Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu (19 total)

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Wilaya ya Muheza ina utajiri wa uzalishaji wa matunda kama machungwa, maembe, machenza, mafenesi na kadhalika:-
Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda Wilayani hapo cha kutengeneza juisi na kuwaondolea usumbufu wakulima hao wa kutafuta soko?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya jukumu la Serikali katika kujenga viwanda ni kwa Serikali kuweka mazingira sahihi na wezeshi ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje wa sekta binafsi kujenga viwanda. Katika kutekeleza hilo, sera na mkakati mbalimbali shirikishi inatoa fursa kwa sekta binafsi na taasisi za uwekezaji kujenga viwanda na kunufaika na vivutio mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tanga ikiwemo Wilaya ya Muheza wamejaliwa kuwa na utajiri wa matunda aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na machungwa, maembe, machenza, mafenesi, mananasi kwa kutaja baadhi. Kwa kutambua upatikanaji huo wa matunda, Wizara yangu inahimiza na kuhamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi wenye nia ya kufungua viwanda vya juisi Mkoani Tanga ikiwemo Wilaya ya Muheza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa kampuni ya SASUMUA HOLDING imeanzisha mradi mkubwa wa kulima matunda katika utaratibu utakaoshirikisha wananchi (out grower). Mradi huo ulioko Kwamsisi – Handeni, Mkoani Tanga ni matengemeo yangu kama ukifanikiwa, wawekezaji wengine watavutiwa na kuweza kuwekeza eneo hilo la Tanga na sehemu nyingine za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) lina utaratibu wa kutoa ushauri jinsi ya kuanzisha mitaa ya viwanda kila mkoa ikiwa ni jitihada za kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuendeleza uzalishaji katika mikoa husika. Hivyo, ningependa kumshauri Mheshimiwa Mbunge tushirikiane kuhamasisha na kuwahimiza wadau wakiwemo wananchi na halmashauri mbalimbali nchini kutoa ushirikiano pindi wawekezaji wanapojitokeza.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Wakulima 1,128 wa msitu wa derema kata ya Amani Muheza wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kupunjwa fidia ya mimea yao kutoka shilingi 3,315 kw a shina moja:-
(a) Je, ni lini wakulima hapo watalipwa stahiki zao,
(b) Je, kwa nini kwenye malip hayo Serikali sijijumiushe fidia ya ardhi yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa jumla ya wananchi 1,128 waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo ndani ya hifadhi ya msitu wa Derema, walihamishwa na kulipwa stahiki zao ili kupisha uhifadhi kati ya mwaka 2001 na mwaka 2009, lakini siyo kweli kuwa wananchi hao walipunjwa fidia ya mazao yao. Ukweli zaidi ni kuwa katika mchakato wa kuhakikisha eneo lote la msitu linahifadhiwa kama ilivyokusudiwa, mazoezi mawili tofauti yalifanyika kwa vipindi tofauti na kwa ufadhili wa taasisi tofauti ambazo ni Shirika la Maendeleo la Nchi ya Ufini, FINNIDA lililofadhili fidia kwa mazao kwenye mpaka na Benki ya Dunia waliofadhili fidia kwa mazao ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zoezi la kwanza lililofanyika mwaka 2001 mpaka 2002 chini ya ufadhili wa FINNIDA kupitia mradi uliojulikana kama East Usambara Conservation and Management Programe, idadi ya wakulima 172 waliokuwa wakifanya shughuli za kilimo upande wa nje wa eneo la msitu walilipwa fidia ya mazao yao. Kwa kuzingatia muda mfupi uliokuwa umebaki hadi mradi kufikia tamati yake, shirika hilo liliwalipa wakulima kiwango cha shilingi 28,000/= kwa kila shina moja la mmea wa Iliki, bila ya masharti au kigezo kingine chochote mahsusi kutumika, lengo likiwa ni kuharakisha uhamishaji wananchi na uwekaji wa mipaka rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2002 hadi 2008 wananchi 1,128 waliokuwa na mazao ndani ya msitu walilipwa stahiki zao zenye jumla ya shilingi 1,633,893,595.85. Malipo hayo yalitokana na ufadhili wa Benki ya Dunia ambayo ilitoa jumla ya shilingi 1,238,653,060.85 na vyanzo vingine mbalimbali ambavyo vililipa jumla ya shilingi 395,240,535/=. Tofauti na zoezi la kwanza ulipaji katika zoezi hili ulizingatia masharti ya Benki ya Dunia, Sheria ya Ardhi 1998 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 pamoja na miongozo mingine ya fidia za mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, thamani ya fidia iliwekwa katika viwango tofauti kulingana na sifa za ukomavu wa mazao, umri wa miche, utunzaji wa shamba na idadi ya mazao. Kulingana na vigezo hivyo, viwango vilivyokubalika vilikuwa shilingi 102/=, shilingi 204/=, shilingi 2,040/=, shilingi 3,315/= na shilingi 5,100/= kwa shina. Tathmini kwa mazao ya wananchi yaliyomo ndani ya msitu ilifanyika kwa ushiriki wa karibu wa timu huru za Wakaguzi kutoa Wizara, Taasisi za Umma na Taasisi Binafsi, Mashirika ya Kimataifa na wananchi wenyewe. Aidha, kiwango cha chini kilichofidiwa ni shilingi 3,315/= na kiwango cha juu ni shilingi 22,832,172.32 kwa mkulima mmoja. Nakala ya nyaraka za tathmini na malipo yaliyofanyika zinapatikana katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Muheza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia ya ardhi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mkoa wa Tanga iliahidi kuwapatia wananchi ardhi mbadala ambapo hadi sasa jumla ya maeneo 408 yenye ukubwa wa hekta tatu kila moja yamekwishapimwa na kwamba zoezi hilo la upimaji linaendela hatua kwa hatua kilingana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya gharama za upimaji. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awasiliane na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ili kufahamu zaidi hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa zoezi la ugawaji wa ardhi na namna linavyoendelea.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Mji mdogo wa Wilaya ya Muheza ulianzishwa mwaka 2007 na ulihusisha
Kata tatu za Muheza Mjini, Mbaramo, Majengo na Masuguru; na tangu wakati
huo, umekuwa ukihudumia wananchi wake na taratibu za mapendekezo ya
kuidhinisha uanzishwaji wa Halmashauri ya Mji wa Muheza tangu tarehe
10/01/2016.
Je, ni kwa nini Serikali imechelewa kuiidhinisha Muheza kuwa Halmashauri
ya Mji huku ikijua kuna ongezeko kubwa la watu na Kata zimeongezeka hadi
kufikia sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab,
Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mapendekezo ya kupandisha hadhi
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Muheza, kuwa Halmashauri ya Mji wa Muheza,
yalifanyika na kupitishwa katika vikao vyote vya kisheria, vikiwemo Baraza la
Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa. Maombi haya tayari
yamepokelewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI baada ya kupitishwa na RCC. Hatua
itakayofuata ni kwenda kufanya uhakiki wa vigezo vinavyozingatiwa katika
kuanzisha Halmashauri za Miji nchini.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Baadhi ya wakulima wa Tarafa ya Amani na Muheza wanalima kwa wingi viungo mbalimbali kama pilipili manga, karafuu, hiliki na mdalasini lakini hakuna viwanda kwa ajili ya kusindika mazao hayo.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia kupata kiwanda wakulima wa mazao hayo kwa ajili ya mazao yao?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuwatafutia wananchi hao wanunuzi wa uhakika wa mazao hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Tanga katika mpango kazi wake wa robo mwaka ya pili yaani Oktoba - Disemba, 2016, imeweka mkakati wa kufanya uchambuzi yakinifu (needs assessment) kwa wakulima wa viungo vya vyakula mkoani humo wakiwepo wa Tarafa za Amani na Muheza. Lengo la mkakati huo ni kubaini mahitaji mahususi ya wakulima hao yakiwemo ya kiteknolojia na masoko ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto wanazokabaliana nazo hivi sasa ya kiwanda cha kusindika mazao hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imetenga fedha za kuratibu utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani yakiwemo mazao ya viungo wenye lengo la kuongeza uzalishaji na tija. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya Viwanda imekuwa ikitoa teknolojia mbalimbali za usindikaji mazao zikiwemo za mazao ya viungo kwa wakulima wa Mkoa wa Tanga kupitia karakana ya uendelezaji teknolojia (Technology Development Centre) iliyopo Arusha ambapo teknolojia za usindikaji mazao yakiwemo ya viungo hutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, viungo vinavyozalishwa nchini vina soko la kutosha ndani na nje ya nchi hususani katika nchi za Uturuki, India na Uarabuni. Changamoto ni namna ya kulifikia soko hilo katika viwango na ubora unaotakiwa. Katika Wilaya ya Muheza kuna Makampuni kadhaa yanayonunua viungo na kati ya hayo ni Jumuiya ya Wakulima wa Kilimo Hai Usambara Mashariki (JUWAKIHUMA), Golden Food Product na TAZOP.
Hivyo, Serikali inaandaa mkakati wa kutoa elimu juu ya mbinu bora za uzalishaji wa viungo ili kuinua ubora wa viungo pamoja na mavuno kwa eneo hili kukidhi mahitaji ya makampuni yanayonunua na kuuza viungo ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la SIDO imekuwa ikiwashirikisha wakulima katika maonesho kwa nia ya kujifunza na kupata masoko. Mathalan kwa mwaka 2015/2016, wakulima wa viungo kutoka Tarafa za Amani na Muheza ni miongoni mwa washiriki wa maonesho ya SIDO Kanda ya Mashariki.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Jimbo la Muheza lina kata 37 na vijiji 135, katika Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mradi wa REA ni vijiji vichache tu vilipata umeme. Je, utekelezaji wa REA III ni vijiji vingapi vinategemea kupata umeme ili wananchi wa maeneo haya waweze kujiandaa katika kujiendeleza kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vijiji 37 ambavyo havijapatiwa umeme katika Jimbo la Muheza na vitongoji 137 vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu utakaoanza mwezi Machi mwaka huu. Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mpango wa Usambazaji Umeme Vijijini kwa nchi nzima unategemewa kufanya katika vipengele vitatu unaojumuisha densification, grid extension, pamoja na off-grid renewable. REA Awamu ya Tatu kwa ujumla wake katika nchi nzima ikiwa ni pamoja na Jimbo la Muheza itaanza mwezi Machi 2017. Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi huu katika Jimbo la Muheza utajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 33 yenye urefu wa kilometa 50; ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 0.4 yenye urefu wa kilometa 82; ufungaji wa transfoma 41; pamoja na kuwanganishia umeme wateja 1025. Mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 3.94.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJABU aliuliza:-
Reli ya Tanga inategemewa sana kiuchumi kwa usafirishaji wa abiria na mizigo. Aidha, ni kiunganishi hadi Bandari ya Tanga:-
Je, ni lini Serikali itaboresha na kuijenga kisasa kwa kiwango cha Standard Gauge ili iongeze uchumi na kuleta maendeleo?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa reli ya Tanga katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini Tanzania. Mpango wa Serikali uliopo ni kuunganisha Bandari ya Tanga na Bandari mpya ya Mwambani kwenye reli ya Standard Gauge ya Ukanda wa Kati (Central corridor) kupitia reli ya njia panda ya Ruvu hadi njia panda ya Mruazi ambayo inaunganisha reli ya kati na reli ya Tanga hadi Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa kina (detailed engineering design) wa reli ya kutoka Tanga hadi Arusha (kilometa 438) umekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuanza ujenzi wa reli ya Tanga hadi Arusha kwa kiwango cha Kimataifa. Aidha, Mhandisi Mshauri, Kampuni ya HP Gauff ya Ujerumani inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, yaani feasibility study and preliminary engineering design kati ya Arusha na Musoma pamoja na matawi ya kwenda Engaruka na Minjingu.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya TBC Radio kwenye maeneo ya Tarafa ya Amani Muheza ni hafifu.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mawasiliano ya redio na televisheni ya Kituo cha Taifa cha TBC?
(b) Je, ni lini Serikali itaboresha mawasiliano kwenye maeneo hayo ya milima ya Amani ya Vituo vya Taifa Redio na TBC ili wananchi waweze kunufaika na vipindi hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mawasiliano ya Redio na Televisheni ya Taifa (TBC) yanaimarishwa na kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi. Katika kutekeleza dhamira hiyo, Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na usikivu wa redio na televisheni ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha usikivu wa redio za Shirika katika maeneo ya mipakani mwa nchi ambayo ni Kakonko, Tarime, Rombo, Longido na Nyasa, na utekelezaji wa mradi huo unaendelea. Aidha, katika hatua ya kuhakikisha changamoto ya usikivu wa redio za Shirika inapatiwa ufumbuzi kwa kiwango kikubwa, Serikali imeendelea kuimarisha bajeti ya upanuzi wa usikivu wa TBC, ambapo katika mwaka 2017/2018 shilingi bilioni tatu zimetengwa ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni mbili ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2016/2017, ambapo kiasi cha shilingi bilioni moja zilitengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uimarishaji wa usikivu wa Redio na Televisheni ya Taifa ni wa hatua kwa hatua, hivyo Serikali itaendelea kutekeleza azma hii katika maeneo ambayo kuna usikivu hafifu kwa kuendelea kutenga fedha kila mwaka.
MHE.BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Vitalu vya miti ya tiki – Lunguza Muheza huuzwa kwa njia ya mnada hali inayosababisha viwanda vidogo vidogo vya Muheza kukosa miti.
(a) Je, ni lini Serikali itahakikisha wenye viwanda katika maeneo hayo wanapata vitalu ili kulinda ajira za wanavijiji?
(b) Je, kwa nini wanaopata vitalu wasichane magogo hayo hapo Wilayani ili kulinda viwanda vidogo vidogo vya Muheza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza lenye sehemu na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye biashara ya miti ya misaji, njia mbili ambao ni mnada na makubaliano binafsi hutumika. Mbinu mbalimbali zimekuwa zikitumika katika kuuza miti ya misaji ili kuongeza bei ya miti kwa kutumia ushindani wa bei iliyopo sokoni. Hivyo, ili kupata bei ya soko, mbinu inayotumiwa ni pamoja na kuuza kiasi kidogo cha ujazo wa miti ya kuvuna kwa njia ya mnada. Hivyo, asilimia 30 ya malighafi inayotarajiwa kuvunwa katika shamba husika huuzwa kwa utaratibu huu. Njia hii inasaidia kubaini nguvu ya soko na kuongeza mapato ya Serikali. Njia ya makubaliano binafsi hutumika pia katika uuzaji wa miti mara baada ya bei ya soko kupatikana katika mnada. Hivyo asilimia 70 huuzwa kwa makubaliano binafsi ili kutoa fursa kwa wadau wengi zaidi kushiriki kwenye biashara hiyo. Utaratibu huu kwa kiasi kikubwa umewawezesha wenye viwanda wanaoshindwa kununua kupitia njia ya mnada kupata malighafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza wigo wa soko la ndani, Wizara imeanzisha utaratibu utakaowawezesha wanunuzi wengi wa miti ya misaji walioko nchini kunufaika. Utaratibu huu unawalenga wale wote wenye viwanda vinavyotengeneza samani vilivyopo nchini. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 asilimia 10 kati ya asilimia 70 ya ujazo wa miti uliotengwa kwa ajili ya kuuzwa kwa njia ya makubaliano binafsi utauzwa kwa watengenezaji wa samani ndani ya nchi ili kuongeza thamani ya mazao yao na kuongeza ajira. Matangazo ya mauzo ya miti hufanyika kwa kubandika katika mbao za matangazo na kutolewa katika magazeti kwa muda wa siku 14 kabla ya mauzo. Wenye nia ya kuvuna na wenye kumiliki mashine za kupasua magogo ikiwemo wana vijiji wanaozunguka shamba letu la miti la Mtibwa na Longuza hupewa matangazo hayo kuhusu mnada huo ili nao waweze kujitokeza katika kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kulinda viwanda vya ndani na kuongeza ajira kwa Watanzania, uchakataji wa magogo yanayovunwa katika mashamba ya miti hufanyika ndani ya nchi. Baada ya kuuziwa malighafi kutoka katika mashamba ya miti, uchakataji hufanywa na mteja mwenyewe kulingana na mahali alipoweka kiwanda chake. Sheria na mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu haimlazimishi mwenye kiwanda kujenga kiwanda mahali malighafi inapopatikana.
Nashauri Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuhimiza Halmashauri zetu ziweke mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa katika maeneo yaliyo karibu na mashamba ya miti ili kuongeza ajira kwa wananchi wanaoishi karibu na mashamba hayo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Wilaya ya Muheza imetenga eneo sehemu ya Chatur kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za NHC za bei nafuu na baadae kuuziwa wananchi na NHC walishalipia eneo hilo. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi, Mbunge wa Muheza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba la Taifa linatambua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kuna mahitaji makubwa ya nyumba. Utekelezaji wa mradi wa nyumba Muheza unakwenda sambamba na mpango wa Shirika wa kujenga nyumba za bei nafuu katika Wilaya mbalimbali hapa nchini. Kwa sasa Shirika la nyumba tayari limeingia makubaliano na Halmashauri ya Muheza ili kujenga nyumba 10 katika makubaliano yaliyofanyika tarehe 29 Septemba, 2017 baada ya Halmashauri kuridhia rasmi ramani ya nyumba ambazo zilipendekezwa. Aidha, Halmashauri imeshalipa malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 100 ikiwa ni sehemu ya malipo ya nyumba hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba lina eneo lenye ukubwa wa ekari 83 katika eneo la Chatur. Kwa sasa watalaam wa Shirika la Nyumba wako katika eneo la mradi wakiandaa mpango wa kina kwa matumizi ya viwanja (site plan). Baada ya kukamilisha kwaundaa mpango wa kina wa matumizi ya ardhi, Shirika la Nyumba litajenga nyumba 20 kwa gharama nafuu ambapo nyumba 10 ni kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na nyumba nyingine 10 zitauzwa kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa halmashauri nyingine kuiga mfano wa Halmashauri ya Muheza pamoja na halmashauri zingine ambazo tayari zimekwisha faidika na huduma hiyo zikiwemo Halmashauri ya Busokelo, Uyui, Momba, Geita na kwingineko ambao kwa kiasi kikubwa wamepunguza tatizo la makazi kwa wafanyakazi wao. Kwa Halmashauri ambazo zilijengewa nyumba lakini hawajanunua nyumba hizo kwa sasa soko liko wazi kwa mwananchi yeyote kununua nyumba hizo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya TBC Radio
kwenye maeneo ya Tarafa ya Amani Muheza ni hafifu.
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mawasiliano ya redio na televisheni ya Kituo cha Taifa cha TBC?
• Je, ni lini Serikali itaboresha mawasiliano kwenye maeneo hayo ya milima ya Amani ya Vituo vya Taifa Redio na TBC ili wananchi waweze kunufaika na vipindi hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mawasiliano ya Redio na Televisheni ya Taifa (TBC) yanaimarishwa na kuwafikia wananchi katika mmaeneo yote ya nchi. Katika kutekeleza dhamira hiyo, Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na usikivu wa redio na televisheni ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha usikivu wa redio za Shirika katika maeneo ya mipakani mwa nchi ambayo ni Kakonko, Tarime, Rombo, Longido na Nyasa, na utekelezaji wa mradi huo unaendelea. Aidha, katika hatua ya kuhakikisha changamoto ya usikivu wa redio za Shirika inapatiwa ufumbuzi kwa kiwango kikubwa, Serikali imeendelea kuimarisha bajeti ya upanuzi wa usikivu wa TBC, ambapo katika mwaka 2017/2018 shilingi bilioni tatu zimetengwa ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni mbili ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2016/2017, ambapo kiasi cha shilingi bilioni moja zilitengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uimarishaji wa usikivu wa Redio na Televisheni ya Taifa ni wa hatua kwa hatua, hivyo Serikali itaendelea kutekeleza azma hii katika maeneo ambayo kuna usikivu hafifu kwa kuendelea kutenga fedha kila mwaka.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Zao la Katani linalimwa kwa wingi Mkoani Tanga hususan Wilaya ya Muheza na ni zao tegemeo la Uchumi Mkoani humo na bei ya zao hili katika Soko la Dunia limeongezeka sana:-
• Je, Serikali ina mpango gani katika kuongeza ulimaji wa zao hilo Wilayani Muheza?
• Je, kwa nini Serikali isitafute mwekezaji mkubwa wa kuwekeza katika kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa zao la mkonge linalimwa kwa wingi zaidi Mkoani Tanga. Kwa sasa Wilaya ya Muheza ina jumla ya wakulima wadogo wapatao 211 ambao hadi kufikia mwezi Desemba walikuwa wamepanda hekta 975 na kuzalisha tani 1,462.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kweli kuwa bei ya Mkonge katika Soko Dunia kwa sasa ni nzuri na inaendelea kuimarika, mathalan mkonge ule wa daraja UG, bei yake kwa sasa imefikia Dola za Marekeni kati ya 1,600 hadi 1,800 kwa tani. Hali inatoa fursa kubwa kwa wakulima wa mkonge kunufanika na kilimo hiki na kupata mazao makubwa na hivyo kuimarisha hali zao za maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania inatekeleza Mpango wa Miaka 10 ya Uendelezaji wa zao wa mwaka 2012/2013 – 2021/2022 (10 Years Sisal Development Plan). Mpango huu pamoja na mambo mengine unalenga pia kuongeza idadi ya wakulima wadogo wa mkonge kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi wengi zaidi kwenye kilimo hiki katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilayani Muheza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imetoa maelekezo kwa Bodi ya Mkonge ya kuhakikisha wadau wa mkonge wanaongeza uzalishaji kufikia tani 100,000 mwakani kwa kupanua na kutunza vyema mashamba yakiwemo yaliyomo Wilayani Muheza ili kuongeza tija. Pia kuhamasisha wakulima wapya kujiunga na kilimo hiki, hususan wakulima wadogo wa maeneo ya Tanga, Kilimanjaro, Singida na Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaunga mkono kabisa wazo la kupata wawekezaji wakubwa wengi zaidi wa mkonge Wilayani Muheza kama ilivyo kwa mashamba ya Kigombe, Muheza/Kitisa na Kumburu ili kupanua wigo wa ajira na mapato kwa Halmashauri. Wilaya ya Muheza ina mashamba makubwa yaliyofutiwa hati na Serikali kwa kutoendelezwa na kwa kuzingatia hali nzuri ya soko la mkonge pamoja na mabadiliko ya tabianchi ambayo mkonge huwa hauathiriki nayo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na uongozi wa Mkoa wa Tanga wa kupanga matumizi ya mashamba haya ikiwemo kuhamasisha uwekezaji mpya katika mashamba hayo kwa kuyaendeleza kwa kilimo cha mkonge. Ni vyema Mheshimiwa Mbunge akashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakatumia fursa hii kwa kutenga maeneo kwenye mashamba hayo kwa ajili ya wawekezaji wakubwa na wa kati wa mkonge.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi zake ikiwemo ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za kutoa maji Mto Zigi kwenda Muheza na Vijiji vyake?
(b) Je, Serikali ina mpango gani zaidi ya huo wa kuwaletea maji wananchi wa Muheza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza kutekeleza ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambapo imekamilisha usanifu wa kutoa maji kutoka Mto Zigi kwenda Mji wa Muheza.
Mheshimiwa Spika, kazi zitakazotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa kitekeo cha maji (Intake) katika Mto Zigi, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilometa 23, uunganishaji wa vijiji vitakavyopitiwa na bomba kuu umbali wa kilometa 12 kila upande, pamoja na upanuzi na ukarabati wa mtandao wa usambazaji maji katika Mji wa Muheza.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imeendelea na utekelezaji wa oboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Muheza, kwa mpango wa muda mfupi. Kazi zinazotekelezwa ni ulazaji wa mabomba urefu wa kilomita 16.9 kutoka Pongwe Jijini Tanga hadi Kitisa Wilaya ya Muheza. Gharama za utekelezaji wa mradi huo nishilingi milioni 413.5
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetenga kiasi cha fedha shilingi bilioni 3.17 kwa ajili ya kuendelea na uboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Muheza na vijiji mbalimbali katika Wilaya hiyo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imekuwa na mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Mafunzo yanayohusiana na tafiti hizo maeneo ya Amani Muheza:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza azma hiyo?
(b) Kama Serikali haipo tayari, je, itakuwa tayari kukabidhi majengo yaliyopo Amani - NIMR kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
i. Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inayosimamia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (National Institute of Medical Research kwa maana ya NIMR Act 2002, Cap 59, haiipi mamlaka ya kuanzisha au kutoa shahada lakini inaruhusu utoaji wa mafunzo mafupi na elimu kwenye maeneo yanayohusiana na tafiti za kiafya. Wizara kupitia NIMR inalenga kusimamia utekelezaji wa jukumu hili la msingi kwa taasisi kwa kuanzisha mafunzo mafupi yatakayoendana na mamlaka na majukumu ya taasisi.
ii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa taasisi haipo tayari kukabidhi majengo yaliyomo NIMR Amani kwa Halmashauri ya Wilaya na Muheza, kwa kuwa Wizara kwa kupitia NIMR ina mpango wa kuyatumia majengo hayo ikiwemo majengo ya ofisi, karakana, maabara, hosteli na watumishi waliobobea katika nyanja mbalimbali kutoa mafunzo ya muda mfupi kwenye eneo la tafiti za afya ili kuwajengea uwezo wataalamu katika sekta ya afya nchini.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJABU aliuliza:-
Chuo cha Kilimo cha Utafiti cha Mlingano Wilaya ya Muheza kipo katika hali mbaya:-
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye Kituo cha Kilimo Mlingano ili kiweze kufanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uchakavu ya miundombinu katika baadhi ya vyuo vya kilimo ikiwemo Chuo cha Kilimo cha Mlingano. Changamoto hizo ni pamoja na uchakavu wa ofisi, madarasa, mabweni ya wanachuo, maabara, nyumba za watumishi, maktaba pamoja na Karakana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuvikarabati vyuo vya kilimo kupitia Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (SDP II) ili viweze kutoa mafunzo ya kilimo kwa ufanisi. Uboreshaji huo unatarajiwa kuviwezesha vyuo kuzalisha wataalam wenye umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika sekta ya kilimo. Aidha, uboreshaji huo pia utavutia wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati kujiunga na vyuo kama ilivyokuwa zamani na hivyo kuliingizia Taifa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2018/2019, Serikali imepanga kuvifanyia ukarabati vyuo vya kilimo vyote nchini ikiwemo Chuo cha Kilimo cha Mlingano ambapo jumla ya shilingi bilioni nne zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya vyuo vya kilimo nchini.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Katika kijiji cha Fanusi, Kata ya Kisiwani, Wilayani Muheza wapo wananchi wanaofanya biashara ya kutega vipepeo na kuvipeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupata kipato na pia njia ya kukuza utalii:-

(a) Je, ni lini wataruhusiwa kupeleka tena vipepeo nje ya nchi badala ya Serikali kuzuia kama ni wanyama hai?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuboresha maeneo hayo ili kuwavutia watalii waweze kuja kwa wingi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Jimbo la Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipepeo ni moja ya aina za wanyamapori waliokuwa wakifanyiwa biashara ya wanyamapori hai kwa kusafirishwa nje ya nchi kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na wafanyabiashara kukiuka Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni zake; Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi kwa muda wa miaka mitatu kuanzia Mei, 2016. Aidha, kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, Serikali imeamua kuendelea kufunga biashara ya usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi. Kufuatia uamuzi huo, Wizara inaandaa namna bora ya kushughulikia wanyamapori waliopo kwenye mashamba/ mazizi. Aidha, wafanyabiashara walioathirika kutokana na zuio la kusafirisha wanyamapori nje ya nchi watarudishiwa fedha zao walizotumia kulipia Serikalini kwa ajili ya huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaboresha maeneo ya kuvutia watalii yaliyopo katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Amani ambapo Kijiji cha Fanusi na vijiji vingine 20 vinapakana. Hifadhi hiyo ina vivutio vingi ikiwemo misitu minene, mito, wanyamapori na mimea adimu isiyopatikana maeneo mengine duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu huo, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS inatekeleza mpango wa kuendeleza utalii wa ikolojia na kiutamaduni katika hifadhi ya Amani. Mpango huu unahusu kuboresha miundombinu ikiwemo barabara ya kuelekea Msitu wa Amani, nyumba za kulala wageni zilizopo ndani ya msitu, vituo vya kupumzikia watalii (camp sites) na njia za watalii (nature trails). Juhudi hizi zinatarajiwa kuongeza idadi ya watalii, kuongezeka kwa biashara, fursa za ajira na uwekezaji kwa maeneo yaliyo karibu na msitu huo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Sera ya Serikali ya Viwanda kuhusu zao la chai hairuhusu wakulima wa chai kufungua viwanda wenyewe ili kuiongeza thamani chai hivyo kufanya Kampuni ya East Usambara Tea Co. Ltd. (EUTCO) iliyoko Amani - Muheza kuathirika.

Je, kwa nini Serikali isiiondoe sera ambayo haiendani na sera ya viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuanzisha viwanda vya chai unafanyika kwa kufuata Sheria ya Chai Na. 3 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 na Kanuni za Chai za mwaka 2010. Kwa mujibu wa sheria na kanuni, mwombaji wa leseni ya kuanzisha kiwanda cha kusindika majani mabichi au kuchanganya chai anatakiwa kukidhi vigezo vinavyotakiwa. Mnyororo wa uzalishaji wa zao la chai unahusisha hatua mbili ambazo ni usindikikaji wa majani mabichi ili kuzalisha cha kavu na uchanganyaji na uwekaji wa chai kwenye vikasha kwa ajili ya kuuzwa sokoni.

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya East Usambara Tea Company Limited (EUTCO) ni miongoni mwa wakulima wakubwa wa chai hapa nchini yenye viwanda vitatu vya kusindika majani mabichi ya chai ikiwa ni hatua ya awali ya kuongeza thamani kwenye zao la chai kwa ajili ya kuuza kwenye soko la nje na kwenye viwanda vya kuchanganya na kufunga chai kwenye vikasha. Kampuni hiyo iliomba leseni ya kuchanganya na kufunga chai kwenye vikasha ikiwa ni hatua ya pili ya kuongeza thamani kwenye zao la chai.

Mheshimiwa Spika, kutokana na sheria ya chai, kampuni ilitakiwa kuanzisha kampuni tanzu kwa ajili ya kutekeleza shughuli hiyo kama ambavyo imeainishwa na sheria husika ya kuchanganya na kufunga chai kwenye vikasha. Kwa utaratibu wa sasa hakuna kampuni ambayo imezuiwa kuchanganya na kufunga chai kupitia kampuni tanzu.

Mheshimiwa Spika, lengo la Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ni kuhamasisha ujenzi wa viwanda kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Souka, hata hivyo, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa hivi sasa Bodi ya Chai inafanya mapitio ya kanuni zake kuhusiana na suala zima la usindikaji majani mabichi ya chai. Kazi hii inafanywa kwa kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, na ni matarajio yangu kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi katika mchakato huo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Katika Kata ya Mbomole maeneo ya Sakale Wilayani Muheza kuna madini ya dhahabu ambayo wananchi wamekuwa wakichimba bila vibali na hivyo kukamatwa kwa kuharibu chanzo cha maji cha Mto Zigi:-

(a) Je, ni lini Serikali itatuma watalaam ili kuweza kujua eneo hilo lina madini gani?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuweka utaratibu mzuri ambao utahakikisha kuwa wachimbaji hao wanachimba eneo ambalo hawatasumbuliwa?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tarehe 02/10/2018, Timu ya Wataalamu wa Madini, Mazingira na Maji kutoka Ofisi ya Tume ya Madini Tanga, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) walitembelea na kukagua eneo la Sakale ili kuangalia athari za uchimbaji uliokuwa unafanywa na wachimbaji wadogo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ukaguzi wa timu hiyo, timu ya wataalam ilibaini uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa katika vyanzo vya maji na Msitu wa Amani na hivyo shughuli za uchimbaji madini zilisitishwa katika eneo hilo ili kunusuru mazingira, vyanzo vya Maji na Msitu wa Amani katika Kata ya Mbomole.

Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali za awali zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia Tanzania (GST) ilibaini uwepo wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Mindu, Tengeni, Segoma na Mbambara Muheza na Korogwe.

Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa wachimbaji wadogo wa Kata ya Mbomole eneo la Sakale kuangalia maeneo mengine nje ya Bonde la Mto Zigi ili kufanya shughuli za uchimbaji.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Wananchi wa Tarafa ya Amani wamelima zao la pilipili manga kwa wingi, hivi karibuni bei ya zao hilo imeanguka sana kutoka 12,000/= hadi 4,000/= jambo linalowaumiza sana wakulima:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutuma wataalam kubaini ni kwa nini zao hilo limeshuka thamani?

(b) Je Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima hao ili waweze kulima kilimo cha kisasa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pilipili manga ni miongoni mwa mazao ya bustani yanayoendelea kupewa umuhimu wa kuzalishwa hapa nchini kutokana na mahitaji yake kama kiungo na dawa za binadamu. Kutokana na umuhimu huo, mwezi Machi, 2019, Serikali ilituma wataalam kufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya viungo ikiwemo pilipili manga kwenye Halmashauri za Wilaya ya Muheza na Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ilibaini kwamba bei ya pilipili manga imeshuka kutoka shilingi 13,000/= kwa kilo mwaka 2017 hadi shilingi 4,500/= kwa kilo katika mwaka 2019 kutokana na ongezeko la uzalishaji kwa zao hili nchini pamoja na nchi wazalishaji wakubwa ambao ni Vietnam, Indonesia, Sri Lanka, Brazili na India. Aidha, uzalishaji wa ndani uliongezeka kutoka tani 7,800 mwaka 2014/2015 mpaka tani 12,300 mwaka 2017/2018. Aidha, uzalishaji duniani kwa mwaka 2017 ulifikia tani 725,000 ikilinganishwa na mahitaji yanayokadiriwa kuwa tani 400,000 kwa mwaka. Hali hii ilisababisha kuyumba kwa soko la pilipili manga, kushuka kwa bei na kipato cha wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wadau wa Mazao ya Viungo imepanga kutoa elimu kwa vikundi na Vyama vya Wakulima katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Muheza kuhusu kilimo bora cha mazao ya viungo likiwemo zao la pilipili manga, uhifadhi na kuzingatia viwango vya ubora ili kukidhi mahitaji ya masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza hatua za kupitia upya Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Viungo na Mkakati wa Kuendeleza Mazao ya Bustani ili kuendana na mahitaji ya sasa. Katika kutekeleza azma hiyo, tarehe 8 Novemba, 2019 Wizara ya Kilimo itafanya kikao cha cha Wadau wa mazao ya bustani ili kuandaa Dira ya Uendelezaji wa Mazao hayo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-

Serikali ilituma wataalam wa madini, mazingira na maji katika Kijiji cha Sakale, Tarafa ya Amani kuangalia uwezekano kama uchimbaji wa dhahabu unawezekana katika maeneo hayo.

Je, Serikali imefikia uamuzi gani kuhusu suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 02/10/2018 timu ya wataalam wa madini, mazingira na maji kutoka Ofisi ya Tume ya Madini Tanga, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, wataalam wa Bonde la Mto Zigi, Maafisa Misitu na Serikali ya Kijiji walitembelea na kukagua eneo la Kijiji cha Sakale na Kiara ili kuangalia athari za uchimbaji uliokuwa unafanywa na wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ukaguzi, timu ya wataalam ilibaini uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa katika vyanzo vya maji na Msitu wa Amani na hivyo shughuli za uchimbaji madini zilisitishwa katika eneo hilo ili kunusuru mazingira, vyanzo vya maji na Msitu wa Amani. Katika kusaidia utunzaji wa mazingira, Mradi wa Matumizi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Mto Zigi unaendelea na unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji kwa manufaa ya sasa kwa wananchi na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wachimbaji wadogo wa Tarafa ya Amani kuangalia maeneo mengine nje ya Bonde la Mto Zigi ili kufanya shughuli za uchimbaji.