Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Makame Mashaka Foum (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAKAME MASHAKA FOUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na kuwa Rais wa Tanzania. Pia namshukuru Mungu na wananchi wa Jimbo la Kijini kwa kunichagua kuwa Mbunge wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uti wa mgongo wa wananchi wa Tanzania. Serikali ikipe kipaumbele zaidi kwani zaidi ya 60% ya Watanzania wamejiajiri katika kilimo. Kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, naishauri Serikali kuweka kipaumbele kwenye kilimo cha umwagiliaji pia kutenga maeneo maalum hasa yenye ukosefu mkubwa wa mvua ili vijana wa maeneo hayo wapate kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana ni nguvu kazi kubwa ya Taifa. Wako vijana wengi waliomaliza kusoma hawana kazi. Naishauri Serikali iweke utaratibu au mkakati wa kuhakikisha vijana wote wenye uwezo wa kufanya kazi wanafanya kazi na mkakati uanze vijijini hadi Taifa. Hali hii itasaidia vijana wengi kutokuhamia mjini na kuzurura hovyo mitaani. Naishauri Serikali iweke utaratibu maalum kwa kuwapatia taaluma nzuri ya uvuvi wa kisasa vijana wetu wanaoishi Ukanda wa Pwani ili wavue uvuvi wenye tija. Kwani uvuvi wa kizamani hauna tija kubwa kwa hivi sasa, mfano uvuvi wa madawa, kuchokoa kwa miguu umepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati sasa kuchukua hatua kali kwa wafanyabiashara wa madawa ya kulevya kwani vijana wengi hivi sasa wanaathirika kiakili, wanakuwa wezi, wabakaji kutokana na kutumia madawa haya ya kulevya. Hivyo, naiomba Serikali isiwe na muhali kwa wasafirishaji na wasambazaji, wote wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuanzia Serikali ya Mitaa hadi Taifa ifanyie kazi kauli mbiu ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli isemayo Hapa Kazi Tu inayoenda sambamba na kutumbua majipu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MAKAME MASHAKA FOUM: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia kuwepo hapa na kutoa mchango wangu. Pia nawashukuru wananchi wa Jimboni kwangu kupitia Chama cha Mapinduzi kwa kunichagua kuwa Mbunge wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea, hivyo bado tutakuwa na mahitaji makubwa ya uchumi na huduma za jamii kama vile upungufu wa hospitali za Wilaya, shule za Msingi na Sekondari. Pia tutakuwa na upungufu wa miundombinu kama barabara na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba hasa Vyama vya Upinzani pamoja na wananchi wote kuunga mkono Serikali hii inayoongozwa na Rais mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais ambaye amedhamiria kwa dhati kuifikisha Tanzania kufikia uchumi wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufikie uchumi wa kati ni lazima kuunga mkono uchumi wa viwanda. Naishauri Serikali kuwa viwanda viwekwe kwa kuzingatia vipaumbele tulivyonavyo mfano, sehemu yenye wafugaji wengi wa ng‟ombe viwekwe viwanda vinavyotumia malighafi hiyo, vivyo hivyo sehemu yenye kuzalisha pamba kwa wingi viwekwe viwanda vyenye kutumia malighafi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ni nchi ya Dunia ya Tatu, naunga mkono uamuzi wa kuchukua miradi kidogo yenye kutekelezeka. Hali hii itatusaidia kupiga hatua nzuri ya maendeleo. Upo usemi usemao haba na haba hujaza kibaba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mfuko wa TASAF wako wajanja huingia katika Mifuko hii na kupewa, nashauri Serikali za Vijiji ziwe makini ili kuzuia wajanja wasipate fursa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MASHAKA MAKAME FOUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya na kuweza kuchangia Wizara hii ya Elimu. Pia namshukuru Waziri na Watendaji wake wote kwa kujipanga vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali ya CCM kwa kupiga hatua kubwa kwa upande wa elimu. Anayesema Serikali haijafanya kitu, je, haoni kwa macho, hasikii, labda ana lake jambo.
Baadhi ya mafanikio kwa Serikali ya CCM ni kujenga shule za awali kutoka jumla ya shule 10,612 mwaka 2010 hadi kufikia shule 14,783 mwaka 2015 zenye Walimu 13,600. Serikali imeandikia watoto wa miaka 7-13 kutoka wanafunzi 6,499,581 mwaka 2005 hadi kufikia wanafunzi 7,679,877 mwaka 2013. Idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu imeongezeka kutoka wanafunzi 139,638 mwaka 2010
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
171
hadi kufikia wanafunzi 218,959 mwaka 2014. Mwaka huu ni mwaka wa historia, Mheshimiwa Rais baada ya kutangaza elimu bure, watoto wengi wamefurika mashuleni, haya ndiyo maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila pawapo na mafanikio na changamoto hazikosi, la msingi ni kujipanga na kuzipatia ufumbuzi. Ufumbuzi wa changamoto kwa upande wa elimu si Wizara peke yake, hili ni jukumu letu sote jamii nzima. Mzazi analo jukumu kwa mtoto kuhakikisha anakuwa na maadili mema kuanzia nyumbani, mzazi ahakikishe mtoto anahudhuria shule na kwa wakati, mzazi ahakikishe mtoto ana afya nzuri na msafi. Serikali ihakikishe kwa kila shule vyombo vitatu viwe vinashirikiana yaani uongozi wa shule, walimu na wazazi kwa ajili ya kumpatia elimu mtoto. Wizara iweke mitaala inayoendana na mapinduzi ya viwanda na kimataifa, vitabu viwe vya aina moja kwa nchi nzima kwa madarasa yote kuepuka kila shule kusomesha mada yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iajiri Walimu wa kutosha ili kuepuka vipindi vingi kwa mwalimu mmoja hasa katika shule za awali. Serikali ihakikishe vitabu vya kiada na ziada ni vya kutosha mashuleni. Walimu waboreshewe maslahi yao ili wafanye kazi kwa hiari. Serikali ifanye ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha Walimu wanafanya kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAKAME MASHAKA FOUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuchangia Wizara hii. Pia namshukuru Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kazi kubwa ya kuiongoza Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ajabu kwa Wapinzani kwamba kazi yao kubwa ni kuelezea kasoro kwa Serikali. Je, hakuna mema yaliyofanywa na Mabalozi wetu? Yako mengi sana, kama kuanzisha Balozi katika nchi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabalozi wetu waongeze jitihada kubwa ya kuitangaza Tanzania katika suala la utalii. Nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii kama mbuga za wanyama sehemu za kihistoria, fukwe nzuri Zanzibar na Tanganyika. Pia bahari yetu ina vivutio vingi, kwa mfano aina ya papa huko Mafia ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba Mabalozi kufanya kazi ya kutafuta wawekezaji wakubwa hasa kwa upande wa utalii. Tunayo fursa nzuri ya kuwapata watalii wa daraja la kwanza iwapo tutapata wawekezaji wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mjusi wa Kihistoria (mabaki) Aliye Ujerumani; namshauri Waziri kuharakisha utaratibu mzuri wa kupata mafao au manufaa yatokanayo na mjusi huyo kwa nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAKAME MASHAKA FOUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa pongezi kwako kwa kazi nzuri ya kuliongoza Bunge Tukufu. Pia namshukuru Mungu kunijalia afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Joseph Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa kwa kazi nzuri ya kuijenga Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2015. Mwenye macho haambiwi tazama, jitihada za Awamu ya Tano tunaziona, Ilani ya CCM imeweza kutekeleza kama ujenzi wa bandari, ununuzi wa ndege, ujenzi wa madaraja na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu zaidi ni kuhusu uwekezaji sehemu ya uvuvi. Tunayo maeneo makubwa ya uvuvi wa maji baridi na bahari. Kwenye bahari yetu tunao samaki wengi ila tuna upungufu wa vyombo vya uvuvi wa kisasa pamoja na utaalam. Pia tuna upungufu wa viwanda vya kusindika na kuchakata mazao yatokanayo na uvuvi. Naomba Serikali yangu kufanya jitihada za kuwekeza vizuri kwenye eneo hili ili kupunguza tatizo la upungufu wa ajira kwa vijana na kuliingizia pato Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kufungua vyuo vya uvuvi hasa maeneo ya pwani ili vijana wetu wapate taaluma ya mazao yatokanayo na uvuvi pamoja na kuhifadhi mazingira ya bahari. Yako baadhi ya mazao ya baharini yako hatarini kutoweka kama kovu, kamba na wengine wengi. Hivyo, tuweke mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunalinda mazao haya muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MAKAME MASHAKA FOUM: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mungu kunijaalia afya njema, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya kutekeleza majukumu ya kulijenga Taifa letu. Pia namshukuru Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii, amani na utulivu tulionao ni kutokana na Jeshi letu.

Mheshimiwa Spika, watu wengi wanafanya makosa kutokana na kutozijua sharia, hivyo naiomba Wizara itumie njia mbalimbali za kuelimisha jamii ili iepukane na kutenda makosa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jeshi la Magereza, naishauri Wizara kupanga mikakati na mipango mizuri ya kuhakikisha Jeshi la Magereza linazalisha chakula cha kutosha kujitosheleza. Sambamba na hilo wanayo maeneo mazuri kwa ajili ya mifugo. Naamini tunaweza kutoa maziwa, nyama na kadhalika kutokana na mifugo.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali pesa za maendeleo zipelekwe kwa wakati ili kutatua changamoto za majengo. Askari wetu wengi wanaishi katika nyumba duni, ili waweze kufanya kazi vizuri tuhakikishe wanapatiwa mazingira mazuri ya kuishi, Askari wetu wengi wanaishi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.