Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Seif Khamis Said Gulamali (20 total)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-
(a) Je, Serikali imefikia wapi katika ujenzi wa bomba la maji la kwenda Tabora- Igunga kupitia Nzega?
(b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kusambaza maji hayo katika Tarafa za Simbo na Choma kupitia Ziba kama Mheshimiwa Makamu wa Rais alivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa … Samahani!
NAIBU SPIKA: Anaitwa Seif Khamis Gulamali!
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza mchakato wa kupata Wakandarasi watakaotekeleza kazi za ujenzi wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na Vijiji 89 vilivyo umbali wa kilomita 12 kutoka bomba kuu. Zabuni ya ujenzi ilitangazwa mwezi Disemba, 2015 ambapo mpaka sasa mchujo wa awali (prequalification) umekamilika na Wakandarasi wanategemewa kuanza kazi katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa za Simbo na Choma zipo zaidi ya kilomita 30 kutoka bomba kuu linalotajarajiwa kujengwa kwenda Igunga kutoka Nzega hivyo kuwa nje ya kilomita 12 zilizosanifiwa kwa mradi huu. Katika kuboresha huduma ya maji katika Tarafa hizi, Serikali inatafuta chanzo mbadala cha maji ili kupunguza tatizo la maji katika Tarafa hizo. Aidha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ili kuendelea kuboresha huduma ya maji.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI) aliuliza:-
(a) Je ni lini Serikali itakwenda kuona hali ya Kiwanda cha Manonga na kukifanya kiweze kufanya kazi na kutoa ajira kwa vijana wa Mkoa wa Tabora?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kukiangalia upya Kiwanda cha Nyuzi Tabora ili uzalishaji uweze kuanza?
NAIBU SPIKA: Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji yupo tayari kwenda Manonga na kutembelea Kiwanda cha Manonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kukifufua Kiwanda cha Manonga Ginnery ili kiweze kufanya kazi na kutoa ajira kwa vijana wa Mkoa wa Tabora. Pamoja na jitahadi za Wizara yangu na Msajili wa Hazina, mkakati wa kufufua sekta ya pamba pamoja na nguo (cotton to clothing strategy) utaongeza uzalishaji wa pamba. Chini ya mkakati huo tunalenga sasa kuongeza uzalishaji wa pamba kwa tija lakini wingi wa pamba utapelekea pia kutosheleza mahitaji na matumizi ya ginneries ikiwemo ikiwemo Ginnery ya Manonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Tabotex kilichopo Mkoani Tabora kimekuwa kikifanya shughuli za usokotaji nyuzi tangu mwaka 1978 chini ya umiliki wa Serikali. Ilipofika Aprili, 2004, Serikali ilikibinafsisha kiwanda hicho kwa kampuni za Noble Azania Investment Limited na Rajani Industries Limited. Kiwanda hicho hakijafungwa bali kimesimamisha uzalishaji kutokana na changamoto ya soko la nyuzi ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha Tabotex kilisimamisha uzalishaji Mei, 2015 kutokana na kuwa na akiba (stock) kubwa ya nyuzi zilizozalishwa mwaka 2013 ambapo hadi sasa zinaendelea kuuzwa. Soko kubwa la nyuzi za Tabotex ni soko la nje huku kiwango kidogo kikiuzwa katika soko la ndani. Kawaida wanunuzi wakubwa wa nyuzi ni viwanda vinavyofanya shughuli za ufumaji wa vitambaa lakini viwanda vyote vinavyofanya kazi ya ufumaji vitambaa nchini vikiwemo 21st Century, Sunflag Limited, Urafiki, NIDA na Musoma Textile vina mitambo yake ya kusokota nyuzi, hivyo soko la ndani la Tabotex kuachwa kwa wafumaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hilo sasa, kiwanda hicho sasa kinatafuta mwekezaji ambaye atakuwa tayari kuingia nacho ubia kwa kupanua wigo wa uzalishaji na kukufua shughuli za ufumaji vitambaa (weaving) hadi ushonaji. Wadau tushirikiane ili tupate mshirika atakayeweza kuboresha shughuli za kiwanda cha Tabotex.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH (K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI) aliuliza:-
Serikali ina mpango wa kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya nchini:-
(a) Je, shirika lisilo la Kiserikali linaweza kujenga chuo hicho katika Kata ya Chuma, Chakola Makao Makuu ya Tarafa ya Manonga na kuikabidhi Serikali?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga chuo hicho ili kiweze kutoa msaada katika Wilaya za Igunga na Nzega?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Manonga, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika Lisilo la Kiserikali linaweza kujenga chuo cha ufundi stadi katika Kata ya Chuma, Chakola, Makao Makuu ya Tarafa ya Manonga na kuikabidhi Serikali. Ili Serikali iweze kupokea chuo hicho, ni vema kabla ya kuanza ujenzi mawasiliano yafanyike kati ya taasisi hiyo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) ili kwa pamoja masuala yote ya kisheria yaweze kuzingatiwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashauri kwamba wakati juhudi mbalimbali za kutafuta fedha na wafadhili wa kujenga vyuo hivyo vya wilaya zinaendelea, wananchi wa Wilaya ya Igunga waendelee kutumia vyuo vya ufundi stadi vilivyopo Mkoani Tabora ambavyo ni Chuo cha VETA Tabora kilichopo Mjini Tabora na Ulyankulu kilichopo Wilayani Kaliua, pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Nzega na vyuo vingine vilivyosajiliwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi.
MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaamua kubadili mita zote za maji ili wananchi wanunue maji kwa mfumo wa unit wao wenyewe kama ilivyo kwenye umeme?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo sugu la baadhi ya wateja wa Mamlaka za Maji kutolipa ankara za maji na kulimbikiza madeni, Wizara yangu inafanya majaribio ya kutumia mfumo wa malipo kabla ya huduma yaani prepaid system. Kupitia mfumo huo, mteja hufungiwa kifaa maalum kinachomwezesha kulipia kwanza kiasi cha maji anachohitaji kabla ya kutumia. Hata hivyo, mfumo huo una gharama kubwa kiuwekezaji na kimatunzo ikilinganishwa na mfumo unaotumika sasa. Kwa sababu hiyo ya gharama Wizara imeagiza baadhi ya Mamlaka kuzifunga mita hizo kwa wateja wake wenye tabia ya kulimbikiza madeni ya ankara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Oktoba, 2017 jumla ya Mamlaka za maji saba zimeanza kutumia mfumo huo kwa baadhi ya wateja wao. Mamlaka hizo ni za Miji ya Makao Makuu ya Mikoa ya Iringa, Arusha, Dodoma, Mbeya, Songea, Tanga na DAWASCO ya Jiji la Dar es Salaam. Mpaka sasa mfumo umeonesha mafanikio makubwa. Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa gharama za mfumo huo, Wizara imeziagiza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Daraja ‘A’ zinategemea kwa gharama zote za uendeshaji kuhakikisha kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao ili kuwezesha kuendelea na ufungaji wa mfumo huo kwa kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu.
MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:-
Tanzania tuna ushindani mkubwa wa Kampuni za Simu na katika Jimbo la Manonga maeneo kama ya Kata ya Mwashiku, Ngulu, Kitangari, Sungwizi, Mwamala, Uswaya, Tambarale na Igoweko hayana minara ya mawasiliano.
Je, ni lini Serikali itazielekeza Kampuni za Simu kusimamia minara yao kwenye maeneo ambayo hayana mtandao wa mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa maeneo ya Kata za, Mwashiku, Ngulu, Ntobo, Kitangiri, Sungwizi, Mwamala, Uswaya, Tambarale na Igoweko hayana minara ya mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uliyaanisha maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Igunga, hususan Jimboni Manonga na kuyaingiza kaitka utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, vijiji vya Matinje na Mwashiku kutoka kata ya Mwashiku, vijiji vya Imalilo na Mwasung’ho kutoka katika kata ya Ngulu, kijiji cha Mwamloli kutoka katika kata ya Ntobo na vijiji vya Igoweko na Uswaya kutoka kata ya Igoweko vitafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi wa Viettel unaotarajiwa kukamilika Novemba, 2017. Aidha, vijiji ya Kitangiri kutoka Kata ya Ndembezi na vijiji vya Sungwizi na Mwamala kutoka Kata ya Sungwizi vimeingizwa katika orodha ya miradi inayosubiri upatikanaji wa fedha ili kutekelezwe, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya suala la kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Chomachankola hasa ikizingatiwa kuwa wataalam wa kilimo walikuja kufanya utafiti na kueleza mpango wa kuchimba bwawa kwa ajili hiyo pale Chomachankola?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA K.n.y. WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali hili naomba kwanza nimpe pole Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kufiwa na kaka yake, na pili nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa kunipa heshima ya kuratibu swali hili alipokuwa safarini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manoga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Chomachankola kina skimu moja ya umwagiliaji inayotumia maji ya Mto Kagon’ho unaotiririsha maji yake msimu wa masika peke yake. Kwenye skimu hii, eneo lililoendelezwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga ni hekta 300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababisha upungufu mkubwa wa maji wakati wa kiangazi mpango wa Serikali ni kusanifu na kujenga mabwawa madogo na makubwa kwenye maeneo kama kama ilivyo Chomachankola yatakayotumika kuvuna maji ya mvua, kuwezesha kilimo cha umwagiliaji katika vipindi vyote vya mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kijiji cha Chomachankola, Serikali imefanya usanifu wa awali wa bwawa lenye uwezo wa kutunza maji mita za ujazo milioni
(a) Mchakato wa bwawa hilo pamoja na yale ya maeneo mengine yaliyoainishwa kuwa yanafaa kuendelezwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya ya Igunga umeingizwa kwenye mpango kabambe wa umwagiliaji utakaoanza kutekelezwa mwaka 2018/2019.
MHE. SEIF K.S. GULAMALI aliuliza:-
Je, ni lini utekelezaji wa usambazaji wa umeme katika Kata za Igoweko, Uswaya, Tambarale, Mwisi, Sungwizi, Mwamala, Ntobo, Ngulu, Mwashiku na Kitangiri utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa usambazaji wa umeme katika Kata za Igoweko, Uswaya, Tambarale, Mwisi, Sungwizi, Mwamala, Ntobo, Ngulu, Mwashiku na Kitangiri utafanyika kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza wa kusambaza umeme vijijini iliyoanza mwezi Julai, 2017 na kukamilika Juni, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kusambaza umeme katika kata hizi inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 zenye urefu wa kilomita 76.48; njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 60.62; ufungaji wa transfoma 36 za KVA 50 pamoja na kuunganisha wateja wa awali 733. Gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 1.22. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa vibali kwa Kampuni za Halotel na Vodacom ili kuweza kuweka minara yao katika Kata ya Igoweko, Uswaya, Tambarale, Mwashiku, Ngulu, Ntobo na Mwamala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kulipatia vizuri kabisa jina langu la kwanza.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haina kizuizi kwa kampuni yoyote inayotoa huduma za mawasiliano kama itazingatia utaratibu wa kuomba vibali vya ujenzi wa minara yao kwa mujibu wa sheria pamoja na kupata cheti cha tathmini ya mazingira kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Hifadhi ya Mazingira (NEMC).

Mheshimiwa Spika, Kata ya Igoweko, Ngulu na Sungwizi zimeainishwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na kuingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambapo TTCL wako katika hatua za mwisho za taratibu za manunuzi ili kuanza kutekeleza miradi hiyo. Miradi hiyo yote inategemewa kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2019.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Kata za Uswa, Tambarale, Mwashiku, Ntobo na Mwamala zitaingizwa katika orodha ya miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kutekelezwa kutokana na upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, tunatoa wito kwa makampuni mbalimbali kuendelea kuwekeza minara ya mawasiliano katika Jimbo la Manonga na maeneo mengine nchini yale hasa yenye uhitaji kwa kuzingatia taratibu.
MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza:-

Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga barabara za Ziba - Puge na Ziba - Choma kwa kiwango cha lami:-

Je, ni lini Serikali itetenga fedha za usanifu wa barabara hizo na hatimaye kuanza ujenzi ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Ziba - Puge yenye urefu wa kilometa 83.06 na barabara ya Ziba - Choma yenye urefu wa kilometa 26.6 ni barabara za Mkoa zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara TANROADS, Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Puge - Ziba na barabara ya Ziba - Choma zitakuwa miongoni mwa barabara zitakazopewa kipaumbele katika kutengewa fedha kwa ajili ya kuzifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo imekuwa ikizitengea fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ili ziendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, kiasi cha shilingi milioni 712.922 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Puge - Ziba na kiasi cha shilingi milioni 170.3 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Ziba - Choma.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. SEIF K. GULAMALI) aliuliza:-

Wilaya ya Igunga ilipata ufadhili wa Benki ya Dunia wa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Simbo, Ziba, Chomachankola na Igurubi ambapo Vituo vya Afya vya Ziba, Chomachankola na Igurubi vimekamilika na vifaa tayari vipo japo majengo na vifaa katika Kituo cha Afya cha Chomachankola na Igurubi bado havijaanza kufanya kazi; Kituo cha Afya cha Simbo bado hakijakamilika na vifaa havipo na Wafadhii walishakabidhi Halmashauri bila kukamilisha ujenzi huo:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kujua nini kilichojificha juu ya Mradi huo kukabidhiwa bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Wilaya ya Igunga ilipata ufadhili wa Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Simbo, Ziba, Chomachankola na Igurubi. Sababu kuu ya kushindwa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati ilitokana na makadirio ya chini ikilinganishwa na gharama halisi za kukamilisha ujenzi. Ili kukamilisha ujenzi wa Vituo hivyo kwa kuzingatia ramani mpya, Serikali ilitoa jumla ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Simbo na Igurubi ambapo kila kituo kilipatiwa shilingi milioni 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Simbo kimekamilisha ujenzi wa majengo ya upasuaji na nyumba ya mtumishi na sasa vifaa tiba vinaendelea kuletwa. Aidha, Kituo cha Afya Igurubi kinaendelea na ujenzi wa majengo manne ambayo ni Maabara, Jengo la Wazazi, Jengo la Kufulia na Jengo la Kuhifadhia maiti. Majengo yote haya yapo katika hatua za ukamilishaji.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mabwawa makubwa na Skimu za Umwagiliaji za Choma Chankola, Ziba na Simbo ambazo zimefanyiwa upembuzi yakinifu kwa zaidi ya miaka sita sasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Bwawa la Choma Chankola lipo katika Kijiji cha Choma Chankola, Kata ya Choma, Wilaya ya Igunga. Usanifu wa bwawa hili umeonyesha kuwa lina uwezo wa kutunza maji mita za ujazo 6,825,757 na maji haya yaliyovunwa yanaweza kumwagilia hekta 400 za mpunga. Hata hivyo, bwawa la Choma pamoja na mabonde yote ya Ziba yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, yameingizwa kwenye Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 kwa ajili ya utekelezaji wake. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Bwawa la Simbo lililopo katika Kata ya Simbo, Wilaya ya Igunga usanifu wake umekamilika. Bwawa hili lina uwezo wa kutunza maji lita 15,228,000 na maji yaliyovunwa yanaweza kumwagilia hekta 1,000 za mpunga. Bwawa hili pia lipo katika Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Mwaka 2018 kwa ajili ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, andiko la Programu ya Ujenzi wa Mabwawa katika Mikoa Kame ya Tanzania (Participatory Dams Development Programme in Semi-Arid Areas of Tanzania) limekamiliika ambapo mabwawa haya ni miongoni mwa mabwawa 88 yaliyopangwa kujengwa katika programu hiyo. Andiko limeshawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kutafutiwa fedha na utekelezaji wake.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano katika Kijiji cha Matinje Ikombandulu ambalo ni eneo la machimbo na lina idadi kubwa ya watu ili kurahisisha biashara katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi mitatu katika Jimbo la Manonga. Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Igoweko; mnara huu unahudumia pia Kata ya Uswaya, Sungwizi pamoja na Ngulu. Utekelezaji wa miradi katika Kata hizi umekamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itakifanyia tathmini Kijiji cha Matinje Ikombandulu na hatimaye kijiji hiki kitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2021/22, ahsante.
MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Tarafa ya Simbo na Manonga katika Jimbo la Manonga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria, ambapo hadi sasa Vijiji vya Ziba, Igumila, Ibologero, Itibula, Mwalamo, Ngulu, Mwabubele, Nyandekwa, Itale na Usongo vilivyoko katika Tarafa ya Manonga, vimefikiwa na huduma ya maji kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuanzia mwezi Aprili, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, utekelezaji wa miradi ya maji utaendelea endapo mradi wa Maji toka Ziwa Victoria utatekelezwa na utanufaisha vijiji vya Ulaya, Nkinga na Barazani vilivyopo katika Tarafa ya Simbo na vijiji vya Imalilo, Ngulu, Igumila, Ndembezi, Itulashilanga, Njia Panda, Mwanzelwa vilivyopo Tarafa ya Manonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zitakazofanyika ni ulazaji wa bomba takribani kilometa 50, kujenga Matenki matano ya kuhifadhia maji katika vijiji vya Igulu (lita 50,000), Ndembezi (lita 100,000), Ulaya (lita 50,000), Kitangili (lita 60,000) na Nkinga (lita 300,000) na kujenga vituo 60 vya kuchotea maji. Utekelezaji wa mradi huu utaboresha hali ya upatikanaji wa maji katika Tarafa ya Simbo na Manonga kufika asilimia 85.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa majosho katika Wilaya ya Igunga, hususan Jimbo la Manonga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Igunga ina jumla ya majosho 20. Kati ya hayo majosho 12 yanafanyakazi na majosho nane ni mabovu na hayafanyi kazi na hivyo kuhitaji ukarabati.

Aidha, halmashauri hiyo inahitaji jumla ya majosho 36 na hivyo ina upungufu wa majosho mapya 16 yanayohitajika kujengwa. Kati ya majosho mabovu nane, majosho matatu yanakarabatiwa na josho jipya moja linajengwa na halmashauri yenyewe kwa kutumia vyanzo vyake vya fedha za ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 jumla ya majosho 10 yatajengwa katika Halmashauri ya Igunga yakiwemo majosho matatu katika Jimbo la Manonga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kukabiliana na upungufu wa majosho, Halmashauri ya Igunga inashauriwa kuendelea kutenga asilimia 15 ya fedha inayokusanywa kutokana na mifugo kwa ajili ya kujenga na kukarabati majosho.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Ziba Wilayani Igunga aliyoitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi 2020?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISMEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif K. S. Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kujenga Vituo vya kutolea Huduma za Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utolewaji wa Huduma ya Afya ya Msingi kwa Wananchi. Ujenzi na Ukarabati wa Vituo unahusisha utekelezaji wa ahadi za viongozi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kutekeleza mkakati huu Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 58.25 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vipya vya afya 233 katika Tarafa na Kata za kimkakati ambazo hazikuwa na miundombinu hiyo. Aidha, Serikali imepeleka shilingi milioni 250 katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Ziba ambapo ujenzi umefikia hatua ya umaliziaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mkakati huu Serikali itaendelea kutoa fedha katika Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi za viongozi za kujenga au kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA K.n.y. MHE. SEIF K. GULAMALI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Choma – Ziba – Nkinga hadi Puge?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Barabara ya Choma – Ziba – Nkinga hadi Puge yenye jumla ya kilometa 109.56 ambayo inapita katika maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Ndala na Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini TANROAD, imeamua kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 kwa lengo la kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kugawa Mkoa wa Tabora na kupata Mkoa wa Manonga ili kurahisisha shughuli za kiutawala na kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuanzisha Mkoa, Wilaya na Tarafa mpya umebainishwa kupitia Sheria ya Uanzishwaji wa Mikoa na Wilaya na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014.

Mheshimwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hii maombi ya kuanzishwa Mkoa mpya hupata ridhaa ya vijiji, kamati za maendeleo za kata, mabaraza ya Madiwani ya halmashauri zilizomo katika mkoa, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ya Mkoa Mama.

Mheshimiwa Spika, katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) cha tarehe 3 Machi, 2022 yaliwasilishwa mapendekezo ya kugawa Mkoa wa Tabora, ambapo ilipendekezwa suala hilo kuwasilishwa katika kikao Maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kitakachofanyika Mei, 2022.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI itakapopokea mapendekezo hayo, itafanya uhakiki na tathmini kisha itawayasilisha katika Mamlaka husika kwa ajili ya maamuzi kadiri itakavyoona inafaa.
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Choma - Ziba – Nkinga - Simbo - Puge utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Manonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Choma – Ziba – Nkinga – Simbo – Puge yenye urefu wa kilometa 109 ambapo Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina amepatikana na ameanza kazi tarehe 24 Agosti, 2023 na anatarajia kukamilisha mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2024. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga mkono wananchi wa Jimbo la Manonga kwa kuwasaidia kujenga madarasa mawili katika kila shule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya mahitaji ya vyumba vya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP imepeleka shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Seif Gulamali. Pia katika mwaka 2021 kupitia mradi wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 jimbo la manonga lilipokea jumla ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 92 kwa shule za sekondari na shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa ya shule za msingi shikizi.

Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 10 vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya Igaunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kadri zitakapopatikana.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga mkono wananchi wa Jimbo la Manonga kwa kuwasaidia kujenga madarasa mawili katika kila shule?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Jimbo la Manonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya mahitaji ya vyumba vya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP imepeleka shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Seif Gulamali. Pia katika mwaka 2021 kupitia mradi wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 jimbo la manonga lilipokea jumla ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 92 kwa shule za sekondari na shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa ya shule za msingi shikizi.

Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 10 vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya Igaunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kadri zitakapopatikana.