Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Seif Khamis Said Gulamali (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwasilisha mchango wangu katika sekta hii. Napenda kuwasilisha mawazo yangu juu ya elimu hasa katika kupanga ada elekezi katika shule binafsi. Ni kweli nchi etu imekuwa na utoaji wa elimu ya Serikali na sekta binafsi katika shule za Serikali. Hilo liko wazi katika ada kwani ni bure, lakini shule binafsi ni shule ambazo wazazi hupeleka watoto kwa matakwa yao bila kulazimishwa na mtu yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi siyo tatizo kwa ada wapangazo, tatizo langu, naiomba Serikali ifuatilie kwa kina kama ada watoazo ni sawa na huduma wapatazo. Maana haiwezekani ada iwe kubwa lakini mahitaji muhimu hayalingani na gharama wazilipazo. Hivyo tunaiomba Serikali ifuatilie kwa kina kama ada zinaendana na huduma zenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwasilisha mawazo juu ya ada zinazotozwa na Vyuo vyetu katika kozi mbalimbali. Mfano Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT katika fani ya Aviation, ada yao ni shilingi milioni 10 ambayo kwa mtoto masikini wa Kitanzania ni bei kubwa sana ambayo hawezi kumudu. Huo ni mfano tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vyuo vingi mfano SAUTI Mwanza, AMUCTA Tabora, Tumaini University, Dar es Salaam na vinginevyo vimekuwa vikitoza ada kubwa katika fani za sheria na nyinginezo tofauti na ada katika Vyuo vya UDSM na UDOM huku vyuo hivi vikipata RUZUKU toka Serikalini. Hili halikubaliki, kwani kwa muda fulani wanafunzi wa vyuo hivi waligoma wakidai ada zishuke. Hivyo tunaomba Wizara ilitazame maradufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Wizara kutoa marupurupu ya ziada kwa Walimu wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi kama Wilaya za Igunga, Nzega, Uyuyi na nyinginezo ili kupunguza wimbi la Walimu kuhama katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sera ya Elimu, inataka kila Wilaya kuwa na VETA, hivyo tuombe Wizara itupe support katika hatua tulioifikia ya uanzishaji wa hivyo basi, katika upungufu wetu tuiombe Wizara itupe ushirikiano katika kufukia azma ya Sera ya Elimu ya Juu na uwepo wa VETA katika Wilaya. VETA ya Manonga Wilaya ya Igunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yetu tuna ujenzi wa Maabara ambapo nyingi zimekamilika lakini tatizo ni vifaa vya Maabara. Tunaiomba Wizara katika Jimbo la Manonga itusaidie vifaa vya Maabara ili iturahisishie upatikanaji wake ili wanafunzi wetu waweze kupata huduma hii ya kusoma kwa vitendo. Shule zote Kata ya Chomachenkole, Ziba, Mkinga, Simbo, Mwisi, Chabutua Ichama, Mtobo-Misana, Ngulumwa, Ndebezi, Igoweko, Mwashiku na Sungumizi tunaomba shule hizi zipatiwe vifaa vya kujifunzia ikiwa ni pamoja na vitabu vya Arts.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapendekezo yetu tunaiomba Wizara itupandishie Shule za Ziba Sekondari pamoja na Mwisi Sekondari ili tuwe na Vidato vya Tano na Sita.
Hili linatokana na shule hizi kwamba ni za Tarafa hapo awali, lakini kutokana na kuwa mazingira ya shule hizo ni mazuri sana ikiwa na ukubwa wa zaidi ya ekari 50 kwa shule ya Mwisi na zaidi ya ekari 10 kwa Shule za Ziba, lakini pia kijiografia shule hizi zimekaa pazuri kwa kuwa tayari kuhudumia wanafunzi wa ndani ya Wilaya hata nje ya Wilaya kutokana na maeneo hayo kuwa na huduma mbalimbali za kijamii. Hivyo, kwa Wilaya yetu ya Igunga kuwa shule hizo zitakuwa zimesaidia kupunguza uhaba wa shule hasa ikizingatiwa kwamba Igunga tayari tuna Shule ya Igunga Day na Nanga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SEIF H. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwasilisha maombi makuu mawili. Moja, ni kuomba Wizara kuweka msukumo wa malipo ya fidia kutoka TANESCO kwenda kwa wananchi wa Kata ya Simbo, Chabutwa na Mwisi kwani kwenye ziara ya Naibu Waziri Mheshimiwa Merdard Kalemani alikuja Jimboni na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tabora aliahidi mbele yake kuwa pesa za fidia zipo na hivyo wanasubiri wamalize tathmini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba Wizara ipeleke msukumo kwa Meneja wa TANESCO ili kuweza kuwalipa wananchi wa Kata hizo husika ili kuondoa misuguano isiyo ya lazima, hizi ni fedha ambazo walipaswa walipwe toka mwaka 2010 mpaka sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Wizara ya Ujenzi na Nishati na Madini, napenda kuwasilisha mawazo yangu juu ya kuongeza substation nyingine ndani ya Wilaya ya Igunga tofauti na ile iliyopo Wilaya ya Nzega katika Mji wa Nzega Ndogo toka pale Nzega Ndogo kwenda Choma ni karibu kilomita 30 na kutoka Choma kwenda Ziba kwenda Igunga ni kilomita 50, jumla umeme umesafiri kilomita 110 bila kuwa na substation. Naomba pale Ziba tuwe na substation, iunganishwe umeme/waya toka Nzega kwenda Ziba ili kupunguza kukatika kwa maana njia ya Nzega Ndogo kwenda Choma nguzo zinapita kwenye majumba hivyo tukipata substation Ziba na network tokea Nzega, Ziba itarahisisha kupunguza tatizo la umeme Wilayani Igunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hayo tu nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi na mimi leo kuchangia katika taarifa hii ambayo imewasilishwa na Kamati ya LAAC.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende ku-declare interest ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC. hivyo basi mambo mengi tumeyaona kupitia ukaguzi ambao tumefanya katika muda ambao tuliokuwa tunashiriki hapa Dodoma na Dar es Salaam. Lakini yako mengi tumeyabaini katika Halmashauri zetu nyingi nchini kama siyo asilimia 100 basi asilimia 99 katika usimamizi hazifanyi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu unaweza ukakuta unapata taarifa ya Halmashauri, lakini ukienda kukagua kwa ndani unakuta wamefanya manunuzi yasiyofuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004. Wanajifanyia utaratibu ambao wenyewe wanaona unafaa sasa mwisho wa siku ukikaa ukagundua ukachimba kwa ndani unakuta tayari wana-interest labda na yule mtu ambaye anataka kufanya ile kazi ama na mambo mengineyo ambayo yapo katika Halmashauri husika na miradi ambayo wanakuwa wanayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii katika report hizi za Halmashauri ambazo tumezikagua na tumeziona, tunagundua kabisa kwamba kutokana na Halmashauri nyingi nchini kupata fedha katika robo ya mwisho au robo ya tatu ya kumaliza mwaka, wanapata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hali ambayo inapelekea hata wao wenyewe Halmashauri kushindwa kutimiza ama kutokukamilisha ile miradi ambayo wamejiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shida hiyo, unaikuta Halmashauri inaingia kwenye mgogoro aidha na wananchi ama inaingia mgogoro na Serikali ama inapokuja kukaguliwa na CAG wanajikuta wapo kwenye matatizo ya kwamba aidha zile fedha walikuwa nazo wameshindwa kuzitumia na baadaye zinakuwa ni bakaa na wakati mwingine zile fedha wanaambiwa wazirudishe Hazina, kwa hiyo, mwisho wa siku ile miradi iliyokuwepo iliyotengewa zile fedha miradi haifanyiki kwa wakati na zile fedha zimerudi Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hali hii kwa utaratibu huu tukiendelea nao kwa namna moja ama nyingine miradi mingi sana itakwama kwa sababu nachukulia mfano hata pale katika Wilaya yetu ya Igunga katika Jimbo la Manonga, yako majengo ambayo wananchi wametoa fedha zao za kuanzisha mfano ujenzi wa zahanati, ujenzi wa nyumba za walimu, ujenzi wa madarasa ya shule, maabara lakini unakuta support wanayotakiwa wapate kutoka kwenye Halmashauri, Halmashauri inaweza ikaandika fedha kuomba kwa ajili ya kumalizia, zile fedha hawapati kwa wakati mwisho wa siku wananchi wanalalamika na sisi Wabunge tukija Bungeni tunalalamika, hali hii inapelekea miradi mingi kukwama na Serikali inapokuja mwaka mwingine wa fedha tunakuja tunaanzisha miradi mipya na tunaenda kuwaambia tena wananchi waanze kuchangia wakati miradi mingine haijafika mwisho, tunaanza kuwaambia wananchi waanze kuchanga tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukianza kumwambia mwananchi achange nyumba ya mwalimu wakati anaona maabara ile pale haijafika mwisho anaanza kukwambia mfano, mbona maabara ile haijamaliziwa na Serikali ilituambia tuchange fedha ili zile fedha wenyewe watamalizia hawajamalizia, leo tujenge nyumba za walimu. Kwa hiyo, hii inaleta mgongano wa kimaslahi kati ya Halmashauri na wananchi lakini pia Halmashauri na Serikali kuu na wakati mwingine hii miradi ambayo inakuwa inaanza haifiki mwisho hivyo basi niiombe sasa na kuishauri Serikali katika suala zima la upelekaji wa fedha, fedha hizi ziende mapema na haraka zaidi ili kuweza kuonyesha kwamba miradi tuliyokuwa tumeipanga katika Halmashauri inatekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tumebaini, Halmashauri nyingi zinakusanya fedha kiholela tu hawatumii EFD machine. Kwa hiyo, kutokana na kutokutumia hizi mashine za EFD inapelekea kukosa mapato makubwa zaidi. Kwa hiyo, niishauri Wizara husika itoe maelekezo kwa Halmashauri zote nchini kwamba watumie EFD machine katika kukusanya mapato yao ya ndani, hiyo yote mpaka katika minada sijui mambo yote wanayofanya vijijini kule. Hii itatupelekea kuongeza mapato yetu katika Halmashauri, lakini itaongeza mapato katika Serikali kuu tukiacha kutumia EFD machine, mapato mengi yatapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuombe sasa Wizara ilichukulie hili na itoe maelekezo na isiwe ombi kwamba toeni maelekezo muda fulani kuhakikisha kwamba Halmashauri zote nchini mpaka kufikia muda fulani sehemu zote za mapato yenu mtumie EFD machine. Hii itasaidia sana kuhakikisha kwamba Halmashauri zinakuwa na hela, Serikali inakuwa na hela, lakini hata ile miradi tuliyokuwa tumejipangia inaweza kutimizwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nipende kuishauri Serikali. Serikali Kuu imetenga fedha mwaka huu asilimia 40 za fedha ziende katika miradi ya maendeleo. Sasa hizi fedha zitakwenda ndiyo lakini huku chini usimamizi wake kama ambavyo tumezungumza, wakati mwingine usimamizi mbovu sasa lazima kuwepo na chombo imara ambacho kitakuwa kinasimamia na kufuatilia na chombo hicho ni chombo ambacho tumekiweka wenyewe kisheria ambayo ni Ofisi ya CAG na kupitia Kamati zetu za LAAC na PAC. Hizi Kamati ndizo jicho la Serikali, lakini ndiyo jicho la Bunge, ndiyo jicho la wananchi kuhakikisha kwamba zile fedha zinazokwenda kwenye Halmashauri zetu zinafanyakazi lazima ukaguzi uwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa zikienda na Ofisi ya CAG ikaenda kukagua, Kamati zikaenda kujiridhisha kuangalia maana yake hata tutakaporudisha Serikalini taarifa maana yake Serikali ichukue taarifa yetu sasa ianze kuifanyia kazi kwamba sehemu fulani wamefanya madudu, sehemu fulani wamefanya madudu. Sasa zinapokosa Kamati hizi fedha kwa ajili ya kufanya shughuli hii ya ukaguzi ama Ofisi ya CAG inapokosa fedha maana yake hata tukipeleka mabilioni ya shilingi kama hamna anayefuatilia maana yake na yenyewe yatapotea, mwisho wa siku maana yake hata yale malengo tuliyokuwa tumejiwekea tutafika 2020 yale malengo yatakuwa hatujayafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niiombe sana Serikali ihakikishe inawezesha Ofisi ya CAG ipate fedha za kutosha za kukagua. Pia Kamati za PAC na LAAC zipate fedha kwa ajili ya kutembelea miradi, hii itaisadia Serikali ya Magufuli kufikia malengo yake iliyojiwekea kufikia mwaka 2020 kwa sababu itakuwa inajua wapi Halmashauri gani imeharibu, taasisi gani imeharibu na hapo hapo inachukua hatua kuhakikisha kwamba zile fedha wanazozitoa zinafanyiwa kazi ili isiwe kwamba vile maana yake Ofisi ya CAG fedha ilizotengewa ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama fedha ikiwa ndogo Halmashauri mwaka huu Ofisi ya CAG inafikiria kwamba inaweza isikague hata Manispaa kumi. Sasa kama itashindwa, maana yake taarifa ya mwakani tutakuwa hatuna hapa na kama Ofisi ya CAG ikikosa kufanyakazi maana yake Kamati hizi za PAC, Kamati ya LAAC itakuwa haina cha kufanya, kwa hiyo, mwisho wa siku niishauri Serikali kwamba hizi ofisi zipewe fedha mapema na waharakishe na washirikiane nao bega kwa bega kuhakikisha kwamba tunafanyakazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilikuwa nataka tu kuishauri Serikali hasa kupitia Wizara husika ya TAMISEMI wafuatilie sana hizi Halmashauri. Kuna hizi asilimia kumi ambazo wenzangu wamezungumza za vijana na akina mama. Hizi fedha ni muhimu sana Halmashauri ikatoa, ziko Halmashauri naona zinafanya vizuri, zinatoa fedha kwa ajili ya kutoa kwa vijana na makundi mbalimbali ya kina mama. Hizi fedha zikitoka kwa mfano, kwenye Halmashauri mapato yetu yawe shilingi bilioni mbili maana yake fedha makundi haya iko zaidi ya milioni 200. Milioni 200 ukazichukua milioni 100 ukapeleka vijana, milioni 100 ukapeleka kwa akina mama, hizi fedha zikaenda kwenye makundi haya na kwenye kata husika maana yake mwisho wa siku…
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana muda wangu umekwisha napenda kuunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi siku ya leo kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kuhakikisha kwamba Tanzania ya viwanda inafikiwa. Pia ninashukuru kwa sababu dhana hii inapozidi kuzungumzwa sana, mwisho wa siku inatafsirika na watu wanaamini na wanaingia katika uwekezaji wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu hiyo Mheshimiwa Waziri mimi nijielekeze, najua unajua nikisimama kuzungumzia kiwanda siwezi nikazungumza mambo mengine nikakiacha kile kilichopo pale kwangu Manonga, Manonga Ginnery. Mheshimiwa Waziri toka nimekuwa Mbunge na siku yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge, nimezungumzia suala la Kiwanda cha Pamba ndani ya Wilaya yetu ya Igunga. Kiwanda hiki ni cha zamani sana, toka enzi za mkoloni mpaka juzijuzi kikabinafsishwa akapewa Rajan, Rajan amekiendesha mpaka na yeye akakishindwa akakiacha, amefikia hatua amefariki, amemuachia mtoto wake, mtoto wake yuko Uingereza mara sehemu mbalimbali. Tumezungumza tukakwambia wapo Igembensabo wanakitaka hiki kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hiki asilimia 80 anamiliki Rajan, asilimia 20 anamiliki Igembensabo. Igembensabo anataka kukinunua hiki kiwanda, ameweka mezani shilingi milioni 500 lakini Rajan amekinunua shilingi milioni 700 anataka kukiuza shilingi 1,500,000,000, kiwanda kimesimama anataka kukiuza kama vile kinafanya kazi, kinaingiza faida na huyu ni mbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, lakini tulikuomba uwakutanishe hawa watu wakae chini, wao wako tayari. Umetuahidi mara nyingi hawa watu utawakutanisha wakae chini wazungumze Igembensabo yuko tayari, hata wao wako tayari, issue yako kama Waziri ni kuwaita hawa ofisini kwako. Juzi juzi hapa katika majibu umesema umefanya jitihada mbalimbali, umetuambia kwamba huyu mtoto wa Rajan yuko Uingereza anakuja baada ya miezi sijui sita au saba, anachelwa. Hivi Serikali hii ya Dkt. John Pombe Magufuli ikitaka kumuita huyu kijana itashindikana kweli? Yaani akakae Uingereza na kiwanda chetu huku, kama hataki kukiendeleza si akiachie wapewe watu wengine waweze kuki-run? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siamini kwamba Serikali hii imeshindwa kumuita, haiwezekani na siamini. Inawezekana, labda Mheshimiwa kwa sababu wewe unasema unapiga-sound inawezekana na mimi kijana wako unanipiga sound, nielewe kwamba hiyo ndiyo sehemu ya kupigana sound, lakini mimi siamini kwamba wewe zile sound unazosema unapiga unamaanisha kwamba unanipiga sound kweli. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, hebu muite huyu kijana ikiwezekana, kama inashindikana si mkitaifishe sasa, mmeshamuita amekataa. Inawezekana hamjamtafuta na wao wako tayari kuja. Mheshimiwa Waziri tunakuomba, na Mbunge mmoja wa Simiyu amesema eti zao la pamba limekufa, si kweli, halijafa, uzalishaji wake umepungua na si kufa. Maana yake ukisema kufa maana yake watu hawalimi kabisa, haiwezekani, kulima tunalima ila si katika kiwango ambacho Serikali ama nchi inataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli uzalishaji wa pamba umepungua si tu katika eneo letu la Wilaya ya Igunga ama Simiyu, katika nchi yetu ya Tanzania uzalishaji wa pamba umepungua; na Serikali haijawekeza vya kutosha na kama hivyo viwanda, ginneries zipo nyingi zimetajwa, na moja wapo ya ginneries kongwe hii ya Manonga ni ginnery kongwe. Katika Mkoa wa Tabora ukizungumza Manonga hakuna ambaye hajui, hakuna Rais ambaye hajui ginnery hii, lakini sijaona Serikali ama Waziri ukiwekeza katika kuhakikisha kwamba kiwanda hiki kinafanya kazi. Waweke chini hawa watu wafanye mazungumzo, watauziana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Tabora uangalie hizi fursa. Sisi tunalima sana maembe Mkoa wa Tabora, tuna nyuki, tumbaku, ngozi nyingi sana, hasa kwa sababu tuna ng’ombe wengi. Hivi Mheshimiwa katika makabrasha haya hauhamasishi katika uwekezaji huku kwetu? Maana kila siku ninasikia tulikuja mpaka airport wawekezaji wameondoka tena, hivi wawekezaji wa kuishia airport kweli? Hawa walikuwa wawekezaji au wasanii?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri, hebu sukuma hili jambo ili kila mkoa uwe na fursa maana ukizungumza viwanda hapa vingi viko pwani na sisi huko kwetu Bara tunahitaji viwanda hivi vije, maana viwanda vikiwepo vitapunguza msongamano wa vijana kuwepo Dar es Salaam. Ndiyo hii unasikia kila siku Dar es Salaam vijana wanavuta bangi, wanavuta dawa za kulevya, hizi vurugu zote zipo Dar es Salaam huko na miji mingine huku kwetu haipo katika kiwango hicho. Hebu tuletee hivi viwanda huko vijana wasikimbie vijijini ama wasikimbie wilayani wakakimbilia mikoa ya pwani huko. Hii itasaidia sana kwa sababu leo hii wanabaki bibi zetu kule nyumbani kwetu wanaonekana vikongwe hawa ama wachawi. Hebu muache kuleta hii dhana, leteni hivyo viwanda ili kupunguza, vijana wawepo wawasaidie wazazi wao, waendeleze maisha na itasaidia kuokoa maisha yetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hili suala la ngozi limekuwa linazungumzwa sana. Ni kweli tunataka tuwe na viwanda vya ngozi ndani ya nchi yetu, sasa ngozi imekuwa nyingi kiasi kwamba wanunuzi hawapo. Tumeweka kodi ku- discourage ku-export ngozi yetu nje ya nchi, lakini sasa hawa ambao tulionao viwanda vyetu havitoshelezi kununua ngozi, mwisho wa siku ngozi zinabaki kwenye machinjio, watu wananunua wanaacha katika maeneo yao. Hebu tupunguze kodi ama tuwa-encourage hawa watu ili kama tumeshindwa kununua ngozi yote badala ya kuharibika wai- export tupate hizo dola ambazo zinatoka nje ya nchi ziingine ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Waziri nafikiri hilo utakuwa umelisikia na utawasaidia hawa wafanyabiashara wa ngozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine mimi ninalotaka kulizungumzia ni hii issue ya One Stop Center. Leo tunaona mtu anapokuwa na kiwanda chake wanakuja watu wa OSHA, NEMC, madubwasha yako mengi. Kwa nini isiwe kwamba mtu yeyote anayetaka kuanzisha kiwanda aende sehemu moja, kama ni TRA alipie madubwasha yote, yeye pale apewe karatasi au sticker moja ambayo ndani yake yumo OSHA, NEMC, TRA na watu wote ili akija mtu wa NEMC iwe ni kujiridhisha tu. Sasa mtu ana kiwanda anaki-run, siku mbili anakuja OSHA anampiga faini anamwambia funga kiwanda, mtu amewekeza kwa gharama kubwa halafu anaambiwa funga kiwanda. Hebu tuwe sehemu ya ku- encourage viwanda vyetu na tuwe sehemu ya kuwasahihisha wenye viwanda ili waweze kuendelea kufanya hii kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi viwanda vinasaidia kutoa ajira kwa vijana wetu na hii inasaidia kupunguza tatizo la vijana mitaani. Unapo-discourage watu wa viwanda unasababisha hawa vijana warudi mtaani wanageuka majambazi, wanageuka vibaka na hatimaye hawa hawa wanageuka kuwa watu ambao si watu wema katika jamii. Tuombe Serikali iwasaidie wenye viwanda hata kama wana matatizo ninyi muwe sehemu ya kutatua matatizo yao na msiwe sehemu ya kuzuia kufanya miradi au kazi zao. Niombe Wizara, nafikiri mtakuwa mmelisikia hilo; naomba sana muwasaidie wafanyabiashara, maana yake tafsiri ya mfanyabiashara sijaelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachojua, mfanyabiashara ni Mtanzania yeyote ambaye anaanza kutafuta kipato chake, mkulima ni mfanyabiashara. Kuna mkulima gani ambaye anazalisha chakula halafu asikiuze? Huyo si mfanyabiashara. Mkulima ni mfanyabiashara kwa sababu anazalisha, anauza. Mwalimu anafundisha, ama sisi Wabunge hapa, wengine tuna hoteli, tuna guest houses, tunafanya biashara, maana biashara ikiharibika mpaka kwenye hoteli zetu biashara zinaharibika huko. Humu ndani ya Bunge katika asilimia 100, asilimia 99 ni wafanyabiashara, tunatofautiana biashara gani tunafanya. Unaweza ukawa Waziri ukawa mfanyabiashara. (Makofi)

Suala lingine kabla sijafika mwisho, nafikiri muda wangu utakuwa si rafiki; kuna mtu alichangia jana hapa akasema Rais wa Kenya amepata chakula kutoka Mexico na chakula kile kinagawiwa kwa bei ya kutoka shilingi 3,000 ya Tanzania kwa maana ya Kenyan shilings 150 kupunguza kwa shilingi 90 ya Kenya sawa na 1,800 ya Tanzania. Hivi kwa saa 24 inawezekanaje Rais akatoa tangazo halafu bei ikashuka kwa kiwango hicho, inawezekana kweli au tunaleta propaganda ndani ya Bunge hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba hata kule alikosema kwamba ametoa chakula kile, Mexico, kwanza tutambue, Kenya sasa hivi kuna Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi Mkuu ni pressure kwa Rais aliyepo hata kwa wapinzani. Kwa hiyo kinachofanyika ndani ya nchi ya Kenya ni siasa, tunachozungumza leo Balozi wa Mexico amekanusha amesema kile chakula hakijatoka Mexico, kwa hiyo tusidanganyane. Mtu analeta taarifa za kutoka huko anasema kwamba eti Kenya wameshusha bei ya chakula, chakula kingi kiasi kwamba…, tuzungume ukweli pale ambapo panastahili ukweli… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia Wizara hii ya Madini. Kwanza kabisa napenda tu kupongeza sana Wizara hii ya Madini ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Angellah Kairuki. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pongezi nyingi sana kwa Naibu Waziri ambaye ni Mheshimiwa Doto Biteko pamoja na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo. Kwa kweli Waheshimiwa hawa wanafanya kazi nzuri kwa sababu tunawaona; siyo kama tukiwaona kwenye vyombo vya habari, lakini pia tunawaona wakiwa field wanakuja katika Majimbo yetu, wanatembea usiku na mchana kuhakikisha kwamba Wizara hii inakwenda mbele. Hongereni sana Mawaziri na timu zenu zote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nataka kuzungumza machache tu, lakini katika mchango wangu nataka nijielekeze kama mchangiaji hapa aliyekuwa akizungumzia kuhusu STAMICO katika usimamizi mzima wa miradi yote ambayo inasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO kwa kweli kama ilivyokuwa na wachangiaji wengine, inafeli katika usimamizi wa miradi na rasilImali hizi za Taifa la nchi hii. Hiyo inadhihirisha wazi, kwa mfano, katika migodi kama STAMIGOLD na hii tunaita Buhemba. Sisi kama Kamati tulienda pale Buhemba tukajionea ule mgodi ulioko pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Buhemba ilikabidhiwa na Mwekezaji mwaka 2008 na ikarudishwa Serikalini kwenye hiki chombo chetu ambacho ni STAMICO. Wakati huo walikabidhi vikiwepo na vifaa; magreda, magari na kila kitu kilichoko mle ndani yakiwemo majumba. Yaani kiasi ambacho unaweza kuanza kesho kuendeleza ule mradi ukasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea, tumekwenda juzi, kabla ya pale kulikuwa kuna kampuni inaitwa G4ST Limited, ni Kampuni ya Ulinzi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba rasilimali zilizokabidhiwa na mwekezaji zinabaki kuwa salama. Hii kampuni ya Ulinzi binafsi iliyokuwa inalinda baadaye ikabidi i-handle kwenye Serikali kwa maana ya Jeshi la Polisi. Ule mgodi sasa ukabaki kama hauna mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichokuja kutokea, pale kuna watu walienda mpaka kung’oa madirisha ya nyumba za watumishi, watu wameng’oa madirisha ya milango ya magari na vifaa vyote vilivyomo mle ndani kwenye mgodi. Yaani sasa imetoka kwenye kampuni binafsi, tumeikabidhi Serikali, Serikalini huko sasa ambako tumekabidhi Jeshi la Polisi wamengo’oa kila kitu, yaani vitu vimeibiwa vyote. Hapo hapo maana yake tayari mgodi umerudishwa STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huu ambao migodi yetu inakuwa ipo chini ya usimamizi wa STAMICO na STAMICO imeendelea kuomba fedha kwa ajili ya kuendesha migodi iliyopo ndani ya nchi yetu. STAMICO imefeli. Binafsi kabisa nasema STAMICO imefeli na tumeipa fedha kwa ajili ya kujaribu. Iendelee kujaribu hivyo hivyo huku ikiendelea kutupa hasara juu ya hasara. Hapa tumeona tuna deni zaidi ya shilingi bilioni 60. Tumezalishiwa na hawa ambao walikuwa wanatusimamia na hatupati faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani sekta binafsi ikisimamia kwenye madini inaleta faida na kampuni inanawiri, mpaka wakati mwingine tunasema kampuni inaiibia nchi yetu. Sasa kama tunaweza tukakabidhi shirika letu wenyewe lisimamie rasilimali lifanye uzalishaji, badala ya kuleta faida linaleta hasara, kwa hiyo hii STAMICO kwa kweli, kwa namna moja ama nyingine, sijui kwa sababu wamesema wamekuja watu wapya wanaanza tena mchakato upya kwenye kusimamia, lakini tunapata wasiwasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kwamba hata hao wataalam ambao wako chini watabadilishwa mpaka huko chini! Maana yake Taifa hili limekosa watu waaminifu. Watu Wazalendo wamepungua, tunawakabidhi rasilimali kuhakikisha kwamba tunapata, nchi yetu tunafaidika kutokana na madini, lakini hao hao tunaowakabidhi na wenyewe imepelekea sasa tunapata hasara badala kupata faida. Mchango wangu kwenye STAMICO ni huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Madini napenda binafsi kuishukuru na kuipongeza kwa sababu katika kuzunguka kwao wamekuwa wanatatua migogoro mbalimbali. Hata walienda kwa Mheshimiwa Kiula pale Jimbo la Mkalama, Kijiji fulani cha Tumuli, wametatua tatizo pale. Mheshimiwa Nyongo nadhani ndio alifika pale, ametatua na sasa hivi tunaenda kupata suluhisho la mgogoro ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge yule alikuwa anakushukuru sana, lakini kwa sababu ni majirani, nami natambua tunahusiana kwa sababu migodi hii inatembea ikitoka pale Tumuli inakuja Shelui na Shelui iko Igunga pale Igurubi. Ametatua mgogoro mkubwa sana katika eneo hili, tunampongeza sana watu wa maeneo ya kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuzungumzia kuna suala hili limeibuka. Tumeona tangazo limetolewa na Mkuu, nafikiri Serikali ya Mkoa wa Geita kwamba inazuia carbon zisisafirishwe kutoka Geita kwenda Mwanza. Sasa hii sijaelewa ni sheria inakuja ama inakuwaje? Ndani ya nchi yetu tunazuia usafiriishaji wa carbon kupeleka kwenye viwanda sehemu nyingine ambayo mtu anataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anaamua kupeleka kwenye kiwanda ambacho anaona kinafaa. Haiwezekani ulazimishe kwamba carbon niliyonayo ifanyiwe processing ndani ya mkoa wangu. Tunatafuta ubora wa kazi zinavyotakiwa kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaniambia nibaki labda nifanyie hizi process zote katika Mkoa wangu wa Geita, lakini ni katika viwanda vilivyoko Geita labda havina ubora wa kuchenjua dhahabu ninavyotaka. Inawezekana nilikuwa na-expect kupata kilo moja au kilo tatu. Nikifanyia Geita ama nikifanyia ndani ya mkoa wangu wa Tabora sipati hizo kilo mbili au tatu, lakini nikipeleka labda mkoa jirani wa Shinyanga, Mwanza au Arusha nikapata kilo tatu, usinizuie mimi ambaye nawekeza, ninayefanya hii kazi kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo tangazo tumeliona, watu wenye sekta hii ya madini wanalalamika. Namwomba Mheshimiwa Waziri alichukue na atoe maelekezo kwamba hii amri ya kuzuia watu wasisafirishe carbon kupeleka mkoa wowote ule katika nchi yetu, iondolewe na isiwepo katika utaratibu ambao ni rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba carbon mtu apeleke sehemu yoyote ili mradi afuate sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini, kwa maana ya vibali na vitu vinginevyo, lakini wasizuie watu wasiende katika mkoa mwingine kufanya kazi ambayo yeye anahitaji. Kazi hizi ni bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nataka kuchangia suala zima la wawekezaji katika migodi. Wanatumia umeme mkubwa sana na pia gharama za uendeshaji wa migodi hii ni kubwa sana. Naomba Wizara ya Nishati isaidie, gharama za umeme ni kubwa sana katika viwanda hivi. Tuna-discourage uzalishaji kwa sababu gharama ya kulipia umeme ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri akae na Waziri wa Nishati ili waone namna gani watakavyoweza kusaidia wawekezaji katika Sekta ya Umeme kwa sababu hizi units ambazo wanalipa zinakuwa ni kubwa sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alichukue hilo na walifanyie kazi ili wapunguze gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanya hizi wata- encourage wawekezaji wengi zaidi wawezeke katika Sekta ya Madini. Nafiri hilo Mheshimiwa Waziri atakuwa amelichukua na wataenda kulifanyia kazi na watavutia zaidi wawekezaji kwa sababu mwekezaji anaweza kutumia generator akapata faida kuliko kutumia umeme wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mtu akiamua kutumia generator, hebu angalia na generator ni gharama kubwa sana. Pamoja na gharama kuwa kubwa mtu anaona ni bora kuliko kutumia TANESCO, namwomba Mheshimiwa Waziri wakae chini waone ni jinsi gani ambavyo wanaweza kuwasaidia hawa watu ili kuhakikisha kwamba nchi yetu haipotezi mapato ambayo inahitaji katika sekta hii kutokana na kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuchangia ni kuhusu suala zima la ruzuku. Hapo siku za nyuma tulikuwa tunatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wadogo katika kuwawezesha kufanya kazi zao na kuweza kufikia katika malengo. Mheshimiwa Waziri nasi kule kwetu kwa maana ya Jimbo la Manonga katika Kata zile za Mwashiku, Nguru na Ntobo tuna madini na wachimbaji wadogo wadogo wapo, waliwahi wakati fulani kupata ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri, hebu tutilie mkazo katika hili zoezi la kutoa support kwa wachimbaji wadogo wadogo, watu wa Jimboni kwangu waweze kupata lakini pia wa maeneo mengine katika nchi yetu wapate hizi ruzuku kutoka katika Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia kuhakikisha kwamba tunawanyanyua wachimbaji wadogo kwenda kuwa wachimbaji wa kati, lakini pia kesho na kesho kutwa watafikia katika level ambayo watakuwa walipaji wa kodi wakubwa sana katika nchi yetu. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunajikwamua na umaskini tulionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa hatufurahii kuona kila siku tukiendelea kuwa walalamikaji ama tukiendelea kuwa katika hali ya ambayo kila siku ni maskini. Hili neno maskini inatakiwa lifike wakati tuliondoe katika nchi yetu ya Tanzania. Kuliondoa ni katika kuwawezesha hawa wachimbaji wadogo wadogo na wao wafikie katika level ambayo kila sehemu akienda anatambulika, huyu mtu anastahili kuwepo katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango wangu huu mdogo, napenda sasa kuishukuru Serikali, Wizara, lakini Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kweli siwezi kuacha kumshukuru kwa sababu anafanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha kwamba rasilimali hii ya madini inalindwa na nchi inanufaika kutokana na rasilimali Mwenyezi Mungu amelijalia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Wizara, Mheshimiwa Dkt. Mpango, pamoja na Naibu wake kwa kuwasilisha, lakini pia watendaji wakuu kwa maana ya Katibu Mkuu - Ndugu James Doto na wengineo, kwa bajeti nzuri ambayo imeandaliwa na kupunguza baadhi ya tozo na ada mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda nichangie kwenye huu ukurasa wa 81 wa hotuba ya Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango ambapo anazungumzia hatua za kisera na kiutawala katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ambapo hapa amependekeza kuweka utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini ambapo wananchi wa kawaida wataruhusiwa kutoa mizigo bandarini bila kuwa na ulazima wa kutumia Wakala wa Forodha kwa maana ya Clearing and Forwarding Agent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nizungumzie hapo kidogo na tujadili pamoja na Mheshimiwa Waziri hapa atuambie, mimi ninavyofahamu uwepo wa hizi agencies za freight clearing and forwarding, kwanza uwepo wao wapo kwa Sheria ya East African Community Customs Management Act ya mwaka 2004 as amended time to time. Lakini pia makampuni haya yanapokuwa yanafanya usajili wake, kwanza yanafanya mitihani katika Chuo cha Kodi na hawafanyi tu mitihani kwa maana huwezi kumchukua mtu yeyote akaenda kufanya mtihani wa kodi pale akafaulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaofanya mitihani utakuta makampuni zaidi ya 1,000 yanaomba yapate leseni ya kufanya kazi ya u-agent ya kutoa mizigo bandarini ama airport na sehemu zingine bandari kavu. Utaratibu huu wa kufanya mitihani inahitaji upate kijana aliyesomea, aliyebobea na kijana aliyesomea aliyebobea anasomea kati ya miezi nane mpaka miaka mitatu kazi ya kutoa mizigo bandarini, kazi ya kutoa mizigo katika bandari kavu, kazi ya kutoa mizigo katika viwanja vyetu vya ndege. Ni kazi iliyosomewa na yenye weledi wa hali ya juu sana, siyo kazi kwamba unaweza kuifanya mtu yeyote kirahisi kama ambavyo inaweza kuzungumzwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naweza nika-declare interest; mimi mwenyewe nimeisomea hiyo kazi, kwa maana ninaifahamu by profession. Kwa hiyo, ninapozungumza naizungumza kwa maana naielewa nje/ndani. Unapofanya registration, unapokwenda kufanya mtihani kati ya makampuni 1,000 yanayokuja kupata leseni hayazidi makampuni 100, kati ya 1,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya makampuni ambayo yanapata leseni ndiyo yanaweza kupewa leseni ya kufanya kazi hii ya kutoa mizigo bandarini. Lakini pamoja na kupewa leseni lazima waweke bond kwa maana ya kwamba chochote kikitokea aidha fraud au chochote, bonds zao zinakuwa ni security ya kulinda kazi zao au kampuni yao au kulinda upotevu wa fedha za kodi katika Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, makampuni haya yanaajiri vijana wasomi, ambao wamesoma. Leo ukiniambia tu kila mtu afanye as huge, utapata makanjanja wengi sana, upotevu wa kodi ya Serikali utakuwepo mkubwa sana, kwa sababu makampuni haya pamoja na kufanya kazi ya clearing agent, yanafanya kazi ya kukusanya kodi ya Serikali. Kwa hiyo, yanapokusanya yanasimama kwa niaba ya Serikali, at the same time hawalipwi na Serikali, lakini wanaisaidia Serikali kukusanya kodi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuwepo kwa ma- agents hawa tuwaboreshee mazingira yawe mazuri zaidi kwa sababu Serikali inahamasisha katika uwekezaji, inahamasisha katika kuwepo kwa viwanda, inahamasisha kuwepo kwa makampuni. Leo kampuni inaweza kuajiri na katika field hii wapo zaidi ya vijana 15,000 wameajiriwa. Leo ukisema kiholela maana yake ajira za vijana waliosoma zaidi ya 15,000 watapoteza kazi zao. Kwa hiyo, unapoteza ajira katika kazi hizo za ukusanyaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vyuo vinavyotoa kozi za ku-clear mizigo, kwa mfano Chuo cha Kodi Dar es Salaam wanafundisha pale miezi nane lakini mpaka mwaka mmoja, mpaka miaka mitatu, wanatozwa ada, makampuni yanalipa ada za wanafunzi hao. Leo unavyosema kila mtu akajifanyie, hivi unafikiri ni kazi rahisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza unaambiwa ukatoe mzigo wako, lazima ufanye classification ya mzigo wako, je mwananchi wa kawaida kutoka Choma cha Nkola anaweza ku-classify mzigo wake? Maana ku-classify mzigo kuna HS Codes, codes za mizigo, lipo likitabu likubwa sana, nani atafanya? Maana yake utaanza kutafuta vishoka wafanye kazi hizo kienyeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, lazima ufanye valuation ya mzigo, valuation hawezi kufanya huyo mwananchi wa kawaida, hawezi. Lakini bado lazima ufanye documentation; nani mwananchi wa kawaida anaweza kufanya documentation. Bado uingie kwenye mfumo wa ASYCUDA ama hii system wanatumia sasa hivi ya TANCIS.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima usomee, unaingia kwenye computer unafaya log documents zinakwenda TRA wanakujibu. Leo mnataka kuturuhusu kila mtu apige simu TRA kuuliza HS Code ya mzigo wangu ni ngapi? Sasa TRA watafanya kazi ya kutoa huduma ya kutoa HS Codes badala ya mawakala wafanye hizo kazi? Hili suala namuomba Mheshmiwa Dkt. Mpango aliangalie kwa makini, lakini atambue uwepo wa mawakala hawa. Wanafanya kwa mujibu wa East African Community Customs Management Act. Kwa maana hiyo kama tunataka kila mtu ashiriki maana yake turekebishe sheria zetu za customs za Afrika Mashariki ndiyo twende pamoja. Kwa sababu suala hili halifanyiki Tanzania peke yake; uwepo wa mawakala Uganda wapo, Kenya wapo, dunia nzima wapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tutambue kwamba kazi hizi, makampuni haya yanapokuwa yanafanya yanaleta ajira. Lakini pili, makampuni yanalipa kodi kama Corporate Tax, PAYE, VAT, Withholding Tax, vyote vinaigiza katika Serikali, inakusanya mapato, leo ukiondoa hizi kodi zote utazikosa. Lakini kingine makampuni haya yana-deal na shipping line, yana-deal na ICDs, TBS, TFDA, Government Chemist; mwananchi wa kawaida ataweza kufuatilia vitu vyote hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango liangalie suala hili kwa undani zaidi. Nikuombe sana tusiliendee kichwa kichwa maana yake leo utapitisha hivyo, mwaka unaokuja utakuja utarekebisha tena; tutakuwa tunakwenda mbele au tunarudi nyuma?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tutambue kwamba mizigo inapokuwa kwenye manifest ni lazima sheria za forodha zi-apply, sheria za kimataifa zi-apply, sheria za uchukuzi zinataka utumie Mawakala wa Forodha. Sasa kama mzigo ukishakuwa kwenye manifest leo umwambie mtu wa kawaida tu aka-clear mzigo wake, anau-clear vipi? Maana yake manifest, Sheria za Uchukuzi za kimataifa zinaelekeza utumie agent; sheria za uchukuzi zinaelekeza utumie agent; sheria za forodha zinaelekeza utumie agent, haiwezekani tu mtu wa kawaida. Lakini utaua makampuni, utapoteza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini utambue mfumo unaotakiwa kimataifa according to World Trade Organization, World Customs Organization wa kuondoa mizigo bandarini ni kutumia mawakala na sisi kama Tanzania tumesaini kwamba tutatumia mawakala, leo unakwenda kuondoa nguvu ya mawakala ama agents.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto za mawakala, lakini changamoto hizo tu-set down, zipo Wizara wanasema hata hawa makampuni hawajawaajiri hawa vjana wetu; tufuatilie kwa sababu sheria inaeleza kwamba makampuni hayo yaajiri. Kwa hiyo, Wizara ifuatilie kwenye makampuni hayo iangalie mikataba ya ajira ya vijana wetu ili wawe na uhakika wa soko lao. Otherwise tutazalisha vijana wanaozurura mitaani, tutazalisha vishoka mitaani, lakini tutaongeza rushwa katika TRA, tutaongeza makanjanja mitaani, kutokuwepo kwa kumbukumbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango, leo unaweza ukaifuata kampuni yoyote kwa sababu kwa mujibu wa sheria kampuni lazima itunze kumbukumbu zake ndani ya miaka mitano. Unaweza kufuata ukamwambia hebu lete niangalie mizigo ndani ya miaka mitano mmefanya nini. Je, mtu wa kawaida utampata wapi akupe kumbukubu za ku-clear mzigo wake kwa miaka mitano, ama mnataka kuruhusu wafanyabiashara au wengine, leo atatumia jina la Seif ku-clear mzigo wake, kesho atatumia jina la Gulamali ku-clear mzigo wake, keshokutwa ataenda Juma Athumani, hutapata kumbukumbu itakuwa ni kupoteza tu. Hata ikitokea fraud utamkamata nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa hiyo nikuombe sana uliangale hili kwa mapana yake kwa maana siyo suala la kuingia kichwa kichwa. Pili, linatunza ajira za vijana wetu. Huko mitaani vijana wako wengi sana wanasoma, wame-qualify. Lakini siyo tu kuajiriwa ndani ya nchi yetu, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, hii ni fani unapoiua maana yake unapoteza vijana wa Kitanzania ambao wanaajiriwa, siyo kufanya kazi ndani ya Tanzania, wanafanya kazi katika dunia. Ukienda Ufaransa utakutana na watu hawa, ukienda Uingereza utakutana na watu hawa, ukienda China utakutana na watu hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo yako masomo na curriculum katika vyuo vyetu yanafundishwa masuala ya kutoa mizigo yetu bandarini. Ukiua kwa urahisi namna hii maana yake unaondoa vijana wetu katika mfumo rasmi, unakwenda kuwafanya wawe sasa katika mfumo, hata mimi ambaye namlipia ada mtoto wangu nitamwambia kwa sababu Serikali imesema mtu yeyote, kwa hiyo achana na masuala ya shule. Kwa hiyo, badala sasa ya kumuweka katika mfumo rasmi, unamuondoa kwenye mfumo rasmi unampeleka awe kanjanja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana katika marejeo yako utakapokuja ninakuomba uje utoe ufafanuzi wa kina juu ya suala hili. Naomba sana Serikali tusiende katika mkanganyiko ambao tunauona huko mbeleni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. Ahsante sana, naunga mkono hoja, hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwisho kwa siku ya leo katika Wizara hii ya Afya. Kwanza nipende kutoa pongezi nyingi kwa waliopata nafasi hii, Mawaziri hawa, Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla. Hongereni sana maana tunatambua jitihada zenu mnazofanya kuhakikisha kwamba Taifa linasonga mbele hasa kwenye sekta ya afya na afya ni uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia kwenye sekta hii ya afya hasa kwenye eneo la CHF. CHF ilipokuwa inaanza mwanzo mfano katika Wilaya ya Igunga ilikuwa ni sehemu mojawapo ya majaribio na ilifanya vizuri sana kiasi kwamba Wilaya zingine zilikuwa zinakuja kuangalia namna gani imefanya vizuri katika Wilaya ya Igunga. Matokeo yake sasa hivi si tu wilaya zilikuwa zinakuja kujifunza Igunga lakini sasa CHF Igunga inafanya vibaya kama ambavyo inavyofanya vibaya katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, mwanzo CHF ilikuwa na Mfuko wake, akaunti yake ambapo zile fedha zilizokuwa zinakusanywa zinahifadhiwa sehemu moja, lakini baada ya Waraka uliotolewa na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba kila Halmashauri iwe na akaunti zisizozidi sita ikapelekea fedha za CHF kwenda kwenye akaunti za halmashauri na fedha zile zikawa zinabadilishiwa matumizi. Kutokana na kubadilishiwa matumizi kunakuwa na upungufu wa fedha za kununulia dawa.
Mheshimiwa Spika, hivyo tunaomba Wizara hizi mbili zikae chini ziangalie upya ili Mfuko huu wa CHF urudi kama ilivyokuwa awali, iwepo akaunti special ya CHF. Ikiwepo akaunti special ya CHF itapelekea kurudisha ubora, lakini pia itapunguza uhaba wa dawa katika hospitali zetu. Maana tunawahamasisha wananchi wajiunge katika CHF, lakini mwisho wa siku akienda kwenye vituo vya afya hakuna dawa. Kwa hiyo, tuombe Wizara ya Afya katika hili waliangalie upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kuzungumzia suala ambalo limezungumzwa na ndugu yangu hapa, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe la ADB. ADB wamekuwa wanafadhili katika nchi yetu katika eneo la afya. Katika Wilaya yetu ya Igunga na wilaya nyingine Tanzania ADB wameweza kujenga majengo mazuri katika vituo vya afya na hospitali zetu. Wamejenga majengo mazuri pale Choma, Nanga katika Jimbo la Mheshimiwa Kafumu, Igurubi, Hospitali ya Wilaya ya Igunga na katika hospitali mbalimbali ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napata wasiwasi jinsi hii miradi inavyotekelezwa kwa sababu sehemu nyingine wanajenga wanafika mpaka mwisho na vifaa vinapelekwa, lakini sehemu nyingine wanajenga jengo linaishia katikati, kwa mfano, katika Tarafa ya Simbo, Kata ya Simbo, jengo limejengwa limeishia katikati na hakuna vifaa vilivyopelekwa. Unajiuliza hizi fedha za wafadhili zinasimamiwa na watu gani? Haiwezekani kwingine zijengwe zifike mwisho na vifaa viletwe, tena vya gharama kubwa, sehemu nyingine jengo tu lisimalizike. Kwa hiyo, naomba Wizara ipitie upya, waangalie hii miradi inayofadhiliwa na wafadhili isimamiwe vizuri ili kuweza kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, siyo tu kusimamiwa maana tumeona pamoja na majengo kwisha na vifaa kuletwa, kwa mfano pale Choma Chankola, Igurubi, Itumba na maeneo mengine ambayo kaka yangu Mheshimiwa Bashe ameyazungumza na mengine yako kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwake kule, wamejenga wameweka na vifaa lakini vituo hivi havijafunguliwa, vinakaa muda mrefu bila kufanya kazi. Wameweka vifaa yenye thamani kubwa ukiangalia unaona kabisa vinatakiwa vianze kutumika.
Mheshimiwa Spika, pia Theater zinajengwa vizuri wanaleta na vifaa safi lakini zinachelewa kufunguliwa, tunajiuliza kuna tatizo gani? Hakuna wasimamizi wanaofuatilia kila siku kuona hivi vitu ambavyo vinawekezwa na wafadhili havipotei ama haviharibiki maana vinatelekezwa mpaka watu waanze kulalamika au watu waanze kupiga kelele majukwani huko mitaani ndiyo tuanze kujua kwamba kumbe kuna miradi ya wafadhili ambayo haitiliwi maanani.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika Wilaya ya Igunga katika Jimbo la Manonga pale Simbo, mradi umeishia katikati unakabidhiwa kwenye halmashauri halafu wanasema eti halmashauri imalizie. Halmashauri inatoa wapi fedha ya kumalizia miradi mikubwa ambayo imeanzishwa na wafadhili hawa? Kwa hiyo, tuiombe Wizara, hii tabia ya wafadhili wanakuja wanafadhili halafu wasimamizi wale wanafikia katikati eti wanawaambia halmashauri wamalizie wanamaliziaje? Hata vifaa vinavyotakiwa viwekwe wanavitoa wapi na fedha ziko wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe Wizara ipitie upya suala hili, warudi waangalie katika wilaya hizo nilizotolea mfano za Igunga, kwa kaka Mheshimiwa Kafumu, kwangu mie, ukienda kwa Mheshimiwa Zedi tatizo lipo, ukienda kwa Mama Sitta kule najua litakuwepo na kwa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla lipo na kwa Mheshimiwa Bashe lipo.
Mheshimiwa Spika, naomba hii miradi inayofadhiliwa na wafadhili waisimamie ili tufike mwisho, isiwe inafika katikati inatelekezwa, baadaye inakuwa kero na kero hii inakuwa moja ya changamoto ndani ya chama na Taifa. Kwa hiyo, niombe Wizara iangalie na kuhakikisha inaboresha katika maeneo hayo niliyozungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Wabunge wenzangu wamezungumza kuhusu masuala ya Basket Funds zinavyokuwa haziendi kwa wakati katika hospitali zetu. Niombe Wizara kwa sababu wanasema hizi Wizara zimeungana au zinafanya kazi pamoja na TAMISEMI wahakikishe wanafuatilia kujua hizi Basket Funds zinakwenda kwa wakati kwenye halmashauri ili kupunguza uhaba wa dawa katika hospitali zetu.
Mheshimiwa Spika, hospitali hazifanyi kazi wanakwambia Basket Funds haijaja matokeo yake kunakuwa na mlundikano wa wagonjwa ambao wanakosa dawa hatima yake wanapoteza maisha hawa ambao wanatakiwa wapate tiba. Kwa hiyo, niombe Wizara iangalie hili zoezi na walipitie upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo nataka kuchangia ni kwenye hizi zonal hospital. Tumeona kuna Hospitali ya Bugando, tumeona Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini lakini sijaona hospitali ya Kanda ya Magharibi. Kwa hiyo, niiombe Wizara iangalie upya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kuwapeleka katika kanda hizi nyingine. Mkiiboresha Hospitali ya Kitete mkaipa hadhi ya kuwa Hospitali ya Zonal, basi hata kama siyo Hospitali ya Kitete mnaweza mkaipa hata Nkinga Hospitali kuwa hospitali ya zonal ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenda katika hizi hospitali zinginezo. Hizi hospitali zilizo ndani ya Mkoa wa Tabora geografically zilivyokaa zinaweza kuhudumia watu kutoka Kigoma, Shinyanga, Singida na wengine kutoka Katavi pamoja na Rukwa. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iangalie zonal hospital katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia hii Hospitali ya Mkoa wetu wa Tabora ya Kitete, toka tumeifahamu ina X-ray ya miaka nenda rudi, inakufa, kila siku wanafanya marekebisho. Hii Wizara iangalie namna gani italeta X-ray mpya ili kuboresha huduma za watu wa maeneo yale lakini iendane na kasi ya ongezeko la watu katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia hospitali zetu za wilaya, japo mmesema kwamba hospitali hizi zipo TAMISEMI na Wizara ya Afya iko kwa mbali sana, naomba sana hospitali hizi ziangaliwe.
Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda niunge mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote, nipende kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo langu la Manonga na wananchi wote kwa ujumla wa Wilaya yetu ya Igunga, Mkoa wa Tabora kwa kunipa fursa hii adimu ya kuwawakilisha na kwa imani kubwa waliyoijenga juu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote leo tupo katika kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais na katika hotuba ile Mheshimiwa Rais alizungumza mambo mengi, mojawapo kubwa …
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, naomba ubadilishe microphone, hiyo uliyopo inaleta mwangwi, naomba uhamie microphone nyingine.
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake…
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ile Mheshimiwa Rais alizungumzia mambo mengi na kwa uzito wa kipekee alizungumzia suala zima la utumbuaji wa majipu. Kwa kweli suala hili la utumbuaji wa majipu linaendana kabisa na suala zima la
rushwa na ufisadi katika nchi yetu. Pia inaendana na kauli ya Mheshimiwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipozungumzia maadui wakubwa katika nchi yetu, ambapo alitaja maadui ujinga, maradhi, umaskini na
rushwa hii sasa inaingia katika maadui wakubwa wanne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili la kutumbua majipu Mheshimiwa Rais alisema sisi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumuunge mkono na tumuunge mkono bila kujali itikadi ya vyama vyetu vya siasa. Tumuunge mkono kwa maana kazi hii si kazi ndogo, ni
kubwa na alizungumza kwa machungu makubwa. Sasa mimi nitashangaa kama kuna watu watakuwa wanazungumza kwa kubeza hotuba ile ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini anavyokuwa anatumbua wakati mwingine utumbuaji wake hauangalii chama cha siasa. Majipu hayo aliyataja yapo ndani ya CCM lakini pia yapo kwenye vyama vya CHADEMA, CUF na wananchi wa kawaida. Maana yake mtu yeyote fisadi
anajifichaficha kwenye vyama wakati mwingine hata nje ya chama ili mradi yeye aangalie namba gani atatuibia. Kwa hiyo, katika utumbuaji huu tushirikiane Wabunge wote kumuunga mkono katika jitihada ambao anazifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii si rahisi na siyo ndogo. Kwa mfano, tumeweza kupata taarifa wengine tuliziona kwenye magazeti na kwingineko kuna baadhi ya watu walioenda kufanya hitilafafu katika ofisi ya TRA na kuiba computer na taarifa zingine. Maana yake nini?
Yote hiyo ni kuficha taarifa ambazo tayari kuna watu ambao wanashiriki kwa namna moja ama nyingine kulihujumu Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati wanatumbuliwa na Mheshimiwa Rais anachukua hatua mbalimbali dhidi ya watumishi hawa maana matatizo haya ni kutokana na watumishi waliopo ndani ya Serikali kwa muda mrefu ambao kila zama zinazokuja wao wamo.
Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walikuwepo, utawala wa Mzee Mwinyi wapo, utawala wa Mzee Mkapa wapo, utawala wa Mzee Kikwete walikuwepo na utawala wa Mheshimiwa John Pombe wapo. Sasa katika kutumbuliwa naamini kabisa kuna wafuasi ambao
wapo kwenye vyama vingine wanaumia jinsi ambavyo Rais anavyochukua hatua dhidi ya hao watapeli wetu na wahujumu uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais katika hatua mbalimbali anazochukua dhidi ya watumishi ambao siyo waaminifu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wasiseme hapa kwamba Mheshimiwa Rais anakiuka Katiba, sheria na taratibu mbalimbali hapana tumuache Rais achukue hatua dhidi ya watu hawa ambao wanatuhujumu katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hujuma hii athari yake inalikumba Taifa letu na ndiyo maana kila siku tunakuja na kauli mbiu za kuhakikisha kwamba tunawakomboa Watanzania kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo. Matatizo haya yapo na yataendelea kuwepo na sisi
viongozi tutamaliza miaka mitano tutaenda kuomba kura tena, maana yake matatizo mpaka tutakufa hatutaweza kuyamaliza. Kila siku ni lazima kuangalia tunapunguzaje hizi kero zilizopo.
Ndiyo maana tunaomba kura kila baada ya miaka mitano mtuchague ili tupunguze matatizo.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika sera ya Mheshimiwa Rais ya „Hapa Kazi Tu‟ katika hotuba yake ukurasa wa 13 amesema kwamba Serikali ya Dkt. Magufuli itakuwa ya viwanda.
Viwanda hivi tunavizungumza hapa vilikuwepo toka enzi ya Mwalimu lakini vingine vilikufa toka enzi hiyo ya Mwalimu, vingine vilikufa enzi ya Mzee Mwinyi na vingine vilibinafsishwa enzi ya Mzee Mkapa na vingine vilibinafsishwa enzi ya Kikwete na watendaji wengine ambao wapo
dhama zote na wamefanya kazi miaka yote hii na katika ubadhirifu huu wameshiriki kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, katika uchukuaji hatua, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais aendelee kuyatumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili suala la viwanda, tuwaombe Mawaziri washirikiane na Rais kuhakikisha kwamba vile viwanda vilivyokuwepo awali tuanze navyo hivyo kwanza.
Tujue status yake, tujue tunawezaje kuanza na hivyo kabla hatujaanza kufungua viwanda vingine. Kwa mfano, kwenye Jimbo letu la Manonga tulikuwa na ginnery ya pamba inaitwa Manonga Ginnery ambayo ilikuwa inasaidia na ku-stimulate wananchi wa maeneo yale kulima kwa wingi zao la pamba. Matokeo yake toka kubinafsishwa kwa kiwanda kile hata uzalishaji wa zao la pamba umepungua. Mwisho wa siku zao hili litapotea maana wananchi sasa wanakwenda kulima mazao ya chakula badala ya biashara na mazao ya biashara yanasaidia
kuongeza pato la nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika hotuba ile ya Mheshimiwa Rais alizungumzia matatizo makubwa ya maji ambayo wananchi tunayo. Kila Mbunge humu anazungumzia tatizo la maji, hilo ni kweli ni tatizo sugu katika nchi yetu na tunatambua tuna vyanzo vingi vya maji.
Niiombe Wizara ya Maji kwa sababu Mheshimiwa Rais anakwenda na kasi ya viwango na yenyewe ikimbie haraka, tuchimbe mabwawa kwenye maeneo ambayo ni makame ili yasaidie kutunza maji kwa kipindi chote cha masika na kiangazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Choma Chankola, Tarafa ya Manonga, walikuja watu wa Kanda ya Magharibi kufanya survey wakatuhakikishia watachimba bwawa kubwa ambalo litahifadhi maji na kilimo cha umwagiliaji kitafanyika. Ni miaka mitatu toka wamekuja wale wataalam hatujasikia lolote.
Tunaiomba sasa hii kasi ya Mheshimiwa Rais na hawa waliopo chini kwenye Wizara waendane nayo sawa, wasipishane. Siyo Rais anakimbia wao wanatembea, hatuwezi tukalikubali na kuliunga mkono na tutalisema hili kuhakikisha kwamba na wao wanakimbia
ikiwezekana wakimbie kuliko Rais. Tena Rais ifike hatua awaambie punguzeni kasi maana ameshawazidi kasi kwa mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia aliahidi kusaidia wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu. Kwenye Jimbo la Manong, kwenye Kata ya Mwashiku, Ntogo na Ngulu kuna wachimbaji wadogo wadogo. Tunaiomba Wizara pia iangalie namna gani itaweza
kuwasaidia hawa wachimbaji kuhakikisha kwamba wanajikwamua kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote, kuna mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ambao unatoka Mwanza kupitia Nzega unaenda Tabora lakini ukifika Nzega unakwenda Igunga, ukiwa unakwenda Igunga unapita pale katikati panaitwa Ziba ambako ni
junction ya kwenda makao makuu ya Tarafa ya Manonga na Tarafa ya Simbo. Tuliahidiwa kwamba yale maji yataweza kufika katika maeneo yale. Tunaiomba Wizara maana tuliona tayari fungu lilishatengwa kwa ajili ya kazi ya kupeleka maji lakini leo kwenye taarifa zetu inaonekana kwamba usanifu utaanza mwaka 2016/2017. Niiombe Wizara ipitie upya taarifa zao ili kuhakikisha kwamba…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali muda wako umeisha, naomba ukae tafadhali.
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafsi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SEIF KHAMIS SAID GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Kwanza napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kumpa nafasi hii Waziri dada yetu, Mheshimiwa Dkt. Ndalichako. Mheshimiwa Ndalichako una historia ndefu sana katika Wizara hii ya Elimu. Tunaamini toka hapo kabla hujapata nafasi hii ulikuwa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Elimu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, Mheshimiwa Waziri, sisi kazi yetu kama Wabunge ndani yetu, umoja wetu, ikiwa Wabunge wa Upinzani au Wabunge wa CCM, kwa ujumla wetu, kazi yetu ni kukusaidia wewe Mheshimiwa Waziri. Siyo kukubebesha mizigo ya lawama ambayo haina sababu za msingi. Sisi kazi yetu ni kukusaidia kujua namna gani utaweza kwenda kwenye mfumo wako, kuurekebisha au kuboresha ili watoto wetu wapate elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kumsaidia Mheshimiwa Waziri. Sehemu moja viko vitabu vinavyotolewa shuleni na baadhi wamezungumza wenzangu, unakuta shule „X‟ inatumia kitabu fulani na shule „B‟ inatumia kitabu fulani; vitabu hivi ni tofauti lakini somo ni moja. Halafu wanakwenda kufanya mtihani mmoja ambao unatofautiana mafunzo ya vitabu vyenyewe. Nakuomba Mheshimiwa Waziri ukaliangalie hili tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwe kitabu kimoja nchi nzima, kama Darasa la Kwanza, kitabu cha Kiswahili cha mwandishi fulani, basi nchi nzima kiwe na mfanano wa syllabus zote iwe mfumo mmoja. Isiwe huku syllabus tofauti huku syllabus tofauti, tukienda kwenye mtihani, watoto hawa wanaenda kukutana na paper ambazo hawajawahi kukutana nazo katika kufundishwa kwao. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie hili, wataalamu wanatusikia, wakalifanyie kazi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, linguine, kuna tatizo la ufujaji wa mitihani. Kuna kipindi fulani ikifika mitihani ya Kidato cha Nne, Form Six unasikia mitihani imevuja na kunakovuja mitihani huku kunaathiri sana watoto wote wa nchi nzima waliofanya mitihani. Wako wenye dhamira njema na wale ambao dhamira yao siyo njema. Wanaovujisha mitihani ni Watumishi ambao wanafanya kazi ndani ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipata kufanya mtihani wa Form Four 2004, mtihani ulivuja. Ulipovuja, wakati wengine hatukupata hata hiyo paper, tulipoenda kwenye mtihani unakutana na paper wanakwambia mikoa mingine ambayo wamepata maendeleo paper ile tayari wanayo. Wakaenda kufanya mtihani wakapata marks za juu, kuna watoto ambao wanaenda kufanya hata paper hawakuwahi kuiona, lakini Wizara ama wataalamu wanao-standardize matokeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ku-standardize matokeo mnapelekea kuwaumiza watoto wengine ambao hawakuweza kupata hata huo mtihani. Hamwangalii nguvu kazi iliyotumika kwa watoto ambao wametoka katika mazingira magumu hasa ya vijijini. Watoto wa Mjini wanapata paper, wanajua jinsi gani wanavyozipata katika Wizara. Mwangalie hao watumsihi ambao sio wema, siyo kuwapa maonyo, ni kuwafukuza kazi na ikiwezekana wachukuliwe hatua za kisheria za kufukuzwa kazi na kuwekwa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la Walimu. Napenda kuzungumzia Walimu. Walimu wanagawanyika katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Yako mazingira mazuri ya Walimu wanayofanyia kazi, lakini yako mazingira ambayo siyo mazuri ambayo Walimu wanafanya kazi. Kwa mfano, katika Wilaya yetu ya Igunga Jimbo letu la Manonga, eneo kubwa ni vijijini. Walimu hawa wanakuja kule vijijini lakini allowance zozote zile, promotions za kuwafanya waishi mazingira yale, hawapewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iangalie hao Walimu wanaokwenda kufudisha katika maeneo hatarishi, maeneo ambayo siyo rafiki kwao, muwape promotion ya kiwango fulani ya fedha ambazo zitaweza kuwashawishi kuweza kumudu kuishi katika mazingira haya. Haiwezekani mshahara na posho ufanane kwa kila kitu. Mwalimu anayefundisha Chomachankola na Mwalimu wa Shule ya Msingi anayefundisha Temeke au Kinondoni. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni lazima mliangalie na mlitilie nguvu kuhakikisha kwamba hili tatizo mnalitatua haraka ili ku-promote hata Waalimu wanaofundisha Kinondoni wawe wana hamu sasa ya kuja kufundisha Choma, Simbo na maeneo mengineyo ya vijijini. Hii itaweza kurahisisha upatikanaji wa Walimu na kuondoa hii kero ya Walimu; kila wakifika Kijijini wanakaa muda wa mwezi mmoja, wanaomba uhamisho. Anakwambia mama yake mgonjwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wa Manonga kwa kutuombea dua familia yetu na hatimaye jana kuweza kufanikiwa kupata mtoto wa kiume, nashukuru sana. Hiyo ni taarifa nawaambia wananchi wa Manonga nimepata mtoto wa kiume ambaye sasa atajulikana kwa jina la Salim, ni mtoto wangu wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye hoja husika katika Wizara hii ya Nishati na Madini, kwanza nimpongeze Waziri aliyepata nafasi ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Medard Kalemani. Ni viongozi imara, shupavu, wanawajibika na wanafanya kazi kweli. Nawaunga mkono kwa sababu natambua juhudi wanazoendelea kuzifanya na natambua vita kubwa ambayo wanapambana nayo ndani na nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hayo yote nipende kuchangia katika sehemu moja inayohusu vinasaba. Niishauri Wizara ama tushauriane, katika sehemu hii jana liliibuka suala hili la vinasaba katika ajenda zetu humu ndani. Limezungumzwa na kuna mtu mmoja ambaye ame-declare interest kwamba yeye ni mfanyabiashara na masuala haya ya vinasaba yanahusika kwake na ameeleza faida na hasara. Siku ya leo tumepata document inatembea humu ndani ikieleza faida ya vinasaba. Sasa mimi hapa nimepata walakini kidogo, inawezekana, maana kuna Wabunge sasa kama wanafundishwa kusifia na wengine wanafundishwa kukataa, mivutano imekuwa mikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tujadili kwa maslahi ya nchi yetu, tusijadili kwa maslahi ya mfanyabiashara au ya Serikali au ya kukandamiza watu au watu wapate mlungula, kwa sababu inaonekana kuna watu humu wanajadili huku hata document yenyewe tunayoisoma mpaka tuisome, ueleweshwe, uanze kuja kusifia, hii document inatoka wapi ya kufundisha watu jinsi gani ya kuzungumza humu ndani?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ni makini sana document hii inazungumzia faida ya vinasaba, umepatikana msukumo kutoka wapi kuja kuwafundisha Wabunge kuzungumza faida ya vinasaba? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe sasa Wizara hii husika, Mheshimiwa Sospeter Muhongo ni mtu makini, isije kuwa hapa kuna watu wanapokea hela kuja kusifia ama kuja kuponda. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, Wizara yake iende ikayafanyie kazi, ajue kwenye vinasaba kumejificha nini? Inawezekana tunapata faida lakini kuna watu wanapata faida kwa kupokea rushwa. Haiwezekani hapa watu wanazungumzia vinasaba, wengine hata biashara hawaijui wala hawajawahi kuifanya!
Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe Mheshimiwa Waziri, hili suala la vinasaba, nimepata wasiwasi kuona document hii imekuja humu, Wabunge wanafundishwa jinsi ya kuchangia, hii hapa ninayo. Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri waende wakaliangalie vizuri hili suala zima. Inawezekana tunawakandamiza wafanyabiashara ama tunawa-favour wafanyabiashara. Kwa hiyo tukaangalie, tusije tukawa tunawaumiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine hata hii EWURA sijaielewa vizuri, hizi Kanuni za uanzishwaji wa petrol stations sheria ziko Dar es Salaam, zinatakiwa zisambazwe kwenye Halmashauri zetu kule. Maana unakuta wafanyabiashara wana vituo vyao vya mafuta wanaambiwa hana hiki, hana hiki, ukiuliza sheria hana sheria, sheria ziko wapi, wanazo ofisini kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Sheria hizi zisambazwe ili wananchi wawe wanafahamu, wawe na uelewa wa jinsi gani ya kuendesha biashara hizi kuliko kukaa tunawabambikiza kesi milioni tano faini, tunawaumiza. Lazima tuangalie pande zote mbili, upande wa Serikali lakini pia tuangalie upande wa wafanyabiashara.
T A A R I F A...
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, dakika zangu zilindwe. Nafikiri hapo sasa Wizara itaangalia jinsi gani ya ku-handle hiki kitu, kwa sababu tayari imeshaanza kuingia migongano ya mawazo, kuna wengine wanasifia na wengine wanaponda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze pia katika matatizo ambayo nilikuwa nazungumzia EWURA kusambaza hizi sheria katika Halmashauri zote nchini ili wananchi wanaotaka kufungua hivi vituo vya mafuta watambue ili kuweza kuhakikisha kwamba wanafanya biashara zao wakiwa salama badala ya baadaye kuwatwisha mizigo na kuleta hasara kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo niiombe Wizara hii ya Nishati ikae chini iangalie kwa kina, fedha za mafuta zinakusanywa na EWURA, Wizara ya Nishati na madini haiwezi ikajitengenezea utaratibu au tukatengeneza sheria hapa ambayo itawasukuma wao ingawa chombo hiki kiko chini yao. Maana EWURA wanasimamia maji, sijui mafuta, na vitu vingine vya kupanga bei. Sasa niiombe Wizara iliangalie kwa kina jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuchangia hayo nijielekeze kwenye Jimbo langu la Manonga. Nipende kumpongeza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Jimboni kwetu akaangalia maeneo yetu, tuna maeneo ya uchimbaji wa dhahabu. Pamoja na kuona changamoto mbalimbali alijionea mwenyewe jinsi gani tuna vijiji karibu 40 havina umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji vya Mwatinje, Mwashiku, kuna Kata ya Ngulu, Kata ya Ntobo, Kata ya Igoweko, Kata ya Uswaya, Kata ya Utambarale, Kata ya Mwamala, Kata ya Sungwizi, Kata ya Kitangiri, maeneo yote hayo hayana umeme. Naiomba Wizara iangalie, inapogawanya mpango wa REA phase III, basi tuwekwe kwenye program hii tupate umeme. Tunahitaji umeme kama vile ambavyo maeneo mengine yanavyohitaji kupewa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo alikuja Naibu Waziri, Mheshimiwa Kalemani alizungumzia ufutaji wa leseni kwa baadhi ya waliomiliki maeneo makubwa ya ardhi ambayo yana rasilimali ndani yake hayaendelezwi kwa miaka mingi sana. Akatoa tamko akasema kuanzia leo nimefuta leseni ya haya maeneo na aliitaja kampuni moja ya Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoshangaza mpaka leo wale wananchi aliowapa maelekezo waende wakafuatilie wapate haki ya kumiliki ardhi ili waweze kufanya kazi ya uchimbaji mdogo mdogo pale, walikwenda pale ofisini Tabora, wakaambiwa process hii bado, hatujapata tamko kutoka Wizarani, hatujapewa maandiko, hao wahusika alikuwa nao, mgongano huu wa kauli mbili tofauti umetoka wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Wizara yake iangalie vizuri ili kuangalia huu mgongano wa kimaslahi usiweze kujitokeza. Leo tunaambiwa kwamba huyu aliyepewa lile eneo la ardhi leseni yake itakwisha mwezi wa tisa, lakini hapo hapo siku ile alifuta ile leseni yake, hapa mgongano unatokea wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wachukue hatua, kama wamefuta leseni maana yake wamefuta from the sport na hapo wanaanza kutoa maeneo kwa wadau wa maeneo husika, mwisho wa siku itakuja tarehe hiyo ya kufuta watatuambia ameomba Mwekezaji mwingine kutoka nje ya maeneo yetu. Naomba sana Wizara iliangalie hili la mgawanyo wa rasilimali hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua mgogoro alikuja Kamishna wa Madini, alikutana na watu kutoka Nzega wakizungumzia mgogoro wa Resolute. Likatoka agizo, amemwondoa yule mtu aliyekuwa kwenye lile eneo la Resolute, aliyekuwa Mwekezaji amekaa kinyume na utaratibu. Akasema from the sport aondoke, lakini mpaka tunavyoongea dakika hii yule bwana anaendelea kufanya kazi zake katika lile eneo la Resolute Nzega.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba hii Wizara ya Nishati, haya matamko yetu ambayo yanatoka Wizarani hawa walioko chini wanayachukuliaje na wanayafuatilia kwa namna gani, ili tunapotengeneza mazingira tutengeneze mazingira ya uaminifu. Siyo tu uaminifu kwa Wabunge, tutengeneze uaminifu pia kwa Serikali yetu ili tuaminiwe. Serikali iaminiwe, Wabunge waaminiwe na wananchi wafanye kazi zao kwa usalama. Hizi kauli mbili zitapelekea kuleta mgongano wa kimaslahi kati ya yule mwekezaji na wananchi ambao wanataka kuwekeza katika lile eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa mgogoro ambao utakuja kujitokeza katika eneo la Resolute Nzega, tulitatue haraka iwezekanavyo kutokana na kauli ambayo Mheshimiwa Waziri alishaitoa ya kwamba hawa watu waondoke, wawaachie hawa wananchi na waweze kujipatia kipato chao cha chini, waweze kuhangaikia kupata vitu viwili vitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimezungumza kuhusiana na matatizo haya ya umeme, hayapo tu katika Jimbo la Manonga, yapo pia katika eneo letu la Wilaya yetu ya Igunga. Mgogoro upo wa madini katika Kata ya Nanga. Kuna mwekezaji Mchina alikuja pale, akasema anataka lile eneo, akataka kuingia contract ya kulimiliki eneo lile, akawaambia shilingi ngapi wakakubaliana milioni mia tano. Wale wananchi wakakubali wakaandikishana mikataba, wakapewa milioni mia mbili za kianzio.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu baadaye tena anakuja anataka sasa awe mbia, waendelee na yeye kama mzawa. Ukienda ukifuatilia Mchina yule amepewa sijui kibali cha uraia cha muda gani. Niombe hata watu wa Uhamiaji wanapotoa vibali vya uraia waangalie, mtu anakaa, ameshaanza kutengeneza mazingira ya mwezi mmoja, miezi miwili, anakwenda Immigration anaomba uraia, anapewa uraia anaanza kuja na documents za kusema nipewe sasa kama mzawa. Wizara hizi ziangaliwe kwa umakini. Tuna mgogoro pale Nanga kati ya Mwekezaji huyo ambaye ni Mchina ili tuutatue.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SEIF K. F. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii nyeti, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu, napenda kujielekeza katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa 128 alipokuwa akizungumzia masuala ya elimu katika masuala mazima ya usafirishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona namna gani ambavyo tuna vyuo mbalimbali vinavyotoa kozi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya usafiri katika nchi yetu. Nijielekeze kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji. Chuo hiki ni Chuo ambacho kiliasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wetu wa Awamu ya Kwanza, mwaka 1975. Ni Chuo cha muda mrefu ambacho kimekuwa kikitoa kozi zinazohusu usafirishaji, kozi ambazo huwezi kuzipata kwenye vyuo vingine nchini. Miaka ilivyokuwa inakwenda, uwezo wa chuo ulikuwa unapungua kwa kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia miaka ya katikati miaka ya 2000, nilipata bahati ya kujiunga katika chuo hiki. Wakati nimeenda kuchukua Bachelor ya masuala ya uchukuzi, nilisoma mwaka wa kwanza na mwaka wa pili nikapata nafasi ya kuomba kuwa kiongozi, nikawa Rais wa wanafunzi pale Chuoni. Kwa hiyo, nilipata fursa ya kuingia katika Bodi za chuo, lakini nilipata fursa ya kutambua changamoto zilizopo ndani ya Chuo kile. Moja ya changamoto, Chuo kile kina majengo ambayo wameanzisha kuyajenga kwa ajili ya maendeleo au kupanua wigo katika kudahili wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walianzisha jengo mwaka 2004 lenye ghorofa nne na likapangiwa phase namna gani Wizara itapeleka fedha kwa ajili ya kulijenga lile kulimalizia; Wizara imepeleka phase; mwisho phase tatu. Phase ya nne wamewaambia wamalizie wenyewe. Chuo hiki kitapata wapi fedha za kumalizia jengo kubwa, linalohitaji gharama kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia jengo limechukua muda mrefu, tunaona Wizara mbalimbali zinavyoweka nguvu katika vyuo vyao katika kuhakikisha kwamba vinapanua wigo wa kuongeza majengo na infrastructure ya chuo, lakini Chuo cha Usafirishaji jengo limejengwa miaka 11 halijakwisha mpaka leo. Naiomba Wizara ya Uchukuzi iangalie hili suala mara mbili mbili; kama siyo macho mawili, basi waongeze na la tatu. Haiwezekani tule ng‟ombe mzima tushindwe kumalizia mkia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda tu kugusia, Chuo hiki kinatoa kozi ambazo sehemu nyingine huwezi kuzipata. Kwa mfano, wameanzisha School of Aviation. Pale kuna kozi ya Aircraft Maintenance Engineering ambayo kwa Tanzania huwezi kuipata; lakini TCAA wanachukua wanafunzi wanapeleka nje ya nchi kuwasomesha watoto wetu wa Kitanzania; gharama ya kusoma hii kozi nje ya nchi ni karibu shilingi milioni 100 kwa miaka mitatu. Chuo kimeanzisha kozi hii, gharama yake ni shilingi milioni 30 kwa miaka mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wa kimaskini wa Kitanzania, wameomba mikopo katika Bodi ya Mikopo. Sera ya Bodi ya Mikopo, katika watu wanaochukua engineering, ada zao hazizidi shilingi milioni moja na nusu, lakini kwa wale ambao wanachukua Udaktari wanapata mkopo mpaka wa shilingi milioni sita. Hawa watoto wanaokwenda kusoma pale wanaambiwa ada kwa mwaka ni shilingi milioni kumi. Sasa naomba Wizara iangalie hii, shilingi milioni moja Bodi ikilipa, wanabaki watoto wale wanadaiwa shilingi milioni tisa.
Wanapata wapi watoto wa kimaskini kulipa shilingi milioni tisa kwa ajili ya kusoma kozi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ikae pamoja na TCAA badala ya kutumia fedha nyingi kwenda kusomesha nje ya nchi ni bora wawalipie watoto wetu wasomee hapa, waboreshe miundombinu ambayo pale chuoni inatakiwa iboreshwe ili kuhakikishwa kwamba hiki chuo kinaendana na hadhi na Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyuo hivi kwa Afrika wakati vinaanzishwa vilikuwa vinne tu; utakipata Tanzania, Afrika ya Kusini, Ghana na Egypt. Vyuo hivi ni adimu. Wakati nasoma, nimesoma na wanafunzi kutoka Botswana na Malawi; lakini sijaona kabisa jitihada za Wizara kuwekeza fedha kwenye chuo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara sasa ichukue jukumu la kuhakikisha kwamba, chuo hiki sasa kinapiga hatua; miundombinu ya pale iboreshwe. Vyuo vimeanzishwa kama UDOM; Chuo cha Nelson Mandela vinaanzishwa miaka mitatu minne mitano kinakamilika. Chuo cha miaka zaidi ya 40 bado tunakitelekeza na bado hiki chuo ni icon ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuchangia katika suala hilo la chuo hicho nipende sasa kujielekeza katika masuala ya ujenzi, nizungumzie Jimboni kwangu, Jimbo la Manonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kipindi kabla ya kampeni Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alikuja kwetu Choma Chankola akaahidi ujenzi wa daraja la Mto Manonga, lakini nadhani Wizara inachanganya, inashindwa kutambua hili daraja liko upande gani. Rais alitoa maelekezo waje watutengenezee daraja kutokea Choma kwenda pale Shinyanga Samuye, daraja lile lillitakiwa lijengwe muda mrefu lakini ukienda kwa wataalam hawa, ukikutana na Meneja wa TANROADS Mkoa anakwambia mara huku, haendi specific sehemu ambayo daraja linatakiwa likajengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe kupitia Wizara hii kuwaambia, Mheshimiwa Dkt. Magufuli alikuja Choma 2011 akatuahidi ujenzi wa daraja la Manonga. Amekuja tena akiwa anagombea Urais akasema sasa nimekuwa Rais, daraja tutajenga na barabara ya lami tutaweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara sasa itambue ahadi hizi kwa muda mrefu. Kipindi ahadi ile inatolewa 2011 walikuwepo dada zangu Halima Mdee pamoja na Sabreena Sungura, walijificha pale Choma mwezi mzima wakiomba kura za CHADEMA, lakini siku hiyo Mheshimiwa Dkr. Magufuli alipofika akawaambia wananchi 2011 tuchagueni, tupeni kura, daraja tutatengeneza. 2011 Dkt. Kafumu akapata kura, 2015 nikawaambia sasa Jimbo limegawanywa, tumepata Jimbo letu, kwa sababu tumepata Jimbo letu maana yake tutatengenezewa daraja hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ahadi zimekuwa ni nyingi, niiombe sasa Wizara iangalie mara mbilimbili, tunahitaji daraja hili lijengwe. Likijengwa Daraja hili kutoka Choma kwenda Shinyanga hazizidi kilometa 50, lakini kutoka Choma ili uende Shinyanga sasa inakubidi urudi Ziba kilometa 30, utoke Ziba uende Nzega kilometa 30, kilometa 60, utoke Nzega kwenda Shinyanga kilometa 80, maana yake utembee umbali wa kilometa 140 badala ya kilometa 45 kwenda Shinyanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ilijenge daraja hili la Manonga, lakini pia mtuwekee ile barabara ambayo Mheshimiwa Rais ametuahidi ya kutokea Ziba kwenda Choma, Ziba kwenda Nkinga mpaka Simbo pamoja na kwenda Ndala na Puge. Barabara hii Mheshimiwa Rais alitoa ahadi hiyo, kwa maana ya kuwa kwanza inapita maeneo ambayo tuna hospitali ambazo zinatoa huduma si tu kwa watu wa Jimbo la Manonga, wanatoa huduma kwa watu wa Wilaya nzima ya Igunga, Wilaya ya Nzega, Wilaya ya Tabora Mjini, Mkoa wa Mpanda na Mikoa ya Kigoma wanakuja kutibiwa katika hospitali ya rufaa. Tuna hospitali ya rufaa, lakini hatuna miundombinu ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Wizara ihakikishe kwamba ile barabara yetu ambayo inapita kwenye hizi hospitali, tuna hospitali mbili kubwa, hospitali ya rufaa ya Wapentekoste na hospitali ya mission ya RC, tunayo pale Ndala. Tunaomba tupate hiyo barabara ambayo itasaidia kupunguza adha ya wagonjwa wanaopita katika maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara ya muda mrefu ambayo iko chini ya TANROADS. Hivyo basi, nipende kuiambia Wizara ya Ujenzi, katika kuja kutujibu basi katika finalize yao sijaona kwenye kitabu chao wameacndika chochote. Hivyo basi, napenda kuhakikisha kwamba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo kuchangia bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza nampongeza Waziri kwa kazi nzuri kwa bajeti aliyoiwashilisha na tumeona asilimia 40 imetengwa kwa ajili ya kutatua kero za wananchi, fedha za maendeleo asilimia 40. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu nijielekeze kwenye ofisi ya CAG. Wabunge wengi wamezungumza juu ya kumpa uwezo CAG ili aweze kufanya kazi mimi binafsi na-declare interest, ni Mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jicho letu ni CAG, lakini pia hata Bunge hili CAG ndiye jicho letu. Pamoja na wote kuwa jicho letu ni CAG hata Rais mwenyewe jicho lake ni CAG. Haiwezekani tuseme hapa kazi tu, tutenge fedha nyingi tupeleke kwenye maendeleo na sehemu mbalimbali halafu tusimtengee fedha mtu ambaye anaweza kuzikagua ili kurudisha feedback kwa Mheshimiwa Rais kwamba, fedha ulizopeleka zimetumiwa kwa kiwango gani kwa utaratibu mzuri au mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Mheshimiwa Rais aweze kutamba ni lazima apate report kutoka kwa CAG na ndipo ataweza kumsaidia yeye sasa kujua wapi wanaharibu na wapi wanafanya vizuri. Hivyo Ofisi ya CAG hiyo bajeti iliyotengwa ya bilioni 42 ambapo maombi yake yalikuwa ni zaidi ya bilioni 65, tuombe Wizara itenge fedha, siyo aje aombe, itengwe fedha kwa ajili ya utendaji kazi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameona kila Mbunge akisimama akizungumza anazungumzia uwezeshwaji wa Ofisi ya CAG, nafikiri ame-take note hapo, kwamba CAG inatakiwa sasa katika ku-finalize akapeleke fedha ili tumwezeshe huyu. Hata PCCB hawezi kufanya kazi bila CAG, haiwezekani PCCB afanye kazi, kwa report kutoka kwa nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopunguza fedha za bajeti ya Ofisi ya CAG maana yake LAAC na PAC zinakuwa hazina kazi ya kufanya, lakini hata Rais report yake ya kutambua wapi kuna udhaifu atashindwa kutambua. Tunaomba sasa Wizara iangalie jinsi ya kuwasaidia hiyo Ofisi ya CAG kwa kuwapa fedha ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nichangie kwenye hili suala; Serikali ina nia nzuri ya kuweka tozo katika crude oil katika alizeti, ina nia nzuri katika kukusanya mapato lakini tuangalie outcome yake isije kutokea kama ile ya sukari. Muda mfupi uliopita ukatokea uhaba wa sukari na mwisho wake tukaanza kufanya kutafuta njia za haraka kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashauri tunapoweka tozo hizi ambayo ilikuwa haipo mwanzo tutasababisha upungufu wa mafuta haya ambayo uhitaji wake ni zaidi ya lita laki sita na uzalishaji wetu ndani ya nchi ni karibu laki moja na nusu, hivyo, kuna asilimia 75 ya mafuta haya tunaagiza nje ya nchi. Kwa hiyo, tuangalie athari yake isije kutokea sasa kwa wauza chipsi hawa maana mafuta yanapanda bei kutokana na tozo hii au ulipaji wa kodi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafuta haya yakipanda bei hata muuza chipsi atazipandisha bei chipsi zake, hata mama ntilie anayeuza chakula pale naye atapandisha bei chakula chake. Hiyo itapelekea yule mbeba zege kununua chakula kwa mama ntilie kwa bei ya juu. Kwa hiyo tunapandisha maisha ya mtu wa chini yaende kuwa ghali zaidi hali itakayopelekea ugumu wa maisha kujitokeza kwa kasi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Serikali iangalie hii tozo isije ikaja kuumiza watu wa chini. Nia ya Serikali ni nzuri; tuangalie, Mheshimiwa Rais ana uchungu sana na watu wa chini, lakini kutowekeza katika sehemu kama hizi ambazo zinawagusa moja kwa moja watu wa chini tutawaongezea ugumu badala ya kuwarahisishia maisha. Niombe Wizara ya Fedha iangalie tozo kwenye hii crude oil hasa kwenye mafuta ya sun flower na mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze lingine la maji. Tumeona jitihada za Serikali katika kutatua kero mbalimbali za nchi yetu, mfano tumeona jitihada kubwa za ujenzi wa barabara Tanzania, tumeona jitihada kubwa inayofanyika katika kutatua tatizo la umeme vijijini lakini hatujaona Serikali ikiwekeza kwa njia ya dhahiri ya dhati kabisa kutatua tatizo la maji nchini kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila Mbunge akisimama hapa anazungumza tatizo la maji, kila Mbunge akisimama maji, maji, maji, sasa kumbe ipo haja, hebu tuongeze fedha, tutenge fedha za kwetu kwa ajili ya kutatua tatizo la maji, kwa maana tuongeze. Wameshauri hapa wengine wamesema tuongeze Sh. 50/= kwenye mafuta na Mfuko wa Maji uwepo, kwa sababu miradi mingi ya maji inayotekelezwa ni fedha za wahisani, fedha zetu wenyewe hatujawekeza vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna uhaba wa maji, uhaba wa maji kwa mama zetu, uhaba wa maji kwa mama lishe, uhaba wa maji kwa wafugaji, uhaba wa maji kwa kada mbalimbali ndani ya nchi yetu. Tuangalie sasa namna gani huu Mfuko wa Maji tunauweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo Sh. 50/= tubariki sasa ipitishwe, ili fedha itakayopatikana ipelekwe kwenye kutatua shida ya maji. Tukisimama hapa tunamwangalia Waziri wa Maji. Mbunge yeyote atakayesimama anazungumzia maji. Kwa hiyo, hii inaonesha suala la maji hatujalipa uzito wa hali ya juu. Sasa ni wakati wa kuhakikisha kwamba, tatizo la maji tunaliondoa ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza wengine hapa tuna mabwawa, tuna maziwa, tuna bahari, tuna vitu vingi, lakini bado tumebaki kuwa na tatizo la maji ndani ya nchi yetu. Ukienda nchi zingine za wenzetu ambazo zina uhaba wa vyanzo vya maji wanatatua tatizo hili la maji wenyewe wakati sisi tunavyo lakini tuna tatizo la maji ndani ya nchi. Niombe Wizara iangalie namna ya kulitatua hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naweza nikachangia ni juu ya suala la bajeti. Tunatenga bajeti hapa, tunaiomba Wizara, fedha hizi ziende kwa wakati, kwa sababu fedha tunavyozipitisha hapa halafu mwisho wa siku tunakwenda kwenye mwezi Machi au Mei mwakani tunakuta asilimia tano, kuna sehemu zimepelekwa asilimia 10, asilimia saba; mwisho wa siku maana yake ile kazi kubwa tuliyoifanya na kutumia muda mrefu kuijadili ile miradi inashindwa kutekelezeka kwa wakati. Niiombe Wizara ipeleke hizi fedha kwa wakati ili miradi na yale malengo ya Serikali yaweze kutimizwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nichangie pia kwenye suala zima la lugha yetu ya Kiswahili. Lugha yetu ya Kiswahili tunatambua mchango wake ndani ya nchi yetu na juzi kati nimesoma katika vyombo vya habari Zimbabwe wameanzisha somo la lugha ya Kiswahili katika mitaala yao. Je, fursa hizi Tanzania tunazitumiaje? Mabalozi wetu watumie fursa hii kwa kuwaangalia vijana wetu, vijana wetu ndiyo hivyo wana-graduate, wamesomea mambo haya ya kufundisha Kiswahili, lakini hatujapeleka Walimu wa kutosha nje ya nchi kwenda kufundisha lugha hii ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Taifa la Kenya linapeleka watu wetu sana wanafundisha mpaka vyuo vikuu, lugha ya Kiswahili. Nilipata bahati ya kuhudhuria kongamano moja nchini Ekuador mwaka 2013. Nilikutana na mwanafunzi ametoka kusoma chuo kimojawapo nchini Marekani, akaniuliza umetokea nchi gani nikamwambia Tanzania…
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wangu umekwisha. Ahsante sna na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SEIF K.S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia leo katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipotoa shukrani zetu hasa kwa watu wa Manonga, Wilaya ya Igunga ama Mkoa wa Tabora kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pia kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji hasa baada ya kusaini ule mkataba wa maji ya Ziwa Victoria Mkoani Tabora hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini mradi huu wa maji ya Ziwa Victoria unaenda kupunguza uhaba ama tatizo la maji hasa kwa wananchi wetu ambao ni wa hali ya chini sana. Mradi huu katika kupita utapita katika maeneo ya vijijini, kwa hiyo vijiji ambavyo vitapitiwa na mradi ule vitapata maji. Hii yote ni shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kuamua kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba analitatua tatizo hili la maji katika maeneo ambayo yalikuwa yana shida ya maji kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, mradi huu wakati unakwenda pale Igunga maeneo kama Ziba, Ibologelo, Nyandekwa, Ndembezi pamoja na Kata zilizopo jirani pale maana ni kilometa kumi na mbili yatapata maji ya Ziwa Victoria. Vile vile naamini mpaka Nkinga pale kwenye Hospitali yetu ya Rufaa maji yatafika kwa sababu ni Hospitali ya Rufaa ambayo inatoa huduma maeneo mbalimbali, maji na wao watapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maji ni uhai na kama alivyosema Mheshimiwa aliyetoka hapa bila maji huwezi kufanya mambo yoyote, lakini kwa programu hii namshukuru sana Mheshimiwa Rais na Wizara. Niombe tu hii progamu iende kama ilivyopangwa na naamini kufikia 2018 maji yatakuwa yanatiririka katika maeneo yetu. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mambo machache ambayo napenda leo nichangie, ni kuhusu masuala ya uchimbaji wa mabwawa. Tumeona kila Mbunge anazungumzia maji hapa na tumeona kuna baadhi ya maeneo mvua zinanyesha kwa kasi sana kiasi kwamba inapeleka mpaka mafuriko.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Wizara hii iangalie katika masuala kama haya maji mengi yanapotea; tungechimba mabwawa makubwa ambayo yangesaidia kuhifadhi haya maji kwa sababu maji mengi yanapotea. Sehemu nyingine Mwenyezi Mungu amejalia tuna mvua za kutosha lakini baada ya mvua kukatika na maji yanapotea na shida ya maji inaendelea kuwepo katika yale yale maeneo ambayo mvua nyingi zilinyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara iliangalie jambo hili kwa macho mawili. Hata nikitolea tu mfano pale kwetu Choma Chankola kulikuwa na survey ilifanyika ilitolewa milioni thelathini na tano ya kuchimba bwawa na usanifu ukafanyika, lakini ule uchimbaji wa bwawa sijui umepotelea wapi, imekuwa kimya. Kila mwaka tunaulizia. Mwaka jana nilizungumza hili suala na mwaka huu tena nagusia Mheshimiwa Waziri amesahau ama ile fedha iliyotolewa milioni thelathini na tano walitoa sadaka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini wanavyotoa fedha baadaye inafuata mipango ya utekelezaji. Sasa tumetoa milioni thelathini na tano, isipotee, naomba mabwawa haya yachimbwe katika maeneo ambayo maporomoko ya maji yapo mengi hasa Choma, Ziba pale kuna maji mengi sana na kilimo cha mpunga, lakini pia mabwawa maeneo ya Simbo nashukuru sasa hivi kuna NGO ya World Vision wana programu ya uchimbaji wa bwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Serikali mshirikiane na hii NGO ili tuweze kuhakikisha kwamba hii programu yao ya uchimbaji wa bwawa kubwa pale Simbo iweze kukamilika na kufikia mwisho ili kuhakikisha kwamba maeneo jirani yanapata haya maji ambayo yatawasaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na kuchangia kwenye ishu ya mabwawa Mheshimiwa Waziri mimi nigusie; tuna miradi inayofadhiliwa ama tunaopata miradi katika maeneo yetu ya maji vijijini. Tunatumia fedha nyingi sana kutengeneza miradi ya maji katika vijiji vyetu, lakini tuna shida ya kukosa wataalam wa kusimamia ile miradi na inapelekea miradi ile baada ya muda mfupi inakufa. Kwa mfano kuna mradi wa usambazaji wa maji katika Kijiji cha Choma namba sita pale Matinje, ukienda Ziba mradi wa maji upo, ukienda Ndembezi, Nkinga na Simbo kote kuna miradi wa maji. Tatizo wanakosa wataalam wanaachiwa Serikali za Vijiji wale Wenyeviti wa Vitongoji na Wajumbe mwisho wa siku wanakusanya fedha na baada ya kupata mapato wanazila zile hela.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sisi Wizara, katika maeneo ambayo kuna miradi, tuajiri au tupeleke mtaalam pale aweze kusimamia na kuwaongoza hawa viongozi na watu ambao wanasimamia huu mradi wa maji. Niiombe Wizara iliangalie hili suala ili ihakikishe kwamba inaokoa fedha ambazo zimekwishatumika katika uchimbaji ama uwepo wa miradi ile ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niiombe Wizara katika ile miradi yao wanayopata ya ufadhili wa World Bank ya uchimbaji wa visima virefu, niombe watuangalie na sisi pale Igunga hasa Manonga kwa sababu yako maeneo yana shida sana ya maji. Tuna shida kweli ya maji hasa ukiangalia kuna baadhi ya vijiji; naweza nikamtajia ama nitamletea Mheshimiwa Waziri kwenye taarifa yake atusaidie. Kuna maeneo kama Kata za Mwamala, Uswaya, Igoweko, Kitangili, Nyandekwa na Mwansugho Ngulu, maeneo yote hayo hayana maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuiombe Wizara katika ule ufadhili wanaoupata kutoka World Bank na maeneo mengine waiangalie Wilaya yetu wahakikishe kwamba tunapata visima hivyo virefu angalau; maana bajeti imekwisha sijaona kisima hata kimoja ndani ya Wilaya yangu ya Igunga. Sasa niiombe Wizara iangalie hili suala na iweze kupitia ili waweze kutusaidia kutatua hii changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nipende kushauri tu kwa Mheshimiwa Waziri, waliangalie kwenye Wizara. Nilihudhuria kwenye bajeti moja ya Kamati ya Fedha Wilayani pale Igunga. Tumekaa zimekuja fedha za maji milioni ishirini nafikiri, kuna mradi fulani wa maji vijijini; lakini wanasema katika hii milioni ishirini mwongozo kutoka Wizarani asilimia 30 ya fedha ni kwa ajili ya usimamizi wa miradi hii. Milioni ishirini, usimamizi ni milioni sita maana yake ni kwamba kwenye milioni ishirini unatoa sita inabaki milioni
14. Sasa kwa vijiji sijui 14 vile vitagawana shilingi ngapi ngapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuangalie kama ni mwongozo kweli wa asilimia 30 kama ni kweli, maana wameniambia wataalam wilayani, huu ni mwongozo wa Wizara, tunakata asilimia 30 kwa ajili ya usimamizi; nikauliza usimamizi gani? Wanasema kwamba sijui kuna mafuta na posho, ukipiga mahesabu hazifiki milioni sita au saba. Sasa leo tuna programu ya bilioni…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali muda wako umemalizika.

MHE. SEIF K.S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja, niiombe Wizara ifuatilie hizi fedha ambazo zinakuja kwenye Halmashauri. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo nami kuweza kuchangia katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri kwa bajeti hii nzuri ambayo ameiwasilisha katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018. Tunashukuru sana kwa sababu bajeti hii sasa inaenda kupunguza ama kuleta picha fulani ya unafuu kwa wananchi wetu ambao tunawaongoza. Nami niseme tu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Manonga, Wilaya ya Igunga pia wananchi wa Mkoa mzima wa Tabora, tumeipokea vizuri sana bajeti hii ya mwaka huu wa fedha, hasa katika kuainisha baadhi ya maeneo ambayo kwa kweli kwa namna moja ama nyingine yanaenda kupunguza makali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa mfano katika uondoshwaji wa hii kodi ya road license, kuna watu watabeza kwa namna moja ama nyingine, lakini niseme tu tumeiondoa kutoka kuilipa moja kwa moja na tumeipeleka kwenye mafuta kwa maana tunapokwenda kununua mafuta ndipo tunakwenda kuilipa kidogokidogo. Hii pia inasaidia kupunguza kero kwa trafiki maana yake Police Traffic walikuwa wanapata usumbufu wa mara kwa mara kusimamisha magari na kukagua kama hawa watumiaji wa magari wamelipia ama hawajalipia, kwa hiyo imewapunguzia kwa namna moja ama nyingine kero ya kusimamisha magari. Naamini kabisa bado tutaendelea kupunguza kero zaidi za hawa Police Traffic itafikia hatua barabarani trafiki watakuwa hawaonekani maana yake tutaweka hata zile kamera zinazoweza kukamata kama ni mwendo kasi na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika bajeti hii, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, katika suala zima ambalo limetokea muda siyo mrefu la makinikia kupitia Wizara hii ya Madini. Hii vita si ndogo kama ambavyo tunaweza tukaichukulia na sisi Wabunge kwa umoja wetu tukiweka itikadi za vyama vyetu pembeni, tuungane pamoja tumsaidie Rais katika jambo hili, vita ya uchumi ni vita kubwa kuliko vita nyingine ambazo tunaweza tukazifikiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vita hii ni kubwa kuliko hata vita ya kudai uhuru wa nchi, kwa sababu vita ya rasilimali ndiyo iliyowafanya hata baadhi ya Marais duniani kuondolewa madarakani. Hii ni vita ambayo kwa namna moja ama nyingine kama Viongozi wa Taifa hili la Tanzania kama tuna mapenzi ya dhati na Taifa hili ni katika sehemu hii sasa tunahitaji kuungana, kusimama pamoja na Mheshimiwa Rais, kumsaidia kuhakikisha kwamba ile dhamira yake safi inatimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wa aina au caliber ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni wachache sana duniani. Hiyo ndiyo napata siri ya kwa nini Mheshimiwa Dkt. Magufuli hajaenda nje ya nchi kwa muda wa miaka miwili sasa. Maana yake unaposafiri kwenda nje ya nchi unakutana na wakubwa, wakubwa hawa watakuomba mambo, mambo mengine wanayokuomba unaweza ukashindwa kuwakatalia. Sasa, sasa hivi kwa sababu tuko katika jitihada za kujikwamua kudai uhuru wetu wa uchumi, sio uhuru wa bendera, uhuru wetu wa uchumi, tupate fedha kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasema Taifa hili linatakiwa liwe donor country, tuwe Taifa la kutoa misaada kwa Mataifa mengine, ni jambo ambalo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina rasilimali nyingi sana, ukiangalia Dubai wana mafuta tu lakini wanaweza kuwa wanafanya mambo makubwa sana, lakini Tanzania tuna kila kitu, kwa sababu tumepata sasa Kiongozi ambaye anaweza akasema bila aibu, bila kupepesa macho, hilo jambo si jepesi, hii kazi tukimpa mmoja wetu tukampa nafasi ile ambayo anaifanya Mheshimiwa Dkt. Magufuli nafikiri kila mmoja anaweza akajificha hapa. Ni jambo ambalo linahitaji uondoe sura ya aibu ndani ya macho yako, sasa inahitaji viongozi na Wabunge tuungane tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua tupo baadhi ya Wabunge tunatumika kusaidia ama kudhoofisha jitihada mbalimbali katika jukumu hili. Hata kama kuna makosa, hayo makosa tuyafanye lakini tuhakikishe kwamba tunapata haki zetu za msingi. Haiwezekani makosa tuyaone tuseme kwa sababu tuna makosa tunaonewa tunaibiwa, tuseme kwa sababu tulikosea, haiwezekani! Tufanye masahihisho katika makosa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo tunamuunga mkono na Wabunge tunahitaji kumuunga mkono na kum- support na kumpa moyo Mheshimiwa Rais, tufikie dhamira ya dhati. Leo hapa Wabunge tunasimama kila mmoja anadai barabara, anadai maji, anadai miundombinu, kila mtu anataka mara afya; fedha zinatoka wapi? Ndiyo hizi fedha za makinikia, ndiyo hizi fedha za rasilimali zetu tulizonazo, tuzidhibiti hizi fedha.Tutakapodhibiti tutaweza kutengeneza fly overs, tutaweza kutengeneza reli ambayo sasa hivi imeshaanza, naipongeza sana Serikali, tumeanza na ujenzi wa standard gauge, hizi zote ili kuhakikisha kwamba tunafikia malengo haya ni lazima tudhibiti rasilimali zetu tupate fedha ambayo itasaidia kujenga miundombinu yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza bado tunaona kabisa katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri tuna ujenzi wa reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam inakuja Mwanza, itapitia Tabora itaenda Kigoma pia in future itakwenda Rwanda, itakwenda Burundi na Congo. Hii yote itasaidia kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua. Tunavyoboresha miundombinu tafsiri yake tunakuza uchumi wa nchi yetu kwa sababu itarahisisha usafiri wa mizigo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, mzigo ambayo ilitakiwa itoke China iende Congo itapita Tanzania kupitia reli hii itakusanya mapato, kupitia mapato haya ndiyo tutatatua changamoto mbalimbali za maeneo yetu tunakotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali katika kuboresha bado tumeweza kuona tumenunua ndege mbili kubwa ambazo zinafanya kazi na bado Serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine, hii yote ni kufufua uchumi wa nchi yetu. Jamani, lazima tuiunge mkono Serikali hii, sasa tusipoiunga mkono mnataka tufanye nini? Kila kitu kukosoa tu, kila kitu kukataa, kila kitu kupinga, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wabunge wa Vyama vyote, Wabunge wa Upinzani wenyewe kazi yao kupinga, haiwezekani. Ifike hatua kwenye mambo ya msingi, masuala ya uchumi tusaidiane, tupeane moyo, ikifika uchaguzi twende tuzungumze kila mmoja anadi yake lakini kwenye masuala ya maendeleo tuungane pamoja ku- support nchi yetu isonge mbele. Ninyi mnasikia furaha gani tunapokuwa na miundombinu mibovu, mnabaki tena mnalalamika, tukija hapa tupitishe bajeti ninyi mnasema hapana! Sasa nashindwa kuelewa ninyi ni watu wa aina gani? Lazima ifike hatua tubadilike, nchi hii inataka tusonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jitihada za Mheshimiwa Rais kwenye ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga, bado kuna watu humu wanapinga. Hebu jamani tuache hizi kasumba za kupinga kila kitu, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, tuiunge mkono Serikali hii mpaka 2020, tukifika kwenye uchaguzi, haya mtaleta sera zenu lakini hapo tayari tutakuwa tumeshapiga hatua mbele ambazo zitahakikisha kwamba tunawakwamua wananchi wetu kuwatoa katika shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengi sana ya kuzungumza lakini pamoja na yote naiomba Wizara kwamba next budget, bajeti iwe imeelekezwa kwa kiwango kikubwa sana kwenye utatuzi wa maji hasa wa vijijini, tuchimbe visima vingi sana vya maji kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo hili ambalo nafikiri kwa namna moja ama nyingine tutamtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama muda wangu utakuwa umekwisha, basi napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii nami kuchangia jioni hii ya leo. Kwanza nipongeze Wizara kwa juhudi mbalimbali ambazo inazifanya katika kuhakikisha kwamba inatatua changamoto za maji ambazo zipo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumza juu ya tatizo la maji katika maeneo yetu na mimi nilipata bahati kuwa katika Kamati hii ya LAAC, tulibahatika kwenda kule Mbeya tukaenda kujionea hii miradi ya maji inavyotekelezwa. Tulienda pale maeneo fulani yanaitwa Kyela na sehemu moja panaitwa Tukuyu. Kuna fedha zilitengwa kule, katika usanifu zikahitajika kama shilingi bilioni moja mradi utekelezwe. Mradi ule umeenda ukakwama katikati, wakafanya tena wakataka kama shilingi bilioni nne hivi. Mradi ule wakagawa kwa wakandarasi wengi sana lakini at the end of the day hakuna ambacho kimefanyika mpaka siku tunakwenda kama Kamati kwenda kushuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukatoka pale tukaenda Tukuyu, tulivyofika tukakuta story ni ile ile iliyoko Kyela iko Tukuyu, shilingi bilioni moja imeenda shilingi bilioni nne, shilingi bilioni nne ikaenda shilingi bilioni saba. Wamegawanyishwa wakandarasi; mkandarasi huyu kafanya kwa hatua fulani , mwingine ameingia mitini, yaani ni kama vile mchezo fulani ambao ndiyo yale yaliyokuwa yanazungumzwa hapa na waheshimiwa wenzangu hapa kwamba ni kama kuna ka-chain ambako kuna fedha zinatiririka zinaliwa na kama kuna- hang yaani hakuna ile kunakuwa kama sintofahamu na miradi hii imekuwepo ndani ya nchi yetu yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani hata juzi walikuja Kamati ya LAAC pia kukagua mradi wa maji Wilaya ya Igunga. Walienda kijiji kimoja kinaitwa Blangamilwa tulipata fedha lakini ni zaidi ya shilingi milioni 700. Katika hii juzi iliyokuja shilingi milioni 900. Wameenda kuangalia utekelezaji mabomba yaliyowekwa ilitakiwa wajenge matenki ya kuhifadhia maji, wameenda kununua matenki ya shilingi laki tatu/tatu kaweka matenki mawili. Ni jambo la aibu kwenye miradi hii ya maji ni janga lingine la kitaifa kwenye hii miradi ya maji ni janga la kitaifa.

Mheshimiwa Spika, tumeona tunaunda tume mbalimbali kufuatilia, Tume ya Makinikia, sijui Tume ya Madini ya Almasi; hebu sasa nikuombe, na juzi tumemsikia Rais alipiga simu pale kila mmoja akamwagiza Katibu Mkuu aende kwenye kile kijiji kutatua tatizo la maji kwa mkandarasi yule. Nikuombe tuisaidie Serikali tuunde tume ifuatilie miradi ya maji nchi nzima ilete taarifa na tutoe way forward ambayo itaweza kusaidia hii Serikali wapi twende. Nimekusikia ulipokuwa unasema hawa watu ni wapya. Ni kweli Mheshimiwa Waziri ni mpya, Naibu Waziri mpya hata Katibu Mkuu ni mpya. Sasa kwa sababu ya upya wao tuwasaidie kuhakikisha kwamba wapi tulikosea, wapi tupo, wapi tunatakiwa twende kupitia miradi hii ya maji na itatatua tatizo ambalo tunalo katika miradi yetu ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumza kwamba Wizara ya Maji haina fedha, lakini hata fedha zilizokuwepo zinazopelekwa ndivyo zinavyoliwa. Leo mimi binafsi naunga mkono tuongeze fedha shilingi 50 iwe shilingi 100 katika kodi ya mafuta, lakini kwa utaratibu huu ambao uliokuwa unaendelea na ukaendelea maana yake tutaweza kuongeza fedha nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu huo huo ambao tunaushuhudia katika maeneo mbalimbali ya ubadhirifu wa fedha hizi za umma unavyojitokeza iko haja ya Bunge kuchukua hatua na kuisaidia Serikali katika utatuzi wa miradi hii ya maji ambayo…(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilitaka kuchangia, Mheshimiwa Waziri alikuja jimboni kipindi ambacho akiwa Naibu Waziri wa Maji. Alikuja akatembelea Choma cha Nkola akaona mbuga kubwa ya ulimaji wa mpunga ambayo ilivyokuwa ikistawi mpunga na aliona maeneo ambako bwawa kubwa lilikuwa limekuwa designed kwa ajili ya kuchimbwa na akaahidi kulifuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilibeba documents zote za feasibility study ambazo zilifanyika kwa ajili ya uchimbaji ule wa bwawa. Bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja kama Naibu Waziri. Leo amekuwa Waziri kamili, kwenye kitabu hiki nilikuwa nataka kuangalia angalau nione labda ametenga sasa fedha za kuanzia uchimbaji wa bwawa lile, sijaona sehemu yoyote ambako ameweka na ukizingatia tunapata mvua na mvua ni nyingi. Sasa tunapoziacha zinapotea na mbuga tunayo kubwa maana yake uzalishaji unapungua badala ya kuongezeka na kama tuna mbuga tungeitumia vizuri tukazalisha mpunga kwa wingi tukaweza kuuza ndani na nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Waziri alichukulie hili suala la bwawa kwa uzito wake wa hali ya juu sana. Hili suala la bwawa, tuna maeneo mengi ya uchimbaji wa bwawa, tunaweza tukachimba bwawa kubwa pale Choma ambapo tayari documents zote anazo mpaka na Mwenyekiti wa Umwagiliaji Taifa alimwita hapa Dodoma kwa ajili ya kulifanyia uchambuzi wa kina tupate fedha, lakini sijaona. Hata ukienda Ziba pale tuna maeneo makubwa sana ya uchimbaji wa mabwawa na maji ni mengi yanapotea pale, tungechimba sisi bwawa lingine pale Ziba, lakini tungechimba bwawa lingine pale Simbo ambako lingeweza kusaidia kilimo cha umwagiliaji ambacho kingeondoa tatizo la njaa. Katika nchi yetu kuwa na njaa ni aibu.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo nilitaka kuchangia ni kuhusu wakandarasi, sasa hivi wako site wanafanya kazi ya usambazaji maji katika miji midogo midogo. Kwa mfano kuna mkandarasi anafanya kazi ya usambazaji maji katika Kijiji cha Isenegeja Kata ya Mwisi amesha-raise zile certificate Wizarani shilingi milioni 180 haijatolewa leo ni muda mrefu. Sasa huyu mkandarasi atasimama na akisimama maana yake atachelewa ataacha kufanya kazi halafu vile vifaa vilivyopo vitaibiwa na vikiibiwa maana yake mradi utaanza kupoteza mwelekeo.

Mheshimiwa Spika, niombe sasa wizara zile certificate ambazo zimekuwa raised pale Kata ya Mwisi na katika Vijiji vile vya Mwamala, Mwakabuta na Mangungu certificate zake ambazo zipo wizarani nimuombe Waziri atoe go ahead ili hawa wakandarasi waendelee. Kwa sababu tunapochelewesha inaweza kusababisha upotevu wa vifaa ambavyo tayari viko katika maeneo yetu. Nimuombe Mheshimiwa Waziri alichukue hili na alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa napenda kuchangia kwa usiku wa leo, katika maeneo yetu yako maeneo ambayo visima vinachimbwa na maji tunapata kwa kiwango fulani. Tafiti zimefanyika katika baadhi ya maeneo imebahatika kuna sehemu kuna maji, tunaweza tukapata, na wao pia wame- raise certificate ambazo ziko wizarani. Nilikuwa nimuombe tu Waziri kwamba aweze kutoa go ahead ili hizi kazi ziweze kufanyika na wananchi waweze kupata maji katika yale maeneo ambako utafiti umefanyika na maji yamepatikana. Tunaishukuru Serikali mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria unatoka sasa Nzega unakwenda Igunga na baadhi ya vijiji vyetu vitapata maji.

Kwa hiyo ni shukrani pekee ziende kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli; lakini pili na watu ambao wako wizarani pale kwa maana ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Timu yao nzima kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa ukaribu mradi huu uweze kutekelezwa kwa umakini sana.

Napenda kuunga mkono hoja ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika majadiliano haya. Kwanza nipende kutumia nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya katika taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri sana, naamini Watanzania walio wengi wanaona; na katika kazi hizi Mheshimiwa Rais lengo lake ni kupunguza matatizo ambayo yalikuwepo ambayo yalikuwa yakileta changamoto mbalimbali katika sekta ya madini na sekta mbalimbali ambazo ziko ndani ya nchi yetu. Juzi tumeona amekutana na wadau wa madini nchini, amejadiliana nao na ameona changamoto ambazo zipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kuona hata baadhi ya wadau ambao wameweza kuchangia wameweza kuchangia, wameweza kuionesha Serikali sehemu ambazo kuna mianya inavyopoteza mapato katika nchi yetu. Hata kule Tanga wameweza kuzungumza habari ya maeneo yenye migodi ambayo watu wanaitumia migodi ile kwa ajili ya kujinufaisha binafsi. Vilevile pia wameonesha namna gani ambavyo baadhi ya watumishi wetu katika Serikali hawawajibiki ipasavyo. Kwa hiyo mimi binafsi nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya na hatuna sababu ya kuacha kumpongeza kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kuzungumzia; ni kuzipongeza Wizara za Nishati na Madini, kazi kubwa sana wanazifanya pia. Tumeweza kuona hata Wizara hii ya Nishati kupitia Mheshimiwa Medard Kalemani pamoja na Mheshimiwa Subira Mgalu, wanapambana sana ili kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vinapata umeme. Katika maeneo yetu, tumeona wakitembelea vijiji. Mimi binafsi kwa kweli nisiseme uongo, wamekuja mpaka jimboni kwangu mara mbili, mara tatu. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, hata Kamati ilifika maeneo ya vijiji vyetu na baadhi ya vijiji vimeanza kupata umeme katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vinapata umeme. Zipo changamoto ambazo zimezungumzwa hapa. Katika utekelezaji wa miradi ya aina yoyote changamoto huwa hazikosekani, tuangalie namna gani ya kuweza kutatua hizi changamoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya hizo changamoto lakini miradi inatekelezwa vizuri na mambo yanakwenda, hata kama zipo lakini ni ambazo zinaweza kuzungumzika na kuweza kutekelezeka. Kwa mfano, niishauri tu Serikali, kwamba itoe fedha kwenye Wizara hii ya Nishati ili iweze kutimiza kazi zake kwa wakati. Wanapotoa fedha hizi zitakwenda kulipwa hawa wakandarasi ambao wanatekeleza miradi hiyo, wakandarasi wataweza kupata fedha ambazo zitawasaidia kununua vifaa ambavyo vitakuja katika utekelezaji wa umeme vijijini. Jitihada kubwa zinafanyika, lakini niiombe Serikali iweze kuongeza fedha katika miradi mbalimbali inayotekelezwa ikiwa chini ya Wizara hii ya Nishati. Kwa hiyo hilo nilikuwa napenda kulizungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ipeleke fedha katika taasisi zake, kwa mfano TANESCO, TPDC, STAMICO, wawape fedha ili waweze kuhakikisha kwamba yale malengo waliyokuwa wemejiwekea waweze kuyatekeleza kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naliona, Serikali iangalie namna ya kuongeza rasilimali watu. Rasilimali watu imekuwa ni changamoto sana katika taasisi mbalimbali za Serikali na hii inasababisha kupunguza uwezo wa Serikali kukusanya mapato kwa wakati. Tunaweza kuona katika sekta za madini, gesi pamoja na mafuta. Kwa hiyo niiombe Serikali iweze kuongeza rasilimali watu ili waweze kuhakikisha kwamba majukumu ambayo Serikali imejiwekea yaweze kutimizwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho ningependa kuchangia ni katika suala zima ambalo Kamati imezungumzia; masuala ya flow metres. Tunaweza kuona flow metres zetu katika maeneo yetu ya bandari. Kuna bandari ya Mtwara, bandari ya Tanga, lakini kuna Bandari hazina flow metres. Kwa hiyo, tunaweza kuona kwamba tunapata mafuta ambayo hayapo katika utaratibu mzuri wa mahesabu. Kwa hiyo tunapofunga flow metres zetu inatusaidia kuweza kupata exactly figure ambayo itatusaidia kupata mapato katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara na pia Serikali ihakikishe kwamba inafunga flow meters katika maeneo ambayo yana uhitaji hasa kwa sababu ni faida kwa Taifa letu. Kwa hiyo walichukulie kama sehemu ya mojawapo ya kudhibiti kuingizwa kwa mafuta pasipo kupata data kwa sababu wanaweza kuchakachua taarifa ambazo zinakuwa zimeandikwa japo zinaandikwa na watumishi wetu. Sasa tukipata flow meters zitatusaidia kurekodi na kupata amount sahihi ya mafuta yanayoingia na vile vile itatusaidia kupata kipato, ambacho nchi inahitaji kukipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Mheshimiwa Hussein Amar atafuatiwa na Mheshimiwa Joram Hongoli na Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani ajiandae.

MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora. Kwanza napenda kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambazo inafanya, ama miradi mikubwa ambayo inatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona miradi kama Stieglers Gorge ambapo kwa ukamilishaji wa mradi huu tutapata Megawati kama 2,100 za umeme, tunaona ujenzi wa Standard Gauge (SGR), ujenzi wa kisasa wa reli yetu, tunaona usambazaji wa umeme vijijini, vijiji vyote vitapata umeme, tunaona vituo vya afya na hospitali karibu 67 zinajengwa nchi nzima. Miradi hii yote ikikamilika, ninaamini Tanzania itakuwa kati ya nchi 10 bora katika Bara la Afrika out of 54 countries. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo za Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa, binafsi naunga mkono na wananchi wa Jimbo la Manonga wanaunga mkono harakati zote za Mheshimiwa Rais kupeleka nchi yetu katika uchumi wa kati. Sasa nianze kwa maombi yangu kama Wilaya na Jimbo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya TAMISEMI, kwanza nawashukuru kwa kunipatia fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Simbo. Kituo kimekamilika, sasa kilichobaki ni vifaa tiba. Naiomba Wizara ya TAMISEMI ituletee vifaa tiba katika Kituo chetu cha Afya cha Simbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nawaomba Wizara ya TAMISEMI, Jimbo letu ni kubwa sana. Mwaka 2018 Agosti, alikuja Mheshimiwa Waziri Mkuu Jimboni, alituahidi kutupatia fedha shilingi milioni 400 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Choma cha Nkola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Choma baada ya Hospitali ya Wilaya ya Igunga kinachofuatia ni Kituo cha Afya cha Choma ambacho kinafanya operation ndogo ndogo. Karibu operation 150 wamekwishafanya, lakini changamoto iliyoko pale hatuna jengo la akina mama na watoto, hatuna jengo la kufulia nguo, hatuna mortuary, hatuna ward ya akina baba. Kwa hiyo, bado operation hizi wanapata changamoto sehemu ya kuwahifadhi wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, nimeangalia kitabu chake sijaona bajeti ya fedha ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi katika ziara yake. Tunaomba fedha kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Choma cha Nkola ili kuweza kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma bora kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona bajeti hapa ya Wizara ya Afya. Tumetenga fedha za ujenzi wa hospitali katika Wilaya mbalimbali nchini. Wilaya yetu ya Igunga Makao Makuu ya Wilaya ni Igunga. Pale tuna hospitali ya wilaya. Hospitali yetu imechakaa sana, hatujapata fedha za maboresho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri tuangalie katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, hatuna ambulance. Nilinunua ambulance nikapeleka kwenye Kituo changu cha Afya cha Simbo. Sasa inachukuliwa ile ambulance ya kijijini, kwenye Kituo cha Afya cha Simbo, inaletwa mjini. Kwa hiyo, ile adha ambayo nilikuwa nimeenda kupunguza kwa wananchi inakosekana. Tunaomba ambulance ya wilaya iletwe, ili iweze kuhudumia kwa sababu mahitaji ni makubwa na katika makao makuu ya wilaya watu ni wengi sana wanahitaji kupata huduma hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena tupate fedha kwa ajili ya kuongeza matengenezo kwani hospitali ya wilaya imechakaa, haina uzio, hakuna maabara ya kisasa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu, mpo hapo Wizara ya TAMISEMI, mtupatie fedha kwa ajili ya kuboresha hospitali yetu ya wilaya ili kuboresha na kusaidia kupatikana huduma za afya katika Wilaya yetu ya Igunga, hasa Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kwenye shule za Serikali za wasichana. Tumeona ujenzi wa shule za Serikali za wasichana zikijengwa maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Tabora Mjini tunayo natambua iko Tabora Girls, nimeona Nzega pale imejengwa. Naomba sasa, katika Wilaya yetu ya Igunga hatuna shule hata moja. Mimi binafsi katika Jimbo langu niko tayari na tuko tayari kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa shule, tukishirikiana na TAMISEMI, tutajenga pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba shule hizo za wasichana zijengwe katika Wilaya yetu ya Igunga pale Choma cha Nkola iweze kusaidia watoto wa kike wanaotembea umbali mrefu kutoka vijijini, kilometa nyingi kuja shuleni. Kwa hiyo, tukijenga shule hii itasogeza huduma, lakini itawarahisishia watoto hawa wa kike kukaa shuleni na kusoma kwa utulivu, itasaidia kuongeza ufaulu wao katika maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachilia mbali hilo, niiombe TAMISEMI, tuna upungufu wa ma-engineer. Engineer (mhandisi) wetu wa Wilaya tuliyenaye kwa masuala ya majengo inawezekana uwezo wake ni mdogo. Naomba TAMISEMI mtuletee engineer ambaye ataweza kutusaidia kuweza kusukuma hizi kazi za Kiserikali ambazo mmetuletea fedha ziweze kwenda kwa usahihi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia engineer wetu, tunanunua vifaa vingi sana mwisho wa siku vinabaki store, halafu inakuwa ni hasara katika maeneo yetu. Mfano ni Kituo cha Afya cha Simbo, tumenunua vifaa vingi hali ambayo imesababisha hata fedha tuliyonayo tumeshindwa kuwalipa wakandarasi wanaotudai. Naomba TAMISEMI ituletee engineer ambaye ataweza kwenda na hesabu ambazo zitaweza kukidhi mahitaji sambamba na maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika upande wa TARURA. Upande wa TARURA fedha inayopata katika Mkoa wa Tabora ni ndogo sana. Mkoa wa Tabora ni mkubwa kijiografia, ni mkoa wenye square metre karibu 75,000, miundombinu yake ya barabara ni mikubwa sana, lakini fedha inazopata ni ndogo, hazilingani na mahitaji ya mkoa wenyewe. Naomba TAMISEMI iangalie kutuongezea fedha katika upande wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi mkubwa sana wa madaraja. Kwa mfano Mkoa wa Tabora kuunganisha na Shinyanga. Kila sehemu kuna madaraja, kuna Mto mkubwa wa Manonga. Kwa hiyo, ili uweze kuvuka upande wa pili inabidi kuwe na daraja. Kwa hiyo, mahitaji ya madaraja ni mengi sana katika maeneo yetu, lakini fedha tunazoletewa ni ndogo, haziwezi kukidhi mahitaji ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TAMISEMI ituongezee fedha upande wa TARURA tuweze kujenga daraja la Mto Manonga upande wa Mondo ili kurahisisha wananchi wetu kuweza kwenda Shinyanga kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia suala la utawala bora, kuna watumishi wengi sana wamekaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga wanakaimu miaka mitatu, miaka minne, wakati tuna uwezo wa kuwapitishia hizo nafasi wakaweza kuzimiliki, wanalipwa fedha za kukaimu muda mrefu. Ni hasara kwa Serikali na Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Gulamali. Thank you. (Makofi)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuamua kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Nchi yetu ilikuwa na changamoto na maamuzi makubwa na maamuzi sasa yanafanyika, pongezi kubwa sana ziende kwake, hasa ununuzi wa ndege, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais; ujenzi wa viwanja vya ndege, kazi kubwa zinafanyika, sisi wote ni mashahidi katika maeneo yetu; ujenzi wa madaraja na barabara kubwa zinazojengwa ndani ya nchi yetu. Haya yote ni maamuzi ambayo Mheshimiwa Rais ameamua binafsi na wananchi wa Jimbo la Manonga tunampongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na tunasema aendelee kuchapa kazi, sisi tuko tayari kumuunga mkono mchana na usiku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze watendaji wakuu, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Mheshimiwa Engineer Mfugale; lakini pia nimpongeze mwalimu wangu aliyenifundisha chuoni, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Mheshimiwa Mr. Ngewe, pongezi ziende kwake. Amefanya kazi nzuri sana na nimeona juzi kapata hati ya utumishi bora, kwa hiyo nitumie nafasi hii kumpongeza mwalimu wangu kwa kazi nzuri anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa Viwanja vya Ndege, Mheshimiwa Dkt. Hamza Johari, Mwalimu wangu, naye anafanya kazi nzuri, hawa wote Walimu wangu wanafanya kazi nzuri sana, nafurahia, naona jinsi gani wanavyo-perform katika maeneo yao, bila kumsahau Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, naye nampongeza kwa siku ya leo. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua tena kwa mara nyingine aendelee kuhudumu kwa nafasi hiyo ya ukuu wa chuo. Natambua alikokitoa chuo, hali ilivyokuwa na ilivyo sasa hivi ni chuo tofauti sana, pongezi nyingi sana ziende kwako Dkt. Mganilwa, kwa kazi kubwa unazozifanya, tunakupongeza, sisi wanafunzi wako tuko Bungeni tunaona matunda unayoyafanya huko ulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niwapongeze Mawaziri; Mheshimiwa Engineer Nditiye pamoja na Mheshimiwa Kwandikwa bila kumsahahu Waziri wake, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe; Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri sana, pongezi nyingi sana ziende kwake maana yake leo nilisema niwapongeze kwa kazi wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisisahau kumkumbusha Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Waziri kwamba wananchi wake wa Mpanda kule wanapokuwa wanatoka huwa wanapewa rufaa kwenda kutibiwa Tabora, wakienda Tabora na kwenyewe wanapewa tena rufaa ya kwenda kutibiwa pale Hospitali ya Nkinga lakini wakifika pale Ziba kwenda Nkinga barabara ni mbaya sana. Naomba Mheshimiwa Waziri aweke lami pale ili wagonjwa wanaotoka Mpanda, Katavi, Majimoto wapate huduma safi pale Nkinga ili kuwarahisishia wananchi wake wapite kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kwamba aanze basi na usanifu; barabara ya Ziba- Nkinga – Puge; barabara ya Ziba – Choma na kwa kutambua kwa sababu Choma Chankola kuna kiwanda kikubwa cha pamba. Kwa hiyo kwa sababu tuna kiwanda lazima miundombinu tuiboreshe na Serikali hii tunanadi ni awamu ya viwanda. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake sijaona akitenga angalau usanifu na barabara hii ya Ziba – Choma, Ziba – Nkinga – Puge ni barabara inayomilikiwa na TANROADS, nimwombe Mheshimiwa Waziri aikumbuke barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Mheshimiwa Waziri, Engineer Nditiye ile minara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii, lakini minara Mheshimiwa Engineer Nditiye pale…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kupongeza juhudi zinazofanywa na Wizara yako katika kuboresha hali ya elimu Tanzania. Tumeshuhudia sehemu mbalimbali za nchi madarasa, madawati, mabweni katika shule za msingi, shule za sekondari na hata vyuo. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu sera ya nchi juu ya kila Wilaya kuwa na VETA. Nipende kurudia tena katika Wilaya ya Igunga, Kata ya Choma Chankole tulipata ufadhili wa ujenzi wa madarasa manne kutoka ufadhili wa NGO ya World Vision IDP Manonga.

Tunawashukuru sana na tayari wameshakabidhi katika Halmashauri. Sababu ya kutokuwa na fedha za kutosha, tunaomba sasa Wizara itusaidie ujenzi wa ofisi na mabweni ili chuo hiki kianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ukitupatia shilingi milioni 400, tunao uwezo wa kuboresha zaidi VETA hii kuwa ya kisasa. Naomba sasa Wizara ipokee ombi hili kwa mara nyingine tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ya kupitisha bajeti yako.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili nichangie katika haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Mipango, Dkt. Mpango na Naibu wake Waziri pamoja na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Kwa kweli inaleta matumaini makubwa sana kwa Taifa letu kwa sababu matokeo ya Mpango yanaonekana katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linadhihirika kwa sababu huwa tunajadili kila mwaka Mpango wa mwaka mmoja mmoja lakini hii ni kwa sababu tumekwishapitisha Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa 2016-2021. Pia Mapendekezo haya ya Mpango yanafuata pia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Ilani ya Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwapongeza waandaaji wote wa Mpango huu wa Maendeleo wa mwaka mmoja wa 2020/2021. Natambua Mpango huu umechukuliwa pia pamoja na masuala mazima ya maendeleo ya Kikanda kwa maana ya East Africa, AU lakini pia SADC. Kwa hiyo, Mpango wetu unaenda sambamba na maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongereni sana waliopanga huu Mpango kwa kutumia maarifa makubwa sana kwa sababu vipaumbele vyote tulivyokuwa tumeviainisha mwanzo ni mwendelezo. Tumeona miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, katika Mpango huu tumeona ni mwendelezo wa mpango wa 2016–2021. Pia tumeona ujenzi wa reli kama Standard Gauge kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro umeshafikia 63% ni pongezi kubwa sana. Vilevile tumeona ujenzi wa reli kutoka Dodoma kwenda Morogoro umeshafikia 16%. Hongera kwenu Mheshimiwa Waziri kwa sababu haya ni maendeleo na tunaendelea kuwekeza fedha kwa ajili ya miradi mikubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona ujenzi wa Bwawa kubwa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere la ufuaji wa umeme karibu MW 2,115, tunaenda kupunguza uhaba wa umeme katika nchi yetu lakini pia tunaenda kusambaza umeme vijiji vyote nchi nzima. Kwa hiyo, suala la nishati kwa wananchi wetu vijijini na mijini litakuwa ni historia baada ya kukamilisha Mpango wetu wa mwaka 2016–2021, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona mpango huu umejikita zaidi katika ku-link na Sera yetu ya Viwanda. Tunatambua sasa katika nchi yetu tuna Sera ya Viwanda inaenda sambamba na uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi napenda kuchangia upande wa kilimo. Wenzangu wamezungumza tumeona sekta zinakuwa sana kwa kasi, sekta ya ujenzi inakua kwa 16%, madini 13%, mawasiliano 10.7%, usambazaji wa maji katika nchi yetu na wenyewe unakua sana kwa kasi. Sasa naiomba Wizara hii ya Mpango, katika mapendekezo yao sasa wajikite katika kilimo. Tuwekeze zaidi kwenye kilimo kwa sababu Tanzania kama ilivyo jiografia yake haifanani, kuna maeneo mengine ni rafiki kwa kilimo na mengine siyo rafiki, kule ambako kuna urafiki kwa upande wa kilimo tuwekeze vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna maporomoko ya maji, kipindi cha msimu wa mvua za masika inapofika mvua nyingi zinazopatikana, maji mengi yanapotea sana. Hasa kwa upande wetu sisi pale Igunga ukiangalia ule upande wa Ziba, Simbo, Choma cha Nkola na maeneo mengineyo Tanzania maporomoko ya maji ni makubwa yanapotea. Maandiko yapo katika Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo juu ya ujenzi wa mabwawa, skimu zile za umwagiliaji, zikijengwa hizi katika nchi yetu itawasaidia wakulima kulima mara mbili au tatu kwa mwaka kwa sababu watakuwa na maji ambayo yamehifadhiwa tofauti na kipindi ambacho maji yanamwagika hayana sehemu yanapokusanywa mwisho wa siku yanapotea. Hii ni kupoteza rasilimali lakini pia nguvu kazi na mapato katika nchi yetu kwa sababu tunapolima mara mbili mpaka mara tatu wananchi na nchi itapata kipato kwa maana ya kodi watakapokuwa wanauza. Kwa hiyo, niombe Mpango wetu sana pia ujielekeze huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ni mzuri na mapandekezo ni mazuri shida ni utekelezaji. Niombe katika kipindi hiki ambacho tumebakiza tujikite zaidi katika kilimo, hii itasaidia kuinua kipato cha wakulima. Tunatambua karibu 70% ya Watanzania wako kwenye sekta ya kilimo, tunatambua changamoto za kupatikana kwa mbegu za mazao yetu kupatikana kwa wakati. Niombe Wizara zinazohusika zisambaze pembejeo zote ikiwa ni pamoja na mbegu ili kurahisisha wakulima kulima kwa wakati lakini pia ufanisi utakuwepo katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata ufanisi kwenye mazao yetu kwa mfano kama pamba, mpunga, korosho, kahawa, hawa wakulima wakipewa pembejeo kwa wakati wakazalisha tunaona tunapoenda kwenye mauzo tunapata foreign currency. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri Mpango muwekeze sana katika kilimo. Pia tusaidie kukuza thamani ya mazao yetu kwa sababu tunaona mazao yetu bado hatujafikia level ambayo tunaiihitaji, kwa kweli niombe sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukiachana na sekta hii ya kilimo, Mheshimiwa Waziri wa Mpango, amezungumza mwenzangu hapa upande huu wa TARURA kuhusu miundombinu. Naomba TARURA iongezewe fedha za kutosha katika ujenzi wa barabara. Tunahitaji barabara za vijijini ambazo ndizo zinazosafirisha mazao kutoka mashambani kuleta kwenye masoko. Tuwekeze huko fedha za kutosha ili barabara hizi ziweze kufunguliwa lakini pia ujenzi ufanyike kwa wakati. Maana leo tunaona TARURA ina fedha ndogo sana ukilinganisha na TANROADS. Katika ule mgawanyo wa fedha kutoka Road Funds karibu 70% inakwenda TANROADS, 30% wanapata TARURA, ni ndogo sana, ingewezekana ingeenda fifty-fifty au TARURA wakapata wakapata 60% TANROADS wakapata 40% kwa sababu miundombinu ya barabara kubwa sasa iko vizuri tofauti na hizi barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge tulio wengi tumetoka vijijini, tuwekeze sana huko kwenye barabara hizo. Tuziboreshe barabara hizi ili wakulima waweze kusafirisha mizigo yao, mazao yao lakini pia tutawarahisishia hata usafiri na kufika kwa wakati katika maeneo mbalimbali. Katika mchango wangu kwa upande huo napenda ukae kwa style hiyo kwamba fedha nyingi zipelekwe kwa upande wa TARURA ili tuweze kujenga madaraja, barabara bora kwa ajili ya kusafirisha mazao yetu lakini pia itaturahishia kukuza pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano tumeboresha sana sekta ya afya, hospitali nyingi zimejengwa, tunajenga karibu hospitali 67 na vituo vya afya zaidi ya 400 nchi nzima vimejengwa. Leo kila sehemu umeme umesambazwa, utazungumza kitu gani ambacho hatukigusi hata watumishi hewa tumedhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpango maana tulikuwa na watumishi hewa wengi lakini mmeweza kupitia upya, mmeangalia na hizi nafasi leo zimekuwa fixed, tumepata watumishi ambao ni active. Pia, mishahara hewa tumeondoa kwa maana tumeshadhibiti huku. Kwa sababu tunaelekea mwishoni Mpango huu umeelekea kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Sisi ambao tunawawakilisha wananchi tunauona utekelezaji wa Mpango wa 2016 – 2021, umekwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii adhimu kuweza kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa Bungeni mwaka 2020 lakini na ile ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Manonga kwa kunipa kura nyingi lakini pia kumpa kura nyingi Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi. Kama unavyotambua leo ni tarehe 5 Februari, Chama cha Mapinduzi, chama adimu, chama kikongwe Barani Afrika na duniani kinakwenda kutimiza miaka 44 toka kuzaliwa kwake. Chama hiki kina heshima kubwa sana siyo tu ndani ya nchi bali na Afrika kwa ujumla. Ni chama ambacho kinajihuisha kila baada ya miaka mitano na tunatarajia mwakani kitajihuisha tena. Kwa hiyo, ni chama pendwa na kinafanya kazi ambayo Watanzania wanakitarajia na wanakitegemea kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo na kukitakia happy birthday Chama cha Mapinduzi, nijielekeze kwenye hoja ya msingi. Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa hotuba zenye maono na mwelekeo wa nchi yetu tunataka kwenda wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya mwaka 2015 alionyesha upingaji mkubwa wa ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Alizungumzia pia masuala ya kufufua Shirika letu la Ndege, ujenzi wa reli na mambo mbalimbali. Leo tumeshuhudia ufufuaji wa Shirika letu la Ndege, tuna zaidi ya ndege 8, ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme ambayo itakuwa bora katika Afrika Mashariki na Kati, lakini pia ujenzi wa Bwawa kubwa la Stiegler’s lenye uwezo wa kuzalisha umeme zaidi ya megawatt 2,115.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba yake amezungumzia kutengeneza ajira zaidi ya milioni 8. Naomba kuchangia kwenye ajira na niwaombe watu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Elimu na Wizara ya Ajira waungane kama timu moja kutengeneza ajira za vijana wetu ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizi ajira milioni 8 niwaombe watengeneze ajira milioni 1 nje ya Tanzania. Watengeneze fursa za Watanzania kufanya kazi nje ya nchi yetu. Yapo mambo ambayo tunaweza tukanufaika nayo kupitia ajira hizi ambazo Wizara itazitengeneza. Kupitia Balozi zetu ambazo zipo nje wanaweza kutengeneza mfumo ambao ukawatengenezea vijana wa Kitanzania waliomaliza vyuo vikuu wakapata kazi formal na informal katika katika nchi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira inaleta ukuaji wa uchumi katika nchi. Mfano nchi kama Philippine wananchi wake zaidi ya milioni 12 wanafanya kazi nje ya nchi na wanapata faida kubwa sana. Mfano tukitengeneza ajira milioni moja wakachangia kila mwezi ndani ya nchi yetu dola mia moja tu wakarudisha kuwapa wazazi wao, tutatengeneza dola milioni 100 zitakazoingia kila mwezi ndani ya nchi yetu. Dola milioni 100 kwa mwezi uki-multiply by miezi kumi na mbili tutapata zaidi ya dola bilioni 1.2, hili ni soko ambalo tunatakiwa tulitumie.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapi tunaweza tukaanzia? Sisi tuna Kiswahili, hii ni bidhaa adimu ambapo nchi nyingine hawana na kama wanayo lakini si kwa undani wake. Tutumie nafasi hii kukitangaza Kiswahili, tufanye lobbing katika nchi kama South Africa ambao wanataka kuanzisha kufundisha Kiswahili katika nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Nje iongee na South Africa tupeleke vijana wetu wakafanye kazi kule, tupeleke vijana wetu Namibia, Zimbabwe, hata kama tukitoa offer katika vijina 100, 20 tutawalipa sisi itaweza kutengeneza ajira kwa vijana wetu. Badala ya kuzagaa mitaani wataweza kupata fursa ya kufundisha Kiswahili ndani ya Afrika lakini pia hata Marekani ikiwezekana kwa sababu viko vyuo vikuu Marekani wanafundisha Kiswahili badala ya kuliacha suala hili liwe la mtu mmoja mmoja ambapo walimu wanajitafutia ajira wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika sekta ya afya tuna uwezo wa kutengeneza ajira za madaktari wetu. Inawezekana tukawa na uchumi mdogo wa kuajiri wanafunzi wote lakini tunaweza kutengeneza ajira za vijana wetu katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu siyo rafiki sana, napenda kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa wa Tatu. Kwanza naipongeza Wizara kwa Mpango tulioumaliza wa 2016 – 2021, pia kwa Mpango huu wa 2021 – 2026. Mpango ni mzuri, tunapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri tu kwenye sekta ya kilimo. Tumekuwa na kawaida ya kutoa fedha nyingi sana kwenye Wizara mbalimbali hasa za Ujenzi, Afya na Elimu. Naomba kama Taifa, katika kuelekea kukabiliana na Mpango huu wa Tatu, tuwekeze fedha nyingi sana kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu tumekuwa na uzalishaji wa mazao mbalimbali kama kahawa, korosho, mahindi, mpunga na mengineyo. Pamoja na mazao hayo yote, ukienda kuangalia katika Mataifa ndani ya Afrika yanayo-export huwezi kukuta nchi yetu katika nchi 10 bora zinazouza mazao yetu nje ya nchi. Sasa tuangalie jinsi gani tunaweza tukatengeneza Mpango ambao ukatufanya nchi ya Tanzania kuingia angalau hata kwenye kumi bora kwa nchi za Afrika zinazo-export mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na Mipango mingi sana. Toka mpango wa Kwanza, wa Pili na sasa tuko Mpango wa Tatu. Hata hivyo, katika Mipango yote hii hatujawekeza vya kutosha katika sekta ya kilimo. Tukichukua fedha zetu tukaenda kuwekeza kwenda uchimbaji wa mabwawa, kwenye maeneo yenye mvua za kutosha, tukakusanya maji, tusiruhusu maji yetu yakapotea; pia tukatengeneza skimu za umwagiliaji; tukatengeneza utaratibu wa kuzalisha mazao ya kutosheleza ndani ya nchi yetu; na tukatengeneza mazingira ya balozi zetu zikafanya kazi ya kutafuta masoko ya mazao ya wananchi wetu. Mheshimiwa Rais anasema anataka kuzalisha mabilionea Tanzania; mabilionea wako kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kule Ulaya wakati wanaendelea ilikuwa ni masuala ya kilimo. Hata biashara ya utumwa ilikuwa ni biashara ya kilimo. Tuwekeze kwenye kilimo, tutapata fedha; tutapata kilimo cha kutosheleza, tutauza nje, tutapata dola, tutatengeneza ajira ndani ya watu wetu, ajira zitaongezeka, tutapunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu na tutaongeza mzunguko wa fedha ndani ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia, kikifika kipindi cha masika hata mabasi hayana abiria, hata treni zinapungua abiria, hata ndege abiria wanapungua; watu wanawekeza kwenye kilimo. Mpango wetu huu ujielekeze kwenye kuwekeza angalau hata shilingi trilioni moja, tuombe tupeleke kwenye kilimo. Tuchukue trekta tuwapelekee wakulima wetu kwenye kila kijiji, tuhakikishe kuwa kuna trekta, kuna zana za kuwawezesha wakulima wetu wafanye kazi ya kilimo cha uhakika, sasa hivi wanatumia kilimo cha jembe la mkono, kilimo ambacho hawana uhakika nacho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kilimo tutajikomboa, tutapata utajiri, tutapata dola za kutosha, mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa, umaskini utapungua na njaa tutakuwa hatuna. Nchi yetu kijiografia imebarikiwa na ardhi ya kutosha, ina mvua za kutosha, imebarikiwa kuwa na kila kitu, tumeshindwa kuwekeza kwenye kilimo, uwezesho ambao inatakiwa tuone matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo kwenye kilimo bado hatujayaona. Mheshimiwa Waziri, kama kweli tunataka tukomboe Taifa hili, tuwekeze kwenye kilimo. Tunatambua wananchi wetu wanavyohangaika, asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima. Sasa kama ni wakulima mbona hatupeleki fedha za kutosha kwenye kilimo? Kwa nini tusiende kujenga mabwawa? Kama tumefanya operesheni ya ujenzi wa shule, operesheni ya ujenzi wa vituo vya afya, tutafanya operesheni ya ujenzi wa mabwawa na ujenzi wa skimu za kumwagilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami kuwa miongoni mwa wachangiaji katika huu Muswada. Pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Elimu pamoja na Naibu Waziri wa Elimu kwa jitihada kubwa wanazofanya kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu. Pongezi nyingi sana kwenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, kwanza nawashukuru na kuwapongeza kwa kuleta huu Muswada. Huu Muswada ulichelewa sana kuletwa ndani ya Bunge hili kwa ajili ya kupitishwa. Muswada huu ambao tunaupitisha, tayari ulishakuwepo katika nchi mbalimbali duniani. Kwa mfano, nchi kama Ghana, Nigeria na South Africa wanao. Hata Kenya walipitisha Muswada huu mwaka 2015. Kwa hiyo, ni Muswada ambao ulikuwa unahitajika hata kabla siku ya leo, lakini nashukuru kwa sababu ya kuliona hilo, mmeuleta na inakuwa sehemu mojawapo ya kuleta mabadiliko makubwa sana katika sekta ya elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mapendekezo katika Muswada huu. Muswada huu umekuja ukiwa unawalenga walimu peke yake. Nafikiria kwamba kama Muswada huu umefika, ndani yake ungewekwa walimu lakini pia na wahadhiri. Kwa nini tunasema wawekwe pia na wahadhiri? Mkiangalia majukumu yaliyopo ndani ya Muswada huu, majukumu haya haya yanawalenga pia wahadhiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahadhiri pia katika vyuo mbalimbali wana taasisi na jumuiya zao. Kwa mfano, ukienda pale University of Dar es Salaam, wana Jumuiya ya Wanataaluma inaitwa UDASA. Hata ukienda University of Dodoma wana Jumuiya ya Wanataaluma inaitwa UDOMASA. Kwa hiyo, unaona hizi Bodi zipo katika vyuo. Sasa hivi vyuo vina Bodi zao kama vyenyewe, je, iko wapi Bodi inayochukua Bodi zote za vyuo hivyo? Kwa mfano, UDOM hata UDSM na vyuo vingine, iko wapi Bodi inayosimamia hao wahadhiri wote kuangalia maslahi yao na ubora?

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni mengine ya hii Bodi ni kutambua viwango vya utaalam wao; kuwasajili; na kutambua wahadhiri waliopo ndani ya nchi yetu. Hili jambo linawezekana kwani ukiangalia nchi kama Marekani unaweza kutambua ndani ya nchi yao kuna wahadhiri wangapi. Marekani wana PhD holders 67,000 na zaidi; Ujerumani wana PhD holders 28,000 na zaidi; Japan hivyo hivyo; na South Africa ina PhD holders 2,060. Je, Tanzania tuna PhD holders wangapi hatujui, hata ukienda ku-search huwezi kupata, sana sana tunafanya guessing. Bodi hii ni muhimu sana kwanza kuwatambua wenye PhD; masters na degree kwa sababu lengo lake ni kuwatambua na kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao kwa utaalam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza ndani ya Bodi hii kukawepo na Wahadhari. Bodi iwe na department labda ya Wahadhiri; ya waliofundisha form five na six, form one mpaka form four lakini pia ya watu wa primary. Kwa kufanya hivi itasaidia kuhakikisha kwamba una-regulate elimu yetu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili wazo Waziri akiliona linafaa anatakiwa alichukue na ali-edit hapa kwenye kichwa cha habari kwa sababu madhumuni haya yapo na katika nchi zote duniani unakutana nayo, ukienda kuangalia USA, UK, India, mfumo ni huu huu. Kwa hiyo, hapa ni kuongeza tu kipengele hicho kwa sababu leo katika kudhibiti tuna wahadhiri wanaofundisha vyuo vikuu, kupitia Bodi hii inaweza ku-monitor wahadhiri wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaweza kukutana na malalamiko ya watoto wa kike katika vyuo vyetu wakinyanyasika kijinsia na mambo mengine tofauti, hata watoto wa kiume wananyanyasika kupitia utaratibu huo huo. Kukiwepo na Bodi, wanafunzi hawa wanaweza kuwasilisha malalamiko yao katika Bodi na ikawalinda kwa kufuatilia mienendo yao. Ukiwasilisha malalamiko chuoni, chuo kinaangalia umuhimu wa mwalimu katika chuo chenyewe kwa sababu kikimuondoa kitaathirika kama chuo kwa hiyo kinabidi kilinde maslahi ya mwalimu au mhadhiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, lazima Bodi hii iwa-include na wahadhiri kwa sababu hata wahadhiri wanalilia Bodi yao. Kwa hiyo, ingekuwa vizuri sana hii Bodi ikawaingiza na hawa wahadhiri, itasaidia sana ku-regulate elimu katika nchi yetu. Katika mchango wangu nilitaka kugusia suala la kuwaingiza hawa wahadhiri katika Bodi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa sababu ukishakuwa na Bodi itaweza ku-monitor hata ubora wa elimu kwa sababu tuna PhD holders wengi fake na tuna fake masters nyingi sana zinaingia ndani ya nchi yetu. Kukiwa na Bodi lazima hawa waliochukua PhD nje ya nchi lazima waje wasajiliwe ndani ya nchi yetu ili tuwatambue ni nani na nani na wamesoma watu na kwa qualification gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kuna wahadhiri ambao wanatafuta kazi ya kufundisha hawawezi kupata vyuo. Anakuja hapa mhadhiri ana elimu yake lakini hapati chuo lakini kukiwa na Bodi atakuwa registered pale kwa hiyo chuo ambacho kitakuwa na uhaba wa mhadhiri fulani, kupitia Bodi hii itaweza kusaidia upatikanaji lakini pia kutambua uhaba wa hizo qualification.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Kenya kuna standard, hata kwa Bodi hii kuwe na standard ya kumtambua huyu mwalimu ambaye tunataka kumpa ualimu. Kwa mfano, Kenya ili uweze kuwa mwalimu lazima ufanyiwe interview na upate alama ‘C’ na sisi kupitia Bodi hii tuna-graduate wengi sana, kila mmoja anasomea ualimu na akishamaliza kusoma tayari naye kawa mwalimu. Kupitia Bodi itaweza kuwafanyia interview au kuwapa mtihani ambao utawasaidia kuchuja walimu, siyo kila anayesomea ualimu naye ni mwalimu. Ni sawa na wanaosomea uhasibu, unasoma uhasibu lakini unaenda kufanya mtihani wa Bodi ya Uhasibu uki-qualify unaenda kufanya kazi ya uhasibu. Kwa hiyo, hata hii Bodi naamini itaenda kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusisitiza sana wahadhiri waingizwe katika Bodi hii. Hii itasaidia ku-monitor elimu yetu kuanzia chuo kikuu mpaka shule ya msingi na chekechea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni huo katika kuhakikisha kwamba tunaboresha elimu yetu. Ahsante sana.