Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bahati Ali Abeid (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanazozifanya. Mheshimiwa Waziri mna kazi kubwa ya kusimamia Taifa letu kuhakikisha mnajitahidi sana ili mila na desturi za nchi yetu na utamaduni wetu uendelee kubaki. Nasema hivi kwa kuona vijana wetu wanajiajiri kwa kuanzisha sanaa ya muziki huu wa kizazi kipya ambao baadhi yao hasa vijana wa kike huwa wanacheza wakiwa wana nguo ya ndani tu.

Mheshimiwa Spika, hivi Baraza la Sanaa la Taifa linaangalia maudhui ya nyimbo tu kama maneno yaliyotumika siyo au linawangalia kundi lote hata wachezaji? Kwani vijana wa kike baadhi yao wanatutia aibu sana. Mheshimiwa Waziri Wanawake tunadhalilika sana wakati mwingine unashindwa kuangalia TV ukiwa na watoto wako wa kiume kuogopa itatokea hiyo nyimbo yenye vijana waliovaa vibaya, Watanzania sio Wazungu hata kama tunataka muziki ukue siyo hivi. Namwomba Waziri akemee vikali kwani mila na desturi za Watanzania ni hazina kubwa aliyotupa Mwenyezi Mungu, tusiwaachie watu watuharibie.

Mheshimiwa Spika, michezo ni jambo ambalo linalitangaza Taifa letu na Tanzania, kwa kweli tunajitahidi ila viwanja vya michezo Tanzania Bara ni kidogo. Ni muhimu kila vinapopimwa viwanja tukumbuke viwanja vya mpira kwani vipaji vya michezo vinaanzia vijijini Wizara ikishirikiana na Wizara ya Ardhi jambo la kutengwa viwanja vya michezo linawezekana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na miradi ya umwagiliaji; maeneo mengi ya nchi yetu haijamalizika na miradi mingi haikuwa kwenye kiwango chenye kuonesha kuwa hata ikimaliza haitanufaisha Watanzania na hasa ile miradi iliyosimamiwa na Kanda. Kanda hizi kwa asilimia kubwa, miradi waliyoisimamia haikumalizika, ilikuwa ni tatizo. Hivi ni kweli walikuwa ni wataalam waliosimamia miradi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai kwa viumbe vyote. Ni vema Serikali tukipanga vipaumbele vyetu, ni lazima maji tuipe bajeti kubwa na siyo kuipunguzia bajeti. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuongeza hiyo sh.50/= ili bajeti iongezeke. Hivi zile pesa za msaada wa India zimefikia wapi na hata kule Zanzibar?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. BAHATI ALI ABEID: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iondoe kodi na tozo ya mitambo na vifaa vya miradi ya gesi ili miradi hii iweze kuendelea na utekelezaji wake kama ilivyopangwa kwani wakati mwingine miradi hii huwa ina mitambo mizito na mikubwa. Kama TANROADS huwa wanataka sheria iliyowekwa kwa ajili ya tozo hizi ziendelee kama zilivyo. Ni sawa, lakini miradi hii au mashine hizi ni za muda mfupi, siyo za kila siku. Naomba tuondoe tozo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.