wananchi wangu katika maeneo ya Nyakabale, Magema, Compound na Katoma wameendelea kuishi kwenye mgogoro wa takriban miaka
20. Ni kweli wako ndani ya leseni ya mgodi lakini mashamba yao ya asili sehemu ambayo mgodi haujataka kuanza kuchimba, hawaruhusiwi hata kwenda kukata kuni. Sasa hivi kuna ulinzi katika maeneo ya Magema hawaruhusiwi hata kupita nyumba moja kwenda nyumba nyingine kwa sababu ni ndani ya mgodi wa leseni. Nataka kushauri, Mheshimiwa Waziri alitolea maelekezo lakini Serikali ya Mkoa imeendelea kuweka askari pale, wananchi wameendelea kunyanyaswa tutoe mwongozo sahihi kama mgodi unataka eneo lile walipe fidia kama wananchi bado wanatakiwa kukaa pale wawaache wafanye kazi zao kwa uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo la pili kwenye ukurasa wa 27 sehemu ya kilimo. Ni kweli kwamba nchi hii inategemea ajira kwenye kilimo ambacho ni zaidi ya asilimia 80 na kimesaidia sana kudhibiti mfumuko wa bei na mimi nakubaliana na hilo. Nataka kutoa challenge kidogo hapa kwamba bado Watanzania wanalima very local na shida ya Watanzania siyo ukubwa wa mashamba. Mheshimiwa Rais anaweza kuendelea kuongeza mashamba, kubadilisha hifadhi, kubadilisha mapori ya akiba lakini shida hapa ni productivity kwenye maeneo waliyonayo wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado wakulima mtu analima heka kumi anapata gunia kumi za mahindi. Nataka kuwaambia Wizara ya Kilimo twenda sambamba na hotuba ya Mheshimiwa Rais, tulime kisasa na hili linaweza likaonekana kabisa kwa macho lakini tupate mbegu za kisasa na tupate huduma za ugani za kisasa. Utasikia tu kwenye magazeti na vitabu huduma zipo lakini kimsingi wakulima wetu bado wanalima kwa kizamani sana, productivity ya heka moja ni sawasawa na mtu aliyelima nyuma ya nyumba. Niiombe Wizara hii katika kipindi cha miaka mitano iweze kufanya jambo hili kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona kwamba kilimo cha kawaida hakitiliwi maanani sana wakati wa mavuno ya mazao ya biashara, maeneo yetu sisi tunalima pamba, store zote za pamba zimeoza, zimeanguka na zimegeuka kuwa nyumba za watu binafsi. Kwa hiyo, niombe Wizara iweze kujipanga vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tunalolipata kwenye kilimo liko pia kwenye mifugo. Utona kuna uboreshaji wa matumizi ya mashamba ya NARCO, lakini bado hata walio katika NARCO kinachowafanya waonekane wanafuga kisasa ni fensi, ukiingia kwenye shamba la NARCO utakuta hakuna mashamba ya nyasi, hakuna teknolojia unaotumika lakini bado ufugaji wa mle ni local, usambazaji wa mbegu za kisasa ni wa kizamani. Kwa hiyo, utakuta wafugaji hawa hata tunazungumza tuna ng’ombe milioni 33 hazijawasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana hasa katika kipindi hiki tunachokwenda nacho mabadiliko haya yaweze kutafsiriwa kwenye level ambayo wakulima na wafugaji wa kawaida wataondokana na kufuga ng’ombe 500 zenye kilo 250 waende wafuge ng’ombe 100 zenye tani moja ambazo zinaweza kuzalisha maziwa mengi lakini teknolojia iweze kusambazwa kwa njia ya urahisi. Tumeangalia maeneo mengi sana unakuta migogoro mingi ya wakulima na wafugaji, kwa nini? Ni kwa sababu mkulima akipata eneo la kwenda kulima akinunua mifugo anahamia hapo na akihamia hapo anajenga, kesho yake anasogea mbele anapata eneo la kulima anahamia na anajenga kwa sababu anafuga ng’ombe nyingi ambazo anashindwa kuzimudu kulingana na eneo alilonalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara katika kipindi iweze kutumia muda wa kutosha kufanya mabadiliko ya kisayansi. Unayaona haya mabadiliko kwenye vitabu lakini wafugaji na wakulima tunaokaa nao sisi bado wanafuga kizamani na wanalima kizamani na hakuna mabadiliko yoyote ambayo yameendelea kuwepo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda la mwisho, nimeona juhudi kubwa za Wizara ya Nishati katika Mikoa ya Pwani, ikisambaza gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Nilitamani kujua mkakati wa Serikali wa gesi hii kuifikisha kwenye mikoa ambayo iko nje ya Pwani, kwa mfano gesi hii itafika lini Mwanza au Geita ili tuweze kuachana na matumizi ya kuni na mkaa? Ziko taasisi zinatumia zaidi ya cubic mita 40 za kuni kwa mwezi, tunafanya nini kuzibadilisha taasisi hizi ziweze kutumia nishati ya gesi asilia tuliyonayo na kuweza kuzuia misitu yetu ambayo inaharibika kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kusema kwamba jana Mheshimiwa Gambo aliuliza swali ambalo lilikuwa linahusiana na tozo mbalimbali ambazo zimeongezwa kwenye Hifadhi zetu za Taifa. Nami nikataka kuongeza kidogo mawazo yangu hapo kwamba wakati COVID inaingia duniani, tuliwashauri watalii tukasema don’t cancel your trip to Tanzania, postpone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wako watu walikuwa wamelipa, fedha zao zilikuwa tayari kwenye account za wateja; na kwa kuwa wali-postpone wanatarajia siku watakapokuja watahudumiwa kwa gharama ile ile waliyolipia mwaka 2020. Sasa haya mabadiliko yaliyofanywa, nataka kuwaambia Wizara ya Maliasili na Utalii wafahamu kwamba mteja aliyelipia mwaka 2019 aka-postpone safari akitarajia kuja Tanzania kukamilisha safari yake anatarajia kuhudumiwa kwa gharama ile ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukumbusha hapa pia kwamba liko tatizo kubwa kwamba tunataka kufikia watalii milioni tano, jambo jema kabisa, lakini watalii hawa wanalipia muda na ukarimu. Ukarimu wanaolipia ni pamoja na consistency ya makubaliano mnayokubaliana tangu siku hiyo unam-convince kuja Tanzania mpaka siku anapopata huduma na kuondoka. Mabadiliko yoyote katikati baada ya kulipia yanafanya watalii wengi zaidi wasije kuliko waliokuja Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka kuongeza jambo lingine moja. Sasa hivi requirement ya airline ni kwamba tunatakiwa tufanye COVID Test. Hii inafanyika nchi nzima lakini laboratory iko Dar es Salaam. Mtalii anahitaji siku tatu mpaka nne kwenda kufanya COVID Test Arusha kusubiri majibu na baadaye kupanda ndege kurudi kwao. Matumizi haya ya muda kwa watalii hayasaidii Tanzania kuongeza idadi ya watalii. Tufanye mabadiliko, tupeleke watumishi kule, tuchukue test tuwapelekee wataalam waweze ku-test. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, liko tatizo hapa linazungumzwa kuhusu tatizo la TRA. Nawapongeza sana kwa kukusanya fedha nyingi, lakini iko shida. Nimemsikiliza mtu mmoja wa TRA kwenye TV akiwa anahojiwa TBC, anasema sawa biashara zinafungwa, lakini zinafunguliwa nyingi zaidi. Tumesema kwa miaka mitano, kuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hii kitu inaitwa Task Force. Tulifanya Mkutano na Mheshimiwa Kalemani pale Geita, tukaita wafanyabiashara wa Mkoa mzima wa Geita. Wanalalamikia TRA makadirio yao siyo rafiki. Kwa nini siyo rafiki? Inawezekana ni kwa sababu ya target kwamba ni kubwa kuliko survey ilivyofanyika ya uwezo wa walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna tatizo na Regional Manager wa TRA, wasaidizi wake huku chini, wanaweza kukukadiria shilingi milioni 400, mwisho mkaishia shilingi milioni 30. Maana yake ni nini? Kuna room hapa katikati ya negotiation na Serikali inapoteza fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Task Force inafanya jambo moja. Wanakuja wanafanya special audit, wakishafanya wanakwambia unatakiwa kulipa shilingi bilioni tano. Wakati huyu mteja ana-appeal wanazuia account, wanachukua fedha zote kwenye account. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikuta kuna fedha kwenye account ya mfanyabiashara leo, kwa mfano, biashara ya utalii; fedha siyo zake, ni za wateja wanaosubiri huduma. Unapozizuia maana yake unamzuia asitoe huduma kwa huyo mtalii, unazuia asilipe mishahara, unazuia asiendelee kufanya kazi. Ushauri wangu kwenye jambo hili, unapofanya special audit, ukagundua huyu mtu anatakiwa kulipa shilingi bilioni tano, akakata rufaa, wewe kabla hujatoa majibu ya rufaa ya aliyekata rufaa, umeshazuia account, umemnyang’anya passport, umepeleka maaskari pale kuzuia biashara. Kodi haitafutwi hivyo. Huwezi kutafuta kodi wakati compliance tax payers duniani wanabembelezwa. Dunia nzima ukiwa na compliance tax payer unawapa stimuli wakati wa shida ili waweze ku-survive walipe kodi. Sisi tunachokifanya tunatumia nguvu nyingi ku-meet target, matokeo yake tunawafanya watu wengi wana-exit business, tunafikiri wanaongezeka, lakini watu wanapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri kwamba lazima tutafute namna bora ya kukusanya kodi, namna bora ya kuwalea wafanyabiashara tulionao. Leo na hapa getini wapo, wafanyabiashara walikuwa wanaingiza vitenge; analipa shilingi milioni 125, karudi ghafla anakuta container shilingi milioni 350, ameacha kulipa. Kesho yake atakachokifanya, akilipa anafunga duka, anatafuta machinga, anagawia watu barabarani. Akishindwa anahamia nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuisaidia Serikali kukusanya kodi, lazima Wizara ya Fedha watusikilize, tunazungumza na wananchi. Inawezekana hawana taarifa sahihi. Biashara zinakufa na watu wana…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga, lakini acha nikuruhusu. Unasemaje Mheshimiwa?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuongezee Mheshimiwa Kanyasu kuhusu wafanyabiashara wa Kariakoo. Kwa kweli hilo ni tatizo kubwa kwa sababu sasa hivi ma-container mengi sana ya vitenge yako bandarini inapata labda miezi minne au mitano wameshindwa kulipa kodi kutokana na hilo ongezeko kubwa sana la kodi. Kodi imefikia mpaka milioni 400 kwa container moja wakati siku za nyuma walikuwa wakilipa milioni 165 au 160. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanaweka zuio, wafanyabiashara tayari walikuwa wameshaweka order viwandani kule China. Mzigo unafika bandarini tayari kuna ongezeko la karibia shilingi milioni 200 na kidogo. Kwa hiyo, sasa mizigo hiyo iko bandarini mpaka sasa hivi hawajui wafanye nini. Kwa hiyo, mimi naiomba Serikali iangalie jinsi ya kuwapunguzia kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kabisa Taarifa hiyo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wameonyesha na wanaendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze alipoanzia Mheshimiwa Katani, mimi ni sehemu ya majimbo ambayo yanatarajia kufaidika na Mradi wa Miji 28 na mji mmoja wa Zanzibar. Kwanza niseme, kama alivyosema kwamba tumekuwa kwenye matumaini tangu mwaka 2015 na nipongeze juhudi ambazo zimefanywa na Serikali, lakini nipongeze zaidi kwa taarifa ambazo ametupatia juzi Mheshimiwa Waziri kwamba sasa wamefikia sehemu, wamekamilisha taratibu zote za manunuzi na wanasubiri sasa fedha hizo ziweze kufika na waweze kuanza kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja ambalo tunasisitiza hapa, tuliahidiwa kwamba mradi huu utaanza kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha. Sasa juhudi hizo Serikali ndizo wajielekeze nazo kama unaanza mwezi huu, kama unaanza mwezi ujao tunataka kuona wakandarasi hawa wakiwepo site, wakiwepo kwenye maeneo husika ili tupunguze maneno ya kuzungumza kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika kila mkutano unaokwenda unazungumzia pesa za miji 28 na kwa bahati mbaya sana tumeshawapa matumaini wananchi kiasi kwamba wanapomwona mtu anachimba kisima wanashangaa kwa nini unachimba kisima wakati tunatarajia maji kutoka Ziwa Victoria. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri tumemwelewa sana, tuna imani kubwa naye, lakini jambo la msingi mradi huu uanze katika mwaka huu wa fedha kama ambavyo amekuwa akituahidi na ambavyo alituahidi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la pili, mwaka jana tulikuwa, tulipewa pesa kwenye bajeti bilioni 1.1 za maendeleo. Mpaka tunaingia kwenye bajeti hii pesa hizo za maendeleo zilikuwa hazijafika. Mwaka huu pia ametoa fedha bilioni 1.1 za maendeleo, napata wasiwasi sasa kama tunatenga haziendi, tunatenga haziendi, usambazaji wa maji kwenye mji wangu unakuwa hauendi kwa kasi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, nimsaidie Mheshimiwa Waziri, GEUWASA wapo pale Geita Mjini, wakati huo huo kuna RUWASA. Kwa hiyo matokeo yake kwenye kata moja kuna GEUWASA, kuna RUWASA. Unakuta mtaa huu GEUWASA wanapeleka bomba, mtaa huo huo na RUWASA anachimba kisima. Kwenye maeneo, Mitaa ya Manga kuna RUWASA wanachimba visima, GEUWASA amefanya survey ya kupeleka bomba.

Mheshimiwa Spika, nataka kushauri, kama GEUWASA Waziri anawaamini na wanafanya kazi vizuri sana, wametoka kwenye bilioni 50 wamefanya mradi kwa bilioni nne. Waziri awape kazi ya Geita Mjini wasimamie wao, hii confusion ya RUWASA, GEUWASA atashindwa ku-coordinate kwa sababu atakuta hizi pesa ndogo anazozipeleka zina authorities mbili za kusimamia. Kwenye kata moja una RUWASA, kwenye kata moja una GEUWASA sioni inawezekanaje kumaliza tatizo la maji kwa sababu kuna watu wawili wa kuuliza maswali.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awape GEUWASA wasimamie au awaondoe GEUWASA awalete RUWASA wafanye kazi pale Geita Mjini. Hii itamsaidia Waziri kuweza kujua value for money ya kazi anayoifanya, lakini kupunguza maswali. Natamani sana kuona GEUWASA wakipewa kazi ile kwa sababu jana amesifiwa mtu wa DAWASA na mimi namsifia kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini wale GEUWASA katika kila pesa wanayofanya saving wamekuwa wakiongeza usambazaji wa maji pale mjini. Kila saving wanayoifanya wanaongeza usambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda Kasamwa, ukienda kwenye kata za pale mjini zina uhaba mkubwa sana wa maji, wanaojua vizuri matatizo ya maji ni GEUWASA. Sasa kwenye hiyo hiyo unapeleka RUWASA kwenye kata hiyo hiyo unapeleka GEUWASA, utajikuta pesa ndogo za Serikali zinashindwa kutoa matunda yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, pale Geita Mjini ni kilometa kama tano kutoka ziwani, mradi mkubwa pekee wa maji ni Mradi wa GGM walioujenga kwa CSR. Kwa hiyo tuna visima visima vingi, usambazaji wa maji kwenye Mji wa Geita katika taasisi nyingi umekuwa ni mdogo sana. Kwenye Kata za Mtakuja tuna vituo viwili vya afya havina maji. Kwenye Kata ya Mtakuja kuna shule za sekondari mbili hazina maji, tunasomba maji kwa kutumia malori.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wakati tunasubiri huu mradi wa fedha za India naomba sana pesa za maendeleo za kusambaza maji kwenye kata hizi ziweze kutolewa ili hizi kata na Taasisi za Serikali ziache kupeleka maji kwa kutumia malori. Wanaposomba maji kwa kutumia malori inabidi wanafunzi waanze kutumia maji kwa mgao, lita tano kwa masaa 24. Mheshimiwa Waziri unajua wanahitaji kuoga, wanahitaji kufua, kwa hiyo, tunawafanya wanafunzi wetu kuwa wachafu, lakini tunawafanya pia kushindwa kuwasimamia.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Waziri, naamini kwamba Mfuko wa Maji kama alivyosema mchangiaji aliyetangulia ni mdogo na tumepiga kelele sana kwenye Bunge hili ili kuweza kuuongezea pesa, lakini hizi pesa zilizopo tuzigawe vizuri, tuzisimamie vizuri, kwa sababu zina uwezo wa kuleta matokeo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, naomba nikushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri na watendaji wake kwa hotuba nzuri ambayo ameisoma. Kwa mara ya kwanza Tanzania imeweza kuuza dhahabu nje yenye thamani ya dola bilioni tatu na mauzo ya thamani ya dola bilioni tatu ya dhahabu sehemu kubwa zaidi ya 60% karibu 70 ya dhahabu hii, inatoka kwenye Jimbo la Geita Mjini kwenye mgodi wa Geita Gold Mine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili mauzo kama haya ya dola bilioni tatu yaweze kuendelea lazima uchimbaji wa madini ambao kuna mgodi mkubwa kule wa Barrick na mgodi mkubwa wa GGM uwe supported na miundombinu ambayo tumekuwa tukiizungumza. Sasa iko Barabara ya kutoka Geita kwenda Kahama ambayo namshukuru sana Mheshimiwa Waziri amesema ameiweka kwenye mpango wa kuijenga, lakini ametenga bilioni sita kilomita karibu 140. Ni barabara muhimu sana katika mchango wa uzalishaji huu wa dhahabu lakini katika mawasiliano kwa sababu hii ndiyo barabara inayounganisha Mkoa wa Geita pamoja na Mji wa Kahama ambapo magari makubwa yote ya mizigo mikubwa yanayokwenda kwenye Mgodi wa GGM na Mgodi wa Barrick yanapita kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii iliombwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007 na Mbunge anaitwa Mheshimiwa Mabina. Alikaa miaka yake 10 akaondoka, akaja mwenzangu marehemu Donald Max naye akaiomba naye akaondoka, nilikuja mimi mwaka 2015 nimeiomba sasa mwaka 2021 kuna dalili za kuanza kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni maoni yangu kwa Mheshimiwa Waziri barabara hii ina umuhimu mkubwa sana, siyo tu mkubwa kama ambavyo watu wengine wanafikiria, ni kwa sababu ni strategic, hii barabara ina umuhimu mkubwa kutokana na mizigo mikubwa ambayo inapita kwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa GGM, kwenda kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Kakola, lakini kuna Mgodi mwingine mkubwa wa Dhahabu wa Nyanzaga ambao unaanza Sengerema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitisha malori makubwa yenye mitambo mikubwa ukayapitisha kwenye daraja linalojengwa hili daraja halitadumu, ndiyo maana Wabunge wote waliotangulia waliomba barabara hii ya Geita kupitia Kakola kwenda Kahama iweze kujengwa, na ni barabara
ambayo mchango wake kwenye uchumi unaonekana wazi, kama leo tumefikisha dola bilioni tatu. Mwanzo nchi hii mapato makubwa ya forex yalikuwa kwenye utalii, sasa hivi mapato makubwa ya forex yako kwenye dhahabu. Dhahabu kama ndiyo madini tunayoyategemea, matarajio yangu ni kwamba barabara hii itapewa umuhimu mkubwa, tutaweka pesa za kutosha siyo bilioni sita ambazo zimewekwa sasa hivi ambazo naona ni kama vile bado tunafanya upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, jana Mheshimiwa Mbunge mmoja alizungumza kuhusu performance ya ATCL na akasema unaweza kwenda kukata tiketi ukaambiwa ndege imejaa, lakini baadaye ukiingia kwenye ndege ukashangaa ukakuta ndege iko nusu. Sasa jambo hili linafanana kidogo na jambo hili. Tumejenga Uwanja wa Ndege wa Chato, wananchi wanataka kuutumia uwanja huo, lakini ili uweze kutoka pale kwenye uwanja wa ndege kwenda Katoro kwenda Chato kwenda Biharamulo kwenda Geita ni lazima kwenye mipango ya Wizara wakati wanajenga uwanja ule wangefikiria jambo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kwenda China tulipelekwa na Bunge, tukateremka kwenye Uwanja wa Ndege wa Fuzhou, kutoka uwanja wa ndege huu kwenda kwenye mji tunaopelekwa ilikuwa ni kilometa 120, lakini facility zimetengenezwa na wenye uwanja, kuna mabasi pale ya kupeleka wale watu. Sasa mtu anajiuliza nikate tiketi ya laki sita kwenda nikatue Chato, halafu nitafute gari ya kunitoa kilometa 110 kunipeleka Geita au kilometa 100 kunipeleka Chato, haiwezekani! Sasa lazima Wizara ije na mpango wawe na airport shuttle ambazo ni za kwao, ambazo zitarahisisha watu wanaopanda ndege kwenda kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ndege zetu zina bei kubwa sana sababu ni nini? Ndiyo maana haziwezi ku-perform. Bei ya ndege ni sawa na kwenda Dubai. Sasa kwanini tusitengeneze bei ambazo zinafanana na network na nchi yetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, kuhusu Agricultural Trust Input Fund (AGTIF), hiki chombo lazima kifanyiwe maboresho, badala ya kusaidia wakulla kinachangia kuua morale wa kilimo Tanzania. Mfano mkulima amekopa shilingi milioni 40 na amewekewa cummulative interest ya shilingi milioni mbili na total ni shilingi milioni 42 kwa miaka mitano, hapa taasisi inafahamu kilimo cha Tanzania ni cha mvua na masoko hayapo. Lakini mkulima baada ya kulima akipata mazao soko hakuna, yanauzwa au anauza underprice wakati huo AGTIF madai yao yapo pale pale.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa kuwa analima kwa kutegemea mvua, kilimo kinategemea msimu na hali ya hewa. Sasa inatokea hakuna mvua ya kutosha, ratiba ya malipo ya AGTIF ipo pale pale, mkulima baada kuona kilimo hakimlipi atakopa pesa popote kulipia mkopo wote wa AGTIF kwa muda uliopangwa wa miaka mitano mitano, lakini atakutana na riba kubwa ya zaidi ya asilimia 50 ya principal.

Mheshimiwa Spika, hili jambo halikubaliki Serikali kuuza mali za wananchi waliokwisha kulipa principal yote pamoja na interest ya Serikali bado AGTIF wanataka kuuza sababu ya penalt interest ya kuchelewa kurejesha.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali inapokopesha mkulima iwe na backstop follow up kujua situation anayo face mkulima na iondoe kabisa riba kwa mkulima aliyelipa mkopo wote ndani ya muda wa mkataba.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa nafasi ambayo umenipatia.

Mheshimiwa Spika, nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wanafanya na wanaendelea kufanya.

Mheshimiwa Spika, pale Geita Mjini miaka miwili iliyopita tulizindua ujenzi wa substation katika Kata ya Mtakuja ambapo mimi pia nilikuwepo na Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake aliahidi baada ya miezi nane watu wa GGM wataanza kutumia umeme kutoka kwenye ile substation. Substation ile inatoa megawatts 98 na imekwishakamilika nadhani sasa karibu mwaka. Pia katika ahadi zake Mheshimiwa Waziri alisema kwamba Kata hiyo ambayo substation hiyo ipo ya Mtakuja ambayo ipo kilometa mbili tu kutoka makao makuu ya mji itapata umeme kutoka kwenye mradi huo.

Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza leo mradi ule umekamilika, Kata ile ina vijiji 11 hakuna kijiji hata kimoja kimepata umeme. Sasa nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri sijui ilikuwa sio sehemu ya package ya mradi huo, sijui kama mradi huo unaendelea, kwa sababu mpaka leo navyozungumza nashindwa kwenda kuzungumzia ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Mtakuja kwa sababu mkandarasi keshandoka site na wananchi hawajapata umeme mpaka leo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, kata katika Jimbo la Geita Mjini zimechelewa sana kupata umeme katika awamu zote tatu. Nimeingia kwenye Bunge hili nikakuta nchi nzima vijiji 2,000 ndiyo vina umeme leo tunazungumzia vijiji 10,000 lakini katika Jimbo la Geita Mjini kata sita hazijapata umeme mpaka leo. Ukiwafuata TANESCO wanakuambia huko ni REA, ukiwafuata REA wanakuambia huko ni Peri-Urban ukienda Peri-Urban wanakuambia hawana pesa, amekuja mkandarasi wa kwanza, wa pili sasa wa tatu. Wananchi wa Jimbo la Geita Mjini wanakusikiliza Mheshimiwa Waziri, Geita Mjini siyo Mjini pale tuna kata 14 na kata zingine zote ziko nje ya Geita Mjini wanataka kujua wanapata lini umeme; Kata za Shiloleli, Bulela, Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Mtakuja ambako kule kote watu wako wa kufanya survey wamefanya zaidi ya mwaka mmoja lakini umeme haujaenda.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi sijui inakuwaje Mheshimiwa Waziri alikuja siku moja akazindua umeme kwenye kijiji kimoja alipoondoka hakuna tena kwenye kata hiyo kijiji kingine kilichopata umeme leo mwaka mmoja na nusu. Sasa sielewi anapoondoka anasimamisha zoezi la usambazaji wa umeme mpaka arudi tena au inakuwaje?

Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati wa kampeni tumefanya zoezi zuri sana la kutoa umeme mjini kuupeleka Nyanguku na Nyanamilo, mwezi wa saba mpaka leo nguzo zimesimama hakuna kinachoendelea. Ukiwauliza TANESCO wanakuambia subiri Peri-urban inakuja. Kwa sababu ya muda Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha naomba awahakikishie wananchi wa Geita Mjini kata hizo nilizozitaja wanapata lini umeme.

Mheshimiwa Spika, nilizungumzia hapa wakati nachangia kwenye Mpango inawezekana shida iko sehemu moja, leo hii pale pale mjini watu wamelipia umeme wana miezi saba hawajapata umeme. Wanalipia umeme palepale mjini wanasubiri miezi sasa nikasema inawezekana centralization yenu ya supply inachelewesha watu kupata umeme. Kwa nini msitafute mfumo mwingine wewe unazalisha umeme running cost zako ziko constant unahitaji wateja wengi uweze kupata faida inachukuaje miezi saba unafanya biashara hujamuungia mtu umeme na mteja yupo?

Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Waziri angalie vizuri watu wake wa planning na biashara kwa nini hawawezi kutafuta mbinu mbadala, unakaa na wateja 400 wamekulipa hauwaunganishii umeme kila siku unawaambia vifaa hakuna, vifaa hakuna wapi? Kama haiwezekani wewe ku-centralize supply tafuta watu ambao utakuwa na uhakika na quality za vifaa vyako ili mtu anapolipia leo kesho apate umeme. Haiwezekani wewe unazalisha umeme lakini wateja wapo halafu mtu amekulipa miezi sita yupo anasubiri, akienda hapa anaambiwa vifaa hakuna au hiki hakuna, kwa nini wakati source zipo? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tazama vizuri hawa watu wako inawezekana kupata source za vifaa sehemu zingine kwa quality unayoitaka kama wanavyofanya watu wa idara zingine ukaweza ku-supply umeme bila kumchelewesha mteja kwa miezi mingi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe na Mheshimiwa Rais kwa kutoa shilingi bilioni 100 kwa Mradi wa Maji Geita Mjini, mkandarasi yupo, tatizo kwa mwaka mzima sasa hakuna kazi ya kuonekana imeanza kufanyika.

Mheshimiwa Spika, zipo taarifa za kuchelewa kuanza kwa mradi sababu ya fidia ndogo sana ya vibanda vya wavuvi nane na nyumba moja, naomba Wizara ilifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, naomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ahadi yake ya ukarabati wa Bwawa la Kasamwa, aliahidi ndani ya Bunge na wananchi wa Kasamwa wanategemea utekelezaji wa ahadi yako.

Mheshimiwa Spika, umekuwepo mradi wa maji katika Kata ya Bulela ambao awali uliwekwa kwenye bajeti ya maji, Wizara kupitia RUWASA shilingi milioni 510; fedha hizi kwa miaka mitatu sasa bado haujatekelezwa, kata hii ina kituo cha afya, shule ya wasichana ya bweni na josho.

Mheshimiwa Spika, Kata za Nyanguku na Ihanamilo visima vinakauka kiangazi kwa kuwa ni vifupi. Naomba Mheshimiwa Waziri maeneo haya yafanyiwe kazi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Wenzangu waliotangulia kwenye Kamati wamezungumza kuhusu usimamizi wa asilimia 10, nami naomba tu kuongezea jambo dogo kwamba ukilisikiliza unaona ni jambo dogo lakini nataka nitoe mfano wa halmashauri yangu. Halmashauri yangu inakusanya takribani bilioni nane mpaka bilioni 11 kwa mwaka, maana yake inatenga kati ya milioni mia nane na bilioni 1.1 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirudisha miaka mitatu nyuma ukawaambia naomba tuangalie akaunti hii ina shilingi ngapi hakuna hela na wanasubiri maombi mapya ya vikundi, wanasubiri makusanyo ya halmashauri ya quarter hiyo ndiyo wawagawie walioomba. Maana yake ni kwamba fedha hizi takribani bilioni tatu za miaka mitatu nyuma hazijarudi na kwa sababu zilifunguliwa akaunti ya kujitegemea maana yake ni kwamba hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni kubwa kuliko tunavyofikiri na tumeshauri kwenye Kamati, inawezekana watumishi wanaopewa kazi ya kusimamia Mfuko huu, ujuzi na uwezo wa kusimamia mafungu makubwa haya ya fedha hawana. Sasa ni juu ya Wizara kuangalia utaratibu mzuri wa kufanya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili nilizungumza mwaka jana wakati wa briefing kwamba Sheria ya Kodi Na. 332, sehemu ya kumi ambayo inawapa mamlaka TRA ya kukusanya fedha inagongana na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Na. 290 na Sheria ya Serikali za Mitaa Na. 288 na matokeo yake inasababisha wapangaji kwenye majengo ya halmashauri kuhama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili liko ofisini kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sheria hiyo ambayo imezipa mamlaka Halmashauri za Miji, Manispaa na Wilaya kubuni na kuanzisha vyanzo vya mapato imeipa pia Mamlaka ya Kodi ya Mapato kutokutozwa kodi. Sheria inasema kwenye Kifungu cha 6(1) kwamba all assets vested in the urban authority by virtue of this section… zimetajwa pale, anasema ni all moneys derived from any trade, industry, works, services and other undertaking properties owned by the Council, zimeelezwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida inakuja sasa tafsiri ambayo wanakuja nao halmashauri wanasema kwamba pamoja na sheria kutoa mamlaka hayo, nashindwa kuisoma sheria kwa sababu ya muda, wanasema iwapo halmashauri imewekeza majengo makubwa na wameweka wapangaji wao wanakwenda kukusanya kodi kutoka kwa wale wapangaji kwenye kodi ya pango ambayo halmashauri inalipwa. Kwa hiyo, yule mpangaji anapolipa pango la halmashauri asipolipa withholding tax ya TRA wanafunga account.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria yake imeeleza vizuri lakini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu tuliomba ufafanuzi kwenye jambo hili na ikaeleza vizuri ikasema kwamba kwa maoni yao wao wanafikiri kwamba sheria iko clear na TRA hawapaswi kutoza kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwanasheria Mkuu atusaidie, Wizara ya Fedha itusaidie, halmashauri yangu wapangaji wanahama kwenye majengo kwa sababu wanalipa kodi mara mbili. Sisi hatutaki kujua kwa sababu sheria inatulinda kwa sababu tunataka tulipe hela tuliyoelewana nayo, anapotulipa anaambiwa akate hela ya halmashauri na matokeo yake asipolipa anafungiwa akaunti. Hii ni Serikali moja ni lazima tukubaliane, jambo hili kwa nini lifanyike Geita peke yake na lisifanyike sehemu nyingine? Kama ni sheria iwe uniform itangazwe ijulikane.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kama utaniruhusu…

MWENYEKITI: Malizia sentensi ya mwisho.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni jambo la ajira, limezungumzwa vizuri kabisa na wenzangu. Tunaishukuru Serikali imeajiri Walimu 11,000, lakini Wizara ilikuja ikatufanyia presentation, mahitaji ya walimu ni 120,000 wa primary na sekondari.

Kwa hiyo utaona ni asilimia kumi ya walimu walioajiriwa, sasa ukiwa na deficit ya 90 percent ukategemea kutengeneza quality inayofanana na ujue hii 90 percent deficit ipo zaidi vijijini ambapo wale waliopo vijijini hawana access na tuition na mengine lazima utegemee product ambayo haifanani kwenye mtihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili liangaliwe vizuri. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ije na mkakati wa kukuza mawasiliano kutokea vijijini, kwa sasa habari zinazotolewa asilimia 95 ni za mjini pekee, hivyo kuna haja ya kuja na mkakati wa kuupatia umma mzima haki ya kutoa na kupata habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ishugulikie tatizo la waandishi zaidi ya asilimia 90 kufanya kazi kama vibarua, hawalipwi mishahara na wale wenye mishahara hawalipwi kwa wakati, Wizara iunde timu maalumu kupitia kila chombo kujua haki za watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kuja na hoja ya minara mingi nchini, lakini bado matumizi ya minara yanatufanya kuwa analogue siyo digital, sasa hivi nchi nyingi zinatumia satellite, kwa nini tusiwekeze huko kuachana na minara?
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Eng. Ezra na imenifanya kufikiri sana. Hivi huu ni msaada, mkopo, huruma au upendeleo? Kwa sababu unashindwa kuelewa uiweke kwenye position gani?

Mheshimiwa Spika, mimi ninao watoto zaidi ya 100, acha hao waliosoma Msalato; amehangaika kwenye shule zetu huko vijijini, akafanikiwa kupata Division One. Ameomba mkopo mwaka wa kwanza, amekopa; wa pili amekosa, akija kupata, anapata asilimia 30. Sasa swali langu hapa bado najiuliza, huu ni mkopo ambao mtu ni haki yake kupata? Ni huruma, upendeleo au ni zawadi? Maana yake kama ni mkopo, imani yangu ni kwamba kila mwenye sifa ambaye amekuwa admitted kwenye university, na anaomba mkopo kwa sababu atalipa, ndiyo maana ya mkopo. Otherwise tukubaliane hapa, tubadilishe jina la hili fungu

Mheshimiwa Spika, mtu ambaye anaomba kukopa, atalipa. Halafu anayemkopesha, anasema sikukopeshi, nakupa asilimia 10. Je, huu ni mkopo, huruma, upendeleo au zawadi? Tutafute jina ambalo litafiti kwenye hili fungu, badala ya kulipa jina kubwa halafu kumbe hatuna uwezo wa kulisimamia jambo hili halafu tukakuta watoto wengi wanakosa haki ya kusoma.

Mheshimiwa Spika, kuna vijana kama wanne walikuwa wanasoma UDOM. Mwaka wa kwanza wakaomba mkopo wakakosa. Nikamfuata Naibu Katibu Mkuu nikamwomba anisaidie, naye akaniambia nipe majina. Akapeleka kule kwenye Bodi ya Mikopo naye akakosa. Mwaka wa pili wakaomba, wakakosa, wakaacha shule. Mwaka huu tena nimempelea Naibu Waziri kwenye simu yake.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi niko Bungeni, Mbunge mwenzangu nimemwomba awasaidie hawa Watoto, nawajua ni masikini, akaenda na yeye akaniambia waambie wa-appeal, wakimaliza waniambie. Waka- appeal wakakosa. Sasa najiuliza hii means test, ina-test nini? Kama amejaza fomu, imepitia process zote, ni authentic form, lakini bado sifa za kupata hiyo fedha hana.

Mheshimiwa Spika, na kama kweli Mheshimiwa Naibu Waziri alichukua yale majina akapeleka na amethibitisha kwamba wame-appeal na bado na yeye aliwapeleka wakakosa, sasa nilitaka nikushauri, kwanza turudi kwenye Hansard. Tulishauri hapa wakati wa bajeti tukasema, inawezekana kweli kwamba tumeweka utaratibu ambao watu tunajikuta tunashindwa kujua nani anahitaji. Mimi hata unaposema tusomeshe watu wa sayansi peke yake, mimi sikubaliani nayo. Nchi hii haiwezi kuongozwa na watu wa sayansi peke yake. Kuna watu wamesoma sheria, wamesoma masomo mengine, wana haki ya kupata mkopo na wana haki ya kuitumikia nchi hii na wana haki ya kuongoza nchi hii, hatuwezi kusema tuwape wanasayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuweke utaratibu ambapo itakuwa ni haki ya kila mtoto aliyesoma. Bado nashawishika kwamba utaratibu wa kupima vigezo vya kuwapa watoto mkopo, hautusaidii kuwapata watu wenye shida. Mtoto wangu akiomba mkopo, najulikana Kanyasu, utaninyima kwa sababu ni Mbunge. Nina Diwani wangu ambaye mtoto wake aliomba mkopo akanyimwa, kwa nini? Eti Diwani. Hivi Diwani ana uwezo wa kusomesha mtoto kwenye ada ya Shilingi milioni nne? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuunga mkono Mheshimiwa Ezra, nadhani tuna shida ya kuutaza upya mfumo mzima wa ukopeshaji, na pengine inawezekana fedha tunazozitoa tunadhani ni nyingi kumbe siyo nyingi.

Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge lililopita tulipitisha bajeti hapa. Mtoto wangu anasoma Chuo Kikuu cha Mweka, akaniambia baba, hivi mbona ninyi wanasiasa wote ni waongo? Nikamwambia kwa nini? Mmepitisha Shilingi bilioni 500, huwa mnampa nani? Hapa nina watoto karibu 20 hawajapata mkopo. Sasa inaonekana wanasiasa wote waongo.

Mheshimiwa Spika, tufumue upya, tuangalie namna bora ambayo kila mtoto mwenye haki ataweza kusoma.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
The Finance Bill, 2016
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naunga mkono sehemu kubwa ya mapendekezo ya sheria hii lakini naomba tu nitoe ushauri kwenye maeneo machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nilitaka Mheshimiwa Waziri wa Fedha akija atuambie, benki na taasisi nyingi zina riba kubwa sana ya mikopo, ni kodi kiasi gani ambayo Serikali inaweza kukusanya kutoka kwenye riba kubwa hizi ambazo wanatozwa wananchi na zina mchango gani? Kwa sababu naona kama hawa watu wanatengeneza faida kubwa na hatupati mapato yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye Muswada huu wa Sheria kifungu cha 65E mpaka 65N, yapo mapendekezo kwamba hesabu za mtu anayetafiti na ambaye yupo kwenye full operations zinabebana, anapoanza operations akija kwenye uchimbaji gharama zile zinachukuliwa zinahamishiwa huku, matokeo yake huyu mtu halipi kodi. Hapa nina mfano mzuri na kama tukiruhusu suala hili makampuni yataendelea kutokulipa kodi katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano nilikuwa Ngara kule kuna kampuni moja inaitwa Kabanga Nickle, kwa miaka 45 wao wanafanya utafiti na kila mwaka kuna watu pale wako kwenye operations, matokeo yake hizi gharama zote siku moja akija mwekezaji zitaingizwa kwenye kampuni itakayokuja, hii kampuni haitalipa kodi milele. Kwa hiyo, nashauri gharama za utafutaji ziwe tofauti na gharama halisi wakati huu mgodi unaanza operations kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya nchi. Tunao watu katika maeneo kama Geita pale, wameshikilia maeneo wana miaka 20, hawachimbi, hawafanyi chochote kila mwaka wana-renew licence. Matokeo yake gharama hizi za kusimamia maeneo haya watakuja kuiwekea Serikali halafu hawatalipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo nataka kusema ni kwamba halmashauri zetu zina migogoro mingi sana kwa sababu ya wafugaji na maeneo mengi ambayo yalikuwa yanafaa kwa ajili ya kilimo ili halmashauri zikusanye kodi yanatumika kwa ajili ya mifugo lakini mifugo hii ilisamehewa kodi. Naomba kuishauri Serikali iziruhusu halmashauri zitoze kodi kwenye mifugo ili mifugo hii iwe na faida kwa halmashauri. Tunaendelea kuiona mifugo haina thamani, haina maana yoyote kwa sababu tuliisamehe kodi sisi wenyewe. Mtu ana ng‟ombe 5,000 anaonekana ni masikini lakini mtu mwenye nyumba moja anakwenda kulipa kodi. Kwa hiyo, mimi sioni kama hapa kuna proportionality. Naomba sana Serikali ifanye mabadiliko kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, napendekeza kwamba tumesamehe kodi kwenye taasisi za umma hasa hospitali na Mashirika ya Dini, tukasahau kidogo kwamba Waraka wa Elimu wa mwaka 1978 unasema elimu ni huduma. Nataka kushauri Serikali kwenye property tax hapa kwamba shule zingewekewa badala ya kuacha hiki kiwango kikawa kinayumbayumba, kuwaachia TRA na Halmashauri waamue wenyewe, tutafute flat rate kwa ajili ya shule kwa sababu hivi vyombo ambavyo vinatoa huduma, ni taasisi za huduma ili tuepuke watoto na wazazi kuja kulipia gharama hizi kwenye Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na mpango aliouleta. Pia naipongeza Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kusimamia bajeti yetu vizuri ambayo tuliipitisha mwaka wa fedha unaoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, nimeona kwenye taarifa ya utekelezaji tayari mmelipia ndege tano, na katika hizo ndege tano, ndege moja ni kwa ajili ya mizigo. Ninaipongeza sana, na hii inatukumbusha kwamba uchumi tunaokwenda kuupigania ni uchumi ambao hakuna namna, lazima kama tunataka kukuza utalii tuwe na ndege za kutosha. Juzi tukio la kuanguka kwa ndege kule Bukoba, linatupa picha kwamba kama nchi tunapaswa kuwa na a very strong airline ambayo inaaminika na yenye ndege ambazo watu wanapokuja Tanzania wana uhakika nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi tunachangia hoja za Kamati juzi, mchangiaji mmoja alisema anashangaa kuona Shirika limewekeza Bima fedha nyingi compared na Precision Air. Sasa factor namba moja ndiyo hiyo kwamba Shirika letu lina ndege mpya nyingi na pengine ndiyo sababu na tahadhari ambazo zimechukuliwa zinaweza kutufundisha kuwa na Bima nzuri zaidi yanapotokea majanga. Mheshimiwa naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nataka kulizungumza haraka haraka, huko nyuma tulipiga kelele sana kuhusu blueprint na ikazungumzwa sana kwenye level ya juu, lakini hii blueprint nadhani imekomea kwenye level za juu na haijatafsiriwa kwenye halmashauri zetu. Mwenyekiti wa Kikao cha wafanyabiashara kwenye Wilaya ni Mkuu wa Wilaya, halafu DED ni Mjumbe (mtu wa kawaida), lakini DED ndiye anaye-deal na wafanyabiashara. Kwa hiyo, naomba Serikali iiteremshe hii blueprint kule chini ili ikasaidie kutafsiri tulichokiwaza wakati tunaianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuzungumza hapa kwa haraka ni utalii. Kwenye eneo hili nazungumza eneo moja tu. Miaka yote ya nyuma nimeangalia bajeti ya Mheshimiwa Waziri, tumetoka kwenye makadirio ya Shilingi trilioni 41, tumekwenda kwenye Shilingi trilioni 43. Tunahitaji kubuni maeneo ambayo tutapata fedha nyingi. Kuna eneo moja ambalo tunaweza tukalifanya vizuri vikiungana mkono na ndege zinazokuja na huu ni utalii wa mikutano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwenye michango yangu muda fulani kwamba utalii wa mikutano siyo kama wa watu wanaokuja kwenye holiday tourism, hapana. Ila ni lazima tuwe na kitengo cha kufanya lobbying kuvuta mikutano mikubwa ije Tanzania. Bila kufanya hivyo, tutaisikia tu mikutano mikubwa inafanyika nchi jirani, halafu sisi hatuwapati hao watalii tunaowazungumzia. Kwa hiyo, sasa lazima Serikali ifanye jambo hilo na ianzishe sasa kwa bidi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nataka kuzungumza sasa kwa kina kidogo ni uvuvi. Nimeona Serikali imetenga eneo la uvuvi, nami nataka kusema kwamba mpaka leo bado hatujatumia vizuri uwepo wa Ziwa Victoria na bahari. Nilikuwa naangalia takwimu za Wizara, nikaangalia trend ya export ya Nile page, ukiangalia kwenye latest report pamoja na ukubwa wa ziwa tulilonalo, tulipata dola 132,000 ambazo ni takribani kama shilingi bilioni 300 za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jirani yetu ambaye anamiliki asilimia saba mpaka tisa alipata karibu shilingi bilioni 400 hadi shilingi bilioni 500, maana yake hatujatumia vizuri. Baharini, huku hali ni mbaya zaidi. Pamoja na ukubwa wa territorial na maji tuliyonayo yote yale, tuliuza nje thamani ya fedha zisizozidi dola 40,000 na Serikali ikapata kodi ya dola milioni 62; na hizi ni taarifa latest kutoka Wizara yenyewe. Naangalia hapa shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, hatujafanya uwekezaji wa kutosha. Ni kweli Waziri amesema tunatenga fedha kwa ajili ya kujenga meli baharini, lakini it is very scientific kwamba meli ile yenyewe tu peke yake haiwezi kutuongezea mapato. Kwa sababu Meli ambazo zinaweza kutuongezea mapato ni lazima ndani ya muundo wenyewe wa meli mle ndani iwe na miundo ya kufanya processing, kufanya parking, freezing na unapovua samaki unapata bycatch nyingi. Kuwe na mfumo wa kutoa zile bycatches lakini na link ya masoko. Naangalia Serikali inataka kufanya hiyo biashara, itaweza? Tutaweza kweli ku-breach hiyo gap tunayoifikiria? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa na TAFICO, nami wakati nasoma fisheries nilifanya field TAFICO. Kwa nini ilikufa? Ni kwa sababu Serikali ilifikiri ikiwa na meli yake inaweza ikafanikisha kupata mapato ya uvuvi baharini, lakini ni jambo lingine kabisa. Sisi tunge- invest kwenye kuhakikisha kwamba tunapata teknolojia latest ikawawezesha Watanzania ambao wanavua samaki Ziwa Viktoria na baharini, kuwa na teknolojia ambayo ni latest wakaweza kuvua kuhifadhi, ku-process na kutafuta masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alizungumza mtu mmoja hapa juzi kwamba kuanzia Tanga mpaka Mtwara hakuna kiwanda cha samaki. Ukitengeneza meli za Shilingi bilioni 40, ukanasa samaki kule tani 60, utauza raw, utapeleka Soko la Kariakoo, na kadhalika, ili uweze ku-transform fikra za kufikiri tukapata fedha za kigeni. Kwa sababu lazima uwe na viwanda na viwanda havijengwi na Serikali. Tuwe na Kiwanda kikubwa kinachoweza kuprocess Samaki, kinachoweza kutafuta masoko nje; na masoko ya samaki ni very competitive. Sisi kwenye Nile page tunapambana na Kenya, Uganda na Tanzania, lakini always Tanzania bei yetu ni ndogo kuliko hizi nchi nyingine. Kwa hiyo, lazima tufikirie ku-invest peke yake na hizi meli kubwa hakutatusababisha tuongeze mauzo ya nje, jambo ambalo nadhani ni la msingi sana kwenye fedha hizi tunazowekeza, kwamba lengo letu ni kuongeza mapato na kuongeza wigo wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia niseme kwanza naunga mkono hoja. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI kwa hiyo sehemu kubwa ya mijadala hii tumeijadili na tumemshauri Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kama walivyosema wenzangu, naomba pia nitumie nafasi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya hasa kwa juhudi kubwa anazozifanya sasa hivi za kuitangaza Tanzania huko nje. Niliwahi kusema kwenye Bunge hili kwamba tuliwahi kusafiri na Kamati ya Bunge kwenda mji mmoja China, tulipofika hawaijui kabisa Tanzania na wakawa wanashangaa ukiwaambia Tanzania mpaka wa-google waangalie Tanzania iko wapi. Kwa hiyo kwa Mheshimiwa Rais kwenda kwenye vyombo vya kimataifa sehemu kubwa ya watu wasioijua Tanzania wataanza kuifahamu Tanzania, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza suala moja kuhusu umuhimu, kwanza kuipongeza Serikali kuhusu ajira mpya zilizotangazwa, lakini umuhimu wa uwepo wa kanzidata kama ilivyozungumzwa na mchangiaji mmoja jana. Tumeshauri sana jambo hili kwenye Kamati, nataka nitoe mfano kule kwangu kuna Kijiji kinaitwa Mgusu, ili mwananchi wa Mgusu aweze kuhudhuria interview moja Dar es Salaam au Dodoma anahitahi karibu siku saba. Moja atatoka Mgusu kuja kulala Geita na pale atalipa shilingi 20,000, atalala guest shilingi 20,000, atatoa nauli kwenda Dar es Salaam shilingi 50,000, akifika Dar es Salaam siku mbili kabla atakaa guest atalipa shilingi 50,000, 50,000. Kwa hiyo mpaka siku anafanya interview ameshatumia 300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania huyu atafanya interview, ataambiwa hakuchaguliwa atarudi. Kwa hiyo mwananchi, huyu Mtanzania ambaye anatafuta kazi anahitaji takribani 400,000 mpaka 500,000 katika kila interview moja inayotangazwa na Serikali. Ili aweze kupata kazi au asipate kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Lusinde atahudhuria interview zisizopungua 10. Wapo watendaji, Watendaji tu wa Mitaa wameenda mikoa karibu 20 kutafuta utendaji wa mtaa na kila akienda jina lake halimo. Vile vile zinatangwa ajira hapa TRA wanatakiwa 1,000 wanaomba 10,000 na wote 10,000 wanaitwa, yakisomwa majina hayumo. Inatangazwa Uhamiaji, wanatangaza nafasi 400, wanaomba na kuitwa 8,000, yakisomwa majina hayumo. Matokeo yake huyu mtu anayekuja kwenye interview Uhamiaji amehudhuria interview karibu 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi nchi hii haiwezekani mimi niliyefanya leo interview nikabaki kwenye database kwa miaka miwili au mwaka mmoja. Jibu la Wizara ni kwamba wanafanya kwa miezi sita, miezi sita haitoshi Mheshimiwa Waziri anao mfano, tumefanya interview mwezi wa 11 za TRA juzi wametangaza zingine, miezi minne, lakini wameita watu wote hawajaita ambao walifaulu. Ukiangalia kwenye orodha walikuwa wanataka watu 400, walifaulu zaidi ya watu 2,000. Matokeo yake ni nini? Kila unapoita zinazokwenda kuajiriwa ni zile fresh mentals. Kwa sababu mtu akitoka chuoni anaweza kujibu maswali ya interview vizuri kuliko mtu aliyemaliza mwaka juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe mfano, mimi ni Mhasibu na wengi humu ni professionals, tukichukuliwa leo kwenda kwenye usaili, kozi uliyosomea unahitaji mwezi kujiandaa, lakini hutajibu sawa na mwanafunzi aliyetoka chuoni jana. Matokeo yake ni nini? Aliyemaliza chuo mwaka 2017, 2018, 2019, 2020 anachanganywa kikapu kimoja na wa mwaka huu, anayefaulu ni wa mwaka huu, wa mwaka jana anabaki mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niiombe Serikali kwa sababu nina uhakika hatuna first in, first out, wanaohudhuria kwenye usaili wakifaulu wawekwe kwenye kumbukumbu tuepuke kuwa na mtu anastaafu kabla ya kufanya kazi, amesema hapa Mheshimiwa Lusinde. Hii inatokeaje huko nje, kwanza tuna shida moja tumeweka carders nyingi kwenye Universities ambapo sina uhakika kama kuna research imefanyika kuangalia ni kozi gani ni muhimu. Mwingine kasoma sijui public sijui nini, mwingine sijui public nini, kwa hiyo huko mtaani watu wana vyeti vingi, hakuna ajira, hakuna kazi, kila akisoma tangazo la ajira kozi aliyosomea haimo. Waliojaa mtaani huko Procurement, sijui Uhasibu, sijui nini, public sijui, lakini akisoma ajira hayumo, matokeo yake wanaotangazwa hayumo, wanaoajiriwa hayumo, miaka 45. Ndiyo maana mwaka jana, mwaka juzi tulijikuta kwenye uchaguzi wa CCM Jimbo moja wamechukua fomu watu 60 asilimia 80 walikuwa ni graduate hawajapata kazi. Ushauri wangu hapa kwa Mheshimiwa Waziri, nafahamu alilichukua jambo hili, tuwe na hii kanzidata, mtu akihudhuria interview mara moja tu-communicate, tumuulize bado una interest na kazi hii. Kama kazi hiyo hana interest nayo hatuna sababu ya kumsafirisha tena kumleta Dodoma, inakuwa ni kero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wote unaowaona wanakuja Dodoma kufanya interview Wabunge tunachangia nauli. Sasa nataka tujiulize, una watu 20 wanakuja hapa, wakifika wanakwambia sisi tumemaliza interview hatukuchaguliwa wote, tunaomba nauli ya kurudi nyumbani, unatoa wapi pesa hiyo? Naomba jambo hili lichukuliwe serious sana, lakini tufanye utafiti kuangalia soko la ajira nchini limekaaje ni ajira zipi ambazo tuhamasishe watu wasome. Watu wanasoma wanamaliza hawana pa kwenda, wanadaiwa mikopo na tumetunga Sheria hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili, tumeiona PCCB, ipo kwenye Kamati yetu, tunawapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya. Nataka kujiwekeza kwenye jambo moja tu, wakati wa uchaguzi PCCB ni very active na inakuwa very, very active kwa Wabunge walioko madarakani. Sasa huwezi kumaliza rushwa kwa kumvizia mtu mmoja unayemjua peke yake. Nilishuhudia uchaguzi ulioisha kila unapokwenda wewe upo monitored lakini mko 40, wale wengine hakuna anayewatafuta. Sasa tuwe na utaratibu, tuna vyombo vingi, wagombea wanajulikana, kama wapo watu wanataka, kwa mfano ukiangalia kuna nchi ambazo wagombea wanajulikana, waanze kufuatiliwa mapema. Ukimsubiri mtu siku ya uchaguzi alishamaliza kampeni, utafanya kazi ya zimamoto na utajikuta siku moja umepata Viongozi wote hawana sifa kwa sababu wameshinda kwa rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninaomba pia kutumia nafasi hii kusema ninaunga mkono hoja, lakini kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Spika, mimi labda nianze kusema tunafanya vizuri sana na CSR kwetu hasa Jimbo langu la Geita Mjini, lakini pia tunafanya vizuri sana na local content kwa hiyo ni vizuri kule ambako bado wanapata shida wakaja kujifunza namna ambavyo tunafanya na hasa kwenye local content namna ambavyo wakulima wameshirikishwa katika maeneo mbalimbali ya Saraguro na Mgusu kwenye kushiriki kuhudumia mgodi, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Mheshimiwa Waziri ulifanya ziara Geita na kwenye ziara hiyo tulikuwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa, ulipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi wa Geita na Mheshimiwa Waziri naomba ni-quote sehemu ya hotuba ya Ndugu Paul Young alipokuwa kwenye World of Engineers huko Australia alisema ‘‘Mining sustainably within a community should provide relief from poverty, hunger and safety hood for local communities, this is not considered to be charity, it is about being a part of a community good health and educational aspiration’’ na akamalizia kusema ‘’however extraction of metals and mining of industrial minerals must be done sustainably, this means giving consideration to people, the environment and the economy, human aspect including heath, social and cultural element’’.

Mheshimiwa Spika, ipo shida nimelazimika ku-quote haya maneno ili Mheshimiwa Waziri aweze kunielewa. Ilikuja ziara ya Mawaziri wanane Geita, wananchi wakazungumzia mgogoro wa miaka 20 karibu na tatu kwa wananchi ambao wanaishi kwenye vigingi na mipasuko, Mheshimiwa Rais wa sasa akiwa Makamu wa Rais alishatoa maelekezo suala hili lishughulikiwe, Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli alitoa maelekezo, Mawaziri wote tangu Profesa Muhongo na Mawaziri wengine na Mheshimiwa Biteko alitoa maelekezo ishughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa mitaa karibu saba wanaishi kwenye mgogoro wa mgodi wa vigingi kwa miaka 23 na matokeo yake wananchi hawa wanaishi kwa umaskini mkubwa kwa sababu Serikali imeshindwa kufanya maamuzi.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, mitaa ninayozungumzia haina barabara, haina maji, haina shule, haina zahanati hawaruhusiwi kupima viwanja kwa sababu tu eneo wanaloishi ni ndani ya leseni ya mgodi. Maelekezo yametolewa na Serikali, Kamati imetoa maelekezo kwamba hawa wananchi wapimiwe mgodi unakataa. Vimefanyika vikao vya kila namna imeshindikana.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema jambo moja hapa, Mheshimiwa Waziri alizungumza na wafanyakazi wa GGM akasifia Serikali kwamba sasa 95 percent ya watumishi wa GGM wa menejimenti, niseme wameondoa 95 percent ni Watanzania, lakini wafanyakazi walimwambia kuwepo kwa sehemu kubwa ya waswahili kwenye menejimenti kumeongoza matatizo makubwa na urasimu kuliko ilivyokuwa Wazungu. Tatizo hili linakuja kwa sababu Waswahili hawafanyi maamuzi ya kum-favor mtanzania hata kama anaona sheria inaruhusu. Nazungumza hivi kwa sababu malalamiko ya watumishi wa GGM ni makubwa mno na uonevu ni mkubwa kuliko ilivyokuwa zamani wakati Wazungu ni wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wananchi wanayo haki ya maeneo yao, lakini wamekataa wanasema sisi hatufanyi. Tumeshughulika na jambo hili kila mkutano, kila hotuba halifanyiwi maamuzi, namwomba Mheshimiwa Waziri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Muda wake umeshaisha anamalizia sekunde thelathini.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri wapo watumishi pale wa mahusiano ambao wanazuia maelekezo ya Serikali achukue hatua, bila kuchukua hatua hatutafikia suluhu ya wananchi hawa ambao wanailamu Serikali bila sababu ya msingi na sheria zipo wazi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nitumie nafasi hii nami kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwenye Wizara hii na kwa mchakato mzima ambao tumeushuhudia wa kupitia upya Sera ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Geita Mjini Serikali ilikopa takribani bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA na Serikali ikafanya mchakato wote, ikatuletea Mkandarasi Skyway, akaanza kazi. Naamini Serikali ilitumia vyombo vyake kufanya due diligence, na katika mchujo mkubwa ikatuletea Mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa ambazo Mheshimiwa Waziri alizipata wa wakati huo, aligundua kuna kasoro na akasimamisha ujenzi kwa takribani miaka miwili. Amekuja kuruhusu ujenzi kuanza, yule Mkandarasi wa awali akaondolewa.Mkandarasi wa awali akiondolewa, alikuwa anadaiwa na wananchi wa Geita takriban Shilingi bilioni moja na laki saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina tatizo na kasoro za mkandarasi kwasababu Serikali ndiyo iliyomleta. Shida yangu ni kwamba Serikali ilitimiza wajibu wake wa kufanya due diligence, ikaleta mkandarasi kwa wananchi wa Geita ajenge Chuo cha VETA kwa fedha za mkopo bilioni 14 halafu Serikali hiyohiyo baadaye ikagundua anakasoro lakini ikawaacha wananchi wa Geita wakiwa na madeni wanadai bilioni 1.7 ikabadilisha mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya juhudi nyingi nimezungumza na Waziri aliyekuwepo, nimezungumza na Waziri Mkuu, nimezungumza na Waziri wa sasa, lakini Serikali inakaa pembeni kuonesha kwamba haihusiki. Sasa, mimi nilitaka kutumia hotuba yangu hii, leo Serikali inisaidie kujua wananchi hawa wanalipwa nani? Imebadili mkandarasi aliyekuja amekuta chini kuna matofali, amekuta chini kuna kokoto, chini kuna mchanga ametumia vilevile walivyo-supply wananchi wa Geita lakini Serikali inasema tulikuwa tumelipa mpaka vilivyo chini ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema ukweli, tumekuwa Serikalini, tunafahamu utaratibu, kwamba mkandarasi analipwa kwa ku-raise certificate, certificate ni ya kazi iliyofanyika. Mheshimiwa Waziri umemtuma Naibu Waziri amekuja lakini majibu ni kwamba mkandarasi yule alishalipwa zaidi ya kazi iliyokuwa imefanyika. Sasa wananchi wangu wa Geita wanalipwa na nani? Wanadai zaidi ya bilioni 1.7; mkandarasi amebadilishwa huku chuo kikijengwa kwa force accounts.

Mheshimiwa Naibu Spika, sioni ni kwa namna gani Serikali inatakiwa ikae pembeni kuhusiana na suala hili. Sisi hatukumtafuta yule mkandarasi, aliaminiwa na Serikali akaletwa kama Serikali hadai mkandarasi hadai maana yake ni kwamba huyu mtu alikuwa ana guarantee ameweka benki; zipo pesa, kazi ilikuwa kubwa, lazima wananchi wale walipwe. Wananchi wa Geita hawapaswi kuachiwa maumivu hayo kutokana na shangwe waliyokuwa nayo ya ujio wa Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la pili Mheshimiwa Waziri; tulifanyiwa presentation ya Ujenzi wa Chuo cha VETA; kinachojengwa sasa hivi ni majengo tofauti ambapo chini kuna matofali juu kuna fabrics sijui fabricated. Lakini, lengo la Chuo Cha VETA katika Mji wa Geita ni ku- capture soko la vijana wanaomaliza shule ili wafanye kazi kwenye migodi mikubwa inayozunguka eneo lile. Na focus yetu ilikuwa ni kuwa na Chuo cha VETA unique kutokana na wingi wa machimbo ya madini katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika leo baada ya mkandarasi mwingine kuja ni majengo ya aina tofauti, ni kubadilika kabisa kwa kitu kilichokuwa presented pale, na aliyekuja ni kukamilisha tu kama anakamilisha majengo yawepo lakini kazi inayofanyika ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie wananchi wa Geita, kwanza chuo kinachojengwa kiwe ni kilekile kwa mahitaji yaleyale ya ku-capture mahitaji ya soko la vijana wa maeneo yale ambao wanahitaji utaalamu kwa ajili ya madini na hakuna mabadiliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili; awasaidie wananchi wa Geita kuhakikisha kwamba chuo kinakamilika na wananchi wale, kama yule mkandarasi hadai Serikali iwasaidie wananchi wale kupata malipo yao, kwa sababu hawakujipeleka pale ,mkandarasi aliletwa na Serikali kama ambavyo wakandarasi wengine wanaletwa na Serikali haiwezi kuvua wajibu wa kuhakikisha wanachi wake wanapata haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kwa nafasi, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba pia nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii.

Lakini kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na wizara nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya, nawapongeza sana; sisi ambao tumekuwa tukiomba maji kwa miaka mingi tangu Bunge lililokwisha mpaka sasa tunaona kazi kubwa ambayo Serikali inafanya kwa sababu kuna sehemu maji yamefika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Geita Mjini inaaminika kwamba ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi zaidi Kusini mwa Jangwa la Sahara. Sababu za kukua kwa Mji wa Geita ni uwepo wa shughuli nyingi zinazohamasisha watu kuja, za kiuchumi, ikiwemo madini. Ongezeko la watu linaongeza sana uwekezaji; na kwa bahati nzuri sana ni kwamba Mji wa Geita Mjini maji yako km 8 kutoka katikati ya mji kwenda Ziwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nianze kuishukuru sana Serikali. Kwanza katika ukurasa wa 53 Serikali inasema mchakato mzima wa miji 24 umekamilika na kwamba sasa utekelezaji utaanza tunakushukuru sana. tunamshukuru Mheshimiwa Rais tulimsikia siku ya wiki ya maji; na tunaamini kwamba kabla Bunge hili halijaisha Mheshimiwa Waziri tunaamini Mheshimiwa Rais atatuzindulia mradi huo uweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali pia tumepata fedha kwa ajili ya kupanua chanzo cha maji; na naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza sana GEUWASA wanafanya kazi yao vizuri, wanafanya kazi yao vizuri katika Mji wa Geita na kwa kweli wanastahili pongezi.

Sasa tunapanua chanzo cha maji umetupa bilioni moja, tunashukuru sana. Lakini yale maji yanatoka Nungwe; yakitoka Nungwe yanapita Manga, Nyakabale na kwenye Kata ya Mgusu. Kule yanapotoka maji, maji wanayopata ni yale ambayo hayajasafishwa; yanayovuja kwenye bomba ambalo linatoa maji ziwani; kwa hiyo, ili wapate maji safi inabidi maji yafike Geita Mjini halafu yarudi km 8 kule yanakosafishwa, kule hakuna usambazaji wa maji. kwa hiyo Mheshimiwa Waziri pamoja na sifa hizi za GEUWASA nadhani GEUWASA wanastahili kuongezewa fedha ili wapeleke mtandao wa maji na salama kule yanapotoka maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Mji wa Geita ni takribani lita milioni 18 mpaka milioni 20. Sasa hivi tunapata lita milioni tano. Kitakapotanuliwa hiki chanzo cha maji tunaamini kitatusogeza karibu lita milioni 8, bado tutakuwa na gape ya takriban lita milioni 12. Jambo pekee ambalo linanipa faraja ni kwamba utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaanza. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri naomba kuishukuru Serikali, mwaka huu wa fedha unaokwisha tulipata fedha na tumepeleka maji katika mitaa takriban 12; na tumejenga matenki mapya takriban matatu. Sasa nimeona kwenye bajeti yako ya sasa unatupatia fedha kwa ajili ya kuongeza usambazaji wa maji kwenye Kata za Shiloleli na Bulela.

Mheshimiwa Waziri zipo kata zingine ambazo tumetafiti maji ya visima yamekosekana; pamoja na kusubiri maji ya bomba Kata za Nyanguku na za Ihanamilo kila walipochimba visima RUWASA walikosa maji. Sasa niombe, wakati tunasubiri mradi huo ambao utachukua takriban miaka mitatu, wananchi hawa, kama unavyosema mwenyewe Kwamba hakuna mbadala wa maji, waweze kutafutiwa njia nyingine ya kupata maji salama na safi kwa ajili ya maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, ni kwa sababu kila inapofika kiangazi, wananchi wa Kata za Nyanguku na Ihanamilo wanaanza kusafiri kutafuta maji kama vile wanavyosafiri watu wa Mikoa ya nchi kavu kama Shinyanga na wapi huko na matela ya ng’ombe kwenda kutafuta maji kwenye mabwawa; lakini sisi tupo kilomita nane kutoka ziwani. Kwa hiyo naamini kwamba, jambo hili linaweza kutafutiwa ufumbuzi katika kipindi hiki ambacho Serikali bado haijasaini na hatujaanza mkataba huo mkubwa wa kupeleka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri juzi niliuliza swali hapa na ulisema kwamba Serikali itaanza mchakato kwa ajili ya ukarabati wa bwawa la Kasamwa, nashukuru sana nimeona kwamba mchakato huo utaanza. Mji wa Kasamwa ni Mji wa pili kwa ukubwa katika Jimbo la Geita Mjini; tuna watu takribani 25,000 mpaka 30,000. Vilevile ni mji ambao unashughuli nyingi za kiuchumi. Tuna maji ya visima, maji ya bomba ya kutoka Ziwa Victoria hayajafika. Tunashukuru kwenye mpango maji yatafika kwenye Mji wa Kasamwa. Kwa hiyo, ombi langu hapa ni kwamba katika fedha hizi chache ambazo tutapata mtuongezee fedha ili huu Mji wa Kaswamwa mtandao wa maji haya ya visima pamoja na kwamba kuna kisima Kanyala na kuna tenki limejengwa pale maji yawafikie wananchi takriban 30,000 ya huu Mji Mdogo wa Kaswamwa. Kwa sababu huu mji ni mkubwa na kama visima hivi viwili vilivyopo vitaendelea kuwepo, uwezekano wa kiangazi maji yanapopungua kupata shida ya maji ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naamni kwamba kama ambavyo watu wote wamekupongeza; wananchi wa Geita Mjini wana matumaini makubwa na wizara yako na kazi nzuri unayoifanya wewe na Naibu wako. Tunaomba tu Mheshimiwa Rais aturahishie mradi wa Miji 24 ili tuweze kupata maji safi na salama. Nashukuru sana.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nashukuru pia kwa kupata nafasi ya kuchangia. Naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa yake nzuri ambayo ameitoa. Kipekee naipongeza Serikali kwa ujumla, Mheshimiwa Rais na Serikali nzima kwa kazi nzuri ambayo tunaendelea kushuhudia inafanyika kwenye diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulialikwa juzi kwenda kushuhudia uwekaji sahihi wa uwekezaji wa madini; niyaite madini adimu (rare minerals). Hizi ni dalili kwamba tunaendelea kuungwa mkono huko nje na watu wanaendelea kutuelewa; na ni dalili kwamba Wizara inafanya kazi yake vizuri. Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watu wote wanaofanya kazi na Mheshimiwa Waziri na kumpongeza sana Katibu Mkuu mpya kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kielelezo cha kwamba kazi zinakwenda vizuri ni mafanikio ambayo yamefika sasa kwenye asilimia 9.7 ya malengo ambayo yaliwekwa na Serikali na Bunge hili ili kuweza kuchangia uchumi kwenye bajeti ya nchi. Jambo hili haliwezi kufanikiwa kama Wizara haizungumzi lugha moja. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio makubwa ya Wizara hii yanatokana na mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo kwa taarifa ya Wizara, wanachangia takribani asilimia 40 ya mauzo ya dhahabu nje ya nchi. Jambo hili ni kubwa na hatuwezi kuliacha lipite hivi hivi. Kwa nini tumefanikiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanikiwa kuondoa usumbufu uliokuwa unawakuta wachimbaji wadogo; tumeondoa urasimu uliokuwa unasababisha sekta hii haikui; tumefanikiwa kuimarisha na kuongeza masoko ambayo sasa siyo tena jambo la ajabu kusikia kwamba kuna soko kila kona ya nchi hii. Sasa Serikali ina jambo moja tu la kufanya katika eneo hili. Ni kufanya sera yake ya kodi kwenye eneo la wachimbaji wadogo iweze kutabirika na iweze kueleweka. Naishukuru sana Serikali, wanafanya utafiti na utafiti huu utawapeleka kwenye kuamua aina gani ya kodi wafanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema hapa kwamba, fedha tunazoziona kwenye mauzo ya dhahabu ya mchimbaji, siyo faida. Mchimbaji mpaka anafikia kwenda sokoni kuuza dhahabu, investment yake aliyoiweka wakati mwingine ni asilimia 200 ya anachoenda kukiuza. Kwa hiyo, ni vizuri sana tuwe na sera zinazotabirika na zinazoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ili uweze kufikia malengo sasa unayokwenda zaidi ya Shilingi trilioni moja point; aliwahi kuzungumza Mheshimiwa Kishimba, hakuna Chuo cha Wizi, Serikali inafundisha tu namna ya kumdhibiti mwizi, lakini kuna watu wanajifunza namna ya kuiba. Mikakati yote ambayo mnafanya, lazima pia mjue kuna watu wanajifunza namna ya kuiibia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unafahamu, kuna watu wanafanya mkakati wa ku-lower purity ya dhahabu, lakini kuna watu wanafanya smuggling na hii smuggling inatuathiri sisi wenye Halmashauri tunazotegemea kupata Service Levy kutoka kwenye mauzo ya dhahabu. Sasa lazima Serikali nzima ifanye kazi kwa pamoja; vyombo vyote, ili tuweze kufikia malengo haya ambayo mimi nayaona tunaenda kufikia, kwa sababu, tayari tumeanza kukaribisha wawekezaji wengine katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kulichangia, nataka kuishukuru sana Serikali. Tumekuwa na mgogoro wa muda mrefu Geita wa vigingi pamoja na mipasuko. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Shigela. Baada ya kufika Mheshimiwa Shigela amekuja na formula tofauti na Wakuu wa Mikoa wengine. Kwanza ameshirikisha makundi yote kwa kukaanayo, akawashirikisha wawekezaji, baadaye akaunda kamati ambayo imefanya kazi yake. Sina uhakika na taarifa ya Kamati, lakini nina imani kubwa, Kamati ile kwa mchanganyiko wake na muundo wake, itakuwa inakwenda kuleta suluhu ya wananchi wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Mheshimiwa Waziri, jambo hili lifike mwisho. Wananchi walikusikia tarehe 09 Januari, ulitoa miezi mitatu, miezi mitatu imekwisha. Wengi wanaomba namba yako wakupigie ili waweze kujua limefikia wapi, lakini siwezi kuwapa namba, nina imani kwamba utakwenda kusema sasa jambo hili linaishaje. Nani analipwa fidia, nani halipwi fidia na kazi zinaendelea kwa staili gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa sababu umeonesha dalili ya kwamba unataka lifike mwisho. Ninawaahidi wananchi wa Geita kwamba Serikali yao inawapenda na kuwasikiliza, na mwakilishi wao ambaye wamenituma hapa sasa wawe na uhakika kwamba nakwenda kulimaliza suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu; tulifanya mabadiliko ya sheria hapa kuhusu local content. Naomba kuipongeza Serikali; imefanikiwa sana kwenye utekelezaji wa local content. Ni miongoni mwa halmashauri ambazo mtu akitaka kujifunza namna ambavyo local content inasaidia kukuza uchumi wa wananchi aje ajifunze Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru sana GGM, ninawapongeza katika maeneo yote. Kwenye michezo nadhani mnafahamu habari ya Geita Gold. Tunayo timu nzuri, tumepandisha timu nyingine ya wanawake, Geita Gold Queens, ambayo na yenyewe tunawashukuru sana Geita Gold kwa sababu bila mchango wao hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru Geita Gold kwa sababu local content imesaidia sasa wananchi wa Geita wanaweza kushiriki kwenye uchumi mkubwa ambao ni uchumi wa madini. Sasa…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kanyasu.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, dakika moja.

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; Twiga Mining pamoja na Geita Gold na mashirika mengine, kwa mfano Twiga Mining wameweka middleman pale katikati ili uweze kufanya biashara na mgodi, inawaongezea gharama wafanyabiashara. Tunashukuru kwa nafasi hiyo lakini tunaomba tupunguze huo urasimu ili kusaidia wananchi wengi kushiriki kwenye uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, naomba nianze kwanza kwa kusema ninaunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwa kweli pia maandiko mbalimbali ambayo Mheshimiwa Waziri amewasilisha na nimemsikiliza vizuri kwenye hotuba yake ambapo kuna wakati alikuwa anaacha kusoma anatuelezea anachokifikiria kufanyika. Ninampongeza kwa maoni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba uvuvi mpaka leo unachangia pato la Taifa kwa asilimia 1.8. Ukitazama namna ambavyo nchi yetu imebarikiwa, namna ambavyo tumezungukwa na maji karibu nchi nzima ukianzia Ziwa Victoria, ukaenda Tanganyika, ukaenda Nyasa, ukaenda baharini na vibwawa vidogovidogo vilivyopo katikati ya nchi, ungetamani kuona mchango wa sekta ya uvuvi unafika asilimia 10 kwenye Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na tumefeli wapi; amezungumza hapa mzungumzaji aliyetangulia kwamba sisi tungeweza kuwa tunaongoza katika mauzo lakini pia tungeweza kutawala soko la Maziwa Makuu. Jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Waziri nataka kukuhakikishia kwamba tumefeli; kwanza, tumekuwa na usimamizi mbaya wa rasilimali hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini sasa hivi tunazungumzia kushamiri kwa uvuvi haramu; miaka michache nyuma tulifaidika na takwimu za mauzo makubwa nje – amesema Mheshimiwa Mwijage – tukafaidika na takwimu za ongezeko dogo la samaki Ziwa Victoria, kwa sababu tulitumia nguvu kubwa ya operesheni kwenye kufikisha ujumbe wa namna ya kutunza maliasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa matokeo ya operesheni ni yapi. Kwanza, tulipata ongezeko la muda la mauzo ya samaki nje, tukaongeza mapato kutokana na faini kwa sababu tulikuwa tunapiga sana faini. Sasa matokeo yake ni kwamba wavuvi wakubwa wote waliokuwa Ziwa Victoria wakaacha kufanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na wanapoacha kufanya hiyo kazi kutokana na kufilisika – na kwa kweli walifilisiwa na Serikali, maana yake ni kwamba wanaokuja ni wavuvi wadogowadogo ambao hawana uwezo wa ku-access gharama kubwa ya zana za uvuvi na lazima watavua kwa uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hatuwezi kuja leo tunashangaa kupungua kwa samaki, genesis yake tuliitoa huko. Tulipaswa kuja na programu ambayo itadumu ya kudhibiti uvuvi haramu na kuhakikisha kwamba tunalinda maliasili katika maziwa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukaja na zimamoto ya operesheni ambayo ninafikiri Mheshimiwa Waziri usipozingatia ndio utakuwa ushauri wako utakaopewa na wataalamu, na operesheni iliwafaidisha zaidi watu wako wa chini ambao walitumia operesheni hiyo kuonea watu na matokeo yake watu wote wakaona uvuvi siyo kazi ya mtu mwenye akili timamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mheshimiwa Mwijage amezungumza habari ya ongezeko la illegal fishing, amezungumzia ongezeko la bycatch. Bycatch kwa nini ni nyingi; ni nyingi kwa sababu watu wa BMU hawafanyi kazi huko chini tulikuwa na BMU zamani na kazi yao kubwa ilikuwa ni kuhakikisha wanamlinda mvuvi wao wenyewe, Wavuvi wenyewe wanalindana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, hatuna wataalam. Ukiangalia ajira za Serikali zote zinazotoka ni kama vile uvuvi tume u-abandon, yaani kama si jambo muhimu. Watu wanasoma kwenye vyuo hawaajiriwi. Unatembea mialo kumi afisa uvuvi mmoja, halafu unategemea kudhibiti Uvuvi haramu, unaudhibiti vipi? Haiwezekani; uvuvi haramu unatoka wapi; ni kutokana na dhana kupanda, wasimamizi hawapo, na ukianzisha operation unakwenda kuonea watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilitaka kushauri; uwepo wa, kuzungungukwa na maji katika nchi yetu bado haijawa baraka, bado sisi tunaona kama vile ni laana. Tunachotaka ukifanye sasa hivi, hakikisha tunapata dhana za uvuvi kwanza kwa bei nafuu, lakini watu wako walioko huko chini waimarishe zaidi kwenye kutoa elimu kuliko kwenye kufanya operation kwa sababu mtu akipata elimu ataambukiza kizazi chake na kizazi kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, na jambo lingine ni lazima to control hizi breeding areas. Maeneo yote ambayo zamani yalikuwa ni mazalia ya samaki sasa hivi yamevamiwa. Hii ni kwa sababu ile operation baada ya operation namna tena mtu anafanya kazi kule ziwani. Mimi nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri ukilisimamia hili samaki watarudi ziwa Victoria, lakini yako mambo ambayo lazima tufanye.

Mheshimiwa Naibu Spika, duniani sasa hivi hawategemei tu mazalia ya samaki ya natural kutokana na uharibifu wa mazingira, ndiyo maana unaona watu wana-invest kwenye cages kwenye uvuvi wa vizimba, ufugaji wa vizimba. Lile Ziwa Victoria na ukubwa wake ukiweka vizimbaa kila kona hatuwezi kuwa na kilio cha samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la samaki liko obvious Tanzania kuna soko la samaki na nje ya nchi kuna soko la samaki. Hatuwezi kuendelea kutegemea kwamba wale wanaozaliwa mle kwa sababu ya asili ndio tuendelee kuwategemee kuuza nje haitawezekana. Ukienda nchi zote ambazo ni leading export wa samaki wanatumia vizimba, kwa hiyo weka fedha nyingi hapo. Shida tuliyonayo Tanzania sasa hivi vizimba ni bei ghali sana, chakula cha kuku ni bei ghali sana; lakini kuna urasimu mkubwa kwenye kufikia malengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu ya muda na kwa sababu sitaki kuacha kuzungumza habari ya mifugo, nataka nikushauri hapo kwamba lazima utakapoamua kulisimamia jambo hili huko chini watu wako miiko ambayo wanapelekewa; lazima tuongeze idadi ya staff lakini watu walitumia vibaya sana madaraka yao na matokeo yake tukawa na mafanikio ya muda yaliyopelekea watu wengi kuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni kuhusu suala la mifugo. Nimeangalia takwimu zako za mapato ya mifugo, kwa mtu akikusikiliza ambaye haijui Tanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nianze kwa kusema ninaunga mkono hoja. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri lakini pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuongeza fedha kwenye Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono mapema kwa sababu najua muda hautoshi; lakini nataka kutoa ushauri ambao Mheshimiwa Waziri usiutafsiri kama napinga lakini nataka kuliboresha jambo hili ili liwe na nyama nzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naangalia kwenye takwimu mbalimbali za kidunia, nikaangalia nchi gani duniani inaongoza kwa kuuza nanasi; na nimekwenda huko kwa sababu kwetu Geita tunalima nanasi, na inauza nanasi za kiwango gani na wanunuzi wakubwa ni kina nani.

Mheshimiwa Spika, Costa Rica wanauza nanasi nje zaidi, wanauza tani 2,900,000, na kupitia nanasi wanapata 1.7 USD billion. Anayefatia pale chini ni Philippines, halafu anafuata Indonesia ambaye anauza tani milioni mbili na kitu, ambaye anafata 1.4 billion. Anakuja Philippines. Afrika nzima mtu anayeuza nanasi kwa wingi ni Nigeria, ambaye anauza 1.5 million tones; na katika hapa anapata zaidi ya dola 700,000,000.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nimechukua eneo hili, na ukiangalia sasa kwenye market share Costa Rica anauza asilimia 51 ya mananasi kwenye nchi hizo za Ulaya. Anafuatia Philippines kama nilivyosema na hao wengine. Kwa nini nimechekua takwimu hii? Tuliwahi kutoa ushauri humu Bungeni, yapo mazao ambayo si kipaumbele na hayajawahi kuwa kipaumbele lakini yana uwezo wa kutuletea mabadiliko makubwa kwenye uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi ambazo ninazitoa ni takwimu ambazo kwetu sisi hakuna muujiza. Kinachowasumbua wakulima walioko Geita leo kwa nini hawauzi nanasi nje, ni kwa sababu wanalima matunda ya kula hawajasaidiwa kutafuta mbegu ambayo wanaweza ku- export. Sasa kama tunataka kuleta mapinduzi katika eneo hili, ni mfano mzauri sana Mheshimiwa Waziri ukapeleka block farming katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, nimefanya hii study nikaenda kwenye andiko moja la mtu mmoja wa Nigeria ambaye alikuwa sponsored na Rockefeller; wamegundua kwamba ili waongeze mauzo ya nanasi na mihogo nchini Nigeria na Ghana wakaingia kwenye block farming. Walichokifanya wao, cha kwanza umefanya wewe, umetafuta ardhi, thats fine; walichofanya cha pili wakatafuta credit facility, nani atakwenda kutoa credit pale, na hii ni MOU ya mkulima na yule anayeenda kutoa fedha. Utapewa fedha unayoitaka kwa MOU. Lakini la tatu huyo anayekupa credit amekuwa connected na masoko, kwa hiyo hautakuwa na tatizo na soko.

Mheshimiwa Spika, sasa sisi ambacho tungeweza kukifanya, wakulima wa nanasi, hao ambao ni kama neglected, wanalima madawa sijui ya kienyeji sijui nini, na Ulaya wanapokea nanasi zilizokaushwa sio nanasi mbichi. Sisi tunashindwa wapi hapa? Miaka michache nyuma avocado ilikuwa inalimwa nchi nzima lakini ilikuwa haiuzwi nje. Kuna mtu akaleta specie ya avocado akajua hii specie ina soko Ulaya akaenda Ulaya, leo tumeangalia kwenye takwimu Mheshimiwa Waziri, nchi inakata kata deni kutokana na mauzo ya avocado. Kwa hiyo kinachosumbua sasa ni aina ya specie ambazo ziko sokoni.

Mheshimiwa Spika, na wakulima wetu wala hawahitaji nguvu nyingi. Nimesema hapa kwamba kule Geita wako tayari, Costa Rica wanalima hekta 40,000 peke yake, wanapata 1.7 bilion USD. Kule Geita ambako mimi natoka, takribani Jimbo zima la Musukuma wanalima nanasi. Kwa hiyo you could make it a block farming halafu wewe ukapeleka credit ukapeleka mbegu inayopuzwa Ulaya, ukapeleka wanunuzi wa masoko yale, uka-transform kile kilimo kuwa kilimo cha kisasa tukapata fedha nyingi kuliko hata fedha ambazo zinapatikana kwenye pamba na mazao mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, Mheshimiwa Waziri alinifata nilipochangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, akaomba ku-share na mimi jambo hili. Sina mgogoro na block farming, shida yangu ni moja tu. Tanzania leo, amesema hapa muhamasishaji mmoja, almost 30 percent ni watu chini ya miaka 18. Ukiwapa watu leo wenye miaka 25, ukawapa hati ya miaka 60 hao wenye miaka 18 ten years to come wenye miaka 15 watakuwa na miaka 25. Kama project unataka iwe sustainable walichokifanya Nigeria wamewa- connect hawa na wale wanunuzi na wakawapa hekta mbili za mkataba. Na yule anapopewa ana-access kwenye fedha, anauza, baada ya miaka ile anayopewa kimkataba ame-graduate anakwenda kufanya kutafuta mashamba kwenye maeneo yake mengine.

Mheshimiwa Spika, sisi kwa population tuliyonayo hawa tulionao wote wakifikia huo umri wa kuhitaji kukopeshwa, kama hii ndiyo source ya ajira, na mimi nafurahi; Mheshimiwa Waziri kwa sababu unataka kutengeneza ajira 1,500,0000; market seekers wa kila mwaka wanaotafuta kazi wanaoingia kwenye kutafuta kazi kila mwaka wanafika takriban 800,000. Sasa ukianza kumilikisha ardhi kwa miaka 60 nataka nikwambie after hii miaka mitatu hautakuwa na ardhi ya kumpa mtu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ziko nchi Jirani tunazo, ardhi nzima inamilikiwa na watu. Nahofia tunaeza kuelekea huko. Kuna nchi ambayo ukienda hata kupata heka moja hakuna, Serikali haina ardhi. Sasa mimi umeshanipa miaka 60 na kuna mtu anategemea kweli, Kanyasu atakuwa mkulima maisha yake yote, yaani mimi nina miaka 25 leo umenipa hati nilime miaka mitano, halafu niendelee kuwa mkulima hadi nifikishe miaka 50 ambayo ninayo leo, kweli? Inawezekana? Zamani mimi nilikuwa mvuvi, nimesomea uvuvi, nime-practice uvuvi miaka 10 nimeacha sasa hivi Mbunge.

Kwa hiyo, hao mliowapa miaka 15 ijayo wamejaa humu Bungeni, watakuja kuwa Wabunge. Sasa una uhakika gani kwamba una mkataba hawatabadili kazi? Mheshimiwa Waziri ni ushauri tu lakini naunga mkono. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuitendea haki Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kwa hiyo sifa zote ambazo Mheshimiwa Rais anapewa na Mheshimiwa Waziri anapewa, naweza kusema ninaziishi kwa sababu nipo kwenye Kamati hii. Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima wanazingatia vizuri ushauri wa Kamati na ushauri wa Wabunge. Kwa hiyo, ninachoweza kusema hapa tu ni kwamba ninaipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo inaendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika Nyerere Hydro – Electric Power, tumefika Chalinze tumeona kazi kubwa inayofanywa lakini tumepata taarifa ya kina kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa TANESCO, kuona namna ambavyo Tanzania ambayo inaandaliwa kuwa na umeme wa uhakika kazi ambavyo inafanyika. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa na timu nzuri. Jambo moja tu la msingi hapa Mheshimiwa Waziri tunacho chombo kwenye Wizara yako kiko EWURA (Consumer, Consultative Council) natamani sana ukiongezee nguvu.

Mheshimiwa Spika, kadri unavyoongeza kupanua huduma za umeme, matumizi ya gesi na kadhalika, wananchi wanahitaji chombo cha kuwatetea, wanahitaji chombo cha kutatua migogoro yao kabla haijawa mikubwa. Utakubaliana na mimi kwamba yamekuwepo malalamiko mengi ya utumiaji wa gesi, wengine mara gesi haitoshi, mara gesi iko hivi mara umeme uko hivi. Lazima chombo hiki kipewe nguvu, kipewe fedha kizunguke nchi nzima, kitoe elimu ili kuwafanya Watanzania wawe salama, naomba nikupongeze sana kwa juhudi kubwa ambazo zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo mawili mahsusi. Kwanza, Jimbo langu la Geita Mjini, limekuwa kwenye kuchelewa kupata umeme kwa takribani sasa tangu awamu ya kwanza ya REA, awamu ya pili sasa tunakwenda lot ya pili phase three kwa nini? Kwa sababu tuko Mjini tunayo ahadi ya peri-urban. Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa juhudi kubwa ulizofanya, ulikuja Geita tukaenda Kata ya Burera ukazungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wakakufurahia sana, ukawaahidi umeme utawaka itakapofika mwezi wa 12 mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sauti ya unyenyekevu nimefika kwenye banda pale nimeona mipango inaendelea, nimepata taarifa wameanza kuchimba nguzo lakini umeme haukuwaka Desemba. Mimi ni imani yangu kwamba baada ya bajeti hii kupita speed tuliyoiona kwenye mabanda yale itakwenda kufanya kazi yake wananchi wapate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe Mheshimiwa Waziri Jimbo la Geita Mjini mitaa 32 bado haijapata umeme na hiyo ndiyo iko kwenye peri – urban, vijiji 10 ambavyo kati ya 18, vinane vimepata umeme, kumi bado ndiyo kazi inayoendelea. Kuna maneno mengi kwamba bado Mkandarasi hajapitishiwa, sijui Mkandarsi bado kuna ushauriano, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama tunaanza mchakato wa kupeleka umeme kwenye vitongoji, lakini tuna vijiji na tuna mitaa yenye tafsiri ya vijiji ambayo haijafikiwa na umeme tutakuwa tunawaacha watu wengine nyuma, tutakuwa na double standard kwenye nchi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kwa kuwa hivi ni vijiji isipokuwa vile viko Geita Mjini, sijui Bukoba Mjini, huyo Mheshimiwa Naibu Waziri ana kesi kama ya kwangu. Ana vijiji na mitaa haijafikiwa umeme kwa sababu peri-urban haijaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama inawezekana tufike kwenye vijiji vyote na mitaa yote, halafu tuende kwenye vitongoji. Ni jambo jema Mheshimiwa Waziri umetushirikisha tutachagua vitongoji ambavyo vina uhitaji wa umeme na Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana kwa jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine la pili Mheshimiwa Waziri mimi ni Mjumbe kama nilivyosema wa Kamati ya Nishati na Madini. Tunakupongeza sana kwa kuchukua deni lililokuwa la TPDF na kuligeuza kuwa mtaji, jambo jema sana. Wanaomba hawa watu na siyo tu wanaomba, ni maoni ya Kamati kwamba, Serikali inadaiwa fedha nyingi sana na fedha hizi ni Serikali yenyewe labda ufanye kama ulivyofanya kwenye deni lile Wizara, zile zikatwe juu kwa juu badala ya kuilipa TANESCO, ili TANESCO waweze kuwalipa TPDF kwa sababu visima ambavyo wanachukua vingine inavyoonekana vimeanza kupungua capacity na kwa nini? Ni kwa sababu pia hata uwezo wao wa ku - service kwa muda, kwa sababu wanakuwa hawana liquid umekuwa mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi kwamba speed yao ya kusambaza hata gesi ambayo ni domestic ni ndogo, kwa nini? Kwa sababu hawana pesa ya kutosha. Sasa kulichukua deni ni jambo moja kuwa na cash mkononi ya kuzunguka ni jambo jingine, Wizara yako iwasaidie kulipwa pesa hizo. Serikali iko humu, bilioni mia tatu na kitu kwa TANESCO ni pesa nyingi zingeweza kusaidia pia maeneo mengine tukapunguza madeni tukawahisha huduma kwa wananchi. Wananchi kwa kweli wanaipongeza Serikali kwa uwekezaji lakini wanasikitika wanapoona umeme upo unapita lakini TANESCO haina uwezo wa miezi miwili, mitatu kumuhudumia mlaji ambaye yuko tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo umewekeza umeme una Megawati 1,800 unatumia 1,400 plus, una surplus ya 300 though haiko very stable, lakini una watu wanataka umeme wakupe pesa ili uweze kujiendesha halafu unachukua miezi minne, mitano haujawapelekea huduma, mimi nadhani hili jambo siyo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maoni tofauti kwa mfano, Mheshimiwa Waziri tunafahamu zamani vifaa vilikuwa vinanunuliwa madukani watu wanafungiwa umeme kwa bahati mbaya hapa katikati pakawa na vitu feki. Pengine mngelikuja na mkakati mwingine wa kuangalia mkawa na quality assurance, mkatafuta vendors, mkaondoa kabisa tatizo la mtu kusubiria mpaka vifaa viende. Unakuta kuna sehemu watu wamelipia umeme wanaanza kushindana na vishoka sasa kutoa rushwa ili waweze kupata huduma ya umeme. Mheshimiwa Waziri nadhani jambo hili siyo jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kule Geita kwangu kuna wachimbaji wa madini. Wachimbaji wa madini wanatumia gharama kubwa sana kusukuma mitambo na kutoa maji kwenye mashimo. Ikikupendeza ungemteua mtu aka-deal na hilo eneo tu, kwa sababu wapo watu kule Nyarugusu, kule Nyakabale, kule Ngusu wameomba umeme, wanataka umeme kwa ajili ya kusukuma mitambo, wanachukua muda mrefu sana na gharama ya uendeshaji inakuwa kubwa, hawa ni watumiaji ambao Mheshimiwa Waziri watakuongezea kipato kikubwa sana hata kuliko watumiaji wa ndani wa umeme wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwa sababu hili ni jambo la kiuchumi nakupongeza sana kwa ku-diversify pia uwekezaji wa umeme, leo tunapokwenda kuanzisha Bwawa la Umeme la Malagarasi tukawa na bwawa la umeme la Julius K. Nyerere, tunaifanya nchi iwe na mitandao ya umeme iliyogawanyika ambayo ni vizuri kuisalama. Wenzetu waliliona hao wa Ukraine kama wangelikuwa wana chanzo kimoja cha umeme na yule jamaa anayewapiga leo wangelikuwa giza, lakini ukipiga mtambo mmoja unawaka wa kaskazini, unawaka wa kusini, unawaka wa magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri kuwa na sources nyingi za vyanzo vya umeme, uwekezaji mwingi ili kusudi siku moja nchi isije ikaingia gizani kwa sababu tu Mwalimu Nyerere Hydroelectric Power imeshindwa kufanya kazi au gesi imeshindwa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana.(Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwanza naomba kusema naunga mkono hoja zote mbili; hoja ya kuibadilisha Kigosi kuwa Hifadhi ya Misitu na hoja ya Kurekebisha Mipaka ya Ruaha.

Mheshimiwa Spika, nimepata bahati ya kufika Kigosi na ukubwa wake wa hizo takribani square kilometer 8,000 lakini nimepata bahati pia ya kufika Ruaha. Nafahamu mateso waliyokuwa wanayapata wananchi wa vijiji vinavyozunguka Ruaha hasa inapotokea mgongano wa kifikra kati ya Wahifadhi na wananchi na lengo ni jema.

Mheshimiwa Spika, kazi tuliyowapa wahifadhi ni kuhakikisha kwamba maeneo tuliyowapa yanalindwa, lakini pia lazima tukubali kwamba kutokana na nchi yetu kuendelea kuongezeka kwa watu imekuwepo haja ya watu kwenda kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ambako kweli ndio maeneo yenye rutuba na maeneo yenye uzalishaji wenye uhakika kwenda kutafuta maeneo ya kilimo. Kwa hiyo kuridhia kurekebisha mipaka ni kuepuka kesi zisizo za lazima, lakini pia kuridhia kurejesha Pori la Kigosi kwa TFS ni kuruhusu shughuli zingine za kiuchumi ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo ambayo Kigosi ilikuwa inazunguka wanarudishiwa maeneo yao kwa sababu historia inaonesha mwaka 1983, Serikali ndio ilibadilisha kuwa Game Reserve na baadae imekuja tukabadilisha ikawa National Park na Sheria zetu zilivyo hazitambui sana kwamba wananchi wa asili ya maeneo haya walikuwa wanafanya kazi gani.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa asili ya maeneo yale ambao kwa asili, maeneo yale ninayoyazungumzia yana watu wa Makabila ya Wasumbwa, Wasukuma, Waha, Wanyamwezi na Wasubi. Hawa ni wafugaji wa nyuki na walinaji wa asali. Kwa hiyo tulipobadilisha sheria tukaweka kizuizi na hii ilikuwa ni kazi kubwa ya kiuchumi na ukiangalia ndio maeneo ambapo Wizara pia ilipeleka Viwanda vingi vya asali kwa ajili ya ku-capture soko la China. Kwa hiyo tulikuwa tumezuia kazi za kiuchumi lakini tulikuwa tumetengeneza mradi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa haiwezekani kabisa watu wakaacha kwenda, walikuwa wanaingia na wakiingia wanakamatwa, kwa hiyo tukajikuta tumegeuza makosa kuwa chanzo cha mapato na kwa sababu watu hawawezi kuacha ndio kazi ya uchumi walikuwa wanaingia. Kwa hiyo maamuzi haya ni maamuzi sahihi, naomba kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na Kamati kwa kuridhia jambo hili liweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, tunapobadilisha kuwa msitu, hatumaanishi kwamba tunakwenda kuua uhifadhi, bado TFS wana wajibu wa kuendeleza ikolojia ya eneo lile kwa sababu hata TFS wana utalii unaitwa eco-tourism ambao unahusisha utalii wa ikolojia na katika maeneo yote yaliyohifadhiwa wanyama wamo. Kwa hiyo bado TFS wanaweza kulilinda eneo hilo likaendelea kuwa na wanyama na likaendelea kufanya utalii, lakini likaendelea kuruhusu wananchi kufanya kazi ambazo hazina athari kubwa kwenye misitu.

Mheshimiwa Spika, wito wangu hapa ni kwamba utaratibu huu uangaliwe pia na maeneo mengine. Nataka kutoa mfano, niliwahi kutembelea Ugala nikakuta kuna mto pale ambao ni mto unao-feed Ziwa Tanganyika. Wakati wa kiangazi ule mto unakauka unaacha mabwawa, yale mabwawa yanakuwa na samaki wengi sana, kwa hiyo wananchi wanavizia kwenda kuvua kwa kuiba, lakini wale samaki wasipovuliwa wanakufa kwa sababu maji yanakauka na wanakufa wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sasa unaona sheria inazuia watu wasiende kuvua samaki, kiangazi kikiwa kikali samaki wanakufa wenyewe, kwa hiyo tuangalie utaratibu ambapo hata ndani ya National Park kama kinachoenda kufanyika hakina madhara kama ni uvuvi wa samaki watu wakavue samaki. Kwa sababu kwa nature ilivyo hata usipowavua wewe watakufa, kwa hiyo jambo hili litufundishe.

Mheshimiwa Spika, la pili, mchango mkubwa wa wananchi kwa maeneo husika. Tunatarajia kwamba baada ya kuwa limerudishwa TFS wananchi wa maeneo yale kwa sababu ni misitu mikubwa watafaidika pia kwenye mazao mengine ya misitu.

Mheshimiwa Spika, nitoe angalizo kidogo, Kigosi ni catchment area kubwa ya Malagarasi…

SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu hicho kisemeo chako ukishika na mkono wa kulia kinazuiwa, kwa hiyo sauti haitoki vizuri. Ukishika na mkono wa kushoto unatusaidia tunakusikia vizuri zaidi.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nilikuwa nasema kwamba pamoja na kuunga mkono nataka kuishauri Serikali mambo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, Kigosi ni catchment area ya Malagarasi ambayo Malagarasi ndio inayotengeneza maji yanayokwenda mpaka Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, tunapoirudisha TFS jukumu la kuendelea kulinda ikolojia ile na uasili wake, lifanyike kama ambavyo lilikuwa linafanyika lilipokuwa chini ya TANAPA.

Mheshimiwa Spika, la pili, Kigosi ni makazi ya wanyamapori na hawa wanyamapori hawatajua kwamba tumebadili Sheria tumewatoa TANAPA, watabaki kwenye misitu na wataendelea kuingia kwa wananchi. Tuliwahi kuishauri Serikali kwamba TFS lazima wajiandae kuthibiti wanyamapori walio kwenye misitu yao. Kuna tembo wa kutosha, kuna simba wa kutosha ambao wakiondoka TANAPA, wakaondoka wale watu wa Game Reserve wakabaki TFS lazima wajiandae kisaikolojia kwamba hawa simba waliokuwa wanazungumzwa hapa wataingia kwenye hizo wilaya zingine. Kwa hiyo lazima jambo hili lifanyiwe uwekezaji wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, la tatu, kuna misitu minene ambayo ndio chanzo cha mvua cha Mikoa ya Kigoma, Geita, Kagera na Tabora. Kwa hiyo aina yoyote ya matumizi lazima iwe rafiki kulinda ikolojia hii kwa sababu tunapofurahia mvua lazima tujue mvua inatoka kwenye misitu.

Mheshimiwa Spika, la nne, niipongeze kwa kweli Wizara, eneo lile tuna hifadhi nyingine nyingi. Tunazo Hifadhi Burigi Chato, Rubondo, Ugala, kuna Game Reserve ya Moyowosi, sasa ni muda wa kuwekeza kwa nguvu kubwa Ugala kwenye National Park ili watalii waweze Kwenda. Nasema hivi kwa sababu hatuwezi kujisifia kwamba kuna watalii kumi tu walienda, hapana, lazima tujue kwa nini watalii hawaendi. Kama watalii wanasafiri kwenda kuangalia magofu Vietnam na wapi, tuwalete Ugala ili waweze kufaidika na ikolojia iliyopo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kusema naunga mkono hoja. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na mapendekezo mengi na kwa kuchukua maoni ya Waheshimiwa Wabunge; na hasa katika maeneo ambayo tuliyasema kwa hisia kubwa. Kwa hiyo nianze kwa kuunga mkono hoja lakini nianze kwa kuipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanya kwenye Jimbo langu la Geita na Mkoa mzima wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu kubwa hapa ni kushauri namna ya kutafuta fedha halafu tukatumie fedha ambazo tumeziomba kwa miezi mitatu. Mimi sasa nianze na eneo la madini. Kwa mujibu wa taarifa yako eneo la madini limekuwa kwa takribani asilimia 10.6; haya ni mafanikio makubwa sana. Lakini nina mapendekezo na ushauri katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza niishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye maeneo ya CYP. CYP tulizonazo ambazo ni za Serikali zilijengwa kama vile za majaribio. Sasa imethibitika kwamba wachimbaji wengi wanahitaji CYP nyingi ili kuweza kuongeza tija. Kwa hiyo Ofisi yako, Wizara yako itoe fedha nyingi kwa sababu kwa mujibu wa takwimu za sasa wachimbaji wanachangia takribani asilimia 40 ya dhahabu ambayo inauzwa nje ya nchi. Kwa hiyo hili ni eneo ambalo tunaomba Serikali iweze kuwekeza zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili katika eneo hili, tuna Watanzania wenzetu na raia wa nje wengi ambao wamekuja wakachukua PL, wamechukua PL wakatokomea; wengine wana miaka kumi, wengine miaka mitano na wengine miaka 20. Kila mwaka wanachokifanya ni kulipia na kujificha. Nimetoa mapendekezo katika michango yangu huko nyuma, kwamba wengi wanafanya kama vile kutegesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na mkakati, mifumo ituambie kwamba huyu mtu ana PL hii kwa takribani miaka kumi na haizalishi na iweke ukomo wa mtu kukaa na PL bila kuitumia. Kwa sababu kama kuna wachimbaji wadogo wanachangia kwa asilimia 40 lakini tunaruhusu mtu anakaa miaka 20 na PL haitumii, hafanyi nini, wakiingia wachimbaji wadogo wanaenda kufukuzwa ni sawasawa na kusema kwamba fedha tunazo lakini tumeshindwa kuzitumia. Kwa hiyo mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tubadilishe utaratibu. Wachimbaji lazima wanapochukua PL watoe mpango kazi na waitumie wasipo itumia Wizara ipewe mamlaka ya kubadilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili nakushukuru sana kwa kufanya marekebisho ya kodi, tulikuwa na mgogoro mkubwa sana kwenye kodi. Wachimbaji kila wanapokwenda kuuza walikuwa wanabishana na TRA. TRA akiona umeuza bilioni moja anajua hii ni faida, lakini palikuwa na gharama kubwa. Nakushukuru kwa asilimia mbili ambayo umeleta. Sasa ombi langu, mimi nimefanya biashara kabla ya kuwa Mbunge; tumepitisha asilimia mbili watu wako watakapoona watu wanafanya biashara na turn over inakuwa kubwa watageuka tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ofisi yako na watendaji wako waheshimu mambo haya ili turuhusu wachimbaji na watu wengine waweze kutumia mifumo ya kibenki. Kwa sababu wachimbaji walikuwa hawawezi kutunza hesabu; wachimbaji kwa nature ya kazi yao wanafanya kazi ngumu mpaka kuja kufika kwenye kuuza mazao kabla ya kuanza kupata faida. Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo mimi nakushukuru sana hapa; lakini naomba sana isije ikabadilika baada ya muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, tunakubaliana kwamba katika nchi hii tumezungukwa na mito, maziwa na maeneo mengine mengi kwa ajili ya kilimo na mifugo. Naomba niishauri Serikali; bado hatujatumia vya kutosha uwepo wa maziwa, mito, bahari na eneo la mifugo. Nimeangalia kwenye maeneo ambayo umeyawekea msisitizo; umeonesha kwamba unakwenda kufanya tathmini na kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais. lakini ukiangalia vizuri nature ya failure ya kwenye mifugo inategemea na uwezeshaji ambao mnaupeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ranch saba Tanzania, ukienda pale Mwabuki utagundua kwamba hawa watu wako dhofulhali, wako pale wana mifugo ambayo imeshakaa miaka. Ukienda hapa Kongwa utaona jinsi shamba lilivyochakaa, lakini utashangaa ukija kwenye bajeti; hawa wanamiliki takriban watumishi 2,000 nchi nzima. Ukija kwenye bajeti leo kurugenzi inayowasimamia ina fedha nyingi kuliko watu walio kwenye sekta za utafiti. Sasa utaona hapa hakuna seriousness. Kama tunataka kufanya mabadiliko lazima tupeleke fedha nyingi zaidi huku kwenye ranch ili waweze kuzalisha mitamba mingi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye taarifa, wamezalisha mitamba 1,000. Mitamba 1,000 kwa nchi ya watu milioni 60 huwezi ku-transform ng’ombe milioni 36. Wanatakiwa wapewe fedha nyingi ili wafanye mabadiliko. Tuwatoe wafugaji kwenye mifugo hii midogo midogo ambayo ina kilo ndogo, na wanakimbizana nayo kwenye mapori na Serikali ilhali maeneo hakuna tuwapeleke kwenye kufuga mifugo ya kisasa. Jambo hili haliwezi kufanikiwa kama Wizara haitoi fedha za kutosha. Tutoe fedha za kutosha kwenye utafiti na kwenye miundombinu. Tupeleke wataalam halafu wao wasambaze hii mitamba bora kwa wafugaji wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kwenye uvuvi. Ukiangalia vizuri tumeanza kuzungumza uvuvi kwa miaka mingi. Wewe umesema umetoa exemption ya tozo na VAT kwa wanao-export; lakini nasoma kwenye taarifa yako sioni wapi umehamasisha uvuvi kwa kutoa kodi kwenye fishing gears. Kwa sababu kinachosababisha sasa hivi tunauza kidogo ni gharama ya uwekezaji kwenye uvuvi. Ili kuongeza uzalishaji wa samaki ziwani, Ziwa Victoria au baharini unahitaji kuwa na zana za kisasa. Tunahitaji kuwa na out body engine, tunahitaji kuwa na boti zenye fiber, watu wanahitaji kuwa na fish finders nets.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo huwezi ukaongeza uzalishaji kwa sababu utakuwa una wavuvi wadogo wadogo wanaokomea mlingotini. Tumezungumzia mkakati wa Serikali wa kuanzisha boti za uvuvi leo takriban ni mwaka wa tatu ama wa nne lakini hatujaona productivity yeyote inayozungumzwa hapa. Kwa hiyo maana yake ni nini? Tunaendelea kuwategemea wavuvi wadogo wadogo ambao kwenye kodi hapa ni kama vile wamekuwa marginalized; Serikali haikuonesha kwamba wanatakiwa wakuzwe walelewe waweze kuwa productive kwenye nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunataka kuongeza uzalishaji kwenye maziwa, na hasa kwenye kilimo cha Samaki Ziwa Victoria na maeneo mengine. Dunia nzima sasa hivi wanapata samaki wengi kwenye cages lakini its too expensive ku-invest. Hii ni kwa sababu mwanzo utahitaji zaidi ya milioni 50. Hakuna mvuvi wa Tanzania ambaye anaweza ku-invest milioni 50 kwenye cages akaanza kupata fedha baada ya mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara, wanafanya kazi yao vizuri. Kwanza naunga mkono hoja na ninaipongeza Serikali kwa ongezeko la bajeti ambalo limefanyika mwaka huu karibu asilimia 255, lakini pia dhamira ya dhati ya kutaka kuleta mabadiliko kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumza ninayotaka kusema, nataka nimkumbushe Waziri, mezani kwake kuna andiko la Ibanda Irrigation Scheme, ambalo lilikuja ofisini kwake mwaka 2021. Ni imani yangu kwamba utekelezaji wa mradi huu utaanza mwaka huu. Mradi huu sisi Halmashauri ya Mji wa Geita tumekubali kwa niaba ya wananchi kutoa takribani Shilingi milioni 500 kusapoti Serikali ili mradi huu uweze kuanza. Kwa hiyo, tunaomba wasituangushe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nataka Mheshimiwa Waziri wakati ana-wind-up aniambie kuhusu ginnery ya Kasamwa na mkakati wa Serikali wa namna ya kuifanya ifanye kazi. Tunazo ahadi za takribani miaka sita, lakini tunaona hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, juzi nilitembelea Morogoro, palikuwa na Maonesho ya Kilimo. Naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri, nilikutana na wadau wake wengi. Nilikutana na PASS nikakutana na TADB, nikakutana na watu wanajiita TACT na wengine wanajiita Tanzania Agriculture Trust Input Funds. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza na Mheshimiwa Waziri, nitatamani ajaribu kutuonesha mchango wa haya mashirika yake yote kwenye kilimo. Nilizungumza na watu wa PASS ambao wanamchangia mkulima asilimia 20 mpaka asilimia 60 na asilimia 40 benki, lakini mkulima huyu akienda benki, anakwenda kukutana na commercial loans ambazo interests zake siyo rafiki wa mkulima. Ukienda TADB wanakopesha mpaka 75 percent halafu nyingine inayobaki ni ya kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ikawa, hivi hii 25 percent kwa nini isitafsiriwe kwenye value ya land ya shamba ili nikiwa na heka zangu 100, hiyo 25 percent wanipe 75 percent kwa sababu tayari value ya land inaweza ikafidia hilo eneo. Sikupata majibu sahihi zaidi. Nilikutana na wengine wanaitwa TACT (Tanzania Agricultural Catalytic Trust), hawa ni private firm hawajulikani sana, lakini ukiwasoma ni kama vile wame-centralize, wako Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu hapa ni nini? Ukikopa leo Tanzania Agricultural Development Bank, wakikupa mkopo, kwa sababu mkulima wa Tanzania analima kwa hali ya hewa, mwakani usiporejesha kulingana na schedule waliyokupa, watakutembelea, watakuuliza sababu, na wata-restructure mkopo wao, kwa sababu interest yao siyo kuuza. Pia katika kipindi chote watakupa ile technical support na kukutembelea na kukufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa uliyonayo kwenye Agricultural Trust Input Fund, wanajifungia ofisini, nami sijui kama huwa mnapima wamefanya nini kwa mwaka? Kwa sababu mimi sijawahi kuona wanachofanya. Wakikukopesha riba yamkopo wao wa Shilingi milioni 30, ni Shilingi milioni mbili labda, lakini mkopo ule ni wa miaka mitano. Shilingi milioni mbili ni kwa mkopo mzima, ni interest. Miaka mitano huyo mkulima kama ali-delay hapa katikati kulipa, utakuta interest ni Shilingi milioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukashangaa, interest ya principal nzima ni Shilingi milioni mbili, interest ya kuchelewesha ni Shilingi milioni 15. Mkulima huyo unayemkopesha ni mkulima ambaye anakopa kwa kilimo cha kutegemea mvua. Matarajio yangu ni kwamba, kabla hujamwekea interest na kabla hujaenda kutangaza kutaka kuuza mali yake, umemtembelea, umeona mwaka huu ali-plan kupata gunia 100 hajapata, umefika pale umegundua kwamba hana sababu ya kutokurejesha, ni kilimo cha hali ya hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajaribu kufanya mabadiliko sasa hivi, mapinduzi makubwa ya kwenda kwenye Irrigation Scheme, lakini asilimia 95 ya wakulima wanategemea mvua ya Mungu. Sasa wewe unanikopesha mimi kwa mkataba wa mvua ya Mungu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: …mazao sikupata, unanipiga fine. Mimi nikanunue mvua wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri hawezi kufumua Agricultural Trust Input Fund, wanapoteza fedha za Serikali. Ni bora mwapeleke huko wakawe Mabwana Shamba au vinginevyo, hakuna kazi wanayoifanya kwa sababu hawam… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kanyasu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, jana sikupata nafasi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa tuzo aliyopata kama mwanamke wa kwanza na ambayo imetuheshimisha sana sisi Watanzania, lakini pia imeendelea kuifanya Tanzania kuonekana kwamba kidiplomasia tunaendelea kunawiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais alisema yeye hastahili tuzo ile, mimi naomba kusema kwamba kama tungepata Rais asikubali kuendeleza yale ambayo alikuwa anaendeleza Rais mtangulizi, maana yake angeanzisha ya kwa kwake mengine leo tungekuwa na migogoro kwenye miradi mingine iliyokuwa inaendelea. Kwa hiyo, mimi nampongeza sana kwa kuyaendeleza yote na kwa juhudi kubwa na kwamba tuzo hiyo inamstahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku mbili zilizopita nilisema kwamba Geita Mjini tulikamilisha uandaaji wa master plan na master plan ya Geita Mjini tuliikamilisha mwaka 2020 na ilitugharimu zaidi ya shilingi milioni 400. Sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri kuwa na master plan ni jambo linguine, ninaona bado maoteo ya makazi yaholela yanaendelea kuwepo katika maeneo ya mengi ya mji pamoja na uwepo wa master plan kwa sababu maeneo mengi ya miji pamoja na kuwa na master plan yanachelewa sana kupimwa na matokeo yake yasipopimwa watu wanajijengea vyovyote vile na baadaye tunashindwa kupitisha miundombinu.

Kwa hiyo, juhudi zilizoanza za kutoa fedha katika baadhi ya Halmashauri na tunaipongeza Serikali kwa juhudi hizo tunaomba atukumbuke na atupatie pia Geita Mjini tuweze kupima maeneo yote ili kuweza kuepuka mji ule kuja kujengwa holela. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba kuchangia kwa jambo moja mahsusi tunazo sheria mbili, Sheria ya Madini inatoa surface right kwa mtu mwenye leseni ya kuchimba na anapopewa surface right anatakiwa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi aidha, awafidie wananchi walioko pale au amalizane nao ili kuweza kumiliki eneo lile.

Sasa tumekuwa na mgongano wa Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi kwenye Mji wa Geita, tunayo mitaa saba; Mtaa wa Katoma, Mtaa wa Compound, Mtaa wa Nyamalembo, Mtaa wa Samina, Mtaa wa Nyakabale na Mitaa ya Katumaini ambayo kwa miaka 23 imeshindikana kuwapimia wale wananchi waweze kupata hati, tuweze kupitisha miundombinu kwa sababu wanapokwenda kuangalia kwenye kumbukumbu wanakuta kwamba eneo lile linamilikiwa na mgodi, lakini kimsingi mgodi unamiliki surface right. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alikuja Mheshimiwa Waziri akiwa na Kamati ya Mawaziri wa Nane, Mheshimiwa Lukuvi, akatoa agizo kwa Kamishna wa Ardhi wa Mkoa ambaye anafanya kazi yake vizuri sana, Mheshimiwa Waziri naomba nikuhakikishie Kamishna anatoa ushirikiano mzuri sana, anafanya kazi yake vizuri sana na ametusaidia sana kumaliza migogoro kwenye eneo letu lile pale. Lakini tumeshindwa kuendelea mbele kwa sababu inaonekana kisheria eneo lile ambalo tayari lilikwishatolewa haki ya kumilikiwa na watu wa mgodi haliwezi kumilikishwa tena kwenye mamlaka zingine kwa watu wengine kwa wamiliki wengine wananchi wa Jimbo la Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokumilikishwa kwa wananchi kwa eneo hili kunasababisha adha nyingi chache zifuatazo; tunazungumzia maeneo ambayo yako kwenye kata tatu ambayo yanahitaji shule, lakini huwezi kwenda kujenga shule kwenye eneo ambalo huwezi kulipima, tunazungumzia maeneo ambayo wananchi wapo wamekutwa na mgodi, lakini ni katikati ya mji hatuwezi kupima kuwapa hati waweze kutumia hati kujiendeleza na kupata mikopo kwa sababu kila unapotaka kwenda kupima watu wa ardhi wanasema mchoro unagongana na mchoro mwingine kwa hiyo, haiwezekani kupima. Lakini siyo hivyo tu maisha ya wananchi katika mitaa hiyo kila siku polisi wanapita, kila siku mgambo wanapita, kwa hiyo, ukichimba choo unaonekana unachimba madini, ukiwa na mifugo umeingia kwenye eneo la mgodi, ukilima unaonekana umeingia kwenye eneo la mgodi. Wananchi wameishi kwa mateso makubwa kwa takribani tangu mwaka 1999. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kwamba sheria zetu zinauwezo wa kulimaliza jambo hili haiwezekani jambo moja Rais wa sasa akiwa Makamu wa Rais alikuja akalitolea maagizo, akaja Hayati Rais Magufuli akalitolea maagizo, Mawaziri wote waliopita kwenye Wizara hii wanakuja kutoa maagizo lakini jambo haliishi. Nafahamu juhudi za Mkuu wa Mkoa ameitisha kamati mbalimbali, amekutanisha watu wa TAMISEMI, wamekuja watu wa madini, wamekuja watu wa Wizara yako lakini bado hatufiki mwisho. Ni jambo gani hili halifiki mwisho!

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu mimi haki ya wananchi wale kumiliki ardhi ni haki yao ya kiasili, walikutwa pale na mgodi, mgodi ukapewa leseni, hatuna tatizo na mgodi tunaupenda, kama wanapenda kumiliki lile eneo basi tuko tayari lile eneo wawalipe fidia wananchi waweze kulichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama lile eneo bado hawajafikiria kuliendeleza watuache tulitumie tunavyotaka mwisho wa siku wakilihitaji waje watulipe. Haiwezekani kwa miaka 20 umeweka matangazo hamruhusiwi kujenga eti leo katika nchi yangu ardhi, ya kwangu nikitaka kujenga lazima nikaombe kibali mgodini ndiyo sheria inavyosema.

Mheshimiwa Waziri nimesimama kuchangia jambo hili, ninaamini ofisi yako ina uwezo wa kulimaliza kisheria, kwa kutumia sheria zilizopo na kama hazipo tuangalie upya sheria zetu ili tuweze kumaliza jambo hili, ni kikwazo kikubwa sana kwa maendeleo ya wananchi wa mitaa saba ya Mji wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Serikali imeridhia kuwaachia zaidi ya vijiji na vitongoji 900. Sasa kinachonisikitisha kidogo, Kata yangu ya Mgusu, Mitaa ya Nyakabale pamoja na Manga…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu ahsante kwa mchango mzuri sana, kengele ya pili.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali nzima kwa kazi nzuri ambayo wanaendela kufanya. Namshukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Geita Mjini na wananchi wa Mkoa wa Geita, kama wiki moja au mbili zilizopita tulikuwa na mkutano mkubwa wa wachimbaji Dodoma, ambapo kwa sehemu kubwa wachimbaji walitoka Mkoa wa Geita. Tunashukuru kwa kukabidhi vifaa vya teknolojia ya madini, tunamshukuru sana na wananchi wanasema sasa wameingia kazini rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha kwa taarifa yao nzuri ambayo nimeipitia. Kama ambavyo malengo au shabaha ya mpango wenyewe imezungumza ni kuongeza thamani kwenye mazao tunayouza nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuishauri Serikali, tunayo Sheria kwenye madini ambayo imeweka ulazima wa kuongeza thamani madini ya dhahabu kabla ya kuyauza nje. Kwa kufanya hivyo, Serikali ilitoa leseni za kujenga gold refinery na zimejengwa gold refinery nyingi lakini bado nashangaa ni kwa nini bado kuna kusita sita kwenye kutumia sheria hiyo kuhakikisha kwamba dhahabu yote inayouzwa nje imekuwa refined.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kuna sababu kubwa ya kulazimisha hivyo? Kwanza; tunapeleka dhahabu nje ambayo tayari itakuwa branded kama dhahabu yetu; Pili, tunaiongezea thamani na pia tunazifanya hizi refinery ambazo zimejengwa kwa gharama kubwa kufanya kazi iliyokusudiwa. Kwa hiyo, lengo hapa ni tusimamie hii sheria tuliyoiweka, tuweke malengo ya kuongeza thamani ya madini haya, tuhakikishe kwamba soko tunalolipata huko nje linatambua kwamba dhahabu hii inatoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapoondoka Tanzania raw gold kwenda nje kama South Africa au Uarabuni wanapoifanyia refinery wanai-brand wao kule kwa hiyo matokeo yake inapoteza uasili lakini sisi tunapoteza thamani yetu kwenye eneo hilo. Naishukuru sana Serikali pia kwa mchakato ambao imetoa ahadi kwamba inauanzisha ambao sasa inajipanga kufanya high resolution airborne geophysical survey ambayo itatusaidia kuijua vizuri nchi hii na kuangalia maeneo mahsusi ambayo yana madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pamoja na mbwembwe zote tulizonazo eneo ambalo limefanyiwa utafiti ni kama asilimia 16. Tukiongeza, tukijielekeza kwenye kukamilisha utafiti kwenye eneo hili makato yanayotokana na madini sehemu kubwa yata-double yatakuwa mengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali katika maeneo ya wachimbaji kuna vituo vya mfano vimewekwa viko vitatu. Kimoja kiko Rubete, kingine Rwamgasa ambapo wamejenga CIP. CIP hizi zingejengwa hata 30 au 50 Tanzania ili ziwasaidie wachimbaji wadogo kumaliza dhahabu kwenye mchanga. Sasa hivi teknolojia inayotumika inaacha dhahabu nyingi sana kwenye mchanga kwa sababu wanatumia plant na hizo plant ni lazima uje urudie kuchukua ule mchanga kuuingiza kwenye plant.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali kwa kuwa dhahabu inatuingizia fedha nyingi za kigeni na kwa kuwa, tayari tumegundua asilimia 40 ya dhahabu Tanzania inatokana na wachimbaji wadogo wadogo, isione aibu kuwekeza, tuwekeze ili tuweze kupata pesa nyingi zaidi kutoka kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, mwaka huu pia nilichangia, kwenye mchango wangu nilizungumzia habari ya kuongeza pesa za mauzo ya nje kutoka kwenye mazao. Sasa hivi tunapata pesa nyingi sana kutoka kwenye avocado na hii ilikuja yenyewe tukapata pesa nyingi. Tanzania kuna maeneo yanajipambanua kwa kulima migomba, kuna maeneo yanajipambanua kwa kulima nanasi. Nilizungumza duniani kuna export ya nanasi inayokadiriwa kufikia dola bilioni 30. Nanasi tulizonazo Tanzania ni kama vile madawa ya kienyeji kwa sababu huwezi kuzi-export. Nilisema tukiboresha eneo hili peke yake, Costa Rica wanapata dola bilioni moja kwa kuuza nanasi, Philippines wanapata dola bilioni 300 kwa kuuza nanasi, Nigeria wanapata zaidi ya dola milioni 100 kwa kuuza nanasi. Sisi hatuuzi nanasi lakini wakulima wa nanasi wapo, tunachotakiwa hapa ni kupata mbegu sahihi ambayo tunaweza kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kuwa wakulima wa nanasi wapo na tuna BBT inaendelea ni kuwapelekea teknolojia, kuwapelekea mbegu bora na kuwatafutia soko kama tulivyotafuta soko la avocado tukaanza kuuza nje tukapata mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nataka kuzungumzia, kwanza naipongeza Serikali kwa kuonesha itapeleka trilioni 15.3 kwenye maendeleo sawa sawa na asilimia 33 nakupongeza sana. Juzi wakati tunajadili taarifa ya CAG ulitokea mjadala wa zaidi ya shilingi trilioni 200 ambazo zimeonekana zimekwenda nje kinyume cha utaratibu. Mawaziri wote wawili wa Fedha na wa Mipango walikuwa wanapinga na mimi nakubaliana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye repoti utakutana na hizo dola bilioni 140 kama pato la nchi lakini kwa mfumo ulivyo duniani Mheshimiwa Waziri wa Mipango ukiangalia kwenye list financial flows duniani pesa ambayo inavuja ni nyingi kuliko pesa inayokusanywa. Pesa tunayoizungumzia hapa ni pesa ambayo haikupita kwenye vitabu vyako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili hii pesa shillingi trilioni 15.3 ambayo ni sawa na asilimia 33 iweze kufanya kazi yake vizuri lazima tujue kwamba corruption ime- imejizalisha, wamebadili mbinu. Corruption sasa hivi inakuwa exported, inakuwa exported kutokea kwenye contract na kutokea kwenye kazi ambazo watu wanazitengeneza leo

MWENYEKITI: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Kanyasu.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuwe na mpango madhubuti wa ku-deal na aina mpya ya rushwa ambayo inaweza, pesa zote hizi zisitusaidie kuona tunachokifanya kutokana na ukweli kwamba kuna watu tayari watakuwa wamejiandaa namna ya kuichukua. Nakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge kuhusu Wakala wa Kimataifa wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (International Renewable Energy Agency - IRENA) na Azimio la Bunge kuhusu mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa ya Afrika wa Mwaka 2019 (Treaty for the Establishment of the African Medicine Agency - AMA)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono Azimio. Kama ambavyo Mwenyekiti wetu amewasilisha sisi kama Kamati tumepata muda wa kutosha kupitia wasilisho la Serikali lakini kuwasikiliza wadau mbalimbali ambao walikuja kuwasilisha maoni yao na ninaomba kutumia fursa hii kuunga mkono hoja na kuomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuridhia ili nchi yetu iweze kuwa mwanachama wa IRENA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ilikubali kuwa mwanachama mwaka 2009 lakini imetuchukua miaka takribani 13 leo kuja kupitisha Azimio. Zilikuwepo sababu za msingi, tuliuliza kwa nini tumechukua miaka yote hiyo wakati tumeendelea kushiriki? Serikali ilisema, ilikuwa inajipa nafasi ya kuona wale walioingia wamefaidika kiasi gani na baada ya kujiridhisha kwamba walioingia wamefaidika sasa nimegundua ni muda muafaka wa kuingia. Jambo hili ni jema ingawa kuchelewa kwetu kumetuchelewesha kwenye kufaidika na faida ambazo wanachama wengine wamepata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ndilo eneo ambalo lina umeme wa bure au lina nishati ya bure. Amezungumza hapa Mheshimiwa Masache aina za umeme unaopatikana kwenye eneo hili pamoja na solar energy. Afrika jua lipo la bure, ziko nchi duniani wanavizia jua litoke, siku jua likitoka wanashangilia. Yaani jua linatoka kwa mwezi mmoja kwa mwaka mzima, sisi tuna umeme wa bure kutoka kwenye jua lakini tuna upepo wa kutosha (wind energy). Tuna joto ardhi (geothermal), yako maeneo yamepimwa na umethibitika kwamba yanaweza kutoa umeme wa kutosha lakini tuna maeneo mengi yanaweza ku-generate hydroelectric power.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali kwa sababu sehemu kubwa ambayo tunataka kutumia ni hydroelectric power lakini bado hatujatumia kiasi cha kutosha fursa hii tuliyonayo. Bado tuna umeme mwingine wa bioenergy sehemu kubwa ya uharibifu wa misitu inatokana na utafutaji wa nishati na watafutaji wengi wa nishati ni wafugaji. Wafugaji wana uzalishaji mkubwa wa kinyesi cha ng’ombe ambacho kinaweza kutumia kutengeneza biogas.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uzembe ambao tunao ni kwenye ku-transform hizi fursa tulizonazo kupelekea hao wanaotumia zaidi ukataji wa kuni waache kutumia watumie biogas. Kwa hiyo, nadhani huu ni muda muafaka ambao Serikali kwa kuridhia Azimio hili, sio twende kama ceremonial, tuweke mkakati wa kutosha kuhakikisha kwamba sasa tunakwenda kupambana kuvuna hizi fursa ambazo tunazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi jirani wanazalisha zaidi ya megawatt 1000 kutoka kwenye geothermal. Mtu anaweza kufikiri kwamba Serikali itapata wapi pesa kwa ajili ya kufanya jambo hili. Tumeshauri Wizara tutumie zaidi PPP au tuhamasishe watu binafsi kuingia kwenye eneo hili na kazi ya TANESCO iwe kuhamasisha wawekezaji lakini kutengeneza mazingira ambapo wao wanaweza kuwa recipient wa umeme na kuhakikisha watanzania wanapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna upungufu wa umeme kwenye nchi yetu na kwenye Kamati tuliambiwa kwamba hata baada ya Mwalimu Nyerere kuingia mahitaji ya umeme wa majirani zetu ni makubwa sana wataendelea kuhitaji umeme. Ni muda muafaka sasa kwa sababu kujiunga kwa Azimio hili kunafungua milango ya teknolojia, kunafungua milango ya mitaji, lakini kunafungua milango ya uzoefu ambao majirani zetu tayari wanao na tayari wateja tunao ambao tunapaka nao kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo tayari yamekwishathibitika, Singida kuna upepo, Kishapu kuna joto lakini Same kuna upepo na maeneo mengine ya geothermal ambayo utafiti unaonesha tayari Wizara ilikwishafanya kazi kubwa lakini shida imekuwa ni kuvutia teknolojia, kuvutia mitaji na kutengeneza sera ambayo inakaribisha watu waje.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, sera tunayo ya ujumla lakini tunapungukiwa sheria mahususi kwenye eneo hili. Tumemweleza Mheshimiwa Waziri na tutaitaka Serikali kutengeneza sheria ambayo wawekezaji ambao wana historia ya kuona kwamba tuna sera zinabadilikabadilika, tuwe na sheria ambayo mtu anaweza kuwa na uhakika nayo. Anapokuja kuwekeza asitarajie kesho au kesho kutwa kujikuta anakosa soko la kuuza umeme au anajikuta anaamuriwa kufunga biashara yake. Tuwe na sheria na sera ambayo Wizara tunaiomba iitengeneze na tuitangaze kuvutia maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono Azimio. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika siku ya leo, pia niwape pole wananchi wa Wilaya ya Biharamulo ambao Mheshimiwa Mbunge wao wa Bunge lililopita Mheshimiwa Anthony Mbassa jana tulipata taarifa kwamba amefariki na niwatakie moyo wa subira kwa familia, ni majirani zetu Geita kwa hiyo tunafahamiana vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa mabadiliko makubwa aliyoyafanya jana ya Wakuu wa Wilaya na kwa kweli naomba nimpongeze kwa sababu ameendelea kuimarisha safu yake ya uongozi. Ninawapongeza walioteuliwa na niwatakie kila la kheri, pia niwapongeze ambao uteuzi wao umetenguliwa au hawakuteuliwa na niwatakie kila la kheri huko uraiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka tu nitoe mapendekezo mawili kwenye sheria hii. Ukiangalia vizuri nia njema ya Mheshimiwa Rais ya kuwateua vijana kuwa Wakuu wa Wilaya ni kwa ajili ya kuwaingiza katika Mfumo wa Uongozi wa Nchi ni nia njema sana na wengine wanateuliwa wakitoka kazini. Nafahamu Serikali iliyopita wakati wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, wapo baadhi ya ma-DC wakiwa Maafisa Tarafa, Maafisa Mipango, wakiwa na miaka 20 mpaka 30, wamehudumia miaka mitano na uteuzi huu wameachwa, ukitazama vizuri sheria hii sasa hawa walipoteza ajira yao huko nyuma na sasa hivi siyo tena watumishi, unaona kabisa kwamba vijana hawa baada ya miaka miwili watakuwa ni watu ambao ni mzigo kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema sheria ukishateuliwa kuwa DC ajira yako ya kwanza inapotea, akija Rais mwingine baada ya miaka 10 akikuacha na ajira yako bado una miaka 38 unapoteza kila kitu. Kwa hiyo, ni sheria ambayo ninaiona kama siyo nzuri. Kwa sababu wapo waliotoka kwenye Utumishi wa Umma sasa zaidi ya 20 ambao wanakwenda kuwa Wakuu Wilaya, baada ya miaka 10 ya Mheshimiwa Rais Magufuli, anaweza akuja Rais mwingine akasema nao hawahitaji, hawawezi kurudi Serikalini umri wao ni miaka 35, ninadhani Sheria hii siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini niwatakie kila la kheri walioteuliwa na niwape pole vijana wenzangu ambao tulikuwa nao na wengi wako chini ya miaka 40 ambao wameachwa, wajipange upya huko uraiani. Nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda sasa kwenye marekebisho ya sheria nianze na Sheria ya Elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imependekeza adhabu kali ya miaka 30, kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kumpa ujauzito mwanafunzi. Nazungumzia wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali sheria ni nzuri, ingawa kwa mtazamo wangu kuna mambo mengi ya kufanya. Mimi niko katika Kamati ya UKIMWI; tumeangalia kwenye taarifa tulizoletewa, tumeona watoto wanaanza kufanya mapenzi wengine wakiwa na miaka kumi na kuendelea. Maana yake ni kwamba waanza kufanya mapenzi na wanapata maambukizi ya UKIMWI chini ya miaka 15; na hawa ni wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari. Upo uwezekano huyu ambaye ameanza kufanya mapenzi katika umri mdogo anaporudi shuleni huyu binti wa miaka 12, miaka 13 akam-convince kijana awa kiume wa miaka 15, miaka 16 na matokeo yake huyu wa miaka 13 hadi miaka 14 akipata mimba unaweza kufikiri ni ya mwanafunzi kumbe amepata uraiani huko. Kwa sababu taarifa zinaonesha kwamba hawa wanapoanza kufanya mapenzi wanafanya na watu wazima wala hawafanyi na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maana yake ni nini? Sheria hii upo uwezekano wa kumfunga mtu miaka 30 mwisho ukagundua kwamba mimba hii haikuwa ya yule aliyefungwa na unagudua haikuwa ya yule aliyefungwa tayari mtu huyu alishatumikia kifungo cha miaka 30, unatoka jela mtoto siyo wa kwako, mtoto ni wa mtu mwingine kwa sababu watoto wetu siku hizi wanaanza kujifunza mambo haya wakiwa na umri mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali iende mbali zaidi kwa kuleta vipimo vya DNA ikiwezekana kwenye level ya kila Wilaya, kwa sababu kwenye ushauri uliotolewa juzi kila Kata haiwezekani, kwenye level ya kila Wilaya, au kwenye level ambayo itakuwa ni rahisi kugundua kwamba ujauzito huu siyo wa mwanafunzi. Ninazungumzia hapa kwa sababu vijana wetu hawa kwenye maeneo mengi ya shule anaweza akatafuta mnyonge wa kumkimbilia, akafuata mwanafunzi mwenzake, lakini kwa sababu mambo haya wanaanza mapema, inawezekana ujauzito huu ameupata uraiani huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza hii kwa mifano sahihi kabisa ambayo tumepata kutoka kwenye Kamati yetu na inaonesha kabisa wazi kwa mba vijana wetu wana wanaanza matendo haya mapema zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tuangalie namna ya kutengeneza adhabu nyingine zaidi, unapomfunga mtu miaka 30 anakwenda jela, halafu baada ya mwaka mmoja anakuwa kama vile amezoea maisha ya jela, inakuwa tena siyo adhabu, ninafikiri pamoja na miaka 30, kila mwezi huyu mtu awe anapata viboko 12, kwa miaka yote 30 mpaka atakapotoka. Hii itamfanya mtu asizoee kile kifungo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekutana na watu wengi sana jela huko, akishafungwa miaka mitatu inakuwa kama vile ni nyumbani, ukienda mtaani unakutana nao, hata Askari Magereza hana tena muda wa kuwachunga wanawaacha tu wanatembea wenyewe kwa sababu walishazoea maisha ni mazuri, anakula vizuri, ameshakuwa mnyampara mle, anapata sabuni mafuta. Kwa hiyo, unamkuta mtu yule huku aliacha ameharibu mtoto wa mtu lakini kule anaendelea na maisha yake kama kawaida. Kwa hiyo, nafikiri kila mwezi akipata viboko 12 mpaka miaka yote 30 itakapoisha itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine huyu binti ambaye sasa amekwishajifungua tunamfanyaje? Kwa vile atajifungua Baba amefungwa, atafukuzwa shule na hatasoma tena. Ushauri wangu ni kwamba baada ya kujifungua binti huyu, uangaliwe uwezekanano wa kubadilisha sheria ili aendelee na masomo, kwa sababu baadaye mtoto huyu atajikuta ana mama hakusoma, ana baba ambaye alifungwa akiwa mwanafunzi naye hakusoma tutakuwa tumetengeneza mtoto ambaye atakosa msaada kwa baba na atakosa msaada kwa mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia sheria itazame vizuri, kuna wakati mwingine unakuta kwenye darasa moja binti ni umri mkubwa kuliko kijana. Labda binti ana miaka 23 alichelewa kusoma. Kule usukumani watu wanaanza shule wakiwa na umri mkubwa, anaweza kuanza kusoma akiwa na miaka 15 ndiyo anakwenda darasa la kwanza, kwa hiyo anajikuta amefika sekondari ana miaka 24; halafu huyu binti anapewa mimba na kijana wa miaka 15; sasa hapa mwenye kosa ni nani, kwa sababu inaonekana kama vile binti atakuwa ndiye aliyemtongoza kijana, halafu unakwenda kumfunga huyu kijana ana miaka 15 unamwacha huyu binti wa miaka 24 uraiani, ni kama vile tunaleta uonezi hapa. Nafirikiri sheria itazame vizuri ili kuangalia namna ambavyo sheria hii inaweza kwenda ikafanya kazi sehemu zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono marekebisho ya sheria nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kifupi sana kwanza niseme naunga mkono muswada huu na labda tu nitoe mapendekezo yangu machache, nilikuwa nimetarajia ningeweza kuchangia kesho, lakini naweza kusema haya machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza naungana na ambao wangependa tutofautishe Ibara ya 18, kuna tatizo la tafsiri kwamba haki ya kupata taarifa na haki ya kupata habari, lakini haki ya kupata habari palepale inalazimishwa ionekane iko sawa na haki ya kupata taarifa. Katika mazingira ya kawaida, taarifa hii inaweza kutolewa katika muda wowote ule ili mradi mlengwa aliyekuwa anataka taarifa anatakiwa apate hii taarifa kadri alivyokuwa anaihitaji. Kwa hiyo, pamekuwa na tatizo la kuichanganya hii kuonekana kwamba mtu asipopata taarifa pale pale Katiba imekiukwa. Siyo kweli kwamba Katiba inakiukwa kwa mtu kutokupewa taarifa pale pale lakini inatakiwa mtu apewe taarifa sahihi wakati wowote baada ya tukio hilo kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi katika hili ni kama walivyosema wenzangu, ni vizuri sana sheria yetu ikatofautisha ni maeneo gani tunaamanisha taarifa za siri. Zipo taarifa za intelijensia ambazo zikiachwa wazi zinahatarisha usalama wa nchi yetu, lakini ziko zingine ni taarifa ambazo zimekuwa tu zikibanwa na walengwa kwa nia ya kuficha baadhi ya siri kwenye taasisi na wengi wamezitumia hizi vibaya. Watu wengi wanasema kwamba kwenye Halmashauri zetu ni rahisi sana kupata taarifa, lakini mimi ambaye ninaamini nimekuwa kwenye Halmashauri kwa muda mrefu kuna wakati hata Mheshimiwa Mbunge kama taarifa unayotaka ina madhara kwa walengwa walioko kwenye Halmashauri ile unaweza ukasubiri taarifa ile kwa muda mrefu na usiipate.
Kwa hiyo, sheria hii ni ya muhimu, ni sheria ambayo kimsingi inawalazimisha wahusika kutoa taarifa sahihi hata kama taarifa ile haitatolewa pale pale lakini taarifa hii itatolewa kwa mtu ambaye anaihitaji na itakwenda kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi hapa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja atusaidie tunatunga sheria hii kwa ajili ya Serikali peke yake au pia kwa ajili ya makampuni binafsi. Kwa mfano, kama ni Serikali peke yake ieleweke lakini tunayo makampuni ambayo yanatuzunguka kwenye maeneo yetu, makampuni yanayofanya biashara na makampuni yanayochimba madini ambayo ni wadau wakubwa wa Serikali. Kuna wakati makampuni haya yanaweza yakalipa service levy bila wadau kujua yanalipa kutokana na mauzo yapi, yanalipa kutokana na mapato gani na unapokwenda kufuata hizi taarifa inaonekana ni taarifa za siri za hizo kampuni.
Kwa hiyo, ni vizuri pia kueleweka kwamba sheria hii inakwenda kugusa kila eneo, kila idara, kila taasisi au ni sheria ambayo inalenga kugusa Serikali peke yake au ni sheria ambayo inalenga kugusa kila sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ndugu zetu wengi wana wasiwasi sana na baadhi ya matumizi ya sheria hii unapofanya makosa. Mimi sijawahi kuona mtu anaadhibiwa bila kufanya makosa na ametusaidia hapa Mheshimiwa Bashe kwamba wadau wa habari wameshirikishwa kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya kawaida tunaamini lengo la sheria ni kujenga nidhamu. Kama watu wanatumia vibaya haki yao ya msingi ya kutoa taarifa na kupotosha umma lazima watu waadhibiwe. Hili lisije likaonekana kama ni suala baya kwa sababu bila kufanya hivyo tutakuwa tunajenga nchi ya watu wanaofanya makusudi, wanaopotosha umma na matokeo yake mtu anapata sifa kwa sababu ya kuharibu sifa ya mtu mwingine. Tumeshuhudia huko nyuma mtu anasimama hapa anatengeneza uongo, huko nje wanamsifu, halafu kesho yake hana hata data moja inayoonyesha kwamba taarifa hiyo ni ya ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema Mheshimiwa mmoja hapa kwamba ni vizuri sana source ya information pia tujiridhishe nayo. Kwa mfano, kama mtu anayetoa taarifa hana uhakika na taarifa ile halafu aliyepewa taarifa ndiye anayekwenda kuadhibiwa nadhani sio sahihi. Ni vizuri sana yule anayetoa taarifa ajiridhishe na taarifa ile kabla ya kuitoa na iwapo taarifa hiyo itakuwa na mapungufu yule aliyepewa taarifa pia asije akaadhibiwa kwa makosa ya taarifa ambayo aliiipata kimakosa kutoka kwa mtu ambaye alikosea. Vinginevyo adhabu hizi ziwekwe kwa watu wote wawili au watu wote wawili wasamehe na adhabu ambayo itakuja kufuatia kwenye sheria yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naomba niwapongeze sana Kamati kwa namna ambavyo wameutendea haki muswada huu. Nilipousoma mwaka 2017 na nilipokuja kusikiliza marekebisho, nimeona Kamati wamefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri pamoja na Watendaji wote katika Wizara hii. Kama walivyosema wenzangu, kimsingi tunaiona nia ya Serikali ya kuunganisha mifuko hii na kuondoa gharama za uendeshaji kama ambavyo zimetajwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Kamati. Kwa hiyo, tunaiona hiyo nia na hilo lengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu hapa, nilidhani baada ya Serikali kuondoa gharama hizo ambazo tumeziona kwenye maelezo ya Mheshimiwa Waziri, basi zingekuja chini zikawa na faida kwa mwanachama wa mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyomalizia kusema Mheshimiwa Mama Mushashu, kwa kweli tulitarajia kuona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba mwisho wa siku sasa haya mafao yanakwenda kuongezeka kwa asilimia ngapi au yanakwenda kuimarika kwa asilimia ngapi? Sasa linabaki kuwa kwenye Pandora box kitu ambacho nadhani tutahitaji pia baadaye kuanza kuhangaika na Mheshimiwa Waziri. Kwa ujumla wake, napongeze sana, marekebisho yamezingatia sana maoni ya wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika section 35 kama walivyosema wenzangu, ni vizuri sana kufikiria kuhusu medical insurance na fao la elimu. Hivi tunapozungumza, watumishi wengi ambao walikuwa wamesoma Diploma, hawapati mikopo tena kwenye Bodi ya Elimu na wengi walikuwa wanakimbilia kwenye mifuko hii kwenda kuomba mikopo na baadaye wanakwenda vyuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokuwa tume-merge na tukaliondoa hili kama ambavyo iko sasa, maana yake ni kwamba liko kundi la watu hawatasoma tena kulingana na gharama za elimu zilivyo juu. Kwa hiyo, ni vizuri sana kwenye section 29 kurudisha fao hili la elimu, kwa sababu mifuko ilikuwa inatoa na wanachama walikuwa wakijiunga katika mifuko hii kwa sababu waliona kuna kitu wanakihitaji kwenye mfuko huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naipongeza sana Serikali kwenye section 43. Mafao ya wastaafu yalikuwa yanaweza kuchelewa mpaka mwaka mzima na hakuna mtu aliyekuwa anajali. Ninao mfano wa watu ambao nimewasaidia, walicheleweshewa mafao yao kwa zaidi ya miezi sita, miezi nane na wako wengine mpaka leo wanasubiri na hakuna interest, wala hakuna mtu aliyekuwa anajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuweka provision hii katika section 42 na 43 maana yake tunaweka commitment kwa mifuko hii kuhakikisha kwamba hii miezi sita ya maandalizi na hizi siku 60 zilizotajwa katika sheria wasipolipa wajue kwamba watalipa kwa interest. Interest haimasaidii sana mstaafu, kwa sababu mstaafu akili yake ikimpelekea kufikiri kustaafu, mara nyingi hufikiri aweze kupata malipo yake na kuendelea na maisha yake mengine. Naipongeza Serikali kwa kuweka commitment hii kwa sababu itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mimi natoka kwenye maneo ya wachimbaji na mgogoro wangu mkubwa siku zote umekuwa ni fao la kujitoa. Ninaishukuru Serikali, maelezo aliyoyasema Mwenyekiti wa Kamati na Mheshimiwa Waziri, yanaleta picha kwamba kuna namna inalishughulikia. Hivi tunavyozungumza, wako wafanyakazi wengi walioko kwenye madini ambao wana zaidi ya miaka mitano, ambao wanasubiri sheria hii ili iwafungue namna ya kuendelea mbele, kwa bahati mbaya sana haijawa clear bado. Bado imekuja ikiwa imefumbwa fumbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, wapiga kura wangu wanataka kufahamu sasa hasa wale ambao tayari wako nje wanasubiri utaratibu kwa ahadi ya Rais aliyoitoa kule Kilimanjaro, ni nini kinafuata baada ya hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimsikia Mwenyekiti wa Kamati anasema kutakuwa na hiyo asilimia 33 kwa miezi sita na baadaye kuangalia kama hakuna tena ajira nyingine, basi mtu analipwa pesa yake, anaondoka. Tulione hili kwenye utaratibu ili liwasaidie watu kuweza kujipanga na maisha yao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, tufahamu kwamba tunapoiunganisha mifuko hii tunaondoa ushindani kwa kupunguza gharama, pia kuna madhara ya kuondoa ushindani. Mara nyingi sana huko nyuma kabla ya mifuko hii kuwa mingi, pia hata customer care ilikuwa very poor. Lazima tulitambue hili kwamba baada ya mifuko hii kuunganishwa, watu watakuwa hawana option; wa umma watakwenda huku na wa upande wa binafsi atakwenda huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa option kunaweza kukawafanya watendaji wakalala usingizi. Kwa hiyo, lazima tuweke mfumo ambao utaendelea kuifanya mifuko hii kuendelea kuhakikisha kwamba inajali huduma za members wake, lakini pia inatoa huduma kulingana na mikataba ambayo ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na wasaidizi wao wote kwa kutuletea muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama walivyosema wachangiaji wengine wengi, ni vigumu sana mwekezaji yeyote makini kwenda kuwekeza mabilioni ya shilingi kama hana uhakika na usalama wa pesa zake. Kwa hiyo, mabadiliko haya ya sheria yalikuwa ni ya lazima kwa sababu wawekezaji wetu wengi duniani ni wawekezaji ambao pesa siyo za kwao, wanazipata kwenye mabenki, wanakopa. Kwa hiyo, anapokuja hapa bila kuwa na uhakika na usalama wa pesa zake hawezi kuja kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo nilitaka nianze kwa taarifa ya Kamati kwenye ukurasa wa tisa ambapo ukienda kwenye item namba 2.2 utagunduakwamba mwaka 2017 tulipitisha hapa sheria ambayo ilikuwa inaruhusu Halmashauri zetu kubuni miradi ya kimkakati na kuwasilisha Serikalini na kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karibuni hapa tulipata taarifa kwamba ni Halmashauri chache sana ambazo zilifanikiwa na moja ya sababu kubwa ambayo ninaiona ni kukosekana kwa ujuzi kwenye Halmashauri zetu na siyo kwenye Halmashauri peke yake. Kwa sababu kama Halmashauri zetu na Wizara zingekuwa na wataalam wa kutosha wangeweza kutoa msaada huu kwenye Halmashauri zetu. Leo tungekuwa tunapata tathmini ya hatua kubwa mbele tuliyoipiga kwenye sheria ambayo tuliiweka, lakini matokeo yake tunaendelea kuwa Halmashauri mbili/tatu ambazo zimetekeleza hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naungana mkono kabisa na Kamati kwamba iwepo programu maalum ya kuwawezesha wataalam wetu ili wapate uwezo wa ku-plan hii miradi, kuisimamia, lakini pia kutengeneza maandiko ambayo yatatupeleka kwenye utekelezaji wa sheria hii bila kuwa na ubabaishaji. Kama tukiendelea bila kujenga uwezo, tatizo tulilokuwa nalo mwanzo la kuwa na watu kwenye ofisi ambao hawawezi kufanya upembuzi yakinifu na pia hawawezi kufanya maamuzi, litaendelea, kwa hiyo, naungana mkono na Kamati.

Naomba sana kwamba katika hatua hii Mheshimiwa Waziri atafute namna ya kufanya investment ya kutosha ili kupata watu ambao wataweza kuisaidia Serikali kwa sababu tunaweza kupitisha sheria nzuri, lakini mwisho wa siku sheria ikaendelea kubaki kwenye Kamati na isiweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingi sana ambazo pamekuwa na sheria hii na hasa katika nchi ambazo zimetolewa mfano hapa, zipo sababu nyingi ambazo zimesababisha ikaonekana kwamba Sheria ya PPP nayo haifai. La kwanza, ni mazingira ambayo Serikali itaweka. Inawezekana kabisa Waziri wa Fedha akawa na nia njema ya kutaka wawekezaji waje na wabia waje, lakini hayuko peke yake, ana watu wengi ambao lazima wafanye kazi pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukaenda kwa Waziri wa Fedha, yuko sawa, wakaenda watu wengine wa Mazingira wakakwamisha, wakaenda watu wa Ardhi wakakwamisha, wakaenda watu wa Mambo ya Ndani wakakwamisha. Kwa hiyo, ni lazima hizi timu zote zifanye kazi kwa pamoja ili wawekezaji wanaokuja wenye nia njema ya kufanya kazi na Serikali waweze kuona kwamba nia kweli tumedhamiria kutumia sheria hii kuleta mabadiliko makubwa katika uwekezaji na katika uchumi na faida ziko nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukitumia pesa nyingi sana za kwetu kufanya miradi mingine. Iwapo tutapata partners, maana yake ni kwamba tutaelekeza pesa zetu za ndani kwenye maeneo ambayo tunadhani wawekezaji hawaoni faida, kwa sababu hakuna mtu amekwenda kuwekeza sehemu ambapo hawezi kupata faida. Jambo hili ni muhimu sana, kwa hiyo, Serikali yenyewe ni muhimu kuwa imejiandaa lakini kuwaandaa wawekezaji waweze kufahamu kwamba ni maeneo gani wakikwama, wakimbilie wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ni kitu muhimu sana kwenye suala hili. Nataka kutoa ushauri kwamba pawepo na kanzidata (database) ambayo itaonesha kutokea kwenye Halmashauri zetu/kwenye Manispaa ambayo itatusaidia kufahamu mtu akiwa duniani popote pale katika nchi yoyote duniani aweze kujua nikienda Tanzania, maeneo ya priorities ni haya hapa ambayo unadhani naweza nikaenda kuwekeza. Isitokee mahali unakuta sehemu hii wanafahamu hiki, sehemu hii hakuna muunganiko wa mawasiliano, tutajikuta kila siku na tunaanza upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kisiasa ni muhimu sana katika suala hili. Naomba tu niseme vizuri kwamba tunategemea sana kwamba kauli na msukumo wa Mawaziri wetu tuweze kuwasaidia wawekezaji. Tunalo tatizo sana kwenye maeneo yetu huku chini kwamba inawezekana huku mna-push suala liende, lakini kwa sababu watendaji wetu huko chini hawaoni faida na kwa sababu watu wengi wamezoea kupata commission, wanaona kwamba suala hili halina faida sana kwao, wakalikwamisha bila sababu. Kwa hiyo, tunataka sana Mheshimiwa Waziri mkono wake huu na wasaidizi wake huko chini uweze kusukuma mambo haya yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la mikataba. Nchi nyingi ambazo zimepata shida kwenye mikataba, haikuja kwa bahati mbaya, ni kwa sababu hapakuwa na transparency. Watu wengi wanaopelekwa kuingia kwenye mikataba aidha uwezo wao ni mdogo au ni mkubwa sana, kwa hiyo, matokeo yake badala ya kuona maslahi makubwa ya nchi wanajikuta wanaweka zaidi maslahi yao binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala linafanyikaje? Anaweza kuja mwekezaji hapa leo, anataka kuwekeza shilingi bilioni 100 na anataka kufanya payback ya mradi ule ule labda miaka 10, lakini anayekwenda kuweka mkataba akasema wewe fanya hiyo miaka 20 na uhakikishe mradi huu unagharimu shilingi bilioni 200. Matokeo yake mradi huu unaonekana tena hauna faida kwa wananchi au una gharama kubwa. Kumbe tatizo kubwa hakukuwa na transparency kwenye mkataba.